Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

SHILINGI (MWANZO KATI NA MWISHO) - 5

   

Simulizi : Shilingi (Mwanzo Kati Na Mwisho)

Sehemu Ya Tano (5)


Maajabu haya ya mkuu wa wilaya, yaliwafanya wakazi wa vijiji jirani wafikie hatua ya kutamani lile tatizo lililojitokeza Ulongoni lingewasibu wao, ili waipate bahati ya kupata sukari na mchele wa hisani.

Mawazo yao hayakuambatanisha madhara ya vifo katika kijiji cha Ulongoni. Walijiwazia mema pekee.

Awali nimekukumbusha kuhusu umaarufu wa kisiasa, niwie radhi sikukugusia juu ya namna bora ya kula na kipofu.

Katu usimshike mkono!

Naam! Mkuu wa wilaya hakuwashika mkono vipofu hawa, na hata alivyoruhusu wataalamu kuyavuna mashamba yao yanayosadikika kuwa yamekumbwa na sumu. Waliendelea kumwona ni shujaa wao.

Mihogo, viazi, hiriki, mahindi, mtama na uwele!

Vyote vikajaa chekwachekwa katika yale magari ambayo awali yaliwaletea mchele. Mwenyekiti wa kijiji akamshukuru mkuu wa wilaya huku akimpigia magoti.

“Asante kwa kutuondolea hii sumu, tulipata wakati mgumu sana kuwalinda watoto wetu wasiingie katika mashamba!” Alizungumza. Mkuu wa wilaya akamshika mkono na kumnyanyua.

“Kesho nitawaleta wataalamu kwa ajili ya kutibu ardhi yetu ya Ulongoni. Wanatokea jiji linaitwa Dasalama… kuna mtu hapa amewahi kufika Dasalama? Huko Dasalama nd’o ipo redio Tanzania Dasalama… yupo?” Akatupa swali huku anaangaza huku na kule kutarajia jibu.

Hakuna!

“Watatokea Dasalama na wameniahidi kuwa hili tatizo limefika mwisho…. Huwa hawashindwi kitu hao wa Dasalama!” Akaweka pumziko kisha akaurusha mtego wake ambao hakuhitaji unase kwa siku moja wala mbili. Alihitaji unase siku isiyokuwa na jina.

“Nimeelezwa na mwenyekiti wenu kuwa kuna watu wamekikimbia hiki kijiji kwa sababu kuna agizo kutoka juu kwamba aliyeiona shilingi ya ajabu anapaswa kukamatwa na kutoa ushirikiano. Kuanzia sasa nasema sitaki kusikia mwanakijiji yeyote wa Ulongoni anasumbuliwa, mbona mimi niliiona na kuikamata katika mkono yangu hamjafika kunisumbua? Sasa nasema hivi, kama askari na mgambo wataendelea kuwasumbua huku mimi wakinikwepa. Nipo radhi kuuacha ukuu wa wilaya na kuja kujumuika nayi hapa kijijini tuteseke na kufa pamoja.” Akaweka pumziko la maksudi ili wananchi waweze kumpigia makofi.

Kimya!

Ulongoni hawazijui siasa, wanamtazama na kumshangaa. Anayoyaongea ni mambo mazito na ya kusikitisha.

Mjini watakupigia makofi hata ukisema kuwa una mpango wa kujinyonga upoteze maisha, watashangilia ukitoa ahadi kuwa utatembea uchi wa mnyama ikiwa ombi lako halitakubaliwa.

Ulongoni wasipokuelewa watakushangaa, wakikuelewa utaishi katika mioyo yao.

Walimuelewa mkuu wa wilaya!

“Kwa hiyo nd’o hivyo sasa nshasema mimi!” Akajikuta anamalizia kinyonge.

Akaondoka huku akiburudika kwa biashara aliyoweza kuifanya, biashara ya mchele na sukari dhidi ya mazao ya shamba yasiyokuwa na idadi.

Kisha akaihamishia turufu yake upande wa pili!

Mjini!.......

__________________

Maji yakichafuka usiseme kuwa hayafai,

Maji hayohayo machafu yanaweza kuzima moto unaounguza nyumba yako.

Jifunze kuwaheshimu unaodhani ni wajinga mbele yako,

Kuna siku ujinga wao utakuwa busara unayoihitaji!

__________________

ALIKUWA bado anachechemea wakati wanafunguliwa geti kutoka katika gereza la mahabusu wakionekana kukosa hatia. Hakuna aliyewaomba radhi kwa kuwaacha wakiteketea katika maisha yale kwa miezi mitatu. Kindo hakuwa na uelekeo maalumu….

Mzee Upara ambaye alikuwa muhusika wa mchechemeo ule alimtazama Kindo anayeweweseka. Akamwendea.

“Nilikwambia hata baada ya haya yote, tutakwenda nyumbani kwangu ukajipange…. Utakaa hapo mpaka utakapohitaji kuchukua uelekeo mwingine…” Upara alizungumza kwa upole.

“Kindo….” Upara akamuita, kisha akaendelea, “Mungu anapokupa nafasi ya kuadhibu ujue kuwa kuna kijisehemu cha huruma anakuachia kwa matumizi ya baadaye. Ni yeye alinituma nikuadhibu na nje ya ngome hii amenikumbusha kuwa aliacha masalia ya huruma….” Upara anazungumza huku akianza upiga hatua ambapo Kindo alimfuata kwa nyuma.

Kindo hakudhani kuwa Upara atawaza lolote kuhusu yeye pindi watakapotoka nje ya ile ngome. Ni muda mrefu tangu walipotenganishwa vyumba baada ya kugombana na kufikia kupigana.

“Unadhani nastahili kuwa rafiki yako?” Kindo akamuuliza.

“Hakuna ajuaye kipi kinachostahili kuwa chake ama kuwa upande wake. Yote haya ni maandishi tunaandika, siku ya kiama yupo wa kutuwekea alama. Tuendelee kuandika Kindo!” Akaweka pumziko. Wanatembea na kuliacha gereza lile.

Viguu na njia hadi wakafika nyumbani kwa Upara.

Majani yameota katika njia ya kuingilia usawa wa nyumba ile, wakapenya hadi wakaufikia mlango.

Upo wazi!

“Hawakujali lolote dhidi ya mali zangu chache, kwa sababu walichokihitaji hawakukipata….” Upara anazungumza huku anaufungua mlango. Anagundua baadhi ya vitu vimepoteza ama kuvurugwa sana.

Kindo hasemi kitu, anashangaa tu!

Wanaingia chumba kimoja baada ya kingine, hakuna ambapo hapajaguswa. Hatimaye wanakifikia chumba walicholala usiku ule wa hekaheka.

“Yule mwanamama aliweza vipi kuchomoka na ile Shilingi angali sisi tumelala? Sijawahi kuacha kujiuliza hili swali hata siku moja…..” Mzee Upara akaweka hoja mezani, amesimama katika chumba kile katikati.

Godoro limechanwachanwa kitanda kimevunjwa.

“Wakadhani imefichwa katika godoro…” Anajisemea peke yake. Kindo bado ni mkimya.

“Unadhani utajiri una thamani kuliko umasikini?” Kindo akamuuliza.

“Utajiri halali una thamani kuliko umasikini wa kujitakia…” Akajibu kwa utulivu.

“Shilingi ya ajabu ni utajiri halali?”

“Ni utajiri wa bahati, na bahati siku zote ni halali maana anayetoa hiyo bahati ni Alah!” Ananyoosha kidole juu wakati analitamka jina lile.

“Umenifundisha jambo mzee Upara… na nimegundua tunafanana” Anatulia na kujiegemeza ukutani kisha anaendelea, “Nilikuja mjini kuiuza shilingi kisha nitende jambo kubwa kwa ajili ya jamii yangu, nilitamani mwanangu ajue kusoma na kuandika, nimejionea wanaojua kusoma na kuandika walivyokuwa wanajadiliana kesi zao kisomi, najua hata wewe ulitamani kuzijadili ila ulijali kuhusu mimi, ukaamua kuwa kimya! Hakika unafanya mambo kwa ajili ya watu kama ulivyonieleza….” Anatua.

“Asante kwa kulitambua hilo bwana Kindo. Hatujakutana bahati mbaya…. Na ninakuahidi kuwa nitalipiza kisasi kwa yule mwanamke aliyetimka na shilingi yako. Kisasi ni haki kama zilivyo haki nyingine…” anazungumza kwa hisia kali sana.

“Si yeye aliyeichukua shilingi!” Kindo anazungumza kwa sauti hafifu lakini anayejiamini.

“Imepotea kimazingara? Haiwezekani, nyumba tuliikagua, na wakatudhalilisha tupu zetu walipotuamuru tuzivue nguo… haikuonekana ile shilingi.” Anabisha.

“Sawa haikuonekana lakini haimaanishi aliibeba yeye…”

“Unanituhumu mimi kuwa nimechukua Shilingi?” Upara anahamanika, mashavu yanamcheza.

“Shilingi ile ni familia yangu, mama, mke na mtoto wangu, shilingi ni kijiji changu….shilingi imeondoka na maisha ya mtumishi wa kijiji chetu. Kisa tu aliwahi kuishika!” Anatulia kisha anajisogeza pembezoni mwa kile chumba. Upara anamfuatisha kwa macho.

“Kuna nyakati Shilingi ilikuwa katika mchago kitandani, na hakuna hata mtu mmoja aliyegundua hilo. Ni hapo nilipotambua kuwa shilingi haina uwezo mkubwa kama inavyotajwa, shilingi inaweza kuleta utajiri lakini haiwezi kuwa bora kuliko akili ya mwanadamu asiyejua kusoma na kuandika kama mimi…”

“Kindo una maana gani wewe… shilingi alichukua nani. Acha mafumbo kaka, acha tafadhali..” Upara ana kimuhemuhe.

Katika kona ya kile chumba, Kindo anachukua maboga yaliyosinyaa kiasi cha kugandiana na sakafu, wadudu wamelifanya kitoweo hadi likapoteza ladha wakalitelekeza.

“Sehemu pekee usiku ule, ilikuwa kuchukua shilingi na kuikita katika mojawapo ya boga katika sinia la yule mama. Nilitambua kuwa baada ya kuiona shilingi ile, si wewe uliyejali kuhusu maziwa yako ya mtindi wala mama yule kujali kuhusu sinia lake la maboga. Aliishia kuyatua humu ndani na hakuna aliyewaza hata kuchukua kipande kimoja kwa ajili ya shibe….. sote tuliwaza kuhusu shilingi….” Kindo anamalizia kwa kupekua masalia yale ya maboga.

Anaunyanyua mkono na kuinyoosha shilingi yake juu!

“Ni hii shilingi iliyoishi humu ndani kwa utulivu kipindi chote cha wenye tamaa walipoitumbulia macho. Uzuri wa Shilingi, inaweza kukaa kimya kwa muda mrefu.”

Macho kodo!

Upara unatoa jasho!

Haamini kuwa iliyopo mbele yake ni shilingi. Kindo anamkabidhi walau aishike, na hapo anajionea kile alichokiona kwa mtumishi wa Mungu kijijini kwao,. Kile kile alichokiona kwa mkuu wa wilaya na daktari.

Mzee Upara alikuwa anatetemeka!.

Baada ya kimya cha dakika kadhaa, Kindo akatoa tamko lake la mwisho juu ya shilingi ile.

Tamko la kushtukiza.

Tamko ambalo liliitoa Shilingi ileile iliyokuwa na mwanzo wa kustaajabiwa na kila mtu, kisha ikazaa Shilingi kati ya kutia majeraha kila kona, hatimaye tamko la Kindo likaitupa Shilingi katika awamu yake ya mwisho!

________________


Woyooooo! Shilingi imerejea pahali pake. Kindo sio kilaza kiasi hicho jama…..

Haya katoa tamko gani huyu bwana?





Kwa mara nyingine Kindo akajikuta katika mikono ya Maalim Upara. Huyu wa sasa ana ghadhabu kuliko yule waliyekorofishana gerezani.

“Gerezani ulipaswa kuniomba msamaha mimi pekee maana Allah alikuwa anakuadhibu kupitia mimi, safari hii hakuna uchaguzi, nakwambia utaomba msamaha hadi matumbo ya akina mama watakaozaa miezi saba ijayo! Wote hawa wametumwa na Allah!” haongei haya patupu pasi na ngumi, takribani kila sentensi iliambatana na pigo la haja. Ngumi za sasa zikiwa nzito kuliko za kule gerezani. Maalim wa sasa ana afya na nguvu tele.

“Huko mjini watu huogopwa kwa fedha walizonazo, hapa Ulongoni tutakuogopa na kukuheshimu kwa hekima zako. Hekima haiji burebure ni kudra za mwenyezi Mungu…. Fedha umeipata kwa bahati nyang’au wewe, unataka uendeshe kijiji chako kwa manyanyaso. Mshenzi wa tabia wewe, watu hunyanyasa visivyo vyao, wewe unalingishia minofu ya kuku wanaUlongoni. Unatuletea Ukoloni wewe mshenzi. Allah kupitia baba wa Taifa na raisi wa nchi hii Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, amesema tuukatae ukoloni mambo leo…. Kweli Wewe Khanithi ni wa kutuletea ukoloni tena Ulongoni. Unajua tumeteseka kiasi gani kwa sababu ya kukusubiri…. Yaani tunasubiri utujengee shule na barabara, unakuja kuturingishia miwani za jua na minofu ya kuku kweli….. nakuhakikishia leo nd’o utajua ipi ina nguvu zaidi ni elimu Akhera ama elimu dunia…..”


Hizo nd’o sentensi pekee ambazo Kindo aliweza kuzisikia kabla hajapoteza fahamu, baada ya kuzidiwa na makonde.

Suruali yake pana ikiwa imepasuka katikati na kumwacha akiwa na bukta mbili alizokuwa amevaa chini ya suruali ile, miwani ilivunjika na watoto wamechukua tayari wakachezee, kofia haipo, nywele zimekuwa vumbi.

Gari zimepasuka vioo na matairi, na kuna wanaUlongoni wanapambana kung’oa viti. Hasira zao zipo juu, wameondoa uhai wa mmoja kati ya walizni wa Kindo aliyejifanya anaweza sana kupambana, watatu wamezimia kama ilivyo kwa bosi wao Kindo.

Ubora wa Ulongoni na vijiji vingine katika wilaya ya Hekaya ni kwamba kijiji kimoja kwenda kijiji kingine ni umbali wa maili za kutosha. Hivyo ya Ulongoni hubaki Ulongoni na kwingineko hayawahusu.

Nani wa kumtetea Kindo na nduguze?

Ni wanaUlongoni pekee waliokuwa na mamlaka ya kuamua aidha Kindo apumue tena ama la! Wakakubaliana kuwa huenda Kindo ameingiliwa na pepo hivyo atakapozinduka watamsikiliza utetezi wake kwanza. Akiwa tayari kukiri kuwa ameingiliwa na pepo, bas watayaruhusu yale mapepo yaondoke kisha atatakiwa kufanyiwa tambiko.

Masaa mawili yalitosha Kindo kurejewa na fahamu zake. nywele zake ziko ti-timka na zimejaa vumbi. Hakuna mwanaulongoni aliyekuwa tayari kuendelea na shughuli zake angali Kindo amepoteza fahamu, walikuwa radhi kungoja hadi atakapotangazwa kuwa amenyanyuka tena.

Macho makali ya wanaulongoni yanamtazama.

“Unaitwa nani?” Lilikuwa swali kutoka kwa bwana Ubwa. Ni huyu alikuwa katika jukumu la kuhakikisha iwapo Kindo ana mapepo ama la.

“Naitwa KIndo…naitwa Kindole Mgagauka Kisendeu!” Kindo alijibu upesi huku akiwa amejikunyata mithiri ya kifaranga cha kuku kinachomnkosa mama yake aliyechinjwa kisha manofu akapewa KIndo akawaringishie wana Ulongoni.

“Mweleze mzee Ukindi kama mapepo yako umemwambukiza na mwanaye huko alipo?” Swali la pili likarushwa.

“Hapana… hapana baba!” Kindo anajibu kwa staha, amenyanyuka na kuketi kitako.

“Sisi kama kijiji tumeamua kukupa ridhaa ya kuchagua wewe unataka kuwa nani… naomba mwenyekiti umweleze.” Bwana Ubwa anamkaribisha mwenyekiti.

Jumla ya wakazi wasiopungua tisini wa kile kijiji wapo makini kumsikiliza mwenyekiti.

“Raisi Nyerere alitueleza kwamba, yeyote ambaye atajifanya mkoloni mweusi, akajitengenezee nchi yake isiyokuwa Tanzania akaishi huko.” Akaanza kwa msisitizo, “Tena akasema tusikubali tena kuwa chini ya mkoloni kwa sababu ameshatupatia uhuru mwaka 1961. Akasema yeye ametupatia uhuru na sisi tuutunze uhuru wetu… wewe Kindo raisi wako ni nani?”

“Muheshimiwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere….” Kindo anajibu upesi.

“Hebu simama kwanza… unataja jina la Raisi huku umekaa ebo!” Mwenyekiti anawaka. Kabla hajamaliza Kindo alikuwa wima, suruali yake imepasuka na shati limenyongorotwa halitamaniki.

“Kama unadharau alichosema raisi, ni kweli unaweza kutuheshimu?” Anatupiwa swali.

“Nisamehe mwenyekiti, sitarudia.” Anajibu kwa nidhamu.

“Ulongoni ya sasa sio ile uliyoiacha, huko mjini wametuzuia kupeleka bidhaa zetu, lakini haohao wameona sisi hatufi wameanza kutuua. Sisi ni washindi, Ulongoni hoyee!”

“Hoyeee!” Wote wanajibu kasoro KIndo.

“Unaona sasa ulivyo na dharau! Watu wanasema Hoyee wewe unanitazama. Hii nd’o dharau uliyofunzwa huko mjini?” Mwenyekiti anawaka, wanakijiji wanahanikiza.

“Hoyeeee!” Kindo anawahi kusema kabla halijajadiliwa lolote la ziada kuhusu tabia zake.

“Sisi tumeamua kukufukuza rasmi kutoka katika kijiji chetu. Hatukutaki mtu ambaye unaamua kutudharau kwa sababu ya fedha ulizoziokota hapahapa katika kijiji chetu…. Bora ungekuwa uliiokota shilingi huko mbali. Wewe unataka kutudhalilisha na umetudhalilisha mno, watoto wetu wanatuomba kuku majumbani, wanatuuliza hayo ma kofia yako yanaitwaje, wanataka kutoana macho kwa sababu ya mawani yako….. tumeamua kukufukuza Ulongoni, na nikiwa mwenyekiti wa kijiji hiki nasema hatukufukuzi hivihivi…..” Anaangalia kushoto na kulia ule ukimya unamkumbusha kuhanikiza ‘Ulongoni Hoyeee’ wanajibu kwa sauti kuu ‘Hoyeee’ Safari hii KIndo pia anajibu pamoja nao. Anatabasamu kisha anaendelea. “Tumekubaliana kuwa kila mwanaUlongoni aliye katika mkutano huu, atakucharaza bakora mbili za makalioni, ukiwa huko mjini ushindwe kukaa vyema ukumbuke kuwa Ulongoni hakuna ujinga ujinga.” Mwenyekiti anazidi kuvumisha sauti yake juu.

“Naomba mnisamehe ndugu zangu, naomba sana ni ulimbukeni wa mjini. Sikuwa na nia ya kuwadharau. Nakipenda kijiji changu na nd’o maana nikarejea….”

“Malimi Upaa amesema tusikuruhusu kujitetea, amesema watu wa mjini mna maneno mengi sana…. Tutakuruhusu baadaye kujitetea. Haya vijana wanne…. Mbanike huyu kiumbe….” Mwenyekiti akamalizia.

Ubwa akawa wa kwanza akifuatiwa na vijana wengine watatu.

Wawili wakakamata mikono ya Kindo, na wengine wawili wakakamata miguu kisha wakamnyanyua juu.

Alikuwa amebakinwa! Anajaribu kufurukuta lakini haikufaa kitu.

“Tunaanzia vitoto vya tumboni, wanafuata watoto, wanawake halafu wanaume tutamalizia mwishoni jama!” Mwenyekiti anatoa maelekezo ya msingi kana kwamba anatoa ratiba ya kuchukua chakula msibani. Kisha lundo la fimbo zilizokwishaandaliwa linaletwa.

Vitoto vilivyopo tumboni! Hapa ni akinamama wote wajawazito, walimcharaza Kindo kwa niaba ya vitoto hivyo ambavyo havijazaliwa.

Kisha wakafuata watoto ambao wanaweza kushika bakora!

Utaratibu ukaenda vyema, Kindo analia hadi sauti inakauka, anapambana fahamu zipotee lakini hafanikiwi.

“Mchape kwenye makalio jamani, msichape mgongoni, chapa kalio chapa kalio jama…..eeh! chapa haswa! Chapa kalio!” Mwenyekiti kazi yake kubwa ni kunadi lile zoezi. Ananadi hadi jasho linamtiririka, analifuta kwa kiganja cha mkono wake.

“Jama mbona sisikii, mbona sisikii zikipenya, kumbuka hautapewa nafasi ya pili, chapa kadri ya uwezo wako. Chapa kalio chapa kalio!” Mwenyekiti anaendelea kutimiza wajibu wake na mara kwa mara akirejersha ari kwa kuwaambia ‘Ulongoni hoyee’.

Hadi zoezi linamalizika, si Kindo pekee aliyekuwa amekaukiwa sauti, hata mwenyekiti hakuwa akisikika tena.

Kindo ametepeta, makalio yanawaka moto wa gesi, si maji baridi yanayoweza kuupoza ule moto. Hawezi kuketi wala kulala vyema.

“Mpatieni maji ya kunywa sasa…”

“Nani ampatie? Aende kuteka kisimani…” Bwana Ubwa anapinga agizo la mwenyekiti.

Kindo analazimishwa kusimama, akiendee kisima ajitekee maji anywe.

Chubwi! Ndo mlio uliosikika baada ya Kindo kukifikia kisima.

“Ametumbukia kisimaniiii!” Sauti ya mwanamke inawakurupua wanaume waliokuwa wameketi katika miti iliyofanya vivuli. Hakuna kujifikiria, hakuna maandalizi.

Chumbwi! Chubwi!

Wanaume wawili wanaye Kindole tayari.

“Niache nife… niacheee!” Kindo anawasihi, lakini hawajali kuhusu nini anasema, wanamtoa nje ya kile kisima wanambwaga katika mchanga.

“Kama hamniachi nife… naomba msinifukuze Ulongoni. Nimekosea sana hakika, nimejiona madhambi yangu…. Sitaishi popote zaidi ya Ulongoni, mkinifukuza leo, kesho myafuate maiti yangu na kunizika Ulongoni.” Anaendelea kuzungumza akiwa amelazwa chini. Chepechepe kalowana.

Maalim Upara ambaye muda mrefu katika zoezi lile alikuwa kimya, akamsogelea Kindo na kuanza kuzungumza naye. Kindo akaomba radhi na kuelezea kuwa ataitimiza kila ahadi aliyoiahidi kuhusu Ulongoni.

“Kindole amesema yupo tayari kuziishi ahadi zooote alizoahidi kuhusu Ulongoni.”

“Hatumtakiiiiii!” Sauti za kiume zikaunguruma.

Maalim akatabasamu huku akiwatazama. Na hapo akaendelea kuwasimulia.

“Kindo aliniahidi kuwa kama ninataka ile shilingi iuzwe basi ninatakiwa kufika kijiji hiki na kumchukua mama yake pamoja na mkewe na mtoto. Nilikuja usiku na niliondoka usiku, pamoja na Nyangeta, Moracha pamoja na mama yake Kindo, Bi. Suku!” Anapumzika kisha anaendelea.

“Tukapambana katika soko la Shilingi, Kindo akaniachia jukumu lote la kuiuza, na nilifanikisha kuuza kwa pesa nyingi mno, pesa ambazo zinaweza kuigeuza Ulongoni kuwa sehemu ambayo kila mtanzania anatamani kuitembelea. Nikamshauri Kindo aende kusoma kwanza, walau aweze kuiokoa Ulongoni. Kumfukuza Kindo Ulongoni hii inamaanisha tuwe tayari kutawaliwa na mtu mwingine asiyeyajua machungu ya Ulongoni……”

“Tumuulize Kindo, na atujibu hadharani! Je! Kindo ipo fedha uliyobakisha kwa ajili ya Ulongoni?” swali hili likawavuta watu kujisogeza wamsikilize Kindo. Naye akasimama.

“Zile gari tatu nilizokujanazo, mbili zilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kupeleka wagonjwa hospitali, akina mama wanahangaika sana wanapotaka kujifungua. Hivyo wakati tunaendelea na ujenzi wa hospitali, nilipendelea tuzitumie hizo gari kutusaidia…..” Akasimama vizuri akaendelea kuzungumza.

“Nilipokuwa naenda mjini nilidhani oparesheni ni kitu ambacho kinauzwa. Lakini baada ya kuwa katika mji ule mkubwa niliokuwa ninasoma, nilijifunza mambo mengi sana, na yote nilitamani kufanya kwa ajili ya Ulongoni. Nakiri kuwa baada ya kufika hapa kijijini kuna masalia ya Ulimbukeni yalikuwa yananiandama, nikafanya ujinga nisioutarajia….” Watu wanazidi kuvutika.

“Leo mama pamoja na Nyangeta na Moracha watakuja kijijini, wataongozana na wataalamu wa afya . Hawa watakuja kutuelezea kuhusu afya na pia kila mwanaUlongoni atagawiwa chandarua mbili bure! Wataalamu hawa wa afya watatueleza kuhusu uzazi wa mpango. Mimi sio mtaalamu, wao watasema nasi zaidi….. ila kwa ufupi, naomba mnisamehe sana na ninawahakikishia kuwa sitarudia nilichokifanya jana…..” Kindo anaanguka chini kwa kutumia magoti yake.

“Naipenda sana Ulongoni, ardhi hii imenipa chakula hata nikakua, ardhi hii imebeba watu walionipenda kwa dhati, hakuna ardhi yenye amani kama Ulongoni. Nawaomba wanaUlongoni kama yawezekana niadhibuni tena kwa bakora nyingi muwezavyo, ili aidha mnisamehe ama laa! Nifie katika ardhi ya Ulongoni.” Sauti ya Kindo inasihi.

Maalim Upara anamwendea Kindo na kumnyanyua kutoka pale chini, akiwa amemshikia KIndo bega lake anaipaza ile sauiti ya mamlaka.

“Yeyote asiyependa Ulongoni iwe na hospitali, kama yupo asiyepenmda watoto wetu wapate elimu wajue kusoma na kuandika, Kama yupo ambaye anayapenda sana maisha haya ya dhiki, maisha ya kudanganywa na mkuu wa wilaya kisha kuibiwa mazao yetu. Basi na achukue bakora na kumcharaza Kindole mpaka apoteze maisha. Maana kufa kwa Kindo nd’o mwisho wa hayo yote.” Sauti inasikika vyema. Na hakuna aliyepiga hatua kuchukua bakora kumkabili KIndo.

Yaliisha katika nama ile! Kindo akaipata nafasi ya kuishi tena Ulongoni katika kijiji chake.

__________________

Ilikuwa kweli kama alivyotamka, jioni ya siku ile. Mama yake pamoja na mke na mtoto waliingia pale kijijini.

Ilikuwa kwa Kindo tu! Hawa walikuwa nadhifu lakini hawakuwa wamekengeuka! Hawakubeba wala kujivesha vitu ambavyo vingeyavuta macho ya walaUlongoni na kuwatesa kisaikolojia.

Waliongozana na wataalamu wa afya, pamoja na vyandarua katika gari walilokuwa wamekujanalo.

Miezi mitano ya uangalizi ilitosha kabisa kumshawishi Maalim Upara kumwacha Kindo pekee Ulongoni. Yeye akajiondokea huku akiiacha Ulongoni ikiwa kijiji kinachotamanisha kuishi.

Wa mjini walitakiwa kufika Ulongoni wao kwa ajili ya kununua mazao, wataanzia kwa mwenyekiti wa kijiji ambaye sasa alikuwa na ofisi pamoja na miwani ya kusomea. Elimu ya utu uzimani ikimwokoa kutoka katika shimo la kutojua kusoma na kuandika walau kidogo.

Zahanati ilikuwa imekamilika ujenzi wake kwa nguvu kazi ya wanakijiji na mafundi kutoka mjini.

Mwenyekiti akisaidiana na washauri wake wa Ulongoni, akaandika barua rasmi kwa serikali kwa ajili ya kuomba msaada wa wataalamu wa afya.

Serikali ya awamu ya kwanza, ya mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikashangazwa na barua ile.

Inawezekana vipi kijiji kujenga zahanati?

Waziri mkuu akaambatana na waziri wa afya kukitembelea kijiji cha Ulongoni.

Barabara zilikuwa zimelimwa vyema, miti ilikuwa imepandwa kwa mfululizo mzuri pembezoni mwa barabara.

Ugeni huu ukapokelewa na mwenyekiti wa kijiji kile na mkewe, walikuwa wamependeza, mwenyekiti akivaa suti kwa mara ya kwanza katika maisha yake, suti ya gharama kwa hisani ya Kindo, na mkewe akiwa amevalia vazi la kitenge lililoshonwa mjini. Nywele zake ndefu zikiwa zimebanwa kwa nyuma.

“Nimeshangazwa sana! Na nitamfikishia salamu raisi Nyerere…. Kuwa kama hajaona maajabu ya kutosha basi asisite kufika Ulongoni.” Waziri mkuu alizungumza na baada ya hayo akaruhusu maoni kadhaa kutoka kwa wanaUlongoni.

“Tukiachana na suala la kumpongeza mwanaUlongoni mwenzetu Kindole kuna ndugu yetu, Malimi Upaa tunamwomba naye aseme jambo…” Mwenyekiti msaidizi wa kijiji cha Ulongoni, Bwana Ubwa alizungumza.

Maalim Upara akasogea mbele akiwa anachechemeza mguu wake katika mwendo uleule wa ‘Mungu hakupi kilema akakunyima mwendo.”

“Muheshimiwa waziri mkuu, mwenyeji wako katika huu msafara… muheshimiwa Matayo Masindeke alitaka kukiteketeza kijiji cha Ulongoni, nasikitika wanaUlongoni hawajamshtaki! Ni kweli tulimshtakia kwa Allah kwa yote aliyotutendea, lakini tunaomba na wewe ulitambue hili….” Anapiga hatua kadhaa kisha anaendelea.

“Mkuu wa wilaya kwa kutambua kuwa kijiji chetu hakuna elimu hata kidogo, alileta pandikizi la hofu katika maisha yetu, akaaminisha wanaUlongoni kuwa ardhi yao ina sumu kali. Wasivune wala kunywa katika ardhi hii. Ninapenda kumweleza kuwa kwa alichotamka, kilisababisha vifo vya wanaUlongoni ishirini na mbili, wanaUlongoni ambao wangeweza kuwa hapa leo kuanduka historia kwa kijiji chao kutembelewa na waziri mkuu. Kama hiyo haitoshi nilipojaribu kusema kwa niaba ya wanaUlongoni, alinifunga gerezani kwa miezi sita na kunivunja mguu muheshimiwa….Tazama siwezi tena kutembea vyema, siwezi hata kukimbia….” Hawezi kuzungumza chozi linamtoka.

WanaUlongoni wanaanza kuhamasishana wamuue mkuu wa wilaya hapohapo mbele ya waziri mkuu. Mwenyekiti anawatuliza jazba zao lakini akiwaeleza kuwa ikiwa mkuu wa wilaya atafanya dharau ya aina yoyote ile basi lile zoezi lifanyike papo hapo. Auwawe!

Kisha waziri mkuu anachukua hatamu ya kuzungumza.

“Najua kuwa huyu bwana haongopi…… na ninawataka askari mmdhibiti mkuu wa wilaya, na ninatamka kuwa kwa niaba ya raisi wetu asiyependa kuona wanyonge wananyanyaswa… huyu sio mkuu wenu wa wilaya tena! Na kama ikigundulika alitumia madaraka yake kuwatenda vibaya, sheria itafuatwa! Na hongera sana bwana Upaa kwa kuwa jasiri kuwasemea wenzako.”

Askari wanamrukia aliyekuwa mkuu wa wilaya na kumvesha pingu.

“Ulongoni hoyeeee!” waziri mkuu anawaamsha.

“Hoyeeeeeee!” Wanajibu kwa sauti kuu zaidi.

“Nimenong’onezwa hapa kuwa kuna magari matatu yanaoza hakuna fundi wa kuyatengeneza, niwahakikishie kuwa baada ya siku kumi, hizo gari zitakuwa zinaunguruma. Ulongoni hoyeee!”

Ombi la kusaidiwa wataalamu zaidi wa afya linakubaliwa na utekelezaji ulifanyika katika ziara hiyohiyo. Wakaachwa pale matabibu sita pamoja na wauguzi wanne.

Watalala wapi?

Hilo sio swali, kwani wanaUlongoni wanalala wapi bwana?

_________________


Baada ya yote haya Kindo alikuwa tayari kulipa mahari yake ambayo hata hivyo hakuwa akiendelea kudaiwa tena na mzee Ukindi na mkewe.

Aliyeongoza jopo la shughuli hii alikuwa ni Maalim Upara. Shughuli hii haikuwa ya kutoa mahari pekee, bali pia kusheherekea kifungo cha miaka thelathini jela alichohukumiwa aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya, Matayo Masindeke.

Shughuli ikaandaliwa ikaandalika katika ukweli wa kuandalika!

Ije sasa hiyo siku ya shughuli!


Hakuna kadi ya mwaliko Ulongoni, uwe mwanaulongoni tu inatosha na uzuri wanafahamiana, hakuna anayekutazama ukiwa unarudia chakula kwa awamu ya tatu. Wewe kula tu, ukivimbiwa lala hapohapo ulipochokea, hali ikiwa mbaya zahanati ipo utapelekwa kwa kutumia gari, mzee Muhando anajua kuendesha na hajalewa. Huduma ni bure masaa ishirini na nne! Kindo alishalipia kabla haujazidiwa.

Kindo huyuhuyu aliyehakikisha kuwa watu wa mjini wanakimbiza kuku zao, ng’ombe na mbuzi kwenda katika kijiji cha Ulongoni kwa ajili ya shughuli ile ya kutoa mahari ya kumchukua Nyangeta moja kwa moja.


Hakuna kutazama muda na kuwa na mashaka kuwa serikali imesema mwisho wa sherehe ni saa fulani. Ulongoni kuna serikali nyingine zaidi ya hii ya mwenyekiti ambaye amelewa chakari analisakata rumba? Ama unamuhofia mwenyekiti msaidizi ambaye haamini kama atakula tena maishani mwake akilitazama tumbo lake lilivyovimbiana kwa uroho wa ubwabwa. Jina’le ni Ubwa acha ale Ubwabwa…


Una mashaka kuhusu nini wewe eti!? Ni hawa mgambo wanne wa kijiji? Eeh! Ni wanne tu, na muda wote wamemzunguka Kindo na mkewe kuhakikisha hakuna lolote linamtokea. Waache kumlinda Kindo wakwambie wewe ukale? Hawana akili au!?


Au labda wasiwasi wako ni watoto na usiku huo mnene. Bwana wee! Ngoma ya watoto haikeshi, Moracha na watoto wenzake walilala tangu saa mbili, wanaota ndoto zao kwa utulivu wakiwa chini ya vyandarua thabiti. Wanasubiri muda ufike tu, wakojoe kitandani zile soda walizokunywa kwa fujo. Asubuhi tutaanika magodoro, tushazoea siye! Kwani wewe inakuuma nini wakikojoa kitandani?



MWISHO!!



0 comments:

Post a Comment

BLOG