Search This Blog

Wednesday, November 18, 2020

DAPHINE SEHEMU YA 5/10

 

 


DAPHINE
MTUNZI….EMMANUEL F.KWAY(THE STORY MASTER)
AGE…(18+)
Watchstrap…+255718 862176
SEHEMU YA 5 KATI YA 10

 


 Hakuna askari hata mmoja kati yao aliyetegemea kitendo hicho kutokea,jambo la kutoroka kwa Ngesa lilikuwa la kufumba na kufumbua.Magari ya maaskari yakapiga breki na wengine walitua ardhini na mitutu kabla ya magari kusimama vizuri, wakaingia katikati ya soko hilo ili kumsaka Ngesa,ilikuwa ni lazima wamrudishe mikononi mwao kwani wangeshindwa cha kujibu mbele ya mkuu wa majeshi, eeti Ngesa kawatoka, tena wakiwa wengi namna hiyo.

Jambo hilo lisingemuingia Rais hata kidogo akilini,ndiyo maana walianza kuwatawanya watu hovyohovyo huku wakielekea alipokimbia Ngesa,kifupi kumkosa Ngesa kungekuwa kuna hatihati ya vibarua vyao kuota nyasi, ukizingatia hali ya maisha ilikuwa ngumu mno.

“Kakimbilia wapi?”

Askari mmoja alimuuliza mwenzake baada ya kuona anaenda sehemu ambayo haielewi.hiyo ilifanya mpaka wafanya biashara wadogowadogo ndani ya soko hilo watandwe na hofu kubwa,staili waliyokuwa wanatumia polisi kukimbia huku na kule iliwafanya waogope zaidi,kilichowaogopesha kupita kiasi ni mitutu walioshika, mbali na hapo hakuna hata askari mmoja aliyekuwa anacheka,hiyo ilimaanisha kuna hali ya hatari mno!

“Kuna mtu tunamtafuta,kaelekea wapi?Amevaa shati jeupe lina damu”

Askari mwingine akamuuliza Mwanamke mmoja,aliyekuwa gengeni anauza nyanya zake.Hofu iliyokuwa imemtanda Mwanamke huyu ilitisha,kwani alionekana kubabaika mno!

“Si.. si… sijui”

“Una uhakika?”

“Ndi..o”

Kila alichozungumza Askari,Ngesa alisikia kwani alikuwa ndani ya genge hilo na aliyempa hifadhi ni mama huyo aliyeonekana ana hofu mno!Kwani hakumfahamu Ngesa,lakini alijisikia kumsaidia sababu aliombwa msaada huo.Staili aliyokuwa amelala Ngesa chali, kama askari huyo angepitisha kichwa chake ndani,angemuona.

“Afande,Ngesa humu hajatoka!Inabidi tupekue kwa umakini,ni lazima atakuwa humuhumu sokoni.Kuweni makini kumtafuta”

Askari mmoja aliyekuwa anahema alitoa ripoti hiyo baada ya kusaka soko hilo zima,alikuwa ana uhakika asilimia zote ya kuwa Ngesa ni lazima atakuwa amejificha humohumo kwani hakukuwa na dalili yoyote ile ya yeye kwenda mbali namna hiyo.

Ilikuwa ni kama ametabiri vile kwani Ngesa alikuwepo na maongezi yao aliyasikia.Kilichomfanya aogope zaidi ni baada ya jeshi la polisi kuanza kusaka sehemu moja baada ya nyingine.Hapo ndipo Ngesa akajua tayari ungekuwa ni mwisho wake na angekamatwa!Licha ya kusikia operesheni hiyo kuanza, alizidi kutulia chali.

“Pekueni kule.We mzee sogea pembeni Kaa kando”

Kazi ya upekuzi ilianza mara moja na staili ilikuwa ni moja tu,kama una duka ama kibanda unatolewa,kama una genge unakaa kando na askari waliingia karibia kumi kufanya msako huo.Mzee mmoja aliyekuwa anauza nazi alitolewa nje,askari kumi wakazama ndani ya kibanda chake.Zoezi hilo halikuwa na ustaarabu hata kidogo kwani askari walitupatupa nazi huku na kule,wakawa wanakanyaga nyanya na kuziharibu.Hiyo iliwakera sana wafanyabiashara.

“Mzee hapa kuna nini?Fungua huu mlango”

Askari wakazidi kufungua na kusaka,hawakutofautishwa na mbwa wa polisi siku hiyo.Soko zima lilijaa askari wakimtafuta mtu mmoja tu,Ngesa!Na mtu huyo mmoja alisakwa kama Osama Bin Laden.

“Nina uhakika humu hajatoka.Tupo radhi kutoa watu wote humu sokoni hata kama itachukua miaka mingapi”

“Upande ule wote tayari?”

“Ndio afande”

“Bado wapi?”

“Kwenye hiko kibanda cha huyo Mama”

Hata ingekuwaje Ngesa asingeweza kutoroka kiurahisi,namna ambavyo askari walivyotanda sokoni alikuwa hana ujanja wowote ule wa kuwatoka, ndiyo maana alianza kukata tamaa na alivyochungulia kwa umakini akaona miguu ya askari inamfuata alipo yeye.Akatulia akisubiri nini kingefuata,alikuwa tayari kajiandaa kwa lolote,mbali na hapo hata kama ingekuwaje asingeweza kutumia nguvu kuwadhibiti askari hao,hiyo ilimaanisha alitakiwa atumie akili nyingi kupita kiasi.

“Wewe Mama sogea hapo,toka nje upesi”

Halikuwa ombi,bali ni amri kutoka kwa askari huyo ili aingie ndani kumsaka Ngesa.Hicho ndicho kibanda alichokuwa Ngesa amelala chali anawaona kupitia kitundu kidogo,pembeni yake kulikuwa na turubai la rangi ya kijana,akajiburuza kama jongoo na kujivuta akitumia mgongo.

“Afande njoo huku”

Baada ya askari huyo kuingia ndani ya genge,akamuita mwenzake ili waendeleze msako.

“Pita kule”

Kulikuwa kuna uwezekano mkubwa sana wa Ngesa kuonekana endapo afande huyo aliyesimama na bastola kugeuka nyuma na kuangalia chini,kwani hapo Ngesa alikuwa amelala chali,anajiburuza taratibu ili ajiviringishe chini ya turubai.

“Huku hayupo”

“Atakuwa wapi?Nina uhakika.Hapa sokoni hajatoka”

“Sasa yupo wapi?Tumemtafuta kila mahali”

“Tuendelee na msako”

Afande huyu alikuwa kama amechezwa na machale vile,akaangalia chini na kuliona turubai la rangi ya kijani.Akalitizama kwa muda kidogo!Kuna kitu kikamwambia,funua turubai,hapo ndipo akaanza kuinama ili kulitoa.

Ngesa alikuwa chini ya Turubai,tayari amejiandaa kwa lolote lile kufa ama kupona,ndiyo maana akawa anamsubiri askari afungue turubai hilo ili amvae.Askari,akalishika turubai,alivyotaka kulivuta radio upepo yake ikatoa sauti.

“Kiiish ova,afande Sambo,unanipata ova”

Hapo ndipo Askari huyo akasitisha zoezi lake,akachomoa radio upepo na kuiweka mdomoni ili kujibu.

“Nakupata ova”

“Njoo huku barabarani ova”

Afande akatoka, hiyo ndiyo ikawa ponea ya Ngesa na ulikuwa ni kama muujiza mkubwa!Maaskari hawakuwa wastaarabu hata kidogo ndiyo maana wafanyabiashara walichachamaa na kuanza kuwarushia askari mawe,kitendo cha wao kuvamia sokoni na kukanyaga nyanya na mali zao kiliwakera mno!Ndiyo maana wakaungana na kuanza kufanya vurugu wakiandamana.

“Hatutaki,huo ni uonevu”

Jamaa mmoja akapaza sauti huku akiwa ameshika jiwe!Hiyo ilimfanya Ngesa aliyekuwa ndani ya genge apate upenyo,akapenya kwa chini na kuzunguka nyuma kwa tahadhari kubwa.


*******

Sio siri,Rais Leslie alihisi kuchanganyikiwa ajabu,siyo yeye tu hadi Mkuu wa Mkoa Mh.Daud Bashonga,kitendo cha Ngesa kuwatoroka maaskari kilimuumiza kichwa na alitaka kupata maelezo yaliyonyooka kwa sababu kwa akili ya kawaida haikuwezekana hata kidogo mtu mmoja kuwatoka askari zaidi ya thelathini.

“Leslie,mimi naona picha ibandikwe kama mara ya kwanza.Ngesa atafutwe!Na safari hii anyongwe.Huo ni upumbavu sasa”

Daudi Bashonga,alimshauri Rais siku hiyo wakiwa Ikulu.

“Hapana”

“Hapana.Kamuuwa George,huyu hawezi kuachwa hai.Kama huwezi,mimi nitafanya juu chini,akamatwe anyongwe au nitatuma watu wasiojulikana wam-malize”

“Subiri kwanza”

“Rais Leslie,hakuna muda wa kusubiri hapa”

“Hatuwezi kwenda kwa spidi kiasi hicho”

“Labda hujanielewa Leslie,huyu Ngesa sio binadamu wa kuishi Tanzania.Hiyo kazi niachie mimi,nitajua cha kufanya”

“Askari wamefikia wapi?”

“Bado hawajamkamata”

Rais Leslie siku hiyo alipelekwesha na Mkuu wa Mkoa,hiyo yote ilitokana na kuchanganyikiwa.Hakuelewa kwamba RC Daud Bashonga, anatumia mwanya huo,kwani alitaka Ngesa afe na hilo ndilo jukumu alilopewa na Brigedia Karanje.

“Naomba niongee na I.G.P”

Rais Leslie,akaomba jambo hilo litokee.Baada ya dakika mbili akaletewa simu na tayari I.G.P alikuwa kwenye laini.

“Sitaki kuongea sana,nahitaji Ngesa apatikane.Kama huwezi niambie”

Raisi Leslie alizungumza kwa kufoka.Na ilionesha fika kabisa alikuwa ni mtu aliyekata tamaa, kiti cha uraisi alikiona cha moto kukikalia,alihisi kujuta kuwa na madaraka na cheo hicho kwani wananchi wote walimuangalia yeye.

Damu za watu zilizomwagika,watu wasiokuwa na hatia kufa ilifanya amwagiwe lawama,nchi zote jirani zilizungumzia juu ya vifo vya watu waliosadikika kunywa sumu.Mbaya zaidi habari hiyo ilirushwa mpaka vyombo vya habari vya kimataifa kama; BBC,ALJA ZEERA na CNN.Kama kiongozi wa Nchi ilibidi ajibu mashtaka hayo,hakuelewa ni jibu gani la haraka la kutoa ndiyo maana hakutaka kupokea simu yoyote ile ya maswali.Kazi ilikuwa ni kumtuma muwakilishi wake ili atulize gasia.Kwa kifupi Rais Laslie alikuwa nyuma ya kila kitu, hakuelewa kwamba mtu anayemsaka ili amfunge ndiye anayepambana kumsaidia ili vifo visiendelee kutokea!


******

Ngesa alitafutwa kwa wudi na uvumba,lakini hakuna hata askari mmoja aliyetoa ripoti ya mtu huyo kuonekana!Habari zake zikasambaa kwa mara nyingine, tena safari hiyo zilikuwa nzito mno!Kesi ya kumuuwa Mh.George Kimpanga ilikuwa mikononi mwake,hivyo ndivyo Rais Leslie alivyoamini ndiyo maana alitaka askari wamsake Ngesa,kila pembe ya mji.Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani isingekuwa rahisi kwa Ngesa kuwachomoka askari hata kidogo,jinsi walivyomwagwa barabarani iliogopesha kwa kiasi cha kutosha,Ngesa alitafutwa kama shilingi.Wakati akiwa anatembea pori kwa pori akili yake yote ilikuwa kwa Dustan,ambaye alimwambia waonane nyumbani kwake,bado alishindwa kumtafakari Dustan ni kwanini yupo upande wake,kuna nafsi ilimwambia ya kwamba yupo kwenye mtego,akienda kwa Dustan ndio utakuwa mwisho wake lakini nafsi nyingine ilipinga, ikiamini Dustan ni mtu mwema.

Ngesa,alikuwa akitembea huku akitafakari vitu vingi sana na alivisikia sana ving’ora vya polisi.Japokuwa alikuwa akijiamini lakini bado alitandwa na hofu kubwa sana!Alielewa ni kiasi gani wananchi walivyokuwa na hasira naye,kwa kitendo cha kupakaziwa amemuuwa George Kimpanga.Ilikuwa ni lazima ajisafishe kabla hajafika mikononi mwa Jeshi la polisi,kwa maana hiyo ilikuwa ni lazima amuweke Karanje mikononi mwake,hiyo ndiyo ingekuwa salama yake.Na alikuwa afanye hivyo kabla hajatiwa mikononi mwa vyombo vya dola.Kuna njia moja,iliyokuwa na majani yamelala,aliiona na kutembea kwa hatua nyingine kama tatu hivi,ndipo alipoona barabara ya vumbi.Akapiga hesabu vizuri ni kitu gani akifanye,lakini kabla ya kutoa maamuzi akaona gari limepaki kandokando yake,hapohapo akapata wazo kabambe.Akatembea taratibu,akaangalia huku na kule akaokota jiwe na kuvunja kioo!Akaingiza mkono ndani na kutoa ‘lock’akafungua mlango na kukaa siti ya dereva,akaanza kuvunja 'switch' ya gari,kwa kutumia jiwe,akazidi kuigonga kwa nguvu mpaka ilivyofumuka yote,akachomoa nyaya mbili hasi na chanya,akazigusisha.

Cheche,zikatoka injini ikaunguruma.Hakutaka kuremba,akapiga gari moto na kuteleza.Ilikuwa ni jioni ya saa kumi na mbili,barabara zilikuwa zote zimefungwa na kila askari alikuwa ana picha yake mkononi,hiyo ikafanya apite njia za panya ili afike Kinondoni,Viwanja vya Biafra,akaonane na Dustan,kutokana na utundu wa njia,akawa ametokeza Mwananyamala,akanyoosha moja kwa moja.Akaibuka upande wa pili na kufika Kinondoni B,hapo akashuka ndani ya gari na kuanza kutembea!

Nyumba ya Dustan ilikuwa mbele yake umbali wa kama mita kumi hivi,akaiangalia kwa umakini kabla ya kujishauri kwenda,ilikuwa ni lazima ajihami kidogo.Ndiyo maana akakaa kidogo na kujificha nyuma ya nguzo ili kuangalia usalama!


*******

Maumivu,aliyohisi Jaqlin Mfinanga yalimfanya afumbue macho yake,alikuwa yupo kitandani bado ana majeraha yaliyosababishwa na risasi alizopigwa.Ingawa hali yake ilionesha unafuu lakini bado alitakiwa kupatiwa matibabu mengine ya ziada Ikulu,ambapo ombi hilo liliombwa na Ngesa.Lakini mambo yakawa kinyume kwani wakati huo Ngesa alikuwa akitafutwa kwa wudi na uvumba,mtu aliyeonesha kuwa mwenye usongo zaidi ni Mkuu wa Mkoa Mh.Daud Bashonga, ndiyo maana hasira zake zikamtuma aingie chumba alicholazwa mpenzi wake na Ngesa,bila kuuliza chochote akatumbukiza kidole chake juu ya jeraha la Jaqlin Mfinanga, lililokuwa mkononi.

“Bwana ako yuko wapi?”

Mkuu wa Mkoa alikuwa anafanya unyama ambao angekutwa na Ngesa,angemtafuna mzimamzima kwa hasira!

“Nakuuliza bwana ako yuko wapi?”

Maumivu aliyokuwa anahisi Jaqlin Mfinanga akiwa juu ya kitanda,hayakuweza kuelezeka kiwepesi.Bado hakuelewa Mkuu wa Mkoa anazungumzia kitu gani,alivyotaka kusimama kwa nguvu akatulizwa na kibao cha uso hiyo ilimfanya arudi kitandani bila kupenda.

“Bwana ako Ngesa yuko wapi?”

Lilikuwa ni swali ambalo lilizidi kumshangaza Jaqlin Mfinanga,kifupi alikuwa yupo ndani ya giza nene.Hakuelewa ni kitu gani kinachoendelea,jeraha alilokuwa akitoneshwa lilianza kuvuja damu nyingi mpaka zikatokeza kwenye bandeji lakini mkuu wa Mkoa,hakujali hilo. Akazidi kumkandamiza kwa nguvu zake zote.

“Ngesa yuko wapi?Nitaendelea kufanya hivi mpaka uniambie”

Msalaba Wa Ngesa alikuwa tayari kaubeba Jaqlin Mfinanga na alikuwa akiteswa kimakosa!


 Mateso kwa Jaqlin Mfinanga yalizidi,hayakukoma maumivu aliyokuwa anahisi hayakuwa na mfano wake kwani alianza kujisikia maumivu mwili mzima, hiyo ni baada ya kidonda chache kuendelea kubinywa,Mkuu wa Mkoa hakuishia hapo.Akachukua mkasi uliokuwa pembeni na kuanza kukichokonoa kidonda hiko,hiyo ilimfanya Jaqlin Mfinanga apige kelele za maumivu lakini hilo halikumsaidia, ilikuwa ni lazima aseme ni wapi Ngesa alipo jambo ambalo hata yeye alikuwa gizani kwani hakuelewa lolote lile.

“Ngesa yuko wapi?Utafia hapahapa leo”

Yalikuwa ni maneno ya kutisha na dalili za kifo zilikuwepo kwani Mkuu wa Mkoa Mh.Daud Bashonga alikuwa tayari kufanya tukio hilo sababu ya hasira alizokuwa nazo juu ya Ngesa,ilikuwa ni lazima amtie Ngesa mikononi mwake ili Karanje aache kumsumbua.Alishaelewa nini maana yake kama angemwambia Brigedia Karanje ya kwamba Ngesa bado hakupatikana.Matatizo aliyokuwa akipata Jaqlin Mfinanga kwa asilimia kubwa yalisababishwa na Ngesa,sambamba na kupata mateso lakini alianza kujuta ni kwanini alijiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na mwanamme huyo ambaye mpaka wakati huo ndiye aliyefanya mpaka yeye akaingia kwenye matatizo makubwa sana!Maumivu, yaliendelea bila kukoma,damu zilikuwa nyingi zinamtoka.Akaanza kuhisi kizungu zungu kikali sana.Kwa mbali akaanza kuona kama giza nene,hakuelewa ni kwanini hali hiyo inatokea,alivyojaribu kushindana na hali hiyo kwa kukaza macho yake,alishindwa kabisa kwani alikumbwa na giza nene!


*******

Alikuwa ni zaidi mafia ama komandoo kwa lugha nyingine, hiyo ilitokana na matatizo pamoja na kupatwa na misukosuko mingi katika maisha yake,bado alikuwa akitafakari mambo mengi kichwani akiwa amejificha nyuma ya nguzo ya umeme, anaitizama nyumba ya Dustan Kyoba,ama DK Kama walivyozoea kumuita wanausalama!Hakutaka kuingia kichwakichwa ndani ya nyumba hiyo, ndiyo maana alitulia kwa kitambo ili asome,siku hiyo Ngesa hakutofautishwa na rada ya jeshi kwani alikuwa akitizama huku na kule.Mara ghafla moyo wake ukapiga kwa nguvu sana,lilikuwa ni tukio lililomshangaza kupita kiasi,kuna gari aliliona linatokea upande wa Magharibi.Gari hilo lilimfanya atulie kidogo kwani alijua, kivyovyote vile lilikuwa ni gari la jeshi la polisi,kwani lilikuwa ni Difenda.Akarudi nyuma kidogo likapita mbele yake,akalisindikiza kwa macho.Wasiwasi ukazidi kumuingia sababu lilisimama nje ya nyumba ya Dustan.

“Kumbe Dustan ni mshenzi mkubwa.Hivi alijua nitaingia kichwakichwa”

Ngesa aliwaza huku akiliangalia gari hilo la polisi ambapo walishuka askari wawili na kuingia ndani ya nyumba ya Dustan,ambapo huko walikaa takribani dakika tano nzima.Taa nyekundu ilianza kuwaka kichwani kwake,akajua ni lazima Dustan atakuwa anashirikiana na jeshi la polisi ili wamuweke ndani kirahisi.

“Kwanini anifanyie hivi?”

Bado alikuwa katika kitendawili kikubwa ambacho asingeweza kukitegua kamwe,katika kutafakari kwake akawaona maaskari wanatoka nje ya nyumba,mbaya zaidi safari hiyo walikuwa na Dustan,akawashuhudia wanavyopeana mikono.Askari,wakaingia ndani ya gari lao na kuondoka zao.

Hapo Ngesa,alibaki akitafakari juu ya kitu gani akifanye,akabana meno yake kwa hasira na kuanza kuiangalia nyumba ya Dustan kwa kitambo kidogo!Akachomoka mafichoni na kuanza kutembea,akaivuka na kuingia kichochoro kimoja kidogo ambacho kilikuwa na ukuta,nyuma ya ukuta huo kulikuwa na geti dogo ambapo ukifungua unatokea upande wa uwani kwenye nyumba ya Dustan,akapiga hesabu zake haraka haraka na kuutizama ukuta huo,akautathmini huku na kule,akachuchumaa kidogo na kuruka kwa juu kidogo ambapo hapo,mikono yake ilishika ukuta kwa juu.Kabla ya kuingia ndani akachungulia mazingira ya ndani ili ajue kuna nini,akaona hakuna dalili ya mtu yoyote Yule kuwepo,akajiweka vizuri na kujivuta juu ambapo hapo alitua ndani,bila kutoa kishindo chochote kile.Akauwendea mlango wa uwani,alivyogusa kitasa mlango ukagoma kufunguka kumaanisha kuwa umefungwa na ufunguo.Akatembea kwa tahadhari mpaka upande wa dirisha,taa zilikuwa zimewaka bado na miale ya luninga ilikuwa ikimulika mulika kuashiria kwamba kuna watu seblen wanaangalia televisheni.Hilo halikuwa tatizo kwake,dirisha lilikuwa mbele yake hiyo ikamfanya ainame ili alivuke bila kuonekana,alivyoibukia upande wa pili,akakumbana na kibaraza.Hapo akatulia kwa kama sekunde mbili,akashusha pumzi kidogo!

“Ngo! Ngoo! Ngooo!”

Akagonga mlango kwa tahadhari huku akijiandaa kishupavu.

“Ngo! Ngo! Ngooo!”

Dustan,alikuwa ndani yupo Seblen mlio wa mlango ulimshtua,haikuwezekana hata kidogo mlango ugongwe wakati geti lilikuwa limefungwa,mtu huyo alipitia wapi?Hapo akatulia tena kidogo ili asikilizie vizuri.Masikio yake,hayakumdanganya.

Kwa tahadhari kubwa,akachomoa bastola yake iliyokuwa chini ya mto,akaishika vizuri na kuiweka kwa nyuma yaani mkono wake ulioshika bastola ukawa kwa nyuma mmoja mbele,akatembea mpaka kwenye dirisha,akavuta pazia ili kujua ni nani aliyekuwa anagonga lakini hakumuona mtu yoyote Yule,Ngesa alikuwa amejibanza kwenye kona kabisa!Dustan akazungusha ufunguo,akanyonga kitasa kabla ya kuufungua vizuri.Ngesa akasukuma mlango kwa nguvu zake zote akiwa nje,hiyo ilifanya Dustan apigwe na mbao ya pembeni ya mlango kwenye kichwa,akarudi nyuma bila kupenda kabla ya kukaa sawa.Ngesa akawa tayari kamfikia,akamkaba kohoni.

“Dustan,kumbe unashirikiana na polisi?”

Haikujulikana kama lilikuwa ni swali ama Ngesa anamtuhumu!

“Ngesaaaa!”

Dustan akaonekana kupigwa na bumbuazi,hakujuwa bastola yake iko wapi sababu kwa wakati huo hakuwa nayo tena mkononi.

“Usinifanye mimi mpumbavu Dustan”

Dustan alikuwa amekabwa,amewekwa ukutani Ngesa anazungumza bila mzaha wowote ule, ilikuwa ni wazi kwamba, alikuwa amekasirika kwa kaisi cha kutosha.

“Ngo..ja nikwambie sa..sa”

“Askari walifuata nini hapa kwako?”

“Walitaka kujua nimef..ikia wapi.Ngesa,niaachi..e nashindwa kuhe..ma vizuri”

“Askari walifuata nini hapa?”

“Nge..sa amini tupo pam.o.ja.Askari wali..taka faili lako ili niwape tu”

“Faili langu?”

“Ndi..io”

“Kwanini?”

“Wanadai kes..i yako kwa sasa hivi,sio ya kiusalama.Ipo chi..ni ya jeshi la polis..i”

“Una uhakika?”

“Ndi…io”

Macho ya Ngesa yalikuwa mekundu mno,alikuwa akimtizama Dustan kwa hasira huku akiwa amemkazia macho,hapohapo akamuachia.

“Koho! Koho!”

Haikujulikana kama Dustan alipaliwa na mate ama roba alilopigwa ndilo lilimfanya akohoe,baada ya hapo alianza kushika shingo yake, ki ukweli alihisi maumivu makali kwenye koho lake la hewa.

“Niambie kwanini umeniita?Unataka nini kutoka kwangu?”

Ngesa akauliza.

“Punguza jazba ndugu,kwanza naomba uelewe kitu kimoja.Nchi nzima inakutafuta wewe!Ni mimi mwenyewe ninayejuwa,ukweli wote.Nahitaji tufanye kazi pamoja!Hata mimi ninatamani Karanje akamatwe”

“Nitakuamini vipi?”

Dustan hakutaka kuongea chochote,akaokota bastola yake iliyokuwa chini na kumkabidhi Ngesa!

“Ngesa,naamini wewe ni mzalendo wa hii nchi.Rais anafanya makosa makubwa sana!Najua sio kosa lake,ni washenzi wachache.Hivyo inabidi tuwaoneshe kazi”

Dustan alikuwa akiongea,Ngesa alikuwa yupo kimya!Anamtizama kwa umakini.Kabla ya kumaliza kuongea kuna kitu kiliwafanya waangaliane kwa kama sekunde tatu nzima,hiyo ni baada ya kusikia muungurumo wa gari nje.

Dustan akaruka mpaka kwenye dirisha akavuta pazia.Gari aliloliona lilimfanya aingiwe na hofu kwani haikuwezekana hata kidogo kupata mgeni kama huyo usiku wa namna hiyo.

“Ngesa,ingia kwenye ule mlango”

Dustan alisema huku akitumia mkono wake kama ishara,Ngesa akatii amri na kuingia njia ya kordo akazama mpaka jikoni na kutulia.

“Ngo! Ngooo! Ngoooo!”

Mlango ulikuwa tayari umeanza kugongwa kuashiria ya kwamba, mgeni huyo keshafika mlangoni,alichofanya Dustan ni kukimbia chumbani kwake haraka,akavua shati na kubaki na vesti.Kuna picha fulani alitaka kuitengeneza,alivyotokeza seblen akawa kama mtu aliyetoka kulala vile,akatembea mpaka mlangoni na kunyonga kitasa.

“Jenipha,karibu”

Dustan,akasema huku akiufungua mlango wote.Jenipha akapita ndani.

“Ahsante,ulikuwa umelala?”

“Nilikuwa nimepumzika tu?Vipi,mbona usiku usiku?”Dustan,akaibuka na swali.Alitaka kujua ujio wa Jenipha nyumbani kwake usiku huo.

“Nilikuwa nakutafuta kwenye simu sikupati”

“Kwelii?”

“Ndio”

Dustan akatizama mezani kwake ili kuangalia simu yake,kama ipo hewani. Hapo ndipo akagundua haina chaji, imezima.

“Chaji,kumbe ilizima.Sikujua kabisa”

“Wanataka faili la Ngesa”

“Jeshi la polisi?”

“Ndio”

“Walinifuata pia”

“Ukawaambia nini?”

“Tuonane asubuhi”

“Ngesa asipopatikana sijui itakuwaje Dustan”

“Atapatikana tu,awe mfu au hai”

Wakati Dustan anazungumza mambo hayo macho ya Jenipha yakawa yameganda shingoni kwake,kuna kitu kisichokuwa cha kawaida alikigundua,akamtizama kwa makini.Kuna alama fulani za mikono aliziona zikiwa na damu kwa mbali!Akamsogelea karibu kabisa na kuigusa damu hiyo,ilikuwa bado haijaganda vizuri.

“Nini hiki?”

Jenipha akauliza,Dustan akajifanya kushtuka akagundua ya kwamba Ngesa alikuwa amemkaba na mikono yake iliyokuwa imegandia damu.

“Ujue tangu mchana sijaoga Jeni”

Jibu hilo halikumuingia Jenipha akilini,akatizama pembeni na kuona kuna stuli imedondoka, sofa limekaa upande.Kuna picha fulani ilianza kumuingia kichwani lakini hakutaka kukurupuka.

“Are you okay Dustan?”(Upo sawa Dustan)

“Yeah,I’m fine”(Nipo sawa)

“Anyway”

Jenipha haikujulikana kwanini ametoka nje.Lakini baada ya dakika moja akawa ameingia tena ndani.

“Naomnba maji ya kunywa”

Mkononi alikuwa ameshika kamera ndogo aina ya Sony ameificha,ilikuwa ni lazima aitegeshe ndani ya seble hiyo ili ajue nini kinaendelea,wasiwasi wake mkubwa ulikuwa ni lazima Dustan alikuwa ana jambo kubwa anamficha,ndio maana akaamua kufanya jambo hilo zito.

Dustan alivyopotea machoni mwake,akaanza kuangalia huku na kule.Ndipo akaona kona ya pembe juu ya kabati,akapanda kwa tahadhari na kuiweka camera hiyo kwa juu!Alivyohakikisha kila kitu kipo sawa,akateremka na kurudi sehemu aliyokuwa.

“Maji haya hapa”

Hakuwa mwenye kiu,bali alitaka kumtoa Dustan ili aweke mtego wake.Alivyomaliza kunywa maji,akamtizama Dustan!

“Ahsante,mimi naenda.Tukutane kesho boss”

“Sawa,usiku mwema”

Dustan,akashusha pumzi ndefu alielewa nini maana yake endapo Ngesa angeonekana ndani kwake!Alivyofunga mlango,akatembea mpaka dirishani na kufungua pazia,alitaka kuhakikisha gari ya Jenipha inaondoka kabisa ndipo aendeleze mazungumzo na Ngesa!Hapohapo,akaingia jikoni na kumtoa Ngesa!

“Ngesa,hupaswi kukaaa hapa.Njoo huku tufanye mambo harakaharaka.Inabidi usafiri mpaka Arusha,Kesho asubuhi sana”

“Itawezekana vipi?Itabidi niondoke usiku huu huu”

“Huwezi kufika popote,utakamatwa”

“Hiyo asubuhi nitaondoka vipi?”

“Ndio maana nikakwambia nifuate”

Dustan mbele,Ngesa nyuma.Wakatembea mpaka kwenye chumba kidogo kinachofanana na stoo,taa ikawashwa!Chumba kilikuwa kidogo lakini kina makaburasha mengi,Dustan akatembea mpaka kwenye moja ya begi kubwa kati ya mengi la rangi nyeusi,alivyolifungua kukaonekana vitu vingi sana!Hiyo ilimfanya Ngesa,ashangae!

“Inabidi tubadilishe muonekano wako kwanza”

Ndani ya begi kulikuwa na vitendea kazi vingi sana!Vitu kama ndevu za bandia,nywele za bandia,matiti ya bandia, vilikuwa ndani ya begi hilo.Dustan akatoa wigi la nywele zenye mvi pamoja na ndevu nyeupe,akamtaka Ngesa alale ili afanye anachokijua.Hicho ndicho kilichotokea kwani Dustan,alichukuwa makopo mawili, ndani yalikuwa na majimaji mazito akatumbukiza ndevu za bandia,akasubiri kama dakika tano nzima.

Akavaa gloves,kisha kuimtaka Ngesa atulie,hapo akaanza kumbandika ndevu hizo taratibu,kuanza kwenye mashavu mpaka chini ya kidevu.Akarudia hatua ile ile kwenye wigi lenye mvi.Kisha kumuwekea kichwani.Akachukua feni na kuliweka spidi ya mwisho ili gundi ikauke!Dakika arobaini na tano baadaye Ngesa akawekewa kioo mbele yake,sura aliyoiona ilimfanya acheke mpaka yeye.Ghafla aligeuka akawa kama babu mwenye umri mwingi!

“Ostadhi, Athuman Mtwenge”

Dustan,akasema hiyo ilimfanya Ngesa aachie kicheko huku akiwa anajitizama kwenye kioo kikubwa.Ki ukweli alibadilika sio mchezo,haikuwa rahisi hata kidogo kugundulika kizembe.

“Dustan!Hakuna askari atakayenijua.Kilichobaki hapa ni kanzu tu”

“Sio kanzu,nitakupa na msaafu kabisa na tasbii”

Kweli Dustan alidhamiria kumsaidia Ngesa kwa hali na mali,ndiyo maana alijitoa kuwa upande wake.

“Dustan,nakuomba kitu kimoja”

“Kitu gani Ngesa?”

“Naomba unisaidie kumlinda Jaqlin,pia kitu kingine kwenye operesheni hii ningeomba Daphine awepo”

Mambo hayo mawili yalimfanya Dustan ashushe pumzi kidogo ya kuchoka,haikuwa kazi ngumu lakini ilikuwa ni nzito mno.Kwani Daphine na Jaqlin Mfinanga walikuwa wapo chini ya ulinzi maalum, hivyo isingekuwa kitu kidogo kuwakomboa.

“Sio kazi rahisi Ngesa”

“Ushaamua kulianza hili,naomba tulimalize”

“Nitajitahidi”

“Ahsante”

Siku hiyo kila mtu alisubiri kupambazuke,japokuwa usiku ulikuwa mrefu lakini kulikucha.Ilivyogonga saa kumi na moja kamili.Ngesa akawa tayari amejikoki,amevaa Kanzu,mkononi kabeba msaafu pamoja na tasbii na tiketi yake ilikuwa tayari imekatwa kwa jina la Athuman Mtwenge!Mpango wao ulikuwa apande shirika la ndege ya Precision Air,ambayo ingemfikisha mpaka K.I.A(Kilimanjaro International Airport)Hapo angekodi gari ambalo lingempeleka mpaka Arusha kisha aingie boda ya Namanga avuke katika mpaka huo akitumia njia za panya.

Jambo hilo waliamini lingefanyika kwa asilimia mia moja.Ilikuwa ni akili kubwa ambayo ingemfanya Ngesa aingie nchini humo bila kukamatwa.

“Nakutakia kila la kheri Ngesa”

“Ahsante sana”

“Ukifika Kenya,mpakani Namanga.Nipigie kwenye hii namba!Mimi nitakuwa nishapata majibu ni wapi Karanje yupo”

“Ahsante”

Wakapeana mikono na wote kutoka,hawakuelewa kwamba nyuma yao juu kuna kamera ambayo ilikuwa inachukua kila tukio.

Hakukuwa na muda wa kupoteza kuanzia hapo,safari ya uwanja wa ndege ikaanza sekunde hiyohiyo!Ngesa alikuwa ana hasira,hakuelewa angemfanya nini Brigedia Karanje endapo angemtia mikononi mwake,zaidi na hayo ilikuwa ni lazima azuie operesheni yake ambayo ingeua mamilioni ya watanzania wengine.


******

Ilikuwa ni hatari kuliko hatari yenyewe,jambo alilokuwa analifanya Jenipha la kumchunguza tajiri yake, liliogopesha.Wasiwasi mkubwa ulimuingia, ndiyo maana alianza kufanya upelelezi wake chinichini,hicho ndicho kitu kilichomfanya akaanza na kutegesha kamera nyumbani kwa Dustan na hata alivyoaga,hakuondoka alienda kupaki gari lake,kandokando ya uwanja wa Biafra,hapo kila wakati alikuwa anatoa darubini yake ndogo na kuiweka machoni, akiangalia nyumba ya Dustan.Darubini hiyo ilikuwa na lensi kali mno.Hivyo ilikuwa ni rahisi kuivuta nyumba ya Dustan mpaka karibu yake kabisa!Usiku mzima alikuwa yupo katika kazi hiyo nzito,iliyomfanya asilale.

Saa 11;32 Asubuhi,ndipo alipoona mlango wa Dustan unafunguliwa,akajivuta vizuri na kuweka darubini yake machoni.Akamuona Dustan,pembeni yupo na babu mwenye ndevu na nywele nyeupe kichwani,amevalia kanzu na mkononi ameshika kitabu cha dini.Hakuweza kujua ni kitu gani wanazungumza,lakini aliwaona wanaingia ndani ya gari.Hapohapo Jenipha hakutaka kufanya makosa!

“Huyu mzee kaingia saa ngapi?”

Hilo ndilo swali lililokuwa linapita kichwani kwa Jenipha,usiku mzima alikuwa eneo hilo.Hakumuona mzee kama huyo akiiingia nyumbani kwa Dustan.Akawasha gari na kulitembeza kwa mwendo wa taratibu sana,akakunja kona na kuzunguka uwanja mpaka upande wa pili.Ambapo hapo aliliacha gari na kuchukua ‘Master keys’funguo hizo hutumia watu wa usalama,zinafungua kitasa chochote kile.Jenipha,akatembea akatizama huku na kule na kusukuma geti la Dustan,ambapo huko alizama mpaka mlangoni.Akafungua mlango na kuzama ndani,cha kwanza kukifanya ni kuangalia juu,akaona kamera aliyoitegesha ipo palepale.Akapanda na kushuka nayo.Akabonyeza ‘stop’ kisha kuanzisha ili aangalie kila kilichotokea.

“NGESA,HUPASWI KUKAAA HAPA.NJOO HUKU TUFANYE MAMBO HARAKAHARAKA.INABIDI USAFIRI MPAKA ARUSHA,KESHO ASUBUHI SANA”

“ITAWEZEKANA VIPI?ITABIDI NIONDOKE USIKU HUU HUU”

“HUWEZI KUFIKA POPOTE,UTAKAMATWA”

“HIYO ASUBUHI NITAONDOKA VIPI?”

“NDIO MAANA NIKAKWAMBIA NIFUATE”

Jenipha,alibaki kinywa wazi.Bumbuazi alilopigwa halikuwa la nchi hiyo,hakuwa tayari kukubali kwamba Bosi wake pamoja na Ngesa wanashirikiana.Jambo hilo lilikuwa ni hatari sana kama Mh.Rais angejuwa.Akaendelea kuangalia video mpaka mwisho ambapo hapo alimuona Mzee huyo anatokea chumbani,kivyovyote vile akajua huyo ni Ngesa na amebadili muonekano.

Hapohapo,hakutaka kupoteza wakati.Akapiga simu makao makuu ya jeshi la polisi ili kutoa tarifa hiyo nzito.

“Unaongea na Jenipha kutoka usalama wa taifa,kitengo maalum.Nisikilize kwa umakini sana!”

Jenipha alivyojitambulisha,akasema kila kitu kinachoendelea na kuomba aunganishwe na jeshi la ulinzi,Uwanja wa ndege Mwalimu Nyerere,jambo hilo likafanyika.Akaanza kujielezea upya!

“Umesema namba za gari ni ngapi ngapi?”

“T65G 453,Verosa.Nyeusi!Ndani ya gari wapo wawili,Dustan na mzee mmoja.Naomba hiyo gari muizuie mara moja”

“Kwahiyo huyo babu ni Ngesa?”

“Ndio”

“Wewe umemjua…tititii”

Jenipha,akawa amekasirika kitendo cha kuhojiwa maswali mengi mfululizo,alikitafsiri kama ni upotevu wa muda ndiyo maana akaweka simu mfukoni na kuanza kukimbia kuelekea ndani ya gari lake,kitendo cha kuzama na kukaa vizuri nyuma ya usukuani,aliliwasha gari na kulizungusha kwa kasi ya ajabu mno kwa safari moja tu,kwenda uwanja wa ndege ili kuzuia safari ya Ngesa!


******

Verosa nyeusi yenye namba za usajili T65G 453 ilikuwa imesimama kwenye lango la kuingilia uwanja wa ndege,askari aliyepokea taarifa muda mfupi akalitizama gari hilo kwa umakini zaidi.Mbele walikuwa watu wawili kama alivyoelezwa!Mzee na Mtu mzima mwenye umri kati ya miaka 30-45,moyo wake ukaanza kwenda mbio.Habari za Ngesa alizisikia na alimjua namna alivyokuwa hatari,kama kweli alikuwa ni Ngesa aliamini siku hiyo ni lazima angekufa.Kwani mtu huyo aliamini alikuwa ni katili zaidi ya Idd amin Dadaa,kama aliweza kuwatoka askari zaidi ya thelathini iweje yeye.Kosa alilofanya ni kutokutoa taarifa kwa wenzake!Verosa ilivyokaribia,akasogea karibu kabisa na kuipiga mkono.

“Fungua kioo”

Kioo kikashushwa sura ya Dustan ikaonekana.

“Afande habari”

“Nzuri tu,za kazi kiongozi?”

“Salama,unaelekea wapi?”

“Swali gani hilo unaniuliza,naenda Airport. Mzee wangu anasafiri”

Ngesa alikuwa kimya,hajitingishi ameshika tasbii anajifanya anaswali.

“Sasa, unaweza kupaki gari pembeni?”

“Hapana siwezi nina haraka kidogo!”

“Weka gari pembeni tafadhali”

Moyo wa Ngesa ukaanza kupiga kwa nguvu kama mtoto mdogo, aliyemuona daktari ameshika sindano.Hapohapo Dustan akashuka,akazunguka upande aliokuwa askari huyo,akatoa kitambulisho cha usalama wa taifa.

“Kuna operesheni,ninaifanya.Nadhani unajua nchi ipo katika janga na kuna mtu anatafutwa!Naomba niwahi,nikimkosa mtu ninaye mfata.Nitakuhusisha moja kwa moja kwa wewe kumtorosha”Dustan,aliongea kwa umakini sana!Hiyo ilimfanya askari huyu ashindwe kuamini,ni kweli mbele yake kulikuwa na kitambulisho cha usalama wa taifa!Akatafakari kwa muda kidogo.

“Unaitwa afande nani?Nakuuliza unaitwa Afande nani?”

“Afande Masumbuko”

“Ngoja nimpigie Rais Leslie,nimueleze”

“Haina haja piteni”

Uwezo wa kupita kwa kutumia cheo chake alikuwa nao,lakini alifanya hivyo ili asiunguze picha.Alivyorudi ndani ya gari,akazidi kusonga mbele mpaka alipofika eneo maalum la kuegesha magari.Wakatoka ndani ya gari,Ngesa akawa mbele na vazi lake la kanzu.Njiani alikuwa anapewa salamu kama ‘Asalam aelukuy’ sababu ya vazi hilo, kwani alionekana kama ni shekh mkubwa jijini.Walivyofika langoni,hawakuwa na muda wa kupoteza.

“Kila lakheri Ngesa,usisahau kunipigia simu ukifika Kenya,Namanga”

Dustan,alizungumza kwa sauti ya chini.Wakapeana mikono na kuachana.

Gari la Jenipha lilipiga breki kwenye maegesho ya magari, alikuwa tayari amefika uwanja wa ndege Mwalimu Nyerere,akachomoka kama mkuki bila kufunga mlango wa gari,akachomoa bastola yake kutoka kiunoni.

“Kacha! Kacha!”

Akaikoki vizuri huku akikimbia kwa kasi ili amuwahi Ngesa,asisafiri.

Begi dogo la Ngesa lilikuwa mbele, yupo kwenye kimlango kidogo amepanga foleni anasubiri zamu yake ili aingie kisha akapande ndege,mlango huo hakuruhusiwa mtu yoyote kuingia isipokuwa abiria tu.Alivyokuwa hapo,alikumbuka vitu vingi sana.Hususani baba yake mzazi, aliyetaka kumuuwa,mbali na hapo uwanja wa ndege ulikuwa bado upo katika ukarabati kutokana na mashambulizi yaliyofanyika miezi michache iliyopita.Ilivyofika zamu yake,akasikia sauti inamuita na nyuma kulikuwa kuna kama kelele nyingi za watu, wakikimbia.

“Ngesaaaaaaaaaaa!”

Alikuwa ni Jenipha,ameshika bastola anaita kwa sauti!Tayari amefika, Ngesa yupo mbele yake umbali wa kama mita kumi hivi,hiyo ilifanya wananchi wazidi kukimbia huku na kule baada ya kuona bastola.Sijui ilikuwaje,waandishi wa habari wakaanza kupiga picha tukio hilo.Jenipha akapigwa picha na baadhi ya watu wakaanza kumrekodi na simu kichinichini.Ngesa alikuwa ameshtuka,alivyogeuka akamuona Jenipha,ameshika bastola akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya mwewe,hakutaka kuonekana mwenye hofu, hata hivyo alikuwa ana uhakika ya kuwa Jenipha asingeweza kufyatua risasi mbele ya umati wa watu,ndiyo maana bila wasiwasi, akazama ndani.Hiyo ilimfanya Jenipha,aanze kukimbia kuelekea alipokuwa Ngesa,lakini alivyofika langoni akazuiwa na maaskari.

“Huruhusiwi kuingia”

“Mimi ni usalama wa taifa”

“Hata kama,kuna utaratibu wa protocol”

“Nimemuona muhalifu wangu”

“Tunaomba documents yoyote ile ili tukuruhusu”

Hiyo ilimfanya Jenipha aishiwe nguvu,akashusha pumzi ndefu na kutoa simu yake mfukoni kwa jambo moja tu,ampigie simu Rais Leslie, amuelezee kila kitu ili atoe kibali na ndege anayoenda kupanda Ngesa,izuiwe!



 KENYA,NAIROBI.11;45 AM


“Budaaa,vipi pau yangu?Aisee usiniletee ukoraaa”

“Inabidi uonane na mkuu”

“Hayakuwanga makubaliano yetu.Usiniletee za ukuda hapaa!Patia mimi chaapaa zangu,niende budaa”

“Bro!Kuwa mwelewa,mimi mwenyewe kama wewe tu.Tumsubiri mkuu kwanza,ndiyo ana huo mzigo”

“Anakuja time gani?”

“Sasa hivi”

“Sinanga Muda wa kupoteza,nataka time hii niruke zangu Kisumu.Kuna dili naenda tengeneza nipatie chapaa bwanaa”

Ilikuwa ni lazima Bwana Opoka apewe pesa zake, alizohaidiwa baada ya kufanya kazi hiyo nzito ya kutafuta sumu kali inayoitwa Neuro na Cardio-toxic!Sumu hiyo ilikuwa ni hatari sana kwa kiumbe hai chochote kile, ilikuwa ina uwezo wa kusimamisha mapigo ya moyo ya binadamu ndani ya dakika mbili tu.

Swala hilo ndilo lilimfanya Brigedia Karanje awatafute vijana wa kazi watakaoweza kuifanya shughuli hiyo kwa siri, kwa miyadi ya kwamba wangepewa pesa ndefu.Kazi hiyo inaonekana kuwa rahisi sana kutokana na mkwanja uliowekwa mezani.Meja Kayihura,alikuwa tayari amepewa begi ambalo ndani yake kulikuwa na chupa mbili za sumu hiyo kali.

“Hii umeitoa wapi kijana?”

Meja,Kayihura ilibidi aulize sababu alishangazwa sana na hakutegemea kama sumu hiyo ingepatikana kiurahisi.

“Snake…Black Mamba”

Bwana Opoka alijibu bila wasiwasi, wala uwoga akamuelezea Meja Kayihura namna ambavyo, alivyoingia msituni na kumsaka nyoka huyo mwenye sumu kali inayoitwa Neiuro na Cardio-Toxic!Ungemsikiliza na kumwangalia kijana anayehadithia,ungebisha mwanzo mwisho.Kwani haikuwezekana hata kidogo kwa binadamu wa kawaida kucheza na nyoka hatari kama Black Mamba!

“Hapo Back,nilikuwa mutuu ya Zuu!Kuna masonkoo walikuwa wakinipaanga kazi hiyoo.Mimi najuanga kuplay na Simba,niko Fiti atiiii Budaa,siongopi kitu yoyote ile”

Meja Kayihura alikuwa katili lakini kijana aliyekuwa mbele yake anazungumza kwa rafudhi ya Kikenya alikuwa ni mwenye roho ngumu kuliko kawaida.Maongezi hayo yalikuwa yalifanyika katikati ya jiji la Nairobi,West.Katika Mgahawa wa Galaxy,hapo walikuwa wakimsubiri Brigedia Karanje ili wampe sumu hiyo kisha ikachanganywe na kemikali nyingine hatari,ambayo tayari ilikuwa imetengenezwa na Ali Lugemo mfungwa aliyeachiwa huru nchini Tanzania,walifanya hivyo kwa siri kubwa sana na ilikuwa ni lazima wachanganye sumu hiyo kali sana na waisambaze kwenye hewa.Yoyote atakayevuta hewa hiyo yenye sumu,hatochukuwa sekunde hata tatu.Dakika mbili baadaye,gari aina ya Subaru nyeusi, ikawa imefika eneo hilo la mgahawa.

“Mkuu keshafika,twende”

Hakukuwa na haja ya mtu yoyote kushuka ndani ya gari hilo.Meja Kayihura alilitambua gari analotumia Karanje,wakatembea mpaka kwenye gari na kuingia ndani.

Jambo moja lililomshangaza Opoka,ni aina ya sura alizozikuta ndani ya gari.Zilitisha,hususani sura ya mtu aliyekuwa pembeni yake,mrefu kwenda hewani mweusi tii kama mkaa.Usoni ana mabaka!

“Mzigo uko wapi?”

Sauti hiyo kutoka pembeni ilimshtua Opoka,aliyekuwa bado anatafakari.

“Pau yangu?”

“Bwana mdogo.Leta mzigo kwanza”

Brigedia Karanje alivyoona hivyo, ilibidi aseme kwa sauti ya ukali,hiyo ilimfanya Bwana Opoka aanze kutetemeka,sura ya mtu huyo ilimtisha.Na kwa jinsi alivyokuwa ilitosha kabisa kumnyamazisha mtoto anaelia kwa neno moja tu,’HUYO KARANJE ANAKUJA’Sio siri Sura yake haikuonekana kama ni mtu mwenye mzaha,ndiyo maana hata Opoka alianza kuhofia usalama wake.Akatoa begi lake na kumkabidhi,Brigedia Karanje akalifungua akatoa chupa na kumkabidhi kijana mmoja aliyekuwa pembeni.

“Ali,uangalie huo mzigo kama ni wenyewe”

Huyo alikuwa ndiye kama Mkemia mkuu,ndiyo maana Brigedia Karanje alipambana ili atoke gerezani,alikuwa anajua sana, umuhimu mkubwa wa mtu huyo.Wakati wote alikuwa naye ili wakamilishe zoezi lao la kutengeneza sumu hiyo kali.

“Ndio wenyewe”

Ali Lugemo,akaitikia.

“Sawa,sasa tunaelekea wapi?”

“Kiambu”

“Vipi sasa ule mzigo?Ni hatari kukaa nao ndani”

“Inabidi tukautoe tuutupe”

“Ikiwezekana tuuchome moto”

“Sawa”

Opoka alikuwa ni Mkenya lakini alielewa ni kitu gani kinazungumzwa,upeo wake wa akili ulikuwa mkubwa ingawa watu waliokuwa ndani ya gari walikuwa wanazungumza kwa mafumbo.

Katika mazungumzo yao walikuwa ni lazima kila baada ya sekunde moja wamtizame,alishaelewa yeye ndiye anazungumziwa.Mzigo ni yeye na ilikuwa ni lazima wamuuwe.Akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya upepo.

“Pau yangu vipi?”

Opoka,akauliza.Alitaka malipo yake lakini kwa upande mwigine ilikuwa ni lazima ajinasue kwenye mdomo wa mamba mapema iwezekanavyo.Gari akawashwa wakaanza kuchukua barabara ya Pridelands Mlolongo,wasiwasi ulizidi kumshika Bwana Opoka kwani kivyovyote vile alijua barabara hiyo inatokea mto Athi.

Ukimya ulikuwa umetawala ndani ya gari,mwendokasi wa gari hilo ulikuwa ni wa kutisha hiyo ilimfanya Opoka azidi kuingiwa na hofu zaidi.

“Naomba mnishushe hapa”

Bwana Opoka,akasema akawa tayari amekata tamaa.Alithamini sana uhai wake kuliko pesa!

“Bwana mdogo hutaki tena pesa zako?”

“No,tufanye next Day.Kuna mtu ananingonja!”

“Inabidi tukupe pesa zako.Si unataka pesa?”

Mbele yao,umbali wa kama mita kumi hivi kulikuwa kuna kona.Kwa hesabu za Opoka ilikuwa ni lazima wangepunguza mwendo kwenye kona hiyo.Kwa kitendo hiko hakutaka kufanya makosa,ilikuwa ni bora auwawe akiwa anajaribu kujiokoa kuliko kufa kifo cha kikondoo!Kichwani akawa anahesabu,kuanzia moja.Ilivyofika tatu, dereva wa gari,akabadili gia na kupunguza mwendo ili akunje kona.Apolo hakufanya makosa,kama Ngedere mtini,akaruka na kushika kitasa cha mlango kilikuwa ni kitendo cha kufumba na kufumba tayari keshafungua mlango wa gari.Akatua juu ya lami,akajibiringisha chini kama mpira,alivyosimama hapo hakugeuka nyuma,akaingia mitini!Dereva alipiga breki Brigedia Karanje akashuka na Meja Kayahira, wakiwa na bastola mikononi mwao,walivyotaka kuzama msituni Meja Kayahira akamshika mkono Brigedia Karanje.

“Tuachane naye”

“Hapana,atatoboa siri”

“Upo nchini Kenya.Mtu mmoja asifanye tukashindwa kumaliza tulichokianza.Twende Mkuu”

Wazo hilo lilimfanya Brigedia Karanje,autizame msitu huo uliokuwa na miti mingi,sio siri alitamani azame ndani amsake Opoka,hiyo ilimfanya abaki anayabana meno yake kwa hasira.

“Shiiiit”

Akasema na kurudi ndani ya gari,ilibidi wageuze gari na kuelekea mbali kidogo,sehemu inayoitwa Kiambu.Huko ndipo kila kitu kilikuwa kinafanyika kwa siri kubwa mno!Waliwasili Kiambu saa 8;32 Mchana,jua lilikuwa kali kiasi.Wakaingia mtaa mmoja wenye vumbi.Wakanyooka nao mpaka wakatokea kwenye nyumba zilizochoka kwa mbali,hapo gari likazimwa wote wakashuka garini na kuzama ndani ya nyumba hiyo.Ambapo walipitiliza mpaka chumbani,huko waliambiwa kabla ya yote wavae ‘Mask’usoni,hiyo ilikuwa tahadhari namba moja kwani walitaka kuanza jaribio lao,kila mmoja wapo akavaa.


Hawakutofautishwa na watu waliokuwa majini,kwani sura zao zilizibwa hususani puani.Mask hizo zilikuwa na ‘pipe’ ndefu iliyochomekwa mwenye mtungi wa hewa ya Oksijeni, kwa maana nyingine walikuwa wakivuta hewa ndani kwa ndani.

“Mkuu,tunaanza jaribio”

Begi likatolewa na Ali Lugemo akatembea mpaka kwenye meza kubwa,juu yake kulikuwa na vibakuli vya bati, nane.Kila kimoja kilikuwa na rangi yake!Hapohapo,akaanza kuweka matone kwenye kila kibakuli.Walivyosubiri kwa dakika moja,wakaona kibakuli cha tatu kimeanza kutokota kama maji yaliyokuwa ndani ya sufuria la moto.Ali Lugemo akamtizama Brigedia Karanje na kuchukua kibakuli kilichokuwa kinatokota,akaingia moja kwa moja kwenye chumba kidogo kilichokuwa na Panya wengi,akaweka na kuanza kuangalia saa yake.Ndani ya sekunde tano Panya wote walikuwa wamekauka hapohapo.Hiyo ilionesha kwamba sumu hiyo ni hatari kuliko kawaida,akamuita Brigedia Karanje na kumuonesha kila kitu.

Jambo hilo lilikuwa furaha kwake japokuwa hakuridhika.Wakaletwa wanyama aina ya paka na kuingizwa ndani ya chumba hiko, hawakuchukuwa sekunde,wakawa wamekauka wamelala chini.Hiyo ilikuwa dalili tosha ya kwamba sumu hiyo ni kali.Jambo lililofanyika ni kuanza kuitengeneza ndani ya vichupa vidogo vidogo mpaka vilivyofika idadi ya Kumi na tano.Zoezi hilo lilivyoisha wakatoka nje na kuvipakia ndani ya gari.

“Tunarudi Tanzania”

Brigedia Karanje alisema baada ya gari kuanza kurudi kinyumenyume,kwa mara ya kwanza alitabasamu na kulishika begi jeusi ambalo ndani lilikuwa na sumu hiyo kali ambayo ingeua mamilioni ya watu.

“Nataka siku moja niandikwe kwenye vitabu vya historia.Kama akina Adolf Hilter”

Brigedia Karanje aliwaza!


********

TANZANIA,Dar es Salaam.Mwalimu Nyerere International Airport!05;42 A.m


Kila kitu kilikuwa kimevurugika,watu walianza kusambaa huku na kule.Bastola aliyoitoa Jenipha mbele ya umati wa watu, ilifanya hofu iwatande hata abiria waliokuwa wanasafiri,hilo lilikuwa ni kosa kubwa sana kisheria lakini alifanya hivyo ili kumuweka chini ya Ulinzi Ngesa,ambaye kwa wakati huo alikuwa tayari keshaingia ndani ya uwanja na angechelewa kwa dakika kumi basi angemkosa kwani ndege ingeruka angani.

Kuingia ndani na kumfuata haikuwa kazi rahisi ilikuwa ni lazima apewe kibali maalum,ndiyo maana akapiga simu moja kwa moja mpaka ikulu.Akitaka kuzungumza na Rais Leslie!Baada ya simu kupokelewa na msaidizi wa Rais,akajitambulisha bila kupoteza wakati.

“Rais,amepumzika sasa hivi”

“Ni dharura!Ni muhimu sana”

“Dada,sijui umeleewa nachozungumza”

“Nimekuelewa.Mwambie kuhusu Ngesa,ataelewa”

Upande wa pili wa simu,ukawa kimya kwa kama sekunde tatu nzima.

“Hallooo”

Alisema Jenipha,baada ya ukimya huo.

“Sawa subiri,ndio nataka kumpelekea simu”

Mr.Pelegreen,alitembea kwa hatua za haraka sana mpaka alipoufikia mlango wa chumba anacholala Rasi Leslie,hapo kulikuwa na watu wawili wamesimama.Walinzi maalum!

“Kuna simu ya Mh.Rais”

“Amepumzika”

“Ni muhimu sana”

Mlinzi huyu akamtizama Mr.Pelegreen kwa kitambo kidogo,akabonyeza kikengele cha juu mara mbili.

Mh.Rais wakati huo hakuwa ana raha hata kidogo, hivyo usingizi wake ulikuwa wa mang’amung’amu.Haraka,akaipokea simu ambayo kwa upande mwingine ilikuwa ni kengele.

“Sema”

“Kuna mtu anahitaji kuzungumza nawewe”

“Nani?”

“Mr.Pelegreen”

Ikulu kulikuwa na Kamera kila kona,Rais Leslie hakutaka kukurupuka kutoka nje,akanyoosha mkono mpaka mezani ambapo kulikuwa na rimoti,akawasha tivii.Kilichotokea juu ya kioo ni Sura ya Peregreen akiwa mlangoni na walinzi wawili kwa maana nyingine nje ya mlango wa Raisi kulikuwa na ulinzi wa Kamera za CCTV.Alivyohakikisha kuna usalama,akasimama na kuvaa bukta,akatokeza mpaka mlangoni.

“Samahani kwa usumbufu Mkuu”

Mr.Pelegreen aliomba radhi.

“Una shida gani?”

“Kuna simu yako”

“Kutoka wapi?”

“Jenipha,ana habari anataka kukupa.Ni dharura”

Rais Leslie,akachukua simu na kuiweka sikioni.Hapohapo Jenipha akaanza kujitambulisha na kusema kila kitu kwa ufupi.

“Wewe umejuaje?”

Ilielekea Jenipha hakutaka kumchomea Dustan lakini swali hilo lilifanya akae kimya kidogo.

“Mh.Leslie nachoomba ni ruksa ya…”

“Jibu swali binti”

“Ni Dustan Mh.Rais”

“Dustan?”

“Yes ni DK”

“Whaaaaaat,haiwezi kuwa kweli”

“Mh.Rais nachoongea nina uhakika nacho,mkanda ninao kama nilivyokwambia.Naomba kibali”

“Anapanda ndege gani?”

“Sijui Mh.Rais”

“Naomba Dustan,akamatwe mara moja”

Hapohapo simu ikakatwa Raisi Leslie,akaiomba simu ipigwe moja kwa moja kwenye kikosi cha usalama wa Anga,swala hilo likafanyika mara moja.


********

Kitendo cha vurugu kutokea uwanja wa Ndege kilimfanya Dustan,asitishe zoezi lake la kutaka kuingia ndani ya gari,alikuwa yupo mita chache tu.Alivyoangalia vizuri akamuona Jenipha.Jambo lililomfanya ashtuke mno!Hakuelewa ni kwanini yupo mahali hapo lakini kitendo cha kuita jina ‘Ngesa’ na kuchomoa bastola kilimfanya aanze kuhisi kitu,kulikuwa kuna kila dalili mbaya za yeye kuhusishwa na mpango aliousuka na Ngesa,akaingia ndani ya gari lake haraka sana.Hakutaka kubaki eneo hilo.Dk alikuwa ni mwanausalama hivyo kivyovyote vile alijua, baada ya hapo ni lazima angetafutwa na kuwekwa chini ya ulinzi mkali ili ataje ni wapi Ngesa alipo.Kifupi mambo yalikuwa sio mambo tena!Akiwa ndani ya gari,hapohapo akatoa simu yake mfukoni akaishika mkononi,mkono mmoja upo kwenye usukani,mwingine kashika simu anasaka majina kwenye phonebook mpaka alipolifikia jina ‘WIFE’akaruhusu simu iruke,kisha kuiweka sikio la kushoto.

“Griii griiiii,Griiii griiiiii griiii griiiii”

Simu iliita bila kupokelewa,akapiga tena lakini wapi,akapiga tena na tena.Alivyopiga kwa mara ya sita ndipo ikapokelewa.

“Jesca…”

Dk akaita.

“Dustan,vipi?Mbona asubuhi sana?”

“Nisikilize kwa umakini”

“Nakusikiliza”

“Paki kila kitu chenye umuhimu.Pamoja na watoto,nakuja hapo sasa hivi”

“Dustan,mbona sikuelewi kuna nini?”

“Fanya nilichokwambia Jesca,nina uhakika wanakuja hapo”

“Wakina nani?”

“Jesca please,fanya nilichokwambia sasa hivi”

“Sawa”

Ilikuwa ni lazima kwanza Dustan,apite Upanga akachukuwe baadhi ya vitu kisha aende posta kwenye nyumba za usalama wa taifa aichukuwe familia yake,akaifiche mbali.


********

Maelezo yaliyotolewa na Jenipha pamoja na ushahidi wa video alioonesha ulifanya pia DK aingizwe moja kwa moja kwenye orodha ya watu wanaosakwa hivyo ilikuwa ni lazima,wamtafute wamuweke chini ya ulinzi.Uwanja wa ndege siku hiyo kulichafuka maaskari.Ilikuwa ni lazima Ngesa akamatwe siku hiyohiyo, kwani picha yake akiwa katika muonekano wa kizee ilionekana baada ya uchunguzi wa CCTV camera.Shirika la ndege aina ya Precion Air 4578 haikuweza kuruka tena mpaka wamshushe Ngesa aliyekuwa ndani ya ndege hiyo,maaskari wakawa tayari wana vibali,wakaingia na kupita moja kwa moja mpaka nje ya uwanja ambapo ndege nyingi zilikuwa zimepaki.Askari saba wakiwa na mitutu wakaanza kupanda ngazi za ndege,wakaingia ndani na kutoa picha kubwa.

“Ngesa,tunajua upo humu ndani.Huwezi kwenda popote pale!Tunajua kuwa unatumia jina la Athuman Mtwenge,simama kwa usalama wako.Hatutoshindwa kumtoa mmoja baada ya mmoja nje ya ndege,hata kama upo kwenye mizigo tutakupata tu.Leo hutoki humu”

Kipaza sauti kilisikika,sauti ilikuwa imatokea kwenye spika,wakatangaza kwa mara ya pili lakini hakukuwa na dalili ya mtu yoyote Yule kusimama, hapo ndipo maaskari wakaanza kukagua mtu mmoja baada ya mwingine.

“Vua miwani”

Watu walipekuliwa,viti vilibinuliwa.Abiria wote walikuwa wamepekuliwa kasoro mtu mmoja tu,alikuwa amekaa siti ya nyuma amevaa kibalaghashee,ameinama chini.Askari wakakoki bastola zao ili kumsogelea mzee huyo wakiwa wana uhakika ni lazima atakuwa Ngesa tu.

“Mzee,vua kofia yako.Tunahitaji kuona sura yako”

Askari mmoja akasema huku akiwa tayari kwa mashambulizi,kwani aliuelewa mziki wa Ngesa!


********

DK tayari alikuwa ameingia kwenye vita kubwa bila kutarajia na alijua kivyovyote vile ni lazima angefungwa kwa kosa la kwenda kinyume na taratibu za jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Kilichomfanya awaze zaidi, hakujua huko Uwanja wa Ndege ni kitu gani kiliendelea,hakuwa ana uhakika kama Ngesa atakamatwa ama atawatoka maaskari kama kawaida yake.Alivyofika Upanga,akabeba kila kitu cha umuhimu,kisha kuzima simu yake.Alielewa kivyovyote vile kupitia simu yake wangeweza kumfuatilia ni wapi alipo kwa njia ya GPRS.Akarudi ndani ya gari na safari ya kwenda Posta kuanza hapohapo!


******

Jesca,alionesha hali ya kupagawa kabisa.Hakuwa na jinsi zaidi ya kuanza kuweka nguo zake sawa akiwa mwenye wasiwasi mkubwa.Simu kutoka kwa Mmewe ilimshtua, alijua kuna jambo zito mbele litatokea kama hatofuata alichoambiwa,alivyomaliza kupanga kila kitu akaingia chumbani kwa watoto wake,akawaamsha.

“Mooom,Where are we going?”(Mama tunaenda wapi)

Mtoto huyu aliuliza kwa kiingereza,alikuwa ni mdogo lakini kwa picha aliyoona alijua siku hiyo hakuna shule,kuna sehemu wanaenda ndiyo maana akahoji.

“Moom”

Mtoto akaita tena lakini ilionekana Mama hakuwa ana jibu la harakaharaka,akawavalisha nguo watoto wote wawili,akabeba begi alivyofika seblen akasikia mlango unagongwa.Mapigo yake ya moyo yakapiga kwa nguvu akajuwa tayari amekwisha.Alivyotulia tena kwa sekunde nyingine,mlango ukagongwa tena!

“Naniii?”

Akauliza.

“Fungua mlango”

Jesca,akapata mshtuko wa wazi.Katika kujishauri sana akasikia kama kitasa cha mlango kinachokonolewa,hazikupita sekunde tatu mlango ukawa umefunguka, wanaume watatu waliovaa suti nyeusi wakawa wameingia ndani.

“DK yuko wapi?”

Bila salamu wakaanza kuuliza.

“Nakuuliza,DK yuko wapi?”

“Hayupo”

“Yuko wapi?”

“Tangu ja..na jana sijamuona”

“Nimekuuliza yuko wapi?”

“Sijui”

“Jesca,usitutanie.Mmeo yuko wapi?”

Jesca,alishtuka hakuelewa watu hao wamelifahamu vipi jina lake!

“Dustan,yuko wapi?”

“Hakulala hapa jana”

“Tunajua alilala Upanga,yuko wapi sasa hivi?”

Mvua ya maswali ilishuka,watu hao hawakuonesha mzaha hata kidogo.Mmoja wao alivyoangalia pembeni na kuona begi la nguo,akashtuka na kumtizama Jesca machoni.

“Sasa hivi asubuhi unaenda wapi?”

“Siendi popote”

“Na hilo begi?”

“Nilikuwa napanga tu nguo zangu vizuri”

Mwanamke huyu alikuwa hajajipanga kujibu maswali,kilichowafanya watu hao wajuwe anaongopa ni baada ya watoto wadogo wawili kutoka wakiwa wamevaa nguo nzuri na viatu.

Jesca alihisi kutetemeka zaidi, baada ya simu yake kuanza kuita,ilikuwa mezani.Wote wakapiga jicho mezani, ilielekea walitaka kujua mpigaji alikuwa ni nani,juu ya kioo namba ndizo zilitokea kumaanisha zilikuwa ni namba ngeni.Simu ikawa inaita,Jesca akapata kitete kuipokea!

“Pokea simu Jesca,weka loudspika”

Kauli hiyo ilitoka kwa mmoja wa mijitu hiyo iliyokuwa haicheki.Jesca,hakuwa na jinsi alivyoipokea akaiweka laudspika ili sauti isikike.

“Jesca,ushajiandaa?”

Upande wa pili wa simu ukasikika,ilikuwa ni sauti ya Dustan, hapo ndipo Jesca akahisi mkojo unampenya akashindwa kujibu chochote.

“Hallooo,Jesca!Hallooo…ttitititi”

Kwa mawazo ya harakaharaka ilikuwa ni lazima Dustan alidhani mtandao unasumbua, ndiyo maana akakata simu,hazikupita hata sekunde mbili.Simu ikaanza kuita tena!

“Ukijaribu kufanya kitu chochote cha kipumbavu,nitakupiga risasi”

Haukuwa utani hata kidogo,jamaa mmoja alichomoa bastola na kumuwekea Jesca kichwani watoto wakavutwa na kupelekwa chumbani,hiyo ndiyo ilimfanya ajawe na hofu zaidi.

“Narudia tena,ukifanya upumbavu wowote……..”

Jamaa huyo akaishia hapo na kumtizama Jesca machoni kikauzu,simu ikapokelewa akaweka laudspika.

“Jesca,tayari ushajiandaa? Nakaribia kufika”

“Mimi mimi nipo tayari”

“Nikukute hapo nyumbani,kuna begi langu dogo jeusi, lipo kwenye kabati droo ya chini litoe nikukute nalo”

“Sawa”

“Watoto ushawaandaa?”

“Ndio”

“Mbona unaongea hivyo?Upo sawa?”

“Dustan,nashindwa kukuelewa maisha gani haya?Maisha gani haya tunaishi,mimi nitashindwa.Siwezi tena si..wezi.Kwanini la..”

“Jescaaa,Jescaaa Mke wangu..Nisikilizeee niku….”

“Siwezi ku..kusikiliza Dustan”

Jesca alikuwa akiongea kwa kwikwi,alikuwa akilia machozi.Mambo yaliyokuwa yanatokea yalimfanya apatwe na uchungu ajabu, kitu kilichomuuma ni baada ya kukumbuka Mimba yake ilivyotoka kipindi alivyotekwa na Brigedia Karanje,yote hayo yalikuwa ni sababu ya Dustan.

“Nisubiri nyumbani….tititi”

Simu ikakatwa huku ikimuacha Jesca analia kwa kwikwi.


********

Katika hatari aliyokuwa nayo ilikuwa ni lazima alijuwa anawindwa kwa wudi na uvumba,hivyo ilikuwa ni lazima achukue tahadhari kabla ya hatari.DK alihisi kuchanganyikiwa ndiyo maana baada ya kutoka kuongea na mkewe simuni alikuwa anakimbiza gari kama mwehu,uhakika wa jeshi la polisi ama usalama wa taifa kuanza kumsaka ulikuwa themanini kwa mia moja, hivyo ilikuwa ni lazima ajihami,ndiyo maana akachomoa bastola yake na kufunga kiwambo cha kuzuia sauti ya bastola isiwe kubwa.Alivyofika posta karibu na mafleti ya usalama wa taifa,akaweka gari mbali kabisa na kuanza kuangalia huku na kule.Hakutaka kupitia mlango wa mbele,ilikuwa ni kama amechezwa na machale vile kwani familia yake ilikuwa tayari ipo chini ya ulinzi.Alivyozunguka uwani,akatembea kwa tahadhari kubwa,alichofanya ni kupita mpaka dirisha la chumba anacholala yeye na mkewe,akachungulia vizuri akaona hakuna mtu yoyote Yule.

Akazunguka chumba cha watoto wake,hapo ndipo alipopigwa na butwaa baada ya kuwaona wanaume wawili wamevaa Suti,wapo na watoto wake.

“Shiiit”

Akachomoa bastola na kuanza kutafakari ni njia gani afanye,hakuelewa ni watu wangapi wapo ndani ya nyumba yake ndiyo maana aliendelea kuizunguka kwa nyuma,alivyofika dirisha la seblen.Napo akachungulia,akamuona mkewe yupo chini ya Ulinzi kawekewa bastola.Akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya umeme,akachomoa simu na kumpigia mkewe,niya yake ikiwa jambazi huyo akae vizuri katikati ili amtungue na risasi.

“Pokea simu”

Mtu huyo hakuwa anaelewa,akasimama na kushika simu akampa Jesca, bila kujua yupo kwenye tageti.

“Pyuuuuuuu”

Huo ndio mlio wa bastola ulivyosikika risasi moja tu, ilipenya na kufumua kichwa chake.Jitu hilo likadondoka chini.Dustan,akavuta pazia na kumuoneshea mkewe kwa ishara asipige kelele!Kwa haraka,akazunguka mpaka mlangoni na kuufungua!

“Usipige kelele”

Dustan,akasema kwa sauti ya chini akimwambia mkewe!Akairuka maiti na kupita kwa niya ya kwenda chumbani kwa watoto wake,akawakomboe!Akanyata taratibu na kufungua mlango,kabla ya kuumalizia wote,akahisi kama kuna kichuma cha baridi, kimemgusa kisogoni.

“Tulia hivyo hivyo Dustan.Weka bastola yako chini”

Sauti nzito ilimuamuru Dustan,akajikuta anaishiwa nguvu

.



.Dustan,akavuta pazia na kumuoneshea mkewe kwa ishara asipige kelele!Kwa haraka,akazunguka mpaka mlangoni na kuufungua!

“Usipige kelele”

Dustan,akasema kwa sauti ya chini akimwambia mkewe!Akairuka maiti na kupita kwa niya kwenda chumbani kwa watoto wake,akawakomboe!Akanyata taratibu na kufungua mlango,kabla ya kuumalizia wote,akahisi kama kuna kichuma cha baridi, kimemgusa kisogoni.

“Tulia hivyo hivyo Dustan.Weka bastola yako chini”

Sauti nzito ilimwambia Dustan,akajikuta anaishiwa.

SONGA NAYO.


Ilikuwa ni sauti ya kukwaruza tena nzito ikitokea nyuma ya Dustan,tayari alikuwa chini ya ulinzi na alijuwa kivyovyote vile kama angeenda kinyume, jambo baya lingemkuta kwani alijua nini maana ya bastola,kwa maana hiyo ilibidi atulie kama maji mtungini.Taratibu alianza kushusha mkono wake uliokuwa na bastola chini.

“Paaaaaaaaa! Paaaaaaaaa! Paaaaaaa!”

Kabla ya kuweka bastola chini ulisikika mlio mkubwa wa risasi, kufyatuka.Jamaa aliyekuwa nyuma ya Dustan alikuwa amefumuliwa na risasi tatu,mbili za mgongo moja ya kichwa.DK baada ya kugeuka nyuma alimuona mkewe akiwa anatetemeka ameshika bastola huku machozi yanamchuruzika,ni wazi tukio alilolifanya lilimuogopesha.Kwani katika maisha yake mwanamke huyu hakuwahi hata kuuwa panya,leo hii ameuwa mtu.Ni jambo lililomfanya atetemeke kwa hofu huku akiwa anaiangalia maiti iliyokuwa chini.

“Jesca,taratibu shusha mkono wako chini Mke wangu”

Ilibidi Dustan aseme hivyo sababu alijua hali aliyokuwa nayo mkewe kwa wakati huo,ndiyo maana akaongea kwa sauti ya chini huku akimsogelea kwa tahadhali,akamfuata mpaka karibu kabisa na kuichukua bastola.

“Du...stan nimeu..a”

Jesca alizungumza kwa kwikwi.

“Ilibidi ufanye hivyo Jesca,umeniokoa”

Wote wakawa wamekumbatiana kwa kama sekunde tatu nzima,watoto wakawa wametokeza.Dustan hakutaka kuishia hapo,alitaka kujua watu hao ni akina nani,akainama kidogo na kuanza kuingiza mkono mifukoni mwa maiti hiyo,akachomoa wallet na kuanza kukagua vitambulisho.

“Jesus Christ”(Yesu Kristo)

Butwaa alilopigwa nalo Dustan halikuwa la kawaida hata kidogo,hiyo ni baada ya kugundua maiti aliyelala alitoka kitengo maalum Ikulu,jambo ambalo lilimtisha mpaka yeye,akamuangalia Jesca kwa umakini.

“Tuondoke,beba vitu vyako haraka Jesca”

“Tunaenda wapi?”

“Tutaongea”

Hivyo ndivyo ilivyokuwa,Dustan na familia yake ilikuwa tayari imeingia kwenye hatari kubwa mno.Watoto wakawa hawaelewi chochote,wote wakatoka mpaka nje na kuangalia katika maegesho ya magari,kabla ya Dustan kuingia ndani ya gari, kuna kitu alikiona.Lilikuwa ni gari aina ya Hiace,gari hilo alilifahamu vizuri lilikuwa la Ikulu.Hivyo akajua tayari ataanza kufuatiliwa.Ni kweli ilikuwa ni kama ametabiri kwani kitendo cha kuingia ndani ya gari lake na kulirudisha kinyume nyume gari hilo aina ya Hiace nalo lilianza kutembea kumfuata.

“Fungeni mikanda”

Dustan,akasema na jambo hilo lilifanyika hapohapo.Ilikuwa ni lazima awatoke watu hao, ambao aliamini walitumwa na Rais Leslie.Hakutaka kukubali kukamatwa kwani angeingia kwenye matatizo mengine zaidi.

Hiace yenye rangi ya kijivu yenye namba za usajili TY56 768, ndani lilikuwa limebeba watu nane kutoka kitengo cha usalama wa taifa,ikulu.Agizo hilo walipewa na Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania,kwamba wamuweke Dustan chini ya ulinzi ili aseme ni wapi Ngesa alipo.

Zoezi hilo kwao lilikuwa ni rahisi sana,walilifananisha na kuuwa mbu ndani ya neti.Ndiyo maana hawakutaka kutumia nguvu,kwao walitumia akili nyingi.Ndio maana hawakuwa peke yao.Mnazi mmoja kulikuwa na gari nyingine za usalama tatu na walikuwa wakiwasiliana ili waliweke gari la Dustan katikati.

“Ndio anatoka.Yupo Posta.Daraja la salenda,zungukeni mkatokee Moroco.Jerry,tokeeni ubalozi,hakikisheni havuki mataa ya Moroco”

“Sawa mkuu”

“Sawa mkuu”Wote wakaitikia,kukubali amri hiyo.

Jukumu la kuendesha Operesheni hiyo ya kumsaka Ngesa na Dustan alipewa Mr.Isaya Msophe.Huyu muda wote alikuwa siriazi sana.Hakuwa mtu wa kucheka na wafanya kazi wake, ndiyo maana alizungumza na kutoa amri mara moja na jambo hilo likaanza, kufanyika.Kwenye simu aliyokuwa anaitumia kuwasiliana, ilifanya wanausalama wote wasikie.Jambo la kumtia Dustan mikononi mwao, lilikuwa ni lazima likamilike,mbali na hapo Mr.Isaya Msophe hakutaka CV yake ichafuke,kumkosa Dustan ingetafsiriwa ni uzembe katika kazi,ndiyo maana hakutaka heshima yake ishuke.Gari la Dustan lilikuwa mbele yao umbali wa kama mita mia mbili hivi.

“Hilo gari lisikupotee Rashid”Mkuu wao, Mr.Isaya Msophe akasema, akimwambia dereva macho yake yalikuwa makini anatizama gari alilokuwa anaendesha Dustan.

“Haliwezi”

Kila kilichotokea kilikuwa ni kama maigizo ya sinema fulani ya kijasusi.Dustan alikuwa akikimbiza gari, niya yake ilikuwa ni kulichenga gari linalomfuata kwa nyuma,kwa kutokufanya hivyo ilimaanisha angeingia kwenye msala mkubwa mno, kifupi jela ingemuhusu kwa kosa la kumtorosha muuaji kwa maana nyingine msalaba wa Ngesa,angeubeba yeye!Hesabu zake zilikuwa ni kali,akunje Moroco na kwenda Kinondoni B,aliamini huko angewachenga.Akazidi kukanyaga mafuta, gari ikazidi kukimbia kwa kasi.Alivyokunja kona ya Moroco,alisikia kishindo kikubwa upande wake wa kushoto.Lilikuwa ni gari aina ya Nissan Patrol limemgonga kwa pembeni,akili yake ikafanya kazi kwa kasi,akapiga gia kurudi nyuma lakini alikuwa amechelewa tayari kwani gari lingine lilifika hapohapo na kusimama mbele yake.Wanaume wawili warefu futi nyingi kwenda hewani, wakashuka wakiwa na bastola mikononi mwao.

“Shuka ndani ya gari Dustan,usifanye zoezi hili likawa gumu”

Midomo ya bastola ilikuwa ikimtizama yeye akiwa ndani ya gari,hapo hakuwa ana ujanja tena ilibidi atoke na kusalimu amri.

“Upo chini ya ulinzi”

Gari la Dustan lilizungukwa ma wanaume hao makini kutoka usalama, ambao walimkamata DK bila kutumia nguvu zozote zile,wao walitumia akili na sio maguvu.Sio siri kitu kilichomuogopesha Dustan zaidi na kumfanya aingiwe na hofu nyingi ni familia yake,yaani mkewe pamoja na watoto wake ambao walikuwa ni wadogo bado!

“Shuka ndani ya gari”

Jesca,alilengwa na machozi tayari maji yalikuwa ya shingo, akamtizama mmewe kwa masikitiko makubwa sana.

“Wote shukeni”

Kauli hiyo ilimfanya Dustan,ashuke kwa kasi akiwa ameweka mikono hewani.

“Naomba muiachie familia yangu”

Watu hao hawakujibu,wakamfunga pingu Dustan kwa nyuma.Mkewe na watoto wake wakashushwa na mmoja wa wanausalama akaingia kwenye gari la Dustan,hapohapo wakaanza kuondoka wakiwa na Dustan chini ya ulinzi.


*******

Askari waliokuwa ndani ya ndege ya shirika la Precision Air wakifanya msako mkali,walionekana kuzidiwa akili kwani Ngesa hakuwepo,hawakukubali waliendelea kusagula sagula ndege nzima mpaka kwenye mizigo lakini hakukuwa na dalili yoyote ile ya Ngesa kuonekana,mzee aliyekuwa amevaa kanzu waliyedhani ni Ngesa ilibidi abaki ameduwaa,akiwashangaa.Tukio hilo askari walilifananisha moja kwa moja na ushirikina.

“Hii sio kawaida”

Mmoja wa maaskari alisikika akimwambia mwenzake.

“Kivipi?”

“Huyu jamaa anatumia nguvu za giza”

“Inawezekana”Mwenzake akaonekana kusapoti hoja hiyo.

“Sio inawezekana,nina uhakika yule mtu ana irizi.Tena irizi yake kali”

Kazi hiyo ilizidi kuonekana kuwa ngumu zaidi na zaidi.


******

Hakuwa mjinga,alikuwa ana akili zisizokuwa za kawaida kuwa nazo binadamu.Alishaelewa ni kwa kiasi gani Askari wangemtafuta na isitoshe wangemuua kwani tayari aliwatia hasira,akili yake bado ilikuwa ikichaji.Zaidi ya yote hakuelewa Jenipha alimgundua vipi, hilo ndilo jambo lililomfanya asitishe zoezi la kwenda kupanda ndege ya Precision Air.Kifupi Ngesa alisomea mambo ya upelelezi, hivyo alijua njia zote wanazotumia.Akiwa na begi lake dogo mgongoni,aliingia chooni na kuanza kutafakari ni kitu gani akifanye,hakuwa tayari kurudi ilikuwa ni lazima asonge mbele kwani maji alikuwa keshayavulia nguo tayari.Akatulia kidogo, akasikia kuna mtu anaingia chooni,akamsubiri mpaka aingie kabisa.Alivyotundika nguo zake juu ili ajisaidie akazivuta.Haraka,akatoka eneo hilo na kuingia ndani ya chumba kingine, huko alibadili nguo na kuvaa alizoiba.Kanzu akaiweka ndani ya begi,akapiga hesabu za haraka haraka na kuona kuna mlango mdogo,akajipenyeza!Huko kulikuwa na watu wamevaa sare maalum,ili kuogopa kugundulika akavuta koti la kijani mithili ya Ovalori akalivaa na kufanana na wafanyakazi wa eneo hilo,akatembea mpaka nje ambapo huko kulikuwa ni upande wa pili.Ndege ndogo zilikuwa zimeegeshwa,akatizama huku na kule,akamuona mlinzi anatembea akipiga doria.Akaitizama ndege ndogo ya kitalii,ndani kulikuwa na rubani anabonyeza bonyeza mitambo.Kumaanisha ndege hiyo baada ya muda mfupi itakuwa angani,hakutaka kupoteza sekunde hata moja.Akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya mwewe,akaokota chuma kidogo kilichokuwa chini,akamsogelea mlinzi aliyekuwa anavuta sigara na kumuwekea kichuma hiko shingoni.

“Ukigeuka tu,nasambaratisha ubongo huo.Tulia hivyohivyo usipige kelele”

Ngesa alizungumza hivyo kwa sauti ya mtu anayejiamini huku akiwa ameshika kichuma hiko kamuwekea mlinzi shingoni.Kutokana na hofu aliyokuwa nayo mlinzi,akajikuta anadondosha kipisi cha sigara kilichokuwa mdomoni bila kupenda,akidhani wenda amewekewa bastola.

“Toa bastola yako,nipatie haraka sana”

Ngesa alizidi kuzungumza na kumfanya Mlinzi, atoe taratibu bastola yake kutoka kiunoni,akampa Ngesa aliyekuwa nyuma yake.Ilikuwa ni lazima mlinzi,anyamazishwe!Akapigwa roba kali lililomfanya ashindwe kutoa hewa vizuri, ndani ya dakika mbili akawa amepoteza fahamu,akaburuzwa mpaka kandokando ya mapipa ya mafuta,Ngesa akakamata bastola vizuri.Akatizama huku na kule.Akaanza kukimbia kuifuata ndege hiyo ndogo ya kitalii.

“Tulia hivyohivyo ulivyo”

Kufumba na kufumbua,rubani wa ndege alikuwa tayari yupo mateka.Ngesa akafungua mlango wa ndege na kukaa naye pembeni.

“Paisha ndege,fanya haraka.Sitorudia tena kwa mara nyingine”

Mdomo wa bastola ulikuwa kichwani kwa rubani,mtu anayezungumza naye hakuwa ana chembe hata kidogo ya masihara!Ndiyo maana hakutaka kupinga kauli yake,akabonyeza kitu fulani kilichokuwa juu.Mapanga boi yakaanza kuzunguka.Akashika kitu kama kirungu,akafanya anavyojua yeye Ndege ikaanza kutembea taratibu sana kisha ikaanza kuchanganya mwendo,ikapaaa angani.Ngesa akashusha pumzi ndefu,hakuamini kuwa kwa mara nyingine alikuwa amewachenga askari.

“Tunaenda wapi?”

Rubani,akauliza.

“Kenya”

“Kenya?”

“Ndiooo,tutaingia baada ya muda gani?”

“Masaa mawili na nusu”

Jibu hilo lilimfanya Ngesa,amtizame Rubani huyu aliyekuwa bize anashughulikia kuipaisha ndege angani zaidi.


*******

Taarifa za Ngesa kutafutwa,zilizidi kusambaa, karibia nchi nzima ya Tanzania.Mbaya zaidi aliingizwa kwenye kundi la magaidi,akapewa kesi mbaya ya mauaji.Hiyo ilifanya picha zake zibandikwe,kila wakati alitangazwa vituo mbalimbali vya televisheni kama SK Tv,Redio One,Clouds Tv na Global Tv.Kitendo cha Daphine kufumbua macho akiwa hospitalini,alikumbana na habari hiyo iliyomfanya ashangae na kupigwa na bumbuazi.Akazidi kukaza macho yake juu ya kioo cha luninga, iliyokuwa juu kidogo,akaona picha ya Ngesa imewekwa na anatafutwa.

“Amefanya nini,yule jamaa?”

Ilibidi Daphine amuulize Nesi,aliyekuwa pembeni yake.

“Gaidi huyo,muuaji.Sindo yule Ngesa wa kipindi kile.Alikuwa anataka kwenda kunyongwa,akasamehewa na Rais”

Nesi,akajaribu kutoa taarifa ndefu kidogo hakuelewa mgonjwa aliyemuuliza hilo swali wana uhusiano wa karibu sana na Ngesa!

“Kamuua nani?”

“Mh.George Kimpanga”

Daphine,akabaki ameduwaa habari hiyo kwake ilikuwa mpya na iliyomshangaza sana!Hakuelewa kama ni kweli ama uvumi.

“Kwahiyo bado hawajampata?”

“Ndio”

Hapo Daphine,akatulia kidogo na kumuangalia Nesi huyo aliyeshika trei juu lina sindano,akatizama pembeni na kuona mikasi pamoja na visu.Kuna akili moja ilimjia ya haraka lakini hakuelewa kama yupo sahihi kulifanya jambo hilo ama ataharibu.

“Lazima nifanye juu chini,nitoke mahali hapa”

Daphine aliwaza na kuangalia juu ya luninga,ambapo aliona sura ya Ngesa imegandishwa chini yake yanapita maneno ya kwamba,anatafutwa….



 Kichwa chake kilijawa na mawazo chungu mzima,alitaka kujua nini Ngesa amefanya mpaka Serikali ya Tanzania imtafute kwa mara nyingine.Ndiyo maana akatamani,amsake ajuwe alipo ili amuulize maswali hayo mengi.Katika kutafakari kwake alipata jibu moja tu,atoroke ndani ya hospitali hiyo ili amsake Ngesa ingawa hakujua ni wapi angeanzia kwani alimuelewa Ngesa harakati zake kama komandoo.

“Sijui,nitaanzia wapi?”

Daphine,alitafakari.Hakuelewa ni njia gani aitumie ili awatoke askari wanaomlinda hospitalini hapo.


*****

Siku zote,Jogoo hafi kwa utitiri!Ngesa alitafutwa na kusakwa karibia na nchi nzima.Serikali ilichachamaa kumsaka na ilikuwa ni lazima wamtie katika vyombo vya dora,kazi hiyo inaonekana kuwa ngumu mno tena ya kutisha.Jeshi la polisi linaonekana kushindwa.Rais Leslie,anaamua kuunda kikosi kingine cha siri kutoka Ikulu ili operesheni hiyo ikamilike.Kitu Kilichomshangaza zaidi ni baada ya kungudua ya kwamba DK yupo bega kwa bega na Ngesa.

Kichwa chake kinazidi kuvurugika vilevile, baada ya kusikia Ngesa hajapatikana uwanja wa ndege,hiyo ilifanya amfokee Mkuu wa Majeshi kama mtoto mdogo!

“Itawezekana vipi?Kama huwezi acha kazi.Nakupa masaa ishirini na manne,Ngesa apatikane.Umenielewa?”

Rais Leslie,alifoka siku hiyo simuni.Jasho la pua lilikuwa linamtoka,macho yake mekundu kama mtu aliyetoka kuvuta cha ukucha.Bado hakutaka kuamini kwamba mtu mmoja, angelitoka jeshi la polisi.

“Sawa mk…”

“Usipomtia Ngesa mikononi mwako,nakuweka ndani.Umenisikia?”

“Ndio Mheshimiwa”

Rais Leslie,alizungumza kwa kumaanisha na maneno hayo yalikuwa ni mazito kutamkwa na Rais wa nchi.Tafsiri yake ilikuwa ni kitisho,hiyo ilifanya Mkuu wa jeshi la polisi,achanganyikiwe na kuhanya.Ulinzi na boda zote zikafungwa,magari yakawa hayapiti bila kukaguliwa.Raisi Leslie,hakuishia hapo!Simu yake ikaruka mpaka makao makuu usalama wa taifa,kitengo maalum ili kujua ripoti ya Dustan ilipofikia,niya yake alitaka kujua ni wapi Ngesa anakwenda.Kupitia DK aliamini wangepata mwanga na sehemu ya kuanzia.

“Hongereni kwa kazi nzuri Mr.Isaya Msophe”

Rais akatoa pongezi,kwa vijana wake wa kazi kutokana na kazi nzuri waliotoka kuifanya.

“Ahsante mtukufu”

“Amesema ni wapi Ngesa alipo?”

“Hapana bado,lakini atasema tu”

“Hilo naliamini.Fanyeni mnavyojua”

“Ahsante kwa ruksa hiyo”

Kwa Rais Leslie, kutamka maneno hayo ilikuwa ni sawa na chizi kupewa rungu kwani DK, alikuwa mbele yake,amekalishwa juu ya kiti.Mikono yake imefungwa kwa nyuma.Pembeni yake kuna kila aina ya silaha za kutisha,hususani za ncha kali.Dk alitetemeka kwa kiasi cha kutosha,akabaki anamtizama Mr.Isaya Msophe, aliyekuwa mbele yake,yupo siriaz.

Ndani ya chumba hicho kulikuwa na mwanga kwa mbali uliosababishwa na taa moja iliyokuwa juu,pembeni kulikuwa na kitanda cha chuma.Dustan alijua sana chumba hiko kina maana gani.Akili yake ikarudi nyuma kwa kasi ya mwewe akamkumbuka,jambazi mmoja aliyewahi kulitingisha jiji la Dar es salaam miaka ya nyuma, lakini alivyoingizwa ndani ya chumba hiko,alisema kila kitu.Kifupi chumba hiko kilikuwa ni Jehanam ndogo!

“DK,nisingependa tufike mbali.Nachotaka kujua,Ngesa yuko wapi na ana mpango gani?Tuokoe muda”

Mr.Isaya Msophe aliuliza huku akivua koti lake la suti,akaliweka pembeni na kulegeza tai yake kohoni,baada ya hapo akakunja mikono ya shati.Hiyo ilimaanisha jambo analotaka kulifanya litakuwa zito.

“Tushajua tayari,unashirikiana na Ngesa.Mkanda tumeuona!Tunachohitaji tu ni ushirikiano wako alafu baadaye,tutajadili swala la wewe kuepuka kifungo cha miaka thelathini jela.Nisaidie,nikusaidie.TUSAIDIANE”

Mr.Isaya Msophe alizungumza huku akimtizama DK usoni,akamsogelea mpaka karibu kabisa.

“Kukaa kwako kimya,hakuwezi kukuweka wewe huru.Ngesa yuko wapi?”

“Sijui alipo”

“DK,sitaki tufike unapotaka”

“Sijui Ngesa alipo”

“Mara ya mwisho alisema anaenda wapi?”

“Nimekwambia sijui”

“Una uhakika?”

“Ndio”

“Nina familia yako kumbuka”

Hapo Dustan,akabana meno kwa hasira na kumuangalia kwa macho makali mwanamme huyu aliyekuwa mbele yake,anamuuliza maswali ya kiwaki.

“Familia yangu,ikidhurika.Utanitambua”

“Ha! Haa! Haaa! Haaaaa!You are not on a right position to make any threat!”(Haupo sehemu sahihi kuleta vitisho)

Mr.Isaya Msophe,akazungumza maneno ya nyodo.Akiamini kwamba Dustan hana nguvu yoyote ya kupiga mkwara,akazunguka nyuma ya DK na kumsogelea masikioni.

“Mkeo ni mzuri sana!Nataka ushuhudie mbele ya macho yako!Nitakachoenda kumfanya!Sitaki aingie kwenye matatizo,Ngesa yuko wapi?”

“Naomba familia yangu isihusishwe kwenye hili”

“Hata mimi nisingependa kuihusisha,jambo hilo lipo mikononi mwako”

“Nitakwambia ni wapi Ngesa alipo.Naomba unihakikishie usalama wa familia yangu”

“There you go,Ngesa yuko wapi?”

Mr.Isaya Msophe,alizungumza kwa dharau.Staili aliyotumia kuongea ilionesha picha hiyo,kwani mdomo alikuwa anaupindua huku anamtizama Dustan kama mtu anayeangalia kinyesi.

“DK,talk to me”

Dustan akashusha pumzi ndefu kidogo,akamtizama Mr.Msophe kwa kitambo kidogo.

“Hakuniambia anaenda wapi,aliniambia anasafiri”

“Sio kweli”

“Ukweli gani unataka sasa?”

“Nataka kujua Ngesa kaenda wapi,tiketi aliyokata ilionesha anaenda Arusha.Alikuwa anataka kwenda kufanya nini huko?Na ana mipango gani?”

“Hilo swali,ungemuuliza Ngesa mwenyewe”

“Shenziii…Subiri,naona unadhani nacheza hapa”

Mr.Isaya Msophe alizungumza kwa hasira za waziwazi,akatembea mpaka karibu na meza kubwa ambayo juu ilikuwa na vichuma viwili,vilivyokuwa vina waya mrefu.Dk alivyoangalia vizuri akaogopa kwani alijua nini maana ya kazi ya vitu hivyo,alivitambua fika baada ya sekunde mbili, atakuwa katika mateso mazito ya kupigwa na shoti ya umeme.

Ni kweli,alikuwa sahihi kabisa!Kwani Mr.Isaya Msophe alimsogelea karibu na kulichana shati lake,kifua cha Dk kikawa wazi.Vidude kama vibanio vya nguo viwili vikasogezwa karibu,vikabanwa juu ya chuchu zake.

“Ngesa yuko wapi?”

Kabla ya kuwasha umeme,ili shoti ipige Mr. msophe akauliza swali hilo kwa mara nyingine.

“Sijui”

DK akajibu,hilo lilikuwa jibu tosha kwamba,zoezi hilo la kumpiga shoti lianze mara moja!Na hicho ndicho kilichotokea,hapohapo umeme ukawashwa.Ilikuwa ni kama mtu mwenye homa ya usiku,DK alikuwa akitetemeshwa na shoti,akahisi kila kitu kinamuuma,akahisi kama damu yake imeacha kutembea,maumivu aliyohisi hayakuwa ya kawaida.

“Ngesa yuko wapi?”

Swali hilo likarudiwa tena,lakini jibu la Dustan liliendelea kuwa lile lile,shoti ikaendelea kufanya kazi yake.

“Dustan,Ngesa yuko wapi?”

Sio kwamba hakujua ni wapi Ngesa alipo,kwa kusema ni wapi Ngesa alipo kulimaanisha operesheni yake kukwama.Kukamatwa kwa Ngesa kungepelekea hata yeye kufungwa jela,alikuwa yupo tayari kuteswa lakini asiseme ni wapi, Ngesa alipo.

“Si..wezi kukwambi..a alipo”

Hatimaye akasema maneno hayo,hiyo ilimaanisha mateso yaendelee kama Mbwai iwe mbwai.Mateso hayakukoma,lakini Dk hakuwa tayari kufungua kinywa chake, kuzungumza chochote kile.

“Dustan,naomba nikuhakikishie!Leo utaongea ukweli!Hakuna mtu yoyote yule aliyewahi kubaki na siri akiwa ndani ya hiki chumba!Amini hilo”Mr.Isaya alizungumza kwa kujiamini,akatembea karibu na meza iliyokuwa na vyuma vingi,akawa kama mtu anayetafuta kitu.Baada ya kuona koleo,akachukua.

“Nakutoa jino moja baada ya jingine,kisha baadaye natoa kucha zako.Utasema tu”

Kitu hiko kilikuwa mbioni kufanyika kama Dk asingeonyesha ushirikiano,Mr.Msophe akamsogelea mpaka karibu akiwa anahema kwa hasira,akaushika mdomo wa Dk na kuupanua vizuri,akaingiza koleo ndani ya mdomo na kubana jino moja la Dustan la juu!Hapo ndipo Dk akahisi kama mkojo unataka kumpenya,kabla ya kutolewa jino alianza kutafakari maumivu atakayohisi, tena mbaya zaidi alikuwa anaenda kutolewa meno bila ganzi,jino la Dustan likabanwa vizuri ili litolewe.

“Griii griiii”

Mlio wa simu kutoka juu ya meza ulifanya Mr.Isaya Msophe asitishe zoezi lake la kinyama,akageuka na kuangalia mezani.Ni simu ya DK ndiyo ilikuwa inaita kwa wakati huo,alivyoangalia vizuri ilikuwa ni namba inayoanzia na +254 kumaanisha, haikuwa ya Tanzania,usajili huo ulikuwa ni nchini Kenya.

Mr.Isaya Msophe akaiangalia vizuri kwa umakini,akaichukua na kuipokea.Akaiweka sikioni.

“Dustan,unaongea na Ngesa!Nipo Kenya tayari.Tunafanyaje sasa?Nipe muongozo”

Sauti hiyo ilisikika kutokea upande wa pili,ikamfanya Mr.Isaya Msophe apigwe na butwaa, alikuwa ni Ngesa anazungumza simuni,hapo ndipo alipogundua mhalifu huyo yupo nchini Kenya.

Bado alikuwa ana maswali yasiyopungua mia moja ya kujiuliza.Ilikuwaje Ngesa ameingia nchini kenya?Tena bila kugundulika?Amepitia wapi?Hayo ndiyo maswali yaliyokuwa yanapita ndani ya ubongo wake kwani jeshi la polisi lilikuwa limetanda mipaka yote, kumaanisha kwamba kusingekuwa na njia yoyote ile ya Ngesa kutoka nchini Tanzania.Ili kuepuka kugundulika,akakata simu na kutoka nje ya kichumba hiko cha mateso!Simu kutoka kwa Ngesa ilifanya zoezi hilo la kumtoa meno,lisitishwe.

“Ngesa kapiga yupo nchini Kenya,nahitaji kujua ni wapi alipo.Sasa hivi”

“Sawa mkuu”

“Sawa mkuu”

Hilo halikuwa na mjadala wowote ule,namba ikaandikwa pembeni kilichokuwa kinasubiriwa ni Ngesa apige kutoka Nchini Kenya.Ni kweli sekunde moja baadaye,simu ikaanza kuita.Wakajaribu kufanya wanavyojua lakini zoezi hilo likaonekana kuwa gumu.

“Mkuu,hatuwezi.Mnara huo upo nje ya Tanzania.Hatuwezi kusoma frequency”

“Kweli?”

“Ndio”

“Mleteni Jesca na watoto hapa,fanyeni haraka”

Kauli hiyo ilivyotoka Jesca pamoja na watoto wa Dustan,wakatolewa ndani ya chumba maalum, walichowekwa na kupelekwa mpaka Kwa Mr.Isaya Msophe!

“Twendeni huku”

Hakukuwa na muda wa kubembelezana kwa wakati huo,kilichokuwa kinatumika ni amri sio ombi.

Ndiyo maana Jesca akawa ameshikwa mkono anatembezwa kwa kasi, mpaka walipofika nje ya mlango,ukafunguliwa.Mbele alikuwa amekaa Dustan,kilichosikika hapo kilikuwa ni kilio kutoka kwa Jesca.Hapohapo Mr,Isaya Msophe akachomoa bastola kutoka kiunoni.Akamuwekea Jesca kichwani.

“Uhai wa mkeo,upo mikononi mwako mwenyewe”

Hakukuwa na punje ya masihara kutoka kwa Mr.Msophe, kulikuwa kuna kila dalili ya Jesca kufyatuliwa risasi ili mradi Ngesa apatikane na alijua kwa kufanya hivyo,asingepewa kesi yoyote ile.

“Ngesa,amekupigia yupo Kenya.Piga hii simu muulize yupo sehemu gani na mnataka kuonana,kumbuka.Ukienda kinyume,sitoshindwa kuusambaratisha ubongo wa mkeo hapahapa una shuhudia”

Yalikuwa ni maneno mazito tena ya kutisha kwa binadamu wa kitanzania kuyatamka hadharani,simu ikawekwa mezani tena loudspika ili isikike kwa kila mtu.Ni kweli ilianza kuita lakini haikupokelewa,ikaita tena lakini wapi.Ilivyokatika,baada ya dakika mbili kupita, simu ya Dustan ikaanza kuita sasa,ilikuwa ni namba ya Kenya lakini namba zilikuwa tofauti na zilizopiga mwanzo.

Kama kawaida Mr.Isaya Msophe alipokea na kukaa kimya,safari hiyo hata upande wa pili wa simu,ulikuwa kimya pia.Ilielekea kila mtu alikuwa akimsikilizia mwenzake aanze kuongea ama kusema ‘Hallo’

“Hallooo”

Mr.Msophe akawa wa kwanza kuzungumza, hapohapo simu ikakatwa!Picha iliyomjia harakaharaka ni kwamba Ngesa,ameshajua mchezo tayari.Hapo ndipo alipohisi kuchanganyikiwa!

“Ngesa yuko wapi?”

Hasira zake zikaanza kumpanda upya,akamuwekea bastola Jesca Kichwani na kumuangalia Dustan ili aseme ni wapi Ngesa alipo.

“Moja,Ngesa yuko wapi?Mbili Ngesa yuko wapi?Tatu kachakacha”

Mr.Isaya Msophe hakuwa ana masihara,akakoki bastola na kumuwekea Jesca kichwani kwa niya ya kumfyatua lakini kabla ya kufanya hivyo akasikia kama kuna kimpira kimedunda na kuingia ndani na chumba hiko,alivyoangalia vizuri,kikaanza kutoa moshi mzito.

Akahisi kama macho yake yanawasha,alivyoanza kuyafikicha akashtukia mlango umefungulia,hakukaa sawa akapigwa teke la kifua kali sana akadondoka chali kama gunia.

“Dustan,tuondoke”

Sauti hiyo ya kike,ilimfanya Dustan ashindwe kumuona mtu huyo vizuri kutokana na moshi huo uliokuwa unamumiza pua na macho!Hapohapo akavalishwa kidude maalum puani,mwanamke huyo akatoka na kuwavalisha Jesca pamoja na watoto wawili,akamsogelea Dustan na kumfungua kamba alizokuwa amefungwa mikononi!

“Wewe nani?”

Dustan,akauliza akitaka kujua ni nani amefanya ukombozi huo wa kijasusi.Mwanamke huyo akatoa 'mask' usoni!Sura hiyo ilimfanya Dustan apigwe na bumbuazi,alikuwa ni mwanamke huyu jasiri,DAPHINE.


 Ndege ndogo ya kitalii aina ya 5H-TZT,ipo angani.Rubani ametekwa nyara,mdomo wa bastola upo kichwani kwake.Kwenda kinyume na taratibu zote, ilimaanisha kifo chake.Kwa kifupi, maisha yake yalikuwa mikononi mwake mwenyewe,hiyo ilifanya atetemeke kwa uwoga na kumsikiliza Ngesa, anayetoa amri.Hakuwa na chaguo lingine zaidi ya kutii kila kitu kinachosemwa.

“Bado masaa mangapi tufike?”

Ngesa akauliza,wakati huo alikuwa amevaa mitambo maalum masikioni ili waongee vizuri, wasikilizane kiufasahaa na rubani,hakutofautishwa na DJ wa club ya billcanaz.Baada ya swali hilo akaangalia chini, ambapo hakuweza kuona vitu vizuri kutokana na kuwa angani.

“Dakika hamsini,tutakuwa Kenya”

“Tunaweza tukatua wapi?”

“Nairobi”

“Hapana”

“Hatuna chaguo lingine”

Hapo Ngesa alimuangalia rubani kwa kama sekunde mbili nzima,akiwa anatafakari ni kitu gani akifanye.

Akaangalia nyuma ya siti kwa juu,akaona mabegi mengi,akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya umeme, akavuta begi moja wapo na kulishika vizuri.Lilikuwa ni begi kubwa kiasi,nyuma kwa juu lina zipu na kwa pembeni lina kamba mbili.Begi hilo alilijua sana kazi yake,kwa kitalaamu begi hilo huitwa parashuti.Aliamini litamsaidia mbele ya safari,hakutaka hata kidogo kufikia jiji la Nairobi,kwa kufanya hivyo aliamini huo ndiyo ungekuwa mwisho wake sababu alielewa ukaribu wa Tanzania na nchini Kenya,taarifa zake kufika nchini humo ingekuwa rahisi sana!

“Tunakaribia kuingia Kenya”

Rubani,alimwambia Ngesa!

“Sawa,sogea mpaka kwenye ule msitu pale!”

Ngesa akasema huku akionesha kidole,hiyo ilikuwa rahisi sababu kila kitu walikiona kwa chini.Rubani akajua ni kitu gani anataka kukifanya Ngesa, ndiyo maana akaanza kubonyeza mitambo,ilikuwa mara ashike hiki mara abonyeze kile.Ndege ikaanza kuelekea kwa chini,walivyokaribia na msitu. Ngesa akaanza kuvaa begi mgongoni kwa tahadhari,akaufunga mkanda maalum kiunoni mwake.

Akashika begi lake vizuri alilotoka nalo Tanzania,akamtizama rubani kwa macho makali.Alivyoyatupa macho yake pembeni kwa chini, akaona kiboxi kidogo, kando yake kuna nailoni ambapo ndani yake kulikuwa na fedha za kimarekani yaani dolla,akazichukuwa akiamini zingemsaidia mbele ya safari.Akatizama chini akaona kuna miti mingi mno!

“Sogeza ndege upande wa huku”

Akamuamuru rubani,ambapo hapo ndege ilianza kuelekea upande wa Magharibi,bila kujiuliza chochote Ngesa akafungua mlango na kujitupa nje.Mikono yake pamoja na miguu akiwa ameitanua huku na kule.Hapo akajibinua kiutaalam ,akajinyoosha kichwa kikiwa kimeelekea chini,sekunde moja baadaye akajipindua tena,miguu ikawa chini hapohapo akavuta kamba.Kitu mfano wa puto likafumuka,akaanza kuelea angani taratibu.

Mikono yake imeshika kamba huku na kule, ambayo ilikuwa kama usukani wa gari,kwani alikuwa akivuta Magharibi.Anahamia Magharibi, akiivuta upande wa Mashariki,anaenda Mashariki.Umakini wake ulikuwa ni mkubwa mno, kuangalia chini ili asiparamie miti,kazi yake ikawa ni kuvuta kamba.Mara upande huu mara upande ule ili akanyage ardhi vizuri akitua chini,alikuwa amebakisha umbali mdogo sana ili miguu yake ikanyage ardhi,akajiandaa vizuri kwa ajili ya kutua.Alivyoweka miguu yake chini akafyatua kichuma kilichokuwa kiunoni,kuna kichuma kikafumuka na kutoboa puto,hapo lilimshinda nguvu likamtupa na kuanza kumburuza,akabiringika na kutulia.Kwa mbali alihisi maumivu sababu alitua vibaya,hapo hakutaka kukaa sana.Akajizoazoa na kuanza kujipukuta michanga.Ki ukweli,hakuweza kujua ni wapi alipo.Mbele yake kulikuwa na miti mirefu inayotisha,hakuwa ana uhakika kama ndani ya msitu huo kuna wanyama wakali ama laa!Uwoga alikuwa nao lakini ilikuwa ni lazima asonge mbele.Akatembea akiwa na begi lake mgongoni,umbali wa kama mita kumi akasimama na kulitoa begi,kuna kitu alikuwa anakitafuta.Baada ya kupekua pekua akakumbana na karatasi iliyokuwa na namba za Dustan, alizopewa ili wawasiliane akiwasili, nchini Kenya.

“Cha kufanya ni kutafuta,barabara ya lami”

Ngesa aliwaza na kuanza kusonga mbele,akikatiza katikati ya miti ambapo huko alianza, kusikia sauti za wanyama pori kama ngedere,mbwa mwitu,mbweha na ndege!Akaanza kukimbia taratibu na kuruka magogo pamoja na miti,akatokeza katikati ya miti mingi,ambapo mbele kulikuwa na miiba.Hapo alianza kutembea kwa tahadhari ili asipate madhara yoyote yale.Hilo likafanikiwa,akazidi kusonga mbele zaidi.Ulikuwa ni umbali wa kama kilomita tatu hivi,ndipo alipotokea kwenye uwazi ambapo mbele aliona kijumba kidogo,kilichokuwa na nyasi juu yake.Kwa haraka nyumba hiyo haikuwa na mtu ama watu waliokuwa wanaishi walihama kwa kipindi kirefu,kwani pembeni yake kulikuwa na majani mengi ya kijani,akatizama huku na kule na kutembea kwa tahadhari kubwa.

Akachomoa bastola yake kutoka kiunoni na kuiweka vizuri mkononi mwake ili kujihami na lolote lile litakalotokea,akatembea mpaka kwenye upande wa mlango ambapo kulikuwa na ukimya wa ajabu,kilichosikika kwa wakati huo ni sauti za wanyama pori bado,akasukuma mlango huo.Moyo wake ukapiga paa na alimanusura akimbie, kutokana na ndege waliokuwa ndani ya kijumba hiko kuanza kuruka huku na kule wengine walimpitia karibu kabisa na uso wake,hiyo ilimfanya arudi nyuma na kuzama tena ndani.

Ndani kulikuwa na mzoga wa nyama.Akashusha pumzi baada ya kugundua chanzo cha ndege hao kuwa wengi,akaweka bastola kiunoni,kitendo cha kupiga hatua moja,alishtukia amepigwa kabali ya shingo ya nguvu kabisa.Wasiwasi ukaanza kumuingia,sababu hakujua ni nani amefanya hivyo.Kwa nguvu za ajabu,akajisukumiza kwa nyuma kwa kasi sana, hiyo ilifanya mtu aliyekuwa nyuma yake,ajigonge kwenye ukuta.Hakuchelewa, kwa kasi ya umeme,akaushika mkono wake kiutaalam,akainama kidogo na kumtupa kwa mbele.Alivyotulia kidogo na kumtizama,akagundua alikuwa ni mwanamme mrefu,mweusi sana! Akakunja ngumi ili kujihami na mtanange huo kwani hakujua jamaa huyo kajipanga vipi.

“Terali aikoree”

Maneno hayo yalimtoka jamaa huyo akizungumza kilugha ambacho Ngesa alishindwa kukielewa,kufumba na kufumbua Ngesa akasombwa na bega, wote wakadondoka mpaka chini.Jamaa akawa anatupa ngumi nyinginyingi zisizokuwa na idadi kamili,nyingine hazikuzaa matunda lakini baadhi zilimfikia Ngesa usoni,akaona isiwe tabu, akaanza kupapasa kiunoni ili achomoe bastola yake.Jambo hilo likaonekana kuwa gumu kwani mtu huyo aliuona mkono wa Ngesa,akamzuia. Vuta n’kuvute ikaanzia hapo.Katika purukushani, bastola ikawa imedondoka kando,jamaa huyo mweusi ambaye hakueleweka ni nani akachomoka kwa kasi ya mkuki mpaka kwenye moja ya pembe,akachomoa sime refu.Bastola ya Ngesa ilikuwa imedondoka umbali kidogo,isingewezekana hata kidogo kwa Ngesa kusimama na kuifikia kabla ya mtu huyo kumvaa na Sime yake.Hapo ilibidi afikirie mara mbili zaidi,akajivuta na mgongo akiwa chini na kusimama huku akimtizama jamaa huyo kwa makini,mkononi akiwa na sime.Alielewa sana kitendo cha kufanya makosa,angekufa kifo cha kinyama cha kukatwa katwa na sime hiyo yenye makali.Hivyo ilibidi awe makini ili kutetea uhai wake.

“Aratiiiii diderii”

Jamaa huyo alipiga kelele na kuchomoka kwa kasi akiwa ameshika sime vizuri ili kwenda kumchoma nayo Ngesa tumboni,ilikuwa ni kosa kubwa sana kuingia kichwa kichwa,kwani Ngesa alimkwepa kidogo, Sime ikapitiliza,hapohapo akarusha teke lililomfikia mbavuni,hakutaka kufanya makosa.Akamvuta kwa nguvu na kuushika mkono huo wenye sime,akaupigiza ukutani.Sime ikadondoka.Akamgeuza na kumtwanga kichwa cha pua,akazunguka kwa nyuma yake na kumpiga roba kali.Hapo ndipo jamaa huyo taratibu alipoanza kuishiwa nguvu huku akitapatapa kutafuta pumzi,akijaribu kukukuruka ili kujitoa mikononi mwa Ngesa lakini swala hilo likawa gumu mno.Ngesa alivyohakikisha jamaa huyo kalegea,hapohapo akamvunja Shingo.

“Kaaaaa”

Ni sauti ya mishipa ya shingo, iliyosikika baada ya Ngesa kufanya unyama huo,jitu hilo likadondoka chini kama embe dodo mtini,tayari mwisho wa maisha yake ulikuwa siku hiyo.

Alichofanya Ngesa ni kusogea mpaka ilipokuwa silaha yake,akaiokota na kuiweka kiunoni.Akaisogelea maiti na kuanza kuikagua mifukoni, ambapo humo alikuta vitu ambavyo vingemsaidia mbele ya safari,akaingiza mkono ndani ya mfuko mwingine na kukuta simu pamoja na fedha za kikenya.Vyote akaviweka mfukoni kwake,akachukuwa begi lake na kulivaa mgongoni,hapohapo akaanza safari yake ya kusonga mbele akikatiza katikati ya miti.

Umbali wa kama kilomita tano,akaanza kusikia muungurumo wa magari.Nguvu mpya ikamjia,akajua hapo angepata ukombozi mpya na msaada walau wa gari, ambalo lingemfikisha mjini ingawa hakujuwa ni wapi alipo.Akazidi kusonga mbele huku akiwa na mawazo mengi sana kichwani kwake,kila kitu kilichokuwa kinatokea katika maisha yake kilikuwa ni kama sinema ya kuigiza.Hata siku moja hakudhani kama angejikuta yupo katika matatizo mazito kama hayo.Mbaya zaidi ni namna ambavyo, alivyokuwa akitafutwa na nchi nzima kama gaidi,jina lake lilichafuliwa kiasi kwamba alianza kujichukia mwenyewe.Hata hivyo aliamini ya kwamba kila kitu kina mwisho,kama aliamua kuianza vita hiyo, ilikuwa ni lazima aimalize.Alitafakari vitu vingi sana siku hiyo,akamkumbuka Mpenzi wake Jaqlin Mfinanga.Roho ilimuuma ajabu sababu alijua kivyovyote vile atakuwa ameshikiliwa na jeshi la polisi lakini kimoyomoyo aliapia ni lazima akamkomboe kisha akamuhifadhi sehemu salama, mpaka vita hiyo nzito itakapoisha.Ngesa hakuwa anapambana na jeshi la polisi bali na serikali yake ya Tanzania,ndiyo maana alihofia kwa kiasi cha kutosha,alisimama kidogo baada ya kuona lami mbele yake.

Hakuwa mwenye uhakika kama atapata usafiri kwa haraka kwani tangu aanze kusikia muungurumo wa magari kupita, yalikuwa yanahesabika, yaani ndani ya dakika tano linapita gari moja tu.Hakutaka kujitokeza barabarani.Alivyosubiri kwa kama dakika mbili nyingine, ndipo aliposikia muungurumo wa gari,akaanza kutembea kuelekea kwenye lami na kusimama kandokando yake,lilikuwa ni gari aina ya landrover,akalipungia mkono lakini halikusimama.Lilimpita,gari la pili likawa hivyohivyo.Akakata tamaa na kuanza kutembea akiifuata lami akiamini kivyovyote vile,magari yanapoelekea huko ndipo mjini.Baada ya kupiga hatua kama thelathini akahisi muungurumo wa gari nyuma yake,hapo ndipo akasimama na kugeuka nyuma ili kujaribu tena bahati kwa mara nyingine.


******

“Tupitie Namanga,nikifika Arusha nitajua cha kufanya”

“Sawa Mkuu,lakini tutapita vipi pale Namanga?Kuna upekuzi”

“Tutapita tu.Lakini ninyi,mtatangulia.Mimi nitawakuta upande wa pili”

“Sawa mkuu”

“Kuna mtu nitazungumza naye pale,atanivusha bila kugundulika.Nikifika upande wa pili,tutawasiliana”

“Hakuna shaka.Na hizi mali?”

“Kwanza tutaanza kujaribia pale pale Arusha”

“Sawa mkuu”

“Naomba uzembe wa aina yoyote ile,usitokee.Ni lazima Leslie,anijue mimi ni nani”

Maongezi hayo yalifanyika ndani ya gari aina ya Nissan Patrol,ndani yake lilibeba watu watano walioshiba,akiwemo Brigedia Karanje.Maongezi yaliyokuwa yakifanyika ndani ya gari hilo,yalitisha kuliko kawaida,mwendokasi wa gari hilo uliogopesha kupita kiasi.Kilichomfanya dereva alikimbize gari ni baada ya tairi kupata pancha zaidi ya mara mbili,alifanya hivyo ili kufidia muda waliopoteza njiani, kubadilisha matairi.Ilikuwa ni lazima waingie nchini Tanzania ndani ya masaa matano yajayo.

“Kibo,nyoosha goti”

Brigedia Karanje,akaamuru.Japokuwa gari lilikuwa linakimbia mwendo wa kilomita kumi kwa dakika lakini Brigedia Karanje aliona haitoshi,ndiyo maana akamwambia dereva aongeze mwendo.Walipokuwa wanapita ilikuwa ni katikati ya msitu yaani pembeni yao kulikuwa na miti mingi na mikubwa,hilo hawakujali walizidi kusonga mbele kwa kasi kubwa.

“Mmmmmh!”

Dereva aliguna ikafanya kila mtu aangalie mbele.Kuna kitu kiliwashangaza,hiyo ni baada ya kumuona Mzee mwenye ndevu nyingi anawapungia ili wasimamishe gari.

“Huyo mzee anataka nini?”

Brigedia Karanje,akauliza huku akiyatumbua macho yake mbele akimuangalia mzee huyo, anayepunga mkono.

“Sijui mkuu,itakuwa anataka msaada”

“Katokea wapi sasa hivi?”

Ni swali ambalo hata mmoja wao asingeweza kulijibu lakini kwakuwa alikuwa ni mkuu wao wa kazi,ilikuwa ni lazima watoe jibu.

“Litakuwa labda basi limemuacha”

“Achana naye, tuwahi”

Dereva alivyosikia kauli hiyo,akapandisha gia nyingine. Gari likazidi kusonga mbele zaidi,wakampita mzee huyo aliyekuwa kandokando.Lakini walivyofika mbele mita kumi,Brigedia Karanje akabadilisha mawazo!

“Twende,tukamchukuwe.Tumsogeze hapo mbele”

Hakukuwa na mtu yoyote yule aliyepinga amri hiyo.Gari likasimamishwa,likaanza kurudi kinyumenyume.


******

Gari aina ya Nissan Patrol,ndilo lilikuwa linakuja kutokea upande wa Mashariki kuelekea Magharibi kwa kasi ya ajabu.Ngesa akapunga mkono ili kujaribu bahati yake,lakini gari likampita.Akakata tamaa,lakini cha ajabu gari hilo lilivyofika mbele.Akaliona linaanza kurudi nyuma, akajua tayari amepata msaada,likaendelea kurudi kinyume nyume mpaka lilivyofika miguuni kwake.


 Hakuna kilichosikika zaidi ya muungurumo wa gari,lililokuwa kandokando ya miguu ya Ngesa.Kioo cha mbele kikawa kinashuka taratibu,sura ya mwanaume mweusi wa miraba minne ikaonekana nyuma ya usukani.

“Habari yako mzee?”

Salamu hiyo ilimfanya Ngesa,atulie kidogo na kutafakari kwa sekunde moja.Akagundua kwamba alikuwa ana ndevu za bandia, ndiyo maana akaitwa Mzee,hivyo ilikuwa ni lazima ajiongeze ili asigundulike.

“Mmmh! Mmh!”

Akaguna kwa sauti ya kizee huku akiweka mkono mdomoni.

“Salama kijana.Niwieni radhii kwa kuwasimamisha.Nahitaji msaada wa lifti”

“Unaelekea wapi?”

“Hapo mbele,mkinifikisha mjini.Itapendeza zaidi”

“Panda twende”

Kama ingekuwa ni sinema ya kuigiza bongo movie wasingemuacha Ngesa,kila kitu alikifanya kimagumashi.Hakuwa mzee,lakini aliigiza mpaka sauti. Mbaya zaidi, alivyoanza kutembea ndiyo kabisa.Hiyo ilifanya mpaka Mwanajeshi mmoja ateremke ndani ya gari na kumfungulia mlango,baada ya kuona mwendo wa kizee huyo.

Ngesa alijipinda kidogo,akawa anatembea kwa mwendo wa taratibu,mlango ulivyofunguliwa aliingia ndani, ambapo alikumbana na sura za wanaume watatu,wawili sura zao zilikuwa wazi lakini mmoja wao alivaa kofia kubwa na miwani nyeusi ya jua.Hakuweza kuiona sura yake kiurahisi.Ndani ya gari hakukuwa na maongezi yoyote na hakuna hata mmoja wao aliyemsalimu.Mlango ulivyofungwa gari ikapigwa gia,safari ikaanza mara moja.Brigedia Karanje,alikuwa mwisho kabisa dirishani,amevaa kofia kubwa kichwani na miwani ili kuficha sura,aliogopa kugundulika sababu alijua kivyovyote vile anasakwa kama Saddam Hussein,ndiyo maana akaamua kubadili muonekano wake,hakuelewa ndani ya gari hilo amempakia Ngesa akidhani ni mzee,hata hivyo hakuwa na muda wa kumuhoji maswali,akiamini mzee huyo hamuhusu.Alichotaka yeye ni kuwasili nchini Tanzania ili aanze ‘ambush’.

Kichwani kwa Ngesa kulipita vitu vingi,alianza kutafakari namna atakavyomuweka Brigedia Karanje kwenye himaya yake,hakuelewa ni kitu gani amfanye sababu ni muda mwingi sana alikuwa akimuwinda bila mafanikio yoyote yale,kwa mujibu wa taarifa alizozipata ni kwamba gaidi huyo, yupo nchini humo Kenya, ndiyo maana alifunga safari ili kumsaka.Hakuelewa kwamba kushoto kwake ameketi na Brigedia Karanje.

“Mzee tunakarabia kufika,jiandae”

Sauti hiyo ilitoka kwa dereva na alizungumza akimtaarifu Ngesa.Ni kweli baada ya dakika tano kupita,wakawa wameingia mjini Isiolo,kulikuwa na makazi ya watu, sambamba na biashara ndogo ndogo,hapo ndipo walipoona ni sahihi kumshusha Ngesa ambaye walidhani ni mzee,kifupi kama Ngesa angemtambua Brigedia Karanje,siku hiyo pasingetosha alkadhalika kwa Brigedia Karanje iwapo angegundua kama aliyempakia ni Ngesa gari lingekuwa dogo,asingetoka mtu.

“Vijana,mbarikiwe sana”

Ngesa alizungumza kwa sauti yake ya kukwaruza ya kizee huku akijifanya anapata shida kuteremka ndani ya gari,alivyokanyaga chini akafunga mlango na kuendelea kutoa shukrani.

Gari likaondoka likimuacha analisindikiza kwa macho,hapohapo bila kupoteza wakati akaweka begi lake vizuri mgongoni na kuvuka upande wa pili,akasogea mpaka kwenye kibanda kidogo,akasimama na kutoa simu mfukoni ambayo aliichukua mfukoni mwa maiti ya mtu aliyemuuwa porini,akatoa karatasi ambayo ilikuwa na nambari za Dustan.Akaweka simu sikioni!

“Dustan,unaongea na Ngesa!Nipo Kenya tayari.Tunafanyaje sasa?Nipe muongozo,”baada ya kuzungumza maneno hayo simu ilivyopokelewa,akasubiri Dustan amjibu ili ajue ni wapi aanzie,katika hali ya kushangaza tena bila kujibiwa simu ikakatika,akaguna na kutulia kwa kama sekunde mbili hivi akitafakari kitu.

Jambo alilokumbuka ni kwamba alimuacha Dustan uwanja wa ndege Mwalimu Nyerere, baada ya kugundulika na Jenipha,hivyo hakuelewa kama huko alipo yupo huru ama chini ya ulinzi.Hivyo kwake, ilikuwa ni lazima atumie akili ya ziada.Alivyoangalia mbele yake umbali wa mita kumi,akaona kuna huduma ya kupigisha simu,akatembea mpaka eneo hilo na kumpa kikaratasi chenye namba msichana aliyekuwa ndani ya kijumba cha kupigisha simu,hapohapo zoezi la kupiga simu likaanza.Simu baada ya kupokelewa, ilikuwa hewani kwa kama sekunde tisa nzima lakini hakusikia sauti ya Dustan ikizungumza,taa nyekundu ikawaka kichwani kwake,akatoa simu sikioni na kuiangalia.Wakati mwingine alidhani wenda,mtandao sio mzuri.Lakini alivyoitizama akaona mnara unasoma vizuri.Hapohapo, akakata na kujua moja kwa moja kuna tatizo kubwa limetokea na kivyovyote vile Dustan,yupo chini ya ulinzi.

Hapo ndipo alipochoka sababu hakuelewa ni wapi angeanzia,kwa kifupi alikuwa yupo kwenye giza nene, sasa hajui wapi apapase!


******

Kuendelea kubaki hospitali na kutafakari kila wakati,kusingemsaidia kitu chochote kile.Ilikuwa ni lazima afanye kweli la sivyo kusingekuwa na muujiza wowote ambao ungetokea na kumtoa,japokuwa hakuelewa ni wapi aanzie lakini akili yake siku zote, ilikuwa inachaji kama kompyuta.Sio siri historia ya Daphine tangu anasoma ilitingisha,alishawahi kuwa miongoni mwa wanafunzi walioongoza nchi ya Tanzania, hiyo ilimaanisha ‘Intelligence Quotient’(IQ) yake ina uwezo mkubwa sana kwenye kufikiria, ndiyo maana alivyomuona Nesi,yupo karibu yake akaanza kupiga kelele kama mgonjwa aliyepandwa na malaria kichwani,zaidi na hapo alianza kupigapiga vitu na kutupa tupa miguu.Nesi,alihisi kuchanganyikiwa hakuelewa ni kitu gani akifanye.

Hapohapo akainua mkonga wa simu na kumpigia daktari,hiko ndiko Daphine alikuwa anataka kitokee.Haikuchukuwa muda sana,dokta akiwa amevaa koti lake akawa ameingia ndani ya chumba alicholawza Daphine,akamkuta bado anapiga kelele za yowe.

“Nitoenii hapa sitakiiiii”

Daphine aliendelea kupiga yowe huku akirusha rusha miguu na kufanya fujo.

“Mchome sindano ya usingizi haraka sana ili atulie”

Hesabu zake zilikuwa zimefanya kazi kwani alitaka chupa hiyo ya dawa za usingizi.Nesi akachukua bomba la sindano pamoja na chupa ndogo ya dawa,akaivuta ikaingia ndani ya bomba.Akamtizama Daphine ambaye hakujua kwa wakati huo kichwani ana hesabu gani.

Kitendo cha Nesi kusogea karibu akiwa na sindano yake mkononi,akawa amebanwa mithili ya panya aliyenasa kwenye mtego kwani miguu ya Daphine ilipita shingoni kwake,hiyo ilifanya shingo yake ipinde,dalili za shingo yake kuvunjika zilikuwepo kama angejigusa na kuhangaika hivyo ilibidi atulie tuli.Ndani ya sekunde tatu,Daphine akawa ameshika sindano ya usingizi,akamchoma nayo nesi shingoni.Kitendo cha Dokta kufika mlangoni na kusikia mikiki hiyo,akageuza shingo lakini alikuwa tayari amechelewa kwani Daphine aliruka kama ngedere na kumkaba shingo.Sindano ya usingizi,ikamuhusu.Haikuchukuwa hata dakika moja,wodini kukawa kimya,sio nesi wala Dokta wote walikuwa hawajitambui kutokana na dawa hiyo kufanya kazi yake ipasavyo.


Daphine,akamuendea daktari na kumvua koti,akalivaa yeye.Kwa mbali alianza kusikia maumivu,hiyo ilitokana na vidonda alivyokuwa navyo mwilini ambavyo kwa wakati huo vilikuwa kidogo vina ahueni.Akanyata mpaka mlangoni na kuusukuma kidogo,akamuona mlinzi yupo mlangoni,ilikuwa kidogo aonekane.

“Hapa nitatokaje?”

Daphine akajiuliza huku akitafakari,hapohapo akapata wazo.Akagonga mlango kwa nguvu kama mara tatu hivi,hiyo ilifanya mlinzi,ashtuke akajua wenda anaitwa ama kuna kitu ndani ya wodi aliloambiwa alinde,akageuka na kuuendea mlango.Kitendo cha kusukuma mlango alikumbana na ngumi takatifu iliyomfikia puani,bila ya kutafakari alivutwa na kupigwa kifuti cha tumbo,alivyotaka kuchomoa bastola,akapokea ngumi tatu za mbavu za haraka,akakaa chini bila kupenda huku akiugulia maumivu kila mahali.Daphine,akachukuwa bastola,askari akageuka na kuwa mateka tayari.

“Ngesa yuko wapi?”

Daphine aliuliza huku akiwa ameshika bastola mkononi kamuwekea askari kichwani,kwenda kinyume naye kulimaanisha ubongo wake ungechenguliwa na risasi na kumwagika kama uji chini.

“Ha..ta sisi tunamtafuta”

“Kwanini?”

“Kamuu…wa Mh.George Kimpanga”

“Ilikuwaje?”

“Sijui”

“Lazima utakuwa umepata tetesi,ni wapi alipo?Au nitampata vipi, nani anaongoza hii operesheni?”

“Ni usalama wa taifa ndio walianza kumtafuta”

“Nataka jina”

“Jina sijui,afande Kapopo ndio anajua”

“Yuko wapi?”

“Sijui ali..”

Kabla ya afande kumalizia sentensi, akapigwa na kitako cha bastola mdomoni,mdomo wake ukachanika damu zikaanza kumtoka.

“Usinijibu hivyo.Nitampata vipi huyo Afande Kapopo?”

“Ni..na namba za..ke.Ninampigia”

“Sasa hivi”

Askari aliyekuwa zamu,hakuna siku aliyokuwa katika wakati mgumu kama hiyo.Tangu aanze kazi yake ya kulitumikia jeshi la polisi,hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuwekwa mateka.Yeye alikuwa akisikia stori mbalimbali na kuwacheka wenzake waliosema walishawahi kujikojolea,kisa kuwekwa chini ya ulinzi.

Siku hiyo kinyesi na Mkojo vilim-bana kwa pamoja,aliamini kabisa baada ya hapo kifo kinamsubiri mbeleni.

“La..kini usiniue da..da nagu”

“Mimi sio dada ako,piga simu”

Jambo hilo lakaanza kufanyika wakati huohuo,akiwa yupo chini ya ulinzi.Mlango wa bastola upo kichwani kwake,nusu dakika afande Kapopo akawa yupo kwenye laini.Baada ya kumsalimia,ilibidi aulize nani anaongoza operesheni ya kumsaka Ngesa!Maswali ya hapa na pale, yalifanya jina la Jenipha likatajwa.Jina hilo halikuwa ngeni masikioni mwa Daphine,alichotaka kujua kwa wakati huo ni wapi mwanamke huyo kutoka kitendo cha usalama wa taifa anaishi ama anapatikana kwa urahisi.

Data zote zikawa zimepatikana na anazo tayari,hivyo kilichofuata hapo ni yeye kuanza kufikiria namna ya kutoroka ndani ya hospitali hiyo bila kugundulika.Akamtizama afande aliyekuwa amepiga magoti anatetemeka kama mgonjwa mwenye kifafa,akarusha macho pembeni, akaona nguo yenye rangi ya kijani.Sare hizo zinakuwa ni maalumu kwa ajili ya wagonjwa mahututi,akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya mwewe,akampiga afande huyo na kitako na bastola kichwani.Akadondoka kama mzigo,damu zikawa zinamtoka kichwani,akachukua sindano ya usingizi na kumchoma nayo mkononi.

Akaziendea sare za wagonjwa mahututi, akachukuwa moja wapo na kumvalisha askari,akamuweka juu ya kiti chenye magurudumu kwa chini,alivyoangalia pembeni akashukuru Mungu baada ya kuona miwani nyeupe ya macho,akaiweka machoni.Alivyojiangalia kwenye kioo cha mlango,akagundua kwamba anafanana na madaktari wa hospitali hiyo akatupa bastola ndani ya ndoo ya taka,akasukuma mlango na kuanza kutoka na baiskeli yenye matairi yaani ‘wheel chair’,ambapo juu alikaa Afande akiwa na sare wanazovaa wagonjwa mahututi.

Hospitali hiyo ilikuwa na madakatri walioajiriwa sio chini ya hamsini, kwenye idara tofauti tofauti,hivyo ilikuwa kazi ngumu sana kutambuana wote kwa sura,hata hivyo kila mtu alikuwa bize na wagonjwa wake.

“Habari daktari”

Dokta mmoja,alimsalimu Daphine akijua ni mwenzake.

“Salama”

Daphine akaipokea salamu huku kichwa chair kikiwa chini,japokuwa hakupona vizuri majeraha yake, yaliyosababishwa na risasi lakini alijikaza kisabuni.Akasonga mbele na kusimama kidogo, baada ya kukaribia mapokezi.

Hapo asingeweza kutoka bila ya kusema anampeleka wapi mgonjwa,huo ndio ulikuwa utaratibu wa hospitali hiyo.Akavaa ujasiri na kuendelea kutembeza kibaiskeli hiko,mpaka mapokezi.

“Natoka na mgonjwa,kuna dharura”

Daphine alizungumza kwa sauti ya ujasiri hakuonesha uwoga hata kidogo,hiyo ilimfanya nesi aliyekuwa mapokezi.Amtizame kwa kitambo kidogo,ilielekea sura hiyo ilikuwa ngeni kwake,ndiyo maana akaanza kumdadisi.

“Naomba,transfer nisaini.Wewe ni dokta nani?”

“Mgonjwa amezidiwa,akifia hapa kwenye kiti.Utawajibika,ana hali mbaya.Unajua maana ya dharura?”

“Sio hivyo Dokta,mimi mwenyewe nimeajiriwa kama wewe.Nina protocol na utaratibu”

“Protocol gani?”

Ghafla,ukaibuka mzozo wa chini kwa chini,hakuna mtu aliyeropoka lakini walipandishiana kibezi.Daphine, alitaka kutoka lakini nesi alikuwa tayari ana mashaka kwani sura hiyo hakuwahi kuiona miaka yake yote tangu aajiriwe.

“Nesiiiii,Nesiii.Kuna mgonjwa njoeeeni”

Hiyo ilikuwa ni sauti ya mwanamke mnene kiasi,alionekana kama aliyechanganyikiwa ndiyo maana akawa anapayuka kwa sauti kubwa, akiomba msaada,hapo hakukuwa na la zaidi.Nesi akachomoka kwa kasi na kumuacha Daphine,ambapo yeye alichukulia jambo hilo kama nafasi ya dhahabu,hapohapo nayeye akajichanganya na kutoka nje. Huko alitembeza kibaiskeli mpaka kwenye bustani,akavua koti la kidaktari akavua miwani,akaitupa na kuanza kutembea kuelekea getini.

“Mabibo Mwisho”

Daphine alimwambia dereva wa pikipiki mmoja wapo, aliyekuwa amesimama pembeni anasubiri abiria wenye haraka kama Daphine.

“Poa sista,twenzetu”

Bila kupatana bei,Daphine akapakia kwa nyuma safari ikaanza hapohapo.Safari hiyo ilikuwa ni kwa lengo moja tu,kwenda nyumba anayoishi Jenipha,ambapo huko aliamini ya kwamba angepata msaada wa kujua ni wapi Ngesa alipo,katika harakati za kupita njia za mkato mitaani wakaibukia,Ubungo Shungashunga,dereva akanyoosha na barabara kubwa ambapo hapo,haikuwachukua hata muda mrefu, wakawa wamefika Mabibo mwisho.

“Kaka,nisubiri kidogo hapa.Nikakuchukulie pesa pale”

Daphine,alijilegeza huku akiwa amemshika bega dereva huyu wa pikipiki.Hakuwa na senti hata moja mfukoni,hivyo ilikuwa ni lazima amtoke dereva huyo kiakili kwani siku zote kumchinja kobe ‘timing’Daphine alivyovuka barabara,akajichanganya na watu wengine na kuingia vichochoroni,huko alianza kukumbuka nyumba aliyoambiwa anaishi Jenipha.

“Anco,samahani”

Daphine alimsemesha,jamaa mmoja aliyekuwa anapita njia.Akasimama!

“Bila samahani”

“Hapa,kituo cha polisi kipo wapi?”

“Cha Mabibo au?”

“Ndio”

“Umekiacha huko nyuma,unaona huu mtaa?”

“Ndio”

“Nyoooka nao,mbele utakuta kuna kona mbili.Nenda kulia,utaona lami.Upande wako wa kushoto”

“Sawa ahsante”

Alama ya kufika nyumbani kwa Jenipha ilikuwa ni kituo hiko kidogo cha Mabibo,hapo ndipo aliambiwa nyumba tatu mtaa unaofuata,akaanza kutembea mpaka alivyofika Karibu na kituo cha polisi,akaanza kuangalia mitaa,akaingia mtaa mmoja wenye vumbi, huko akatokeza katikati ya makazi ya watu.

Nyumba ya kwanza akaivuka,ya pili ya tatu.Akaliona geti jeusi,pembeni kuna nguzo.Hapo ndipo aliamini ni nyumbani kwa Jenipha.Hakuelewa kama yupo ama hayupo,alichofanya ni kuchungulia kwa ndani,hakukuwa na dalili yoyote ile ya mtu kuwepo.Akatembea mbele kidogo na kuona ukuta,bila kujiuliza,akaangaza huku na kule.Akaruka ukuta na kutua ndani.


Kazi yake ikawa ni kutafuta mlango,ambao angeingia ndani kwa urahisi.Bahati mbaya ilikuwa kwake,sababu milango yote ilikuwa imefungwa.Hapo ilibidi ajiongeze na ilikuwa ni lazima aingie ndani kwa gharama yoyote ile.

Alivyotizama pembeni,akaona tindo iliyochongoka kwa mbele,akaokota na kutembea nayo mpaka kwenye mlango.Akaanza kuchokonoa kitasa,akakipiga kwa nguvu,kikaanza kuachia.Kilivyotoka kabisa,akaupiga mlango kwa nguvu ukafunguka,akawa ametokeza jikoni.Akaurudishia mlango taratibu na kuanza kutembea,akatokeza seblen,akatizama picha ukutani na kuona kuna moja kubwa iliyokuwa ya Jenipha.Pembeni kulikuwa na picha nyingine,sura hizo hakuzitambua.Kwa kuwa picha hazikumuhusu,akaanza kuingia chumba hadi chumba,hatimaye akazama ndani ya chumba cha Jenipha,kilichokuwa kikubwa kiasi,kina kabati refu,akaanza kupekua pekua bila kujua ni kitu gani,anakitafuta.

Akaona boxi,lililojaa risasi,uchunguzi wake ukazidi kuendelea na kuanza kupekenyua huku na kule,akatoa begi kubwa na kuanza kulifungua,akaona kamera.Akaitupa juu ya kitanda.Alivyomaliza kila kitu,akakaa kitandani na kuanza kutafakari,hakuwa na shughuli ya kufanya zaidi ya kumsubiri Jenipha ili amueleze ni wapi Ngesa alipo.

Ghafla,akakaa sawa kama mwanajeshi aliyesikia kombora linapigwa,hiyo ni baada ya kusikia muungurumo wa gari,sekunde mbili baadaye akasikia tena geti linafunguliwa.Akavuta pazia na kumuona Jenipha,anaingia getini.Hiyo ilimaanisha ni lazima ajiweke sawa kwa lolote lile,japokuwa hakuwa ana silaha yoyote ile ya kujitetea,akajibanza nyuma ya mlango na kujificha.

Kama angezunguka na kupitia mlango wa uwani,angeanza kujihami mapema sababu kitasa kilikuwa kimevunjwa,kupitia kwake mlango wa mbele kulimfanya asihisi chochote kile,Jenipha siku hiyo alikuwa amechoka kuliko kawaida,ndiyo maana akaanza kutupa mkoba wake juu ya kochi seblen,akavua kikoti kidogo na kukitupa juu ya meza.Ndani kwake aliishi mwenyewe, ndiyo maana alikuwa anajiachia,baada ya hapo,akavua nguo ya juu na kubaki na sidiria peke yake.Akachomoa bastola na kuiweka mezani,hakuelewa kwamba anafanya kosa kubwa sana kuacha silaha yake!Akawasha feni na kupitiliza mpaka kwenye friji,akachukua maji baridi na kuanza kunywa kwa kasi,ilielekea alikuwa ni mwenye kiu sana,baada ya kufanya hivyo,akavua viatu na kuvirusha kando,akajihisi ni mwepesi.Alivyotaka kuvua suruali akasita kidogo.

“Nikapumzike sasa”

Jenipha,alijisemea mwenyewe na kuanza kutembea kuelekea chumbani kwake,ambapo hapo alinyonga kitasa na kuzama ndani.

Kitendo cha kufunga mlango,alishikwa bega na kuvutwa ukutani kwa kasi.Jenipha hakuwa lelemama,akachomoka kiutaalam akainama chini na kurudi juu ambapo aliona ngumi inakuja,akahepa kulia,ngumi ikapita hewani.

Hakukaa sawa,akaona teke linakuja,akainama kidogo na kupangua ngumi nyingine iliyokuwa inakuja kushoto kwake,kifupi mwanamke huyu kwenye maswala ya ndondi,alikuwa yupo vizuri mno.

Ndio maana ngumi na mateke aliyokuwa anarusha Daphine,yote aliyaona.Akatisha kama anarusha ngumi ya kushoto kwa Daphine lakini alitupa ya kulia ambayo ilimfikia Daphine ya shavu,hakuishia hapo akatupa mateke mawili yaliyomfikia Daphine kwenye mbavu.Daphine,akaelewa hapo alipo anapambana na mtu mtaalum,ambaye hakutakiwa kucheza naye na kumfanyia masihara hata kidogo.Ngumi ya Jenipha ikawa inakuja upande wa kulia,akainama na kuishika,ambapo hapo alimvuta kwa nguvu na kumtuliza na kichwa cha pua.Hakuishia hapo,akamviringisha na kumpiga vifuti viwili vya tumbo.Akamsukuma na kumsindikiza na teke aina ya ‘round kick’.Puuuu,kichwa cha Jenipha kikajigonga kwenye kabati,akawa amelala chali.Daphine,akamsogelea karibu na kumkanyaga tumboni!

“Nataka kujua kitu kimoja tu,yuko wapi Ngesa?”


 Kila alivyotaka kujitoa,alishindwa.Kuna namna ya kitaalam, Daphine aliuweka mguu huo tumboni kwa Jenipha.Akazidi kuukandamiza zaidi mguu wake,hiyo ilimfanya Jenipha ahisi maumivu makali mno!

“Ngesa yuko wapi?”

“Sijui,Da..phine unataka nini?”

“Kujua Ngesa alipo”

“Si..jui unazungumzia nini”

Alijibu kwa taabu,Daphine akainama kwa hasira na kukamata nywele za Jenipha akamburuza msobemsobe mpaka bafuni ambapo huko kulikuwa na choo cha kukaa,akasogeza kichwa cha Jenipha mpaka karibu na sink.

“Ngesa yuko wapi?”

“Sij..ui”

Kitendo cha kujibu hivyo,akatulizwa na kifuti cha mbavu, kilichomfanya adondoke chini mbaya zaidi alidondoka na kuteleza,kwani kulikuwa na malumalu chini zinazoteleza mno!Kilichofuata hapo ni Daphine,kumshushia mateke yasiyokuwa na idadi kamili.Akazivuta nywele za Jenipha kwa mara nyingine,safari hiyo alizishika vibaya tena kwa nguvu,ikapelekea Jenipha ahisi maumivu yasiyokuwa ya kawaida,alivyojaribu kutaka kujitoa ndipo maumivu yalizidi, hiyo ilimfanya atulie tuli.

“Yuko wapi Ngesa,sitokuuliza tena”

Unyama aliokuwa anafanya Daphine na urembo wake,vilikuwa ni vitu viwili tofauti kabisa!Alikuwa ni mwanamke mzuri,aliyepaswa kuwekwa ndani na kuolewa ili alee familia lakini kwake ilikuwa kinyume sababu alikuwa gaidi wa kutisha.Akakamata nywele,sawasawa na kumuweka usawa wa sinki la choo,akakindumbukiza kichwa chake ndani ya sinki hilo lililotumika kutoleo haja kubwa na ndogo,kichwa cha Jenipha kikawa ndani ya sink,akawa anashindwa kupumua vizuri kwa sekunde tano nzima, ndipo Daphine alipomuibua.

“Nitakuuwa Jenipha,historia yangu unaifahamu vizuri.Ngesa yuko wapi?”

Hakuwa Daphine wa kawaida,kifupi alibadilika na kuwa zaidi ya mnyama mwenye roho mbaya ya kutisha.

“Ngesa yuko wapi?”

Kichwa cha Jenipha kikazamishwa tena ndani ya sink,safari hiyo aliwekwa humo kwa takribani dakika moja nzima, hiyo ilifanya arushe rushe mikono yake huku na kule, akijaribu kusaka hewa ya oksijeni lakini ilikuwa vigumu.Ilivyofika dakika moja na sekunde tatu,Daphine akamuibua na kumsukumiza kando!

“Sitaki tufike mbali,Ngesa yuko wapi?”

Usingetokea muujiza wowote ule,ambao ungeweza kuzuia mateso hayo isipokuwa ni kusema ni wapi Ngesa alipo ama ni vipi atapatikana.Jenipha aliuelewa mziki wa mwanamke huyo Daphine gaidi,ambaye ana historia ya kuuwa kipindi bado yupo na Brigedia Karanje,hiyo ilimaanisha kukaa kimya kungehatarisha maisha yake kiujumla.Ndiyo maana alijivuta na kuweka mikono yake kwenye kona ya kitanda ili awe tayari kuzungumza,alitulia huku akimwangalia Daphine aliyekuwa amesimama mbele yake.

“Dus..tan..D.K”

Jenipha,akaanza kusema.

“Dustan?Ndio nani?Kafanya nini?”

“Ndio anajua ni..ni wa..pi Ngesa alipo”

Jenipha alivyojibu hivyo,akajigusa mdomoni na kugundua kuwa amechanika kutokana na maumivu aliyohisi,uso wake ulikuwa umelowa chapachapa kutokana na kulowekwa ndani ya sink la chooni.

“Usinitanie,Ngesa yuko wapi?”

“Nak..kwambia ukweli.Dustan anajua kila kitu”

“Nitampata vipi?”

“Yupo usalama wa taif..a”

“Unaniongopea”

“Sina sababu ya kukudanganya,huo ndio ukweli”

“Nahitaji kumpata Dustan”

“Huwezi kumpata kirahisi”

“Kwanini?”

“Yupo chini ya ulinzi”

Hapo Daphine,alinyamaza kwa kama sekunde tatu hivi.Akitafakari mambo fulani fulani,hakuwa ana uhakika kama maelezo anayopewea yana ukweli ama anapigwa changa la macho.

“Kwanini?”

“Alikuwa akisaidiana na Dustan”

“Mbona sikuelewi”

“Alikuwa akimsaidia Ngesa”

Jenipha,alizungumza kwa kiwewe, ikapelekea mpaka kuchanganya majina, badala ya kusema Ngesa akasema Dustan.

“Ilikuwaje?”

“Kamera hiyo hapo,tizama”

Daphine,akatupa macho kitandani na kuchukua kamera kwa tahadhari kubwa akaiwasha na kuanza kutizama tukio zima lilivyoenda,akamuona Dustan pamoja na Ngesa.Baadaye akaona sura ya kizee!Akashusha pumzi kidogo na kumuangalia Jenipha, aliyekuwa yupo chini.

“Namuhitaji Dustan”

“Yupo chini ya ulinzi”

“Wapi?”

“Usalama wa taifa”

“Nataka kufika huko”

“Sio kirahisi kama unavyodhani”

“Fanya iwe rahisi”

“Itakuwa ngumu”

Haukuwa utani,ulinzi uliokuwa usalama wa taifa, haukuwa wa kawaiada,mbaya zaidi kulikuwa na kamera za Cctv kila mahala.

Jenipha ilibidi achambue kila kitu,ilielekea kwa ridhaa yake alikuwa tayari yupo bega kwa bega na Daphine lakini hakutaka kulionesha hilo waziwazi.Akasimama na kuchukua Ipad,akaanza kumuonesha Daphine njia za kupita bila kuonekana.

“Hapa kuna kamera,utapitia huku na kutoboa hii paipu,chumba cha kwanza cha pili.Kina silaha,kushoto kwako hapa ndio Dustan yupo.Ukimpata Dustan,umempata Ngesa”

Maelezo hayo hayakumfanya Daphine,awe upande wake kwani siku zote aliamini ya kwamba ukitafuta amani wakati wa vita utakufa mapema,ndio maana baada ya hapo,alimvuta tena Jenipha na kusogea naye mpaka karibu na kabati,akachukuwa boxi la risasi.

“Naomba silaha yako”

“Sina”

“Nipatie silaha yako”

“Nimeiacha ofisini”

Akili za Jenipha zilifanya kazi kama mchwa,hakutaka kukubali kutaja ni wapi bastola yake ilipo.Hesabu zake zilikuwa kali na alitaka wakitokeza tu seblen, achukuwe bastola ili amuweke Daphine chini ya ulinzi.Hakuelewa ya kwamba Daphine ana akili kuzidi yeye.

“Usinitanie Jenipha,nipe silaha yako”

Daphine akaanza kufanya msako,akampekua Jenipha kila mahala na kumgeuza geuza!Akaanza kuvuta madroo,ilikuwa ni kama Mungu vile alimwambia afungue mlango, alivyopiga jicho mezani akaona bastola.Hapohapo akageuka na ngumi kali iliyomfikia Jenipha,mdomoni ikamfanya aung’ate ulimi wake!Hakukuwa na muda wa kupoteza,Daphine akashika bastola na kubeba risasi zilizokuwa ndani ya boxi,akaiendea pochi ya Jenipha na kukuta pingu,akamfunga kwa nyuma.

“Tulia hivyo hivyo”

Ingekuwa hatari kubwa sana kumuacha Jenipha mwenyewe,aliamini ingepelekea kuharibu operesheni yake nzima ya kwenda kumkomboa Dustan,katika idara ya usalama wa taifa.

Akaingia stoo ambapo huko alikuta gundi kubwa na nzito,akambandika nayo Jenipha mdomoni, akabeba funguo za gari zilizokuwa mezani na kumvuta mpaka nje,akafunga mlango vizuri na kuingia naye ndani ya gari.

Kwa safari moja tu,usalama wa taifa kwenda kufanya ukombozi.Ndani ya dakika hamsini walikuwa tayari wapo nje ya majengo ya usalama wa taifa,idara ya upelelezi.

“Ndio hapa?”

Daphine akauliza akiwa amekaa nyuma ya usukani, anamtizama Jenipha aliyekuwa na gundi mdomoni.

“Mmmh mmh”

Akaitikia kwa kichwa na kuchukua ‘tab’,akaangalia ramani ili ajuwe jinsi ya kuingia ndani ya jengo hilo kirahisi.

Akiwa nje,ndani ya gari aliona mkusanyiko wa watu.Wengine wakiingia wengine wakitoka,niya yake ilikuwa ni kuyasoma mazingira kwanza kabla ya kuzama ndani!Alitambua kwamba akifanya kosa na akionekana operesheni yake,ingekwama hivyo ulihitajika umakini mkubwa sana!Akatafakari kwa muda na kuchunguza vizuri, ambapo aliona kuna ukuta kwa nyuma na kichochoro,akatizama ramani ili kujua kama angetumia njia hiyo kamera zingemuona ama la.Ikawa ngumu kwake,akazidi kufikiria zaidi.

“Inabidi nifanye juu chini niingie ndani ya hiki chumba chenye silaha”

Daphine,alijisemesha mwenyewe huku akiitizama ‘tab’ iliyokuwa na ramani,hesabu zake zilikuwa ngumu mno.Kupita mpaka kukifikia chumba hiko halikuwa jambo la mchezomchezo hata kidogo, ndiyo maana akawa anausumbua ubongo wake,akajiangalia vizuri kwenye kioo na kuweka nguo vizuri kisha kuteremka ndani ya gari bastola kiunoni,akazunguka nyuma ya jengo.

Huko ilikuwa nafuu sababu aliona kuna kimlango kidogo,akatizama huku na kule.Akaona hakuna mtu anayemuona,akazama ndani na kujifungia,mbele yake kulikuwa na kioo kidogo,chini kuna nyundo!Alivyochungulia ndani ya kioo hiko,hakuona mtu wa aina yoyote ile.Akaokota nyundo na kuvunja kioo,haraka akapanda na kujipenyeza kwa shida!Hatimaye akawa ameingia ndani lakini hakuelewa ni wapi yupo,akahisi kama kuna mtu anakuja.Akatembea haraka na kujificha nyuma ya mlango.Ulivyofunguliwa akaingia mzee mnene,bonge mwenye kitambi.Bila kuuliza chochote,akamsogelea na kumpiga na kitako cha bastola cha kichwa,mzee akadondoka kihasarahasara kwani alikuwa ni tukunyema, yaani minyama uzembe.

“Sasa sijui,usalama wa taifa gani huyu.Mnene namna hii”

Daphine alijisemea na kufungua mlango,akatizama huku na kule akachomoka,akakunja kushoto alivyohisi kuna kelele za watu,akajificha kwenye moja ya kona.

Wanaume wawili,wakapita bila kumuona!Akashukuru Mungu na kuweka bastola yake vizuri mkononi,ilikuwa ni bado kama vyumba vitatu ili akifikie chumba kinachowekwa silaha,alivyopiga hatua ya kwanza ya pili,akahisi kama kuna kichuma kimemgusa shingoni.

“Tulia,wewe ni nani?”

Sauti hiyo ilikuwa nyuma yake,kupitia kioo cha mlango kilichokuwa mbele yake kilimfanya amuone mwanaume huyo mrefu aliyekuwa nyuma yake,akampigia hesabu ni kitu gani akifanye kwa haraka ili ajikomboe.

“Weka silaha chini binti”

Jamaa huyo,akatoa amri.Hiyo ilifanya Daphine taratibu aanze kushusha mkono wenye bastola chini,kwa kasi ya umeme akageuka na teke lakini Jamaa huyo aliliona, akainama chini kidogo na kurusha ngumi ambayo hata Daphine pia aliiona akahepa kushoto ngumi ikapita hewani.

Kiutalaam Daphine,akakanyaga ukuta na kuruka mateke ya hewani.Jambo hilo lilikuwa ni kama sinema ya kikorea lakini huo ulikuwa ni ukweli kwani hakukuwa na mtu kati yao anafanya maigizo,mateke aliyorusha Daphine, yalifanikiwa kumdondosha, ambapo alifikia mgongo.Hapohapo Daphine, akamsogelea na kumshika vizuri,akaanza kum-miminia ngumi za pua, zisizokuwa na idadi kamili kisha kum-malizia na teke zito la kolomeo.

Jamaa akatulia,haikujulikana kama alifariki dunia ama amezirai.Kwa wakati huo hilo halikuwa swala la Daphine tena,jambo alilolifanya ni kuweka bastola yake vizuri na kuanza kusonga mbele,hatimaye akawa ameufikia mlango wa chumba kinachotumika kuhifadhi silaha.Lakini kuingia kwake halikuwa jambo la kawaida,ilikuwa ni lazima uweke namba za siri ama kadi,hiyo ilimfanya arude mpaka kwa jaama aliyelala baada ya kumpiga,akachukua kadi na kurudi nayo mpaka mlangoni.

Kitendo cha kuigusisha kwenye mlango,ukaachia silaha zote zikaonekana.Alichokiwaza ni kimoja tu,kuchukuwa mabomu ya machozi na silaha zingine kali ndogo ambazo angeweza kuzimudu.Pembeni yake kulikuwa na begi,akaanza kupakua silaha na mabomu ya machozi,siku hiyo hakutofautishwa na mtu anayechagua nguo mlimani City,alivyotizama pembeni akaona ‘Mask’maalum za kuziba pua.

Akazipakia ndani ya begi,hakuwa ana sababu nyingine ya kubaki eneo hilo,chumba kilichofuata aliambiwa ndipo Dustan amehifadhiwa,akavua begi na kuchukua kitu kilichofanana na kiazi,akakifungua kisha kuvaa ‘mask’ hapohapo akakitupa kwa chini huku kikiwa kinafuka Moshi,hakupoteza muda.

Akaupiga mlango teke kwa nguvu na kuzama ndani ambapo alimuona Dustan yupo juu ya kiti,akampiga teke kali jamaa aliyekuwa pembeni yake.Teke alilopigwa Isaya Msophe,lilimuingia vizuri,alivyojaribu kusimama wima akapokea teke lingine la tumbo, akajikunja na kutulia.Mwanaharakati Daphine alikuwa tayari ndani ya chumba hiko kwa ajili ya kufanya ukombozi,kazi ya kuwavalisha ‘Mask’ kila mmoja ilivyokamilika,Dustan akafunguliwa,mikono yake ikawa huru.

“Subirini hapo,Dustan….”

Daphine akasema na kumuita Dustan, akamrushia bastola ili imsaidie mbeleni,hapohapo Dustan bila kuchelewa akaikoki kwa ajili ya mashambulizi.

Siku hiyo Daphine alikuwa kama mkuu wao kwani ndiyo alikuwa anaongoza operesheni hiyo ili watoke salama salmin.

Hakuna njia nyingine mbadala, waliyotumia zaidi ya kutupa mabomu ya machozi kila mahali, hiyo ilifanya usalama wa taifa waliokuwa ndani washindwe kuona vizuri,macho yao yalijaa machozi na yaliwasha mno.Huo ndio ulikuwa upenyo wa Daphine pamoja na familia ya Dustan kutoka nje,haraka wakaingia ndani ya gari na kuvua ‘mask’.

Kichwani kwa Dustan kulijawa maswali mengi yaliyokosa majibu kamili,alikuwa akiwaza ni kivipi Daphine alifika eneo hilo, lakini alishtuka zaidi, baada ya kuingia ndani ya gari na kumkuta Jenipha akiwa mwenye pingu,amevaa sidiria peke yake,mdomo wake una gundi anavuja damu kwa mbali.

“Huyu naye kafata nini huku?”

Dustan akauliza kwa jazba,kifupi alimchukia sana Jenipha kwa kitendo alichokifanya cha kumchomea, mpaka akashikiliwa na kuwekwa chini la ulinzi.

“Nina biashara naye”

Daphine alijibu,akipiga gia.Akarudisha gari kinyumenyume kwa kasi ya ajabu na kuzungusha usukani na kuliweka sawa,hapo alilitoa mbio.

Kasi yake ilitisha.Alizidi kukanyaga mafuta mengi mpaka alivyofika daraja la salenda,akapitisha gari chini kidogo, ambapo kulikuwa na mitimiti kiasi,akaweka gari kando.Akashika bastola yake na kuikoki,akashuka kwa haraka na kuuendea mlango wa nyuma, akaufungua na kumtoa Dustan,akamuwekea bastola kichwani.

“Ngesa yuko wapi?”

Daphine,aliuliza huku akiwa amekunja sura yake.Hakuwa ana masihara hata kidogo, hiyo ilimshangaza Dustan sababu muda mfupi uliopita walikuwa wanacheka wote.

“Ngesa yuko wapi?”

“Kenya”

“Nitampata vipi?”

“Ni ngumu kwa sasa hivi”

“Kivipi?”

“Amenipigia simu na tumeiacha kule uliponikuta”

Hiyo ilimfanya Daphine achoke.

“Lakini kuna njia nyingine ya kuweza kumpata”Dustan,alionekana kama mtu mwenye wazo kabambe!

“Njia gani?”

“Tumtumie Jenipha”

Dustan akatoa pendekezo, hiyo ilimfanya Daphine amuangalie kwa umakini zaidi akaangalia ndani ya gari na kumuona Jenipha amelala nyuma ya kiti,amepigwa pingu kwa nyuma.

Kabla ya kufanya chochote waliona magari matatu yanapita kwa kasi ya ajabu na kupiga breki za ghafla,wakashuka kwenye magari na kutoa bastola.Hapohapo Daphine,akamlaza Dustan chini kidogo na kufyatua risasi, kabla wao hawajaanza mashambulizi.

“Paaa! Paaaaa!”

Kilichosikika hapo ilikuwa ni mirindimo ya risasi.Ilikuwa ni wazi kabisa usalama wa taifa walikuwa wakiwafuatilia kwa nyuma, hivyo waliwaona, ndiyo maana walianzisha mashambulizi.

“Paaaa! Paaaaaa!”

Risasi ziliendelea kurushwa,Daphine na Dustan walikuwa nyuma ya gari wamejificha,ilikuwa ni kama wapo vitani.Jambo hilo lilimkumbusha Daphine mbali sana,akawa anatumia utalaam wa kuhama upande.

“Dustan,Cover me”(Dustan,nilinde)

Ilikuwa ni lugha ya kivita,ikimaanisha kwamba Daphine anahitaji kuhama upande,Dustan alilielewa hilo ndiyo maana akawa anarusha risasi nyingi nyingi upande wa pili.Hiyo ilifanya Daphine akimbie kutoka nyuma ya gari mpaka nyuma ya mti ambapo hapo ilikuwa rahisi kwake kuwaona wana usalama wote,akabana jicho lake moja na kuanza kufyatua risasi.

“Paaa!Paaa!Paaaa”

Kila risasi iliondoka na mwanausalama mmoja,sio siri mwanamke huyu mbali na kujua michezo hatari ya kupambana lakini alikuwa mwenye shabaha sana, hasa linapokuja katika swala la kutumia bastola.




Hakukosea,kila risasi iliondoka na mwana usalama mmoja.Kifupi risasi alizokuwa anafyatua Daphine hazikupotea hewani bure, kwa utaalam wa hali ya juu akawa anabadili upande,akitoka kwenye mti huu anabiringika mpaka kwenye mti mwingine.

Jambo alilokuwa analifanya lilifanya wanausalama hao washindwe kumpata vizuri.Ndiyo maana wakaanza kurudi nyuma na kukaa nyuma ya magari yao.Wakipeana ishara za mikono.

“Psiii psiiiiii”

Mwanauslama mmoja alitumia mluzi kumuita mwenzake,akampa ishara kwamba apite upande wa pili.Kitendo cha jamaa, kutokeza akijaribu kupita upande mwingine alitunguliwa na risasi ya bega,akadondoka chini.Daphine aliwachanganya sio kawaida.

“Dustaaaaan”

Daphine akaita huku akiangalia upande wa nyuma aliokuwa Dustan,anarusha risasi hovyohovyo.

“Washa gari,lilete huku”

Dustan,akatii amri.Sio siri,siku hiyo Mkewe pamoja na watoto wake walitandwa na hofu wakiwa wapo ndani ya gari, wamelala chini ya viti.

“Daaad,I’m scared”(Baba naogopa)

Mtoto huyo wa kwanza ambaye alipenda kuzungumza lugha ya kiingereza, alilalamika,hiyo ni kutokana na milipuko ya risasi kusikika,Dustan akakaa nyuma ya usukani,akapiga gia.Kichwa kikiwa chini!Akamsogezea gari Daphine karibu, ambapo hapo alizama ndani.

“Pita nyuma”

Daphine akazungumza,Dustan akaruka siti ya nyuma.Mahesabu ya Daphine yalikuwa yana hatari kuliko hatari yenyewe,kwani ndani ya sekunde moja.Akalizungusha gari kama feni, hiyo ilifanya tairi za nyuma zirushe mchanga na kuzunguka kwa kasi mno.Tukio hilo lilikuwa ni kama sinema lakini ndio ukweli,hakuchelewa akachukua kitu kilichofanana na kiazi,akatoa pini ya juu na kurusha upande wa wanausalama.

“Grenadeeeeee!”

Ukelele huo aliachia,mwanausalama mmoja aliyeshika bastola.Hilo lilikuwa ni aina ya bomu, lililofanana na kiazi hivyo likirushwa na kutua chini hufumuka ndani ya sekunde chache.Kitendo cha kutoa taarifa hiyo kwa sauti,wanausalama wote wakajitupa mbali kwani walijua kitendo cha bomu hilo kulipuka kila mtu angegeuka na kuwa kama vipande vya mishkaki.Huo ndio ulikuwa upenyo wa Daphine kulirudisha gari nyuma kwa kasi na kuliweka sawa,kilichofuata hapo lilikuwa ni vumbi kali kwa nyuma.Akaingiza gari barabarani na kulitoa kasi!

“Tunaenda wapi?”

Dustan akatupa swali.

“Wewe ndio uniambie”

“Kama nilivyokwambia,simu nimeacha usalama wa taifa, tumtumie Jenipha”

“Sio wazo zuri,hatuwezi kurudi tena nyuma inabidi tusonge mbele.Ni hatari sana”

“Nimekumbuka kitu”

“Kitu gani?”

“Si,unamtaka Brigedia Karanje?”

“Kwa wudi na uvumba”

“Makamu wa Rais,anajua ni wapi Karanje alipo”

Jambo hilo lilimshtua Daphine,alikuwa nyuma ya usukani macho yake yapo mbele lakini ilimlazimu amgeukie Dustan na kumtizama kwa umakini, hakuelewa kama amemsikia vibaya ama Dustan aliropoka.

“Mh.Cosmas Ngailo?”

Daphine aliuliza kwa mshtuko.

“Ndio”

“Una uhakika?”

“Asilimia zote mia moja!Nilimsikia marehemu Kimpanga kabla ya kukata roho alimtaja”

“Kwamba?”

“Anahusika na anajua ni wapi Karanje alipo alisema hivyo mbele ya Ngesa”

“Makamu wa Rais,anaishi wapi?”

“Kwa sasa hivi yupo Ikulu lakini familia yake,ipo Goigi pale”

“Unapafahamu?”

“Ndio”

Kitendo cha kujibu sentensi hiyo Daphine,alizungusha usukani kwa kasi na kukunja kona,ilikuwa kidogo amgonge mlevi aliyekwa anavuka barabara.

“Pumbaaavuuu,ungenigonga nikafa ungenikomaaa”

Mlevi huyo aliropoka baada ya gari analoendesha Daphine kumkosa kosa!Daphine hakujali alipandisha mori,katika watu ambao walikuwa wenye usongo na Brigedia Karanje,ni mwanamke huyo, ndiyo maana alizungusha usukani kwa safari moja tu,kuelekea Mbezi Goigi ili akaonane na familia ya Mh.Cosmas Ngailo!


******

Saa kumi ya Jioni waliwasili mpakani Namanga,gari lilikuwa chafu mno.Limejaa tope zito, hiyo ilitokana na kupita njia za panya na njiani walikwama kwenye matope mara nne,ilikuwa ni lazima siku hiyo waingie nchini Tanzania hata ingekuwa saa saba ya usiku.Brigedia Karanje alikuwa ndani ya gari,siti ya nyuma.Jambo aliloliona lilimshtua,siyo yeye tu hata dereva aliyekuwa anaendesha gari aliingiwa na hofu.Hiyo ni kutokana na watu kupekuliwa na kutolewa ndani ya magari.Kulikuwa na msako mkali mpaka mbwa wa polisi walishirikishwa,hakukuwa na namna ya mtu yoyote yule kuvuka Tanzania wala kuingia nchini Kenya bila ya kukaguliwa,kuna wengine walipekuliwa mpaka mifukoni.Wakaingizwa ndani ya vyumba maalum na kuvuliwa nguo.Gari alilopanda Brigedia Karanje lilikuwa kwenye foleni,nyuma kabisa.Anachungulia.Hofu ikamtanda akajuwa yeye ndiye anasakwa!

“Kuna nini?”

Uvumilivu ukamshinda,akauliza.

“Sijui mkuu.Kuna msako navyoona”

“Nani wanamtafuta?”

“Sina uhakika,ngoja nikaangalie”

“Fanya hivyo”

Ilibidi dereva,ambaye hata yeye alikuwa mwanajeshi japokuwa alivaa kiraia akateremka na kwenda mpaka mbele kabisa.Alichokiona kilimuogopesha sana!Aliona picha imebandikwa kwenye ukuta,mzee mwenye mvi anasakwa na kutafutwa na jeshi la polisi.Sura hiyo haikuwa ngeni machoni mwake kwani masaa mawili na nusu nyuma, walikuwa naye ndani ya gari wakimpa lifti.Katika kudadisi kwake,akagundua mzee huyo alikuwa ni Derrick Ngesa, ambaye mkuu wake alikuwa akimsaka kwa muda wa siku nyingi sana.Akarudi mbio mbio mpaka kwenye gari akaingia.

“Kuna nini?”

Brigedia Karanje,akauliza.Ilibidi dereva,aseme alichokiona.Hiyo ilimshangaza mpaka Brigedia Karanje,japokuwa alijiamini lakini alianza kuogopa,akageuka nyuma ili kuangalia usalama kwanza akahisi wenda Ngesa anamfuata kwa nyuma.Taa nyekundu ya hatari ikawaka kichwani kwake,akajua kivyovyote vile Ngesa alimfuata yeye nchini Kenya.

“Ina maana yule mzee tuliyempakia ni Ngesa?”

“Ndio mkuu”

“Haiwezi kuwa kweli.Itakuwa umeona vibaya.Mpigie simu Cosmas Ngailo,nahitaji kuongea naye ili tupite hapa haraka sana kabla mambo hayajaharibika!”

Ngesa alimtisha lakini hakutaka kuliweka jambo hilo wazi kwa wafanyakazi wake,aliogopa kudharaulika na kuonekana mwoga.Hiyo ingemshushia sifa, ndiyo maana akajitutumua akionekana kujiamini.

“Mpigie sasa hivi.Kama ni yeye nitamuua kwa mikono yangu”

Ilibidi Mh.Cosmas Ngailo apigiwe simu ili wapite kiurahisi kwenye mpaka huo bila kukaguliwa.Ni kweli simu ilipigwa na Mh.Cosmas Ngailo,akawa kwenye laini.Brigedia Karanje akasema shida yake na mwisho alihitimisha kwa swali kuhusu Ngesa.

“Nilivyosikia yupo Kenya”

“Amefata nini Kenya?”

“Sijui”

“Usijue kwanini? Hivi mnashindwa nini kumkatama huyo Ngesa?Sasa ngoja mimi niwasaidie”

“Yupo mbioni kukamatwa lakini,ndiyo maana tumeweka ulinzi.Kila boda,hawezi kutoka na sasa hivi yupo kwenye muonekano tofauti anafanana na babu kizee”

“Naelewa, nipo Namanga hapa nimeona picha zake.Kitu kingine, nataka kupita bila kukaguliwa,najua natafutwa sana”

“Upo kwenye gari gani?Nitajie namba za gari!”

Jambo hilo likafanyika mara moja,Mh.Cosmas Ngailo.Akapanda hewani kwa kutumia simu ya Ikulu,mpaka kwa mkuu anayeongoza operesheni hiyo ya msako.Akatumia mgongo wa ikulu ili kuruhusu gari alilokuwemo Karanje lipite bila kufanyiwa upekuzi wowote ule, akisema kwamba kuna dharura hivyo,lisibugudhiwe.

“Mboka,Dingo na Chuma.Shukeni,rudini aliposhuka yule Mzee.Ni Ngesa nataka afe.Kichwa chake mniletee mkimuuwa”

“Sawa mkuu”

“Sitaki kosa lolote lifanyike”

“Sawa mkuu”

Brigedia Karanje alitoa amri na kuwaamuru vijana wake watatu walioshiba na warefu wateremke ndani ya gari ili wakamsake Ngesa,wamuuwe na Brigedia Karanje alitilia mkazo ya kwamba wakishamuaa Ngesa wakikate kichwa chake ili iwe kama ushahidi namba moja!

Wanajeshi hao waliovalia nguo za kiraia walivyoshuka wakakodi Taxi, ambayo angewapeleka mpaka Isiolo walipomuacha Ngesa!


*****

Ngesa alikuwa kwenye giza nene,hakuelewa ni wapi aanzie.Ndani ya nchi hiyo alikuwa bado mgeni.Mbaya zaidi alikuwa akimtafuta Dustan ili amuelekeze ni wapi Brigedia Karanje alipo,lakini zoezi hilo likaonekana kuwa gumu sababu hakumpata Dustan kirahisi.Hakuelewa ni kitu gani akifanye zaidi ya kutafuta mgahawa mdogo,atulie na kunywa soda.Akitafakari juu ya kitu gani akifanye.Masaa yalizidi kwenda,alitamani kurudi nchini Tanzania ili aonane na Mpenzi wake Jaqlin Mfinanga lakini hakuwa ana uwezo huo, kwa kufanya hivyo bila kurudi na Brigedia Karanje, ilikuwa ni sawa na kujiingiza kwenye mdomo wa mamba.Alitafakari vitu vingi sana siku hiyo, hususani maisha yake kwa ujumla.Akamkumbuka Baba yake mzazi,ambaye hata yeye alionekana kabisa yupo upande wa Karanje!Alisikitika mno alivyokumbuka siku aliyomtesa,akitaka kumuuwa!Muda ulizidi kwenda.Lisaa limoja baadaye akasimama na kuanza kutembea akiingia katikati ya makazi ya watu, akiamini huko angepata sehemu ya kujificha na kupumzika ili kesho yake, aanze kufikiria upya.Huko alipata sehemu yenye uwazi kidogo,pembeni kulikuwa na kiti kilichotengenezwa na miti,akaketi.Hapo alisubiri,kutokana na upepo kuwa mzuri na mwanana alianza kuhisi usingizi mzito alivyojaribu kushindana nao,alishindwa kwani uchovu aliokuwa nao ulichangia kabisa!Hivyo hakuweza kushindana nao!Usingizi mzito ukampitia hapohapo.


******

Wanajeshi waliotumwa kumsaka Ngesa waliwasili mjini Isiolo,ndani ya lisaa limoja na nusu.Hapo wakawa na kazi ya kumuulizia mzee huyo.Haikuwa kazi ngumu kumpata kwani wakazi wa eneo hilo walimuona.Wanajeshi hao wakaanza kuingia katikati ya makazi ya watu,walifurahi na kujua kazi yao tayari imekwisha sababu walimuona Ngesa mbele yao,tena akiwa amelala fofofo.Mmoja wao akachomoa kisu kirefu kwa niya moja tu,amuulie Ngesa akiwa usingizini.Lakini mwingine akaona jambo hilo lingehatarisha maisha yao,ilikuwa ni lazima wamuuwe kisailensa,bila mtu yoyote yule kuwaona.

“Shika huu mfuko”

Mmoja,akatoa mfuko mzito wa nailoni!Akaushika vizuri mikononi mwake,akamsogelea Ngesa karibu na kumvisha nao kwa nguvu usoni.Kitendo cha Ngesa kukurupuka,akawa amechelewa kwani alidakwa miguu na kunyanyuliwa juujuu kama kindama!Akashindwa kukurupuka na kutoka sababu hakuona mbele,wanajeshi hao wakambeba msobe msobe mpaka katikati ya miti.

Wakazidi kwenda mbele zaidi!Ngesa akawa ana kazi ya kuhangaika ili kuutoa mfuko huo, uliokuwa usoni mwake,kitendo cha kutumia nguvu nyingi kuliko akili kingemgharimu mno.Ndiyo maana akaamua kutulia,kwa kutumia meno,akaanza kuuchana.Akafanikiwa kuutoboa, hiyo ilimfanya aweze kuona nje, akitumia jicho moja!Mbele yake akaona mti mkubwa,kosa walilofanya wanajeshi hao ni kutomfunga mikono yake.Ngesa akapiga hesabu za kikomandoo!Alivyoukaribia mti,akajiandaa vizuri alivyoufikia tu.Akaruka kama Ngedere,haikujulikana aliwatokaje lakini alivyowaponyoka iliwafanya wanajeshi hao wayumbe,Ngesa akashika mti.Alivyotua akakimbia hatua kama kumi mbele na kuutoa mfuko uliokuwa usoni kwake.Hapo alibahatika kuziona sura hizo,ambazo hata yeye alizikumbuka,mmoja wa wanajeshi hao alikuwa ana kisu mkononi, huyo ndiye alitakiwa awe naye makini sana.Akajua tayari kuna hatari mbele yake,kama asipo jihami.

“Leo ndio mwisho wako Ngesa”

Mmoja wa wanajeshi akaropoka,hiyo ilimshtua Ngesa sababu alijua tayari amegundulika japokuwa hakujua watu hao ni akina nani.Wanajeshi wakaanza kumfuata.mmoja akarusha ngumi,ikapita hewani baada ya Ngesa kuinama chini.Alivyoinuka kwa kasi,akatupa ngumi, ambayo ilimfikia mwanajeshi huyu mbavuni.Aliyeshika kisu,alivyotaka kumchoma Ngesa tumboni, akahepa kushoto.Kikapita pembeni!Ngesa akakunja ngumi,akitambua kwamba watu anaopambana nao, walikuwa ngangali na sio watu wa mchezomchezo!




Haukuwa utani hata kidogo,wanajeshi walikuwa na miili mikubwa.Warefu futi nyingi kwenda hewani, wamekomaa mno,zaidi na hayo walikuwa na misuli iliyofanya wawe ngangali.Hiyo ilimaanisha Ngesa atumie akili nyingi, kupambana nao vinginevyo angekufa kibudu, jambo ambalo hakutaka kuruhusu litokee,ndiyo maana alivyoona teke limerushwa akainama chini na kurudi juu,ambapo huko alibugi kwani alipokea ngumi ya mbavu,alivyogeuza shingo upande wa nyuma akadakwa shingo na kuinuliwa juu kama karatasi,shingo yake ilikuwa imekabwa, miguu yake inaning’inia kama nyama buchani.Akatupwa chini na kufikia mgongo, ambapo hapo alihisi maumivu makali mno!Alivyokuwa chali,aliona buti linakuja na kutaka kumponda tumboni,akabiringika pembeni buti zito likakanyaga chini ardhini kiiii,hapo Ngesa akasimama ‘sharp’ ingawa alikuwa mwenye maumivu makali,ilikuwa ni lazima ajitetetee kwa njia moja ama nyingine!

Akakunja ngumi kwa mara nyingine, safari hiyo alimuangalia kila mmoja wao kwa zamu,mwanajeshi mwenye kisu kirefu, akaanza kumsogelea karibu akiwa amekishika kwa hasira kitendo cha Ngesa kuonesha michejo, alikitafsiri kama upotevu wa muda,ndiyo maana alitaka amchome kisu ili amuuwe,wafanye mambo mengine.Lilikuwa ni kosa kubwa sana kwake kusogea kichwa kichwa na kutaka kumchoma Ngesa,ambapo kilipita pembeni,Ngesa akarusha mateke mawili yaliyomfikia mwanajeshi huyo kwenye misuli ya mkono,akayumba kidogo akakusanya konde la nguvu na kumchapa nalo la mbavu,hakuishia hapo alirudi nyuma kidogo na kumrukia mateke ya hewani.Mwingine alivyotaka kuibuka,akampiga ngumi tatu za haraka mbavuni,akamrudia mwenye kisu.Akamkanyaga kifuani,kama ngedere akampandia mpaka juu kabisa kichwani.Kutokana na jamaa huyo kuwa mrefu futi nyingi kwenda hewani hiyo ilimfanya Ngesa atumie vidole vyake viwili,akavitumbukiza machoni kwa mwanajeshi huyo.Hiyo ilimfanya ayumbe na hapo Ngesa hakufanya makosa,akiwa kichwani kwake alifanikiwa kumpokonya kisu,akakiinua juu kwa nguvu na kukiingiza shingoni kwa Mwanajeshi.Kilichofuata hapo zilikuwa ni damu nyingi kuruka.Lilikuwa ni tukio la kinyama, lililomfanya Ngesa aruke sambasoti na kumrukia mwanjeshi mwingine, ambapo hapo walipambana,haikuwa kazi rahisi hata kidogo kwani wanajeshi hao walikuwa Ngangari,mpambano huo ulikuwa mzito mno.Ngesa alikuwa anapambana na Wanajeshi wawili kwa wakati mmoja, ambao hata yeye aliwatoa jasho kwani alikuwa akidunda kama kitenesi,mara apenye huku mara atokee kule.Hakutaka kufanya makosa ya kuwakaribia akiamini wangemtia mikononi, ndiyo ungekuwa mwisho wake,ndiyo maana alikuwa akiruka mateke na kutupa ngumi wakati mwingine alidunda na kuruka mabeki.Akafanikiwa kumdondosha mwanajeshi mmoja chini,akamkaba shingo kwa nguvu za ajabu,akamvunja!Wanajeshi wawili wakawa tayari wamepoteza maisha yao.Akabaki mmoja ambaye hakucheleweshwa,akawa chini Ngesa akawa ameshika Kisu.Akamtoboa nacho mguuni.

“Nani kawatuma?”

Ngesa akauliza huku akiwa ameshika mpini wa kisu hiko,makali yote yamezama ndani ya mguu wa Mwanajeshi huyo,aliyekuwa anapiga kelele za maumivu ya kisu.Mbaya zaidi Ngesa, alikuwa anakizungusha zungusha.

“Mim….i mwe…nyeweee”

“Huna mamlaka hayo.Nani kakupa oda?”

“Mku….uu”

“Nani?Nataka unitajie jina”

Ngesa alizungumza hivyo huku akizidi kuzungusha kisu chake,hiyo ilifanya damu zitoke nyingi pajani mwa Mwanajeshi huyo.

“Siwe….eziii”

Mwanajeshi huyu hakuelewa anamjibu mwanaume gaidi kuliko kawaida.Hapohapo Ngesa akachomoa kisu, kutoka mguuni mwake na kukichomeka kwenye mguu mwingine kwa nguvu.Ukelele aliopiga kwa mara nyingine ulitisha.

“Nadhani hunijui mimi vizuri”

Ngesa akazungusha kisu huku akiwa kama anachokonoa kitu ndani ya mguu wa mwanajeshi,alichotaka kujua ni kitu kimoja tu.Mtandao huo ni wa nani.Serikali ya Tanzania? ama usalama wa taifa?Ili ajue ni wapi angeanzia.Akaendelea kumsulubisha binadamu mwenzake.

“Nilimtesa baba yangu mzazi,nikataka kumuuwa.Sababu ya kitu kimoja tu,hakutaka kuniambia kitu nachotaka kujua.Nadhani unajua nini maana yake.Nani kakupa oda?”

Ngesa akauliza kwa mara nyingine,akachomoa kisu mguuni na kumuweka vizuri.Akamkanyaga shingoni,akakishika kisu vizuri na kukiweka karibu na jicho la kushoto la mwanajeshi huyo.

“Nani kakupa oda?”

Kulikuwa kuna kila dalili ya Ngesa kumtoboa macho mwanajeshi ambaye alionekana kuwa mkaidi.

“Kar…aaanjeee,Bri…gedia Kara…aanjee”

“Naniii?”

“Mkuu Karan..je”

“Karanjee?Alijuaje nipo hapa?Yuko wapi?Unanitania sio”

“Alikuwa akiwasiliana na Makamu wa Rais”

“Kivipi?”

Ilibidi mwanajeshi huyo atoboe siri,aseme kila kitu kilivyokuwa tangu walivyompakia Ngesa,akaelezea mipango yote itakavyokwenda mpaka kuingia Arusha,hakuwa na sababu ya kubaki na vitu hivyo kifuani.Hiyo ilimfanya Ngesa ashtuke zaidi,kumaanisha!Masaa mawili mbele Arusha ingekuwa katika msiba mkubwa kwani mamia na maelfu ya watu, wangekufa kutokana na sumu aliyoitengeneza Brigedia Karanje.

“Nipe simu yako”

Ngesa akasema,akapatiwa simu!Hapohapo,akaanza kubonyeza namba fulani kisha kuweka simu sikioni.

“Halloo,naomba niongee na Mh.Rais.Ni dharura”

Ngesa alizungumza harakaharaka baada ya kupiga simu ikulu,kwa lengo moja tu.Amwambie kila kitu Rais Leslie Benjamin ili azuie msafara wa Brigedia Karanje unaoingia nchini Tanzania kupitia Mpaka wa Namanga.

“Wewe ni nani?”

Sauti nyororo ikasikika kutokea upande wa pili wa simu.

“Kujua jina langu sasa hivi,haitokusaidia.Nahitaji kuzungumza naye”

“Sio kirahisi namna hiyo”

“Binti,mpe simu Rais Leslie sasa hivi”

“Nimekwambia taja jina lako kwanza”

“DERRICK NGESA”

Kuanzia hapo,ukimya ukatawala ilielekea binti huyo kuna kitu alikuwa anatafakari kichwani kwake.

“Hallo,umenisikia”

Angel Massawe,secretary wa Rais Leslie.Alipigwa na butwaa la waziwazi akiwa ofisini kwake.Alielewa ni namna gani Ngesa anatafutwa na nchi nzima, akiwemo Rais Leslie,hapohapo akasimama na kuweka sketi yake vizuri.Akachomekea na kutembea mpaka kwenye mlango mkubwa,akagonga akiwa ameshika simu mkononi,akazama ndani na kumkuta Rais Leslie, akiwa katika mawazo mengi kashika tama.

“Una shida gani Angel?”

Rais Leslie aliuliza kwa sauti ya uchovu.

“Kuna simu yako”

“Imetoka wapi?”

“Derrick Ngesa”

Moyo wa Rais Leslie,ukalia paa!Akamtizama Mwanamke huyo wa Kichaga aliyesimama mbele yake,akahisi wenda amechanganyikiwa.

“Ngesaaa?!”

“Ndio,Mh Rais”

“Nipatie simu”

Rais Leslie akaweka simu sikioni na kusema ‘Halloo”

“Mh.Rais,unaongea na Derrick ngesa”

Ngesa akazungumza.

“Upo wapi wewe mwanaharamu?”

“Mh.Rais hatuna muda,unachotakiwa kufanya ni kuzuia msafara wa Brigedia Karanje,anaingia Tanzania.Ana sumu kali na…”

“Uko wapi nimekuuliza Ngesa”

“Mh.Rais,naomba nikwambie ndani ya masaa Machache,watu wasiokuwa na hatia watakufa Arusha.Najua una uwezo wa kuzuia jambo hilo lisitokee,fanya hivyo kabla hujachelewa”

“Ngesa sitaki kukuuliza kwa mara nyingine,uko wapi?”

“Siwezi kukutajia nilipo Mh.Rais”

“Unazungumza na Rais wako,uko wapi?”

“Mh.Rais,sikuwahi kukudanganya hata siku moja tafadhali,fuatilia nachokwambia.Mamia na maelfu ya watu watakufa leo!”

“Jisalimishe kwanza”

“Lakini si…tititi”

Rais Leslie akakata simu na kusimama kwa hasira.

“Tonny yuko wapi?”

Lilikuwa ni swali kutoka kwa Rais huku akimuangalia, Angel Massawe.

“Ofisini kwake”

“Kamwite,sasa hivi”

Angel Massawe, aligeuka na kutoka nje ambapo huko alinyoosha moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya Mkurugenzi Tonny Mteketa,katika idara ya usalama wa taifa.Akasema kilichompeleka na Mr.Tonnny akasimama,dakika moja baadaye akawa amesimama mbele ya meza ya Rais Leslie.

“Nimepigiwa simu na Ngesa,sasa hivi.Nimekuita hapa kwa vitu viwili.Moja,nahitaji u tresi hiyo simu nijue wapi imetoka,cha pili.Nahitaji umpigie simu mkuu wa Mkoa wa Arusha!Niunganishe naye lakini kabla ya hapo nahitaji kuzungumza na Daudi Bashonga”

“Sawa mtukufu”

Kutoa amri hiyo ilimaanisha kazi hiyo ifanyike muda huohuo,ndiyo maana ndani ya dakika mbili Rais Leslie alikuwa hewani anazungumza na Daudi Bashonga,mkuu wa mkoa wa Dar es salaam.Bila kuficha chochote akamueleza kila kitu kilivyoenda mpaka Ngesa alivyompigia simu na kumpa habari hizo nyeti.

“Sio kweli,Ngesa akamatwe.Na nina uhakika sasa hivi wapo bega kwa bega na Karanje”

Daudi Bashonga akatoa ushauri,Rais hakuelewa mtu anayezungumza naye ni joka la mdimu!

“Nisikilize kwa makini,mpigie Ngesa jifanye umekubali.Ili tumtie mikononi kirahisi”

“Ni wazo zuri sana hilo Daud,ubarikiwe”

“Amen,usijali.Nipo kwa ajili yako”

Kitendo cha Daudi Bashoga kukata simu,akampandia hewani Mh.Cosmas Ngailo.Akampasha habari kila kitu kilivyokwenda, akimwambia kwamba kila kitu kipo wazi.

“Nani kamwambia sasa?”

“Nimekwambia Ngesa”

“Kajuaje?”

“Hapo sijui,wasiliana na Karanje.Mwambie asitishe zoezi lake leo,mambo yameharibika”

“Hivi kwanini huyo Ngesa asikamatwe?Mtu mwenyewe hata mkononi hajai!Mimi nitamkamata mwenyewe kwa mikono yangu”

“Mr.Cosmas,Ngesa ni mtu hatari kuliko unavyodhani.Ni kutumia akili wala sio nguvu,mimi nitaongea na Rais,nitajua namna ya kufanya”

“Mimi nitamkata Ngesa,subiri tu”

Yalikuwa ni mazungumzo kati ya Mkuu wa Mkoa na Makamu wa Rais,wote walikuwa wapo upande wa Karanje na ilionekana wazi kabisa ya kwamba, Ngesa ndiye kidudu mtu anayefanya operesheni zao zikwame!


*******

  ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG