Simulizi : Zawadi Ya Adhabu
Sehemu Ya Pili (2)
Historia wanaandikiwa washindi tu! Hakuna historia yoyote ya waliowahi kushindwa. Daudi alipigana na Goliathi, akamshinda, na historia yake ikaandikwa kwa usahihi kuanzia Mwanzo mpaka mwisho. Hakuna anayeijua historia ya Goliathi kwa undani wake!! Hata mawazo yetu tunayopaswa kuyaenzi na kuyaandikia historia ni yale yenye harufu za ushindi tu. Tukipoteza muda kujenga juu ya mawazo ambayo yalishashindwa, huenda tukajikuta tunakuwa upande ulioosahaulika wa historia maisha yetu yote!
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA NNE ***
Chiziza nini bwana?
Ndugu wa karibu wa Nunu walipatikana.
Akina dada wawili waliovutia mno kuwatazama, mama mmoja wa makamo aliyekuwa na lafudhi ya kisukuma, vijana wawili watatu waliokuwa wakibadilika badilika kutokana na mazingira pamoja na msururu mrefu wa marafiki zake wakatambulishwa kwa Clifford, ingawa kila mmoja kwa wakati wake. Huyu akaitwa dada, na huyu mama mdogo, huyu akaitwa ndugu wa yule dada wa siku ile, na huyu mtoto wa yule mama mdogo ambaye dada yake nilikuonesha siku ile.
Karata zikachangwa na kuchangika.
“Cliffie wangu… Huyu ni rafiki wa kaka yangu dear, kaka ambaye baada ya yule dada wa siku iiileee, anafuatia yule dada angu wa siku ile usiku pale Posta, halafu sasa kuna dada yuko Zanzibar, yeye na huyu kaka mama yao ni mmoja ila baba tofauti” Alitambulisha Nunu siku moja wakiwa kwenye matembezi.
Alichoambulia Clifford hapo lilikuwa ni maneno mawili tu…
“Dada” na “Zanzibar” tu, naye akajikuta amesharopoka.
“Oooooh.. Zanzibar… Dada yangu wa kwanza naye yuko Zanzibar, anaitwa Claritha” Alisema huku tayari mkono wa Nunu wenye kucha ndefu za kubandika ukiwa unazihesabu kwa umakini mkubwa pingili za uti wa mgongo wa Clifford aliyeishia kutabasamu kama katuni za Mickey Mouse. Mjadala wa kaka rafiki wa dada na dada ambaye dada ake ni ndugu na kaka yake na dada mkubwa wa Zanzibar ukawa umefikia ukongoni.
Hivyo tu yani!!!
Clifford angehitaji ndugu gani tena wa kumzuia kumvisha pete ya uchumba Nunu? Aliowafahamu walitosha kabisa. Hao wengine kama wazazi wangejulikana taratibu wakati wa michakato ya mahari, ndoa na wengine angewatambua baadae kabisa watakapokuja kusalimia watoto atakaowazaa yeye na Nunu wake. Hivyo ndivyo alivyofundishwa na Nunu kila siku. Kwanza hata yeye Clifford, hakuwa na ndugu wa maana ambao walikuwa anawatambua. Alimfahamu baba na mama yake, dada yake na watoto wa dada yake, kisha ndugu wengine kadhaa wa mama yao… Kwa upande wa baba, aliwafahamu wachache ambao walikuwa wakiwatembelea pale nyumbani…
“Tena yule gaidi akiniuliza next time nitamuuliza ni ndugu zake alikuwa anawafahamu wakati anaoa, au ni ndugu wa mama wangapi anawafahamu, anitajie na majina kabisa, asilete ubabe wa kizamani hapa” Alijisemea siku moja alipokuwa akitoka ofisini kuelekea kwa sonara mmoja maarufu aliyekuwa amempa kazi ya kumtengenezea pete ya uchumba. Mipango yote alikuwa ameiweka tayari kwaajili ya kumvisha Nunu wake pete ya uchumba.
Mwezi mmoja kabla ya siku hii maalumu ya kumrasimisha Nunu kuwa mchumba wake na kisha kupuliza kipenga cha ndoa ilimkuta akiwa ameshakamilisha maandalizi yote muhimu kwaajili ya shughuli ile. Baadhi tu ya marafiki zake ndio aliwapa taarifa huku akiwa amejipanga vilivyo kumkabidhi mpenzi wake yule zawadi kemkem.
Alishakamilisha manunuzi na makabidhiano ya nyumba maalumu aliyoamua kumnunulia mpenzi wake kama zawadi ya uchumba. Hakukuwa na hitaji lolote la kuhesabu fedha alizokuwa ameshazitoa kwaajili ya Nunu, wala hakukuwa na haja ya kuikagua kadi ya gari jipya ambalo sasa lilikuwa mali halali ya Nunu ingawa ni yeye aliyekuwa mnunuzi.
Clifford alishapenda, na kama ungemuuliza kusudi la maisha yake, hangesita kukwambia kuwa, aliishi kumpenda Nunu!
Hakujua kuwa kunguru si wa kumfuga, na kwamba ipo siku angelikimbia jiji la Dar es Salaam mchana kweupe watu wakiendelea na shughuli zao.
******
Jumamosi ilianza kwa utulivu kabisa.
Orodha ndefu ya nyimbo zilizowekwa kwenye mfumo wa muziki ikiendelea kuyakata mawimbi ya chumba kile kwa sauti ya chini kabisa isiyoleta aina yoyote ya bugudha. Nunu alikuwa wa kwanza kuamka na tayari staftahi nzito ilikuwa imeshaweka mezani ikimngoja “baba yake” mwingine aje ajipendelee. Clifford alipoamka, huduma zote zilikuwa pembeni ya kitanda.
Kwanza, alikutana na Nunu akiwa ameshika bakuli kubwa lenye maji pamoja mswaki wenye dawa ya meno ambao hata hivyo hakuruhusiwa kuushika. Akasaidiwa kupiga mswaki palepale huku Nunu akikisafisha kinywa kile kwa ufasaha mkubwa utadhani chakwake. Kisha kitambaa chenye uzito wa taulo dogo kilichomo kwenye maji ya moto kiasi kikatumika kusafisha uso wote kwa umakini, kisha akalazwa katika kochi maalumu lililokuwepo pale chumbani, akafutwa mwili mzima kwa kitambaa safi na sabuni maalumu. Akapakwa na vijimafuta ambavyo hata hakuelewa viliitwaje.
Aliyekwambia eti kuoga ni mpaka maji meeengi kama ya mto yakumwagikie ni nani? Acha ushamba wewe, kamuulize Clifford!!
Akajihisi msafi kuliko alivyowahi kujihisi hata alipooga masaa mawili mfululizo.
Alitakata mwili na roho!!
Mengine yote yakaenda kama yalivyopangwa. Chai ikanyweka na vimichezo vya hapa na pale vikiendelea huku Mhadhiri yule wa chuo kikuu akiwa mwanafunzi wa chekechea akifundishwa namna ya kujificha na kujifichua, namna ya kuchuchumaa na kurukaruka na vingine vingi. Mara akavalishwa jinsi ya kuvaa brazia, akasimama kwenye kioo na kujicheka.. Wakacheka pamoja na kukumbatiana. Mara akajaribu kuvaa nguo za ndani za Nunu, zilipofika mapajani zikagoma.. Wakacheka tena..
Ungewaona ukiwa mbali, usingekawia kuhisi kuwa ni watu wazima wenye mtindio wa ubongo au aina nyingine ya wendawazimu mkubwa. Lakini kwao, yalikuwa mapenzi na tenzi zake!!
Muda sio mrefu, wakajichafua tena makusudi, kisha wakaoga.
Wakacheka na kufinyana kitoto!!
Tukio zima la kuvishana pete lilipangwa lifanyike kuanzia majira ya saa tatu usiku katika ufukwe wa Mbalamwezi. Maandalizi yote yalikuwa chini ya marafiki wateule wachache wa Clifford ambao mpaka inafika saa kumi jioni, walikuwa wameshakamilisha kila kitu. Vyakula maalumu viliandaliwa pamoja na vinywaji, huku shamra shamra zikitarajiwa kuwa chache tu lakini zenye kuvutia sana!
Jambo moja ambalo alikuwa akimpendea mpenzi wake yule ni kuwa, ilikuwa ni nadra sana kwake Nunu kukubali kwenda kulala nyumbani kwa Clifford huku mara zote akisisitiza kuwa, mtoto wa kile kuonekana mara kwa mara nyumbani kwa mwanaume kutaondoa ladha ya kuingia rasmi akiwa mama mwenye nyumba na mke wa ndoa. Alishauri kuwa kule kwake Makongo yaendelee kuwa makutano kwa kuwa watakapooana, makazi yale yatakuwa yamevunjwa rasmi na hakuna kitakachoharibika.
Hata wewe ungekuwa ni Clifford, hapo ungekataa kwa misingi gani? Labda uwe kiburi tu!! Clifford mtoto wa watu hakuwa ana kiburi!!
Majira ya saa saba mchana, Clifford aliondoka nyumbani kwa Nunu na kwenda kujiandaa. Walikubalina na mpenzi wake kuwa, itakapofika majira ya saa moja kamili, watakutana Mlimani City kupata walau chai ya jioni na kisha kuna pahala angependa asindikizwe, na Nunu akakubali bila kusita. Wakakubaliana na aina ya mavazi ya kuvaa huku gauni alilolileta Clifford wiki moja kabla likichaguliwa. Wakaagana kila mmoja akiwa na lake kichwani.
Mmoja aliwaza kujenga…
Mwingine akawaza kubomoa na kuharibu…
Saa moja kasoro dakika ishirini ilimkuta Clifford akiwa nyuma ya usukani akiegesha gari lake katika maegesho ya magari ya Mlimani City. Alishuka na kujipapasa mfukoni, akachomoa poshi yake na kuhesabu kilichokuwepo. Hakuridhika nacho. Akazama katika mfuko wa suruali safi ya rangi ya kijivu aliyokuwa ameivaa. Akaibuka na kibunda cha pesa. Akakihesabu kwa haraka. Laki na themanini. Akasonya kwa dharau!!
Haikutosha kwa siku muhimu kama ile. Vipi kama angepata wageni zaidi?
Akazama kwenye koti la kijivu lililoendana sawia kabisa na suruali yake. Huko akaambulia kitambaa tu. Akasonya tena huku akishuka na kuiweka sawa suti yake. Haraka akapiga hatua na kuifikia mashine ya ATM ya mojawapo kati ya benki aliyokuwa anaitumia. Akaizamisha kadi yake na kuiamuru mashine ile imsikilize kila alichokuwa anakitaka. Ikamsikiliza na akakipata. Makaratasi yenye rangi nyekundu yakaanza kupuputika baada ya mlio uliokera masikio yake kwa sekunde moja au mbili. Yakatoka, yakatoka tena, yakaendelea kutoka. Aliyekuwa anangoja kwenye foleni akalazimika kungoja sana.
Yakatoka.. Kisha… Kimya!
Kadi yake ikafyatuka na kumchungulia ikiwa imechoka na kuonekana kuanza kupauka ndani ya muda mfupi.
Hakujali. Akatabasamu. Akaichukua na kuiweka mfukoni. Akayakusanya makaratasi yale kana kwamba si chochote cha maana kwa muda ule ukilinganisha na kilichokuwa mbele yake. Hakuyahesabu. Akayafutika kwenye mfuko wake wa koti kwa upande wa kushoto na kuanza kupiga hatua. Huku nyuma, mashine ile ikamkumbusha kuwa ilikuwa na utaratibu wa kuwapa risiti wateja wake. Hakuijali, akaipuuza na kuiacha ikining’inia pale juu kwa fedheha kubwa.
Yanini sasa makaratasi wakati tayari ana hela? Mchumi na muhasibu makini anayewafundisha wengine kanuni za kifedha akajikuta akiwashangaa wataalamu waliokuja na utaratibu wa kuwapa wateja wao karatasi eti wakiziita risiti baada ya kuchukua pesa.
Wapumbavu tu, pesa ndio muhimu katika usiku huu maalumu!
Alirejea garini na kujifungia huku akiruhusu hewa safi iendelee kutembea mule garini kwa kufungua kidogo madirisha. Hakutaka kuonekana na wanafunzi wake ambao walipendelea kuwepo maeneo yale hasa siku za mwisho wa wiki, au watu wengine wowote aliofahamiana nao. Ile haikuwa siku yake na mtu mwingine yeyote isipokuwa Nunu na marafiki kadhaa.
Waniache mie!!
Akiwa katikati ya mawazo simu yake ikapata uhai. Alipotazama kioo cha simu, akakutana na jambo ambalo alilitegemea ingawa hakutaka litokee.
“Captain Chiziza” Jina lilisomeka.
Hakuwahi kuacha kupokea simu ya baba yake bila sababu ya muhimu. Na jioni hii aliamua asiipokee. Ndio, alikuwa na sababu maalimu! Mzee huyu alitaka kuitumbulia nyongo furaha yote aliyokuwa nayo siku ile. Mzee huyu lazima angekuja na hotuba ndefu kwa kuwa alihisi tayari alishapata taarifa za yeye kuviisha mtu pete.
Dunia ndogo na walimwengu hawana kifua. Mzee yule angeweza kumwita nyumbani muda ule ule kisha aanze kumchezesha “kinyuki chapenyapenya” kwa hotuba zake ndefu zenye maneno ya kejeli. Hakutaka kuipokea. Akaamua kuikata, lakini kabla hata hajaikata, iliacha kuita. Akashusha pumzi kwa nguvu na kujilaza tena kitini akiendelea kuwaza.
Kabla hata akili yake haijakaa sawa, ujumbe ukaingia na haraka akausoma akijua kuwa, ni Nunu aliyekuwa ameutuma. Jina lilelile alilolisoma katika kioo cha simu dakika chache nyuma likazikaribisha mboni zake katika ujumbe mfupi wa meneno.
“Wala sikutaka upokee baradhuli weee, na kwa kuchelewa kwako tu kupokea unanithibitishia kuwa, niliyosikia kuwa unavisha mtu pete ya uchumba ni kweli. Ningekuwa na nafasi ya kukwambia ‘Ole wako’ ningefanya hivyo, lakini kwakuwa sina, nakukumbusha tu kuwa, ‘Kunya kuna staili moja, sasa wewe endelea kujitia unaweka mbwembwe na manjonjo”.
Kudadadeki!!
Clifford alikereka. Akamtukana Mzee yule tusi jepesi na kisha akaachana kabisa na habari zake. “Wazee kuna saa inabidi tuwahurumie tu, hata biblia inasema hilo. Yule mzee anahitaji msaada wa kisaikolojia yule”
Jalada la Chiziza likatupwa kando jioni ile.
Saa moja na nusu ilifika.
Nunu hakuonekana.
Hakuhangaika kumpigia simu, akajipa muda zaidi. Saa mbili kamili. Ama! Hapo sasa akatoa simu na kumpigia Mpenzi wake. Akampata. Baada ya salamu za hapa na pale, Nunu akajitetea kuwa amepata dharura na amekwenda Kigamboni kumwona mama yake mdogo kwa kuwa alikuwa akiumwa sana, na kuwa atarudi muda sio mrefu.
Clifford moyo ukampaa.
Alihoji maswali yote ambayo yeyote angehoji. Mama mdogo yupi? Kigamboni sehemu gani? Mbona hukuniambia? Umeenda sangapi? Anaumwa nini? Nani alikwambia? Kwanini? Kwanini? Ni vipi? Na mengine meengi, lakini yote hayo, Nunu aliyajibu kwa ufasaha mkubwa bila kuumauma midomo. Mwalimu wa chuo kikuu aliyekuwa akifelisha wale wote ambao hawako makini kutoa majibu yanayoridhisha kwenye mitihani yake akatoa maksi tisini na nane kwa mwanafunzi Nunu.
Eee, ndio maana yake.. 98%!!!
Akatangulia Mbalamwezi huku akithibitishiwa kuwa, ndani ya saa moja Nunu angeungana naye. Akiwa na matumaini tele, akaelekea Mbalamwezi huku njia nzima akiliwazwa na wimbo mtamu alioupenda wa Don Williams uitwao “Love is on the roll”..
Mapenzi yako kwenye mwendo..
Saa tatu kasoro dakika tatu akawa ameungana na wenzake. Wakajadiliana hili na lile huku vyakula na vinywaji vikiendelea kunyanyasika. Akamwita mkuu wa sakafu na kuteta naye, akamweleza mabadiliko ya mpango na kuwa Nunu atakapofika shughuli ndio iende kama walivyopanga, na kwa muda ule, maisha magumu yaendelee kunyanyaswa, kuzomewa, kusutwa na kutukanwa!!
Hakuna msamiati uitwao maisha magumu hapa!!
Wa maji walikunywa maji, wakaanza kubadilika rangi kuwa weupe. Wa bia walizigida mpaka wakaanza kushindana kwa kutoa kauli za kimombo. Wale wapenda kula waliyatanua mashavu na matumbo yao kwa soseji, sambusa, kuku na mishkaki ya samaki, wakashushia na mboga za majani na vipande vya matunda. Wakusakata rumba walilisakata mpaka viuno vikaanza kutepeta, lakini si Nunu wala picha yake aliyetokea!
Maisha magumu yakaanza kumnyanyasa Clifford..
Saa sita kasoro ikawakuta wale wapenda pombe wakiwa hoi taabani huku wale wengine waliojidai mabingwa wa pombe kali wakiwa wameshajiondokea kitambo huku wakiacha baadhi ya vitu vyao pale pasipo na uelewa. Clifford koti lilikuwa mezani na kitambaa cha jasho mkononi. Nunu hakuwa anapatikana kwenye simu wala kwenye mtandao wowote wa kijamii!
Ni kama vile Nunu alikuwa ametoweka katika uso wa dunia!!
Clifford akaaga akiwa amepandwa na hasira na kuelekea nyumbani kwa Nunu ili kujua ni nini kilichompata. Donge zito lilikuwa limemkaa kooni. Akafanya malipo yote yaliyokuwa yakihitajika huku fedheha kubwa ikiwa imemjaa usoni. Zile fedha alizokuwa nazo mfukoni alitamani awaite wote waliokuwa mbele yake awagawie ili tu wakamlete Nunu wake. Alipoingia garini, zawadi alizomnunulia Nunu zilizokuwa kwenye kiti cha nyuma zikamkodolea macho kama vile zinamuuliza; “kulikoni, mbona hujatufikisha tunapokwenda?”
Alizitazama kwa hasira, akazisonya na kuzitukana kwa tusi zito la nguoni..
Akaridhika kidogo…
Safari ya Makongo kwa Nunu ikaanza.
Laiti angelikuwa na pua ya kunusa ya kesho, angejiunga na wale walevi pale ili japo alewe ingawa haikuwa tabia yake, kisha aende akalale nyumbani kwake hadi asubuhi ndipo aanze kuhangaikia habari za Nunu.
Lakini pua haikunusa, jicho halikuona, ingawa akili iliamuru mwili kwenda, na mwili ukatii. Ndani ya dakika arubaini, Gari ya Clifford ikaegeshwa mbele ya nyumba aliyokuwa anaishi Nunu, nyumba ambayo ni yeye aliyekuwa amempangishia na kuilipia kwa mwaka mzima, na kwa haraka akaanza harakati za kuingia ndani…
We Clifford wewe!!
Wewe!!!
******
Nimefundishwa kuwa…
Waliosema kuwa hakuna ajuaye kesho wala hawakutumia akili kubwa kiiiivyo kulitambua hilo. Hata dakika tano tu zijazo hakuna azijuaye. Hili si la kujadili. Lakini, maisha ya baadae, ni mwendelezo wa maisha ya sasa. Kile ambacho unakiishi leo, utakapoenda kulala, unajiandaa tu kuamka nacho kesho na kuendelea kukiishi, mpaka utakapiamua vinginevyo. Na labda ni kutokana na ukweli huu, wenye busara wanajifunza kuitumia hali njema au mbaya wanayoijua sasa kuweza kujiandaa kwa hali ambayo hawaijui baadae au hata kesho.
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA TANO ***
Alifika Makongo…
Taazote zilikuwa zikiwaka. Hapo hofu iliyokuwa ikikatiza mara kwa mara katika kichwa cha Clifford yakayeyuka kwa kiasi kikubwa.
“Atakuwa yuko salama tu” Alijisema huku akiufikia mlango na kuugonga mara mbili, kisha akakishika kitasa na kukikunja kwa kujiamini. Ile harufu tamu ya marashi aliyoachana nayo mchana wa siku iliyotangulia ikamfunika mwili mzima na kumpa msisimko wa ajabu. Ingawa alikuwa anainusa mara kwa mara, hakuweza kuizoea. Ilikuwa mpya kila mara. Hasira zake zote zikaanza kupotelea kusikojulikana lakini ile sifa yake ya kuwa Mwanaume ikampiga konzi na kumkumbusha..
“Acha kuwa laini laini wewe, huyu mwanamke amekudhalilisha mbele ya rafiki zako, lazima umuulize maswali ya kipelelezi na kihasibu mpaka aseme kinagaubaga alipokuwa, na asiposema mpige chini haraka sana, hakufai!” Sauti nzito iliyosadifu sauti yake ilimnong’oneza sikioni. Akaisikiliza na kuafiki huku akitikisa kichwa. Akaruhusu uso wake kujenga matuta kadhaa ya hasira. Akaikagua sebule ile. Hakuona kipya. Akashusha pumzi na kuelekea chumbani huku sauti ile ikiendelea kumtia moyo wa kisasi na hamu ya kujua ukweli wa lile lililotokea.
Mlango wa chumbani ulikuwa wazi pia, lakini taa ilikuwa imezimwa. Akausukuma kwa hasira na kuingia mzimamzima, kisha akawasha taa. Akasimama akiwa ameduwaa. Nunu alikuwa amejilaza kifudifudi kitandani huku akilia kwa kwikwi. Ule mzigo uliokuwa ukimchanganya Clifford kila siku ulikuwa umesitiriwa na kanga nyepesi na kufuli ambalo Clifford alionekana kulitambua, huku ukitikisika kwa nguvu kila mara mwanamke yule alipovuta kamasi kwa kilio.
Mwanaume chali!!
Clifford akanyong’onyea. Ile sauti sasa akaiona ni sauti ya usaliti. Zile hasira akaziona kuwa ni kutaka kumkosanisha na Nunu wake, Nunu ambaye sasa alikuwa akilia mwenyewe pale Kitandani. Akaitukana sauti ile kimoyomoyo na kuionya kuwa isirudie tena kumshauri ujinga!!.
Shabash!!
Anawezaje kuendelea kuuliza maswali ya ufahamu,ya kihasibu na kipelelezi wakati Nunu Analia? Amewezaje kumlaumu mpenzi wake njia nzima na kumbe mpenzi wake huyu alikuwa peke yake nyumbani akilia kwa kwikwi?
Clifford akajiona mkosaji. Akamwomba Mungu amsamehe na kumuahidi kuwa hatarudia tena. Akajiapiza kuwa, atakapokwenda tena kuungama kwa padre, atakumbuka kuungama dhambi ya kumuwazia mwenzake mabaya!
Akamsogelea Nunu wake pale kitandani na kumgeuza. Akakutana na ile sura nzuri ikiwa imekolewa na kilio.
“Pole mpenzi.. Nini tatizo mama? Mama mdogo ame… Amefariki? Aliuliza Clifford na hilo ndilo la kwanza lililomjia kichwani.
“Ha….. Hap…. Ha… Aaaaagh.. Hapan… Hapana baba… Huwez… Huwezi kuelewaaa… Nenda tu Cliff.. N…Nen.. Nenda” Nunu kilio kilikuwa sasa kinafikia kilele cha mafanikio yake. Alikuwa akilia haswa!
“Niende? Niende wapi Nu? Niende wapi mama yangu? Cameon, tell me what is not working.. Tell me what is not happening.. Nieleze” Maneno yalimtoka Clifford huku akihangaika kuilegeza tai yake na wakati huo huo akimweka Nunu sawa.
“Nen… Hu… Huwezi… Siwezi.. Ah.. Nu… Cliff nendaaaa…. Huwezi nielewa baby.. Huwezi…” Nunu alizidi kulia.
Kama Nunu alihisi kuwa kile alichokuwa anakiongea au kutaka kuongea kilikuwa kinaingia masikioni mwa Clifford basi alikuwa anajidanganya kwa kiwango kikubwa. Clifford alikuwa akijishughulisha na kupunguza nguo zake mwilini. Dakika mbili tu zilimtosha kumwacha akiwa kifua wazi na chini akiwa na boxer yake tu. Akampandisha vema Nunu kitandani na kumvutia kifuani pake.
Nunu naye hakusita!! Akajisogeza!!
Akalihisi vema joto lake la kike haswa huku akiyaacha yale machozi yatiririke juu ya kifua chake bila kuhangaika nayo. Ahangaike na machozi wakati Nunu wake yupo? Akamsugua taratibu mgongoni huku akitamani kumwimbia wimbo mzuri utakaomnyamazisha ili wazungumze. Nyimbo tamu hakuwa nazo, lakini maneno yakamjia. Elimu yake ya chuo kikuu na uzoefu wa kitaaluma ulimkumbusha kuwa ilikuwa ni vigumu kwa mtu kuzungumza akiwa na hasira, huzuni au akiwa analia. Akaliweka hilo katika vitendo.
Akaongea.. Akasema.. Akazungumza.. Akabembeleza…
Wewe, acheni bwana, kuna wakati hata pikipiki inaweza kutoa mlio wa Scania au buldoza!! Kuna mtu atasema eti kitaalamu hilo halipo…
Achana na wataalamu, nisikilize mimi asee!!!
Dakika thelathini zikamkuta Nunu akiwa anahema tu juu juu huku ile mito ya machozi ikiwa imekutana na ukame katika kifua cha Clifford na kukaukia humo. Alikuwa amenyamaza. Ukimya ule haukuwakumbusha kuwa walikuwa na la kujadili. Ukawakumbusha kuwa, wao walikuwa mume na mke watarajiwa, na kuwa haikuwa hatia yoyote kwao kushiriki yale ambayo walikuwa wakiyatarajia.
Hakuna aliyewaambia ‘anzeni sasa’!
Wakajikuta tu wakiwa katika kukurukakara zisizo na mshindi wala mshindani.. Kijasho kikiwa kinawachuruzika bila wao kujua. Kisha ghafla, kama vile dunia nzima iliamua kuwazomea, kishindo kikubwa kikasikika!
Baang!!
Mlango ukawa wazi!
Mwanaume mrefu mwenye sura iliyokosa matumaini ya kusifiwa kwa uzuri alisimama mbele yao akiwa na vijana ambao hesabu za haraka za Clifford zilitambua kuwa walikuwa wanne. Na hakukosea, yeye si mwalimu wa hesabu za kihasibu? Wote wakatawanyika mle chumbani kwa fujo na papara nyingi.
“Nyie.. Aargh! Weezii.. Ah, nyie vipi bana?” Aliropoka Clifford huku akihangaika kutafuta shuka ajisitiri. Mmoja wa wale walioingia akamsogelea na kumkamata vema mkono. Akamvuta na kumtandika ngumi safi chini kidogo ya sikio. Kuna baadhi ya kanuni za hesabu, kanuni za kisayansi pamoja na matukio mbalimbali ya kihistoria ambayo Clifford alivisoma akiwa kidato cha pili vikamjia kichwani na akavikumbuka kwa ufasaha wake kabisa!!
Ile Archimedes Principle ilitiririka vema kichwani kwake!
“Taratibu kijana.. Kama utakaa sawa na kukiweka vema kichwa chako, utagundua kuwa wewe ndio mwizi na unapaswa kutueleza udokozi wa wake za watu umeanza lini”. Kidume kile ambacho sasa kilikuwa kimesimama kwenye kona moja kule chumbani kilikoroma kwa upole huku kikimkazia macho Clifford.
Sura yake ilikuwa mbaya, lakini sauti yake ilikuwa mbaya kuliko ubaya wenyewe!!
Ama!! Wake za watu? Hawa jamaa vipi hawa??
Haraka akasimama akiwa anajiamini. Hakujali kuwa yu uchi, umbile lake likiwa limenywea na kubaki kuangalia chini kwa soni kubwa. Aliamua kupambana. Hawezi kumruhusu mtu acheze na hisia zake kwa Nunu kiasi kile.
“Jamani tafadhali.. Kama ni pesa semeni niwape, najua ninyi ni majambazi tu. Tafadhalini tuachieni uhuru na mke wangu.., please guys. Na hamjui tu mnaongea na mtu mkubwa kiasi gani hapa, huu mchezo…..” Aling’aka Clifford lakini hakuweza kumaliza.
“Hebu kaniletee maji ya kunywa Agatha” Lile pandikizi la mtu likatamka huku likimgeukia Nunu. Ajabu hii!! Tayari Nunu alikuwa amejisitiri kwa upande wa kanga na machozi yalikuwa yakimtoka bila utaratibu.
“Agatha?? Ndio nini wewe? Ah.. We Bwege vipi? Ni nini hiki mnanifanyia ninyi? Mchezo ga…..” Alijaribu kulalamika Clifford.
“Mchezo?? Yani unakuja kwangu, unakaribishwa ndani. Unaparamia kitanda change. Hata muda wa kutazama ukutani kujua umeingia nyumba yenye picha za mwanaume mwenzako hutaki, unaishia kuangalia makalio ya mke wangu tu na kuyashika shika. Halafu nakuja kukufumania kisha unauita huu mchezo? Sasa hapo mchezaji ni nani, mimi au wewe?” Jitu lile lilisema huku likisogea karibu na Clifford. Kofi zito likakutana na kisogo kisichozoea shuruba cha Clifford. Akarudia kuwahesabu wale waliokuwepo chumbani kule.
Inawezekana mwanzo alikuwa amekosea. Walikuwa nane sasa!
Akarudia tena kuwahesabu…
Walikuwa sita!! Eeeeh.. Hapana.., sio sita… Tisa!!
Hesabu za kujumlisha na kutoa zilikuwa zimegoma kabisa!
Kama vile aliyepewa ishara, kijana mmojawapo akachupa na kubembea katika uume wa Clifford.. Loh!! Dunia nzima ilikuwa inamjia machoni.. Akaziona sayari zote kwa ukubwa wake sahihi.. Akazihesabu kwa haraka haraka.. Wanasayansi walikuwa wanadanganya kwa kusema ziko tisa. Zilikuwa kumi na mbili huku zikiwa zinagongana gongana kwa fujo..
Akamwachia na kumkandamiza ngumi ya tumbo iliyokuwa na lengo la kumtapisha vyote alivyokula siku ile. Ilikuwa ni bahati tu kuwa hakuwa amekula chochote jioni ile. Akaishia kutema hewa iliyoambatana na damu.
Ndani ya nusu saa, hakuna rangi ambayo Clifford hakuwa ameacha kuiona. Nunu alikuwa amekiri mbele ya wote waliokuwepo mule chumbani kuwa alimweleza Clifford kuwa yeye ni mke wa mtu lakini wakakubaliana kufanya kwa siri, na katikati ya kilio akaomba msamaha kwa “mumewe yule”. Clifford alipotaka kuja juu akaonyeshwa vyeti halisi vya ndoa. Ndoa ya kikatoliki baina ya AGATHA MBISE na MARTIN BAZU. Bado haikumuingia akilini. Akajitahidi kukurupuka hadi sebuleni. Huko sasa akajua idadi kamili ya nguvu kazi ile.
Wanaume watano walioshiba vema walimweka mtu kati na wakamsaga kwelikweli. Jicho moja ndilo pekee lililoachiwa nafasi ya kuona, huku lile lingine likitiwa uvimbe kwa makusudi bila sababu yoyote ya msingi. Akiwa karibu na kupoteza fahamu, macho yake yakatua katika pembe mojawapo mule sebuleni. Ilikuwepo picha moja kubwa ya wana ndoa wawili waliokuwa na mavazi yao rasmi ya harusi.
Nunu ndiye aliyekuwa bibi harusi na yule bazazi mwenye sura mbaya aliyekuwa akimchachafya kwa ngumi nzitonzito akiwa bwana harusi. Alipoiweka sawa sasa shingo yake, juu ya kabati ambalo alitengeneza kwa gharama zake mwenyewe na kumwekea mpenzi wake Nunu kulikuwa na picha nyingine kubwa ambapo mwanaume yule alikuwa amesimama peke yake akiwa na mavazi nadhifu ya kijeshi.
Picha hizi hazikuwepo wakati anaingia pale.. Na hazikuwahi kuwepo kabisa!!
Fahamu zikaondoka bila kusubiri walau mazungumzo mafupi na bosi wake!
Akazimia!!!
***
Hakukumbuka alitumia muda gani akiwa mbali na fahamu zake. Hakujua ilikuwa bado ni jumapili au vinginevyo. Hakukuwa na chochote mwilini mwake kilichokuwa kinamsikiliza hata kidogo. Alipotaka kunyanyia mkono, aliishia kuchora chini bila kujua alichofanya. Alipotaka kufumbua macho, yaligoma makusudi! Akajitutumua ili ateme mate walau kusafisha kichwa.. Yote yakaishia kidevuni. Lakini kwa mbali akahisi kuwa ubongo wake bado ulikuwa ukifanya kazi. Akaujaribu..
“Revenues are recognized when… When… Argh.. Wheeeeen….”
Hamna kitu!! Hata akili ya Clifford ilikuwa imeyumba vibaya mno. Hakuwa anakumbuka chochote. Hata angepewa mwanafunzi wa chekechea wakati huo, angeishia kumwambia moja na moja jibu nane!! Kiza kikaendelea kujenga urafiki na macho yake.
Alipokuja kushtuka tena, alihisi kwa mbali sasa akipata afueni kidogo. Aliweza kufumbua macho yake yaliyokuwa yamevimba. Hakupatambua alipokuwa lakini sura ngumu ya Martin Bazu ilikuwa imemkodolea macho.
“Umeamka mhadhiri wa wake za watu?” Alimsemesha Bazu huku akimshika kidevu na kumvuta karibu. Akamcharaza kofi, la haja. Kuna hali ilimjia Clifford kwa wakati mmoja.. Alihisi kucheka na kulia, akabaki ameegesha uso katikati ya tabasamu na kilio. Akagumia kwa maumivu. “Mbona sasa mke wangu hujamfundisha zaidi namna ya kupangilia mambo yenu ya uhasibu sijui uchumi na badala yake nimekukamata kirahisi tu panyabuku wewe?”
“Mkuu… Basi yam.. Yameisha kaka…Nimekos.. Nimekosa mimi, nimekosa… Kama.. kama… kama mmeamua kunifanyia uhuni kiasi hiki sawa tu, nakubali yaishe. Niachieni roho yangu nikaanze maisha yangu na Nun…, I mean.. Ah… Maisha yangu kivyangu.. Peke yangu” Alisema Clifford kwa sauti uliyokata tamaa.
“Mbona hueleweki sasa.. Yani bado unahisihisi kuwa tumekufanyia uhuni? Kwanini usithibitishe kwanza?” Cheko baya lilimtoka Bazu.
Akili ikamkaa sawa Clifford. Hapo sasa ndipo akagundua kuwa pamoja na maumivu makali aliyokuwa nayo mwilini, kuna jambo lisilo la kawaida lilikuwa limemtokea. Akataka akae vema kwa kuwa hakuwa amefungwa popote. Zoezi likaishia katikati. Alikuwa na maumivu makali sehemu zake zote za siri.
“Aaah.. Yan… yani… Yani mme…. Aaah.. Yani mmenilawiti kweli?” Clifford alisema huku uchungu mkubwa ukimtambaa kooni hadi kwenye tumbo. Kichefuchefu kikali kikamkata! Hakuwa na cha kutapika, akaishia kukodoa!
“Sio kukulawiti tu, na ushahidi tumeweka. Kama unafikiri kutembea na mke wa mtu ni jambo jepesi jepesi tu, basi sasa umeingia pabaya dogo. Na ukitoka hapa nataka niwe nimehakikisha hauna kabisa hicho kilichokufanya uitwe Clifford” Alikoroma Bazu huku yale macho yake makavu yakiwa yamemwelekea Clifford. Bila kuambiwa na mtu, Clifford akashusha mikono yake kufunika sehemu zake za siri. Bazu na wengine wakacheka, na hapo ndipo Clifford akajua kuwa kulikuwa na zaidi ya watu wawili mule ndani.
Itoshe tu kusema, Clifford hakuwahi kupitia wakati mgumu katika maisha yake kiasi kile. Mijitu ile ilimwachia baada ya kupukutisha zaidi ya milioni thelathini zilizokuwepo katika akaunti yake ya benki. Kwa mkono wake mwenyewe, alipelekwa benki na kujaza fomu za kutoa pesa, akapewa na kuwakabidhi.
Alitishwa!!
Aliambiwa kuwa, ikitokea akaleta usumbufu wowote ule, picha zile chafu zingekuwa ni mabango ya matangazo ya mtandao mmoja maarufu wa simu Tanzania nzima. Kuongeza mkwara, kidume kile kikatoa kabisa na kitambulisho kilichoonesha kuwa, alikuwa mtu mkubwa sana wa usalama wa taifa. Clifford akanywea.. Hapa na pale, bazazi lile likapokea simu huku na kule huku kila mara likiongelea kuhusu “kuua”, “kutesa”, “serikali”, “usalama”, “gerezani” na mada nyingine za kutishia tishia tu!!
Picha zake akishiriki michezo michafu ya kuingiliwa kinyume na maumbile zilimuweka pabaya zaidi. Hakuwa na nguvu ya kudai chochote kwa Nunu. Yote, hata gari lake, simu zake na vingine vilibaki kwa Nunu. Angemfwata nani amwambie kilichomtokea? Angeweza vipi kuificha aibu ile? Akaamua kufa kiume. Lakini mibazazi ile haikumuachia.
Kila siku ilikuja na maombi mapya. Mara tunataka milioni mbili, mara laki tano, mara kuna dada tunataka umfaulishe mitihani, mara kuna mkopo tunataka utudhamini na mengine mengi. Alipojitutumua kudai uhuru, akakumbushwa juu ya picha zake chafu.Akajikuta akingia katika mtihani wa maisha. Hata kazi sasa hazikuwa zinaenda tena! Clifford yule mtanashati akaanza kuingia katika madeni yasiyoeleweka huku maisha yake yakiishia katika hofu kubwa.
Bila kuambiwa na mtu, akaomba apumzika kazi mwenyewe!! Ingekuwa ni aibu ikiwa picha zake zingeanza kusambaa chuo kikuu cha Dar es Salaam huku naye akiwepo. Ni afadhali akimbie upesi!! Kibaya zaidi, Nunu yule aliyekuwa akimtambua kama mpenzi na mke mtarajiwa aliendelea kumpita barabarani akiwa hajali lolote.
Kibaya zaidi, siku ya siku ikaja ikiwa na picha zingine.
Picha za ajabu zaidi!!!
Katika picha hizi, Clifford mwenyewe, (au mtu mwingine aliyefanana sana naye) alikuwa akisimama akiwa amevaa suti nzuri, huku mkononi akiwa ameshika ua! Pembeni yake, dume la kizungu lililokuwa na umbo kubwa kama wacheza mieleka wa kimarekani lilikuwa limesimama likiwa limetabasamu. Hata mtoto mdogo angejua moja kwa moja kuwa, hawa walikuwa mke na mume!! Picha zingine kadhaa zikawaonesha watu walewale wakiwa uchi wa mnyama wakiwa katika mikao tofautitofauti.
Basi bwana, basi!! Sitaki tena!! Imetosha!!
Clifford alichoka, na moyoni, sauti yenye mamlaka ikamwambia tena kuwa, IMETOSHA!! Kimbilio pekee lilikuwa kwa mwanaume mmoja tu aliyemuamini kuwa ni mbabe kuliko wote duniani…
Mwanaume ambaye huko nyuma hakuwa akimwelewa hata kidogo!!
Gaidi Captain Chiziza!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment