Simulizi : Wakala Wa Siri (2)
Sehemu Ya Pili (2)
“ Adele! Nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kazi nzuri uliyoifanya kwa weledi wa hali ya juu. Hakika tunajivunia kuwa na wewe, nafikiri wote tuliiona video iliyoletwa na Dr. Binamungu iliyoonyesha kazi kubwa aliyoifanya Adele, ilikuwa ni kazi nzuri sana. Dr. Binamungu kama mtakumbuka siku ile alituambia kuwa siku waliyokaa kikao kujadili tukio la kuibiwa mwili wa Meja Venance, karibu watu wote waliokuwa kwenye hicho kikao walisema kuwa aliyefanya tukio hili alikuwa mwanaume….” Yule mtu alikatishwa na vicheko vya wanakikao wengine, naye akaungana nao kucheka. Kisha akaendelea.
“These people are so stupid, I can't understand their ignorance is endless or what it is, kumuita Adele ni mwanaume wakati ni mwanamke mrembo kuna maana mbili ambazo ni; mosi, hawana elimu ya ujasusi katika utambuzi wa miondoko na utendaji wa wahusika katika matukio ya uhalifu; pili, walikuwa wamejawa na hofu au kuchanganyikiwa kwa kile kilichotokea” Yule mtu akameza mateka kisha akaendelea;
“ Natoa zawadi ya Milioni hamsini kwa Adele, kisha kila mtu humu atapatiwa milioni ishirini kama sehemu ya kujipongeza kwa kuuokoa mwili wa kiungo wetu, Meja Venance” Yule mtu akasema kisha sauti za makofi yakikijaza chumba kile.
“Naomba tutulia tafadhali, hatuna muda wa kutosha” Yule mtu akasema akijaribu kuwatuliza wanakikao.
“ Nimewaiteni hapa kuwajulisha kuwa kikao chetu kilikuwa na agenda kuu mbili ambayo ya kwanza nimeshawaeleza, kuhusu mdororo unaoendelea katika mpango wetu, lakini jambo la pili ni kueleza kuhusu hali inavyoendelea katika utafutaji wa chipu ambayo kwa taarifa za kiungo wetu anasema chipu hiyo ipo mikononi mwa kijana mmoja aitwaye Sajenti Jacob Warioba…..” Yule Mtu akasema lakini akakatishwa na Adele.
“ Sajenti Warioba?” Adele akabwatuka kwa sauti jambo lililowafanya wanakikao wamtazame kwa mshangao.?
“ Unamfahamu?” Yule mtu akauliza.?
“ Sajenti….! Kama ni yeye basi tuna kazi ya kufanya” Adele akasema wenzake wakimtazama. Kisha akaendelea.?
“ Sajenti ndiye alinifanya nifungwe kwa miaka miwili kabla hamjaja kunitoa, kijana huyu ni hatari, nimeshtuka kusikia jina lake mahali hapa” Adele akasema akiwa amehamanika.
“ Unataka kuniambia ndiye Yule aliyefanya uchunguzi wa kifo cha Ramla na walioharibu harusi ya Ismaiya na Robert?” Yule Mtu akauliza.
“ Sina uhakika kama ndiye, lakini majina yake ni hayohayo”
“ Huyu si ndiye aliyepambana na kundi letu la Ambagon kule Mogadishu, Somalia? Si ndiye huyuhuyu aliyeleta fujo katika meli yetu ya ambagoni na kuua watu wetu? Kama ndiye naapa he must pay, he will regret getting into the crocodile's mouth” Yule mtu akasema huku sauti yake ikiwa imebadilika kwa kiasi kikubwa, ilikuwa sio ile sauti ya mwanzo, aliongea kwa hasira midomo ikitetemeka.
“ Huyu mbwa wakati huu hatanikimbia, alinikatili katika mipango yangu ya kumuua Ismaiya wakati ule, akasababisha nikafungwa na kusota jela nikila maharage na kuishi maisha kama panya buku. Sajenti I swear by the name of the world, I will teach you. Nitakapokukamata nitakuua kifo kibaya ambacho tangu dunia iwepo hakuna aliyeonja uchungu wake” Adele alikuwa akiwaza.
“ Taarifa tulizonazo ni kuwa, Sajenti kwa sasa hana makazi maalumu na haifahamiki anaishi wapi, hiyo haitatuzuia kumtia mikononi mwetu. Tunakila nyenzo zitakazotusaidia kumkamata mtu huyu. Hana uwezo wa kutukimbia, wengi waliofanya kama yeye walijileta wenyewe pasipo kujua” Yule mtu akasema kisha akamtazama Adele;
“ Adele tupo pamoja? Maana naona upo mbali kimawazo”
“ Ndio Mkuu tupo Pamoja” Adele akasema wakati huu akiwa makini kumsikiliza Yule Mtu.
“ Tutamkamata Sajenti kwa sababu kuu mbili; yakwanza ni kuhusu suala la chipu, hili ndilo la muhimu kwa sasa, alafu lapili ni kulipa kisasi cha aliyotufanyia, kwa kweli hatuwezi kumsamehe kwa aliyotufanyia huyu Panya. Niwaombe jambo moja, hakikisheni Sajenti anakamatwa mzima mzima akiwa hai, sitaki aletwe hapa akiwa amekufa, kwani kwa akiwa hai ndio itakuwa nafasi yetu ya muhimu kutimiza mipango yetu” Yule Mtu akiwa anaongea mara simu yake iliyokuwa mezani ikaita, jambo lililowafanya wote waitazame na kimya kidogo kitawale. Yule mtu akaichukua simu yake akapokea na kuiweka sikioni.
“ Hallo! Kweli! Upo wapi! Sawa nakuja sasa hivi” Yule mtu akasema akiongea na mtu wa upande wa pili simuni, kisha simu ikakatika.
“ Samahani nimepata dharura hapa, simu hii imetoka kwa moja ya viungo wetu waliopo maeneo mbalimbali hapa jijini, mambo yanazidi kunyooka, nafikiri niwaache muendelee na kikao mimi nikakutane na kiungo wetu huyu ili mambo haya yasilale. Mr. Gombe utaendelea kuendesha kikao hiki alafu utanipa maazimio” Yule mtu akasema kisha akatoka akiwaacha wenzake wakitamani kujua anaenda wapi.
Ni katika chumba ambacho kulikuwepo na kitanda cha futi 3*6, pembeni lilikuwepo dirisha lenye pazi jeusi, kuta za chumba kile zilikuwa za rangi ya maziwa, sakafu ilikuwa ya vigae. Pembeni ya kitanda kulikuwa na stuli ambayo juu yake ilkuwepo taa ya sola iliyokuwa ikiwaka na kutoa mwanga uliotosha watu kuonana ingawaje haukuwa mwanga mkali. Juu ya kile kitanda alikuwa amelazwa Fernanda aliyekuwa hajitambui kwani alikuwa amepotza fahamu. Hapakuwa na mtu mwingine.
Muda kidogo ulipita, Fernanda akarejewa na fahamu, alijikuta akiwa amelala kwenye kitanda kisicho na godoro akiwa amefungwa mikono na miguuni huku mdomoni akiwa kawekwa kitu ili asiweze kupiga kelele.
“ Sasa hapa nitakuwa nipo wapi, yule mtu aliyeniteka kaenda wapi? Simu! Simu! Ile simu ndio ya muhimu. Kama wameichukua watakuwa wamenirudisha nyuma maili kadhaa” Fernanda akawaza huku akigeuza shingo yake upande huu na upande huu kukagua chumba kile. Kwenye kona kabisa akaona kimeza chenye droo, lakini hakuona vilivyopo juu yake kwani mwanga haukuwa na nuru ya kutosha kumfanya aone
“ Yule mtu aliyeniteka atakuwa ni nani? Anashida gani na mimi? Au ni hawa wanaomtafuta Sajenti, kwa kweli mambo haya yamenichosha, kila siku kusumbuliwa, nashindwa kufanya kazi zangu kisa kuwafahamisha alipokimbilia Sajenti. Hata kama ningekuwa nafahamu naapa nisingewaambia ng’oo” Fernanda akawaza lakini mawazo yake yalikatishwa baada ya mlango wa kile chumba kufungulia/ Akatangulia mwanaume mmoja aliyevaa tisheti iliyombana iliyochora kifua chake, akiwa kavalia na suruali ya kadeti, kisha akafuatia mtu aliyevalia suti ya kijani iliyomkaa vyema uso wake ukiwa nyuma ya miwani ya macho. Ndiye yule aliyekuwa akiongoza kikao cha siri.
“ Umefanya kazi nzuri sana. Alafu kumbe ni binti mrembo kabisa. Sasa inakuwaje binti mrembo kama huyu kujiingiza katika kazi za hatari namna hii?” Mtu yule akasema huku akisogea karibu na kitanda alichokuwa amelazwa Fernanda.
“ Embu washa taa nimuone vizuri” Yule mtu akasema na jambo hilo likafanyia, nuru ya taa ya umeme ikakijaza chumba chote na kuimeza nuru ya taa ya sola.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment