Search This Blog

Wednesday, November 18, 2020

DAPHINE SEHEMU YA 4/10

 

 


DAPHINE
MTUNZI….EMMANUEL F.KWAY(THE STORY MASTER)
AGE…(18+)
Watchstrap…+255718 862176
SEHEMU YA 4 KATI YA 10

 


Mdomo wa Daphine ulikuwa ukivuja damu,pua yake imechanika vibaya sana na sura nzima ililowa damu, hakutofautishwa na nyama iliyotundikwa buchani hiyo ilitokana na kipondo alichokuwa anapigwa na Ngesa,aliyekuwa ana hasira zilizopitiliza hiyo haikufanya asitishe zoezi lake la kumsulubu.

“Nitampata vipi Karanje?”

Ngesa aliuliza kwa sauti na kumtandika ngumi Daphine ya uso.

“Karanje yuko wapi?Nitakuuwa”

“Tuuuuup”

Badala ya Daphine kujibu alimtemea mate Ngesa usoni yaliyochanganyika na madonge ya damu hiyo ilimaanisha kuwa hayupo tayari kuongea chochote,hiyo ndiyo iliyompandisha Ngesa hasira zaidi akamshika shingo na kumvuta mpaka ukutani kisha kulibana koo lake la hewa.

“Karanje yuko wapiiiiii?Najua wewe ni komando lakini nakuhakikishia utataja kwa njia moja ama nyingine”

“Goo..o to he..ll”

Daphine alijibu kwa shida na alikuwa yupo tayari kufa na siri hiyo kifuani mwake kwani mateso aliyokuwa anakula hayakuwa kitu kabisa, kifupi alikuwa nunda ama sugu.Wakati Operesheni ya kuteswa kwa Daphine inaendelea Dustan na Jenipha walikuwa nje ya kioo wanashuhudia kila kitu kinachoendelea.

“Griiii griiiii”

Simu ya Dustan iliita na alivyotoa alikumbana na jina ‘WIFE’ na ilikuwa usiku sana hivyo ilibidi atoke kando kidogo ili aweze kujiachia vizuri na mkewe.

“Ngoja nipokee simu kidogo,Jesca anapiga”

“Okay”

Alimwambia Jenipha kisha kusogea pembeni kidogo.

“Yes halloo Mke wangu”

“Unaongea na Karanje”

Moyo wa Dustan ukapiga kwa nguvu alimanusura utokeze nje ya kifua,wakati mwingine alidhani amesikia vibaya.

“Hallooo,halloo”

“Una masaa matatu peke yake la sivyo mkeo atakuwa mzoga Dustan”

“Naomba niongee na Mke wangu……..”

Simu ikawa kimnya kwa sekunde mbili.

“Dustan,tafadha……Nadhani umemsikia kwa sasa yupo salama.Nina watoto wako pia James na Caroline.Naomba nikukumbushe kitu kimoja nimeua zaidi ya watu elfu moja tayari,sitoshindwa kuuwa hawa sisimizi.Njoo na Daphine saa nane leo, Ubungo Terminal ukiwa naye.Usijaribu kuonya maaskari sababu utamkosa mkeo”

“Lak…”

“Tititiii…..”

Simu hapohapo ilikatwa na kumuacha Dustan anatokwa na jasho jembamba mwili wake wote umekufa ganzi,anahisi joto mwili mzima.Kibarua alichokuwa nacho hakikuwa chepesi kwani Daphine alikuwa mikononi mwa Ngesa na hakuelewa atamtoaje ndani ya jengo hilo.Katika siku ambayo Dustan alikuwa na mtihani mkubwa ni hiyo! Na kivyovyote aliamini angempoteza mkewe kama asingefanya alivyoagizwa na Brigedia Karanje.

“Siwezi kuacha familia yangu ife.Lazima nifanye kitu”

Hapo hapo akapata wazo la haraka,akatembea mpaka kwa Jenipha.

“Mwambie Ngesa aje nje mara moja kuna jambo nataka kuongea naye”

“Upo sawa DK?”

Jenipha alihoji sababu Dustan hakuwa kawaida alikuwa na majasho mengi na anahema juujuu.

“Ni ni nipo sawa,Mwambie Ngesa atoke nje,nataka tuongee kitu”

“Sawa”

Jenipha akagonga mlango Ngesa akafungua na kutoka akiwa amevimba kama chura.

“Ngesa nina njia nyingine,njooni huku”

Dustan alisema na kutangulia mbele ambapo walifuata nyuma Ngesa na Jenipha,wakakunja kona na kunyoosha mpaka ndani ya chumba cha mitambo.

“Nataka iwe siri yenu,nisubirini humu kuna kitu nataka kuwaonesha”

“Kitu gani?”

“Usiwe na haraka Ngesa,ninakuja”

Mahesabu ya Dustan yalikuwa mengine kabisa kwani baada ya kutoka alifunga mlango kwa nje na funguo taratibu sana kisha kuanza kutembea harakaharaka mpaka chumba alichowekwa Daphine.

“Simama tuondoke”

Bila kumalizia kitu kingine chochote kile akamuinua Daphine na kuanza kutoka naye nje.Hakukuwa na mtu hata mmoja aliyeweza kumuhoji Dustan anaenda wapi na mtuhumiwa Daphine sababu alikuwa mkuu wao,hivyo walijua ni mambo tu ya kiusalama zaidi.Dustan alitoka nje na Daphine, akamfungua pingu na kutoa bastola.

“Sikiliza,nakupeleka kwa Karanje.Ameniambia nikupeleke”

Hapohapo Dustan akapiga gia na kurudi nyuma kwa kasi,akaweka gari sawa na kuanza safari ya kwenda Ubungo ili akakutane na Brigedia Karanje amkabidhi Daphine nayeye apewe familia yake.

********

“Sasi hakikisha mnakaa Ubungo pale,kuweni makini anaweza akawa na maaskari”

“Sawa mkuu.Na tukimpata Daphine?”

“Mkimpata Daphine muuwe Dustan,mkewe na watoto wake”

“Sawa mkuu”

Hiyo ndiyo ilikuwa mipango ya Karanje wakishampata Daphine,ilikuwa ni lazima Dustan,mke wake pamoja na watoto wake wapigwe risasi wafe.Bila kupoteza wakati mke wa Dustan aliingizwa ndani ya gari aina ya HIACE nyeusi akiwa amefungwa na kamba mikononi pamoja na watoto wake.Wanajeshi wakaingia ndani ya gari wakiwa na mitutu,safari hapohapo ikaanza ya kwenda Ubungo ili kumchukuwa Daphine!



Ndani ya chumba walichofungiwa Jenipha na Ngesa kulikuwa na ukimnya wa ajabu,hakuna hata mmoja kati yao aliyejuwa mpango mbaya wa Dustan na waliamini baada ya muda mfupi angerudi kwani aliwaambia kuna jambo nyeti anataka wazungumze ndiyo maana aliwaweka ndani ya chumba hiko, hawakuelewa kwamba wamefungiwa kwa nje na mke wa Dustan amewekwa mateka akiambiwa kuwa amkomboe Daphine lasivyo familia yake ingekufa kibudu.

“Mbona anakawia huyu?”

Ngesa aliuliza baada ya kuona muda unayoyoma,Jenipha hakujibu chochote isipokuwa alitembea mpaka mlangoni ili kufungua kwa niya ya kwenda kuchukuwa simu yake kwani aliiacha ofisini kwake lakini alivyonyonga kitasa aliguna kidogo na kunyonga tena!

“Ngesa”

Akaita huku akimtizama Ngesa kwa macho fulani ya mshangao huku akinyonga nyonga kitasa,hapo ndipo Ngesa aliposogea karibu na kugundua kuwa mlango umefungwa kwa nje.Na hata kama wangepiga kelele kwa kiasi gani hakuna mtu yoyote yule ambaye angewasikia kwani walikuwa chumba cha mwisho kabisa kilichokuwa na mitambo kwa ndani.

Wakaanza kujaribu kuvuta mlango lakini haikuwa kazi rahisi, mlango ulikuwa mgumu kupita kiasi.

“Ngesa,kuna kitu kimempata Dustan sio cha kawaida”

“Kwa nini?”

“Kuna simu alipokea,baada ya hapo sura yake ilibadilika.Kuna kitu kinaendelea”

Ngesa akapiga hesabu za harakaharaka kichwani, akajumlisha na kutoa huku akikitizama kitasa,akaangalia pembeni kidogo akaona chuma kilichofanana na tindo,akakibeba.

“Kaa pembeni”

Jenipha alisogezwa pembeni Ngesa akaanza kupiga kitasa kwa nguvu zake zote,kitasa kikawa kinaachia taratibu,akapiga tena bila kuacha!Alivyoona kitasa kimelegea akaingiza tindo katikati ya uwazi wenye kitasa,akakipindua kikanyofoka.Akaingiza mkono na kugusa chuma kirefu kisha kukitoa ukabaki uwazi.

“Hapa hatuwezi kutoka bila kuvuta kwenye kichuma pembeni,ingiza mkono hapa mimi nivute”

Yalikuwa ni maelezo ya Ngesa na Jenipha alitii wakaanza kusaidiana kufungua mlango,haikuwa lelemama kwani kitasa kilikuwa ni aina ya ‘Union’ kutokana na uzoefu wa Ngesa alijua ni wapi akiguse kiachie ndiyo maana akatumia taaluma, hiyo ilimshangaza mpaka Jenipha.

“Vutaaa”

Hapohapo Jenipha akavuta mlango huku Ngesa akijaribu kuunyanyua kwa juu na kuuvuta kwa ndani.Akaupiga kwa nguvu,ukafunguka hakukuwa na muda wa kusubiri wote wakaanza kukimbia kuelekea ofisini, kilichowashangaza zaidi ni baada ya kupita kwenye mlango aliofungiwa Daphine,ulikuwa wazi.

“Dustan yuko wapi?Weka CCTV Camera na ninataka kujua alikuwa anaongea na nani dakika kumi na tano nyuma”

Zilikuwa ni kelele kutoka kwa Jenipha akiongea harakaharaka bila nukta baada ya kubaini kwamba Dustan na Daphine hawapo, kulikuwa kuna kila dalili mbaya kutokea mbeleni.

Wafanyakazi wa usalama wa taifa kutoka katika idara mbalimbali walikuwa makini kwenye kompyuta zao.Na sura ya Dustan akiwa na Daphine ilitokea juu ya kioo kikubwa akiwa nje wanaingia ndani ya gari.

‘YES HALOO MKE WANGU..UNAONGEA NA KARANJE..HALLOO HALLOO..UNA MASAA MATATU PEKE YAKE LA SIVYO MKEO ATAKUWA MZOGA DUSTAN…NAOMBA NIONGEE NA MKE WANGU….DUSTAN TAFADHA……NADHANI UMEMSIKIA KWA SASA YUPO SALAMA.NINA WATOTO WAKO PIA JAMES NA CAROLINE.NAOMBA NIKUKUMBUSHE KITU KIMOJA NIMEUA ZAIDI YA WATU ELFU MOJA TAYARI,SITOSHINDWA KUUWA HAWA SISIMIZI NJOO NA DAPHINE SAA NANE LEO.UBUNGO TERMINAL UKIWA NAYE..USIJARIBU KUONYA MAASKARI SABABU UTAMKOSA MKEO…LAKINI….TITITIII’

Ilikuwa ni sauti iliyosikika na kuenea chumba kizima kutoka kwenye mtambo maalum, sauti ya Dustan na Brigedia Karanje ndiyo iliyokuwa inasikilizwa kwa wakati huo.

Hiyo ilifanya Ngesa abanwe na hasira kupita kiasi, lilikuwa ni jambo la hatari sana endapo Daphine angeachiwa na alijuwa fika ni lazima wangemfanyia kitu kibaya Dustan kwani alimjua sana Brigedia Karanje kuliko mtu yoyote Yule ndani ya chumba hiko.

“Nipe funguo za gari kabla hajafika Ubungo”

Ngesa alizungumza kwa hasira,alikuwa ana kila sababu ya kufanya hivyo.

“Hapana twende wote.Edward James,Trace simu ya Dustan nitumie kwenye Ipad yangu sasa hivi.Batuli Noordin nipatie bastola mbili na begi la risasi”

“Sawa”

Baada ya kuongea maneno hayo, alikabidhiwa silaha akampa Ngesa Bastola moja ndogo akaiweka kiunoni, wakaaanza kutoka nje harakaharaka wakiongozana na Ngesa na walivyofika karibu na gari akatoa funguo na kumrushia Ngesa,akaudaka hiyo ilikuwa ni sawa na kumpa chizi rungu kwani kitendo cha kuingia ndani ya gari aina ya Mark x na kukaa nyuma ya usukani alilirudisha nyuma kama mwendawazimu,akaweka gia na kukanyaga mafuta mengi hiyo ilifanya mpaka matairi yasugue rami na kutoa kelele.

“Nina uhakika atakuwa amepita daraja la Salenda,funga mkanda”

Aliongea Ngesa huku mkono wake mmoja akiwa anafunga mkanda sababu mwendokasi aliokuwa anautoa haukuwa wa kawaida hivyo ilibidi ajihami ndiyo maana alimwambia pia Jenipha afanye hivyo,ni kweli kitendo cha kuingia barabara kubwa alizidi kukanyaga mafuta na akashika usukani kwa mikono miwili, mshale wa spidi ulikuwa unazunguka na kusoma 120 lakini ulizidi kusogea zaidi,kutokana na usiku kuwa mwingi ilifanya barabara iwe nyeupe hiyo ilimfanya azidi kupepeza gari ikafanya mpaka Jenipa ajishike vizuri kwani mapigo yake ya moyo yalikuwa yanaenda kwa kasi ya ajabu kwa mwendo alioutumia Ngesa ilikuwa ni sawa na kulichungulia kaburi.

“Keshakutumia GPRS?”

“Anatuma sasa hivi”

“Tiiiiiii”

Ipad maalum kwa ajili ya kazi kama hizo za kiusalama ililia kuashiria kuwa ujumbe umeingia,Jenipha alivyoangalia juu ya kioo kilimuonesha ramani nzima ya jiji la Dar es salaam na katikati ya ramani hiyo kulikuwa na kidoti chekundu.

“Yupo Namanga”

Jenipha akasema baada ya kuona kidoti hiko kipo eneo hilo,hiyo ilimfanya Ngesa azidi kunyoosha mguu zaidi na zaidi.

“Keshafika Shoppers plaza”

Yalikuwa ni maelekezo mengine baada ya dakika mbili kupita, hapohapo Ngesa akazungusha usukani kwa kasi hiyohiyo na kuhama upande akapandisha tuta na kuingia saiti nyingine ya magari yanayoenda posta,kama kungekuwa na gari nyingine basi wangegongana uso kwa uso na hapo ndiyo ungekuwa mwisho wao.

“Ngeeesaaa”

Jenipha aliita kwa hofu baada ya kuona gari linakuja mbele yao.

“Nimeliona”

Taa za gari zilizokuwa zinamulika kwa mbali zilifanya Jenipha aanze kuogopa kwani hawakuwa saiti yao mbali na hapo Ngesa alikuwa akikimbiza gari kama mwehu.Spidi aliyokuwa anaendesha Ngesa ilitishia uhai kwa dada huyu Jenipha na tangu aanze kazi yake usalama wa taifa hakuwahi kukutana na mtu gaidi kama Ngesa,ndiyo maana alianza kutetemeka na kujishika tena vizuri huku akimuangalia Ngesa mara kwa mara aliyekuwa makini akitizama mbele.

“Tunaingia Mikocheni,wako wapi?”

Ngesa akauliza huku macho yakiwa mbele,bado gari lilikuwa linakuja mbele yao na alikuwa ana mahesabu makali sana kichwani.


Hakutaka Dustan agundue kama yupo nyuma yake kwa kufanya hivyo wangeharibu, kifupi alitaka kumshtukiza ndiyo maana aliingia upande wa pili wa barabara.

“Wale pale”

Kwa mbali Jenipha aliona taa nyekundu na kilichompa uhakika ni namba za gari sababu alilijuwa gari la Dustan.Ulikuwa ni kama umbali wa mita ishrini Ngesa akazidi kukanyaga mafuta.

“Pipiiiiiiiiiiiiii”

Honi ilisikika kutokea mbele yao gari lililokuwa linakuja,ilionekana dereva huyo alidhani wenda watu wamelewa lakini haikuwa hivyo kwani walikuwa katika harakati nzito za kumfukuzia Dustan,kwa kasi ya umeme Ngesa akazungusha usukani na kupanda tuta la katikati,akaingia upande lilipokuwa gari la Dustan,akazidi kukanyaga mafuta na kulipita kwa mbele kisha kuzungusha usukani na kupiga breki gari likazunguka na kupiga msele, kabla halijakaa sawa kwa kasi ya mwewe Ngesa akashuka akiwa na bastola mkononi.Gari ya Dustan ilipiga breki hapohapo kwani asingeweza kusonga mbele sababu gari la Ngesa lilikuwa limeziba barabara mbali na hapo alimuona akiwa ameshika bastola,alihisi kuchanganyikiwa sababu hakuelewa Ngesa alitokaje na alijuaje yeye yupo mahali hapo.

“Dustan toka nje ya gari sasa hiviii,mikono hewani”

Ngesa alizungumza kwa sauti ya juu huku akiwa amekabwa na hasira,akasogea karibu hiyo ilimfanya Dustan afungue mlango na kutoka mikono yake ikiwa hewani,Jenipha hakuwa mbali bastola yake ilikuwa mkononi nayeye kamuweka chini ya ulinzi Daphine.

“Tunajua familia yako imetekwa na tumesikia maongezi yako na Karanje,hii ndiyo nafasi pekee ya kumkamata.Sio kwenda peke yako”

Jenipha alizungumza akitoa maelekezo huku bastola yake ikiwa mkononi kidole kipo kwenye triga anamtizama Daphine ndani ya gari.

“Nawewe Malaya shuka ndani ya gari”

Daphine akashuka mikono yake ikiwa hewani,kawekwa chini ya ulinzi.

“Ngesa nisikilize wamechukuwa familia yangu,wana mke wangu.Ana watoto wangu,mke wangu ni mjamzi…”

“Nyamazaaa”

“Ngesa watamuuwa mke wangu,nina watoto wadogo”

Dustan aliongea kwa uchungu wa hali ya juu sana!

“Naelewa lakini kumbuka kuna watanzania zaidi ya milioni moja wamepoteza maisha yao na wataendelea kupoteza endapo hatutokuwa kitu kimoja.Hii ndiyo nafasi ya kumkamata Karanje”

“Kivipi?”

“Lazima uwe na backup”

“Hapana Ngesa sitoweza kufanya hivyo,ataniua”

“Una uhahika gani?Una uhakika kama hatokuuwa nawewe vilevile.Una uhakika gani hatouwa familia yako kama akimpata Daphine,sikiliza nikwambie um…griii griiiiii”

Simu ya Dustan kutokea mfukoni ilisikika na kumkatisha Ngesa.

“Itoe taratibu”

Ngesa akasema na Dustan akatii.

“Ni Karanje”

“Pokea muweke loudspika”

Hivyo ndivyo alivyofanya,baada ya kupokea.

“Umefika wapi?”

“Nakaribia kufika”

“Hujajibu swali”

“Ndio naingia barabara ya Mwenge”

“Mbona umechelewa?”

“Haikuwa kazi rahisi”

“Umeniweka Loudspika,nasikia sauti ya mwangwi”

“Naendesha gari ndiyo maana nimefanya hivyo”

“Naomba niongee na Daphine”

Kuanzia hapo ukimnya ulisikika kidogo,akamuangalia Ngesa kwani hakujuwa ni kitu gani akifanye.

“Nipe Daphine niongee naye,usinichezee akili yangu”

“Sawa subiri”

“Sasa hivi”

Ngesa akakwapua simu na kukata hapohapo,akamfuata Daphine na kumuwekea bastola kichwani.

“Ukiongea neno lolote la kipumbavu,nakichengua kichwa chako”

Ngesa akaongea huku bastola ikiwa kichwani mwa Daphine na ilikuwa wazi kabisa endapo angeongea kitu chochote kumuonya Brigedia Karanje angeuwawa hapohapo.

“Griii griiii,griii griii”

Simu ikaita tena.

“Pokea ,mwambie mtandao sio mzuri ndio maana simu ilikatika”

“Najua cha kufanya”

Ngesa alimsogezea Dustan simu,alivyopokea alikutana na sauti ya ukali kutoka kwa Brigedia Karanje.

“Sikiliza Karanje,uwa hao watoto muuwe mke wangu wauwe wote.Usiniendeshe na kuniburuza kama unavyotaka umenisikia?Nimemtoa Daphine,hiyo ni risk kubwa natafutwa kila mahali sasa hivi,baada ya hapo najuwa nitatafutwa na nchi nzima.Usinifokee,unamtaka Daphine humtaki?”

Dustan nayeye alipandisha sauti ya juu zaidi lakini nyuma ya yote alikuwa anatingisha kiberiti ilikuwa bahati kwake kwani alifanikiwa kwa asilimia sabini na sita!

“Mpe simu nizungumze naye”

Simu akasogezewa Daphine huku bastola ikiwa kichwani kwake imemgusa kabisa,kidole cha Ngesa kilikuwa kwenye triga tayari kwa kumfyatua Daphine kama angeleta kibuli mbali na hapo alikuwa ana usongo naye.

“Halloo”

“Daphine,upo salama?”

“Ndio….Nipo salama”

“Utakuja nyumbani.Kuna kazi ya kufanya usiogope”

“Sawa”

“Tititiiiii”

Simu ilivyokatwa harakati zikaanza hapohapo,simu ikapigwa makao makuu usalama wa taifa watu kumi wakaitwa na baada ya hapo askari wakapewa taarifa ya ambush nyingine itakayotokea.

“Umefanya vizuri sana Dustan,vaa huu waya tutakuwa tunasikia kila unachozungumza.Hii vaa sikioni tutakuwa tunakuongelesha na kukupa maelekezo”

Maelezo hayo yalitoka kwa mpelelezi mwingine aliyeitwa Dalton Bayeke huyu nayeye alikuwa mwanausalama lakini alibobea zaidi kwenye maswala ya mawasiliano,akaweka mitambo yake vizuri na msafara ukaanza hapohapo,ulikuwa ni usiku sana.Moyo wa Dustan ulikuwa unapiga kwa kiasi cha kutosha sababu aliamini endapo Brigedia Karanje angejuwa yupo na maaskari angepoteza familia yake.

“Halloo ova ova unanisikia Dustan”

Ni sauti kupita sikioni mwake kwenye kidude maalum cha mawasiliano ambacho kiliingizwa ndani kabisa ya sikio,haikuwa rahisi kwa mtu yoyote kukiona ama kusikia maongezi.

“Ndio nakusikia”

“Dustan najuwa una wasiwasi sana lakini naomba nikutoe hofu,unaenda kuokoa mamia na maelfu ya watu,sisi tupo nyuma yako na ninavyoongea nawewe kuna Diffenda zipo Ubungo mawasiliano tayari”

“Sawa nimekuelewa Ngesa”

“Ahsante kwa ushirikiano wako”

Nissan Patrol aliyokuwa anaendesha Dustan ndani alimpakia Daphine peke yake,nyuma umbali wa mita kumi kulikuwa na gari aina ya Mark x nyeusi hiyo alikuwa Ngesa pamoja na Jenipha wanafuata nyuma,gari lililofuata lilikuwa limebeba wapelelezi wengine.

Kazi hiyo ilikuwa nzito naya kiusalama zaidi ndiyo maana iliendeshwa kimnya kimnya,dakika thelathini baadaye walifika Ubungo mawasiliano,Dustan akakunja kushoto na kuacha barabara ya lami,akazidi kusonga mbele zaidi ambapo aliingia mpaka stendi.Hapohapo akachukuwa simu na kumtaarifu Karanje kuwa amefika tayari.

“Toka nje ya stendi,nyoosha kama unaenda Sinza”

“Alafu?”

“Fanya nilichokwambia”

Dustan akawasha gari na kulirudisha nyuma,akatoka mpaka nje ya kituo na kuanza kusonga mbele kuelekea Sinza,mbele yake akakutana na magari mawili yamepaki!

Hapohapo akapigiwa simu na Karanje na kuambiwa kuwa amteremshe Daphine!

“Dustan,usifanye hivyo.Mwambie mpaka uone familia yako”

Maneno hayo yalitoka kwa Ngesa kupitia kifaa maalum alichovaa sikioni sababu alisikia mazungumzo yao.Dustan akasema kama alivyoagizwa!

“Dustan usinijaribu”

“Naomba nione familia yangu”

“Sawa”

Baada ya sekunde tatu kupita mlango wa gari la mbele yake ukafunguliwa,mkewe akashuka akiwa na watoto wake.

“Umewaona?”

“Ndio”

“Mtoe Daphine”

“Siwezi,mpaka nihakikishe ametoka eneo hili ndio niwape Daphine”

“Dustan”

“Ndio hivyo”

Jambo lililokuwa linaenda kufanyika lilikuwa zito kuliko neno lenyewe kwani baada ya hapo ingetokea ambush kali ndiyo maana jeshi la polisi la Tanzania lilikuwa makini, pia jeshi la Usalama wa taifa walitega kila pembe wakiwa na bastola zao,wakisubiri biashara hiyo imalizike ili mashambulizi yaanze!

Ngesa nayeye alikuwa mstari wa mbele na bastola yake ilikuwa na risasi kumi na nane tayari kaikoki kwa ajili ya mashambulizi makali.




Ilikuwa ni operesheni nyingine kali na ngumu mno ya kumtia mikononi gaidi Brigedia Karanje,ilikuwa ni lazima wamtie mikononi mwa sheria ili vifo vya binadamu wasiokuwa na hatia visiendelee kutokea,ndiyo maana kila askari alikuwa makini kuangalia gari nyeusi aina ya HIACE ambayo ndani ilibeba wanajeshi,kivyovyote vile waliamini kuwa ni lazima Karanje atakuwa ndani ya gari hilo ili kumaliza biashara ya kubadilishana Daphine na familia aliyoiteka nyara.Dustan muda wote alikuwa akitetemeka kupita kiasi na jasho jembamba lilimtoka usoni, alielewa nini maana yake endapo Karanje angejua kwamba amelishirikisha jeshi la polisi na watu wa usalama wa taifa,jambo alilokuwa analifanya lilikuwa ni hatari kuliko hatari yenyewe,licha ya kuwa na wasiwasi lakini alipiga moyo konde na kuamini kuwa kila kitu kitaenda sawa kwani alikuwa tayari kayavulia maji nguo ilikuwa ni sharti ayaoge.

“Daphine yuko wapi?”

Aliulizwa tena simuni.

“Naomba familia yangu na watoto wangu watoke eneo hili,waje mpaka nilipo”

“Daphine kwanza”

Dustan alitafakari kwanza,kabla ya kusema kitu kingine chochote sauti kutokea sikioni kwake kutoka kwa Ngesa ilimwambia kuwa asijaribu kufanya hivyo kwanza.

“Dustan usifanye hivyo,Radio one mmemuona Karanje?”

Ngesa aliuliza akiwa amejibanza kwenye kona ya ukuta ambapo mbele yake mita kumi na tano kulikuwa na gari ya Dustan na Hiace iliyobeba wanajeshi.

“Hapana bado,vioo ni tinted”

“Radio two nipe ripoti”

“Hapana bado hatujamuona”

“Shiiit”

Bado kilikuwa ni kibarua kizito, ilikuwa ni lazima kwanza wamuone Brigedia Karanje ndipo ambush ianze dakika hiyo lakini bado hakuonekana.Wakati maaskari na jeshi la usalama wa taifa wakiwa wanajadili namna ya kuvamia na wanajeshi pia ilikuwa hivyohivyo, ilikuwa ni lazima wakimuona Daphine wamuuwe Dustan pamoja na familia yake,ndiyo maana walikuwa tayari wamekoki mitutu yao tayari kwa kumwaga risasi.

“Sasa tunafanyaje?”

Luteni Ecko alimuuliza mwenzake aliyekuwa pembeni.

“Mwache aende.Hawezi kufika mbali”

“Hapana bado hatujamuona Daphine,tukirudi bila Daphine Mkuu hatoelewa”

“Wewe una wazo gani?”

“Tumuone kwanza Daphine lakini kwa sharti moja”

“Lipi?”

“Tumuwekee huyu mama Bomu na watoto wake kisha tulilipue wakifika kwenye gari”

“Haina haja,subiri uone”

Ndani ya gari kulikuwa na wanajeshi nane na walipanga mikakati jinsi watakavyomuua Dustan na familia yake kisha kumchukuwa Daphine,hawakuelewa kuwa wapo katikati ya kundi la Jeshi la polisi na wamezingirwa na Usalama wa taifa.Luteni Ecko alishuka na mtutu mkononi,akamuendea mke wa Dustan na kumuwekea kichwani.

“Una sekunde tatu tu za kutuonesha Daphine,fanya haraka.Sekunde moja ishakatika”

Dustan alitetemeka na alitandwa na uwoga sababu Luteni Ecko hakucheka na aliongea maneno hayo akiwa hana hata punje na masihara ndani yake.

Bila kujifikiria chochote akaingia mpaka ndani ya gari,akabandika gundi juu ya mdomo wa Daphine na kumfungua pingu iliyokuwa imefungwa karibu na dashbord,alivyofanya hivyo akaizungusha tena, mikono ya Daphine kwa nyuma,Mikono ya Daphine ikawa kwa nyuma,mdomo wake umefungwa hawezi kuongea chochote!

“Daphine huyu hapa.Nahitaji familia yangu”

“Sawa tupe Daphine”

“Hapana,Mke wangu na watoto wangu waanze kutembea kwanza kuja kwangu”

“Okay”

Hicho ndicho kilichotokea,Mkewe pamoja na watoto walianza kutembea tararibu kumfuata Dustan alipo huku nyuma wakiwa wameweka mitutu ya bunduki sawa kumaanisha kuwa kitendo cha kufikia hatua tano mbele wamimine risasi kisha wamuuwe na Dustan wamchukuwe Daphine, hawakuelewa hata wao tayari walikuwa katikati ya tageti.

Mlenga shabaha mashuhuri kutoka usalama wa taifa alikuwa kushoto umbali wa mita ishirini, mtutu wake upo begani,jicho moja lipo katikati ya Lensi ambayo ilifanya amuone Luteni Ecko karibu kabisa na kidole chake kilikuwa kwenye triga,anasubiri amri kutoka kwa Ngesa ili amtungue Luteni Ecko ambaye hata yeye alikuwa ana hesabu za kumlenga Mke wa Dustan na watoto,kifupi mwinda aligeuka kuwa mwindwa!

Kitendo cha Luteni Ecko kutaka kuachia risasi, kilifanya mtaalum huyu Erick avute triga hapohapo ikamfikia Luteni Ecko ya kichwa!

“Paa paaaa gegegege”

Kilichosikika hapo zilikuwa ni mirindimo ya risasi,Ngesa alitoka mafichoni na kuanza kurusha risasi huku mara kadhaa akijificha nyuma ya ukuta.

“Paaa paaaa”

Ngesa akazidi kusonga mbele,hapo ndipo jeshi la polisi lilitokeza kwa wingi na kuanza kumimina risasi nyingi,Wanajeshi walivyoona wamezidiwa wakawasha gari ili wakimbie lakini hawakufika mbali kwani matairi yalipigwa risasi.Ngesa akaruka kama swala mpaka mbele ya kioo na kuweka bastola mkononi akiwataka wanajeshi hao wawili ambao walikuwa hai washuke ndani ya gari.

“Shukeni ndani ya gari”

“Paaaaaa”

Ngesa hakujishauri,aliachia risasi ikampiga dereva ambaye alionekana kujishauri,risasi hiyo ilipasua kioo na kupasua fuvu la kichwa chake kisha kumuelekezea mwanajeshi ambaye tayari alianza kutokwa na majasho baada ya kuona mwenzake kachenguliwa na risasi ya kichwa.

“Unaona nilichomfanya mwenzako?Shukaa ndani ya garii sasa hiviii”

Askari nao hawakuwa mbali walikuwa makini na mitutu yao, wameikoki tayari.

“Karanje yuko wapi?”

“Sijui”

Baada ya kutoa jibu hilo alipigwa na kitako cha bunduki akadondoka chini,Ngesa hakumuachia aliendelea kumshambulia na mateke ya tumbo,akamuinua na kumtwanga kichwa cha pua.

“Karanje yuko wapi?”

“Sij..ui”

Mwanajeshi alijibu huku akiwa anavuja damu puani tayari.

“Jenipha mpakie ndani ya gari huyu,ataeleeza tu alipo Karanje!Mrudishe Daphine ndani ya gari pia nina biashara naye”

Hakuna siku aliyochukia kama siku hiyo baada ya kumkosa Karanje,nguvu zilimuisha bado hakuelewa ni kwa namna gani angempata.

“Ngesa”

Dustan alimsogelea Ngesa na kumuita,Ngesa akageuka!

“Ahsante sana,umeokoa maisha yangu”

“Usijali”

Wote wakapeana mikono na Ngesa hakuwa na muda wa kupoteza akaingia ndani ya gari akiwa na Jenipha,akarudisha gari nyuma na safari ya kurudi usalama wa taifa kuanza mara moja akiwa bado ana usongo wa kumpata Karanje,kwa maana hiyo ilikuwa ni lazima mwanajeshi waliyemtia mkononi apewe kipondo cha mbwa ili aseme ni wapi Karanje alipo kwa wakati huo.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani walivyofika tu,Daphine akarudishwa ndani ya chumba chake, mwanajeshi aliyekamatwa akaingizwa ndani ya chumba cha mahojiano.

“Ngesa,tunaomba bastola kabla kuingia ndani”

Kabla ya kuingia ndani ya chumba cha mahoajino, Jenipha alitaka swala hilo litokee kwani alijua hasira za Ngesa zipo karibu,hiyo ingefanya amuuwe mtuhumiwa bila kupata ushahidi wowote ule.

“Unadhani nitamuuwa?”

“Hapana lakini naomba silaha yako”

Ngesa hakuwa na kipingamizi chochote akaichomoa kutoka kiunoni na kumkabidhi Jenipha kisha akaingia ndani ya chumba hicho maalumu kwa ajili ya mahojiano na watuhumiwa!

“M.P Ndomba.Tushajua tayari Karanje ameweka sumu kali kwenye soda za Coca Cola na Kwenye Kimea cha bia za TBL mamia na maelfu ya watu wamekufa.Hapa kuna mawili ufe wewe ama useme ni wapi Karanje alipo na nisingependa tupotezeane muda,najua wewe ni mwanajeshi na umefundishwa kukaa kimnya bila kutoboa siri lakini naomba nikuhakikishie kuwa,utaniambia kile nachotaka kujua.KARANJE YUKO WAPI?”

Macho ya Ngesa yalikuwa mekundu tayari, anamtizama M.P Ndomba kwa hasira kali mno na ilielekea alikuwa anasubiri jibu chafu ili amvae na kumrarua kama chui.

“Karanje yuko wapi?”

“Naongea nawewe”

“Sijui”

Kilichofuata hapo zilikuwa ni ngumi za uso zisizokuwa na idadi kamili kutoka kwa Ngesa na alikuwa akimpiga kama mwizi.

“Karanje yuko wapiiiiiiiii?”

“Sij..ui”

Kipondo alichotoa Ngesa hakikuzaa matunda kwani M.P Ndomba hakuongea chochote kile hiyo ilimfanya Ngesa asimame kidogo na kutafakari kitu gani akifanye,akatoka nje na kumtoa Jenipha pembeni.

“Naomba unisaidie kitu kimoja”

“Kitu gani Ngesa?”

“Wazazi wa Daphine,nawahitaji hapa mara moja”

“Wa nini?”

“Unataka kujua ni wapi Karanje alipo,walete wazazi wa Daphine”

“Okay”

Kazi ya Jenipha ilikuwa ni kuingia mitandao ya simu na kupiga moja kwa moja TCRA kisha kutaja majina ya wazazi wa Daphine.

“Yes ni Hans na Beatrice”

Hata kama ungekuwa umejificha mapango gani ilikuwa ni lazima usalama wa Taifa wajue ni wapi unaishi.

“Wanaishi Kawe Mwisho,subiri kidogo tuangalie minara hapa ya wapi kwa sasa walipo”

Zoezi hilo lilifanyika na mawasiliano yakaruka mpaka mtandao wa Tigo,taarifa zikarudishwa usalama wa taifa kazi ya kumsaka Hans na Betrice ikaanza mara moja!

“Unataka kuwafanya nini Ngesa?”

Jenipha alimfuata Ngesa na kumuuliza,wote walikuwa wakimtizama Daphine kupitia kioo kikubwa cha nje na kumuona akiwa ndani ana pingu mkononi.

“Kupitia wazazi wake,atasema”

“Unataka kuwafanya nini wazazi wake?”

“Nataka kumfanya Daphine aseme nina amini kuna mengi anayajua kuhusu Karanje,Mengi sana”

“Wazazi wake lakini hawahusiki chochote”

“Naelewa,wako wapi?”

“Irene amewafuata”

“Wakija naomba nijue”

“Sawa”

Ngesa akatoka kidogo pembeni na kutoa simu yake ambapo aliipiga moja kwa moja mpaka ikulu na dhumuni la simu hiyo alitaka kujuwa hali ya mpenzi wake Jaqcline Mfinanga,alichoshukuru ni kwamba anaendelea vizuri.

“Mmefikia wapi?”

“Mh.Rais napenda kukuhakikishia kuwa Karanje tutampata”

“Lini Ngesa?”

“Tumefanikiwa kumpata mmoja wa watu wake.Ndio tunamuhoji”

“Ngesa,nina kuamini tafadhali usiniangushe kwenye hili”

“Sawa Mh.Rais na Ahsante kwa kila kitu”

Simu ikakatwa Ngesa akatoka nje kidogo ili kupunga upepo,alivyoangalia saa yake ya mkononi ilikuwa imetimu saa kumi na dakika mbili ya asubuhi.Alihisi kuchoka sababu hakupata usingizi kabisa!

*****

Hans na Beatrice waliingia makao makuu usalama wa taifa saa kumi kasoro moja,wakapelekwa moja kwa moja mpaka ofisini na walitaka kujua ni kwanini wapo mahali hapo.

“Ni mtoto wenu Daphine”

“Daphine?Kafanya nini?”

“Njoeni”

Jenipa,Hans pamoja na Beatrice walichukuliwa na kupelekwa moja kwa moja mpaka chumba alichokuwa Daphine,mlango ukafunguliwa.

“Daaaad Mooom,Kwanini mpo hapa?”

Daphine aliuliza akiwa ana pingu mkononi,alijisikia uchungu sababu hakutaka wazazi wake wajuwe mambo anayofanya,alijisikia aibu na hakuweza kuwaangalia kwa dakika tano nzima.Jenipha alitoka nje na kumtafuta Ngesa.

“Tayari wamefika”

“Nitafutie Soda ya Coca Cola yenye sumu,nataka ashuhudie wazazi wake wanavyokufa mbele yake”

“Nges…”

“Jenipha,fanya hivyo”

Ilikuwa ni lazima Ngesa awanyweshe soda ya Coca Cola wazazi wake na Daphine na awaache akiwashuhudia wakikakamaa mbele yake, aliamini hilo lingekuwa pigo kubwa.

Jenipha hakufanya makosa akaingia mpaka chumba kilichokuwa na chupa za Coca cola,akarudi ndani ya chumba alichokuwa Daphine.

“Unataka kufanya nini? Tafadhali usifanye hivyo”

Daphine alilalamika kwani machale yalimcheza na alielewa soda hizo wangeenda kupewa wazazi wake!

Hapohapo mlango ukafunguliwa, Ngesa akaingia akiwa kayabana meno yake kwa hasira hacheki,lakini moyo wake ukapiga kwa nguvu baada ya kumuona Hans mbele yake,hakuelewa kama anamfananisha ama ni yeye kweli,kumbukumbu zake zikarudi nyuma kwa kasi kama kompyuta isiyokuwa na mafaili,akakumbuka siku aliyomkabidhi mtoto mdogo mchanga wakiwa mkoani Morogoro miaka mingi iliyopita na baada ya hapo hawakuonana tena.

“Haaaans”

“Ngesaaaaaa”

Jambo hilo lilimfanya hata Daphine apigwe na bumbuazi, hakuelewa watu hawa wamejuana wapi mbaya zaidi walikumbatiana na kupigana migongoni kwa furaha sana.

“Haaans ulikuwa wapi?Mungu wangu.Unafanya nini hapa?”

“Nimekuja kumuangalia Daphine”

“Una mfahamu?”

“Ngesa,huyu ndiye Daphine.Uliyenipa kipindi unaondoka Morogoro”

Moyo wa Ngesa ulipiga kwa nguvu,akaganda kama barafu,akapata kigugumizi cha ghafla!



Nguvu za miguu zilimuishia,akawa anarudi kinyumenyume mithili ya gari lililofeli breki,akagota kwenye ukuta,akaserereka mpaka chini kwa mgongo bila hiyari yake.Kwake ulikuwa ni mshtuko wa ghafla kuliko kitu chochote ambacho alichowahi kukisikia katika maisha yake, tangu atoke tumboni mwa Mamaye!Mawazo ya Ngesa yakarudi nyuma kwa kasi ya roketi,akakumbuka alivyosulubishwa na Brigedia Karanje kisa mtoto mdogo mchanga,ambaye Karanje na Jeshi lake walitaka kumuaa sababu tu waliua wazazi wa mtoto huyo mchanga,akamkingia kifua,akawa tayari kuwa kama Yesu,kujitoa Muhanga!

Jambo hilo likafanikiwa, akamkabidhi Mtoto mchanga kwa rafiki yake anayeitwa Hans ili akimbie naye jijini Dar es salaam,kilichofuata hapo, alitekwa na kupokea kila aina ya mateso ili tu ataje ni wapi mtoto alipo,mdomo wake ukawa kama una gundi,hakuthubutu kuufumbua na kusema chochote,akateswa kwa zaidi ya miaka mitatu na kutupwa katikati ya msitu wa Mabira nchini Uganda!

Hayo yote yalipita kichwani kwa Ngesa,akamwangalia Daphine pasipo kuamini kwamba ndiye mtoto aliyemkabidhi kwa Hans miaka mingi iliyopita,mbali na hapo walikuwa kama paka na panya ndiyo maana kwake ilikuwa ngumu kukubali ukweli uliokuwa mezani.

“Ha..pana”

Ngesa akasema machozi yakimlenga,haikujulikana ni hasira ama majuto.

“Ngesa,huyu ndiye Daphine.Huyu ni Mke wangu,tulimlea wote Daphine, tulipitia matatizo makubwa sana”

Hans alizidi kuongea maneno yaliyomfanya Daphine abaki njia panda,hakuelewa chochote,bado alikuwa amevishwa pingu mkononi,anatizama watu hawa waliokuwa mbele yake!Hapohapo Hans akamgeukia Daphine,akamsogelea karibu,akaanza kumuhadithia kila kilichotokea tangu Ngesa alivyompigia simu wakiwa Morogoro,akakabidhiwa kwake.

“Da..phineee”

Ngesa akaita tena,akiwa amekaa chini, kitako!

“Wazazi wako waliuwawa na Karanje,katika msitu wa Mikumi.Mimi ndio niliokuokoa”

“Hapana,wazazi wangu ni hawa hapa, Hans na Beatrice hizo ni njama tu”

“Hapana”

Ulikuwa ni ukweli mchungu na upande mwingine kwa Ngesa aliamini ni muda muafaka wa kujua ni wapi Brigedia Karanje alipo,akasimama kwa kujikaza na kuingia ofisini bila kumsemesha mtu yoyote kitu chochote,akabeba laptop na kurudi nayo,ambapo huko aliingia katika email yake,sehemu maalum alipokuwa anahifadhi ripoti zake kwani kipindi cha nyuma alikuwa ‘Detective’ akawa makini, macho yake yapo juu ya kompyuta mpakato,anapeleka peleka picha,mpaka alipofikia picha ya mwanamke na mwanamke waliolala juu ya majani,miili yao imetobolewa na risasi,hapohapo akageuza laptop upande wa Daphine.

“Wazazi wako ni hawa hapa,Brigedia Karanje na jeshi lake aliwauwa.Mama yako alikuwa ana ujauzito wako ndiyo siku aliyokuzaa wewe akauwawa”

Ngesa akatoa historia fupi kinagaubaga,hiyo ilimfanya Daphine agande kidogo lakini akili nyingine ilimwambia kwamba ni danganya toto tu wanataka kumchezea akili,haikuwezekana hata kidogo jambo hilo kutokea,ndiyo maana akaendelea kubisha na kusogeza kompyuta pembeni.

“Mimi sio mpumbavu..Stop fooling me”

“Hiii D.N.A pia,nina uhakika unajua kusoma”

Ngesa akasogeza tena kompyuta na kumuonesha sampuli za damu yake na wazazi wake ikiwa dakika mfumo wa PDF,hiyo ilimfanya agande kidogo,akajaribu kuvuta akili yake nyuma,akakumbuka maneno ya Brigedia Karanje siku aliyomteka Ngesa’Leo tena tumekutana,mtoto mchanga yuko wapi?Leo unaenda kufa Ngesa’ Kauli hiyo kwa Daphine hakuelewa lakini siku hiyo baada ya tukio hilo lilifanya apate picha kamili.

“Hawa ndio wazazi wako Daphine”

“Kwanini ulimuuwa Vital Kamere?”

Daphine akatupa swali,alitaka kujuwa mkasa mzima.Ngesa akaingia tena kwenye kompyuta na kuanza kumuonesha picha mbalimbali, walizopiga na Brigedia Karanje!

“Huyu ndiye aliyeingiza mabomu ya Nuclear nchini Tanzania,alikuwa wakala wa Brigedia Karanje,anawachukuwa watoto wadogo anawasomesha kisha baadaye anawapeleka Cuba kwa ajili ya mafunzo ya jeshi….”

Ngesa siku hiyo alibadilika kuwa mwalimu,akaanza kumwambia Daphine kila kitu,ambaye mpaka wakati huo alianza kumwaga machozi ya uchungu,hakutaka kuamini hata siku moja kama angepewa habari kama hizo mbaya za kutisha,alivyoangalia juu ya kioo,ndipo alipoumia zaidi kwani watu alioambiwa ni wazazi wake, walikuwa wameuwawa vifo vibaya sana kwa kupigwa risasi za vichwa na vifuani.

Hiyo ilimfanya ajenge chuki ghafla tena ya waziwazi,alilia mpaka akaanza kupata kwikwi.Ngesa akatoa funguo na kufungua pingu za mikono yake,akamuinua na wote wakakumbatiana!

“Pole sana Daphine”

“Kwa..ni hukunia..mbia muda wo..te?”

“Sikuwa najua kama ndio wewe”

Daphine alilia siku hiyo mpaka kamasi zikaanza kumtoka,ilikuwa ni picha ya kuuzunisha, hiyo ilifanya mpaka Ngesa alengwe na machozi, japokuwa alikuwa mwanaume wa shoka na mkakamavu,lakini alijikuta anaingiwa na huruma.

“Waza…zi wangu walizi..kwa wapi?”

“Morogoro”

“Nao..mba nipeleke”

“Sawa,lakini tutajie sasa hivi yuko wapi Karanje”

“Nataka nimuuwe kwa mikono yangu.Ngesa,nataka nimuuwe Karanje kwa mikono yangu!Sasa hivi ni lazima atakuwa Mlandizi ingawa sina uhakika lakini kuna namba ninayo,ikitokea dharura ndiyo huwa nampigia”

Ngesa alivyosikia hivyo,akamtoa Daphine mikononi mwake na kuongozana naye mpaka ofisini ambapo huko alitaja namba za dharura ambazo Brigedia Karanje hutumia.

“Naenda Morogoro,naomba Karanje akamatwe”

Ngesa akamwambia Jenipha.

“Sawa Ngesa,pole sana Daphine”

Historia hiyo iliwaacha watu midomo wazi,hakuna mtu aliyekuwa tayari kuamini kwamba Daphine ambaye wazazi wake waliuwawa na alikuwa bega kwa bega na Brigedia Karanje sasa yupo upande wao na mpaka anatoka nje ya jengo hilo alionesha chuki za waziwazi,kifupi alikuwa ana usongo na Brigedia Karanje kuliko mtu yoyote yule.


Ngesa,Hans,Beatrice pamoja na Daphine wakaingia ndani ya gari aina ya Mark X kwa safari ya kwenda mkoani Morogoro,kulikuwa tayari kumepambazuka na aliyekuwa nyuma ya usukani ni Ngesa,ilikuwa ni lazima waende Mkoani Morogoro siku hiyo na kugeuza jioni yake.

Kazi ya Jenipha siku hiyo ilikuwa ni kusaka namba alizopewa kama dharura,akaingia kwenye kompyuta maalumu ya Usalama wa taifa,akapiga simu moja kwa moja TCRA kwa mkurugenzi wa mawasiliano,akampatia namba.

“Naomba namba za watu kumi ambao wanawasiliana na hii namba kuanzia miezi miwili iliyopita”

Jenipha alikuwa simuni anazungumza na Mkurugenzi wa mamlaka hayo ya mawasiliano aliyefahamika kwa jina la Magreth Katinda,dakika moja baadaye baada ya simu kukatwa ujumbe ukarudi kwenye kompyuta yake.Pembeni,kushoto mwa Jenipha alikuwa ameketi Dustan yuko bize kwenye kompyuta yake.

“Mungu wangu”

Jenipha aliropoka kwa mshangao, hiyo ni baada ya kuona orodha ya majina ya watu waliokuwa wana mawasiliano ya karibu na Brigedia Karanje.

“Vipi?”

Dustan akauliza,sababu Jenipha alisema kwa mshangao tena kwa sauti kubwa.

“Jesus Christ”(Yesu Kristo)

“Nini Jenipha?”

Jenipha hakutaka kuongea chochote, alichofanya ni kugeuza kompyuta upande wa Dustan,hiyo ilimfanya asimame ili asogee karibu zaidi, kutazama juu ya kioo.

“Oh My God”(Mungu wangu)

Hata Dustan alionekana kushangaa baada ya kuona jina juu ya kioo,hiyo ilifanya mpaka yeye aogope zaidi na zaidi.

“Lakini Ngesa nachojua mimi baba yake mzazi alifariki”

“Jina lake ndiyo hili hapa, Robert Ngesa”

“Ngesa anajuwa?”

“Sidhani kama anajua”

“Kwahiyo baba yake mzazi pia ana husika?”

“Ndio,sababu simu nyingi hapa ziliingia mwezi uliopita.Juzi pia waliwasiliana na Karanje kwenye hii namba”

Hakuna taarifa iliyokuwa ya kutisha kama siku hiyo,hawakuelewa ni kivipi wangemueleza Ngesa!Na kila mtu alionekana kuogopa kutoa taarifa hiyo kwa Ngesa, kifupi walianza kusakiziana mipira!

*****

Kutokana na mwendo kasi aliokuwa anatumia Ngesa barabarani akiwa na gari aina ya Mark X ambapo alikimbiza kwa spidi 120-180 ilifanya waweze kuingia mkoani Morogoro ndani ya masaa matatu na dakika arobaini,walichomshukuru Mungu walifika salama salimin.

Walivyowasiri Msamvu,stendi ya mabasi.Ngesa alizungusha gari kwenye round about na kuzidi kusonga mbele kama anaelekea misitu ya Mikumi,baada ya kuzikata kilomita kumi hivi,akapunguza mwendo kasi na kuacha barabara ya lami,akazidi kuingia ndani zaidi, ambapo huko kulikuwa na miti mingi mirefu,akasimama kandokando kidogo ambapo kulikuwa na uwanja mdogo ambao,ulikuwa na vifusi vilivyofukiwa.

“Hapa ndipo wazazi wako walipozikwa..Tushuke”

Muda wote Daphine alihisi kutetemeka tangu anatoka Dar es salaam,hakuelewa kama ni hasira ama baridi.Mazingira waliozikiwa wazazi wake ndio ilimfanya apate usongo zaidi,akashuka kutoka ndani ya gari mlango wa nyuma na kuanza kutembea mpaka sehemu yenye uwazi.

Alimfuata Ngesa nyuma,mpaka walipofika kandokando ya kifusi,kilichokuwa kinafanana na kichuguu,pembeni kuna majani-majani!

“Hapa ndipo wazazi wako walipozikwa na site,hakuna mtu aliyewatambua sababu pia hatukukuta vitambulisho vyovyote vile.Lakini kulikuwa na gari lililokuwa limechomwa moto ili kupoteza ushahidi nadhani.Baada ya hapo Karanje akaniteka kabla ya kumalizia ripoti yangu”

Ngesa alijieleza,Moyo wa Daphine ulichoma,akadondoka juu ya kaburi la wazazi wake ambao walizikwa kwa pamoja, akalia kwa sauti kubwa na kulala juu yake akigalagala.Siku hiyo ilikuwa siku ya uchungu kwake na alilia mpaka basi,Ngesa akajaribu kumtuliza lakini haikusaidia chochote, ilikuwa ndio kwanza anamuongezea maumivu.

“Daphine,pole sana.Inuka tafadhali”

“Nge…sa..”

Daphine aliendeleza kilio tu,akazidi kulia na kulia, tena na tena.

“Wames..mpata Karanje?”

Akauliza huku akisimama kwa hasira za waziwazi na namna alivyomuuliza Ngesa kwa Jazba iliogopesha,kifua chake kilikuwa kinapanda juu na kushuka,mapafu yake yalijaa hewa,midomo yake ilimcheza na pua zake zilitingishika.

“Ngesaa,Karanje yukoo Waaapiiiiii?Naongea nawewe”

Akauliza tena kwa hasira, safari hii ilikuwa kidogo atupe ngumi sababu hasira zake zilizidi kipimo.

“Ngoja nipige simu niulize Daphine,punguza Jazba”

“Jazba zangu zitaisha nikimtia Karanje mikononi mwangu”

Ngesa ilibidi atoke kando kidogo,akainua simu na kumpigia Jenipha,hakutaka kuzunguka mbuyu,akanyoosha swali lake!

“Mmempata?”

“Ngesa ilibidi tujue kwanza Brigedia Karanje,anafanya mawasiliano na nani ili twende kwa process”

“Mmempata?Hayo maelezo hayasaidii sasa hivi”

“Ndio,tumepata mtu wa karibu yake”

“Ni nani?”

“Ni baba yako mzazi”

Moyo wa Ngesa ukabadili mapigo,akachukulia swala hilo kama utani,ndio maana akatoa simu sikio la kushoto,akaiweka sikio la kulia.

“Jenipha…”

“Ngesa baba yako ndiyo anahusika kwenye hili”

“Baba yangu alishafariki miaka mingi iliyopita.Usicheze namimi,nitajie…”

“Ngesa njoo Dar es salaaam tuongee”


*** *****

“Mwanao ndio anafanya kila kitu hakiendi sawa”

“Kwani mnashindwa kumthibiti?”

“Sio tunashindwa, anashirikiana na watu.Kikosi changu cha pili hiki kimeuwawa kisa yeye,Mzee Ngesa”

“Huyu ni mtoto wangu,niachie mimi najuwa cha kufanya.Nitamuuwa mwenyewe,mabomu yako wapi?”

“Tayari yapo ndani ya gari”

“Vijana wako tayari?”

“Ndio”

“Kwahiyo Rais Leslie amekataa kumuachia Ali Lugemo kutoka Gerezani?”

“Ndio”

“Nilichofanya Wastegate ndio kinaenda kutokea uwanja wa ndege,pakia mabomu mengine.Waambie vijana waanze safari sasa hivi”

Kilikuwa ni kikao kidogo lakini kilichotisha endapo ungebahatika kupita na kukisikia.Ndani ya nyumba hiyo alikuwa mzee mweusi,kidevu chake kimejaa ndevu nyingi za rangi nyeupe,huyu alifahamika kwa jina la Robert Ngesa,kila alichofanya Brigedia Karanje basi nyuma yake alihimizwa na mzee huyu hatari ambaye alikuwa ana roho mbaya kuliko kawaida,huyu ndiye pia aliyesuka mchongo wa Kenya,Nairobi ‘Wastegate’ akauwa raia wa Kenya kisa Raisi wa nchi hiyo alikataa kutoa majeshi yake nchini Iraq,hiyo ilifanya mkuu wa kikosi cha Al shabab bwana Arafat Mohamedi Khadira, amtume Mzee Ngesa kazi hiyo,kifupi mzee huyu aliogopeka mpaka na Brigedia Karanje mwenyewe,ndiyo maana alimuhakikishia kwamba atamuuwa mtoto wake Derick Ngesa, aliyekuwa anafanya kazi kwa wakati huo na usalama wa taifa,kazi hiyo kwake ilikuwa ni sawa na kuuwa mbu ndani ya neti.

“Huyu Derrick hawezi kunisumbua kichwa,nitaongea na Mkuu wa Mkoa Daudi Bashonga”

“Rc Bashonga?”

“Ndio,Rais anamsikiliza sana.Nitamtumia,waambie vijana waingie ndani ya gari.Acha tuanzishe vita vya tatu vya dunia”

Mabomu yalipakiwa ndani ya gari na dakika kumi na tano baadaye Hammer mbili za jeshi,pamoja na Landcruiser Mkonge, zilikuwa njiani kwa safari moja tu,kuelekea uwanja wa ndege usiku huo wa saa nne ili kuteka nyara na kuanza kuua mtu mmoja baada ya mwingine na walipanga kufanya hivyo ili Rais Leslie amuachie mfungwa anayeitwa Ali Lugemo kutoka magereza ya Segerea.

“Unahisi Rais Leslie atamtoa Ali?”

Brigedia Karanje akamuuliza Mzee Robert Ngesa, wakiwa siti ya nyuma huku safari ikiendelea.

“Atamtoa tu,damu itamwagika na nitamfanya aone watu watakavyouwawa mmoja baada ya mwingine pale Mwalimu Nyerere”

Mzee Robert Ngesa akajibu, akiwa anajiamini kuliko kawaida.


 Kabla ya kufanya mikakati ya kumwaga damu za watu na kuwauwa ili kumtingisha Rais Leslie amuachie huru mfungwa anayeitwa Ali Lugemo,walichofanya ni kujigawa.

Kuna jeshi, liliingia Mikocheni kituo cha stesheni cha Itv,wakakiteka nyara,baadhi ya makamanda wa jeshi waliteka kituo cha Clouds Tv,hakikusahaulika kituo kikubwa, TBC.

“Tulia kimnya,tutatoa ubongo huo”

Mmoja wa waandishi wa habari katika kituo cha Clouds Tv,alipigwa mtama na kutulizwa na mtutu wa bunduki wa kichwa na mwanajeshi huyu aliyekuwa anapiga mkwara,hiyo ilifanya kituo hiko kiwe kimnya,kila mtu alitandwa na hofu ya kifo.

“Nachotaka ni ushirikiano wenu.Hakuna mtu atakayeumia kama mkifuata matakwa yetu,nani mrusha matangazo hapa?”

Mmoja wa wanajeshi, aliuliza huku akitizama huku na kule,waandishi wa habari walikuwa wamelala vifudi fudi,hakuna kitu kingine walichofanya zaidi ya kusali sala zao za mwisho,kwani walijua huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kuishi duniani.

“Nauliza tena nani mtoa matangazo?”

“Mimi hapa”

Msichana mmoja mrembo,mnene kiasi, mfupi! Akasimama kwa kujiamini ingawa alikuwa akitetemeka kwa hofu.

“Jina lako nani?”

“Zuwena Juma”

“Utaondoka na sisi,kuna habari nataka uwende ukachukuwe live.Chukua mitambo yote.Fanya haraka kabla sijabadili maamuzi,nikakupiga risasi za kichwa”

Kwa kutetemeka na hofu kubwa mwilini,Zuwena Juma!Akaanza kuchukua kamera,baadhi ya kompyuta pamoja na vinasa sauti, yaani ‘Microphone’ kwa kizungu.

Kitendo cha kila kifaa kuwa tayari,wafanyakazi wa kituo cha Clouds waliamriwa wote wasimame.

“Wote simameni…”

Mwanajeshi huyu aliyevaa kombati za jeshi aliamuru kwa sauti ya ukali na kukoki mtutu tayari kwa kuwamiminia risasi.

“Ongozeni mbele,ingieni chumba kile.Kwanza, kila mtu atoe simu yake hapa.HARAKA SANA”

Simu zao zote zikakusanywa na baada ya zoezi hilo kuisha, wakaingizwa ndani ya chumba kidogo,huko walifungiwa kisha wanajeshi hao wakaondoka na Zuwena Juma,mpaka nje.Hivyo ndivyo walivyofanya katika vituo mbalimbali vya habari kama ITV na TBC.


******

Saa tatu kasoro na dakika moja, Hammer ya jeshi pamoja na msululu wa Landcruiser mkonge,zilikuwa tayari zimefika Kipawa,uwanja wa ndege, ndani ya magari, kulikuwa na wanajeshi waliobeba silaha kali pamoja na mabomu mazito mno.

Hakukuwa na njia yoyote ya kupita ndani ya uwanja wa ndege bila kupekuliwa tena kwa staili ya mtu mmoja baada ya mwingine kutoka ndani ya gari,kuruhusu jambo hilo litokee ingemaanisha operesheni ya Brigedia Karanje kukwama,hawakutaka swala hilo litokee, ndio maana wakaanza kuweka bastola zao viwambo vya kuzuia kelele.Gari la tatu aina ya Hammer ya jeshi ndimo alipokuwa Brigedia Karanje pamoja na Mzee Ngesa.

“Hakikisheni mnafanya,kimnya kimnya.Bila mtu yoyote kujua”

“Sawa mkuu”

Brigedia Karanje alitoa angalizo,hakutaka swala uzembe litokee katika hatua hiyo ya kwanza ya kuingia, maana ingeharibu kila kitu!Walikuwa kama wametabiri sababu kitendo cha kukunja kulia kuingia katika lango la uwanja wa ndege walikumbana na msongamano wa magari,Landcruiser mkonge ya mbele iliongozwa na Luteni Kelvin Mahugo,alikuwa ni mwanajeshi aliyesifika kwa roho mbaya, hiyo iliendana na matendo yake ya kinyama,swala la kuuwa binadamu mwenzake kwake lilikuwa la kawaida sana kama kula ugali na samaki,ndiyo maana walimuweka mstari wa mbele ili asafishe njia.

Magari yalizidi kusogea karibu zaidi,akashuka na kutembea mpaka kwa walinzi hawa, waliokuwa na bunduki mabegani, wapo doria.

“Ah Mkuu,vipi?”

Askari mmoja alisalimia baada ya kumuona Luteni Kelvin Mahugo akiwa ndani ya jezi za kijeshi,hakujuwa kwamba huo ndio ulikuwa mwisho wake kuishi duniani.

Luteni Kelvin hakuwa na sababu na kutumia silaha yoyote ile kwani kwake askari wawili kuwathibiti ilikuwa kazi rahisi kama kumsukuma mlevi mtaroni.

“Safi,naona mnaimarisha ulinzi”

“Ndio mkuu”

Hakukuwa tena na muda wa kupiga stori,Luteni Mahugo akazunguka nyuma ya askari huyu,akapitisha mkono wake shingoni na kumvuta kando,kazi ilikuwa ni kukaza mkono, ambapo ilifanya askari akose pumzi hiyo ilifanya mpaka ajambe na kutoa haja kubwa ndani ya kaptula yake ya ndani.

“Arrghhh aarghhh”

Askari alikoroma kama kondoo huku akipapatika kama kuku, akijaribu kujitoa mikononi mwa Mwanajeshi,hakuna mtu aliyeona tukio hilo sababu walikuwa kwenye giza.Alivyohakikisha shingo yake imeregea,akaivunja.

“Kaaaa”

Hiyo ndio sauti iliyosikika baada ya shingo ya askari kuvunjwa,marehemu huyu akaburuzwa mpaka kandokando ya majani,akahifadhiwa hapohapo!Akamrudia Askari mwingine, aliyekuwa anakagua magari ili yaingie uwanja wa ndege,alivyoona gari yao aina ya Landcruiser Mkonge ndio inakaguliwa hapohapo akachomoka akiwa na kisu mkononi,bila kuuliza chochote,akakichomeka juu ya shingo ya askari,akamvuta kando na kuvunja shingo yake.Askari wa getini maisha yao yakaishia hapohapo wakiwa wanalinda tena kimnya kimnya.

Luteni Mahugo, akachukuwa kitambaa na kujifuta damu.

“Kazi nzuri,twendeni sasa”Mwenzake,akampongeza.

Magari yakaingia ndani ya uwanja wa ndege bila kugundulika,kifupi kama kuna mtu alikuwa ana safiri siku hiyo ya Jummanne, wenda ndio ungekuwa mwisho wake kwani wanajeshi hawa walikuwa wana usongo wa kuuwa abiria wote na kuteka uwanja wa ndege mzima.

“Inabidi tuwasubiri hao waandishi wa habari nataka habari hii iruke live,watanzania wote wajue.Nataka nchi itingishike.Lazima Rais Leslie atafuata nilichosema”

Hayo yalikuwa maneno ya Robert Ngesa,akiongea huku akiyabana meno yake kwa hasira.Simu ikaruka hapohapo ili kuuliza mchakato wa waandishi wa habari.

“Tupo njiani”

“Okay,fanyeni haraka.Kabla ndege hajizaanza kuruka”

“Sawa”

Lisaa limoja baadaye,Pajero tatu zilikuwa nje ya uwanja wa ndege,waandishi wa habari mbalimbali kutoka katika vituo tofauti tofauti vya televisheni na mitambo, walikuwa tayari wamewasili wakiwa mateka,hivyo kilichobaki ni wanajeshi hawa kuanzisha ambush!Mipango yote ilikuwa imepangwa kwa hatua na umakini wa hali ya juu sana.

*****


Ngesa aliingia jijini Dar es salaam saa sita ya mchana,aliendesha gari kwa mwendo usio wa kawaida, mara nyingi alisimamishwa na askari wa usalama barabarani,kilichomsaidia ni kusema kuwa yupo usalama wa taifa na ana dharura, hivyo walimruhusu kwa sababu alimpigia simu Dustan,hata alivyofika Kibaha alipigwa mkono, kutokana na mwendo wake ulikuwa una hatarisha maisha ya abiria wake pamoja na wavuka barabara,Kibaha hakusimama hiyo ilifanya askari wapige simu Mbezi mwisho.Akapigwa mkono,ilikuwa kidogo awatukane matrafiki hawa ambao walikuwa wanampotezea muda,isingekuwa Jenipha,siku hiyo zingepigwa ngumi.Jenipha alipigiwa simu akamkingia kifua.

Alivyofika Kariakoo,msongamano wa magari ulimuudhi, akaamua kutanua pembeni.

“Ngesa taratibu kuna watoto.Hapo mbele kuna pundamilia”

Hans alimwambia rafiki yake Ngesa kwani alijuta kukaa mbele,muda wote roho yake ilikuwa mkononi na wakati mwingine alihisi kichefuchefu cha kutapika,tangu azaliwe hajawahi kukimbizwa namna hiyo,hiyo ilifanya mpaka kichwa kumuume siku hiyo.


Mawazo ya Ngesa yalikuwa juu ya Jenipha, aliyemwambia kuwa Baba yake mzazi anahusika,zilikuwa ni habari zilizomshtua sana, akatamani afike mapema.Alivyopaki gari baada ya kufika hakulizima,akachomoa mkanda na kuingia ndani ya jengo hilo kubwa la usalama wa taifa,akazama ndani ya lifti na kubonyeza namba 12,lifti ikaanza kupanda juu,ilivyofika ikapiga mlio na kufunguka.Ngesa akaanza kutembea kwa haraka mpaka mezani kwa Jenipha.

“Pole na safari Ngesa”

“Naomba niambie.karanje yuko wapi?”

Bila kupokea salamu alihoji.

“Kama nilivyokwambia Baba yako amehusika,yupo karibu na Karanje”

“Baba yangu alishafariki,sio kweli Jenipha, usicheze na akili yangu”

“Ngesa ni kweli.Baba yako alivyofariki haukuuona mwili wake nina uhakika na hilo,walisema kuwa aliteketea na moto.Haikuwa kweli,tazama hizi picha huu ni mwaka 1997.Hapa ni Pakstan”

Jenipha baada ya kugundua kuwa Baba yake Ngesa alikuwa hai,ilibidi achambue kila kitu tena kwa umakini ili aweze kumshawishi Ngesa, ambaye aliamini angekuwa mtata mno,kila kitu alikianika na mpaka anaingia nchini Kenya,hiyo ikawa haitoshi akaweka kinasa sauti,Ngesa akamsikia Baba yake,anazungumza na Karanje,hapo ndipo alipochoka mwili, mpaka akili kabisa.

“Ngesa,najua utaweza kujua ni wapi Baba yako alipo”

“Hapana,NO.Kwanini anafanya hivi?”

“Mtafute ndio utajuwa kwanini”

Ngesa alipatwa na hasira za waziwazi,akapiga meza kwa nguvu.Na kukiweka kichwa chake mezani.

“Nitafutie jina la Harrison Ngesa”

Ngesa akamwambia Jenipha.

“Huyo ni nani?”

“Ni mdogo wangu,anaweza akajua baba alipo.Alikuwa ana mahusiano mazuri na baba”

“Sawa”

Jenipha akaingia kwenye mitambo yake,akapiga simu TIGO,AIRTEL,ZANTEL na VODACOM.

Kutokana na taratibu za nchi ya Tanzania, huwezi kutumia laini ya simu bila kusajili,ilikuwa rahisi kumsaka mtu dakika yoyote ile,jina la Harrison Ngesa likaanza kusakwa, mitandao yote lakini cha ajabu yaligongana majina zaidi ya matano,huku zikiwa na picha kwenye vitambulisho.

“Ngesa,hapa yuko wapi mdogo wako?”

Ngesa akageuziwa kompyuta na kuanza kuisaka sura ya mdogo wake, ambaye takribani miaka nane hawakuwahi kufanya mawasiliano,Ngesa akayatupa macho yake kwa umakini sana,akiangalia sura moja baada ya nyingine.

“Huyu hapa”

Akasema kwa njia ya kuweka kidole juu ya kompyuta.

“Okay”

Hapohapo Jenipha akapiga simu makao makuu TCRA na kutuma namba ya Harrison Ngesa ili wajue ni minara gani anapatikana,ndani ya dakika kumi majibu yakawa yamerudi.

“Yupo hapa Dar es salaam,minara ya Mbezi kwa msuguli na Mikocheni hizo ndio sehemu zake”

“Nipe namba zake za simu nimpigie”

Kumpata Harrison kulimaanisha kujua ni wapi Mzee Ngesa alipo, ambaye angesema pia maficho ya Brigedia Karanje!

Hapohapo, Ngesa akapiga simu,akaweka Loudspeaker.

“Griiii griii”

Simu ikaanza kuita upande wa pili,kumaanisha kuwa namba ya Harrison ipo hewani.Kila mtu alikuwa kimnya kusikiliza kitakachoongelewa!

“Halloo,nani mwenzangu?”

Harrison alipokea simu kwa swali.

“Harrison,Mimi Derick.Kaka yako!Derick Ngesa”

“Mungu wangu Derick!Uko wapi?Ulikuwa wapi?”

“Nipo,nahitaji kuzungumza nawewe.Uko wapi kwa sasa?”

“Sasa hivi niko Mbeya,labda wiki ijayo”

Ngesa akamwangalia Jenipha,ambaye alitingisha kichwa Magharibi na Mashariki na kusema neno ‘Muongo’Kwa sauti ya chini kwani mnara ulikuwa unaonesha yupo Yombo Vituka, jijini Dar es salaam.

“Sawa basi,hii ndio namba yangu”

“Ulikuwa unataka nini?Maana ni muda mrefu sana,nilivyosikia upo hai nilishangaa,tulikutafuta sana Derick”

“Ukirudi Dar nitafute”

“Sawa Kaka Derick”

Simu ikakatwa,kuna kitu alijifunza kutoka kwa mdogo wake Harrison,hakuwa mkweli na kuna mambo mengi anayafahamu.

“Naomba nitajie Harrison alipo sasa hivi”

Kitu hiko kilikuwa rahisi,usalama wa taifa hawakuwa watu wa mchezomchezo!Hapohapo, namba ya Harrisom ikaingizwa kwenye mtandao maalum wa kusaka watu.Akawa anaonekana Maeneo ya Yombo Vituka,kidude chekundu kikaanza kusogea taratibu na baadaye kilisimama Tazara,Mchicha!

“Ahsante,nataka kumtafuta.Ninajua anajua mengi sana”

Ngesa alivyotaka kusimama, akakumbana na Daphine akiwa katika hali ya hasira,macho mekundu, swali lake lilikuwa moja tu.’Yuko wapi Karanje?’Jambo hilo lilimfanya Ngesa amwombe waongozane mpaka nje,ambapo huko waliingia ndani ya gari na safari ya kwenda Tazara kuanza mara moja.

“Unamfuata Karanje?”

Daphine,akauliza.

“Hapana”

“Tunaenda wapi sasa?”

“Kwa mtu ambaye atatuambia Karanje alipo”

“Wapi?”

“Tazara”

Ngesa alikuwa tayari keshaingia barabarani,macho yake yapo mbele.Hapohapo simu yake ikaita,alivyopokea alipewa taarifa juu ya Harrison.

“Anaendesha gari aina ya Pajero SMG 3216.Amesimama Tazara bado”

“Sawa utaniambia zaidi”

Uhakika huo ulimfanya,azidi kunyoosha mguu na dakika arobaini baadaye alikuwa mataa ya Tazara,hapo alitaka kujua ni wapi Harrison alipo baada ya kupiga simu kwa Jenipha.

“Buguruni Sokoni,baa ya sewa”

“Sawa”

Ngesa badala ya kunyoosha,akakunja kulia.

Akaipita Buguruni Chama na kukunja tena kona,huko aliingia barabara ya sokoni na kupunguza mwendo,akazidi kuangalia huku na kule.

Kwa mbali aliona gari aina ya Pajero,imepaki katika baa hiyo inayosifika kwa wanawake wanaojiuza!

“Nisubiri hapa Daphine”

“No,twende wote”

Ilibidi washuke wote,Ngesa akaingia kwenye baa na kukaa siti ya mwisho kabisa pamoja na Daphine,wakawa wanaangalia huku na kule,wakamuona Harrison amesimama na mwanamke aliyevaa kinguo kifupi, picha ilioonesha mwanamke huyo anajiuza, japokuwa ulikuwa ni mchana kweupe.

“Daphine”

“Yes”

“Mtu mwenyewe ni Yule pale.Naomba fanya unavyojua ili tuondoke naye bila mtu yoyote kujua”

“Okay”

Daphine alivyotaka kusimama Ngesa akamzuia,akamvuta karibu na kushika shati lake ambapo alikata vifungo viwili vya juu,maziwa ya Daphine yakawa nusu yapo nje.

“Unaweza ukaenda”

Daphine,akatembea kwa mikogo kidogo mpaka aliposimama Harrison,akamshika shingoni kimahaba!

“Nimekupenda,njoo huku”

Harrison, alihisi kupagawa sababu mkono wa Daphine ulishuka mpaka sehemu zake za siri,akawa hana kauli tena,akili yake ikahama akamuacha mwanamke aliyekuwa anataka kumnunua.

“Tu..tu..tu tunaenda wapi?”

Akapata kigugumizi cha ghafla kwani Daphine aliendelea kupapasa zipu yake.

“Njoo baby”

Daphine akaongea kimahaba na kurembua huku akitoka na Harrison nje kabisa.

Hapohapo Ngesa akatokea kwa nyuma na kumpiga na kitako cha bastola kichwani,Harrison akadondoka kama gunia la mpunga,wakambeba na kumuingiza ndani ya gari,wakaondoka naye!


 Kwa mbali alihisi maumivu kichwani,kumbukumbu zikawa zinaingia na kupotea mithili ya saa mbovu.Akiwa bado amefumba macho,akajaribu kukusanya matukio,akakumbuka mara ya mwisho yupo baa ya Sewa,Buguruni!Anataka kununua dada poa.Mara ghafla akapigwa na kitu kizito kichwani,mpaka hapo alivyojaribu kukumbuka kilichoendelea,akashindwa!

Akajaribu kuinua mkono wake,lakini ikashindikana pia,hapo ndipo alipofumbua macho yake,akagundua kuwa yupo juu ya kiti.Amefungwa kamba,miiguuni na mikononi.Mbele yake akaona meza, juu yake kulikuwa na vitu vya kutisha, kama; kisu,mikasi na mifuko ya nailoni.Hiyo ilimfanya aogope, sababu alikuwa pia ndani ya chumba kidogo,dirisha moja lipo juu!

Mlango, uliokuwa mbele yake,ukafunguliwa.Akaingia mwanamke,ambaye alimkumbuka mara ya mwisho, alikuwa naye.

“Wewe Malaya unataka nini?Embu nifungulie upesi”

Harrison alisema kwa hasira baada ya kumuona Daphine kaingia.Akatulia kidogo baada ya kuona mwanaume anaingia,sura hiyo ilimfanya aanze kutetemeka ndani kwa ndani,alikuwa ni kaka yake toka n’toke Dericik Ngesa,maswali aliyokuwa anajiuliza kichwani,hayakuwa na majibu ya hapohapo.Sababu mara ya mwisho ,alimdanganya kuwa yupo mkoani Mbeya.Ngesa hakuongea chochote, akapita moja kwa moja kwenye meza iliyokuwa na silaha za kutisha.

“Nimeamua kukufuata hukuhuku Mbeya mdogo wangu”

Ngesa akasema,hakuonesha kucheka.Macho yake yalikuwa mekundu,akimtizama mdogo wake,Harrison!

“Derrick una..”

“Baba yuko wapi?”

“Baba?Baba alishafariki mbona.Kwani ulikuwa hujui?”

“Harrison..Baba yuko wapi?”

“Baba,Baba alifariki kwenye ajali ya moto.Derrick,mbona sikuelewi?Umeanza kuchanganyikiwa?Embu naomba nifungue niondoke zangu usinikumbushe machungu”

“Harrison,nakuuliza mara ya mwisho, baba yuko wapi?”

“Sijui unazungumzia nini?”

“Naomba niambie baba alipo ili uokoe mamia na maelfu ya watu, wasiokuwa na hatia.BABA YUKO WAPIIIII?”

Swali hilo liliulizwa na Ngesa kwa mara nyingine tena,akipaza sauti ya ukali sana,ilionekana alichoka kuuliza kitu kimoja na kukosa anachotaka,hapohapo akainua mfuko wa nailoni,akamvalisha usoni na kuubana kwa nguvu,hiyo ilimaanisha ni lazima Harrison baada ya sekunde tano, atakosa hewa ya Oksijeni na kuanza kupata shida,hivyo ndivyo ilivyokuwa.Sekunde sita baadaye, Harrison alianza kutingisha miguu yake huku akitetemeka, akijaribu kutafuta hewa,lakini Ngesa aliendelea kuzuia mfuko,kwa sekunde sitini nzima yaani dakika moja,akautoa.Hiyo ilimfanya Harrison,akohoe kwa nguvu na kuanza kuvuta hewa kwa pupa.

“Baba yuko wapi?Harrison nitakuuwa.Baba yuko wapi?”

“De De De Deric..k sasa kwa..nini unani..tesa?”

“Niamini,hapo sijaanza.Baba yuko wapi Harrison?”

“Si..jui alipo.Ameku..fa”

Mfuko ukawekwa tena usoni,safari hii Ngesa hakuutoa mpaka dakika moja nzima na sekunde thelahini zilipo katika,ulivyotolewa Harrison hakuwa ana nguvu tena,alibaki anahema tu.Daphine alikuwa pembeni,anashuhudia kila kitu,hakuwahi kumuona Ngesa akiwa katika hali kama hiyo ya hasira,kilichomshangaza zaidi alikuwa akimtesa mdogo wake wa tumbo moja.

“Baba yuko wapi?”

Hilo ndilo lilikuwa swali la Ngesa, akizunguka na mfuko wa Nailoni.

“Derric..k Baba amekufa”

“Harrison,nitakuuwa.Nakwambia ukweli nitakuuwa,niamini.BABA YUKO WAPI?”

Ngesa hakutania,akasogea karibu na kutaka kumvisha tena mfuko.

“Nana nanataja..Baba yu..”

Mateso yalizidi,aliamini hayatoisha.

“Yupo wapi?”

“Derrick la…”

“Baba yuko wapi?”

“Baba hakufa,..YU..yupo Yu..po hai ndio”

“Najua yupo hai ndio,yuko wapi?”

“Si..jui”

Ngesa akataka kumvisha mfuko kwa mara nyingine.

“Derric…k subiri.Nataja alipo”

“Sema”

“Sasa hivi atakuwa uwanja wa ndege Mwalimu Nyerere,ndi ndi ndio walipanga saa nne leo”

“Kuna nini?”

“Anapanga kulipua na kuwauwa watu.Mtafute Karanje anajua kila kitu”

Ngesa,akamwangalia Daphine!Alivyoangalia saa ya mkononi,ilikuwa tayari saa nne kasoro na dakika tano,usiku!

********

“Mama,sijui nikupe zawadi gani lakini nikirudi tu nitakuja na kitu special”

“Usijali sana Josephat mwanangu,ukifika huko usome kwa bidii wewe ndiye mtoto wa kiume nakutegemea”

“Nitafanya hivyo”

“Yaani dada zako wote wameng’ang’ania ili kukusindikiza”

“Ngoja tupige selfie,niwatumie wakina Tizo na Devi kwamba naenda Marekani leo”

“Nawewe una sifa mwanangu.Endesha gari”

“Lazima,maana tulivyohangaika kupata viza sio mchezo”

“Sawa basi tuwahi”

Siku hiyo, ilikuwa ni furaha sana kwa Josephat Masangula,baada ya safari ya kwenda nchini Marekani kuwadia,hiyo ilikuwa ni moja ya ndoto yake kubwa sana katika maisha yake.

Ilikuwa ni familia ya kawaida na siku hiyo wote walikuwa ndani ya gari kumsindikiza Josephat,ilikuwa tayari imegonga saa nne kasoro ishirini, usiku.Hawakuelewa siku hiyo ndiyo wanaenda kukifuata kifo chao, uwanja wa ndege Mwalimu Nyerere,kama wangekuwa na uwezo huo wa kujua, basi wangeghaili safari.Josephat ndiye alikuwa nyuma ya usukani,kushoto alikaa Mama yake,nyuma dada zake Josephine na Julieth,kila mtu alikuwa mwenye furaha iliyozidi kifani.

“Ndege inaondoka saa ngapi?”

“Saa sita kamili”

“Kumbe bado umewahi”

Walivyovuka mataa ya Tazara,wakazidi kusonga mbele zaidi,mpaka wanaingia lango la uwanjani, kulikuwa hakuna kizuizi,hiyo ilikuwa tofauti na siku nyingine, ambapo walinzi hukagua magari,walivyofika waliona magari ya jeshi,walipuuzia na kuanza kushuka kuingia ndani,ambapo walijumuika na wasafiri wenzao,juu ya benchi kusubiri shirika la ndege la KLM ili safari ianze.

“Njooni basi,Julieth na Josephine.Nitakuwa siwaletei zawadi nikitoka Marekani,njooni tugonge selfie.Nitupie Facebook na Instagram”

“Mademu zako watakukoma”

“Na lazima Neema arudi,si alikuwa anakataa subiri sasa.Tuweke snapchat sasa hivi”

Hawakuelewa kwamba siku hiyo ingekuwa ya machozi kwao.Ghafla wakaona,Hiace mbili zimefika na kusimama nje,wakashuka wanajeshi watatu wakiwa na mitutu.Gari la pili wakashuka,wanajeshi wengine wakiwa na watu wengine nane,mikononi wameshika kamera na vipaza sauti.


*********

Saa nne kamili, ndiyo muda uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na Brigedia Karanje pamoja na Robert Ngesa,waandishi wa habari walikuwa tayari wamefika wakiwa mateka na kundi la wanajeshi lilizidi kumiminika uwanja wa ndege,kabla ya kufanya kitu chochote wakauweka uwanja huo katikakati,kumaanisha kuwa hakuna mtu kutoka wala kuingia.Wanajeshi walijipanga kuanzia nje ya uwanja yaani langoni.Kila kitu kilivyokuwa sawa.Hapohapo Brigedia Karanje,akasimama na kupiga risasi tatu hewani.

“Paaa! Paaa! Paaaa!”

Askari wa usalama walivyotaka kuleta shida,wote walimiminiwa risasi wakadondoka chini kama kuku wenye vifaduro.

Tayari hofu ilianza kuwatanda wasafiri, waliokuwa ndani ya uwanja,wengine walitaka kukimbia lakini walipigwa risasi za migongo wakandoka na kumaliziwa na risasi,wakapoteza maisha yao hapohapo.

“Wote laleni chiniiiiiii”

Ilikuwa ni sauti kutokea kwenye spika,ikaenea uwanja mzima.

“Nasema hiviii.Kama mkitaka kutoka salama humu ndani,wote laleli chini,mkae kimnya”

Ilikuwa ni hofu isiyokuwa ya kawaida,hofu ya kifo ndiyo ilitanda kwa kila mmoja wao.Waliojuta zaidi ni wale waliokuwa wanawasindikiza ndugu zao,kila mtu alikuwa akisali sala yake ya mwisho!

“Wewe hapo,simama”

Brigedia Karanje akanyoosha kidole,kikamfikia mwanamke mrembo aliyekuwa amelala kifudifudi.

“Wewe mwanamke uliyevaa shati jeusi,njoo hapa haraka”

Maskini ya Mungu,alikuwa ni Mama yake mzazi na Josephat Masangula, furaha yake ikabadilika na kuwa kilio,akasimamishwa.Amri ikatoka kuwa kamera zote ziwekwe sawa kwa kazi,kuanzia Clouds Tv,Tbc na ITV.

Mitambo ikaanza kufungwa!Ndani ya dakika moja,kila kitu kikawa kinaonekana Tanzania nzima ‘live’.

“Hii ni kwako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Mh.Leslie Benjamin.Damu hizi zote zipo mikononi mwako na yote umetaka wewe”

Brigedia Karanje, alikuwa ameshika bastola mkononi, kila mtu aliyekuwa amewasha televisheni,alikuwa akimuona live, kuna wengine wakiwa majumbani, walidhani labda ni kipindi tu na sinema inarushwa ya kijasusi, kumbe ni ukweli.

“Piga magoti”

Mwanamke huyo alipigishwa magoti, mbele ya Kamera huku Brigedia Karanje akiweka bastola yake kichwani mwa mwanamke huyo aliyekuwa analia machozi ya uchungu,ahurumiwe.

“Paaaaaaa”

Risasi moja tu ya kichwa,damu zikaruka.Mama akadondoka chini,ubongo nje! Lilikuwa ni tukio la kutisha kupita kawaida,ambalo halikuwahi kutokea katika historia ya nchi ya Tanzania, inayosifika kwa amani na watu wapole, Duniani kote.

“Wewe Mzee Njoo hapa”

Babu mmoja mwenye mvi kichwani,akaitwa!Nayeye akapigwa risasi ya kichwa hapohapo.

“Griii griiiiii griiiii”

Simu hiyo ilimshtua Brigedia Karanje,akiwa katika operesheni yake ya kuuwa watu,ilikuwa ni namba ambayo hakuitambua lakini alielewa sana ni lazima mtu huyo ni miongoni mwa watu wake, sababu simu hiyo hupiga watu wenye dharura!

“Nani anaongea?”

“Daphine”

Upande wa pili wa simu ukasikika,Brigedia Karanje,akatoka kando kidogo!

“Uko wapi?”

“Nimetoroka Usalama wa taifa.Upo wapi mkuu?”

“Safi sana.Njoo uwanja wa ndege tufanye kazi,upo na nani?”

“Nina zawadi yako,mtu uliyekuwa unamuwinda muda mrefu”

“Nani?”

“Ngesaa!”

“Good,mlete hapa”

Brigedia Karanje,akatabasamu na kumuangalia Robert Ngesa aliyekuwa kando kidogo,aliamini habari za Ngesa kuletwa hapo,angefurahi nayeye.

“Okay”

Daphine alikata simu huku akiwa ameyabana meno yake kwa hasira,isingekuwa kujikaza na kuigiza,angeunguza picha!Pembeni alikuwa Ngesa na ilikuwa ni lazima watumie akili, kuingia uwanja wa ndege, ndiyo maana walipanga njama kabambe ya KIMAFIA.

Jambo hilo lilikuwa ni hatari, endapo Karanje angejuwa mchezo huo.

“Tunafanyaje Ngesa?”

“Inabidi tuucheze mchezo huu vizuri bila kukosea stepu.This is our last chance,tukikosea wote tutakufa”

Ngesa akatoa bastola na kuikoki.

“Chukua”

Daphine,akajua nini kinachotakiwa kufanyika.Akamuangalia Ngesa,akashika bastola vizuri.

“Paaaaaa”

Akajipiga risasi ya mkono,damu zikamtoka na kupiga kelele za maumivu.Akachana nguo yake kidogo ili kuweka uhalisia wa operesheni yao,jambo hilo lilimfanya Ngesa ayatumbue macho yake na kushangazwa sana na mwanamke huyu jasiri!

“Twende,nitajua cha kusema”

Ngesa akapiga gia na safari ya kuelekea uwanja wa ndege kuanza, ambapo tayari walishaona kwenye luninga jinsi watu walivyokuwa wanapigwa risasi na kufa,walikuwa ni lazima waokoe mamia ya watu waliobaki.

Walivyofika Kipawa,Ngesa akaweka gari pembeni na kumuangalia Daphine,hapohapo akapigwa roba ya shingo kwa nguvu,Ngesa hakupata hewa na alibinywa mshipa mmoja wa shingo uliomfanya apoteze fahamu zake,akachukuliwa na kuwekwa nyuma ya buti,likafungwa!

Daphine,akaingia nyuma ya usukani akiwa mwenye hasira kama mkizi,akapiga gia na safari ya kwenda uwanja wa ndege kuanza,akiwa na usongo wa kumuweka Brigedia Karanje,kwenye himaya yake,kidigitali bila kutumia nguvu!

 Alikuwa ni mwenye hasira zilizozidi kipimo,mpaka mikono yake ikawa inatoa jasho na kutetemeka japokuwa ilikuwa imeshika usukani,picha ya wazazi wake kuuwawa katika mbuga za wanyama huko mbugani Mikumi ilipita kichwani kwake,akaanza kuangalia kama muvi kichwani,akavuta picha namna ambavyo walivyopigwa risasi nyingi za vifua na vichwani,alijilaumu sana kuwa karibu na mtu huyu mbaya Karanje,ambapo hapo mwanzo kwake alikuwa ni Mungu Mtu,historia ya wazazi wake alipewa na Ngesa,ambaye kipindi cha nyuma walikuwa ni maadui wakubwa kuliko kawaida,mambo yalikuwa kinyume sasa!Macho yake yalikuwa mekundu,mkono wake mmoja unavuja damu,hiyo ni baada ya kujipiga risasi mwenyewe ili kuweka uhalisia kwa tukio atakaloenda kulifanya dakika tano zijazo,Ngesa alikuwa nyuma,ndani ya buti amezirai,hana fahamu kabisa,hiyo ndiyo mbinu waliyoona inafaa kwa wakati huo,gari aliyokuwa anaendesha Daphine ikatembea na kufika lango la uwanja wa ndege,hapo alikutana na mwanajeshi mweusi,akiwa ameshika ‘Short gun’.Akashusha kioo.

“Daphine”

Mwanajeshi huyu,alishtuka baada ya kuona sura ya Daphine ndani ya gari,hakuwa ana habari yoyote na alishangaa sababu alijuwa yupo chini ya ulinzi,usalama wa taifa.

“Nimekuja kumuona Mkuu”

“Yes,yupo.Subiri kidogo”

Mwanajeshi huyu,akaenda kando kidogo,akatoa redio upepo.

“Kiiishhh..Mkuu ova,Daphine yupo hapa nje Ovaa”

“Kiiishhh Mruhusu apite”

Kauli hiyo ilifanya,Mwanajeshi huyu atembee kwenye gari la Daphine,akamruhusu apite.Kichwani kwa Daphine kulipita vitu chungu mzima,na kadri alivyozidi kusogea mbele ndipo hasira zilizidi kutikisa kifua chake,kikawa kinapanda juu na kushuka,japokuwa alijitahidi kujizua lakini kwake zoezi hilo, likaonekana kuwa gumu.Kukurupuka na kufanya maamuzi ya ghafla,ingemfanya auliwe,hilo alijuwa wazi kwani alimjua Brigedia Karanje.Akapaki gari kwenye maegesho,hapo alipokelewa na baadhi ya wanajeshi waliokuwa nje,wakamsindikiza ndani,alivyopiga jicho pembeni,akaona watu wengi,wapo mateka,kushoto walisimama wanajeshi nane wakiwa na silaha kali,mbele wengine kumi.Daphine hakuwa eneo hilo kumleta Ngesa peke yake,ndani kwa ndani alianza kuhesabu wanajeshi waliokuwa ndani ya jengo hilo huku akipanga mikakati ya kimafia,ni jinsi gani ataanza kuwatoka na kuanzisha ambush,haikuwa kazi rahisi hata kidogo kwani wanajeshi walikuwa wengi kama njugumawe!

“Daphiiiine”

Ni sauti ya kukwaruza ndiyo iliyotokea nyuma yake,Brigedia Karanje ndiye aliyetokeza na kutabasamu,akasogea mpaka karibu na kumkumbatia.

“Karibu,vipi mkono?”

“Nilipigwa risasi,wakati najaribu kutoroka”

“Sio mbaya karibu tena,nakutegemea.Ngesa yuko wapi?”

“Kwenye gari,ndani ya buti”

Hapohapo,wanajeshi wenye silaha mikononi, wakaamriwa waende kumtoa Ngesa ndani ya gari,wakamchukuwa na kumbeba,wakambwaga pembeni ya Brigedia Karanje!

“Mzee Ngesa,mwanao huyu hapa”

Sura ya mzee Ngesa ilikuwa ngeni kabisa machoni mwa Daphine,hakuwahi kumuona hata siku moja katika maisha yake.

“Huyu anaitwa Daphine,tupo naye.Ni mkakamavu”

Brigedia Karanje,akatoa utambulisho.Robert Ngesa,akamwangalia Daphine kwa macho makali bila kusema chochote!

“Kacha kacha”

Akakoki bastola na kumpa Daphine,kisha kuendelea kumtizama Machoni.

“Muuwe,mpige risasi”

Daphine akahisi kutetemeka,jambo aliloambiwa alifanye lilikuwa gumu kupita kiasi,tayari alikuwa ana bastola mkononi na aliamriwa amuuwe Ngesa,kwake lilikuwa ni jaribu kubwa kupita kiasi,akamuangalia Ngesa aliyekuwa chini,amelala hana fahamu,akamuangalia tena mzee huyu Ngesa,ambaye hakuonesha chembechembe yoyote ile ya utani.

“Muuwe,fanya haraka”

Mzee Robert Ngesa,akasisitiza.

“Binti.Muuwe fanya haraka”

“Okay”

Daphine alikuwa bado anatafakari,kichwani kwake alihesabu wanajeshi waliokuwa mbele yake,alitamani awageuzie kibano na kuwapiga risasi lakini asingeweza kufanya hivyo kwani walikuwa ni wengi kuliko kawaida na walimtizama yeye ili ampige risasi Ngesa.

“Kacha kacha”

Mzee Ngesa,akachomoa bastola nyingine kutoka kiunoni,akaikoki.Akamuwekea Daphine kichwani,hiyo ilimaanisha endapo atashindwa kufanya tukio hilo,kichwa chake kitachenguliwa na risasi.Sio siri,ulikuwa ni mtihani mkubwa sana kwa mwanamke huyu jasiri!

“Ukishindwa nitakuuwa mimi.Na nitamuuwa pia vilevile huyu Derick,Maisha yako yapo mikononi mwake binti”

Mdomo wa bastola ulikuwa umegusa,paji la uso la Daphine huku akiambiwa maneno hayo ya kutisha kupita kiasi!

“Inaonekana umeshindwa kumuuwa.Okay”

Kidole cha Robert Ngesa,kilikuwa taratibu kinasogea kwenye triga,na endapo kingefika risasi ingechomoka, Ubongo wa Daphine,ungekuwa chini.Na hakukuwa na masihara katika swala hilo.Hapohapo Daphine,akafumba macho, akavuta triga ili kumuuwa Ngesa.

“Karakacha karakacha”

Ni mlio wa bastola ya Daphine kuashiria kwamba,haikuwa na risasi ndani.Hapo ndipo alijuwa kwamba alikuwa akijaribiwa tu,ili wampime.Jasho lilikuwa linamtoka!

“Paaa paaa paaa”

Robert Ngesa,akampigia makofi kumpongeza, hiyo ilimaanisha kuwa tayari amemuamini na kwamba yupo upande wao.

“Muamshe Derrick,nataka nimuuwe mwenyewe.Daphine kamata hii bastola haikuwa na risasi nilikuwa nakujaribu,kamera ziwe tayari”

Amri hiyo ilivyotoka,wakafanya kila njia za kumzindua Derrick Ngesa,wakafanikiwa.Alivyofumbua macho yake,akiwa chini sura ya kwanza kuiona mbele yake,alikuwa niya baba yake mzazi,hapo ndipo alipoamini kwamba yupo hai wala hakufa kwa ajali ya moto kama alivyofahamu.

“Ba..ba”

“Derrick”

“Kwani..ni unafanya hivi?”

“Bado ni mdogo sana kujua.Muinueni”

Ngesa akabebwa msobemsobe, baada ya kauli hiyo kutoka kwa Baba yake mzazi,akapelekwa mpaka mbele ya kamera,baba yake mzazi ndiye aliyetaka kumuuwa mwenyewe kwa mikono yake.

“Baba,unaisaliti nchi yako?Unamsaliti Rais wako,kwanini unafanya hivi?Kwanini unauwa watu wasiokuwa na hatia?”

“Rais wako ndio kataka.Angekubali mapema,tusingefika huku”

“Unadhani kwa kufanya hivi,atakubali?”

“Rais wako ni dhaifu sana”

“Nakuchukia Baba”

“Piga magoti,nikutume kuzimu”

Siku zote Ngesa alijuwa kwamba uchungu wa mwana aujuaye mzazi lakini kwa Baba yake ilikuwa ni tofauti,kwani alibadilika na kuwa mwenye roho ya kinyama,mbali na hapo alikuwa amemshikia bastola,anataka kumuuwa!

“Piga magoti”

“Siwezi kufa nikiwa nimepiga magoti hata siku moja.Nitakufa kiume huku nimesimama.NIUE Baba”

*****

Rais Benjamin Leslie,alihisi tumbo la kuharisha linamuuma,mauaji yanayoendelea kutokea uwanja wa Ndege ,Mwalimu Nyerere yalimuogopesha kwa kiasi cha kutosha akiwa katika chumba kikubwa cha mkutano,kilichokuwa na wanasiasa kumi na wawili.Kila mtu alitoa pendekezo lake,huyu alisema lile na huyu akasema hili ili kumshauri.Ukatokea mvutano mkubwa na ilikuwa kidogo washikane makoti,wapigane vichwa!

“Wewe ni mjinga wa Mwisho.kwahiyo una ona raha kuona watu wanauwawa,sio?”

“Sio hivyo Samweli, tatizo unaongea hovyohovyo sijui umekula maharage ya wapi wewe?”

“Unanitukana?”

“Nakwambia ukweli”

Waziri mkuu,akaja juu na kupiga meza kwa ngumi,akionesha kukasirishwa na tusi la makamu wa Rais Mh.Kanyika Zahorro!

“Ukweli gani? Wakati unanitusi.Bwege nini wewe”

“Jamani,punguzeni Jazba”

Huyu alikuwa Waziri wa Fedha,akawatuliza baada ya kuona malumbano ya muda mrefu yanaendelea.

“Itakuwaje?”

“Mimi naona,bora zitumwe chopa.Lipigwe bomu kazi iishe hapo tutakuwa tumemuuwa Karanje na watu wake wote,kwisha habari”

Hili lilikuwa wazo kutoka kwa Bwana Bonifasi Kilwanzinza,kila mtu akamshangaa.

“Hivi umekisikia ulichokiongea?”

“Ndio”

“Siku nyingine kama huna hoja,uwe unakaa kimnya.Mh Rais,naomba Ali Lugemo atolewe la sivyo,watu wataendelea kufa kila siku”

Mkuu wa Mkoa bwana Daudi Bashonga,alipendekeza.Rais Leslie akamtizama,ukaribu wake nayeye ukafanya alifikirie wazo hilo mara mbili.

“Daudi,una uhakika na wazo lako?”

Rais Leslie akauliza,akionekana kukata tamaa.

“Ndio,fanya hivyo”

“Sawa fanya utaratibu huo”

Kikao,kikahitimishwa.

******

Dustan Kyoba ama D.K,yupo ndani ya chumba kidogo kilichojaa silaha za moto,anajikoki.Kitu alichokiona kwenye televisheni kiliibua hasira za kutaka kwenda na kufanya ukombozi,hiyo ni baada ya kumuona Ngesa,amewekewa bastola na ni zamu yake kuuliwa tena na baba yake mzazi,ilikuwa ni lazima nayeye alipe fadhila na kwenda kumuokoa ingawa hakuelewa kama atarudi salama!

“Dustan”

Jenipha,aliingia ndani ya chumba hiko na kuita,jambo alilokuwa anataka kulifanya Dustan hata yeye lilimtisha!

“Naam”

“Una uhakika na unachotaka kukifanya?”

“Ndio,Ngesa aliokoa maisha yangu lazima nilipe fadhila”

“Dustan la…”

“Jenipha,baki na familia yangu kama sitorudi”

Dustan,akaongea huku akipakia silaha za moto ndani ya begi dogo!Risasi,Visu,mitutu na mabomu ya machozi pia.Akachukuwa na kisu kidogo,akakiweka ndani ya kiatu,bastola moja ndogo akaiweka kiunoni.

“Dustan”

“Jenipha,kila la kheri”

Maisha ya Dustan hayakutofautishwa na mchezo wa kamali,kufa ama kupona.Akatembea kidogo mpaka mlangoni,Jenipha akamsimamisha.

“Dustan,Good Luck”

Jenipha akasogea karibu na kumkumbatia kwa nguvu huku machozi yakimlenga,akimtakia mafanikio mema!

“Thank you”(Ahsante)

Dustan,akatoka akiwa na begi kubwa mgongoni lenye zana za maangamizi,akatoka nje na kuingia ndani ya gari,akalipiga moto na kuliondoa kwa kasi ya ajabu.

Ulikuwa ni mwendo wa hatari na alitakiwa kumuwahi Ngesa kabla hajapigwa risasi na kufa,japokuwa hakuwa na uhakika kama angewahi hata hivyo,alikuwa tayari pia kuokoa roho za mateka wengine waliokuwa uwanja wa ndege!

Badala ya kusimamisha gari Kipawa,yeye alipita moja kwa moja na kuliingiza mafichoni,nyuma ya ukuta mrefu,akashuka na begi na kutoa,darubani yenye lenzi kali,akaiweka machoni ili kuangalia usalama.Wanajeshi wawili walikuwa ukuta wa nyuma wanalinda,wameshika mitutu mikononi,akaangalia pembeni kushoto na kuwaona wanajeshi wengine,hapo hapo akarudi ndani ya gari.Alivyoangalia kulia,umbali wa mita kama kumi,kulikuwa na ukuta mrefu kiasi,ilikuwa ni lazima apande,azame ndani,akavaa begi mgongoni.

“Kacha kacha”

Akakoki bastola na kuirudisha kiunoni,kifupi alitaka kufanya ukombozi peke yake na akajiita jeshi la mtu mmoja.

Akatembea mpaka kwenye ukuta,akaangalia huku na kule,akarudi chini na kuruka ambapo mikono yake ilishika ukuta,akajivuta na kuibuka juu.

“Puuu”

Akatua,akachomoa bastola na kuangalia huku na kule,akatembea kwa tahadhari kubwa,mwanajeshi mmoja alikuwa mbele yake,anawasha sigara,haraka akapata wazo,akaiweka bastola yake kiunoni na kuchomoa kisu kirefu,akanyata kama chui,mpaka nyuma yake,akamkaba shingoni,kwa nguvu za ajabu akatumbukiza kisu kifuani mwa Mwanjeshi huyu tena upande wa kushoto,niya yake ilikuwa ni kutumbukiza kisu ndani ya moyo.Jambo hilo lilifanikiwa kwani Mwanajeshi,ndani ya Sekunde mbili,akawa ameaga dunia,akamvuta pembeni na kuendelea kuchapa mwendo!

“Hey”

Ni sauti iliyomshtua kutoka nyuma,akaganda.

“Mikono juu”Sauti ya nyuma yake,ikaamuru.

Hakutaka kufa kizembe,ndiyo maana alitaka kujitetea ingawa aliamini ilikuwa ni hatari,alishaamua kufa ama kupona kwanini aogope sasa?Alivyogeuka,akarusha teke lililompiga mwanajeshi huyu tumboni,lilikuwa ni kosa la jinai kuyumba kwake,hapohapo akarusha ‘round kick’mwanajeshi huyo akadondoka chini,silaha yake kando alivyotaka kuisogelea,Dustan akamuwahi,akamchoma kisu cha shingo!

 Ndani ya Uwanja wa ndege kulikuwa na mateka zaidi ya elfu moja na mia tano, na maisha yao yalikuwa hatarini siku hiyo,ilikuwa ni lazima wauwawe, mmoja baada ya mwingine endapo Rais Leslie,angeshindwa kumtoa mfungwa anayeitwa Ali lugemo kutoka gerezani awe huru, ambaye walimuhitaji kwa wudi na uvumba.Kifupi hali ya amani iliondoka nchi ya Tanzania,kila mtu alitandwa na hofu ya kifo!Lakini, katika watu wote mwanaume huyu jasiri Dustan ama D.K, alikuwa ndani ya uwanja huo wa ndege,akitaka kufanya ukombozi.Ndiyo maana, aliingia kimnyakimnya na kuanza kuuwa walinzi waliokuwa doria wanalinda,hilo likafanikiwa kwani baada ya dakika kumi na saba akawa amedondosha walinzi tisa,akazidi kusonga mbele kwa tahadhari kubwa sana,alivyoona pipa kubwa la mafuta akajificha kwa nyuma,akachomoa darubini na kuanza kuangaza huku na kule,kwa mbali aliwaona bado wanajeshi wapo wengi,wanatembea huku na kule.Hakika kulikuwa na ulinzi mkali kuliko kawaida!Alivyorudisha, darubini ndani ya begi,akaendelea na safari yake,ambapo mbele alikumbana na senyenge,kwa chini ilikuwa imelegea kidogo,akaivuta kwa juu na kupenya kama paka,staili aliyotumia hapo,ilikuwa ni kutambaa chini kama nyoka sababu kitendo cha kutembea wima, kingehatarisha maisha yake,akazidi kujiburuza kama nyoka mpaka alipofika karibu kabisa na mwanajeshi,anayezunguka,zunguka kulinda usalama.

“Psiiiii”

Dustan,akapiga kimluzi ili kumzubaisha mwanajeshi huyu,ambaye alionekana kuganda,akitizama huku na kule,akaweka mtutu vizuri.

Kupambana na wanajeshi haikuwa lelemama,Dustan alikuwa akitumia akili nyingi sana, sababu alijuwa fika kwamba watu hao wana mafunzo na wakakamavu,hivyo ilikuwa ni sawa na kumchinja kobe ‘Timing’ndiyo maana alitulia kidogo nyuma ya gari kubwa la mizigo,akapiga tena kimluzi,mwanajeshi akaanza kusogea taratibu aliposikia mluzi huo umepigwa,Dustan kwa tahadhari akazunguka upande wa pili,yaani akawa nyuma ya mwanajeshi,kwa kasi ya mwewe akachomoa kisu na kukitia shingoni mwa mwanajeshi huyu.

“Arggg arggggg”

Mwanajeshi alikuwa akikata roho,huku akiwa amezibwa mdomo.Anaenda chini taratibu,baada ya hapo Dustan akachomoa kisu,alivyotaka kugeuka, akahisi amepigwa na kitu kizito usoni,hakukaa sawa.Akatulizwa na teke la kifua,akadondoka chali chini,ni mwanajeshi mrefu futi nyingi kwenda juu mweusi tii,ndiye alikuwa akipambana naye.Dustan alivyosimama,alipigwa ngumi ya pua,alivyoona ngumi nyingine inakuja,akainama ikapita hewani,alivyoinuka akatupa ngumi iliyomfikia mjeda huyu kidevuni.

Hapohapo akachomoa bastola lakini ikapigwa teke ikadondoka kando,akavutwa na kupigwa kifuti cha tumbo,wakati anayumba akatulizwa na teke la shingo,akadondoka chali kama mjusi mtini.Mwanajeshi,akakoki bastola!

“Wewe ni nani?”

“Nakuuliza wewe ni nani?”

Mwanajeshi,akauliza huku silaha yake ikiwa mkononi.Akitaka kumfyatua Dustan na risasi za kichwa,hiyo ilikuwa wazi sababu kidole chake kilikuwa kinasogea kwenye triga, kumaanisha kuwa,endapo ikichomoka ubongo wa Dustan,ungekuwa chini kama nyanya iliyokanyagwa na tairi la gari!Mapigo ya moyo ya Dustan yalikuwa yakipiga kwa kasi,alijua tayari anaenda kufa na kilichomuuma zaidi, alikuwa anaenda kufa hata kabla hajafika nusu safari,damu zilikuwa zinamvuja mdomoni,anamtizama mwanajeshi huyu,asiyekuwa na huruma hata punje,anataka kumuuwa.Hilo lilikuwa mbeleni kutokea,alijua hilo.Hakuwa na njia nyingine ya kujinasua,zaidi tu ya kutulia kimnya na kusubiri kifo chake.

“Pyuuu! Pyuuu! Pyuuuu!”

Ni risasi tatu,zilisikika.Ubongo ukamwagika chini,ukimnya wa ghafla ukatokea!


*********

“Beliud Martin,Fransic,Ahmed,Sadick,Hamza,Haule,Irene Simon,Eve Mihenga.Nashukuru kwa kufika kwenu mapema hapa,naelewa mnajua nini kinachoendelea sasa hivi.Ndani ya hii nchi”

Jenipha,Mwanamke jasiri alikuwa amesimama mbele kabisa kama mwalimu darasani, anafundisha huku kwenye viti akisikilizwa na wafanyakazi wa usalama wa taifa,alikuwa akizungumza kwa ujasiri ndani ya kikao hicho, kilichokuwa kinasikilizwa na watu nane tu.Kilikuwa ni kikao kidogo lakini ni kizito.Jenipha, aliumia moyo,hakutaka kumuacha Dustan aende peke yake,wakati yeye yupo nyuma.Isingekuwa na maana yoyote ya kazi yake,ndiyo maana akawaita vijana wa kazi ili wavamie uwanja wa ndege, wakafanye ukombozi,Jenipha alizungumza kila kitu na mbele yake kulikuwa na projecta iliyoonesha ramani ya uwanja wa ndege.

“Uwanja wa ndege umetekwa, akiwemo mkuu wetu Dustan.Pia Umezungukwa na watu hatari wa Karanje.Beliud na timu yako,mtaingilia hapa,Ahmed na timu yako.Mtapitia kwa mbele.The rest tutaingia hapa katikati…..”

Jenipha,alitoa maelekezo utadhani ni komando vile,ni wazi kwamba swala hilo lilikuwa ni la jeshi la polisi lakini watu hawa, walijitolea muhanga,kikao kilivunjwa baada ya dakika tano tu,hakukuwa na mtu yoyote mwenye swali,hivyo wakaingia ndani ya chumba kilichojaa silaha za mahangamizi, kila mtu akipakua silaha anayoona inamfaa.Kilichosikika huko ni mitutu kukokiwa na bastola kujazwa risasi.

“Mpo tayari?”

“Ndio”

“Ndio”

Wote, wakaitikia kwa pamoja na kutoka nje, ambapo huko waliingia ndani ya magari na safari kuanza mara moja!

Dakika ishirini baadaye, wakawa wametia timu na tayari wamejigawa na waliingia kimnyakimnya kama walivyopanga iwe,wanajeshi walikuwa wakichezea visu na wengine, walinyongwa na kamba.

“Irene,cover me”(Irene,nilinde)

Jenipha,alimwambia mwanamke mwengine aliyeonekana kuwa machachali sana, akimwambia kuwa amlinde ili yeye avuke upande wa pili,akatembea kidogo na kuona mwanajeshi yupo chini amelala,anavuja damu amekufa,akasonga mbele na kuinua senyenge na kupita kwa tahadhari kubwa sana!Kilichomshtua, mbele yake ni mwanajeshi mrefu,alivyoangalia vizuri akamuona Dustan yupo chini kawekewa bastola,hapohapo akaweka bastola yake sawa mkononi,akabana jicho moja!

“Pyuu! Pyuu! Pyuuu!”

Mwanajeshi akawa amepigwa risasi tatu za kichwa,akadondoka chini.

“Dustan,Dustan”

Jenipha,akaita huku akikimbia mpaka alipo Dustan chini,amelala anasubiri kifo chake,alivyomuona Jenipha akashtuka, alivyogeuka pembeni na kumuona Irene,akashtuka zaidi.

“Are you okay?”(Uko sawa)

“Yaah”

Jenipha,akampa mkono ili kumuinua.Dustan akaushika mkono wa Jenipha,akasimama wote wakaendelea kusonga mbele.

*****

Ngesa alikuwa katikati ya maombi,akimuomba Mungu wake, amsamehee dhambi zake zote,hakusahau kumuomba Mungu ailinde Tanzania,alikuwa akiomba huku akiwa amefumba macho yake,anasubiri risasi ifumue kichwa chake,alikuwa jasiri mwazo lakini ghafla hofu ikaanza kumtanda,akajaribu kuanza kukitafakari kifo kinafanana vipi na watu wakifa wanaenda wapi na kushindwa kuelewa.Ndiyo maana ujasiri ukaanza kumtoka,wakati mwingine aliona kama anachelewa kufa!Dakika moja nzima ilipita lakini hakuhisi kitu chochote kile,alivyofumbua macho yake.Akamuona Baba yake,yupo kando kidogo,anazungumza na Karanje,hakuelewa ni kitu gani wanateta.

“Kwahiyo amesema atamtoa Ali Lugemo?”

Mzee Robert Ngesa, akamuuliza Karanje.

“Ndio,nimepigiwa simu hapa na Daud Bashonga”

“Ndio nani?”

“Mkuu wa Mkoa,RC”

“Una uhakika?”

“Nina muamini,yupo upande wetu”

“Ushawaambia vijana?”

“Ndio wanaenda Magerezani kumchukua sasa hivi”

“Mpaka tuhakikishe”

Ilikuwa ni furaha kubwa kwa Robert Ngesa kwani kutoka kwa Ali Lugemo, kungemaanisha hatari nyingine kubwa kutokea sababu, alikuwa ndiye mkemia mkubwa wanayemtegemea,ambaye angetengeneza virusi hatari,ambavyo vingechanganywa kwenye hewa watu wangekufa kama kuku,kifupi kumuachia Ali Lugemo ilikuwa ni hatari kuliko jambo linalotokea uwanja wa ndege siku hiyo.

Dakika kumi baadaye simu ikapigwa,ilikuwa ni habari nzuri kuwa Ali Lugemo yupo huru.

“Mpandisheni Helkopta,atoke kabisa ndani ya hii nchi.Mpelekeni Nakuru,Kenya.Baada ya hapo tutawasiliana”

Karanje alikuwa akiongea na upande wa pili wa simu,baada ya kila kitu kufanyika!Na walichobakisha hapo ni kupanda magari yao na kuondoka,ilikuwa ni furaha kubwa sana kwao.

“Paaaa! Paaa! Paaa! Paaaaa!”

Risasi zilifyatuliwa hewani,mateka wakazidi kutandwa na hofu.

“Wote laleni chiniiiii”

Huo ulikuwa ni mkwara.

“Vipi huyu mtu?”

Karanje,akamuuliza Robert Ngesa,akimaanisha wamfanye nini Derrick Ngesa, aliyekuwa amesimama, anasubiri kifo chake!

“Muuwe tuondoke,Ali Lugemo yupo huru”

Baba mzazi,akatoa ruksa mwanaye auwawe!Karanje akachomoa ‘magazine’ na kuangalia risasi kama zipo ili asifanye makosa,alivyohakikisha akairudisha ndani na kuikoki kwa hasira.

“Kacha kacha”

Akamuwekea kichwani, Ngesa.

“Nilikuwa naisubiri hii nafasi kwa muda mrefu sana,leo nimeipata.Wasalimu kuzimu!”

Karanje akasema,historia yake na Ngesa, ilikuwa mbaya huko nyuma.

Daphine,alikuwa pembeni,anamuangalia Karanje kwa hasira,picha ya wazazi wake kuuliwa mbuga za wanyama Mikumi ikamjia kichwani,akashindwa kuvumilia, hasira zikamjaa kifuani,akainua bastola,alivyotaka kumfyatua Karanje,mlipuko mkubwa ukasikika kutoka pembeni kidogo,ardhi ikatingishika.Hawakukaa sawa,mirindimo ya risasi ikaanza kusikika.

“Gegegegege,Pyuu pyuuu!”

Jeshi la Jenipha na Dustan,likawa tayari limeingia kwa kasi ya ajabu,walikuwa wakimimina risasi sio mchezo,wanajeshi wakawa wanadondoka chini, kama maembe mtini.

“Pyuu! Pyuu! Pyuuu!”

Daphine alivyoona hivyo,cha kwanza alimkimbilia Ngesa na kumfungua Kamba mikononi,Ngesa akawa huru.Mtu aliyekuwa anamsaka ni mmoja tu,Baba yake mzazi.Hasira zikawa juu yake,kwa mbali akamuona anakimbia,akiwa na Karanje.

“Babaaaaaa”

Ngesa akaita kwa sauti,Baba yake akasimama na kugeuka!

“Simama hapohapooo”

Ngesa,akasema huku akiwa na bastola mkononi, kaishika kwa mikono miwili, kidole kipo ndani ya triga,anahema kwa jazba.

“Mimi ni baba yako nimekuzaa,huwezi kufanya hivyo”

Mzee Ngesa, alizungumza kwa kujiamini na kuanza kukimbia lakini Ngesa,hakuwa na chaguo lingine.Ilikuwa ni lazima aokoe mamia na maelfu ya watu.

“Paaaaaaaa!”

Akaachia risasi, ikafumuka na kupenya moja kwa moja mguuni kwa mzee Ngesa,akadondoka chini.

Hapohapo, akamsogelea mpaka karibu,akamuangalia Karanje aliyekuwa anakimbia kuelekea kwenye gari.

“Paaa! Paa! Paa! Paa! Paaa! Paaaaaa!paaa!paaa!paa!”

Daphine sijui alitokea wapi mwanamke huyu,aliachia risasi nyingi kama mwehu,akiwa anamlenga Karanje na alikuwa akikimbia kwa kasi akiwa na hasira chafu,katika risasi nyingi alizoachia mbili, ndizo zilimjeruhi, Karanje!

“Paa! paaa!”

Daphine,akaendelea kufyatua risasi nyingine mbili lakini hizo zilipasua kioo cha gari na kumkosa Karanje.

“Karakacha karakacha”

Alivyotaka kufyatua risasi nyingine,zikawa zimeisha!Akarusha bastola kama mpira,ikamkosa kosa Karanje sababu aliinama kidogo.Hapohapo Daphine,akaruka teke kali ambalo lilimfikia Karanje kifuani.Akatupa ngumi kali,iliyomfikia tena Karanje shingoni,akamvuta na kumpiga kifuti cha tumbo.

“Kwanini uliwauwa wazazi wangu?Nakuuwa leoooo”

Karanje hakuelewa ni kwanini Daphine,amebadilika.Lakini alivyoona ngumi nyingine inakuja,akahepa kushoto akadaka, mkono wa Daphine na kumvuta kwa nguvu,akamtuliza na teke la tumbo!Daphine akayumba na kukaa sawa,akarusha ngumi lakini ilipita hewani Kwani Karanje,aliiona akahepa kulia.Dereva aliyekuwa ndani ya gari, anamsubiri mkuu wake wa kazi, akaona huo ni upotevu wa muda,akachomoa bastola.

“Paa! Paaaa!”

Daphine, akapigwa risasi mbili za bega,akadondoka chini.

“Twende mkuu”

Karanje,akaingia ndani ya gari huku damu zikiwa zinamtoka mkononi.

Jinsi gari lilivyogeuka na kupiga msele,ilitisha!Daphine alivyotaka kusimama alishindwa,maumivu yalikuwa makali mno,akabaki analitizama gari, alilopanda Karanje mpaka likatokomea kwenye uwepo wa macho yake!

 Uwanja wa ndege,tayari kulikuwa na mchafuko.Jeshi la Usalama wa taifa walikuwa katika vita kali na Jeshi la JWTZ,jambo hilo halikuwa la mchezomchezo kwani risasi ziliendelea kurushwa,baadhi ya wanajeshi na kikosi cha usalama wa taifa, walipoteza maisha yao hapohapo, kutokana na risasi!Mambo hayakuwa mazuri sababu wakazi wa maeneo ya Kipawa,Tazara,Banana mpaka Gongo la Mboto walisikia mirindimo ya risasi,wakahisi kuchanganyikiwa, watu walikimbia huku na kule ili kuokoa nafsi zao!Sio siri, jambo lililokuwa linatokea Uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere kama ungesimuliwa ungedhani wenda ni sinema za kijasusi za kuigizwa za akina Jean Claude(Van Damme),lakini ukweli wa mambo ulikuwa ni kwamba mambo yaliyokuwa yanaendelea, katika nchi ya Tanzania yalikuwa ni halisi kabisa.

Chanzo cha vita hiyo kali iliyoanza siku nyingi chini ya kapeti ni Brigedia Karanje,mambo hayakuwa mazuri kwani yaliendelea kuwa makubwa ndiyo maana mpaka Ngesa, mwanaume jasiri akahusishwa,leo hii mwanaume huyu aligundua pia hata baba yake mzazi yupo nyuma ya matukio yote ya kigaidi yaliyotokea,mbaya zaidi alitaka kuuliwa na baba yake mzazi.Ndiyo maana alivyochomoka tu baada ya kikosi cha usalama wa taifa kumkomboa,alitaka kula sahani moja na baba yake mzazi.Akafanikiwa baada ya kumtandika risasi ya mguu!Alivyomfikia tu,akamuangalia kwa macho ya hasira huku bastola yake ikiwa mkononi mwake,anatetemeka kidole kipo ndani ya triga.Akaipiga teke bastola, iliyokuwa pembeni, chini karibu na baba yake,ikaenda mbali kabisa!

“Simama”

Ngesa akazungumza kwa hasira,akimuangalia baba yake kwa chuki za waziwazi,bado hakutaka kuamini kuwa baba yake mzazi aliyemzaa leo hii amekuwa gaidi, mtoa roho za watu.

“Nimekwambia simama”

Ngesa akasema tena,akasogeza bastola ikamgusa baba yake kichwani kabisa!

Kila kitu kilikuwa kinaenda sawa,kwani Jeshi la polisi nao waliingia kwa mbwembwe na mikwara,diffenda kumi na saba zilipiga misere na kabla hazijasimama vizuri askari wakatua ardhini, wakiwa na mitutu begani,hawakuchelewa wakaanza kumwaga risasi!Jenipha, nayeye hakuwa mzembe alikuwa akipigana misumbwi na mwanajeshi mmoja ambaye alionekana kumzidi nguvu,kwani alikuwa amenigwa kwenye kona ya ukuta shingo yake,imekabwa.Anajaribu kujinasua.Alivyoona hali ni mbaya,akanyanyua vidole vyake viwili na kutumbukiza machoni mwa mwanajeshi huyo mwenye misuli mingi mikononi,hapo ndipo alipomuachia na kosa alilolifanya ni kuinama, hapo ndipo Jenipha,alipomfuata na kuizungusha miguu yake shingoni mwa mwanajeshi,kwa nguvu za ajabu akadondoka naye chini,akatumia miguu yake kuinyonga shingo ya mwanajeshi huyo, aliyekuwa anatapatapa!Wakati hayo yanatokea,Daphine alikuwa chini anavuja damu nyingi sana,anajiburuza taratibu mpaka pembeni.Dustan, alivyomuona, akamuendea kwa haraka na kumnyanyua.

“Pole sana,njoo huku”

Dustan na Daphine wakaongozana kwa staili ya kukokotana, mpaka Daphine alivyokalishwa nyuma ya gari.

“Kaa hapo”

Dustan akachomoka na kuanza kurusha risasi,Wanajeshi walivyoona jeshi la polisi linazidi.Wakaanza kukimbia.Ndani ya dakika arobaini na tano mirindimo ya risasi ikawa imepungua!

“Ngesaaaaa”

Dustan,akaita kwa sauti huku akimsogelea Ngesa!

“Muweke chini ya ulinzi huyu,ataenda kutaja ni wapi walipo wenzake”

Ngesa akasema na kutizama pembeni,ambapo alimuona Daphine!Amekaa,damu zinamvuja,akamsogelea kwa kasi!

“Vipi?”

“Ngesaa mtafute Karanje,amekimbia”

“Tutampata,inabidi uwende hospitali”

Kuanzia dakika ishirini baadaye, magari ya waandishi wa habari pamoja na magari ya kubeba wagonjwa yalikusanyika kama utitiri,wagonjwa waliojeruhiwa walipakiwa ndani ya magari maalum na maiti pia zikapakiwa kwenye magari ili wakahiifadhi miili.

*******

Hakuna siku aliyochanganyikiwa na kupandisha mori kama siku hiyo baada ya Ngesa kwa mara nyingine kuingilia mipango yake,alishindwa kumfafanua mwanaume huyo ni wa aina gani kwani kila mpango, ataopanga ilikuwa ni lazima Ngesa,aingilie! Jambo hilo lilifanya atake kumfuta kwanza katika uso wa dunia!Kitu ambacho alishindwa kukielewa ni baada ya Daphine kumbadilikia pia,alijiuliza maswali mengi lakini majibu hakupata!Wakati huohuo pia alikuwa mwenye furaha sababu Ali Lugemo alikuwa huru lakini kilichomuumiza kichwa sana ni Mzee Robert Ngesa,kushikiliwa na jeshi la Usalama wa taifa.Ilikuwa ni lazima afanye kitu ili Mzee Robert Ngesa atoke!

“Nipe simu”

Karanje alimuamuru dereva wake,ulikuwa bado ni usiku.Safari yao ilikuwa ni kwenda Arusha na kuingia mpaka wa Namanga kinyemela kisha baadaye Kuingia Nairobi hapo angeonana na Ali Lugemo, ambaye alisafirishwa kwa usafiri wa anga.Alivyopewa simu,akamuendea hewani mkuu wa mkoa Mh.Daudi Bashonga,huyo ndiye aliyeamini atakuwa msaada kwake!

“Uko wapi Karanje?”

Daudi Bashonga,akauliza baada ya kupokea simu.

“Sikiliza,swala la mimi kuwa wapi haijalishi.Watu wako wamemkamata Robert Ngesa.Tunafanyaje?”

“Hili swala lipo nje ya uwezo wangu”

“Una maana gani Daudi?”

“Liko mikononi mwa Amiri jeshi mkuu.Rais Leslie”

“Nachoomba Robert atoke.Na kitu kingine,nahitaji Ngesa afe!”

“Afe?”

“Ndio”

“Pigia mstari”

“Maana amekuwa kimbelembele sana,najua hatokata tamaa kunisaka popote pale mpaka anipate.Tuna historia mbaya”

Karanje,alishaanza kumhofia Ngesa tayari ndio maana alijihami na kwa wakati huo mategemeo yake yote yakaegamia kwa Mkuu wa Mkoa, Daudi Bashonga,akapata tena matumaini ya kwamba Derrick Ngesa angeuwawa na mipango yake, ingeenda vizuri kama alivyopanga!

******

“Ndio mpenzi wangu.Nipo salama!Unaendeleaje?”

“Sasa hivi nina nafuu lakini maumivu tu,kifuani na mgongoni”

“Utapona mpenzi.Nakupenda sana”

“Naomba ukimpata huyo mwanamke umuuwe Darling”

Ngesa alivyosikia sentensi hiyo,akageuka nyuma na kumtizama Daphine, aliyekuwa juu ya machela pembeni amezungukwa na manesi,Jaqlin Mfinanga hakuelewa kwamba wakati huo, anavyoongea na mpenzi wake, Daphine na Ngesa wapo pomoja na isitoshe wameungana!

“Sawa nitamuuwa”

Ilibidi ampe moyo kwanza!

“Nakupenda Ngesa,uje unione tafadhali”

“Nitakuja”

“Lini?”

“Kuna kazi namalizia mpenzi wangu”

“Naogopa Ngesa”

“Usiogope,kila kitu kipo sawa”

“Tafadhali,naomba uje tukae wote”

“Sawa”

“Nakupenda”

“Mimi pia”

Ngesa,alivyokata simu.Akamtizama Daphine!Maneno aliyoambiwa na mpenzi wake yalimchoma,ni wazi kwamba Daphine ndiye aliyempiga risasi Jaqlin Mfinanga, kipenzi cha roho yake na kumjeruhi vibaya sana,hakuwa na la kufanya sababu tayari walikuwa ni marafiki na wameungana!Msafara wa magari ya usalama wa taifa, yakishirikiana na jeshi la polisi, yalikuwa katika mwendo wa kasi yakipiga ving’ora!Usiku, ulikuwa ni mnene.Baadhi ya wagonjwa walipelekwa mahospitalini na maiti,Monchwari.

“Ngesa,inabidi ukae hapa upatiwe matibabu”

Dustan,alitoa wazo!Wakiwa tayari wamefika hospitali ya Mwananyamala.

“Hapana nipo sawa,nahitaji kuongea na baba yangu”

“Ngesa,tafadhali nisikilize mimi”

“Siwezi,nimekwambia hivi nahitaji kuongea na baba yangu.Siwezi kubaki”

Ngesa,akakomaa!Alikuwa ana usongo na baba yake mzazi,ilikuwa ni lazima amuhoji maswali ni wapi Karanje alipo ili waweze kumpata binadamu hatari anayeitwa Ali Lugemo,haikuwezekana kumpata mtu huyo bila ya kuzungumza na Baba yake mzazi, ambaye alikuwa tayari yupo chini ya ulinzi wa jeshi la polisi.

********

Mkuu wa Mkoa wa jiji la Dar es salaam Mh.Daudi Bashonga,alikuwa kama mtu aliyepagawa.Kazi aliyopewa ya kumuuwa Ngesa ilionekana kumchanganya akili,alikuwa katika wakati mgumu kuliko kawaida na ilitakiwa afanye hivyo haraka iwezekanavyo, ndiyo maana kulivyokucha tu,akaingia ndani ya gari lake na safari ya kuelekea magogoni kuanza mara moja,huko alitaka kukutana na Rais Leslie Benjamin,ili amchimbe na kujua ni wapi Ngesa alipo kisha atume watu wake wakammalize,katika kuwaza sana ndipo akamkumbuka mwanaume machachali,aliyefahamika kwa jina la Simba,jambazi sugu aliyetokea kulisumbua jeshi la polisi miaka ya 1989.Hapohapo, hakutaka kupoteza wakati,akainua simu yake na kumtafuta kwenye laini.

“Simba”

Upande wa pili wa simu ulivyopokelewa tu,Daudi Bashonga akazungumza!

“Naam mheshimiwa”

“Kuna kazi hapa nataka kukupa”

“Ipi?”

“Upo tayari?”

“Inategemea na aina ya kazi”

“Navyojua mimi simba huwa hachagui kazi”

“Naelewa”

“Nitakupigia simu baadaye”

“Okay”

Daudi Bashonga alivyokata simu,akawa tayari amelifikia geti la Ikulu,Magogoni.Askari wa usalama wakafika na kuanza kulikagua gari kwa uangalifu mkubwa!

“Karibu mheshimiwa”

Askari mmoja akasema huku akijichekesha baada ya kuona sura ya mkuu wa Mkoa,ndani ya gari.

“Ahsante”

Gari likapita mpaka kwenye maegesho maalum kabisa na kupaki,hapo mlango ukafunguliwa, Daudi Bashonga akashuka na kuingia ikulu ambapo huko pia alifanyiwa upekuzi

“Karibu”

“Ahsante”

Hakukuwa na muda wa kupoteza kwa kuwa aliijua ofisi ya Rais, alinyoosha moja kwa moja na kusubiri sababu alikutana na sekretari.

Dakika mbili zilikuwa nyingi,akakaribishwa,alivyoingia alishangazwa na namna ambavyo Rais alivyokuwa amechoka,ameshika tama!Ana mawazo tele,akakaa kiti cha pembeni!

“Daud,bora umekuja ndugu yangu”

Rais Leslie akazungumza huku mikono yake ikiwa bado juu ya mashavu yake,uwazi ni kuwa alikuwa amechoka na kiti cha urais kwani kilikuwa cha moto!Lawama zote alitupiwa yeye na wananchi kwani kwa kipindi kifupi,mamia ya watu waliuwawa,ukawa kama msiba wa taifa.

“Pole Leslie”

“Pole haitosaidia,nimechanganyikiwa.Sijui nifanye nini?Natamani kuachia madaraka”

“Usifanye hivyo”

“Nifanye nini sasa?Embu nishauri,ungekuwa wewe umekalia hiki kiti,ungefanya nini?Unashuhudia wananchi wako wanakufa.Inaniuma na nimechanganyikiwa,sijalala yapata wiki sasa”

“Kila kitu kitakwisha,changamoto ndio kipimo cha akili”

“This is too much”(Hili limezidi)

“Usiseme hivyo,mimi nina wazo”

“Wazo gani?”


*******


Ngesa hakuruhusiwa kumuhoji Baba yake,walimuelewa sana akiingia ndani ya chumba hiko nini kingetokea, ndiyo maana wakamzuia na akawa kama mtizamaji tu wakati mahojiano yanaendelea,majibu aliyokuwa akiyatoa baba yake, aliyasikia na yalizidi kumpandisha midadi, akitamani kupasua kioo azame ndani.Mwanaume huyu alikuwa ana hasira chafu,hakujali huyu ni nani na yule ni nani.

“Unajisumbua bure!Jina lako nani tena?Jennipha si ndio?Nisikilize nikwambie.Sitosema chochote”

Mzee Robert Ngesa, alikuwa akijibu kwa nyodo huku akimuangalia Jenipha usoni kwa dharau.Kidonda chake kilichosababishwa na kupigwa risasi,kilikuwa kimefungwa bandeji mguuni na kimewekewa dawa,hivyo maumivu aliyokuwa anayahisi yalikuwa niya kawaida tu.

“Ukisema ukweli,hautoweza kufungwa kifungo cha maisha”

“Usipoteze wakati,kama una shughuli nyingine.Nenda kafanye”

Namna Jenipha alivyokuwa anamuhoji mzee huyu utadhani kwamba alikuwa anambembeleza mtoto mdogo anywe uji,jambo hilo ndilo lilizidi kumkera Ngesa aliyekuwa nje kama simba mwenye njaa kali aliyefungiwa ndani ya banda alafu nje kuna swala.Hata alivyoingia Dustan kumuhoji,Mzee Robert Ngesa alikuwa anamjibu kiburi.

“Jenipha,mnapoteza muda.Huyu ni baba yangu.Ninamfahamu,naomba mnipe dakika kumi tu,nikae ndani”

Ngesa akazidi kubembeleza ili apewe nafasi hiyo!

“Hapana Ngesa”

“Hapana nini?Mamia na maelfu ya watu wamekufa kwa ajili ya hawa wapumbavu wachache…”

“Ngesa,punguza jazba”

Ngesa akatulizwa.Hakuna kitu kilichobadilika,Mzee Robert Ngesa aliendelea kukaa kimya mpaka kunakucha.

“Dustan,nisikilize…”

“Ngesa huwezi kuingia.Hatuwezi kukuruhusu kwa sasa hivi.Huyu mtu yupo chini yetu,yupo chini ya usalama wa taifa.Nawewe sio mfanyakazi wa hapa.Hauna mamlaka ya kutoa amri yoyote ile,nachokuomba ukae chini”

Dustan aliongea kwa kupaza sauti ya juu kidogo,ilionekana aliongea kwa hasira sababu ya uchovu wa siku za nyuma.Ngesa,akawa mpole na kutulia, lakini kichwani alikuwa anafikiria vitu vingi mno!

*******

“MKUU TUSHAINGIA HOSPITALINI”

“FANYENI NILIVYOWAAMBIA,HAKIKISHA MNAMUUWA”

“HAKUNA SHAKA”

“MSIFANYE MAKOSA”

Mpango ulikuwa tayari umekamilika na vijana wa kazi watatu walikuwa wameshaingia ndani ya hospitali ya Mwananyamala,kwa lengo moja tu.Kumuuwa Daphine, akiwa kitandani anatibiwa,haikuwa kazi rahisi kutokana na ulinzi aliowekewa mwanamke huyu,cha kwanza kukifanya ni kutafuta makoti ya madaktari.

Ilikuwa ni lazima wamuuwe Daphine siku hiyo, kivyovyote vile.Haikujulikana ni kwa namna gani Brigedia Karanje alijuwa ni wapi Daphine kalazwa lakini kifupi alikuwa mwenye mtandao mkubwa sio kitoto.Vijana watatu waliovaa makoti ya kidaktari na miwani usoni,wakaanza kutembea kwenye korido, wakitafuta wodi alilolazwa Daphine baada ya kufanyiwa upasuaji.

“Ndio hapa”

Daktari huyu feki,akawaambia wenzake baada ya kuona namba ya chumba alichoambiwa kwamba Daphine ndipo amelazwa.Wakasukuma mlango,walishtuka sana kwani ndani kulikuwa na askari mwenye mtutu.Wakamuangalia kwa umakini.

“Inabidi tumchome dawa”

Dokta feki,alimwambia Askari.

“Sawa,mchome”

“Unaweza kutupisha,ili tufanye kazi yetu”

“Sitoweza kuwapisha,fanyeni taratibu zenu nikiwa hapahapa”

Askari akagoma,hiyo ilitokana na mkuu wake wa kazi kumwambia asibanduke wodini hapo,aimarishe ulinzi.Kufumba na kufumbua askari alipigwa kipepsi cha pua,hakukaa sawa.Akachomwa kisu cha tumbo na kuzibwa mdomo,jambazi mwingine alivyoona hivyo,akakaa mlangoni ili mtu yoyote asiweze kuingia!Daphine alikuwa juu ya kitanda,hailewi kinachoendelea kutokana na usingizi mzito aliokuwa nao baada ya kutoka katika chumba cha upasuaji,mkononi alikuwa amewekewa dripu ya maji, yaliyochanganywa na dawa za kumpa nguvu.

Kuna kitu,alikihisi lakini macho yake yalikuwa mazito kufunguka,akajitahidi kufumbua macho yake, cha kwanza kuona alikuwa ni daktari aliyelala chini,anavuja damu,alivyoangalia pembeni alimuona mwanaume aliyevaa koti jeupe anamalizia kuchoma sindano kwenye dripu yake ya maji,sura hiyo haikuwa ngeni kwake walikuwa ni watu wa Karanje,kwa kasi ya umeme akachomoa dripu iliyokuwa kwenye mshipa wake wa damu kwani alielewa kivyovyote vile alikuwa akichomwa sindano ya sumu.Majambazi hawa walivyoona Daphine amezinduka ilibidi watake kutumia njia nyingine mbadala, ndiyo maana mmoja wao, akachomoa kisu na kutaka kumchoma Daphine tumboni,lakini aliishia kuchoma kitanda kwani Daphine alijibiringisha na kujidondosha chini,majambazi hawakutaka kuishia hapo,wakamuibukia upande aliokuwepo.Hapo, ndipo Daphine akajuwa kwamba asipokuwa makini atapoteza uhai wake,hivyohivyo akiwa mwenye maumivu na dhaifu,alisimama na kukunja ngumi,tayari kwa mapambano!


 Kila kilichotokea, Daphine aliamini ya kwamba watu hao wametumwa kumuuwa,ndiyo maana aliweka akili zake zote mbele, dhidi ya majambazi hawa wa Brigedia Karanje.Alikuwa ana maumivu,sawa!Lakini ilikuwa ni lazima apambane ili kutetea uhai wake kwani jambo hilo lilikuwa mikononi mwake,hata kama angeuwawa isingekuwa kizembe namna hiyo.Ndio maana akakunja ngumi ili kupambana na majambazi hawa,mmoja kati yao alikuwa ameshika kisu kirefu, chenye makali kotekote.

Akakirusha kushoto,Daphine akaruka kidogo kikapita kulia,akaudaka mkono wa jambazi huyu mwenye kisu na kumvuta karibu,akamtuliza na kichwa cha pua.Hakuishia hapo,akarudi nyuma kidogo na kubinua kitanda,akakanyaga kiti na kuruka teke, aina ya ‘round kick’ ambalo lilimfikia jambazi mwingine usoni,kuyumba ikawa kosa kubwa sana kwake kwani alimtuliza na kifuti cha tumbo.Sekeseke lilikuwa ni kubwa ndani ya wodi hilo,kasheshe alilokuwa kalianzisha Daphine, lilikuwa sio la kitoto,kilichosikika ni vitu kuvunjwa vunjwa.Hapo ndipo dakatri aliyekuwa anapita karibu na mlango akafungua na kuona,hakutaka kupoteza wakati, haraka akapiga simu kwa walinzi waliokuwa nje!Majambazi, kuona hivyo,wakaanza kukimbia lakini mmoja wapo, alishindwa kwani alikuwa amekabwa na Daphine,kisawasawa!Alivyojitahidi kujinasua akashindwa kwani roba la Daphine lilikuwa kali kuliko kawaida,ndiyo maana akahisi kama kinyesi kinataka kumtoka!

“Karanje yuko wapi?”

Daphine akauliza huku akizidi kuukunja mkono wake,hapo hapo askari wakatokea wakiwa na mitutu mikononi.Kila mtu alimshangaa Daphine,na kilichowafanya wapigwe na bumbuazi ni baada ya kuona kwamba mwanamke huyo mmoja tu, ndiye alipambana na wanaume zaidi ya wawili,wakati akiwa mgonjwa!

“Wawekeni hawa chini ya ulinzi.Muamisheni huyu Mgonjwa wodi lingine,ulinzi uwekwe mara mbili yake”

Kamishna wa polisi Afande Kurwa Mgoli,akatoa amri hiyo na jambo hilo likafanyika, dakika hiyohiyo.

*******

Kila njia alizotumia Ngesa kutaka kumuhoji Baba yake, zilionekana kugonga mwamba,hata alivyomshawishi Dustan ilionekana ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu yasagike, jambo hilo kwa Dustan lilikuwa ni gumu kufanyika kwani alimjua Ngesa,kuhoji kwake kungeambatana na mateso makali sana!Ikabidi Ngesa atulie na kukaa,akatafakari ni njia gani azifanye lakini akakosa jibu la harakaharaka!Mara ghafla kuna kitu alikumbuka na kilikuwa kabambe sana!

“Rais Leslie”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikuwa ni mtu wake wa karibu na ilikuwa ni wazi kabisa ndiye mwenye mamlaka ya kutoa amri kwani ndiye alikuwa mwenye amri ya mwisho kwa kikosi cha usalama wa taifa,hapohapo akatoa simu na kumtafuta hewani,lakini cha ajabu simu ilikuwa haipokelewi,akajaribu tena na tena lakini jambo, lilikuwa ni lilelile.

Mpaka kunakucha, asubuhi, Ngesa hakuruhusiwa kuingia chumba, alichowekwa baba yake.

Alichowaambia Ngesa kilikuwa ni kitu cha ukweli kabisa kwani Mzee Robert Ngesa,bado alikuwa mbishi na hakuwa tayari kuongea chochote kile,hata walivyomtishia kuwa watamfunga kifungo cha maisha, ndiyo kwanza alifurahi.

“Ha! Haa! Haaa!Nifungeni,lakini mjuwe kuwa!Mimi ni kifaa kidogo sana ndani ya injini kubwa.Hata mkinifunga leo,hakitobadilika kitu chochote”

Yalikuwa ni maneno ya kutisha kutoka kwa Mzee huyu mwenye kiburi,ambapo kwa wakati huo alikuwa amefungwa pingu,mbele yake yupo Jenipha anajaribu kumchimba ili aweze kujua ni wapi Brigedia Karanje alipo!

“Ukisema ni wapi alipo Karanje,tutakuachia huru”

“Binti,unajisumbua bure!Mimi sio mtoto mdogo.Usipoteze muda wako.Kamuhudumie mumeo nyumbani”

Mzee Robert Ngesa akajibu kwa kujiamini sana huku akimtizama Jenipha usoni,alionekana ni mtu ambaye hana wasiwasi wowote,hakutofautishwa na abiria aliyekuwa ndani ya ndege anasubiri vinywaji.Hapo ndipo Jenipha,akajawa na hasira akafungua mlango na kutoka nje,moja kwa moja mpaka ndani ya ofisi ya Dustan,bila ya hata, kubisha hodi akazama ndani!

“Vipi?”

Dustan,akauliza.Akaacha kubonyeza kompyuta iliyokuwa mbele yake na kumtizama Jenipha.

“Hatutoweza kujua ni wapi Karanje alipo”

“Kwanini?”

“Nimemuangalia Mzee Robert Ngesa machoni,hayupo tayari kuongea chochote”

“Sasa itakuwaje?”

“Tumpe Ngesa ajaribu kumuhoji”

Jenipha, akatoa pendekezo hilo.

“Unajua maana yake, lakini?”

“Naelewa boss”

“Chochote kikimpata mtuhumiwa,naomba nisiusishwe”

“Sawa”

Jenipha hapohapo,akatoka ofisini na kumuedea Ngesa ambaye alikuwa amekaa mwenyewe,ana mawazo mengi sana!

“Ngesaa”

Jenipha akaita lakini Ngesa,hakuitikia akageuka na kumtizama tu bila kusema chochote!

“Unaweza kumuhoji Baba yako.Lakini naomba usivuke mipaka”

“Nataka kufahamu ukweli,nipeleke”

Ngesa,akasema kwa sauti ya chini huku akiyabana meno yake kwa hasira!Wakaongozana na Jenipha mpaka mlangoni,ukafunguliwa Ngesa akazama ndani.

Mlango ukafungwa kwa nje!Cha kwanza alichofanya Ngesa ni kuanza kugosha vidole vyake huku akimuangalia baba yake mzazi,ambaye kwa muda mrefu alikuwa ana usongo naye!Mbali na hapo, Baba yake huyo alitaka kumuuwa,masaa machache yaliyopita.

“Sitopenda kujua,ni nani aliyekutuma ama ni kitu gani kilichokufanya,Uisaliti nchi yako.Nachotaka kujua.Karanje yuko wapi?”

Ngesa,aliuliza swali hilo na macho yake taratibu yakaanza kubadilika rangi na kuwa mekundu!

“Derrick,mwanangu!Unajua unachokifanya?Achana na hayo mambo utajiingiza kwenye matatizo mwanangu”

“Tayari nipo kwenye matatizo.Ni lazima nimalize nilichokianza.Karanje yuko wapi?”

“Sijui”

“Karanje yuko wapi?Nakuuliza mara ya mwisho,kistaarabu”

Ngesa tayari akawa amekunja uso wake,anamuangalia Baba yake kwa hasira!Mzee Ngesa yeye, hakuonesha wasiwasi wowote ule ndiyo kwanza alitabasamu kana kwamba aliambiwa anapewa mkopo wa pesa nyingi!

“Derrick…Usijisumbue!Huwezi kufanya chochote kile,siwezi kusema alipo”

Ngesa,akapandwa na hasira ajabu, bila kuuliza chochote kingine akamtandika ngumi ya pua baba yake mzazi,akamvuta kwa nguvu na kumkaba shingo akamuinua, msobemsobe na kumkandamiza ukutani.

“Karanjee yuko wapiiii?”

Ngesa akauliza kwa hasira huku akitema chembechembe za mate,sura ameikunja anamtizama Baba yake kwa jazba kupita kiasi,akampiga kifuti cha tumbo.Kutokana na hasira chafu, alizokuwa nazo hakujali kama mtu aliyekuwa anamtembezea kisago ni baba yake mzazi,ndiyo maana aliendelea kumtia vifuti na ngumi.

“Karanje yuko wapi?”

Mpaka hapo Mzee Robert Ngesa,alikuwa tayari ana majeraha usoni!Amechanika juu ya paji la uso,haamini kama mwanaye ndiye, anamtembezea kisago hicho kikali.

“Karanje yuko wapi?”

Nje,Jenipha na Dustan walikuwa wakishuhudia kila kitu,wakiwa kwenye kioo kikubwa, wanamtizama mawanamme huyu aliyewafanya wote wamshangae na wadhani wenda akili zake, hazipo sawasawa sababu haikuwezekana mtu mwenye akili timamu kumtesa baba yake mzazi, namna hiyo.

“Jenipha,fungua mlango.Ngesa keshapoteza!Atamuuwa”

Dustan,akashauri.

“Hapana subiri kidogo”

Maongezi yalifanyika nje,ndani kulikuwa na kipondo kinaendelea kisichokuwa cha kawaida!Ni Kweli,Ngesa alikuwa kama mwendawazimu,kwani aliuliza kwa sauti ya juu sambamba na kisago, kizito!Hasira zilikuwa,zimempanda kuliko kipimo chake!Akamvuta kwa nguvu na kumkaba shingoni tena!

“Yuko wapi Karanjeeeeeeeee?”

Ngesa alivyoona kazi yake,haifui dafu.Akaipiga meza na kuiburuza mpaka mlangoni, hiyo ilimaanisha kwamba mtu yoyote asiingie ndani kuikatisha operesheni yake,ni kweli hata kama ungekuwa nje na kusukuma mlango usingeweza kuingia, hiyo ndiyo ilikuwa niya na madhumuni ya Ngesa,ambaye tayari alikuwa kama kichaa!Alivyopiga jicho pembeni,akaona chuma kikubwa akakiokota, akakirudisha kwa nyuma kwa nguvu na kumpiga nacho baba yake,juu ya kichwa.Hakuishia hapo,akamuinua na kumburuza!

“Karanje yuko wapiii?”

Ngesa,akamshushia tena chuma cha mguu juu ya ugoko!Hapo ndipo Mzee huyu alipoona mateso, hayatoisha!

Timu ya watu tisa,ilikuwa mlangoni wanahangaika kuufungua mlango ili wamtoe Ngesa,tayari walihofia Ngesa angeweza kuuwa na hiyo ingekuwa kesi kwao!Walichofanya ni kujaribu kusukuma mlango huo, wakitumia nguvu nyingi,ukawa unasogea taratibu.

“Karanje yuko wapiiiii?”

Ngesa akauliza tena na kumpiga na chuma kingine cha usoni,Mzee Robert damu zilikuwa nyingi tayari usoni,zinamtiririka!

“Yuko wapi Karanjee?”

Hapohapo, mlango ukapigwa kwa nguvu puuu.Ngesa alivyoona hivyo akazidi kumshambulia Baba yake na chuma, alichoshika.

“Mta..fute Mh.George Kimpan..nga…”

Mzee Robert akaongea kwa tabu sana,kwa sauti ya chini hiyo ni kutokana na maumivu!

“Rais mstaa..fu Georg..e Kimpa..nga”

Kitendo cha kuongea hivyo,wana usalama nane wakawa wamefika na kumshika Ngesa kwa nyuma.

“Ngesa upo chini ya ulinzi”

Dustan akaongea kwa hasira,baadhi ya wana usalama wamkavaa na kumtoa nje kinguvu.

“Nataka kuongea na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania,Mh.Leslie”

Ngesa akasema na kuwasukuma kidogo wanaume hawa wa usalama, waliokuwa wamemshika wanamburuza na kumpeleka puta.

“Niachie,nataka kumpigia simu Rais Leslie.Sasa hivi!”

Hapo hapakuwa na kipingamizi kingine chochote kile,akaenda pembeni kidogo kandokando ya ukuta na kutoa simu mfukoni,akamtafuta Rais Leslie hewani!Simu,ikaita sana na baada ya dakika mbili kupita ndipo, ikapokelewa!

“Ngesa”

Upande wa pili wa simu,ukasikika.Alikuwa ni Rais Leslie, ndiye yupo kwenye laini.

“Pole na kazi Mh.Rais”

“Ahsante,umefikia wapi?”

“Mh.Rais ninavyoongea nawewe sasa hivi,nishajua wapi pa kumpata Karanje”

“Ni wapi Ngesa?”

“Ni habari za kushtusha sana”

“Kwanini?”

“Rais mstaafu,ndio anajuwa”

“Nani?”

“George Kimpanga”

“Whaaaaaat?”(Nini)

“Ndio hivyo Mh.Rais!Naomba kwenda kumuhoji ili nijuwe ni wapi Karanje alipo”

“Nani amekwambia, ni George?”

“Baba yangu mzazi,leo hii”

“Una uhakika?”

“Ndio”

“Unajuwa nini maana yake,Ngesa?”

“Naelewa Mh.Rais”

“Hilo swala niachie Mimi”

“Mh.Rais,hatoweza kutaja chochote!Naomba nimalize nilichokianza”

“Ngesa….”

“Mh.Rais niamini nachokwambia”

“Kuwa makini”

“Lakini Mh.Rais,nahitaji kitu kimoja”

“Kitu gani?”

“Sitoweza kuingia ndani ya nyumba yake bila kibali maalum,alafu isitoshe mimi sio usalama wa taifa”

“Nitaongea na Dustan,akupe kitambulisho.Uwe katika hiyo field na atakupa kibali”

“Ahsante Mh.Rais”

“Kuwa makini Ngesa”

“Sawa!Ahsante sana”

Rais Leslie,tayari presha ilikuwa juu!Hiyo ni baada ya kujuwa ya kwamba, Rais aliyestaafu pia yupo katika sakata hilo zito, ambalo lilifanya mpaka nchi yake itingishike,watanzania wasiokuwa na hatia wafe.Kutajiwa jina la George Kimpanga, ilifanya atandwe na hofu,mahusiano yake na raisi mstaafu yalikuwa ni makubwa sana,ndiyo maana jasho likawa linamtoka, hakuelewa ni kitu gani akifanye!Akazidi, kutafakari zaidi na zaidi ni maamuzi gani ayachukuwe,hapo ndipo alipopata wazo la kumpigia Mkuu wa Mkoa, RC Daudi Bashonga!

“Ushaondoka?……Njoo ofisini kwangu sasa hivi”

Hiyo ilimaanisha,kwamba RC Bashonga, bado yupo eneo hilo la ikulu,baada ya dakika mbili mlango wa ofisi ya Rais,ukafunguliwa.Mh Daud Bashonga,akaingia na kukaa juu ya kiti cha pembeni.

“Leslie,vipi?”

Wakati mwingine wakiwa wawili,Daud Bashonga humuita jina lake, moja kwa moja!

“Kuna kitu kizito nataka kukwambia”

Rais Leslie,akazungumza kwa unyonge na upole.

“Kitu gani?”

“George Kimpanga,ana husika kwenye hili la Karanje”

Moyo wa Bashonga ukapiga kwa nguvu,hofu ikamtanda!Kwani nyuma ya yote alikuwa anajua kila kitu,kumaanisha kwamba ilikuwa ni lazima siku moja mambo yamrudiye yeye na jina lake litwaje pia!

“Nani amekwambia?”

“Ngesa”

“Ngeeesaaaaa?”

“Ndio”

“Amejuaje?”

“Baba yake yupo Usalama wa taifa,chini ya ulinzi.Ndiyo amesema yote!Na hapa ninavyoongea, Ngesa yupo njiani kwenda nyumbani kwa George Kimpanga.Kumuhoji”

“Mungu waangu,unafanya nini Leslie?Unakosea sana”

“Kwanini?”

“Ngesa asiende,utaharibu kila kitu.Usimruhusu aende,mzuie!Haraka sana,nina maana yangu kukwambia hivyo”

“Una maana gani?”

“Atasema siri zote,unakumbuka zile pesa ulizopiga wewe na Mh.Kibote mwaka juzi!Unakumbuka ule mradi wa Umeme,ulivyosaini kuingia ili Magreth aachiwe china,alivyokamatwa na madawa ya Kulevya.Leslie,hili jambo litakutokea puani ni lazima George, ataongea kila kitu,mzuie Ngesa na umuweke chini ya ulinzi haraka sana”

Bashonga,aliongea huku akihaha na maneno hayo pia yalimuogopesha Rais Leslie,hususani alivyokumbuka baadhi ya vitu viovu alivyofanya,akatulia kwa muda kidogo na kuinua mkonga wa simu yake ya mezani.


********

Ilikuwa ni lazima siku hiyo Ngesa aende Mbweni,alipokuwa anaishi Rais Mstaafu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh.George Kimpanga.Ambaye alikuwa bado analindwa na walinzi,kutokana na heshima pamoja na wadhifa aliokuwa nao!Hiyo ilimaanisha asingeweza kuingia nyumbani kwake kiholela, mpaka apewe ushirikiano mkubwa sana, ndiyo maana alikuwa ndani ya chumba kidogo,anavaa suti nyeusi.Akaweka tai yake vizuri kooni,niya yake ilikuwa ni kufanana na jeshi la usalama wa taifa,akiamini kwamba ingekuwa rahisi kuingia ndani ya Jumba la Mh.George Kimpanga.Kila kitu, kikaonekana kwenda sawa kwani baada ya hapo,akachukuwa bastola aliyopewa pamoja na kitambulisho maalum!

“Kacha kacha”

Ngesa,akaikoki bastola na kuiweka kiuoni.Akaifunika na koti la suti.

“Tunaweza tukaenda”

Alivyotoka nje,wakaanza kuongozana na Dustan,mpaka kwenye maegesho ya magari, ambapo gari liliendeshwa na Dustan,Ngesa akawa kushoto!Safari ikaanza mara moja.Kabla ya kufika mita kumi na saba,simu ya Dustan ikaita!Akaitoa kutoka mfukoni na kuangalia,aliyekuwa akipiga ni Jenipha,akaipokea na kuiweka sikioni!

“Usitaje jina langu Dustan.Upo na Ngesa?Sema, ndio au hapana”

Sauti hiyo ilimfanya Dustan,atoe simu na kuiweka sikio la kulia, kama mwana usalama alielewa kuna jambo nyeti, alitakiwa kulifanya.

“Ndio”

Akajibu kifupi,Ngesa akageuka na kumuangalia.Kuna kitu alijifunza kutoka kwenye simu hiyo ingawa hakuwa mwenye uhakika.

“Sikiliza kwa makini sana.Rais Leslie,ameghaili hiyo operesheni”

“Kwanini?”

“Sijui,fanya unavyojua Ngesa asijue.Muweke hata kituo chochote cha polisi, awekwe chini ya ulinzi.Ni amri kutoka kwa Rais”

“Sawa Afande Tobi.Nakuja hapo”

Dustan akazuga na kukata simu, akatabasamu kidogo huku akimuangalia, Ngesa aliyekuwa pembeni yake.

“Afande Tobi huyu,anasema nikampitie kituo cha polisi hapo mbele”

Niya ya Dustan,ilikuwa ni kumuweka Ngesa kituo cha polisi kama alivyopewa amri, ndiyo maana akazuga!Lakini cha kushangaza na kilichomfanya ahisi mkojo unataka kumpenya ni baada ya Ngesa kutoa bastola na kumuwekea kichwani,juu ya paji la uso.

“Nusu saa lililopita,nilitaka kumuuwa baba yangu!Sababu alikataa kunipa ushirikiano,nadhani unajua nini maana yake”

“Nge..ngesa”

Dustan akapata kiwewe!

“Paki gari pembeni,nadhani unanijua vizuri,sitorudia mara mbili”

Dustan,akawasha Hendiketa.Kukiuka amri ya Ngesa, kulimaanisha kujichimbia kaburi,kwani kama aliweza kumtesa baba yake mzazi na kutaka kumuuwa isingekuwa vigumu kufanya kwake ndani ya dakika moja,ndiyo maana akaweka gari kando bila kubisha!

“Lisogeze ukutani.Nimemsikia Jenipha,kwenye simu!Zima gari nipe funguo”

Dustan,akatii kwani bastola ilikuwa kichwani kwake kidole cha Ngesa kipo ndani ya triga,hacheki.Hapohapo Ngesa,akamvuta na kumkaba shingo kwa nguvu,kwa takribani dakika moja nzima.

“Tulia”

Dustan,akawa amezirai.Alichofanya, Ngesa ni kumtoa juu ya usukani na kumuweka viti vya nyuma,akamfunga pingu na kuingia nyuma ya usukani.

Jinsi alivyorudisha gari nyuma ilitisha kwani ilifanya matairi yazunguke na kutimua vumbi lililofanya watu,waanze kukohoa!Hapohapo akaingiza gari barabarani kwa safari moja tu,kwenda kuonana na George Kimpanga,ana kwa ana!


 Kasi aliyotumia Ngesa kuendesha gari,ilitishia amani.Hiyo ilitokana nayeye kupita njia za panya ili awahi kufika,huko ndipo alipopata nafasi ya kunyoosha mguu!Hakukuwa na msongamano wa magari,akaibukia Magomeni,akazidi kusonga mbele mpaka alipotokeza Kinondoni huko alikunja na kuitafuta barabara inayoelekea Tandale kwa Tumbo,akazidi kusonga mbele mpaka alipotokeza Sinza Mori!Akanyoosha moja kwa moja,akatokeza Mwenge,kanisa la Kakobe, hapo ndipo ilimbidi asimame ili atafute njia nyingine mbadala.Ilikuwa ni lazima afike Mbweni, akutane na Mh.George Kimpanga,amueleze kile anachotaka kujua!Alikuwa ana kila sababu ya kuwahi kwani bila ya kufanya hivyo,kitumbua kingeingia mchanga.Alishaelewa jambo alilokuwa analifanya, lilikuwa ni hatari kuliko hatari yenyewe.

“Griii griiii”

Alihisi kuchanganyikiwa baada ya kusikia simu ya Dustan inaita,akageuka nyuma!Dustan, alikuwa bado amezirai hana fahamu ya juu ya jambo linaloendelea,simu ikaita tena!Ikabidi,ageuke taratibu na kuitoa mfukoni kwa Dustan,alikuwa ni Jenipha anapiga!Akaiacha mpaka ikakata,ikaita tena,ikakata.Ilivyoita kwa mara ya tisa na kukata,yake ikawa inaita.Alivyotoa akaona jina Jenipha juu ya kioo,hapohapo akaipokea na kuiweka sikioni!

“Jenipha”

Ngesa akasema baada ya kupokea simu.

“Upo na Dustan?”

Jenipha akauliza,akitaka kutingisha kiberiti.

“Simu ameacha ndani ya gari”

“Kwani mpo wapi?”

“Hapa kituo cha polisi”

“Kituo kipi?”

“Mabatini”

“Yeye yuko wapi?”

“Ameingia kituoni,Jenipha kuna nini?Mbona Dustan,ananicheleweshea muda”

“Hapana msubiri,kuna mambo ya kiusalama zaidi”

“Sawa namsubiri”

Kwa Jenipha alijiona yeye ni mjanja kumbe Ngesa ni mjanja zaidi yake!Alivyokata simu,akazidi kusonga mbele,dakika thelathini baadaye akawa amefika Tegeta kwa ndevu,akakunja kushoto na kuingia vichololoni,akasimamisha gari na kushuka!Akamtoa Dustan nje ya gari na kumuweka pembezoni karibu na nguzo,akiwa mwenye pingu.Akamsachi mifukoni na kuchukua simu yake nyingine!Baada ya hapo,akarudi ndani ya gari na kuendelea na safari yake.Tayari alishaelewa jambo alilokuwa amelifanya ni hatari na ndani ya masaa machache, serikali ya jamhuri ya Muungano ingemsaka kwa wudi na uvumba,ndiyo maana alitaka kufanya jambo hilo kwa kasi ya kimondo!

Akazidi kuchanja mbuga,alivyofika Mbweni.Kituo cha mabasi akaweka gari kando,baada ya kuona barabara mbili!Hapo alionekana kuchanganyikiwa, hakuelewa ni wapi kwa Mh.George Kimpanga.Hakuwa na njia nyingine ya ziada,zaidi ya kuuliza.Akateremsha kioo cha gari.

“Samahani broo”

Akamsimamisha mpita njia mmoja!

“Bila samahani”

“Nahisi nimepotea,kwa Mheshimiwa Kimpanga ni wapi?”

Jina hilo hata kama ungeulizia kutokea Tegeta,ungeelekezwa kwani ni Rais Mstaafu, eneo alilokuwa anaishi lilikuwa maarufu sana!

“Ni kule,unanyoosha na hii barabara.Moja kwa moja!Unakutana na barabara ya vumbi,mtaa wa kwanza wa pili,kushoto kwako.Kuna gorofa jeupe.Ndio hapohapo”

Maelekezo aliyokuwa anatoa jamaa huyo,hata kama ungekuwa bubu ungeleewa kwani alitumia mikono yake kumuelekeza Ngesa aliyekuwa ndani ya gari, kanyonga suti na tai.

“Shukrani”

“Sawa tajiri”

Ngesa,akapiga gia na kulitimua gari.Maelezo aliyoambiwa yakamfikisha baada ya dakika mbili,akawa yupo nje.Akaweka gari kando ili kuangalia mazingira na namna ya kuingia ndani ya jumba hilo, ambapo nje kulikuwa na walinzi wawili!Akachukuwa kitambulisho maaluum,alichokuwa amepewa na kukiweka mfukoni,akawasha gari na kuliweka vizuri akalisogeza mpaka getini,akashusha kioo!Na kumtizama mlinzi,hakucheka!

“Habari kiongozi”

Mlinzi akatoa salam baada ya kuona Ngesa kaweka ngumu,hacheki amenuna yupo siriazi.

“Nzuri,nahitaji kuonana na Mheshimiwa”

“Una appointment?”

“Mimi ni mtu wa usalama,nina appointment pia”

“Kitambulisho”

Ngesa,akatoa kitambulisho na kuonesha.Askari akafanya kazi yake,akakiangalia kwa umakini na kumtizama Ngesa kama sura ya kwenye kitambulisho na yake zinarandana.

“Appointment sheet?”

Ngesa,akatoa karatasi maalum,ilivyokaguliwa akaingiza gari ndani.

“Pita kule”

Mlinzi mwingine,akamwambia.Jumba lilikuwa kubwa na walinzi walikuwa wakiranda huku na kule,akajishika vizuri kwenye kiuno ili kuhakikisha kama bastola yake ipo.Akazidi kusonga mbele na kuingia ndani.


*******

Shingo yake ilikuwa inauma ajabu,kumbukumbku zake zilikuwa zinarudi taratibu mno.Picha iliyomjia kwa haraka ni Ngesa kumuwekea bastola kichwani,alivyofumbua macho yake akajikuta yupo kandokando ya nguzo kubwa ya umeme,mkononi ana pingu.Akili yake moja kwa moja ikamtuma kwa Ngesa,kwamba huko alipo anafanya jambo la hatari sana!Bado alishindwa kumtafakari binadamu huyo kama ni mtu wa kawaida ama ni mzimu, sababu haikuwezekana hata kidogo kwa mtu mwenye akili timamu kufanya jambo la hatari namna hiyo.Hakutaka kuendelea kubaki alipo,ilikuwa ni lazima atoe taarifa ngazi za juu ili mambo yasiende mbali,alivyo na pingu zake akasimama na kutafuta barabara ya lami,akasimama huku akipunga mikono ili apewe msaada lakini cha ajabu,magari yalimpita.Akaona njia sahihi ni kusimama katikakti ya barabara.Isingekuwa kupata akili hiyo magari yote yangempita kwani alionekana kama mtu aliyerukwa na akili,Escudo nyeusi ilipiga breki miguuni mwake,hapohapo akaruka mpaka kwenye kioo cha gari.

“Mimi ni askari,naomba simu yako”

Dustan,alizungumza kwa haraka kama mtu aliyemeza kaa la moto.Hiyo ilifanya mzee aliyekuwa ndani ya gari adhani wenda mtu aliyekuwa pembeni yake ni muhalifu,katika kujishauri nini akifanye akashtukia kapigwa kiwiko cha mdomo,Dustan akaingiza mkono ndani na kuchukuwa simu iliyokuwa mfukoni mwa shati la mzee huyo.Akatembea pembeni na kupiga namba za usalama wa taifa, makao makuu.

“Naomba niunganishe na Jenipha,code namba zake ni 4457.Haraka sana”

Kitendo cha kuongea maneno hayo,simu yake ikasubirishwa.Sekunde nne baadaye Jenipha akawa yupo kwenye laini.

“Jenipha,unaongea na Dustan”

“Dustan?Uko wapi?Mbona simu yako hupokei?”

“Ngesa,ameondoka na gari”

“Niniiii?Sijakuelewa?Kivipi?”

“Sijui imekuaje lakini alikusikia”

“Mungu wangu,Rais Leslie anajuwa?”

“Hapana”

“Inabidi aambiwe sasa hivi”

“Subiri kwanza Je..”

“Inabidi ufanye hivyo mapema,kabla Ngesa hajafika”

“Nataka niende mwenyewe”

“Hapana,mshirikishe Rais,mwambie kila kitu.Au unamwogopa?”

“Hapana”

“Au,mimi nitamueleza”

“Sawa,acha mimi nimuwahi Ngesa,naenda Mbweni.Tutawasiliana”

“Okay”

Pingu ndizo zilikuwa kikwazo kikubwa cha kumfanya asitembee kwa uhuru,alichofanya kwa wakati huo ni kulivua shati la juu,akazifunika ili mtu yoyote asione,akatembea kwa kama umbali wa mita kumi na kuingia ndani ya kichaka chenye mitimiti,huko alianza kuangalia chini akionekana kutafuta kitu kisichojulikana,alivyopiga jicho chini pembeni, akaona spoko ya baiskeli iliyokuwa nyembamba sana.Akaokota na kwenda kukaa chini ya mti mkubwa.

Akaangalia matundu ya pingu kwa umakini,akapitisha spoko ndani yake,hakuelewa kama zoezi analotaka kulifanya litazaa matunda lakini alijipa moyo sababu, mbinu hiyo alifundishwa akiwa mafunzoni namna ya kupachua pingili za pingu,akajaribu zoezi hilo kwa shida sababu alikuwa amefungwa mikono yote kwa mbele,hivyo alitumia kidole kilichoshika chuma hiko kidogo kuchokonoa.

“Karachaa”

Mlio ulisikika,Dustan akatabasamu sababu Pingu ziliachia.Akafungua na mkono wa pili,hatimaye mikono yake ikawa huru.Akakimbilia barabarani na kufanya zoezi alilofanya mara ya kwanza.Gari aina ya Nissan patrol,ikapiga breki karibu yake.

“Mzee toka ndani ya ga…”

Dustan hakuwa na muda wa kumalizia sentensi yake,akamteremsha jamaa aliyekuwa nyuma ya usukani na kumtoa nje,alivyoingia ndani ya usukani,akapiga gia.Namna gari lilivyotoka ilitishia amani kwani tairi zilizunguka kwa kasi ya ajabu.

******

Mlango wa Mh.George Kimpanga,ulifunguliwa Ngesa akaingia ndani na kumkuta yupo nyuma ya meza kubwa,amekaa anamsubiri.Ilielekea ujio wa Ngesa aliufahamu sababu tangu anaingia getini,alimuona kupitia Kamera na sura hiyo haikuwa ngeni kabisa machoni mwake,mbaya zaidi alivyoonesha kibali kutoka ikulu, ikamfanya awe na amani kwani alijuwa ya kuwa ametumwa na Rais Leslie.

“Karibu Ngesa”

Mh.Kimpanga akasema huku akitabasamu lakini kabla ya kukaa vizuri simu yake,ikaita kutokea mfukoni.Alivyoitoa akaona jina Rais Leslie, juu ya kioo!

“Yes,Leslie za masiku?”

Alivyopokea simu,akaropoka hiyo ilimfanya Ngesa amuangalie machoni.Kadri sekunde zilivyozidi kwenda mbele,sura ya Mh.Kimpanga ilikuwa ikibadilika,hapo ndipo Ngesa akajua kuna mambo hayapo sawa ni lazima tu,Rais Leslie ana taarifa tayari.

“Weka simu chini”

Ngesa,akakatisha maongezi hayo akiwa na bastola mkononi,hakutaka kumpa nafasi Mh.Kimpanga aendelee na mazungumzo kwani kwa kufanya hivyo ingekuwa ni upotevu wa muda,ndiyo maana akachomoa bastola na kumuwekea usawa wa kichwani.

“Kijana weka bastola yako chini”

Mh.Kimpanga akazungumza bila wasiwasi,hakuelewa akili ya Ngesa sio nzuri.

“Nimekwambia weka simu chini”

Hapo,George Kimpanga akakata simu na kuiweka juu ya meza.

“Sogea huku,fanya haraka”

“Una..unataka nini?”

“Kujua ukweli,nataka kujua Karanje alipo”

“Sijui,unaongelea nini”

Haikujulikana ni sekunde ngapi alitumia Ngesa kumfikia George Kimpanga na kumpiga na kitako cha bastola kichwani.

“Simama,Karanje yuko wapi?”

“Sijui unaongelea nini”

George Kimpanga,hakuelewa anacheza na moto wa kifuu.Akawa anajibu kwa nyodo akidhani wenda Ngesa ni mtu wa mchezomchezo,akashikwa shati na kupigwa kichwa cha pua,akawekewa bastola shingoni.

“Karanje yuko wapi?”

Mambo yaliyokuwa yanafanyika ndani ya chumba hiko,yalikuwa ni kimya kimya ingawa walinzi walikuwa nje lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa ana habari yakuwa tajiri yao,yupo mateka.Mpaka simu ilivyopigwa kutoka makao makuu ya jeshi la polisi, kutoka kituo cha Oysterbay,wakapewa taarifa ya kuwa Mh.George Kimpanga yupo mateka hivyo wafanye wanavyojuwa, Ngesa asiondoke eneo hilo bila kuvishwa pingu.Hazikupita hata dakika mbili,diffenda nane zikapiga msele nje ya geti la Mh.George Kimpanga!

“Bado yupo?”

Kamishna wa polisi wa kanda ya Ilala Kamanda Salvatory Mkude ,akauliza baada ya kushuka kutoka ndani ya diffenda.

“Ndio mkuu”

“Mheshimiwa yupo chumba gani?”

“Chumba cha mkutano”

“Sawa”

Kilichofanyika hapo,ni Kamanda Salvatory Mkude kuwapanga maaskari wote!Wakaiweka nyumba katikati ikawa imezingirwa na jeshi la polisi,wakiwa na mitutu mikononi mwao!Hata ingekuwaje,Ngesa asingeweza kutoka ndani ya jumba hilo bila kutiwa mikononi mwa sheria.Kipondo alichokuwa anakula Geogre Kimpanga ndani,kilitisha.

Tayari alikuwa amelowa damu,Ngesa hakuishia hapo,akachukua peni juu ya meza,akamuwekea karibu na jicho kwa niya ya kumtoboa jicho.

“Karanje yuko wapiiiii?Kinachofuata hapa,nakutoboa macho!Na utaenda kuwa kipofu ama chongo kwa ajili ya mpumbavu mmoja,unayemficha”

Ngesa hakutania,akaishika vizuri Shingo Mh.George Kimpanga,akaweka ncha ya kalamu vizuri ili kuitumbukiza jichoni.

“Derrick Ngesaaaaaaa”

Sauti hiyo ilimshtua Ngesa,kilikuwa ni kipaza sauti kutokea nje!Akatembea na kuchungulia dirishani,akaona lundo la maaskari wengi wasio na idadi kamili.

“Najua upo humo ndaaniiii,kwa usalama wako toka nje mikono ikiwa juu hewani.Upo chini ya ulinzi”

Kila kilichozungumzwa nje,kilimfikia Ngesa ndani.Haikuwa rahisi kwake kukubali kukamatwa bila kumalizia zoezi lake,ilikuwa ni lazima afanye hivyo vinginevyo kifungo kingemuhusu.

“Ngesaaaa,tunahesabu mpaka kumi..Usipotoka,tutaingia sisi!Hatutaki kufika huko,toka nje ya nyumba.Jisalimishe,huna pa kukimbia nyumba yote imezungukwa na polisi.Toka kwa usalama wako”

Hilo lilikuwa ni kosa kubwa kusema kwamba nyumba imezingirwa,ilikuwa ni lazima Ngesa atumie akili ya ziada kutoka nje ya jumba hilo.

“Ha..uwezi kutoka Nge..sa umekwi..sha!Utaenda..Jelaaa”

George Kimpanga akiwa juu ya kiti,aliongea kwa taabu sana!Damu zilikuwa zinamtoka,matumaini yake yakarudi upya,akajua tayari ukombozi upo mbioni kutokea!Ngesa akatulia kidogo,akamvuta George Kimapanga,akamuweka mbele kama ngao,akachukuwa bastola na kumuwekea kichwani.Akawa anamsukuma kutoka nje,alivyotokeza mlangoni.

“Paaaaaaaa”

Ngesa akaachia risasi moja juu hewani,akairudisha tena kichwani kwa Mh.George Kimpanga!

“Wekeni silaha zenu chini”

Ngesa alizungumza kwa sauti huku akiwatizama askari waliokuwa mbele yake,wengi tena wameshika mitutu mikononi mwao, tayari kwa kumwaga risasi.

“Wekeni silaha zenu chini,Mojaaaa”

Jambo hilo lilifanya mkuu wa Kikosi,nayeye apaze sauti.

“Ngesa,weka bastola chini.Upo chini ya ulinzi”

“Paaaaaaaaa”

Askari wote wakashtuka na kuanza kuogopa,baada ya risasi kulia na ilikuwa imepenya mguuni mwa Mh.George Kimpanga, Ngesa ndiye aliyefanya hivyo,hakuwa na masihara hata kidogo.

“Wekeni silaha chiniii mbiliiii.Nitamuuwa”

Ngesa akaongea huku akitetemeka kwa hasira,alikuwa tayari keshampiga risasi Mh.Kimpanga na kwa wakati huo, alikuwa akipiga kelele kama mtoto mdogo.Hiyo ikafanya mkuu wa Kituo ajue Ngesa,hatanii na wangefanya mchezo Mh.Kimpanga angekufa, ilikuwa ni lazima wasalimu amri kwanza.

“Askari wote,wekeni silaha chini”

Hatimaye mkuu wa kikosi akatoa amri hiyo.

“Nasema askari wote,wekeni silaha chini”

Mkuu wa kikosi,akasisitiza tena, hapo ndipo jeshi lote likafuata amri hiyo,wakaweka mitutu yao chini.Ngesa akamshika Mh.George Kimpanga na kuanza kumvuta kwa nguvu kwani alikuwa akivuja damu nyingi mguuni.Wakatoka mpaka nje,ambapo kulikuwa na gari,akamuingiza mlango wa nyuma.

“Paa! Paa! Paaaa! Paaaaa! Paaaaa!”

Alichofanya Ngesa ni kupiga risasi matairi ya magari yaliyokuwa mbele, alifanya hivyo ili wasimfuatilie kwa nyuma,kitendo cha kuingia ndani ya gari alilitoa gari kwa kasi ya umeme.Askari wote wakabaki wameduwaa!

“Sikutaka kufika huko Mh.Kimpanga,niambie ukweli.Karanje yuko wapi?”

Ngesa akauliza tena na kugeuza shingo yake nyuma,akimtizama Mh,George Kimpanga ambaye bado alikuwa anaugulia mguu wake,unaovuja damu.

“Yu..po Ken..yaaa ana..”

Kabla ya Mh.George Kimpanga kumalizia sentensi yake,ulitokea mtikisiko mkubwa sana kwa nyuma.Gari ya Ngesa ilikuwa imegongwa kwa pembeni,alivyogeuza shingo akaona Nissan Patrol ya rangi nyeusi.

Alivyozungusha usukani vizuri na kuweka gari barabarani, akagundua aliyekuwa anatumia gari hiyo ni Dustan.

“Shiiit”

Ngesa akakema,akakanyaga mafuta mengi lakini haikuwa rahisi kuliacha gari hilo aina ya Nissan Patrol.Dustan alikuwa ana usongo kuliko kawaida, ndiyo maana alikuwa anakula sahani moja na Ngesa,ilikuwa ni lazima amuweke mikononi mwa Sheria ilia CV yake irudi kwenye mstari.Akazidi kumgonga kwa nyuma,alivyoona haitoshi,akampita kwa mbele na kuanza kumgonga kwa ubavuni.

“Paaaaa”

Risasi ikasikika Ngesa alikuwa akijaribu kujitetea akilipiga gari la Dustan,lakini zilipita kwenye kioo cha mbele kikapasuka.Hapo Dustan akazungusha usukani kwa nguvu na kuligonga kwa nguvu gari la Ngesa ubavuni,kutokana na mwendokasi aliokuwa anatumia Ngesa, ikamfanya ashindwe kulikwepa jiwe kwa haraka,akagonga gema lililokuwa pembezoni mwa barabara,alivyojaribu kurudisha gari kwenye mstari,akawa amechelewa kwani lilimshinda na kumpeleka mabondeni,huko lilibiringika kama mpira mpaka chini kabisa!Dustan,alishuhudia kwa macho yake namna ambavyo gari alilopanda Ngesa,lilivyokuwa linabiringika.

Akapiga breki,akashuka kwa tahadhari na kuingia katikati ya miti, kulifuata gari la Ngesa lilipo!Akatembea taratibu kwa tahadhari,alivyozidi kusonga mbele akaliona,lilikuwa limebinuka,chini- juu,juu chini, yaani matairi yapo kwa juu!Hiyo ilimfanya,atembee kwa wasiwasi kidogo kwani alijua Ngesa ni hatari na isitoshe ana silaha ya moto!Akaliruka jiwe na kusonga mbele,alivyolikaribia gari akajificha nyuma ya mti mkubwa akisubiri Ngesa atoke,amvae! Lakini alikaa hapo kwa dakika mbili nzima bila,kumuona Ngesa!Akatembea taratibu mpaka kwenye gari,alivyoinama na kuchungulia kiti cha mbele akapigwa na mshtuko wa ajabu kwani siti ilikuwa nyeupe,Ngesa hayupo!Ghafla,akahisi kama kuna kichuma kwenye kisogo chake, kimemgusa.

“Nilikwambia,usinifuatilie hukusikia.Nakuuwa Dustan”

Dustan,akawa amewekewa bastola kichwani.Tayari yupo mateka!


 Dustan alipata ngekewa,alihisi tumbo linamuuma, hakuelewa nila kuharisha ama uwoga!Nyuma yake alikuwa amesimama Ngesa,mbaya zaidi mdomo wa bastola upo kwenye kisogo chake, kumaanisha ya kuwa muda wowote ule ubongo wake engechenguliwa na kusambaratishwa na risasi,hilo halikuwa na ubishi wowote ule kwani akili za Ngesa alizifahamu, japokuwa alimjuwa kwa muda mfupi tu.Kile alichokuwa anawaza Dustan, ndicho kilikuwa kichwani kwa Mwanamme huyo Ngesa aliyekuwa mwenye hasira za mbogo,kitendo cha Dustan,kuingilia Operesheni yake kilimpandisha mori ndiyo maana nafsi yake ilimwambia ampige risasi amuuwe sababu huyo ndiye alikuwa kama kikwazo kwake,akaanza kusogeza taratibu kidole chake karibu na triga,kumaanisha kitendo cha kuvuta triga risasi ingechomoka ndani ya chemba na kuumwaga ubongo wa Dustan chini,akiwa katika jaribio hilo la kutaka kumuuwa Dustan,ghafla nafsi nyingine ikamwambia aachane naye kwanza.

“Wiiuuu! Wiuuu! Wiuuuuu”

Mara ghafla ving’ora vya magari ya polisi vikaanza kusikika kwa mbali,hiyo ilimaanisha kuendelea kubaki eneo hilo polisi wangemtia mikononi na wenda ungekuwa mwisho wake kuishi kwani tayari alikuwa amejiingiza kwenye majanga makubwa sana.

Ilikuwa ni bora ucheze na kitu chochote kile duniani kuliko kucheza na Serikali,ndiyo maana Ngesa hakutaka kukubali kushindwa kirahisi mpaka ukweli uwe hadharani na huo ndio ungefanya yeye awe huru.

“Twende huku,mtoe Mheshimiwa ndani ya gari haraka sana.Kabla sijabadili maamuzi”

Dustan akageuka na kuwa kama mfuasi wa Ngesa kwani kila alichosema yeye alitii ili tu kutetea roho yake,akatembea taratibu mpaka karibu kabisa na gari lililopinduka,akainama na kuingiza shingo ndani, ambapo huko kulikuwa na Mheshimiwa George Kimpanga,anavuja damu nyingi sana!Ana majeraha usoni,damu zinamchuluzika mguuni kutokana na risasi aliyopigwa na Ngesa.

“Fanya haraka Dustan”

Ngesa akasema kwa hasira,Dustan akaanza kumvuta majeruhi huyo,akamtoa kabisa nje ya gari.Ngesa akasimama nyuma yao,akaanza kuwaamrisha wasonge mbele.

“Mheshimiwa,sina muda wa kupoteza!Karanje yuko wapi?”

Ngesa akauliza,hakujali Mheshimiwa ana maumivu kiasi gani,alichotaka yeye kujua ni wapi Brigedia Karanje alipo.Dustan alibaki kimya, kazi yake ilikuwa ni kumkokota Mheshimwa George,haikuwa kazi rahisi hata kidogo kwani mikono ya Mheshimiwa aliiviringisha shingoni kwake akawa anatembea naye kwa tahadhari kubwa.

“Uhai wako sasa hivi,upo mikononi mwako mwenyewe.Yuko wapi Karanje?”

“Nge…sa,nakuonea huru..ma sana Mdogo wang..u”

Mh.George Kimpanga alizungumza kwa tabu na Mateso, akijaribu kumwambia Ngesa ni namna gani alivyojiingiza kwenye mtandao wa hatari namna hiyo.

“Nachotaka kujua ni wapi Karanje alipo”

“Yu..po Kenya Nairobi.Kwa usalama wa..ko achana na hayo Mam..bo,Karanje ni Mtu hatari”

“Kwanini yupo Kenya,anafanya nini?”

“Kun..a sumu kali ya Kemikali,aina ya DDT Fresher ni sumu hatari sana,ana mpango wa kua...ngamiza mamia na Ma..elfu ya watu”

“Niniiiii?”

“Na hivi navyo..ongea nawewe,tayari keshapata hi..yo sumu..Nge..sa mdogo wan..gu!Katika hi..lo jambo wat..u wengi wa serikali…ni wana husika,sio mtu mmoja”

“Nitajie majina yao”

“Nach..okwam.bia kaa mb..”

Mh.George Kimpanga alizungumza kwa shida mno,damu zilikuwa zinamtoka kuliko kawaida, ilikuwa ni wazi kabisa alikuwa akienda kupoteza maisha kama sio fahamu zake kwani alipoteza damu nyingi sana mwilini,ndiyo maana baada ya kupiga hatua nyingine tano akadondoka chini kama mzigo puu!Dustan nayeye akaenda chini bila kupenda,hapo ilibidi watulie kidogo,japokuwa walikuwa wakisikia ving’ora vya polisi lakini ilibidi kwanza wakae hapohapo.

“Nge..sa nin..a familia,nina mke wangu anaitwa Vanessa James,nin..a watoto wawili naomba nikifa nitunzi..e.Rais Leslie ni mtu mzuri sa..na lakini kuna watu wachache wanat..ka kuchafua jina la..ke”

“Mheshiwa,nitajie majina ya watu wanaohusika”

“Maka..mu wa Rai..s pia yup… Akksss aaaarggg”

Alivyosema maneno hayo,akaanza kukoroma kama kondoo aliyechomwa kisu cha shingo,damu zilikuwa zikimtoka mdomoni,akamshika kwa nguvu shati Ngesa,akawa kama mtu anayetaka kujaribu kuongea kitu lakini anashindwa.Kwa haraka Dustan akaanza kumkandamiza kwenye mapafu, kazi ya Ngesa yeye ilikuwa ni kuuliza maswali tu,alitaka kujua ni nani anahusika kwenye sakata hilo zima.

“Mheshiwa,nitajie majina”

“Mak..amu wa Rais..Mkuuu wa Mk…arrggg arrggggg”

Hapohapo Mh.George Kimpanga,akatulia.Ngesa alivyomshika shingo akagundua tayari Mheshimiwa amefariki dunia,akabana meno kwa hasira na kumtizama Dustan,ambaye hata yeye alionekana kuchanganyikiwa.

“Amekufa,songa mbele”

Mwanamme huyu sijui alikuwa ana roho gani kwani kifo cha Mh.George Kimpanga,hakikumtingisha moyo hata kidogo kwake yeye ilikuwa ni shwari tu.Ndiyo maana alimtaka Dustan asonge mbele na kila kitu kingejulikana mbele ya safari,walivyokaribia barabara ya lami wakasikia tena ving’ora vya magari ya polisi.Ngesa akamtaka Dustan arudi nyuma na atulie kama maji mtungini.

“Ukifanya kitu chochote cha kipumbavu,nakuuwa.Nadhani unanifahamu”

Hilo lilikuwa wazi kabisa ya kwamba maisha ya Dustan yalikuwa mikononi mwake mwenyewe,kwenda kinyume na Ngesa anavyotaka, kilimaanisha kujichimbia mwenyewe kaburi, hivyo aliendelea kuwa mdogo kama kidonge cha pilton,wakaanza kuona Diffenda zinapita mbilimbili tena kwa kasi ya upepo,ikapita ya kwanza ya pili,ya tatu.Dustan alikuwa akizihesabu,akamtizama Ngesa aliyekuwa mbele yake,kampa kisogo,akaangalia chini pembeni akaonekana kama aliyekuwa anatafuta kitu,akatupa macho yake huku na kule.Mbele yake kidogo akaona mti mkubwa kiasi.Akamtizama Ngesa mara mbilimbili,jambo alilokuwa mbioni kulifanya lilimfanya aogope endapo angebugi stepu.Ilikuwa ni lazima afanye zoezi hilo kwa umakini zaidi,ndiyo maana alianza kutetemeka.Ngesa akamgeukia!Akamtizama kwa kama sekunde tano nzima bila kusema chochote kile.Laiti angejua kichwani kwa Dustan kulikuwa kuna nini,angekuwa makini zaidi.Kwa kasi ya roketi Dustan akaokota gogo la mti,akampiga nalo Ngesa kichwani puu!Hakuchelewa hapohapo,akamrukia na kuukamata mkono wa Ngesa ulioshika bastola,wakaanza kushindana nguvu,bastola ikadondoka kando,huku na kule wakadondoshana chini,kilichofuata hapo kilikuwa ni kupigana misumbwi, baada ya kusimama kila mtu akakunja ngumi,Dustan akarusha ngumi lakini ikapita hewani sababu Ngesa aliinama kidogo na huko hakufanya makosa kwani alimpiga Dustan ngumi za harakaharaka tatu za mbavu,alivyorudi juu akamvuta mkono na kumrusha kwa nguvu pembeni,ki utaalam Dustan baada ya kutua chini hapohapo akajibinua kwa sambasoti,akakaa sawa na kutisha kama anarusha ngumi,Ngesa akayumba alivyokaa sawa akapokea nayeye ngumi ya pua.Huo ndio ukawa mwanya wa Dustan kurusha ngumi kama mvua.Alipokosea ni kurusha teke ambalo Ngesa alilidaka na kumtuliza na kifuti,Dustan chini.Mungu akawa kwake sababu alidondoka karibu na bastola.

“Paa! Paaaa!”

Baada ya kuokota akaifyatua, akiwa ameelekeza juu hewani,hapo ilibidi Ngesa atulie kidogo kwani alijua nini maana ya bastola.

“Piga magoti chini mikono nyuma,haraka Ngesa”

Mlio wa bastola ulifanya maaskari waliokuwa katika msako wa kumtafuta Ngesa kwa wudi na uvumba,wapige breki na kuelekea upande wa bastola ulipolia wakiwa na mititu yao tayari kwa vita hiyo ambayo kwao ilikuwa nzito kwani walimfahamu Ngesa ya kuwa ni moto wa kuotea Mbali.

Dakika moja ikawa nyingi wakawa wameuzunguka msitu wakiwa na mitutu yao,wakasogea karibu na kumuona Dustan akiwa ameshika bastola Ngesa yupo chini,amepiga magoti mikono yake yote miwili kaizungusha nyuma ya kisogo chake,kumaanisha amesalimu amri.

“Upo chini ya ulinzi simama Ngesa”

Dustan akazungumza kwa ukali,akampiga kifuti cha nguvu Ngesa akadondoka chini akamuinua na kumtandika kibao cha uso kwa hasira.

“Afande nipe pingu,George Kimpanga amefariki dunia,yupo kule chini”

Alichokitaka Dustan ndicho kilichotokea kwani alipewa pingu na hapohapo akaizungusha mikono ya Ngesa na kuifunga pingu kwa nyuma.

“Simama.Leo ndio mwisho wako, bloodfool”

Dustan akazungumza kwa sauti ya hasira huku akimuinua Ngesa kwa nguvu,askari wote waliomuona walimpongeza kwani kazi ya kumtia Ngesa mikononi waliamini haikuwa lelemama hata kidogo.Walivyofika nyuma ya gari kabla ya Ngesa kupakiwa, Dustan akasimama na kumuangalia!

“Funguo hizi hapa,kama tulivyopanga!Leo tuonane nyumbani kwangu saa moja usiku.Usikose”

Kumbe Kilichokuwa kinafanyika mbele ya maaskari baina ya watu hawa wawili Dustan na Ngesa,kilikuwa ni maigizo.Walikuwa wamepanga kuwa kitu kimoja.Na ili Dustan asishtukiwe ilikuwa ni lazima awapumbaze maaskari ili kazi ya kumsaka Brigedia Karanje iwe rahisi zaidi.Ngesa akawa amepewa funguo za Pingu bila askari yoyote yule kuona!

“Kuwa makini”

Dustan akasema kwa sauti ya chini!

“Ahsante Dustan”

“HAYA ONGOZA MBELE,TWENDE”

Askari alivyotokeza,Dustan akapaza sauti.Akamuingiza ndani ya Diffenda.Yeye akaingia ndani ya gari lingine,alivyofika mbele akageuka na kumtizama Ngesa,akampa ishara kwa vitendo ya kuwa kila kitu kitakuwa sawa!

Ilikuwa shangwe kwa jeshi la polisi kumuweka Ngesa chini ya ulinzi, ndiyo maana waliondoka kwa mikwara mizito mno!

“Wewe ni kunyongwa tu,umemuuwa Mh.George Kimpanga.Kenge wewe alafu yaani hata mkononi hujai”

Askari,aliyekuwa pembeni ya Ngesa alizungumza.Na haukuwa utani,tayari Ngesa alibambikiwa kesi ya mauaji kwa maana hiyo hilo halikuwa na mjadala kifungo cha maisha kilimuhusu ama kunyongwa,ukweli wa mambo ya ushahidi wote alikuwa nao Dustan peke yake kwani Kabla ya umauti kumkuta Mh.George Kimpanga, alizungumza mambo mengi mazito!Diffenda zilizidi kuchanja mbuga huku polisi wakipashana habari juu ya Ngesa,yupo chini ya ulinzi tayari wakitumia redio upepo, kwao ilikuwa kama sherehe na ndani ya dakika tatu taarifa zilimfikia Rais Leslie,akaonekana kuwa na furaha lakini kwa wakati mmoja alionekana kusikitishwa mno na kitendo cha Ngesa kufanya jambo hilo,bado hakuelewa ni kwanini Ngesa amebadilika na kuwa kama mnyama wa kutisha.Laiti kama angejuwa Ngesa anapambana na nchi yake,asingetoa maamuzi ya kutaka kumfunga jela,kifupi Rais Leslie alikuwa ndani ya giza nene, hakuweza kuona mbele.

Diffenda za polisi zilikuwa katika kasi ya ajabu,isiyoweza kuelezeka kiwepesi.Ngesa alikuwa ndani ya Diffenda ya katikati,kawekewa mitutu pande zote,maaskari walifanya hivyo sababu walikuwa na historia ya Ngesa jinsi alivyotoroka maaskari ndani ya Diffenda,hivyo siku hiyo maaskari macho yao yote yalikuwa kwa Ngesa, ambaye hata yeye alikuwa akiwasoma akili zao.Ilikuwa ni lazima atumie akili nyingi kuliko kawaida,ndiyo maana alikuwa akipanga mikakati ya kijeshi,mikono yake ikiwa nyuma.Hakuna askari yoyote aliyekuwa anajua kwamba ana funguo za pingu alizofungwa.

Taratibu akaanza kujaribu kwa uangalifu,akachukuwa kidole kimoja akashika vizuri kitaalam.

“Vipi?Umekalia kipisi cha karoti nini?”

Afande mmoja,akamdhiaki baada ya kumuona Ngesa,ananeng’eneka.Mara akae hivi mara ajigeuze hivi.Hawakuelewa kuwa mtuhumiwa waliyekuwa naye,alikuwa mbioni kujikomboa na baada ya muda mfupi, mshikemshike ungeanza!

“Matako yanawasha”

Ngesa nayeye akawajibu choo!Alifanya hivyo kwa makusudi ili kuwaharibu kisaikolojia.

“Nikukune?”

Baada ya Askari kuuliza hivyo,askari wenzake wakaanza kucheka, jambo hilo kwao wakalifananisha na kibonzo!Hapo ndipo Ngesa akapata uwazi wa kujiinua zaidi na kupachua pingili za pingu lakini akajikausha kwanza,mikono yake ikawa huru japokuwa aliendelea kuiweka kwa nyuma!

Akatizama nje na kuona namna gari linavyokimbia kwa kasi ya ajabu,akamuangalia dereva alivyoushikilia usukani,akageuka nyuma na kuona Diffenda nyingine tatu.Upande wa pili kulikuwa na soko lililokuwa na nyanya, pamoja na mboga za majani,akawatizama maaskari wawili waliokuwa pembeni yake,wanamcheka huku wakiwa wameshika mitutu,hawakuelewa Ngesa tayari yupo kwenye hesabu kali za kutoroka.

Kwa kasi ya risasi,akampiga kiwiko cha pua askari wa kushoto kwake,akavuta mtutu wake na kumpiga nao askari wa kulia,dereva aliyekuwa anaendesha gari alivyogeuka nyuma ili kujua kuna nini,akatulizwa na ngumi ya uso,Ngesa akaibua kivumbi ndani ya gari,akaruka kama ngedere juu ya usukani,akazungusha kushoto kwa kasi,gari ikapoteza uelekeo.Hapohapo hakufanya makosa.Kama komando akafungua mlango na kujitosa nje,hakujali angefikia wapi lakini alitua kwa bega na kujibiringisha mpaka sokoni.Hapo akasimama na kutoa mbio za kipepe huku akiruka nyanya na mboga za majani.Kufumba na kufumbua Ngesa akapotea machoni mwa askari,ambao bado walikuwa wakihangaika kupaki magari yao.

 

0 comments:

Post a Comment

BLOG