Simulizi : Wakala Wa Siri (2)
Sehemu Ya Nne (4)
“ Njia ya kutoka humu ni ipi?” Fernanda akauliza.
“ Hautafanikiwa kutoka humu ndani. Upo gorofa ya chini kabisa katika jengo hili. Umejiingiza katika matatizo makubwa sana Fernanda” Abidin akasema. Fernanda akampiga na kitako cha bastola,
“ Nimekuuliza njia ya kutoka humu ni ipi? Sitaki maelezo mengine” Fernnda akasema akiwa amekasirika. Kabla hajajibu sauti za watu wanaokimbia zikasikika zikija mkukumkuku upande walipo wakina Fernanda. Hapo Fernanda akajua sauti ya risasi waliisikia.
“ Nimekuambia hautafanikiwa kutoka hapa, ni bora ujisalimishe huenda ukaonewa huruma lakini kwa kitendo ulichokifanya cha kuua vijana wangu sina uhakika kama hilo litawezekana” Abidin akasema huku akitabasamu, sauti yake sasa ilijawa na nguvu baada ya kusikia wenzake wakija kumuokoa. Fernanda bila kupoteza muda akamkokota Abidin upande mwingine wa korido ambao hakusikia watu wakija.
“ Huku unaenda wapi msichana mzuri? Huku hakuna njia” Abidin akasema lakini Fernanda hakuwa akimsikiliza alimkokota wakatokea sehemu yenye mgawanyiko wa njia mbili zenye korido ndefu pia.
“ Nambie njia ya kutokea ni ipi, nitakuua usiniletee upuuzi. Sema njia ni ipi?” Fernanda akampiga Abidin risasi ya paja, abiding akapiga ukulele wa maumivu.
“ Unaniua! Unaniua wewe shetani! Nakuhakikishia utalipia” Wakati Abidin akisema hayo mara wale watu waliokuwa wakija wakatokea wakiwa na silaha za moto, Fernanda akawarudisha kwa kupiga risasi jambo lililowafanya wajibanze. Fernanda akazidi kumkokota Abidin akisonga kuwakimbia watu wale, punde jengo zima likaanza kulia alamu ya kuashiria kuna hatari,
“Kumekucha! Kazi ndio imeanza hapa, hawa mbuzi wanaitana humu. Lazima niharakishe kuondoka, nikileta mchezo inaweza kuwa hatari kwangu, hii ndio nafasi ya pekee ya kujiokoa ambayo naamini haiwezi jirudie tena” Fernanda akawaza huku akimkokota Abidin kama mzigo, Hata hivyo akaona Abidin anamuelemea.
“ Chagua nikuue au unasema njia ilipo?” Fernanda akamsukuma Abidin akaanguka chini alafu akamuwekea bastola kichwani.
“ Subiri Fernanda, usiniue. Pita njia hii itakutoa” Abidin akasema kwa maana macho aliyoyaona kwa Fernanda hayakuwa macho ya kibinadamu, yalimuambia kuwa akileta mchezo yatafyonza roho yake. Fernanda akampiga Abidin kitako cha bastola, Abidin akapoteza fahamu. Fernanda akampekua Abidin mifukoni lakini kabla hajafika mbali sauti kali ya amri ikitokea mita kama hamsini ikasikika ikisema;
“ Tulia hivyo hivyo”
“ Tulia hivyo hivyo”
Fernanda akageuka nyuma ilipotokea sauti hiyo akaona watu wawili waliomuelekezea bunduki wakiwa wamevaa suti nyeusi na miwani nyeusi usoni.
“Sipaswi kuchelewa kufikiri, lazima nifanye upesi kujinasua hapa wasije kuninasa” Fernanda akawaza akiwa kasimama akiwatazama. Kwa upesi wa kustaajabisha akajirusha chini akajiviringa kama jongoo, akaanza kuviringa kama gunzi la muhindi wakati huo risasi zikimfuata kwa uchu, kila alipoondoa mwili wake risasi za moto zikichimba eneo hilo, ilikuwa ni mchezo hatari aliokuwa akiucheza Fernanda ambao unafanana kabisa na kuchezea kifo. Wale wavaa suti wakaendelea kumrushia Fernanda risasi wakijaribu kuipata shabaha lakini kila walipojaribu walimpunyua punyua; Punde kiza kikatawala baada ya Fernanda kuipiga taa ya umeme iliyokuwa inawaka kwenye korido ile. Watu wale walishikwa na mduwao kwa sekunde, giza liliwapumbaza lakini ghafla akili zao zilirejea mchezoni baada ya Fernanda kuachia risasi, wakaanza kupiga hovyo hovyo risasi kwani walikuwa hawamuoni kutokana na giza, Risasi za moto walizokuwa wakiziachia zilifanya eneo walilosimama kuwa na mwanga, moja ya wale wavaa suti akamshika mwenzake bega;
“ Stop! Acha! Nimesema Acha! Kupiga hivi tunaweza kumpiga mwenzetu Abidin,” Mmoja wa wale wavaa suti akasema, kisha kimya kizito kilichopambwa na giza kikatawala katika korido ile. Wale wavaa suti wakagawana ukuta katika korido ile wakaanza kutembea kuelekea kule alipokuwa Fernanda,
“ Kuko kimya sana, atakuwa keshakimbia” sauti ya moja ya wale wanaume ikasema. Fernanda alikuwa keshakimbia kwenye ile korido. Sauti ya watu wanaokimbia zilikuwa zikisikia zikija upande wa ile korido, haikuchukua dakika walifika wakiwa na silaha nzito; wakawakuta wale wavaa suti wakiwa kwenye kiza totoro.
“ Hakuna mwenye tochi” Sauti ikasikika kutoka kwa wale wanaume, sekunde chache tochi ikawaka na korido yote ikajazwa na nuru. Wale wavaa suti wakamulika upande alikokuwa Fernanda, hawakumuona, alikuwa keshawakimbia, wakamuona Abidin akiwa kalala pale chini wasijue kama ni mzima au amekufa. Wakamkilimbia bado bunduki zao zikiwa makini mikononi tayari kwa kukabiliana na hatari yoyote endapo ingejitokeza.
“ Mapigo yake yapo chini sana, wawili wambebe wampeleke kwenye chumba cha matibabu. Sisi wengine tuliobaki tutaendelea kumfukuzia huyu mdudu mdogo aliyefanya haya, lazima tumkamate, nina hakika hawezi kutoka ndani ya jengo hili kwani upande alioelekea hakuna njia rahisi ya kutokea, Alafu ni mtoto wa kike, hawezi akatushinda wanaume,” Mwanaume mmoja mwenye ndevu nyingi na uso mrefu akasema, akameza mate kisha akaendelea.
“ Tupo saba hapa, wawili wakimpelekea Abidin tutabaki watano, tunatosha kabisa kuifanya kazi hii. Haya kazi ianze” Yule mwanaume akasema, bila kujadiliana wanaume wawili wakambeba Abidin kumpeleka chumba cha matibabu, kisha wale watano wakasonga mbele kuufuata uelekeo aliokimbilia Fernanda, walitembea kwa kasi huku miendoko yao ikiwa yakibabe yenye tahadhari zote za kivita. Wakatembea kwa dakika moja wakafika mahali ambapo kuna njia mbili, njia ya kwanza ilikuwa ni korido ya upande wa kuchoto; njia ya pili ilikuwa upande wa kulia lakini ni ngazi zinazoshuka chini. Hapo wakasimama, yule mwanaume mwenye ndevu na uso mrefu akaonyesha ishara wawili wataenda upande wa kulia, alafu watatu wataambatana naye kuifuatanjia iendayo chini yenye ngazi. Muda wote kulikuwa na giza, walikuwa wakisaidiwa na taa ya kurunzi pamoja na taa za simu walizokuwa nazo.
“ Mkuu hili giza kwetu linaweza kuwa ni mtego wa kifo, huyu mwanamke mshenzi inaonekana kila alivyopita alipasua taa kwa risasi ili kutupa sisi changamoto ya kutokuona vizuri. Napendekeza tuagize kurunzi ziletwe zitakazotusaidia, hasa ninyi mnaoelekea upande wa chini kabisa wa jengo hili” Mwanaume mmoja akasema, jambo ambalo likaonekana kukubaliwa na wengi.
“ Kwa muono wangu, hakuna haja ya kwenda kuchukua kurunzi, naamini huyu mwanamke mshenzi atakuwa katumia njii hii ishukayo chini, giza la upande wa korido ya kushoto naamini limekomea pale kwenye ile kona, si unaona pale kuna mwanga hafifu?” Yule mwanaume mwenye uso mrefu na midevu akasema, wenzake wakageuka kutazama korido ya upande wa kushoto, walipoona kwa mbali mwanga hafifu wakakubaliana na yule mwanaume ambaye bila shaka ndiye mkuu wao.
“ Sisi tutakaoenda upande wa chini ndio tutakaoenda na kurunzi, ninyi wawili mtaenda hivyo hviyo. Sawa? Haya tutawanyike. Hakikisheni mkimuona mnamtia nguvuni iwe akiwa hai au akiwa amekufa. Sawa?” Mwanaume yule akasema kwa sauti yenye amri na wote wakatawanyika. Wakasonga wakishuka ngazi kwenda chini kwa kitambo wakizunguka ngazi zile zilizokuwa zikienda chini, kila walipopita kulikuwa kiza. Fernanda alikuwa amezipasua taa zile kwa risasi.
*****************
Fernanda akaokea upande wa chini kabisa, huku hakukuta taa yoyote, kulikuwa na giza totoro ambalo lilimfanya asione hata hatua moja kwenda mbele. Akayafumba macho yake na kuyaminya kwa nguvu kama sekunde thelasini alafu akayafumbua, mbinu hiyo hutumika kuyafanya macho yalizoee giza, hasa giza totoro, angala kidogo sana akaweza kuona mbele kama hatua moja. Akasonga hatua mojamoja za tahadhari kuifuata ile korido ambayo hakujua ingemfikisha upande gani. Mkononi akiwa bado ameishikilia bastola yake akasonga mpaka alipofika ukingo wa ile korido ambapo mbele yake alipata kizuizi, hapakuwa na njia. Moyo wa Fernanda ukakosa utulivu, mapigo ya moyo yakawa kama yametelekezwa, yakawa yanadunda bila mpangilio, tayari alinusa hatari iliyokuwa inamkabili, akapapasa ukute ule uliokuwa kizuizi kwake, punde akashtuka kugusa chuma, akagusa zaidi , ilikuwa ni geti dogo la chuma lililokuwa limefungwa, Kwa jinsi alivyokuwa akilishika, akili yake ikamuambia kuwa geti lile lilikuwa limeshika kutu, na lilikuwa na mchanganyiko wa vumbi na utando wa buibui.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment