Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

THAMANI YA FUKARA - 1

  

IMEANDIKWA NA : MKAPA JR

********************************************************************************

Simulizi : Thamani Ya Fukara

Sehemu Ya Kwanza (1)


Sehemu ya kwanza-01.


"Kama unajua hujavaa soksi au sare zako ni chafu naomba upite mbele mara moja kabla sijaanza kukagua,hakuna mda wa kupoteza na endapo nikikuta huko adhabu utakayoipata lazima ukasimlie".Ilikuwa ni sauti ya mwalimu wa zamu katika shule ya Rombo juu iliyopo mkoani Arusha,kila mwanafunzi alijiangalia kuhakikisha kama yuko salama kabisa.

"Naanza sasa kukagua nikikukuta huko utanitambua"mwalimu yule aliyekuwa anaitwa Bernard aliongea huku fimbo ikiwa mkononi,alianza kupita kwenye mistari ya wanafunzi huku akimkagua kila mmoja,taratibu alianza darasa la kwanza mpaka la saba bila kumkuta hata mmoja, wengi wao walikuwa mbele wakingoja adhabu kutoka kwa yule mwalimu aliyeonekana kuwa mkali sana,alikuwa anafundisha masomo ya hesabu kutokana na ukari wake alichukiwa na wanafunzi karibia wote,kila mwanafunzi alikuwa anahakikisha hafanyi makosa mbele ya yule mwalimu.

"Haya wengine wote mwende madarasani na huko sitaki kusikia kelele,viongozi wa madarasa hakikisheni mnaandika majina ya wale watakao piga kelele"Mwalimu Bernard aliongea kwa sauti ya juu sana,wanafunzi walitawanyika kimya kimya kwenda madarasani kwao.

"Eeh! Nanyinyi kwa nini hamfati sheria za shule zinavyosema?kila mmoja anyooshe mikono juu aanze kuita mvua"aliongea mwalimu Barnard.Wanafunzi wote walifanya vile,hakika yalikuwa mazoezi magumu yaliyokuwa yanaumiza mikono, mwalimu Barnad aliendelea kuwasimamia huku wanafunzi waliokuwa wanaonekana kuchoka mikono walikuwa wakichapwa fimbo nyingi sana.

"Kila mmoja ashike ndoo aende mtoni,nahitaji ndoo saba saba za maji kwa kila mmoja"mwalimu Bernard aliongea huku akiingia ofsini na kuchukua vitabu kwa ajili ya kuanza kipindi,lakini alipotoka ofsini kwake alishangaa kumuona mwanafunzi mmoja aliyekuwa amekaa kibarazani.

"We sinimekwambia kuwa uende mtoni?na hapo unafanya nini?mwalimu Bernard alimuuliza yule mwanafunzi wa kiume aliyekuwa anaitwa Gabi.

"Hapana mwalimu mkono wangu unauma,hebu cheki ulivyovimba"aliongea Gabi huku akimuonyesha mwalimu ule mkono.

"Nimesema sitaki sababu ninachotaka ni maji ndoo saba,kadri unavyozidi kuchelewa ndivyo utakavyokosa vipindi"

"Sasa mwalimu hapa ndoo nitaibebaje?Gabi alimuuliza mwalimu.

"Huwa sitaki mabishano na mwanafunzi yeyote,piga magoti hapo"mwalimu Bernard aliongea huku akirudi tena ofsini,hazikupita sekunde nyingi alirudi na fimbo mkononi,moyo wa Gabi ulienda mbio sana,kipigo cha yule mwalimu alikuwa anakijua vyema.

"Shika kucha"aliongea mwalimu Bernard huku akinua fimbo yake na kuanza kumchapa Gabi,Gabi hakuwa na ujanja wowote pamoja na kuwa mkono wake ulikuwa unamuuma lakini alikubari adhabu ile.

"Narudia tena,nataka maji tena wewe adhabu imeongezeka nahitaji maji ndoo kumi,unaona wenzako wale wanarudi wewe bado uko hapa?ole wako nitoe maswali ukose hata moja ndo utanitambua"mwalimu Bernard aliongea huku akichukua vitabu nyake na kuelekea darasani.

Gabi alibaki akiugulia maumivu ya fimbo zile,alienda mpaka stoo akachukua ndoo kisha akaelekea mtoni,kwa mwendo wa taratibu kabisa alikutana na wenzake waliokuwa wakirudi kwa mara ya pili.

"Yule mwalimu sio wa kumletea jeuri hata kidogo,anaweza kukua"aliongea mwanafunzi mmoja lakini Gabi alibaki kimya,moyoni alimchukia yule mwalimu lakini hakuwa na lakufanya,mkono wake wa kulia ndo ulikuwa unamuuma,hakuweza hata kubeba ndoo iliyokuwa tupu,yote hayo mwalimu Bernard hakuweza kumhurumia.

Baada ya kufika mtoni walichota maji kisha wenzake wakamsaidia kumtwisha ile ndoo.Hadi inafika saa sita mchana Gabi hakuwa amemaliza,wenzake walimaliza na kumuacha yeye aliyekuwa anasuburia wanakijiji waje pale mtoni ili wamsaidie kumtwisha ile ndoo.

Saa saba ndo alikuwa anamaliza ile adhabu,aliingia darasani na kukuta yale yaliyofundishwa yakiwa yamefutwa tayari, hakuweza kuelewa kitu chochote.

Mida ya masomo iliisha, wanafunzi wote waliruhusiwa kurudi makwao.

"Mwanangu vipi mbona unaonekena mnyonge sana leo au maumivu ya mkono yamezidi?ilikuwa ni sauti ya mama yake Gabi aliyekuwa anaitwa Bi Gaudensia.

"Hapana mama,leo tumepewa adhabu wanafunzi wote waliokuwa hawana soksi"Gabi aliongea huku akionekana kusikitika.

"Ngoja nimalizie kile kibarua, nadhani ndani ya wiki hii nitakununulia"aliongea mama yake Gabi.Gabi alikuwa anaishi na mama yake hasa baada ya baba yake kufia machimboni,maisha yao yalikuwa ya kikawaida sana,mda mwangi mama yake alikuwa mtu wa kufanya vibarua kwa ajili ya kuendesha familia yake ile Gabi alikuwa mtoto wa pekee.Jioni ya siku ile waliambatana wote Gabi na mama yake mama yake kwenda shambani Gabi hakuweza kufanya chochote zaidi aliishia kumtazama mama yake aliyekuwa analima kwa juhudi kubwa ili aweze kumarizia kile kibarua apate pesa ya kumnunulia mwanaye soksi pamoja na matumizi mengine ya pale nyumbani.

Kesho yake asubuhi kulipambazuka na hali mvua ndani ya hilo jiji la Arusha, Gabi alijikuta anachelewa kuamka hivyo alifika shuleni na kukuta vipindi vikiwa vimeshaanza tayari,alimkuta yule mwalimu Bernard.

"Piga magoti,kwanini umechelewa?yule mwalimu alimuuliza.

"Hapana mwalimu kwenye hali kama hii mkono wangu unauma sana"aliongea Gabi.

"Haya pita ukae"Gabi alifurahi kuepukana na bakora za yule mwalimu.

"Jana nimeacha zoezi hapa bila shaka kila mtu alilifanya,hivyo monita kusanya madaftari yote uyalete hapa"mwalimu Bernard aliongea.Mara moja lile zoezi la kukusanya daftari lilianza.

"Mwalimu huyu hajayafanya yale maswali"ilikuwa sauti ya monita ikimwambia mwalimu.

"Nani?apite mbele"moyo wa Gabi ulienda mbio sana alisimama kisha akamfuata yule mwalimu.

"Yaani wewe kila kosa ni wewe,uchelewaji wewe uchafu wewe nimekusamehe asubuhi lakini hapa siwezi kukusamehe tena,shika masikio"aliongea mwalimu Bernard huku fimbo ikiwa mkononi.

"Mwalimu,usimpige huyo adhabu yake nitaibeba mimi mwenyewe"ilisikika sauti ya kike kutoka nyuma darasa,wanafunzi wote waligeuza shingo kumtazama aliyesema yale maneno.


Ile sauti iliposikika kila mwanafunzi aligeuka kumtazama yule binti aliyesema yale maneno.Alikuwa ni binti aliyekuwa anaitwa Layla Gozibert.Lalya alikuwa binti kutoka kwenye familia ya kitajiri sana,mda mwingi shuleni pale alikuwa anakuja na gari la kifahari huku akiwa na dereva wake.Jambo lile lilimpa umaarufu sana,baadhi ya wanafunzi walikuwa wanamuogopa sana.Shida ni moja alitokea kumpenda kijana fukara sana.Hakuwa mwingine bali ni Gabi.Mara nyingi alimuonyesha vitendo vya wazi lakini Gabi hakuweza kuelewa chochote,hata Layla alipokuwa anamsalimia Gabi hakuitikia ile salamu.Jambo lile liliweza kumuumiza sana Layla,hata shuleni hakujisomea zaidi ya kumuwaza Gabi.

"Mwalimu naomba usimpige huyo,adhabu yake nipe mimi"aliongea Layla bila kuhofia chochote.Mwalimu alibaki ameduwaa sana.Hata Gabi mwenyewe jambo lile lilimshangaza sana alibaki kumtazama Layla.

"Mna undugu gani hadi ubebe adhabu yake ilhari wewe haikuhusu?"aliuliza mwalimu Bernard.

"Nimejitolea juu ya hilo"Layla alijibu kwa ujasiri.

"Sawa kwakuwa umejileta nawe adhabu lazima uipate"aliongea mwalimu Bernard,alimchapa Layla fimbo za miguuni,mara baada ya kumaliza kwa Layla alihamia kwa Gabi.Mwalimu Bernard alipomaliza kutoa adhabu zile aliendelea na kipindi.Layla alidondosha chozi si kwa kulia kwa sababu ya fimbo bali kulia kwa kumuona Gabi akipigwa mbele yake.

"Layla shoga yangu hivi nawe leo umekuwaje?"alimuuliza mwanafunzi mmoja aliyekuwa anaitwa Doris.

"Tafadhali Doris naomba niache"aliongea Layla kwa ghadhabu.

"Shoga yangu unanichekesha ujue,hivi hata kama ni upendo ndo kwa kijana hoe hae kama yule?naamini bado ana mambo ya kitoto sio bure,haya shoga yangu"Doris alionekana kumshangaa rafiki yake yule aliyejitolea kuibeba adhabu ya Dabi.Kila mwanafunzi alitamani kumuuliza Layla lakini wengi wao walimuogopa.Layla hakuwa na rafiki yeyote pale shuleni zaidi ya Doris mtoto wa tajiri Kama ilivyokuwa kwake.

Mda wa masomo ulipoisha kila mwanafunzi alirudi makwao tofauti Layla aliyebaki pale shuleni akimngoja dereva wake.Haukupita mda mwingi dereva wa Layla alilipaki gari kisha Layla akaingia ndani ya gari akiwa kimya kabisa.Yule dereva wake aligeuza shingo kumuangalia Layla lakini alishtuka kumuona akidondosha chozi,

"Leo una nini?au tupitie hospital unaumwa?aliuliza yule dereva aliyekuwa inaitwa Juma.Lakini Layla hakujibu zaidi aliendelea kuyafuta machozi yaliyokuwa yanamtoka,

"Endesha gari kwa kasi"aliongea Layla kwa sauti ya kwikwi,dereva alitii wito.Safari yao iliishia kwenye jumba la kifahari sana,hapo ndipo palikuwa nyumbani kwao na Layla.Gari ilisimamishwa na Layla akashuka huku macho yake yakiwa mekundu sana kwa sababu ya kilio,alipitiliza mpaka chumbani kwake bila hata kuwasalimia wazazi wake aliowakuta sebuleni.

"Leo huyu ana nini?"aliongea Gozibert akimuuliza mkewe,

"Nenda chumbani kwake ukamuulize kama anaumwa"aliongea Gozibert,mkewe alitii wito, baada ya kufika chumbani kwa Layla alimkuta bado akiwa anadondosha machozi,

"Leo unaumwa au umepatwa na tatizo gani?"aliuliza mama yake,lakini Layla hakutaka kusema kitu zaidi alimuonyesha mama yake alama za fimbo miguuni,

"Mwaliimu kanichapa bila kos.."alishindwa kuongea, aliangua kilio kwa sauti kubwa,jambo lile lilimfanya baba yake aliyekuwa sebleni kukisikia kile kilio,aliinuka mpaka chumbani kwa mwanaye,

"Nani kakufanya hivi?"aliuliza baba yake kwa sauti ya ukali,

"Mwalimu Bernard babaa kanipiga bila kosa lolote"

"Haya sawa yafute machozi naamini hataweza kukaa pale shuleni lazima atahama"aliongea baba yake Layla.Layla alifurahi sana kwani ndo jibu hilo alilokuwa analisubiri.

Kesho yake asubuhi pale shuleni ilikuwa siku ya usafi pale shuleni,walimu watatu walianza kukagua kila mtu,wale waliojihisi kutokamilika walikuwa wakijipeleka mbele kabla hata walimu hawajawafikia,Gabi hakuwa na soksi na hata mkono wake ulikuwa haujapona vizuri,alizipiga hatua kwenda mbele lakini alishangaa anashikwa mkono,aligeuka macho yake yalikutana na Layla,

"Usijali wewe bado mgojwa hivyo acha adhabu yako niibebe mimi,wewe chukua hizi soksi uvae"aliongea Layla huku akizivua zile soksi na kumkabidhi Gabi aliyebaki kushangaa tukio lile,hata baadhi ya wanafunzi walibaki kushangaa, Gabi hakuweza kuzikataa alizipokea Kisha akazivaa na kurudi msitalini.Layla aliungana na wale ambao hawakuwa na soksi pamoja na sare chafu.

Kutokana na kuwa mdogo kijana Gabi hakuelewa chochote hasa kuona binti wa kitajiri kama yule anajitoa kwa ajili yake,marafiki zake walijitahidi kumshauri kuwa tayari Layla kazama kwake lakini Gabi alipingana nao.

"Acheni masihara bhana FUKARA kama mimi atanipeleka wapi?"

"Wewe huoni anajitoa kwa ajili yako,yuko tayari hata kupigwa lakini wewe usiguswe,mtoto kapenda yule sema anashindwa kuongea tu",

"Bahati kama hizi huwa hazitokei kwangu,yaani mtoto yuko waziwazi kabisa yule,ama kweli penye miti mingi hapana wajenzi".Yalikuwa maneno ya marafiki zake na Gabi wakijaribu kumshauri kuwa tayari kapendwa,lakini hakuweza kukubaliana na yale maneno,yeye alijiona kuwa hana hadhi ya kupendwa na mtoto wa kitajiri kama yule.

Layla aliendelea kuumia moyoni,lakini moyo wake ulikuwa mzito sana kumtamkia Gabi kuwa anamhitaji,kawaida ya wasichana walio wengi wanapenda lakini wanashindwa kumtamkia yule waliyempenda,hatima yake wanaendelea kuumia moyoni,hakuna ugojwa mbaya kama kupenda,ugojwa huo ni hatali sana,huo ndio ugojwa uliompata Layla kwa kijana Gabi,moyo wake ulikuwa mzito sana kufunguka,yeye aliamini kuwa kwa vitendo anavyomuonyesha Gabi huenda atamuelewa lakini jambo lile lilikuwa tofauti,Gabi hakuelewa chochote hasa hali aliyokuwa naye alijiona mtu wa chini sana.Mpaka sasa wapo wasichana wengi wanaopenda lakini wanaogopa kumwambia yule waliyempenda kwa kuhofia kuwa wataonekana malaya,hii inaendelea kuwafanya wabaki kuumia.

"Nifanyeje ili Gabi awe mikononi mwangu?mbona kila ishara nimemuonyesha kuwa namhitaji kimapenzi lakini bado hataki kunielewa?alijiuliza Layla,machozi nayo hayakuwa mbali na mboni zake yaliendelea kumtoka mithiri ya mtu aliyempoteza ndugu yake.




Jambo la Layla kumfikiria sana Gabi lilisababisha aanze kushuka kimasomo,kwenye nafasi kumi za juu hakuwemo tena,mda mwingi alikuwa mtu wa mawazo, wazazi wake walipojaribu kumuuliza tatizo hakuweza kuliweka wazi.

Ilikaribia mitihani ya mwezi ya sita,Doris rafiki yake Layla alijaribu kumshauri kuwa aachane na yale mawazo lakini Layla hakutaka kusikia la mtu,furaha yake ingerejea pindi ambapo angeliweza kumuweka Gabi mikononi mwake,lakini angemweka vipi mikononi mwake ilihari moyo wake ni mzito hautaki kusema hisia zake?yalikuwa maumivu ya kila siku.

"Shoga yangu utanisaidia vipi ili nimuweke kwenye himaya yangu?",Layla alimuuliza Doris,

"Kwakweli shoga yangu bado ni mtihani mgumu sana, nadhani tufikirie masomo kwanza halafu haya mambo tutayafanya baada ya kumaliza mtihani"aliongea Doris,

"Nini?"aliwaka Layla,yaani tuachane nayo?hivi unajua moyo wangu unaumia kiasi gani?au hujui kila siku natoa chozi kwa ajili ya Gabi?sasa unaponiambia hizi habari tuziweke kando nashindwa kukuelewa kabisa".

"Naelewa shoga yangu lakini huna budi kuyaacha hayo mambo,unatakiwa ufikirie mitihani itakayoanza wiki ijayo"aliongea Doris akijaribu kumtuliza Layla lakini juhudi zake ziligonga mwamba Layla hakutaka kusikia chochote.Wakiwa kwenye maongezi yale mara mbele yao alipita Gabi,Layla alinyanyuka na kumuita Gabi lakini hakusimama zaidi alikaza mwende,Layla alibaki amesimama huku machozi nayo hayakuwa mbali.

"Umemuona?umeona alivyo sijui nimfanyie nini mimi"aliongea Layla huku kitambaa kikiwa mikononi mwake kwa ajili ya kufutia machozi.Doris alikuwa na kazi ya kumfariji Layla,

"Kesho nitaandika barua kisha nitakupa umpelekee"aliongea Layla kwa sauti ya chini na yenye huzuni ndani yake.

"Basi jitahidi twende darasani shoga yangu"aliongea Doris huku akimuinua Layla.Hata mda wa masomo macho ya Layla yalikuwa kwa Gabi mda wote.Mda wa masomo ulipoisha wanafunzi waliruhusiwa kwenda makwao,Gabi alifika nyumbani kwao na kumkuta mama yake akiwa nje anachambua njugu mara baada ya salamu maongezi ya hapa na pale yalishika nafasi,

"Leo nimekimaliza kila kibarua hivyo saa moja jioni naenda kuchukua hera halafu soksi nitakununulia kesho"aliongea mama yake Gabi,

"Soksi ninazo tayari kuna rafiki yangu kanipa tena ni mpya kabisa"aliongea Gabi,mama yake alishtuka na taharuki akauliza,

"Usije kuwa umeiba halafu unadanganya"

"Hapana mama we niamini tu mimi sina sifa za wizi"alijibu Gabi,mama yake alifurahi hiyo hera aliyokuwa amepanga kununua soksi ilifanya matumizi mengine.

Usiku huo kwa upande wa Layla ulikuwa mgumu kabisa,hakupata hata lepe la usingizi,hakuukumbuka tena kuwa kuna mitihani itakayoanza siku chache zijazo,kalamu ilikuwa mkononi mwake huku karatasi ikiwa juu ya meza,alikuwa ameliangalia paa la nyumba huku mkono wake mmoja ukiwa shavuni,alifikiria maneno ya kumwandikia Gabi,lakini alipokuwa kwenye hali ile mara machozi yalimtoka na kudondokea kwenye ile karatasi,alitafuta nyingine lakini nayo aliilowesha kwa machozi,hadi inafika saa saba za usiku alikuwa bado hajaandika neno lolote pale kwenye karatasi,alifikiria maneno yatakayomfurahisha Gabi lakini kila neno aliliona halifai,mpaka usingizi ulimpitia pale pale akiwa bado hajaandika neno hata moja.Asubuhi ya siku ile alichelewa kuamka mpaka pale mama yake alipomuamsha,alinishangaa kujikuta akiwa amelala pale pale mezani,mikono yake ilikuwa na upele uliosababishwa na kung'atwa na mbu,alipoitazama karatasi ile alikumbuka kuwa jana yake usiku alikuwa ameiandaa kwa ajili ya kumwandikia barua Gabi,

"Au shuleni utaenda kesho? maana mda umeenda sana sahivi saa mbili"aliongea mama yake Layla,

"Hapana mama wacha niende, mwambie Juma ajiandae basi"aliongea Layla huku machoni kwake kukiwa bado na usingizi,

"Sasa nisipoenda shuleni Gabi wangu nitamuona wapi?lazima niende hata kama ni saa nne"alijisemea Layla.Majira ya saa mbili nanusu asubuhi ndo alikuwa anafika shuleni,alikuta vipindi vikiwa tayari vimeanza,lakini hakuhofia kitu chochote,alishuka kwenye gari na kuingia darasani ambapo alimkuta mwalimu akiwa anaendelea na kipindi,yule mwalimu hakumuuliza kitu chochote zaidi ya kumrusu kuingia darasani,walimu waliokuwa wanamjua baba yake Layla hakuna aliyeweza kumpiga Layla tofauti na Bernard ambaye alikuwa mwalimu mgeni kwenye shule ile.Baada ya kuketi kwenye nafasi yake Layla alihakikisha anamuangalia Gabi kwanza,alipohakikisha amemuona alitoa madaftari yake na kuanza kujisomea,lakini hakukawia usingizi ulimpitia,hadi kipindi kinaisha yeye alikuwa bado amesinzia.

Jumatatu mitihani inaanza hivyo kwenye somo langu ukipata chini ya hamsini ujue ntakula nawe sahani moja"aliongea yule mwalimu aliyekuwa anafundisha somo ya kiswahili,sauti ile ilimshtua Layla aliyekuwa usingizi alikurupuka usingizini na kumkuta mwalimu akimalizia kipindi.Mda wa kipindi cha mwalimu Bernard uliwadia,kila mwanafunzi alijiandaa kwa kipindi na mda mfupi aliingia mwalimu Bernard,Kama kawaida yake fimbo zilikuwa mikononi mwake,

"Shikamooni mwalimu"wanafunzi wote waliinuka na kumsalimia,

"Sihitaji salamu zenu,nawaomba mketi chini huku kila mwanafunzi daftari lake alifunue na kuliweka juu ya meza,au kama unajua hujaifanya kazi yangu pita mbele mapema tusije kusumbuana"aliongea mwalimu Bernard.Layla ile kazi hakuifanya hivyo alipita mbele mapema,mwalimu Bernard alianza kukagua mmoja baada ya mwingine, hatimaye alimfikia Gabi, alibaki kumtazama kazi alikuwa ameifanya lakini kati ya maswali matano hakupata hata moja,

"Nyie ndo vilaza darasani sasa mitihani inaanza jumatatu mnategemea nini?hebu shika huko fimbo tano zinakuhusu"aliongea mwalimu Bernard,Layla aliweza kuliona tukio lile hakuwa tayari kumuona Gabi akiadhibiwa kwa kuwa alikuwa amesimama mbele hivyo alianza kuzipiga hatua kumfuata mwalimu Bernard alikuwa tayari kumuadhibu Gabi.




Layla alizipiga hatua mpaka kwa mwalimu Bernard aliyekuwa anataka kuadhibu Gabi,darasa zima lilibaki kunshangaa Layla kila mtu alibaki na shauku ya kutaka kukijua kile atakachofanya Layla,

"Mwalimu mimi sijafanya kazi yako hivyo adhabu ya huyu ijumlishe na yangu"aliongea Layla kwa kujiamini hakuwa tayari kumuona Gabi akipigwa hivyo alisimama kidete kumtetea.Mwalimu Bernard kile kitendo cha Layla alikiona kama zarau,alimfuata na kumuadhibu fimbo nyingi za mabegani lakini bado hakuwa tayari kumuona Gabi akipata adhabu,

"We kama unaniua niue tu lakini mkaka wawatu muache"aliongea Layla, mwalimu Bernard alimshika mkono na kwenda naye ofsini mpaka kwa mwalimu mkuu,Mwalimu mkuu alipomuona Layla akilia haraka alimkataza mwalimu Bernard kuwa asimpe adhabu yeyote,ukali wa Gozirbert ambaye ni baba yake Layla aliujua vyema,hivyo Layla alirudi darasani na kumuacha mwalimu Bernard huko ofsini,kila mtu alitamani kujua kilichotokea kule ofsini lakini Layla hakuongea chochote,hiyo ndo ikawa pona pona ya Gabi,wanafunzi wengi waliuona upendo wa Layla kwa Gabi lakini bado Gabi alikuwa hajaelewa hasa kwanini Layla anajitoa kwa ajili yake swali lilibaki kichwani mwake.Mda kidogo alirejea mwalimu Bernard na kuendelea na kipindi hata zoezi lake kukagua alilisitisha baada ya kupewa onyo na mwalimu mkuu kuwa asimguse tena Layla.

"Ujue Gabi nakushangaa sana,hivi kwanini wewe ni mgumu kuelewa?unataka akufanyie nini mtoto wawatu?au unataka afe kwa mbele yako ndo uuone upendo wake?zinduka naamini bado umelala wewe"yalikuwa maneno ya rafiki yake Gabi aliyekuwa anaitwa Anord,

"Doh!we Anord acha kabisa sasa ananipenda mimi kwa lipi hasa?

"Ngoja nikwambie wewe siku zote upendo hauchagui,wewe unajiona FUKARA lakini una thamani kubwa kwake,na siku zote dalili za mtu anayekupenda utaziona tu,mfano awe tayari kujitoa kwa ajili yako,pili awe tayari kwa lolote juu yako,je hizo dalili hujaziona?nakumbuka juzi hukuwa na soksi lakini kavua zake kakupa huku adhabu yako akiibeba yeye,kilichobaki ni kunywa sumu na kufa mbele yako"aliongea maneno yale Anord kisha akanyanyuka kwenda kuketi kwenye nafasi yake akimuacha Gabi akiyatafakari yale maneno.

Ulifika mda wa mapumziko Layla alitoka nje akiwa na rafiki yake Doris,

"Shoga yangu leo umenifanya nivunjike mbavu kabisa"aliongea Doris,

"Kwanini?aliuliza Layla huku akisitisha mwendo na kusimama,

"Hivi mbona unataka kuelekea pabaya?yaani unataka kupenda kusiko pendeka na hakuna ugojwa mkubwa kama huo,hebu jaribu kujizuia vijana wengine huwaoni?aliongea Doris,

"Layla hakuwa na lakujibu zaidi alibaki emeinama,alitoa noti ya elfu kumi na kumkabidhi Doris,

"Mpelekee basi hiyo mwambie nimempa hela ya chai"aliongea Layla wakati akimkabidhi ile pesa Doris,Doris aliipokea na kuzuga Kama anaipeleka lakini alilizunguka darasa na kurudi huku akitabasamu,

"Eeh!amesemaje"aliuliza kwa shauku kabla hata hatamfikia,

"Kaipokea halafu kasema eti anashukuru sana na kila siku uwe unampa"alitunga uongo Doris,

"Waoooh!basi mpelekee tena na hii"aliongea Layla huku akitoa noti nyingine ya elfu ya tano Doris aliipokea lakini hakuifikisha kwa Gabi.

"Leo nalala tajiri hahaha mapenzi hayalazimishwi kama hakupendi hakupendi tu"alijisemea Doris,

"Yaani shoga yangu hakuna linaloshindikana mbele ya pesa huwezi amini kaonekana kutabasamu kabisa,hivyo lazima atajileta mdogo mdogo na mda sio mrefu atakuwa mikononi mwako"aliongea Doris maneno yale ya uongo yalimfanya Layla atabasamu na kupata matumaini mapya kuwa kama alivyosema rafiki yake siku sio nyingi Gabi atakuwa kwenye himaya yake.Hata usiku wa siku ile aliandika barua ndefu na kuweka pesa kiasi cha shilingi elfu arobaini,

"Hapa hawezi kuruka lazima nitamnasa"alijisemea Layla wakati akiikuja ile bahasha.Kesho yake asubuhi kulipambazuka na hali ya hewa nzuri hivyo Layla alijiandaa vyema na kuingia kwenye gari kisha safari ikaanza kuelekea shuleni,njiani alionekana kuwa na furaha tofauti na siku zote hadi Juma dereva wake alimshangaa,

"Leo sijui unanini maana sio kawaida yako"aliongea Juma,

"Yaani we acha tu kuna vitu vinaweka kukufurahisha bila kujali ni mda gani mimi kama mimi tangu jana nilikuwa na furaha mpaka sasa"aliongea Layla maongezi yao yaliishia pale walipofika shuleni,Layla alimuaga dereva wake kisha akaelekea darasani,baada ya kuhakikisha madaftari yake ameyaweka vyema alianza kuzunguka kumtafuta rafiki yake Doris ili ikiwezekana ujumbe ule umfikie Gabi asubuhi hiyo hiyo.Kila mwanafunzi alionekana kuwa bize na kufanya usafi,

"Nambie shoga yangu"Layla aliongea kwa uchangamfu wa hali ya juu mara baada ya kumfikia Doris,salamu ilishika nafasi yake,

"Sasa shoga yangu ujumbe wangu huu hapa mpelekee sasa hivi"

"We naye si usubiri nimalize kufanya usafi? aliongea Doris lakini moyoni alifurahi kwani alijua ule ujumbe kwa jinsi ulivyokuwa lazima pesa ingelikuwemo,

"Shika hii hapa lete ukute naendelea kufagia"aliongea Layla.Doris alikuwa mtoto wa kitajiri kama ilivyokuwa kwa Layla lakini alionekana msichana mwenye tamaa sana hata alipokuwa anamshauri Layla alikuwa na jambo lake kichwani.Doris aliupokea ule ujumbe alizunguka nyuma ya darasa na kuanza kuusoma,macho yake yalikutana na elfu arobaini,

"Wajinga ndio waliwao"alijisemea hayo maneno wakati zile pesa akiziweka kwenye mfuko wake wa sketi,hata ule ujumbe hakutaka kuusoma zaidi aliishia kuuangalia kwa nje jinsi ulivyokuwa umepambwa kwa maua mazuri,uliuweka mdomoni na kutafunatafuna kabisa,baadaye alirudi kwa Layla,alionekana kutabasamu hata Layla alipomuona alisitisha zoezi lile kufagia na kubaki kumtazama,

"Eeh!shoga yangu"aliongea Layla,

"We naye utulie nakwambia siku zote mambo mazuri huwa hayataki haraka,yaani nimemkabidhi ule ujumbe na ameusoma mbele yangu na baada ya kumaliza kuusoma nimemuona akitabasamu sijui maneno uliyoyandika kwenye ule ujumbe umeyatia asali nini?maana katoa tabasamu pana"aliongea Doris,Layla aliruka na kumkumbatia Doris kwa furaha bado hakuamini kama kweli Gabi aliyemuonyesha kila aina ya ishara leo hii kaukubali ujumbe wake hii aliiona kuwa ndo njia ya kuanza mapenzi na Gabi, Doris naye alitoa tabasamu la kinafiki huku moyoni akiwa na furaha ya kupokea elfu arobaini asubuhi ile,

"Yaani hapa jitahidi kila baada ya siku mbili uwe unampa hela naamini siku so nyingi atakuwa mikononi mwako"aliongea Doris,Layla hakuweza kupingana naye yeye alichokuwa anawaza ni kumpata Gabi,

"Lazima niwe tajiri kwa mwendo huu doh! elimu ya mjinga siku zote anaifaidi mjanja.




Siku hiyo ilikuwa siku ya furaha kwa Layla,alijiona mwenye bahati sana hivyo hata walipoingia darasani yeye alibaki kutabasamu kila alipokuwa anayakumbuka maneno ya rafiki yake kuwa ule ujumbe kaupokea Gabi,alijiamini hasa kwa maneno aliyokuwa ameyaandika kwenye ule ujumbe,hakujua kuwa rafiki yake ule ujumbe hakuufikisha alibaki kuachia tabasamu kila alipokuwa anamwangalia Gabi ambaye alikuwa bize na kujisomea,

"Mbona hata hageuki kunitazama?au atakuwa anatafakari yale maneno yangu matamu?lakini mbele ya pesa hawezi kuruka"alijiuliza Layla kisha jibu akalipata kichwani mwake,hata walimu walipoingia kufundisha Layla hakuwa na mda na masomo yeye aliendelea kumtazama Gabi tabasamu nalo halikuwa mbali na mashavu yake.Mapenzi yalimchanganya sana Layla hata masomo hakuyawaza tena,ile siku ilikuwa ijumaa hivyo mda wa masomo ulipoisha walimu walitoa tangazo kuwa jumatatu inaanza mitihani,

"Hivyo basi wanafunzi wote hakikisheni mnasoma kwa bidii"yalikuwa maneno ya mwalimu mkuu,alipokwisha kusema hayo kila mwanafunzi alirudi makwao.Layla siku hiyo alitamani angalau atembee na Gabi lakini alipoangaza macho Gabi hakumuona tena,

"Lakini ngoja hata kesho lazima nimtafute"alijisemea Layla.Layla alipofika nyumbani kwao kwanza alimuita baba yake na kumwambia kuwa afanye mpango mwalimu Bernard atolewe shuleni pale,mwalimu ambaye alikuwa anamnyima furaha hasa kila alipokuwa anamuona akimpa adhabu Gabi,baba yake hakutaka kumnyima furaha mwanaye hivyo alitoa simu na kuiweka sikioni,moja kwa moja alianza kuongea na mwalimu mkuu,

"Kwa gharama yeyote hakikisha yule mwalimu anatolewa pale shuleni"baba yake Layla alisikika akisema, mwalimu mkuu hakuweza kuyapinga maneno ya Gozirbert hivyo alianza kufanya mchakato wa kumpata mwalimu mpya.Layla alifurahi hasa baada ya kuyasikia maneno ya baba yake,alijua kabisa akitolewa mwalimu Bernard hakutakuwepo tena na mwalimu mwingine atakayemsumbua.

Kesho yake ilikuwa siku ya jumamosi,siku hiyo Layla alipanga kumutafuta Gabi mida ya mchana alijipitisha kwao na Gabi lakini hakumuona alipakuta pako kimya,kwa wakati huo Gabi alikuwa na mama yake shambani mbali na pale nyumbani kwao,

"Ngoja nitarudi badae"alijisemea Layla wakati anaongoza njia kuelekea nyumbani kwao,lakini alipofika nyumbani kwao baba yake alimwambia kuwa waende mjini kwakuwa ilikuwa wikendi hivyo walipanga kwenda kujifurahisha,Layla alikubali kwa shingo upande japo hakuwa na jinsi ya kukataa,hata jumapili nayo hakuweza kumuona Gabi zaidi aliandaa hela atakayompa kesho yake ambayo ilikuwa ni juma tatu.Usiku huo huo aliandika barua tena na kuweka pesa kisha akaikunja vizuri, kesho yake asubuhi kama kawaida alipofika shuleni alimkuta kila mwanafunzi yuko bize na kujisomea kwakuwa ndo ilikuwa siku yenyewe ya mtihani,

"Muwahishie basi ili hata kama atafanya mtihani aufanye akiwa na furaha"alisema Layla huku akimkabidhi ile bahasha iliyokuwa na pesa ndani yake, Doris aliupokea na kama kawaida yake alitoa pesa na kumdanganya kuwa ujumbe umepokelewa,

"Sasa rafiki yangu kamwambie basi leo tuonane walau niweze kuongea naye"aliongea Layla,

"Yaani wewe nakwambia kila siku kuwa mambo mazuri huwa hayataki haraka,unaweza kuharibu subiri mpango wote ukamilika usitake papara"aliongea Doris,Layla hakuweza kupingana naye,

"Kuja kushtukia mchezo lazima nitakuwa tajiri Tayari"alijisemea Doris.Mitihani ilianza kwa upande wa Layla maswali mengi yalikuwa magumu sana kutokana na kutokujisomea,baada ya wiki mbili mitihani iliisha hivyo walingoja matokeo.Mwalimu Bernard ndo alikuwa anatangaza yale matoke,

"Haya darasa la sita sikilizeni matokeo yenu"ilikuwa ni sauti ya mwalimu Bernard ikiwataka wanafunzi wawe makini kusikiliza matokeo,hadi wanatangazwa watu ishirini hakuna Layla wala Gabi,wanafunzi wote waliendelea kusikiliza kwa makini,darasa la sita lilikuwa na wanafunzi hamsini mwalimu Bernard alipotangaza hadi mtu wa thelathini na tano alimeza funda moja la mate kisha akaendelea,

"Namba thelathini na sita ameishika Layla Gozirbert naomba asimame"aliongea mwalimu Bernard,Layla alisimama kisha akakaa,tangu ajiunge na shule ya msingi hakuwahi kuvuka kwenye kumi bora,dhahili mapenzi yalichangia kwa kiasi,mwalimu Bernard aliendelea huku namba ya arobaini akiishika Gabi,mara baada ya yale matokeo wanafunzi waliruhusiwa kuondoka huku wakipewa likizo ya mwezi mmoja.

Doris na Layla waliagana huku wakihaidiana kukutana siku mbili mbeleni.

Siku zilisogea,Layla hakuacha kumuwaza Gabi mara nyingi alikuwa akijipitisha nyumbani kwao na alipokuwa anamuona moyo wake ulilidhika, alitamani walau shule zifunguliwe ili aweze kumpata Gabi kwa urahisi.Kwa upande wa Gabi yeye hakuwaza kitu mapenzi,hata shuleni aliona kama anapotezaa kutokana na kupata matokeo mabovu lakini mama yake alimtia moyo kuwa ajitahidi kuhitimu shule ya msingi.

Ilikuwa siku ya Juma pili,siku hiyo Doris alimtembelea Layla maongezi yao yaliendelea huku mada kubwa ikiwa ina mzungumzia Gabi,

"Umeona nilivyofanya vibaya kwenye matokeo yangu?sababu kubwa ni Gabi yaani nikimpata niko tayari hata nirambe damu yake,

"Hahahaha usiwaze sana mtu mwenyewe ataingia kwenye anga zetu siku sio nyingi uko nami tulia kabisa"aliongea Doris,Layla hakuwa nalakuzungumza maongezi yao yaliendelea na baada ya mda Doris aliaga kisha akaondoka,

"Aliyekwambia kuwa mapenzi yanatumia nguvu ya pesa ninani?hahaha unajaribu kupiga mbizi nchini kavu"alijisemea Doris wakati akirudi nyumbani.Baada ya kupita mwezi mzima hatimaye ilibaki siku moja ili shule zifunguliwe,Layla aliandika barua huku ndani ya ile barua akiweka maneno ya kumtaka Gabi waonane,hakuacha kuweka pesa noti tano za elfu kumi kumi alizikunja vyema na kuziweka ndani ya bahasha,

"UKIWA NA SHIDA YA PESA MPENZI USISITE KUNIAMBIA"yalikuwa maneno ya mwisho kwenye ila barua aliyokuwa ameiandika,usiku ule hakupata usingizi zaidi alizidi kumuomba mungu kuwahi kupambazuka ili akaonane na Gabi.




Kesho yake asubuhi Layla alijiandaa kwa haraka sana,mara baada ya maandalizi kukamilika akaingia ndani ya gari kisha safari ikaanza kuelekea shuleni.Baada ya kufika shuleni alimtafuta Doris na kisha akamkabidhi ile bahasha,Doris alichekea moyoni,

"Vipi leo umeandika nini?"alimuuliza Doris,

"Peleka bwana unachelewa"aliongea Layla moja kwa moja Doris alizunguka nyuma ya darasa na kuichana ile barua kisha pesa akaitia mfukoni,hata aliporudi alimkuta Layla akiwa na shauku ya kujibiwa,

"Ameipokea ila sasa sio kila ukitaka kutuma pesa uandika na barua anaweza kuchukia kila siku kusoma barua si unajua mtu mwenyewe bado tunambembeleza?kwa hiyo siku nyingine tuma pesa tu"aliongea Doris,Layla hakuweza kupingana naye alikubali.Siku zikasonga,baada ya wiki moja kupita Layla hakuona dalili yeyote ya Gabi kukubali ombi lake,Doris alizidi kumtia moyo kuwa awe na subira,

"Moyo wangu unaumia Doris nampenda sana Gabi,sasa kamuulize nini nimfanyie ili aweze kukubali kuwa namimi,kamuulize ili niweze kupata furaha yangu"aliongea Layla kwa uchungu mpaka machozi yakamtiririka,hakujua mtu anayemuwaza kiasi kile yeye hana hata mawazo naye,Doris alizidi kumfariji.

Ilikuwa siku ya juma tano usiku wa siku ile Doris aliwaza kuwa naye anahitaji mwanaume wa kuweza kumuondoa mawazo,alijaribu kuvuta picha mwanaume anayeweza kumpa furaha fikira zake ziligota kwa kijana Gabi,licha ya kwamba alitambua fika kuwa rafiki yake Layla anampenda japo hajamtamkia,

"Ngoja nitamuonyesha kuwa siku zote hisia hazifichiki,yeye si hataki kumwambia anamuogopa sasa mimi nitatoboa sufuria japo moyo wangu umempenda ghafla sitajali lolote litakalo tokea,mficha maradhi kifo humuumbua walisema wazee wetu"alijisemea Doris maneno hayo,hata usingizi hakuupata mawazo yote yalihamia kwa Gabi,

"Ngoja kupambuzuke,na zile hera alizokuwa ananipa Layla lazima nizipeleke kwake hakuna lishindikanalo mbele ya pesa"alijisemea Doris hakujali hisia za rafiki yake juu ya Gabi,usiku huo huo alianza kuandika barua ambayo alihakikisha anaipamba kwa maua mazuri huku maneno mazuri yakitawala kwenye barua ile,mara baada ya kulihakikisha hilo aliikunja vyema kisha akavuta shuka lake na kuutafuta usingizi ambao haukuwa mbali ukampitia.Alikuja kushtuka asubuhi na mara baada ya kumaliza kujiandaa alianza safari ya kwenda shuleni,hakutumia gari licha ya kuwa baba yake alikuwa tajiri na magari alikuwa nayo ya kutosha,hata baada ya kufika shuleni moja kwa moja alimtafuta Gabi na kumkabidhi barua ile,mkono wa Gabi ulikuwa mzito kuipokea ile barua lakini Doris alimlazimisha mpaka akaipokea Doris hakutaka kukaa pale zaidi aliondoka na kumuacha Gabi akiwa ameishika barua ile alisogea kwenye kona ya darasa na kuifungua kabla hajaanza kuusoma moyo ulimuenda mbio,mapigo ya moyo yaliongezeka hasa alipoona noti nyekundu za elfu kumi kumi,alizishika na kuziweka mfukoni huku akiwa bado na shauku ya kusoma ile barua,ilikuwa barua ndefu sana iliyokuwa na maneno yalizidi kumchanganya Gabi,kubwa lililomchanganya ni pale aliposoma kuwa,

"Sili wala silali kwa ajili yako,licha ya kuwa mimi ni mtoto wa tajiri na wewe

ni FUKARA lakini naomba utambue kuwa pesa hainunui furaha"maneno yale aliyasoma vyema Gabi mwisho kabisa wa ile barua kulisisitiza kuwa kama Gabi atakuwa na tatizo lolote la pesa asisite kumwambia.Gabi alibaki ameduwaa mawazo yake yalianza kumfikiria Layla aliyejionesha waziwazi kumtaka kimapenzi,

"Hii sasa itakuwa vita"alijisemea Gabi,ile barua aliikunja vyema nakuiweka mfukoni mwake, aliendelea na zoezi lake la kufanya usafi.Saa sita mchana ulikuwa mda wa mapumziko,Gabi alikuwa chini ya mti wenye kivuli kikubwa huku akioneka kuwa kwenye dimbwi la mawazo,Doris aliweza kumuona hajusita alimfuata mpaka pale alipokuwa,

"Nambie"alisalimia Doris Gabi aliinua uso wake kumtazama,

"Powa"alijibu Gabi kwa mkato,

"Samahani kama nimekukera lakini ukweli ndio huo,moyo wangu sio chuma naomba nipe nafasi"aliongea Doris,

"Mbona mnanipa wakati mgumu?hivi mimi nina nini hasa kilichokuvutia kwangu?"aliuliza Gabi,

"We kwanza ni kijana mzuri tukiachana na hali ya uchumi pia umekaa vyema una kila sababu ya kuitwa mwanaume hivyo nipe nafasi moyoni mwako"aliongea Doris hakutaka hata Gabi aongee kwa kuhofia kuwa atakataa hivyo alochomoa noti ya elfu kumi na kuiweka kwenye mfuko wa shati la Gabi,

"Hiyo utaenda kunywa chai mpenzi"aliongea Doris huku akizipiga hatua kuondoka.Gabi alibaki kumtazama hadi alipoishia,alishusha pumzi ndefu kisha ile pesa akaiunganisha na zingine.

Doris alienda moja kwa moja mpaka darasani na kumkuta Layla akiwa amelalia meza, aliketi pembeni yake kisha maongezi ya hapa na pale yakashika nafasi,

"Kesho uje hata na elfu ishirini ili tumpe Gabi,siku zote lazima upande ili uje kuvuna badae tuliza mawazo atakubali tu"aliongea Doris.Layla alikubaliana naye.Kesho yake asubuhi Layla alifanya kama alivyokuwa ameambiwa na rafiki yake,hata baada ya kumkabidhi pesa Doris alienda mbio mbio mpaka kwa Gabi aliyekuwa ameshika fagio anafanya usafi,

"Nambie mpenzi habari ya asubuhi?"alisema Doris,

"Salama"aliitikia Gabi huku akisitisha zoezi lake la kufagia,Doris alitoa pesa ile na kumkabidhi Gabi,

"Ya chai hiyo kwa siku ya leo"alisema Doris punde baada ya kusema hayo aliondoka na kumuacha Gabi ameduwaa,yote hayo aliyaona Layla kupitia kwenye tundu la dirisha,moyo wake ulifarijika alipomuoa Gabi kapokea ile pesa,mchezo aliokuwa anachezewa hakuutambua.

"Nimewaona,lakini mbona kama anakuwa mzito kupokea zawadi zangu?"aliuliza Layla baada ya Doris kumfikia na kumkuta pale dirishani,

"Hapana wala sio mzito macho yako tu, nadhani umeona nilivyokuwa naongea naye yaani hata yeye anafurahi"alisema Doris,

"Haya mimi sina neno ila mwambie wikendi nionane naye"aliongea Layla.

Mapinduzi hayo,unapenda unashindwa kutamka?haya Sasa Doris kaongea,




Mchezo wa Doris uliendelea pasipo Layla kufahamu,kila baada ya siku mbili Layla alihakikisha anampa Doris hela za kumpelekea Gabi,huku naye Doris alipokuwa anafikisha kwa Gabi alimwambia kuwa hiyo ni ishara ya mapenzi kwake,

"Lakini hizi ndo fursa hii pesa itaweza hata kunipa utajiri,ngoja nifanye kitu"alijisemea Gabi,pesa yote aliyokuwa anapewa hakumwambia mama yake,zaidi alichimba shimo dogo katikati ya chumba chake hata mama yake hakujua,pesa yote aliyokuwa anapewa na Doris aliihifadhi kwenye lile shimo hakutaka hata kuzihesabu zaidi alizidi kuziweka,

Hadi tunamaliza shule nitakuwa tajiri tayari"alijisemea Gabi,hata shuleni alianza kuonyesha ushirikiano kwa Doris lengo lake azidi kupata pesa,

"Mpenzi nakupenda sana"aliongea Gabi, maneno yale yalimchanganya sana Doris, hakuwahi kusikia neno lolote lenye maneno matamu kama lile,

"Hata mimi mpenzi naomba usiende kwa mwingine"aliongea Doris,

"Naanzaje kwa mfano, ntakupenda wewe hadi nakufa"aliongea Gabi,


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG