Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

SHILINGI (MWANZO KATI NA MWISHO) - 4

   

Simulizi : Shilingi (Mwanzo Kati Na Mwisho)

Sehemu Ya Nne (4)


Wajipasue kwanza wao, kama kweli ni rahisi.

Kindo hajapata kuona tukio la namna ile.

Na inakuwa heri asiendelee kulikona kuliko darasa lile kuwa mama yake.

“Ni lazima iwe mjini, huku haiwezekani hatukubeba vifaa kwa ajili ya kazi hiyo.” Daktari anajibu kwa niaba ya mkuu wa wilaya.


Mkuu wa wilaya akaaga kwa mara nyingine tena, alikuwa anajaribu kuingiza gia lakini gari analoliondoa hata halitikisiki.

“Kwa hiyo mtakuja vipi mjini sasa?” Daktari akamsaidia kulainisha barabara.

“Kwani, ninyi mnaelekea wapi?” akamuuliza daktari lakini likiwa swali kwa wote.

“Tunarudi zetu mjini!” mkuu wa wilaya mheshimiwa Matayo Masindeke akajibu. Nafsi inamliwaza kuwa Kindo anaelekea kulainika, na kwa kuiskia kuwa wanaelekea mahali ilipo hiyo ‘oprishini’ basi atakubali kuandamana nao.

“Sawa na sisi tutakuja hukohuko.” Kindo akajibu tena. Anatabasamu jepesi usoni.

“Sawa mtakuja kwa kutumia njia zipi sasa.” Jazba inampanda mkuu wa wilaya. Anahoji kana kwamba ni amri kwa Kindo kumpeleka mama hospitali.

“Hii hii mnayoitumia nyie kuondokea nasi tutataitumia kufika mjini.” Kindo akajibu. Mawazo yake hayakuwa pale, alikuwa anamuwaza mkewe na mtoto. Alitambua kuwa daktari na mkuu wa wilaya wanatamani ashawishike kuondoka pamoja nao.

Lakini, aondoke vipi amuache mkewe na mtoto nyuma??

Haikuwezekana!

Daktari akamvuta mkuu wa wilaya pembeni, tayari alishatambua kuwa yule bwana anaanza kuingiza mguu katika bwawa la ghadhabu na muda si mrefu atazama humo.

Akanong’ona naye pembeni, wakafikia makubaliano. Wakarejea na kumuaga tena Kindo.

Safari hii hawakujali ni kipi anajibu.

Kama walivyokuja ndivyo walivyoondoka.

Kuondoka kwao, ikawa ni nafasi kwa Kindo kuondoka kuelekea nyumbani kwa mzee Muhando.

________


“Karibu!” sauti iliyopoa ya mzee Muhando ikamkaribisha. Alikuwa katika vazi kuukuu la kanzu pamoja na balaghashia inayotamani kupumzishwa baada ya kufanya kazi miaka mingi kukifunika kichwa chenye mvi cha mzee Muhando. Imelainika teketeke lakini bado inasota.

“Mimi si mkaaji sana.” Kindo akajibu huku akiketi katika jiwe la kusugulia miguu.

“Nakusikiliza Kindo.”

“Nahitaji kuongozana nawe ikiwezekana leo hii hii tuka...” kabla hajamaliza mzee Muhando akajikohoza kisha akazungumza.

“Tuka... tuka, wewe na nani bwana?. Kindo wewe ni mtu mbaya, unaweza kusababisha watu wakaingia matatizoni na uzee huu. Wewe ni mtu wa kuingia mikataba na watu wazito halafu unaniacha na uzee huu nabwabwaja kwako kujikomba unipatie kazi ya kuuza sarafu yako kweli?” Akahoji.

“Sijawahi kushiriki mkataba katika maisha yangu, mkataba pekee ninaoufahamu ni huu tulioingia na Mwenyezi Mungu, wa kuishi na kufa.” Anastaajabu angali anajibu vivyo.

Mzee Muhando akatazama kushoto na kulia, kisha akaukwapua mkono wa Kindo, akamvuta pembeni. Wakasimama nyuma ya choo cha makuti.

“Jana tumevamiwa, wamekuja watu wanne yani foo pipo na mitutu ya bunduki, zinatutazama sebuleni kwa mzee Ukindi, mkewe anajikojolea yeye mzee Ukindi tumbo la kuhara limemshika alalama ka kitoto kichanga. Wanatuonya kuwa tunakushawishi wewe utupatie sarafu yako ya ajabu. Wakatuahidi kuwa watavifyatua vichwa vyetu tukiendelea kukutana na wewe. Yaani hapa nimekukaribisha kwa sababu tu ya u- alwatani wangu na vile kidogo nilipata mafunzo ya mgambo. Vinginevyo ningekukimbia hapa. Wewe ni bomu Kindo!” mzee Muhando akatiririka huku macho yake yakitazama huku na kule kwa mashaka.

“Mzee Muhando!” Kwa mashaka Kindo akamuita.

“Nakuapia, sijawahi kufanya biashara wala kuzungumza bei na mtu yeyote yule.” Kindo akajitetea.

“Unaamini kabisa mwivi hujitaja kwa wivi alioufanya. Huanza kwa kupinga katakata mpaka abanwe vizuri nd’o husema. Wengine wabishi hadi siku ya kiama wanabishana na mitume wa Mungu huko tena wanaapa kabisa kuwa sio watu wabaya. Niondokee Kindo usijenizulia balaa.” Mzee Muhando akachachamaa.

Kindo hakuwa na kauli nyingine ya kumlainisha mzee yule. Akaanza kuondoka kinyonge. Tumaini la kuiuza sarafu yake ya ajabu linafifia.

“Kindo!” mzee Muhando akamuita, “Kama unayoyasema ni kweli. Kuwa makini na hiyo sarafu, badala ya raha ambayo kila mmoja anaiona mbele yako, inaweza kukuletea balaa.” Akamsisitiza.

Kindo akaondoka. Kichwani kwake akikumbuka kauli ya mama yake, kuwa sarafu ile imebeba familia yake. Maamuzi yaliyokuwa karibu kabisa na utekelezaji, ni kuhakikisha sarafu ile inauzika na kisha anarejea kijijini kuichukua familia yake.

Kindo akaamua kuwa hakuna kurudi nyuma, hakuna kuaga mtu.

Akaifuata barabara ya kuelekea mjini, lengo likiwa kuiuza sarafu yake ya ajabu.

_____



SAFARI YA KINDO (SHILINGI KATI)


TAYARI alikwishaamua kuwa liwalo na liwe. Hivyo hakupiga hatua yoyote kurudi nyuma. Kila kitu kikafuata mbele kwa mbele. Ni kama aliyekuwa amekanyaga mdudu, mguu unawasha na tiba yake ni kutembea tu ili kumsulubisha yule mdudu.

Kindo anaondoka kuutafuta mji. Kitambo kirefu hajakanyaga huko.

Angekwenda kufanya nini? Hana shilingi ya kuuza, hana shilingi ya kufanyia manunuzi.

Anayo sababu sasa!

______

Ilimlazimu kutembea kwa miguu yake, mwendo wa kilomita zipatazo sitini kuweza kuviacha vijiji na mapori yake kuingia katika mji na nyumba zake.

Alipanda milima na kushuka mabonde kwa juhudi huku kila mara akikumbuka kuhakikisha ikiwa shilingi ipo mahali pake.

Ilikuwepo!

Jasho lilimtoka, kiu kikamkabili akakitibu kwa kuzifanyia ziara chemichemi kadhaa alizokutana nazo.

Njaa! Hii alishindwa kuitibu, kwani katika mapori aliyopita aliishia kuyaona matunda yanayosadikika kuwa ni sumu inayoua upesi. Yanatamanisha kuyatazama, ni kama yanayokuita yakuue.

Hakuyakaribia.

Miti ya matunda mfano wa maembe na machungwa ilikuwa imekauka. Ama la ina matunda machanga yasiyofaa kitu.

Kindo akapiga moyo konde, akaendelea kutembea. Fikra za kesho yake bora zilimjaza nguvu zaidi.

“Nikifanikiwa kuiuza shilingi yangu, nitanunua baiskeli nzuri mbili, nitawalipa ujira maskini wenzangu wawili, mmoja ataniendesha mimi, mwingine ataiendesha baiskeli iliyosheheni mapochopocho ya kurudi nayo nyumbani. Nafasi ikitosha nitabeba hiyo opresheni katika baiskeli na kumpelekea mama, sitakosa mtu wa kunionyesha mahali pa kuipata.” Fikra hizi zinamwacha katika tabasamu.

Macho yake yakatua tena katika miti ya matunda iliyokaunda. Kindo akajiwekea agano kuwa katikia utajiri wake, sio tu kula na maskini wenzake, bali hata miti hii isiyoweza kuzifuata chemchemi na kunywa maji, inaishia kunyauka na kukosa matunda.

Kindo akaiahidi kuwa lazima inufaike na utajiri wake. “Jambo la msingi mniombee heri, niuze kwa bei iliyo bora” Akaisemesha miti ile ambayo kitu pekee ilimpatia ni kivuli kidogo akapumzika hapo.

“Nitanunua mbolea na mbegu, kisha nitasaidiana na wanakijiji wenzangu kuzipanda hizo mbegu pembezoni mwa barabara, kisha mbolea ya kutosha itawezesha ukuaji wa miche itakayochipua.

Matunda haya yatakuwa mali ya kila mwanakijiji.

Watakula na kusaza.”

Aliendelea kuzimaliza kilometa hata akaifikia njia ya kwenda mjini.

Kindo hakuwa mwenyeji wa mji, hakuwahi kuipata bahati ya kuokota sarafu ya kawaida ambapo angeufikia mji na kuiuza kwa mabadilishano ya shilingi kadhaa za kawaida ama hata chakula kutoka mjini.

Nyama na samaki!

Hii ni mara ya kwanza na katika mkwiji wake amehifadhi sarafu. Sio sarafu tu, hii ya kwake ilikuwa ya ajabu.

Watu walikuwa wengi na kila mmoja kwa nafasi yake akionekana kujihangaisha kwa sababu alizozijua mwenyewe. Hawakuwa na utaratibu wa kutupiana salamu kama ilivyokuwa katika kijiji chao cha Ulongoni. Hajakaa sawa akapigwa kikumbo akayumba huko, hakupewa neno la samahani.

Kindo akamwendea mwanamama mmoja aliyeketi katika jiwe, mbele yake pakiwa na sinia lililosheheni maboga yaliyokwishachemshwa na kukatwa vipande.

“Karibu baba!” mama yule akamchangamkia.

“Asante sana!”

“Kipande shilingi tano, boga zima shilingi thelathini.” Mwanamama akainadi biashara yake, akiamini Kindo amejisogeza pale kununua kipande cha boga.

“Samahani!” Kindo akazungumza, mwanamama yule akamtazama kwa kukata tamaa. Ile ari ya kuwa mteja ishatoweka.

“Naulizia maduka ya kuuza shilingi.” Kindo akaulizia kwa nidhamu ya hali ya juu.

“Hata mimi nanunua, ikiwa bei yako ni nzuri.” Mwanamama akamshangaza Kindo.

“Unanunua kwa pesa ngapi?” akamsaili asiamini kuwa aliye mbele yake ni mteja sahihi.

“Una sarafu ngapi ngapi?” Mama akatupa swali.,

“Ninayo moja.” Kindo akajibu kwa kujiamini.

“Shilingi moja na unaulizia maduka ya wanaonunua shilingi? Watakufukuza na kukutukana, kwa shilingi moja naweza kukupatia maboga mawili na kipande kimoja cha kukuongeza uende kuridhika wewe na familia yako huko utokapo.” Mwanamke akazungumza huku akionyesha hana mzaha.

Kindo macho yakamtoka pima, akayakumbuka maneno ya Mzee Muhando kuhusu ile biashara ya kuuza shilingi za Nyerere.

“Unashangaa?” mwanamke akamuuliza Kindo ambaye hakuwa ameweza kusema neno lolote.

“Shilingi yangu haiwezi kulinganishwa na maboga mawili na kipande kimoja. Nayapenda maboga na ninayo njaa, lakini siwezi kukupa shilingi yangu kwa ulinganisho huo, hata ungesema unanipatia maboga yote bado sitakubali.” Kindo akamweleza huku anajiondokea. Mwanamke anatamani kutusi lakini pembeni yupo mtoto mdogo. Anampuuzia.

Hakufika mbali, akamwona bwana mmoja anampungia mkono kumuita. Kindo alijaribu kumtazama kama mtu ambaye waliwahi kuonana mahali. Lakini hadi anamfikia hakupata jawabu.

“Ninaweza kuinunua shilingi yako, shilingi aliyoshindwa kuichukua yule mwanamke maskini.” Mzee mwenye upara unaotiririka jasho alizungumza bila kutoa salamu.

“Utanipa kiasi gani?”

“Chupa mbili za maziwa mgando!” Akaitaja ofa yake kwa kujiamini huku akielekeza mikono yake katika safu ya chupa kadhaa zilizosheheni maziwa.

Kindo akachoka!

Safari ya kilometa zaidi ya hamsini kuja kubebeshwa chupa mbili za maziwa yaliyogandishwa?

“Shilingi yangu kwa chupa mbili za maziwa? Unanidharau?” Akahoji, taharuki ikijiweka jirani naye..

Bwana yule badala ya kumjibu, akachukua kopo lililokuwa katika meza, akalifunua na kuzimwaga chini shilingi zilizokuwa humo.

Shilingi nyingi!

Almanusura Kindo aishiwe pumzi zake bwana yule alipodai kuwa wote waliomuuzia shilingi zile waliambulia chupa moja tu ya maziwa wakaondoka kwa furaha.

“Nimekuonea huruma, unaonekana umechoka na unayo maisha magumu nimekupatia chupa mbili, unadai ninakudharau. Haya niondokee hapa. Na kamwe usirejee” Akafoka bwana kipara.

Kindo hakuondoka, bado anazikazia macho sarafu zile zilizokuwa zinafanana na ile moja ya kwake aliyoificha mbali kwa kuamini kuwa inayo thamani kubwa. Huyu bwana kipara anazimwaga kiholera mbele yake kama kitu kisichokuwa na maana yoyote.

“Nimesema unipishe katika duka langu, na usirejee tena? Ama niwaite polisi?”

Kindo kulisikia suala la polisi, akili ikamkaa sawa.

Akajiondokea pale, nyuma akalisikia cheko la mwanamke muuza maboga.

Anamcheka yeye!

Mara Kindo akasimama ghafla, kuna kitu kilikuwa kimekaa sawa katika akili yake na sasa amekumbuka jambo. Upesi akarejea katika lile duka.

“Umerudi tena!” akauliza bwana upara huku akiwa anazirejesha katika kopo sarafu zake. Jasho linamtiririka, hajishughulishi kulifuta.

“Sarafu yangu ina thamani kubwa sana, unatakiwa kuniheshimu.!” Akamweleza.

“Hata polisi utakaowaita wataniheshimu na kunilinda kwa sababu ya sarafu yangu.” Akaendelea kuzungumza. Na hapo akaitoa sarafu yake na kuionyesha kwa kuinyanyua juu yule muuzaji aione vizuri.

Lahaula! Kopo likamponyoka na kuanguka chini, sarafu zikakimbilia huku na kule. Hakujali, bado amekodoa macho yake kuishangaa sarafu ya Kindo.

Hakuwahi kuiona katika maisha yake yote zaidi ya kuisikia ikisifiwa thamani yake.

“Bwana mkubwa!.... bwana mkubwa” Bwana upara anababaika.

Kindo anataka kuondoka.

“Nakusihi tafadhali usiondoke, karibu ofisini kwangu nikusikilize. Karibu tuzungumze” Alisihi, huku akijisahau kuwa kibanda chake kilikuwa kinamtosha yeye na chupa zake za maziwa pekee. Kindo aingie wapi?

Kindo anataka kuondoka, bwana yule akaufungua mlango na kutoka nje.

“Nisikilize! Usiende katika duka lolote nakusihi.”

“Hutaki niiuze sarafu yangu kwa bei halali?” Kindo akamuhoji.

“Hapana!”

“Ila, unataka uinunue kwa chupa thelathini za maziwa mgando?”

“Siwezi kuinunua hata kwa kukupatia nyumba ninayoishi.”

“Nini sasa wahitaji, nielekeze maduka yalipo.” Kindo akamsihi.

“Usiende katika duka lolote. Nakujua wewe na ninataka kukusaidia... nimekujua tayari”

Kindo akastaajabu, “Unanijua, tangu lini? Unijue na unifukuze kama mbwa koko katika duka lako huku ukinitishia polisi. Mbona haunitishi tena...” Kindo akahoji.

“Tafadhali..” Bwana kipara akamsihi Kindo kisha akaingia katika kibanda chake, akazikanyaga sarafu zilizotapakaa pale chini, akazipuuza. Akafungua mtoto wa meza, sehemu anayoitumia kuhifadhi pesa zake za mauzo. Akakitoa kikaratasi.

“Wewe ni Kindo!... Ndio, Kindo nd’o jina lako” akamsemesha.

Paah! Moyo wa Kindo ukapiga kwa nguvu sana, jasho likaanza kumtiririka.

Akaikosa amani.



Akakikosa amani.

“Sikulazimishi kuniamini, lakini laiti kama ungemuonesha mama yule shilingi yako ya ajabu. Angepiga mayowe. Na wale askari unaowaona wanazagaa huku na kule, wote wangepambana kukudhibiti.” Alizungumza kwa kusihi bwana yule.

“Nimekosa nini mimi? Mpaka wanitende hivyo” aliuliza Kindo huku akizama katika hofu kuu.

Hofu ambayo iliishindilia tamthiliya ya shilingi katika shimo la kati, kwa nia njema kabisa ya kuifikisha safari hii mwisho wake.


_____________________


KUNANI’ULONGONI?


Mnamo mwezi wa Shaaban, mwezi wa nane katika uislamu. Mwezi mmoja pungufu kabla ya ule mwezi wa Ramadhan. Mashamba tayari yalikuwa yamecheka.

Wa magimbi walifanya palizi la mwisho, wale wa viazi mbatata, viazi vitamu na mihogo, wao walibaki kuyatazama matawi jinsi yalivyowapendeza machoni.

Familia ziliandaliwa tayari kwa ajili ya kufanya mavuno. Mavuno ambayo yatahifadhiwa vyema gunia kwa magunia tayari kwa kupelekwa mjini.

Mji ambao unakaliwa na waungwana wanaoishi kwa kuiamini na kuitukuza miezi ya Kwarezma na huu wa Ramadhani wanaokaribia kuupokea.

Mwezi wa kwarezma licha ya kuwa mrefu kuliko huo wa Ramadhani, hauhesabiki kama fursa ya kuiota usingizini. Mara kwa mara zile siku arobaini hupita kama hakijatokea kitu.

Wanakula nini hawa baada ya funga yao?

Swali hili lilikosa jawabu, taratibu wakaipuuza fursa ile na kujikita katika mwezi wa Ramadhani, huku ule mwezi wa Shaabani ukiwa maalumu kwa ajili ya mavuno.

Fursa kuu! Mwezi wa Ramadhani.

Kijiji cha Ulongoni kinatumia fursa hii kuwahudumia kwa chakula kiwafaacho katika funga yao tukufu.

Utukufu uso’ nafasi wala mantiki katika kijiji cha Ulongoni.

Mazao yamestawi na wanahesabu siku kabla hawajayavuna na kuyakimbiza mjini.

Mambo yanabadilika katika ghafla inayokosa neno sahihi la Kiswahili zaidi ya ghafla kubwa kuliko.


Zilianza kama tetesi, kijiji chenye wakazi wachache kama Ulongoni ilikuwa rahisi sana tetesi kutapaa kwa haraka. Kwamba kuna sumu inasambaa kwa kasi kutoka katika vijiji vya jirani na muda wowote ule unaingia Ulongoni.

Sumu hii inapitia chini ya ardhi katika mkondo wa maji. Ikitokea maji yale yakatumika basi sumu ile itasambaa kwa njia ya hewa.

Nani aliyeileta taarifa ile?

La! Haikuwa taarifa.

Ni nani alisambaza tetesi zile?

Hajulikani!

Kwani kuna tofauti gani kati ya tetesi na taarifa katika kijiji cha Ulongoni?

Hakuna!

Kuna vitu vya kuuliza mara mbilimbili na kisha kuleta ubishi, lakini sio jambo lolote linalohusu uhai.

Nani aliwahi kuujaribu ukali wa upanga kwa kuitega shingo yake?

Nani angeyajaribu maji ya chemichemi na visima kijijini Ulongoni baada ya tetesi kuwa yanayo sumu kali kutapataa?

La mgambo likalia, onyo kali likatolewa. Sio tetesi tena, ni taarifa rasmi kuwa visima, chemichemi na mabwawa ya kijiji cha Ulongoni yamepitiwa na sumu kali, hivyo sio ya kuyasogelea. Hayafai kwa kunawa, kuogea wala kunywa.

Wanakijiji wa Ulongoni wakajiongeza kuwa hayafai walau kuyatazama kwa macho.

Ushauri ukatolewa wa wapi yanapopatikana maji yasiyokuwa na sumu.

Vijiji kadhaa mbele!


Kijiji ambacho kilipendekezwa, walilazimika kutembea kwa kilometa kumi kukifikia. Hivyo ili kuyapata maji, utatembea kilometa kumi na chombo chako kitupu kisha kilometa nyingine kumi ukiwa na maji kichwani. Na hapo haujasimama masaa kadhaa katika foleni kuingoja ifike zamu yako.

Wanawake wakasaidiana na wanaume katika tabu hii. Wanavipita visima vyao huku wazazi wakiwaonya watoto wao kutosogelea kisima wala chemichemi aina yoyote. Kuonya pekee kwa mdomo haikutosha, kuna watoto walifinywa masikio yao, huku vichwa vikibeba mizigo ya makwenzi mazito.

Kisa, kuvitazama sana visima.

Kuvitazama sana tu!

Wazazi walikuwa makini sana.

La mgambo lililia, likazungumza na kueleweka.


Zilikuwa ni kilometa ishirini za kwenda kuyafuata maji na kurejea nyumbani, ukitimiza awamu tatu za kwenda na kurejea. Basi una matembezi yapatayo kilometa sitini.

Kila siku!

Hesabu ngumu, lakini jibu kwa wana Ulongoni lilikuwa la upole sana, ‘tutavumilia’.

Kweli walivumilia na haikuonekana kama ni pigo kwao. Yeyote aliyeisambaza taarifa hii, akatafsiri hali ile kuwa ni kama matusi ya nguoni.

Akidhani amewaweza wanakijiji, anajiona kuwa hakuna kilichobadilika. Wanayafuata maji hukohuko, wakati wa kwenda wanacheka, katika foleni wanapiga soga na wanaburudika wakati wa kurudi.


La mgambo likalia tena, safari hii walizungumza watu waliojiita wataalamu. Wakaelezea kuwa wanakijiji wanapaswa kuwa makini katika mashamba yao, inasemekana sumu ile ikawa inazidi kuusogelea uso wa dunia, hivyo kiazi utakachokifukua kinaweza kuwa na sumu kali ya kuangamiza, muhogo utakaoutafuna unaweza kuhatarisha maisha yako. Na hata gimbi utakalolipapasa linaweza kukuletea kilema cha maisha.

Bado!

Mahindi ishia kuyazama tu, ukiyatia kinywani jino litang’oka moja baada ya jingine.

Sumu hiyo!

Waliaswa kuwa makini, lakini hakuna aliyeweza kuipima maana ya makini. Walichotafsiri kaya kwa kaya ni kwamba, jembe litulie ndani mashamba yaliyostawi yabaki kutazamwa kwa mbali mpaka tatizo hilo litakapotangazwa kuwa limetokomea. Kama walivyowanukuu wataalamu waliosema kuwa wanafanya kila jitihada kupambana na tatizo lile.

Baa la njaa!

Hiki nd’o kilichofuatia baada ya mashamba kuogopwa mithiri ya malaika wa kifo ameweka makazi mashambani, ukijisogeza anakujumuisha katika hesabu zake za siku. Aheri ya maji yalikuwa yanapatikana bure katika kijiji cha jirani hata kama ni kwa foleni, lakini chakula hakikugharimu kilometa ishirini pekee, ulitakiwa uwe na pesa kuweza kukinunua. Kuvumilia pekee haikuwa jawabu.

Na hapa ndipo vilio rasmi vilipoanza. Nguvu ya kwenda kuchota maji itatoka wapi angali hakuna chakula?

Hofu ikatanda! Na mara katikati ya shida zile zilizojenga daraja la kuyafikia mauti kwa mateso, likaibuka jina moja la kuweza kuzishusia lawama zote zile.

Wapi lilianzia, nani wa kwanza kulitamka? Haikujulikana lakini mara ikawa kila anayelia, analia na jina lile.

Kindo!

Kijiji cha Ulongoni kikatitia katika Sununu.

Kila aliyelia alilia kwa namna yake lakini mwishoni wote wakabaki na kauli moja ya kuwa, Kindo aliipata sarafu ya ajabu katika namna za ulozi. Hivyo ameikasirisha mizimu ya kijiji kile, imechukizwa na wanakijiji kulifumbia macho suala lile, sasa imeishusha hasira yake katika ardhi na kila kinachoota juu yake.

Wanakijiji kwa hasira zote na kitendo cha kutomuona Kindo wakajikuta wakimkabili mama yake mzazi ambaye walikuwa wakimuhifadhi tangu Kindo atoweke kuelekea pasipojulikana. Walimuhifadhi kwa wema ili Kindo akirejea mama yule awatangaze kwa mema na waweze kunufaika na maisha ya kifahari ya Kindo.

Hawazitaki tena fadhila hizo, wamekengeuka.

Wamevurugwa wakavurugika.

Tangazo likatolewa kuwa, yeyote anayeshirikiana na mama wa mchawi basi na yeye atahesabiwa na kuadhibiwa kama mchawi vilevile.

Hata lisingekuwa tangazo hili, ni nani angeweza kujinunulia chakula chake na kisha anunue chakula kwa ajili ya mama asiyekuwa wake?

Labda alikuwepo, lakini kwa persa gani?


Mama yake Kindo akabaki kuisubiri siku ambayo hatakuwa na namna zaidi ya kukutana na malaika muhesabu roho zisizotakiwa duniani.

Wanakijiji nao wakaziweka sawa pua zao kuisubiri siku ya kuweka ushuhuda kuwa mama yule ameaga dunia tayari. Wakaamini kuwa kuondoka kwa mama yule yawezekana ikawa nafuu kwao na laana ile itaondoka naye.

Wenye mashamba walitamani sana laana hii itoweke kabla ya mwezi wa Ramadhani.


Ikawa siku moja inayozaa nyingine pasi na hiyari, hatimaye siku tano. Hakuna mwanakijiji anayemtembelea mama yake Kindo, hata wale waliokuwa wakitarajia mema kutoka kwa Kindo sasa walimuombea mabaya popote alipo kwa sababu ya madhira aliyowaletea. Wale wachache waliowahi kutamka kuwa Kindo aliipata sarafu ya ajabu kwa njia za kishirikina walitunisha vidali vyao huku mbavu zikichomoza kwa njaa kali. Walikuwa wakilifurahia anguko la Kindo huku wakisahau kuwa na wao wapo katika daraja la kifo.




Litengeneze tatizo angali upo katika kiza kinene, waathirika wote wamezama katika uzingizi mzito.

Litatue tatizo hilohilo kibabe angali waathirika wote wanakutazama.

Hakuna atakayeubeba umaarufu mwingi wa kisiasa kukuzidi wewe.

____________

KWA mara ya kwanza katika kijiji cha Ulongoni hekaheka haikuwa ya punda na ng’ombe wanaocharazwa ili kubeba mizigo mizito ama kulima mashamba. Siku hii ilikuwa ya tofauti sana, zilikuwa ni hekaheka za magari. Hili linatoka lile linaingia, na halikuwa la mgambo lililolia ili kuwavuta watu. Ni haya magari yaliwavuta,sio kwa ajili ya kuyatazama pekee bali lile kilichokuwa kinashushwa kutoka katika magari hayo.

Chakula na maji!

Ajabu iliyoje, yule aliyejitambulisha kama mkuu wa wilaya miezi kadhaa nyuma. Alikiweka cheo chake pembeni na ule ukuu unaokaribiana na utakatifu katika ardhi anayoitawala, alikuwa anashiriki katika kuishusha mizigo ya vyakula. Jasho linamtiririka na ajishughulishi kulifuta.

Alifute? Ili iweje wakati ana uchungu uliopitiliza dhidi ya linalotokea kwa wananchi wake?

Maguduria ya maji yakashushwa, magunia ya chakula yakabebanishwa.

Wananchi wa Ulongoni ambao tayari walikuwa wanaanza kupoteza kumbukumbu ya watu wangapi wamepoteza maisha kwa dhiki, walipanga foleni kuweza kuchukua shehena ya chakula.

Mchele waliokuwa wakiupata kwa nadra, uligawiwa kwa kiwango cha muhitaji kuridhika, ndizi, unga na sukari. Vyote kwa hisani ya mkuu wa wilaya.

Matayo Masindeke mkombozi wa wanyonge!

Hiki ndo alikiacha katika midomo ya wanakijiji wa Ulongoni.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG