Simulizi : Wakala Wa Siri
Sehemu Ya Tano (5)
Usiku wa saa sita, Fernanda aliamka kutoka usingizini; hakuona haja ya kuendelea kulala kwa raha zote ilhali yupo katika majanga. Kuendelea kulala ni kuwapa adui zake nafasi ya kumuangamiza jambo ambalo hakutaka litokee. Akaingia bafuni akakoga kisha akarudi chumbani kujiandaa. Kutokana hakuwa na nguo zingine alizobeba, alivaa nguo zilezile alizokuja nazo. Alijitazama kwenye kioo akaridhishwa na jinsi alivyojipodoa. Ni kweli kuwa alikuwa amependeza licha ya kuwa alivaa nguo zilezile. Uzuri wake ulichangia kwa sehemu kubwa. Fernanda alikuwa mwanamke mzuri kupita kiasi.
Alitoka nje ya ile lodge, kisha akaende mahali alipoegesha gari lake, akiwa anatembea alikagua huku na huku kuangalia usalama wake. Hali bado ilikuwa shwari kabisa, hakuona dalili yoyote ya hatari ingawaje haikumfanya aamini eneo lile ni salama kwa asilimia zote, hivyo Bastola yake aliiweka mahali rahisi ambako kama hatari ikitokea angeweza kuichukua kwa haraka. Aliingia ndani ya gari kisha akaondoka eneo lile na kupotea katika barabara za Bagamoyo akiitafuta barabara inayoenda Dar es salaam.
Akiwa njiani alipata wazo la kwenda kwa Meja Jenerali, Mr Venance Kagoda, ambaye alikuwa akiishi na familia yake maeneo ya Masaki. Kutokana na mwendokasi aliokuwa akiendesha gari haikuchukua saa moja tayari alikuwa kashaingia Bunju, Dar es salaam. Ilimchukua dakika arobaini kufika maeneo ya Masaki akiitafuta nyumba aliyokuwa anaishi Meja Venance Kagoda. Haikumchukua muda akaiona, ilikuwa nyumba ya kisasa iliyozungushiwa uzio wa tofali zilizopakwa chokaa. Ndani yake zilikuwepo bustani za maua mazuri na miti kadhaa ya hapa na pale iliyozidisha uzuri wa mandhari ile.
Fernanda aliendesha Gari yake polepole akapita Geti la ile nyumba ya Meja Venance Kagoda akaenda kusimamisha gari mbele umbali wa hatua mia moja, akaegesha gari pembezone kabisa mwa barabara. Kisha akachungulia nyuma na mbele kuona usalama wa eneo lile. Bado eneo lilikuwa tulivu, nyumba za eneo lile zilikuwa kimya zikiwaka taa, huku wadudu wa usiku wakisherekea kwa sauti za nyimbo walizozijua wao. Fernanda akashuka, hapo akiwa kava koti la rangi ya ugoro, kichwani akiwa kavaa Kapero, alitembea kwa tahadhari mwendo wa kilimbwende kama paka. Alipotembea hatua hamsini akiwa nusu kwa nusu kati ya alipoegesha gari lake na ile nyumba ya Meja Venance, alishtushwa na sauti ya gari lililokuwa linakuja upande wa nyuma alipoliacha gari lake.
Kwa upesi alikimbia akajificha kwenye mti upande wa kulia wa ile barabara. Ile gari iliyokuwa inakuja ikasimama kule alipoegesha gari lake. Moyo wa Fernanda ukaanza kupiga kwa hofu, huku mwili ukipandisha joto la woga. Fernanda akachungulia kule liliposimama lile gari, akaona wanaume wawili wakishuka kwenye lile gari. Wanaume wale walivalia nguo nyeusi, mikononi wakiwa wamebeba bastola na mmoja alikuwa ameshika kurunzi akimulika gari la Fernanda. Wakalisogelea gari la Fernanda kwa tahadhari kubwa wakiwa wamelielekezea bastola walizokuwa wamezishikilia.. Yule mwanaume mwenye kurunzi alipomulika kwa ndani hakuona mtu, akajaribu kufungua milango ya gari lakini hakuweza kwani ilikuwa imefungwa. Hapo akageuka na kumulika mbele alipokuwa amejificha Fernanda, ule mwanga wa kurunzi ulimkosa kosa Fernanda, kama sio Fernanda kujificha kwa upesi basi wangeweza kumuona, lakini Fernanda alikuwa mwepesi kama chui. Hata hivyo moyo wake ulipiga kite kwa hofu ya kutaka kuonekana.
Wale wanaume wawili ambao mpaka muda huo Fernanda alikuwa hawaelewi ni akina nani walianza kumulika mulika upande huu na upande huu wakimtafuta aliyeegesha lile gari pale. Waligawana upande, mmoja akaende upande aliopo Fernanda, mwingine akaenda upande lilipokuwa linaelekea gari la Fernanda. Mwanaume mwenye kurunzi ndiye aliyekuwa anakuja kule alipokuwa kajificha Fernanda. Mwanga wa Kurunzi ulikuwa ukizichanga mirindimo ya moyo wa Fernanda, Yule mtu alikuwa akimulika mulika bila mpangilio, mara juu mara chini, mara kushoto na kulia hali iliyowashtua mbwa wa eneo lile na kuwafanya waanze kubweka. Yule mwanaume tayari alikuwa amekaribia pale alipokuwa amejificha Fernanda, ni kama hatua tano tuu. Fernanda aliitoa bastola yake mafichoni akaishikilia mkononi tayari kujihami na kushambulia.
Yule Mwanaume mwenye kurunzi alipunguza hata zake kama mtu aliyehisi kuwa eneo lile lina mtu, polepole akawa anasogea.. anasogea mpaka usawa wa alipojificha Fernanda, kwa upesi akageuka kulia akimulika na kurunzi yake pale alipokuwa amejificha Fernanda lakini hapakuwa na mtu. Fernanda alikuwa kahama eneo lile muda mfupi tuu uliopita usiozidi sekunde thelasini. Mtu Yule alipoona hakuna mtu akarudi kule alipokuwa mwenzake.
Kisha wale wanaume wawili wakapanda gari lao wakaondoka, wakipita palepale alipokuwepo Fernanda,
Fernanda alishangaa kusoma maandishi yaliyoandikwa kwenye lile gari yaliyosomeka TK SECURITY, kumbe walikuwa walinzi wa kampunzi za Tk Security. Fernanda alidhani wanaume wale walikuwa ni watu wabaya waliokuwa wakiwasaka kwa udi na uvumba. Fernanda akaondoka pale mtini alipokuwa amejificha akatembea kama hatua ishirini akawa amefika kwenye nyumba ya Meja Venance, nyumba ilikuwa giza, hata taa za nje zilikuwa hazijawashwa; Fernanda akapanda juu ya ukuta kama paka kwa tahadhari, kisha alipofika juu ya ukuta akaziruka zile nyaya za umeme na kutokea upande wa pili ndani ya ukuta. Moja kwa moja akaisogelea ile nyumba ya Meja Venance ambayo ilikuwa na giza la kutisha lisilo na dalili ya uhai wowote.
Akazunguka kwa nyuma, kisha akachungulia ndani Kupitia dirisha la kioo lakini giza lilimfanya asione chochote, akapasua kioo na kitako cha bastola, alafu akapitisha mkono akafungua dirisha na kuingia ndani. Alisimama kwa muda akijaribu kuzoea giza la mule ndani, macho yake yalipozoea giza la mule chumbani akaiona kitanda kilichotandikwa shuka lenye midoli midoli na mto wake, juu ikiwepo chandarua iliyokuwa imening’inia. Pembeni ya kitanda kulikuwepo na kijikabati kidogo na pembeni yake ilikuwepo meza na kiti cha watoto cha kusomea, hapo akajua kuwa chumba kile alikuwa akilala mtoto mdogo mwenye umri usiozidi miaka kumi, Hakuona la maana ambalo lingemsaidia, akaufuata mlango wa kile chumba akaufungua, ulikuwa upo wazi, akatoka kuifuata korido iliyokuwa ikimtazama, akakata kushoto bado giza likiwa limeshamiri eneo lile. Upande wake wa kulia ulikuwepo mlango uliokuwa umefungwa, akaenda kushika kitasa cha mlango ule akakitekenya ukafunguka, akatembea polepole huku akiyapa masikio yake umakini wa kuweza kusikia chochote ambacho kingetoa sauti. Fernanda akawasha taa na kufanya giza likimbie na kukiacha chumba kile kwa aibu, huku mende wakikimbia huku na huku kushangaa ugeni ule wa dharura ambao hawakuutegemea.
Sasa Fernanda aliweza kukiona vizuri chumba kile. Kilikuwa chumba kikubwa zaidi ya kile cha awali. Aliona kitanda kikubwa kabisa cha kisasa, pembeni ya kile kitanda kulikuwa na sofa la mtu mmoja, mbele ya sofa kulikuwa na meza ndogo ya kioo, pembeni kabisa lilikuwepo sofa jingine dogo lililotazamana na ile meza. Upande wa pili ilikuwepo Luninga bapa kubwa ya inchi arobaini na nne iliyofungwa ukutani kwa ustadi wa hali ya juu. Chini ya ile Luninga ilikuwepo seti ya sabufa za muziki za kisasa kabisa. Kwenye pembe kabisa karibu na Ile Luninga bapa Lilikuwepo Jokofu kubwa kiasi, kilikuwa chumba kikubwa kilichokamilika.
Upande mwingine wa chumba kile ulikuwepo mlango tofauti na ule mlango alioingilia Fernanda. Akili yake ikamtuma aufuate ule mlango, akatembea muda huu alikuwa na wasiwasi mno, alishikilia bastola yake akasonga polepole kwa umakini wa hali ya juu, akatekenya kitasa cha ule mlango lakini haukufunguka, ulikuwa umefungwa. Hiyo ikaongeza hamu ya kutaka kujua ndani ya kile chumba kuna nini. Fernanda akaangaza macho yake huku na huku akikagua chumba kile kama mtu anayetafuta jambo Fulani, macho yake yakatua ilipodroo ya kile kitanda. Upesi akaenda kwenye ile droo akaifungua, kwa bahati ilikuwa wazi. Alipoifungua macho yake yalikutana na makarabrasha na bahasha ya kaki, akapekua pekua kwenye yale makarabrasha lakini hakuona la maana, kisha akaichukua ile bahasha ya kaki, nayo akaipekua hakukuta cha maana, alipokuwa akirudisha yale makarabrasha na bahasha alishtuka kuona kitu mfano wa chipu yenye muundo wa funguo ikianguka pale chini. Akaiokota ile chipu, akaikagua, kisha akageuka kuutazama ule mlango uliokuwa umefungwa, akaachia tabasamu kama mshindi.
Alafu akaufuata ule mlango akiwa kabeba ile chipu, alipofika kwenye ule mlango akaiingiza ile chipu kwenye ule mlango, akaachia tena tabasamu mlango ulipofunguka. Ndani alipokelewa na harufu kali ya vumbi, hii ilionyesha kuwa chumba kile kilikuwa na muda mrefu hakijafunguliwa. Aliiona korido iliyonyooka moja kwa moja mpaka kilipo choo na bafu, Fernanda akatembea kufuata kile choo na bafu alipofika alishangaa kuona mlango mwingine mkono wa kulia, akaghairi uelekeo wa chooni na bafuni, akaugeukia ule mlango uliokuwa mkono wa kulia, akakitekenya kile kitasa lakini haukufunguka, Fernanda akashusha pumzi kama mtu aliyechoka. Akatazama kwa umakini ule mlango alafu akajaribu kuingiza ile chipu lakini mlango haukufunguka, akajaribu kukorokocha lakini bado mlango ukagoma, Hiyo ilimfanya akate tamaa. Akapata wazo la kuigeuza ile chipu na kuiingiza kinyume, alipoiingiza alishangaa kuona mlango ukifunguka. Hiyo ikamfanya atoe tabasamu la kujipongeza. Akaingia ndani ambapo alipokelewa na giza totoro na harufu ya uvundo, Fernanda alipapasa ukutani mpaka alipoikuta swichi ya kuwashia taa ya chumba kile. Alipowasha chumba chote kilikuwa uchi mbele ya macho yake. Kilichukuwa chumba cha kubadilishia nguo, kilichokuwa na kabati kubwa la nguo pamoja na Birika la kuoshea uso na kioo cha kujiangalizia. Upande wa nyuma ya mlango Fernanda aliona nguo chafu zilizokuwa zinatoa harufu mbaya ya uvundo, harufu ile ilikuwa inakera jamani mpaka akawa anahisi kutapika,
Bila kupoteza muda Fernanda akalisogelea lile kabati la nguo na kuanza kuzipangua pangua zile nguo, kama mtu anayetafuta kitu Fulani. Hapo akaona Sare ya kijeshi akajua ilikuwa ni sare ya Meja Venance kagoda, akaichukua ile sare na kuanza kuipekua lakini hakuona la maana, aliendelea kupekua karibu nguo zote bila mafanikio ya namna yoyote yale. Sasa nguo zote zilikuwa zimetapakaa pale chini, kabati lilikuwa tupu, macho ya Fernanda yalikereka kuona mende wakikimbia kimbia huku wengine wakiruka na kumparua na kucha zao kwenye mikono yake. Kama kuna wadudu ambao Fernanda alikuwa hawapendi basi ni mende, alichukizwa na tabia za wadudu hao, lakini muda ule ilimpasa ajikaze tuu.
Fernanda akaachana na lile kabati baada ya kuona halina maana yoyote ile. Akaangaza macho yake huku na huku ndani ya kile chumba, akakinaiwa na kile chumba kwani hakikuwa na jambo lolote la maana zaidi ya kero ya ile harufu ya uvundo, Fernanda akaamua kutoka kwenye kile chumba, alipofika mlangoni ili atoke, akili yake ikamtuma azikague zile nguo zinazotoa Uvundo, aone harufu ile inatokana na nini. Akafuata akili yake, akaenda nyuma ya ule mlango wenye zile nguo zenye harufu inayotapisha. Akaziengua pale juu, zilikuwa ni Suruali ya Kijeshi na tisheti ya kijeshi pamoja na koti lake.
Fernanda alishtuka kuona nguo zile zikiwa na damu nzito iliyooza inayotoa mafinyo finyo, Fernanda alivozichangua zile nguo harufu ndio ilizidi kuongezeka maradufu; akashika pua yake huku akipata shida kupumua. Kwa kinyaa na kujilazimisha aliibeba ile suruali juu chini kisha akaanza kuikung’uta ili kama kuna vitu vipo mfukoni viweze kuanguka chini. Alipokuwa akikung’uta alishuhudia funza wakianguka chini ya sakafu kama kumbikumbi, wale funza walikuwa wamenona haswa, Fernanda alipoona ile suruali haina la maana, akachukua lile koti la kijeshi, nalo akalikung’uta kwa nguvu mara kadhaa, punde alishtushwa kusikia kitu cha chuma kikianguka sakafuni kikitokea katika lile koti; lakini hakukiona kimeangukia wapi. Akaacha kulikung’uta na kuanza kukitafuta hicho kilichoanguka, aliangaza macho yake huku na huku, upande huu na upande huu lakini hakuweza kukiona kitu hicho ambacho alikisikia kimeanguka wakati akiwa anakung’uta lile koti. Fernanda akahisi huenda alisikia vibaya, akapuuza lakini kabla hajaendelea kukung’uta alihamaki kukiona kitu mfano wa funguo karibu na miguu yake, akajua ndio kile kitu alichokisikia kikianguka,
Fernanda akahisi huenda alisikia vibaya, akapuuza lakini kabla hajaendelea kukung’uta alihamaki kukiona kitu mfano wa funguo karibu na miguu yake, akajua ndio kile kitu alichokisikia kikianguka,
Aliiokota ile funguo akaanza kuitazama kwa umakini huku akijiuliza ni funguo ya wapi. Akaigeukia ile kabati ya nguo lakini hakuona droo yoyote ambayo ingetumia funguo ile. Fernanda akatoka kwenye kile chumba kisha akaenda kule kilipokuwepo kitanda. Alipofika akaanza kukagua kona na kingo zote za kitanda akitafuta droo ambayo ingetumia funguo zile lakini hakuona droo wala mahali popote ambapo funguo ile ingetumika. Akawa anajiuliza sasa ile funguo inafungulia wapi, na kama haifungulii mule ndani kwa nini Meja Venance Kagoda awe nazo mfukoni. Fernanda akafikiri aende katika vyumba vingine au sebuleni huenda angekuta mahali ambapo funguo ile ingetumika, lakini kabla hajatoka macho yake yalitua kwenye jokofu lililokuwa pembeni kabisa kwenye kona ya kile chumba, Fernanda akalisogelea lile jokofu alafu akafungua mlango wake, macho yake yakapokelewa chupa za pombe na wine mbalimbali, lakini chini kabisa ilikuwepo kufuli, moyo wa Fernanda ukapiga kite kwa nguvu huku akili yake ikipoteza mhimili wake. Aliitazama ile funguo alafu akaitazama na ile kufuli, akafungua ile kufuli na kuvuta ile droo ya jokofu hapo alishtuka kuona kitambaa cha kijeshi kilichofunika kitu Fulani, kwa shauku ya kutaka kujua kilichofunikwa akanyosha mkono kufungua kile kitambaa, alipokifungua alishtuka kuona simu janja aina ya Samsung A12. Akiwa anaichukua, mara alihisi nyuma yake kuna mtu, na kabla hajathibitisha jambo hilo, akashangaa kitu kigumu cha baridi kikigusa shingo yake kikifuatiwa na sauti kavu iliyombali kabisa na mzaha.
“Weka mikono yako juu, tulia hivyohivyo, udanganyifu wowote utakugharimu” Fernanda bila kuleta ukaidi aliiacha ile simu na kunyosha mikono juu kama mateka, akilini akijiuliza aliyenyuma yake alikuwa nani.
“Unajifanya mjanja sana!! Hahahah! Huwezi shindana na serikali Fernanda” Yule mtu mwenye sauti ya kavu aliongea kwa kejeli huku akijichekesha kwa dharau.
“Nani anashindana na serikali?” Fernanda akauliza akiwa kaweka mikono juu.
“ Humjui? Si wewe na Yule panya buku ajiitaye Sajenti” Yule mtu alimjibu Fernanda bado akiwa kaiweka bastola kwenye kichwa cha Fernanda,
“Adui wa serikali ni huyo bwege aliyekutuma wewe mjinga mwenye akili ya nguruwe; unawezaje kumuita Sajenti adui wa taifa..” Fernanda akasema lakini alikatishwa na ngumi nzito ya kichwa iliyompeleka chini. Akagugumia kwa maumivu makali ya ngumi ya Yule mtu mbaya. Ngumi ile ilimjulisha Fernanda kuwa aliyenyuma yake alikuwa anamikono migumu na mikakamavu.
“ Usilete kiburi chako wewe Malaya, nitakuua sasa hivi, usifikiri upo yule mbwa koko wako” Yule mtu aliongea wakati huu Fernanda akiwa amemuona baada ya kuanguka pale chini. Alikuwa mtu mrefu kama jitu, mweusi mwenye kovu kubwa kwenye paji lake, kichwani alikuwa amenyoa kiduku huku shingoni akiwa kava mkufu wa silva. Macho yake yalikuwa mekundu kama damu yaliyoficha dhuluma na ukatili aliowafanyia watu. Mikono yake ilikuwa na mishipa mingi iliyotuna kama mizizi hiyo ilidhihirisha kuwa jitu lile lilikuwa na nguvu nyingi mno. Alivalia Fulana nyeusi na kaptura ya kijeshi iliyopita magoti yake, chini alivalia mabuti marefu meusi yenye soli ngumu. Yule mtu wa kutisha alimtazama Fernanda kifua chake kikiwa kimetuna kwa mazoezi, Fernanda hakuwahi kuona mtu wa kutisha kama Yule katika maisha yake, alimfananisha na zimwi la kivita lenye kiu ya kumwaga damu.
Yule mtu akamsogelea kwa kasi Fernanda na kumrushia teke ambalo lingempiga Fernanda kwenye kichwa lakini Fernanda aliigundua hila yake, akakwepa kwa upesi kama ngedere; alafu akahamia upande wa pili, lakini lile jitu bado halikumuacha, kwa haraka ya upepo Yule mtu alimgeukia Fernanda kwa kasi iliyomshangaza Fernanda na kumpiga ngumi iliyompata Fernanda sawia kwenye bega lake, Fernanda akagugumia kwa maumivu akiwa kalala sakafuni. Yule mtu alikuwa na ngumi nzito yenye maumivu ya mauti.
Yule mtu ambaye Fernanda aliliona kama jitu likamkamata kwa nguvu alafu likamtupa ukutani, looh! Fernanda hakuwa na ujanja, alipiga ukuta na kuanguka chini kama kiroba cha nazi, hapo akajinyonga nyonga kama nyoka aliyejeruhiwa akamwagiwa mafuta ya taa, yalikuwa maumivu makali ambayo Fernanda alihisi uti wa mgongo umevunjika. Licha ya mapigo hayo ya kifo lile jitu bado lilimuandama; likamfuata na kumshika kwenye shingo na kumning’iniza juu. Fernanda aligugumia kwa maumivu akijaribu kujitetea kwa kutoa ile mikono migumu iliyokaba shingo yake kama nyaya. Alipumua kwa shida lakini Yule mtu hakujali.
“Kabla sijakuua kifo kibaya ambacho tangu kuzaliwa hujawahi kukiona wala kukisikia, nambie Sajenti yupo wapi?” Yule mtu akasema huku huku akimkazia macho Fernanda.
“ Hapa.. nitaongeaje wakati umenikaba sana mpaka siwezi kupumua?” Fernanda akaongea sauti yake ikitoka kwa shida kutokana na kukabwa sana. Sauti yake ilishindwa kutoka vizuri.
Yule mtu akampigisha chini akamuachia, kisha akasema;
“Haya nimekuachia, sema wapi alipo Yule Panya buku, usithubutu kuleta ujanja wowote nisije nikaichomoa roho yako bila ganzi”
“ Panya buku…!! mimi simjui” Fernanda alijibu huku akikohoa. Yule mtu akampiga kofi la shavu lililofanya uso wa Fernanda kuwa mwekundu na kuchora alama za vidole kadhaa vya lile jitu.
“Unaleta mzaha eeh! Nafikiri sina haja ya kukuonea huruma sasa, naenda kukuua kabla ya kupambazuka” Yule mtu akaongea huku akimsogelea Fernanda uso wake ukitisha zaidi. Fernanda akaona akileta mchezo pale ule unaweza kuwa mwisho wake. Hivyo akaona ni bora atumie akili kuchelewesha kifo chake hata kama angepaswa afe siku ile.Hata hivyo maneno ya Yule mtu kusema habari za huruma yalimchefua sana Fernanda, kwani mtu Yule hakuwa na sura ya huruma, sura yake ilifanana kwa kiasi kikubwa na Sokwe jeuri lenye ukatili wa kila namna.
“ Subiri! Nitakuambia kila kitu, wala usinipige” Fernanda akasema hapohapo Yule mtu akasimama, akimtazama kama mtu anayesubiri habari ya maana
“Umesema unataka nini kutoka kwangu wewe zimwi baya?” Fernanda aliuliza tena swali lililomghadhibisha sana Yule mtu.
“Wewe Malaya usinichezee akili, nambie wapi alipo Sajent Warioba” Yule mtu aliongea kwa sauti mbaya ambayo Fernanda hakuijua hapo kabla, mtu Yule alisema hayo akiwa kashika kidevu cha Fernanda kwa nguvu huku akimkazia macho yake.
Kwa upesi Fernanda alijipachua na kumpiga yule mtu teke la makende, yule mtu akagugumia kwa uchungu akiwa kashika nyeti zake. Lilikuwa pigo baya mno lililomuingia sawia. Fernanda aliamka pale chini kisha akampiga yule mtu teke la mdomo, yule mtu akaanguka chini akiwa ameiachia ile bastola na kupiga yowe la uchungu. Fernanda bila ya kupoteza muda akamfuata pale chini akamuongeza teke jingine la uso yule mtu akabamiza ukutani na kauchia kishindo. Fernanda hakulaza damu, hakutaka kumuachia nafasi kwani alijua hatari ambayo ingeweza kumkabili. Akaiwahi ile bastola ya yule mtu iliyoanguka chini, kisha akamuwekea shingoni. Yule mtu hakuamini kilichokuwa kinatokea muda ule, alikuwa akihema kwa pupa mithili ya mnyama aliyekoswa na mtego.
“Umetumwa na nani? Sema upesi kabla sijatoboa hii shingo yako” Fernanda aliongea kwa sauti isiyojali akiwa anathema hema.
“Toboa..wewe itoboe hiyo shingo, sitasema aliyenituma” Yule mtu akasema maumivu bado yakiwa yanamsugua vilivyo. Fernanda akampiga risasi ya begani. Yule mtu alipiga yowe la uchungu alafu akasema;
“ Umechelewa! Haitasaidia kitu hata nikisema”
“ KELELE!”
“Nataka unambia nani amekutuma?” Fernanda aliongea kwa kufoka na kufanya chumba kizima kiwe na uhai. Yule mtu hakutaka aseme jambo lolote, akataka kumgeukia kwa upesi Fernanda lakini alichelewa, hila yake ilishtukiwa na kabla hajafanikiwa kichwa chake kilipasuliwa vipande vipande na risasi. Chumba kizima kilitapakaa damu za jitu lile. Fernanda hakutaka kupoteza muda alichukua ile simu aliyokuwa ameiacha kwenye Jokofu, kisha akarudi kumpekua yule mtu wa kutisha kama zimwi, hakuona la maana kwenye mifuko yake. Akamuacha na kuondoka. Aliiifuata ile korido akiwa kashika bastola mkononi, huku bastola nyingine akiwa ameisunda mafichoni nyuma ya mgongo.
Alitokea sebuleni ambapo kulikuwa na giza kutokana na taa ya sebuleni ilikuwa imezimwa, akatafuta swichi ya kuwashia taa ya pale sebuleni, alipoiona akawasha taa, macho yake yalipokelewa na sebule kubwa iliyosheheni samani za kisasa kabisa, lilikuwepo zulia la manyoya zuri lakini lenye vumbi, juu ya dari ya sebule ilikuwepo Pangaboi nyeupe pamoja na urembo urembo wa dari za kiarabu. Ukutani aliiona saa kubwa ambayo ilikuwa ikionyesha ni saa kumi na dakika hamsini. Upande wa kulia kulikuwa na dirisha kubwa lililoangaliana na korido aliyokuwa ametokea. Dirisha jingine lilikuwa mbele yake, yote yalikuwa na mapazia mazuri ya kisasa kabisa. Luninga kubwa ya inchi hamsini na tano pamoja na seti ya muziki vilikuwa vipo upande usiokuwa na dirisha. Juu ya Luninga kabisa ukutani kulikuwa na picha kubwa iliyomuonyesha Meja Venance Kagoda akiwa na sare ya kijeshi na Kofi kichwani. Huyu ndio yuleyule ambaye mwili wake ulikuwa umeibiwa katika hospitali ya Boreti, ile Cadaver iliyokuwa inafanyiwa uchunguzi.
Meja Venance Kagoda mwili wake ulikutwa umeuawa nyumbani kwake bafuni, huku mke na mtoto wake wakiwa hawajulikani walipo, licha ya uchunguzi mkubwa uliokuwa ukiendelea lakini mpaka muda ule bado haikujulikana kama mke na mtoto wake wako wapi, haikujulikana kama wapo hai au walikwisha uawa na watu wasiojulikana. Taarifa ya kifo cha Meja Venance Kagoda zilizua gumzo kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii.
Fernanda alitoka kwenye ile nyumba akiwa kaichukua ile simu janja.
SURA YA 5
Asubuhi na mapema majira ya saa mbili hivi; Sajenti Warioba aliondoka kwenye Ghetto alilokuwa amepanga, Maeneo ya Mtoni Mtongani, kwa Azizi Ally. Akiwa kavalia suruali ya kadeti yenye rangi ya udongo, Tsheti nyeusi yenye kola huku kichwani akiwa kava Kapero. Chini alivaa viatu vigumu vilivyofanana na American buti vilivyokuwa na rangi nyeusi. Akatembea mpaka ilipobarabara kuu iendayo Mbagala, hapo akasimama akisubiri usafiri. Macho yake yalikuwa makini kutazama mienendo ya wapita njia waliokuwa wakienda na kurudi katika eneo lile. Alijua kuwa bado alikuwa akitafutwa hivyo asingejidanganya kuwa yupo salama.
Kitambo kidogo, alisimamisha Uber akachoma ndani.
“Nipeleke Posta” Sajenti aliongea baada ya kufunguliwa mlango na Derava wa Uber.
“Haina shida Boss” Dereva wa Uber akaongea akiwa anatabasamu kama ishara ya ukarimu kwa mteja wake. Baada ya kufunga mkanda, safari ikaanza ya kuelekea Posta.
Sajenti alichungulia nyuma kukagua usalama wa safari yake kuona kama kuna watu waliokuwa wanamfuatilia, lakini hali ilikuwa shwari. Aliona daladala, na bajaji tuu zilizokuwa zinaheka heka za kusafirisha abiria. Aliingiza mkono mfukoni alafu akatoa ile chipu akawa anaitazama kama mtu mwenye kuchunguza jambo Fulani, akiwa anataitazama akili yake ikamtonya kuwa dereva wa Uber atakuwa anamtazama Kupitia kioo cha gari kilichopo juu ya dereva, Sajenti alinyanyua macho yake kiujanja na kutazama kwenye kile kioo, alishtuka kugongana macho na Dereva wa Uber, kumbe Yule Dereva alikuwa akimtazama.
Sajenti Warioba akanyanyua kichwa chake, muda huo dereva akiwa kaacha kutazama kwenye kioo, alikuwa akitazama mbele huku akiendesha gari. Sajenti aliudadisi uso wa Dereva kuona kama angegundua lolote lakini hakuona tashwishwi yoyote kwa dereva. Ukimya ulikuwa mkubwa mule ndani ya gari, hakuna aliyeongea. Dereva akawasha Redio kufukuza ukimya ule, aliweka stesheni yenye uchambuzi wa Magazeti kwani ilikuwa asubuhi. Watangazaji walikuwa wakisoma vichwa vya habari vilivyokuwa vimeandikwa kwenye magazeti. Sajenti alikuwa katulia naye akisikiliza uchambuzi wa magazeti uliokuwa ukiendelea kwenye Redio. Ghafla alishtuka kusikia mtangazaji akisoma moja ya vichwa vya magazeti, kilichoandikwa; Dokta Beatus Kortin; wizi wa chipu watajwa” moyo wa Sajenti ulilipuka kwa mshtuko, mapigo yake ya moyo yalikimbia na kufanya damu iende kasi sana hali iliyosisimua ngozi yake. Wachambuzi wa magazeti hawakuichambua hiyo habari sana tofauti na habari zingine walizokuwa wamezisoma. Jambo hilo Sajenti alilitambua kuwa ni kutokana na usiri uliomo kwenye chipu yenyewe.
Sajenti Warioba alimtazama yule Dereva wa Uber kumdadisi kama alikuwa amegundua jambo lolote. Lakini Dereva hakuwa na hili wala lile, alikuwa kashika usukani akiwa kaangalia mbele akiendesha gari lake. Hali hiyo ilimfanya Sajenti aumbe tabasamu dogo usoni mwake. Sajenti aligeuka nyuma kuangalia kama kuna gari iliyokuwa inawafuatilia lakini hakuona hatari yoyote.
“Boss nikushushie Posta ipi?” Dereva aliuliza na kumfanya Sajenti ashtuke na kugeuka mbele upesi kwani alikuwa amegeukia nyuma ya gari kutazama usalama wa safari yake.
“anhaa! Nipeleke mpaka ulipo Mtaa wa Madaraka” Sajenti akaongea huku akiangalia mbele mahali alipokuwa akimuelekeza Dereva wa Uber.
“Nikushushe wapi Boss?” Dereva wa Uber akauliza baada ya kuingia mtaa wa Madaraka.
“ Nishushe hapo karibu na hiyo shule”
“ Sawa Boss” Dereva akajibu, kisha baada ya nusu dakika akasimamisha gari, Sajenti akashuka; wakaagana.
Baada ya Uber kuondoka, Sajenti akaangaza macho yake huku na huku, mtaa ule haukuwa na msongamano mkubwa wa watu, isipokuwa magari machache yaliyokuwa yakipita, eneo lile kulikuwa na ofisi nyingi na magari kadhaa yaliyokuwa yameegeshwa. Sajenti pasipo kupoteza muda alichukua uelekeo kuifuata barabara ya kivukoni, ndani ya dakika chache alikuwa amesimama lilipo jengo la wizara ya mambo ya nje. Akasimama kwa sekunde kadhaa huku akiangalia nyuma kuona kama kuna mtu aliyekuwa akimfuatilia, hakuona hatari yeyote, mambo yalikuwa shwari, akatazama lango kuu la kuingilia wizara ya mambo ya nje, akaona walinzi walioshikilia silaha, walikuwa walinzi wanne wenye sare kichwani wakiwa wamevaa vikofia vya rangi nyekundu. Sajenti bila ya kupoteza muda akasonga kulifuata lango kuu la kuingilia wizara ya mambo ya nje.
“ Habari yako, unahitaji kuonana na nani humu?”
“ Habari yangu ni nzuri, Samahani nilikuwa nataka kuonana na Dr. Jimmy Nicholas” Sajenti akajibu huku akimtazama Yule mlinzi ambaye uso wake ulikuwa mkavu usio na dalili ya mzaha.
“ Dr. Jimmy Nicholas?” Yule Mlinzi akauliza, macho yake yakijaribu kumtambua mtu huyo aliyetajwa na Sajenti.
“ Yes, Dr. Jimmy Nicholas, haumfahamu?”
“ Mimi simfahamu kwakweli, unauhakika anafanya kazi hapa?” Yule Mlinza akauliza, Sajenti akashtuka kuona Dr. Jimmy hafahamiki pale.
“ Nina uhakika anafanya kazi hapa, yeye ni katibu wizara ya mambo ya nje” Sajenti akajibu.
“ Dr. Kalunde?”
“Ewaah! Huyo huyo, Dr. Kalunde. Mimi napenda kumuita Dr.Jimmy. Kumbe ninyi mnamfahamu kwa jina la Ukoo.” Sajenti akasema huku wote wakicheka.
“sisi tunamfahamu kama Dr. Kalunde Rafiki, je unamiadi naye?”
“Hapana, ila ukimuambia tuu kuwa nataka kuonana naye nafikiri haitakuwa shida” Sajenti akasema huku akijaribu kuumba uso wa ushawishi. Macho yake yaliendelea kuangaza huku na huku kuhakikisha usalama wake haupotei. Alijua fika kuwa bado kuna watu wanamfuatilia usiku na mchana.
“ Sasa ndugu yangu, kama huna miadi naye unafikiri ni rahisi kama unavyoongea hapo? Sisi haturuhusiwi kumruhusu mtu yeyote kuingia humu pasipo kupewa maelekezo na Maboss zetu” Yule mlinzi akasema huku akimtazama Sajenti kwa uso wa kutokukubaliana naye.
“ Ndugu yangu, naomba unisaidie, nahitaji kuonana na Dr. Kalunde, naomba unisadie, kuna jambo la muhimu sana napaswa nizungumze na…” kabla hajamaliza kuongea akakatishwa na Mlinzi mwingine aliyekuwa amefika.
“ Hemed huyu anashida gani, naona mmezungumza kwa kirefu”
“ Anahitaji kuonana na Dr. Kalunde, lakini hana miadi naye, najaribu kumueleza hapa anakuwa mbishi” Mlinzi aitwaye Hemed akasema.
“ Ati ndugu, unamhitaji Dr. Kalunde kwa shida ipi, sema huenda naweza kukusaidia”
Yule mlinzi aliyekuja akamuuliza Sajenti huku akimtazama.
“ Ni kweli namuhitaji Dr. Kalunde ndugu yangu, lakini siwezi eleza shida yangu kwenu” Sajenti akasema.
“ Wewe ni nani kwakwe, na unaitwa nani kutokea wapi?”
“ Mimi ni rafiki yake niliyesoma naye tangu shule ya sekondari, naitwa Mr. Warioba, kwa sasa naishi mkoani Kilimanjaro” Sajenti akasema huku akiwa ameshaanza kukasirishwa na hali ile. Hakutaka tena maswali.
“ Hawa walinzi nao wanamaswali ya kitoto sana, yaani wangejua wanavyoniudhi kwa kweli wasingeendelea kuniuliza, kama sio eneo hili kuwa na ulinzi mkali, hakika ningewafunza adabu” Sajenti akawaza.
“Kwani hupajui kwake mpaka uje huku ofisini ndugu, huku hakuna mambo ya urafiki, huku ni mambo ya kikazi, tulijua umekuja kwa shida za kikazi kumbe wewe unaleta mambo ya urafiki, sijui kusoma wote. Tafadhali naomba uondoke hapa. Mtafute Dr, Kalunde nyumbani kwake au mahali pengine isipokuwa hapa. Sawa?” Yule mlinzi aliyekuja akasema kwa sauti kali ya amri, Sajenti akamuelewa alikuwa akimaanisha.
“ Ndugu zangu, mnaweza wasiliana naye nikiwa hapa hapa, mkamuuliza..” Sajenti akaongea lakini akakatishwa.
“ Ndugu embu ondoka hapa, usijiletee matatizo, kwanza Dr. Kalunde hayupo hapa, wameondoka tangu saa mbili asubuhi, wanakikao na Mhe. Rais…” Akameza fumba la mate kisha akaendelea;
“Ondoka, akirudi tutampa taarifa ulikuja, kisha tutampa namba zako, haya taja mawasiliano yako” Yule mlinzi akasema kisha akatoa simu akiwa tayari kumsikiliza Sajenti.
Baada ya Sajenti kutaja namba zake akaaga pale akaondoka.
“ Sasa muda wote siwangesema tuu kwamba hayupo, yaani kuna watu wanaroho ya korosho, sijui kwa nini watu kama hawa walipewa namba za kuja huku duniani, wanakera sana. Hata hivyo wana bahati, kama sio eneo lile hakika ningewafunza adabu” Sajenti akawaza huku akikatiza mtaa wa pili akiukaribia mtaa wa mirambo. Punde ikapita bajaji akaisimamisha,
“ Habari kijana, nipeleke Mnazi mmoja..” Sajenti akasema.
“ Sawa kiongozi haina shida. Elfu tano tuu”
“ Hatutashindwana, twende tuu” Sajenti akasema na safari ikaanza.
Njiani Sajenti mawazo yalibisha hodi na kuingia katika kichwa chake.
“Hivi aliyeiba Cadaver ni nani? Na aliyechukua zile sampo za uchunguzi ni nani? Tayari chipu ya darubini nimeshaitia mikononi. Hii kwangu inanipa matumaini ya kurejea katika uhuru wangu, nimechoka kukimbia kimbia kama digidigi, uhuru wangu ulikuwa upo matatani kutowehswa na wahuni. Lazima walipie! Lazima…! Watalipia, hawezi kunifanyia hivi. Anyone involved in this will pay for it” Sajenti akawaza bado bajaji ilikuwa ikichanja barabara, kama sio foleni za hapa na pale basi wangekuwa wameshafika mnazi mmoja lakini, jiji la Dar linachangamoto ya foleni, kero ambayo wengi wanailalamikia.
“ Dr, Binamungu! Tayari nimeshamjua msaliti mmoja, huyu anaweza kujua mambo mengi maovu yanayoendelea, yeye ni sehemu ya haya yanayonipata, nikianza naye nafikiri naweza pata mwanga wa kufika kwa wabaya wangu. Wapi anapokaa Dr. Binamungu?” Akawa Sajenti Warioba.
“ Nimekumbuka, lazima nionane na Dr, Beatus, yeye ndiye atanielekeza anapoishi Dr. Binamungu. Nikishampata huyu nitajua uelekeo wa haya. Ule mwili ulioibiwa ulikuwa mwili wa nani, maana niliitwa tuu na kupewa kazi ya kuitafuta chipu, sampo, na mwili ulioibiwa maabara ya boreti, lakini sikuambiwa mwili ule ulikuwa wa nani. Walioiiba ni kina nani na kwa nini wauibe, yaani maswali ni mengi alafu ni magumu kupata majibu yake” mawazo ya sajenti yalikatishwa na sauti ya dereva bajaji.
“ Boss tumeshafika”
“ Nipeleke kwenye jengo la SHDC” Sajenti Warioba akasema huku akitazama mbele kulitafuta jengo hilo ambalo anakumbuka lilikuwa mitaa hiyo hiyo.
“Jengo la SHDC liko wapi, mimi silifahamu Boss” Dereva Bajaji akauliza.
“ Nakumbuka lipo mitaa hii, endelea kuendesha nikiendelea kutazama kulitafuta. Juu kabisa limeandikwa kwa herufi kubwa SHDC ” Sajenti akasema huku dereva bajaji akiendesha polepole huku naye akiangaza macho yake huku na huku kusoma majina ya majengo marefu yaliyopo mitaa ile.
“ Lile! Nimeliona Boss” Dereva bajaji akasema. Sajenti naye alipoliona akamwambia ndilo hilohilo, Walipofika akampa Dereva pesa yake, kisha akashuka na dereva bajaji akaondoka.
Sajenti akatembea kidogo kufuata ngazi za jengo lile, kisha akaifuata moja ya nguzo kubwa ya jengo lile akasimama kwa sekunde kusoma nyendo za weatu wa eneo lile, akajiridhisha kuwa hakuna anayemfuatilia, kila mtu alikuwa na mihangaiko yake. Alipojihakikishia kuna usalama akapiga hatua kufuata mlango wa kioo ambapo alipoukaribia ulitawanyika kushoto na kulia kumpisha apite katikati, ilikuwa ni ile milango yenye detector ambayo hufunguka pale mtu anaposimama mbele yake. Milango hii hutumia optical sensors or motion detectors. Sajenti akaingia ndani moja kwa moja na kupanda lifti mpaka ilipoghorofa ya kumi. Akaifuata korido ndefu iliyokuwa mkono wa kushoto, akatembea mpaka alipokuta kibao kilichoandikwa “SHDC” ambacho kilimuelekeza afuate mkono wa kulia, alipokatisha akakutana na mlango wa aluminiamu na kioo ambao juu yake yaliandikwa maneno “welcome SHDC” akasimama mbele ya ule mlango, kwa pembeni mkono wa kulia ambapo hukaaga kitasa cha mlango akaona sehemu ya kuweka dole gumba, akaweka dole gumba lake la mkono wa kulia. Baada ya kuweka kikatokea kioo kidogo kama kioo kilichopo kwenye ATM MASHINE, kisha yakatokea maandishi “please wait!”Sajenti akasimama kusubiri, kitambo kidogo Sajenti akashtushwa na kile kioo baada ya kuandika “You are not registered, you are not recognized, Contact the office” Kisha chini yake ziliandikwa namba za ofisi. Sajenti akapaniki, iweje mashine ile imuambie hajasajiliwa na hatambuliki ilhali yeye ni mwanachama, na analipa kwa wakati ada ya uanachama. Akili ya Sajenti ikapoteza utulivu akaitoa simu mfukoni akaanza kuiandika ile namba ya simu ili awapigie, akiwa karibu kuipiga akakumbuka jambo ambalo likamfanya atabasamu na kusonya papo hapo.
“nimekumbuka, kijanja cha mkono wangu wa kulia kilivalishwa ngozi ya kiganja cha mtu aitwaye Peter Mirambo kule Brazil nilipopelekwa na Fernanda kwa mzee Da silva. Hakika teknoljia inakua, inamaana mkono wangu wa kulia unaalama za vidole vya mtu mwingine aitwaye Peter Mirambo” Sajenti akawaza huku akiweka dole gumba la mkono wa kushoto kwenye ile mashine, Alipoweka akaambiwa asubiri, kisha baada ya muda ujumbe mfupi ukatokea kwenye kioo cha ile mashine, welcome Mr. Jacob Warioba. Kisha mlango ukafunguka akaingia ndani. Macho yake yalipokelewa na vijiofisi vingi vilivyodizainiwa kwa vioo na aluminium na kila kijiofisi kulikuwa na mtu akiwa anachezea kompyuta. Sajenti akasonga moja kwa moja mpaka ilipokijiofisi kilichoandikwa SHDC21. Akamkuta Dada mmoja aliyekuwa makini na kompyuta.
“ Habari yako Dada” Sajenti akasalimia
“ Nzuri sana, karibu”
“Ahsante. Nimekuja kuna kitu nataka kukichukua” Akasema Sajenti.
Yule Dada akampa Sajenti kidude Fulani kisha akamuambia aweke dole gumba lake, Sajenti akataka kuweka dole gumba la mkono wa kulia, lakini ghafla akaacha baada ya kukumbuka kuwa dole gumba lile halina taarifa zake isipokuwa taarifa za Peter Mirambo. Upesi akabadilisha mkono na kuweka dole gumba la mkono wa kushoto, mshtuko aliouonyesha ulimshtua mpaka Yule dada.
“ Mbona umebadilisha mkono? Alafu umeonyesha kushtuka mpaka nimeogopa, kuna shida yoyote kaka?” Yule dada akauliza.
“ Hapana! Hakuna shida yoyote, nilisajilia na dole gumba la mkono wa kushoto, sasa nilipotaka kuweka mkono wa kulia ndio nikakumbuka, ndio maana ukaona nimeshtuka” Sajenti akasema huku akitabasamu.
“ Hahaha! Wewe kaka! Hivi hujui alama za dole gumba za mkono wa kulia na kushoto zipo sawa?” Yule dada akasema macho yake yakimshangaa na kumuona Sajenti kama mtu mshamba asiyejua lolote. Kumbe alikuwa amedanganywa, Sajenti alitumia mbinu ya kujifanya mjinga na mshamba kumdanganyadada Yule.
“Karibu sana Mr. Jacob Warioba”Yule dada akasema baada ya jina la Sajenti wa Warioba kutokeza kwenye Kompyuta.
“ Nifuate” Akasema Yule Dada, kisha sajenti akaongozana na Yule dada kumfuata alipokuwa akielekea. Walitembea wakizipita ofisi zilizokuwa mule kwenye ule ukumbi, mpaka waliposimama mbele ya mlango ambao mara waliposimama sauti kutoka katika spika zilizochomekwa kwenye ule mlango ikasikika “Please specify a code” hapo hapo Yule dada akataja “SHDC216” alipotaja msimbo huo, ikaja mishale miwili kwenye kioo cha mlango, mshale mmoja wa kijani na mwingine mwekundu. Akabonyeza mshale wa kijani, kisha ikasikika sauti kama ile ya mwanzo ikisema “Code SHDC 216 Given 10 minutes” Kisha mlango ukafunguka.
“ Mr. Warioba tumepewa dakika kumi tuu. Nafikiri unafahamu taratibu” Yule Dada akasema, sajenti akaitikia kwa kutumia kichwa.
“ Unaweza kuingia, mimi narudi kuendelea na kazi, kukiwa na shida yoyote utawasiliana na mimi” Yule Dada akasema kisha akamtajia Sajenti namba yake ya simu, akaondoka na kumuacha Sajenti akiwa ameingia ndani katika ukumbi ule uitwao SHDC400.
Mazingira ya SHDC400 hayakuwa na mabadiliko makubwa tangu alipoyaacha Sajenti, kulikuwa na makabati mengi sana ambayo kila moja lilikuwa na visanduku vilivyoandikwa namba Fulani kama msimbo. Juu ya paa zilikuwepo taa nyingi kubwa zilizofanya eneo la ukumbu kuwa na nuru ya kutosha, ubaridi uliotokana na uwepo wa AC ulifanya ukumbi ule uwe na hali nzuri ya hewa. Ukumbi wa SHDC400 ulikuwa kimya sana, Sajenti hakuona mtu yeyote mule ndani, akasonga akiwa katikati ya shelfu ndefu za makabati, akakatisha kulia, akatembea kidogo kama kisha akakata kulia tena, akasonga kwa nusu dakika akakata kushoto. Hapo akatembea kidogo lakini kabla hafika alipokusudia alishtushwa na macho yake yalipomuona Mzee mmoja mwenye upaa katikati ya kichwa lakini pembeni zikiwepo nywele zenye mvi nyeupe na kijivu, kidevuni akiwa na ndevu nyingi, Kilichomshtua Sajenti ni kuwa, hakujua kuwa mule ndani kulikuwa na mtu, hivyo kitendo cha kumuona Yule mzee kilimfanya akose utulivu. Yule mzee hakuwa amemuona Sajenti Warioba, alikuwa akiendelea kubonyeza vitufe vilivyokuwa katika lile kabati.
Sajenti akaachana naye, akasonga mpaka lilipokuwepo kabati lenye shelfu la rangi ya dhahabu, akafika kwenye kisanduku kilichoandikwa JW16. Akabonyeza kitufe Fulani, taa ya kijani ikawaka kisha kioo cha kile kisanduku kikawaka na kumuamuru aweke dole dumba, akaweka. Akaambiwa asubiri wakati ombi lake linashughulikiwa, baada ya dakika moja unusu, yakatoke maandishi “ Welcome Jacob Warioba” “Kuthibitisha kuwa ndiye, weka msimbo wako” Sajenti akaweka msimbo wa siri. Kwenye kioo pakaandika “ Welcome” kisha sanduku likafunguka. Sajenti akatoa ndani ya lile sanduku bahasha ya kaki, kisha akaifungua ile bahasha akaangalia ndani yake, akajiridhisha, akachukua bahasha nyingine, akaitoa kisha akaingiza mkono mfukoni na kuitoa ile chipu alafu akaiweka ndani ya ile bahasha. Akairudisha ndani ya sanduku. Akiwa anaendelea na hayo punde sauti katika lile kabati ikasikika ikisema “Jacob Warioba has two minutes left, hurry up to avoid inconvenience” Sajenti kwa upesi akazikagua zile nyaraka zingine na alipojiridhisha akiwa amebakiwa na dakika moja akarudisha vizuri akiwa kaiweka ile chipu kwenye bahasha.Akafungu sanduku, kisha yakatokea maandishi yakimtaka aweke msimbo mpya wa siri, akaweka, akaamriwa aweke dole gumba akaweka, akaondoka.
Zikiwa zimebaki sekunde akaondoka akiwa amebeba bahasha moja ya kaki ile aliyokuwa ameishika mwanzoni, akasonga mpaka alipofika mahali alipomuona Yule mzee mwenye mvi, hakumuona, mzee alikuwa ameshaondoka. Akaenda mpaka kwenye lile kabati alilokuwa Yule mzee, akakuta kabati lile limeandikwa BL21. Sajenti akatoka, akafika mpaka zilipoofisi ya Yule Dada SHDC21.
“ Umeshakamilisha ulichokuwa unakihitaji?” Yule akauliza akimtazama Sajenti.
“ Bilashaka! Nimekamilisha. Nashukuru sana Dada” Sajenti akasema. Yule Dada akampa karatasi Fulani, Sajenti akaijaza, alipomaliza akamrudishia. Wakaagana, wakati Sajanti anaondoka akakumbuka jambo. Akarudi kwa Yule Dada.
“ Samahani Dada kama nitakuwa msumbufu, umenihudumia vizuri kabis, nimefurahi sana. Sitakuwa na muungwana endapo sitauliza jina lako, tafadhali naomba nikufahamu unaitwa nani?” Sajenti akasema huku uso wake akiweka sura ya urafiki.
“ Naitwa Belinda, mbona nimekuhudumia kawaida, Mr. Jacob” Belinda akasema huku akitabasamu na kufanya uzuri wake uliokuwa umejificha udhihirike.
“ Niite Mr. Warioba, sipendi kutumia Jacob, niite jina hilo nitashukuru sana Belinda” Sajenti akasema kwa utani na kumfanya Belinda azidi kucheka.
“ Hahah! Nimekuelewa Mr. Warioba, nitakuita kama ulivyosema” Belinda akasema akimtazama Sajenti kwa hamu ya mazungumzo yaendelee. Lakini jambo Fulani la kushtusha akaliona Sajenti, alishangaa kuona kusoma jina “Agricola Kihohozi” katika beji aliyokuwa ameivaa Belinda. Macho yake yasimama kwa sekunde katika beji aliyokuwa ameivaa Belinda jambo hilo likampa wasiwasi Belinda na kumfanya ajitazame kifuani, Belinda akashusha pumzi baada ya kugundua alichokuwa akikiangalia Sajentim kisha akasema;
“ Umenishtua sana. Kumbe ni hii beji. Jina langu la ofisini na Agricola kikohozi. Ila jina la ubatizo naitwa Belinda. Nalipenda Belinda na ndilo ninalolitumia kwa marafiki zangu, hata hapa ofisini nalitumia pia. Ulidhani nimekuongopea?” Belinda aliongea akiwa ametabasamu.
“ Hapana, ila sijui kilichonifanya nishtuke ni nini. Huenda nilidhani umenidanganya. Hahah” Sajenti akasema akiwa anacheka. Kisha akaendelea;
“ Nimefurahi kukufahamu Belinda, naomba nikuache, si ulinipa namba zako. Nimezihifadhi, nikifika nyumbani tutawasiliana kwa mengi zaidi” Sajenti akasema kisha akamuuacha Belinda pale ofisini.
Baada ya kuondoka katika jengo la SHDC Ambalo kirefu chake ni Storage and Handling of Documents Collection; ambalo ni shirika lisilo la kiserikali ambalo makao yake makuu yapo uingereza. Ambapo kazi yake ni kuhifadhi na kutunza nyaraka za wazi na za siri za watu binafsi, makampuni, mashirika ya kiserikali, miongoni mwa nyaraka zingine, SHDC huhifadhi nyaraka kwa mfumo wa nakala ngumu na nakala za kieletroniki ambazo zipo kwenye mfumo wa softcopy. Kutokana na kukua kwa teknolojia na uibaji wa nyaraka za watu binafsi, mashirika, na makampuni, shirika hili limejipa kazi ya kuhifadhi nyaraka hizo mahali salama na tangu kuanzishwa kwake mwaka 1940 huko nchini uingereza haijawahi kutokea kuibiwa au kupotea kwa nyaraka zilizowasilishwa katika shirika hili. Hii ndio sababu watu wenye nyadhifa kubwa serikali, wamiliki wa makampuni na mashirika hulitumia shirika hili kuzihifadhi nyaraka zao hasa nyaraka zilizo za siri. Katika shirika hili Sajenti Warioba alihifadhi nyaraka zake na vitu vyake vikiwemo Kadi za siri za benki pamoja na funguo za nyumba ya siri aliyokuwa ameijenga ambayo watu wengi walikuwa hawaijui.
Sajenti alivyotoka aliingia moja kwa moja Benki akiwa na kadi yake aliyoitoa kwenye ile bahasha aliyoichukua kule SHDC. Kadi ile ya Benki ilikuwa imesajiliwa kwa majina mengine ambayo Sajenti alikuwa akiyatumia. Katika kazi za kijasusi ni kawaida kwa jambo hili. Majasusi huwa utambulisho wa majina mbalimbali, na hata katika masuala ya kifedha husajili akaunti zenye majina tofauti tofauti kwa usalama wa baadaye. Sajenti baada kutoa milioni ishirini benki akatoka, na moja kwa moja akaelekea kwenye Yard za kuuzia magari. Tayari aliona usumbufu wa kupanda magari ya kukodisha, lakini pia aliona hatari ya kufahamika kwa urahisi Kupitia kupanda usafiri tofauti tofauti.
Akafika katika Yard moja yenye magari mazuri iliyopo maeneo ya Mnazi mmoja iliyopo pembeni ya barabara iendayo kariakoo.
“ Sasa hapa nitakuwa huru kufanya kazi zangu, haya masuala ya kupanda usafiri wa umma yatanihatarishia usalama wangu” Sajenti akawaza.
“ Niwekeeni tinted kwenye vioo, si mnafanya na huduma hiyo?” Sajenti akawauliza wale wauzaji wa magari baada ya kukamilisha malipo ya ununuzi wa gari.
“ Ngoja tukuwekee Boss, haichukua muda mrefu” Moja wa wauzaji magari akasema. Baaada ya muda kitambo tayari shughuli ya kuweka tinted kwenye vioo ikawa imekamilia,. Sajenti akamalizana nao, kisha akaondoka pale akiwa na gari lake jipya.
“ Fernanda masikini, sijui yupo wapi, miezi kadhaa imepita tangu ni nimkimbie pale hotelini. Sijui atakuwa salama, atakuwa amenitafuta mpaka amechoka, I’m sorry for this Fernanda. Haikuwa lengo langu kukukimbia, sitaki uingie katika shida, hawa watu sio wazuri kabisa. Lakini Fernanda atakuwa wapi” Sajenti alikuwa akiwaza huku akiendesha gari yake akiwa tayari keshafika maeneo ya fire, sasa alikuwa akiitafuta magomeni.
Mawazo yake yakampeleka mpaka kwenye ile meli ya ambagon, siku alipokutana na Fernanda, alikumbuka siku ile akiwa kwenye Casino lililomo ndani ya Meli ya Ambagon. Fernanda akiwa katika mavazi ya kikahaba akamfuata,
“ Fernanda was sweet, cute with the power of love” Sajenti akasema kwa sauti ndogo huku uso wake ukichanua kwa tabasamu. Akakumbuka walivyofika kisiwa cha Montenegro kule Brazil kisha wakaenda kwenye nyumba ya Fernanda iliyopo Juques.
“Lazima nitarudi Copacabana, raundi hii sitaenda kwa kazi bali nitaenda kustarehe na kipenzi change Fernanda. Fukwe za Copacabana na Ipanema ni kama fukwe za peponi kwa uzuri. Sikuwahi kuhisi kuna upepo wenye ladha tamu kama upepo wa fukwe za Copacabana, Fernanda uko wapi mpenzi wangu, nimekumbuka raha ulizonipa kule Copacabana” Sajenti akawaza bado akiwa ndani ya gari. Kumbukumbu akiwa Brazil jijini Rio de jeneiro zilikuwa ziliranda randa katika kichwa chake. Zilikuwa kumbukumbu zilizorejesha furaha yake moyoni, licha ya kuwa zilikuwa zimepita lakini zilikuwa zimeacha alama ubongo isiyofutika. Mawazo ya Sajenti yalikatika baada ya kufika mbele ya geti jeusi, alikuwa ameshafika, akasimamisha gari kisha akachukua ile bahasha ya kaki aliyoichukulia kule SHDC kisha akatoa funguo na kifaa Fulani chenye vitufe viwili. Ilikuwa rimoti ya geti, akabonyeza geti likafunguka, Sajenti akapokelewa na jumba kubwa ambalo mbele yake kulikuwa na majani yaliyoota hovyo hovyo kutokana na kutokutunzwa. Sajenti akaingiza gari kisha akabonyeza rimoti geti likajifunga.
“ Oooh! Nimerejea tena, ni mieiz kadhaa tangu niondoke hapa, bado hapajaharibika sana, majani haya yameota hovyo hovyo kutokana na kutokuwepo mtu wa kuyatunza, Sajenti baada ya kuegesha gari lake akashuka, akaanza kuzunguka kwenye nyumba yake kuikagua. Maua ya bustani yaliota hovyo hovyo, alizunguka upande wa pili lilipo bwawa la kuogelea, hapo akakuka maji yakiwa na majani majani yaliyopeperushwa na upepo, akazunguka kwa nyuma kabisa, moja kwa moja akaliendea bwawa la samaki wa mapambo aliokuwa akiwafuga, alisikitika kuona samaki wote walikuwa wamekufa siku nyingi kutokana na kukosa chakula. Sajenti akachukua fungua na kuingia ndani. Ndani kulikuwa na vumbi licha ya kuwa jumba lilikuwa limefungwa kwa vioo. Harufu ya uvundo kwa mbali ilizichezea pua yake, upesi akaenda kufungua mapazia na madirisha kuruhusu hewa iingie. Akaingia ndani kabisa kulipo na maktaba ya ile nyumba, akachukua kijarida kimoja chenye picha ya mtu aliyeshika ndoo ya maji pamoja na brashi. Akatoa simu akabinya binya kisha akaweka namba sikioni.
“ Hallo! Mr. Zaburi hapa, naomba mje hapa Mbezi Magari Saba kunifanyia usafi, msichelewe. Nashukuru” Sajenti akaongea na simu kisha akakata. Baada ya dakika thelasini, kampuni ya usafi ya TCS Iliwasili ikiwa na vijana wawili na mabinti wawili.Sajneti aliwapa maelekezo kisha akatoka kwenda kula kwani tayari ilikuwa imefika saa sita mchana, njaa ilikuwa imembana kwani tangu jana alikuwa hajatia kitu mdomoni..
SEASON 1 INAISHIA HAPA, ENDELEA NA SEASON 2
MWISHO
0 comments:
Post a Comment