Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

ZAWADI YA ADHABU - 5

   

Simulizi : Zawadi Ya Adhabu

Sehemu Ya Tano (5)


“Sijauliza swali lingine, nadhani jibu lako la kwanza linatosha” Alijibu Masagida, kisha akawageukia wale wengine.

“Kuna mwenye maelezo mengine yanayokinzana na haya?” Alihoji.

“Hapana, Hapana bwana” Walijibu kwa pamoja kwa haraka kuliko walivyotaka. Walishaanza kukiona kizungumkuti

“Vema sana. Hicho mnachokiita mwili wa Neema kiko wapi?” Alihoji tena

“Tumefika hapa jana usiku na tuli….”

“Nimeuliza swali moja tu.. Kiko wapi mnachodhani kuwa ni Neema?” Akikatisha Mzee Masagida.

Jasho lilimtoka Mzee Upodo, akajiapiza kuwa angekuwa makini tangu muda ule kujibu maswali ya Mzee Masagida kama ilivyo kwa Mzee Chiziza.

“Penguin Hotel.. Ndipo magari ya waombolezaji yalipofikia kwa muda kuingoja alfajiri” Alijibu Upodo.

“Mzee, Haya sasa, ngoja uone.. Kwanini mlifikia Penguin Hotel??” Akamkazia macho mzee upodo ambaye alikosa jibu la haraka.. “Ni wazi kuwa itakuwa mlifikia hapo kuingoja alfajiri. Jifunze kuwa, kila swali unaloulizwa, toa jibu lake na uishie hapo. Acha kutoa majibu ya maswali ya kesho. Utafeli” Mwalimu alirudi darasani, kisha kwa haraka akaanza kuongoza njia huku akisema,

“Vema sana. Twendeni” Aliongoza Masagida na kuanza kuelekea kwa mguu kwenye njia iliyokuwa ikiiacha nyumba ile.

“Lakini Mzee… Kwanini… Sisi… Eeh, si tungekuja tu moja kwa mo….” Alijaribu kujieleza Tegu.

“Tegu.. Unajua vile tunaheshimiana Mzee mwenzangu. Hebu usicheze michezo ambayo hukujifunza ujanani ukiwa mzee. Utajavunja mgongo ukose wa kukuokota.. Acha tuliocheza ujanani tumalizie uzeeni” Alimjibu na haraka akapotea machoni pao.

Waliduwaa!!

Kengele za hatari zikaanza kupiga makelele masikioni mwao.

Ana mpango gani huyu?

***

Walirudi upesi Penguin Hotel na walipokuwa njiani, Mzee Upodo alimpigia simu Clifford na kumwomba atafute pahala pa kwenda kwa muda na awe mbali na pale kwa wakati ule. Walifika na kupokelewa na waliokuwepo lakini hawakusema chochote badala ya kuwaomba muda kidogo wa kujadili jambo. Lakini hawakutumia hata dakika kumi, wazee watatu wakawasili pale wakiongozwa na Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu.

Wazee wale wale watano wakawapokea na kuweka kikundi kidogo cha wazee pembeni. Wakajadiliana huku hapa na pale wakionekana kuvutana na kuelewana, na baada ya muda, vijana kadhaa wakaombwa kushusha jeneza lililokuwa limeuhifadhi mwili wa Neema. Wazee wale watatu wakaingia garini na kukaa huko kwa dakika kadhaa, na baada ya muda wakatoka. Kimya kikuu kilikuwa kimetawala na hakuna hata mmoja aliyezungumza na mwenzake.

Wakajadiliana tena kwa muda.

Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu akiwa na nduguze hawakusema neno. Wakaomba waende nyumbani kwa mazungumzo ya muda mfupi na kisha watatoa jibu.

Wakaondoka!!

******

Saa nne kamili.. Kimya!!

Saa tano kamili.. Hola!!

Saa sita kamili.., Hamna kitu!!

Saa nane na nusu, waapi!!

Tisa kamili, kumi kamili, kumi na nusu.. Malikiti!!!

Joto likageuka kuwa baridi.. Kila mmoja alitetemeka. Njaa iliuma lakini hakuna chakula kilichonunuliwa kikalika!

Macho ya watu wote yaliwaelekea wazee watano. Wao kwa wao pia, kila mmoja akimgeukia mwenzake, lakini kama vile walionong’onezana, kila mmoja akamgeukia Upodo!! Upodo yule mwerevu wa maneno ni kama alikuwa kwenye dunia ya peke yake huku wengine wote wakimtupia mawe.

Saa kumi na moja kamili, simu ya Mzee Tegu ikaita, na alipoangalia, herufi tatu zikajitokeza mbele yake zikimsanifu…

MKM!!!

“Masagida Kaswalala Masalu…” Alinong’ona huku akiipeleka simu yake sikioni.

“Halo Mwalimu” Alianza kusema lakini akagundua kuwa koo lilikuwa limekauka.. Akameza mate kwa nguvu ili kulilainisha lakini hakuwa na mate mdomoni. Akaishia kunong’ona tu.

“Hebu nizungumze na Upodo” Alisema mara moja Masalu. Mzee Tegu akatii na kumpa simu.

“Sasa bwana Upodo. Familia nzima imekutana na kujadili kwa kina. Ni kweli huo ni mwili wa Neema.. Hatuwezi kuutesa mwili wa binti niliyemzaa na kumlea kwa tabu kubwa kama Neem….” Ni wazi Mzee Masalu alikuwa akilia moyoni ingawa sauti yake ilijitahidi kubaki katika muhimili wake bila mafanikio.

“Sasa bwana.. Huyo kijana sijui Cliff nani huyo, mimi sina shida nae. Huenda kweli mwanangu ndiye alikuwa mbwa wa kujirahisi kwa wanaume.. Lakini nataka mnitendee heshima moja… Namtaka Mzee mwenzangu hapa.. Namtaka baba wa huyo kidume cha mbegu aliyenizalishia mwanangu na kupelekea kifo chake. Namtaka na huyo kiumbe aliyekuwa tumboni mwa Neema.” Alianza na kuendelea

“Nataka na taarifa ya daktari kuthibitisha kilichomuua Neema.. Vikipatikana hivyo hata sasa hivi, njooni na msiba tuzike. Pasi na hayo matatu, wala msijali. Nendeni makaburini, chimbeni, mfukieni Neema.. Ipo siku Neema wangu atarudi…” Alimaliza Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu na kubaki kimya kama vile aliyetaka kusika kutoka upande wa pili.

Damu iliwasisimka wale wazee!!

Ama kweli hili lilikuwa ni tukio la mwaka..

Mwili upo, hii haina shaka.

Taarifa ya daktari na kibali cha mazishi, ipo, haina maneno!

Kichanga cha marehemu, hiki kipo pia.. Ila kiko mbali, ingawa kinaweza kuletwa..

Shida sasa…

“Chiziza” Alijisemea Upodo pasi na kujua kuwa simu bado ilikuwa hewani… Akaiweka mezani, akavua kikofia kidogo alichokuwa amekibandika kichwani, akakuna upara wake ulikuwa umezungukwa na mvi kwa mbali. Akashusha pumzi ndefu zilizotoka na aina fulani ya mlio kama wa vuvuzela.

Alichodhani kipo, sicho alichokikuta!

******

Simu ilipigwa…

Mazungumzo yakafanyika… Zulfa akaombwa asaidiane na kina mama wengine wawili, mmoja aliyekuwa rafiki mkubwa wa Clifford akifanya kazi kama muuguzi wa afya katika hospitali ya Mkoa wa Singida, kuwa wafanye juu chini kumchukua yule mtoto kule hospitali na kuja naye Mwanza upesi. Kazi ile ikafanywa kwa upesi na mpaka kufikia saa nne ya usiku, walikuwa wanaanza safari ya kutoka Singida kuelekea Mwanza.

Mwili wa Neema ukashushwa na kupelekwa tena chumba cha maiti katika hospitali ya Rufaa ya Bugando ili usije kuharibika wakati ule wa sintofahamu. Waombolezaji wale wakagawana majukumu na namna ya kujikimu ikawekwa sawa, na ikaonekana kuwa, wengi walikuwa na ndugu, marafiki au jamaa pale Mwanza. Wakaenda kujisitiri huko.

Kazi ikabakia moja tu..

Kumshawishi Chiziza!!

Ee bwana wee!!

Upodo aliongea, Tegu akasema, Laswai akadakia, Ng’wanzalima naye akaweka neno, Makamba akaweka na uswahili kidogo, lakini ngoma ilikuwa inadundwa bila kutoa mlio. Mtu pekee aliyebaki kuwa na msaada akaonekana kuwa ni Clifford mwenyewe.

Usiku kucha wazee wale walifanya walichoweza lakini hakukuwa na matumaini. Asubuhi ya siku iliyofuata ikafika.

Siku ya nne tangu Neema aage dunia!!

Clifford alifanya maamuzi magumu!!

“Nataka niongee na Baba mimi mwenyewe, tafadhali wazee hebu niruhusuni” Alisema Clifford macho yakiwa mekundu kupita kiasi.

“Aah. Lakini Clifford, kwanini tusinge…” Aliingiliza Mzee Babudi

“Hapana.. Hebu tumpe nafasi.. Mwacheni ajaribu.. Damu nzito kuliko maji kumbukeni” Alishauri Upodo akiwa anaonekana mchovu kupita kawaida.

Simu ikapigwa, ikaita!!

“Shkamoo baba” Alisalimu Clifford akionekana kulemewa na machozi

“Ningekuwa namfahamu baba anayedharaulika kama mimi ningemtafuta ili tuunde umoja wa kina baba wapumbavu Tanzania” Alijibu Chiziza.

“Baba.. Sijawahi kuacha kukuheshimu Baba yangu” Alijieleza Clifford

“Iambie maneno hayo maiti ya huyo binti wa watu.. Iambie kuwa wewe Clifford, ulimuheshimu sana baba yako mzazi na ulimshirikisha hata juu ya mpango wako wa kuoa.. Iambie, iambie baradhuli mkubwa weye…” Chiziza alinguruma.

“Siwezi kushindana nawewe hata kwenye ujinga baba yangu. Hata kwenye kuchezea matope ni wewe ndiwe ulikuwa mwalimu wangu, siwezi kukushinda. Wewe umenizaa na umenifikisha hapa nilipo. Kujifunga mkanda na kutaka kushindana na wewe ni kuiambia dunia kuwa elimu yangu haijawahi kunisaidia. Ujanja wangu kwako ni upumbavu mtupu, na hamna chochote kinachonifanya kuwa bora kuliko wewe baba angu” Clifford alisema huku chozi likimtoka.

Kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake, alikuwa amemjibu mzee Chiziza jambo na kisha mzee huyo akaacha kusema. Ikamlazimu kuendelea.

“Mimi ni mtoto mjinga ambaye daima sitakua mwerevu mbele yako. Baba, si kwamba dunia nzima ina akili kama ulivyo wewe. Mimi ni mtoto, na huenda hata wewe hungependa kunikumbatia chini ya mbawa zako daima. Kuna wakati unaniacha niende huku na kule kuokota okota kama kifaranga. Si yote ninayokutana nayo yanafanana na yale unayonipa wewe baba. Sio akina baba wote wana busara kama za kwako. Lakini ni wewe wa kunifanya nijione niko salama tena baba yangu. Hata pale kila mtu anaponifungia mlango, nakuwa na imani kuwa upo mlango mmoja ambao haujafungwa. Na mlango huo ni wewe baba” Clifford machozi yalikuwa yakimtoka.

“Anhaaa.. Kwahiyo unafanya upuuzi wako kwa vile unajua kuwa Mzee Chiziza ataelewa tu, si ndio? Sasa imekula kwako fala wee.. Malizia mwenyewe ujinga uliouanza, fisi maji wewe” Alijibu Chiziza lakini ni wazi kuwa , hakuwa na hasira kama awali.

“Hapana baba.. Hapana hata kidogo. Kama leo nikiulizwa nimtaje baba aliye bora kuliko wote duniani, bado Mzee Chiziza anabaki kuwa the best. Ni wewe uliyenizaa na kila kitu chema ninachokifanya kimetoka kwako. Haya mabaya yoote ninayoyafanya nakiri tu kuwa nimetoa kwingine, lakini sio kwako baba yangu. Mimi si tu fisi maji.. Ni zaidi ya hata hayawani wote wa mwituni, majini na nchi kavu” Alijieleza Clifford.

“Acha kuniremba hapa. Kila mtu anakosea duniani..” Chiziza alijibu. Ilikuwa ni mara ya kwanza katika maisha yake Clifford kusikia kauli ile kutoka kwa Chiziza!!! Damu ikamsisimka. Bila kujielewa akajikuta akisema.

“Umesema sawa baba, daima najua kuwa kila mtu anakosea. Lakini napiga magoti yangu mbele yako leo baba, sio ili kuanza kukumbushana kuwa nani alikosea wapi, na kwanini. Leo hii, kuna baba ambaye mtoto wake yupo kwenye jokofu kwa siku ya nne leo. Kuna baba ambaye yeye pia anajua kuwa kila mtu anakosea, na anaugulia kifo cha mtoto wake.. Sitaki awepo baba mwingine atakayeumia kwa kupoteza mtoto wake Mzee Chiziza!” Clifford alisema kwa utulivu uliowatisha wenzake.

Hewala!! Wazee wale nywele za shingo ziliwasimama!! Hakuna hata mmoja aliyetegemea kauli nzito kama ile kutoka kwa Clifford. Mzee Upodo akafuta chozi!

“Kwahiyo unanitisha kuwa nawe unaweza kufa sio? Unataka ujiue ili nami niwe baba mwingine anayelilia mtoto sio?” Sauti kavu ya Chiziza ilihoji.

“Hapana baba. Siwezi kukutisha kwa kujiua hata siku moja. Nikifa leo ili kukukomoa, sitakuwa nimejifunza chochote. Kama niliwahi kukuita baba kwa kumaanisha, nadhani wakati huu nakuita baba nikiwa namaanisha mara mia zaidi. Sikuwahi kujua jukumu lililopo mabegani mwa baba.Wakati huu ninapoongea na wewe, na mimi ni baba. Nami ni baba wa mtoto mmoja. Kuna kiumbe sasa kinaniangalia na kusema “baba, baba”. Nitakuwa baba wa ajabu zaidi duniani kama nitakiacha kiumbe hiki kiendelee kuchekwa na dunia wakati mimi baba yake nikiwa hai!” Alimaliza Clifford.

Halafu…

Kimya!!!

“Mwili wa marehemu mmeuhifadhi wapi?” Katika hali isiyo ya kawaida, Mzee Chiziza alibadili uelekeo wa mazungumzo baada ya kimya kifupi.

Ndani ya dakika arobaini, Mzee Chiziza, Mkewe pamoja na dada mkubwa wa Clifford aitwaye Claritha ambaye kwa bahati tu alikuwa jijini Dar es salaam kibiashara walikuwa njiani kuelekea uwanja wa ndege ili kuelekea jijini Mwanza.

Joto lilirejea.

Taarifa ilitolewa kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu juu ya ugeni ule ili taratibu za msiba zianze mara moja. Kweli kabisa. Nusu saa tu tayari nguvukazi ilikuwa ikishambulia majukumu kama mchwa. Ilipangwa kuwa, siku hiyo jioni kifanyike kikao kikubwa cha familia zote mbili na kuweka mambo sawa, na panapo majaliwa, kesho yake mazishi yafanyike.

Naam!

Walikuwa wakimngoja Chiziza…

Na wakati huo, kumbe walikuwa wakingoja kizaazaa kingine cha karne!!

Ama kweli likiandikwa, litatimia!!




Nimefundishwa kuwa…

Si lazima uanze kila jambo likiwa katika ubora mkubwa. Hata magwiji wa elimu wanaamini kuwa, awali yaweza kuwa na changamoto zake nyingi tu. Lakini, daima lenga kuhitimisha kila jema unalolifanya kwa mafanikio makubwa. Azimia kuwa, ni muhimu kukamilisha kila unachokifanya kwa namna ambayo watu wote wataamini kuwa, daima ulikuwa ukilenga kufanikisha kwa mafanikio. Hatima nzuri sio tu inakupa moyo wa kuanza tena kwa nguvu, lakini inawajengea wengine Imani kuwa, misukosuko ya njiani haiwezi kuzuia mwisho Mwema wa safari!!

Una hiyari ya kukubali au kukataa….

******

*** NAWAANDIKIA HAYA KATIKA TAMATI ***

Jua liliwaka, likafika utosini…

Adhana ya alasiri ilimkuta Chiziza na familia yake wakiwa wamewasili jijini Mwanza, na wakafikia Charity Hotel. Ingawa alishawaeleza mkewe nab inti yake juu ya yaliyomkuta Clifford, bado yeye pia alitamani amwone Clifford na amweleze mwenyewe kwa kinywa chake Mwanzo mpaka mwisho wa kisa kile. Waliyozungumza asubuhi ile yalionekana kumuingia moyoni mwake na hapa na pale alitamani kumwona Clifford.

Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Chiziza alisikia uchungu usio wa kawaida!!

Naam.. Kikao cha kwanza kikakubaliwa kufanyika Charity Hotel. Wazee wale wale watano wakaongozana na Clifford hadi hotelini na baada ya hatua zote za utambulisho, mazungumzo yakaanza.

Wale wazee watano walikuwa wakimtumbulia macho Mzee Chiziza na familia yake kama vile walikuwa wakiwatoka sayari nyingine. Hapa na pale, walionekana wakinong’ona peke yao lakini ule ukali na uimara wa Chiziza uliwatisha! Ingawa hakuoneka kuwa mkubwa sana kuwazidi, alikuwa akiongea kwa mamlaka na kuhoji hapa na pale. Walizungumza kwa zaidi ya saa moja na hapo wakakubaliana kuanza safari ya kuelekea kwa mzee Masalu. Wakati huu, Clifford naye akaruhusiwa kuambatana nao!

Safari ya kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ikaanza. Njia nzima, wazee wale watano walikuwa wakikonyezana na kuzungumza kwa ishara, lakini ni kama kila mara Mzee Chiziza alikuwa akiwanyima uhuru. Mzee Upodo akanyanyua kinywa ili kusema jambo, lakini Mzee Tegu akamuwahi na kumkanyaga kwa nguvu huku yeye mwenyewe akipaza sauti na kuuliza.

“Vipi hali ya hewa ya Mjini bwana Chiziza.. Kule joto majira yote bwana” Alihoji Mzee Tegu.

“Umefanya vema kujiuliza na kujijibu bwana mkubwa” Jibu rahisi lilimtoka Chiziza.. Tegu akafikicha mikono na kuegamia kiti… Uso umemshuka na joto kali likimpita kwenye makwapa na sehemu nyingine muhimu.

Aliishiwa kauli!!

Kimya kikatanda hadi walipofika kwa Masagida Kaswalala Masalu..

******

Giza lilikuwa linaanza kubisha hodi kwa mbali, na nyumba ilikuwa na pilika pilika kiasi. Gari mbili zikawasili kwa pamoja. Moja walishuka Chiziza, Clifford aliyekuwa akiendesha, Tegu, Upodo na Claritha. Gari jingine wakashuka Mkewe Chiziza, Mzee Ng’wanzalima, Mzee Lasway, Mzee Makamba na Mzee Amri. Wajumbe wengine kutoka Singida walipaswa kufika baadae baada ya mazungumzo ya awali. Wageni wakapokelewa sebuleni, ingawa kila walikopita, miguno ilikuwa ikibaki nyuma huku wao wakisonga mbele.

Kuna jambo halikuwa saw ahata kidogo..

Hata kidogo, Hapana!!!

Sebule pana ilikuwa tayari na watu nane.. Watu kumi wakazidi kuinyanyasa kwa kuingia na kusambaa. Ilikuwa ni bahati kubwa kwamba, Masagida Kaswalala Masalu hakujenga nyumba ile kichoyo.. Ilikuwa sebule pana iliyoweza kuwachukua wote ingawa wengine walilazimika kuketi kwenye mkeka uliokuwa chini.

Kimya kikuu kikatanda…

Alikuwa anangojwa baba mwenye mji, Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ili afike na mnakasha uanze.

Akafika!

Halafu!!

Kila mtu alibaki kimya…

Kioo kimoja kilikuwa kimesimama mbele ya kingine..

Kama vile walioambiwa na mtu, Mzee Chiziza na Mzee Masagida Kaswalala Masalu wakasimama na kutazamana.

Kilikuwa kituko cha mwaka!!

Alikuwa ni mtu mmoja aliyevalia mavazi tofauti… Walifanana kuliko mayai ya kuku wa kisasa yanavyoweza kufanana. Walikunja sura kwa pamoja, hapo wakazidi kuwashangaza waliokuwa wakiwatazama..

“Wewe … Ndiye mwenye nyumba?” Alianza Chiziza huku akimtazama vizuri mwenyeji wake.

“Naam.. Karibu.. Kwani wewe ni…” Alijibu Masagida Kaswalala Masalu

“Nimeuliza swali moja.. Ningependa lijibiwe kwanza” Chiziza alijibu haraka.

“Ndiye haswa.. Kwani wewe ni nani? Aliuliza tena Masagida..

“Mzee Chiziza.. Ni baba yake na …” Alianza Mzee Chiziza.

“Kuwa mstaarabu.. Habari za umezaa watoto wangapi nitakuuliza baadae” Masagida akajibu kwa haraka.

“Lakini.. Nahisi kama vile…..” Chiziza alianza tena, lakini akakatizwa.

“Kuhusu hisia zako tutaongea tukiwa na muda, keti tujadili uhalisia” Masalu alijibu huku akiketi.. “Nilikuwa na wazo.. Nadhani tuanze na…” Aliendelea Masalu, lakini naye hakumaliza.

“Habu tuachane na wakati uliopita.. Kama ulikuwa na wazo sio pahala pake hapa. Nadhani kama una wazo ndio tuanze nalo” Chiziza alisema huku akiketi.

Upodo, Makamba, Lasway, Tegu, Babudi na Ng’wanzalima waliangaliana kwa haraka. Hali ya sintofahamu ilikuwa imetawala.

Utambulisho ukaanza mara moja na baada ya utambulisho, mazungumzo yakaanza. Lakini hakuna aliyetaka kujadili kuhusu msiba kwanza. Wazee wale wawili wakawa ndio wa kuzungumziwa pale. Hata wao walionekana kuwa na sintofahamu, lakini upesi, Chiziza akasafisha koo lake na kujiweka sawa, kisha akasimulia.

***

Anasimulia Chiziza

Kwakweli nashindwa kuelewa ikiwa hiki ninachokipitia ni ndoto ama la, lakini naona kuna jambo fulani zito hapa. Mimi jina langu la kwanza ni Adolph.. Sijui ni nani hasa alinipa jina hili, lakini ninachojua ni kuwa, nilikuwa mtoto pekee wa Mzee Aidani Chiziza na mkewe Anastella. Mzee Chiziza alikuwa ni mfanyabiashara maarufu sana jijini Dar es Salaam, lakini hakuwa kuniambia hasa asili yake ni wapo ingawa baadae nilikuja kujua kuwa, alikuwa mgogo wa Dodoma.

Nilikuwa peke yangu nyumbani kwetu, na nililelewa kwa ukwasi kiasi kutokana na hali ya kiuchumi ya Mzee Aidani.

Hata hivyo, wakati nilipokuwa na akili timamu kabisa, mara kwa mara nilikuwa nikimsikia mama akilalamika kwa baba kuwa, kuna watu walikuwa wanamsema na kumcheka kuwa amebaki kuokotaokota watoto, lakini sikuelewa chochote. Wakati nilipofika darasa la saba, mama yangu alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya kizazi. Nikabaki na baba yangu ambaye alinilea kwa upendo mkubwa mpaka nilipoingia kidato cha kwanza.

Pengo la mama yule halikuniathiri mimi peke yangu. Hata baba alionekana mara kwa mara akiwa na mawazo kupita kiasi na kuna wakati alikuwa akiniangalia kwa huzuni sana na kutoa machozi. Sikujua nini hasa kilimliza baba na kuna wakati mimi nami nilijikuta nikilia pamoja naye.

Siku moja usiku, baba aliniita na tuliongea naye kwa muda mrefu sana. Kwenye mazungumzo yake, alikuwa akiomba sana kuwa, siku moja nikiwa mtu mzima, niende nikaishi Mwanza. Sikuwa namwelewa kwa kuwa hakuniambia kwanini alitaka nifanye vile, lakini nilimkubalia na baadae akaniruhusu nikalale.

Siku iliyofuata, nakumbuka ilikuwa siku ya jumapili, nilimwamsha baba ilitujiandae kwenda kanisani kama kawaida yetu. Lakini baba hakuamka. Nikahisi huenda kule kuchelewa kulala kulikuwa kumemchosha, hivyo nikaamua kwenda peke yangu na kumwacha. Hata niliporudi, hali ilikuwa vilevile. Bado alikuwa amelala.

Baadae, iligundulika kuwa, Mzee Aidani alikuwa amefariki dunia. Nilihisi dunia nzima ikiniacha peke yangu!! Ingawa ndugu walikuja na kunifariji, sikuwa nimewazoea na sikuwahi hata siku moja kwenda kwa ndugu!!

Tukazika salama! Lakini baada tu ya mazishi, ndipo kikao cha familia kikaambiwa ukweli. Kwamba wakati mimi naletwa pale nyumbani, mama yangu hakuwa na mimba yoyote na baadae akasema kuwa amejifungua. Ndugu walipotaka sana kujua ukweli, baba yangu aliwajibu kuwa,nilitolewa kwenye kituo cha watoto yatima kwa kuwa yeye (baba yangu) na mama yangu walikuwa wameshatumia miaka ishirini ya ndoa bila kuwa na mtoto, na hivyo waliamua kupata mtoto hata kwa kuasili.

Niliumia sana siku ile!! Niliwaza sababu ya baba yangu kuniambia nije Mwanza. Familia ile ikanitenga, lakini sikuwa hata kwangu pia ilikuwa na nafuu. Sikutaka tena kuishi kinyonge. Nikaendelea kujibana bana pale nyimbani mpaka nilipomaliza kidato cha nne. Nafasi zikatoka na nikaenda jeshini, na tangu wakati huo, sikuwahi kujua habari zao tena!!!

Nilipokuwa jeshini, kuna bwana mmoja kutoka Mwanza alikuwa akipenda sana kuniita Teacher.. Siku moja nilipomuuliza, alinicheka na kuniambia.. “Mwalimu hata kama umekimbia chuo cha ualimu na kuingia jeshi, wewe ni mwalimu tu”..

Nilipuuza kauli ile na kuendelea na maisha yangu ya jeshi. Nikahitimu na kulitumikia jeshi hadi nilipostaafu kwa hiyari ili nifanye mambo yangu. Lakini maisha yangu yote, nimekutana na zaidi ya mtu mmoja ambao kila mara wanaishia kuniangalia sana na kuondoka bila kusema neno, au pale ninapowagombeza kwa kuniangalia ovyo!!

Sasa nashindwa kujua huyu aliyesimama mbele yangu leo ni nani hasa

******

Kikao kilizizima!

Kila mmoja mdomo ulikuwa wazi!!

Ni mtu mmoja tu ambaye alionekana kuwa na cha kusema lakini hata hivyo alikuwa na wasiwasi mwingi..

“Kwa kweli sijui kama hiki ninachokiona ndicho ama naota.. Lakini nakumbuka nilikuwa binti mwenye ufahamu wakati wifi alipokuwa mjamzito. Akiwa hospitali ambako alilazimishwa kwenda baada ya kanisa kujenga hospitali pale kijijini, kuna taarifa zilikuja kuwa wifi yetu ameleta mkosi nyumbani”.

“Tuliambiwa kuwa, amepata watoto wawili. Wazee walikusanyika na kuanza kupanga nini cha kufanya. Watoto hatukuruhusiwa kusogelea karibu na watu wazima walipokuwa wanajadili.. Lakini baadae, tulisikia kutoka kwa kina mama kuwa, watoto wale wangeuwawa baada ya kufika nyumbani” Alizungumza mama mmoja mtu mzima kabisa ingawa kwa mbali alionekana na nguvu kiasi”.

“Tulingoja wifi arudi na watoto wawili kwa kuwa hatukuwahi kuona watoto wawili wachanga kwa pamoja, lakini baadae alipokuja, haikuwa hivyo. Alikuwa na mtoto mmoja tu.. Basi ile habari iliishia pale. Sasa leo hiki nnachokona….” Alimaliza mama yule.

******

Mjadala uliendelea mpaka karibu saa sita usiku.. Ya Adolph Chiziza na Masagida Kaswalala Masalu yalikuwa pasua kichwa. Kwanza kuna saa wao wenyewe walikuwa wakibadilikiana kupita maelezo.

“Nimeuliza swali Mzee, maelezo yako ni mazuri lakini siyahitaji” Chiziza alianza

“Swali la jibu hilo ninalo, tafadhali tunza jibu lako utalitoa baadae”Masalu naye akalipuka

“Nisikilize bwana, hata wanasayansi wanasema…” Alijaribu Masalu

“Achana na wanasayansi, nisikilize mimi” Chiziza akadakia!

Hata kama wasingekuwa mapacha wa kuzaliwa, tabia zao tu zilitosha kuwaita mapacha!!

***

Mwili wa Neema ulizikwa!!

Kila mtu alikuwa akiongea lake!

Juu ya nini kilitokea hata Chiziza na Masalu wakatenganishwa utotoni hakuna aliyekuwa na haja ya kukitafuta. Ukweli kuwa jamii nyingi zamani zilikuwa na utamaduni wa kuamini kuwa mapacha ni dalili ya laana ilijadiliwa, na kukawa na uwezekano kuwa, huenda wakati wakiwa hospitali pale, mtoto mmoja aliruhusiwa kuondoka na mama yake na mwingine akabaki na kutafutiwa malezi sehemu nyingine.

Hakuna aliyetaka kujua sana. Wazee wawili wakorofi walikuwa wamekutana, na kwa mara ya kwanza kwa ndugu zao, walionekana muda mwingine wakiongea na kucheka huku wakijitenga na watu wengine.

Damu nzito kuliko maji..

Halafu sasa kuhusu damu…

Ilishatokea.. Watoto wa ndugu wawili wamekutana na kuzaa mtoto.. Ndugu wawili waliopotezana wamekutana.. Alimuradi kila mtu alizungumza la kwake. Lakini ukweli ukabaki palepale.

Hakukuwa na haja ya DNA kupima undugu wa Adolph Chiziza na Masagida Kaswalala Masalu!

Matanga yalivunjwa na taratibu za kumpa jina mtoto wa Clifford zikafanyika. Hakukuwa na jina jingine zaidi ya kumwita Neema, na familia ambayo sasa ilikuwa umeunganika na kuwa moja, ikaridhia. Taratibu zote za kimila zikafanyika. Ndugu wakaitwa na wakatambuana. Wa kupigwa faini akapigwa na wa kusemwa akasemwa.

Watoto wakakumbushwa tena umuhimu wa kufuata taratibu hasa katika mambo muhimu kama vile kuoa, wakakumbushwa ubaya wa kuamua tu kuishi na mtu pasipo kuwafahamu vema ndugu zake, wale waliokuwa wakiishi pasi na ndoa wakanyooshewa vidole na kupewa muda wa kufanya maamuzi upesi pamoja ne mengine mengi. Wazazi nao wakakumbushana yaliyowahusu. Chiziza na pacha wake wakapanga ni lini wanakwenda kuyatembelea makaburi ya wazazi wao huku Chiziza kwa mara ya kwanza katika maisha yake akiuhisi sasa uchungu hasa wa kutokuwa na wazazi.

Ni wakati huu ndipo alipokumbuka pia, pamoja na vifo vya wazazi waliomlea na kumpa jina, moyo wake ulikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuwahifadhi japo kwa kumbukumbu ya picha tu wazazi wake halisi!!

Wakaonyana na kuwekana sawa, wakapena mikono na kubadilishana namba za simu. Wakapiga na picha za familia pamoja na “selfie”.

Chiziza akarejea Dar es Salaam akiwa na Amani ya kumjua ndugu yake, familia yake na ukoo wake.

Clifford alirudi Singida na kuendelea na majukumu yake kwa muda. Moyoni mwake alishaamua kuwa, sehemu iliyobaki ya maisha yake angeitumia akiwa Singida kwa namna wakazi wale walivyokuwa faraja wakati wa dhiki kuu iliyomfikia. Ingekuwa ngumu kwake kumchukua mwanae Neema na kuishi naye, hivyo familia nzima ilikubali kuwa, Neema aende akaishi kwa shangazi yake Claritha, dada yake na Clifford mpaka Clifford atakapokuwa tarayi kumchukua na kuishi naye.

Baada ya miezi miwili tangu mkasa wa kifo cha Neema, Clifford alikuwa jijini Dar es Salaam kumsalimu Baba yake..

“Kijana… Nadhani sasa umejifunza nini maana ya ukali wangu juu ya maswala yahusuyo familia. Ujinga ulioufanya awali, na labda unaoendelea kuufanya hata sasa maana inawezekana bado hujajifunza, wa kukutana tu na mwanamke na kuzoana ulitaka kuitoa roho yako. Lakini hakuna kosa kubwa kama kuishi na mtoto wa mtu bila kutoa taarifa kwa ndugu. Unaweza kuingia matatizoni mpaka ukahisi dunia hii ni chungu..” Mzee Chiziza alieleza.

“Ni kweli baba.. Unakumbuka nilichokuambia mara ya mwisho kabla hujaja Mwanza?”

“Naam.. Nakumbuka”

“Well.. Wakati wa nyuma, sikuwa nakuelewa vizuri ulipokuwa ukizungumza kama Baba.. Lakini sasa, najifunza kuwa, nitakapoamua kuoa, sipaswi tu kuangalia kuwa ni kiasi gani niko tayari kuoa peke yake, au watu wengine wananiambia nini kuhusu kuoa.. Napaswa kujichukulia kwanza kama Mume, lakini zaidi, bila kujali iwapo nina mtoto au la, nijichukulie kama BABA!!

“Na ndio maana niliamua kukupa adhabu ili akili ikae sawa. Na ole wako urudie Clifford.. Hakyamungu nakuapia nakunyongelea mbali, mbulula weye” Ingawa aliyasema kiutani, kulikuwa na chembe za hasira katika kauli yake.

“Mzee Chizi.. Wala hujanipa adhabu.. Hii imekuwa ni zawadi kubwa sana kuipokea kutoka kwako. Umenipa zawadi ya adhabu. Zawadi ambayo imeukomaza moyo wangu na kunifanya imara. Hakika zawadi ya adhabu uliyonipa imenibadili. Ikiwa hili halijanibadili, hakuna lingine lolote chini ya jua litakalonifundisha baba angu” Alimaliza Clifford.

******

Geti kubwa la nyumba ya Mzee Chiziza lilikuwa likigongwa kwa nguvu. Haraka, Clifford alinyanyuka kwenda kufungua huku kule kukatishwa mazungumzo na baba yake kukimkera waziwazi.

“Nahisi kama Janeth ameenda kufungua, ama?” Alisema Mzee Chiziza huku naye akionekana kutamani kukaa karibu na mwanae.

“Achana na hisia mzee na rudi kwenye uhalisia, Janeth na mama wameenda mjini kitambo tu. Umekuwa msahaulifu tena?” Alisema Clifford huku akiufikia Mlango.

“Pumbavu kabisa. Clifford nitakupiga risasi we chalii. We sio wa kunijibu jibu kisanii mimi” Chiziza alisema huku akisimama kwa utani.

“Nilikuuliza swali mzee, hilo tusi ungeliweka akiba, utalihitaji baadae. Halafu sikujua kuwa nawe huwa ni msanii unayewajibu wenzako kisanii” Clifford alibamiza mlango huku akikwepa mto mdogo wa kochi aliorushiwa na Mzee Chiziza na kuelekea getini.

Alifungua mlango na kuchungulia nje.

Gari yake nyeusi ambayo mara moja aliitambua kuwa ni ile iliyopotea kihuni ilikuwa imepaki ikiwa tupu ndani, huku mtu fulani akionekana kuanza kuondoka eneo lile.

“Oyaa.. Vipi? Nani?” Aliuliza Clifford..

Mtu yule akageuka na kumtazama kwa macho yaliyolegea na kuonekana kuchoka.. Alitia huruma

Alikuwa Nunu!


*************** MWISHO***************


Mungu ni mwaminifu na kazi zake ni takatifu!

Nunu atarudi tena!!


Nakushukuru sana msomaji na msikilizaji wa simulizi hii kwa kuwa sehemu ya kazi hii tangu mwanzo mpaka kituo cha mwisho. Sijajua imekuwa ni safari ya aina gani kwako, lakini kwangu imekuwa ni neema ya nguvu ya Mungu kunipa nafasi ya kuyabadili mawazo yangu kuwa simulizi hii. Ni faraja kwangu pia kujua kuwa, huenda kuna sehemu ya maisha ya mtu fulani imebadilika baada ya kusoma au kusikiliza simulizi hii.

Ni wazi kuwa, hata nawe umejifunza jambo. Lichukue na kulihifadhi moyoni. Kama halitakufaa siku ya mvua, litakusitiri siku ya jua. Na kama halitakunufaisha katika maisha yako, ligawe kwa mwenzako, huenda likawa ni Mwanzo mpya wa maisha ya mtu mwingine.

Kwa uzito wa kipekee pia,

Izingatiwe kuwa simulizi hii ni kazi ya Sanaa. Iwapo mazingira, majina ya wahusika au mfululizo wa matukio unafanana na tulio lolote halisi, tafadhali ichukuliwe kuwa imetokea hivyo kwa bahati mbaya tu na kama matokeo ya kazi ya sanaa na wala haikukusudiwa.


TAFADHALI TOA MAONI YAKO


MWISHO


0 comments:

Post a Comment

BLOG