Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

MASHARIKI YA MBALI - 3

   

Simulizi : Mashariki Ya Mbali

Sehemu Ya Tatu (3)



Hata kama unataka kumweleza kuwa mkewe kaolewa na bwana mwingine inabidi upayuke tu. Ama mkewe katoa ile mimba aliyomwacha nayo, bado inabidi upayuke.

Lakini hakuna la kujali we payuka tu. Hakuna anayesikiliza la mwenzake pale.


Kwanza ukishahukumiwa na kwenda jela, ile siku ya hukumu ndo siku yako ya mwisho ya kuwa na haki. Huko kwetu mfungwa ni mdogo wake na shetani baba mmoja mama mmoja na wamenyonya titi la mama mmoja kwa zamu wakipokezana katika ukuaji wao.

Mtazamo huu mmeturithisha ninyi watu weupe, mmetufundisha vitu viovu sana ambavyo ninyi hamvifanyi.

Hata nje ya gereza ujinga mwingi tu mmetupatia halafu mkatuacha tuubebe tukijidanganya na ninyi mmeubeba.

Wakati mnatutawala huko mlitunyanyasa sana, sina maana mbaya tena bali najaribu kukusimulia uifahamu vyema nchi yangu, na hii itakusaidia sana siku moja ukifika huko bahati mbaya japo natambua huwezi kufikiria kwenda huko.

Kabla ya uhuru magereza yalikuwa kwa ajili ya watu weusi pekee huko nchini kwetu, mlituweka huko na kutuacha tufe kwa mateso na kukosa chakula. Kwa makosa kama, kuchoka na kushindwa kulima mashamba yenu katika ardhi yetu, kosa la kuugua na kushindwa kupanga vyuma vya reli ambayo mtaitumia kusafirisha bidhaa zetu, kuna ambao walipelekwa jela kwa kosa tu la kukutana na ngozi nyeupe barabarani na kisha kupishana naye. Hebu fikiria kosa la kupishana na mtu barabarani bila kumbughudhi unahukumiwa kunyongwa. Hatutasahau kamwe na sidhani kama waliofanyiwa hivyo wakiamshwa katika usingizi wao sasa watakubali walau kutoa msamaha.

Kama ilivyo ada, vimbelembele huwa hawakosekani, yaani sisi wenyewe weusi kwa weusi tukaanza unafiki. Tukachomeana utambi…

Wale mabingwa wa kuchomea wenzao utambi ili wakamatwe na kutupwa gerezani wakapewa vyeo na kuwa askari wasiokuwa hata na mafunzo.

Hawa wakafanywa wahudumu wa magereza. Walijionea na kukenua meno wakitazama mweusi mwenzao akikatwa sikio, akinyongwa akichapwa viboko mbele ya hadhara.

Kitendo chao cha kuwa waaminifu mbele ya wakoloni pamoja na kuwaiga kila wafanyacho kukaimarisha urafiki wao. Wakaanza kujiona na wao ni ngozi nyeupe ndani ya mioyo yao huku wakiwa na rangi nyeusi nje kwa bahati mbaya kabisa.

Wakaanza kusahau kwao.

Hata ulipopatikana uhuru ni walewale watu weusi wanaojiongopea wana roho nyeupe walibaki kuwa viongozi wa magereza.

Ule ‘uuaji’ waliorithi kutoka kwenu ninyi wakauhamishia kwa waajiriwa wapya.

Sasa askari alifundishwa kuwa kutesa ni mojawapo ya sifa kuu za kuwa askari. Wakajazwa upepo mchafu pia wa kikoloni ulioitwa lamensia-tanganyikana. Yaani ni heri watu mia moja wasiokuwa na makosa wafie gerezani kuliko mkosaji mmoja kubaki uraiani.

Kama nilivyosema awali, mlitupa vilivyooza ninyi mkaondoka na visafi. Kwenu hata sasa naiona lamensia-anglikana. Hii inasema kuwa ni heri waasi mia moja wabaki mtaaji kuliko mwenye haki mmoja kwenda jela kimakosa.

Sasa fikiria mwenye haki yungali gerezani nchini Mashariki ya mbali, anateswa vikali sana ili akili kuwa yeye ni mkosaji.

Danstan! Fumba macho na ufikirie kuhusu hili na isibaki kuwa fikra kwani ni hayo yanatokea nilipozaliwa. Unasimamishwa mbele ya kaburi ambalo limechimbwa tayari, ghafla unasukumwa humo katika shimo hilo linalozidi futi sita, wanakueleza kuwa ukikubali kuwa wewe ni muuaji basi hawakufukii, lakini ukiendelea kukataa wanakufukia na kukuacha ufe kwa mateso wakati ukiziwania pumzi zako. Fumbua macho na unijibu….”

Sauti ya Daniel katunzi ikakoma ghafla….. Danstan akaanza kutapatapa huku na kule.

“Nakubaliii… nakubalii…. Nakubaliii nimeuaaa… nakubaliii” alipiga mayowe yale huku akizidi kutapatapa.

Wenzake waliokuwa katika chumba kimoja wakawahi kumdhibiti kwa sababu alikuwa akijibamiza ukutani na hata asijue nini kimejiri.

Walipofanikiwa kumtuliza, naye akafanikiwa kuyafumbua macho vyema.

Alikuwa yungali katika chumba kilekile cha mahabusu hali yake ikiwa taabani.

Fikra za kuwa yu Mainstream anazungumza na Daniel zikatoweka.

Alikuwa katika nchi ya Mashariki ya mbali.

Hakuwa huru! Alikuwa gerezani akiwa amepondwa akapondeka vilivyo. Uso umemtutumka mithiri ya mtu aliyeng’atwa na mdudu aina ya mavu.

Muonekano wa Danstan ulitisha, alikuwa anakoroma huku donge la damu lililogandiana katikaa pua zake likiwa linapumua kama kiumbe hai. Linavimb n kusinyaa kadri anavyozidi kukoroma.

Shabani, alilaani huku akiwasihi wenzake wafanye japo dua kwa sababu lililomtokea Danstan linakuja kwao pia.

Wesu alimtazama kwa jicho lililokataa tamaa, tayari walijiona wao si wa Mungu walaa wa shetni. Walikuwa tyari ni wanaharashi wasiokuwa na chao duniani, peponi wala motoni.

“Nawaomba ndugu zangu, mniombee hiyo dua. Sijiwezi ninakufa mimi….” Alizungumza kwaa tabu sana Danstan.

“Kama mmojawetu akifanikiwa kutoka humu akiwa hai, basi anisaidie kumtafuta mchumba wangu anaitwa Cherry. Ajue nilipofia… ajue nilipofukiwa.” Danstan alizungumza kwa uchungu mkubwa.

Shaban, alijaribu kumkandakanda lakini nafuu haikupatikna.

Shaban aliyekuwa walau na masalia ya imani kwa mwenyezi Mungu aliamua kutokaakimya. Akaanza kupig kelele akimuita askari magereza yeyote aliyekuwa karibu.

Hii ni kwa usalama wa Danstan.

Alikiona kifo kikimtwaa!





“Ni afadhali kua na jeshi la kondoo linaloongozwa na SIMBA kuliko jeshi la Simba linaloongozwa na KONDOO.”

Tafsiri kadri ya uwezo wako.


NA HII NI SEHEMU YA KUMI.


MTAANI kila mwenye kujua kuongea aliongea, mwenye uwezo wa kuandika aliandika. Magazeti na mitandao mbalimbali ya kijamii iliendelea kuandika tena na tena.

Kila mmoja akijifanya anajua zaidi juu ya sakata la ‘zungu la unga’.

Sifa kemkem zilipeleka kwa mkuu wa majeshi ambaye aliviita vyombo vya habari kwa lengo moja tu.

Kujinadi! Akiwa ameambatana na mkuu wa mkoa.

Kujikweza juu ya mpango madhubuti uliotumika kumtia mikononi zungu la unga.

Mpango gani sasa? Hilo alitambua yeye. Alibaki kuuita mpango madhubuti mbele ya vinasa sauti vile.

Mwandishi mmoja akaomba mpango ule ufafanuliwe kidogo kwa manufaa ya wananchi, mkuu yule akaanza kung’aka kuwa zile ni siri za jeshi na mwananchi anachotakiwa kujua ni kitu kimoja tu.

Zungu la unga ametiwa mikononi mwa jeshi la polisi.

Ajabu! Hilo si tayari kila gazeti lilikuwa limeandika? Aliita vyombo vya habari kwa ajili ya kurudia kusema yaliyokwishasemwa.

Sijui gari yake ilijazwa mafuta ya bei gani kwa safari ile kuufikia ukumbi wa mikutano.

Hilo anajua yeye!

Mkutano ukamalizika waandishi wakibaki bila jipya la kuandika.

Ili wasikose yote, siku iliyofuata wakachapisha picha yake katika kurasa za mbele za magazeti, akiwa amezungukwa na vinasa sauti kutoka vyombo vya habari tofauti.

Gazeti moja likapamba picha ile na maandishi yaliyokolea ino mweusi.

“SIMBA WA MAJESHI AUNGURUMA”

Sitaki kujua alitapatwa na cheko kubwa kiasi gani kwa sifa zile kemkem.

Dhihaka!!


_________


BAADA ya kuzungumza na vyombo vya habari. Habari ile ikapaa hadi nchini Semedari katika jiji la Mainstream.

Daniel Katunzi ambaye siku kadhaa zilizopita akiwa hajapata ujumbe wowote kutoka kwa Danstan alizipa uzito habari zile zilizomtaja zungu la unga bila kutaja majina yake wala picha.

“Isijekuwa Danstan ohoo!” alimweleza mama yake Danstan huku akimwonyesha habari ile katika mitandao ilivyozungumzwa.

Diana aliachia cheko hafifu huku akioneka kutoshtushwa na taarifa ile na ulinganisho wa Daniel.

“Aaah! Danstan havuti Sigara, hanywi pombe, soda zenyewe hanywi anataka juisi pekee. Leo hii awe zungu la unga. Dunia itafikia kikomo chake.” Alizungumza katika namna ya madaha, ikia ni namna ya kumshushua Daniel Katunzi.

Daniel akashusha pumzi zake kisha akaanza kuzungumza pasi na kumkatisha Diana shughuli zake.


DANIEL ANASIMULIA.

KIPINDI cha ukoloni watu weupe waliotutawala pamoja na kuna kitu kibaya sana walituachia bila hata ya wao kujua, na hata wangejua wasingeweza kujali.

Hawajawahi kujali!

Kwa mujibu wa mababu zetu wakoloni walikuwa wanapenda sana sifa.

Yaani wakinyenyekewa wanajiona milango ya mbingu hii hapa wanaitwa waingie. Walipoondoka wakaziacha zile sifa nchini kwetu, bora hata zingekuwa sifa za maana. Walituachia zigo la sifa za kijinga.

Shuleni, katika ofisi mbalimbali. Bosi mkuu anataka sifa za kijinga mbele ya kijana wa masjala, kijana wa masjala anataka sifa za kijinga mbele ya msafisha ofisi, msafisha ofisi anaenda kuzichota sifa kwa mlinzi, mlinzi yeye hana pa kwenda zaidi ya kuzisubiri sifa za kijinga palepale getini.

Hebu fikiria unapeleka barua ya maombi ya kazi, mlinzi wa getini ambaye ana elimu ya ukakamavu pekee anataka aifungue ile barua yako aisome. Kama hautaki ondoka na uchafu wako. Akishaifungua anakutupia swali la kijinga, ‘unatafuta kazi?’. Unatamani ummeze lakini hafai hata kwa kumeza.

Unamjibu ‘ndio’ anakutazama juu hadi chini anakuuliza ‘unataka mshahara shilingi ngapi?.’

Huyo ni mlinzi anajitahidi awezavyo kuikashfu elimu yako na uhitaji. Anafanya jitihad zile kwa sababu anajua fika kuwa ukiipata kazi unayoitafuta itakuwa zamu yake kuogelea katika bwawa la sifa zako.

Hiyo ndo hali halisi ya mashariki ya mbali. Nchi imekaa kisifasifa tu.

Sifa za kijinga!

Sasa usiombe akatokea mtu akafanya jambo la maana, badala asubiri sifa zimfuate atazitafuta kwa nguvu, na akigundua haujamsifia kama alikuwa rafiki yako, basi umeingia katika kundi la maadui zake.

Kupenda huku sifa za kijinga kunaanzia ngazi za chini kabisa na kuweka makazi makuu katika ngazi za juu.

Nikikwambia hadi mkuu wa wilaya anapenda sifa za kijinga utashangaa na kujiuliza iko wapi nidhamu ya uongozi.

Tena akikaa muda wa mwezi mzima bila kupata walau sifa moja ya kijinga hapo ndo anakuwa kama mwendawazimu aliyepoteza makopo yake wakati anakula chakula. Yupo radhi kukiacha kile chakula aanze kukimbia huku na kule akiyasaka makopo yake.

Atafanya kila awezalo aweze kurejesha sifa yake.

Usipokuwa makini unaweza kudhani SIFA ZA KIJINGA zinaleta ongezeko la mshahara nchini Mashariki ya mbali.

Sasa isijekuwa Danstan amekutana na kichaa aliyepoteza makopo akaamua kulala naye mbele kwa kumshutumu kuwa ni yeye ameyaiba makopo yake.

Ile ni nchi yangu na ninaifahamu vyema, akitokea kichaa mmoja mwenye madaraka akasema ni amri kulala saa kumi na moja na nusu jioni na kuamka kumi na moja alfajiri, wewe jifanye mjinga fuata anachosema. Sifa zimjae mpaka kumwagika.

Usitake kuniuliza kama kuna sheria ama la! Nchi yangu ina sheria tena sheria zenyewe ni kali kwelikweli.

Ajabu ni moja tu, sheria zetu zinafanya kazi kwa msimu maalumu. Likitokea jambo ambalo linawagandamiza wasionacho vitabu vya sheria vitafutwa vumbi kisha kifungu nambari mia tisa na nane mlango ‘Ba’ wenye vifungu vidogovidogo vinane, katika kifungu kidogo cha nane kilichogawanyika katika mapande manne madogomadogo, lile pande la nne linasema kwa lugha ya kigeni ambayo maana yake ni kwamba ‘LILILOTOKEA KWA ASIYENACHO NI SAWA TU’.

Awe amenyongwa? SAWA TU!

Kwani wangapi wamekufa?

Labda amekatwa mikono? SAWA TU!

Kwani yeye wa kwanza kuishi bila mikono?

Ama nyumba yake imevunjwa na hajapata stahiki zake? Sawa tu, acha alale nje!

Kwani wangapi wanalala nje?


Asiyenacho anabaki analia na kusaga meno. Wanaita vyombo vya habari na kujitoa hatiani wakidai kuwa asiyenacho asilielie hii nchi inaongozwa na sheria.

Vyombo vya habari vitaanza kumnanga asiyenacho kwa kushindana kuandika maneno machungu dhidi yake.

Nchi yangu mimi kama kweli kuna mchawi anayeweza kuroga eneo kubwa namna ile basi acha niamini kuwa tulirogwa halafu mchawi akaikimbia nchi kama nilivyoikimbia mimi.

Kama Danstan amenasa katika tego la kichaa, nasikitika kuwa atapata tabu kubwa sana. Atayaonja machungu yote ya ukoloni ambayo babu yetu waliyanywa kila kukicha.

Eeh Mwenyezi Mungu muepushie ndugu yangu janga hili.”


DANIEL alimaliza kuzungumza, sasa Diana macho yalikuwa yamemtoka pima. Ule uchungu wa mwana aujuaye mzazi (mwanamke) sasa ulikuwa umeamka upya na kuutawala mwili.

Uso ukawa mwekundu kana kwamba amepakawa basbasi, akashika hiki akaacha akashika kile akakitupa.

Alikuwa amechanganyikiwa kupindukia.

“Kwa hiyo wanataka kusema mwanangu anauza madawa ya kulevya. Hapana huu ni uonevu. Yaani wawachezee haohao, sio kwa mwanangu nasema…” alifoka kama mtu aliyepandwa na maruhani. Yaani ni kama aliyekwisha ambiwa kuwa huyu wa kuitwa Zungu la unga ni mwanaye.

Daniel akamtazama hata asifanye jitihada za kumtuliza.

Kisha akajisemeza yeye na nafsi yake.

“Ukijipeleka huko, na wewe wanakukamata halafu wanaita waandishi wa habari anasema wameweka mitego yao kiintelejensia na wamefanikiwa kulinasa ‘jike la shupa’ pacha wake ‘zungu wa unga’.

Mnaijua Mashariki ya mbali mnaisikia??”

_______


Mlango wa chumba alichokuwa amelala Cherry uligongwa. Mashaka yalikuwa yamejenga urafiki wa dhati na nafsi yake. Danstan alikuwa hajaonekana .

Lugha gongana ikatawala kikao kile kisichokuwa rasmi. Kikao ambacho wajumbe wanne walikuwa wamesimama wima wakizungumza pasi na kupokezana mithiri ya chiriku.

Mjumbe aliyetembelewa ghafla akibaki kusema neno moja kwa kurudiarudia kuwa hakuna anachoelewa. Wale wajumbe walioonekana kuwa na akiba kidogo ya msamiati wa lugha ya kigeni wakapandwa na jazba pasi na sababu za msingi. Wakaanza kutumia nguvu ili waeleweke.

Wakamsisitiza Cherry kuwa mume wake yu mahututi hospitali amekumbwa na ajali mbaya ya gari.

Na hapa walilazimika kutumia lugha ya picha na maneno machache.

“Zis man is sick, very sick in accident. Les go!”

Kwa jasho sana hatimaye wakaeleweka.

Cherry akatoka nduki akiandamana nao.

Akakwea karandinga la polisi.

Likatoweka kwa fujo.


Haikuwa safari ya hospitali. Bali katika nyumba iliyoitwa salama japo usalama wake haukuonekana.

Pengine ilikuwa salama kwao kwa sababu wangeweza kukufanyia lolote na jamii ising’amue.

Akakalishwa chini!

Alipouliza mchumba wake yu wapi aweze kumuona. Akatulizwa na bwana ambaye huyu alikuwa anaweza kuzungumza vyema lugha ya kigeni.

Kwa utulivu kabisa akamweleza Cherry kuwa Danstan yupo gerezani kwa tuhuma za uzalishaji na uuzaji wa madawa ya kulevya.

“Tena baada ya kumbana sana amesema kuwa mnashirikiana bega kwa bega katika shughuli hii. Binti mrembo kama wewe unauza madawa? Kwanini sasa” alizungumza kwa utulivu aliyepewa dhamana hiyo.

Cherry ambaye alikuwa roho juu kuhofia usalama wa Danstan ambaye aliongopewa kuwa alipata ajali, akaongezewa tena hili la kutisha zaidi.

Drug cartel!


Moyo uliokwishalalamika sana kwa kuwekwa juujuu tangu anarushwa katika karandinga, ukakosa uvumilivu wa ziada. Ukapunguza zile sifa zake za kukita sana kifuani, ukanywea usiamini hata kidogo kuwa ulikuwa umebebwa katika kifua cha ‘drug dealer’. Moyo ukafanya mgomo wa kusukuma damu kwa kasi, ubongo ukaunga mkono harakati za moyo uliochukia.

Cherry akatoa kauli isiyoeleweka kisha kama mzigo akateleza kutoka kaltika kile kiti akatua chini.

Puu!



“PROPAGANDA ikitumika vizuri inaweza kumfanya mtu aone kuwa paradiso ndio jehanamu na jehanamu ndio paradise.” Tafsiri kadri ya uwezo wako.


NA HII NI SEHEMU YA KUMI


Zilikuwa zimekatika siku kumi na nane tangu Danstan afungiwe katika chumba cha mahabusu. Hakuwa na tumaini tena, lile wazo la kwamba alikamatwa bahati mbaya lilikuwa limetoweka na sasa alikuwa anaionja shubiri ya kuingia Mashariki ya mbali. Kipigo cha haja alichopokea kikamwacha katika masalia ya maumivu katika mwili wake, japokuwa sasa aliweza kusimama vyena na kutembea kwa kusuasua.

“Hivi kwanini sikumsikiliza Daniel?” Kwa mara ya kwanza tangu aingie katika dhahama ile, Danstan alijikuta akimkumbuka Daniel na masimulizi yake juu ya Mashariki ya mbali.

Akajikuta akiuma meno yake kwa uchungu mkubwa.

Chozi likapenya na kutua katika uso wake uliokuwa umepauka.

“Nd’o maana Daniel aliamua kukimbia.”

___

Siku ya kumi na tisa usiku akiwa amejikunja vyema sakafuni huku akiwaachia mbu na kunguni mgao wa damu, lango la gereza lilifunguliwa na kama kawaida kila likifunguliwa hupiga kelele zinazoudhi na kukatisha usingizi mnono wa mahabusu na wafungwa.

Ikiwa tu jela kuna usingizi mnono!

Na kila linapotokea tukio kama hilo basi kuna jambo. Aidha kuna mtu analetwa gerezani ama kuna mtu anakuja kuchukuliwa.

Na mara nyingi watu waliokuja kuchukuliwa usiku walikuwa hawarejei kamwe.

Wanaachiwa huru? Wanauwawa? Wanahamishwa vyumba?

Hilo lilibaki kuwa fumbo zito. Na ili ulifumbue basi ni wewe uchukuliwe kisha utajua yapi yanajiri huko.

Usiku huu ilikuwa zamu ya Danstan ambaye hakuwa amepona vyema majeraha yake. Kurunzi kali ilimmulika machoni kisha akaamuriwa ainuke. Upesi akazivaa vyema nguo zake.

Nguo zake ambazo hazikuwa nguo tena bali mararumararu yanayostiri utupu wake.

Aliendelea kumurikwa machoni.

Kurunzi ile kali ilimwonyesha barabara kiasi gani alikuwa amekongoroka na kusababisha hata bufuru la kichwa chake kuonekana.

Mwonekano aliokuwanao ni sawasawa na fuvu la mwanadamu lililosalia na nyama kidogo kimakosa.

Macho yalikuwa mekundu na yamemtumbuka mithiri ya kinyago kilichochorwa kwa nia ya kuchekesha.

Lakini huyu hakuchekesha bali alitia simanzi.

Ngozi ilikuwa haieleweki rangi yake, mabaka si mabaka, mba si mba.

Dantan alikuwa hajaipata haki yake ya msingi ya kuuosha mwili wake kwa siku zote alizokuwa gerezani.

Kana kwamba akiachiwa huru kwa sekunde kadhaa atajilipua na kuzua janga kubwa la kitaifa, alipotoka nje askari wakakamavu wakamdaka na kumfunga kamba kwa kumkaza mikono yake iliyozungushwa kwa nyuma.

Alipothubutu kuguna, alichabangwa kofi kali asilolitarajia, kofi lile la mwanaume aliyeshiba likatua katika uso wake.

Badala ya kuona mwanga mkali akabaki kuona vimurimuri vikimweka, ni kama aliyekuwa akiitazama anga kwa mbali sana.

“Inukaaa!” alifokewa. Akajikongoja ili ainuke, likatua tena kofi jingine hili la sasa likatua sikioni. Paa!

Milio ya gari la wagonjwa ikavuma katika sikio lake ‘wiuwiuwiuwiu’.

Akadakwa safari hii asianguke, akabebwa mzobemzobe hadi katika karandinga, wakamlaza kifudifudi na kuondoka naye kwa kasi kubwa.

Niseme nini sasa kuhusu maumivu aliyopitia? Kwani wewe huwezi kuyakadiria?


Mwendo wa dakika thelathini gari likasimama, akateremshwa na kuongozwa katika jumba lililochakaa.

“Wanaenda kuniua Mungu wangu!… sijui watanichinja kama kuku, ama watanipiga kwa risasi.?” Danstan alizungumza peke yake.

Alizongwazongwa hadi akaingia katika lango la kwanza. Akafunguliwa zile kamba na baada ya hapo akaamriwa kuvua nguo zake zote.

Wanaume sita mbele yake walioficha tupu zao wakaukashifu uume wa Danstan na vyovyote walivyoweza kuviona.

Geuka, inama, chuchumaa!!, geuka tena!Hizi zilikuwa amri zilizotolewa hovyohovyo.

Danstan asiyekuwa na nguo mwilini mwake akazitii.

Ghafla walimvamia kana kwamba alikuwa akijaribu kupambana nao. Wakamtia kamba mikononi na kuanza kumburuta. Wakalifikia shimo wakamwamuru atumbukie ama wamtumbukize. Lakini pia akapewa uchaguzi wa kukubali kwa neno moja tu kuwa anajihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya.

Kosa moja ni pale Danstan alipothubu kuhoji kuwa yawezekana wamemfananisha.

Ikawa ni kama aliyezikebehi tupu za mama zao. Mmoja akamvamia na kumbandika gundi katika mdomo wake hata asiweze kukifumbua kinywa chake.

Akiwa hajakaa sawa anasukumwa katika lile shimo.

Lilikuwa ni mfano wa bwawa la maji.

Danstan akazikumbuka simulizi za Daniel juu ya sakata mojawapo katika gereza. Unaweza kuzikwa ukiwa hai.

Hofu ikatamalaki!

Wakamzamisha huko na kisha kumwacha ajione anavyopitia hatua za roho kuuacha mwili. Alikosa pumzi, na mikono ikiwa imefungwa kwa nyuma.

Baada ya muda walimuibua na kumuuliza kama anakubali ama anakataa.

Wanaume sita wa mashariki ya mbali wanabaki kusubiri jibu kwa mtu waliyemziba kinywa chake.

Atanena kwa kutumia masikio?

Uwaweke kundi gani watu hawa, ni mazuzu!

Walipoona hatoi jibu wakamzamisha tena.

Danstan aliyewahi kudhani kuwa kifo alikiona siku ambayo alipigwa na kusogezwa jirani na domo la umauti, akivuja damu na kuvimba mwili mzima.

Leo hii aliweza kuiona sura ya yule malaika anayepewa sifa za kwamba ni yeye hutoa roho za walimwengu.

Alikuwa anazama naye majini na kumsisitiza kuwa kama vipi afe waondoke.

Danstan anajaribu kukubali kwa kusema ‘ndio ni heri nife’ lakini kinywa kimezibwa na gundi.

Ndani ya maji yale njia pekee ya kupumua ilikuwa ni pua.

Pua ivute hewa ndani, hiyohiyo itoe nje.

Na hapo alikuwa ndani ya maji.


Wakamuibua tena nje baada ya muda waliojipangia kutamati.

Safari hii walimtolea lile gundi mdomoni, macho yake yalikuwa mekundu sana. Ni kama alikuwa katika sekunde za mwisho za kuushika mkono wa malaika mtoa roho na kuondoka naye kwa amani.

Mafedhuli wakaizuia tena safari hii!

Danstan alikohoa mpaka akaanza kutema damu, sahau kuhusu haja kubwa na ndogo zilizopenya pasi na hiari yake.

Wanaume wale wasiojali utu wakalifanya tukio lile ni kichekesho.

Tuwalaumu hawa sita ama tumlaumu aliyewaagiza?

____________


NANI atamvisha paka kengere? Swali hili liliibuka nchini Semedari katika jiji la mainstream.

Diana, mama mzazi wa Danstan alikuwa amecharuka na hakutulia kabisa baada ya sakata la zungu la unga nchini Mashariki ya Mbali. Hisia juu ya mwanaye kuwa matatani zilimuandama mno.

Jambo zito likawa ni nani atakayeenda Mashariki ya Mbali kwa ajili ya kufuatilia jambo lile? Aujue ukweli.

Daniel akamsihi Diana awe mtulivu. Wakajaribu kumuandikia Danstan barua pepe kutazama iwapo watapata majibu kwa wakati.

Hilo likafanyika, siku tatu zikapita bila majibu kutoka Mashariki ya mbali.

Tayari walikuwa wamejaribu kupitia mitandaoni na kuitafuta habari iliyoelezea kwa kina juu ya sakata hilo. Hakuna sehemu walipoambulia jina la muhusika wa kuitwa ‘zungu’.

Maamuzi magumu yakachukuliwa.

Lazima atumwe mjumbe kwenda Mashariki ya mbali.

Wakati wajumbe wa kwenda nchi nyingine hulindwa na ule usemi wa mjumbe hauwawi.

Mashariki ya mbali, mjumbe anapigwa, anavunjwa, na aliyemuagiza naye cha moto atakiona.


Ndivyo ilivyo, mgeni kwenda kumwokoa mgeni ni kuwapa faida maadui. Walau mwenyeji anayezijua chochoro za hapa na pale anaweza kuwa msaada dhidi ya mgeni.

Turufu ikamwangukia Daniel Katunzi.

Turufu gani hii ya kurejea Mashariki ya mbali?

Aliwahi kutetemeka katika maisha yake, kwa uoga na baridi pia. Lakini hii ya kuambiwa kurejea Mashariki ya mbali, Daniel Katunzi alijikuta akipatwa na homa kali, ikapandwa na Maralia juu yake, Kichocho na tumbo la kuhara vyote vikatokea bila dalili katika mwili wake.

Hiki nini? Alijiuliza akiwa chumbani kwake. Waliopo nje walikuwa wamejikita katika kumwandalia safari yake.

Alifahamu vyema kuwa sio tu dhana ya ugeni inayosababisha wasiwe tayari kwenda Mashariki ya mbali, bali uoga na sasa walikuwa wamefahamu vyema nini maana ya Mashariki ya mbali.

Ni kweli Daniel aliwahi kuapa kuwa siku moja atarejea nchi yake pendwa ya Mashariki ya mbali. Lakini hili la kurejea kwa ajili ya kumwokoa mtu kutoka katika sakata la uuzaji wa madawa ya kulevya, lilikuwa zito sana.


Ile hali ya kuendelea kukaa ndani ilizidi kukaribisha magonjwa mengine. Daniel akajiweka swafi mwili wake kisha akatoka nje na kuzunguka mitaa ya Mainstream kona tofauti tofauti hadi akaifikia maktaba kubwa iliyopo jijini pale.

Akaingia humo na na kuzama katika vitabu vya kihistoria, hususani historia za kiafrika.

Alijaribu kusoma mambo kadhaa ambayo walau yanaweza kumtia hasira na hamu ya kurejea mashariki ya mbali. Lakini karibia kila kitu alikuwa anakifahamu tayari.

Kubwa aliloendelea kuliboresha katika kichwa chake ni juu ya wakoloni waarabu kwa wazungu jinsi walivyoitendea ubaya afrika.

Alitazama ukurasa mmoja ukitangaza dini ya kikristo na kuelezea kuwa Yesu ni bwana na mwokozi wa maisha ya wanadamu. Katika ukurasa mwingine anawaona hao watumishi wa Mungu wanaoeneza hayo maneno ya busara wakiwa wamesimama mahali wakishuhudia watu weusi wakiwa wananyongwa.

Akasoma kwa chini kuwa, watu wale walinyongwa kwa sababu walikuwa wakicheza mpira na watoto wa kizungu ambao ni ndugu wa anayejiita kiongozi wa kiroho.

“Madhalimu wakubwa…. Unahubiri nini na nini hiki unafanya?” Daniel alisema kwa sauti kuu, chozi likikaribia kumtoka.

“Na huu ndo mzigo wa ujinga waliouacha Mashariki ya mbali. Si kwa waislamu wala wakristo wote sawa tu. Waarabu walituchapa mijeledi na baadaye wanatuambia Tumsalie Mtume Muhamad sala na salaam zote juu yake, hawa wengine nao walinyonga babu zetu na kisha wanawajaza maneno kuwa Yesu ndiye mkombozi wa maisha yao. Mkombozi? Mbona basi mnajivesha vyeo vya kuua na kuhuisha?? Tumsalie Muhamad, mbona basi ninyi hammsalii na mnatunyanyasa??

Tazama nchi yangu sasa, makanisa yanavyorundikana. Mtu akiamka asubuhi na mke wake wanaanzisha kanisa na wanatoa mapepo, keshokutwa mwingine naye anaanzisha kanisa lake. Dini zimekuwa biashara inayolipa zaidi, na hii ni kwa sababu ndugu zangu wana msongo wa mawazo. Wanatafuta popote pa kuponea, wengi wanaitafuta nafuu ya maisha kupitia dini, wakati huohuo aliyeanzisha kanisa naye ananufaika na sadaka. Na ili tuzidi kuchanganyikiwa vyema, hawa watu weupe wanatoa misaada mikubwa kwa ajili ya makanisa zaidi kujengwa. Ukoloni mamboleo! Na nikirudi huko siendi cha kanisani wala msikitini!!” alimaliza kwa kufoka Daniel Katunzi.

Halafu akajikuta anacheka mwenyewe alipofanya tathimini na kugundua kuwa maamuzi yake hayamkomoi mtu yeyote. Kwani tangu aondoke huko nani anaathirika??

Akajiondokea pale maktaba huku ile picha iliyopigwa miaka ya sitini, ya vijana wa kiafrika wakinyongwa kisa kucheza mpira na watoto wa kizungu ikitembea katika kichwa chake katika namna ya kuudhi.

Madhalimu wakubwa!!! Alijisemea tena.

Hakujua alitumia muda gani kufika nyumbani, lakini akili ilimkaa sawa alipoelezwa kuwa wamefanikiwa kupata nafasi katika ndege inayoondoka usiku majira ya saa tatu!

Akaishika ile tikiti ya ndege, akaangaza huku na kule hatimaye akakiona kituo chake cha mwisho.

MASHARIKI YA MBALI MAJIRA YA SAA MOJA USIKU!

Kijasho chembamba kikamtoka mgongoni kikateremka hadi katika mihimili ya makalio yake.

Akabaki kuwa mkosa kauli, aseme asante baada ya kukabidhiwa tiketi ilea ma atoe kauli gani.

Daniel akajitambua kuwa bado hakuwa na utayari wa kurejea Mashariki ya mbali.

Lakini tayari sasa anayo tiketi mkononi.

Hakuna namna!





“Tofauti kuu kati ya UJINGA na AKILI ni kuwa AKILI ina kikomo lakini UJINGA hauna kikomo.”… Tafsiri kadri ya uwezo wako…..


NA HII NI SEHEMU YA KUMI NA MBILI.


ILIKUWA yapata saa tano takribani dakika kumi na sita wakati macho ya Daniel yalipoitazama kwa ukaribu kabisa mandhari ya kupendeza ya nchi yake ya kuzaliwa.

Mashariki ya mbali!.

Aliyatazama mandhari ya kupendeza yaliyopo katika uwanja ule yakisindikizwa na harufu nzuri ya manukato.

Alipepesa macho yake huku na kule na kuvutiwa na vibanda kadha wa kadha vya kukatisha tikiti za ndege. Katika baadhi ya vibanda alivyowqeza kuvitupia macho, alikutanisha macho yake na sura za vijana waliokuwa na tabasamu muda wote. Walicheka na kutaniana huku wakikumbuka kugonga mikono yao.

Sura zao ziliwaka vyema, hawakuonekana kuwa na shida!

Vilevile kama nilivyoondoka.

Daniel alijisemea huku akiunyanyua mguu wake na kuanza kujongea taratibu akiuacha uwanja ule wa ndege baada ya kuwa amebadili kiasi cha fedha kutoka fedha ya Semedari na kuwa fedha halali kwa malipo ya Mashariki ya mbali, akaingia barabarani.

Hapo sasa madereva wa taksi wakaanza kumdandia, wakimvisha vyeo mbalimbali vikubwa.

Afisa, Bosi, mkurugenzi, muheshimiwa!

Daniel akawatazama, kisha akajisemea katika moyo wake kwa masikitiko.

Hivi nd’o vyeo vya kijinga, huwa mnawavisha viongozi wetu hadi wanavimba vichwa, miguu na mikono.

Daniel hakutaka kujikweza na kujisahaulisha hali halisi ya nchi yake ya Mashariki ya mbali. Licha ya kwamba alikuwa anaamini kabisa pesa aliyokuwa anaimiliki, ilitosha kabisa kuabiri taksi. Hakutaka kufanya hivyo.

Sio kilichokuwa kimempeleka huko!.

Akawapuuza madereva wale, akaendelea kwenda mbele, hadi akaifikia barabara kuu. Huku napo akatulia kidogo akaisaili hali ya barabara. Ilikuwa katika kiwango kizuri, na hata vile vigari vidogo vya abiria alivyoviacha wakati anatimka hakuviona.

Sasa zilikuwa ni gari kubwakubwa zilizoipendezesha barabara ya lami. Barabara iliyopendezeswa na bustani iliyotengenezwa katikati yake.

Akafanikiwa kuwaona madereva kadhaa waliokuwa wanaendesha magari hayo, walikuwa wana sare maalumu.

Tumeendelea aisee! Alijisemea huku akitokwa na tabasamu hafifu.

Hakuwa na uelekeo maalumu, hivyo popote angeweza kwenda kwa wakati wowote ule kisha atoe taarifa kwa Diana aliyesalia katika jiji la Mainstream huko Semedari.

Hivyo aliendelea kusaili kila kilichokuwa kinapita mbele yake, akajiweka katika pembe ambayo hataleta umakini kwa watu kuhisi labda amepotea ama kuna jambo analifuatilia.

Hakuwa amewasahau nduguze wa Mashariki ya mbali kwa kupenda kushughulika na yasiyowahusu.

Macho yake yakatua kwa mabinti watatu waliokuwa wanakatiza mbele yake, maumbo yao yalionyesha kuwa wanakula vizuri, wameridhika na maisha na wanaufurahia utandawazi.

Nguo zao zilikuwa zimeyashika vyema mauongo yao katika namna ya kufurahisha macho. Mwingine alivaa sketi fupi kiasi kwamba mguu pekee haukuridhika kuwa nje, paja nalo likatoka kuchungulia faida za kuwa nje.

Lilikuwa linatokwa na machozi yasiyokauka yaliyotengeneza michirizi isiyoudhi kuitazama.

Bila kujua ametumia muda gani kuwashangaa, mmoja kati yao akamtupia salamu ya kumsanifu ama kumtoa katika mshangao wake.

“Hai!”

Daniel akajikohoza kidogo kabla ya kujibu lolote, ilikuwa ni katika hali ya kujirejeshea ujasiri aliokuwa ameupoteza tayari. Hakuweza kujibu kitu, wakacheka wakagonga mikono yao na kuendelea kutembea.

Sasa walikuwa wanatikisika zaidi.

Pengine labda walisubiri apatikane mtazamaji.

Tena mtazamaji mtanashati kama Daniel.

Acha wajitikise!.

Mwingine akaziweka sawa nywele zake bandia kichwani, kisha akazirusha nyuma kwa kutupa kichwa kana kwamba amezaliwa nazo. Kama tu wanavyofanya akinamama wa Semedari.

Ukoloni mamboleo!


Aliendelea kubaki akitazama wingi wa gari za kifahari zilizokuwa zikipita bila kuachiana hata nafasi ya sekunde mbili. Nyingi kati ya gari hizo zikiendeshwa na wanawake wenye umri mdogo kimakisio.

“Mashariki ya mbali kumekucha!!” Daniel alijisemea huku akisogea hatua kadhaa na kuifikia barabara, akatazama umbali wa magari yalipokuwa kisha akavuka upande wa pili.

Sasa alikuwa amejichanganya katika kituo cha daladala, na kwa sababu hakuwa na uelekeo maalumu alipanda daladala iliyokuwa ikielekea popote na atashuka atakapojisikia.

Daladala haikuweza kuondoka kabla kondakta na mpiga debe hawajakwidana mashati. Mpiga debe akilalamika kuwa ujira aliopewa hautoshi.

He! Haya mambo hayajaisha tu? Daniel alijiuliza huku akikumbuka miaka kadhaa nyuma.

Walikuwepo na walidai pesa kwa kazi isiyokuwa kazi.

Kusimama kituoni, abiria wanaliona gari na kuliwania kisha unataka ulipwe, tena kiasi unachotaka wewe mwenyewe.

Ni nani aliyetukamata akili kisha akaziroga? Daniel alistaajabia.

Kondakta akawa mbabe zaidi, ugomvi ukamalizika kwa kutukaniana ndugu wasiokuwepo. Mama mzazi akiwa muhanga namba moja.


Ndani ya daladala aliendelea kujiridhisha kuwa Mashariki ya mbali palikuwa pamekucha, si mkubwa wala mdogo wote walimiliki simu ambazo kwa harakaharaka zilikuwa za bei ghali.

Wanawake wengi walikuwa weupe na wanaume pia walikuwa katika uelekeo huo.

Wanajipaka nini hawa? Likawa swali juu ya swali katika fikra zake.

“Haya ni mabadiliko makubwa sana ya hali ya hewa ama?” alijiuliza asiwe na yeyote wa kumjibu.

Tofauti na Semedari ambapo abiria waketio viti vya kufuatana hupeana salamu na mara nyingi sana kubadilishana mawazo.

Hali ya Mashariki ya mbali ilianza kumtisha, kila mtu alikuwa yungali kimya na simu yake. Ni kama kila mmoja alikuwa na mashaka na mwenzake. Waliketi kama watu wanaosubiri la mgambo lilie kisha wazue jambo.

Wamekuaje? Alijiuliza.

“Samahani ni saa ngapi sasa hivi?” alijaribu kumuuliza jirani yake waliyefanikiwa kukaa viti vya kufuatana.

Yule bwana akamtazama usoni, hata asimjibu chochote.

“Saa nane kasorobo” akajibiwa na mtu aliyekuwa ameketi siti ya nyuma yake.

Daniel Katunzi akageuka na kumshukuru. Alikuwa ni binti aliyekuwa amejitanda vyema katika hijabu yake.

Safari iliendelea, wanaoshuka walishuka na kuwapisha waliokuwa wanapanda. Daniel yeye alikuwa akifanya shughuli ya kutazama mabadiliko makubwa nchini kwake.

Barabara zilikuwa za lami na alitabasamu alipogundua kuwa kumbe kuna mataa pia ya kuongoza magari yametapakaa sehemu tofauti tofauti.

Kituo kingine anapanda kijana, kingine anashuka mtoto wa shule, hatimaye akapanda baba mtu mzima ambaye nywele zake zilikuwa nusu zimekubaliana na hali ya kuwa nyeusi na nyingine zikisalimu amri na kuwa mvi.

Ujamaa ulikwisha ondoka, maisha ya Mashariki ya mbali yalikuwa ya ubinafsi.

Kimfaacho mtu chake!

Yule mzee akakosa pahali pa kuketi, Daniel akasimama na kumpisha.

Kwa tukio lile, akawa kama kivutio. Watu wakawa wanamuangalia kwa macho ya kuibiaibia.


Waliendelea kuingia abiria, na wote hawakupata pa kuketi, wakarundikana. Na kero ikaanza.

Haikupita dakika ishirini zaidi katika safari kabla mama mmoja hajaangua kilio kuwa ameibiwa simu yake.

Yowe lake kubwa likamsababisha dereva aweke gari pembeni na kuisikiliza ile kesi.

Mama akadai kuwa aliingia na simu yake katika daladala hivyo mwizi yungali pamoja nao katika safari.

Vuta n’kuvute ikatawala, mwishowe wakakubaliana gari lipelekwe kituo cha polisi kwa ajili ya ukaguzi.

Na hapo ndipo kizaazaa rasmi kilipoanzia!!

Daniel alikuwa katika mafadhaiko wa aina yake kwa tukio lile, akabaki kujiuliza ni nini thamani ya simu dhidi ya thawabu kutoka kwa Mungu.

Sio kwamba Semedari hapakuwa na wezi wa namna hii, hakutaka kujua kuhusu wao aliwaza kuhusu nchi yake ya Mashariki ya mbali. Sifa pekee iliyokuwa imesalia ni hiyo ya amani upendo na utulivu.

Zipo wapi tena??

Wakakifikia kituo, wakapokelewa na askari asiyekuwa na cheo chchote. Alikuwa amekunja sura yake. Haieleweki kama alifanya maksudi ili aonekana kama anatisha ama la.

Kama alimaanisha kutisha, hakutisha bali alionekana ni kijana anayejizeesha kwa kuzikunja ndita zake pasi na sababu.

Aliingia ndani ya gari lile na kuanza kufoka asijulikane ni kitu gani alikuwa anamaanisha.

Lililoeleweka ni kwamba gari zima washuke na ukaguzi unapita.


Ikawa kama ilivyoamriwa. Kila mmoja akashuka na kukaguliwa, wanawake wakikaguliwa na askari wa kike na wanaume wakiangukia mikononi mwa yule askari anayejizeesha bila sababu.

Hamaaad!! Simu ikakutwa katika koti la suti ambalo muda wote Dany alikuwa amelining’iniza begani, hii ni baada ya kukutana na hali ya hewa ya joto.

Looh! Miguno ya fadhaa ikawatoka akinamama, wakamtazama Dany katika jicho la dharau, ufedhuli na kila aina ya kebehi.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG