Simulizi : Shilingi (Mwanzo Kati Na Mwisho)
Sehemu Ya Tatu (3)
Paja likauzidi ujazo mchuzi likachungulia juu.
Minyoo ikaunguruma katika tumbo la Kindo, ikasahau wema iliyotendewa na mchungaji kwa kupata ndizi mchemsho, sasa inapiga mayowe inatamani kuku.
Meza imezungukwa na wanaume watatu wa shoka. Mzee Ukindi baba mzazi wa Nyangeta, Mzee Muhando rafiki yake wa karibu na Kindo aliyemuoa binti yake pasi na kumtolea lepe la mahari.
Punde akaingia Debora, akawapatia maji wakanawa mikono.
Sufuria lililokuwa linangoja awamu yake ya kufunuliwa likafikiwa.
Ugali mkubwa wa udaga uliochanganganywa na mtama!
‘Jama jama! Mnatuchelewesha’ Minyoo ikapiga yowe tena.
Kindo anaisikiliza, anaisihi iwe na subira walau kidogo.
Wakafanya sala waliyokaririshwa na mtumishi, kisha kila mwenye kiganja kikubwa na alikate tonge lake.
Midomo inatafuna, pua inaishia kunusa tu na kupumua kwa kasi.
Hiki nd’o kitu kilichokuwa kinasikika kwa wakati huo.
Mapaja mawili yote kwa Kindo, firigisi moja kwake. Halafu anaambiwa ‘baba kula huyu kuku tumekuchinjia wewe, ukimaliza mboga ongeza’.
Kindo alikuwa anayaishi maisha ya kifalme, kama kweli mfalme huwa hajui kusoma wala kuandika na anapatikana katika kijiji cha Ulongoni.
Ugali ukashuka kwa kasi, mabakuli yakakauka mchuzi. Ukajazwa tena.
Ugali ukamalizika, wa kubeua akabeua.
“Kindo!” Mzee Ukindi akamuita.
“Baba!” anajibu huku anahema kwa shida.
“Kwanza asante sana kwa kuuitikia wito huu wa ghafla, umeniheshimu sana tena sana mkwelima wangu,”
“Nimeonelea nikuite wakati huu baada ya mkakati wa muda mrefu niliokuwa naufuatilia kuelekea kukamilika..... siku zote mimi na mke wangu tulikuwa tunaota juu ya wewe na mwenzako kuwa katika ndoa ambayo imebarikiwa kabisa. Baada ya muda mrefu wa kuvutana huku na kule, hatimaye mtumishi amekubali kuwa sasa mnaweza kufunga ndoa yenu.”
Mzee Ukindi akaendelea kujieleza kinaga ubaga, ikafikia hatua mabapo alimuita mkewe, naye akazungumza kwa furaha zote juu ya ndoa hiyo.
Hawakugusia lolote kuhusu mahari ambayo hayajalipwa hata kiduchu, na hapakuwa na swali juu ya habari nzito iliyozagaa pale kijijini.
Shilingi ya ajabu!
“Kesho hakikisha unakuja na mwenzako, tuna mazungumzo ya pamoja na kutazama maandalizi ya suala hili. Sisi hatutaki lichelewe tena, mwishowe mtumishi aje kuhairisha” Mama mkwe akamweleza wakati wanaagana. Kicheko kinaichukua nafasi
“Tutakuja mama!” akajibu kinyenyekevu.
Akajiondokea, huku tumbo likimuuliza kuwa ana uhakika kuwa yule kuku aliyezama katika tumbo lake inalingana na wito aliouitikia??
Hapana! Lilikuwa jibu.
“Kindoo!” Sauti ikamuita kwa jitihada. Akasimama, akageuka kuangaza katika giza lile ni nani alikuwa anamuita na amemuonaje.
“Mzee Muhando.... kulikoni?” Kindo akahoji, mzee huyu tayari walikuwa wameagana baada ya kula chakula cha maana nyumbani kwa baba yake Nyangeta.
Kuna lipi ambalo alisahau kuzungumza.
Anahema juu juu.
“Nimefanya zoezi la usiku usiku.”
“Pole sana.”
“Kindo bwana nikisema mimi nina maneno mengi nitakuwa muongo sana. Ninayo machache tu na sitaki kukata kona nyingi kama baba yako.”
“Mzee Ukindi?” Kindo akauliza.
“Haswaa, kuku amemfuata mjini kwa kutumia senti zake zote za akiba. Lakini tatizo haingii moja kwa moja katika lengo.”
“Lengo lipi?”
“Shilingi ya ajabu! Hakuna jingine..... achana na hayo ya mzee wako, mimi naingia moja kwa moja. Bwana Kindo, mimi ninawajua walanguzi wa shilingi naomba katika fikra zako utakapohitaji ushauri sahihi wa wapi uuze shilingi yako nakuomba unitafute. Na ninavyopenda kuwa wazi, ninakuomba tu mzee Ukindi asijue, maana ataona nimeziingilia anga zake.”
Anga zake!? Kindo alijiuliza. “Zinakuwaje anga zake wakati kinachozungumzwa ni kuhusu mali yangu?” swali jingine.
“Unazijua bei za shilingi ya ajabu?” mzee Muhando akamswalika Kindo.
“Nikienda mjini nitawauliza, atakayenitajia bei nzuri kuliko mwenzake nitamuuzia huyo. Sitaiacha shilingi yangu kwa atakayetangaza bei chee.” Kindo alijibu.
“Bei chee kwako ni sawasawa na pesa ngapi ya Tanganyika?” Muhando akamuuliza.
Kindo hajawahi kushika pesa inayoweza kuwekwa katika fungu la pesa nyingi. Atajibu nini?
“Kwani bei sahihi ya hii sarafu ni pesa ngapi?” Kindo akauliza huku akianza kuuona uzito kuimiliki sarafu ile.
“Bei sahihi ni ile namna tu ambayo utaweza kuzungumza na mlanguzi huku ukijitahidi sana kuifanya bidhaa yako iwe na thamani ya juu zaidi. Mimi katika enzi za ujana wangu nilikuwa ninaweza kumshawishi mtu akanunua jiwe huku akiamini litamnufaisha siku za usoni.” Muhando akajipeperusha.
“Hakuna mlanguzi aliyejiweka tayari kununua bidhaa kwa bei ya juu, atalalamika hata atakipata kwa bei chee kisha atakiuza kwa bei ya juu, hata mteja akilalamika kiasi gani hatakubali kumuuzia kwa bei chee. Kwa hiyo unapaswa kujua namna ya kucheza na maneno....” Mzee Muhando akazidi kutoa somo.
“Mimi sijawahi kufanya biashara yoyote, nitaweza vipi kuiuza hii sarafu kwa bei itakayoridhisha?” Kindo akahoji.
“Nipe ujira, mimi nitazungumza na mnunuzi, halafu wewe utamkabidhi mali yake pindi atakapokuwa ametupatia fedha.” Mzee Muhando akatoa ushauri.
“Nitakuona kesho baada ya kutoka kwa mzee Ukindi. Asante sana mzee Muhando..” Kindo akashukuru wakaagana.
Mazungumzo baina yake na mzee Muhando akayaona yana thamani kuliko wengine wote waliozungumza juu ya sarafu yake. Mzee Muhando alikuwa muwazi na hakutumia muda mwingi kuwananga watu wengine, yeye alijitengenezea njia kwa malipo ambayo yatamfaa kuiendesha familia yake. Zaidi alimweleza Kindo kitu ambacho wengine wote walikuwa hawajamueleza.
Soko la sarafu na ujanja wa kupenya huko kwa manufaa zaidi.
Katika mazungumzo yake hakuwataja wanasiasa wala viongozi wa kidini, alitupa kijembe kwa mzee Ukindi lakini hakikuwa na madhara yoyote katika mazungumzo yale.
“Nitamshawishi Nyangeta tumtumie huyu mzee katika biashara yetu.” Kindo akajisemea.
Mguu na njia kuelekea nyumbani kwake.
Anabeua chukuchuku la kuku wa kienyeji.
__________
NYANGETA alimpokea kwa bashasha kubwa Kindo.
Wale majirani na wanakijiji wataka ushuhuda hawakuwa na jambo la kuwaweka nje tena kwa sababu Kindo ambaye ni mmiliki wa sarafu ile ya ajabu alikuwa ametoweka kuelekea alipojua yeye mwenyewe na haikueleweka atarejea muda gani.
Nyangeta akajisogeza kumwachia nafasi Kindo katika kile kitanda chao kilichokuwa kinapiga kelele kwa juhudi kana kwamba kinaelewa kuwa zile zilikuwa kelele za mwishomwisho kabla hakijageuzwa kuwa kuni.
“Nimezungumza na mzee Muhando, yule rafiki yake mzee Ukindi.” Kindo akaanza kuzungumza.
“Kwanza huyo daktari na mkuu wa wilaya wameelekea wapi?” Kindo akawakumbuka wageni wake wa ghafla kutoka walipotoka.
“Wameenda kupumzika. Watakuja asubuhi. Mzee Ukindi anasemaje kwanza?” Kwa hali ya matamanio ya kujua yaliyojiri nyumbani kwao, Nyangeta alihoji.
“Mzee alikuwa anafuatilia kimyakimya suala la ndoa yetu, ameniita kunipatia jibu kuwa mtumishi wa Mungu amekubali kutufungisha ndoa takatifu. Halafu eti mzee ananiuliza, ‘Kindo upo tayari kumuoa binti yetu?’”
“Ukamjibuje?”
“Nikamwambia hapana!” Kindo akajibu. Nyangeta akaketi kitako, kitanda kikapiga kelele, midomo inamchezacheza. Anatamani aseme neno lakini hata hasemi kitu.
“Baba naye alianza kutetemeka kama wewe tu. Kumbe umerithi kwa mzee Ukindi” Kindo akazungumza huku anacheka.
“Cha kuchekesha ni kipi hapo Kindo? Ni kipi niambie na mimi nicheke basi...” Nyangeta akahoji kwa ghadhabu.
“Nikamwambia mzee binti ninayemuona hapa ni Debora, sipo tayari kumuoa huyu mimi nina wangu tayari anaitwa Nyangeta. Huyo nipo tayari kumuoa leo, kesho na keshokutwa!” Kindo akazungumza huku anatabasamu.
Nyangeta akamsogelea Kindo, akajilaza katika kidali chake, chozi la furaha linamtoka.
“Nakupenda sana mume wangu!”
“Nakupenda pia mama wa mwanangu na wanangu wengi wanaofuata. Kesho tumepata mualiko nyumbani kwenu, mzee amesema twende wote.” Kindo akamalizia. Kisha likafuata suala la mzee Muhando, nalo akaliwasilisha vyema kwa mkewe, wakakubaliana kuwa asubuhi ijayo ipambazuke na jawabu la nani wa kumwamini.
Wakaagana!
Licha ya kuagana hakuna aliyepitiwa na usingizi.
Kindo alikuwa hawazi juu ya ndoa wala maneno asali ya mzee Ukindi, alikuwa tayari kuwaza juu ya mapaja ya kuku lakini sio fitna za yule mzee. Aliamini fika kuwa kama mzee Muhando alivyokwisha mueleza, mzee Ukindi amegharamia kuku wa kienyeji kwa sababu ya uwepo wa sarafu ya ajabu.
Kindo alifahamu fika kuwa angemueleza Nyangeta mtazamo huo dhidi ya baba yake mzazi angeweza kuzua tatizo, hivyo akachagua kuyafanya mambo mengine pasi na kumshirikisha mkewe.
Akafikiria kutafuta namna ya kukutana na mzee Muhando bila mkewe kufahamu.
Cha muhimu sarafu hii iuzwe!! Akajiaminisha.
Nyangeta yeye alijifunika shuka huku akiisubiri kwa hamu siku mpya ijayo. Aliitamani sana ndoa, alitamani kuona wazazi wake wanayabariki mahusiano yao. Jambo hili lilikuwa linamuumiza kichwa sana, ni vile hakuwa na lolote la kufanya lakini alijiona mkosaji mbele ya wazazi wake kwa kuamua kuishi na Kindo kuibeba mimba na kuzaa bila kubarikiwa na wazazi wake ambaop walikuwa wakililia mahari yatolewe ndipo waishi pamoja.
“Nitawaomba msamaha na kisha maisha mapya yataanza.” Akajisemea katika nafsi yake.
Mara akamuwaza mdogo wake, aliamini fika kuwa ipo siku na yeye atabebeshwa mimba hapo hapo kijijini, vijana wa Ulongoni hawajui lolote kuhusu kinga, mabinti nao hawauelewi mzunguko wao wa uchevushwaji wa mayai.
Kama hazioni damu atashiriki tu mapenzi. Mimba ikitungwa wataambiwa waishi pamoja. Hawana pa kuanzia wala pa kuelekea, mwishowe binti atajifungua mtoto akiwa nyumbani kwao.
Nyangeta hakutaka hili litokee kwa mdogo wake, akapanga kuwa baada ya kufunga ndoa na kuamua kwenda kuishi mjini atamshawishi Kindo waongozane na Deborah.
Kindo hawezi kukataa! Aliamini.
_______
Pambazuko likawadia.
Nyangeta akaendelea na ratiba zake za siku zote, kudamka alfajiri na sasa tayari uji wa mtoto ambao pia angemchotea mama mkwe kiasi kwa ajili ya kupasha tumbo moto ulikuwa tayari.
Kindo alipoamka alikutana na kikombe cha uji mbele yake. Akaugida huku akijaribu kutazama kila jambo kana kwamba hatalitazama tena. Jambo mojawapo ni huu uji usiokuwa na sukari ndani yake.
Kindo, hakuyajua vyema maisha ya watu wenye kipato ambao huitwa matajiri. Kitu pekee alichokitambua ni kwamba katika kila kauli nne watakazozungumza hawakosi kutupia kauli yenye sitizahi kwa ajili ya kumfanya msikilizaji atambue kuwa anazungumza na tajiri.
Sitizahi!
“Katu siwezi kumdharau mtu mimi, siwezi kamwe kutumia maneno ya dharau kwa mwanadamu mwenzangu” Kindo hakutaka utambuzi ule umchote na yeye.
Akajaribu kufikiria kwa kina zaidi, akamfikiria daktari wa kijiji chao, ukiondoa nyumba yake kuwa na paa la kuvutia, hana maisha ya tofauti sana ya kujipambanua kutoka kundi la maskini.
“Hana utajiri wowote. Yule sio wa kujifananisha naye” Kindo akahitimisha.
Ujapongo! Akaifikiria tabia ya kulakula hovyo, kisa tu pesa ipo. Akaamini matajiri wengi wanakulakula hovyo, n’do maana wanapata miili minene.
Wazo hili likamkumbusha mlo wa usiku uliopita, kuku wa kienyeji asiyehitaji mafuta, kitunguu wala nyanya.
Kindo akaafiki kuwa baada ya kuiuza sarafu yake ya ajabu lazima atakuwa anakulakula. Tabia ya ujapongo aliamini kuwa hawezi kuikwepa.
“Nitakula vyote vitamu, nitakula hata bila kujua majina yake ilimradi tu havina sumu. Kula sio dhambi ati!” akajifariji.
“Mbona haunywi uji sasa.” Sauti ya Nyangeta ikamkurupua. Kindo akabaini kuwa mawazo yake yalichukua kitambo cha kutosha kusababisha ule uji kupoa.
Akaunywa vilevile upesiupesi.
Nyangeta alikuwa amelishika chanuo na kuziweka nywele zake katika mtindo wa ‘sunzu’ mtindo maarufu kwa enzi zao, unazichana nywele vyema kisha unazichana tena zile za mbele kwa kuzinyanyua juu.
“Mimi nd’o namalizia hivyo twende. Hii nd’o mapema yenyewe mume wangu.” Nyangeta akasema.
Kindo akatikisa kichwa, akatoka na kile kikombe nje.
Tayari! Majirani walikuwa wameizunguka nyumba waweze kuona kipi kinajiri.
Kindo akakisuuza kile kikombe, kisha akachota maji na kuuosha uso wake.
Mume, mke na mtoto wakatoka wakiiacha nyumba yao. Kindo akauegesha mlango!
Shilingi ya ajabu ikiwa imehifadhiwa sehemu salama kabisa.
Macho ya watu yakawasindikiza. Baadhi wakiamua kujiaminisha kuwa Kindo na familia yake wamejawa na dharau, wengine wakiamini kuwa Kindo na mkewe ni walozi, hawajaipata hiyo sarafu kwa njia za kawaida.
Ilimradi hayo mawazo yao, hayakuwafikia akina Kindo, basi wao wakazidi kudundika kuelekea wanapoelekea.
Kindo akatumia nafasi hii kuanza kumsimulia Nyangeta juu ya chakula walichokula usiku uliopita. Kuna nyakati alijaza chumvi kunogesha simulizi.
“Mama akanifungia nikubebee kuku mwingine, nikasema mama hapana, akila kuku huyu atakuwa haji kesho! Acha ataikuta huku” Kindo anamsimulia mkewe.
Nyangeta anahamasika, anatamani waongeze mwendo wawahi kufika.
Haamini kile anachosimuliwa!
Hatua moja na moja nyingine huzaa mbili na kuendelea.
Wakaufikia mlango wa kuingia nyumbani kwao Nyangeta.
Hakuna harufu kama walivyohamasishana kuwa yawezekana siku hii ya leo ikawa kubwa zaidi. Nyangeta akiwa anawaza juu ya kuku aliyebakishiwa.
“Kindo!” Sauti kavu ya mzee Ukindi ilisikika. Alikuwa ameketi chini ya mti wa machungwa.
“Baba kumbe upo hapa. Sisi macho yetu yote ni kulee” Kindo anajibu kwa uchangamfu. Kisha anamsalimia, Nyangeta naye anamsalimia baba yake.
“Marahaba Nyangeta, hebu nenda ndani kaonane na mama yako kwanza. Niache na huyu bwana kidogo” Kwa unyonge Mzee Ukindi anamweleza.
Kama mzee Ukindi angekuwa amezaliwa na pacha wake. Huyu angekuwa ni pacha’ke na sio yule mzee Ukindi wa siku uliopita.
“Kindo, naomba uondoke nyumbani kwangu, asante kwa sababu binti yangu yupo salama. Mtoto huyu ni wako, lakini hauwezi kuondoka naye akiwa katika umri huo. Akikua ataelekezwa alipo baba yake na atakuja kwako!” Mzee Ukindi akatia kauli staajabishi.
“Baba sija...”
“Toka nje!” Akafoka, sauti yake ni ileile ambayo ilikuwa ikimfokea Kindo wakati wa sakata la mahari.
Mzee Ukindi halisi!
“Sasa Nyange..”
“Ulimzaa wewe? Nakuuliza, Nyangeta alizaliwa hapa, na hapa panabaki kuwa kwao. Sihitaji mahari yako tena, ninachohitaji utoke ndani ya uzio huu. Upesi!!” akamalizia kauli yake huku akiwa wima.
Kindo akaliona balaa likinukia, akapiga hatua kinyumenyume akatoka. Haelewi, haamini, anastajabishwa!
Awali aliingia katika uzio ule akimini fika kuwa yale maneno ya Mzee Muhando juu ya unafiki wa mzee Ukindi. Akaishi na ile kauli kuwa huyo kuku sio bure, ni kwa ajili ya sarafu.
Alitarajia mapokezi makubwa sana, lakini ameishia mlangoni. Mkewe kaingia ndani na hakutoka tena.
Mzee Ukindi hajaulizia lolote kuhusu ile sarafu, na katu kinywa chake hakikuwa kutamka lolote juu ya ile sarafu.
Amemfukuza mithiri ya paka wa jalalani aliyejipendekeza chini ya miguu ya mteja katika mgahawa.
Kindo anatembea kuelekea kaskazini, mara anabadilisha uelekeo anaifuata kusini, huko hapamridhishi anaifuata mashariki.
Haeleweki!
Hajielewi!
Anapatwa na shambulizi la ghafla anapoikumbuka sarafu yake, sehemu alipoihifadhi anafahamu yeye na mkewe tu!
Anahisi kusalitiwa, huenda mke wake ameungana na wazazi wake kumsaliti.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake anamweka mkewe katika kundi baya.
Mbio!
Anatimka kuelekea upande sahihi sasa, anaelekea nyumbani kwake.
Wanakijiji wanamfahamu Kindo, na penyenye kuhusu bahati aliyoipata ziliwafikia kila mmoja kwa namna yake ya kipekee.
Wanamuona Kindo anatimua mbio, wanamuita haitiki.
Kachanganyikiwa! wanaamini hivyo. Ya kwamba Kindo ameiuza sarafu yake ya ajabu na wingi wa pesa alizolipwa umemtia wazimu.
Wale walioamini kwa ile haikuwa bahati bali ulozi uliofanywa na Kindo, wakaamini kuwa balaa alilojichumia sasa limemgeukia na kumtia wazimu.
Huyu alisema jingine yule akatengeneza la kwake. Hakuna aliyekuwa na uhakika.
Akiwa anahema juu juu alifika nyumbani kwake. Watu wanageuka kumtazama.
Wanamshangaa!
“Ana nini huyu?” Mkuu wa wilaya aliuliza, Daktari naye akauliza swali hilohilo. Kindo akaingia katika chumba alichokuwa amelala mama yake. Kindo akapiga goti na kumkumbatia taratibu asimuumize.
“Unaendeleaje mama yangu kipenzi. Nakupenda sana mama yangu!” Kindo anazungumza kwa ukarimu.
“Naendelea vizuri mwanangu, lakini kuna jambo...” Mama akazungumza kwa utulivu.
“Utapona kabisa mama yangu, utapona na utarudi shambani kulima. Hata usijali, jambo lipi tena?” Kindo akazungumza, akiwa bado amemkumbatia begani.
“Natakiwa kufanyiwa opereshoni nd’o daktari amenieleza.”
“Opereshini ni kitu gani hicho? Si akufanyie tu ikiwa kitasaidia wewe kusimama imara tena ama?”
“Amesema kinafanyika mjini huko katika hospitali yake kubwa. Kwa hiyo tunatakiwa kusafiri.” Mama alizungumza kwa sauti tulivu.
“Amesema hakuna kitakachoshindikana kwa sababu kwa sasa tayari una mali ambayo inaweza kugharamia haya yote.” Mama akamalizia.
“Mama, sina mali tena.” Kindo akazungumza huku anasimama wima.
“Umeigawa sarafu yako ya ajabu?” Mama akauliza huku akiketi kitako.
“Sarafu sio mali kitu kwangu, sinaye tena Nyangeta na sijui ni kipi kimetokea, baba yake amenipokonya mke na mtoto wangu, hataki kupokea mahari yangu na amenifukuza nyumbani kwake kama mbwa koko.” Kindo alilalama kwa hisia kali.
“Sarafu yako unayo lakini?” Mama hakujali kuhusu simulizi za Kindo, anawaza juu ya sarafu na utajiri. Sarafu itakayowezesha kupona kwake.
“Mama haujasikia lolote kuhusu Nyangeta unaniuliza kuhusu sarafu ya ajabu??” Kindo akauliza kwa hisia chanya. Kisha akamsogelea mama yake, akaketi pembeni yake.
“Sarafu ya ajabu ina msaada gani kwako pasipokuwa na upendo?” anainama kama anayejiuliza.
“Mwanangu, ukiiuza ile utapata pesa za kutoa mahari, mzee Ukindi hatayakataa mahari yako ukiyajaza chekwachekwa, hatakubali kuikosa sherehe kubwa kupita zote hapa kijijini. Pesa hiyo itanitibia mimi opereshoni mjini, nitacheza ngoma za kwetu katika harusi yako.” Mama akamfariji mwanaye, anajaribu kubinyabinya kiganja cha Kindo.
“Kipi kina thamani kwako mama, Nyangeta ama sarafu ya ajabu?” Kindo akaweka hoja nzito mezani.
“Vyote mwanangu!” mama anajibu upesi.
“Sikia mama, Nyangeta huamka asubuhi na kukukorogea uji wa moto hata kama hauna sukari ni kuendana na hali zetu,” anamtazama mama yake, anajisogeza zaidi karibu yake kisha anaendelea “hukushika mkono na kukuongoza uani ambapo hukumwagia maji na kukuogesha, anakutandikia kitanda unalala anaikanda miguu yako, anahakikisha unakunywa dawa, ni huyuhuyu Nyangeta alinilazimisha kutembea kilometa nyingi kwenda kuitafuta dawa kwa ajili yako, huko nikakutana na sarafu ya ajabu, sarafu ambayo katu hatukuwahi kuiwaza katika familia yetu.
“Licha ya kuimiliki sarafu ya ajabu, Nyangeta hakubadili ratiba zake, hata leo ameamka alfajiri na kukuhudumia. Lakini sarafu hii ya ajabu imekufanyia kipi hata sasa?” Kindo akalalama huku akimtupia mama yake swali.
Mama kimya! Maneno yanamuingia vilivyo.
“Hadi sasa sarafu ile unayoipa thamani sawa sawia na Nyangeta, imekutendea nini?” Kindo anamuhoji mama yake kwa upole na sauti isiyoshurutisha.
Halisubiri jibu anaendelea.
“Nilipoondooka na Nyangeta, huku nyuma ulipata hitajio gani ambalo lilihitaji uwepo wetu?”
“Nzi walinisumbua nikahitaji chandarua kishushwe.” Mama anajibu kwa utulivu, anajiona yu hatiani.
“Ulijua kuwa sarafu ya ajabu ipo katika mchago unaolalia?” Kindo akatupa swali la ghafla. Mama anagutuka na kutazama uchagoni.
Kindo anauchukua ule mchago uliochama kinywa chake kwa maumivu ya kugandamizwa na vichwa mbalimbali. Anapenyeza mkono na kuibuka na ile sarafu.
Kisha akauchukua ule mchago, akaingiza mkono na kutoka na sarafu ya ajabu.
“Ilikufanyia nini sarafu hii ulipobaki nayo hapa katika upweke, ilikueleza nini kilichokutia tumaini? Ilifanya nini mama zaidi ya kulala usingizi mzito katika mchago? Sarafu ambayo hata jambo dogo tu la kukushushia chandarua ilikwama, sarafu ambayo hata nzi pekee hawaiogopi. Unamweka Nyangeta katika thamani moja na sarafu inayolala usingizi wa pono?” Kindo hakuweza kuzungumza zaidi, akatoka nje. Anajihofia sauti yake inapanda juu kwa jazba.
Hapendi kupandisha jazba dhidi ya mama yake.
“Kindo” sauti ya upole kutoka ndani ikamuita.
“Naam! Mama” anaitika kwa sauti iliyopwaya.
“Njoo!”
Kindo akaingia ndani, hana amani, furaha haiishi naye mkononi ana sarafu ya ajabu lakini ameikamata kama uchafu.
“Sio kwamba nimeichagua sarafu dhidi ya mkamwana wangu Nyangeta. Hapana, sogea hapa...” Kindo akajisogeza, akaketi pembeni ya mama yake.
Machozi yanamchonyota.
“Tuseme umeitupa hiyo sarafu kwa sababu haina maana, nakuapia mwanangu hapo utakuwa umemtupa Nyangeta pamoja na mjukuu wangu. Yule mzee namfahamu mimi utata wake, tangu nikiwa binti mdogo namfahamu vyema. Hatakuruhusu umchukue binti yake tena, na anaweza hata kukuzushia tuhuma za wizi ukiikaribia nyumba yake. Suluhisho la matatizo yako yote ya kidunia ni sarafu ya ajabu, suluhisho la kiroho nadhani unajua linapopatikana. Chukua maamuzi sahihi, mkononi mwako umeibeba familia yako.” Mama anaongea kwa hisia kali. Kindo hakutarajia shambulizi lile kutoka kwa mama yake.
“Haya nenda ulipokuwa unataka kwenda.” Mama akamaliza, Kindo hakusimama, badala yake aliitazama ile sarafu, ilikuwa tofauti.
Wakati anauacha mlango ule kwa mara ya kwanza aliichukulia kama mkosi katika maisha yake na akapanga kuitupilia mbali. Lakini sasa ilikuwa imepanda thamani maradufu. Maneno ya mama yake yalikuwa yamemuingia moja kwa moja.
Kindo akajivesha ujasiri mpya. Akaihifadhi sarafu ile katika pindo la ule mchago. Akatoka nje.
Mkuu wa wilaya alikuwa anahitaji kuagana naye, pamoja na daktari.
“Sisi tunakuaga sasa, tumezungumza na mama na kama alikwishakueleza. Mnatakiwa kufika mjini kwa ajili ya oparesheni.”
“Ameniambia! Lakini kwa nini asipewe hapahapa” Kindo akahoji.
“Apewe nini?” Mkuu wa wilaya anahoji kwa utulivu lakini uso wake unalipoteza tumaini.
“Hiyo opreshini” Anajibu kwa uhakika Kindo. Mkuu wa wilaya anashikwa na donge la hasira, anatamani kumrarua Kindo kwa kushindwa kuelewa maana ya oparesheni. Kindo hana uelewa wowote.
Na ilikuwa heri ambavyo hawakufafanua nini maana ya hicho wanachozunguza.
Abadani! Kindo asingekubali kusikia eti mama yake anapasuliwa.
Apasuliwe?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment