Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

WAKALA WA SIRI - 1

 

IMEANDIKWA NA : ROBERT HERIEL

********************************************************************************

Simulizi : Wakala Wa Siri 

Sehemu Ya Kwanza (1)


MAABARA YA BORETI.

Jokofu maalumu kwa ajili ya kuchunguzia maiti lilikuwa limezungukwa na Madaktari bingwa wa maswala ya uchunguzi, ndani yake ilikuwepo maiti iliyofungwa kwa karatasi jeupe la nailoni. Ilikuwa ni maabara ya kuchunguza maiti za watu ambao walikufa vifo tata au kuuawa. Kitaalamu maiti za namna hii huitwa 'cadaver' (tamka Kadava). Cadaver ni mwili wa binadamu aliyekufa ambao hutumiwa na Madaktari wa uchunguzi kubaini sababu ya kifo cha mhusika. Pia Cadaver hutumiwa na Wanafunzi wa utabibu, wanafizikia wanaojifunza Anatomia kubaini magonjwa, kutoa tishu au viungo kwa wanadamu waliokuwa hai. Walikuwa Madaktari saba waliokuwa katika maabara wakifanya uchunguzi wa maiti iliyokuwa mbele yao juu ya meza, huku wao wakiwa wameizunguka. Daktari mmoja alikuwa yupo mbele ya Madaktari wengine. Huyu ndiye alikuwa Daktari Mkuu wa uchunguzi huo. Walivalia makoti meupe ya kidaktari yaliyofika mpaka magotini. Pua zao waliziziba na barakoa ya puani ya kufanyia upasuaji (surgical mask) nyeupe huku kichwani wakiwa wamevaa kofia maalumu za kufanyia upasuaji (surgical cap). Mikononi walikuwa wamevaa Gloves nyeupe kwa ajili ya kujikinga na hatari yoyote ya maambukizi endapo ingetokea.

Pembeni ya lile Jokofu lenye maiti kulikuwa na meza ndogo yenye ukubwa wa mita mbili, ambapo juu yake kulikuwa na sinia kubwa lenye mikasi, visu na vifaa vingine maalumu vya upasuaji. Juu ya dari kulikuwa na Taa ndefu iliyokuwa inamulika na kukifanya chumba kile kiwe na nuru ya kutosha kabisa. Daktari Mkuu aliisogelea ile maiti kisha akalifungua lile karatasi la Nailoni jeupe lililokuwa limezungushwa kwenye ile maiti. Sasa Maiti ilikuwa uchi kabisa bila ya nguo wala ile nailoni. Wale Madaktari sita wengine walisogea zaidi karibu na Daktari mkuu wote wakiutazama ule mwili. Daktari Mkuu alipeleka mkono wake kwenye macho ya ile maiti akalifungua jicho moja la ile maiti. Akatazama kwa muda kisha akalifunga. Akapeleka macho yake mpaka iliposhingo ya ile maiti, kisha akaigusa kama mtu anayepima jambo. Kisha akatoa. Madaktari wengine walikuwa wakimtazama Daktari mkuu jinsi anavyofanya. Daktari Mkuu akasogea mpaka lilipotumbo la ile maiti. Kisha akalishika na kulibinya kidogo huku akitazama mdomoni mwa ile maiti. Akabinya mara tatu kwenye tumbo la ile maiti. Akaacha. Akaagiza kifaa maalumu, kitambo kidogo akaletewa kifaa kilichofanana na mpira akakishika mkononi. Kisha akafungua mdomo wa ile maiti akatazama kwa makini. Kisha akaufunga.

"Embu binya tumbo la hii maiti mara tatu" Daktari Mkuu aliongea huku akichomeka kile kifaa kama mpira Mdomoni mwa ile maiti huku akiziba pua ya ile maiti. Kisha Daktari mwingine alisogea na kubinya tumbo la ile maiti mara tatu. Kitendo hicho kilifanya hewa ijae kwenye kile kifaa cha mpira kilichobandikwa mdomoni mwa ile maiti. Kisha Daktari Mkuu akasogea mahali zilipo sehemu nyeti za ile maiti. Ilikuwa maiti ya mwanaume. Hapo akaushika uume wa ile maiti akaubinya ukatoa maji maji. Kwa upesi akapewa na Daktari mwenzake kioo maalumu akakinga yale maji maji yaliyotoka kwenye uume wa ile maiti. Kisha walimalizia kwa kuufanyia mwili Scanning(tamka Skani). Alafu wakachukua dawa fulani wakapaka ile maiti na kuifunga na lile lile karatasi la Nailon jeupe la awali.

"Nadhani kazi itakuwa imekamilika. Sasa twendeni tukachukue vipimo kwenye hizi sampo tuone tatizo lilikuwa ni nini" Daktari mkuu wa uchunguzi aliongea miwani yake ikiwa imeshikiliwa na pua yake pana kama pua ya ng’ombe

"Sasa nyie mnaweza kurudi nyumbani hii kazi nitaimaliza mwenyewe. Kesho asubuhi tukutane Room 66 kwa ajili ya kuwapa mrejesho" Daktari Mkuu aliongea akiwatazama Daktari wenzake ambao nao walikuwa wakimtazama. Walitingisha vichwa vyao kuashiria kukubaliana na kauli yake, kisha wote wakatoka mule kwenye ile maabara na kuondoka kwenda makwao wakimuacha Daktari Mkuu hospitalini.


Ilikuwa yapata mida ya saa saba za usiku wakati Daktari mkuu akiwa yupo ofisini kwake ambapo ni Room 33, akifanya uchunguzi kwenye zile sampo alizozipata kutoka katika ile maiti kule maabara. Alichukua Darubini(Microscope) kifaa maalumu cha kimaabara kinachotumika kuangalia viumbe wenye maumbile madogo yasiyoonekana kwa macho. Alichukua yale maji maji aliyoyatoa kwenye uume wa ile maiti ambayo aliyalebo kama Sampo B. Kisha akaanza kufanya uchunguzi. Daktari alishtuka kile alichokiona kwenye Darubini. Alitoa macho kama mtu aliyeshangazwa na kile alichokuwa amekiona. Alipeleka macho yake tena kwenye darubini kuangalia sampo B. Aliacha tena. Kisha akachukua kalamu na kuanza kuandika kwenye kitabu kuhusiana na kile alichokiona katika hatua ya awali ya uchunguzi wake. Akiwa anaandika punde akasikia kitasa cha mlango wa ofisi yake kikicheza. Hapo akaacha kuandika akatazama Mlangoni, akaona bado kitasa kinacheza.

" Devis...! Devis.." Aliita jina la Mlinzi wa zamu wa siku hiyo ambaye alikuwa anaitwa Devis. Kwa muda ule alijua fika kuwa eneo hilo wapo wawili, yeye na Mlinzi, Devis.

Hata hivyo hakuna aliyemuitikia ingawaje kitasa bado kilikuwa kinacheza. Alinyanyuka kuelekea mlangoni, alipofika mlangoni alikumbuka bastola yake aliyokuwa ameiacha kwenye droo ya meza. Akarudi kuichukua. Tayari alikuwa na mashaka. Hali ilie haikuwa ya kawaida kwake kwani tokea aanze kazi Hospitalini humo haikuwahi kutokea jambo kama hilo. Alipokishika kitasa kikaacha kucheza. Akafungua na funguo mlango ukafunguka. Hamadi! Alishtuka akaanguka chini. Loooh! Alikuwa ni Popo Mkubwa aliyempiga usoni baada ya yeye kufungua mlango. Hapakuwa na mtu mwingine kwenye ile korido zaidi ya yule popo aliyempiga usoni, Yule popo alianza kuranda randa kwenye ile korido ambayo ilikuwa ndefu yenye milango mingi na mwanga wa taa. Daktari Mkuu alitembea kwa hatua fupi fupi huku akiangalia nyuma na mbele kwenye ile korido kuona kama ataona mtu lakini hapakuwa na mtu, na korido yote ilikuwa kimya mno. Kwenye ile korido kwa juu kulikuwa na taa moja ambayo kulikuwa na wadudu wadogo wadogo na vipepeo waliokuwa wanaruka kufuata mwanga . Daktari alitembea huku akijaribu kuita Devis mkononi akiwa kaishika vyema Bastola yake.

"Shiiti! ni mawenge ya usingizi? Mbona hakuna mtu wala dalili ya kuwa na mtu korido hii?"


Daktari Mkuu alipuuzia, aliona huenda ni usingizi ndio ulikuwa unamchanganya, Akaamua kurudi ofisini kwake, Room 33.

Alipokuwa akirudi mara alishtuka baada ya macho yake kuona jambo geni chini kwenye sakafu. Aliona karatasi ya rangi nyeupe ikiwa pale chini. Alishangaa ni kivipi alipita pale pale na hakuiona. Hata hivyo alijipa sababu kuwa huenda ni kutokana muda ule alikuwa na hofu, ukizingatia pia katarasi ile ilikuwa nyeupe. Aliiokota na kuigeuza upande wa nyuma ambapo alishangaa kuona picha ya ile maiti kwenye ile karatasi. Chini yake kukiwa na maandishi ya kitaalamu yenye alama nyingi za kikompyuta. Wasiwasi ulimuingia, nani aliyekuwa kaiangusha ile karatasi. Kwa nini ipo pale. Daktari alishika tena Bastola yake vizuri akageuka huku na huku lakini bado korido ilikuwa tupu ikimtazama.

Aliichukua ile karatasi akaenda nayo moja kwa moja ofisini kwake. Alipofika ofisini kwake alishangaa kukuta mabadiliko ya kuogopesha. Alishangaa kuona Darubini ikiwa imehamishwa kutoka pale alipokuwa ameiacha akaikuta ipo juu ya kabati wakati yeye alikuwa ameiacha juu ya meza. Akiwa anajiuliza maswali yaliyomfanya mwili wake kusisimkwa na kuhisi kuna hali isiyo ya kawaida inayoendelea, punde alihisi kitu kikigusa kichwa chake kwa nyuma huku sauti nzito isiyo na mzaha ikisema;

" Ukijaribu kuleta ujanja wowote nitapasua kichwa chako. Tulia hivyo hivyo tafadhali"

Hapo Daktari akaona tayari yupo chini ya mikono hatari. Maisha yake yapo hatarini.


************

Siku iliyofuata wa kwanza kufika katika hospitali ya Boreti alikuwa ni Dokta Festo. Ilikuwa ni kawaida kwa Dokta Festo kuwahi asubuhi na mapema. Hata Wafanyakazi wengine wa hospitali hiyo walimzoea kwa tabia yake ya kuwahi asubuhi . Dokta Festo aliingiza gari lake baada ya kufunguliwa na Devis ambaye ndiye aliyekuwa Mlinzi wa zamu.

" Mambo Vipi Devis" Dokta Festo alimsalimia Devis huku akifunga mlango wa Gari lake.

"Salama Kabisa. Naona kama kawaida yako"

" Hahaha! Acha maneno yako Devis. Kazi ni nyingi, usipowahi huwezi zimaliza"

" Kweli kabisa. Kama Watanzania wengine wangekuwa kama wewe, nchi hii ingefika mbali sana"

Wote wakacheka kisha Dokta Festo akaondoka kwenda ofisini kwake akimuacha Devis akifunga geti.

Ofisi ya Dokta Festo ipo Room 22 ambapo yeye ni Daktari wa Mfumo wa Neva.


Moja kwa moja aliingia kwenye jengo la hospitali ambapo alichukua uelekeo wa upande wa kushoto, Kulikuwa na korido ndefu yenye milango mingi. Kisha alifika sehemu yenye ngazi inayopandisha ghorofani akapanda, akatokea juu ilipo ghorofa ya kwanza. Akatembea kidogo kisha akasimama mbele ya mlango uliaondikwa Room 22, chini yake yalikuwepo maandishi yaliyosomeka NEUROLOGIST.

Alitoa funguo mfukoni kisha akaufungua ule mlango akaingia ndani. Alipoketi aliwasha Kompyuta iliyokuwa mezani. Kisha akawa anaandika jambo fulani. Ghafla aliacha kuandika baaada ya kukumbuka jambo. Alitoka upesi upesi moja kwa moja mpaka aliposimama mbele ya mlango ulioandikwa Room 33, chini yake yalikuwepo maandishi yalisomeka SURGEON GENERAL (ambaye ni Daktari Mkuu wa Upasuaji).

Dokta Festo alibisha hodi mara tatu lakini kulikuwa kimya. Alikishika kitasa cha mlango akakitekenya, Mlango ukafunguka. Akaingia ndani. Alishtuka kuuona mwili wa Daktari Mkuu ukiwa umelala chini kama Maiti.

" Dokta Beatus! Dokta...! Doktaa! Amka..! Nini kimetokea?" Dokta Festo aliita huku akimtingisha Dokta Beatus ambaye ni Daktari Mkuu wa hospitali hiyo, aliyekuwa amelala pale chini kama maiti.

" Devis..! Devis... Ooh! Shiiit! Nini hiki tena" Dokta Festo alimuita mlinzi lakini sauti yake haikutosha kumfanya Mlinzi asikie. Alitoa simu akabinya binya huku akiwa kachuchumaa pale chini alipokuwa amelala Dokta Beatus.

"Ndio Devis,. Njoo haraka huku juu. Dokta Beatus kapatwa na tatizo. Fanya haraka" Dokta Festo alikata simu baada ya kuwasiliana na Mlinzi, Devis. Dakika mbili hazikuisha Mlango ulifunguliwa na Devis aliingia.

" Kuna shida gani Festo?"

" Mwenyewe ndio nashangaa. Nimefika nimemkuta Dokta Beatus kalala hapa chini"

" Hee! Shida itakuwa nini? Vipi umeangalia kama ni mzima?"

Devis aliongea akiwa tayari amesogea alipochuchumaa Dokta Festo.

" Mapigo yapo chini sana" Dokta Festo alisema.

" Huenda alipatwa na shinikizo la damu" Devis aliongea akimtazama Dokta Festo aliyekuwa akimkagua Dokta Beatus aliyekuwa amelala pale chini.

" Tumbebe tukamlaze kwenye wodi ya Staff"

Dokta Festo aliongea na mara moja zoezi la kumbeba Dokta Beatus likaanza. Walimbeba mpaka ilipo Wodi maalumu ya Staff ambapo wafanyakazi wa Hospitali hiyo wakipatwa na matatizo hulazwa hapo.

"Habari za asubuhi Dokta Binamungu. Upo wapi? ahaa! Sawa. Fanya hima. Dokta Beatus amepoteza fahamu. Wee njoo tutaongea huku yote"


Dokta Festo alikata simu, alimtazama Dokta Beatus aliyekuwa amefumba macho pale kitandani walipomlaza. Devis alitoka upesi upesi baada ya kusikia honi ya gari kwa nje. Walijua aliyefika ni Dokta Binamungu ambaye ni Daktari mwenye cheo cha pili baada ya Dokta Beatus. Kitambo kidogo Dokta Binamungu alifika kwenye wodi ya Staff ambapo Dokta Festo alikuwepo akiwa anauchunguza mwili wa Dokta Beatus.

"Habari Festo. Poleni sana. Kwani imekuwaje?" Dokta Binamungu alisema.

" Tumeshapoa. Hata sielewi Binamungu. Kama unavyoona. Dokta Beatus tumemkuta amepoteza fahamu ofisini kwake"

" Jana si tuliagana na alikuwa mzima wa Afya kabisa au alikuambia anaumwa?"

" Hakuniambia kama anaumwa. Lakini mbona alikuwa sawa tuu" Dokta Festo alisema huku akimfungua jicho moja Dokta Beatus.

" Aisee! Kwa hiyo bado hujabaini tatizo ni nini?"

" Ndio nilikuwa namfanyia uchunguzi hapa. Ila nimegundua kuna kitu hakipo sawa"

" Kitu gani hiko? Lakini si atakuwa salama?"

Dokta Binamungu aliongea kwa hofu.

" Sumu..!"

" Imefanyaje? Dokta Festo mbona unanitisha"

" Sumu ndio imemfanya apoteze fahamu"

" Umewezaje kujua hilo?"

Dokta Binamungu aliongea akimtazama kwa makini Dokta Festo.

" Embu fungu macho yake utagundua hilo"

Dokta Festo alisema, Binamungu akafungua jicho moja la Dokta Beatus.

" Beatus anawezaje kujipulizia Sumu"

Binamungu aliongea akifunga jicho la Dokta Beatus.

"Lazima kuna kilichojificha. Hapa kuna jambo halipo sawa. Alafu hata ile maiti tunayoichunguza si unajua mazingira yake yalivyotata"

Dokta Festo aliongea akitazamana na Binamungu.

" Kwa hiyo unataka kusema kuna msaliti kati yetu? Mimi sidhani"

" Hudhani! Hatupo hapa kudhani. Hii kazi ni kubwa na ngumu. Usaliti kutokea ni kawaida"

Dokta Festo aliongea kwa ukali kidogo.

" Hivi umesahau mimi ni nani kwako? Umesahau nakuuliza? Unamfokea nani sasa? Festo unataka kunipanda kichwani?"

" Samahani Mkuu. Nimeghafilika. Haya mambo yanachanganya"

" Chunga adabu yako. Mimi ndio nimekuleta hapa. Sawa..?"

" Sawa Mkuu"

Kimya kidogo kilitokea wakati wawili hao wakigombana huku Dokta Beatus akiwa kalazwa akiwa hajitambui kitandani.

" Jana niliacha Wallet yangu kule Maabara. Embu kaniletee" Dokta Binamungu alisema akatoka na kumuacha Dokta Festo akiwa amesimama akimtazama Dokta Beatus aliyekuwa amefumba macho.


Dokta Festo naye akafuatia kutoka kisha akaenda moja kwa moja Maabara kuchukua Wallet aliyoagizwa na Boss wake. Alipofika alishtushwa mno mpaka akasahau alichokuwa ameagizwa. Hakuiona ile maiti waliyoifanyia uchunguzi jana usiku. Alitoka upesi akakimbia mpaka kwa Dokta Binamungu.

" Dokta.. Dokta.. Mwili haupo. Cadava haipo" Dokta Festo aliingia ofisi ya Binamungu kwa papara akihema kwa pupa kama Panya aliyekoswa na mtego.

" Unasema nini Festo?"

" Cadava haipo" Bado anahema kwa pupa.

" Unauhakika kuwa haipo Festo. Embu acha mzaha"

" Nimefika pale... Nikashangaa jokofu lipo tupu bila ya mwili"

Festo aliongea akiwa anakiwewe. Dokta Binamungu alitoka bila kusema chochote, Festo naye akamfuata nyuma nyuma, Wote wakaelekea Maabara.

"Tumekwisha! Nani atakuwa amechukua huu mwili?" Binamungu alisema,

" Devis anakesi ya kujibu. Yeye analinda nini ikiwa maiti zinaibiwa humu ndani"

Binamungu alisema tena huku akiangaza macho yake mule ndani. Dokta Festo hakuwa na majibu.

" Huu mlango uliukuta wazi?" Binamungu aliuliza.

" Hapana, Niliukuta umefungwa. Nilifungua kwa funguo ulizonipa" Festo alijibu.

" Mimi na Dokta Beatus ndio tunafunguo za maabara hii. Embu twende huku" Binamungu aliongea, wakatoka. Moja kwa moja waliingia chumba maalumu cha Mitambo ya Kamera ambacho ni room 44. Hapo wakafungua Mtambo maalumu wa kukusanya video na picha zote zilizorekodiwa kwa usiku mzima.

" Haufunguki bila Nywila(Password) Shiit" Binamungu aliongea huku akitazama kioo kikubwa cha ule mtambo ambacho kilimtaka aweke Password.

" kuna njia nyingine naweza kuufungua huu mtambo bila hata hiyo Password" Festo alisema akimtazama Binamungu.

" Embu ifanye hiyo njia haraka haraka tuone kilichotokea usiku"

"Nadhani tungemsubiri Mr. Darmian kuliko kufanya hivi bila ruhusa yake" Festo aliongea kwa sauti ya kuogopa lakini akijua kile anachosema yupo sahihi.

" Hivi wewe Unaakili kweli? Yaani tumsubiri mtu ambaye hatujui leo kaamkaje. Embu fungua huo mtambo. Mimi si ndio mkuu wako? alafu tangu lini nikikupa maelekezo unapinga, haya fungua upesi" Binamungu alifoka na kumuamrisha Dokta Festo afungue ule Mtambo wa Kamera.

Festo alikosa chaguo ikabidi afungue ule mtambo wa kurekodia Video na picha za eneo la hospitali. Dakika tano mtambo ulifunguka. Na video zikaanza kuonekana.

" Rudisha kuanzia mida ya saa saba za usiku baada ya sisi kuondoka" Binamungu alisema, Kisha Festo akafanya kama alivyoagizwa.

Video ilimuonyesha Dokta Beatus akifanya vipimo vya zile Sampo walizozitoa kwenye ile maiti. Waliona pia Dokta Beatus akishtuka baada ya kuona kitasa kinacheza.

" Embu chezesha upande wa kwenye korido tuone aliyekuwa anachezea kitasa" Binamungu alisema na Festo akafanya kama alivyoagizwa.


Wakashtuka kumuona Mtu aliyevalia nguo nyeusi akiwa kaufunika uso wake kama Ninja. Punde walimuona akitoka upesi pale mlangoni na kuingia chumba kingine. Alivyomalizikia walimuona Dokta Beatus akifungua mlango akishangaa huku na huko kwenye ile korido. Hakuona mtu. Waliona kila kitu mpaka Dokta Beatus alivyorudi ofisini kwake akakuta Darubini yake imehamishwa na kuwekwa kwenye Kabati. Hatimaye walishtuka kuona yule mtu aliyevaa kininja akitokea kwa nyuma akiwa kamuwekea Bastola kichwani Dokta Beatus.

" Hamtaweza kufanikiwa Kukwamisha mipango yetu"

Walimsikia yule mtu akimuambia Dokta Beatus.

" Ninyi ni akina nani? Mnataka nini?" Dokta Beatus aliuliza.

" Sio kazi yako kujua mimi ni nani"

Yule mtu aliyevaa kininja alimjibu Dokta Kwa dharau.

" Mnataka nini kwangu?" Dokta Beatus aliongea, lile jitu likamzaba kofi la kichwa, Dokta beatus akadondoka chini. Kisha kwa wepesi yule mtu aliyevalia kininja akatoa kitambaa kutoka katika mfuko wa suruali yake, akamziba Dokta Beatus puani. Matukio yote haya yalikuwa yanaonyeshwa kama mkanda wa filamu kwenye ule mtambo wa kurekodia, Wakina Dokta Binamungu na Festo walibaki wamepigwa na butwaa kwa yale waliyokuwa wanayaona. Kila mmoja alitamani amjue mtu yule aliyevalia kininja kuwa ni nani. Walitamani ile baroka aliyoivaa usoni idondoke na sura yake iwe dhahiri lakini hilo halikutokea.

Punde mtambo ulimuonyesha yule mtu akimuachia Dokta Beatus baada ya kuona amepoteza fahamu. Kile kitambaa bila shaka kilikuwa na sumu ya kumfanya mtu azirai. Yule mtu alielekea mahali ilipo Darubini kisha akachungulia kama alivyokuwa anafanya Dokta Beatus, akaacha. Kisha alichukua zile Sampo A na B na kuziweka kwenye mfuko mweusi alioutoa katika mfuko wa suruali yake. Alipomaliza, alianza kukagua kagua ofisi ya Dokta Beatus mahali ilipokabati. Alichakura chakura mafaili kisha akayarudishia vizuri kama alivyo yakuta.


Akasimama kama mtu anayetafuta kitu alichokisahau au kama mtu ambaye hataki kusahau jambo. Hapo akaona kijitabu juu ya meza, kilikuwa kimefunguliwa na katikati ilikuwepo kalamu. Yule mtu aliyevalia kininja akainama kisha akasoma kilichopo kwenye kile kitabu. Akachana ile karatasi akaiweka kwenye mfuko wa Suruali. Dokta Binamungu na Festo waliyaona hayo yote. Walitulia ungedhani wanatazama filamu ya kusisimua. Ukimya wao uliashiria jambo moja. Nalo ni udadisi na uchunguzi wa hatua zote za mtu yule. Walimuona yule mtu Ninja akitoka kwenye ofisi ya Dokta Beatus lakini walishangaa kumuona akirudi haraka kama mtu aliyesahau jambo. Hii iliwafanya wavute umakini wao kumtazama kuona ni kitu gani alichokuwa amekisahau.

Yule mtu Ninja alifika ilipomeza akaishika Darubini kama mtu anayeikagua. Jambo hilo Walilielewa akina Dokta Binamungu na Festo. Walijua alichokuwa anakitafuta mtu yule. Sura zao zilibadilika mno, ni kama walikuwa wakiomba dua yule mtu asifanikiwe. Lakini dua lao lilikuwa kama dua la kuku ambalo katu halimsogelei Mwewe.

Yule mtu alibinya sehemu fulani kwenye ile Darubini, kikatoka kitu mfano wa Chipu.

" oooh! tumekwisha. Tupo uchi jamani. Sijui itakuwaje" Dokta Binamungu aliongea akiwa kachanganyikiwa huku uso wake ukiendelea kumtazama yule mtu Ninja kupitia video ya ule mtambo. Yule Ninja alitoka, moja kwa moja alielekea ilipomaabara.

" Huyu mtu aliwezaje kujua kwa urahisi mahali maabara yetu ilipo? Hii inawezekanaje?"



Endelea...

" Huyu mtu aliwezaje kujua kwa urahisi mahali maabara yetu ilipo? Hii inawezekanaje?"

Dokta Festo aliongea baada ya kumuona yule mtu akitembea kwa hatua makini kuelekea room 55 ilipomaabara. Yule mtu alitoa funguo Malaya akafungua mlango wa maabara kisha akazama ndani. Wala hakupata shida kuufungua ule mlango. Hapo alifika moja kwa moja lilipokuwa lile jokofu maalumu la kiuchunguzi ambalo ndani yake ilikuwepo ile maiti iliyokuwa ikichunguzwa usiku wa jana.

Yule mtu alipiga Saluti na kupiga ishara ya kijeshi mbele ya ile maiti. Jambo hilo liliwafanya akina Dokta Binamungu kushangaa, maswali yalikuwa ni mengi yaliyopiga vichwa vyao. Kwa nini mtu yule aipigie ile maiti saluti. Inamaana ilikuwa maiti ya kiongozi mkubwa au jemadari wa kijeshi. Sintofahamu iliwashika. Punde walishangaa kumuona yule Mtu Ninja akiwa anakikagua kile chumba, alikuwa akitafuta jambo fulani. Hatimaye aliona Kamera, sasa akawa anaitazama ile kamera iliyokuwa mule ndani jambo lililofanya akina Binamungu waone kama wanatazamana naye. Kisha akachomoa Bastola yake akaipiga risasi ile kamera, video ikawa na giza. Akina Binamungu hawakuweza kumuona tena kwenye video.

" Huyu mtu atakuwa ni nani hasa?" Dokta Binamungu alijiuliza, kwa sauti isiyohitaji jibu.

"Huyo anatoka na ile maiti" Festo aliongea baada ya kuwasha video ya koridoni ambapo walimuona yule mtu akitoka maabara akiwa amebeba ile Maiti. Yule mtu aliiona tena kamera akaipiga risasi ikazima. Hali iliyowafanya kina Binamungu kutokumuona tena.

"Tupo uchi Festo, sijui hata itakuwaje"

" Kivipi? Mbona sikuelewi"

" Huwezi elewa. Ila mpaka sasa mambo ni magumu. Sijui hata Kamanda atatuelewa"

" Huyu mtu atafutwe haraka iwezekanavyo. Tukimkamata atajuta"

Dokta Festo aliongea huku akizima ule mtambo wa kurekodia video na picha.

" Embu tuondoke, twende Wodini alipo Dokta Beatus huenda amezinduka"

Dokta Binamungu alisema, wakatoka moja kwa moja mpaka wodini alipokuwa Dokta Beatus. Walimkuta bado akiwa hana fahamu, Walimuacha wakaondoka.


*************


Tayari ilikuwa imehitimu Saa tatu alfajiri. Wafanyakazi wote wa Hospitali ya Boreti walikuwa wakiendelea na shughuli zao.

Room 66 kulikuwa na kikao cha watu kumi, Wawili walikuwa wamevaa Sare za jeshi, mmoja alikuwa kavaa mavazi ya kawaida, Alikuwepo na Mwanamke mmoja mrembo aliyevalia suruali nyeusi na blauzi ya rangi ya udongo, wakiwepo na Madaktari sita. Agenda kuu ya kikao hiki ilikuwa ni Kuibiwa kwa Maiti ya uchunguzi, kuibiwa kwa sampo A na B za uchunguzi, kuibiwa Chipu ya Darubini, na kupigwa kwa Dokta Beatus. Kilichowaumiza vichwa zaidi ni kitendo cha kuibiwa kwa ile Chipu ya Darubini, Ambayo ilikuwa na siri nyingi ambazo kama zikifahamika zinaweza athiri mipango yao.

"Kama mlivyoona hapo kwenye video iliyorekodiwa. Tumevamiwa na kuibiwa. Mpaka sasa hakuna hatua yoyote tuliyochukua dhidi ya adui yetu" Kamanda Aliongea kisha akaweka kituo akisafisha koo lake.

"Adui anaonekana anaujuzi wa kijeshi, na huenda sio mgeni katika jengo hili. Pengine miongoni mwetu yupo msaliti anayetoa mambo yetu au aliyeuza ramani ya jengo hili" Kamanda anakohoa kidogo kisha anaendelea kuongea.

" Je kuna yeyote anayeweza kusema lolote?" Kamanda aliuliza akiwatazama wanakikao waliokuwa wametulia, nyuso zao zikiwa na hofu ya kile kilichotokea.

"Hii ni aibu kabisa. Ikiwa eneo letu linavamiwa kirahisi hivi. Vipi raia wa kawaida? Hakikisheni Habari hii isitoke nje. Sawa..!"

"Ndio Afande" Wote wanaitikia. Kisha Kamanda anatoka lakini kabla hajafika mlangoni anasimama na kugeuka nyuma.

"Sajenti Warioba, Kamanda Fernanda.."

" Ndio Mkuu" Sajenti Warioba na Fernanda waliitikia, Kamanda mkuu aliwaonyesha ishara, kuwa wamfuate. Kisha wakatoka wakiongozana moja kwa moja mpaka nje. Wakapanda ndani ya Gari wakaondoka. Wakiwa ndani ya gari ukimya ndio ulikuwa umetawala. Kamanda Mkuu aliendesha gari akiwa mwingi wa mawazo. Sajenti Warioba na Fernanda Waliiona hali hiyo. Walimjua fika Kamanda Mkuu akiwa katika hali hiyo asivyopenda mzaha. Maneno maneno kwa muda ule hayakuwa na nafasi, tena huweza yakakugharimu. Gari ilikuwa bado ipo kwenye mwendo. Wakwanza kuvunja ukimya alikuwa ni Kamanda Mkuu.

" Fernanda..!"

" Ndio Mkuu"

"Unafikiri ni akina nani waliovamia na kuiba Chipu ya Darubini"

" Bado sijafahamu Mkuu"

Sauti ya Fernanda ilikuwa ya woga sana. Ilikuwa ni haki yake kwa maana kamanda mkuu akiwa katika hali ile huweza kufanya lolote. Kamanda mkuu alitoa sigara wakati akiendelea kuendesha gari, akaanza kuvuta huku moshi akiuelekezea dirishani.

" Warioba..!"

" Ndio Mkuu"

" Unafikiri ni akina nani wanaoweza kuja kuvamia na kuiba chipu ya darubini katika eneo letu?"

" Mkuu bado natafakari, sijafahamu"

" Hivi nyie mnaakili kweli. Mpaka muda huu msijue ni akina nani walioiba Cadava na chipu..! Bado mnataka muitwe Makamanda? Hivi mnajua nchi inawategemea ninyi kwa kiasi kikubwa, alafu ati hamjui mpaka muda huu nini kinachoendelea?"

Kamanda Mkuu aliongea kwa ukali, moshi wa sigara ukimzingira usoni. Sajenti Warioba na Fernanda walibaki kimya bila ya kujibu. Walijua Kamanda Mkuu alichohitaji muda ule ni majibu ya walioiba Cadava na chipu na sio maneno mengine. Walijua fika maneno mengine yangeweza kuwasababishia madhara ikiwezekana hata kifo. Walifika kwenye Hotel iliyokatikati ya jiji la Dar es Salaam wakaingiza gari lao kisha wakashuka, moja kwa moja wakakaa kwenye kona iliyojificha kiasi. Watu walikuwa wakiwashangaa sana kutokana na kuona Vazi la kijeshi lililovaliwa na Kamanda Mkuu. Fernanda ndiye yule mwanamke aliyekuwa amevalia Suruali nyeusi na Blauzi ya rangi ya udongo. Sajenti Warioba yeye alivalia kawaida.

Baada ya kuletewa vinywaji walianza mazungumzo kuhusiana na tukio zito lililotokea.

" Miongoni mwetu kuna msaliti. Anaweza kuwa mtu yeyote. Msaliti huyu ni lazima adhibitiwe kabla hajafika mbali" Kamanda Mkuu aliongea, akachukua Glass ya wine akameza mafumba mawili.

" Ninyi ni vijana wangu ninao waamini. Hamjawahi kuniangusha katika majukumu niliyowahi kuwapa. Naamini hata hili mtalimudu. Tupo pamoja?"

"Ndio Mkuu, tupo pamoja" Sajenti na Fernanda waliitikia kwa pamoja kama mtu mmoja.

" Hii ni nchi yenu. Ipiganieni. Kazi hii inaweza isiwe rahisi, lakini pia isiwe ngumu, ugumu wa kazi hii utategemea zaidi ujuzi wenu na uwezo wa kumtambua msaliti, tukishamfahamu msaliti basi kila kitu kitakuwa kipo sawa. Nadhani kazi hii mtaifanya kwa ukamilifu na kwa haraka sana. Nipo sawa? "

" Ndio Mkuu" Waliitikia na wote wakagongeana Glass kama ishara ya kuwa pamoja. Lakini katika hali isiyotarajiwa ghafla walianza kulewa, Vinywaji ni kama viliwekwa madawa ya kulevya. Kwa hali ya kawaida isingewezekana wao kulewa kutokana na vinywaji walivyokuwa wamechukua ambavyo havikuwa na kiwango kikubwa cha kilevi kuwafanya walewe. Sasa nini kilikuwa kimetokea na kuwafanya walewe, nani aliyekuwa kawawekea madawa ya kulevya ukizingatia wao ni watu wakubwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. Dakika tano zilitosha kuwafanya wasinzie, wote walikuwa wamepoteza fahamu.




Masaa mawili baadaye walijikuta wapo kwenye chumba wakiwa wamefungwa mikono na miguu huku midomoni wakiwa wamefungwa na kitambaa kilichokuwa kimekazwa vizuri ili wasiweze kuzungumza wala kutoa sauti. Mazingira ya chumba yalikuwa ya kawaida, lilikuwepo dirisha moja lenye pazia la rangi ya kijivu, ambalo liliingiza mwanga hafifu kutokana na pazia kuziba dirisha na kuzuia mwanga kuingia katika chumba kile. Hapakuwa na kitu kingine kwenye kile chumba zaidi yao, hii ilimaanisha kuwa chumba kile kilikuwa tupu kabla ya wao kuingizwa mule ndani. Hilo pengine lisingewapa hofu, lakini haikuwa hivyo, kuta za chumba kile zilikuwa zinatisha kama nini, hata ingekuwa ni wewe kwa hali ya kuta zile zilivyokuwa nakuhakikishia ungeogopa sana. Licha ya kuwa wao walikuwa ni wanajeshi tena makomando waliofuzu mafunzo ya juu kabisa lakini michoro ya kuta za kile chumba ilitia ganzi ya hofu nyoyo zao.

Michoro ya mafuvu ya watu ilikuwa inatisha jamani, mchoraji wa picha zile alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuchora picha za mafuvu yanayotisha sana. Mara kwa mara Fernanda alikuwa akifumba macho yake kila alipoona mchoro alioona unamtishia. Looh! Mamaa weee! Jamani kuna mchoro ulikuwa unatisha duniani hujaona, ulikuwa ni mchoro wa mtu anayechinjwa huku matumbo yakiwa nje huku akitoa macho ambayo yalikuwa yanatisha vibaya sana. Michoro hiyo iliwaambia jambo moja tuu, kuwa wapo mahali hatari, mahali ambapo wanaweza kupoteza maisha.


Kamanda Mkuu alinguruma kwa sauti kama beberu kuwashtua Sajenti Warioba na Fernanda, na wote wakatazamana. Hawakuweza kuongea kutokana na kamba zilizokuwa zimefumba midomo yao. Waliwasiliana kwa njia ya ishara ya macho huku wakitingisha vichwa vyao, Hizi ni ishara za kijeshi endapo mtu akitekwa na kufumbwa mdomo wake asiongee, basi hutumia macho na vichwa kuzungumza kwa ishara. Walipatana wafanye kila wawezalo watoke mule ndani. Kwa upesi, Sajenti alijiviringa kama tairi mpaka alipo Fernanda, kumbuka wote wamefungwa miguu, na mikono kwa nyuma, pia mdomo nao umefungwa na kamba hivyo ni ngumu kujifungua. Watajiokoaje embu nawe jiulize maana ingekuwa afadhali endapo midomo yao ingeachwa bila kufungwa basi wangeitumia kufungulia zile kamba ngumu walizokuwa wamefungwa mikononi na miguuni.

Sajenti Warioba aliibinjua mikono yake iliyokuwa imefungwa kwa nyuma akaipeleka mbele. Kisha akamsogelea Fernanda akashika nywele zake, akakitoa kibanio cha nywele kilichokuwa kimebana nywele za Fernanda. Alafu akaanza kukitumia kile kibanio kukata kamba alizofungwa Fernanda mdomoni. Haikuchukua dakika mbili, kamba ikafunguka, Fernanda alihisi ganzi mdomoni baada ya kamba kufunguliwa. Bila kupoteza muda, Sajenti alimnyooshea mikono Fernanda ili amfungue na mdomo wake kwa kutumia meno, kitambo kidogo mikono ya Sajenti Warioba ilikuwa huru, hapo akajifungua kamba ya mdomoni na miguuni, kisha akawafungua wote lakini kabla hajammalizia kumfungua kamanda Mkuu, ghafla walisikia watu wakija. Hapo Sajenti ikabidi afanye haraka haraka kuzikata zile kamba za mikononi zilizomfunga Kamanda Mkuu. Muda huo Fernanda alikuwa yupo mlangoni akiwa kajiandaa kumvamia yeyote atakayejitokeza. Ulikuwa muda wa vita, muda wa kukimbia chumba kile ambacho kilifanana na kuzimu.

Mlango uliguswa na kitasa kikatekenywa, punde mlango ulifunguliwa na mdomo wa bunduki ndio uliokuwa umetangulia ndani huku aliyeishika akifuatia. Kwa upesi Fernanda alimpokonya mshika bunduki na kumpiga teke la taya Yule hasimu akapiga ukutani, huku wenzake wakitaka kumshambulia Fernanda lakini walikuwa wamechelewa, kabla risasi haijalia walijikuta wote watatu wakiwa wamelala sakafuni huku damu zikiwatoka sehemu mbalimbali za miili yao. Walikuwa wameshakufa. Lilikuwa ni tukio ambalo halikumaliza sekunde thelasini lililonyonya roho za wale mahasimu watatu.


Tayari Kamanda Mkuu alikuwa keshafunguliwa kamba zote, walipongezana kisha muda wa kuondoka ulikuwa umefika.

“Mmefanya kazi nzuri sana, sasa tuondokeni humu bila shaka wengine wanakuja, hii milio ya risasi lazima itakuwa imewashtua. Haya tuondoke” Kamanda Mkuu alizungumza kwa sauti ya kawaida yenye kushukuru lakini pia yenye amri.

Walitoka kila mmoja akichukua silaha za wale mahasimu waliokufa pale chini. Kwa tahadhari wakaingia ilipokorido fupi iliyokuwa inakatisha kushoto hapo walilakiwa na kundi la watu waliokuwa wanakuja Mkukumkuku, vita ikaanza ya kurushiana risasi. Walipiga risasi huku wakijibanza kwenye kona kukwepa risasi za wale mahasimu ambao mpaka muda huo hawakujua ni watu gani, hawakujua ni kundi gani, na kwa nini liwateke wao.

Hapo Sajenti Warioba akawaacha,akarudi kwenye kile chumba walichokuwa wamefungwa, akafungua pazia la lile dirisha, akaona kwa nje kuna uzio wa ukuta uliokuwa umezunguka nyumba ile. Hakuona msaada wowote Kupitia lile dirisha, alidhani kwamba dirisha lile lingewaruhusu wao kupita lakini haikuwa hivyo. Dirisha lilikuwa la Grili pasipo na mbao. Hapo akarudi kule kule kwenye vita kuwasaidia wenzake. Vita ya kutupiana Risasi ilidumu kwa dakika thelasini mpaka pale sauti ya helikopta iliposikika kwa nje. Mahasimu tisa waliuawa pale pale huku wengine wakikimbia baada ya ndege ya kipolisi kufika. Upande wa nje, walimkamata hasimu mmoja aliyejeruhiwa vibaya na risasi, kikosi cha polisi cha anga, na ardhini kilikuwa kimeshatia timu. Na hii ndio ikawa pona pona ya kina Sejenti na wenzake.

************


‘’Hakikisheni mnamlinda huyu, huu ndio ushahidi ambao tunaweza kuwajua adui zetu, ndio ushahidi wa haraka wa kujua ni nani miongoni mwetu ni msaliti. Sitaki kusikia uzembe wowote. Itawagharimu” Kamanda Mkuu alisema kisha akatoka.

Kamanda Mkuu aliamua kwenda nyumbani kwa Dokta Beatus ambaye alikuwa akiishi SINZA MORI. Ndani ya nusu saa alikuwa ameshafika mbele ya geti kubwa jeusi, alishuka ndani ya gari akaenda kuligonga geti, kitambo kidogo geti lilifunguliwa na msichana mdogo mwenye umri unaokadiriwa miaka kumi na sita ambaye alikuwa amesuka rasta kichwani. Alikuwa ni mtoto wa Dokta Beatus ambaye hata Kamanda Mkuu alikuwa akimfahamu.

“Ahh! Kumbe ni Baba. Shikamoo Baba Mkubwa” Binti alisalimia

“Marhaba Ansola, hujambo”

“Sijambo, karibu ndani Baba” Ansola aliongea kwa sauti ya adabu na ukarimu, akamkaribisha Kamanda Mkuu ndani.

“Shukrani sana, Vipi nimemkuta mzee?”

“Yupo ndani, tena ndio alikuwa anataka kutoka”

“ Haah! Basi atakuwa anaendelea vizuri, nilifikiri muda huu ningemkuta amelala” Kamanda Mkuu alisema tayari walikuwa wameufikia mlango wa sebuleni. Ansola alifungua mlango kisha wakaingia ndani.

“Aaaah! Kamanda..! Karibu sana Mheshimiwa” Dokta Beatus alisema huku akimpelekea mkono Kamanda Mkuu kumsalimia.

“Ahsante sana Dokta, Pole sana, vipi unaendeleaje Dokta” Kwa sauti ya kutoa pole Kamanda mkuu aliongea huku wote wakikaa na Ansola akiwaachia Sebule.

“ Mungu ni mwema Mkuu, Yaani wee acha tuu. Ninaendelea vizuri, ungechelewa kidogo usingenikuta, nilikuwa natoka naelekea Hospitalini”


“ Aisee! Hivi ni nani Yule mtu aliyekuvamia siku ile, je hukufanikiwa kabisa kumtambua?” Kamanda Mkuu alisema sauti yake ikiwa ya udadisi na hamasa ya kumjua mtu aliyemzimisha Dokta Beatus, kisha akaiba chipu ya Darubini na kuiba Cadava.

“ Mkuu, mpaka sasa hivi sifahamu ni nani aliyekuja siku ile akanivamia, tena akaiba chipu, cadava na sample zetu ambazo zingetusaidia kupata majibu ya kile tunachokitafuta” Dokta Beatus alisema akimtazama Kamanda Mkuu.

“Nani atakuwa nyuma ya jambo hili? Sisi tulileta Cadava kwenye hospitali ya Boreti tukijua kuwa huku hakuna atakayejua, hata adui zetu wasingeweza kuhisi kuwa uchunguzi huu ungefanyikia katika hospitali hii. Haiwezekani, lazima kuna mmoja wetu katusaliti. Cadava imeibiwa, chipu ya Darubini imeibiwa, sampo za vipimo zimechukuliwa, unafikiri Mhe. Rais akijua jambo hili itakuwaje. Ile chipu imebeba siri nyingi Dokta..” Kamanda Mkuu aliongea sauti ya kulalamika na kukata tamaa.

“ Yule mtu alikuwa na sauti nzito kama mzimu lakini kilichonishangaza mikono yake aliponishika kabla sijapoteza fahamu ilikuwa ni mikono laini kama ya mwanamke anayetumia mafuta ya kulainisha ngozi. Nahisi alivaa kitu cha kuibadilisha sauti yake ili kupoteza uhalisia…..” Dokta Beatus alipiga mwayo kisha akaendelea;

“ Inaonekana ni mwanamke aliyepitia mafunzo ya kikomandoo, kwa maana alikuwa mwepesi sana, tena mjanja” Dokta Beatus alisema.

“ Mmmh! Haiwezekani kabisa, Dokta Beatus Yule mtu nilimuona Kupitia video ya Mtambo wa Hospitali, hawezi kuwa mwanamke. Kwanza utembeaji wake ulikuwa kama mwanaume, pia hata alivyobeba Ile Cadava begani, alibeba kama mwanaume. Yule hawezi kuwa mwanamke, nilimuona hata mimi” Kamanda Mkuu aliongea kwa sauti ya kutetea kile anachokiamini.

“ Kamanda Mkuu, hata marashi yake yalikuwa ya kike, ninauhakika Mkuu Yule alikuwa mwanamke”

“Sawa tuachane na hayo, Kuna mateka mmoja nimemuacha hospitalini, mpaka sasa huyo ndiye tunamtegemea anaweza kutupa mahali pakuanzia, Ngoja nikuache lakini kama kutakuwa na jambo lolote utakalohisi litasaidia usisite kunijuza Dokta” Kamanda mkuu alisema kisha akaondoka.


Akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake ambapo alikuwa akiishi Goba, mawazo mengi yalimjia. Maneno ya Dokta Beatus yalimfanya ahisi kuchanganyikiwa. “Mwanamke aliyepitia mafunzo ya Kikomandoo” alirudia maneno aliyoyasikia kwa Dokta Beatus. ‘Huyo mwanamke ni nani, ametumwa na nani, mbona anaujasiri mkubwa kiasi hicho, haogopi? Haiwezekani na wala hayupo mwanamke kama huyo’. Kamanda Mkuu alisema kwa sauti ya chini chini huku akielekea nyumbani kwake. Muda huo alikuwa amefika Mwenge.

Alichukua simu yake akabonyeza bonyeza kisha akaiweka sikioni;

“Marhaba, sasa ikifika saa mbili usiku uende hospitali ya Boreti ukamlinde Yule Mateka, hakikisha hatoroki wala mtu yeyote haji kumtorosha, nakuaminia sana, tafadhali naomba usije kuniangusha. Haya jioni njema” Simu ikakatika, Kamanda Mkuu akachukua sigara yake kisha akaiwasha akawa anavuta huku mawazo mengi yakipambana na moshi wa sigara aliyokuwa akiivuta. Aliwaza itakuwaje Rais akigundua habari ile ambayo moja kwa moja alijua hataeleweka. Hakutaka kuonekana mzembe ikiwa Mhe. Rais alimuamini na kumpa kazi hiyo. Pia jambo lile litamfanya apoteze kazi ikiwezekana kupewa adhabu kali ya uzembe.




Sajenti Warioba aliitazama saa yake ya mkononi iliyomuambia ni saa moja na robo usiku. Muda ulikuwa umefika, aliamka kitandani kisha akavaa suruali nyeusi ya kadeti na tisheti ya rangi ya udongo juu yake akavaa jacketi. Aliifungua Bastola yake kuikagua kuona kama inarisasi, ndio ilikuwa na risasi za kutosha. Akaifunga na kuiweka kibindoni. Alitazama tena saa yake ya mkononi, alishtuka kuona ni saa moja na nusu, looh! Muda ulikuwa umeenda sana. Hapo kwa upesi alichukua viatu vyake na kutoka nje, giza tayari lilikuwa limeingia. Alichukua pikipiki yake aina ya Boxer 150 na kuacha eneo la nyumba yake iliyoko Mikocheni. Hospitali ya Boreti ilikuwa maeneo ya Upanga, aliendesha kwa mwendo wa kasi mpaka alipokaribia eneo la hospitali ndipo alipopunguza mwendo. Umbali wa mita thelasini aliliona gari jeusi Aina ya Verosa likitoka kwenye Geti la hospitali, alipishana nalo kisha akageuka nyuma kulitazama, hapo akashtuka, lile gari halikuwa na Plate namba. Moyo wake ulilipuka kwa wasiwasi huku akili yake ikipoteza utulivu. Tayari hisia mbaya zilishalamba nyayo za ubongo wake, alihisi huenda kuna jambo la hatari limeshatokea hospitalini, nalo ni kutoroshwa kwa mateka.


Bila kupoteza muda aliendesha pikipiki yake na kuingia ndani ya geti la hospitalini, Hakuona mtu kwenye chumba anachokaa mlinzi pale getini jambo ambalo sio kawaida kabisa chumba hiko kutokuwa na Mlinzi. Kengele ya hatari iligonga katika kichwa chake, mazingira yale yalimuambia kuwa kuna tukio baya limefanyika kitambo kidogo kilichopita. Aliangaza macho yake huku na huko katika eneo la nje la hospitali, taa zilizokuwa zikiwaka zilimsaidia kuona. Alichomoa bastola kisha akaanza kutembea kuelekea ulipo mlango mkuu wa kuingia hospitalini. Alitembea kwa kunyata bila kusababisha sauti, punde si punde alishtushwa na kitu kisicho cha kawaida alichokiona umbali wa hatua kumi kwenye lango la kuingia hospitalini. Mapigo ya moyo wake yalikimbia upesi kama upepo wa kiangazi. Mwili ulimsisimka, akili yake ilimlaumu kwa kuchelewa, kama angefika nusu saa kabla huenda mambo yale yasingetokea lakini siku zote majuto ni mjukuu. Ulikuwa ni mwili wa mtu uliokuwa umelala sakafuni baada tuu ya lango la kuingia hospitalini. Mwili ule ulikuwa umelala kifudifudi ukiwa na sare ya mlinzi wa ile Hospitali. Sajenti aliusogelea kwa tahadhari huku akiwa ameishika bastola yake kuuelekezea ule mwili, tayari alikuwa ameshaukaribia, akaugusa na buti lake akiwa kaunyooshea bastola. Sajenti aliubinua chali, Alikuwa ni Devis, Mlinzi wa hospitali ya Boreti ambaye alikuwa ameshauawa. Mwili wake bado ulikuwa wa moto kumaanisha kuwa tukio limefanyika muda mfupi uliopita. Hakuwa na Kovu lolote mwilini mwake, je Devis alipuliziwa sumu? Hapana, haikuwa hivyo, Sajenti alipomkagua vizuri aligundua kuwa Devis aliuawa kwa kuvunjwa shingo yake. Sajenti aliondoka upesi kwa tahadhari kuelekea wodi maalumu aliyokuwa amelazwa Mateka wa Ushahidi. Alipanda kwenye ghorofa ya pili, njiani mashaka yalizidi alipoona miili miwili ya watu waliouawa. Mmoja alivalia kidaktari wakati mwingine akiwa na mavazi ya kawaida, alipowakaribia wale watu waliouawa aligundua Yule mtu alievalia mavazi ya kawaida alikuwa ni moja ya walinzi walioachiwa wamlinde Yule mateka wa ushahidi. Kufikia hapo Sajenti alipandwa na kiwewe cha kukata tamaa, aliharakisha mpaka alipofika kwenye mlango ilipowodi alipokuwa amelazwa Yule mateka. Alijiweka sawa, kisha taratibu kabisa akashika kitasa cha mlango na kuufungua kwa tahadhari huku akili yake ikimuonya.

Alishangaa kuona miili minne ya watu waliouawa, mmoja ulikuwa upo karibu na kitanda alichokuwa amelazwa Yule mateka wa ushahidi, alimsogelea, looh! Alisikitika sana kuona mtu Yule jinsi alivyouawa kifo cha kikatili, shingoni alikuwa amenyongwa na mpira wa dripu, bila shaka ni dripu alilokuwa ametundikiwa Yule mateka wa ushahidi. Kitanda kilikuwa kimetapakaa damu, Sajenti aliishiwa nguvu, alibaki anaitumbulia macho ile miili mingine mitatu. Sajenti aligundua kuwa wawili walikuwa Madaktari na wawili walikuwa ni walinzi walioachwa na Kamanda Mkuu mchana ambao walipaswa wamlinde Yule mateka mpaka pale Sajenti atakapokuwa amefika. Maswali mengi yalifanya kichwa chake kianze kuuma, alijiuliza inawezekanaje walinzi wote wauawe kirahisi namna hii. Sajenti alikuwa anajua fika kuwa walinzi wa Hospitali ya Boreti ni Makomandoo wenye mafunzo ya hali ya juu ambayo waliyachukulia nje ya nchi. Sasa iweje wauawe kirahisi kama vile. Hii ilimfanya aone waliofanya tukio lile baya kuwa ni watu wenye ujuzi wa kijeshi na wenye mafunzo makali ya kikomandoo.


Sajenti alichoka mwili na akili, sasa atamuambia nini Kamanda Mkuu, alijua kuwa Kamanda mkuu alikuwa anamuamini sana. Hakuwahi kutumwa kazi akafeli kwenye misheni alizopewa tokea aingie kwenye kazi ya Ujasusi na masuala ya ulinzi na usalama. Alikumbuka baadhi ya operesheni zake ngumu alizowahi kuagizwa na akazifanya kwa weledi mkubwa. Sajenti aliumia sana, alijilaumu kwa kitendo cha kuchelewa, moyoni alisema; laiti angewahi hata nusu saa kabla huenda yale yote yasingetokea. Aliuona ule ni uzembe mkubwa na ambao umemshushia heshima na huenda ukamgharimu. Alitoka akaanza kukagua wodi moja baada ya nyingine, lakini hakuona litakalomsaidia. Aliteremka mpaka chini, ghafla alisikia gari kwa nje likiingia, hapo akachungulia nje Kupitia dirishani, alishtuka kuona Difenda ikiwa imebeba wanajeshi waliovalia kijeshi, na vichwa vyao vikiwa vimevalishwa kofia maalumu ya kujikinga na risasi. Kabla Difenda haijasimama baadhi ya wanajeshi waliruka juu ya gari kwa ukakamavu na ujuzi usiotia shaka, kisha upesi upesi kama watu wanaotaka wasipoteze muda kiongozi wao aliwaashiria waingie ndani ya hospitali. Sajenti alipoona hivyo alipanda juu upesi kuwakimbia, hakujua kwa nini anawakimbia, huenda ni kutokana na hofu na wasiwasi wa kutokujua kuwa wale ni wanajeshi kweli wa serikali au ni watu wabaya ambao ndio waliohusika kumtorosha Mateka wa ushahidi. Sajenti alikimbia akipanda ngazi chapu chapu bila kutoa sauti ya hatua zake kama paka akimbiavyo. Wale watu waliingia ndani kijeshi silaha zao zikiwa usawa wa nyuso zao na mikono yao miwili ikiwa imeshikilia bunduki. Mwendo wao wa kupokezana kutoka kona mpaka kona ilionyesha ujuzi wao wa kivita katika operesheni za msako. Mmoja alienda kona hii wenzake wakiwa nyuma kumlinda, akifika wenzake nao wanakuja hivyo hivyo mpaka walipofika ghorofa ya pili.

Sajenti alikuwa amepanda ghorofa ya tatu ambayo ndio ya mwisho, alihangaika kutafuta sehemu ya kujificha ili kujiokoa na watu wale ambao mpaka muda ule hakujua wanataka nini, na wamekuja kufanya nini. Punde akili yake ikamuambia azime umeme kusudi isiwe rahisi kuonekana. Akiwa wodi ya juu kabisa alienda dirishani akachungulia, kwa bahati aliona sehemu umeme unapoingilia kutoka kwenye nguzo kuja pale hospitalini. Aliichukua bastola yake iliyowekwa kiwambo cha kuzuia sauti isitoke. Akapiga waya mmoja wa umeme mara tatu ukakatika. Sajenti alikuwa mahiri na mbobezi wa kulenga shabaha, hivyo hilo halikumpa shida.


Eneo lote la hospitalini likawa giza, jambo hili liliwashtua wale wanajeshi waliokuwa wameingia hospitalini humo. Walisimama, kisha wakawasha tochi zilizokuwa kwenye bunduki zao. Wengine walifunga tochi kwenye nyuso zao, walisonga kwenda juu ilipoghorofa ya tatu nayamwisho.

Sajenti akiwa kajificha alishtuliwa na tochi yenye mwanga mkali iliyopita na kumkosa kosa usoni, akajivuta kwa nyuma kujificha chini ya kitanda. Aliishika bastola yake vizuri akiwa amejiandaa kwa mapambano. Alijiuliza maswali yasiyo na majibu, Punde mwanga wa tochi ulimulika chumba chote na kitambo kidogo Sajenti alishtuliwa na mabuti meusi makubwa yakitembea hatua moja moja na kusimama huku mwanga wa tochi ukihama hama huku na huku. Moyo wa Sajenti ulicharuka na kurukaruka ukipiga kite. Kitendo cha yeye kuona ya mabuti yale ni kama mtu aliyeona mabuti ya kifo. Ingawaje hakuona mvaaji wake lakini ukubwa wa mabuti yale ulitosha kumwambia jinsi mvaaji wake alivyo. Yalikuwa ni mabuti makubwa ambayo mvaaji alikuwa na mguu mkubwa ajabu, hii iliashiria kuwa hata mvaaji wake alikuwa ni pande la jitu. Sajeti aliendelea kutazama mabuti ya lile jitu lililokuwa likitembea tembea mule chumbani huku akiwa kabana pumzi zake kuzuia kasi ya kupumua ili sauti isijekutoka.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG