Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

MASHARIKI YA MBALI - 4

   

Simulizi : Mashariki Ya Mbali

Sehemu Ya Nne (4)


Kofi! Paaap! Likatua katika mgongo wake kabla hajapokea teke lililoizoa miguu yake akatua chini kwa fujo matako yakitangulia. Puuh!

“You is a very thief man si ndio. Utakiona leo” Askari yule akajitutumua hata aseme kisemedari. Sijui kipi kilimsibu hata apayuke hivyo.

Kupinga kwa vitendo ile dhana ya ajira ya uaskari nchini Mashariki ya mbali ni kwa waliokimbia umande?

Sijui! Anajua yeye….

Pole kwa mwalimu aliyepoteza muda wake kumpigia kelele katika somo la lugha hiyo ya kisemedari.

Mwanafunzi huyu hakuna alichoambulia!


Daniel alikuwa amepigwa bumbuwazi, asiamini kuwa muda si mrefu alikuwa anatua uwanja wa ndege na kupewa vyeo vya kuitwa hadi profesa. Sasa ameangukia katika kesi ya wizi.

Yule mama muibiwa simu alikuwa anamtazama Dany kwa jicho la chuki sana, asiamini kuwa bwana yule nadhifu mwenye ngozi laini kabisa iliyobeba weusi wake vyema alikuwa amekaribia kuimiliki simu ile kwa njia za wizi.

“Mimi sijafanya kitu kama hicho kaka.” Alijitetea.

“Nani kaka yako schupidi wewe. Sina kaka mwizi mimi!” akafoka yule askari, kisha akambutua teke kali la mbavuni.

Daniel akapiga mayowe. Watu wakashangilia.

Ni nini hiki?

Akajigalagaza, hakuna aliyemuonea huruma. Kila aliyepita alikuwa amejikita katika shughuli zake.

Akabebwa mzobemzobe hadi mapokezi. Akaandikisha jina lake na alipoanza kupekuliwa akakutwa na pesa za Semedari pamoja na za Mashariki ya mbali vyote hivi vikiambatana na pasi ya kimataifa ya kusafiria.

“So you my friend come zea from Semedari to thief?” yule askari ambaye haifahamiki kama kuna kitu alivuta kikawa kinamwaminisha anaongea kisemedari sahihi. Wakati anazungumza haya alikuwa anahesabu zile pesa.

Zilikuwa za kutosha kununua simu mpyampya aina ya ile anayosadikika kuwa ameiiba kwa makadirio. Simu mia moja na ushei.

“Mimi sijaiba chochote jamani, nd’o kwanza nimefika nchini kwangu baada ya miaka mingi.”

“Si ni nyie mliotoroka baada ya kufumaniwa mkiuza sukari na sabuni kwa njia za magendo. Kwa hiyo nyinyi ni wasaliti wa taifa hili la Mashariki ya mbali.” Askari mwingine aliyekuwa pale mapokezi akadakia.

Hili la kuondoka kimagendo lilimbabaisha Dany, ni kweli hakuondoka kwa njia halali. Na ni kweli aliondoka wakati huo sukari na sabuni zikiwa ni bidhaa za anasa sana nchini Mashariki ya mbali.

“Kijana mdogo kama wewe unaweza vipi kumiliki pesa nyingi kiasi hiki? Unafanya kazi gani?” alihoji askari aliyekuwa amejikita katika kuendelea kuhesabu zile pesa.

Alikuwa anazishangaa!

“Aaahm! Sina kazi ila…. Ila hii pesa nimepewa nilipotoka.” Alijiumauma.

“Kwa hiyo walikupa hii pesa ili uje kuhujumu tena nchi yetu…” sasa kesi ya kuiba simu ilikuwa imepotea na mahakama rasmi ilikuwa imefunguliwa katika kituo kidogo cha polisi. Askari ambaye hajui hata ladha ya darasa la sheria analazimisha kumweka mahakamani mtuhumiwa.

Mtuhumiwa sio mshtakiwa…

“Haya wewe mama tunafanyaje sasa, maana supu yote imeisha tumboni kwa hii shughuli yako” askari anayejizeesha sura yake kwa kukunja ndita alimweleza yule mama.

Bila kusita mama yule akatoa tabasamu, kisha akatoa senti kadhaa akampa yule askari. Bila hata kuhesabu naye akampatia ile simu akaondoka zake.

Hiki kitu kikamduwaza Daniel, yaani askari amefanya kazi yake ambayo inamuingizia mshahara halafu hapohapo mlalamikaji anamlipa pesa kwa kutimiza wajibu.

Wapi tunaelekea? Alijiuliza huku akiutazama mkanda katika kiuno cha yule askari.

Bendera ya taifa katika kiuno cha mla rushwa.

Huzuni.


Hakujua kuwa ule usemi wa mwenzako akinyolewa zako tia maji bado unaishi!!

Daniel akatupwa rumande kimasihara kabisa.

Karibu tena Mashariki ya mbali Daniel!

Tukio lile ni kama lilimweleza haya.

____

Wakati Daniel anaingizwa mahabusu, upande mwingine katika gereza la mahabusu alipokuwa amefungwa Danstan lango lilifunguliwa, Danstan akafungwa macho yake kwa kitambaa cheusi, akafungwa mikono yake kwa kamba ngumu, akapakizwa ndani ya gari na kuelekea asipopajua na hakujua wanapanga kumfanyia nini tena cha maudhi.

__________


DANIEL KATUNZI mikononi mwa polisi…. Je ataweza kutimiza azma yake iliyomrejesha Mashariki ya mbali?

cherry yupo wapi

Nini hatma ya Danstan pia…




Kuwa hai nd’o sababu kubwa ya kufa, kuugua nd’o mitihani ya kuishi. Kufaulu ni kuliliwa na walio hai kwa sababu ya wema wako.



Kule kuzurura kwake usiku kulimpa nafasi ya kulisanifu jiji la Fununu vyema. Lilikuwa na upya wake mwingine.

Hapakuwa na dalili ya watu kulala, ama la walikuwa wakifanyiana zamu kulala. Wengine walinyoosha mbavu zao mchana, na hawa sasa nd’o wamegeuka popo usiku huu.

Mabanda ya chakula hususani viazi vya kukaangwa yalikuwa wazi na wateja walikuwa si hapa.

Mabasi ya abiria yaliendelea kuita abiria, japokuwa yalikuwa tupu lakini hayakukosa kabisa abiria. Waliingia mmoja baada ya mwingine.

Vibanda vidogovidogo vilivyokuwa na bidhaa chache vilileta nuru barabarani, kumbi za michezo ya kubahatisha ilisheheni vijana lukuki. Walitokwa jasho katika mbanano ndani ya maduka hayo ya michezo ya bahati nasibu.

Hawakuonekana kuwa na dalili yoyote ya kutaka kuondoka, njia pekee ya kuondoka ni muda wa kufunga maduka yale.

Wengi wao walikuwa katika riadha ya kuisaka miaka kumi na minane ama chini ya hapo.

Wanaishi na wazazi kweli? Alijiuliza Daniel huku akiendelea kusonga na njia. Macho yake yakiangaza bango litakalomwelekeza pahali pa kuweza kupata huduma ya maradhi.

Hatimaye akalisoma bango lililomweleza nia yake.

Akalifuata pasi na kuwa na haraka yoyote huku akitembea kwa tahadhari kubwa mno.


Huko alikutana na rundo la akina dada wakiwa katika biashara ya kuuza miili yao, kwa bei isiyokuwa rasmi.

Ni wewe na uwezo wako wa kubembeleza bei.

Walipomwona akiwa katika ileile suti yake ya kuvutia walianza kumpapatikia.

Hawakutofautiana sana na wale madereva wa taksi uwanja wa ndege, tofauti ilikuwa moja tu.

Hawa walifunua bidhaa zao na kuzinadi kwa madaha wakati wale madereva walinadi magari yao kwa kusihi.

“Kwanini wasiolewe?” Daniel alimuuliza muhudumu wa ile nyumba ya kulala wageni iliyokuwa jirani na eneo lile la mauzo.

“Wewe umeoa kaka?” yule binti alijibu swali kwa njia ya kumswalika tena Daniel.

“Aah! Mimi badobado.”

“Na wenzako husema hivyohivyo, sasa unataka hawa waolewe na miti ama mbwa koko waliokosa makazi? Eeh!” alijibu huku akimkabidhi funguo za chumba.

“Nyie mabazazi mmekalia kutuongopea tu, kabla hamjafanikiwa kuzichoropoa nguo zetu hamuishiwi mashairi ya kututangazia ndoa. Mkishazifunua mnageuka mbogo. Hebu nipishe kule…. Kalaze korodani zako huko babuwee!” alifoka dada yule.

Jibu lile lilimtosha kabisa Daniel hakutaka kuuliza tena.

Aliingia chumbani kwake, akazivua zile nguo zilizokuwa zingali na masalia kidogo ya manukato.

Akaingia maliwatoni na kujikosha mwili wake ipasavyo kabla hajalala fofofo.

___________


KILICHOMTOA katika usingizi mzito ni kelele za watu wazima chumba kilichokuwa mkabala na kile alichokuwa amelala usiku ule.

Alijikaza asiyafumbue macho yake lakini kelele zilizidi akaamka.

Sauti zilikuwa zimepamba moto, yalikuwa ni mabishano makali mno.

Mwanga ukamkaribisha ulimwenguni tena, tayari palishakucha na lile eneo ambalo usiku akinadada hujiuza, ni sehemu ya kuuzia magazeti.

Wana mashariki ya mbali walikuwa wakibishana kwa juhudi zote huku wakiwa mbele ya meza ile ya magazeti.

Hawa walibishana michezo, wale wakarushiana vijembe vya kisiasa. Wengine hawakuwa na uchaguzi lolote wanarukia.

Na kama ilivyo ada, wakimaliza wanaondoka zao pasi na kununua gazeti.

Daniel Katunzi, akajinyoosha kivivu kisha akainuka na kuingia maliwatoni. Akakoga tena kwa mara nyingine kuuweka mwili wake sawa.

Akalifungua begi lake na kuchagua nguo iliyoendana na hali ya hewa ya joto iliyolikabili jiji la Fununu. Akaitazama saa yake ilimwelekeza kuwa tayari ilikuwa ni saa tatu asubuhi.

Azisondeka zile nguo chafu pahala pake, kisha akajiondokea.

Kituo cha kwanza kikiwa katika kile kijiwe cha magazeti pale nje.

Akapitia habari mbili tatu pasi na kuiona tena habari ya zungu la unga.

Habari kuu iliyomrejesha nchini Mashariki ya mbali na sasa yungali katika jiji la Fununu. Jiji ambalo analikumbuka vyema, lilikuwa ni jiji lake la mwisho kuishi kabla hajaikimbia nchi na kufanikiwa kufika Semedari.

Akajaribu kudodosa kwa muuza magazeti ikiwa ana gazeti ambalo lina picha ya kumtambulisha zungu la unga.

Muuza magazeti aliacha kuyapanga magazeti yake akamtazama. Ulikuwa ni mshangao wa aina yake, hakutarajia swali kama lile kutoka kwa mteja.

Kwa sababu tayari waziri alikwishalitolea ufafanuzi kuwa hatua za kiintelejensia zinaendelea ili kuwabaini wengine hivyo hakuwa tayari kuionyesha picha yake.

“Sasa nanyi mnaamini vipi kama kweli kuna kitu kinachoitwa zungu la unga kama hakuna ushahidi?” aliuliza bila kumlenga yeyote.

Wale wasiokuwa na upande wa kujenga hoja wakaichukua na hii.

“Wasanii wakubwawakubwa wamewekwa ndani. Yaani watu na pesa zao wamelala mahabusu we unasema nini bwana. Serikali ya safari hii haina mchezo ati!” alizungumza kwa majigambo kana kwamba anahusika katika oparesheni anayoizungumza.

“Je? Kama wameonewa ili serikali ionekane inafanya kazi japo si kweli?” aliuliza Daniel huku akiachia tabasamu hafifu la kumsanifu aliyemjibu.

Kimya! Akakosa cha kujibu.

“Tatizo wewe bado mdogo sana, hauna hata mdogo wako aliyepatwa na madhara ya madawa ya kulevya na bange. We, endelea kuwatetea ipo siku yatakukuta nd’o utajua sasa kama serikali ilikuwa inawaonea ama la.” Mzee mwingine pembeni alivamia mada akiwa katika kulaumu.

Kuwatetea? Sasa mimi nimewatetea wapi? Alijiuliza Daniel na katika nafsi yake akakiri kuwa Mashariki ya mbali bado ni ileile yenye lundo la wananchi wasiojua kujenga hoja na kuzitetea. Ukiwazidi wanahamia katika malalamiko yasiyokuwa na msingi.

Akajiondokea huku akiachia tabasamu usoni, moyo wake ukiwa katika majonzi


_________


MWANGA mkali ulimmulika usoni kwa muda wa sekunde kumi hadi kumi na tano. Kisha ukapotea likawa giza nene kabla ya mwanga wa kawaida haujachukua tena nafasi.

Alikuwa ameketi katika kiti cha kunesanesa na mbele yake kulikuwa na maafisa wawili wa jeshi waliotakata kwa tepe kadhaa katika mabega yao na zile zilizokosa nafasi zikitupwa katika vifua vyao.

Walikuwa wananukia vyema, naye hakuipata asilani ile harufu mbaya ya mwili wake usiokoga kwa majuma mengi.

Mbele yake alimjia binti ambaye wakisimamishwa wanaojiita warembo, hata kama hatashika chati za juu lakini atakuwa miongoni mwao.

“Hi!” akamtupia salamu huku anatabasamu.

Danstan akataka kujibu lakini koo liliukuwa kavu mno.

“Utatumia kahawa yenye maziwa, ama kahawa kavu?” akamtupia swali lile.

Danstan akastaajabu, leo hii anapewa huduma maalumu.

Kunani?

“Sitakunywa chochote!” alijibu, yule dada hakuonekana kushangaa. Akatoweka.

“Mletee kahawa yenye maziwa, mwekee sukari kiasi.” Sauti nzito ya mwanaume ikaunguruma.

“Ok! Boss!” akajibu kwa nidhamu huku akiinama kidogo.

“Mr. Danstan!” sauti ile nzito ya kiume ilimuita. Akamtazama na kuitikia kwa unyenyekevu.

“Haya unayoishi sio maisha unayopaswa kuishi asilani. Wewe sio wa huku… kuna watu wakubwa ambao wamesababisha uwe huku. Sasa tunahitaji msaada wako.” Aliendelea kuzungumza afsa yule asiyejitambulisha jina lake.

“Ni nani huyu. Mimi sifahamiana na mtu yeyote katika nchi yenu. Namfahamu Cherry tu mwanamke wangu.” Alijaribu kujitetea.

“Ooh safi kabisa. Tulidhani ametutania..”

“Nani amewatania? Yupo wapi Cherry… tafadhali nifahamisheni.” Alizungumza kwa kimuhemuhe.

“Alitueleza kuwa wewe na yeye hakuna mnalofichana na wewe ni mwanaume wa maisha yake. Ni kweli ama si kweli?”

“Kweli tupu.” Alijibu.

“Basi hatutapoteza muda katika hili Mr. Danstan. Tunapaswa kushirikiana hili nalo liweze kupita kwa amani. Au sio?” aliuliza kwa sanifu.

“Amani hii ya kunifunga bila kunieleza kosa langu? Amani ya kunichapa mijeledi na kujaribu kuniua mara kadhaa. Ni kweli hii unaiita amani?” alilalama.

Afisa yule bila kujali malalamiko yale aliendelea kuzungumza.

“Tunahitaji uwe shahidi wa kumuumbua yule kizito ambaye anakutumia wewe kuingiza dawa za kulevya nchini kwetu….. najua unashtuka sana kuona unatoka hatiani kirahisi kwa jambo linalokuhusu, lakini baada ya upelelezi wa kina na maelezo ya wazi kutoka kwa mwanamke wako pasi na kulazimishwa tumeridhika kwamba hauhusiki moja kwa moja katika uletaji wa madawa nchini Mashariki ya mbali. Kizito alikuongopea kuwa madawa haya yanaruhusiwa nchini kwetu hivyo, sio kosa lako hata kidogo. Ninaposema tusaidiane kwa pamoja na’maanisha utakapofika mahakamani utoe ushahidi ambao sisi tumekuandalia. Ushahidi uliobobea kisheria. Ushahidi utakaomtia kizito hatiani tumfunge na hii biashara ikome kabisa wewe na Cherry mrudi nchini kwenu. Ama hata mkiamua kubaki hapa kwetu tupo tayari kuishi na ninyi. Hii ni nchi ya upendo na amani.” Afisa alizungumza kwa utulivu wa hali ya juu.

Danstan hakuamini kile alichokisikia kikipikika katika kinywa cha afisa yule wa ngazi za juu mwenye afya njema ya mwili na akili.

Hayajui madawa ya kulevya yalivyo kwa kuyashika, hamjui kizito yeyote nchini Mashariki ya mbali, na mbaya zaidi anaelezwa kuwa kipenzi chake Cherry amethibitisha yote aliyosema afisa yule.

Nimepatikana! Danstan alijsemea huku akigeuka upande wa mlangoni, hapo akakiona kioo. Akaiona sura yake kwa mara ya kwanza tangu awekwe mahabusu ghafla.

Alikuwa anaelekea kufanana na fuvu!!

Alikuwa amekwisha kabisa.

Nywele zake zilikuwa chafu mno, sura ilijaa mabakamabaka na madonge ya damu yaliyovilia katika mashavu yake, yalimweka katika mfanano na kiumbe wa kustaajabisha asiyetamanisha kutazama.

“Sijawahi kuuza madawa ya kulevya. Huenda mmenifananisha.” Alijibu kwa unyonge.

Jibu lile likamkasirisha yule afsa, akamvamia na kukikamata kichwa chake akaenda naye kwa nguvu mpaka ukutani akambamiza pale huku matusi mazito mazito yakimtoka.

Damu zikaanza kumchuruzika, kilio ndani ya moyo wake kikavuma.

Moyo uliugulia uonevu!.

“Mpeleke jehanamu upesi!!” aliamrisha.

Waliokuwa na vyeo vya chini wakachumpa na kumdaka Danstan ambaye sasa damu ilikuwa imechachamaa.

Danstan alibahatika kumwona yule mlimbwende, alibaki na kikombe chake cha kahawa iliyotiwa maziwa na sukari kwa mbali.

Macho yao yakagon gana, yule binti akakwepesha.


Safari ya ‘jehanamu’ kwa mujibu wa afisa ikafuata kama ilivyoamriwa!!!

Kwanza alivuliwa zile nguo zote kama kweli yafaa kuziita nguo. Asma la!, basi ni mararumararu, akabaki mtupu. Uume wake ukikashfiwa kwa mara nyingine mbele ya wanaume wenzake waliovalia nguo zao nadhifu.

Akaongozwa vilevile pasi na kuwa na nguo, kichwani kwake akijiuliza nini maana ya jehanamu.

Lakini hakulipata jibu zaidi ya kujua kuwa kila hatua aliyokuwa anapiga ilimsogeza karibu zaidi ya kifo.

Lawama zake sasa alimlaumu malaika aliyepewa madaraka ya kutoa roho. Ina maana haioni roho yake ipo tayari kutoka, anaendaje kutoa roho za watu wasiokuwa tayari na anaipita roho yake.

“Huu ni upendeleo mkubwa sana ananifanyia malaika huyu!” Danstan alilalamika.

“Mwenyezi Mungu uwaalani viumbe hawa, wakizaa watoto wa kike wabarikie na utasa, wajaze fistula zisizokuwa na tiba. Wakibahatika kupata watoto wa kiume wabariki wazae mashoga na jamii nzima ijue, wajaze mabusha katika namna ya kutisha, hata wakipita mtaani watoto wadogo wawazomee. Walie na kusaga meno huku wakiliita jina lako kuu kupita yote na kamwe usiwasikilize zaidi ya kuwajalia mabalaa zaidi. Na utakapowapa yote haya eeh baba, niwekee kizazi changu cha kuwa shuhuda” Danstan alijifanyia dua ya chuki dhidi ya wote alioamini wanamnyanyasa.

Wakaifikia Jehanamu…… Miguu ya Danstan ikawa mizito baada ya macho kutazama kilichokuwa mbele yake.

Waja laana wale wasiokuwa na huruma wakambeba juu juu wakimshurutisha kuingia katika kikombe kile kilichoamriwa na afisa mwenye wadhifa wa juu kabisa.

Alipotua chini licha ya maumivu makali aliweza kuyasoma yaliyokuwa mbele yake.

Ni maandishi yaliyoandikwa kwa kutumia kitu kama mkaa.

Danstan, ute wa damu ukimtiririka aliyasoma.

“MATESO ya mwenye haki ni mengi na makali mno, lakini Mungu atakulinda nayo yote. Wataaibika, watafedheheka, nafsi zao zitahangaika. Eeh Mungu wanyime amani siku zote za maisha yao. Waaibike, wateseke, na vitawanye vizazi vyao visishikane kamwe”

Alipoyamaliza hayo na kiza kikatanda hata asiweze kuona kitu kingine mbele yake.




WATUHUMIWA walioshindikana hupitia magumu sana kwa sababu wanaaminika kuwa hadi kufikia kushindikana huko basi ni mikuki mingi sana waliyoweza kuikwepa hapo kabla.

Ukiwekwa katika fungu la walioshindikana basi utambue kuwa utapewa malezi ya walioshindikana. Kuanzia salamu, maradhi na hata jicho litakalotumika kukutazama wewe halitakuwa jicho la kawaida.

Watu watakaokuzingira watakuwa ni wataalamu wa saikolojia, ambao ukisema ndio wanatambua kama unaongopa ama unamaanisha.

Wataalamu hawa huweza kuchanganua na kupembua, kisha kuweka bayana nani yumo na nani hayumo. Japokuwa hawawezi kutenda haki kwa silimia mia moja. Lakini walau huikaribia asilimia themanini.


Nchini Mashariki ya mbali wale watu wenye roho mbaya za kurithi, wenye miguvu mingi kuliko akili katika vichwa vyao, wale wapenda sifa za kijinga kulikoni uhalisia. Wale waliopewa masikio lakini hawayatumii kusikiliza bali kutumika kama viegemeo vya miwani zao nyeusi.

Hawa hukabidhiwa kitengo cha kuwahoji watuhumiwa wanaotupwa katika kundi la walioshindikana.

Na siku zote mwili ukiizidi nguvu akili basi kifuatacho hapo kitakufurahisha wewe pekee lakini hautakuwa sahihi.

Ni haya yalitokea na yanaendelea kutokea nchini humo. Nchi ambayo mshitakiwa ukilalamika chakula ni kibovu, basi wewe unawekwa kundi la walioshindikana.

Danstan akatupwa katika kundi hili, wakamuita jina la ‘MAFIOSO’ ama kwa lugha za kigeni ‘Mafia’.

Mafia yupo tayari kuukata ulimi wake ilimradi tu asitoe siri yoyote ile itakayowaathiri wenzake, na kabla ya kuiva kabisa na kuwa mafia huwa wanapitia suluba kali sana, hivyo akikamatwa kinachofanyika ni marejeo tu.

Hatavujisha siri na atakuwa tayari kufa peke yake.

Danstan asiyejua mbele wapi na nyuma wapi, akajikuta anatajwa kama mtu hatari zaidi kuliko mahabusu wote katika jumba la gereza alilokuwa akishikiliwa. Kisa tu alisema hajawahi kuyaona madawa ya kulevya.

Hivyo!


Aliyesababisha ulinzi uongezeke ni mkuu wa jiji la Fununu, aliyekunywa maji yaliyofua bendera za chama hapo kabla, akajipendekeza kwa kulamba miguu ya viongozi waliporidhika kuwa bwana huyu ni kibaraka mashuhuri wakampatia majukumu ya kuutawala mkoa.

Sahau kuhusu kuuongoza!

Alipewa autawale.

Hakuwahi kupitia mafunzo yoyote ya kijeshi, lakini hiyo siku akaketi na wanajeshi wenye tepe zao waliopitia suluba ya kuwa katika shughuli za kijeshi. Akawa kama anayewafundisha kazi.

Akawatoa wote akili na akabaki yeye pekee kuwa na akili timamu, akawaeleza kuwa Danstan ni ‘mafioso’ hatari sana na wakifanya mchezo anaweza kuwabadilikia na kuwateketeza wote kwa pamoja. Akafikia mbali na kutaja hadi vikundi vya ki-mafia alivyopitia.

Alivijulia wapi?

Usiulize swali hilo na ubaki salama.

Akawaamuru wambane zaidi ili aseme ukweli, yumkini kuna wenzake bado wanarandaranda katika viunga mbalimbali nchini Mashariki ya mbali.

Akamaliza kutema mashudu yale akasimama, na wao wakasimama upesiupesi kwa heshima zote wakampigia saluti bwana yule asiyekuwa na akili yoyote zaidi ya kupenda sifa.

Sifa za kijinga.


Alipotoweka, kiti chake akakichukua aliyekuwa na vyeo kuwapita wenzake. Huyu alikuwa na akili hapo zamani. Lakini siasa zilivyopenya na kuingia katika jeshi la wananchi zikapeperusha akili yake.

Kwa kuutetea ugali wake huyu akatoa shauri la kumbana Danstan hata kumlazimisha atoe ushahidi wa uongo. Akiri kuwa anahusika na usambazaji na uzalishaji wa madawa ya kulevya.

Ushahidi ambao utajaza kichwa kikubwa cha mkuu wa jiji na kumfanya ajione alikosewa adabu na wasahihishaji wa mitihani yake ya kumaliza vidato alipoambulia sifuri moja isiyokuwa na mwenzake.

Mjinga na mjinga mwenzake!

Mazao ya ujinga ule yakamwangushia Danstan dhoruba.

Akaanza kutajiwa mambo ya ajabu ajabu asiamini kuwa wanaofanya vile ni wanadamu. Anapewa kahawa ya maziwa yenye sukari kwa mbali ili akiri kuwa anauza madawa ya kulevya. Ahukumiwe kunyongwa.

Ugumu aliouleta Danstan ukawapandisha mori maafisa wale. Amri ikatoka atupwe jehanamu.


Alisindikizwa na teke kali, kabla lango halijafungwa na kutawaliwa na kiza kinene.

Maneno ya mwisho aliyoyasoma yalimweka katika tafakari nzito sana. Tafakuri katikati ya maumivu makali.

“MATESO ya mwenye haki ni mengi na makali mno, lakini Mungu atakulinda nayo yote. Wataaibika, watafedheheka, nafsi zao zitahangaika. Eeh Mungu wanyime amani siku zote za maisha yao. Waaibike, wateseke, na vitawanye vizazi vyao visishikane kamwe”

Akavuta taswira, ni nani aliyesukumwa katika chumba kile hata akaweza kuandika maneno yale yenye ukakasi wa kiwango kile.

Akaachana na huyo aliyeandika, akajiuliza tena juu ya mwenyezi Mungu.

Akamuuliza Mungu iwapo yule bwana aliyeandika maneno yale aliweza kupona? Maana kwa maandishi yale alitangaza kudhulumiwa.

Mara akapata jibu.

“Wala Mungu hakumuokoa. Mbona aliomba wafedheheshwe lakini wanazidi kunenepa na wanazidi kucheka, aliomba nafsi zao zihangaike. Mbona hakuna wanachohofia katika maisha yao? Aliomba uwanyime amani…. Mbona wana amani kubwa sana wanaisukumia kwa mchanganyiko wa kahawa yenye maziwa katika viti vya kuzunguka”

Chozi la uchungu likaserereka katika bufuru la Danstan na kutua katika sakafu ile kavu, iliyolilia maji mpaka ikachoka na sasa imezoea. Ghafla inapata unyevunyevyu wa chozi.

Ikayameza upesi na kuyangoja mengine!

Yalikuja tena na tena lakini hayakutosha.


Madonda ya tumbo yakabisha hodi, subira ilifika kikomo.

Tumbo likaanza kumkata Danstan. Akalia kwa sauti kuu, lango likawa makini likaidaka sauti na kuizima palepale bila kuruhusu angalau mwangwi urejee katika masikio ya Danstan.

Baada ya kuita sana, sasa akawa anaunguruma mithiri yap aka aliyekabwa na fupa lisilomezeka.

Masulupwete katika mwili wake yakawa mzigo. Akayatoa na kubaki mtupu.

Akili yake ikiwa imesahau kabisa ni kwa nini paliitwa jehanamu katika chumba kile.

Tumbo lilipopoa, maana ikabisha hodi.

Lilianza kama joto la kawaida, likaanza kuongezeka kwa kasi mithiri ya jua lililoshuka sentimeta moja chini zaidi.

Joto likawa joto, hana masulupwete katika mwili wake. Ataondosha nini kingine kukabiliana na hali ile.

Jasho likaanza kumtoka kwa wingi, kuna mvuke ulikuwa unapenya na kuingia katika chumba kile.

Kufa hakufa, alibaki kupumua huku cha moto kikiishi naye chumba kimoja.

Alikuwa anapata mlo mmoja tu kwa siku, kikombe kimoja cha uji. Hakupata fursa ya kuona mwanga, hakupata kusikia sauti ya mtu.

Hakupewa nafasi ya kuosha mwili wake.

Mzungu alikuwa amepatikana.

Siku saba za moto!

Siku ya nane akatolewa akiwa amefungwa kitambaa cheusi usoni. Akaongozwa kwa kubebwa mzobemzobe hadi walipohitaji wao. Hakufunguliwa kitambaa.

Na kwa mara ya kwanza akaisikia sauti.

“U muumini wa dini gani?….”

Akajaribu kuongea sauti haitoki, alikuwa na kiu kikali mno.

“Naomba maji!” akajitutumua akazungumza.

“Huna haja ya kunywa maji, hapa unapaswa kuchagua moja. Mwanadamu u mavumbi na mavumbini utarudi ama, Kullu nafsin zaikatul maut!” alizungumza kishujaa.


Hatimaye nazikwa nikiwa hai! Alijisemea kinyonge kabisa Danstan!

“Kama alivyonikanya Daniel” hilo likawa neno la mwisho kumtoka

Na hata kabla hajauliza kama anapaswa kujifanyia sala yake ya mwisho. Alisukumwa na kutua katika lile shimo, akichubuka vibaya sana. Na hakuwa naona lolote.

Alitupwa kama mzoga. Mzoga usiofaa!

Lakini hakuwa mzoga…..

Pua yake ikatangulia chini, kitambaa kikaendelea kuyaziba macho yake.

Haikuwa ndoto alikuwa yungali kaburini kwa sababu ya akili ndogo, zilizofunikwa kwa ukungu wa upumbavu juu yake.

Looh! .


Haya sasa, mambo si mambo ndani ya MASHARIKI YA MBALI…..

Unazikwa ukiwa hai….. wanaokuzika wanachekelea…..




MJOMBA MACHACHE ANASIMULIA.


Hadi sasa sielewi kosa langu kuu zaidi lilikuwa lipi. Najiuliza tena na tena na bado silipati jibu la uhakika.

Wale watu walitumwa kunikomesha ama nini kiliwasibu?

Watumwe kunikomesha mimi kwa kosa gani zaidi? Ama kwa sababu mimi ni nani. Maisha yenyewe nilikuwa naishi ni ya chumba kimoja tu, ndani ni vitu vichache vya msingi ambavyo hata mwivi akinijia anaona haya kuvichukua.

Nguo chakavu, kiredio kidogo kinachoelekea umauti wake, godoro la pamba zito kubeba kuliko wepesi wa bei yake.

Wachukue wapeleke wapi? Godoro ambalo hata ukitoa msaada kituo cha watoto yatima wanasema asante ya kutimiza wajibu.

Walinijia asubuhi majira ya saa moja na nusu nakumbuka nilitazama saa yangu ya mkononi.

Wakajitambulisha kuwa wao ni wanamgambo na wapo pale kwa ajili ya kufahamu mimi ninatupa wapi takataka zangu, kwa sababu majirani wamelalamika kuwa kuna mtu ambaye badala ya kuzipeleka takataka jalalani anazitupa katika vibaraza vyao. Na mashaka yao ni juu yangu.

Nilishtuka sana! Sipiki nyumbani kwangu, wake zangu halali ni mama lishe wanaonipikia kila siku huko barabarani.

Takataka nazitoa wapi mimi?

Wakaniuliza lipo wapi debe langu la kutupia taka, nikawajibu huku natabasamu kuwa mimi ni ‘bachela’ tu bado sina hata mke.

Jibu lile likawa kikwazo kwao, wakabwatuka kuwa wao hawakuja kujua yu wapi mke wangu? Wanataka kujua wapi ninapotupa takataka zangu.

Nikawaeleza kuwa sina sehemu ya kutupa takataka, kwa sababu sinazo hizo taka.

Wakanicharukia na kunieleza kuwa napaswa kulipa faini shilingi elfu ishirini. Na ninatakiwa kutoa shilingi elfu kumi ya ziada ili nisajiliwe rasmi katika daftari la jalala la mtaa ambapo nitaweza kuwa natupa taka zangu.

Mjomba!! Nilistaajabu sana, wanamgambo wale walikuwa wanatema maneno ya ajabu sana kwangu. Yaani nikawafungulia mlango ili watazame huo uchafu mimi nautoa wapi. Wakaliona jiko la stovu, maarufu kwa jina la ‘mchina’.

Hapo ndipo hasira zao zikapanda maradufu, wakasema nimewaona wao wajinga nawaambia kuwa sipiki.

Nikajaribu kuweka lugha sawa kuwa mara mojamoja huwa najichemshia chai. Na chai haina uchafu wowote wa kutupwa kwenye nyumba za majirani.

Hawakutaka kunisikiliza, wakaniamuru niufunge mlango wangu na twende mguu kwa mguu hadi serikali za mtaa ama la niwalipe fidia yao waondoke zao.

Mjomba! Elfu ishirini?? Nimpe mwanaume mwenzangu tu ghafla! Nadhani unanijua vizuri mjomba wako, sipendi kuonewa hovyo! Nikawadindia nikisimamia kidete kauli moja kuwa sina kosa lolote na si mimi ninayetupa uchafu popote wanapolaumu majirani.

Balaa likazuka, wakaitana wakafika wanamgambo wapatao sita. Wakaibadilisha kesi na kusema kuwa nimewatishia amani.

Mjomba!! Nikageuzwa asusa, wakaanza kunipiga mbele ya mlango wa chumba changu, wengi wamenikamata miguu na mikono. Mwingine akinitwanga na rungu kama mwanadamu auaye nyoka.

Hebu fikiria mjomba, mtu anapiga mwanadamu mwenzake hadi anachoka anamwambia mwenzake amsaidie.

Huo ni mwili wa mtu wanapiga!

Mtu huyo ni mimi mjomba. Wakanitwanga miguu ipasavyo, wakanipiga mateke mbavuni na kila mara wakijinadi kuwa wao ni serikali.

Sipaswi kucheza na serikali!

Nilipigwa hadi nikawa nahisi kichefuchefu lakini siwezi kutapika, natamani kutukana mama wa mtu kwa mara ya kwanza katika maisha yangu lakini sauti hainitoki. Koo limekauka mjomba najiona yuleee nakufa.

Siwezi kusema, siwezi kulia siwezi kujitetea. Wanaume wale walioikosa shilingi elfu ishirini wameamua kuniua.

Baada ya kunilainisha ipasavyo nikiwa nimepasuka vibaya vibaya, hawakuniacha pale. Wakanibeba juu juu huku wakinitunuku matusi ya kila namna.

Nikaishia kutupwa mahabusu.

Sikujisemea wakanisemea wao kuwa mimi ni mwizi niliyejaribu kuwaponyoka.

Polisi wakanipokea kwa makofi mazito yaliyonipa zawadi ya kuona nyotanyota zisizovutia.

Nikatupwa katika kaburi lile wanaloliita mahabusu.

Niliwahi kukutana na kifo mjomba, kikaniuliza kama kiishi nami daima ama kiniache niishi kidogo peke yangu. Nilitamani kukieleza kinichukue, lakini sauti ipo wapi ya kusema haya. Kifo kikajiondokea zake kikiniacha mahabusu nikiteseka.

Niliachwa pale kwa siku tatu, miguu yangu ikiwa imekufa ganzi kabisa. Siwezi kusimama ninajiburuta. Nikijiburuta wanasema najidekeza.

Nitazame sasa mjomba, nadeka mpaka sasa. Mabaradhuli wameuondoa uwezo wangu wa kutembea! Wameondoa hata ile hadhi yangu ya kuwa mwanaume mjomba!

Wamenidhulumu kila kitu!

________


Mjomba Machache akashindwa kuendelea kuzungumza akaanza kulia kilio cha kwikwi. Daniel Katunzi akambembeleza huku na yeye machozi yakimbubujika. Alikuwa ameusikiliza mkasa wa mjomba wake, na kuikumbuka sauti ya hayati mama yake mzazi ambaye pia alinyanyasika hadi kufikia hatua ya kuuondoa uhai wake kwa kitanzi.

Huyu hapa kaka wa mama yake, naye amepotezewa uwezo wake wa kutembea.

Washenzi wameithaminisha miguu ya mjomba wake kwa shilingi elfu ishirini za mashariki ya mbali.

“Serikali haikuingilia kati suala hili?” Dany akajitahidi kuuliza.

“Wasiingilie kati kwanini? Waliingilia kati vizuri kabisa. Wakawasisitiza askari polisi waifanye kazi yao vizuri zaidi, na sifa kubwa zikienda kwa wale wanamgambo kwa kunidhibiti. Ikabaki kidogo sana mimi kwenda gerezani kwa sababu za wizi. Mungu si wao Mungu si mimi! Akaniepusha na hilo. Msamaria aliyeifanya kazi hiyo ya Mungu kwa kuniepusha na balaa hilo ndiye aliyenisaidia namna ya kurejea huku kijijini.

Sitaki kusikia kuhusu mji wa Fununu.

Lakini licha ya kuukimbia mji ule nikakutana na karaha nyingine kubwa tena huku kijijini. Nikakutana tena na hao mgambo wamesambazwa na huku, wamekuja na upuuzi wao mwingine. Wananiona kabisa kuwa siwezi kutembea ninajiburuta, lakini wananilazimisha niwe kwenye zamu ya kulinda usiku. Wakauita mkakati wao, ulinzi shirikishi.

Mimi nalinda nini mjomba, wakati hata mbwa kwa sasa ananidharau kwa sababu tunalingana ufupi angali yeye ananizidi mwendo? Mimi nalinda nini?

Hutaki kulinda unapaswa utoe pesa ya ulinzi.

Mjomba mimi kulinda siwezi kutoa pesa siwezi. Nizitoe mimi nazipata wapi?? Haka kagenge shangazi yako huyo nd’o anabangaiza tunapata kutia kitu kinywani. Hiyo pesa ya ulinzi aitoe wapi?

Sijui hata hii tunayoiita serikali inawatazamaje watu wasiojiweza kama mimi. Hiki kiburi cha uzima kimetapakaa kutoka kwa viongozi wa juu hadi hawa wa chini.

Mtu anakusimamia na kirungu chake anasema atakupiga hadi utasimama wima, anakupa matusi yote ya nguoni.” Akasita baada ya kukatishwa na Daniel, “Sasa mjomba watu kama hao ni kuwakariri sura zao na kwenda kuwashtaki usiwaonee huruma”

Mjomba Machache akacheka kidogo kisha akaendelea, “Kwa sasa kila kitu ni lazima kujuana, hadi hawa wanaojiita mgambo wa kijiji. Hiyo nafasi waliyopo wameipata kwa sababu wanajuana na mtu katika serikali ya kijiji. Hivyo wanakula rushwa pamoja, wanatunyanyasa wanakijiji pamoja, kwanini katika kuwashtaki wasikae pamoja na kukugeuzia kesi wewe mwenyewe ama la wakupotezee muda wa kujiburuta kila siku kwenda serikali za mitaa pasi na mafanikio yoyote. Wanakuchora tu.” Mjomba machache akatulia akamtazama Daniel Katunzi machoni kisha akampa swali la ghafla.

“Umerudi kufanya nini huku jehanamu mjomba wangu!!”

Swali lile likamteteresha kidogo Daniel, hakuwa amepanga kujieleza nia yake mapema kwa mjomba wake. Alihitaji kupanga namna ya kufanya uwasilishaji wake.

“Nimekuja kupalilia kaburi la dada yako na pia kukujulia hali wewe mjomba na mama yangu uliyebakia ulimwenguni!!” alijibu huku akiwa analazimisha tabasamu.

“Kaburi gani? Lile tulilochimba kule ng’ambo?”

“Kwani mama yangu alizikwa makaburi mawili mjomba?” aliuliza kimasikhara.

“Matatu!” alijibu mjomba kwa ufupi.

Daniel akataharuki. Akidhani mjomba anafanya mzaha.

“Hii serikali ya sasa ni chungu sana, usijaribu kuilamba maana uchungu wake haupoi hata uilambie asali. Serikali hii ukifa ni nafuu kwao, haina kitu kinaitwa upendo kwa waliotutangulia. Wanaoongoza serikali hii wanaishi maisha kana kwamba wao hawatakuja kuzikwa, wataishi milele. Mashariki ya mbali imepoteza ile sifa yake kuu ya upendo iliyokuwa ikivuma kona mbalimbali za ulimwengu.

Yaani kisa kuna kibopa kawajaza mamilioni huko, wakaamua kuikashfu miili ya marehemu. Wakatangaza ndani ya mwezi mmoja kuwa eneo la makaburi linahamishwa hivyo watu waliohifadhi ndugu zao wafike makaburini, wakaitaja siku maalumu kuwa miili itafukuliwa na utapatiwa kipande cha sanda kwa ajili ya kufunga mabaki ya mwili wa marehemu. Kisha utapewa maelekezo ya pahali pa kwenda kumzika upya.

Mjomba hebu tuachane na hii habari, iliniumiza mno mjomba wako. Ilinitia uchungu nikautamani utajiri, na hii ni sababu mojawapo ya kukimbilia mji wa Fununu kwenda kuuchukua ulemavu wangu huu. Nilienda kule kwa ghadhabu ya maisha.

Unajua ni kiasi gani nilimpenda dada yangu! Leo hii anafukuliwa, wananipa hovyohovyo tu mabaki ya mwili wake. Nililia mjomba nililia sana……. Achana na hii habari mjomba, nakuomba sana acha kabisa. Wakamaliza wakatupooza kwa shilingi elfu mbili za nauli. Elfu mbili mjomba! Sio elfu mbili ya huko ulipotoka, ni ya hapa kwetu isokuwa na thamani yoyote.

Upuuzi! Dharau! Matusi!

Hakika walituweza.

Walivyoutambua udhalimu wao, hawakuruhusu hata picha moja kupigwa eneo lile la makaburi.

Mwekezaji akaligeuza eneo la makaburi kuwa mashamba, akafanya utafiti akaona panafaa kwa korosho.

Akawekeza!

Baada ya miaka majibu yakatoka.

Muwekezaji sasa anavuna korosho zake kwa kutumia mbolea ya miili ya wanakijiji waliotangulia mbele ya haki, akiwemo dada yangu!

Katika mashamba yaleyale wakatangaza neema kwa wanakijiji kwenda kujipatia ajira. Wanapita mtaa kwa mtaa wakitangaza fursa ile waliyoiita ya kipekee kwa wanakijiji.

Nilikataa kwenda kuvuna zao lililotokana na rutuba ya mwili wa dadangu.

Nilikuwa tayari kubaki maskini hata nife na umaskini wangu, sio kuvuna juu ya shamba lile.” Mjomba akaanza kulia tena. Safari hii kilio kikubwa kuliko cha awali huku akilitaja jina la marehemu dada yake ambaye ni mama mzazi wa Daniel.

Getruda Mazengo Katunzi.


Hakuwepo wa kumbembeleza kwa sababu Daniel alikuwa anaomboleza huku akiiuma midomo yake na kuiachia. Alimlilia mama yake!

Alilia kwa sababu mwili wa mamaye haukuachwa upumzike walimnyanyasa angali akiwa hai, uchungu ukamuelemea akakubali kushindwa akawaachia dunia yao, hawakuridhika wakamfukua tena na kuunyanyasa mwili wake uliopumzika.

Msiba ukaanza upya, hasira ikajikita mioyoni.

Daniel akaapa!



Danstan anapewa huduma bora kabisa ili kurejesha afya yake, haya yakiwa ni maandalizi ya kwenda mahakamani.

Kukiri kuwa anahusika na uuzaji wa madawa ya kulevya.

Akiwa katika matunzo maalumu, unatokea wito wa ghafla.

Anaandaliwa na kusisitizwa kuwa ikiwa swali halielewi basi jibu ni SIJUI.

Danstan anakaririshwa anachukuliwa na kutangulizwa mbele…



Wanaingia katika chumba kikubwa kilichokuwa kimepangwa katika mfumo wa kupendeza. Ilikuwa ni sebule ya kisasa sana.

“Keti!” akaamrishwa, kwa sauti iliyopoa ya kamanda aliyemsindikiza.

Baada ya dakika tatu za kusubiri. Akaingia mwanaume aliyehifadhi kitambi kidogo panapo tumbo lake. Kitambi kisichokuwa mzigo.

Vazi lake la suti lilipunguziwa koti, hivyo alibaki kuwa mwanaume aliyechomekea shati lake vyema katika suruali iliyonyooka.

Hata Danstan alikuwa amevaa suruali na shati, yeye pia alichomekea.

Tofauti ilibaki kuwa moja tu, Danstan alichekesha angali mwenzake alipendeza sana.

Danstan aliyekuwa anamuhofia kila mtu, alisimama na kumsalimia kwa heshima zote.

Yule bwana mwenye kichwa kikubwa kilichobeba lundo la nywele akaitikia kwa madoido, kisha akamruhusu aketi!

Wakawa wanatazamana!

“Danstan eeh!” Bwana Yule akalinukuu jina la Danstan katika karatasi zilizokuwa mbee yake.

Danstan, akaitika kwa nidhamu. Almanusura amsalimie tena…

Bwana yule akajikuna kichwa chake, kisha akaendelea kuzungumza.

“Umefika kwa mara ya kwanza mwaka gani nchini Mashariki ya mbali?”

“Hii ni mara yangu ya kwanza mkuu.”

“Ulifikia kijiji gani? Na mlikuwa wangapi?”

“Silikumbuki jina la kijiji nilichopita, na nilikuwa mimi pamoja na Cherry.” Danstan akajibu kwa nidhamu kubwa sana.

“Sikiliza Danstan, huwezi kuwa umefika nchini kwanu kwa mara ya kwanza na unazungumza lugha hii vyema hivi. Usinidanganye. Nia yangu ni kukusaidia, kama ulihisi kuna mtu amehitaji kukusaidia hapo awali basi hajakusaidia kitu. Mimi nataka kukusaidia kwa vitendo…. Lakini nd’o ue mkweli….” Alizungumza huku anamkazia macho Danstan.

“Kwa yote niliyopitia hadi kukitamani kifo. Sina lolote la kudanganya. Hata sababu ya kudanganya pia sinayo. Mimi ni mgeni katika nchi yenu, nimeangukia katika majanga…” alijieleza kinyonge.

“Wakati ukiwa gerezani, ni akina nani walikuwa marafiki zako? Nitajie walau wawili tu!”

“Sijawahi kuwa na rafiki gerezani, nimeendelea kuwa mgeni mpaka sasa. Wanakuja na kupita bila walau kuyafahamu majina yao.”

“Hebu tuliza akili yako, hakuna rafiki ambaye majina yake mawili yanaleta ufupisho wa CD. Yeyote hataambaye jina lake lilianza na herufi C…” Alizidi kuhoji kwa kusihi.

Danstan hakujaribu kufikiri kitu chochote. Jibu lilikuwa jepesi tu. Hakuwahi kuwa na rafiki wa kufikia kujitambulisha majina. Wala kusikia jina na kulikariri.


Bwana yule alifungua kishikizo cha juu cha shati lake.

Hapakuwa na joto lakini ni kama alikuwa anamiliki fukuto lake binafsi.

Akasimama akauendea mlango, akaufungua. Akaingia chumba cha pili.

“Amesemaje?” swali kavu kutoka katika kinywa cha mwanamke.

“Inaonekana ni mkaidi sana…..” hakuweza kuimalizia sentensi yake.

“Mark! Mark! Nisikilize tafadhali, naomba jibu moja. Amesemaje?” alifoka mwanamama yule ambaye nguvu ya pesa iliutetea sana uso wake na kuonekana bado wamo.

Uzee ulikuwa unamuita!

Aliyeitwa kwa jina la Mark, akashusha pumzi kwa nguvu kisha akasema ‘hajui, hana rafiki, hajawahi kuwa na rafiki jela.”

“Basi wape jina….” Akazungumza kwa mkato.

“Darling, hatuwezi kupeleka mambo kirejareja namna hii mke wangu…”

“….. Oooh! Kirejareja sio, kwa sababu ni dada yangu. Huna uchungu naye sivyo! Haya yapeleke kijumlajumla tuone” alifoka. Akachukua mkoba wake akatoweka.

Mark! Akanyanyua simu, akabofya nambari kadhaa.

“Mrudisheni!” akaongea kwa ufupi, akakata simu.


_________________


Waliohitaji kuonana na mkuu wa jiji la Fununu, walilazimika kujitukana wao na nafsi zao. Kwani walingoja sana ofisi ifungulie bila mafanikio.

Taarifa kwa katibu muhtasi zilikuwa haba pia.

Hadi katibu muhtasi hakujua lolote.

Nini kimemsibu Muheshimiwa Mark Dunguli.

Wachache walijiuliza.

Haikuwa kawaida yake hata kidogo, alitambulika wazi kuwa ni mjivuni. Angeweza kuwa ofisini na bado utasubiri sana hadi uweze kuonana naye.

Leo hii hayupo ofisini na hakuna taarifa yoyote.

Mark! Alikuwa amebananishwa!


Alibanwa pabaya!

Ujumbe mpya kutoka kwa mkewe.

“Wamesema watamuacha afe kwa njaa,hawana maji ya kumpa anywe wala mkate wa kumlisha. Akifa watatoa msaada wa kumfukia kisha watakuja kivingine.”

Ujumbe huu ulimuumiza sana.

Akakilaza kiti katika gari lake,akajaribu kulala. Usingizi utoke wapi?

Akabaki kujiuliza aliyempiga hilo kofi zito kiasi kile alijificha wapi?

Alikuwa ameyumbishwa!

CD!

Mtumaji wa jumbe zote alijitambulisha kwa jina hilo.

Na alichohitaji ni kitu kimoja tu.

Majina mawili ya anayetajwa kama Zungu la unga.

Mkuu wa jiji akajitia ushupavu, akaamua kumuhoji Danstan moja kwa moja juu ya nasaba zake na hawa watu ambao wamezikamata korodani zake na wanazinyonga taratibu wakimwachia muda wa kupima maumivu ya sasa na yale yaliyopita.

Akiwa hajatulia baada ya kukorofishana na mkewe, wananyonga tena.

Ujumbe kutoka watokapo!

Niwatajie jina halafu! Kwamba nd’o watamuachia huru?

Waongo? Wauaji!

Loh!

Kitendo cha kuwatambua kuwa hao watu ni wauaji. Nafsi yake ikapaa na kukikalia kiti cha uoga.

Kiti kikanesanesa na kumsababisha ayaone majuto yakimnyemelea kwa kasi.

Akaikumbuka siku aliyoamua kumkamata Danstan kisha kujizolea sifa kedekede kuwa yeye ni simba wa jiji la Fununu.

Zikamjia na zile kumbukumbu za kuwasisitiza maaskari juu ya kumtesa sana Danstan ili awataje na wenzake wanaohusika katika umiliki wa ‘drug cartel’ na uuzaji wa madawa hayo.

Kichwa kisingeuma pasi na kukumbuka siku aliyomuita mkuu wa polisi nyumbani kwake, wakanywa na kula huku wakitazama runinga zikiwasifia utendaji kazi wao.

Akakumbuka uongo wote aliomjaza bwana yule mwenye dhamana ya juu katika jeshi la polisi.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG