IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA
********************************************************************************
Simulizi : Shilingi (Mwanzo Kati Na Mwisho)
Sehemu Ya Kwanza (1)
Alikuwa wa kwanza kuyafumbua macho yake, tayari nuru ilikuwa imeanza kuchukua hatamu.
Akamtazama mwanamke ambaye alikuwa bado katika dimbwi la usingizi, licha ya kuwa katika kifo hicho cha muda, bado aliweza kuupa kazi maalum mkono wake wa kumlinda mtoto ambaye alikuwa usingizini. Ukimuita hakusikii lakini mtoto akinyanyuka tu, upesi anamdhibiti huku akiwa ameyafumba macho yake.
Mtoto ni wa mama hakika.
Macho ya kijana yule mfupi yakazunguka huku na kule katika chumba, kisha yakarejea tena kwa yule mwanamke aliyesinzia.
Akairuhusu akili yake kujifikirisha iwapo amewahi kukutanana mfano wa mwanamke yule, mwenye mvuto wa wastani aliyeamua kumchagua yeye tu na shida zake zote. Alimpenda akiwa katika shida, wakajipa tumaini kuwa haipo shida ya kudumu ulimwenguni, ipo siku yatawanyookea.
Mambo hayanyooki na bado mwanamke yule haonyeshi kuchoka.
Fikra zikagota kitanda kilipopiga kelele baada ya mtoto aliyekuwa katika himaya ya yule mwanamke kujinyoosha. Akakitazama kitoto na mama yake.
Akatabasamu!
Mbu walikuwa wametanda kwa wingi nje ya chandarua kilichokuwa kimetawaliwa na mafundo fundo sehemu ambazo zilikuwa zimechanika, ni kama waliokuwa wanamshutumu bwana yule kwa kuwanyima ridhiki yao stahiki.
Damu!
Madirisha yalikuwa na vipande kadhaa vya nondo, visivyohitaji utaalamu mwingi ikiwa mtu atahitaji kuving’oa ili aingie ndani pasi na matakwa ya wenyeji.
Nani?
Mwizi?
Aingie kuiba nini?
Taratibu akafunua chandarua kile na kutanguliza miguu yake kisha mwili uliobakia ukajumuika.
Akazituliza nyayo zake katika viatu vyake vilivyotengenezwa kwa kutumia vipande vya tairi.
Akainuka na kukiacha kitanda kikipiga kelele zake za siku zote.
Akauendea mlango, akabandua kinu kikubwa kilichokuwa kinauzuia mlango usifunguke, akakiondoa.
Mlango ukabaki wazi, akajinyoosha mwili wake huku akitoka nje.
Huko akakutana na salamu za hapa na pale kutoka kwa majirani ambao tayari walikuwa katika hekaheka za alfajiri.
Alitembea taratibu huku akiipekecha mikono yake ili kujitengenezea joto la asubuhi.
Takribani kilometa moja, hali ikiwa ile ile. Kujuliana hali na wapita njia.
‘Habari! Njema!, kwema?.. kwema ndugu’
“Habari za muamko bwana Kindo!” salamu hii ilimlazimu kusimama, msalimiaji alijiandaa kumpatia mkono wa heri, huku akilitaja jina lake.
“Salama bwana!” Kindo akajibu kivivu huku akimtupia mkono.
“Mguu huu ni wako!” Akazungumza yule bwana wakiwa bado wamepeana mikono.
“Ukate basi niondoke nao kabisa! Ni fahari kuwa na miguu mitatu ati!” Kindo akafanya mzaha huku akijaribu kutoa cheko.
Bwana yule hakucheka, hata hakutabasamu.
“Hali ya Bi. Sikununu sio nzuri, hapa ameniagiza nikufikie na hizi taarifa. Mungu si Athumani na wewe huyu hapa.” Akatoa maelezo yale, tayari wameachanisha mikono yao.
“Nini tena cha mno. Mgongo au?” Akajaribu kubashiri.
“Kindo, mama yako anaumwa sana.” Sasa alizungumza kwa msisitizo.
Kindo hakuuliza swali tena, akaondosha viatu vyake miguuni akaanza kutimua mbio. Mwenda kwao si mtumwa.
Kindo hakuhitaji kuelekezwa. Mfikisha ujumbe hakuambatana naye.
Mama sakafuni!
Chumba kinatoa harufu kali.
“Mama!!... Bi. Suku!” Kindo akaita.
Mama anaona lakini hasemi, anatapatapa.
Kindo hana cha kusubiri, anamtwaa mama yake. Anamtupa mgongoni. Anatoka naye nje, kutazama kama kuna lolote anaweza kufanya.
Atokee wa kumsaidia?
Hakuna, wanamtazama tu....
Kila mmoja anahangaika na jambo lake.
Ilikuwa heri yeye mwenye mama, wengine waliwazika kitambo kirefu.
Wakalitazama tatizo hili kana kwamba ni dogo tu.
Kindo akabaki kuhangaika na mama yake.
Hangaiko ambalo lilizifanya nyakati kuchukua utawala, nyakati hizi zikimuamlia Kindo wapi pa kwenda na nini cha kufanya.
Ama! Nyakati zikampeleka Kindo mahali asipopatarajia.
_________________
YALIBAKI kuwa maisha yao, ya huyu yana afadhali kuliko ya yule kwa siku ya leo. Kesho yake yote yanafanana. Hawachekani hawanuniani, hakuna wa kumsaidia mwenzake linapotokea tatizo.
Serikali ni kama ilikuwa imekisahau kijiji cha Ulongoni, walitambua uwepo wake kimaandishi lakini sio kwa vitendo.
Vijiji vilikuwa vingi, viongozi walijawa na tabia ya kupuuzia. Wakapuuza Ulongoni.
Kilimo kiliwatunuku chakula kidogo, ufugaji ukawabariki na kitoweo japo mara mojamoja.
Thumni na shilingi zikawa nguzo kuu ya kipato cha bahati, vijana, wazee, akinamama wote waliishi katika maisha ya kuchimbachimba. Wanaitafuta sarafu ya thumni ama shilingi ambazo zilikuwa hazipo katika matumizi tena katika mzunguko wa fedha.
Lakini bado zilihitajika kwa udi na uvumba, waliokuwa wanazihitaji walitambua matumizi yake. Wachimbaji hawakuambulia kitu.
Wanachimbachimba tu!
Hawajali kuhusu elimu, ni wachache wanaojua kusoma na kuandika. Lakini hii haiwafanyi kuwa bora kuliko wasiojua kusoma na kuandika.
Kindo akiwa mmoja kati yao!
Hajui kusoma wala kuandika na maisha yanaendelea hivyohivyo. Hata angejua kusoma bado yangebaki kuwa kama yalivyo.
Ukiipata thumni utafunga safari hadi katika makao makuu ya wilaya kukutana na walanguzi.
Watainunua kwa bei ya kukulalia huku wakilalama kuwa soko lake linashuka kwa kasi.
Ukiondoka wanakuzomea.
Wanajiondokea na kwenda katika makao makuu ya mkoa, huko watauza thumni ile kwa walaji wa daraja la kati kwa kipato kinachoridhisha.
_______________
Kindo, alijiona kama asiyekuwa na bahati. Kila kona ya dunia aliyoifahamu aliona ikimzomea. Akipita njia ile atayavuka mashamba yanayomilikiwa na baba wa mke wake, atamkwepa baba lakini mara atakutana na mama.
“Mwanangu huoni soni kuishi na mwanamke hujamtolea hata senti?” Mama mkwe atamdhihaki huku akikataa kujibu salamu yake.
Atajaribu kukumbuka ni ahadi ipi hajawahi kuitoa, atagundua kuwa tayari alikwishatoa ahadi zote pasi na kuzitimiza.
Atabaki kusimama, mama mkwe atampaka matope kisha ataondoka akimwachia burudani ya msonyo mrefu.
Kindo atautamani muujiza. Akihitaji walau ushauri atajaribu kukimbilia katika nyumba ndogo ya ibada katika kijiji chao cha Ulongoni. Huku hataupata usikivu wa kiongozi wa kiroho.
Amsikilize angali hatoi sadaka?
“Kindo, Mungu anawasikiliza wanaojitoa kwa ajili yake. Hajibu maombi ya watu wanaotega tu mkono wao hawatoi. Mimi nakuomba usipoteze muda wako kutarajia muujiza wakati hutoi chochote kwa mtumishi wa Mungu.” Atatemewa cheche hizi huku anatazamwa moja kwa moja usoni.
Atarejea nyumbani mikono mitupu, mke na mtoto wanampokea kwa shangwe. Mkewe ana umri mdogo lakini ni jasiri na mwenye nguvu.
Tayari ameivisha chakula. Mboga ameitoa maili nyingi kutoka katika kijumba kilichowastri, safari ya kutafuta mboga hakumwacha mtoto wao nyuma. Alimbeba mgongoni, mama mgonjwa alimuacha chumbani baada ya kuwa amemuogesha na kumchemshia uji usiokuwa na sukari.
“Chakula tayari mume wangu mpenzi!” sauti tulivu ya kike itamkaribisha.
Nafsi inafadhaika, anamtazama binti yule.
Ananionea huruma tu! Anajisemea.
Atakuwa hivi mpaka lini? Anajiuliza.
“Hali ya mama sio nzuri mume wangu!” Nyangeta anamweleza Kindo wakiwa wamemaliza kula.
Kindo anashusha pumzi zake kwa nguvu. Minyoo inaunguruma tumboni kana kwamba imekerwa na taarifa ile.
“Sasa tunafanyaje?... mke wangu!” nd’o kitu pekee anaweza kuchangia, Kindo.
“Mzee Ugwadu amenielekeza dawa ya kienyeji, amesema ina nguvu zaidi kulikoni dawa za huyo daktari wa kijiji.”
“Aaah! Ametufariji tu mke wangu, dawa ya kienyeji iwe inatibu kuliko ya daktari wa kijiji, watu wasingeweza kumnyenyekea kiasi kile.” Kindo anamjibu mkewe huku akiwa anapoteza tumaini.
“Ilimradi dawa hiyo haiui, basi tutaenda kuichimbua. Kesho alfajiri, huwezi kujua pasi na kuthubutu.” Kauli ya Nyangeta haikuwa inahitaji majadiliano ya ziada.
Kindo alimfahamu vyema, ni mfupi wa kimo kuliko yeye, hana mwili mkubwa na bado umri wake ni mdogo. Lakini alikuwa na kasumba moja.
Akilitaka lake liwe liwakuwa tu!
Na mara zote ilikuwa ni kwa manufaa ya familia kwanza.
Kindo akapita katika chumba cha jiko ambacho alikuwa anakitumia mama yake kulala, akamtazama na kufanya dua fupi kisha akaondoka kwenda kulala.
Alfajiri sana Nyangeta akamkurupusha, tayari alikuwa ameuchemsha uji kwa ajili ya mama, akauacha jikoni. Akamnywesha mtoto wao uji, kisha akamkurupua Kindo kwa ajili ya safari.
Haukuwa mwendo mfupi, Kindo alitamani kulalamika. Lakini aibu iliyoje, binti anauchapa mwendo na alikuwa na shughuli za kufanya asubuhi, wewe mwanaume uliyekurupushwa tu na kukutana na uji vikombe viwili vikubwa uanze kulalama.
Akajikaza!
Wakalifikia pori ambalo Nyangeta alikiri kuwa ndipo alipoelekezwa.
Wakaanza kuitafuta ile dawa, wakakata mti huu Nyangeta akajaribu kunusa na wakati mwingine kulamba kidogo.
Haikuwa yenyewe wakaendelea kutafuta.
“Nyangeta mke wangu!” Ghafla Kindo akamuita mkewe. Nyangeta hana kasumba ya papara, akageuka na kuitika ‘rabeka’.
“Njoo Nyangeta wangu! Njoo upesi mke wangu” Kindo akapiga kelele, sauti yake inaufanya mwangwi!
“Shilingi ya ajabu mke wangu.” Akasema huku akiwa anatetemeka akakifungua kiganja cha mkono wake.
Nyangeta akajikaza asishtuke. Lakini moyo wake ulipiga kwa jitihada zote.
“Tazama kichwa cha Nyerere kimegeukia kushoto!! Ni hii mke wangu, tumetajirika sasa... tumeupata utajiri.” Alizungumza kwa hisia za furaha zilizochanganyikana na taharuki.
“Achana na hizo dawa za mitishamba, tutaiuza pesa nyingi hii shilingi, tutamlipa daktari wa mkoa atakuja kumtibia mama. Achana na yule daktari wa kijiji mwenye nyodo...” Kiganja kinatetemeka. Nyangeta hana la kusema bado amepigwa butwaa.
Ni kweli ilikuwa ile shilingi iliyotajwa na mababu zao, waliisifia angali hawakuwa wamewahi kuiona hata wao walisimuliwa na wakoloni.
Wakahenyeshwa kuyafyeka mashamba, wakaiharibu misitu wakiitafuta hiyo shilingi ya ajabu.
Shilingi ambayo ilitengenezwa kwa madini ambayo baadaye yalitoweka kabisa duniani.
Shilingi nyingine zilichovywa kiduchu katika madini hayo. Nd’o maana thamani yake haikuwa kubwa sana.
Lakini shilingi ambayo kichwa cha mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilikuwa kinaangalia kushoto badala ya kulia ilikuwa ya kipekee.
Na ilitengenezwa hivyo kwa sababu maalumu.
Kuwalaghai watanganyika kuwa zote zinafanana ili baada ya kuupata uhuru wao basi wakoloni wakiingia nchini wanazikusanya zile sarafu na kutoweka na madini.
Mpango ukafanikiwa!!
Jumla ya shilingi nane tayari zilikuwa zimepatikana na zilikuwa zimesalia sarafu mbili pekee.
Hii hapa moja mkononi mwa Kindo.
Utajiri katika kijiji cha Ulongoni.
_________
Atakupeleka wapi huyu?
Hana uwezo hata wa kulipa mahari yako?
Ananuka umaskini, ataisambaza harufu hata kwa watoto wako.
Tazama anakuzalisha, mtamtunza vipi huyu mtoto.
Umelaaniwa wewe!!
Kauli hizi ni kama zilizikwa na sasa zimefufuka ghafla kutoka katika kaburi la fikra za Nyangeta.
Hawa waliomsemea hawa wakatakiwa kuwa wa kwanza kabisa kuipokea taarifa juu ya Kindo kuipata shilingi ya ajabu.
Mhh!
Hawaamini.
Wakashikana mikono familia nzima hadi kitoto kichanga, safari kuelekea nyumbani kwa Kindo.
Huu ukawa mwanzo wa habari hii kusambaa kwa kasi ya ajabu kuliko ilivyosambaa habari ya mama yake Kindo kuugua, na kubebwa katika mgongo wa Kindo hadi kukifikia kibanda chake.
Akahifadhiwa jikoni, akiwa wa kula na kulala tu.
Kila mmoja anaitilia maanani habari hii na kujaribu kujiweka katika namna ipi ambayo ataweza kunufaika nayo.
Wale marafiki waliokuwa wakikutana kijiweni waliamini fika kuwa katika maisha yake ya kifahari Kindo hatawatupa, hatakuwanao karibu tena, lakini hawezi kuwaacha patupu.
Masikini akifanikiwa husaidia kwanza maskini wenzake! Wakabaki na kauli hii.
Wale walanguzi wa shilingi, ambao mara zote walitandika miguu yao katika vijumba vyao vya ofisi na kuwangoja wanakijiji waliobarikiwa kuokota shilingi wawapelekee huku wakijiandaa kuwadhulumu.
Wanaifanya dhuluma lakini wao hawataki kudhulumiwa na walanguzi wakubwa.
Sasa kila mmoja aliyeipokea habari hii ya shilingi ya ajabu kuokotwa katika kijiji cha Ulongoni. Mawazo ya kuendelea kubaki miguu juu ofisini yakapotea.
Kila mmoja akatamani kuwa wa kwanza kuzungumza na Kindo kuhusu hiyo biashara.
Hawakutarajia kupata mteremko tena kama inavyokuwa katika shilingi za kawaida ambazo kichwa cha mwalimu Julius Nyerere, kinaangalia kuume.
Bila kutamkiana, mmoja mmoja akatoweka ofisi ikabaki tupu. Wakaingia mawindoni.
Sarafu ya ajabu haitakufuata ofisini! Ni kama walijisemea.
Yule kiongozi wa kiroho aliyekuwa anamlalamikia Kindo kuwa hatoi sadaka hivyo hawezi kubarikiwa, akajisahaulisha yote ambayo aliwahi kumnenea bwana yule.
Akafikiria kujiweka karibu naye na kumuongoza katika sala mbalimbali za baraka kisha amtolee ushuhuda wa kumwongoza wapi na lini anapaswa kuiuza shilingi ile ya ajabu.
Na ikiwezekana atamwonyesha kuwa maandiko yanadai kuwa amkabidhi yeye ndiye atakayemtunzia. Akifanikiwa katika hilo atamtafuta mteja. Ataiuza na kumpatia Kindo kiasi cha fedha naye atachukua kiasi kikubwa.
Ataondoka katika kile kijiji na kufungua kanisa lake katika miji ambayo atanufaika na sadaka kutoka kwa waumini. Sio hawa wa kijiji cha Ulongoni wasiotoa sadaka.
Ugonjwa wa mama yake Kindo ambao hata Kindo alikuwa haujui majina yake tayari ulikuwa unafahamika kwa daktari wa mkoa.
Daktari ambaye katika maisha yake yote hakuwahi kukifikia kijiji cha Ulongoni, alikuwa anakisikia tu!
Lakini sasa yupo tayari kwa safari hata kama ni usiku wa manane. Na tayari aliutanguliza msafara wa wasaidizi wake katika kijiji cha Ulongoni. Nia ya wazi ikiwa ni kumtibu mama yake Kindo.
Ajabu! Daktari wa mkoa awe na nia ya dhati kumtibu mama wa kijana maskini asiyekuwa na ramani yoyote ya kimaisha?
Inafikirisha!
__________
Mkuu wa wilaya aliipokea habari ile akiwa anafurahia maisha katika mikoa mingine.
Ratiba zote zikahairishwa!
Akajitengenezea ziara ya kukitembelea kijiji cha Ulongoni. Akiita ziara ya kikazi.
Kazi gani ya ghafla kiasi hicho?
Washauri wake wakampatia silaha mbili tatu za kumteka Kindo.
Akazisikiliza, akazikariri bila hata kuzipima akakiri kuwa ni silaha tosha kabisa.
Akalikariri jina Kindo vyema kuliko kiapo alichokikariri wakati anaapishwa.
________
Walanguzi wakubwa waliisikia hii taarifa kutoka kwa madalali wa shilingi na thumni. Wakaipokea kwa kuipuuza, lakini ilipozidi kuwavumia wakaamini.
Kabla wajanja hawajaidaka ile shilingi ya maajabu, wakaamua kuwahi biashara kule kijijini, wa kubeba gunia la pesa wakabeba, wale wa kubeba mali za kubadilishana wakajitwisha.
Ndani ya muda mfupi sana, kijiji cha Ulongoni kikapata ugeni mkubwa sana.
Hapakuwa na nyumba za kulala wageni, hivyo kwa wazawa ilikuwa fursa ya kipekee. Vinyumba vyao visivyopendeza machoni, vilikodishwa kwa wageni waweze kulala, wao walilala nje.
Kijiji wanakijua, hakiwatishi ilimradi tu wamelipwa pesa ambayo hawakuwahi kuimiliki hapo kabla.
Ulongoni kumekucha!
Kiongozi wa kiroho alikuwa wa kwanza kufika nyumbani kwa Kindo, alipishana kidogo sana mchomozo wa jua.
Aliongozana na waimba kwaya wote waliokuwa wanalivumisha kanisa lake dogo. Walivaa zile sare zao ambazo huzitinga pindi wanapofanya ziara ya kwenda kutoa huduma wilayani.
“Amani ya bwana itawale eneo hili.” Alisalimia kwa bashasha huku akimwaga maji ambayo yanaaminika kuwa yana Baraka ndani yake, na ulihitajika kufanya malipo uweze kuyapata.
Maji yanayoweza kuwafukuza wachawi, yanafukuza dhiki na magonjwa pia yanavuta utajiri na kukuheshimisha katika jamii.
Walioyatumia walihifadhi masalia ya heshima kwa kiongozi yule. Lakini mioyoni mwao walikiri kuwa hayakuwa na maajabu hayo yanayotajwa.
Kiongozi yule kwa kutambua kuwa nyoyo za wateja wake zimekunjamana, alihubiri kwa maksudi juu ya imani dhaifu.
Akaongezea kuwa pasi na kuwa na imani, basi hakuna lolote linaweza kuwa la neema kwako.
Wanunuzi kila mmoja kwa wakati wake akajipima imani yake.
Haba!
Leo hii inakuwa siku ya maajabu! Maji yale yanamwagwa hovyo nyumbani kwa Kindo ambaye hajalipia hata senti moja kwa ajili ya huduma ile.
“Mama yetu mpendwa yupo wapi?” Kiongozi wa kwaya aliyejitahidi kuvaa katika hali ya unadhifu zaidi aliuliza. Wakati huo mkungu wa ndizi ukitangulizwa katika eneo lililokuwa linatumika kwa ajili ya kupikia chakula.
Majirani macho kodo! Wanausindikiza ule mkungu wa ndizi, ilikuwa nadra sana kuona vitu kama hivi katika kijiji cha Ulongoni tena katika nyumba ya kijana maskini, Kindo!
Hata Kindo alistaajabu.
“Siku ile ulinielekeza juu ya ugonjwa wa mama yako mzazi. Sikuweza kukujibu palepale.... sisi watu wa imani tunapaswa kumshirikisha mwenyezi Mungu, na kama ilivyoandikwa kuwa Mungu wetu hakawii wala hawahi kutoa majibu, yeye hufanya yake kwa wakati sahihi. Jana usiku mama yako amenijia katika ndoto. Unaweza kujiuliza baba amejuaje kama mama hayupo kijiji cha tatu badala yake yupo hapa. Nimeonyeshwa! Nimemuona mama ni kiasi gani anahitaji huduma ya kiroho. Lakini huduma ya kiroho pekee haitoshi, mama anahitaji kupata chakula kizuri, wanakwaya watamuandalia chakula kizuri siku hii ya leo kisha wqatafanyiana zamu kuendelea kumuhudumia” Kiongozi wa kiroho akazungumza kwa ubora wake uleule, kuzungumza bila kupumzika huku akirusha mikono yake huku na kule.
Baada ya kuweka kituo anachukua kitambaa chake na kujifuta matone ya jasho yaliyounda vinundu vichache katika paji la uso wake.
“Ameen!” wanakwaya wawili wakalipuka kwa shangwe la ghafla, mwingine anapiga vigelegele.
Wanashangilia namna yake ya kufuta jasho?
Hayo ni yao, yaache kama yalivyo!
Kindo ametulia tuli! Anamfikiria mtumishi yule ambaye aliamini kuwa hawapo daraja moja, na siku zote Kindo aliwahesabu watu wa sampuli hii kama mabepari.
Kindo alikuwa akiishi kwa jasho kwelikweli lakini mtumishi yule aliishi kwa sadaka ya wanakijiji masikini. Jasho pekee lililomtoka nd’o hilo alilolifuta na kushangiliwa.
Mdhalimu mkubwa! Kindo alimtazama kwa jicho hilo.
Lakini pia uwezo wa mtumishi yule kujua kusoma na kuandika lilikuwa jambo jingine lililomtikisa Kindo. Akatamani walau angekuwa na uwezo wa kawaida tu wa kusoma, walau basi angekikamata kile kitabu cha kiimani na kukisoma kwa utulivu.
Yawezekana anatudanganya tu! Alijisemea na akili yake ikaruka maili nyingi kutoka pale, akafikiria juu ya sarafu yake.
“Nikishaiuza, nitahakikisha Moracha anaenda shule, atajua kusoma na kuandika na katika uzee wangu nitamuomba anisomee kile kitabu cha mtumishi, aniambie kimeandikwa vitu gani?” wazo likampitia, akatabasamu kisha akasema ‘Amen’ kana kwamba alikuwa pamoja na bwana yule.
Majirani hawaendi tena katika mihangaiko yao, kila mmoja anafuatilia hatua kwa hatua juu ya nyendo za waliyemuona kama tajiri mtarajiwa, ‘Kindo’.
“Acha tumuangalie mara ya mwisho mwisho, huyu hakai nasi tena hapa, anaenda kujenga ghorofa huko mjini, marafiki zake ni wakuu wa wilaya, watendaji wa kata na matajiri wenzake.” Mama mjane alijisemea huku akiitandika kanga yak echini na kuketi.
Rasmi kwa ajili ya kumuangalia Kindo.
Hivyo tu!
“Ataenda kuongeza mke wa mjini, ataoa wake watano wamzalie watoto wawili kila mmoja, atakuwa na watoto kumi wenye afya tele na anawahudumia vizuri, natamani angekuwa amemuoa binti yangu. Asingeondoka kijijini bila kunijengea nyumba nzuri isiyovuja maji, nyumba ambayo kila mwanakijiji angetamani kuishi humo. Nami nisingekuwa na choyo, ningewakaribisha haki ya Mungu!” Akaapa kwa hisia kali mama mwingine. Binti yake aliyekuwa pembeni akabaki kujifinyafinya, anatamani maono ya mama yake yawe kweli.
Anajutia kimyakimya kujiweka mbali na Kindo angali akiwa kapuku mbele na nyuma.
Yaani hata salamu tu! Hakuwahi kumpatia.
“Labda angenitazama hata kwa uchache katika mgao wa mapesa mengi atakayoyamiliki!” Akajisemea huku moyo ukileta aina fulani ya maumivu yaliyotekenya kisanduku kinachohifadhi machozi. Akainama na kuanza kulia.
Anamlilia Kindo.
“Wenye pesa wataiona mbingu kwa urahisi sana....” Kijana mmoja katika kikundi kingine akazungumza, watu walivyompa umakini wao akaendelea, “Mchungaji huyuhuyu alitueleza kuwa tajiri ni ngumu sana kuuona ufalme wa mbingu, lakini huyuhuyu tena amekuwa wa kwanza kumtembelea tajiri Kindo! Ni kipi alichotufundisha sasa?” akaishia katika swali.
“Wewe ungekuwa mchungaji ungejikausha usimtembelee tajiri, tazama kwa ziara hii moja anaweza kuwekewa paa katika eneo lake la ibada, labda hata akanunuliwa baiskeli mpya akaachana na karaha ya kuziba pancha kila baada ya ibada.” Kijana mwingine akauliza huku akiacha mswaki wake wa mti uwe kama kiongozi cha maongezi yake.
Wakatikisa vichwa kukubaliana kuwa hata kama ni wao wangekuwa katika viatu vya mtumishi yule wangefanya safari kwenda kwa Kindo.
___________
“Baada ya kufika hapa naambiwa na mwanakwaya wangu juu ya habari ya sarafu ya ajabu? Ni kweli umeiokota ama ni maneno yamezagaa ghafla?” Mtumishi akahoji kama asiyejua lolote.
Kindo akaitoa kibindoni sarafu ile, ilitaka kufanana na zile sarafu nyingine lakini kasoro moja tu, hii ilikuwa nzito na kichwa cha aliyekuwa raisi wa wakati huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilikuwa kimetazama kuume.
Mtumishi akaunyoosha mkono wake, akaipokea sarafu ile, anajikaza kuficha hisia zake za kutetemeka lakini hawezi.
“Hakika hii ni sarafu ya ajabu!” kauli ikamtoka. Anameza funda la mate, anatafuna hewa tupu!
“Shetani hujitokeza wakati huu, huu ni wakati ambao Mungu humfungua minyororo shetani na kumwelekeza wapi pa kwenda kushambulia. Sasa ameelekezwa kukushambulia, hakuna wakati unahitajika kuwa karibu na wanaomjua Mungu kama sasa. Unahitaji kukomazwa kiroho ili shetani akijaribu kukupiga akute ngome yako ipo imara sana.” kiongozi yule wa kiroho alizidi kuzungumza, jasho linamtoka na kila mara koo linamkauka anameza mate.
“Tumeelewa baba! Na tutakutegemea sana.” Nyangeta, mke wa Kindo anamjibu kwa utulivu wa hali ya juu sana, huku akionyesha dhahiri kumnyenyekea.
Mtumishi anatamani Kindo amuachie sarafu ile lakini Kindo tayari ameirejesha Kibindoni.
“Kindo mwanangu,” anamuita kwa upendo.
“Naam!”
“Hata iwe usiku wa manane, ukihitaji msaada wangu usisite kunifikia nyumbani kwangu. Mke wangu na watoto wote wanafahamu juu ya maono niliyopata, watakupokea na wataniamsha..... usikubali wasiomcha Mungu wakakufundisha njia gani za kupita, watakupitisha katika miiba yenye sumu, na wakati huo hautaweza tena kutembea kuifuata njia salama. Na milango ya uzimani itakuwa imefungwa!” Mtumishi akasisitiza, Kindo akatikisa kichwa kuwa ameelewa. Mtumishi akaondoka akifuatana na wanakwaya wake.
_________________
“Alichokisema mtumishi ni sahihi Kindo, watakujia watu wengi. Unapaswa kuchagua nani wa kumsikiliza, nani wa kumpuuza na nani wa kumkwepa kabisa.” Nyangeta aliyaendeleza mazungumzo, sasa akiwa yeye na Kindo.
“Na ninaamini vipi kuwa huyu aliyekuja sasa ni sahihi kumsikiliza ama anafaa kupuuzwa?” Kindo akahoji.
“Kindo mume wangu, amezungumza nawe huku ameshika kitabu cha uzima na bado haumuamini, unataka kumwamini nani?”
“Umewahi kukisoma hicho kitabu?” Kindo akamuhoji kwa utulivu.
“Sijui kusoma!” Nyangeta akamjibu
“Na bado unakiita kitabu cha uzima....” Kindo akauliza katika namna ya kumsuta mkewe.
“Unataka kumaanisha kuwa haukiamini? Kindo mume wangu, tayari shetani amefunguliwa minyororo, ameikamata akili yako na sasa haukiamini kitabu ambacho tumekiamini tangu tukiwa watoto wadogo...” Nyangeta akalalama.
“Nakiamini mke wangu, lakini nimehoji tu. Na hata nilipokuwa na mtumishi niliwaza juu ya mwanetu, baada ya kuiuza sarafu hii aje aende shule ajifunze kusoma. Siku moja atusimulie uhondo wa kitabu cha uzima.” Kindo akamfariji mkewe.
Nyangeta akatabasamu, kisha akaenda jikoni akarejea na sahani lililosheheni ndizi zilizopikwa na kuungwa kwa mafuta, nyanya na kitunguu.
Uhondo!
Mara ya mwisho kula pishi la namna hii, walikula kwa harufu tu, siku ambayo mtoto wa daktari wa kijiji alipokuwa anaagwa anakwenda shuleni.
Leo wanakula na kusaza!
Hata mama mgonjwa alichangamka sana.
Amakweli hata shibe lilikuwa ni tatizo.
Barabara zilikuwa mbaya kiasi kwamba gari waliyofika nayo kijijini hapo haikuweza kuhimili vishindo vyote.
Ikiwa imepakia jumla ya watu sita. Wakiwemo daktari wa mkoa pamoja na mkuu wa wilaya ya Hekaya.
Wilaya ambayo ndani yake kuna vijiji vingi, kikiwemo hiki cha Ulongoni ambacho kwa mara ya kwanza katika miaka yake mitatu ya kuwa mkuu wa wilaya alikuwa anakitembelea.
Dereva alikuwa anajaribu sana kuwa makini kuyakwepa mashimo, atafanikiwa kuzivuka kilometa kadhaa, mara atakutana na bonde la ghafla.
Kuuh! Analivaa na gari inazimika hapohapo.
Matengenezo yanachukua dakika arobaini na tano hadi sitini, mkuu wa wilaya anafoka lakini dereva halioni kosa lake. Hawezi kujitetea, anayapokea malalamiko ya muheshimiwa kwa nidhamu.
Wanapanda garini tena, limetengemaa tayari, linatembea nusu kilometa tairi linajichoma katika jiti lililochongoka vizuri na limejipweteka katika usawa wa barabara.
Paa!
Pancha.
Safari hii wote wanalazimika kuwa mafundi, mkuu wa wilaya anavua koti lake la thamani na kulitandika chini, hekaheka za kubadilisha tairi inachukua nafasi.
Zoezi linahitimishwa kwa jasho kumtiririka kila mmoja. Mkuu wa wilaya anamlaumu mwenyeji wao kuwa hakuwaeleza kabla juu ya ubovu wa barabara ile.
“Sijawahi kupanda gari kuja huku, nisingeweza kujua” anajitoa hatiani.
Mkuu wa wilaya anabaki kuhuzunika, daktari anamgawia dawa za kutuliza maumivu.
Mara wanakutana na bwawa, wote wanashuka ili kujadiliana. Daktari anasahau taaluma yake haihusishi somo walau moja la mambo ya usafiri wa ardhi wala wa anga anajaribu kuyakaribia maji yake anavua kiatu chake cha mguu wa kuume, anaingiza mguu mmoja kwa kunyatia.
“Pafupi sana hapa, uoga wenu tu. Gari ina ‘Fo-wili draivu’ mbona inapita bila tatizo.” Wanaomsikiliza wanaiheshimu taaluma yake ya utabibu wanaamini kuwa hata masuala ya barabara pia alifundishwa kama somo la ziada na akalibukua kisawasawa.
Twende! Wanakubaliana, dereva anaushika usukani.
Twaaa!
Wanatitia.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment