Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

WAKALA WA SIRI (2) - 1

  

IMEANDIKWA NA : ROBERT HERIEL

********************************************************************************

Simulizi : Wakala Wa Siri (2)

Sehemu Ya Kwanza (1)



Ndani kulikuwa na vumbi licha ya kuwa jumba lilikuwa limefungwa kwa vioo. Harufu ya uvundo kwa mbali ilizichezea pua yake, upesi akaenda kufungua mapazia na madirisha kuruhusu hewa iingie. Akaingia ndani kabisa kulipo na maktaba ya ile nyumba, akachukua kijarida kimoja chenye picha ya mtu aliyeshika ndoo ya maji pamoja na brashi. Akatoa simu akabinya binya kisha akaweka namba sikioni.

“ Hallo! Mr. Zaburi hapa, naomba mje hapa Mbezi Magari Saba kunifanyia usafi, msichelewe. Nashukuru” Sajenti akaongea na simu kisha akakata. Baada ya dakika thelasini, kampuni ya usafi ya TCS Iliwasili ikiwa na vijana wawili na mabinti wawili.Sajneti aliwapa maelekezo kisha akatoka kwenda kula kwani tayari ilikuwa imefika saa sita mchana, njaa ilikuwa imembana kwani tangu jana alikuwa hajatia kitu mdomoni..


SEASON 2 >>> EPISODE 01


“Hii simu ya Meja Venance Kagoda lazima iwe na mambo makubwa ya siri, inaweza ikawa msaada mkubwa kwangu. Lakini kwa nini Meja Venance auawe, kama hiyo haitoshi familia yake mpaka sasa haijulikani mahali ilipo, hakuna anayejua wako hai au wamekufa. Waliomuua ni kina nani; Baada ya mwili wake kuchukuliwa kwa ajili ya uchunguzi na kupelekwa katika maabara ya Boreti ukaibiwa, Who did this?” Fernanda akawaza huku akitoka katika nyumba za Meja Venance akiwa ameibeba ile simu janja aliyoikuta sirini, chumbani kwa Meja Venance. Akapanda ukutani kama mjusi, akatoa kichwa akachungulia nje kukagua usalama wa eneo la nje. Hali ilikuwa ni tulivu, giza na mwanga hafifu wa taa za nyumba za eneo lile zilimfanya Fernanda awe macho, hakuyaamini kabisa mazingira yale. Upande wa kulia aliliona gari lake alilokuwa ameliegesha, akatazama kwa kitambo akiwa bado amening’inia juu ya ukuta; akaona hali ni shwari. Akaruka kwa nje. Akasonga kulifuata gari akiwa mkononi kaishika bastola vizuri. Kila alipopiga hatua tano aligeuka huku na huku kuangalia usalama mpaka alipolikaribia gari lake. Akasimama, akaangalia alipotoka kisha akaangalia saa yake ya mkononi iliyomuonyesha ilikuwa saa saba za usiku. Fernanda hakutaka kupoteza muda akabonyeza rimoti ya gari, mlango ukafunguka akatoma ndani. Akaitoa ile simu janja, kisha akajaribu kuiwasha lakini ikagoma kuwaka,


“ Itakuwa haina chaji, nikifika nyumbani, nitaichaji kisha niikague, mbona akili yangu inanituma kuwa ndani ya simu hii kuna mambo mazito ya siri. Nafikiri itakuwa hivyo, maana hata ilipofichwa lazima itakuwa na jambo zito la siri.” Fernanda akajiwazia huku akiirudisha simu mfukoni. Alafu akawasha gari lakini kabla hajaweka gia alishtushwa na kitu kigumu kikigusa kisogo chake, na kabla akili yake haijampa cha kufanya, sauti nzito isiyomzaha ikasema;


“ Tulia hivyo hivyo, usijitingishe wala kufanya jambo lolote, nisije nikapasua bichwa lako” Yule mtu akaongea kisha akameza mate alafu akaendelea;


“Weka mikono yako juu…..”


“ Wewe ni nani, unashida gani na mimi??” Fernanda akamkatisha huku akiweka mikono yake juu.


“ Kaa kimya! Ukithubutu kufungua mdomo wako nitakichangua kichwa chako. Fuata maelekezo” Yule mtu akasema, sauti yake ilikuwa ikitokea nyuma ya kisogo cha Fernanda, ilikuwa sauti iliyomfanya Fernanda achore picha ya mwanaume jeuri mwenye sura ya kikatili, ilikuwa sauti nzito na mbaya. Fernanda akakaa kimya akisubiri maelekezo, kitambo kidogo kilipita pakiwa kimya hali iliyomfanya Fernanda atake kugeuka nyuma ili amuangalie mtu Yule. Alipogeuka bahati haikuwa yake, akakutana na kitu kizito kilichompiga usoni, Fernanda akaanguka na kupoteza Fahamu.


****************************************************************




Taa zilikuwa zikiwaka katika ghorofa ya nane katika jengo hili. Lilikuwa jengo refu la ghorofa zisizopungua kumi na tano. Pamoja na kuwa ilikuwa usiku wa manane lakini ndani ya jengo hili kulikuwa na kikao kizito kilichokuwa kinaendelea. Watu kumi walikuwa wamekaa kwenye meza yenye muundo wa Herufi U “U-Shape Style” Wote walikuwa wamevaa suti maridadi zilizokuwa zimewakaa vyema. Kiongozi wa kikao hiki cha siri alikuwa amekaa amevaa suti ya kijani uso wake ukiwa nyumba ya miwani ya macho.


“ Mipango yetu imesimama, kila mmoja wetu anafahamu sababu ya kusimama kwake, inaweza kuwa ni uzembe wa baadhi yetu humu, kama sivyo, leo hii tungekuwa tumeshafika mbali. Inashangaza kuona mpaka muda huu tumedorora, tupo katika mdororo, tangu kiungo wetu muhimu auawe na hasimu wetu mambo yetu yamesimama kama sio kurudi nyuma, tulifanikiwa kuiba mwili wake katika maabara ile, najaribu kufikiria kama tusingemuwekea IN-BODY GPS iliyotusaidia kutoa taarifa ya mwili wa Meja Venance Kagoda ulipo, tungepata kazi ngumu na yaziada kujua ulipo mwili wa ndugu yetu. Kazi hii aliifanya Adele kwa weledi mkubwa kabisa” Yule mtu akasema kisha akameza funda la mate, akamgeukia mwanadada mmoja aliyevalia suti ya kijibu iliyomkaa vyema.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG