DAPHINE
MTUNZI….EMMANUEL F.KWAY(THE STORY MASTER)
AGE…(18+)
Watchstrap…+255718 862176
SEHEMU YA 6 KATI YA 10
“Ndio hapa?”
“Yes”
“Nipe darubini”
Nyuma ya usukani alikuwa mwanamke huyu wa shoka DAPHINE,wapo nje ya nyumba ya Mh.Cosmas Ngailo ndani ya gari.Kitu kilichowapeleka hapo ni kujua data za kumpata Karanje,ilikuwa ni lazima wazipate siku hiyo kwa njia moja ama nyingine.Ndiyo maana Daphine hakutaka kuliweka jambo hilo kiporo.Ilikuwa ni lazima usiku wa siku hiyohiyo,apate pa kuanzia.Akakamata Darubini na kuanza kuangalia huku na kule,kwa juu gorofani aliona watu watatu wanatembea.
“Daphine”
Dustan,akaita.Alionekana alikuwa ana jambo anataka kushauri.Daphine,akamtizama kwa macho yaliyosema ‘Nakusikiliza ongea’
“Kwanini tusifanye zoezi hili usiku?”
“Kwanini isiwe sasa hivi?Unaogopa?”
“Hapana,tusiingie kichwa kichwa.Tusubiri kwanza”
“Mbona unakuwa mwoga hivyo?”
“Ni pendekezo tu nimekupa”
“Sawa,wazo zuri.Saa moja kamili”
Gari lao lilipaki umbali wa kama mita mia mbili kutoka kwenye nyumba ya Mr.Cosmas Ngailo,makamu wa Rais.Hakukuwa na mjadala, ilikuwa ni wazi kabisa kulikuwa kuna ulinzi wa kufa mtu ndani ya jumba hilo kubwa,ndiyo maana Dustan akashauri giza likiingia ndiyo waanze kazi.Masaa yalikimbia huku wakiendelea kujipanga,ilivyotimu saa 12;57 jioni.Daphine akaanza kukoki bastola yake,akachomeka kiwambo cha kuzuia sauti isitoke!Akamtizama Dustan, ambaye hata yeye alikuwa anaweka silaha zake vizuri,wakatizamana.
“Tunaenda?”
Daphine akauliza.
“Ndio”
“Pita kule,mimi napita huku”
Kila kitu kikapangwa kabla ya kuingia ndani,alichofanya Daphine ni kuzunguka uwani, huko geti dogo lilifungwa,alivyoangalia ukuta.Ulikuwa una waya zenye shoti juu yake,akapiga hesabu za harakaharaka na kushindwa afanye nini.Yeye Dustan,alifika getini na kugonga.Haikujulikana ni kwanini anajiamini namna hiyo,geti likafunguliwa akatoka askari ameshika mtutu.
“Nikusaidie nini?”
“Mimi Usalama wa taifa,kuna dharura.Naomba niingie”
“Hapana”
“Nimekwambia ni dharura,ni mambo ya kiusalama, unavyozidi kunichelewesha.Ndiyo hatari inazidi kuwa kubwa.Familia ya Mh.Cosmas Ngailo ikipata matatizo,utahusishwa moja kwa moja”
Dustan,aliongea kwa umakini akiwa na kitambulisho mkononi kutoka usalama,hiyo ilimfanya mlinzi huyu aanze kuhaha!Akamkaribisha Dustan.Hilo kwake lilikuwa ni kosa la jinai kwani kazi ya Dustan ilikuwa ni kuhesabu walinzi wapo wangapi ndani.
“Mheshimiwa yupo?”
“Yupo njiani anakuja”
“Okay”
Kitendo cha Dustan,kujua idadi ya walinzi.Akatembea hatua tatu mbele,hapohapo akageuka.
“Pyuu! Pyuuuu!”
Askari akapigwa risasi mbili za mguu,mlio wa sauti ya bastola ulikuwa ni kama ushuzi wa mtoto mchanga akijamba, sababu ya kiwambo kilichowekwa mbele,walinzi wengine wawili.Wakapigwa risasi.Wakadondoka chini, alichofanya Dustan ni kuwasogelea na kuzichukua silaha zao,akatembea mpaka kwenye geti la uwani.Akalifungua,Daphine akaingia akiwa mwenye usongo!
“Cosmas,yupo njiani”Dustan akasema!
“Sawa,mimi naingia ndani kuweka mambo sawa.Wewe baki hapa”
“Poa”
Zilikuwa ni mbinu za kijasusi,Daphine akazama ndani.Ambapo hakukaa sana akasikia mlio wa honi.Alichofanya Dustan ni kumsogeza askari aliyelala chini mpaka pembeni,akabonyeza kitufe maalum,geti likafunguka!Gari tatu zikaingia ndani!Kitendo cha walinzi kuanza kumfungulia mlango wa gari Mh.Cosmas walichezea risasi kutoka juu gorofani, kutoka kwa Daphine kama kawaida hakufanya makosa,kila risasi ilimuangusha mlinzi mmoja.Mbaya zaidi mbele yake,alikuwa amemshika mwanamke mnene kiasi,huyo alikuwa mke wa Makamu wa Rais, Mh.Cosmas Ngailo.
“Uhai wa mkeo upo mikononi mwako”
Daphine akasema akiwa juu gorofani,hiyo ilimfanya Mh.Cosmas Ngailo,aanze kutetemeka akiangalia juu.Hakukaa sawa,akahisi kama kuna kichuma kimemgusa nyuma ya kisogo chake!
“Brigedia Karanje yuko wapi?”
Dustan,akauliza.
“Karanje yuko wapi?”
“Pyuuuuuuuuuu”
Mlio huo wa bastola ulisikika kutoka juu,risasi ilipenya mkononi mwa mke wa Mh.Cosmas Ngairo,akaachia ukulele wa maumivu jambo hilo,Cosmas alilishuhudia.Akapata uchungu ajabu.
“Risasi nyingine ya kichwa,nina amini sura hii sio ngeni kwako sitokuuliza tena kwa mara nyingine.Nahitaji kujua Karanje alipo”
Daphine akauliza,bastola akiwa ameiweka kichwani kwa mke wa Cosmas Ngailo,hana punje za mzaha hata kidogo!
“Yuuyuuuyuupo Arusha,SAKINA”
Mh.Cosmas Ngailo akasema kwa uwoga huku tayari suruali yake ikiwa imelowa,kutokana na uwoga aliokuwa nao,ilifanya mpaka ajikojolee bila kujua.
Halikuwa jambo rahisi kama walivyodhani,hawakuelewa ya kuwa kwa wakati huo wameingia kwenye hatari kubwa sana, kiasi kwamba ingegusa serikali na kuwaanika viongozi wa nchi,hiyo ingepelekea kuanzisha vita kali baina yao na jamhuri ya muungano wa Tanzania,hususani chama kilichokuwa madarakani.Sio Dustan wala Daphine,hakuna hata mtu mmoja kati yao aliyekubali swala hilo waliachie, ndiyo maana walikuwa wapo tayari kujitoa muhanga kwani maji tayari walikuwa wameyavulia nguo,hivyo hawakuwa na budi kuyaoga!
Mr.Cosmas Ngailo alikuwa katika wakati mgumu kuliko kawaida,siyo yeye familia yake ilikuwa tayari ipo mateka,mkewe anavuja damu nyingi hiyo ilimaanisha angefanya mchezo mkewe angepoteza maisha yake siku hiyohiyo, kisa tu kumkingia kifua Brigedia Karanje,kwa maana nyingine maisha ya mkewe yalikuwa mikononi mwake mwenyewe ili kuyanusuru ilibidi azungumze kila kitu.Mh.Cosmas Ngailo mbele, Dustan nyuma,wakapandisha mpaka juu gorofani, ambapo huko alinyeshewa mvua ya maswali.
“Mount Meru Hotel,ndio atakuwa pa…le!Lakini msini..ue”
Mheshimiwa Cosmas Ngailo alizungumza huku akitetemeka,waliokuwa mbele yake siku hiyo walimtisha, alikuwa yupo tayari kuwasujudia ili tu wasiutoe uhai wake.
“Tutakuuwa kama hatutopata ushirikiano wako”
“Ndi..o hayo tu”
Daphine,akamgeukia Dustan na kumuangalia usoni,kuna kitu ilielekea alitaka kumwambia lakini akasita kidogo!
“Daphine”
Dustan akaita na kumpa Daphine ishara ya kichwa watoke pembeni kuna jambo anataka kumueleza,hiyo ilimfanya asogee mpaka karibu na mlango lakini macho yake yote yalikuwa kwa Mh.Ngailo na Mkewe.
“Tuna masaa machache tu”
“Naelewa”
“Tunafanyaje?”
“Mamia na elfu ya watu,Dustan”
Daphine alizungumza kwa uchungu,hapohapo vifo vya wazazi wake vikamjia kichwani,akaiona sura ya Brigedia Karanje na kubana meno yake kwa hasira.
*****
Muda haukuwa rafiki tena kwa Ngesa,akili yake ilifanya kazi kwa kasi ya risasi, kubaki nchini Kenya kwa muda huo kungemaanisha kuruhusu roho za watu kufa kwa sumu kali ambayo Brigedia Karanje,alitaka kuiweka katika mtungi wa kiyoyozi ndani ya hoteli ya nyota tano, inayoitwa Mount Meru, hapo ingesambaa na kumuua mtu yoyote ambaye angevuta hewa hiyo,siri hiyo aliipata kwa mwanajeshi mmoja ambaye alivyoangalia kitambulisho chake alifahamika kwa jina la Luteni Akio Jumbe,mwanajeshi huyo hakuweza kubaki na siri hiyo kifuani kutokana na mateso makali ambayo tangia azaliwe hakuwahi kukutana nayo.Hapo ndipo alisema operesheni nzima itakavyokuwa na baada ya hapo ni lazima Brigedia Karanje,atakutana na jeshi lingine huko Mkoani Arusha wakafanye ambush Ikulu,akaropoka kila kitu hata vingine ambavyo hakuulizwa,wakati mwingine alidiriki kutaja hadi jina lake la utotoni.
“Ku..na kikos..i kingine Arus..ha ni laz..iam wakuta..ne”
Luteni Akio Jumbe,alizungumza akiwa katika mateso makali kupita kiasi,alivuja damu mwili mzima.Hususani kwenye miguu yake!
“Uliniambia serikalini kuna viongozi wana husika?”
“Ndi..o”
“Nitajie majina yao”
“Siwa..jui kwa maji..na”
“Una uhakika?”
“Sina sa..babu ya kukuda..nganya”
“Mpigie sasa hivi mkuu wako,mwambie tayari umenikamata na umeniua nataka kujua ni wapi alipo.Kumbuka kitu kimoja,ukienda kinyume!Hautokuja kunisahau katika maisha yako”
Ngesa alizungumza,hakuwa mwenye punje ya masihara hata kidogo,kile alichoongea alikimaanisha.
Luteni bado alipenda kuishi duniani japokuwa hakuwa mwenye uhakika kama angeachwa hai baada ya hapo,akachukuwa simu na kumtafuta Brigedia Karanje hewani,ndani ya dakika moja akawa tayari kwenye laini akampa ripoti.
“Luteni,una uhakika?”
Brigedia,aliuliza huku akiwa amepigwa na butwaa, hata yeye hakuwa tayari kuamini taarifa za kifo cha Ngesa,kirahisi namna hiyo.
“Ndio Mkuuuu”
Luteni,alizungumza akiwa katika mateso makali.Mlango wa bastola upo kichwani kwake kumaanisha kwenda kinyume, ubongo wake ungechenguliwa na risasi na ungemwagika chini.
“Una uhakika ni Ngesa?Msije mkawa mmemuuwa mtu mwingine?”
“Ndio yeye”
“Ulifanya nilivyokwambia?”
“Kichwa chake?”
“Ndio nachotaka kama ushahidi,mnacho?”
“Ndo tunataka tukichukuwe”
“Kazi nzuri,sisi ndio tumeingia Arusha kazi itaanza rasmi leo saa moja jioni,Uwahi.Nahitaji kuona hicho kichwa cha Ngesa”
“Sawa mkuu”Kitendo cha Luteni Akio Kumaliza mazungumzo yake akiwa anasikika na Ngesa, hapohapo alichomwa kisu cha shingo!Akadondoka chini akiwa ameishikilia,ndani ya dakika moja kasoro akawa tayari amekata roho!Ngesa hakutaka kupoteza wakati,akaanza kukimbia kuelekea upande wa barabara ya lami, damu zilikuwa nyingi mikononi mwake,hakujali.Alichofanya ni kutulia kwanza na kupiga hesabu za harakaharaka,alichoshukuru Mungu ni baada ya kusikia muungurumo wa Pikipiki,akakaa sawa ili kufanya anachotaka kukifanya.Pikipiki hiyo aina ya Baja, ilipotokeza karibu usawa wake,akamrukia dereva kama ngedere anavyodandia mti mwingine,wote wakadondoka chini pikipiki ikaruka kando,akamvuta dereva wa pikipiki na kumtuliza vichwa viwili vikali vya pua ili atulie,alivyohakikisha zoezi hilo limetimia,akakimbilia pikipiki.Akaisimamisha kwa haraka na kuiweka sawa,jinsi alivyoizungusha iliogopesha kwani kufumba na kufumbua akapotea machoni mwa wanakijiji walioshuhudia tukio alilolifanya.
Pikipiki ilikua katika mwendo wa kilomita kumi kwa dakika,jinsi Ngesa alivyoikimbiza pikipiki iliogopesha, mbaya zaidi hakuvaa ‘helment’ kumaanisha kwamba nzi angemgonga kwenye jicho lake,angepata ajali mbaya sana, zaidi na hayo upepo ulikuwa mkali mno.Hiyo haikumfanya yeye apunguze mwendokasi, ilikuwa ni lazima aingie nchini Tanzania ndani ya masaa machache,aokoe maisha ya watanzania ambao wangekufa bila hatia,ndiyo maanaa alitimua chombo hiko kwa kasi ya ajabu.
Ndani ya masaa manne alikuwa mpaka wa Namanga unaotenganisha Kenya na Tanzania,hapo aliitelekeza pikipiki kando na kuanza kupita njia za panya,picha zake zilikuwa kila mahali.Akatembea mpaka kando kando kabisa na kubandua ndevu pamoja na nywele za bandia akarudi katika sura yake halisi.
Alivyotizama huku na kule na kuona kuna usalama akaendelea kusonga mbele,ambapo alitembea kwa kujificha ficha.Hiyo ni kutokana na ulinzi wa mpakani, ulimwogopesha hata yeye,hakuwa ana uhakika kama angepita salama salmin bila kugundulika,kilichomsaidia ni kujiamini kwake, mikono iliyokuwa imegandia damu aliiweka mifukoni na kuendelea kudunda,akapiga jicho huku na kule.Akamuona askari mmoja akiwa amezubaa akapita kandokando yake na kuzidi kuchapa lapa!
“Arooo,arooo,wewe kijana.Simama hapo.Hey arooo nitakuripua”
Sauti ya askari kutokea nyuma yake,ilimshtua sana!Akajua tayari amekwisha na huo ndio ungekuwa mwisho wake sababu aliziona picha zake zimebandikwa karibia boda nzima ya Namanga!
*******
Brigedia Karanje na timu nzima ya wanajeshi ishirini na tatu waliohasi nchi ya Tanzania walikuwa tayari wameweka kambi nje ya hotel ya Mount Meru, majira ya saa moja jioni,ilikuwa ni lazima siku hiyo wafanye ambush.Kwa maana hiyo kila kitu kilikuwa kimepangwa ngazi kwa ngazi hatua kwa hatua,hawakutaka kukurupuka kama askari migambo wa jiji.Hatua ya kwanza kabisa kuifanya ilikuwa ni kuharibu jenereta kubwa, ambalo lilikuwa linawaka lenyewe baada ya sekunde kumi endapo umeme utakatika,walivyohakikisha mtu wao kafanya uharibifu huo,mwingine akazama kwenye mfumo mzima wa umeme,akakata waya!Hapohapo umeme ukakatika,hazikupita dakika tano wakatokeza wanaume watano waliovalia jezi za kampuni ya TANESCO!Na kujitambulisha mapokezi.
“Tumetokea Tanesco,tumepigiwa simu na meneja!Tuje hapa,kuna tatizo kidogo kwenye system ya umeme!Inabidi tukaangalie wayaring nzima”
Jamaa mmoja aliyekuwa na kitambulisho kifuani alizungumza,akiwa amevalia jezi za kampuni hio ya Umeme,msichana mrembo wa mapokezi hakuelewa lolote!Kutokana na kukerwa na tatizo hilo la umeme kukatika ukizingatia siku hiyo kulikuwa na wageni wengi ndani ya vyumba hakutaka kuhoji sana,akamuita msaidizi wake.
“Kawaoneshe main switch”
“Tunahitaji pia chumba cha Ac,tuanze kuangalia kuanzia huko.Nina imani shoti itakuwa imesababishwa na hizo mashine”
Kila kitu kilipangwa na watu makini,ndiyo maana waliingia ndani ya hoteli hiyo kiulaini kabisa,walivyooneshwa chumba kikubwa cha mitambo wakaingia wenyewe ambapo humo hawakufanya makosa.
Wakatega vikopo vidogo viwili kwenye kila mtambo unaotoa hewa.Baada ya hapo,wakaseti dakika kwani juu ya vikopo hivyo kulikuwa na kitu kama saa ambayo waliitegesha ndani ya dakika thelathini,vikopo hivyo vitafyatuka watawasha umeme na baada ya hapo hewa yenye sumu itaanza kutoka na yeyote ambaye angevuta hewa hiyo, huo ndio ungekuwa mwisho wake!
******
Akili ya Ngesa ilifanya kazi kwa kasi isiyo ya kawaida ingawa hakuelewa kama zoezi analotaka kujaribu kulifanya lingezaa matunda endapo askari huyo,asingekubali.Kiutaalam akaingiza mkono mfukoni na kuchomoa noti ya dolla mia moja,akaifinyanga kidogo kama ugali wa dona,akamshikisha askari mkononi mwake.Hiyo ilifanya askari huyo,atizame huku na kule kama askari wa usalama barabarani wanavyopewa,kifuta jasho!
“Tembea haraka bwana mdogoo,nisije nikakuarrest”
Askari huyo,akasema kwa sauti ya chini,hiyo ilimfanya Ngesa aendelee na safari yake,pesa ikawa imefanya kazi yake!Akatembea kwa staili ile ile,alivyofika upande wa Tanzania,bila kupoteza wakati akaingia ndani ya gari, ambalo nyuma ya usukani alikuwepo muhindi!
“Taka nini wewe?Itia mwizi mimi”
Muhindi,alianza kufoka kwa sauti kubwa,akimwambia Ngesa ambaye alipanda ndani ya gari lake.
“Washa gari,fanya haraka”
Ngesa,akaongea huku mkononi akiwa na bastola.Muhindi bila kuongeza kitu kingine chochote akawasha gari na safari ikaanza mara moja!Walivyotembea umbali wa kama kilomita ishirini,Ngesa akamtoa Muhindi huyo ndani ya gari na kumtupa nje.Akachukuwa usukani,kwa kasi ya ajabu, akazidi kusonga mbele ili awahi Mount Meru hotel, azuie vifo vya watu wasiokuwa na hatia.
Hivyo kwa upande wake,alikuwa anakimbizana na muda ilikuwa ni lazima afanye hivyo,hakuelewa ingekuwaje endapo atakuta tayari Brigedia Karanje,keshaweka sumu hiyo kali.Bahati nzuri gari aina ya Landcruier V8, aliyokuwa anaendesha ilikuwa yenye uwezo mkubwa kukimbia,hivyo saa 12;52 jioni, akawa tayari ameingia Mjini,dakika nyingine zilimtosha kupita njia za panya na kuibuka karibu na hoteli ya Mount Meru,alichokiona kilimuogopesha zaidi, akajua tayari Brigedia Karanje,ameshafika kulikuwa na giza nene kwenye hoteli.Bila kupoteza wakati akaanza kukimbia kuelekea ndani kama mwizi,anayekimbizwa!Alivyofika mlangoni,ambapo hapo kulikuwa na mlinzi anayekaa kwenye lango kubwa alimsukumiza kwa nguvu na kuzama ndani kabisa!Akaanza kukimbia hovyohovyo,hakuelewa ni wapi anaelekea lakini alichojua yeye ni lazima sumu hiyo itegwe kwenye chumba cha mtungi wa gesi mkubwa!Hapo ndipo alipoangalia vizuri na kuanza kupandisha ngazi mbilimbilli,mpaka gorofa ya tano chumba cha kushoto,akafungua mlango taratibu,akachomoa bastola yake!Ndani kulikuwa na giza totoro lakini mbele kulikuwa na miale ya tochi ina mulika mulika,alivyopiga hatua mbili mkono wake ukapigwa teke bastola ikadondoka chini akakabwa kwa nguvu shingoni,alivyotaka kujigeuza akatulizwa na kifuti cha mbavu.Ngesa hakutaka kukubali,akatuliza akili na kugeuka na ngumi ambayo ilimpata mtu huyo mdomoni,akatumia nafasi hiyo bila kufanya makosa akatupa ngumi nyingine lakini ilipita hewani,kulikuwa na mwanga hafifu hiyo ilimfanya aangalie kwa makini ngumi zinazorushwa,alivyotuliza akili yake.Akashtuka kidogo!
“DAPHINE”
Ngesa akaita, baada ya kugundua anapambana na mwanamke huyu jasiri, Daphine.
“Ngesa!”
Daphine nayeye akapigwa na butwaa,akiwa katika mshtuko wa ajabu kwani hakutegemea kumuona Derrick Ngesa, mahali hapo!
Sio Daphine wala Ngesa,kila mtu alipigwa na butwaa la waziwazi.Kwa macho yaliyosema ‘Umefikaje hapa?’Daphine alimshangaa Ngesa na Ngesa alibaki akimtumbulia macho Daphine.Hapo walishindwa kuzizuia hisia zao na kujikuta wanakumbatiana kwa nguvu huku wakipigana pigana migongoni,japokuwa walikuwa wana furaha lakini walizungumza kwa sauti ya chinichini.
“Ulikuwa wapi Ngesa?”
Daphine,akauliza alishindwa kujizuia.
“Nitakwambia”
Ngesa akajibu na kutizama mbele ambapo huko kulikuwa na miale ya tochi, zikimulika huku na kule,kuashiria kwamba kuna watu.Hiyo ilimaanisha ya kwamba hawakuwa na muda wa kuendelea kubaki hapo na kuulizana maswali kwani kilichowapeleka hapo ni kuokoa mamia na maelfu ya watu, ambao wangekufa siku hiyo baada ya sumu hiyo kali kusambaa.Kwa kutumia ishara ya mikono,kila mtu akajigawa upande wake,Ngesa alivyookota bastola yake kutoka chini akaelekea Mashariki na Daphine Magharibi.
Mwendo wa taratibu alioutumia Daphine kutembea, isingekuwa rahisi kugundulika hata kidogo,alitembea taratibu ili awakaribie majangili hao, wanaotegesha sumu kali kwenye mtambo wa kiyoyozi,alivyopiga hatua kama saba hivi, akajificha nyuma ya mashine kubwa,hiyo ilimaanisa kitendo cha kujitokeza kizembe angeonekana kabla ya kufanya anachotaka,kwa umakini wa hali ya juu akasogea taratibu na kuuzungusha mkono wake shingoni kwa mwanajeshi aliyekuwa amesimama kando kizembe,kwa nguvu za ajabu akamvuta kwa nyuma kwenye mashine na kuendelea kukandamiza koo lake bila wenzake kujua chochote.Hiyo ilifanya mwanajeshi huyo akukuruke lakini hakufanya lolote sababu Ngesa alitokea na kumchoma kisu cha shingo!Damu nyingi zikaruka kando,mwisho wa maisha yake ukawa umeishia hapo.
Mbele yao kulikuwa na wanaume wengine watatu!Wanahangaika kuweka vitu vyao sawa ili waondoke,waliamini kila kitu kipo sawa bila kujua tayari, watu hatari Daphine na Ngesa wapo nyuma yao,sijui ilikuwaje Daphine akagonga kichuma kilichokuwa pembeni kikatoa kelele, hiyo ikafanya wanajeshi hao wageuke nyuma.
“Moses!Moses!Moses!”
Mmoja wapo aliita kwa sauti ya chini akidhani wenda ni mwenzao lakini ukimya uliendelea kutawala,wasiwasi ukamuingia akapiga jicho huku na kule.
“Moses yuko wapi?”
Ilibidi awaulize wenzake.Hakuelewa tayari Moses anayemuulizia ni maiti,ukimya huo haukumuingia akilini hata kidogo, hapohapo akachomoa bastola na kuangaza upande wa mashine kubwa ilipo,ambapo nyuma yake Ngesa na Daphine walikuwepo.Wao walitumia uwazi mdogo sana kumuona Mwanajeshi huyo anayekuja usawa wao akiwa na bastola mkononi,Daphine alivyoangalia pembeni akaona mwili wa Mwanajeshi aliyekufa unachuluzika damu,hiyo ilimaanisha ingeendelea kusambaa na wangegundua muda mfupi ujao.
Wakatizamana kwa sekunde tatu,mwanajeshi aliyeshika bastola akazidi kusogea upande wao.
“Sirgent”
Akaita,kuna kitu alianza kuhisi kisichokuwa cha kawaida.Pua zake zilihisi harufu ya damu.
“Nini?”
Mwenzake akauliza kwa sauti ya juu kidogo yenye mkwaruzo.Kwa kutumia ishara akamuita karibu yake,wakawa wawili wanasogea karibu na mashine,kuna kitu walihisi,machale yaliwacheza.
“Sssssh”
Akamnyamazisha mwezake kwa kutumia kiganja cha kidole huku wakinyata,hawakuelewa wamezidiwa akili na kila hatua waliyokuwa wanafanya walionekana.Ngesa na Daphine, wakaweka bastola zao vizuri na kupeana ishara kwamba mmoja amfyatue wa kulia mwingine wa kushoto.Wakaanza kuhesabu kwa sauti ya chini!
“Moja..Mbili..Tatuu..Paaa paaaa”
Mlio wa bastola ulisikika risasi zote zilizaa matunda kwani wanajeshi wawili walidondoka chini kama mizigo puu,mmoja aliyekuwa kwenye mitambo anaweka vizuri alivyosikia mirindimo ya risasi,akafyatua kitufe cha juu kilichokuwa kama baruti,hapohapo gesi ikaanza kutoka.
“Paaaaaa”
Daphine akaachia risasi lakini hiyo ilimkosa kosa kisogoni kwani alikimbia na kupotelea gizani.
“Ngeeesaaa”
Daphine akaita kwa sauti huku akiwa kama mtu aliyechanganyikiwa kabisa,wakasogea karibu wakakuta tayari kikopo cha gesi kimefyatuka.Hiyo ilimaanisha sumu imeanza kusambaa ndani ya vyumba tayari.
“Daphiiineeeee”
Kasi aliyochomoka nayo Daphine,haikuwa ya kawaida alianza kukimbia huku akikata kona kama gari lililofeli breki,ingawa Ngesa alimuita lakini haikusaidia.Ilikuwa ni lazima amtie mikononi mwanajeshi huyo,haikuchukuwa sekunde tano umeme ukarudishwa sababu tayari sumu ilikuwa imetegeshwa hiyo ilimaanisha ni lazima ipite ndani ya matundu ya kiyoyozi, atakayevuta ni lazima adondoke chini na kukakamaa hapohapo.
“Paa! Paaa! Paaaa!”
Milio ya risasi ilisikika, Daphine alikuwa akipiga hewani ili mwanajeshi aliyekuwa anamkimbiza asimame,hakuweza kumfyatua, hiyo ilitokana na msongamano wa watu wanaokimbia huku na kule.Kufuatia mlio huo,kila mtu alisambaratika.
“Zima a.c zote,sasa hivi”
Kila kitu kilikuwa kimeharibika,watu walipigana vikumbo wengine walichanja mbuga wakakimbia mpaka miguu yao ikagusa visogoni.Lakini Daphine alilala sahani moja na mwanajeshi aliyetoka nje.Akamuona anaingia ndani ya gari,akalikimbilia gari mpaka barabarani huku akirusha risasi kwenye gari la mbele yake,akatokeza katikati ya lami kwenye magari yanayoenda kwa kasi,kuna gari lilikuwa linapita likapiga breki kali,akafyatua risasi moja hewani.
“Shuka ndaniii ya gari”
Mzee aliyekuwa ndani ya gari,alitetemeka na kukosa nguvu, mbele yake alisimama mwanamke ameshika bastola.Mwili wake ukawa kama umepigwa ganzi mpaka Daphine alivyofungua mlango na kumtupa nje,hakuchelewa akaweka gari gia na kulitoa kwa kasi ya risasi.Kila kilichotokea kilikuwa ni kama sinema ya kijasusi.
*********
Kila aliyevuta,hewa ndani ya hoteli hiyo alidondoka chini na kutingisha miguu kisha kukakamaa na kufa hapohapo,ndani ya dakika mbili watu ishirini na saba walikuwa chini wanapambana na umauti,sumu hiyo iliuwa vibaya sana na kabla hujafa ni lazima ukakamae,hatari ilikuwa kubwa sana.Kazi ya Ngesa ilikuwa ni moja tu,kutoa watu nje akiwa na kifaa maalum cha kuziba pua, ambacho alitumia ili hewa hiyo ya sumu isimdhuru.
“Njoo huku,usiogope”
Mtoto mdogo wa kizungu kati ya umri wa miaka 10-17,alikuwa mbioni kuvuta pumzi hiyo na kupoteza maisha yake.Ngesa akajitosa na kubana pumzi zake,akavua kifaa kilichokuwa puani mwake na kumuwekea puani.Akamuweka begani na kuanza kutoka naye nje!Kitendo cha kumuweka nje ya hotel,askari zaidi ya kumi na tano walimzunguka wakiwa na mitutu mikononi mwao!
“Piga magoti, weka mikono yako juu.Upo chini ya ulinzi”
Askari walikuwa wengi,hiyo ilitokana na kusikia mirindimo ya risasi pamoja na kupigiwa simu,kilichowafanya wajihami zaidi ni badaa ya kugundua mtuhumiwa huyo alikuwa ni Ngesa,mtu waliyekuwa wanamsaka kwa muda mrefu sana,wakakoki mitutu yao, tayari kwa kum-miminia risasi.Hata angefanya nini asingeweza kufanya lolote lile,hiyo ilimfanya apige magoti, akaweka bastola yake chini na kuweka mikono yake hewani kusalim amri.Askari walikuwa na usongo naye kwani kazi ya kumsaka Ngesa, iliwafanya wasumbuliwe na kuonekana wazembe katika kazi yao.
Mmoja wa maaskari hao aliyefahamika kwa jina la Kamanda Steve Nanyaka,alimsogelea karibu na kumpiga na kitako cha mtutu kichwani,Ngesa akadondoka chini akiwa ana maumivu makali,hakukaa sawa akapigwa buti la tumbo na kushindiliwa na mguu wa shingo.
******
“Naomba nizungumze na Mkuu wa Mkoa,mwambie ni dharura”
“Yupo kwenye press conference na waandishi wa habari”
“Mwambie ni dharura,simu imetoka Ikulu Rais anahitaji kuzungumza naye”
“Sawa”
Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha bwana Isaya Ponjoro,alikuwa simuni anazungumza na simu kutoka Ikulu.Hapohapo alitoka kidogo mpaka kwa maaskari, ambao walikuwa wanamlinda mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh.Reonald Mlaki.
“Kuna simu imetoka ikulu ni dharura”
“Subiri kidogo”
Mlinzi moja akaitwa pembeni na kupewa kikaratasi kidogo chenye maandishi ambapo hapo,bila kuharibu utaratibu sababu Mkuu wa Mkoa alikuwa hewani na Watanzania wote wanamuona kwenye luninga,akapewa karatasi na kuisoma kwa macho ya kuibia ‘Mkuu Kuna dharura,Rais anahitaji kuongea nawewe’Ujumbe huo ulisomeka juu ya karatasi ndogo, kumaanisha anatakiwa atoke pembeni mara moja.
“Ninachoomba kuwaambia kwamba,wananchi wangu wa Arusha muwe katika hali ya utulivu huohuo.Malalamiko yenu nayasikia sana lakini ningependa,kuwahaidi nitatimiza kila kitu,ahsanteni sana”
Ilibidi afupishe kile alichopanga kuzungumza na waandishi wa habari pamoja na watanzania, akatoka pembeni, ambapo huko alipewa simu,akawa kwenye laini na Mkuu wa nchi, Rais Leslie.
“Mh.Rais”
“Mlaki”
“Naam mkuu”
“Kuna jambo naomba ulifuatilie kwa kina”
“Jambo gani?”
“Mpakani pale,nadhani unaelewa ni jinsi gani sasa hivi nchi inavyoenda.Kifupi nimepata taarifa,Karanje ameingia Tanzania kupitia mpaka wako wa Namanga.Hakikisha kama hizo habari ni ukweli ama ni uvumi”
“Brigedia Karanje?”
“Ndio”
“ Nitakupigia nikipata ripoti kamili”
Hilo halikuwa ombi, ilikuwa ni amri kumaanisha ya kwamba itekelezwe haraka iwezekanavyo,ndiyo maana Rc Mlaki akapiga simu moja kwa moja makao makuu Namanga,akatuma askari wafuatilie kama kuna jina la Brigedia Karanje,haikuwa kazi rahisi kwani jina hilo halikuonekana.Ikabidi watumie njia nyingine mbadala.Uchunguzi ukaanza mara moja,kwa msaada wa CCTV kamera wakagundua kuwa Karanje aliingia na gari ambalo halikukaguliwa.Taarifa hizo zikarudi moja kwa moja kwa RC Reonald Mlaki,kama zilivyo nayeye akamwambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Leslie Benjamin!
“Mungu wangu,Kumbe Ngesa alikuwa sahihi!”
Rais Leslie akaonekana kama mtu,anayejutia kitu.
“Mheshimiwa una maana gani?”
“Tuma askari wako sasa hivi kwenye hotel ya Mount meru uk..”
“Mh Rais”
“Reonald fanya hivyo sasa hivi”
Hivyo ndivyo ilivyokuwa,hapohapo bila kupoteza wakati, RC Reonald Mlaki jioni hiyo alituma askari kwenda kwenye hotel hiyo lakini badala ya kufika,walisikia mirindimo ya risasi. Hapo ilibidi na wao watoe mitutu yao tayari kwa kufanya Ambush,hawakuamini walichokiona baada ya kumuona Ngesa anatoka nje ya hoteli hiyo, akiwa amebeba mtoto mdogo wa kizungu,hapohapo wakamuweka chini ya ulinzi.
“Afande,muweke chini ya ulinzi.Mfunge pingu”
Mdomoni alivuja damu nyingi sana, kutokana na kupigwa na kitako cha mtutu wa bunduki,hapo walimfunga pingu kwa nyuma na kuanza kumpakia nyuma ya Deffenda,mitutu yote ilikuwa kwake na siku hiyo, walikuwa makini kuliko kawaida,historia ya Ngesa waliisikia, ndio maana walijihami kupita kawaida.
“Ukijitingisha kidogo,nakumwagia risasi.Mfunge na pingu miguuni huyu jambazi sugu”
Hakuwa ana ujanja mwingine wowote ule,maaskari walikuwa wengi waandishi wa habari ndio usiseme.Mkuu wa jeshi la polisi Wilaya ya Arumeru kamanda Ernest Chonjo,alikuwa kwenye operesheni hiyo nzito,yeye hakutoka ndani ya Diffenda.Tukio zima aliliona na kumuona Ngesa amekamatwa tayari. Swala hilo aliamini kivyovyote vile lingempa ujiko mkubwa sana,simu yake ikaita alivyoitoa akagundua kwamba anapigiwa na mkuu wa Mkoa,Reonald Mlaki alielewa fika ni lazima alitaka ripoti ya operesheni inavyokwenda,ni kweli alikuwa ni kama ametabiri vile kwani Rc Mlaki alitaka kujua kila kitu.Akaambiwa kuwa ni Ngesa ndiye amefanya vurugu hiyo nzito.
“Umesema ni Ngesa?”
“Ndio”
“Ngoja nimtaarifu Rais Leslie”
“Lakini Mheshimiwa”
“Nakusikiliza”
“Kuna maiti ndani ya Hoteli”
“Maiti?Ina maana Ngesa alivamia na kuwauwa?”
“Itakuwa ni hivyo tu lakini bado tunafanya uchunguzi”
“Subiri,nitakupigia”
Taarifa alizopewa na Mkuu wa jeshi la Polisi akazibeba kama zilivyo na kumtafuta Rais Leslie hewani, taarifa hizo zilionekana kumchanganya sana, Rais Leslie simuni.
“Naomba Ngesa aachiwe huru sasa hivi,nahitaji kuzungumza naye”
“Mheshimiwa Rais ung..”
“Nadhani umenisikia.Nahitaji kuzungumza na Ngesa sasa hivi,mwacheni huru”
Kauli hiyo asingeweza kuipinga hata kidogo sababu ilitoka kwa mkuu wake wa kazi.Amri hiyo kwa njia ya simu, akapewa pia Kamanda Ernest Chonjo,akateremka ndani ya Diffenda na kuwaamuru vijana wake, wamfungue pingu Ngesa.
“Mfungueni pingu zote,Ngesa Rais Leslie anataka kuzungumza nawewe.Shika simu”
Bado akiwa na damu mdomoni na puani,akachukuwa simu na kuiweka sikioni.
“Mh.Rais..”
“Derrick Ngesa,kitu ulichoniambia ni kweli.Tuliweke hili pembeni kwanza, nachokuomba umtafute Brigedia Karanje alipo na watu wote wanaohusika na tukio zima”
Kauli hiyo ilitoka moja kwa moja kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Leslie Benjamin,ni kweli kwamba alihisi kujuta sababu mpaka dakika hiyo, watu sitini na mbili wasiokuwa na hatia walikuwa wamepoteza maisha, ndani ya hoteli ya Mount Meru.
“Sawa,Mheshimiwa. Lakini sitoweza kufanya peke yangu.Nahitaji ushirikiano”
“Usijali,jeshi la polisi litakusaidia nitawaambia pia watu wa usalama wa taifa wakupe ushirikiano”
“Hapana sihitaji jeshi wala usalama wa taifa”
“Unahitaji nini Derrick?”
“Nahitaji watu wawili tu wanisaidie kwenye hii operesheni”
“Nani na nani?”
“DAPHINE na DUSTAN”
“Usijali,nitafanya hivyo”
“Kingine nachohitaji ni silaha za kutosha”
Ngesa aliongea huku akibana meno kwa hasira, kwake ilikuwa ni kama muujiza,hasira zikampanda upya, baada ya sura ya Brigedia Karanje kumjia kichwani.Kitendo cha Rais Leslie kumpa mamlaka hayo ilikuwa ni sawa na chizi kupewa rungu!Kwani kwake,kama picha lilikuwa ndio kwanza linaanza.
Jeshi la polisi,lilifyanta mkia.Hakuna hata mmoja kati ya,o aliyeelewa ni kwanini Mtuhumiwa ama jambazi sugu aliyetokea kutingisha nchi nzima ya Tanzania na nchi nyingine jirani kwa ujumla,kuachiwa huru kizembe namna hiyo.Japokuwa walikuwa wenye usongo na Ngesa lakini iliwabidi watulie tu,hiyo ilitokana na kauli ya mkuu wao wa kazi,ambaye hata yeye alipokea oda kutoka kwa Rais Benjamin Leslie.Maagizo aliyopewa baada ya kupokea ni kumpa ushirikiano Ngesa na si vinginevyo, kwa Ngesa huo ulikuwa ni kama muujiza mkubwa sana kutokea kwani sekunde chache nyuma, alikuwa chini ya ulinzi mkali kumaanisha kwamba, bila raisi kupiga simu wenda hukumu yake ingekuwa kubwa mno!Alichoomba kwa wakati huo ni uokoaji wa wateja waliokuwa ndani ya hotel hiyo ya Mount Meru,jambo hilo lilifanyika haraka iwezekanavyo.Askari wakavaa mitungi ya hewa ya oksijeni na kuzama ndani.Walichokikuta hata wao kiliwaogopesha,kulikuwa na maiti nyingi chini, sakafuni.Huo haukuwa utani, watanzania pamoja na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi walifia humo,kilichofanyika ni kuzima mtungi mkubwa wa gesi ambao ulikuwa na kazi ya kusambaza hewa.Zoezi hilo likafanikiwa lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kuokoa idadi kubwa ya watu,kazi iliyofanyika hapo ni kutoa maiti nje huku waandishi wa habari wakifanya kazi yao ya kupiga picha.Lilikuwa ni tukio lililovuta hisia za watu,zaidi na hapo Tanzania ilitandwa na hofu kubwa sana, sababu fununu zilianza kuzagaa ya kwamba gaidi aliyefanya hivyo, bado hajatiwa mbaroni hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuendelea kuuwa watu.Ni kweli,walikuwa ni kama wametabiri kwani Brigedia Karanje alikuwa ana mpango mwingine kabambe wa kuendelea kuteketeza binadamu wenzake.
“Kazi nzuri sana,lakini imekuwaje askari wamefika mapema namna hiyo?”
Brigedia Karanje alimuuliza mwenzake, aliyekuwa pembeni.Mbele yao kulikuwa na Luninga ndogo ya kichogo,taarifa ya habari ilikuwa ikiruka ‘live’ kutokea moja kwa moja katika hoteli ya Mount Meru,badala ya kusikitika wao tukio hilo lilikuwa kama sherehe kubwa.
“Hata hivyo wamechelewa,ile sumu sio ya mchezo”
Jamaa akajibu,huyo alifahamika kwa jina la General Matola,jicho lake moja lilikuwa bovu yaani chongo!Sura yake ilitisha kidogo na alikuwa ana baka moja kubwa, katikati ya paji lake la uso,katika wanajeshi magaidi General Matola alitisha,katika watu ambao Karanje aliwaamini pia na kuwapa kipaumbele zaidi ni huyu, General Matola, sababu swala la kuuwa kwake, lilikuwa la kawaida na aliwahi kumnyonga mke wake chumbani, baada ya kumfumania na kijana muuza samaki feli,hiyo ilifanya atafutwe ili afungwe lakini badala yake, alimsaka Brigedia Karanje na kuungana naye.Ndani ya chumba hiko kidogo kulikuwa na wanajeshi wengine kumi na tisa, ukitoa Brigedia Karanje.Waliamua kuweka kambi huko Simanjiro wakiwa wanasubiri vijana wao wengine warudi ili mikakati mingine ianze.
“Mitungi mingine iko wapi?”
“Ipo pale pale mkuu”
“Hiyo tunaingia nayo Dar es salaam,kesho asubuhi sana”
“Ikulu je?”
“Ngoja tumalize hili kwanza,kabla ya kumfuata Leslie huko huko Ikulu.Ni lazima alie na kusaga meno”
Hivyo ndivyo ilivyokuwa na pembeni yao, kulikuwa na meza kubwa ambayo juu ilikuwa na ramani ya mchoro wa Ikulu,kumaanisha kwamba siku za usoni ilikuwa ni lazima wavamie na kumteka nyara Rais Leslie,huo ndio ulikuwa mpango wao hatari,nyumba waliokuwepo isingekuwa rahisi hata kidogo kugundulika.Katikati ya msitu ambao ulikuwa na miti mingi sana!Haikuwa rahisi kwa mtu yoyote kufika eneo kama hilo sababu hakukuwa na dalili za binadamu yoyote yule kuishi.
******
Daphine alikuwa yupo makini sana ameshika usukani kwa mikono yake yote miwili,macho yake yapo mbele. Bastola ameikoki, ipo pembeni juu ya kiti cha kushoto.Mbele yake umbali wa kama mita kumi na saba kulikuwa na gari aina ya Mark II Grande,alikuwa akiifuatilia nyumanyuma sababu iliendeshwa na mwanajeshi, ambaye alitoka kumfukuzia ndani ya hoteli ya Mount Meru,hesabu zake zilikuwa ni kujua ni upi mwisho wake.Ndio maana, alimfuata taratibu nyuma nyuma,akijificha ficha.Kwa kuwa ilikuwa ni usiku tayari, mwanajeshi ama kada wa Brigedia Karanje hakuweza kujua kama anafuatiliwa kwa nyuma.Alizidi kusonga mbele zaidi,kwa kutumia mkono mmoja kushika usukani huku mwingine akiutumbukiza ndani ya mfuko wa suruali,akatoa simu na kubonyeza namba fulani fulani,wakati akifanya hivyo alikuwa makini sana, mara aangalie simu, mara mbele ilimradi asipate ajali barabarani.
“Mkuu,tayari”
Kitendo cha upande wa pili wa simu kupokea,akasema maneno hayo.Ilikuwa ni wazi kabisa, alikuwa anampa taarifa mkuu wake wa kazi.
“Safi,nimeona!Uko wapi?”
“Njiani narudi”
“Fanya haraka,kuna kazi nyingine inakusubiri”
“Okay”
Kitendo cha simu kukatika,akakanyaga mafuta mengi na kuzidisha mwendokasi wa gari.Ilikuwa ni safari ndefu kiasi, mpaka kufika Simanjiro!Usiku ulikuwa mnene mno,magari barabarani yalikuwa machache ya kuhesabika,mbele yake kulikuwa na kona ambayo haikuwa na lami.Akakunja na kuingia ndani ndani,ambapo huko akatokeza njia iliyokuwa na miti mingi,ina kimsitu kwa mbali.Hakuishia hapo gari lilizidi kwenda mbele zaidi.Daphine,alikuwa makini nyuma yake, hakumuacha sana,alihakikisha anakula naye sahani moja, mpaka ajuwe ni wapi mwisho wake,alivyoona anazidi kuingia ndani ndani,akatoa simu yake na kumtafuta Dustan hewani.Akamuelezea kila kitu kwa kifupi!
“Nilizungumza na Rais Leslie pamoja na Ngesa wanasema u….”
“Hallooo,Hallooo,Hallooo Dustan..Hallooo”
Kanzia hapo,mtandano haukuwa mzuri tena, simu ilikuwa ikikoroma mithili ya redio inayokaribia kuisha mabetri na mwisho mawasiliano kukatika kabisa kabla ya Daphine kupatana vizuri na Dustan,alivyoangalia simu yake akaona mnara upo chini kabisa, kumaanisha kwamba huko alipo swala la mtandao lilikuwa mtihani sana.Alivyoweka simu mfukoni,akatupa macho yake mbele na kuona kwa mbaali gari aliyokuwa anaifuatilia,imesimama!Hapo hapo nayeye akazima taa za gari na kuliweka kando.Akachukuwa bastola na kuchomoa ‘magazine’ ili kuhakikisha kama ina risasi,alivyoridhika akairudisha.
“Kacha kacha”
Akaikoki na kuiweka nyuma kiunoni,akafunga mlango wa gari taratibu na kuanza kunyata kwa tahadhari kubwa.Mbele yake kulikuwa na giza nene,isipokuwa umbali wa mita kumi mbele yake aliona kijumba kidogo hiyo ni kutokana na mwanga uliokuwa ndani ya kijumba hiko,kilichokuwa katikati ya miti mingi.Akasimama nyuma ya mti ili amchore mwanajeshi ambaye alikuwa anatembea kuelekea njia hiyo,akamuona anaingia ndani ya kijumba.
“Safi,kazi nzuri.Umehakikisha hakuna mtu anayekufuatilia?”
“Ndio mkuu”
“Tutakaa huku mpaka hali kidogo itulie”
“Alafu,Ngesa yupo hai”
Hapo Brigedia Karanje,akaganda kidogo na kukunja sura yake!Habari hizo zikawa zimemshtua, wakati mwingine alihisi kama amesikia vibaya.
“Umesemeje?”
“Ngesa yupo hai”
“Sio kweli,hapa nasubiri kichwa chake”
“Hajafa mimi nimemuona kwa macho yangu”
“Itakuwa umemfananisha”
Brigedia Karanje,alijaribu kupinga hoja hiyo lakini moyoni aliingiwa na wasiwasi, ambao hakutaka kuuonesha waziwazi.
“Ulimuona wapi?”
“Alikuwa na Daphine,Mount Meru Hotel”
“Na Daphine?”
“Ndio Mkuu”
“Unasema ukweli?”
“Sina sababu ya kukudanganya mkuu,nimemuona kwa macho yangu mawili.Siwezi kumfananisha”
Kufuatia hapo,ukimya ukatawala kidogo.Hawakuelewa kwamba Daphine, tayari yupo eneo hilo la karibu na wanavyozungumza alikuwa dirishani anasikia kila kitu.
“Nitajua namna ya kumdhibiti,safari hii nitamtafuta nimuuwe kwa mikono yangu mwenyewe.Hatonisahau yeye na kizazi chake.Nahitaji kuzungumza na Daud Bashonga,anileteee Malaya wa Ngesa.Yule Jaqlin Mfinanga”
Brigedia Karanje,akaibua mkakati mwingine mpya, akimuhitaji mwanamke anayeitwa Jaqlin Mfinanga,alijuwa kivyovyote vile ni lazima Ngesa angeumia na kupata pigo kubwa mno.Wakati hayo yote yanaendelea Daphine alikuwa nje anawahesabu, wapo wangapi ili akiingia apambane nao,aliyemtia hasira zaidi ni Karanje,matukio mengi sana yalipita kichwani mwake,akakumbuka alivyopelekwa Cuba na kupewa mafunzo ya kigaidi akawa kama baba yake mlezi kumbe haikuwa hivyo,Karanje alikuwa ni katili, kuliko binadamu wa kawaida na huyo ndiye aliyewaua wazazi wake,hasira zilimkaba na kuweka bastola yake vizuri tayari kwa kuingia ndani kufanya ambush,ilikuwa ni lazima amuuwe Karanje kwa risasi moja tu ya kichwa.Akasimama vizuri dirishani na kuweka bastola vizuri jichoni kwa niya ya kufyatua risasi, amuuwe Karanje,akabana jicho lake moja sawasawa,kichwa cha Karanje kikawa kimejaa kwenye saiti. Kilichotakiwa ni yeye tu kuvuta kifyatulio cha bastola.Hakuwa mwenye uhakika kama baada ya shambulio hilo, angetoka mahali hapo salama.Akaanza kuhesabu kimoyo moyo,moja mbili tatuu.
“Paaaaaaaaaa”
Risasi ikachomoka,mlio mkubwa ukasikika.
*******
Rais Benjamin Leslie alihisi kujuta sana,laiti angemsikiliza Ngesa tangu awali yasingetokea yanayoendelea, japokuwa alipiga vita waandishi wa habari wasisambaze habari hizo mbaya ambazo aliamini zingemchafulia nchi yake lakini alikuwa tayari amechelewa kwani tukio hilo lilisambaa kwa kasi ya moshi wa kifuu,nchi jirani kama Kenya,Uganda na Rwanda.Taarifa hizo zikaenea mpaka Mashariki ya mbali.Rais Leslie akahisi kuchanganyikiwa,kazi yake ilikuwa ni kuzunguka huku na kule, akimpigia Ngesa kila wakati ili ajuwe ni wapi amefikia.
“Mh.Rais kama nilivyokwambia,nahitaji kuzungumza na Makamu wa Rais Cosmas Ngailo,anajua ni wapi Karanje alipo.Nachokuomba,wazuie waandishi wa habari kusema kwamba yupo chini ya Ulinzi”
“Sawa Ngesa nakusikiliza.Umefika wapi?”
“Ndio nimeshushwa na Helkopta,naelekea Kimara!Kitu kingine,operesheni yoyote nayoifanya,iwe siri”
“Usijali”
Siku hiyo Ngesa aligeuka na kuwa kama mshauri wa Rais vile, sababu alisikilizwa kuliko kawaida,haikuwa utani mategemeo yote na imani yake kwa ujumla ikaegemea kwa Ngesa,hakuwa na mtu mwingine yoyote Yule ambaye alidhani angemsaidia kwenye sakata hilo zito.
“Ahsante Ngesa”
“Nashukuru Mheshimiwa Rais”
Kila kitu kilikuwa wazi na Makamu wa Rais alikuwa chini ya ulinzi mkali, akihojiwa maswali,operesheni hiyo nzima aliisimamia Dustan ama DK!Maelezo, aliyopewa ni kwamba amsubiri Ngesa angefika yupo njiani,masaa mengi yalipita bila ya Cosmas kuonesha ushirikiano wowote ule.Dustan alitumia kila njia kumuhoji lakini hakuweza kuambulia chochote,ndani ya chumba hicho kidogo.
“Mh Cosmas.Karanje yuko wapi?”
Dustan,akarudia swali hilohilo zaidi ya mara ishirini.
“Nim..eshakwa..mbia kil..a kitu”
“Hapana nahitaji kujua alipo kwa sasa hivi,naelewa unanificha”
“Si..jui”
Kwa Dustan,habari za Ngesa, sambamba na kupewa jukumu na Rais Leslie la kumsaka Karanje alilijua,ndiyo maana alimuhoji Mh.Ngailo kwa kiburi sababu tayari alikuwa amekabidhiwa rungu na ana mamlaka ya kila kitu,wakati akiwa anamuhoji Mh.Cosmas Ngailo,mlango ukafunguliwa.
“Umefikia wapi?”
Alikuwa ni Ngesa,bila salamu.Akaibuka na swali!
“Bado hajataja ni wapi alipo”
“Niachie mimi”
Ngesa alizungumza,hakuwa mwenye punje ya masihara hata kidogo.Akamtizama Ngailo kwa jicho kali na kumsogelea karibu zaidi.
“Mpaka sasa hivi kuna maiti themanini na saba,wakiwemo watoto wadogo na watanzania wenzako vilevile.Wote wamekufa,sababu yako wewe na mpuuzi mwenzako Karanje.Ukitoka hapa nadhani unajua hukumu gani inakuhusu,kifungo cha maisha ama kunyongwa.Ungependa kufa na madhambi yote hayo?Jibu ni hapana,nachotaka kujua ni wapi Karanje alipo ama ni kwa njia gani naweza kumpata”
Maneno ama maelezo aliyokuwa anatoa Ngesa yalimfanya Mh.Ngailo atafakari kwa Muda kidogo,hata hivyo alishikwa na wasiwasi alielewa nini maana ya mwanaume huyo kukaa mbele yake,ndiyo maana alitafakari mara mbilimbili.
“Mimi sio mtu wa maneno mengi,nadhani unaijua historia yangu.Nakuuliza tena kwa mara ya mwisho,Karanje yuko wapi?”
“Kusema ukweli sijui alipo”
“Usinijaribu”
“Huo ndio ukweli”
“Sawa,wacha tuone”
Ngesa akajibu,akatembea kidogo mpaka kando kando, ambapo kulikuwa na kamba ndogo aina ya manila,akaichukuwa na kumvisha nayo shingoni kama mbuzi anayepelekwa malishoni.Kufuatia hapo,akanyanyua mfuko wa nailoni,akamvisha nao usoni.Kumaanisha kwamba ndani ya sekunde kumi Mh.Ngailo, atakosa hewa safi ya Oxygen.
******
Sijui ni Mungu ama mizimu ya kwao,kitendo cha kusimama ili kupokea simu iliyoanza kuita, risasi ilimpitia kisogoni ikamkosa kosa,ikampata Mwanajeshi aliyekuwa kando yake.Hiyo ndiyo ilikuwa ponea ya Karanje, simu ikawa imeokoa maisha yake,kifupi aliponea kwenye tundu la Sindano!Daphine akawa ameshindwa kumuua.
“Shiiit”
Akakema na kuanza kuzunguka kwa nyuma sababu wanajeshi waliokuwa ndani,walianza kurusha risasi, hovyohovyo kuelekea nje.Daphine alivyoona hivyo,akalala chini na kuanza kujiburuza kama nyoka.
“Paaa! Paaaaa!”
Nayeye hakuwa nyuma nyuma,akaanza kurusha risasi akijibu mapigo!Kutokana na utaalam wake,akafanikiwa kuwadondosha wanajeshi wawili.Hiyo ilizidi kuwatia mori wanajeshi hao,ambao walizidi kupata usongo wa kumjua ni nani anafanya hivyo,mawazo yao yaliwatuma ni lazima anayefanya hivyo ni askari na tayari walivamiwa.Hiyo iliwapelekea,wamimine risasi nyingi nyuma ya jiwe kubwa ambapo hapo risasi ndipo zilikuwa zinatoka.
“Tonny”
Mwanajeshi mmoja aliyeshika mtutu, alimuita mwenzake na kumpa ishara,azunguke upande wa pili.Ambapo hapo, Daphine alikuwa amejificha,aliamini angetokeza tu angemiminiwa risasi nyingi mwilini,ndiyo maana akatulia.Kazi yake ilikuwa ni kuchungulia na kujibu mapigo.
“Paaa! Paaa!gegege gegege gegeee”
Milio ya bastola pamoja na mitutu ilirindima,wanajeshi wanarusha risasi, Daphine anawajibu.
“Karakacha karakacha”
Sauti ya bastola ya Daphine ilisikika kumaanisha risasi ndani ya chemba zimeisha tayari,hapo alijua tayari kihama chake kimefika.Hakukaa hata sekunde nyingi,akahisi kuna kichuma kimemgusa kichwani.
“Simama”
Ilikuwa ni sauti nzito yenye kutisha,mwanajeshi mrefu kwenda hewani alikuwa ameshika mtutu.Daphine alifikiria kufanya mbwembwe,akaona kuna lundo lingine la wanajeshi,wakamvuta na kumuweka mateka,wao wakiwa nyuma wakamuingiza mpaka ndani.Ambapo huko alikutana macho kwa macho na mbaya wake, Brigedia Karanje,mwanaume anayemchukia kuliko wote duniani.
“Daphine!”
Karanje akaita kwa mshangao,akasimama juu wima na kumsogelea karibu zaidi.Bila kuuliza chochote,akamzaba kibao cha nguvu, kilichomfanya Daphine ayumbe kidogo!
“Mpumbavu mmoja,usiye na akili hata kidogo”
Kitendo cha kumalizia sentensi hiyo,akamzaba tena kibao kikali.Kilichomfanya Daphine aende chini mzima mzima!Karanje alikuwa mwenye hasira kupindukia,hasa alivyoangalia chini na kuona maiti za wanajeshi wenzake watatu,hawakuelewa hata Daphine nayeye ana hasira za mbogo,picha ya wazazi wake kuuwawa, ndiyo ilijijenga kichwani,ikaleta taswira ndani ya ubongo wake,akawa kama anatizama filamu ya kusisimua tena ya kutisha akamtizama Karanje na kubana meno yake kwa hasira.
“Wazazi wangu walikukosea nini?”
Daphine akauliza.Hakuelewa kwamba, hata Karanje pia hadithi hiyo ilikuwa mpya!
“Unaongelea nini?James...”
“Naam mkuu”
“Mfungie stoo,hakikisha hatoki”
“Sawa mkuu”
Hapo hapo,Karanje akatoka nje na kutafuta simu yake maalum ambapo,alimtafuta Daud Bashonga hewani ili ampashe habari,akitaka kumwambia kwamba kuna gesi nyingine ya sumu wanahitaji kuitegesha Dar es salaam.Haikuchukua hata dakika tano,wakawa kwenye laini.
“Dar es salaam sehemu gani?”
“Nitakwambia,natafuta mkusanyiko wa watu wengi kwanza”
“Hakuna shida,nitasimamia zoezi zima.Alafu kuna habari nataka kukupa”
“Habari gani?”
“Ngesa amekamatwa lakini Rais amemwambia akutafute”
“Una maana gani?”
“Nina maana ya kwamba,Ngesa amepewa jukumu la kukusaka.Sasa chunga,ufanye haraka.Mambo yakibumbuluka,nitaozea jela.Fanya haraka umalize hilo zoezi”
“Hakuna shaka,nitajua cha kufanya.Mke wa Ngesa,bado yupo ikulu?”
“Ndio”
“Fanya unachojua,uwe naye.Namuhitaji mke wake”
“Kivipi?Mbona unanipa kazi ngumu”
“Kama hutaki kufungwa namuhitaji mke wa Ngesa”
“Ina maana nimteke?”
“Ndio,fanya unavyojua.Rais anakusikiliza sana,tumia nafasi hiyo”
Hapo Daud Bashonga,akashusha pumzi ndefu kidogo.Ilikuwa ni katikati ya usiku na alizungumza seblen akiwa amejificha kandokando ya ukuta.Hakuelewa ya kwamba kila kitu anachozungumza mkewe anamsikia,yupo pembeni akitaka kujua mumewe,anazungumza na mchepuko gani.Habari alizosikia zilimuogopesha hata yeye,hakutaka kuamini hata kidogo ya kwamba, mumewe ni katili namna hiyo,isitoshe anashirikiana na Brigedia Karanje!
“Sawa,nitafanya utaratibu wote.Niachie mimi,nitazungumza na Dokta Mlope.Ndiye anayesimamia matibabu yake.Andaa vijana wako,waweke standby”
“Vijana wangu,muda wote wapo kazini.Ukiwa tayari niambie”
“Kesho mchana,kila kitu kitakuwa shwari”
“Hakuna shaka”
Mke wake aliyefahamika kwa jina la Ashura Bumarwa,akawa amesikia kila kitu.Moyo wake,ulipiga kwa nguvu jasho jembamba lilimtoka,hofu ilimtanda.Hakujua ni kitu gani akifanye sababu miguu yake ilikufa ganzi ghafla,akahisi kama anashindwa kutembea!Angekuwa mwenye dhambi kubwa sana kama jambo hilo asingelifikisha Kwa Rais Leslie,hapohapo akaanza kunyata na kukimbia kuelekea chumbani ili ampigie simu Rais Leslie usiku huo huo,ukaribu wa mumewe na Rais Leslie ulifanya hata yeye ajenge naye urafiki.Kwa haraka,akakwapua simu na kuanza kubonyeza namba fulanifulani,akaiweka simu sikioni, ambapo ilianza kuita lakini haikupokelewa.
*******
Suruali ya Mh Cosmas Ngailo,ilikuwa imelowana mkojo!Mateso aliyokuwa anapata kutoka Kwa Ngesa,hayakuwa ya kawaida hata kidogo!Vidole vyake,kimoja baada ya kingine kilikuwa kinaingizwa pini iliyochongoka mbele,hususani chini ya kucha.
“Karanje yuko wapiiiii?”
Kidole cha tatu kilikuwa kimeshikwa,Ngesa ameshika pini tayari kwa kuingiza chini ya kucha endapo Mh.Ngailo akisema ‘Sijui’.
“Yu..pooo Arushaaaa”
“Arusha kubwa,ongea alipo.Kabla sijaingiza pini nyingine na safari hii,naingiza kwenye kibofu chako cha mkojo”
“Sijui kwa kweli,mambo meng,…i anajua Daud Basho..nga”
“Naniiiii?”
Dustan,akauliza kwa mshangao.Jina hilo,lilifanya mapigo yake ya moyo yapige kwa nguvu.Alishtuka sababu hakutaka kuamini kama pia, RC Bashonga yupo kwenye sakata hilo.Hata Ngesa nayeye,aliishiwa nguvu,akajua kivyovyote vile, mtandao huo ni mkubwa kuliko alivyodhani, akazidi kupandwa na hasira za ajabu,kumaanisha kwamba ni lazima Daud Bashonga afuatwe pia, ikiwezekana aminywe ili aseme ni wapi Gaidi Karanje alipo.Huo,ndio ulikuwa mpango wa Ngesa kwa muda huo,ikiwezekana hata usiku huohuo,amuibukie.
Zilikuwa ni taarifa mbaya za kutisha,Watanzania waliogopa kupita kiasi.Boda zote zilifungwa, hakukuwa na mtu yoyote aliyeruhusiwa kutoka nje ya Tanzania ama kuingia nchini humo.Hali ilikuwa ni mbaya mno!Licha ya magazeti kuzuiwa na serikali kupiga marufuku kuchapa habari hizo za sumu kali iliyouwa watu lakini ilishindikana kwani kulikuwa na mitandao ya kijamii,picha zilirushwa Facebook na WatsApp,maiti zilitisha kwa kiasi cha kutosha!Ilikuwa ni picha mbaya katika sura ya Tanzania,tukio hilo liliibua simanzi kubwa na hofu kumtanda kila mtu.Mbaya zaidi,Rais Leslie bado hakuongea chochote kile, hiyo iliwafanya watanzania washindwe kuelewa,hatimaye minong’ono ya chini kwa chini ikaanza.
Vyama pinzani,vikaanza kupiga kelele ya kwamba serikali iliyoko madarakani,imekaa kimya kwani jambo hilo lilikuwa ni zito mno!Hapo ndipo kila mmoja akazinduka,wakaanza kushika mabango na kutembea barabarani.Kwa mara ya kwanza,ilikuwa kama mzaha lakini hali ilikuwa mbaya,raia wenye hasira chafu walichoma maduka na kuanza kutembea barabarani, wakiandamana.Mbaya zaidi walimtaka Rais Leslie,aachie ngazi.Polisi wakapata kazi ya ziada, walivyojaribu kutuliza gasia kwa kupiga mabomu ya machozi walipigwa mawe na kuumizwa.
“Mkuu,fujo imekuwa kubwa sana.Maduka yanachomwa moto.Tufanye nini?”
Simu hiyo ilikuwa imepigwa moja kwa moja ikulu na IGP Nassoro Kazimoto,hata yeye hali ilimtisha kupita kiasi,barabara karibia zote zilifungwa, watu wakiwa na mabango mikononi mwao!Fujo hizo hazikuwahi kutokea katika nchi ya Tanzania, iliyosifika kwa amani na upole.
“Jaribuni kuwatuliza”
“Kwa kufanya nini?”
“Kupiga mabomu ya machozi”
“Imeshindikana”
“Pigeni risasi hewani mkiona haitoshi,mwageni maji ya pilipili”
Magari makubwa yaliyobeba maji ya pilipili yalikuwa katikati ya barabara ya Morogoro road,yameziba njia.Askari wapo juu ya magari, wameshika mitutu mikononi mwao pamoja na mabomu ya machozi.Hali ilikuwa ni mbaya sana,mkusanyiko wa watu ulikuwa ni mkubwa mno!Wakipiga kelele kutaka Rais Leslie ang’oke mara moja, madarakani.
‘TUNATAKA HAKI NA DEMOKRASIA ITENDEKE,KILA SIKU WATANZANIA WANAKUFA HAKUNA HATUA YOYOTE’
‘RAIS LESLIE,TOKA.TUMECHOKA SANA NA SERA ZAKO’
Kilitowatia chachu zaidi ni kitendo cha Ngesa kukamatwa kisha kuachiliwa huru bila kuambiwa sababu ya msingi,walivyokumbuka mabomu yaliyouwa watu Uwanja wa kimataifa Mwalimu Nyerere, walipandisha Mori zaidi.Kifupi kila kitu kilikuwa kimevurugika hakukuwa na amani tena,hiyo ilimfanya Rais Leslie, akione kiti chake ni cha moto sana,akahisi kujuta.Aliyekuwa akimpa moyo siku zote ni mkewe tu.
“Leslie,usiwe na mawazo.Wewe ni mwanaume,simama imara.Wewe ni kama Simba, msituni.Ongea na wananchi wako,usiwaogope”
Rais Leslie, alionekana kukata tamaa kabisa mategemeo yake yote yakawa kwa mkewe akawa kama mwanga kwake,akimfariji.
“Nataka kujiuzuru,kujivua urais”
“Hapana Mme wangu,usifanye hivyo.Tuliza akili!Ngesa amefikia wapi?Ushawasiliana naye?”
“Hapatikani”
“Dustan?”
“Pia hapatikani”
“Hata Daphine?”
“Wote hao”
Mbali na vitu nyeti vinavyoendelea nchini lakini Mke wa Rais, alivijua.Rais Leslie,hakumficha mkewe kitu chochote kile,hata hivyo alimchukulia kama mshauri wake namba moja!Wakati vurugu zinaendelea kupamba moto, Ngesa alikuwa njiani kuelekea mkoani Arusha ili akamvamie Brigedia Karanje, swala la Bashonga,akaliacha mikononi mwa Dustan,alifuatilie akiamini kabisa kwa kugawana huko, ingekuwa rahisi kuuwa ndege wawili kwa wakati mmoja.
Ubize aliokuwa nao Rais Leslie,ulimfanya Rc Bashonga achukuwe jukumu la kutuliza gasia ya wananchi wa mkoani kwake Dar es salaam,hapo ndipo alitumia mwanya huo pia kumtorosha Jaqlin Mfinanga Ikulu,bila ya mtu yoyote yule kujua.Ilikuwa ni lazima mwanamke huyo afikishwe mikononi mwa Brigedia Karanje,jambo hilo likafanikiwa kwani usiku wa saa saba, Daud Bashonga alikuwa amejificha maeneno ya Uwanja wa Ufi,anasubiri maelezo mengine za ziada.
“Kuna gari litakuja hapo”
“Saa ngapi,Karanje?Waambie wafanye haraka”
“Wapo njiani wanakuja,atapakiwa kwenye ndege ndogo afike leoleo huku”
“Nawasubiri”
Hakukaa sana eneo hilo,Marced Benzi nyeusi ikawa imefika eneo hilo,watu watatu wakateremka na kujielezea.Jaqlin Mfinanga akiwa hajielewi, amechomwa sindano ya usingizi,akaingizwa ndani ya gari hilo la watu wasiojulikana,hakukuwa na maongezi mengine ya ziada.
Gari ikaondoka hapohapo kwa kasi ya ajabu!
*******
Mateso ya ajabu,ambayo mengine hayakuwahi kutumiwa na mtu yoyote Yule yalimfanya Makamu wa Rais,Mh Cosmas Ngailo.Azungumze kila kitu kwa Ngesa,akataja ni wapi Brigedia Karanje alipo na angempata kiurahisi,akataja siri nyingine nyeti kwamba ana mtoto wa kike yupo nchini Uganda,anasoma chuo kikuu cha Makerere lakini analindwa na makomandoo ambao muda wote wanavalia nguo za kiraia.Hilo, halikuwa swala la Msingi kwa Ngesa,alichotaka yeye ni kumuweka Brigedia Karanje mikononi mwake ili gasia zipungue,hata yeye alisikitishwa sana na maandamano yanayoendelea jijini Dar es salaam.Kumuweka Brigedia Karanje mikononi mwa Sheria, ndilo lingekuwa suluisho la tatizo hilo.Ndio maana alifika Simanjiro usiku wa saa tano,akaingia mpaka msituni akitumia gari aina ya Landcruser mkonge,operesheni hiyo ilifanyika kimya kimya,hakuna askari hata mmoja aliyeshirikishwa kwenye operesheni hiyo kali.Ngesa akazidi kusonga mbele zaidi,akifuatisha barabara ya vumbi iliyokuwa na milima na mabonde,pembeni yake kulikuwa na miti mingi na vichaka vikali,hata hivyo hakuogopa sana sababu pembeni yake kulikuwa na begi lililojaa silaha za moto pamoja na vitendea kazi vyote!Alivyotembeza gari kwa umbali wa kama kilomita ishirini,akaona kuna gari limepaki pembeni.
Hilo lilikuwa ni gari alilotumia Daphine,kumfuatilia gaidi aliyekuwa ametega mabomu ya sumu katika hotel ya Mount Meru.Alichofanya ni kuliegesha gari pembeni kabisa ya miti ili lisionekane kirahisi,akazima taa na kubeba begi lake dogo lenye mkanda mmoja,akalivaa begani.Akachomoa bastola iliyokuwa kiuoni mwake na kuangalia magazine,alivyokagua na kukuta kuna risasi za kutosha, akarudisha na kuikoki.Akavuta begi kwa mbele na kuchomoa kisu,ambacho alikichomeka kwenye kiatu chake kirefu aina ya Travota,akakamata bastola vizuri na kuanza kusonga mbele,kwa mbali aliona kijumba kidogo, ndani kilikuwa kina waka taa,nje kuna mwanaume mrefu kwenda hewani,akafungua begi na kutoa darubini yenye lenzi kali,akaiweka machoni ili kuangalia vizuri.Kwa ndani aliona vivuli vya watu vinapita pita,niya yake ilikuwa ni kujua ataingiaje ndani ya kijumba hiko.
Alielewa fika ya kwamba kitendo cha kuingia kichwa kichwa, angekufa kiboya.Ndio maana alijihami,akaanza kutembea taratibu mpaka nyuma ya mti mkubwa ambapo hapo,alijificha na kuangalia tena!Kwa tahadhari kubwa,akalala chini na kuanza kutambaa kama komando vitani.Kuna gogo la mti lilikuwa mbele yake,akalishika vizuri.Na kulirusha kwa mbele,hiyo ilifanya mwanaume mwenye mtutu analinda,kutizama huku na kule.Akaangalia vizuri na kushika mtutu wake kwa nguvu kwani kishindo cha gogo hilo kilimtisha.
*******
Mikono yake ilikuwa juu hewani,damu zinamvuja mdomoni kutokana na kusulubishwa vya kutosha,miguu yake inaning’inia kama nyama buchani.Ungemuangalia Karibu, usingeweza kutambua kama huyo ni Daphine,ilikuwa ni vigumu sababu uso wake ulivimba kwa kupigwa na vitako vya bastola.
“Nani mwingine anajua?”
Lilikuwa ni swali kutoka kwa General Kitwana,mwanajeshi huyu alikuwa gaidi kuliko kawaida na huyo ndiye waliyemtumia kumsulubisha Daphine.Brigedia Karanje alikuwa ameketi,anamtizama kwa hasira za waziwazi.Hakutegemea hata siku moja kama Daphine, mwanamke aliyemtegemea angemsaliti.Hapohapo akasimama na kumsogelea!Akamtandika ngumi kali ya tumbo,hiyo ilimfanya Daphine ajikunje akiugulia maumivu hayo makali ya tumbo.
“Mpuuzi mmoja,asiye na akili hata kidogo.Nini kilikupata?”
Brigedia Karanje,alizungumza huku hasira zikiwa zimemkaba kohoni,anamtizama Daphine kwa chuki kali sana.
“Chagua kimoja,nikuuwe ama uungane namimi?”
Hasira alizokuwa nazo Daphine hazikuwa na kipimo chake,hiyo ilifanya mpaka ashindwe kujibu chochote, akabaki anamtizama Karanje.Wakati hayo yote yanaendelea, Ngesa alikuwa nje, anajitahidi kusogea karibu ili ajue kinachoendelea,akafanikiwa kusogea karibu zaidi na kujificha nyuma ya jiwe kubwa,hapo alisikia sauti ya Karanje inazungumza kwa kufoka,akashika bastola yake vizuri.Alivyotaka kusimama,akasikia muungurumo wa gari na taa zinamulika kutokea upande wa Kaskazini,akatulia kidogo ili kuliangalia vizuri.Akaliona limefika mpaka nje ya kijumba hiko likasimama.Milango ikafunguliwa,sauti ya mwanamke aliyoisikia,ilimfanya ashtuke kidogo sababu aliifananisha licha na hayo,hakutaka kulipa wazo lake kipaumbele!
“Niacheni,mnanipeleka wapi?Niacheni nimesema”
Moyo wa Ngesa ukapiga paa!Alikuwa ni Mpenzi wake anayempenda kuliko kitu chochote kile chini ya jua,Jaqlin Mfinanga,ameshikiliwa na watu wawili wanamvuta huku na kule akatafakari imekuaje wakati alikuwa ikulu akilindwa,kilichomtia hasira ni baada ya kushuhudia anapigwa kofi kali.
“Shiiiiiit”
Akakema kwa hasira na kubana meno yake,alivyotaka kujitokeza akili yake ikampiga stop,kwani kwa kufanya hivyo angekosa vyote na kuuwawa.Akatulia kidogo kwanza na kumuona anaingizwa ndani,akaangalia huku na kule na kutembea kwa kujihami,akiangalia pande zote.Akafika mpaka dirishani,alichokiona kilimshangaza zaidi!
Alimuona Daphine,amelowa damu usoni ametundikwa juujuu.Akachungulia vizuri na kusogea dirisha la pili, akiamini akisimama hapo, itakuwa rahisi kwa Daphine kumuona,ilikuwa ni kama ametabiri vile kwani macho yake na Daphine yaligongana,Daphine akapata nguvu mpya!
“Mkalishe hapo.Wewe kahaba,unanifahamu mimi?Yote haya,ametaka Ngesa bwana ako,anayekugonga.Kwa ajili yake,utaenda kufa”
Brigedia Karanje,alizungumza kwa hasira huku akimtizama Jaqlin Mfinanga aliyekuwa mbele yake,ameshikiliwa na watu wawili.Haukuwa utani,Jaqlin alitetemeka kwa kiasi cha kutosha, mbele yake alisimama mwanaume mrefu mweusi,mwenye sura ya kutisha.
“Kifo chako,kitakuwa cha kutisha sana!Nakuonea huruma”
Yalikuwa ni maneno ya kuogopesha mno,Ngesa alikuwa nje dirishani anasikia kila kitu.Akavuta begi lake na kutoa kitu kama kiazi.Akamuangalia Daphine na kumpa ishara ya kwamba akae tayari,lolote linaweza kutokea kuanzia muda huo!Akatembea kama paka shume kwa kunyata,akasimama mlangoni na kuchomoa kisu chake kilichokuwa mguuni,akaweka bastola kiunoni,akasubiri hapo kidogo.Mlinzi mmoja alivyotoka,akamvuta na kutumbukiza kisu kifuani mwake upande wa kushoto, niya yake ikiwa kutoboa moyo,hilo likafanikiwa.Akamziba mdomo kwa nguvu akamvuta na kutulia tena pembeni,akimuacha mwanajeshi huyo anaghalaghala na kutupa miguu,hapohapo akakata kauli.
“Naitiii alasi alasiiii,naitii alasii alasiiiii”
Maneno hayo yalimtoka Daphine,akizungumza vitu visivyoeleweka.Alifanya hivyo kwa mahesabu makali.
“Unasema nini?Ongea kwa sauti”
Jamaa hilo likauliza kwa sauti huku akimtizama Daphine.
“Naitii,alasiii alasiiii”
Hakuna siku aliyojichanganya mwanajeshi huyu kama kusogeza sikio lake karibu ili amsikilize,hapo Daphine hakufanya makosa.Akapanua mdomo wake na kumng’ata sikio, alihakikisha hafanyi makosa,alinga’ng’ania sikio mpaka meno yake yakagusana.Mwanajeshi alipiga kelele za nguvu,hiyo ilifanya wenzake wasogee karibu na Daphine,hapo ndipo Ngesa alipoingia na kumimina risasi.
“Paaa! Paaa! Paaa! Paaa! Paaaa!”
Kila risasi iliondoka na mwanajeshi mmoja,Ngesa hakuishia hapo.Akarusha bomu lililofanana na kiazi upande wa pili ambapo kulitokea mlipuko mkubwa na kuwatupa wanajeshi mbali,Daphine hakutaka kutulia.Akawa ana kibarua cha kujifungua kamba,Ngesa akakimbia kwa kasi mpaka kwa Jaqlin Mfinanga,akamvuta na kumlaza nyuma ya kochi.
“Usipige kelele,nisubiri hapa”
Alivyosema hayo,akaibuka na kuanza kufyatua risasi.Kila kitu kikawa kimeharibika,mirindimo ya risasi ndiyo iliyosikika.Alivyogeuka nyuma kwa ghafla,akapigwa ngumi kali,alivyotaka kukaa sawa,akatulizwa na teke la kifua.
Akayumba na kurudi nyuma,akagundua mwanaume huyo alikuwa Brigedia Karanje,hakukaa sawa.Akapigwa kifuti cha tumbo,Brigedia Karanje alivyotaka kumfuata amshindilie,sijui Daphine alitokea wapi.Akaruka mateke aina ya ‘Round kick’ yakamfikia Brigedia Karanje usoni,akayumba. Hakukaa sawa.Akapigwa tena ngumi tatu za haraka mbavuni,Daphine akawa kama chui aliyejeruhiwa na mkuki,huo ndio ulikuwa wakati wake sasa.Ndio maana alipambana kwa hasira,akamvuta Brigedia Karanje huku akiendelea kumshindilia ngumi nyingi za mbavu na chembe.Ngesa,akasimama kwa kasi, hapo ndipo walipoanza kumshambulia Brigedia Karanje kama mpira wa kona!
Ngumi ukichanganya na mateke aliyokuwa anachangiwa na Daphine pamoja na Ngesa,zilimfanya Karanje ayumbe na kurudi kinyume nyume kama gari,kila alipojaribu kukinga mikono yake kuzipangua, alishindwa kwani alivyokinga mbavu ili Daphine asiendelee kumsurubu huku Ngesa alimshambulia ngumi za chembe.Hiyo ilimfanya arudi nyuma kidogo na kupanda juu ya meza,akarusha teke Ngesa aliliona,akainama kidogo na kumkata ngwala,Brigedia Karanje akadondoka chini kama mzigo puu,Daphine akasogea na kumkanyaga tumboni.Alivyojaribu kujigusa,akapigwa shuti kali na Ngesa aliyekuwa mwenye hasira chafu,hakuna hata mmoja kati yao siku hiyo aliyetaka kufanya makosa,sio Ngesa wala Daphine kila mtu alikuwa mwenye usongo tena kapandisha mori, ndiyo maana walimshambulia kama mpira wa kona hiyo ilimfanya Karanje azidiwe lakini hata hivyo hakutaka kukubali kirahisi,akajibiringisha kwa nyuma na kuukamata mguu wa Daphine,alivyotaka kuuvuta akawa amechelewa kwani Ngesa,alimshindilia teke kali la tumbo.Siku hiyo hali ilikuwa ngumu sana na kulikuwa kuna kina dalili ya yeye kuzidiwa nguvu na kuwekwa chini ya ulinzi, hiyo ilimaanisha yeye kunyongwa na kuuliwa na serikali ya Tanzania, kutokana na matukio mbalimbali ya kinyama aliyoyafanya.Alivyokumbuka hilo akajitutumua kwa mara nyingine.Alivyotaka kusimama akatulizwa na kifuti cha mgongo, huyu alikuwa Daphine,akamrukia shingoni na kuanza kumkaba kwa nguvu za kutosha.Hapo ndipo Brigedia Karanje,alipopata akili mpya,akarudi nyuma kwa kasi mpaka kwenye ukuta, ambapo hapo alimbamiza Daphine kichwani.Ngesa,akafika kwa kasi,alivyorusha ngumi ikadakwa,akatupa mateke mawili kwa haraka, akaongezwa jingine la kifua,akadondoka chali kando.Brigedia Karanje akageuka,akawa kama amepata nguvu mpya vile,akarusha ngumi ili imfikie Daphine lakini ilipita hewani, baada ya Daphine kuinama.Sio siri,lilikuwa ni pambano kubwa na zito la kutisha,hakukuwa na kitu kilichokuwa rahisi hata kidogo.Ngumi zilirushwa sio masihara,hakuna siku iliyokuwa ngumu kwa Karanje kama hiyo,Ngesa na Daphine walimvuruga kwa kiasi cha kutosha,nyumba ilikuwa ndogo kwake. Ki ukweli, alitamani kukimbia lakini hakuwa mwenye uwezo huo,hata hivyo alijitahidi kuona ngumi na mateke yaliyokuwa yanarushwa.Mateke aina ya ‘Round kick’ aliyokuwa anarusha Daphine, yalimfanya arudi nyuma huku akiyakwepa,bila kuangalia nyuma.
Ngesa nayeye alikuwa mwenye usongo,akakanyaga kochi na kuruka sambasoti hewani,akatua kwa teke juu ya kifua cha Karanje.Hapohapo akaenda chini mzima mzima.Wakati hayo yanaendelea, Jaqlin Mfinanga alishuhudia,kwake yeye ilikuwa kama sinema ya kusisimua aliogopa mno,mpambano huo ulimuogopesha na alikuwa mwenye hofu muda wote nyuma ya kochi amejikunyata,katika kuangalia kwake umbali wa mita kumi kushoto kwake, kulikuwa na bastola,moyo wake ukapiga kwa nguvu bila kujua ni kitu gani akifanye.Ni kweli alishawahi kuiona bastola lakini hakuwahi kuitumia,ndiyo maana alitetemeka sababu nafsi yake ilimtuma aichukuwe na kuitumia mara moja!Kwa hofu na mashaka,akaanza kutambaa chini kwa chini,bahati nzuri ikawa kwake akaishika vizuri huku akiwa mwenye hofu kubwa sana!Hata alivyoishika mkononi ungemuangalia ungepata jibu kabisa, hakuwa mzoefu kwani alitetemeka kama mtu mwenye homa kali ya usiku huku jasho likimtoka,kilichomfanya abanwe na hasira ni baada ya kumkumbuka Daphine,mwanamke aliyempiga risasi na kumfanya akae hospitali kwa kipindi kirefu.Huyo ndiye alitaka kumlenga na kumpiga risasi bila kujali yupo upande wa Ngesa,ndiyo maana aliikamata bastola vizuri na kuilenga usawa wa Daphine,aliyekuwa mbele yake!Akiwa katika hali ya kutetemeka kwa hasira iliyochanganyika na uwoga,akawa anavuta kifyatulio cha bastola,hiko alikifahamu sababu aliona sinema mbalimbali za kijasusi,ilikuwa ni lazima siku hiyo amuuwe Daphine ili alipize kisasi.
“Paaaaaaaaa!”
Mlio mkubwa wa bastola,ulisikika.Baada ya Jaqlin Mfinanga kuvuta triga risasi ikachomoka kwa kasi ya kimondo na kupita kandokando ya mgongo wa Daphine,isingekuwa kumrushia ngumi Karanje na kuhama upande basi risasi hiyo ingepenya mgongoni mwa Daphine na kutokeza upande wa tumboni,hiyo ingemaaanisha kifo chake.Kufuatia mlio huo wote wakaganda kama walivyo, wakataka kujua ni nani kafyatua bastola,Ngesa alipigwa na bumbuazi.Hiyo ni baada ya kumuona, Jaqlin kashika bastola,mbaya zaidi kamuelekezea Daphine.
“Jaqlin tafadhali,weka bastola chini”
“No...Nge….sa siwezi kufanya hivyo.lazima nimuuwe !Hujui ame..nifanya nini?”
Jaqlin alizungumza kwa kwikwi akilia huku akitetemeka, hakuwa ana uhakika na kitu anachotaka kukifanya kwa wakati huo ingawa alidhamiria kumuuwa Daphine, aliyekuwa mbele,picha mbaya ya yeye kupigwa risasi na kufanyiwa unyawa ilimjia kichwani,akalia kwa uchungu.Alivyomwangalia Ngesa akaumia zaidi,haikuwezekana hata kidogo awe bega kwa bega na muuaji, katili.
“Jaqlin,nakuomba tutaongea kuhusu hili”
Wakati Ngesa akizungumza na Daphine akiwa ameduwaa,Brigedia Karanje akatumia mwanya huo kuinama chini taratibu na kuokota chuma kizito,akakishika vizuri na kumpiga nacho Ngesa shingoni,hapohapo Ngesa akadondoka chini.Daphine akachanganyikiwa ajabu,akashindwa achukuwe maamuzi gani,mbele yake kulikuwa na bastola imelengwa kwake,kushoto nyuma yake yupo Karanje,Ngesa kadondoka chini hana fahamu.Akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya umeme,akaruka teke aina ya round kick,likamfikia Jaqlin Mfinanga,kwenye mkono alioshika bastola,akajitupa chini na kubiringika ili kuiokota bastola iliyondoka,hesabu zake zilienda sawa kwani baada ya kuishika tu,akageuka kwa kasi.
“Paa! Paa! Paaa!”
Akaachia risasi tatu, upande aliokuwa amesimama Brigedia Karanje,bahati mbaya ikawa kwake kwani Karanje aliinama na kutoka mlangoni akikimbia,risasi zote zikapiga ukutani hiyo ikawa ponea yake,hakusimama hata kidogo akazidi kusonga mbele zaidi.Kumuachia Karanje ni kitu ambacho hakutaka kitokee hata kidogo, ndiyo maana nayeye akatoka nje bastola ikiwa mkononi mwake,ameishika vizuri tayari kwa kumfyatua risasi.
“Paaa paaaa”
Risasi mbili zilichomoka,lakini zote zilimkosa Karanje, ambapo tayari akawa ameingia katikati ya miti mirefu,giza lilikuwa totoro hivyo haikuwa rahisi kwa Daphine kuona tena vizuri!Licha na hiyo haikumfanya aogope kuingia ndani ya msitu huo wa kutisha,kwa mikono miwili akiwa ameshika bastola yake,akaanza kutembea kwa mwendo wa taratibu.
Brigedia Karanje,hakuwa mwanaume wa kawaida,alikuwa ni shupavu mwenye mafunzo yote ya kijeshi, hivyo kwake yeye jambo hilo alilifananisha na vita kali,ndiyo maana akajificha nyuma ya mti mkubwa,akamuangalia Daphine anavyotembea kwa taratibu,akawa tayari kwa lolote litakalo tokea,kitendo cha Daphine kupita mbele yake alimvuta kwa nguvu na kumtwanga kichwa cha uso,kwa kasi ya umeme akaukamata mkono wake ulioshika bastola,akauzungusha, yeye akawa mbele,akampiga na kipepsi cha tumbo,bastola ikadodoka chini.Wote wakakunja ngumi tayari kwa mpambano mwingine!
******
Nchi tayari iliingia matope,hakukuwa na maelewano tena!Maandamano yalizidi kila pembe ya jiji la Dar es salaam,kila kona wananchi walishika mabango yao wakikemea uongozi wa Rais Leslie,hiyo ilifanya mikoa jirani wahamasike,mikoa kama Morogoro,Tanga na Pwani.Wakaiga,mambo hayakuwa mazuri,polisi waliokaa barabarani wakijaribu kuwatawanya wakashindwa!Vurugu ikawa kubwa sana,watanzania wakabadilika,hawakuwa wale wanyonge tena ambao kipindi cha nyuma, waliburuzwa kama magari mabovu.Mabango,yalisimamishwa juu hewani,raia walichoka.Kilichowachanganya zaidi ni matukio ya vifo vya kutisha.Mbaya zaidi mtuhumiwa aliyeitwa Derrick Ngesa,alikamatwa kisha kuachiliwa huru bila Rais Leslie kusema chochote,hii ilikuwa picha mbaya sana kwao!Jambo hilo lilimchanganya sana Rais Leslie,akaogopa kuongea chochote wala kutoka nje,alichofanya ni kumtuma muwakilishi wake lakini hilo halikufanya kazi.Kichwa chake kilimuuma mno!
“Grii griii”
Simu yake ya mezani,ikamshtua kutoka katika dimbwi la mawazo,akaiangalia kwa muda na kuokota mkonga wa simu,akauweka sikioni.
“Mheshimiwa Rais,unaongea na Dustan”
“Upo wapi?”
“Nipo njiani nakuja Ikulu”
“Ngesa yuko wapi?”
“Yupo Arusha”
“Simpati kwemye simu”
“Hata mimi,kuna jambo nataka kukwambia”
“Nakusikiliza”
“Naomba nionane nawewe”
“Huwezi kuniambia kwenye simu?”
“Hapana,ni mambo ya kiusalama zaidi”
“Hakuna shaka”
Mambo aliyobeba Dustan ndani ya kichwa chake yalikuwa mazito,kama angeweza kuyatoa na kuyaweka juu ya mzani ni lazima mzani ungevunjika.Habari ya mkuu wa Mkoa,kushirikiana na Brigedia Karanje ilimshtua kuliko kawaida,ndiyo maana alitaka kuonana na Rais Leslie ili amueleze kila kitu,alielewa sana ni jinsi gani Rais Leslie angeumia, kutokana na ukaribu wake na RC Daud Bashonga.
Barabara ya Samora Avanue kulikuwa na msongamano wa watu, ilibidi anyooshe moja kwa moja ili atokee soko kubwa la samaki Feli,huko aliamini ingekuwa rahisi sana kwake kufika Ikulu,Magogoni.Akasonga mbele na kuona namna watu walivyofunga barabara wakiwa na mabango,akapitiliza.Dakika kumi na mbili baadaye, akawa tayari amefika Ikulu,huko msongamano wa watu ulikuwa mkubwa pia,akapita mpaka getini na kujitambulisha.Simu ikapigwa ndani,akaruhusiwa kupita.Kwa Rais Leslie, hakukuwa na mgeni wa aina yoyote ile,haikuwa kazi ngumu kuonana naye!Kwa heshima kubwa, akamsalimia kisha kuketi kitini.Sura ya Rais Leslie,ilionekana kuchanganyikiwa hakuwa katika hali ya kuonesha tabasamu kama alivyozoeleka siku zote, alikuwa katika muonekano wa hofu kubwa sana.
“Umefikia wapi?”
Rais Leslie,akauliza ili kufupisha maongezi.Dustan,akakaa vizuri na kumtizama Rais, tayari kwa kumpa habari hizo nyeti sana tena za kuogopesha,ilikuwa ni lazima amtaje Daud Bashonga kama muhusika mkuu,kwenye kila kitu kilichotokea.
“Dustan,nakusikiliza endelea.Nani anahusika umeniambia?”
Rais Leslie,akataka kujua.Hapo ndipo Dustan,akataja kila kitu!Hakuacha kitu chochote kile nyuma,akamuelezea mpango mzima wote, utakavyokuwa mpaka namna walivyopanga kuingia Ikulu na kuiteka nyara.Wakati huo wote Rais Leslie,alikuwa kimya anamtizama Dustan,akashusha pumzi ndefu ya kuchoka!Moyo wake ulipiga kwa nguvu mno,hakuelewa kwamba kwa miaka yote hiyo, alikuwa amelikumbatia bomu na sasa limemlipukia mwenyewe.
“Hapana,sio kweli.Nimemfahamu Daud kwa miaka mingi sana!Nilimuingiza kwenye siasi akiwa mdogo,haiwezekani.Hapa kuna kitu”
Hapohapo,Rais Leslie akasimama na kumuacha Dustan,juu ya kiti.Akafungua mlango,alivyorudi ndani baada ya dakika mbili kupita,nyuma yake walifuata askari wapatao sita.Wakamnyanyua Dustan kinguvu na kumuweka ukutani,wakatoa pingu na kumfunga kwa nyuma.
“Mheshimiwa Rais,unafanya makosa makubwa sana”
Dustan,alizungumza maneno hayo kwa sauti,lakini ikawa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa,askari wakamtoa nje akiwa chini ya ulinzi bila kujua ni lipi kosa lake kubwa.
*******
Ngumi pamoja mateke aliyokuwa anarusha Brigedia Karanje mithili ya feni,Daphine aliona,kazi yake ilikuwa ni kuinama na nyingine kuzipangua akitumia mikono yake,mwanamke huyu hakuwa wa kawaida hata kidogo alikuwa ni mwanamke wa chuma!Mbaya zaidi alitumia mafunzo yote, aliyofundishwa na kambi anayomiliki Brigedia Karanje,kifupi Kinyago alichokichonga Brigedia Karanje kilianza kumtisha mwenyewe.Daphine, alivyoona ngumi ya Karanje inakuja upande wake wa usoni,akainama kidogo na kumpiga ngumi tatu za haraka mbavuni,akarudi juu na kumchimbua ngumi nyingine ya kidevu!Hakuishia hapo,akakanyaga kipande cha gogo na kuruka fly kick,lililomfikia Brigedia Karanje kifuani,akayumba kidogo!Hapo Daphine, hakufanya makosa, kama Ngedere,akampandia kifuani kiutaalam na kujifiringisha shingoni mwake,akamshushia kifuti kikali cha shingo.Kila Brigedia Karanje alipojaribu kujitoa,alishindwa.Wakadondoka wote chini puu,Daphine akaendelea kung’ang’ania shingo ya Karanje kwa nguvu sana,bila kuachia.Matukio mbalimbali ya kinyama,yalimfanya apandishe Mori na kujawa na hasira,akazidi kumpiga kabali Brigedia Karanje kwa nguvu,akiwa katikati ya zoezi hilo huku jasho likimtoka jingi,akahisi kama kuna kitu cha chuma kimemgusa utosini.
“Simama,juu!Kabla sijafumua ubongo wako”
Ilikuwa ni sauti nzito,kutokea nyuma.Huyu alikuwa ni mwanajeshi,kutoka katika kundi la Brigedia Karanje,alikuwa mwenye hasira ajabu!Hakutaka kumuacha Daphine akiwa hai kwani kwa muda mrefu, alikuwa msumbufu mno kwao!
“Paaaaaaaaa!”
Kilichosikika hapo, ulikuwa ni mlio mkubwa sana wa bastola,damu zikaruka na kutapakaa chini.Mwanajeshi aliyeshika bastola alikuwa chini,ubongo wake umemwagika,Daphine akageuka ili kujua ni nani kafyatua risasi hiyo,akatabasamu baada ya kumuona mwanamme wa shoka, DERRICK NGESA kashika bastola,hiyo ilimpa nguvu nyingine mpya.
Hakukuwa na dalili yoyote ile ya Brigedia Karanje kutoka akiwa salama katika mikono hiyo ya watu hawa wawili,Daphine na Ngesa!Bastola ilikuwa mbele yake,kumaanisha kwamba angeenda kinyume kifo kingekuwa halali yake,hilo lilikuwa wazi kabisa.Ndiyo maana akatulia akiwa chali,amelala juu ya majani.
“Ngesaa,Shoot him”(Ngesa,mfyatue)
Daphine alizungumza akimwambia Ngesa,alikuwa ana kila sababu ya kutaka Karanje apigwe risasi na kufa,kutokana na mambo yaliyotendwa na gaidi huyo, mbaya zaidi ndiye yeye,aliyewauwa wazazi wake kipindi alipokuwa mtoto mchanga.
“Ngesa,what are you waiting for?”(Ngesa unasubiri nini)
Daphine aliuliza kwa mara nyingine tena kwa ukali,baada ya kumuona Ngesa ameshika bastola, hachukuwi hatua ya aina yoyote ile.
“Ha!Haa!Haaa!Haaaa!shoot me,pull the trigger!Niueee niuee sasaaa”
Yalikuwa ni maneno ya Brigedia Karanje,akiwa na damu mdomoni amelala chini anataka Ngesa ampige risasi,alifanya hivyo kwa makusudi ili amtie hasira Ngesa!Alielewa nini maana yake endapo angewekwa chini ya ulinzi na jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,aliona ni bora afe hapohapo kwa kupigwa risasi moja, kuliko kutangazwa katika kila chombo cha habari sambamba na kupewa adhabu kali.
“Ha!haa!Haaa!Haaaa!Ngesa!Wewe ni mwanaume,nimeua watu wengi sana!Nimenyonga,alafu ki ukweli.Nilimuua na Mama yako mzazi,mimi ndio niliunguza nyumba yenu moto”
Hapo Ngesa alibana meno yake kwa hasira,alitamani kufyatua risasi lakini nafsi nyingine ilimpiga ‘stop’ asifanye hivyo,sababu ilikuwa ni lazima mtu huyo apelekwe akiwa hai kwanza ili Tanzania ijuwe kwamba Brigedia Karanje yupo chini ya ulinzi,alichofanya Ngesa ni kumsogelea karibu na kumpiga na kitako cha bastola kichwani,akamfumua na teke la shingo!
“Simama”
Ngesa akaamuru,Daphine bado alikuwa mwenye hasira alitamani Brigedia Karanje afe mara moja,siku hiyo aliamini ndiyo nafasi yake ya kufanya jambo hilo.
“Ngesa,kwanini unamuacha?Muuwe”
“Hapana,lazima tumpeleke akiwa hai”
“Kwanini?”
“Rais Leslie anamtaka akiwa hai”
“Shiit,Ngesa.Nipe bastola”
“Hapana Daphine,tumchukuwe”
Kishingo upande bila matwaka yake,Daphine akakubali wakamuweka chini ya ulinzi Brigedia Karanje,wakamuinua kinguvu huku bastola zote zikiwa nyuma yake.
Wakasonga mbele mpaka kwenye kijumba kilichokuwa eneo hilo,ndani walimkuta Jaqlin Mfinanga amejikunyata analia kwa kwikwi,bado hakuamini kama kwenye vita hiyo angetoka salama.Ngesa akamsogelea na kumkumbatia kwa nguvu.
“Pole sana mke wangu”
Hakuna hata mmoja kati yao aliyeamini kama amepona,sio Ngesa wala Jaqlin Mfinanga, walikumbatiana kwa nguvu na mahaba yote,hiyo ilifanya mpaka Daphine aangalie pembeni,akashusha pumzi ndefu kidogo na kumtizama Brigedia Karanje aliyekuwa pembeni yake,aliyeonekana anatafakari kitu fulani kikubwa.
“Mshukuru sana Ngesa,leo ningekuuwa”
Daphine alimwambia Brigedia Karanje,ilibidi kabla ya kuondoka eneo hilo wafanye mawasiliano na Rais Leslie, kumtaarifu kuhusu habari hiyo ambayo, waliamini ingekuwa njema kwa upande wake.Rais Leslie,alionesha kufurahi na kuchangamka kuliko kawaida, hakuamini kama zoezi hilo limefanyika. Shukrani alizotoa kwa Ngesa hazikuwa na mfano wake.
“Hongera sana Ngesa,baada ya hapa.Naomba nikukatie tiketi wewe ni timu yako nzima.Mkapumzike nchi yoyote ile mnayotaka”
“Ahsante Mheshimiwa Rais”
“Nitawatumia Helkopta ya jeshi la polisi,nitajie ulipo ili nitume jeshi”
Ilibidi Ngesa aseme alipo,hapohapo bila kupoteza muda Rais Leslie, akatoa amri ya kwamba Ngesa na Daphine wafuatwe na helkopta pamoja na Brigedia Karanje!
“Namuhitaji Ngesa na Daphine hapa Ikulu”
Rais alisema baada ya kukata simu.
“Sawa Mheshimiwa”
******
Halikuwa jeshi mchezo mchezo,hata siku moja wasingekubali Brigedia Karanje mkuu wao wa kikosi,akamatwe kikondoo namna hiyo walikuwa tayari kupambana kufa kupona,ndiyo maana wanajeshi wengine walikimbia niya yao ikiwa kwenda kuungana na wenzao ili wamkomboe Mkuu wao wa kazi kwani bado walikuwa na kibarua kingine zaidi mbeleni,kumuachia Brigedia Karanje abaki mikononi mwa Jeshi la polisi kulimaanisha mipango yao kukwama na pengine kukamatwa na hilo lilikuwa wazi kabisa,vitanzi vingewahusu.Ndiyo maana wakakimbilia makao makuu yao ili kujipanga,huko walichukuwa wanajeshi wengine themanini na mbili na magari ya kivita kumi na saba,walielewa kabisa ingeibuka vita kubwa sana kwani kivyovyote vile ni lazima jeshi la polisi, lingeingilia kati.
“Mkuu,nina uhakika yupo chini ya ulinzi.Kuruhusu aingie mikononi mwa Jamhuri,tutakuwa tumefanya kazi bure.Tuungane vitani!Hata ikitokea vita vya tatu vya dunia,kuna mwenye kipingamizi?”
Huyu aliitwa Captain Kavishe,mwanajeshi mrefu mweusi kuliko wenzake.Kupewa taarifa za Brigedia Karanje kuvamiwa zilimfanya apandishe mori na usongo!Ndiyo maana alisimama kidete na kutoa maelekezo hayo ya mwisho usiku huohuo!Magari ya kijeshi matatu aina ya Hammer, yalikuwa pembeni,mengine yalikuwa maroli ambapo nyuma yangepakia wanajeshi wengine,hiyo ilikuwa ni sawa na kwenda vitani kwani kila mtu alikwa na mtutu begani na bastola kiunoni.
“Kurudi nyuma ni mwiko”
“Sawa mkuu”
“Sawa mkuu”
Wanajeshi wote wakaitikia kwa pamoja.
“Twendeni”
Kitendo cha kauli hiyo kutoka kwa Captain Kavishe,wanajeshi wote walianza kudandia magari,safari ikaanza hapohapo wakiwa tayari kwa ajili ya mpambano huo wa kivita kwa ajili ya ukombozi.
*****
“Tuku! Tukuu! Tukuuu! Tukuuu! Tukuuuu!”
Ulikuwa ni mlio mkubwa wa Helkopta ikizungusha mapangaboi kwa kasi,ambayo ubavuni ilikuwa na bendera ya Tanzania na nembo kubwa ya jeshi la polisi,ilikuwa karibu kutua ndiyo maana Ngesa na Daphine waliiona vizuri ubavuni wakiwa karibu,ilikuwa ikiwaka taa kila mahali na chini ilikuwa na tochi kubwa inawamulika,hapo walipunga mikono kuashiria helkopta hiyo itue mahali hapo.Bila kuuliza chochote walishaelewa kwamba Helkopta hiyo, imetumwa kutoka Ikulu kuwakomboa,wakati Helkopta ikiwa katika harakati za kutua hapo ndipo Hammer za jeshi zikaingia, hawakutaka kuchelewa mwanajeshi mmoja akafungua mlango wa gari akiwa na kombora kubwa,akaliweka begani vizuri.Akalenga Helkopta!
“R.P.G”
Ngesa alipiga kelele kwa sauti,akamrukia Daphine na kujitupa pembeni kwani alielewa nini maana ya kombora hilo hatari ambalo likifumuka ni lazima lisambaratishe kila kitu.Kitendo cha kujitupa chini tu,ulitokea mlipuko mkubwa sana! Kilichoonekana ni moto mkubwa, Helkopta ilikuwa imepasuliwa pasuliwa vibaya sana,mbaya zaidi kuna kipande kimoja kikubwa kilimdondokea Jaqlin Mfinanga kichwani na kumfunika hapohapo,Ngesa alikuwa juu, Daphine yupo chini yake amemlalia.
“Koho kohoo”
Vumbi na moshi ndio ulitanda,ikamfanya Ngesa akohoe kwani alipaliwa,alivyotaka kuinuka akatulizwa na mguu mgongoni,alivyogeuka akakutana na mwanamme mrefu begani ana mtutu.
“Karanje yuko wapi?Sitokuuliza tena”
Ngesa alikuwa chini bado,amekanyagwa hakujibu kitu chochote hiyo, ilimfanya apigwe na kitako cha mtutu mdomoni,akapigwa na teke kali la kichwa.
“Karanje yuko wapi?”
Swali hilo,lilivyoulizwa wanajeshi wengine wakawa tayari wamefika, wanatizama huku na kule bahati nzuri wakamuona Mkuu wao Karanje,amelaliwa na pangaboi la Helkopta,wakamvuta na kumchukuwa wakampakia ndani ya gari.Hiyo haikufanya wawaache Daphine na Ngesa,wakabebwa juu juu,mpaka ndani ya Hammer za jeshi,wakiwa mateka tayari.Hiyo ilimaanisha huko wanapoenda,wangeenda kufanyiwa kitu kibaya kama sio kuuwawa!
*******
Kupotea kwa mawasiliano angani ghafla kulifanya Jeshi la anga lipate wasiwasi mkubwa sana,helkopta iliyotumwa iende kuwachukuwa Ngesa na Daphine pamoja na gaidi Brigedia Karanje,ilipoteza mawasiliano .Hiyo ilimaanisha kuna tatizo limetokea,hakukuwa na muda wa kupoteza!Rais Leslie,akapewa taarifa hizo,mapigo yake ya moyo yakapiga kwa nguvu.Akapiga simu moja kwa moja mkoani Arusha,ili jambo hilo lifuatiliwe mara moja.Taarifa alizopewa dakika ishirini baadaye,zilimfanya atake kulia machozi,helkopta ilikuwa imelipuliwa.Daphine pamoja na Ngesa hawaonekani,hiyo ilimaanisha kuna dalili mbaya sana zimetokea,isitoshe hata Brigedia Karanje hayupo pia.Jasho jembamba lilianza kumtoka,akahisi joto japokuwa ndani ya ofisi yake kulikuwa na kiyoyozi.
“Grii griiii”
Kilichomshtua ilikuwa ni simu yake ya mkononi,alivyoangalia juu ya kioo akaona Private number.Yaani namba haionekani mpigaji hakutaka namba yake ijulikane,akashusha pumzi ndefu na kuiweka sikioni baada ya kuipokea.
“Leslie,nilikwambia.Hii vita,hutoweza!Sasa basi,nakupa masaa ishirini na nne,jisalimishe kwangu ili nchi yako iwe katika hali ya amani na utulivu.La sivyo,utajuta na damu za Watanzania zitakuwa juu yako”
“Kara…”
“Nakupa masaa ishirini na nne,sikubembelezi.Una uamuzi pia wa kukataa lakini utajuta katika maisha yako yote”
“Sa…tititi”
Hapohapo simu ilikatwa na kumfanya Rais Leslie,hofu imtande. Yalikuwa ni maneno ya kutisha mno kwake kutoka kwa Brigedia Karanje,alielewa nini maana yake kwa yeye kujisalimisha kwa Brigedia Karanje,moyo ulimuuma na kuanza kutafakari mara mbilimbili ni kitu gani akifanye,ilikuwa ni lazima achague kitu kimoja.Kujitoa sadaka kwa ajili ya watanzania ama kuwaacha wafe,hapo ndipo akachoka zaidi.
****
Safari ya jeshi la Brigedia Karanje, ilikuwa ndefu,walitumia pori kwa pori,hawakutaka kutumia barabara kubwa ya lami, kuhofia usumbufu barabarani kwani waliamini huko jeshi la polisi lililatanda kuwasaka ili kuwadhibiti.Safari yao iliishia katikati ya miti mingi mno,hapo Brigedia Karanje akashuka na wanajeshi wengine nane!Daphine na Ngesa wakateremshwa kama mizigo, mpaka mbele ya Karanje.
“Leo Mtaku….tuuup”
Karanje alikatishwa sentensi yake baada ya Daphine kumtemea mate usoni,sio siri mwanamke huyu alikuwa na hasira pamoja na jeuri nyingi.Kitendo hiko kilifanya wanajeshi wengine waangalie chini,mkuu wao kufanyiwa hivyo ilikuwa ni aibu kubwa.Brigedia Karanje akafuta mate usoni akitumia kiganja chake,kwa hasira za waziwazi akamzabua kibao kikali kilichomfanya Daphine aende chini mzima mzima,Ngesa alilishuhudia hilo lakini hakuwa nala kufanya zaidi ya kumuinua Daphine na kumsimamisha,walichosubiri hapo sio kitu kingine ni kifo chao tu kwani waliamini wasingetoka salama ndani ya mikono hiyo ya watu hatari.
“Mkuu,kuna simu yako”
Mmoja wa makamanda,akachomoka na kutembea akiwa na simu kubwa mkononi,akamkabidhi Brigedia Karanje,akaiweka sikioni.
“Yes”
“Unaongea na Daud Bashonga”
“Nakusikiliza”
“Ndio nipo kwenye process za kumtorosha pia Mzee Ngesa maabusu”
“Ukikamilisha,nambie”
“Hakuna shaka”
Simu ilivyokatwa Brigedia Karanje,akamtizama Ngesa kwa macho makali.
“Muda mfupi,tutakuwa na Baba yako!Nadhani unajua nini maana yake”
*****
Dustan,alikuwa nyuma ya nondo nzito,anahangaika kutafakari namna ya kujikomboa.Fununu za Ngesa pamoja na Daphine kupotea katika mazingira ya utata zilimpagawisha,uhakika alikuwa nao moja kwa moja ya kwamba ni lazima wapo kwenye hatari kubwa na Karanje ndiyo yupo nyuma ya yote hayo sababu alimjua vizuri tu, gaidi huyo na historia yake ya kutisha.Kwa maana hiyo yeye ndiye alikuwa ni nuru pekee,alivyomkumbuka Rc Daud Bashonga,hasira zikampanda zaidi.Akatembea na kuchungulia kwenye nondo,hapo alimuona askari mmoja amesimama,akatafakari kwa muda kidogo na kurudi ili apate akili nyingine mpya!Ilikuwa ni lazima atoroke ili akaonane na Daud Bashonga uso kwa uso huyo angemsaidia kuwataja ni wapi Daphine na Ngesa walipo,kwa njia moja ama nyingine!
“Mkuu”
Dustan,akaita huku akiwa ameshikilia nondo kwa mikono miwili.
“Mkuu”
Askari,akageuka na kumtizama bila kujibu chochote!
“Mkuu,nina shida kidogo”
“Mkuu,njoo mara moja”
“Nyamaza,siwezi kukusaidia chochote kile”
“Nakuomba unisikilize kidogo”
“Nimekwambia siwezi”
“Dakika moja tu.Nitakupa kiasi chochote cha pesa”
Dustan,akazidi kumshawishi akitumia maneno ya kumtega askari huyo, ambaye kiunoni kwake alining’iniza funguo za kufuli kubwa, lililofungwa kwenye nondo alizokuwepo yeye,dakika tano baadaye ndipo askari huyo akakubali.
“Nakusikiliza,sema”
“Sogea nikwambie”
Askari akajifikiria kwa sekunde kama tano hivi,akatizama huku na kule na kumuangalia Dustan kwa umakini wa hali ya juu sana,akapiga hatua mpaka kwenye nondo.
“Pale naniiii…”
Lilikuwa ni kosa kubwa tena la Jinai kwa askari huyo kusogeza kichwa chake karibu na Dustan,aliyekuwa kwa ndani kwani shingo yake ilivutwa kwa nguvu,akawa kama kuku aliyebanwa na kicheche.Akashindwa kufanya chochote.
“Fungua mlango,haraka”
Dustan alizungumza hivyo huku akiendelea kumbana kwa nguvu kwenye nondo hizo za chuma,hiyo ilimfanya askari huyo apate maumivu makali shingoni na kichwani, hapo ndipo alipoanza kupapasa kiunoni na kutoa funguo,kwa shida na tabu akaanza kusaka kufuli na kufungua.Dustan,akachomoka na kumvuta kwa nguvu,akampiga kichwa cha mdomo na kumuweka yeye nyuma ya nondo.Akamsukumiza na teke kali la shingo!
“Tulia hapohapo”
Hakutaka kupoteza wakati,akachomoka na kuanza kutembea taratibu huku akiwa katika tahadhari kubwa sana,mbele yake alimuona askari ameshika bastola.Hapo ndipo akawa makini zaidi,akatembea taratibu na kumkaba kwa nyuma,akachomoa bastola ya askari iliyokuwa kiunoni.
“Nitamwaga ubongo wako,tulia hivyohivyo”
Dustan akazungumza kwa ukali akiwa na bastola mkononi,kamuwekea mlinzi kichwani.
“Nataka kutoka nje,twende”
Dustan alizungumza na kutoa amri hiyo,ambapo waliingia mpaka ndani ya chumba kidogo.Hapo akachukuwa pingu na bisibisi,akaingiza kwenye matundu na kupachua loki zake,kumaanisha kwamba hata bila funguo zake unaweza kufungua,akajivisha mikononi mwake kwa mbele.
“Twende,nataka unitoe nje ya geti”
Mlinzi,akawa keshajua ni kitu gani anatakiwa kukifanya,mbaya zaidi bastola ilikuwa tumboni mwake Dustan ameshika kwa pembeni ili askari wengine wasione.
Picha ilionesha kwamba mlinzi huyo,amemuweka Dustan chini ya ulinzi kumbe yeye ndiye yupo mateka.Akafanikiwa kuwapumbaza askari walioko geti la kwanza,la pili walivyohoji pia wakapita.Walivyofika geti la mwisho.Wakazuiliwa,hapo Dustan akashusha pumzi ndefu!
“Onesha transfer document”
Afande mmoja wa getini akataka barua maalum.
“Ni dharura”
“Subiri,nipige simu niulize”
Ilikuwa ni lazima Dustan,atumie akili nyingine ya ziada, vinginevyo angerudishwa ndani!Akabaki anatizama maaskari,akamuangalia askari aliyeingia ndani ya kijumba chake kwa ajili ya kupiga simu huku akitafakari na kupiga hesabu za haraka ya jinsi gani ya kuwatoka dakika hiyohiyo.
Mashujaa waliojitolea kuikomboa nchi ya Tanzania kufa au kupona ambao Daphine na Ngesa leo hii kiza kipo mbele yao,hawaelewi ni kitu gani wakifanye, baada ya Brigedia Karanje kuwaweka mateka,hiyo ilimaanisha kifo kipo mbele yao bila ubishi wowote ule.Historia ya watu hawa ilikuwa ni kuwindana kama paka na panya.Kwa Gaidi huyu Brigedia Karanje, siku hiyo kwake ilikuwa ni kama sherehe kubwa kuwaweka watu hao katika himaya yake kwani walimsumbua na kufanya harakati zake zikwame,ndiyo maana ndani ya mtima wake alijawa na furaha ajabu,mpango wake ulikuwa mkubwa sana na ilikuwa ni lazima aipindue nchi ya Tanzania kwa mabavu,hilo lilikuwa ni wazi kabisa kutokea sababu alijiamini na watu waliokuwa nyuma yake walimuonesha kumuunga mkono!
Mambo aliyofanyiwa na Rais Leslie,hakuweza kuyavumilia hata kidogo.Aliamini kabisa kwa kufanya mauaji hayo ingemlazimu Rais Leslie aachie ngazi,maandamano yaliyokuwa yanaendelea nchini humo yalimpa moyo na kujua kivyovyote vile ni lazima Rais Leslie angeachia madaraka,japokuwa aliamini swala hilo halikuwa rahisi kama anavyodhani.Mpango wa kwanza ulikwama baada ya kutegesha sumu kali lakini pia walikuwa na mpango mwingine wa kuvamia ikulu kama sio msafara wa Rais Leslie.Ngesa,alimuangalia kila mwanajeshi aliyesimama mbele yake,akamtizama Brigedia Karanje, ambaye kwa wakati huo alikuwa akifanya mawasiliano na watu kupitia simu.Maongezi hayo yalikuwa ya kutisha mno kwani kulikuwa na mpango mwingine wa hatari wa kutegesha sumu ya hewa, ambayo ingeendelea kuuwa mamia na maelfu ya watu.
“Ndio,baada ya Mzee Ngesa kutoka!Tutatega lingine,fanya huyo mzee atoke.Nadhani unajua ana maana gani,kila kitu kipo sawa.Hakuna kitakacho haribika,Derrick nipo naye!Na huyu Kahaba Daphine.Wasikutie wasiwasi,ninawamudu.Hapa wamefika,sawa?Mapambano yaendelee”
Brigedia Karanje baada ya kuhitimisha mazungumzo hayo ya kutisha simuni, alimtizama Ngesa kwa macho makali,akamsogelea karibu kabisa.
“Una masaa machache hapa duniani,tumia pumzi yako vizuri.Kama una Sali,fanya hivyo”
Brigedia Karanje alizungumza,hiyo ilimaanisha baada ya muda mfupi,angemmaliza kwa kumpiga risasi ama kumnyonga.Kumuacha hai Ngesa kulimaanisha mipango yake yote kukwama.
“Nilizaliwa mara moja,nitakufa mara moja”
Ngesa akajibu kwa kujiamini,sawa alikiogopa kifo lakini hata hivyo aliamini ilikuwa ni lazima siku moja afe tu.Hiyo ikamfanya Brigedia Karanje,atabasamu kwa dharau na kumuhurumia sababu aina ya kifo ambacho angekumbana nacho Ngesa, hata Shetani mwenyewe angeshika mdomo kwa uwoga.
*****
Kibandani wanapokaa maaskari walikuwa makini kumtizama Dustan ambaye kwa wakati huo walidhani yupo chini ya ulinzi kumbe ilikuwa kinyume chake,niya ya kuwazuia getini, ilikuwa ni kupiga simu ndani ili wajue ni kweli ruhusa hiyo imetoka kwa Mkuu wao wa kazi,lakini matokeo yake simu iliita bila kupokelewa,hapo ndipo wakaamua kuchukua maamuzi mikononi mwao!Wakamruhusu askari aliyemshika Dustan atoke nje,kwa Dustan ikawa ahsante Mungu,kitendo cha kutoka nje na kutembea mpaka kwenye maegesho ya magari,kilimfanya Dustan ageuke na kumuwekea askari bastola kichwani.
“Ingia ndani ya gari”
“Tunaenda wapi?”
“Nimekwambia ingia”
Askari alikuwa katika wakati mgumu usioweza kuelezeka,gari liliwashwa kwa safari moja tu!Kuelekea viwanja vya Biafra,nyumba anayoishi Jenipher.Kivyovyote vile aliamini huyo ndiye angekuwa msaada kwake kwa wakati huo ingawa hakumuamini sana kama kipindi cha nyuma!
Alichokifanya ni kumfunga askari pingu huku mkono wake akiuzungushia kwenye usukani, kumaanisha kwamba asingeweza kwenda popote pale.Dustan,akashuka huku akiweka bastola kiunoni!Akatembea mpaka kwenye geti la nyumba hiyo, aliyokuwa anaishi Jenipha,mpelelezi kutoka serikalini ambaye waliwahi kufanya kazi kitengo kimoja!Hapo akatulia kidogo ili kuangalia mazingira,alivyoona kila kitu kipo sawa!Akaruka ukuta na kutua ndani kama ninja, bila ya kutoa kishindo cha aina yoyote ile.Kwa kuwa,aliingia mlango wa nyuma Jenipha aliyekuwa ndani alishindwa kusikia sababu yeye alikuwa chumbani,mbaya zaidi alikuwa anaangalia luninga hakuelewa kwamba Dustan,yupo nyumbani kwake tayari.Staili aliyotumia kutembea Dustan haikuwa rahisi kwa mtu yoyote Yule kugundua kwamba kuna mtu nje sababu alinyata kwa mwendo wa paka shume,alivyojaribu kunyonga kitasa cha mlango haukufunguka kwake ikawa vigumu kuingia ndani ikabidi awaze njia nyingine ya kutumia!
Kwa Jenipha asingeweza kufungua mlango kama angeugonga, ilibidi azunguke na kuligonga geti,hilo ndilo wazo lililomjia ingawa hakuwa mwenye uhakika kama litafanya kazi vizuri kama anavyotaka yeye,taratibu kwa kunyata akazunguka mpaka mbele,hapo alianza kuligonga geti huku akiwa amejificha, alifanya hivyo mpaka alivyohisi milango ya ndani inafunguliwa,akatembea kwa kasi mpaka mlangoni ili amsubiri Jenipha.
Kitendo cha mwanamke huyo kufungua mlango,akakutana na mlango wa bastola usoni kwake.
“Jenipha,usijaribu kupiga kelele.Nitakuuwa,sitaniii”
Tangu wafahamiane na Dustan hakuwahi kumuona katika hali kama hiyo,Dustan alibadilika rangi akawa mwekundu,hiyo ilimfanya Jenipha arudi kinyume nyume kama gari lililofeli breki kwenye mlima.
“Dustan.....”
“Kimya”
Hapo Dustan alifunga mlango,Jenipha alianza kutafakari ni kwa njia gani Dustan alitoroka ikulu wakati alishikiliwa na alikuwa chini ya ulinzi.
“Nahitaji msaada kutoka kwako”
“Siwezi kukusaidia,umeniwekea bastola kichwani unless uniambie nipo mateka”
Dustan,akamuangalia mwanamke huyu kwa umakini na macho makali sana!
“Ukijaribu kufanya kitu chochote cha kipumbavu,nitakuuwa Jenipha”
Baada ya kuongea maneno hayo kwa hasira,akashusha bastola chini na kuiweka kiunoni.
“Unahitaji msaada gani?”
“Ngesa na Daphine,wametekwa!Anayejua ni wapi walipo ni Bashonga”
“Una maana gani?”
“Bashonga na Karanje,wanashirikiana kwenye hili”
“Una uhakika?”
“Asilimia zote”
“Hapana Dustan,sihitaji kuingia kwenye matatizo sasa hivi.Hapa nilipo kuna vitu vingi vinaniumiza kichwa changu!Nishaelewa unahitaji nini?Kifupi siwezi”
Hapo ilibidi Dustan awe mpole,hakutaka kutumia nguvu sababu aliamini angefanya hivyo ilikuwa ni sawa na kumlazimisha Ng’ombe kunywa maji,alitakiwa aende na Jenipha mdogomdogo sababu alimjua alikuwa ni mwanamke anayependa kubembelezwa kwa upande mwingine,huo ndio ulikuwa udhaifu wake ndio maana akafanya hivyo,ikamchukuwa nusu saa lizima mpaka Jenipha kukubali kumpa kifaa maalum cha kunasa sauti, kwenye simu pamoja na GPS ya kujua ni wapi mtu alipo,hiyo haikutosha Dustan alihitaji silaha za kutosha,alijua kivyovyote vile huko anapoelekea hapakuwa salama kama angeenda kizembe!
****
Mchakato wa kumkomboa Mzee Ngesa,ulianza usiku huo huo baada ya mkuu wa kituo cha polisi kupigiwa simu moja kwa moja na mtu aliyejitambulisha kwamba anatoka ikulu.Hiyo ilikuwa ngumu kwake kwani alitishiwa maisha baada ya kutajiwa majina ya watoto wake, pamoja na mkewe!Sio siri askari huyo ambaye alikuwa anamsimamia Mzee Ngesa, katika kesi yake alikuwa katika wakati mgumu kuliko siku zote.
“Una nusu saa,nahitaji umlete Uwanja wa Ufi”
“Lakini in..”
“Maisha ya mkeo na watoto wako,yapo mikononi mwako”
Hapohapo simu ikakatwa,yalikuwa ni maongezi ya kutisha usiku huo ukizingatia yeye ndiye alikuwa zamu na funguo zote zilikuwa katika ofisi yake!Hakuelewa ni kitu gani akifanye lakini alishajua kwamba mtu aliyempigia simu ana madaraka makubwa sana serikalini zaidi na hayo,ana mkono mrefu ambao hata angeenda popote pale angegundulika kwa haraka,hivyo ilikuwa ni lazima achukuwe maamuzi magumu na baada ya hapo akimbie mbali sababu kesi hiyo ingekuwa kubwa mno,alichokifanya bila kutafakari mara mbili,akachukuwa funguo na kutembea mpaka chumba alichofungwa Mzee Ngesa,akafungua na kumfunga pingu!Wote wakatoka nje na kuingia ndani ya gari,safari ya kwenda uwanja wa Ufi ikaanza mara moja!Kwake ilikuwa ni bora kumtoa sadaka mtu mmoja kuliko kukubali familia yake iuwawe, bila kuelewa kwa kumtoa Mzee Ngesa,kungesababisha mamia na maelfu ya watu kufa!
*****
“Una nusu saa,nahitaji umlete Uwanja wa Ufi”
“Lakini in..”
“Maisha ya mkeo na watoto wako,yapo mikononi mwako”
Walikuwa ndani ya gari,mbele yao kuna kifaa maalum!Kila alichozungumza RC Bashonga walikisikia na walishajua baada ya hapo,makutano yao yangekuwa uwanja wa Ufi.Ndio Maana Dustan akawasha gari kwa haraka, Jenipha akakoki bastola yake na safari ya kuelekea uwanja wa ufi usiku huo kuanza mara moja,ilikuwa ni lazima wazuie swala hilo lisitokee.
“Jenipha,nina wazo”
Dustan akasema huku macho yake yakiwa mbele,ameshika usukani anaendesha gari kwa kasi ya ajabu.
“Wazo gani?”
“Inabidi tujuwe kwanza ni wapi Derick na Daphine walipo”
“Kivipi?”
“Tuhakikishe tunaenda nao,kumzuia Bashonga asiondoke itakuwa kazi bure!Hatutoweza kumpata Karanje”
“Wazo zuri”
“Nina jambo lingine”
“Lipi?”
“Mtumie Rais Leslie,hiyo sauti”
Dustan,akazidi kukimbiza gari,alivyofika mabibo akapunguza kasi sababu walikuwa tayari wanakaribia kufika!Alivyofika umbali wa mita mia mbili,akaweka gari kando hapo alichukua darubini yenye lenzi kali na kuiweka machoni,bado hakuona kitu chochote kile!Akatulia kidogo,wakasubiri mpaka dakika kumi zilivyopita ndipo wakaona taa za gari zinamulika,hapo Dustan akatoa darubini na kutizama akaona Diffenda ya polisi,dakika mbili mbele akasikia mlio mkubwa wa Helkopta!
“Jenipha”
Dustan,akaita na kumpa DarubiniJenipha nayeye akatizama mbele!
“Shiit”
Alichokiona kilimuogopesha sana,Rc Bashonga alikuwa anashuka kwenye helkopta,anamuangalia Mzee Ngesa!
“Jesus Christ”(Yesu Kristo)
“Nini?”
“Tizama”
Dustan akachukua nayeye Darubini,akamuona RC Bashonga kashika bastola kamuwekea kichwani askari aliyemtorosha Mzee Ngesa,bila kufanya chochote askari akadondoka chini baada ya kupigwa risasi ya kichwa,hakuna mtu aliyesikia sababu bastola hiyo ilikuwa na kiwambo cha kuzuia sauti isitoke.
Hapo ndipo Dustan,akatupa darubini chini na kuchomoka kama mkuki akiikimbilia Helkopta kabla haijapaa angani,mapanga boi ya helkopta yalizidi kuzunguka kwa kasi na tayari helkopta ilianza kupaa angani,Dustan akazidi kukimbia Helkopta ikaanza kuelekea juu akawa tayari ameikaribia,akazidisha kukimbia kwa kasi,akakanyaga kichuguu na kunyoosha mikono yake hewani kama ngedere,akaruka na kuyashika machuma ya chini ya helkopta ambayo tayari ilikuwa inazidi kupaa angani,miguu yake ikawa inaning’inia anajaribu kujiweka sawa.
“Tuku tuku tuku”
Helkopta ilizidi kupaa angani,ikiwa tayari Dustan amedandia.
Ndani ya gari alikuwa Jenipha,kila kitu alikishuhudia kwa macho yake mawili.Dustan alikuwa ameshika chuma la Helkopta ananing’inia hewani, kumaanisha kwamba asipokuwa makini atadondoka na kupasuka vibaya sana,hata hivyo ilikuwa ni lazima atoe msaada kwa kupiga simu akiamini kwamba Dustan, asingeweza kufanikisha operesheni hiyo mwenyewe,bila kujiuliza chochote akapiga gia na kulirudisha gari kinyume nyume kama mwendawazimu,shingo yake kaigeuza kwa nyuma,alivyokaa vizuri akazungusha usukani na kupiga gia kwa haraka,namna gari ilivyozunguka ilitisha. Isingekuwa utaalam na utundu katika magari basi gari hilo lingeingia ndani ya mtaro wa maji na kupinduka,Jenipha hakutaka kupunguza mwendo. Kwa kasi aliyokuwa nayo,akatoa simu yake mfukoni huku mkono wake mmoja ukiwa juu ya usukani.Kwa umakini sana, akaanza kusaka namba fulani mpaka alipofikia jina la Masud Ndunguru,huyu ndiye mwanamme ambaye aliamini kwa wakati huo, angekuwa karibu na Rais Leslie,hapohapo akapiga simu na kuiweka sikioni ambapo ilianza kuita, haikuchukuwa muda mrefu ikapokelewa.
“Masudi,upo wapi?”
Jenipha akauliza swali baada ya simu kupokelewa, macho yake yote yalikuwa mbele makini ili asije kusababisha ajali.
“Ikulu”
“Upo na Rais Leslie”
“Ndio”
“Kuna kitu nakutumia,tafadhali.Mjulishe mwambie asikilize”
“Kitu gani?”
“Subiri”
Alichokifanya Jenipha ni kuingia kwenye simu yake na kutuma sauti, wakati huohuo.
“Kingine,Dustan,anahitaji msaada.Yupo kwenye helkopta mpigie simu Captain Roi aangalie kwenye rada zake kis..”
“Dustan,yupo chini ya ulinzi.Anatafutwa”
“Masud,nakuomba.Fanya nilichokwambia”
“Sawa”
“Okay”
Safari ya Jenipha ilikuwa ni kunyoosha moja kwa moja mpaka kwa Captain Roi,kamanda wa jeshi la polisi katika kikosi cha anga huyu ndiye angemsaidia kujua ni wapi Helkopta aliyokuwa Dustan ilipo,mbali na kutoa maagizo hayo aliamini swala hilo lisingekuwa na uzito, pasipo yeye kuwepo naye karibu,ndiyo maana alikimbiza gari kama mwendawazimu mpaka Kipawa,ambapo hapo alikunja moja kwa moja mpaka uwanja wa ndege mwalimu Nyerere,kitendo cha kupiga breki aliteremka bila kufunga mlango wa gari na kuanza kukimbia moja kwa moja mpaka chumba maalum,hapo alitoa kitambulisho chake cha usalama wa taifa.Akapita sababu alisema ni dharura!
“Roi”
“Jenipher,nimepewa ujumbe wako hapa.Ndio naufanyia kazi”
“Umefikia wapi?”
“Ndoo najaribu kupitia hapa,kwenye satelite.Hawa hapa”
“Naomba Helkopta”
“Una maana gani?”
“Nahitaji kwenda”
“Lazima uwende na escota”
“Muda unakwenda”
“Subiri kidogo”
*****
Kitendo cha Helkopta kutingishika kidogo kilimfanya Rubani, ahisi ni lazima kuna kitu,ni kweli alikuwa sahihi sababu Dustan ndiye aliyedandia akiwa kwenye chuma moja amejishika vizuri,chini kulikuwa ni mbali sana sababu Helkopta hiyo ilizidi kupaa juu angani.Ndani ya Helkopta alikaa Mzee Ngesa na Rc Bashonga, kushoto kwao kulikuwa na mwanamme mwingine mweusi,huyo ndiye alipewa jukumu la kusimamia zoezi hilo zima la kuwafikisha Mzee Ngesa na Rc Bashonga Arusha,ilikuwa ni furaha sana kwao, sababu mamia na maelfu ya watu, walikuwa ni lazima wateketee!Mbali na hapo, mwanamme huyu ambaye alikuwa mlangoni, alihisi kitu sababu helkopta ilitingishika,alivyochungulia dirishani akaona miguu ya mtu inaning’inia hapo ndipo aliposhika bastola yake vizuri na kuufungua mlango ili ampige risasi Dustan, bila kuelewa kwamba Mwanamme huyo naye alikuwa makini akisubiri mlango ufunguliwe,ilikuwa ni hatari kubwa sana lakini alijishika kwa umakini wa hali ya juu,kitendo cha Mwanamme mwenye bastola kutoa mkono wake Dustan,akajiweka vizuri miguu yake akaipandisha kwenye chuma na kuiviringisha vizuri,akaushika mkono wa mwanamme huyo na kumvuta nje.Kilichotokea hapo kilikuwa ni kitu cha kutisha sana.Rc Bashonga, hakuamini baada ya kuona mwanamme huyo kavutwa na kudondoka nje,kumaanisha kwamba ni lazima akifika chini awe amepasuka vibaya kama nyanya,kabla ya kufanya uamuzi wowote ule Dustan akawa ameingia alichokifanya ni kumvuta Rc Bashonga na kumpiga ngumi ya pua,alivyomuona anataka kutoa bastola, akamuwahi na ngumi ya shingo,Mzee Ngesa alivyojaribu kumpiga Dustan, akatulizwa na kifuti cha pua,Dustan akachukuwa bastola na kuwaweka chini ya ulinzi.
“Endelea na safari”
Dustan akasema huku akimuwekea bastola rubani kisogoni kwake,hiyo ilikuwa ni amri sio ombi.
“Kijana,unajiingiza kwenye matatizo makubwa,yaache haya mambo kama yalivyo”
Rc Bashonga alitia neno,akijifanya kumsikitikia sana Dustan,kuanzia hapo hakukuwa na mtu yoyote Yule aliyezungumza!
“Mr.Ngesa,Baba yangu alifariki mwaka 1992,nilikuwa mdogo sana!Nilimpenda baba yangu na alinipenda sana,tulikuwa maskini lakini alikuwa yupo tayari kufanya lolote ili kutetea haki yake.Nilijivunia sana kuwa na Baba kama yeye sababu tulikuwa marafiki.Alikuwa kada wa chama hiki tawala,alivyotaka kuhama wakamtishia kumuuwa.Hakukubali sababu kuna vitu aliviona haviendi sawa,alivyohama tu baada ya siku mbili.Ndipo akafariki dunia,niliumia nikasema ipo siku nitaliipa kisasi,Derick si……”
Maneno hayo alikuwa anazungumza Dustan,akisimulia hadithi ya kusisimua sana huku akimtizama Mzee Ngesa,helkopta ilizidi kusonga mbele na baadaye taratibu ilianza kushuka chini.
****
Derrick Ngesa, pamoja na Daphine walikuwa wakisubiri kifo chao,wapo mateka wamezungukwa na jeshi kubwa tena lenye silaha kali za moto!Mbele yao, amesimama Brigedia Karanje,mwanamme gaidi aliyetokea kuitingisha Tanzania na nchi jirani.Gaidi huyo alisakwa kama Osama Bin Laden,haikuwa kazi rahisi kumuweka mikononi mwao kwani alikuwa ana jeshi kubwa sana lenye kila aina ya mbinu za kutumia silaha.Usiku wa siku hiyo, walikuwa wakimsubiri Mzee Ngesa, pamoja na Rc Bashonga,mpango wao ulikuwa ni mmoja tu waendelee kuuwa watu, wakitumia sumu hiyo kali sana.Na baada ya hapo,ilikuwa ni lazima Daphine na Derrick Ngesa wauwawe,wakati akiisubiri Helkopta ifike mahali hapo,akili ya Ngesa ilikuwa ikifanya kazi kwa kasi ya risasi,alikuwa akitafakari namna ya kujikomboa.Akawatizama wanajeshi wengi waliokuwa mbele yao,akapiga hesabu za harakaharaka lakini akakosa jibu,siku zote mwanamme huyo huwa hakubali jambo kirahisi rahisi,hakutaka kufa kikondoo!
“Tuku tuku tuku”
Mlio wa Helkopta ulisikika kwa mbali,Walivyoangalia juu wakaiona.Brigedia Karanje akaitizama kwa makini na kuwaangalia wenzake, kuashiria ya kwamba tayari mambo yameiva hivyo wakae mkao wa kula na wajitayarishe kwa kazi iliyokuwa mbeleni,Helkopta ikazidi kushuka chini,huku vumbi likitimka kutokana na mapanga boi yake kuzunguka kwa kasi,ikatua taratibu mpaka chini kabisa na kutulia.Hakuna mtu yoyote aliyeweza kuona ndani sababu ya giza totoro lililokuwepo!Brigedia Karanje alikuwa anasuburi kwa hamu kubwa sana ili amuone mzee Ngesa,waanze kupanga mipango yao.Ndani ya sekunde mbili,mlango ukavutwa akatokeza mzee Ngesa lakini nyuma yake alisimama Dustan akiwa na bastola, amemuwekea kichwani kumaanisha kwamba wanajeshi wote watulie.
Ngesa alivyoona tukio hilo,moyo ulimdunda kwa nguvu,lilikuwa ni kosa kubwa sana la jinai Kwa Dustan kufanya hivyo kwani wanajeshi walikuwa wengi sana lakini ilibidi atulie ili ajuwe nini kingetokea!Brigedia Karanje,alimuangalia Dustan kwa dharau kubwa na kucheka japokuwa hakutegemea kuona tukio kama hilo mbele yake.
*****
Helkopta aliyopanda Jenipha,ilibeba wanausalama wanne!Wakiwa na bastola zao mikononi tayari kwa kumkomboa Dustan,haikuwa kazi yao lakini ilibidi watumie nguvu kubwa kufanya hivyo.Hata hivyo walikuwa wanafanya mawasiliano na jeshi la polisi Mkoani Arusha na wao walikuwa tayari wamewasha Diffenda zao kwa ajili ya ambush hiyo ambayo waliamini ingefanya jiji la Arusha litingishike.Diffenda kumi na moja, ziliondoka kutoka Usariva kwa kasi, zikiwa zimebeba maaskari tisini na mbili,wote wakiwa wameshika mitutu.Hiyo haikuwa ambush tena,bali ni vita kubwa sana!
“Shusha Helkopta chini,wasiliana na RPC Asenga!Waaambie sisi tunaanza kuingia kimya kimya,kila kitu tutawaambia”
Ilielekea Jenipha ndiye alikuwa kiongozi wa msafara huo sababu alitoa maelekezo wakiwa ndani ya helkopta,hakutaka kushuka karibu na wanajeshi, alichokifanya ni kumuamuru Rubani ateremshe Helkopta mbali kidogo umbali wa kilomita mbili,hivyo ndivyo ilivyokuwa.Helkopta ikatua!
“Kacha kacha”
Jenipha akakoki bastola yake na kuiweka kiunoni kwa nyuma,akaanza kutembea akiingia katikati ya miti huku akiongozana na wenzake,walitembea kwa umbali mrefu kidogo huku wakiangalia kifaa chao kidogo ambacho kiliwaongoza,hatimaye wakafika eneo la tukio,wanajeshi walikuwa wengi.Mbaya zaidi Dustan alikuwa amezungukwa na wanajeshi hao japokuwa alimuweka Mzee Ngesa, chini ya ulinzi.
“Nipe silensa”
Jenipha,akataka kiwambo cha kuzuia sauti ya bastola akapewa na kuanza kukifunga mbele ya bastola yake,alivyohakikisha kila kitu kipo sawa.Akaweka bastola vizuri kiunoni na kuchomoa kisu kirefu, kwenye kiatu chake,akatembea taratibu kwa tahadhari,akamvuta mwanajeshi aliyekuwa amesimama kihasarahasara na kumchoma kisu cha shingo,chuuup.Akamziba mdomo ili asipige kelele,akamvuta kando na kuendelea kumkaba mpaka alivyohakikisha ametulia.Akamsogelea mwanajeshi mwingine na kufanya hivyo hivyo.
“Kijana,weka bastola chini.Huoni upo peke yako?Weka silaha yako chini,panda Helkopta uondoke nakupa zawadi ya uhai.Hatuna shida nawewe”
Brigedia Karanje alizungumza huku akimuangalia Dustan,alisema hivyo akiwa ana uhakika ya kwamba kuna mwanajeshi mwingine anazunguka nyuma ya Dustan na kumpiga risasi afe!Ni kweli ilikuwa ni lazima Dustan afe sababu mwanajeshi mmoja alikuwa anazunguka taratibu akimtafutia saiti nzuri, akiwa na mtutu mkononi,alivyopata saiti nzuri akamlenga Dustan.
“Pyuuu pyuuuuu”
Katika watu waliokuwa makini ni mwanamke huyu Jenipha,macho yake yalikuwa waluwalu kwani tangu mwanajeshi huyo anamlia denge Dustan alimuona,ndiyo maana alimuwahi na kumpiga risasi mbili za kichwa, mwanajeshi akadondoka chini,Brigedia Karanje akageuka hapohapo akapokea risasi ya bega kutoka kwa Jenipha,hiyo ilimfanya adondoke chini!Hapo ndipo ambush, ikaanza na risasi zikaanza kurindima kila pembe.
Kilichosikika hapo ni milio ya risasi kila pembe,kila mtu alijificha sehemu inayomfaa kwake.Ngesa alivyoona hivyo hakufanya makosa,akajidondosha na kuanza kubiringika,akajificha nyuma ya mti mkubwa wa mbuyu!Hapo ndipo akawa ana kazi nyingine ya kujifungua kamba alizofungwa kwa nyuma.Haikuwa rahisi kwake kwani kamba zilifungwa barabara,alihangaika vya kutosha huku akishuhudia askari wanavyopigwa risasi na kudondoka na wanajeshi hao, waliokuwa na silaha kali za moto.Hakujali,alichotaka yeye mikono yake iwe huru kwanza ili atoe msaada,akahangaika hivyo hivyo,mwishowe akaamua kujikunja kunja na kuizungusha mikono yake, kupitia kwenye miguu ili itokeze kwa mbele,zoezi hilo lilikuwa gumu la lilifanya aumie misuli,akafanikiwa kuizungusha mikono yake kwa mbele,kwa kutumia mdomo akaanza kung’ata kamba!Hatimaye mikono ikaachia,akashika kamba na kuitupa kando,akatizama huku na kule akamuona Mwanajeshi mmoja wapo kashika mtutu,huyo huyo akamsogelea na kumpiga roba la nguvu kwa nyuma,kabla mwanajeshi huyo, hajafanya lolote akatulizwa na kifuti cha mbavu,kabla ya kufanya kitu kingine chochote, akachotwa mtama wa nguvu.Akachukua mtutu na kum-miminia risasi za kutosha,hapohapo akasimama nyuma ya mti na kuanza kazi ya kuwalenga wanajeshi, waliokuwa katika operesheni hiyo nzito!Akamuona Daphine yupo pembeni chini,anahangaika kujifungua kamba,akatambaa chini kwa chini na kumfikia.
“Subiri”
Ngesa akasema na kuanza kumsaidia Daphine,kufungua kamba alizokuwa amefungwa mikono yote kwa nyuma.
“Ahsante”
“Paa! Paaa! Paaaaa!”
Ilikuwa kidogo wapigwe risasi za vichwa bahati nzuri ikawa kwao,zikapiga mti.Hapo Ngesa akainua mtutu na kumshambulia mwanajeshi huyo, aliyekuwa kushoto kwao!Ilikuwa ni vita kubwa,iliyofanya milio ya risasi isikike kwa sauti kila pembe.Gari za polisi, zilikuwa zinapigwa makombora na kulipuka,askari walidondoka chini na kufa lakini hiyo haikumaanisha wakate tamaa na kusalimu amri.Diffenda nyingine za polisi sita zikafika askari wakaruka ardhini kama makomandoo huku wakirusha risasi.Wakati hayo yote yanaendelea,Brigedia Karanje alikuwa chini amepigwa risasi ya bega,anajiburuza kama nyoka ili akimbie!Akafanikiwa kuufikia mti mkubwa na kutulia hapo.
“Karanje yuko wapi?”
Lilikuwa ni swali kutoka kwa Daphine,anamuuliza Ngesa!Katika watu waliokuwa na usongo na jasusi huyo ni mwanamke huyu Daphine,ilikuwa ni lazima amuweke mikononi mwake, ikiwezekana amuuwe kabisa, kumbukumbu ya wazazi wake kuuliwa kinyama, ilimtesa kichwani kwake,ndiyo maana bila kupoteza muda akaanza kutizama huku na kule.Akamuona Karanje,yupo kwenye mti mkubwa ametulia.
“Ngesa,cover me”(Ngesa nilinde)
Ilikuwa ni lugha ya kivita, kumaanisha kwamba Daphine anataka kuvuka upande wa pili, hivyo Ngesa amlinde,hivyo ndivyo ilivyotokea kwani Ngesa alianza kupiga risasi upande wa Magharibi walipokuwa wanajeshi,Daphine akaanza kukimbia mpaka upande wa pili,ambapo huko alifika na kumuinua Karanje kwa juu,hakuuliza kitu zaidi ya kuanza kumshambulia mateke na ngumi zisizokuwa na idadi kamili.Mkono wa Brigedia Karanje ulikuwa na jeraha la risasi,anahisi maumivu makali lakini hiyo haikufanya ashindwe kujitetea,akajitutumua na kutupa ngumi lakini ilipita hewani baada ya Daphine kuinama,alivyotaka kurusha ngumi nyingine ikashindikana sababu Daphine aliidaka na kumzungusha kitaalam,akampiga kifuti cha tumbo.Brigedia Karanje alikuwa tayari amezidiwa kila alipojaribu kujitetea akashindwa.Mbaya zaidi mwanamke aliyekuwa mbele yake, anapambana naye,ndiye aliyemfundisha na kumpika katika swala zima la ndundi,kifupi kinyago alichokichonga mwenyewe kilianza kumtisha.
“Upo chini ya Ulinzi,piga magoti weka mikono juu”
Walikuwa ni askari watatu, waliofika na mitutu na mmoja kati yao alikuwa ni Dustan,akiwa makini na bastola yake ana usongo na Brigedia Karanje.
“Weka mikono juu piga magoti”
Brigedia Karanje hakujigusa kabisa,akabaki anawatizama askari hao kwa zamu.Akatabasamu kwa mbali.
“I only kneel to God and i don’t see him here”(Nampigia Mungu magoti peke yake na simuoni mahali hapa)
Hiyo ndiyo Sentensi aliyotamka Brigedia Karanje kwa dharau na kiburi chote,laiti kama Daphine angekuwa ana silaha mkononi angemmaliza hapohapo, sababu alimuangalia Dustan kwa macho makali yaliyosema ‘fyatua risasi’.Kwa kuwa waliambiwa wampeleke Karanje akiwa hai,hawakuwa na uwezo wa kumpiga risasi wamuuwe,walichokifanya ni kusogea karibu na kumfunga pingu kwa nyuma wakamuweka chini ya ulinzi.
“Mnajisumbua,mkiniua hamtoweza kujua ni wapi mabomu mengine yalipo.Ile ni sumu kali sana”
Brigedia Karanje alizungumza maneno ya kutisha huku akiwa amefungwa pingu kwa nyuma, hiyo ilimfanya Ngesa amtizame kwa macho ya hasira,akamsogelea mpaka mbele yake kabisa.
“Huu ndio mwisho wako,labda nife mimi”
Ngesa,akazungumza lakini kabla ya kuongeza neno lingine zaidi, akamuona Dustan amewekewa bastola na kuwekwa chini ya ulinzi.
“Vipi?”
Ngesa akauliza baada ya kufika eneo hilo.
“Yupo chini ya ulinzi”
“Kwa kosa gani?”
“Uhaini,Ngesa kaa mbali na hili”
“Haiwezekani”
“Ni amri,acha tufanye kazi yetu”
Kilichofuata hapo ni Dustan,kuingizwa ndani ya Diffenda akiwa na pingu mkononi Jenipha,Daphine pamoja na Ngesa wakabaki wanamuangalia kwa huruma.Hawakuwa nala kufanya,zaidi ya kuapia kwamba wangekuwa naye bega kwa bega mpaka anakuwa huru na baadaye washeherekee ushindi.
Mh Rais alikuwa mwenye furaha kubwa sana baada ya kusikia kwamba Brigedia Karanje yupo chini ya ulinzi,akapata amani kabisa.Akataka kuzungumza na Ngesa kwenye simu,hapohapo OCD Peter Ngosha,akamsogelea Ngesa na kumpa simu.
“Zungumza na Rais Leslie,yupo kwenye laini”
“Ahsante”
Ngesa akachukua simu na kuiweka sikioni.
“Mheshimiwa Rais”
“Derrick Ngesa,ahsante kwa kila kitu.Nchi yangu ya Tanzania,haitokusahau kabisa kwa juhudi na jitihada zako zote,hakika wewe ni mfano wa kuigwa”
“Ahsante Mheshimiwa Rais”
“Naomba wewe na timu yako nzima,kesho mje Ikulu”
“Sawa Mheshimiwa Rais”
“Ahsante kwa kila kitu.Tusahau yaliyopita,sasa tushikamane na kulijenga taifa letu la Tanzania”
“Sawa Mheshimiwa Rais”
Simu ilivyokatwa akamtizama Daphine pamoja na Jenipha,akawapa mkono na kuwaambia alichoambiwa na Rais Leslie.
“Ahsanteni”
“Kwa kitu gani?”
“Kwa kila kitu”
“Nawewe tunashukuru sana”
Baada ya mazungumzo hayo,wakasikia mlio wa Helkopta.Hapohapo ikatua,hawakuwa na sababu ya kuuliza kitu kingine, zaidi ya kupanda sababu ilitoka usalama wa Taifa wote wakaingia ndani,wakafunga mlango.Helkopta ikaanza kupaa angani!
****
Kukamatwa kwa Brigedia Karaje,gaidi aliyesumbua nchi ya Tanzania kwa miaka mingi ndiyo jambo lililokuwa ‘topic’katika kila gazeti siku hiyo,kwenye vyombo vya habari walitangaza habari hizo!Hapo kidogo kasi ya maandamano ikapungua kwa kiasi chake,wananchi wakawa na amani kabisa sababu walijua ni jinsi gani mwanamme huyo alivyokuwa hatari kwani aliua maelfu ya watu wengi sana,akachafua jina la nchi ya Tanzania iliyosifika kwa kuwa na amani na upendo!Kilichokuwa kinasubiriwa siku hiyo ni Rais Leslie,atoe hotuba yake!
“Wamemkamata”
“Nani?”
“My Dad”
“Naelewa,you should calm down”
“Nani amehusika kwenye hili?”
“Jeshi la Tanzania”
“Wataenda kumuuwa, I know.Nataka kufanya kitu”
“Kitu gani?”
“Kabla hawajamuua”
“Sijakuelewa”
“Ni vigumu sana kunielewa,Dennis”
Yalikuwa ni mazungumzo marefu yaliyofanyika ndani ya chumba kidogo.Kilichokuwa na wanaume wanne tu,katikati ya mji wa Entebbe nchini Uganda.Mwanaume aliyekuwa anazungumza kwa kujiamini alifahamika kwa jina la Aron Karanje,mtoto pekee wa Brigredia Karanje.Kukamatwa kwa baba yake na kuwekwa chini ya ulinzi kulimfanya ashindwe kupata usingizi wala kufanya kitu chochote kile,aliwaza ni jinsi gani atalisumbua jeshi la Tanzania na kuwapa adhabu kubwa ambayo ingewafanya wamuachie baba yake huru, hata hivyo alipanga kulisumbua jeshi la Tanzania na mtu yoyote ambaye alihusika na kukamatwa kwa Baba yake.Haikuwa kazi kubwa kwake,kutokea nchini Uganda akawatuma vibaraka wafuatilie zoezi hilo.Ambapo baada ya siku tano, akawa amepata orodha ya majina ‘DAPHINE,DERRICK NGESA,DUSTAN,JENNIPHA’ Pamoja na majina mengi ya wana usalama.
“Itabidi nianze na mmoja baada ya mwingine!”
Aron Karanje,akasema akiwa na ujasiri mkubwa uliosindikizwa na hasira huku akibana meno yake!
****
Brigedia Karanje,alikuwa ana kesi kubwa ya kujibu.Mauaji aliyoyafanya ilitosha kabisa ahukumiwe kifungo cha maisha ama kunyongwa,lakini wasingeweza kufanya hivyo bila kujua mabomu mengine ameyahifadhi wapi,aliulizwa kila aina ya maswali lakini hakuwa tayari kutoboa siri hiyo nzito,ambayo pia aliamini angesema huo ndiyo ungekuwa mwisho wake kifupi siri hiyo ndiyo ilikuwa inamuweka hai.Ni muda mrefu sana Ngesa aliomba kuingia ndani ya chumba hicho ili amuhoji lakini walimkatalia katukatu,walimuelewa Ngesa alivyokuwa mwenye hasira za waziwazi.
“Ngesa,hatuwezi kukuruhusu.Tuache tufanye kazi yetu utaharibu ushahidi”
“Kwa kumuhoji hivyo,hatoweza kusema chochote.Namfahamu Karanje,tuna historia kubwa sana”
“Hap..”
“Anachosema Ngesa,ni sahihi mkuu”
Mwanausalama mmoja aliyefahamika kwa jina la Adam Ingo, akaingilia mazungumzo hayo.
“Hatuwezi kumruhusu,sio mwana usalama”
“Lakini ana mchango mkubwa sana,hata Rais Leslie anajua.Tumpe nafasi hiyo mkuu”
Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa taifa,hakuwa nala kuongeaza.Akakubali kila kitu!Ngesa,akawa amekabidhiwa mamlaka,alichokifanya ni kugosha vidole vyake kwanza,akatembea mpaka mlangoni ambapo ulifunguliwa,akasimama mlango ukafungwa!Mbele yake alikuwa amekaa Brigedia Karanje.
“Ngesaa!”
Brigedia Karanje,akaita kwa mshangao!Huku akiwa ana uwoga fulani ndani ya moyo wake, sababu hakutegemea kumuona Ngesa ndani ya chumba hicho,hata hivyo alishaelewa nini kipo mbioni kutokea kama asingeonesha ushirikiano.
“Derrick Ngesa,kabla ya kufanya chochote tambua kwamba kuna mabomu yenye uwezo wa kuuwa mamia na maelfu ya watu hapa Tanzania,fikiria hilo!”
Brigedia Karanje alianza kujihami kwa kuongea maneno hayo.Ngesa hakusema chochote akabaki anamtizama kwa hasira kali.
“Mbali na hapo,huwezi kuyapata.Na sipo tayari kusema chochote kile”
“Umemaliza?”
Ngesa akauliza huku akimsogelea karibu zaidi,wanausalama walikuwa nje wanaangalia kupitia kioo kikubwa,kila kilichoongelewa walikisikia.
Kila kitu hakikuwa vizuri,wanausalama wote walihaha wakitaka kujua ni wapi mabomu yenye sumu kali yalipo,hiyo ilimaanisha ni lazima wafanye juu chini ili Brigedia Karanje azungumze na kutoboa siri hiyo ambayo hata yeye kwake,halikuwa jambo rahisi.
Alikuwa yupo tayari kufukiwa kaburini na siri hiyo nzito lakini sio kuzungumza,mbali na hapo alielewa fika kwamba uhai wake upo kwenye siri hiyo,kitendo cha kutaja ni wapi mabomu hayo yenye sumu kali yalipo, huo ndio ungekuwa mwisho wake duniani.
Kila mtu aliyeingia ndani ya chumba hiko,ili kuhoji na kumuuliza maswali alishindwa kutoka na jibu la kueleweka,brigedia Karanje aliwajibu nyodo na kugoma kuzungumza chochote kile.Hapo ndipo Derrick Ngesa akapewa ruksa ya kuingia ndani ya chumba hiko ili amuhoji.
Jambo hilo ndilo alikuwa akilisubiri kwa muda mrefu sana,alivyoingia ndani ya chumba hiko Brigedia Karanje alionekana kutetemeka na kuzungumza hovyohovyo,alichokifanya Ngesa ni kumtizama na kumsikiliza mpaka amalize,akasogea karibu kabisa na kukaa juu ya kiti huku akimtizama machoni kwa hasira,akayabana meno yake.
“Nadhani unajua,tunazungumzia sumu ya aina gani Ngesa?Mamia na Maelfu watakufa usipoangalia,fikiria hilo jambo kabla hujaamua kufanya chochote,nikifa hamtopata kitu chochote kile”
Brigedia Karanje,alitokwa na maneno mengi siku hiyo.
“Unataka nini?”
“Nahitaji Immunity,iliyosainiwa na Rais Leslie,nikitoka hapa nisihukumiwe na….”
“Hilo haliwezekani,mabomu yako wapi?”
Ngesa akamkatisha na kuuliza na swali juu yake,macho yake tayari yalikuwa mekundu kumaanisha kwamba muda wowote angemvaa Brigedia Karanje.
“Nimekwambia nachokitaka”
“Mabomu mengine yako wa….”
Hapo hakuweza tena kuuliza,kwa kasi ya umeme Ngesa akasimama wima na kumuinua Brigedia Karanje kwa kabali ya shingo akamsogeza mpaka ukutani,kwa kuwa Brigedia Karanje alikuwa ana pingu mkononi,hakuweza kufanya chochote,hapo ndipo Ngesa alipokuwa kama mbogo,akampiga ngumi tatu za mbavu,alivyoinuka akampiga kichwa cha pua,akamkaba kwa nguvu.
“Ule sio utaratibu wa kuhoji,mtoeni haraka sana”
Ilikuwa ni kauli kutoka kwa Mkurugenzi wa Usalama wa taifa Ramadhan Mpelembe,akiwa kwenye kioo anatizama kila kitu,hapohapo mlango ukafunguliwa wakaingia wanaume sita na kumtoa Ngesa wakitumia nguvu kubwa sana kwani koo la hewa la Brigedia Karanje liling’ang’aniwa.
Kitendo cha kutolewa kilifanya Brigedia Karanje akohoe mfululizo kama mtu aliyepaliwa na maji ya kunywa.
“Ngesa,tuliaa.Kaa hapo”
“Noo,.niachieni.Mnataka kujua ukweli ama hamtaki?”
“Kaa hapo nimesema”
“Nataka kuongea na Rais Leslie”
Hasira za Ngesa zilikuwa zimezidi kipimo chake.
***
Aron Karanje hakuwa sawa,kichwa chake kilimfikria Baba yake mzazi na namna atakavyomkomboa.Alielewa kabisa jambo hilo, halikuwa rahisi hata kidogo kwani alitambua fika ni kwa jinsi gani baba yake alivyokuwa akiwindwa mchana na usiku ili akamatwe lakini walishindwa.
Kwa mabaya yote aliyokuwa anafanya baba yake kwa kuwauwa watu na mengine mengi, aliamini kwamba nyuma ya kila kitu kuna sababu kubwa kwani baba yake asingeweza kufanya vitu kama hivyo sababu miaka ya themanini alikuwa ni mwanajeshi mwenye cheo kikubwa serikalini,akiitumikia nchi yake!Akajua kabisa ni lazima kuna mambo mabaya yalifanywa na serikali ya Tanzania, ndiyo maana akaamua kufanya mambo ya kinyama.
Kukamatwa kwa baba yake,kulimfanya ahangaike usiku na mchana asilale wala kufanya kitu chochote kile,hakuwa gaidi wala mwenye mafunzo yoyote yale ya kivita,hiyo ilikuwa kazi nyingine kubwa kwake.
Kwa kuwa baba yake,alimpa walinzi kazi hiyo kidogo ikampa ahueni.
“Tushapata majina yale,sasa tufanye nini?”
Aron Karanje,akamuuliza mlinzi mmoja wapo aliyefahamika kwa jina la Nabulele.
“Sio jambo la kukurupuka Aron”
“Ningetaka kukurupuka,nisingekuuliza”
“Nina jambo,nataka kukwambia”
“Nakusikiliza”
“Si unahitaji baba yako wamuachie huru?”
“Ndio”
“Jambo rahisi,tuanzishe tamasha la watanzania.Tuliite Bongo party,watanzania wote wanaoishi huku nchini Uganda,najua wanapenda kula bata”
“Baada ya hapo?”
“Tutawaweka mateka,hapo tutampigia simu Rais Leslie”
“Then?”
“Akikataa,tunaua mmoja baada ya mwingine!Raisi Leslie ni dhaifu sana,wakati tunafanya hayo,tunamtuma mtu aende Tanzania kimya kimya kuwashikilia hao wanaohusika kumkamata baba yako,kifupi tunaua ndege wengi kwa jiwe moja”
Kwa maneno ilikuwa rahisi lakini haikuwa rahisi kama walivyodhani kwani walijua fika baada ya hapo,wanaenda kupambana na jeshi la Tanzania,hiyo ilimaanisha vichwa vya habari vingewazungumzia.
Aron Karanje,alikuwa tayari kwa lolote lile ili baba yake awe huru, ghafla roho ya kinyama ikamuingia,katika maisha yake hakuwahi kuuwa hata mjusi lakini aliamini yupo mbioni kuuwa binadamu wenzake.
“Sawa,wazo zuri.Organize party,waambie hakuna kiingilio.Watanzania wanapenda sana vya bure”
“Okay,consider it done sir”
Jambo hilo lilipitishwa,mikakati ikapangwa siku iiliyofuata wakaanza kuchapa vipeperushi kwamba kutakuwa na tamasha kubwa, litakalo wakutanisha watanzania wote wanaoishi nchini Uganda,wanamuziki maarufu kutoka ndani na nje ya nchi, watakuwepo.Kwa kuwa ilikuwa ni habari ya kula bata, ikasambaa kwa kasi sana.Wanafunzi waliokuwepo Jinja,Kabale,Entebbe na Mukono, wote walipanga kujikusanya jijini Kampala, ili kuwapagawisha zaidi tamasha hilo lilitangazwa kwamba ni bure.
Vijana wengi walipania kwenda ili wakutane na mademu,mabinti warembo walitafuta nguo nzuri siku hiyo wakienda wawafunike wenzao, bila kujua kwamba walikuwa wanakifuata kifo.
Vyuo vikuu vya nchini Uganda kama Makerere,Kyambogo,UCU,K.I.U na Cavendish University, ndivyo ambavyo wanafunzi wengi wa kitanzania walisomea humo,taarifa hizo zilikuwa rahisi kuenea kutokana na utandawazi kukuwa,magrup ya WatsApp yalifanya kazi yake,kila kona ya vyuo vikuu habari iliyosikika ni ‘Bongo Party’ mabango yalibandikwa kila mahali.
“Tayari,naona kazi inaenda vizuri sasa”
Ripoti ikafika kwa Aron Karanje,siku hiyo akiwa mjini Entebbe kwenye makazi yake.
“Nimekubali”
“Wanazidi kutumiana taarifa, kwenye meseji za Watsap”
“Umejuaje?”
“Kila grup la chuo kuna vijana wangu,wananipa taarifa na ninavyokwambia hapa nipo kwenye grup la wanachuo la Makerere”
“Idadi ya wanafunzi wangapi watakuwepo?”
“Zaidi ya mia tano”
“Good,ukumbi ule utatosha?”
“Yes,Galaxy unabeba zaidi ya watu elfu moja kuna eneo kubwa sana.Tutaomba nafasi pia kwenye basement wana ukumbi wa chini vilevile”
“Vijana wa kazi,washaandaliwa?”
“Kazi gani?”
“Watakaoteka?”
“Ndio,kuna vijana shupavu wataingia kesho kutoka Sudan”
“Kazi nzuri,mambo yanaenda kuwa mepesi sana”
“Kila kitu kitakuwa sawa”
“Nenda kwenye redio zote,tangaza hilo tamasha.Weka msisitizo,nadhani litaleta uzito pia”
“Ondoa shaka Aron”
Hilo lilimaanisha utekelezaji uanze mara moja,pesa zikamwagwa katika vyombo vya habari mbalimbali kama magazeti,redio na televisheni kifupi ‘Bongo party’ilikuwa ndio habari ya mjini.
Kila mwanafunzi akawa ameipania,waganda wanaosoma vyuoni pia wakaona wivu wengi wao wakatamani kuzamia na kujifanya watanzania ili wasipitwe na disco hilo kabambe,shamrashamra zikawa nyingi.
Siku moja ikabaki ili parti hiyo ifanyike katikati ya Jiji la Kampala,hiyo ndiyo siku ambayo Opoka na kundi lake waliwasili wakitokea nchini Sudan,wakapokelewa jijini Entebe na kupelekwa mpaka anapoishi Aron.
Kwa kuwatizama tu,walikuwa wanaume kwelikweli,weusi tii na hawakucheka hiyo ilitosha kabisa kwa Aron kuwaamini,kila kitu kwake kikaonekana kuwa chepesi mbele ya safari.
Kwa nchi kama Uganda,haikuwa vigumu kutafuta silaha, walichokifanya ni kuzungumza na jeshi la polisi,wakatoa hongo ili wapewe silaha za moto,walitoa pesa nyingi sana hata hivyo kwa wakati huo pesa kwao hazikuwa kitu kabisa,ndani ya masaa thelathini na saba kila kitu kikawa kimepangwa.
****
Kitu walichokitegemea ndicho kilichoenda kutokea,kama wanafunzi wangeambiwa kuna tamasha la dini wasingejitokeza kwa wingi namna hiyo, lakini kwakuwa walielewa wanachuo wengi hupenda bata, ndiyo maana wakaandaa disco,wanafunzi wa vyuo mbalimbali walikuwa wengi nje ya ukumbi wa galaxy,wasichana walivaa vimini laiti kama wazazi wao wangeona namna walivyovaa wasingeamini.
Wavulana walivaa herein masikioni na ‘jeans’ zilizochanika wakawa kama machekibobu,kila mtu akiwa mwenye furaha kubwa sana.
Mmoja mmoja akaanza kuingia ndani, ambapo kulikuwa na mziki mkubwa,kilichowapagawisha zaidi ni Dj kupiga nyimbo za Kitanzania ambazo kwa muda mrefu walizimisi,mziki ulikuwa mkubwa,aliyepita nje ilikuwa ni vigumu kusikia sababu kulikuwa na mitambo maalum iliyoitwa ‘soundproof’wakiwa katika starehe ya muziki saa saba ya usiku,Opoka na timu yake wakawasili,gari tatu zikapaki nje ya ukumbi.Wakauzunguka hapohapo kisha wengine kuingia ndani,kitendo walichokifanya ni kuzima mziki ghafla.
“Tulieniii”
Sauti,nzito kidogo ikasikika kutoka katika kila pembe ya spika kwani mtu huyo alishika maiki.
“Aaaaah,unazogoa zaa wapiii hizo baabuuuu go to hell,weka muzikiii”
Wanafunzi,walikasirishwa na kitendo hiko wengi wakidhani mwanamme huyo amelewa.
“Paaaaaaaaa!”
Ulisikika mlio mmoja wa risasi,mwanafunzi mmoja aliyekuwa mbele anaropoka,akadondoka chini baada ya risasi kumfikia kichwani damu zikaruka, huyo akawa wa mfano,hapohapo akafyatua risasi nyingine hewani na kuwaamuru wanafunzi wote wakae kimya.
“Wote laleni chini,mkifuata nayosema mtatoka salama, vinginevyo mtakufa”
Ilikuwa ni kauli ya kutisha,wanafunzi wote waliogopa wakalala chini, kila mmoja wao akisali, sala yake ya mwisho.
***
Jasho jembamba lilimtoka Rais Leslie akiwa ofisini kwake,ndani ya Ikulu.Simu aliyopigiwa ilimtisha na ilizidi kumfanya achanganyikiwe zaidi.Wanafunzi wa kitanzania waliokuwa nchini Uganda,zaidi ya mia tano walikuwa mateka na watatu walikuwa tayari wameuwawa kumaanisha kwamba asingefuata wanachokitaka basi wanafunzi wote wangekufa kikatili na ilikuwa wazi kabisa kwamba mwanaume aliyetoka kumpigia simu hakuwa mtu wa masihara,ndiyo maana akamtumia picha ya maiti za wanafunzi zilizokuwa chini.Akiwa katika hali ya kutoelewa ni hatua gani achukuwe akamuita mshauri wake Mr.Kafuto Kayaga!
“Kaa hapo Mr.Kayaga,kuna tatizo kubwa sana”
“Lipi Mheshimiwa Rais?”
Bwana Kayaga,akauliza kwa shauku kubwa la kutaka kujua ni kitu gani kinamsumbua Rais Leslie,sababu alionekana kama mtu mwenye wasiwasi mkubwa sana.
“Nimepigiwa simu kutoka Uganda,kuna wanafunzi wa kitanzania wametekwa”
“Whaaaaat?”(niniii)
“Watatu wameuwawa kwa kupigwa risasi”
“My God,kwanini?”
“Wanamuhitaji Brigedia Karanje,lakini pia wanamuhitaji sana Ngesa”
Ukimya ukatokea wa kama sekunde tano nzima,Rais Leslie akazidi kufafanua zaidi kwamba wanahitaji Brigedia Karanje, awe huru na Ngesa wamsafirishe nchini Uganda,kumaanisha kwamba walitaka kumuua.
“Wanataka kumuua Ngesa?”
“Nina uhakika huo”
“Mheshimiwa Rais,kumbuka kuna wanafunzi wengi kule wapo mateka”
“Nadhani unaelewa,nini maana ya kuwapa Brigedia Karanje”
“Ndio”
Ulikuwa ni mkutano wa watu wawili lakini mzito mno,kila mtu alikuwa mzito kutoa maamuzi, mwisho wa siku akaitwa Mkurugenzi wa usalama wa Taifa bwana Ramadhan Mpelembe ili atoe mchango wake,yeye hakuwa ana longolongo akashauri atolewe Ngesa, akauliwe ili wanafunzi zaidi ya mia tano waachiwe huru.
“Mh Rais,huo ndio uamuzi unatakiwa uchukuwe kwa sasa ili kuwatuliza makali.Bado tunamuhoji Karanje ni wapi mabomu yalipo.Nina uhakika atasema ni wapi yalipo”
Mbali na Mkurugenzi wa usalama wa taifa kusema hivyo lakini nyuma ya kila kitu alikuwa ana bifu na Ngesa,alikuwa ana wivu, alielewa kwamba muda wowote cheo chake kingepinduliwa na Ngesa kuchukuwa nafasi yake, hiyo ni kutokana na Rais Leslie kumpa kipaumbele.
“Mheshimiwa Rais,wapigie simu waambie tutawapa Ngesha kisha baadaye Karanje”
Haikuwa rahisi kwa Raisi Leslie kukubali lakini kishingo upande alikubali hivyohivyo,moyo ulimuuma kumtoa sadaka Ngesa lakini hakuwa na jinsi.
“Sawa,nitawapigia simu”
“Naelewa ni kwa namna gani unaumia,lakini nina amini ni maamuzi mazuri sana Mheshimiwa Rais”
“Tumwambie ukweli ama tutafanya utaratibu gani,kumpeleka?”
Lilikuwa ni swali kutoka kwa Rais Leslie akitaka kujua, mbinu watakazo tumia kumchukuwa Ngesa na kumshawishi.
“Tukimwambia,naelewa atatoroka.Hatutomwambia,tuachie sisi tutajua cha kufanya”
“Kuweni makini”
“Usijali,Mheshimiwa Rais”
“Mtaniambia kinachoendelea”
****
Pembeni yake,alikaa Jennipher.Wako barabarani ndani ya gari wanaelekea Masaki,nyumbani kwa RC Bashonga kwa lengo la kumuhoji mkewe kama anajua chochote kile au aliwahi kusikia fununu juu ya mabomu hayo yenye sumu yalipo,Jenipha alikuwa makini nyuma ya usukani akili yake inawaza mambo chungumzima,alijiona msaliti kwa kitendo anachoenda kukifanya.Moyo ulimuuma lakini hakua na jinsi, ilikuwa ni lazima afate oda kutoka kwa wakuu wake wa kazi,waliomuamuru afanye hivyo.
Mpango waliopanga ulikuwa kabambe na waliamini ni lazima wangemuweka Ngesa chini ya ulinzi kabla ajashtuka kisha baada ya hapo wamsafirishe mpaka nchini Uganda ili kunusuru maisha ya wanafunzi, wasiokuwa na hatia,nyuma ya mpango huo kulikuwa na wanausalama kumi na mbili ambao walitegesha magari yao Mlimani City,wakiwa na silaha za moto ilikuwa ni lazima Ngesa atekwe kiakili, vinginevyo ingekula kwao sababu walielewa huyo ni mwanamme wa aina gani wanaye enda kukabiliana naye.
“Ngoja tupite huku,naona huko kuna foleni”
Jenipha alisema hivyo,baada ya kufika Mwenge Rufungila, niya yake ikiwa apite Mwenge Mlimani City ili wanausalama wavamie gari lao kisha wamchukuwe Ngesa.
“Sawa,una uhakika tutamuwahi huyo mwanammke?”
“Yes,yupo.Anatusubiri,mimi niliongea naye”
“Okay,ongeza mwendo tuwahi”
Ngesa alikuwa kwenye giza nene,haelewi chochote wala hakua ana wazo ya kuwa anaenda kukamatwa ili auwawe,akiwa katika kutafakari, mlio wa simu ukamshtua akaitoa kutoka mfukoni ili ajuwe ni nani,alivyoangalia akaona ni namba ngeni,akatafakari kwa muda na kupokea.
“Ngesa,unaongea na Rais Leslie,usitaje jina langu.Nisikilize kwa makini….”
Upande wa pili wa simu ulisikika,Rais Leslie alikuwa kwenye laini akiongea kwa sauti ya chini, hiyo ilimfanya Ngesa abadili sikio, akaitoa sikio la kulia na kuiweka simu sikio la kushoto.
“Yes”
“Wanaenda kukuteka ili wakupeleke Uganda wakuuwe,fanya juu chini utoroke.Nenda popote pale salama kisha nipigie simu.Usimwambie mtu kama tuliwasiliana”
“Mzee naona kama umekosea namba,mimi sio Juma…”
Ngesa,akajiongeza ilibidi azuge ili Jenipher asielewe kitu chochote kile,alivyokata simu aliiweka mfukoni na kumuangalia Jenipher kwa umakini akatizama mbele,umbali wa kama mita ishirini kulikuwa na mataa,akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya umeme.Gari lilivyofika kwenye mataa,taa nyekundu zikawaka, Jenipha akasimamisha gari,kama swala Ngesa akamvuta Jenipha na kuanza kumkaba kwa nguvu shingoni huku akimziba pua na mdomo,kazi ya Jenipha ikawa ni kutupa miguu na mikono.Hakuna mtu yoyote nje, aliyeelewa kwani gari hilo lilikuwa na vioo vyeusi yaani tinted.Hakuwa ana uwezo wa kutoka kwenye mikono ya Ngesa,aliyemkaba shingoni japokuwa alijitahidi kuitoa.
“Pipiiiiiiiii”
Magari ya nyuma yalianza kupiga honi baada ya taa za kijani kuwaka,Ngesa akazidi kumkaba Jenipha kwa nguvu mpaka alivyopoteza fahamu,akamvuta kwa nguvu na kumtoa kwenye usukani,akaingia upande upande akaanza kuliondoa gari kwa lengo moja tu,atafute usalama ulipo ili azungumze vizuri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Leslie Benjamin.
Mwanamme huyu alikuwa ni mtu makini kuliko kitu chochote kile,kitendo cha kuambiwa kwamba anataka kupelekwa nchini Uganda ili akauwawe kilimfanya azidi kuwa makini kuliko kawaida,ndio maana muda wote macho yake yalikuwa kwenye vioo vya nje ili kujua ni gari gani lipo nyuma yake linamfuatilia,alichokifanya cha kwanza ni kukunja kona na kuingia kituo cha kujazia mafuta,hapo alisimamisha gari na kumtizama Jenipha aliyekuwa siti ya pembeni amezirai.
Akachukua simu ya mwanammke huyo na kuanza kumsachi mifukoni,ambapo kiunoni mwake kulikuwa na bastola,akaichukuwa na kuihifadhi kibindoni mwake,hakuishia hapo akazidi kumpekua mifukoni ambapo kulikuwa na kifaa kidogo maalum, ambacho hiko aliamini wanakitumia kujua ni wapi Jenipha alipo,alivyoridhika akafungua mlango wa gari.
Akatembea taratibu mpaka kwenye gari aina ya kirikuu iliyopakia mbao pamoja na mabomba marefu,simu ya Jenipha pamoja na kifaa cha GPRS akaviweka nyuma ya gari hilo,kisha kurejea ndani ya gari.
Akapiga gia na kuanza kuondoka eneo hilo.
Mkurugenzi wa Usalama wa taifa Mr.Ramadhani Mpelembe alikuwa mwenye usongo wa kumtia Ngesa mikononi mwake,aliamini fursa hiyo ingemuweka sehemu nzuri na kumpa ujiko sababu angeenda kuuliwa.Ndio maana muda wote alikuwa makini ndani ya gari lake ameshika ‘ipad’ kubwa,juu kuna ramani inayoonesha kidoti chekundu,hiyo ilimsaidia kujua ni umbali gani Jenipha yupo.
“Sikilizeni,wanakaribia kufika.Kitu kimoja,Ngesa ni mtu hatari!Ana mafunzo ya kijeshi,amecheza michezo hatari yote ya ngumi.Mkiona anakaidi mpigeni risasi,mimi nitajua nitakavyoandika ripoti”
Hayo yalikuwa ni maelezo kutoka kwa Mkuu wa usalama wa Taifa, Ramadhani Mpelembe,sikioni alikuwa ana kifaa maalum, alivyoongea wanausalama wote waliokuwa eneo hilo walisikia,kila mmoja akaitikia kwa heshima kwani waliambiwa Jenipha yupo karibu kufika, hivyo wakae mkao wa kumkamata Ngesa.
“Kacha kacha”
Mr.Ramadhani Mpelembe akakoki bastola yake baada ya kuona gari la Jenipha lipo kwenye mataa,hiyo ilimaanisha baada ya mataa hayo kuruhusiwa basi isingechukuwa muda mrefu wangefika.
Badala yake,akaona kidoti chekundu kinatembea na kukunja kona, mwisho kikasimama baadaye kikaanza kutembea upya,hapo ndipo akawaambia vijana wake wakae vizuri kufanya uvamizi huo kimyakimya na tena uwe wa dakika sifuri yaani wa kufumba na kufumbua.
“Wanakaribia kufika,anzeni”
Magari matatu aina ya Prado,yalianza kutoka taratibu ndani ya jengo la mlimani City,yakaingia barabarani.Kilichowashangaza ni baada ya kuona wapo nyuma ya gari aina ya kirikuu wanalifuata nyuma kwani ilitakiwa wawe nyuma ya gari la Jenipha, ambalo lilifahamika na kila mtu.
“Mkuu,una uhakika?”
“Sijawahi kukosea kazi,mtoeni Ngesa kwenye hilo gari kabla hajajua”
“Lakini mkuu tu..”
“Hakuna cha lakini Thomas,huwezi niambie.Hata mimi naweza hiyo kazi,maana nipo hapahapa karibu”
“Okay”
Kwa kuwa ilikuwa ni amri, hakukuwa na jinsi,mwana usalama huyo aliyefahamika kwa jina la Thomas,akakoki bastola yake na kukanyaga mafuta mengi,akalipita kirikuu na kugeuza shingo,ambapo ndani ya gari alimuona Mwanamme mmoja wa makamo,nyuma ya usukani,akazidi kupeleka gari mbele alivyomvuka akaweka gari mbele na kusimama,hiyo ilimfanya dereva wa Kirikuu apige breki kali na kusimama hapohapo,hiyo ilimfanya Thomas ashuke kwa haraka na kumfuata.
“Kijana shuka ndani ya gari,fanya haraka”
Ilikuwa ni kauli ya kutisha na mbaya zaidi Thomas alikuwa na bastola mkononi kaiweka kwa chini,isingekuwa rahisi kwa mtu yoyote aliyepita pembeni kuona.
Thomas hakuishia hapo,akaanza kukagua ndani ya gari,alivyoangalia nyuma kulipokuwa na mizigo ya mabomba pamoja na mbao ndipo alipochoka baada ya kukuta simu ya Jenipha pamoja na GPRS,hapo ndipo alipogundua kwamba kuna mchezo wamechezewa na Ngesa keshajua tayari,hakuchelewa akamueleza mkuu wake wa kazi kile alichokiona.
“Shiiiiiit”
Ramadhan Mpelembe,akakema kwa hasira hakutaka kuamini kama Ngesa amemtoka kirahisi namna hiyo.
“Jenipha yuko wapi?”
“Hayupo,nimekuta simu yake tu”
****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment