Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

MASHARIKI YA MBALI - 2

   

Simulizi : Mashariki Ya Mbali

Sehemu Ya Pili (2)


Danstan alijikuna bila kuwashwa. Alikuwa ameropoka na kujiona amejenga hoja.

Muuguzi akamtazama na hata asiruhusu kinywa chake kusema lolote bali akijisemeza yeye na nafsi yake.

“Kumbe hata hawa wenye rangi nyeupe wanaweza kuwa wa mwisho darasani eeh! Tazama hiki kiazi mbatata, kinaropoka tangu kilipofika hapa. Huyu darasani hata mimi ningemburuza vizuri tu.”

Na hata fikra zilipofikia ukomo akatoa tabasamu kwa mara ya kwanza kufurahia yaliyojadiliwa katika kichwa chake juu ya bwana yule.

“Ni nani aliyekufundisha kuzungumza lugha yetu adhimu. Unazungumza vizuri sana.” Akasindikiza tabasamu lake kwa kauli ile isiyomaanisha kitu.

“Samahani anaweza kurejewa na fahamu zake muda gani?” Danstani alihoji bila kujibu swali la muuguzi.

“Kama alivyoondoka tu..” kwa utaratibu wake uleule naye alijibu.

“Una maana gani?”

“Wakati anazipoteza fahamu hakumweleza mtu yeyote kuwa sasa napoteza fahamu. Na hata kwenye kuamua kuzirejesha hatamwambia yeyote. Hiyo ni siri yake” Muuguzi alijibu, jibu lile likaambatana na kibatari kuiaga dunia baada ya kuchoma sana utambi wake.

Mshumaa ukabaki kusambaza upendo.

Danstan alichoka akili, roho na mwili!



Lingalipo jua usilalame kuwa lakuunguza, waliokanyaga kaa la moto waseme nini?

Acha mvua ikunyee kimyakimya, usipige kelele. Waache walalamike wanaodondokewa na theluji.

Kama lalamiko lako kuu ni kupata watoto jinsia moja mfululizo basi hakuna unalolalamikia mbele ya wasiowahi kamwe kupata mtoto katika maisha yako.

Usijijengee dhana ya kuwa mtu wa kuhisi anaonewa kila mara, tembea ujionee hautalalama tena.


NA HII NI SEHEMU YA SITA.


Katika sehemu ya tano, iliishia Danstan akipitia hekaheka nzito akiwa Mashariki ya mbali, Cherry mchumba wake anapatwa na balaa la kuanguka na baiskeli. Jiwe linauchana vibaya mguu wake anakimbizwa katika kituo cha afya ambacho kinasimamiwa na muuguzi mmoja tu. Yaliyotokea huko yanakuwa ishara ya ukaribisho kwa Danstan.

Karibu Mashariki ya mbali.


¬¬¬_________


MAJIRA ya saa nne asubuhi daktari alipita katika kituo kile, kwa kauli ya muuguzi ni kwamba daktari yule huwa anapita kuwasalimia, kusikiliza malalamiko kadhaa kutikisa kichwa kwa masikitiko makubwa kisha kuondoka kana kwamba anarejea na suluhisho.

Baada ya wiki kadhaa nd’o anarejea, hajatatua lililomsikitisha mara ya mwisho anaanza kusikitishwa na mengine tena.

Alizoeleka hivyo!

Lakini siku hii mambo yalikuwa tofauti, alipopita katika wodi ya wagonjwa isiyokuwa na vitanda aliona hali tofauti.

Sura ya mtu mweupe!

Daktari akashtushwa sana, akawaza ni misaada mingapi wazungu wamewahi kuagiza ifike katika zahanati ile badala yake akaihamishia njia ikaenda katika zahanati yake iliyopo mjini.

Hatia ikatia nanga katika moyo wake.

Daktari akaanza kujuta kimyakimya kwa udhulumati wake alioufanya. Akaiweka vyema suruali yake kiunoni kisha akajikumbushia maneno mawili matatu katika lugha ya Samaradi, ni muda sana alikuwa hajazungumza lugha ya kigeni hivyo alihofia kubabaika atakapoanza kuhojiwa na bwana yule.

“Huyu muuguzi naye mbona hakunipanga mapema nijiandae. Nadhalilika leo…” Daktari alizungumza kwa sauti ya chini na sasa alikuwa hatua kadhaa kumkaribia bwana yule.

“Habari ya asubuhi..” mzungu yule akaanza kumsalimia kwa heshima kubwa. Daktari akashtuka, akamtazama kwa makini iwapo ni mzungu kweli ama vinginevyo.

Alikuwa mzungu!

“Bila shaka wewe ni daktari. Nina mgonjwa wangu hapa. Naomba umsaidie tafadhali. Nilimleta jana usiku”

Danstan alizungumza kwa kusihi.

Daktari akafuatisha mikono ya Danstan ilipokuwa inaelekeza. Akamwona Cherry akiwa amejilaza, fahamu zikiwa zimemrejea.

Daktari akasahau ile hatia iliyokuwa inamwandama akaitazama fursa iliyokuwa inajipitisha mbele yake.

Fursa kubwa asubuhi asubuhi!! Akajisemea.

Harufu ya dolali!

______

Upesi akamwita muuguzi, wakasaidiana pamoja na Danstan wakambeba Cherry kwa uangalifu mkubwa mno mpaka katika gari ya daktari.

Wagonjwa wengine wakabaki kunung’unika kuwa mgonjwa huyu amependelewa, wao wana matatizo makubwa lakini kila kukicha ni danadana hadi wengine mauti yanawakuta kwa uzembe wa daktari huyu.

Ajabu ya mwaka! Daktari huyu mjivuni, leo hii kwa mikono yake anambeba mgonjwa.

Utumwa huu utakwisha lini? Muuguzi alisaidiana na wagonjwa wengine kujiuliza swali lile wakati gari ikitimua vumbi kwa fujo angali ikitoweka.

Haukuwa utumwa, hawakujua tu.


________


SAMARADI, MAINSTREAM


Ilikuwa barua pepe ya kwanza kutoka Mashariki ya mbali, ukiwa ujumbe umetumwa na Danstan.

Daniel alifurahi sana kupokea ujumbe kutoka nchi yake ya kuzaliwa na kukua. Na alitamani sana kufahamu ni kipi ambacho Danstan alikuwa amemuandikia, Dany anaingia chumbani kwake na kisha kuifungua barua pepe ile iliyokuwa imesheheni insha yenye aya za kutosha jumla yake yafaa kutengeneza kitabu cha hadithi kadhaa za watoto.


DANSTAN ANAANDIKA.


Salaam Daniel, nisalimie Mainstream nzima hususani familia yangu. Ya huko mengi nayafahamu… ni mgeni sana kwa haya yanayotokea huku ulipozaliwa wewe na kuishi. Hata sasa najiuliza uliweza vipi?

Nimejionea mengi na bado majibu sina. Nimejionea ng’ombe wakilimishwa shamba kubwa huku wanachapwa viboko hadi ngozi zao zinachanika. Katika vidonda hivyo inafungwa nira nzito. Kisha anapigiwa kelele alime kwa juhudi.

Hata baada ya suluba hii, waliomcharaza watajipakiza katika mkokoteni kisaha watamwamrisha tena kwa viboko ng’ombe huyu awaburute mpaka nyumbani.

Kwa mara ya kwanza nimeliona chozi la uchungu likitoka katika macho ya ng’ombe. Ni kweli watu wako hawawezi kusoma lugha nyepesi kama hii, kuwa ng’ombe anaumia?

Nimewaona watoto wadogo wakienda umbali mrefu sana kuitafuta shule, matumbo yao nje na miguuni hawana viatu. Hili ni jipya ama lilikuwepo wakati unaishi huku?

Tukiachana na hayo waliyoyazoea, kuna hili la ajabu. Huko kwetu kifo ni kitu ambacho tunafahamu kipo na ni mipango ya Mungu lakini hatukubali vifo vinavyosababishwa na uzembe. Huku kwenu kifo ni mipango ya Mungu inayoharakishwa na wanadamu wenyewe. Na baada ya uzembe wao wana kauli yao ya alipangalo Mola mwanadamu hawezi kuzuia.

Usipokuwa na pesa kifo chako kinawahi, ukiwanazo unaweza kununua maisha.

Waambie wanadamu wa huko wanaotawaliwa na usemi huo wa kisemedari wa ‘money can’t buy life’ waje huku Mashariki ya mbali pesa inanunua maisha.

Cherry alipatwa na ajali ya baiskeli na kuchanika vibaya mguuni, katika zahanati hii tulipata huduma ya kwanza kwa mbinde na hapakuwa na mwendelezo wowote, kwa macho yangu nimeshuhudia wagonjwa wakiwa wameikumbatia sakafu. Hii ndo namna yao pekee ya kulala.

Daniel! Hakuna vitanda wala magodoro, eti daktari alihamishia nyumbani kwake.

Nimeliona chozi la damu likitoka katika macho ya mgonjwa aliyelia kwa muda mrefu kwa sababu ya uchungu anaoupitia bila msaada.

Hakuna madawa katika zahanati hii, lakini hii haimaanishi kuwa kuna uhaba wa dawa katika nchi yako.

Dawa zipo, jipekue uweke pesa mbele na utaziona dawa hizo.

Mimi yamenisibu….. kuumia kwa Cherry limekuwa funzo kwangu.

Nilithubutu kumletea jeuri muuguzi ambaye ugumu wa maisha umemfanya kuugua ugonjwa uitwao ‘hakuna ninaloogopa’. Nikajaribu kuweka vitisho, badala atishike ananiuliza ni nani amenifundisha kuongea lugha yenu.

Nikalazimika kuwa mpole kwa usalama wa Cherry. Kweli akamshona na kumwacha naye akiikumbatia sakafu ya baridi sana.

Hizi ndizo zahanati za kwenu Daniel. Amakweli uliyonisimulia yalikuwa rasharasha acha nijionee mwenyewe.

Asubuhi alifika daktari na kuonyesha ukarimu wa hali ya juu.

Nilistaajabu daktari alivyonishughulikia kwa upendo na wepesi sana, nikabaki kujiuliza kuwa kumbe watu wema bado wanaishi, lakini kumbe naye alikuwa katika kuisaka ridhiki yake. Tulipofika katika zahanati ambayo inasemekana kuwa ni mali yake akishirikiana na diwani wa kata hii, mambo yakabadilika.

Nilitakiwa kununua sindano, dawa, nikatakiwa kununua chupa za dripu nikatakiwa pia kulipia kitanda na kumpatia daktari kile alichokiita ‘hela ya supu’.

Nilipojaribu kuleta ujuaji wangu kuhusu masuala ya afya akanieleza kuwa atanipatia chumba bure kabisa, niingie mimi na mgonjwa wangu kisha nikamtibu.

Niliduwaa lakini yeye hakuwa na muda na alikuwa ameanza kunipa mgongo kabla sijamuita na kumweleza kuwa nipo tayari.

Duka ambalo nilinunua vifaa vyote hivyo ni mali ya daktari huyo.

Hivyo hapo tulikuwa katika biashara ya kisasa, mteja kudhani amependelewa na anapogeuza mgongo muuzaji anachekelea.

Nilihisi daktari amenipendelea aliponitoa katika ile zahanati isiyokuwa na vitanda, kumbe alikuwa ananivuta kwenda kunufaika na mimi. Ninachoshukuru ni kwamba baada ya kuitoa hiyo pesa, Cherry ametibiwa vyema kabisa na yu buheri wa afya kwa sasa.

Nitaendelea kukuandikia kadri ninavyopata wasaa wa kufanya hivyo, nia yangu bado ni thabiti nina imani itatimia. Nisalimie familia yangu….


Wako,

Danstan Mcdonald

Mashariki ya mbali.


________


DANIEL alimaliza kuisoma barua ile huku akiishia kutikisa kichwa chake. Alijisikia aibu ndani ya moyo wake, kwa mambo ambayo nchi yake inayatenda hata kwa wageni.

Baada ya tafakari ya muda mrefu, hatimaye Daniel aliamua kujilaza kitandani ambapo aliendelea kufikiria kuhusu barua ambayo aliipokea kutoka kwa Danstan.

Daniel alisikitishwa na mengi, lakini kubwa zaidi ni kwamba aliona kuwa bado Danstan hajapitia chungutamu za Mashariki ya mbali na bado ameweza kuandika barua ile akionekana kama anayelalamika.

Magumu ya Mashariki ya mbali yakapita katika kichwa cha Daniel kwa kasi ya ajabu na bado hayakumalizika upesi, nchi hiyo isiyoisha vibweka haikuwa sawa kabisa kwa mwanaume ‘laini’ kama Danstan kuitembelea.


“Anashangaa wagonjwa kulala sakafuni? Hilo tu…. Yaani daktari kuomba pesa ya supu kwake ni ajabu la mwaka, huyu akikutana na daktari aliyevurugwa na pombe za kienyeji akamfanyia mtu upasuaji wa kichwa wakati katika vyeti amesomea magonjwa ya akinamama. Si atachangayikiwa huyu kijana.

Kabla hajachanganyikiwa huyu kijana na kisha familia yake kutupa laana katika nchi yangu ambayo ni kama imelaaniwa tayari nadhani napaswa kufanya kila namna aweze kurejea huku nchini kwao. Ya huko Mashariki ya mbali atuachie sisi wana mashariki ya mbali. Asubuhi nitazungumza na mama yake…… asije akampoteza kijana wake ghafla.”

Daniel alipitiwa na usingizi akiwa katika wazo hilo.

Lakini wakati yeye analala nchini Semedari, kule Mashariki ya mbali ndo kwanza mchana ulikuwa unaingia na Danstan tayari alikuwa katika hekaheka.

Katika hekaheka hizo, likazuka jambo!

Jambo lililozua mambo….



Utafanya jitihada na kuyakwepa mengi kwa utashi wako, lakini ni jambo gumu sana kumkwepa mwenye CHUKI YA ASILI. Ukicheka naye atachukia, ukiachana naye atachukia, ukiimba, ukiongea, ukinyamaza… bado atachukia. Huyu ni yule ambaye siku ukifa atachukia na ukiendelea kuishi pia atachukia….. WAPO TUNAISHI NAO.


Na hii ni SEHEMU YA SABA.


Hali ya Cherry kiafya ilitosheleza kabisa kuitwa yenye ahueni. Japokuwa hakutanabaisha kuwa alikuwa amechukizwa na ile safari ya Mashariki ya mbali lakini dhahiri nafsi yake ilibubujikwa na machozi huku moyo nao ukijutia kuanguka katika penzi la Danstan.

Sasa penzi linauzidi nguvu uhalisia Cherry hana budi anavumilia shubiri ile. Ule usemi wa ukipenda boga, mahaba yahamishie kwenye ua lake yalitembea hadi nchini Semedari.

Danstan mtafiti yeye alianza kuburudika na maisha yale ya kujifunza kitu kipya kila siku, Cherry alijaribu kutumia mafumbo mazito kumsihi warejee nchini kwao lakini Danstan hakujifanya mwerevu wa kuyang’amua mafumbo.

Akajifanya haelewi be wala te.

Maisha yakaendelea, wakisafiri huku na kule kuifahamu vyema mashariki ya mbali, lengo la Danstan bado likiwa kufanya mapinduzi ya kifikra ili ikiwa heri basi achanganywe katika vitabu vya kihistoria na watu mashuhuri kama Mahatma Gandhi, Martin Luther King, Malcom X na wengineo wengi.

Awali aliamini katika kuwabadilisha watu waishio vijijini kwanza kisha ataingia katika miji, ajabu huko vijijini akaishia kuwa kivutio kwa watoto na mama zao. Akipita wanamshangaa na wengine kumfuata nyuma kana kwamba ni ndege aina ya tausi amekatiza huku amechanua mbawa zake za kuvutia. Nani ataacha kumshangaa?

Akijaribu kuzungumza nao wanaishia kucheka tu, mwishowe akakabiliana na balaa la muuguzi aliyechanganyikiwa.

Baada ya sakata hili akaamua kubadili mbinu.

Akazungumza na Cherry ambaye siku zote alibaki kuwa msikilizaji mkuu. Akamweleza nia yake mpya.

“Mjini kuna wengi wameelimika tuanze na hao kisha hawahawa wataelimisha ndugu zao wa huko vijijini. Maana hata hao wa mjini waliwahi kuishi vijijini” Alifanya mawasilisho yale, Cherry akakubali kwa kutikisa kichwa.

Baada ya siku tatu walihamishia makazi katika mojawapo ya jiji kubwa huko Mashariki ya mbali.

Kitendo cha kutambua kuwa wameingia jijini sasa Danstan alitarajia kuzipata zile starehe za jiji la Mainstream anapotokea. Usafiri wa kisasa usiokuwa na changamoto za kubanana na kuharibu ratiba na mengineyo.

Lakini mambo yakawa zaidi ya kinyume ikiwa pana neno linaloweza kumaanisha hivyo.

Maji ukiyavulia nguo abadani uyaoge.

Danstan akalazimika kuvumilia. Japokuwa akilala usiku zinamjia ndoto za mauzauza, anajiona yu katika daladala iliyosheheni abiria waliozidi kiasi, anakumbwa na fukuto la joto kali kutokana na ule mbanano, na bado kuna foleni kubwa sana kiasi cha kutisha.

Alikuwa anatishika yeye na Cherry tu!

Wengine walikuwa wanatabasamu huku majasho yakiwatiririka, walikuwa wanabadilishana masimulizi ya michezo na siasa kwa furaha zote. Mwisho walifika katika vituo vyao wakaagana na kukubaliana kukutana tena siku inayofuata katika karaha ile ya usafiri.

AJABU hawakutumia maneno mabaya juu ya namna ile ya usafiri! Hawakuulaani, hawakuonyesha chuki za wazi.

Nani ajuaye, yumkini walifanya hivyo miaka iliyopita. Wakalaani na kulalamika lakini hakuna lililobadilika ya nini sasa kuendelea kuipiga ngoma isiyosikilizwa na yeyote.

Kasoro Danstan na Cherry! Wao walilalamika kila kukicha.

Hawa nduguze wa hiari aliowakuta Mashariki ya mbali ni kama walikuwa na utaratibu maalumu wa kukutana katika kumbi za starehe kwa ajili ya kujipongeza kwa shida walizokuwa wanapitia.

Ama la, waliokuwa wanajazana katika kumbi za starehe pasi na kujali hii ni siku ya kazi ama la, walikuwa ni wale waliosababisha maisha yawe magumu kiasi cha kutisha.

Walinyanyua chupa zao juu na kugonganisha kwa furaha.

Wanasherekea nini hawa?

Haya yalibaki maswali ya kujiuliza. Asingetokea wa kukupatia jawabu.

________


Mwishowe penzi likawa mzigo mzito, Cherry akamwomba Danstan aanze kwenda peke yake katika hizo anazoziita hekaheka za ukombozi. Siku hii alizungumza kwa jazba sana.

“Upumbavu kiasi gani kuwabeba watu wasiobebeka. Watu hawajihurumii wewe unawahurumia, kwani umekuwa msaidizi wa Mungu ulimwenguni, kuna waraka umepewa uutimize, haupo katika njia sahihi laazizi, umebeba mzigo usiokuwa salama.” Alizungumza mengi. Danstan akamruhusu abaki nyumbani yeye ataendelea kwa muda wa siku tatu kisha watakata tikiti na kurejea nchini kwao.

Pakapambazuka. Ili ianze kuhesabika siku ya kwanza, ije ya pili kisha ifuate siku ya mwisho katika nchi ya Mashariki ya mbali.

Masaa sabini na mawili ya mwisho.

Mapambazuko yakatua habari mpya katika jiji lile.

Jiji la Fununu!

Ile Danstan anatoka nje kukiendea kituo cha daladala tayari kwa ajili ya kuzianza hekaheka, akafuatwa na watu wawili waliokuwa wakimtazama kwa makini na hadhari kubwa kana kwamba ameshika bomu na muda si mrefu anajitoa muhanga.

Danstan akahisi ni vibaka, maana alikwishayasikia mengi sana. Akajiandaa kutimua mbio iwapo watamkaribia.

Kosa kubwa sana!

Walipomkaribia kweli akaanza kurudi nyuma.

“Simama!” wakamuamuru…. Danstan akapigia mstari ile dhana yake ya awali, akaamua kutimua mbio.

Mara ikasikika amri kwa sauti ya juu sasa.

“Shoot!” ilipomalizika kauli ile iliyokuwa inangojewa kwa hamu, mlio wa risasi ukasikika. Danstan kwa macho yake akashuhudia binti asiyezidi miaka kumi na nane aliyekuwa mbele yake akirushwa mbele zaidi huku kifua chake kikifumuka na kuupunguzia moyo kazi ya kusukuma damu kila siku bila kufanikisha azma yake ya kuitoa nje.

Damu ilitapakaa! Danstan akasimama ghafla kana kwamba ni muhusika katika filamu ameambiwa agande vile alivyo.

Alikuwa anatetemeka sana. Alikuwa ameshuhudia rangi ya kifo mbele yake.

Akiwa palepale ghafla alirukiwa na watu watatu, alichoambulia kuona ni ngumi iliyolenga sikio lake, akainama kuikwepa. Hakuambulia kutambua ni kitu gani alipigwa nacho hadi akawa laini katika maungio yake ndani ya muda mfupi.

Baada ya hapo akatiwa pingu mikono ikiwa nyuma, akazongwazongwa akiwa anatazama na mitutu ya bunduki, mtaa mzima ukiwa unamshangaa yeye na lile tukio kiujumla.

Akafikishwa katika karandinga akarushwa kama mzigo wa mahindi usiokuwa na mwenyewe.

Gari ikatimua vumbi na kuwaacha wanamashariki ya mbali kila mmoja akijitengenezea simulizi yake ya kuvutia juu ya tukio lile.

Kila mmoja akaamini simulizi yake na akikataa katakata simulizi ya mwenzake.

Wakaimaliza siku na kuwahi kufunga ofisi zao ili wakawasimulie wake na waume zao nyumbani.

Ili iweje? Mi sijui labda unajua wewe!!


__________


Safari ile ilichukua dakika zipatazo arobaini na tano hadi kufikia kikomo. Akateremshwa akiwa chini ya ulinzi mkali mno. Maswali yote aliyoulizwa ni aidha asijibiwe ama la alijibiwa kwa kipigo bila kujalisha ni wapi amepigwa.

Mzobemzobe akarushwarushwa hadi akakifikia chumba alichopangiwa kuhifadhiwa.

Alirushwa humo baada ya kufunguliwa zile pingu na kisha lango likafungwa.

Harufu kali ya uvundo ikampokea. Akili yake ilikuwa malikiti, akishindwa kuunganisha ku na ni ili atambue kuna’ni kimejiri. Alibaki kulitazama jambo lile kama mchezo wa kuigiza ambao hapo awali hakuwahi kuushiriki.

Macho yake yalipokizoea kile chumba, akaona wadudu wadogo wadogo wakiwa wanatambaa. Macho yakaona na wakati huohuo mwili nao ukaanza kuhisi kuwashwa.

“Bed buds!” alitokwa na kauli ile kwa mshtuko!

Alikuwa amekutana na kunguni kwa vitendo, achana na yale aliyoyasoma kwenye daftari akiwa nchini kwao.

Walikuwa wametapakaa kila kona, na bila shaka walikuwa wameinusa harufu ya damu na ulikuwa muda wao muafaka kupata chakula wakipendacho, na baadhi tayari walikuwa wameanza kunywa damu ya Danstan.

Raha iliyoje kwa wadudiu hawa siku ya leo. Damu yenye ladha tofauti…

“Nitoe humuuuu! Nimefanya nini mimi… nitoeni!” alianza kupiga kelele, hakujibiwa hadi sauti yake ilipoanza kukauka.

Akabaki kububujikwa na machozi, kamasi zikitiririka pasi na kuzuiliwa. Kunguni wao waliendelea kufanya sherehe.

Kunguni wa Mashariki ya mbali, hawajali wewe ni mfungwa ama mahabusu kwa kudhulumiwa haki yako ama la. Unanyonywa na serikali na wao wanakunyonya kikamilifu.

Baada ya masaa tisa, akapata ugeni kwa mara ya kwanza. Mgeni huyu hakuzungumza neno lolote licha ya Danstan kujitia bingwa wa kuzungumza kauli zilizojaa vitisho.

Alichofanya yule bwana ni kumsukumia sahani ndogo ya bati isiyokuwa katika hali ya usafi.

Sahani ile ilibeba shehena ndogo ya ugali na majimaji yaliyojitia yana undugu na zile mbegu za maharage zinazohesabika. Ilimradi tu litokee la kuitwa ‘ugali na maharage’

Hakuelezwa lolote zaidi alipaswa kujiongeza.

Kwa hasira za ki-Semedari, Danstani akakipiga teke kile kisahani, ugali ukaruka kivyake, yale majimaji yakafuta undugu na mbegu za maharage kila mmoja akaishi kwake.

Mleta chakula hakutikisika hata kidogo, akaendelea na shughuli zake katika vyumba vingine.

Labda alikuwa na dharau!

Ama alikwishazoea kuziona hasira za namna ile.

Danstan alijisahau kuwa pale sio Semedari, ambapo mahabusu ukiomba kahawa yenye mchanganyiko wa maziwa na sukari kwa mbali unaletewa, ukilalamika baridi shuka zito linaletwa. Na hapo bado hujaomba mwanasheria wako afike haraka iwezekanavyo.

Masaa tisa baadaye kiza kikiwa kinene Danstan akiwa hana uwezo wa kuona kabisa, tumbo lilimkumbusha kuwa hata kupapasa ni ishara ya kutafuta na kamwe njaa haimfai mtu!!

Danstan akaanza kupapasa ni wapi ulipojificha ugali na zipo wapi zile mbegu za maharage!!

Wakati yeye anapapasa kutafuta chakula, kunguni nao walikuwa hawataki kufanyiana zamu. Walimnyonya kwa pamoja hadi akanyonyeka!!

Haikuwa ndoto!

Danstan alikuwa gereza la mahabusu nchini Mashariki ya mbali, asijue cha wala chu iliyosababisha awe pale.




“KIBURI CHA UZIMA ni gonjwa sugu linaloishi katika asilimia 90 ya wanadamu. Maisha ya kujisahau kuwa kuna kesho, ujivuni wa kudhani hata pumzi hii inanunulika, urefu wa kuhisi lijalo tunaliona unatuendesha. Kwa sababu maumivu si yako usidhani hautaumia kamwe, kwa sababu kiu si chako usiamini koo lako litaburudika milele. Maisha ni mchezo wa riadha, ipo siku mwenye shida atakukabidhi kijiti.


NA HII NI SEHEMU YA NANE.


Alichoambulia kupata ni kile kipande cha ugali, akajaribu kukigugumia, kilikuwa kigumu sana akajaribu kukilainisha na mate kiduchu yaliyochanganyikana na ute wa damu katika kinywa chake. Akafanikiwa kumeza tonge la kwanza japo kwa shida.

Tonge la pili la ugali ule mkavu akaliskia lilivyochubua koo lake, na hakuweza kuthubutu kumeza tonge la tatu japo alikuwa yungali katika uhitaji mkubwa sana.

Njaa ilikuwa inamsulubu. Lakini angeweza vipi kulimeza angali mate yalikuwa yamemkauka kinywani na kiu kikali kikivuma katika koo lake?

Danstan alikuwa amepatikana.


Ikawa haiwi hatimaye ikawa mapambazuko. Jua likachomoza na kuleta mwanga katika kile chumba kilichomuhifadhi yeye anayetambua mema na mabaya pamoja na kunguni wanaotambua ladha ya damu pekee.

Haukupita muda mrefu tangu mwanga ukijulie hali chumba kile, aliyeleta ugali siku iliyopita akafanya ziara tena katika kile chumba. Sasa alikuwa na kikombe kilichosheheni uji.

Kama kawaida yake hazungumzi zaidi ya kutenda. Akaiomba sahani kwa vitendo kisha akaacha uji pale.

Danstan hakuleta madeko tena na hasira za ki-semedari.

Akakitwaa kile kikombe na kufakamia kwa fujo uji ule usiokuwa katika viwango vya kuitwa uji.

Ilimradi uji! Kama una jina bora zaidi waweza kuubatiza.

Haukuwa na sukari, na mabuje yalijitengeneza kwa wingi.

Mabuje ambayo ukiyapasua ni unga mbichi kabisa.

Uji ule ukatuliza kwa kiasi kidogo njaa kali iliyokuwa ikiishi katika tumbo la Danstan.

Upweke ukaendelea kwa masaa kadhaa kabla hajasikia vishindo kuelekea upande aliokuwa, akajiuliza iwapo ni muda wa chakula tena ama. Maana alikuwa amepitiwa na usingizi na hakujua ni saa ngapi.

Naam! Ule ujio ulielekea alipokuwa yeye, lango likafunguliwa, wakasukumwa watu watatu wakaungana naye katika kile chumba. Mmoja akajikwaa katika ndoo iliyotumika kwa ajili ya kuhifadhi haja ndogo. Almanusura imwagike, ikayumba kushoto na kulia kisha ikatulia.

Ingizo lao likaambatana na harufu kali ya damu ya mwanadamu.

Walikuwa wametoka kuchakazwa kabla ya kufikishwa pale.

“Zungu vipi?” mmoja kati yao akamjulia hali kwa lugha ya mashariki ya mbali ambayo alikuwa akiitambua vyema.

“Safi! Poleni” alijibu kwa utulivu Danstan. Huku katika nafsi yake akikiri kuwa wale jamaa walikuwa wamepigwa wakapigika.

“”Mbona umetuingiza katika kesi isiyotuhusu mzee?” mwingine akamtupia swali.

Kesi! Alistaajabu Danstan.

“Kesi gani angali mimi mwenyewe sijui kwanini nimedhalilishwa namna hii mpaka sasa. Nataka niwaombe niongee na wakili wa familia yetu, afunge safari aje kutazama haya yanayotokea kama ni haki kwangu. Sikubali na sitokaa nikubali hili jambo liishe hivihivi.” Alilalamika Danstan, sasa nafsi yake ikipata nafuu kidogo kwa sababu alikuwa walau amepata mtu wa kuzungumza naye.

“Wakili? Yupo wapi wakili wa familia yako…”

“Mainstream Semedari” alijibu kwa kujiamini.

Mmoja kati ya wale watu aliangua kicheko na kusababisha wenzake nao kuanza kucheka.

“Kesi yako ni nzito sana, sisi tunakuomba Zungu, tusaidie tutoke. Sisi hatukujui wala wewe hautujui. Yawezekana umeteswa sana ndo maana umetuweka katika orodha…. Tunakuomba sana. Mfano mimi nina mke na mtoto halafu mke wangu ni mjamzito kwa sasa, kila kitu ananitegemea mimi. Sikatai kuwa nauza majani ya bangi lakini sio hii kesi niliyopewa mimi” Mmojawao aliendelea kusihi kwa sauti iliyotawaliwa na unyonge.

Danstan akalazimika kuelezea kwa ufupi juu ya ujio wake katika nchi ya Mashariki ya mbali hadi kufikia kukumbwa na mkasa ule wa kustaajabisha. Mkasa ambao hadi wakati huo hakukijua chanzo chake.

Simulizi yake ikawachanganya wale mabwana walioamini kuwa mle ndani wapo pamoja na mtu sahihi kabisa ambaye kusema kwake ukweli kutawapa nafuu katika kesi hiyo.

Kesi ya uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya.

Danstan alisisimka sana kutambua kuwa amehusishwa katika kesi kubwa kiasi kile, jasho lilianza kumtiririka kuanzia kichwani, likashuka mpaka mgongoni na kisha kupenya hadi katikati ya miamba miwili ya makalio yake.

Alikuwa amechanganyikiwa!

“Ndugu yetu kama hili jambo hujafanya kweli, hata usihangaike kudai kuitiwa wakili wako. Usitarajie kuwa ataitwa…. Sembuse kukusikiliza tu.

Kama katika kukupekua ungekutwa na vipoozeo vizuri kama wenzetu watatu walioachiwa huru basi ingekuwa nafuu. Hapa Mashariki ya mbali ni tofauti sana na nchini kwenu. Hapa kwetu kumiliki kadi ya chama tawala ni turufu isiyokuwa na kifani, huwezi kujua hilo mpaka uingie matatani, wao wa chama tawala wanajiamini kuwa ni malaika watakatifu wasiofanya makosa angali wale wanaokipinga chama tawala ni mashetani wenye vichwa tisa ambao unatakiwa kuishinao kwa makini mno. Wenzetu katika kupekuliwa wamekutwa na kadi za chama tawala, hawa hawakupata mateso makali kama tuliyopata sisi, na ghafla bin vuu wameachiwa huru. Sisi nduminakuwili tusioeleweka tupo hapa tunasota na wewe.

Na wewe zungu nchi hii itakusumbua sana, kama shughuli zako nd’o hizo za kufungua akili za watu kifikra basi umefanya kosa la jinai linalofanania na kuua watu thelathini kwa kuwachinja shingo zao kisha unatarajia kushinda kesi.

Mashariki ya mbali tuachie sisi wana-mashariki, hapa mashariki wachache sana wanaojua, wengi ni wajuaji, ukijifanya unautoa ule ujuaji wao wanakupachika kile cheo chao wasichokijua wanakuita wewe mjuaji. Kumweleza mtu kuvuta sigara katika hadhara si jambo la kistaarabu na ni hatari kwa afya, hapa kwetu mtu huyo atakuhukumu kana kwamba umeutukana uchi wa mama aliyemzaa.

Sijafika katika nchi yako lakini naamini fika kuwa mtuhumiwa anaweza kumshtaki askari iwapo alimpiga ama kumnyanyasa wakati wa kumuhoji. Ila huku kwetu ni tofauti, jitazame vyema hadi sasa haujavunjika zungu, kwa kitendo hicho cha wewe kuweza kusimama wima hii ni dharau tosha kwa waliokukamata na huko walipo wanachekwa kuwa wao ni dhaifu. Uimara wa askari wetu ni kuweza kuvunja taya ya mtuhumiwa, kumtoa meno, kumvunja miguu na kumpasua kichwa. Na kuna wale wanapewa hadi vyeo kwa kufanikiwa kumuua mtuhumiwa nasisitiza ni mtuhumiwa so mshtakiwa wala mfungwa. Kwa kifupi baadhi ya askari wetu akili kichwani hakuna hata kile kielimu kidogo cha kutofautisha mtuhumiwa na mshtakiwa hawajui. Lakini naomba nisiwashushie lawama sana, naamini ule upuuzi na ushenzi wanaofanyiwa wangali katika kambi za jeshi unachangia unyama huu.

Zungu ukijiunga na jeshi la nchi yetu ya Mashariki ya mbali umejiunga katika chuo kidogo cha jehanamu kinachotoa mafunzo katika ngazi ya astashahada.

Utafundishwa matusi na kulazimishwa kuyasema katika namna ya kughani, utayumbishwa imani za dini unayoamini, utatukaniwa wazazi wako wote na utapaswa kushukuru baada ya kutukanwa.

Usiombe ukakutana na askari aliyetoka huko. Atakuviringisha asua zilizobeba kende zako huku anakutazama usoni jinsi mwanaume mzima unavyotoa machozi na kutoa kijisauti kama mtoto wa kike. Hiyo nd’o furaha yake.

Zungu jiandae kisaikolojia, wewe ni zungu la unga na ni mtu hatari sana kwa taifa hili kwa sasa. Utaviringishwa korodani zako, zikipasuka hiyo ni juu yako, utavunjwa miguu, ukipelekwa hospitali hautakuwa na uchaguzi wataamuru ukatwe, ukijifanya jeuri sana hutaki kukiri kuwa wewe ni zungu la unga. Watakuzika ukiwa hai.

Pole zungu!” alimaliza bwana yule ambaye alionekana kuwa ni mzoefu sana wa maisha yale ya jela.

Zungu akaanza kulia kama mtoto mdogo aliyefokewa ghafla na mama yake baada ya kuomba nyonyo. Na kwa mara ya kwanza kwa dhati kabisa akaijutia ile siku aliyoamua kufunga safari kuitembelea Mashariki ya mbali.

Lakini majuto yale yangesaidia nini angali tayari yu nyuma ya milango ngangari ya chuma.

Milango ambayo wachawi wanakiri kuwa hata wao wakiingizwa mule uchawi wao unakimbia kwa jinsi panavyotisha.

Alipokumbuka kauli ya asua zake kufinyangwa, alijikuta akibana miguu yake kana kwamba anazuia zisifinyangwe.




ILIANZA kama siku moja ya kukamatwa bahati mbaya, labda kwa kufananishwa, kisha ikawa siku ya pili na kuendelea na sasa zilikuwa zimetimia siku thenashara tangu Danstan akamatwe ghafla, na hakuna hatua yoyote iliyokuwa imechukuliwa dhidi yake. Hakuwa ameandikishwa maelezo na wala kusikia dalili ya kupelekwa mahakamani.

Zaidi aliishia kuzikariri ratiba za ugali na maharage pamoja na uji uliojitwika mabuje.

Midevu ilikuwa imeweka kambi katika kidevu chake na masharubu yakimning’inia katika namna isiyopendeza.

Alikuwa amekonda hadi kichwa kiasi kwamba macho yake yakachukua utawala na kuonekana ukubwa waake kana kwamba ameyakodoa muda wote, mbavu zake zilikuwa zinafanya maonyesho ya wazi hata mtoto anayejifunza kuhesabu angeweza kuzihesabu vyema pasi na kuzigusa.

Kwa kutumia macho tu!

Waliingizwa watu mle ndani wakatoka wakaingizwa wengine yeye akiwa palepale. Yeye pamoja na wenzake kadhaa waliounganishwa katika shtaka moja.

Danstan hakuijua hatma yake, kila wanapoletewa chakula alikuwa akimuuliza yule askari mwenye dhamana ile kuwa ni lini atafikishwa mahakamani. Askari yule aliishi kama asiyekuwa na uwezo wa kuongea lakini anayesikia.

Alikuwa akimtazama tu kisha anaendelea na shughuli za kugawa chakula kile kibovu cha gerezani.

Siku ya kumi na mbili ustahimilivu ukamshinda Danstan, akajikuta akimtolea maneno makali yule askari anayesikia na asijibu chochote.

Kama kawaida mchezo ukawa uleule, akaishia kutazamwa na kisha akapuuziwa.

Lakini siku hii alitazamwa mara mbili.

Haijawahi kutokea.

“Umeyaona macho yake yaliyokutazama mara yaa pili” Uwesu alimuuliza Danstan baada ya bwana yule kuondoka.

“Vyovyote atakavyonitazama cha msingi nimemueleza ukweli na natakiwa kupewa haaki yangu.” Alifoka Danstan.

“Nakuuliza uliyaona macho yake lakini!” Uwesu akarudia kauli yake.

“Yamefanya nini?” aliuliza Danstan.

“Yamewaka kwa ghadhabu, ni kama yupo tayaari kukuua.” Alizungumza kwa sauti ya chini huku akipambana kuumuua kunguni aliyemnasa akimnyonya dmu.

“Nipo tayari kwa lolote.ni heri waniue tu kama wamenuia kufanya hivyo.” Alisisitiza Danstan

“Unavyozungumza kishujaa utasema uliwahi kufa ukafufuka na sasa umezoea kifo.” Uwesu mmoja kati y wanaoshutumiwa kuwa pamoja na zungu la unga akamdhihaki.


_______________

Majira ya saa kumi na moja jioni, jua likiwa linaanza safari yake kuiaga Mashariki ya mbali na kuibukia kwingine. Lango la gereza lilifunguliwa kisha zikasikika hatua za mabuti mazito ya kijeshi zikipishana.

Zilianza kusikika tokea mbali na kituo kikawa ni katika lile lango alilokuwa akiishi Danstan na wenzake.

Lango likafunguliwa, mwanajeshi mmoja aliyevalia magwanda yake rasmi akapiga hatua moja kubwa.

“Wewe! Kuja huku.” Alizungumza akimtazama Danstan. Kwa hofu Danstan akasimama wima, mwanajeshi akatoka na lango likafungwa.

Danstan nyuma mwanajeshi mbele.

Walipofika nje, akapokelewa na wanajeshi wengine wanne, hawa walikuwa wamebeba mitutu ya bunduki.

Akaamrishwa kuchuchumaa chini, na amri iliyofuata ni kuwafuata nyuma huku akiwa anaruka ruka kama chura mwenye furaha.

Haikuwa safari fupi. Na wao hawakuonekana kujali zaidi ya kumpiga mateke pindi alipokuwa akipumzika.

Danstan alilia kama mtoto mdogo huku akiwalaani kimoyomoyo.

Baada ya hali kuwa ngumu Danstan akafanya kosa kubwa ambalo hufanywa na wanadamu wengi.

Ulimi wake ukateleza akaropoka, ‘Fuck!!’.

Japo neno lile hakulitoa kwa kumtusi yeyote, lakini likasafiri kwa kasi hadi katika masikio ya wanajeshi wale vijana waliovimba kwa mazoezi.

Ni kama waliambizana kwa pamoja ‘tumnyooshe mbweha huyu’.

Hakuwepo wa kumzuia mwenzake katika ule ukumbi bali kupambana nani apige zaidi ya mwenzake, mwingine alikuwa na rungu kubwa akalituliza katika mguu wa Danstan, yowe kubwa likamtoka. Lakini lingeenda wapi yowe lile zaidi ya kuishia katika kuta nene za gereza, kuta zinazoficha kila aina ya uovu, uzandiki na chokochoko zote ambazo zinaileta ile maana ya jela ya Mashariki ya mbali ni sawasawa na kaburi lenye mateso makali lakini hakuna wa kuyasimulia maana ukizikwa humo hutoki.

Zile mbavu zilizokuwa zinachungulia kinachojiri ulimwenguni, zilikutana na buti zito la kijeshi, Danstan akajikunja kwa maumivu makali lakini sasa hakuweza hata kutoa sauti ‘nyee!’. Maumivu yalikuwa makali mno.

Baada ya kipigo cha paka shume aliyenaswa katika tego, Danstan alitelekezwa pale akiwa robo tatu mfu, na robo pekee akiwa na uhai.

Aliachwa katika ukumbi ule akiwa anavuja damu, na mguu wake ukiwa umekufa ganzi asijue kama umekatika, umevunjika ama vyovyote vile.

Baada ya dakika thelethini, akaburutwa na askari magereza hadi katika chumba alichokuwa amehifadhiwa awali.

Akiwa hana hali hata kidogo. Macho yake yaliishia kuona ukungu mbele yake huku masikio yakivumishwa na sauti za vipyenga vinavyorindima kana kwamba kuna lundo la watu wanashangilia jambo.

Hakuhisi uwepo wa mwili wake hata kiduchu, pua zake zilibaki kutambua harufu kali ya damu.

Damu iliyokuwa inamvuja katika paji la uso wake na popote walipoamua kumpasua.

Hatimaye macho yakajifumba na alipoyafumbua katika fikra zake akajikuta yungali nchini Semedari jijini Mainstream.

Alikuwa ameketi na Daniel katunzi wakibadilishana mawazo baada ya kuwa wamecheza mchezo wa ‘chess’ kwa muda mrefu hata wakachoka.

Danstan akamuuliza jambo.

“Mbona tulipokwenda kumsalimia Anko Paul gerezani haukuwa sawa kabisa, ni kama uliyekuwa katika mchanganyiko wa kushangaa na kukumbuka jambo. Vipi ilikuwa mara yako ya kwanza kufika gerezani, usitake kuniambia kule mashariki ya mbali ulipozaliwa watu hawaruhusiwi kutembelea wafungwa.

Daniel akaketi vyema, akajikohoza.


DANIEL ANASIMULIA.


Tunakwenda kuwasalimia ndugu zetu katika magereza.

Lakini utakapolifikia geti la kuingia gerezani ndipo utagundua kuwa mfungwa katika nchi yetu sio mwanadamu tena. Utawakuta akina mama pale nje wanauza matunda kama ndizi na machungwa. Pia wanauza karanga. Na hawa wote ukifuatilia ni wake na mahawara wa ma askari magereza. Watakuuzia kwa bei ghali na wanakusisitiza kuwa usije ukathubutu kuingia na chakula ulichotoka nacho nyumbani hata kama ni ndizi kama zao.

Unabaki unajiuliza wanaogopa nini. Wanazuia sumu gerezani ama ni kitu gani.

Vipi nikinunua hizohizo ndizi zao kisha nikazitia sumu? Itabadili maana?

Wehu!

Ikifikia sasa namna ya kusalimia ndugu ndipo utalazimika kucheka huku macho yakitoa machozi.

Mnaruhusiwa kuingia watu ishirini hadi thelathini kwa pamoja. Na wafungwa wanaingia zaidi ya ishirini. Mmetenganishwa na wavu, na vyuma vya kutosha na hapo mpo umbali unaoweza kufikia mita sita.

Unapaswa kupaza sauti haswa ili ndugu yako akusikie, naye atapaswa kupayuka ili upate jawabu.

Hakuna siri! Hakuna uhuru!

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG