Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

ZAWADI YA ADHABU - 1

  

IMEANDIKWA NA : TIMOTHY PETER MSUYA 

********************************************************************************

Simulizi : Zawadi Ya Adhabu

Sehemu Ya Kwanza (1)


Nimefundishwa kuwa…

“Kuwaza jambo jema ni jambo la kwanza halafu kutenda jambo jema ni jambo la pili tofauti kabisa!! Kuna wakati unawaza jambo jema ukiwa katikati ya kutenda uovu, au ukawa uko katikati ya kutenda mema huku akili yako ikijiwazia uovu mtupu!!

Ingawa mara kadhaa nafsi inaweza kukusuta, si mara zote unaweza kuwa imara kiasi cha kuamua kutenda kile chema unachokiwaza. Lakini daima, uamuzi juu ya kutenda jema, uwe umeliwaza ama la, unao mwenyewe.. Ukiamua kutenda jema, hakuna cha kukuzuia!

Una hiyari ya kukubali au kukataa….

******

NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA KWANZA

Alikuwa ndani ya bajaji…

Jua kali lililoambatana na upepo mkali uliobeba vumbi la kutosha vilishindana kuonyesha umwamba wake! Jua lilimulika kana kwamba lilikuwa likitafuta kitu fulani kilichopotelea ardhini bila mafanikio. Upepo ukashirikiana na vumbi kuichafua hewa kwa makusudi bila kujali kuwa kuna viumbe waliihitaji hewa ile kwa matumizi yaliyohalalishwa. Ulikuwa ni mwanzoni mwa mwezi wa kumi na moja.

Vumbi lilikuwa likitimka bila sababu yoyote ya msingi!!

Kwa wakazi wengi wa Mji wa Singida, hii ilikuwa ni hali ya kawaida kabisa na walikuwa wameizoea na kuifanya sehemu ya maisha yao ya kila siku. Yeye hakuwa na sifa ya kuitwa mkazi mzoefu wa mji huu wa Singida. Vurumai hii ilimkera! Alijikuta akipiga chafya mfululizo huku kamasi nyepesi zikimkereketa puani, akaufikia mfuko wake wa suruali na kukitoa kitambaa safi cheupe, akapenga pua zake asiambulie chochote cha maana.

Akasonya moyoni huku akikunja uso wake uliojaliwa uzuri wa kiume. Ule upepo mkali uliokuwa ukiipuliza bajaji iliyokuwa ikitimka mbio ulimwingia machoni, machozi yakawa yanamchonyota machoni.

Alikereka.

Kwa mbali, mawazo yake yalimpeleka Dar es salaam, jiji ambalo pamoja na kukulia na kupatia elimu yake yote, ya darasani na ya maisha, ndilo aliloanzia kufanya kazi. Alitamani sana kuwa Dar es salaam lakini akalipuuza hilo mara moja. Alishaamua kubadili kabisa maisha yake na mojawapo kati ya mabadiliko ya muhimu aliyoyafanya ilikuwa ni kuhamishia makazi yake mkoani Singida. Yaliyomkuta jijini Dar es salaam hakutaka kuyakumbuka hata kidogo, na muhimu kwa wakati ule ilikuwa ni kuyaanza upya maisha yake ambayo almanusura yapotee alipokuwa jijini Dar es salaam. Kwa mbali, ile kero ya vumbi na upepo vilivyokuwa vimemzunguka akavikubali na kujikuta akitabasamu tabasamu hafifu.

Alishaanza kupazoea na kupapenda Singida.

“Tumefika bro” Sauti ilimzindua kutoka mawazoni na akajikuta akishtuka kidogo.

“OK”. Aliitikia huku akishuka kutoka kwenye bajaji ile. Akalipia na kuvuka barabara huku akiiweka sawa tai iliyokuwa imemkaba kooni. Hapo tena, lile timbwili la upepo mkali uliochanganyika na mchanga pamoja na vumbi vikaubusu uso wake na kumuingia kidogo kwenye macho yaliyokuwa nyuma ya miwani aliyokuwa amevaa. Kwa hatua za haraka haraka akalifikia geti la Tanzania Institute of Accountancy ambacho wakazi wengi wa mji ule walipendelea kukiita “uhasibu”. Bado upepo na vumbi havikumuhurumia msomi huyu, viliendelea kumzomea vikimsindikiza mpaka alipozifikia ngazi za kuingilia ofisini kwake. Hapo vikambusu kwa mara ya mwisho na kumwacha huru.

Naam.. Hapo akawa amefika ofisini kwake. Kule kutembea kwa haraka na kurukaruka kukwepa vumbi na mchanga sasa vikakoma na mwendo wake wa maringo na mikogo ya kisomi vikarejea.

Clifford Chiziza ndilo jina lililokuwapo kwenye vyeti vyake vyote vya shule na vitambulisho vingine vyote. Msomi wa shahada ya uhasibu aliyesajiliwa na bodi ya taifa ya uhasibu na mmiliki mwenza wa kampuni ya Elites Financial Consultants, Clifford aliyependa zaidi kuitwa Cliff alikuwa mkufunzi katika chuo cha TIA tawi la Singida akijikita zaidi katika masomo ya ukaguzi wa hesabu pamoja na uhasibu. Akiwa na miaka 30 tu, alikuwa na sura ya kuvutia iliyotumika pia kuhifadhi tabasamu tamu lililochanua mara kwa mara alipokuwa na watu.

Clifford alitosha kabisa kutumika kumwelezea mwanaume mtanashati. Mavazi yake alijua kuyapangilia vema, mwendo wake wa kiume kabisa, namna alivyozungumza na kupangilia maneno yake pamoja na elimu ya kutosha katika fani yake vilitosha kabisa kumfanya mwanamke yeyote, hata wale walioolewa kumtazama kwa jicho la husuda.

Clifford alikuwa mwanaume hasa!

Haraka aliifikia ofisi aliyokuwa akiitumia kwa kushirikiana na mkufunzi mwingine wa kike aliyeitwa Zulfa Moses. Kwa bahati, alimkuta akiwa amezama katika jitabu kubwa akipekua pekua hapa na pale.

“Hallo Malkia… A very good afternoon to you” Alisabahi huku akimfikia Zulfa na kumpa mkono, kisha akaupokea ule wa Zulfa na kuubusu.

“Afternoon Chiziza.. Za uzima wako?” Aliitikia Zulfa huku kiaibu kikikatiza katika mitaa ya macho yake kwa kule kupokea busu laini kutoka katika papi za midomo ya Clifford..

“There we go again.. Chiziza is that old fella bana.. Mi ukiniita Chiziza nahisi nimezeeka wakati ndio kwanza damu inachemka. Clifford is a name and a half to me” Alisema Clifford huku akiijongea meza yake na kukaa juu yake huku akilegeza tai yake na kutupia kibegi maalumu cha kubebea kompyuta alichokuwa nacho.

“C’moon Cliff.. Umri nao unakwenda bana, na kutumia jina lako naona kama vile nakupa sifa za utoto ambazo zimekupita siku nyingi. Mbona mimi kuna watu wananiita Madam Mosses and I’m jus’ cool with’it?” Alijitetea Zulfa

“You see.. You see… Haya sasa, umeniita Cliff, just the way I like it to be and it sounds really really cool.. Cliff umefupisha Clifford. Hiyo Chiziza ukiifupisha si tunakuwa tunatukanana?” Clifford alilalamika huku uso wake ukichomoza lile tabasamu ambalo alikuwa akilitumia nyakati muhimu hasa awapo na mwanamke mzuri.

Alichokuwa anakitaka akakipata. Kicheko cha kilegevu kikamtoka Zulfa huku akilazimika kukifunika kile kitabu kilichokuwa mikononi mwake. Alicheka kwa sekunde kadhaa huku macho yake yaliyolegea yakimwelekea Clifford.

“Mh.. So you mean Chizi? We mwanaume una vituko kweli” Alisema katikati ya kicheko kile.

Walijadili hili na lile, huku Clifford akitumia muda mwingi kulalamika juu ya hali ya hewa ya mji ule, namna upepo na vumbi vilivyokuwa vikimchachafya na namna usiku alivyokuwa akikosa usingizi kwa kelele za paa la nyumba ambalo lilikuwa likiadabishwa ipaswavyo na upepo ule. Alilalamika pia kuhusu mwenye nyumba kuonekana kutokujali adha ile aliyokuwa akiipata ya kulazimika kukesha akiwa analisikiliza paa lililokuwa likilalamika pasi na msaada wowote. Kwa kusulubiwa na upepo.

“We nawe unadeka sana.. Nyumba uliyopata ni mpya kabisa, na huenda ni changamoto tu za upepo mkali au kuna pahala mafundi hawakuwa makini. Badae nitampigia fundi mmoja mzuri ninaishi naye jirani, we jiandae tu na mwenye nyumba wako aje akusaidie. Umeridhika?” Alimaliza Zulfa.

“Kwakweli hilo limekaa poa, ndio maana nakupendaga mamalake, mmmmmwaaaah” Alichombeza Clifford huku akiachia busu hewani. “Na yule mzee wala sihangaiki kumtaarifu. We nipe namba za huyo jamaa aje anisaidie, mengine tutajua mbele kwa mbele”

“Au kama usumbufu umezidi hamia kwangu basi mpaka atakapotengeneza” Zulfa alisema huku lile jicho lake kubwa lililolegea bila utaratibu akilitumia ipasavyo. Alivaa sura ya utani lakini kwa mwanaume mwerevu kama Clifford alitambua upesi kuwa sehemu fulani ya akili ya mwanamke yule ilimaanisha kile alichokisema.

“Ah.. Wanawake wazuri kama ninyi tena wenye elimu ya kutosha huwa mna wakubwa wanawaweka mjini. Usinitafutie kesi ya mauaji bure mwana wa Chiziza mie.. Hivi una kipindi baadae? Nadhani nitahitaji projector yako, ya kwangu wanaitumia kule procurement” Clifford alibadili mada upesi na aliona waziwazi namna Zulfa alivyokerwa na kitendo kile lakini hakujali.

Hili lilipoisha, wote wakazama katika kujiandaa kwa vipindi vya mchana ule. Mara kwa mara Clifford alikuwa akinua mkono na kutazama saa yake ili kujua muda, na ilipotimu saa nane mchana, akainuka na kompyuya mpakato na kibegi kingine kilichokuwa na projector ya Madam Zulfa na safari ya darasani ikaanza.

Kufundisha masomo ya ukaguzi wa hesabu za fedha na masomo mengine ya uhasibu ilikuwa ni kazi aliyoipenda na aliyoifanya kwa moyo sana huku wanafunzi wake wengi wakimsifia kwa kile kipaji chake kikubwa cha kuweza kufundisha masomo magumu lakini kwa namna iliyowasaidia wengi kumwelewa vema. Pia alikuwa na ukaribu mkubwa na wanafunzi wake, na hakusita kuwasaidia popote walipohitaji msaada wake. Hakika alikuwa kipenzi cha wengi.

Hakuwahi kujua kuwa ufanisi wake katika kazi yake hiyo ungekuja kumgeuka na kumuingiza katika adhabu…

Hakujua kuwa ufanisi huo ungemtunuku zawadi kubwa…

Zawadi ya adhabu….




Nimefundishwa kuwa…

Hakuna gharama yoyote unayoitumia kumwamini mtu mwingine. Unachokihitaji ni akili za kujua ni sehemu gani katika wengine unayoiamini. Hii ni kusema tu kwa lugha rahisi kuwa, huwezi kumwamini mtu mmoja kwa kila kitu. Huenda ukamwamini sana katika mwenendo wake, lakini ukakosa imani katika maneno yake. Binadamu mwenye akili isiyoweza kusomeka kutoka nje hawezi kufikia hatua ya kuaminika kwa asilimia mia moja. Acha usiamini hili leo ninapoliandika, halafu kesho, mtu mwingine atapata nafasi ya kukuthibitishia hili kwa vitendo!!

Una hiyari ya kukubali au kukataa….

******

*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA PILI ***

Sasa alikuwa akiishi Singida…

Hakuhamia mkoani Singida kutokana na mapenzi yake. Hakuwahi kuwaza kuwa angeishi nje ya jiji la Dar es Salaam katika maisha yake. Alikuwa yuko sahihi kabisa. Maisha yake yote aliishi jijini Dar es Salaam, yeye pamoja na familia yao, yeye akiwa mtoto wa pili kati ya wawili tu wa Kapteni mstaafu wa Jeshi, Mzee Adolph Chiziza na Mama yao, Rabeca Shamte, au Mama Claritha.

Dada yake kifungua mimba alikuwa akiishi Zanzibar na mumewe na watoto wawili mapacha, huku akiwa amejikita kufanya biashara mbalimbali hasa za vipodozi na vifaa vingine vya wanawake huku pia akiwa mwajiriwa wa shirika la bima la Zanzibar.

Kama kuna watoto waliopata bahati mbaya ya kuzaliwa na wazazi wakorofi na waliokuwa na kile ambacho vijana wengi walikuwa wakikiita “ukoloni”, basi Clifford na dada yake Claritha walikuwa na bahati mbaya kwelikweli. Mzee Chiziza hakuwa mtu wa kauli mbili! Awali, wengi walidhani kuwa huenda kule kufanya kazi jeshini ndiko kulikuwa kunamfanya kuwa mbabe kiasi kile, lakini hata baada ya kustaafu akiwa bado na nguvu za kutosha kabisa, ukali wake uliokuwa una kila sifa ya kuitwa udikteta uliendelea kushamiri! Alikuwa akisema jambo mara moja, na ikiwa lisingetendeka, hangesita kumchukulia mtu hatua ambazo zingeweza kumwacha hospitali kwa muda!

Chiziza hakuwa mtu wa kauli mbili!

Ukali wake haukuwa nje tu ya familia. Mara kadhaa alishamsweka Clifford au ndugu mwingine yeyote ndani na kumwacha huko hata wiki nzima kwa kile ambacho alikiita kuwafunza adabu. Kwa kiasi kikubwa alifanikiwa na kweli, yeyote aliyemfahamu vema Chiziza alijitahidi kuituza nidhamu yake kwa viwango vya juu ili asije akaingia matatizoni pasi na sababu!! Hii ilikuwa ni sababu pekee ya Clifford kupendelea kujita Clifford tofauti na wengine walipotaka kumwita jina lake la pili, Chiziza, jina ambalo kila kona ya jiji lilitambulika kwa ubabe, visasi, ujeuri na fujo za kukata na shoka!

Elimu ya Clifford ilimsaidia kwa kiasi kikubwa kujitenga na ukorofi wa baba yake. Alipohitimu tu chuo kikuu cha Dar es Salaam, alipata nafasi ya kubakishwa ili kufundisha katika chuo kile huku akiendelea na masomo yake ya kuthibitishwa na bodi ya taifa ya Uharibu na ukaguzi wa fedha, NBAA. Hii ikamtenga na nyumbani kwa yule aliyemwona kuwa gaidi. Ndani ya mwaka mmoja tu, akawa amekamilisha masomo yake na kuwa ni mhasibu aliyethibitishwa. Hakutaka kutafuta kazi nje ya kufundisha, hivyo kitabu kikaendelea.

Jua likachomoza na kuzama, akamaliza shahada yake ya pili ya uchumi wa viwanda na biashara za kimataifa.

Hapo sasa akawa ameiva kwelikweli kwenye taaluma. Kwa kushirikiana na mhadhiri mwenzake kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha, IFM, wakaanzisha kampuni ya Elites Financial Consultants huku Clifford akiwa ndiye hasa injini ya kampuni. Wakaajiri vijana machachari kwenye masuala ya usimamizi wa biashara, biashara za hisa, fedha na sheria za kikodi, na ndani ya muda mfupi wa kuanzishwa kwake, Elites ikawa ni mojawapo kati ya sehemu za kusuluhisha matatizo ya makampuni makubwa ya kibiashara ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam.

Upepo wa mafanikio ukaanza kuipuliza pwani ya maisha ya Clifford, na ule ukorofi wa baba yake ingawa hakuujali sana, uliendelea kama kawaida. Ukwasi alioanza kuupata katika umri mdogo ukampa heshima kati ya watu na ule ugwiji wake katika taaluma yake pamija na kufundisha chuo kikuu cha Dar es Salaam ukamketisha miongoni mwa vijana wachache ambao haingepita dakika kumi bila majina yao kutajwa midomoni mwa watu.

Halafu sasa likazuka jambo…

Kikaja kisa!!

Kisa ambacho kilimweka Clifford katika wakati mgumu na kulazimika kulihama jiji alilolipenda na lililokuwa limemwashia jua la mafaniko na kumpa mwangaza wa mafanikio. Kisa hiki kilipochanganyika na ukali wa Mzee Chiziza likawa kumbo la kuumiza na tufani la kupoteza meli ya mafanikio aliyokuwa ameipanda.

Tufani lilipoisha, akajikuta yuko Mjini Singida, ingawa hakufika kwa meli wala jahazi!!

***

Kungekuwa ni kutokumtendea haki kama ungemwita mwanamke aliyejikatia tamaa ya kimaisha. Ni kweli maisha yake hayakuwa na matumaini, na kwake, usiku na mchana havikuwa na tofauti kubwa. Vyote alivitumia kusaka pesa. Hakuwa na sura iliyomtosha kusimama katikati ya kundi kubwa la wanawake na kujitambulisha kuwa ni mzuri wa kupindukia, lakini alichonacho kilitosha kabisa kumpa sifa ya mwanamke mzuri, na kuwageuza wanaume wakware shingo na kumtazama huku wakimeza mate na kuendelea na safari zao. Pamoja na kutokuwa na uzuri wa kumuingiza kwenye orodha ya wanaoweza kushindania mashindano ya ulimbwende, alikuwa na sifa ya kipekee.. Aibu!!

Hakukuwa na mwenye hakika kuwa sifa ile ilikuwa ni ya kuzaliwa, lakini ilitosha kabisa kumuingiza katika kundi la wanawake wenye aibu. Asingeweza kuongea maneno mengi mbele ya mwanaume bila kujikuta akiwa akafikicha viganja au kutazama chini.

Alikuwa na elimu ya kutosha juu ya mazingira yanayomzunguka, na huenda angefaa kabisa kuwa mkufunzi wa elimu dunia. Aliyafahamu maisha ya tabu, raha, karaha, huzuni, furaha, ugomvi, purukushani na polisi na zingine zinazoendana na hizo. Hakika angeweza kuwa mwalimu mzuri iwapo ingeanzishwa shule ya kuyafundisha hayo, lakini kwa bahati mbaya, shule hiyo haikuwepo.

Akaishia kuyaishi yale aliyoyajua!

Kwa darasani, wala hakuwa anakumbuka hata kilipo cheti chake cha darasa la saba, kiwango cha juu kabisa cha elimu alichokuwa anakitambua duniani. Kuna wakati angetumia hata dakika mbili nzima akijaribu kukumbuka jina la shule ya msingi aliyosomea!. Hakuwa na habari nayo. Kwake, darasa la saba alilohitimu lilikuwa ni zaidi ya zawadi ya mtende kuota jangwani kwa kuwa pia, hakulimaliza kirahisi.

Alipokuwa akisoma, alitamani sana siku moja akamilishe safari ile ya miaka saba ya mateso makubwa. Ungekuwa mtu wa ovyo machoni pake kama ungepoteza muda wako kujadili naye kuhusu maisha ya shule uliyowahi kuyapitia, utamu wa masomo au majina ya walimu wake. Kwake hayo yalikuwa yamesahaulika siku nyingi na wala hakuwa na mpango wa kufanya bidii yoyote kuyakumbuka.

Kwanza ayakumbuke ili iweje kwa mfano?

Mbali na hilo, hakuwa anakumbuka ni lini alifika jijini Dar es Salaam, lakini baadae alielezwa kuwa, baada ya kifo cha mama yao yeye akiwa na miaka mitatu tu, baba yake alipendekeza kuwa ni heri yeye aende akaishi na dada yake wa kwanza ambaye alikuwa akiishi jijini Dar es Salaam. Hili halikuwa na kipingamizi kwa kuwa, msaada pekee wa kimalezi wakati ule ulikuwa ukitoka kwa dada yake huyu ambaye hakukuwa na yeyote kijijini kwao, Isimbira, Sikonge mkoani Tabora ambaye alikuwa akifahamu ni shughuli gani hasa aliyokuwa akiifanya jijini Dar es Salaam, lakini kila alipokuwa akirudi pale Isimbira, kila mmoja alikuwa akimzungumzia yeye. Alikuwa ni kivutio kwa misuko yake ya nywele, mavazi yake, namna alivyozungumza, kutembea na mengine mengi. Hakika aliwavutia wengi.

Lakini yote haya, yeye alisimuliwa tu. Nunu hakuwahi kukumbuka habari za Isimbira. Dada yake alimlea jijini Dar es Salaam na wakati alipokuwa akipata akili za kiutu uzima, aliishia kuambiwa tu kuwa Mama yao alianza kufariki na baadae, baba yao pia akafuata. Isimbira walibaki ndugu tu wa karibu. Ndugu ambao wala hakuwa anawafahamu.

Isimbira ikazikwa kwenye kaburi la sahau, na Dar es salaam ikawa ndiyo Mwanzo na mwisho wake wa fikira!

Jina lake lilikuwa Nunu.. Nun utu, basi! Kwanza hakuwahi kufika sehemu yoyote ambako alilazimishwa kutaja majina mawili. Kote alisema anaitwa Nunu, akaeleweka! Kitambulisho cha nini kwenye maisha yake? Kwanza atambulishwe kwa nani wakati mdomo wake tu ungetosha kutoa utambulisho wa kutosha?

Naitwa Nunu… Nunu tu, basi! Hujasikia? Nimesema ‘NU’ halafu ‘NU’ tena, yani Nunu.., Ndio… NUNU!

Kama kilikuwa ni kifupi, kirefu, kinyume nyume au vinginevyo, hakuna aliyejua!

Nunu aliendelea kukua akiishi katika chumba kimoja na dada yake aliyeitwa Kalunde Kwera. Labda Nunu naye aliitwa Nunu Kwera, lakini ole wako umwite hivyo… Maisha yao hayakuwa mabaya ingawa hakukuwa na kazi yoyote ya maana ambayo Kalunde alikuwa akiifanya. Kila siku angeondoka majira ya jioni na kurudi alfajiri akiwa fedha pamoja na baadhi ya mahitaji ya muhimu na maisha yakaendelea.

Mara kadhaa alikuwa akirudi akiwa na mwanaume ambaye Nunu aliishia kulazimishwa kumuita “Baba”, naye bila ajizi kwa kukosa ule utamu wa kuita jina hili, akajikuta akitii bila shuruti. Siku kama hii, angelazimika kulala chini huku akisikia purukushani huko kitandani, lakini hakuwa anaelewa chochote!

Kila mwanaume aliyevaa suruali au kaptula, makobazi au mokasi,aliyefunga mkanda au mshipi, alipofika pale alikuwa baba. Wengine walikuwa “baba wema” na wakaitikia kwa bashasha huku wakimpa shilingi kumi au ishirini, na wengine walikaza sura kama magumegume na wakaishia kumuuliza maswali magumu ambayo hakuwa ameyafundishwa shuleni wala popote inapopatikana elimu yoyote kwa umri wake.

Hali ikabadilika baadae. Kalunde angeweza kupotea hata siku mbili au tatu, na baadae hata wiki! Awali alikuwa akijitahidi kuacha matumizi, lakini baadae, hali ikawa tofauti. Kuna siku Nunu angeshinda njaa huku akiwa hana nauli ya kumwezesha kufika shuleni kwa wakati. Akajikuta akilazimika kukabiliana na mwendo mrefu wa kuifikia shule, au kutumia uongo na utapeli kuwasomesha makonda wa daladala ili aende bure. Kushindwa kufika shule kwa wakati kukamjengea urafiki wa kudumu na viboko vya walimu ambao hawakujaliwa kipaji cha kuuliza maswali mara mbilimbili. Alivizoea viboko na adhabu za hapa na pale, na wakati mwingine akajua hata namna ya kuvikwepa kijanja.

Nunu akawa Nunu wa shoka.

Akajifunza yote, kushiba na kusota na njaa.

Lakini yapo ambayo hangeweza kuyavumilia. Ni nani angemweleza kwa ufasaha juu ya vile vilima viwili vidogo vilivyoanza kuchomoza kifuani mwake kwa fujo huku nyonga zake zikitanuka na kuipa miguu tabu ya kubeba kamzigo cha haja cha makalio yaliyotutumuka ghafla kama kitunguu maji kikubwa? Ni nani angemweleza kwa ufasaha kuwa hata kule kuingia kwa siku zake za kila mwezi lilikuwa ni jambo la kumuingiza ukubwani? Ni nani? Nani angemjali kama si Kalunde dada yake?

Lakini kivuli chake kikamtazama na kumcheka kwa nguvu… “Yuko wapi dada yako tangu wiki iliyopita?” Kabla hajakijibu, kikamsaidia kumpa jibu lenye kukera. “Hayupo.. Hayupo na anaweza asirudi leo wala kesho”

Na kweli hilo likawa. Kalunde aliendelea kutokuonekana mara kwa mara, na alipoonekana kwa nadra, angekuja tu kubadili nguo na kuacha pesa kidogo ya matumizi kisha akapotea tena. Nyuma yake akaacha msururu wa wale akina “Baba Nunu” waliokuwa wakija mara kwa mara kumuulizia. Hapo Nunu akawa kwenye mtihani mwingine! Wanaume!

Wakamparamia na kumkumbusha kuwa alishaiva. Wengine walijua kabisa kuwa, wala hakuwa ameiva tayari, lakini wakajipa moyo kuwa, hata embe likiliwa na chumvi linakuwa na ladha tu! Wakamsaidia kulishibisha tumbo lake kwa chakula ambacho Nunu alikipokea kwa furaha bila ya kujua gharama zake. Taratibu wakamwingiza darasani. Darasa lisilo na viboko wala mitihani.

Hili akalipenda kweli kweli! Anafundishwa na kulipwa!!

Nunu taratibu akajifunza hiki na kile, na akiwa darasa la saba, tayari Nunu akawa ni moto wa kupikia kande! Ungemwambia nini Nunu huyu ambaye sasa angeweza kumkuna mwanaume mtu mzima pahala ambapo si kucha wala jiwe vingeweza kukuna? Ungemweleza nini Nunu kuhusu mapenzi ambacho asingekuwa akikijua kinagaubaga?

Lakini bahati ikawa upande wake. Akahitimu hilo la kuitwa darasa la saba salama. Hao wanaojihusisha na kusahihisha mitihani na kupanga matokeo nadhani walipagawa kila walipokamata mtihani wowote wa Nunu, wakaishia kughadhibika na kumchorea kila aina ya kinyago ambacho wangeweza kuchora. Angethubutu kupita mbele yao, nadhani kila mmoja angemmwagia matusi hata yale ambayo hayapo kwenye kamusi ya mtaani!!

Ingemuhusu nini Nunu ambaye wakati huo alikuwa mtaani akikabiliana sasa na maisha ya mtaani huku akiwa mwanafunzi asiye na sare?

Akajifunza maisha! Akafanya kazi za ndani, uhudumu wa bar, kupiga magengeni, kuuza mitumba, kazi za saluni na kwingine kote, lakini kote hakukumlipa. Angefanya kazi ipi nyingine ya kulipa zaidi ya kuuza kile ambacho anacho, na hakipungui wala kuchakaa? Nunu akawa kahaba wa kiwango cha lami! Ile haiba yake ya aibu na ukimya ukawa mtaji wa kutosha kumkutanisha na wanaume wenye fedha za kuchezea, wakamtumia kwa ujira ambao walipanga wao. Kwake yeye la muhimu lilikuwa pesa tu!

Wengine walikuwa wanaume wa shoka, wakampa ujauzito. Angezaa mtoto ili ampeleke wapi? Akazichoropoa kwa kasi bila wasiwasi, na kazi ikaendelea kama awali. Akaachana rasmi na dada yake na kujitafutia makazi yake peke yake maeneo ya Changanyikeni. Biashara sasa ikafanyika kwa uhuru na faida kubwa. Mbinu za kukabiliana na maisha zikaongezeka na akawa na mbinu nyingi za kuhakikisha kuwa halali wala kushinda njaa kama alipokuwa akisoma shule ya msingi.

Kukuru kakara zake zikamkutanisha na Clifford Chiziza!




Nimefundishwa kuwa…

Kama kungekuwa an kanuni moja tu ambayo kwa kuifuata maisha ya binadamu yangekuwa ya kuvutia zaidi, huenda ingekuwa ndiyo kanuni ngumu kuliko zote katika masomo, nab ado binadamu wote wangejifunza kwa bidii kubwa mpaka waweze kuielewa kanuni hii. Lakini hata hivyo, bado kuna ambao wangeshindwa!! Maisha ninayoshi leo sio matokea ya kanuni, lakinni bado ninayafurahia. Hata wewe, unayo nafasi ya kuyafurahia kwa kuwa, unachokiishi leo ndicho kilichopo ndani yako, na hayo ndio maisha yako halisi mpaka utakapoamua vinginevyo!!!

Una hiyari ya kukubali au kukataa….

******

*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA TATU ***


Haikuanza kama tufani wala aina yoyote ya mkasa, na wala halikuanza kama tukio la wapendanao wawili kukutana. Ulianza kama msaada kutoka kwa kijana wa kiume msomi anayeshiriki pia kuibua wasomi wengine kila siku huku mwingine akiwa mwanamke msomi wa mtaani mwenye kuijua vema mitaa na madhila yake. Halafu msaada ukageuka kuwa penzi la ghafla tu, lenye ahadi kemkem.

Ilikuwa ni Ijumaa moja wakati Clifford alipokuwa akitoka kazini kwake kurejea nyumbani kwake Kunduchi. Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha na mwanamke mmoja alikuwa akihangaika kujikinga na mvua kwa mikono bila mafanikio huku akionekana wazi kuwa na kila nia ya kuomba msaada. Clifford akasimamisha gari na dada yule akapanda huku akiwa ameshalowa sehemu kubwa ya mwili wake.

“Pole sana dada angu.. Hii mvua ya Dar hainaga hata dalili. Dakika mbili jua dakika mbili mvua” Clifford alimpa pole dada yule aliyekuwa anahangaika kuiweka sawa sketi fupi iliyokuwa imemkaa vema ingawa sehemu ndogo ya mapaja yake yalikuwa yakichungulia nje. Kokwa mbili ndogo zilizovimba zilisimama wima kifuani pake na kule kulowana kwa mvua kukazifanya kuwa kama zenye kumdhihaki Clifford.

“Asante kaka” Aliitikia dada yule akiwa kainamisha uso wake chini.

“Sijui unaelekea wapi” Aliuliza Clifford

“Naelekea hapo Mwenge kupanda gari za kwenda Kunduchi” Alijibu.

“Waaaoooo… Kumbe unaishi Kunduchi?” Alihoji Clifford huku akijiiba na kumtazama hasa maeneo ya kifuani. Akameza mate.

“Hapana kaka ‘angu.. Nna mteja wangu naenda kumwona mara moja” Alijibu.

“Kumbe niko na mfanyabiashara?” Clifford alijibu huku sasa gari ikishika mwendo

“Ah.. Kubangaiza tu kaka angu” Zile aibu zake akazipachika hapo kwa kukuna kuna vidole huku sasa akianza kuzoea lile joto ndani ya gari na kule kujikunyata kukaisha. Kifua chake kikawa wazi machoni wa Clifford.

Mwanaume akameza mate tena kwa nguvu huku wakati huu jicho akiwa kalikodoa.

“Mimi naishi Kunduchi, kwa hiyo safari yetu inaweza kuwa moja. Ingawa hujaniambia unafanya biashara gani, huenda nami nikawa mteja ukajikuta unapata wateja wawili leo” Clifford alinogesha mazungumzo. Dada yule akatoa tabasamu jepesi la makusudi, na tabasamu lile likawa kama mapigo mawili ya nguvu katika moyo wa Clifford ambao haukuwahi kusukwa sukwa ukasukika vema!

“Ni biashara za wanawake tu.. Nauza vitenge na vitu vingine wanavyotumia wanawake.. Samahani kwa kukuangusha” Dada yule alisema huku akiachia kakicheko cha aibu na kudeka kidogo.

Pigo la tatu la nguvu! Clifford pamoja na ukufunzi wake wa uhasibu muda huo ungemuuliza sifa ze mdaiwa angekuwa sifa za mdai na zile za mdai akizifanya za mdaiwa!

“Ona sasa ulivyo na ubinafsi. Kwa hiyo bidhaa zako wanaume hatuwezi kununua? Si tuna marafiki, wake, mama zetu na wengine tunaweza kuwapelekea?” Alijikaza na kuuliza. Kwa mbali alianza kuhisi kule kujiamini kwake kukiisha.

“Kwani umeoa kaka?” Aliuliza dada yule huku akijitahidi tena kukwepesha macho yake. Hapo sasa akawa ndio akawa ameutandika teke kabisa moyo wa Clifford. Akajikuta akichekacheka kama bwege.

“Sijaoa kwakweli, siku hizi waolewaji wapo basi? Kupotezeana muda tu” Clifford alijitetea kipuuzi na pale dada yule alipoonesha kutokujali sana kuhusu jibu lile, mara moja Clifford akagundua kuwa alikuwa ametoa sababu ya kipuuzi. Kwanza hakuulizwa. “Nimekuwaje mimi? Mbona ni kama vile napoteza umakini wangu? What is happening? Mwanaume atapotezewaje muda dada na mwanamke?” Alijikemea kimya kimya na kujiweka sawa ili asiendelee kusema vitu vya kitoto mbele ya mwanamke yule.

Lakini hakuna chochote kilichobadilika. Mpaka anamshusha dada yule katika kituo cha London alipokuwa anakwenda, Clifford alikuwa amejiweka mwenyewe miongoni mwa wanaume wapumbavu waliokuwa wanapatikana jijini Dar es Salaam jioni ile. Pamoja na upole wake na aibu zake, dada yule alikuwa fundi kwenye kila idara ya mazungumzo.

Hata pale Clifford alipojitutumua na kuanza kuongelea habari za uchumi wa nchi iliyokuwa ni miongoni mwa fani zake na masomo aliyoyafaulu vema, alikatwa kidomodomo na maswali pamoja na maelezo mafupi mafupi ya Nunu, akajikuta akijiona goigoi asiyejielewa! Mpumbavu kabisa!!

“Kwani wewe kwako uchumi wa nchi kukua kutakusaidia ikiwa mshahara wako unachelewa kutoka kwa mwezi mmoja na nusu? Hapo sijaongelea kutokuwa na mshaara, ni kwamba mshaara tu umechelewa?” Lilikuwa mojawapo kati ya maswali aliyotupia pale alipoanza kujitia mjuaji wa uchumi.

Akajitia mjuaji, akajieleza weeee, mwishowe akaulizwa tena..

“Achana na hizo sijui TLP sijui GNP sijui manini.. Uchumi ukikua, na leo ukasikia kuwa uchumi sijui umekuwa kwa asilimia ngapi.. Hapafu mshahara wako wewe ukachelewa.. Hapo nimesema umechelewa, sio kwamba umekosa kabisa, umechelewa kwa miezi miwili tu.. Hiyo utaiongeleaje?” Dada yule akakazia swali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu tena mjuzi kabisa wa uchumi akaufyata mkia.

Wakajadili hili na lile huku binti akiendelea kuwa kiungo mchezeshaji wa mauzungumzo. Mpaka anamshusha, alichokumbuka kuomba kilikuwa ni namba ya simu tu, na wakati alipopewa, akazidi kuingizwa darasani na mwanamke yule.

“Asante sana Clifford kwa lifti kaka angu. Ingawa kwako namba yangu imekuwa ya muhimu kuliko hata jina langu.. Haya baba, Vodacom labda watakusaidia kulipata jina” Binti alisema huku kwa mbali akionekana kulalamika.

Ama! Hivi leo nimekuwaje mimi? Mbona kama vile nna kapepo kananiandama?

Clifford alijaribu kukiweka sawa kichwa chake lakini alikuwa ameshachelewa. Nunu alikuwa ameshashuka kwenye gari huku akiwa anajitahidi kuiweka kadi ya mawasiliano aliyopewa na Clifford kwenye mkoba wake mdogo aliokuwa ameupakata. Kama alifikiri kuwa mwanamke yule alikuwa wa kawaida kama alivyokuwa anaonekana, alikuwa amejidanganya vibaya.

Wakati anaweka sawa koo lake na kuyapanga vema maneno kichwani mwake, tayati Nunu alikuwa akivuka barabara kwa mwendo wa kuchuchumia ulionakshiwa na vile viatu virefu alivyovaa. Hapo sasa Clifford akajionea kile ambacho mwanamke yule alipewa pasi na hiyari yake. Mzigo uliofungwa kwa umakini mkubwa ulikuwa ukiihangaisha hewa iliyokuwa imetulia na ule ubaridi wa mvua ambayo bado haikuwa imeanza kunyesha mitaa ile.

Alipokuja kuwa tayari hata kujigusa, alikuwa akitazamana na askari wa usalama barabarani aliyekuwa akimuhoji juu ya kusimama katikati ya barabara. Haraka akajiweka sawa na kuimalizia safari yake huku mawazo yake yote yakiwa yamezama katika bahari yenye upepo mkali.. Bahari ya mwanamke yule wa ajabu.

Ijumaa hiyo ikamuingiza rasmi kahaba kwenye maisha ya mhadhiri wa chuo kikuu!!

***

Kama ungeambiwa yule alikuwa ndiye Nunu yule ambaye alishazoea purukushani za mgambo na maaskari wa jiji basi ingekulazimu kuingia kwenye vitabu kadhaa vya Imani kutafuta sehemu ambako ungeweza kumuingiza huko ili vizazi vijavyo wamsome! Makazi yake yalishahamishwa kutoka Changanyikeni kwenda Makongo. Hayakuwa makazi ya mwanamke asiye na kazi maalumu. Yalikuwa ni makazi ya mwanamke anayefanya kazi yenye kipato kikubwa na marupurupu juu.

Kule kushinda nyumbani muda wote kukaipa nyumba ile sifa ya unadhifu uliopitiliza. Hata nzi, ingawa ni mjinga daima, angejiona mjinga zaidi iwapo angejivika ujasiri wa kijinga wa kuisogelea sebule ile. Wachache waliokuwa na ujasiri wa kuruka na kutua popote, walijikuta wakizomewa na harufu ya kuvutia iliyowakumbusha kuwa yale hayakuwa makazi yao. Wakajiondokea kwa aibu tele huku wenzao wakiwazomea.

Clifford aliaazimia kuyabadili maisha ya Nunu. Alimtambua Nunu kama mwanamke sahihi wa maisha yake, mbangaizaji aliyekuwa akiuza vifaa mbalimbali vya wanawake kutoka ndani na nje ya nchi, na akakazana kumkuzia mtaji kila siku. Ndani ya miezi minne tu ya uhusiano wao, walishaanza kufanana hadi sura. Kila kona walikuwa pamoja huku marafiki kadhaa wa Clifford wakimtambua Nunu kuwa shemeji yao. Hata kama kuna ambao kwa bahati mbaya tu waliwahi kuonana na Nunu huko nyuma, haingewawia rahisi kumtambua Nunu huyu wa sasa aliyepambwa kwa kila aina ya stara na nguo ya heshima. Ule usemi wa duniani wawiliwawili ukawafunga midomo, na maisha yakaendelea.

Lile tufani lililoupiga moyo wa Clifford siku ya kwanza kuonana na Nunu halikutaka kutulia wala kupunguza makali. Siku hadi siku Clifford akaendelea kuwa dhaifu na asiyejiweza kwa Nunu. Akaungwa kwa viungo vyote, akawekwa na nazi ya tui zito la penzi la mnyamwezi ambaye hakuwahi kupajua unyamwezini. Akaongezwa na ladha ya maneno matamu yaliyopangwa vema kutoka katika midomo midogo ya Nunu, akakandamizwa kwa zile aibu za Nunu zilizokuwa zikitoka kwa mpangilio wa aina yake.

Chali!!!

Mwanaume usomi akauweka mfukoni, na haraka akaiulizia gharama ya pete ya uchumba. Wauza magari wakapata mteja, wenye maduka ya kuuza urembo wakawa na mteja wa kudumu, na madalali wa nyumba na viwanja namba zao zikatafutwa na kuhifadhiwa kwenye simu. Aliazimia kumuoa Nunu tena haraka iwezekanavyo.

Mzee Chiziza akapewa taarifa za kijana wake kuadhimia kumvika binti fulani pete ya uchumba. Ule ubabe na ukali wake vikamjia upesi kutaka kujua taarifa zote muhimu za huyo wa kuitwa mchumba wa mwane na mkwewe. Akam’bana kijana wake ili amweleze vema kuhusu sifa za mchumba wake huyo huku akitaka taratibu zote za kifamilia zifuatwe.

Hapo ndipo Clifford akakumbuka kuwa, hakuwahi kupata nafasi hata ya kumuuliza vizuri Nunu juu ya maisha yake hasa ya kifamilia. Angeuliza sangapi wakati kila alipokuwa akifika nyumbani kwake angejikuta wakati wa kukaa kwenye kochi tayari ana baadhi tu ya nguo mwilini? Angeuliza sangapi wakati kila alipotaka kufungua mdomo alikutana na mdomo mwingine ukiwa unamsubiri wakutanishe ndimi zao? Ni wapi angekuwa na wakati wa kuuliza maswali mengi wakati kila mara yeye ndiye alikuwa mwanafunzi na akamruhusu Nunu, pamoja na aibu zake tele, azungumze kila kitu?

“Ona sasa ulivyo mpumbavu. Yani unakutana na jianamke huko linakupumbaza mpaka unataka kuoa lakini hata hujui habari za familia yake? Hivi elimu yako inakusaidia nini fala wewe? Mbona unakuwa bwege namna hiyo?” Alifoka Mzee Chiziza huku akiwa anagonga gonga meza kwa mkono. Tusi zito la nguoni likamtoka bila kujali yule aliyekuwa mbele yake alikuwa mtoto wake wa kumzaa.

“Hapana dady.. Listen.. You know it is the matter of… the matter of…”

“The matter of what you swine? Unataka kuoa mtu ambaye hata kumfahamu tu is the matter of God knows what? Wewe ni mpumbavu Clifford, sorry kama niliwahi kukwambia hili nilikuwa nakutania tu, now I’m telling you from the depth of my heart.. Wewe ni mpumbavu, and I’m ashamed of you, bastard” Alipigilia msumari Mzee Chiziza, akatema mate kwa nguvu ingawa hayakutoka!!

“Dady calm down.. Ndio maana nimekuja tuongee baba angu.. Sasa unapoanza kuja juu….” Alilalmika Clifford

“Unanipanga sio? Unanilainisha, si ndio? Unadhani mimi ni fala wa zamani? Nakwambia hivi, ufala wangu kwako ndio taaluma zote ulizonazo na usizo nazo, kuku kishingo wewe. Eti ‘Nimekuja tuongee’, umekuja tuongee au umeniletea taarifa fala wewe? Lini ulikaa na mimi ukaniambia uko tayari kuoa na kuwa umeshaanza kusaka huyo mchumba? Lini mwanaharamu wewe? Lini umenipigia simu hata kuuliza juu ya mambo ya muhimu ya kufanya kabla ya kuoa, maluhuni mkubwa weye? Umekuwa eeh? Kufundisha wanafunzi wavaa uchi kumekufungua akili umeamua kuoa sio?” Chiziza alimkazia macho mwanae.

“Baba tafadhali usifike huko, na sifundishi wavaa uchi, nafundishha wanafunzi wa chuo kikuu cha…” Clifford alijisemea kinyonge bila kumtazama zaidi baba yake.

“Listern young man… Wenye akili huwa hawaoi wanapodhani kuwa wako tayari kuoa au wanapokutana na watu wanaofaa kuolewa. Wenye akili wanaoa pale wanakuwa tayari kutimiza wajibu wa ndoa.. Jifunze vema hapo, nimesema wajibu, sio majukumu. Sasa kama wewe kufungua na kufunga zipu unadhani kuwa uko tayari kuoa, au kwa vile una kazi inayokusaidia kula kunya na kulala unahisi umeshaweza kutimiza wajibu wa kuoa, sina cha kukuzuia. Nenda kaoe.. Ila kumbuka, baada ya kuoa, Utaitwa BABA, hata kama huna watoto. Halafu nisikie unaniita kwako kuwa ndoa ina shida, “ooh, baba nisaidie”. Hakyamungu namuapia baba yangu mzazi na kaburi lake kama lipo, nakupiga risasi mwanaizaya weee!” Wakati anayasema haya tayari alikuwa ameshalifikia jokofu na kujimiminia glasi nzima ya maji.

“Lakini baba.. Nahisi niko tayari kutimiza wajibu wangu wa ndoa. Nahisi niko tayari kuwa baba. Yaliyobaki ni madogo tu ya kusikia kama wosia wako kwangu” Clifford alijikaza mpaka mwisho kuweza kuyatoa maneno haya. Maneno ambayo hayakumzuia Mzee Chiziza kumaliza glasi yake ya maji, akaongeza na ya pili, kisha akapiga mbwewe kwa nguvu huku akitikisa kichwa.

“Unahisi Clifford.. Unahisi… Wewe mwenyewe unasema unahisi halafu unataka mimi nikuamini? Ngoja nikuulize swali rahisi. Uko tayari kweli kuoa?”

“Ndio baba, na tayari nna mtu amba….”

“Jibu moja kwa swali moja, usinipe majibu ambayo maswali yake nitakuuliza kesho tafadhali. Nimekuuliza, uko tayari kweli kuoa?”

“Ndi… Ndio Mzee.. Nipo tayari” Alijibu kwa kitetemeshi Clifford.

“Well then, very well… Uko tayari kuoa kwa kuwa uko tayari kuoa au kwa vile watu wengine wanadhani kuwa uko tayari kuoa?” Aliuliza Mzee Chiziza huku akiwa amemkazia macho Clifford.

“Vyote baba. Watu wengi wa umri wangu… unaju….”

“Pumbavu kabisa. Siku ukiwa tayari kuoa ndio uje kuongea na mimi. Mbona wengi wanajiuliza utakufa lini ili warithi mali zako ila hujanijia hapa na ombi la kufa? Tumia akili Mwalimu wa chuo kikuu wewe, shenzi wa tabia” Mzee Chiziza alikifunga rasmi kikao kile kibabe huku akisimama na kuanza kuelekea chumbani kwake akimwacha Clifford akiwa ametumbua macho yake, nusu akiwa haamini kilichotokea, na nusu akiwa anamtukana baba ake mzazi kimoyomoyo kwa ule ukorofi wake usio na msingi.

***

Alijiondokea akiwa ameinamisha kichwa chake chini. Hakuwa na mahapa popote pa kuirudisha furaha yake iliyofifishwa na Mzee Chiziza zaidi ya kwa Nunu. Huko alipokelewa na kukalishwa kwenye kochi safi lililokuwa likimtosha peke yake. Akavuliwa nguo zote na kukandwa hapa na pale huku akiulizwa juu ya kilichomnyong’onyeza. Akajikuta akibwabwaja yote huku akimtupia lawama baba yake kwa ule ukali usio na mfano.

Akabembelezwa na kuwekwa sawa. Akafanyiwa na uhasibu mwingine ambao hakuwahi kuusoma katika kitabu chochote. Nguo zake zote zikafunguliwa akaunti na kuwekwa huko kwa muda. Mguu huu ukatolewa huku na kupelekwa kule, huku mkono huu nao ukafunguka upande mmoja na kujifunga upande mwingine. Akili yake ikawekwa sawa na ndani ya dakika arubaini, hakuwa anakumbuka kuwa kuna Mzee laghai na tapeli aliyekuwa anaitwa Chiziza.

Alimwona tapeli aliyekubuhu aliyekuwa anataka kumpokonya Nunu wake. Akajiapiza kuwa hangeruhusu tapeli yule wa kizazi kipya awaingilie.

Asichokijua ni kuwa, tayari kisu kilikuwa kikikata nyama yake laini na muda sio mrefu kingekutana na mfupa! Angejua kinachomkabili mbele, angempa Mzee Chiziza tuzo ya utakatifu.

Lakini ambacho macho ya kawaida kabisa yangeona waziwazi, ama pua kunusa, au hata sikio kusikia, kwa Clifford kingekuwa ni kitu cha kusadikika kisichokuwepo popote chini ya mbingu.

Akazidi kujificha chini ya mbawa chakavu za Nunu!!

******



Nimefundishwa kuwa…


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG