Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

WAKALA WA SIRI - 4

  

Simulizi : Wakala Wa Siri 

Sehemu Ya Nne (4)



Hakuwa na ujuzi wa kumkamua ng’ombe maziwa, awali alidhani ni jambo rahisi ambalo angelifanya kwa wepesi lakini alijikuta akishindwa. Hatimaye Mzee Mkwizu alimaliza kukamua ng’ombe maziwa, Sajenti alienda kuwasha moto jikoni. Lilikuwa jiko la kizamani lililojengwa kama tanuru. Alichukua makorokocho kisha akawasha moto. Makorokocho ni kuni zinazotokana na katani iliyokwisha kukauka. Katika kijiji cha Nkwini Makorokocho hutumiwa kupikia.

“ Warioba, miaka kumi sasa hatujaonana, tangu ulipokuja kwenye mazishi ya Bibi yako ukapotea moja kwa moja. Umekuwa mtu mzima kweli” Mzee Mkwizu alisema kikombe cha maziwa kikiwa mkononi.

“ Hivi kumbe miaka kumi imeisha, ama kweli siku zinaenda” Sajenti aliongea, wote walikuwa wanakunywa kifungua kinywa pale sebuleni.

“Haya nambie, mbona umekuja kama mauti, umenivamia usiku kama mwizi. Tena mguu wako unajeraha. Je, umekuwa mtu wa kuja kwa mikosi, mara ya mwisho umekuja kumzika Bibi yako, mara hii umekuja kunizika Mjukuu wangu?” Mzee Mkwizu alisema kikombe akiwa kakiweka kwenye meza ya mbao.

“ Hapana Babu, usiseme maneno hayo, ingekuwa ni heri kuvumilia maumivu ya jeraha langu la risasi mguuni kuliko maumivu ya maneno yako. Sijaja kukuzika Babu, ila kuhusu mkosi sikatai, ni kweli mara hii nimekuja nikifukuzwa na jinamizi baya, siwezi kukimbia tena, wanaonikimbiza wanamiguu elfu wakati mimi ninamiguu miwili,tena mguu mmoja wameujeruhi, wanambio kuliko farasi, nimekuja huku…” Sajenti alimeza mate kisha akaendelea;

“ Njama, na hila wamenibebesha. Wamenipa jina baya lenye kunitusi mimi mtu wa watu, nimekuwa kama paka shume niliyeiba chakula cha wasela, nafukuzwa mimi. Nimekuwa adui wa nchi” Hapo Sajenti akaanza kulia sauti ikiwa inatetemeka.

“ Tafadhali usilie, nyamaza mjukuu wangu. Hila zao hazitafanikiwa. Nani amefanya haya?” Babu alimbembeleza Sajenti, aliuona uchungu aliokuwa nao Sajenti.

“ Babu nakimbizwa na watu nisiowaona kama upepo, nisiowajua kwa sura kama shetani, ingawaje sitajiongopea kuwa ni watu wabaya, wenye ukaribu na mimi. Huenda kuna mpango mbaya wa kulibomoa taifa hili, utafikiria namna chipu ya darubini ya taifa, iliyobeba siri na mikakati ya taifa jinsi ilivyoibiwa, utafikiria namna Cadava ya uchunguzi ilivyoibiwa na sampo zake, pia Mateka wa ushahidi alivyotoroshwa, yote hayo kwako utayaona kama mageni, tena mambo magumu usiyoyajua. Hayo yote ni mazito, yote nimebebeshwa mimi, ati ndio mwizi, adui na msaliti wa nchi” Sajenti alimeza fumba la mate, kisha akapumua pumzi nzito kama pumzi ya mwisho. Uso na macho yake yalieleza zaidi kuliko maneno aliyoyaeleza kwa Mzee Mkwizu.

Mzee Mkwizu alisikitika sana kusikia taarifa hizo japokuwa hakuwa anazielewa lakini alimuelewa Sajenti kwa jambo moja tuu, nalo ni kubebeshwa zengwe la usaliti, Mzee Mkwizu alijua adhabu ya msaliti ilikuwa ni kifo cha ukatili. Ingawaje hakuwahi kuwa katika nyadhifa za serikalini lakini aliwahi kusikia hadithi za watu waliosaliti nchi jinsi walivyofanywa. Kwenye ujana wake, aliwahi kusikia kuwa watu wasaliti hasa wa nchi waliuawa kwa kunyongwa ama kuuawa kwa maumivu makali mno.

Hapo akajua jambo lililokuwa linamkabili Sajenti Warioba lilikuwa ni kubwa mno.

“ Mjukuu wangu, pumzika. Kila kitu kitakuwa sawa. Ngoja niende machungani kuwalisha hawa viumbe, Usiogope, wewe ni hodari, mtu mwema usiye na hila” Mzee Mkwizu alisema kisha akamuaga Sajenti akaenda Kuchunga.

Siku zikapita nazo hazikurudi, wiki ikaisha Sajenti akiwa kwa Babu yake, sasa tayari mguu wake ulikuwa umepata nafuu hata ile hali ya kuchechemea ikawa imeisha. Mzee Mkwizu alikuwa mahiri wa madawa ya jadi, aliijua mitishamba kwa majina na matumizi. Alimtibu Sajenti Warioba Kijadi mpaka pale alipopata ahueni na mguu wake kupona. Ilichukua wiki mbili kwa Sajenti Warioba kupona kabisa.


Pesa kidogo aliyokuwa nayo Sajenti ilisaidia kwa matumizi pale nyumbani. Hata hivyo pesa isiyozalishwa huisha haraka kama barafu kwenye jua. Ndivyo ilivyokuwa, Pesa ya Sajenti iliisha. Sajenti hakutaka awe mzigo kwa Babu yake. Wiki mbili zote alikuwa ndani kama mwali, hakutoka kwenda mbali zaidi ya kuzunguka mulemule ndani kwenye eneo la Nyumba ya Babu yake.

Sajenti aliona amsaidie Babu yake kwenda kuchunga ng’ombe, mbuzi, na kondoo. Alienda kwenye mapori kwa mapori akiwaongoza mifugo kwenye malisho akiwa na Mbwa wa Mzee Mkwizu aitwaye Kajiru. Kajiru alikuwa Mbwa mkubwa mwenye miguu yenye nguvu, alikuwa mweusi, na hiyo ndiyo iliyomfanya aitwe “Kajiru” ambayo kwa Kiswahili humaanisha “keusi”. Alikuwa ni Mbwa mwenye adabu, uso wenye soni lakini ulioficha ukali na hasira, Meno yake yalikuwa yamechongoka, makali yasiyo na mzaha. Huyo ndiye Kajiru rafiki Mpya wa Sajenti awapo machungani. Sajenti hakuwahi kuwa mchungaji wa mifugo ingawaje kiasili yeye ni Mkurya kabila ambalo pia hufanya ufugaji japo sio kwa kiwango kikubwa. Hivyo Kajiru ndiye alimsaidia kuchunga hasa kuwadhibiti Mbuzi waliokuwa wasumbufu.

Mwezi Sasa uliisha, Sajenti alichoka kukaa ndani na kwenda machungani kulisha mifugo ya Babu yake. Hilo Mzee Mkwizu aliliona, Hakutaka Sajenti ajisikie vibaya, tena akose amani. Siku ya Gulio ilipofika, ndiyo siku ya Jumatano katika kijiji cha Makanya kilichopo kaskazini mwa kijiji cha Nkwini, Mzee Mkwizu alimuagiza Sajenti akanunue vitu vya ndani, alimuagiza Ngogwe ambayo pia huitwa Nyanya Chungu, nyanya, Kweme, Viazi vitamu, kahawa na vitunguu.


Sajenti hakuwahi kufika katika mji wa Makanya. Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza. Kutokana na kukaa sehemu moja alijawa na hamu ya kuuona mji wa Makanya. Pengine alivuta picha jinsi mji huo ulivyo, au hata aliuona kabisa kwenye fikara zake. Lakini yote ilikuwa hamu ya kuufahamu mji wa Makanya. Mzee Mkwizu alitamani sana kuambatana naye kwenda Gulioni, Makanya. Lakini uzee ulishanyonya nguvu za mwili wake, miguu yake haikuwa na nguvu kabisa ya kutembea umbali mrefu, hata huko kuchunga mifugo ni kwasababu alishaifunza mifugo ile kuongozwa. Ungeshangaa namna Mzee Mkwizu akiiongoza Mifugo yake. Kila ng’ombe alikuwa na jina lake licha ya ng’ombe kuwa wengi, ajabu ni kuwa ng’ombe nao walitambua majina yao.

Sajenti alishuka stendi ya Makanya ambapo upande wa mashariki kulikuwa na Katani na safu ya milima ya upare. Katani zilikuwa zimepandwa kwa mpangilio wa mistari iliyonyooka, hakika zilikuwa zinapendeza. Kilimo cha katani ni moja ya kilimo kilichoanzishwa na wakoloni hapa nchini, ni muhimu sana kwani kinazalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo kamba nzuri za katani, mifuko ya katani na mazulia. Katani pia huzalisha mbolea nzuri Ambayo hutumika kwenye kilimo. Kilimo cha Katani Makanya husaidia baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kujipatia kipato baada ya kulima vibarua katika mashamba makubwa ya katani.


Upande wa Magharibi macho yake yalipokelewa na mji mzuri wa Makanya uliokaa kwenye tambarare inayovutia. Aliona vifusi vifusi vya mawe meupe, hayo yalikuwa mawe ya jasi ambayo hujulikana kama gypsum kwa lugha ya kingereza. Mawe ya Jasi hutumika kutengenezea saruji kwa ajili ya sakafu, pia hutumika kutengenezea Cealing board ya gypsum. Machimbo ya gypsum ni moja ya shughuli muhimu katika mji wa Makanya, watu wengi hasa vijana huenda machimboni kuchimba mawe hayo na kujipatia kipato.

Sajenti alishangaa kuona vijana wakitafuna vitu midomoni, alipochunguza akabaini vijana wengi wa Makanya hutafuna Mirungi, bado ilikuwa ni asubuhi Sajenti akiwa pale Stendi ya Makanya akiwa amekaa kwenye kijimgahawa akiangalia mienendo ya watu pale Stendi. Tofauti na alivyozoea kuona katika stendi za miji mingine ambapo Mabasi yakifika Stendi, vijana waliobeba bidhaa mbalimbali hulikimbilia Basi na kuanza kuuza bidhaa zao, Stendi ya Makanya hali ilikuwa tofauti kabisa, aliona vijana wenye bahasha za kaki zilizotuna wakikimbilia mabasi yaliyokuwa yamesimama pale stendi, kisha wanamkimbilia dereva au konda alafu atakayewahi basi ndiye humpa moja ya zile bahasha ya kaki zilizotuna. Hiyo ikamfanya Sajenti adadisi ndani ya zile bahasha kuna nini, Looh! Kumbe ni Mirungi.

Sajenti aligundua kwamba Makanya lilikuwa ndio soko kubwa la mirungi ambalo madereva walikuwa wanatumika kama wateja na wasafirishaji wa bidhaa hiyo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Wateja wakubwa wa Mirungi walikuwa madereva wa malori yanayofanya safari ndefu, madereva wenye asili ya kisomali na kiarabu, vijana, na watu wazima.


Sajenti alimuita kijana mmoja akamuuliza;

“ Habari kijana, vipi naweza kupata mrungi?”

“ Gomba ipo Broo, vipi unahitaji kete ngapi?” Kijana alimjibu huku akiingiza mkono wake kwenye bahasha kutoa mrungi.

“ Kete moja tuu” Sajenti alijibu akiwa kajua jina jingine la mrungi kumbe lilikuwa ni Gomba. Hata hivyo alisubiri aone kete moja inalinganaje kwani hakuwahi kujua habari za mirungi.

“ Hii hapa Broo, hii sio Kilaza, hii ni Og kabisa haijalala, inatoka Tae. Si unaona mzigo ulivyo wamoto” Kijana alizungumza lugha ya kibiashara uso wake ukiwa umejawa na tabasamu.

“ Shilingi ngapi?” Sajenti aliuliza akiwa kapokea ile kete ya mrungi huku akiikagua.

“ Elfu mbili tuu braza, hiyo kitu ni mang’anyu”

“ Duuuh! Mbona ndogo hivyo, Mang’anyu ndio nini?” Sajenti alishangaa kuona kete ya mrungi ilivyo ndogo lakini bei yake ilivyokuwa kubwa.

“ Broo, huu ni msimu wa kiangazi, gomba bei yake ipo juu, miti ya gomba kipindi cha kiangazi haichipui sana, hivyo gomba inaadimika mpaka msimu wa mvua” Kijana alijibu akijaribu kuelezea kwa ufasaha ili mteja wake aelewe ajipatie kipato.

“ Kumbe! Hiyo mang’anyu ndio nini sasa?”

“Hhahaha! Broo bhana, Mang’anyu ni lugha tuu za kijiweni, maana yake ni kitu kizuri” Kijana alicheka sana, Sajenti naye alicheka baada ya kujua maana ya neno hilo.


Sajenti baada ya kuzungumza na Yule kijana, aligundua mambo mengi yahusuyo mji ule wa Makanya. Hatimaye alienda mnadani kununua vitu alivyoagizwa. Alipofika sokoni alikuta umati mkubwa wa watu wakiuza biashara zao na wateja wakinunua bidhaa. Lilikuwa soko kubwa kiasi. Lugha alizozisikia mbali na Kiswahili ilikuwa lugha ya kipare. Hapo akajua eneo lile limetawaliwa na watu wenye asili ya kabila la wapare. Pia aliwaona Wamasai wengi upande wa nyuma lilipo soko la mifugo.

Hatimaye alimaliza kununua bidhaa zote alizoagizwa, lakini alivutiwa na matunda Fulani yaliyokuwa na maganda ya rangi ya njano, alipouliza aliambiwa yanaitwa ‘Sambia’ aliyaonja, Dooh! Yalikuwa yana sukari na ukakasi, ndani yake yakiwa na mbegu za rangi ya huzurungi.

Muda ulikuwa umeenda sana, jua lilikuwa kali yapata mida ya saa sita. Sajenti akarudi Nkwini kwa Babu yake akiwa amefurahia safari yake, roho yake ilisuuzika, mji wa Makanya uliamsha chemchem ya uhai na ari moyoni mwake.

***************************




Usiku uliingia, giza nalo likafungua mdomo wake likaumeza mji wa Nkwini. Siku ile anga lilitawaliwa na Mawingu makubwa meusi yenye kutisha. Sajenti na Mzee Mkwizu walilala kama ilivyokuwa desturi ya wanadamu wote kulala usiku. Siku hiyo Sajenti alikuwa amechoka kuliko siku zote, alichoshwa na mizunguko ya mchana ya sokoni, Makanya. Leo alilala fofofo mithili ya pono. Hata angeota ndoto lazima ingekuwa ndoto yenye kutisha, yenye kufisha na kulegeza mwili na roho.

Huko nje Kajiru alikuwa akibweka Huu! Huuu! Wakati wengine wakiwa wamelala wasijue nje kuna zimwi linalokuja kuwala. Kajiru alibweka, sasa muda huu sauti ikiwa imeongezeka ikiwa na wehu ndani yake. Tayari mvua ilianza kunyesha hali iliyofanya sauti ya kubweka kwa Mbwa, ndiye kajiru kutosikika vizuri kutokana na bati kupiga kelele zilizosababishwa na matone ya mvua. Nje walikuwepo wanaume sita, waliovalia makoti makubwa meusi ya mvua, wakiwa wameshikilia bunduki aina ya SMG. Walishaingia kwenye uzio wa nyumba ya Mzee Mkwizu, Sauti ya Mbwa iliwafanya waongeze tahadhari, wakimtafutia shabaha ya kumlenga ili kumuua asiendelee kubweka kwani walihofia sauti yake ingewaamsha wakina Sajenti.

Wakwanza kushtuka usingizini alikuwa Mzee Mkwizu, akiwa kitandani alisikia kwa mbali Mbwa wake akilia huku Mvua kubwa ikinyesha. Aliamka kitandani na kuwasha tochi yake aliyokuwa kaiweka chini ya mto wa kitanda, kisha akachukua gobore lake, akatoka kwenda sebuleni.

Alipofika sebuleni alishtuka kuona mlango ukicheza cheza, ni kama kuna mtu alikuwa anataka kuvunja kitasa. Hapo akakoki gobore lake akimulika mlango. Mapigo ya moyo wake yalienda upesi mno, miguu na mikono yake ilianza kutetemeka. Muda huo Sajenti hana hili wala lile, kalala kwa starehe ungedhani dunia anaimiliki yeye. Asijue hatari inayowakabili.


Kitu pekee kilichowashinda ni ule mlango jinsi ulivyotengenezwa, pia ulikuwa ni mlango wa mbao ngumu ya mninga. Hivyo haikuwa rahisi kwao kuuvunja. Basi walichukua baruti ya kuvunjia wakaitega pale mlangoni, kisha wakasogea umbali wa mita kadhaa, wakati huo Mzee Mkwizu kasimama akiwa kajiandaa kumpiga yeyote atakayetangulia. Masikini, hakuwa na bahati. Mlango ulifumuliwa na baruti, Mzee Mkwizu alipigwa na kipande cha mbao kichwani akaanguka chini. Mshindo na sauti ya baruti ilimshutua Sajenti. Upesi akaamka akaichukua bastola yake.

Aliamka akiwa na kaptura, akachungulia sebuleni. Hapo macho yake hayakuamini, alimuona Babu yake akiwa kaanguka akiwa kashika tochi iliyokuwa inamulika mlangoni, alipagawa alipoona mlango umevunjwa. Hapo akajua kuna hatari kubwa inakuja. Akili yake ilimuonya, ikamuambia asifanye haraka kwenda kumuangalia Babu pale chini. Punde alishtuka kuona jitu kubwa lililovaa koti kubwa jeusi la mvua likiwa limenyeshewa likiingia kwenye ule mlango wa sebuleni. Jitu lile lilikuwa limebeba bunduki mkononi. Sajenti hakutaka kuwa na haraka kulipiga risasi, alisubiri aone kuwa lipo lenyewe ama lipo na wenzake. Punde akatokea mtu mwingine, huyu alikuwa mfupi mfupi, naye alikuwa kavaa koti la Mvua. Yule mtu wa pili aliingia akaichukua ile tochi na kuanza kumulika mulika. Kosa! Alifanya kosa ambalo hatajisamehe daima. Wote wawili walijikuta wakianguka chini baada ya Sajenti kuwapiga risasi. Jambo hilo lilifanya wale maadui wanne waliobakia nje kupiga risasi bila mpangilio. Sajenti akajua kuna maadui wengine lakini hakujua hesabu yao.

Sajenti alimuona Mzee Mkwizu akizinduka kichwani akiwa na jeraha lilokuwa linavuja damu, Mzee Mkwizu kabla hajafanya chochote wale watu walimtandika risasi tatu za kifuani wakiwa wapo kwa nje.


Sajenti aliumia sana. Alikumbuka maneno ya Babu yake siku alipofika aliyomwambia kuwa amekuja na mkosi. Sajenti roho yake ilizimia kwa maumivu. Alisikitika kuona maneno ya Babu yakitimia.

Akatoka kwenye ile kona akaenda kwa kunyata mpaka karibu na mlango wa sebuleni, akalala chini alafu akachungulia kwa nje, hapo akawaona watu watatu wakiwa wamesimama wakitazama ndani wakiwa wamebeba bunduki zao. Alichukua bastola yake kisha kwa upesi alijiviringa kama gunzi la mhindi na kuwapiga kwa mpigo, wote watatu wakadondoka chini. Awali niliwaambia kuwa hakuna mchezo anaoupenda na kuuweza Sajenti Warioba kama mchezo wa kutupiana risasi. Sajenti alikuwa na shabaha, hakuwahi kukosa pale atakapo kulenga mtu. Jeshini walimfahamu kama mkono wa Shabaha. Akipewa risasi kumi auwe watu kumi basi tambua kuwa kila risasi itaondoka na mtu mmoja kama alivyoagizwa. Sasa kulikuwa kimya kabisa, Sajenti akajua amemaliza kazi. Sajenti alisimama akaenda kwa Babu yake, alimkuta tayari ameshakufa. Alilia kama mtoto mdogo, alijiona yeye ndio chanzo cha kifo cha Babu yake. Kama si yeye kuja hapo basi Mzee Mkwizu asingekufa.

“Kweli mimi ni Mkosi, Babu mimi ni mkosi. Tazama sasa maneno yako yanatimia. Bora ningekuja kukuzika lakini sio kusababisha kifo chako. Babu yangu nisamehe” Sajenti alilalamika mwenyewe akilia kama mwendawazimu huku Mvua ikiendelea kunyesha.

Punde akiwa kapiga magoti akilia aliduwaa baada ya kisogo chake kuguswa na kitu kigumu, ndio alikuwa kawekewa bastola kisogoni na yule mtu wa sita, masikini Sajenti alijua amewamaliza wale watu wabaya lakini kumbe alikuwa amembakiza mmoja. Huyo ndiye sasa aliyemuweka chini ya ulinzi.

“Mikono juu, utulie hivyo hivyo, vinginevyo leo hii utamfuata Babu yako kuzimu” Yule Mtu aliongea kauli ya kibabe sana sauti yake ikikaribia sauti ya jinamizi mkatili asiye na chembe ya huruma.


Sajenti aliinua mikono yake juu bila ya ubishi, sauti ile aliielewa sana. Hakutaka kuleta ubishi ambao alijua ungegharimu maisha yake. Ghafla Mbwa alitokea akamvamia Yule mtu kwa nyuma na kuanza kumshambulia yuule jambazi akiwa kaanguka chini. Sajenti akaona ile ndio nafasi ya kujinasua, alinyanyuka chapuchapu kama umeme lakini alichelewa, kabla hajafanya chochote Yule mtu aliachia risasi ikampiga na kumuua Yule Mbwa, ndiye Kajiru. Sajenti hasira zilimpanda kama mbogo wa Mikumi aliyejeruhiwa, alimpiga Yule mtu risasi mfululizo hata alipopoteza maisha Sajenti aliendelea kumpiga risasi bila kuacha, Risasi ziliisha kwenye bastola ikawa ndio mwisho wa Sajenti kumpiga risasi.

Usiku huohuo Sajenti alitoka nje akaenda kuchimba kaburi la Babu yake karibu na Zizi la ng’ombe huku manyunyu ya mvua yakimdondokea. Mwanga wa jua la asubuhi ulimkuta akiendelea kuchimba, ng’ombe, mbuzi na kondoo walimtazama Sajenti wakiwa na nyuso zenye simanzi. Leo hii Bwana wao, Mzee Mkwizu amekufa kwa kuuawa na watu wabaya wasio na huruma. Ndama mmoja mweupe alikuja karibu na kaburi akawa anamtazama Sajenti akiwa ndani ya kaburi akichimba kaburi. Sajenti alimuona yule ndama, hapo akajikuta akipatwa na huzuni.


Alimaliza kuchimba Kaburi, hapo akarudi ndani jua lilikuwa limeshapanda juu kabisa. Maiti Saba ya watu pamoja na mzoga wa Mbwa, ndiye kajiru zilikuwa zimelala pale chini. Aliubeba mwili wa Babu yake kisha akaenda kuusafisha vizuri bafuni. Alafu akaenda ndani akachagua nguo nzuri aliyoiona itamfaa Marehemu Babu yake kumzikia. Aliona Suti nzuri mno ya rangi nyeusi, akamvalisha Babu yake. Kisha akaendelea kukagua lile sanduku la nguo, hapo akaona kanzu nzuri ya zambarau na kikofia cha kichifu. Akaivaa ile kanzu na kile kikofia.

Akaubeba ule mwili wa Babu yake, kisha akarudi kuuchukua mzoga wa Kajiru, baadaye akauingiza mwili wa Babu yake kaburini na mzoga wa Mbwa wake. Alipoiingiza kaburini hiyo miili, akaenda kufungulia ng’ombe. Mbuzi na kondooo. Hao ndio walikuwa mashuhuda wa mazishi ya Mzee Mkwizu Mifugo yote ililizunguka kaburi. Kisha Sajenti akiwa kavaa kanzu ya zambarau na kofia nyekundu akiwa kama Kuhani anayeendesha maziko hayo. Sajenti aliomba dua ya kumuombea Babu yake, kisha akamzika Babu yake pamoja na Mbwa wake.

Hivyo ndivyo shujaa Mzee Mkwizu alivyozikwa kwa heshima na Sajenti pamoja na mifugo yake. Akaliliwa na Mjukuu wake na mifugo yake kwa siku tatu. Sajenti akachukua maziwa aliyoyakamua kwenye ng’ombe na mbuzi na kuyamwagia kwenye kaburi lake. Kisha akachukua mafuta ya mkia wa moja ya kondoo zake akayamwagia katika kaburi lake. Mwisho akachinja kuku na kuchoma manyoya yake katika kaburi lake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa, na habari zake Sajenti akazichukua ili kuziandika kama alivyozikuta katika sanduku la kuhifadhia historia ya maisha ya Mzee Mkwizu.





Ikawa baada ya Sajenti Kumzika Babu yake, ndiye Mzee Mkwizu. Sajenti aliondoka katika Kijiji cha Saweni akiwa kauza mifugo ya Babu yake, aliuza ng’ombe, mbuzi, kondoo na Kuku. Hapo akapata fedha ambazo ni shilingi milioni tisa, akiwa kauza kwa bei ya kutupa. Lakini kama angeuza kwa bei halisi basi Sajenti angekuwa amepata zaidi ya pesa hizo. Sasa alikuwa karudi Dar es Salaam, hakutaka kubaki pale kwenye Kijiji cha Saweni kwani tayari ilishagundulika kuwa anaishi pale.


Alichukua chumba Mtoni Mtongani, akanunua kitanda na Godoro. Sasa alianza maisha mapya ya kujificha, maisha kama panya ndiyo aliyoanza kuyaishi. Aligeuka popo, akawa analala mchana na kutoka usiku kwenda kuzunguka zunguka katikati ya mji.

Mtoni Mtongani mpaka kwa AZIZI ALLY alikutana na Mateja wengi wa Unga, alisikitika kuona vijana wengi wakiteketea kwa madawa ya kulevya.

“ Hii yote ni nguvu kazi ya taifa inayopotea bure, laiti vijana hawa wangekuwa hawajajiingiza kwenye uraibu huu. Basi familia zao zingenufaika na nguvu zao”

Sajenti alijiwazia mwenyewe akiwa anatembea yapata mida ya saa tano usiku akiwa maeneo ya Uhasibu akirudi Ghetoni kwake. Magari yalikuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa. Mtu mmoja mmoja ndiye aliyekuwa anaonekana akitembea, Ghafla bin vuu Sajenti alishtuka kuona kundi la vijana wapatao saba wakiwa wamesimama mbele yake. Walikuwa vibaka, mateja wa Temeke ambao kundi lao waliliita CHURA MAJI YA MOTO. Vijana hawa walikuwa ni moja ya makundi tishio katika jiji la Dar es salaam. Walijulikana kwa uporaji, ubakaji, uvunjaji na hata mara nyingine walikuwa wakisababisha mauaji kwa watu walioonekana wabishi wakiwapora.

Leo walikutana na Sajenti, mtu hatari mwenye rekodi chafu ya mauaji, komando mwenye mafunzo ya kiwango cha juu ngazi ya kimataifa. Hawakujua mtu waliyemtaitisha, lati wangemjua huenda wasingethubutu hata kupita njia hiyo achilia mbali kumsimamisha. Walifanana kama kikundi cha mbwa mbele ya simba dume lenye hasira ya kupokonywa ufalme.

“ Oyaaa! Toa kila kitu ulichonacho jombaa!” kiongozi wa wale vijana alimuamrisha Sajenti.

“ Salama wakubwa, uungwana ni kupeana salama kwanza” Sajenti alisema akiwa anajiandaa kuwakabili.

“ Hizo sisi hazituhusu, tunachotaka ni pesa. Toa pesa, simu weka chini haraka, vinginevyo tukugeuze mishikaki” Kiongozi wao aliongea wakati tayari wamemzunguka na kumkaribia wakiwa wameshika silaha za jadi.

“ Sina chochote wakubwa….”


“ wee fala nini..! Huna chochote nini kimekufanya utembee sasa hivi, hatutaki kujua umetoka wapi, tunachotaka ni pesa” kijana mmoja aliongea akiwa amemchapa kirungu cha mgongo.

Sajenti hakutaka kupoteza muda, alianza na Yule aliyempiga kirungu aliyekuwa upande wa nyuma yake. Alimrushia teke kwa upesi usiotarajiwa, teke likampiga kwenye shingo Yule kijana akadondoka chini. Walishikwa na butwaa na kabla akili yao haijakaa sawa Sajenti alimrukia kiongozi wa wale vijana teke la kifua akadondoka chini, hapo kizaazaa kikaanza. Moto ukalipuka. Sajenti alikuwa amechochea kuni kwenye tanuru la moto. Wale vijana walimfuata na kumshambulia kwa pamoja wakiwa na silaha zao za jadi. Sajenti kwa nguvu aliwapangua, na kuwaangusha wote chini.

Jambo moja nisisahau kulieleza ni hili; Vijana wale wengi wao walikuwa ni mateja, Afya mgogoro. Walikuwa na miili dhaifu ambayo kwa macho tuu walionekana ni watu wasiopata milo mitatu kwa siku. Hii ilifanya wawe na miili dhoofu na ngozi zilizofubaa. Walikuwa wana kila dalili za hali ngumu ya maisha, mafukara wasiohitaji kujitambulisha.

Hiyo ndio sababu ya Sajenti kuwashinda nguvu, Sajenti aliwapiga mpaka wengine wakakimbia huku wengine wakiwa wamezirai pale chini, mmoja ndiye alikuwa yupo mikononi mwa Sajenti. Sajenti alimchukua.

“ Nisamehe Mjeda, nikaushie brother. Tafadhali Broo!” Yule kijana aliyebebwa na Sajenti aliongea kwa sauti ya kuonewa huruma lakini Sajenti alimchapa kofi zito la uso kisha akafoka;

“ Kelele..! Ukisema tena natoa roho yako”

Hapo kijana akashika adabu huku akishika uso wake wenye maumivu ya kibao alichopigwa na Sajenti. Kibao kile kilikuwa kizito mno, pengine hicho ndicho kilimfanya aielewe kauli ya Sajenti kuwa aache kelele vinginevyo atatolewa roho yake. Sajenti alimchukua Yule kijana mpaka kwenye chumba alichokuwa amepanga, akaingia naye ndani. Kisha akainama uvunguni mwa kitanda akatoa maembe mawili, akampa embe moja Yule kijana, na wote wakaanza kula maembe.


“Sitaki kukudhuru, wala sijapenda kukupiga lakini sikuwa na njia nyingine kutokana na uovu wenu. Naitwa Peter Mirambo, ukipenda niite PM. Wewe waitwa nani rafiki?” Sajenti alifukuza ukimya wa kile chumba akamuuliza swali Yule kijana.

“ Naitwa Feisal Athumani Alimaarufu kama Osama, sina jina jingine Broo” Kijana alijitambulisha mara hii hofu ikiwa imepungua.

“ Vizuri. Umefikaje hapa ukaweza kuwa kibaka, hujui huo ni uhalifu Osama? Huogopi kukamatwa na vyombo vya dola?” Sajenti aliuliza.

“ Vyombo vya Dola..! Hahahaa! Broo unachekesha, vyombo vya dola ningeviogopa kama kusingekuwa na Rushwa.” Osama alijibu akiwa ananyonya kokwa la embe alilopewa na Sajenti.

“ Kwa hiyo wewe huogopi kabisa polisi?”

“ Mbona huamini kama siviogopi, au broo wewe ni polisi?” Osama aliuliza hofu ikiwa imeshika uso wake.

“ Hapana, ila nimeshangazwa na maelezo yako,..” Sajenti aliongea lakini akakatishwa;

“ Sisi vibaka hofu yetu ni kuuawa na raia lakini kuhusu polisi kwa kweli hatuogopi hata kidogo. Nimeshaingia sero mara kibao na kutoka nikiwa na kosa la ukabaji, wizi na uvunjaji” Osama aliongea kama mtu anayejisifu huku akimtazama Sajenti kama mtu aliyekuja mjini siku ile asiyejua mambo ya mjini.

“Kwa nini hamuwaogopi polisi wakati nyie ni wahalifu? “ Sajenti aliuliza kwa msisitizo.

“ Broo PM, nikujibuje uelewe.. Nimekuambia Rushwa ndio mbeleko yetu. Siku Rushwa ikitoweka nasi tutawahofia polisi. Mimi hata sasa hivi unikamate na kunipeleka polisi, nakuhakikishia kesi haitofika mahakamani, tutahonga polisi na nitaachiwa. Mara ngapi nimefanya hayo” Osama aliongea muda huu akitoa maelezo yaliyomfanya sajenti aridhike.

“ Haya nimekuelewa, hujanijibu swali la pili”

“ lipi tena, kwani uliniuliza mangapi?”

“Nilikuuliza imekuwaje mpaka unaishi maisha haya ya uhalifu? Umekumbuka sasa?” Sajenti alimuuliza Osama akiwa anaosha mikono yake baada ya kumaliza kula embe.


“ Nimekumbuka. Broo.. Tamaa mbaya. Kupenda mambo ya mkato ndio kuliko nifikisha hapa. Kama sio kupenda mkato huenda leo nisingekuwa hapa. Ningekuwa mtu msomi ninayeheshimiwa” Hapo akatoa sigara yake iliyokuwa mfukoni, ilikuwa imevunjika, nadhani ni kutokana na mbilinge mbilienge ya kupigwa mabuti na Sajenti muda ule.

“ Unaniruhusu niwashe na kuvuta..” Akamuuliza Sajenti;

“ Hamna shida, endelea; tamaa ilikufanyaje mpaka leo hii umekuwa mhalifu?”

“ Tamaa ya kuwa na maisha mazuri iliniingia nilipofika kidato cha pili, nilipokuwa nasoma shule ya sekondari Mugabe pale Sinza. Rafiki zangu niliokuwa natembea nao ndio walionishawishi kuingia kwenye uuzaji wa madawa ya kulevya. Wao walikuwa wakivaa nguo nzuri, viatu vizuri pia walikuwa na simu nzuri mno za bei ya juu, mwanzoni nilikataa kwani nilijua kujiingiza katika biashara hiyo ni kuhatarisha maisha yangu. Lakini rafiki zangu waliniwekea vikwazo mno, hawakutaka tena kunilipia pesa za chai na chapati, wala hawakutaka kunipa pesa ya chakula cha mchana..”

“ Kwani hukuwa unapewa pesa na wazazi wako?” Sajenti alimkatisha Osama kwa swali.

“Mama alikuwa ananipa pesa ya nauli tuu, shilingi mia nne. Mia mbili kwenda, mia mbili kurudi. Kwetu tulikuwa masikini. Mama yangu alikuwa anatembeza mchicha, kipato hakikuwa kinamkidhi. Najua unafikiria habari za Baba yangu, sikulelewa na Baba. Mara ya mwisho kumuona Baba nilikuwa na miaka sita, Mama alinambia alienda South Afrika kutafuta maisha” Osama aliongea kama mtu mahiri sasa wa kusimulia stori. Alikuwa ametulia uso wake ukikumbuka mengi sana. Sajenti naye alijikausha akimsikiliza ungedhani anasikiliza mahubiri ya siku za mwisho.


“ Basi ningefanya nini, nikajiunga na rafiki yangu ambaye kwa sasa nasikia yupo kwenye Meli ya Ambagon..”

“ Meli ya Ambagon…?” Sajenti alishtuka kusikia habari za Meli ya Ambagon. Alipoteza umakini na kujikuta akihamaki kwa sauti kubwa. Ni kama alisikia jambo kubwa linalotisha. Hakutegemea kabisa kama angesikia habari za Meli ya Ambagon kutoka kwa Osama. Sasa akajua Osama atakuwa na taarifa nyingi za siri ambazo alikuwa akizitafuta kwa muda mrefu.

“ Mbona umeshtuka unaifahamu Meli hiyo?” Osama aliuliza baada ya kumuona Sajenti akiwa ameshtuka.





“ Mbona umeshtuka unaifahamu Meli hiyo?” Osama aliuliza baada ya kumuona Sajenti akiwa ameshtuka.

“ Hapana Dogo, eehe! Endelea, huyo rafiki yako anaitwa nani?”

“ Omary Saidi” Osama alijibu,

Moyo wa Sajenti ukapiga paa! Alimkumbuka Omary aliyekutana naye ndani ya Meli ya Ambagon. Sasa hapo akajihakikishia kuwa maneno ya Osama yalikuwa ni kweli kabisa. Hapo akataka kujua zaidi, aliona kuna kitu anaweza kukipata kutoka kwa Osama.

Osama akaendelea kusimulia;

“ Mama yake Omari alikuwa ni konda wa Mbagala kwenda Makumbusho, alikuwa ni rafiki yake mama yangu. Urafiki wa Mama zetu ndio ulitufanya mimi na Omary tuwe marafiki, tena ndugu. Omary akanipeleka kwenye vilinge vya madawa ya kulevya, huko wanapouzia na wanapovutia. Basi nikapewa elimu ya biashara hiyo hatari. Mimi nilianzia kuwa msambazaji wa dawa za kulevya palepale mtaa wa Tandale, bahati nzuri mji wa Dar nilikuwa naufahamu vizuri. Hivyo mitaa yote yenye wateja wetu nilikuwa nasambaza” Hapo akameza mate huku akiwafukuza mbu waliokuwa wanamng’ata miguuni.

“ Nami nilianza kupata vijisenti ambavyo vilinisaidia shuleni na pale nyumbani. Hiyo ikanifanya niingie rasmi na kuongeza juhudi ya uuzaji wa madawa ya kulevya. Pengine ungetaka kujua ni aina ipi ya madawa nilikuwa nauza, nilikuwa nauza Cocaine na heroine, Bangi na mirungi”

“ Samahani kwa kukukatisha, hukuweza kutambua madawa hayo yanatoka wapi, na mpaka yanafika kwako yamepitia wapi?” Sajenti aliuliza.

“ Cocaine na heroine nilisikia zinatoka Mexico, na Brazil huko, alinambia Omary kuwa, kwenye ile meli ya Ambagon. Lakini Mirungi na Bangi nyingi huzalishiwa hapahapa nchini. Cocaine na Heroine huingia nchini kwa njia tatu, Viwanja vya ndege, bandari bubu, na njia ya magari. Mara nyingi hupenda kutumia njia ya magari na bandari Bubu kwani huku hakuna ukakuguzi mkubwa tofauti na kwenye viwanja vya ndege. Madereva wengi wa malori ndio hutumiwa zaidi, hawa wanaotoka nchi moja kwenda nchi nyingine. Pia baadhi ya misafarsa ya vongozi wakubwa wa kitaifa hutumiwa kama fursa na baadhi ya viongozi wasiowaaminifu. Wasanii wakubwa baadhi yao husafirisha madawa kwa kumeza, wengine huagizwa na viongozi wa nchi. Unakuta msanii mkubwa kutoka marekani anakuja hapa nchini kufanya tamasha la burudani lakini nyuma yake kaja na mzigo wa maana” Osama alimeza mate, Sajenti alikuwa anamsikiliza kwa umakini mkubwa sana. Ilikuwa simulizi ambayo Kwa Sajenti ilikuwa na msaada kwa sehemu kubwa kutokana na kazi yake ya upelelezi.

“ Pia wachungaji wakubwa baadhi yao ni wauzaji wazuri wa dawa za kulenya, Kupitia mikutano yao kimataifa husafirisha madawa hayo kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine”

“Aisee! Mabona unajua mambo mengi na makubwa kiasi hicho, ehee! Inakufikiaje wewe?” Sajenti aliongea akiwa amemkatisha Osama.


“ Mimi mzigo nauchukulia kwenye vilinge vya madawa ya kulevya, hapo ndio sokoni. Unaweza kwenda kuuza au kununua. Unaweza kwenda ukakuta kilinge hakina mzigo ukauza, au ukaenda kununua mzigo na kwenda kuuza sehemu nyingine” Osama alijibu kisha akamtazama Sajenti kama mtu anayemwambia aulize swali jingine.

“ Masoko ya mitumba ya nguo yanafahamika, mbogamboga tunayajua, sasa mtu atajuaje kuwa hili ni soko la Madawa ya kulevya?” Sajenti aliuliza kama mwanafunzi mwenye nidhamu.

“ Vizuri. Kuna ishara kadhaa huwekwa na wauzaji na watumiaji wa madawa ya kulevya. Ishara ya kwanza ni kuning’niza viatu juu ya waya za nguzo za umeme. Uliwahi kuona viatu vilivyoning’inizwa juu ya waya za nguzo za umeme Broo?” Osama alimuulzia Sajenti.

“ Ndio Osama, nimewahi kuona”

“Ulijiuliza inamaana gani?” Osama alimuuliza akitabasamu.

“ Kwa kweli naonaga, ila sijawahi kujiuliza, mimi najua ni wahuni tuu ndio hufanya hivyo, kumbe ni ishara!”

“ Hiyo ni ishara ya kuwa eneo hilo ni soko la madawa ya kulevya”

“Looh! Sikuwahi kufikiri hata kidogo..” Sajenti alizungumza akiwa ameshangazwa na ishara hiyo ya soko la madawa ya kulevya.

“ Basi ipo hivyo. Sehemu nyingi zenye ishara hiyo ni masoko ya madawa ya kulevya. Japo sio kila sehemu kutokana na kuwa wengine hurusha viatu juu ya nyaya za nguzo za umeme bila ya kujua maana yake. Ila tambua sehemu nyingi humaanisha ni masoko ya madawa ya kulevya” Hapo akanyamaza akajilaza akilalia mgongo. Kisha akaendelea;

“ Ishara ya pili, majengo yenye michoro na maandishi yakihuni, michoro hii huwa kwenye kuta na majengo yasiyokaliwa na watu, majengo ambayo hayajaisha, hapa huwa ni soko la watumiaji asilimia kubwa” Osama aliongea muda huu akipiga miayo, alikuwa amechoka yapata saa nane za usiku.

Sajenti baada ya kutosheka na maelezo ya Osama alimruhusu akaondoka, akabaki akitafakari mambo yote aliyokuwa amesimuliwa na Osama. Yalikuwa mambo mazito sana ambayo hakutegemea kama angeyasikia, Kilichomshtusha zaidi ni kusikia habari za Omary, hakutegemea kabisa kwamba siku moja angekutana na mtu anayemfahamu Omary kwa undani kabisa.

********************


Upepo wenye ubaridi ulimpiga kwenye kifua wakati akiwa anaendesha pikipiki, bado giza lilikuwa limefunika dunia huku nyota zikiwa zimepamba anga, hiyo ilikuwa saa tisa na nusu za usiku wakati Sajenti Warioba akiwa juu ya pikipiki akiwa maeneo ya Kongowe akielekea Mwembe Mtengu. Alikatisha kushoto barabara ielekeayo Kigamboni ambapo ndipo Mwembe Mtengu ilipo.

Hiyo ilikuwa ni mara yake ya pili kupita katika barabara hiyo, mara ya kwanza ilikuwa kipindi kile akiwa anamfukuzia Yule mtu mweusi kama msudani aliyekuwa ndani ya gari aina ya Subaru. Ni miaka mitatu imepita tangu apite barabara hiyo, mazingira kwa sehemu kubwa yalikuwa yamebadilika, na hicho ndicho kilimfanya aendeshe pikipiki kwa mashaka ya kupotea, alihisi amepasahau lakini alipofika eneo linaloitwa Twangoma alikumbuka kuwa bado alikuwa hajapapita Mwembe Mtengu.

Hatimaye alifika Mwembe Mtengu, kisha akakata upande wa kulia, moyo wake ulilipuka baada ya kuona jumba kubwa lenye geti jeusi. Alilikumbuka jumba lile ambalo miaka mitatu iliyopita almanusura lingeondoa roho yake. Alipunguza mwendo kisha akasimamisha pikipiki mahali ambapo anakumbuka Kijana Joseph alipigwa risasi. Sasa alikumbuka kila kitu baada ya kushuka na kuchukua udongo pale chini mahali alipopigiwa Joseph risasi. Alikumbuka maneno aliyoambiwa na Joseph; Mtafute BLM umuue. Maneno hayo ndiyo yalimkumbusha maneno ya Nasoro aliyemuua kwenye ndege iliyotekwa na Kundi baya la Ambagon.


Sajenti akaamka, kisha akaikokota pikipiki yake bila kuiwasha na kuificha kwenye moja ya vichaka vilivyokuwa karibu na lile jumba ambalo lilikuwa na uzio. Sasa kazi ilikuwa imeanza, kwa wepesi bila kesi akaurukia ukuta kama paka asiye na shaka, Tayari alikuwa juu ya ukuta mrefu ambao juu yake ulikuwa na nyaya za umeme, akachungulia kwa ndani akaona mazingira yalikuwa yaleyale isipokuwa kulikuwa ongezeko la magari manne. Moja lilikuwa Toyota Pick Up, Land Cruiser Mkonga V8, Pajero na RAUM ya rangi ya samawati. Taa za nje zilikuwa zinawaka kama kawaida.

Kwa ndani vyumba vya chini vyote vilikuwa na giza isipokuwa sebuleni ambapo kulikuwa na mwanga wa taa huku mapazi marefu yakiwa dirishani yaliyomfanya Sajenti asione chochote sebuleni. Sajenti bado alikuwa juu ya Ukuta akidadisi eneo la ndani la jumba lile. Kwa upande wa ghorofani vyumba vyote vilikuwa vinawaka taa kwa ndani isipokuwa chumba kimoja ambacho kilikuwa na giza. Sajenti alishuka taratibu kwa adabu isiyo ya adhabu mpaka chini asitoe mshindo.

Alinyata mithili ya paka aviziapo panya, akaende kuchungulia kwenye dirisha la sebuleni lakini hakufanikiwa kuona chochote kutokana na pazia kuziba dirisha lote, tena dirisha lilikuwa la grili lenye vioo. Sajenti aliutazama Mlango wa kuingilia sebuleni ambao ulikuwa chini ya kinoki alafu kulikuwa na taa. Alihofia jambo moja, nalo ni uwepo wa kamera au vifaa vya kunasia sauti au mienendo ya mtu atakayekaribia mlango ule. Alikagua eneo la Kinoki na kwenye ile taa akiwa amesimama karibu na dirisha kwa nje, macho yake ya udadisi yaliukagua mlango, hapo akajiridhisha kuwa hakuna kamera yoyote iliyokuwa imetegwa.


Sasa alikuwa amefika kwenye mlango wa sebuleni, akachungulia kwenye kitundu cha kitasa, hapo macho yake yakaona masofa meusi, akapeleka macho upande wa pili, akashtuka kumuona mzee mmoja mwenye ndefu nyingi akiwa amesinzia akiwa kakaa chini kwenye kapeti huku ameegemea sofa, aligundua mzee Yule alikuwa amelewa pombe baada ya kuona glass na chupa ya bia ikiwa pembeni yake. Sajenti alikitekenya kitasa cha mlango kuona kama mlango utafunguka, kwa mshangao asioutarajia, mlango ulifunguka kumbe ulikuwa wazi. Hapo akafungua mlango nusu akiwa kaingiza kichwa ndani akichungulia huku akihofia isijekuwa ulikuwa mtego kwake. Polepole akaingia akinyata huku uso wake ukikagua sebule ile. Haikuwa na mabadiliko makubwa, luninga ilikuwa ni ileile, masofa yaleyale, kabati pamoja na jokofu kubwa, kilichokuwa kimebadilika ni zulia ambalo lilikuwa la manyoya lenye rangi nyeusi na nyeupe.

Alipanda ghorofa ya pili akiwa kashika bastola yake mkononi, alipofika juu ghafla akasimama baada ya kusikia sauti ya watu wakizungumza. Alitulia kisha akasikiliza;

“ Haiwezekani mpaka sasa hivi hatujaipata Chipu ya Darubini, mwezi sasa umeisha bado mnahangaika bila mafanikio yoyote. Ingekuwa bora kama mngekosa hizi sampo na Cadava kuliko kukosa chipu ya darubini ya hospitalini” Maneno hayo yalimchanganya sana Sajenti akiwa kajificha kwenye korido pembeni ya mlango wa kuingilia kwenye chumba ambacho kulikuwa na kikao cha siri.





“ Nafikiri kuna mchezo tumechezewa, na mwenye uwezo wa kucheza mchezo huu ni mtu mmoja. Sasa naweza kuelewa” Sauti nyingine ya mwanaume ilizungumza, Sajenti akiwa makini kusikiliza bila ya kuwaona watu wale.


“ Mtu gani huyo Dokta Binamungu? Nakuahidi donge nono zaidi ikiwa utatufungulia njia ya kumfahamu huyo adui ambaye anavuruga mipango yetu. Tuambie ni nani mtu huyo?” Sajenti aliamini sauti hiyo ilikuwa ya kiongozi wa kikao hicho. Alishtuka pia kusikia jina la Dokta Binamungu, alikuwa akimfahamu kama Daktari wa hospitali ya Boreti ingawaje alikuwa hanamazoea naye. Kufikia hapo Sajenti akaanza kuona mwanga wa kile kinachoendelea, tayari aligundua kuwa Dokta Binamungu ni miongoni mwa wasaliti waliowageuka na kutoa siri za taifa kuhusu hospitali ya Boreti.


“ Nadhani Dokta Beatus atakuwa anafahamu chochote kuhusu kupotea kwa Chipu, yeye ndiye mhusika tuu” Dokta Binamungu alisema.


“ Sidhani..! Ile siku nilivyomzimisha akazirai hakuwa na ujanja mwingine, nilichukua hiyo chipu kwenye darubini na kuondoka” Sauti ya mwanamke iliongea. Sajenti alishtuka kusikia sauti ya kike. Kilichomchanganya zaidi ni kusikia kuwa kumbe Yule mtu aliyevaa kininja aliyemuona siku ile alikuwa ni mwanamke. Sajenti hakudhani kama mtu Yule waliyemuona kwenye Kamera siku ile wakiwa room 66 angekuwa mwanamke. Jinsi alivyokuwa akitembea, alivyomvamia Dokta Beatus na pia alivyoibeba ile Cadava hakuna ambaye angeamini mtu Yule alikuwa ni mwanamke. Watu wote walijua ni mwanaume. Sajenti alitaka kumuona Yule mwanamke aliyekuwa akiongea angalau sura yake.


Habari za Dokta Beatus kutajwa kwenye kile kikao kilimfanya akili yake ikose utulivu. Aliona ipo haja ya yeye kumuwai Dokta Beatus kabla hajafikiwa na wale watu wabaya. Hakutaka kuchelewa kama alivyochelewa kwenye hospitali ya Boreti mpaka Mateka wa Ushahidi akatoroshwa.


Ghafla akiwa bado pale mlangoni alisikia mtu akipanda ngazi kuja ghorofa ya pili kule alipokuwa amesimama. Akajua ni Yule Mzee mlevi aliyekuwa amelala pale sebuleni ndiye aliyekuwa anakuja. Upesi alifyatuka kumfuata kulekule alipokuwa akija, hamadi! Walikutana kwenye ngazi Yule mlevi akiwa anapanda akiwa kashika chupa yake. Mlevi alishtushwa kwa uwepo wa Sajenti mule ndani, alikuwa kama kaona jini wa kaburini aliyesimama mbele yake. Mlevi hakutarajia kutokea kwa Sajenti. Sajenti hakutaka kumchelewesha alimpiga teke la kifua akadondoka na kuanza kubilingita mpaka chini ilipo ngazi ya kwanza. Masikini Mlevi wa watu kabla hajafikiri cha kufanya Sajenti alimzima kwa buti la kifua kama Mjeshi anayepiga guu pande. Hapo hapo Mlevi akapoteza fahamu.


Sajenti alitoka akaenda sebuleni, akakagua kagua lakini hakuona la maana, akatoka nje na kuondoka.


Moja kwa moja aliazimia kwenda nyumbani kwa Dokta Beatus, alichukua pikipiki yake na safari ya Sinza Mori ikaanza. Njia zilikuwa nyeupe pasipo na magari, ilikuwa tayari imehitimu saa kumi na nusu. Ndani ya Lisaa limoja alikuwa kashafika Sinza Mori yapata saa kumi na moja na nusu kukiwa kumekucha, Daladala na magari yakiwa yameshaanza kutembea barabarani. Alipaki pikipiki yake mbele ya geti la Nyumba ya Dokta Beatus. Bila kupoteza muda alizunguka kwa nyuma akaruka ukuta na kuzama ndani. Nyumba ya Dokta Beatus ilikuwa kimya, hii ikamfanya Sajenti kuwa makini zaidi. Alichungulia kwenye dirisha la sebuleni, hakuona mtu yeyote ingawaje taa ya sebuleni ilikuwa inawaka. Punde Sajenti alishtuka kumuona msichana akitokea pale sebuleni, Yule msichana alikuwa akipikicha macho yake yaliyozingirwa na utando wa tongo tongo za usingizi. Msichana Yule bila ya kujua kuna mtu anamtazama alifunua kanga yake ambayo aliifungia kwenye shingo kwa mtindo wa mtu anayetoka kuoga. Woooh! Sajenti soni ilimshika kuona msichana Yule akiwa uchi kama alivyozaliwa. Sajenti hakutaka kuona mambo kama yale, alificha macho yake kwa aibu ili asiuone uchi wa Yule msichana mdogo ambaye kwa umri alionekana anamiaka kumi na nane.


Ghafla Sajenti akiwa kaficha macho yake na viganja vyake, alisikia sauti ya viatu ndani ikitembea, akachungulia. Hapo akamuona Dokta Beatus akitokea chumbani akiwa kavaa kwa umaridadi, Yule msichana alivaa kanga haraka lakini alikuwa ameshachelewa kwani Dokta Beatus alikuwa amemuona. Kwa aibu Yule msichana alifunga kanga yake huku akizuga kwa kuitengeneza sebule. Chakushangaza Dokta Beatus alipofika pale sebuleni alimfuata moja kwa moja Yule msichana na kusimama nyuma yake huku akimkumbatia kwa nyuma. Jambo hili lilimshangaza sana Sajenti. Iweje Dokta mwenye elimu kubwa, na anayeheshimika kwenye jamii afanye mambo kama yale. Jambo hili lilimchukiza sana Sajenti lakini hakuwa na lakufanya zaidi ya kushuhudia aibu ile.


Aliwaona Wakinyonyana ndimi huku wakishikana kwa mahaba mazito, Sajenti aligundua kuwa ule ndio ulikuwa mchezo wao kwani kila mmoja wao alimfurahia mwenzake. Walipinduana mpaka kwenye sofa huku kanga ya Yule binti ikianguka, na hapo akawa uchi kama alivyozaliwa. Hii ilimpa nafasi Dokta Beatus kuufaidi mwili wa msichana Yule ambaye Sajenti alihisi kuwa ni Mfanyakazi wa ndani. “Mtoto mdogo lakini anamambo makubwa jamani” Sajenti alijisemea kimoyo moyo huku uhondo ule ukizidi kupamba moto.


Punde jambo lakushangaza lilimshtua Sajenti, alimuona Yule msichana akiingiza mkono wake kwenye mfuko wa Suruali ya Dokta Beatus, hapa Sajenti akawa macho kushuhudia kile anachotaka kukifanya Yule binti, lakini kabla Yule binti hajatoa mkono wake ndani ya mfuko wa Dokta ghafla sauti ya mlango wa chumbani ikasikika, na wote wakakurupuka huku Yule binti akiiwahi kanga yake pale chini na kujifunga. Dokta Beatus alijiweka sawia na kitambo kidogo alisimama mke wa Dokta Beatus akiwa kavaa nguo za kiofisi na mkoba wake begani huku akijiangalia kwenye kioo. Mke wa Dokta hakuwashtukia, ni wazi alikuwa hajawaona. Waliondoka na kumuacha Yule msichana pale sebuleni akiwa haamini kama hajafumaniwa.


Sajenti alimlaumu sana kimoyomoyo Yule binti kwa yale aliyokuwa anayafanya lakini hata hivyo alimtetea kuwa huenda alikuwa amelazimishwa na Dokta. Hivyo wakulaumiwa ni Dokta Beatus. Bado akiwa dirishani kwa nje alishangaa kuona Yule binti akijibwaga kwenye sofa huku akichekelea kama mtu aliyefanikisha jambo Fulani. Hii iliongeza umakini kwa Sajenti, alitaka kujua ni kwanini Yule binti anacheka kwa namna ile. Hapo akakumbuka muda ule Yule binti akiwa anaingiza mkono katika mfuko wa Dokta Beatus. Akili ya udadisi ikabisha hodi, na macho ya uvumbuzi yakachomoza kama jua la wakati wa kiangazi.


Yule msichana akiwa kakaa pale Sofani alitoa kifaa kilichofanana na Chipu. Sajenti alipagawa alipokiona. Akili yake ilimuambia ndio ileile chipu wanayoitafuta, ndio ileile chipu ambayo kama ataipata inaweza kumfanya akawa huru. Mapigo ya moyo yalienda upesi kama kimbunga, mwili ulimsisimuka mno. Akili yake ilikosa utulivu huku ikipiga kite. Angeachaje kupagawa ikiwa chipu hiyo ndiyo inayodaiwa kuwa yeye ndiye kaiiba. Chipu iliyomgeuza kuwa mkimbizi katika nchi yake mwenyewe. Ingawaje kulikuwa kuna kupotea kwa Cadava, lakini aliona kama angepata ile chipu ingempunguzia mzigo kwa kiasi Fulani. Lakini iweje Yule msichana aibe ile chipu kwenye mfuko wa dokta Beatus, anakazi nayo gani? Kama ametumwa, nani aliyemtuma? Mbona ni msichana mdogo lakini jambo alilolifanya ni kubwa?


Sajenti alivamiwa na msururu wa maswali yasiyo na majibu. “Huyu msichana anamuda gani katika nyumba ya Dr. Beatus? “ Sajenti alinong’ona Wakati huo Yule binti akinyanyuka na moja kwa moja akaelekea chumbani jambo ambalo lilimfanya Sajenti kuangalia anaelekea chumba kipi. Basi baada ya kujua chumba alichoingia Yule msichana, Sajenti akazunguka mpaka lilipodirisha la kile chumba. Alipofika dirishani alimsikia Yule msichana akiongea na simu.


”Ilikuwa kazi rahisi sana tofauti na nilivyotegemea, nilimlaghai na penzi zito mpaka likampofusha, likamlewesha akili yake ikawa chakari. Mke wake ndio alitaka kuwa kigagula lakini kabla hajatokea tayari nilishaiweka mikononi chipu ya Darubini. Nasubiri maelekezo yenu” Yule Binti aliongea kwa wasiwasi huku akiangalia huku na huku kama mtu asiyejiamini licha ya kuwa pekee yake. Hakutaka mtu yeyote ajue yale aliyokuwa akizungumza kwenye simu.


“ Mfanye haraka kabla hajarudi, maana ninauhakika atarudi muda mfupi ujao atakapogundua hana ile chipu. Sawa nawasubiri” Yule Binti aliongea kisha akakata simu. Akaichukua bahasha akaiweka ile chipu kisha akaiingiza ndani ya begi lake la nguo. Kisha akatoka kwenda sebuleni kuendelea na shughuli zake.


Basi Sajenti hakutaka kupoteza muda, hapohapo aliondoka upesi na kwa umakini wa ajabu aliingia sebuleni bila ya Yule binti kumuona wakati huo Yule binti alikuwa akipiga deki, kilichomshtua Yule binti ni mlango wa sebuleni kujigonga lakini alipoutazama aliukuta umefungwa.




Aliutazama kwa kitambo kama mtu mwenye mashaka lakini baadaye aliupuuzia. Kumbe kishindo cha mlango kilisababishwa na Sajenti alivyoingia na kuurudishia ule mlango.


Sajenti kwa upesi bila ya kupoteza muda, huku akijua kuwa wale watu waliokuwa wanaongea na Yule binti kuwa wapo njiani wanakuja hivyo wasije wakafika kabla hajaitia ile chipu mikononi mwake. Akafika kwenye ule Mlango wa chumba cha Yule msichana,. Looh! Haikuwa rahisi kama alivyotarajia, alikuta mlango umefungwa kabisa. Aling’ata meno kwa hasira, huku akijiona kama Yule msichana kamzidi ujanja.


Sajenti alirudi kwa kunyata mpaka sebuleni bila ya kuonekana, kama paka anayewinda alipeleka macho yake huku na huku akitafuta mahali ilipofunguo. Aliziona funguo nyingi juu ya meza ya kulia chakula. Akili yake ikamuambia pale hakuna funguo za kile chumba cha Yule msichana. Alitazama zaidi na zaidi lakini hakuona dalili ya kuwepo kwa funguo za kile chumba. Sasa akili yake ilikaribia kukata tamaa, mwili ulianza kupata joto, aliona kama anaenda kushindwa kuipata ile chipu ya darubini. Akili yake ikamuambia amfuate Yule binti na kumuweka chini ya ulinzi aseme wapi ilipofunguo ya chumba chake. Kabla hajafikia maamuzi akiwa anawaza jambo hilo punde simu ya Yule msichana iliita. Sajenti alishtushwa sana na sauti ya mlio wa ile simu. Sijui nini kilimshtua, labda akili yake iliamua kumshtua tuu.


Yule binti aliacha kupiga deki akaenda kupokea simu, kumbe simu ilikuwa juu ya meza ya kuwekea luninga. Sajenti alishtuka kuona funguo kwenye meza yakuwekea luninga, kumbe ile funguo ya kile chumba Yule binti aliiweka pamoja na simu. Basi Yule binti baada ya kupokea simu aliongea kwa sauti ya chini kisha akatoka nje. Sajenti kagundua kuwa mule ndani hakuwa binti pekee yake, kwani kama angekuwa pekee yake asingeongea kwa sauti ya chini. Yule msichana alitoka nje na hapo hapo Sajenti akaitumia hiyo nafasi kuichukua ile funguo. Moja kwa moja akaenda kwenye kile chumba cha Yule msichana, akafungua upesi bila kupoteza muda. Akafungua lile begi na kuchukua ile chipu. Moyo wake ulifurahi sana, ile chipu ilikuwa ni ukombozi wake, ilikuwa ndio funguo la gereza lake ambalo limemfanya kuwa mfungwa asiyehuru.


Baada ya kuichukua akaondoka kuelekea sebuleni. Punde akiwa sebuleni akasikia Geti la nje likifunguliwa, hapo akaenda kuchungulia dirishani. Alimuona Yule binti akiwa anaingia getini akifuatana na mwanaume mweusi. Yule mwanaume alibaki pale getini kisha Yule msichana akaingia ndani. Sajenti alijificha kumpisha Yule msichana apite bila ya kumuona. Kisha kwa upesi akarudi dirishani kuchungulia; alimuona Yule mwanaume mweusi akichungulia mara kwa mara nje ya geti. Uso wa Yule mwanaume mweusi ulikuwa na wasiwasi ulioficha hila na uovu wa siku nyingi.


Kitambo kidogo Yule Msichana alitoka, Sajenti akajibanza bila kuonekana. Kisha akawahi dirishani kuwaangalia; alimuona Yule mwanaume mweusi akitabasamu baada ya kumuona Yule msichana akija. Yule msichana baada ya kufika na kusimama mbele ya Yule mwanaume mweusi, aligeuka nyuma kutazama dirisha la sebuleni, hali iliyomfanya Sajenti kujificha kwa haraka kama umeme huku akipumua kwa pupa mithili ya panya aliyekoswa na mtego. Baadaye Sajenti alichungulia tena, akamuona Yule binti akiendelea kuangalia huku na huko kama mtu anayehakikisha kuwa hakuna anayemuona. Baadaye Yule binti alipohakikisha hali ni shwari akafungua ile kanga yake akaitoa ile bahasha yenye chipu akamkabidhi Yule mwanaume mweusi; Wote wakatabasamu, kisha Yule mwanaume mweusi akaingiza mkono kwenye ile bahasha akatoa ile chipu ya darubini ya maabara kuu ya Boreti. Sajenti akatabasamu, kitendo cha Sajenti Warioba kuipata ile chipu ya Darubini kilifufua upya nguvu ya uhai katika mifupa yake; tumaini lililokuwa limepotea likarejea.


************************************************

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG