Simulizi : Wakala Wa Siri (2)
Sehemu Ya Tano (5)
Fernanda akapapasa zaidi akagusa kitu kama kufuli, “Mlango huu unaonekana haujafunguliwa muda mrefu, mpaka kufuli linashika kutu” Fernanda akawaza akiwa anaendelea kulishika lile kufuli. Akajaribu kulivuta kwa chini kuona kama litafunguka lakini wapi, halikufunguka, akapata wazo kuwa atumie bastola kuivunja ile kufuli, wazo hilo akakubaliana nalo. Akaikoki bastola, akasimama alafu akalenga shabaha kwenye lile kufuli. “PAAAH” Kufuli ikavunjika na kufunguka,
“ Mlio huu wa risasi utawapa uelekeo wale majitu na kujua mahali nilipo. Yanipasa niharakishe” Fernanda akawaza. Kisha akauvuta ule mlango kwa nguvu lakini bado mlango ukagoma kufungua. Fernanda akapandwa na hasira. Akauvuta tena lakini haukufunguka, akaona ausukume lakini juhudi zote zilikuwa sawa na bure. “ Nini kinazuia huu mlango usifunguke, mambo haya yananichosha sasa” Fernanda akawaza, ghafla nuru hafifu kutokea upande wa nyuma ikazuka. Fernanda akageuka nyuma, hakuona mtu lakini akaona mwale wa kurunzi ulioangza ile korido umbali wa mita thelasini.
“ Ohh Come on! Haya mashetani yanakuja, Mlango funguka tafadhali” Fernanda akasema kwa sauti ya chini akijaribu kuuvuta na kusukuma lile geti. Ule mwanga ukawa unazidi kuongezeka, kadiri ulivyokuwa ukiongezeka kwa kasi ndivyo hofu ilivyozidi kuziharibu hisia za Fernanda, jambo asilolitegemea likatokea, macho yake yakajawa na mshtuko, Fernanda akaona mnyororo kwa juu kabisa uliozunguka kulifunga geti lile, kama sio mwanga ule kuongezeka basi Fernanda asingeweza kuuona ule mnyonyoro. Kwa upesi akainyanyua bastola yake akaupiga ule mnyororo Paah! Lakini mnyororo haukukatika, mlio wa risasi ukafanya mwanga uzidi kuongezeka kwa upesi, hii ilimaanisha kuwa wale watu wabaya waliokuwa wakimfukuza walikuwa wakikimbia kumfuata, Fernanda akapiga risasi ya pili, mnyororo ukakatika. “ Vizuri sana. Umefanya kazi nzuri, siku zote nakuaminia” Fernanda akasema kwa sauti ndogo akiiambia bastola yake na kuibusu. Kisha akaanza kuvuta lile geti, akaona halifunguki, akatazama nyuma kwa wasiwasi kuangalia kule mwanga unapotokea, akaona asukume kwa nguvu lile geti badala ya kulivuta, “ Vizuri” Geti likafunguka Fernanda akiwa hoi hofu ya kifo ikimsakama. Fernanda hakutaka kupoteza muda. Akasonga kufuata njia ile, lilikuwa ni handaki kubwa la mviringo ambalo lilimfanya atembee kwa uhuru pasipo kichwa chake kugusa dari. Mwanga ule hafifu ulimsaidia kidogo kuona mbele yake lakini kadiri alivyokuwa akitembea ndivyo giza nene la lile handaki lilivyokuwa likimlaki. Nusu dakika wale wanaume waliovalia suti wakatokea wakiwa wanakuja mbiombio wakilifuata geti lililovunjwa na Fernanda. Hatua zao zilidhamiria, sura zao zilizingirwa na hasira kali zenye kiu ya kumwaga damu. Kadiri walivyokuwa wakimfukuza ndivyo hamu ya kuinyonya damu yake ilivyoongezeka. Fernanda akageuka nyuma akiwa anakimbia katika handaki lile, aliona wanaume watatu wakiwa wamelikaribia lile geti alilolivunja. Fernanda akaongeza kasi lakini kwa woga kwani alikuwa haoni vizuri mbele, Akasonga na kusonga nyuma yake wale watu wabaya wakimuandama pasipo kuchoka, ingawaje watu wale bado walikuwa hawajamuona ila waliamini kuwa Fernanda hakuwa mbali na eneo lile kutokana na mlio ule wa risasi waliousikia.
Fernanda akakimbia lakini macho na akili yake vikashikwa na machale kuwa mbele yake kunatatizo, akapunguza mwendo, akatembea kwa tahadhari, kitambo kidogo macho yake yakashtuka kuona kizuizi kilichozuia njia, Fernanda akasogelea kile kizuizi, akashusha pumzi nzito na matumaini ya kuwatoroka wale watu wabaya yakayeyuka. Njia ilikuwa imezibwa na kizuizi mfano wa Pangaboya kubwa lenye kutu, Fernanda akaenda kulishika lile pangaboya kubwa lenye kutu; akalizungusha kwa nguvu zake zote lakini hakuwa na nguvu hata kidogo ya kuweza kulizungusha, akajaribu tena kwa nguvu zake zote lakini ilikuwa kazi bure, halikuzunguka, Fernanda akaona ajaribu kupitisha kichwa kwenye nafasi ndogo iliyokuwepo kwenye lile pangaboya ili apite upenda wa pili, kichwa chake kikafanikiwa kupita akapokelewa na harufu mbaya ya uvundo iliyokuwa upande wa pili na giza nene kushinda alipokuwa anatoka. Lakini ingekuwa bora harufu hiyo kuliko kukamatwa na wale watu wabaya wenye roho za kikatili. Fernanda akajaribu kupitisha mabega yake lakini hilo likashindika, akajaribu zaidi na zaidi lakini hakuweza, akarudisha kichwa chake akawa anapumua kwa kasi, akageuka nyuma akaona kwa mbali mwanga wa kurunzi ukisogea kwa kasi kuja kule aliko
“ Sasa hapa nitafanya nini? Mbona nimekamatika kirahisi hivi, sitakubali kukamatwa mzima mzima kama kuku wa sikukuu” Fernanda akawaza huku akiuangalia ule mwanga wa kurunzi unaokuja upande wake. Akili yake ilikuwa kama ngeredere anayerukia tawi hili na hili kumkimbia mkulima aliyeiba mahindi yake. Fernanda akageuka tena upande wenye kizuizi mfano wa pangaboya kubwa ya chuma iliyoshika kutu, mara hii mwanga ulikuwa umeongezeka kutokana na miale ya kurunzi ya wale watu wabaya, Fernanda akalikagua lile pangaboya kwa juu akaona kitu mfano wa Mkasi kilichozuia lile pangaboya lisizunguke, kwa upesi huku akijua hana muda mwema uliobaki, akarukia ule mkasi na kuuvuta kwa chini, lile pangaboya likaanza kuzunguka, “Vizuri” akasema kimoyomoyo. Akageuka nyuma wakati huu wale watu wabaya walikuwa washamuona na kuanza kumrushia risasi ambazo zilikuwa zilimpunyua na kulipiga lile pangaboya. Fernanda hakuwa na muda wa kupoteza, akasubiria upande wa pangaboya wenye nafasi kubwa ya yeye kupenya, hata hivyo kumbe lile pangaboya lilikuwa likizunguka polepole lakini kadiri linavyoendelea kuzunguka ndivyo linavyoongezeka kasi yake. Fernanda kwa kuona hivyo akarukia ile nafasi na kuzamia upande wa pili, kisha akalishika lile pangaboya na kulizungusha kwa kasi kuliongezea kasi yake ili wale wavaa suti za mauti wasimfikie. Kitendo cha kufanya kulizungusha lile pangaboya kulifanya kasi yake iongezeke maradufu asiwepo mtu awezaye kupita katikati yake. Fernanda akashusha pumzi kwa nguvu baada ya kukamilisha kazi hiyo nzito.
“ Nimeweza kuwaponyoka, lakini sasa huku ninakoenda ni wapi, nitatokea wapi. Giza la humu ndani linanitia hofu, harufu ya mahali hapa ni mbaya kama nini, sijui huku wanatupaga nini?” Fernanda akawaza huku akitembea polepole akiliacha lile panga boya likizunguka kwa kasi na kutengeneza upepo wenye harufu mbaya ya uvundo wa lile handaki. Fernanda akasonga mpaka alipofika sehemu ambayo akakanyaga kitu mfano wa matope, “ Sijui ni chemba ya maji take?” Fernanda akawaza. Akasonga akizidi kukanyaga majimaji na matope ya maji taka huku harufu mbaya ikishambulia pua yake, giza nene lililomfanya asione hata hatua moja lilizidi kumfunika, wala hapakuwa na tofauti yoyote kama angetembea kwa kufumba macho au akiwa ameyafumbua. Lilikuwa ni giza kuu,
“ Sikuwahi kufikiri kama kuna giza kama hili tangu nimezaliwa” Fernanda akawaza huku akizidi kusonga. Harufu ilizidi kuongezeka lakini hakuwa na chaguo, ilikuwa ni kheri harufu mbaya na giza kama lile kuliko kukamatwa na wale watu aliowaona kama mashetani wa makaburini. Akiwa anatembea mawazo yake yakaanza kuchora taswira katika ubongo wake;
““ Naitwa Stanslaus Mahige, naingia popote, hakuna mlango ambao utafungwa nisiufungue. Hata hivyo sijaja hapa kueleza habari hizo. Kilichonileta ni jambo moja tuu. Tafadhali nambie, Sajenti Warioba Yupo wapi?”
“ Tokea lini Sajenti Warioba anaishi hapa? Au kuna mtu kakuambia Sajenti yupo hapa? Mmeenda kwake hamjamkuta?” Fernanda alisema.
“ Sikiliza wewe Mwanamke, sijaja hapa kujibishana na wewe, nambie Sajenti yupo wapi?”
“ Sijui Sajenti yupo wapi? Mwenyewe namtafuta, nani kakutuma umtafute Sajenti, na unamtafuta kwa nini?”
“ Hakuna asiyejua kuwa Sajenti ni adui wa nchi, yeye ndiye aliyeiba chipu ya Darubini ya maabara, yeye ndiye kaiba Cadava, yeye ndiye kaiba sampo za uchunguzi, tena akamtorosha Mateka wa ushahidi, sasa kaamua kutoroka. Huyajui mambo haya au upo pamoja naye kwenye uovu wake? Embu niambie Sajenti yupo wapi hiyo ndio salama yako, usiponiambia utajiingiza kwenye matatizo makubwa” Fernanda ubongo wake ulikumbuka tukio lake la Stanslaus Mahige, kijana huyu ndiye alikuwa wakwanza kumvamia nyumbani kwake akimuamuru amwambia mahali alipo Sajenti Warioba.
“ Itakuwa Stanslaus Mahige alitumwa na hawa watu, lakini watu hawa ni kina nani? Inaonekana ni watu hatari sana, wakatili wenye roho za kishetani, lakini ikawaje Meja Venance Kagoda akawa na ushirika nao, mambo haya yananichanganya sana, lakini naamini majibu yote yatakuwa katika simu niliyonayo niliyoichukua chumbani kwa Meja Venance” Fernanda akawaza wakati akiwa anatembea katika matope yanayonuka giza likiwa limemfunika asiweze kuona anakanyaga nini.
Kitambo kidogo akavuka eneo lenye matope akawa anakanyaga mchanga wa changarawe, “ angalau hapa” akajisemea mwenyewe huku mkononi akiwa bado anabastola yake ambayo aliamini haikuwa na risasi zaidi ya mbili, hata hivyo bado aliiona itamsaidia kwa namna moja ama nyingine. Harufu na eneo lile ikawa imebadilika kutoka katika kuwa harufu mbaya kama ya maji taka na sasa akawa anasikia harufu mbaya ya kemikali kama ya madawa hivi. Akasonga lakini kadiri alivyokuwa akisonga akaanza kuhisi kuzunguzungu, bila shaka ni ile harufu mbaya ya kemikali ndio ilikuwa inamuathiri,
“ Harufu hii inaweza kuwa ni sumu, au pengine inaweza kuwa kemikali inayoathiri mfumo wa ufahamu. Nahisi kichwa kizito” Fernanada akawaza wakati anaongeza mwendo haraka haraka kuondoka eneo lile akitarajia mwendo mfupi ujao atakuwa ameepa harufu ile ambayo tayari imeanza kumdhuru. Akasonga kwa kitambo cha dakika mbili kwa mbali macho yake yakaona mwanga, moyo wake ukalipuka kwa tumaini, akazidisha mwendo lakini muda huu akaanza kuuona mwili wake unazidi kuwa mzito na macho yake yakiona mawenge,
“Fernanda don't die in this place, do your best! Move forward. There is hope, the Light is waiting for you. Come on Fernanda! Jikaze! Usikubali Fernanda” Mawazo ya Fernanda yalimsemesha akiwa anatembea akiyumba yumba kama mlevi kutokana na kizunguzungu, akishika ukuta huku akijikokota kuufuata mwanga aliouona mbele yake. Tayari alikuwa keshazidiwa, hali yake ilikuwa tete, asingejiongopea kuwa hana uwezo tena wakusonga mbele, ingawaje moyo wake ulikuwa radhi lakini mwili ulikuwa dhaifu. Fernanda akasimama akiwa kalegea kama mlenga, akakaa chini, akiwa pale chini, taswira nyingi kama filamu iliyorekodiwa zilipita katika kichwa chake. Akamuona Sajenti akiwa amepanda Farasi wa rangi ya udongo mwenye doa jeupe kichwani, Sajenti alikuwa kava kofia kubwa kama cowboy wa mexico, alikuwa amevaa shati jeupe ambalo hajalifunga vishikizo na pensi, akawa anakuja kwa kasi na farasi akiwa anatabasamu huku shati lake likipepea kwa upepo wa kasi ya Farasi, Fernanda nate akatabasamu. Sajenti akasema ; Don’t die in this place” kisha akaanza kumeguka na yule farasi kama vile kichuguu cha mchwa kinavyomeguka. Fernanda akashtuka, kumbe yalikuwa ni mawazo yaliyovurugwa na zile kemikali.
Fernanda akaanza kutambaa kama mtoto mdogo akiwa amebakiza hatua kadhaa aufikie mwanga hafifu uliokuwa mbele yake. Alipoukaribia ule mwanga akashangaa kukuta reli ya treni iliyokuwa ikitoka upande wake wa kushoto ikielekea kulia na hivyo kutengenaza makutano kama alama ya jumlisha. Eneo hili halikuwa na ile harufu ya kemikali, ingawaje bado Fernanda mwili ulikuwa mzito na kizunguzungu kilimzingua. Fernanda akaona apumzike pale, akakaa kwenye ile reli. Akiwa kapumzika usingizi ukimmendea huku mawazo mengi yakiweka foleni ndefu ubongoni mwake, mara akashtuliwa na sauti ya gari moshi iliyokuwa inatokea upande wa kushoto. Akageuka upande wa kushoto lakini hakuona kitu kutokana na giza lakini bado sauti ya gari moshi inayokuja alikuwa anaisikia. Fernanda muda huu akiwa amepata nguvu kidogo baada ya kupumzika akaona muda wa kuondoka mahali pale umewadia, Fernanda akawaza kuwa ataitumia Treni hiyo inayokuja kujikomboa kutoka mahali pale. Dakika moja iliyofuata Fernanda alikunja uso wake na kuyafinya macho yake baada ya mwanga mkali kutoka kwenye gari moshi uliokuwa ukimmulika usoni akiwa katikati ya reli. Gari moshi lilikuwa umbali wa mita hamsini lakini mwanga wake uliweza kuangaza umbali mrefu, Fernanda akaweka mkono wake usoni kuziba mwanga usimpige machoni huku akijitahidi kuangalia ile Treni kwa umakini. Looh! Macho yake hayakuweza kukubali, akiwa bado kasimama alishtuka kuona mdomo wa bunduki na mlengaji akiwa juu ya kichwa cha Treni vikiwa vinamtazama, upesi akajirusha pembeni huku akifukuzwa na milio ya risasi, Fernanda akaamka upesi na kuanza kukimbia akiiacha Reli, akanyooka moja kwa moja kule mwanga ulipokuwa unatokea, Treni ilipofika mahali alipokuwa amesimama akasikia watu wakishuka huku wengine wakimshambulia kwa risasi, Fernanda alikimbia kwa nguvu zake zote huku mwanga hafifu ukimsaidia. Nyuma yake wale watu hawakutaka kumpa nafasi ya kutoroka, walimuandama kama kivuli cha kifo. Ghafla bin vuu jambo baya likatokea, mbele ya Fernanda kama hatua kumi lilikuwepo shimo refu lakini juu yake kulikuwepo na tundu kubwa linaloingiza mwanga kutokea juu. Nyuma yake wale watu wabaya walikuwa hawapo mbali, walikuwa wakija kwa uhakika wa kumpata Fernanda; Akasimama, akageuka nyuma kuwatazama watu wale, kisha akageuka kulitazama lile shimo ambalo ndani yake mwanga ulikuwa ukiingia, chini kabisa ya lile shimo kwa mbali akaona kuna kamba mbili, wakati bado hata hajatambua rangi ya kamba zile, akahisi maumivu yakipenya katika bega lake la kulia, na punde akaanguka chini ya lile shimo refu lenye giza kwa chini licha ya kuwa kulikuwa na mwanga ukitokea juu yake.
***************************
MWISHO WA SEASON 2 ENDELEA NA SEASON 3
MWISHO
0 comments:
Post a Comment