Search This Blog

Saturday, February 26, 2022

THAMANI YA FUKARA - 3

    

Simulizi : Thamani Ya Fukara

Sehemu Ya Tatu (3)





Ulikuwa ujasiri wa hali ya juu sana aliouvaa Layla,wanafunzi wote walibaki wameshika midomo huku walimu walijaribu kumpa Doris huduma ya kwanza kwa kwa kuzuia ile damu lakini lakini ilishindikana,Doris alikuwa hajitambui,Gabi aliganda kama mtu aliyepigwa shot ya umeme, lakini Layla alibaki kifuani kwa Gabi kana kwamba hajafanya tukio lolote,

"Nadhani nilichokwambia kwenye ile barua leo nimekitimiza"aliongea Layla,alijisikia faraja sana kuwa kifuani kwa Gabi,

"Ameua!.."alisema yule mwalimu,haraka alitaoa simu yake na kuwapigia Askari police pamoja na wazazi wa pande zote mbili,wa kwanza kufika walikuwa askari waliombeba Doris na kumuwahisha hospital huku Gabi na Layla wakipelekwa kituoni,shule haikusomeka tena kila mwanafunzi aliongea lake lakini lile lilikuwa tukio la kihistoria.Wapo waliosema kuwa Layla yuko sahihi huku wengine wakisema kuwa ni ulimbukeni wa mapenzi,wengi walijawa na hofu ya kumpoteza Doris.Layla alidhamilia kuua kabisa kile kisu alikilenga sehemu ulipo moyo.Mzee Herman alizipata zile taarifa ila alikuwa jijini Dar es salaam kwenye biashara zake.

"Ninani huyo anayecheza na jela"aliuliza mzee Herman,

"Mtoto wa mzee wa Gozirbert,kisa mapenzi ndo umezuka ugomvi ule"alikuwa mama yake Doris akimwambia huku akitoa sauti ya kwikwi,Doris alipelekwa moja kwa moja mpaka kwenye hosipital ya Mount meru iliyoko Arusha,Layla na Gabi walipelekwa mpaka kituoni kisha wakawekwa ndani kusubiri wazazi wa pande zote mbili wafike eneo lile,Baba yake Layla alipopata taarifa ile alikuja moja kwa moja mpaka kituoni,alitanguliza hongo kwanza kuwa kesi ile isifike mahakamani, mawasiliano yalifanya kati ya Daktari aliyekuwa anamshughulikia Doris,

"Kapoteza hafamu tu ila bahati nzuri kisu hakiufikia moyo hivyo ondoeni shaka hali yake itakuwa vizuri"yalikuwa maneno ya Daktari akiwaambia askari police.Maneno yale alipoyasikia baba yake Layla alifurahi sana hivyo hata baba yake Doris aliyekuwa jijini Dar es salaam walimwmambia kuwa hata asipokuja hali ya mwanaye sio mbaya zaidi.Baada ya masaa matatu Doris alirejewa na fahamu na kujikuta mazingira tofauti aliangaza macho kulia na kushoto na kujigundua kuwa yuko hospital,alikumbuka mara mwisho kuwa alichomwa kisu na Doris,

"Kwa kuwa hajaniua bado hajanishawishi kumuacha Gabi"alijisemea Doris na kujiangalia sehemu za kifua chake na kuona jeraha lililokuwa limefunikwa kwa bandage,

"Pole sana binti,nyie bado watoto wadogo acheni kugombania mambo ya kipuuzi kama hayo"alisema yule Daktari,mama yake Doris aliyekuwa na hofu na mwanaye aliachia tabasamu alipomuoana mwanaye amezinduka.

Kwa mda huo mama yake Gabi ndo alikuwa anazipata taarifa zile kutokana na kutokuwa na simu aliambiwa na wanafunzi majirani zake,alishtuka sana bila hata kuoga aliwahi kituo cha police,hata alipofika hakupewa ruhusa ya kuonana na mwanaye machozi yalimtoka kama mzazi,

"Mama tulia mgojwa kapata unafuu,hata usijali hii kesi nitaimaliza hapa hapa"aliongea baba yake Layla maneno yale kidogo yalimpa nguvu mama yake Gabi.Gabi alijilaumu sana lakini jambo lilikuwa tayari limetokea,

"Ningelijua kweli huja badae,leo Gabi mimi naenda kuozea jela,doh!mungu nisaidie"alijisemea Gabi alianza kwa kushusha pumzi.Layla hakuwa na hofu alijiamini kupita kiasi,alijua fika wazazi wake watampigania,

"Hakuna linaloshindikana mbele ya pesa naamini nitatoka pia furaha yangu nitaiona"alijisemea Layla huku mkono wake shavuni.

"Sasa hawa watu watalala ndani kwa siku ya kesho yule aliyepelekwa hospital atakuja hapa tuchukue maelezo yao"aliongea mkuu wa kituo.Mama yake Gabi kila alipokuwa anafikiria shida alizonazo halafu mwanaye kamuweka kwenye matatizo aliishia kuyafuta machozi.

Kesho yake asubuhi Doris aliletwa moja kwa moja mpaka kituoni,Layla alipotolewa ndani na kuletwa nje akamuona Doris alishtuka,

"Kumbe huyu kinyago hajafa?alijiuliza Layla kimoyo moyo.Maelezo yalianza kuchukuliwa huku askari akiwa makini kuyaandika yake maelezo,baba yake Layla hakuzungumza lolote kwa kuwa alijua fika kuwa kesi tayari imekwisha,alibaki kujivunia kuwa na pesa,

"Mwanagu alikuwa anaenda jela kabisa kama sio pesa"alijisemea Baba yake Layla.Mama Gabi alikuwa na hofu na mwanaye yule wa pekee hivyo kimoyo moyo akizidi kumuomba mungu atende miujiza kesi iishie pale,

"Yaani kitu cha kipuuzi kama hiki ndo kinasababisha mnachomana visu?'okay mama kesi imekwisha zaidi tunakuomba umkanye mwanao aache mazoea na hawa mabinti vinginevyo ataozea jela"aliongea mkuu wa kituo,baba yake Layla alilipa gharama zote za matibabu ya Doris pamoja na za pale kituoni.

"Kabla hatujawaruhusu hapa napenda kuwaambia kuwa msiishi kwa visasi mkae kana zamani pia musome kwa bidii muachane na hayo mambo ya mapenzi ambayo yapo siku zote na hataisha na yataendelea kuwepo"alisema mkuu wa kituo.Yote aliyoyasema mkuu wa kituo haya kumuingia Layla,hata Doris naye,

"Eeh mama kwa kumalizia nawe waweza sema kitu kama mzazi ambacho mwanao atakuelewa,alisema mkuu wa kituo na kumpa nafasi mama Gabi,

"Nashukuru sana kwa kuwa yameishia hapa,mwanangu kama unajua nilikuweka tumboni na kukuzaa pia kukupa malezi yaliyo bora mpaka umefika hapa,naomba kuanzia leo usitishe mawasiliano na Hawa mabinti,fanya kilichokupeleka shuleni"alisema mama yake Gabi.

Gabi alikaa kimya ameinamisha kichwa chake aliona ndoto yake ya kuwa tajiri unaenda kuzimika,lengo la kuwapenda wale mabinti ni kwa ajili ya kujipatia pesa ili akishamaliza shule awe na mtaji wa kumkwamua kiuchumi hivyo swala la kusema awaache wale mabinti lilikuwa gumu,

"Sawa mama nimekuelewa"alijibu Gabi lakini moyoni akiwa na lake jambo,

"Sawa sawa na nyie mabinti mmesikia kilichozungumzwa?"aliuliza mkuu wa kituo huku macho yake akiyakaza kwa Layla na Doris.

"Ndio tumewaelewa"alisema Doris lakini Layla alibaki kimya bila kusema chochote,ndipo mkuu wa kituo alipomgeukia,

"Bila shaka ulitaka kumuua mwenzako kwa mambo haya ila shukuru mungu kasaidia hivyo nakuomba usitishe mawasiliano na huyu kijana"alisema mkuu wa kituo,

"Ni rahisi sana kulikausha ziwa Victoria ila sio rahisi kumuacha huyu kijana"alisema Layla kwa kujiamini...





"Ni rahisi sana kulikausha ziwa Victoria ila sio rahisi mimi kumuacha huyu kijana"aliongea Layla kwa kujiamini,mkuu wa kituo alibaki kumtazama akiwa hana la kusema,hata baba yake Layla alitingisha kichwa chake,

"Mtoto wako anaonekana jeuri sana huyu"aliongea Mkuu wa kituo..

Waliruhusiwa kutoka pale kituoni huku Doris akirudishwa hospital kuendelea na matibabu.Shule nzima ilimuogopa Layla hasa kutokana na maamuzi magumu aliyoyafanya mbele ya wanafunzi pamoja na walimu,

"Acha pesa iitwe pesa laiti angelikuwa ni masikini aliyefanya kitendo kile sahivi ashafika jela lakini mwenye pesa hazijapita hata siku mbili"alijisemea wanafunzi mmoja alipomuona Layla akirudi shule.

Moyo wa mwanamke ukipenda umependa,ndicho kilichokuwa kwa Layla,licha ya kukatazwa na mkuu wa kituo pamoja na baba yake lakini hakuwa tayari kumuacha Gabi,siku hiyo hiyo alimfuata,

"Usijali mpenzi kilichotokea ni kawaida sana hivyo hakiwezi kutuyumbisha,siku zote kukimbia tatizo sio kumaliza tatizo nakupenda sana Gabi wangu"aliongea Layla lakini Gabi alikaa kimya huku akiyakumbuka maneno ya mama yake,lakini dhamira yake ilikuwa ni utajiri hivyo ilikuwa lazima kuyapuuzia maneno ya mama yake na kuanzisha uhusiano mpya na hao watoto wa matajiri lakini alijiwekea tahadhali kubwa.Baada ya kutafakari kwa mda aliinua uso wake na kumtazama Layla kwa mda wa sekunde kadhaa kisha akasema,

"Sawa natambua ila siko tayari tena kuingia matatizoni kama awali,kama kweli unanipenda subiri nimalize shule ili nijue nini nitafanya lakini kwa sasa acha kabisa siku zote tunajifunza kupitia makosa"alisema Gabi,

"Ati nini kwa hiyo unataka tusitishe uhusiano wetu?hapana kama ni hivyo nitajiua mimi halafu najua wewe wazazi wangu hawatakuacha salama"aliongea Layla kwa vitisho"Gabi moyoni alifurahi kumwambia vile Layla aliona mpango wake utakamilika haraka,

"Nakupenda sana ila hapa nimeng'atwa na mbu jana usiku najihisi maralia kabisa,ningelikuwa na hela sahivi ningeenda kufanyiwa vipimo kabla ugojwa haujawa mkubwa"aliongea Gabi huku akilenga kupewa pesa,mbinu yake ile ilizaa matunda alipewa elfu kumi na Layla,

"Nashukuru sana Layla lakini yatupasa kuwa makini sana tusigundulike tena"aliongea Gabi.Kwingineko Doris ndo alikuwa anaruhusiwa kutoka hospital,alipewa siku kadhaa za kutulia nyumbani.Moyoni mwake bado hakutaka kumuacha Gabi pamoja na kwamba alichomwa kisu na Layla lakini aliamini kuwa hivi ni vitisho ambavyo haviwezi kumfanya aachane Gabi kijana fukara lakini ana thamani kubwa kwa hao watoto wa matajiri,

"Uoga ni dhambi hata maneno ya mungu yanasema,kama ni vita wacha naiwe vita"alijisemea Doris huku naye kisu akikiweka kwenye mfuko wake wa shule.Baada ya siku tatu mbeleni alianza kwenda shuleni,wanafunzi wengi walimpa pole huku wengine wakimkanya kuachana na hayo mambo lakini hakutaka kusikia lolote,

"Shujaa ni yule anayerudi nyumbani na sio yule anayefia vitani, hivyo kisu hakiwezi kunifanya nisitishe mahusiano na mtu niliyemuweka moyoni tayari lazima nipambane kufa na kupona ili moyo wangu ufurahi"alisema Doris akiwa na baadhi ya marafiki zake,

"Lakini kuna msemo kuwa asiyekubali kushindwa sio mshindani wazee wetu hawakuwa wajinga kutuambia msemo ule hivyo kubali kushindwa"alisema mwanafunzi mmoja,lakini Doris aliondoka mbele yao dhahiri yale maneno yalimkera.Walimu walijaribu kuwaweka sawa lakini hakuna aliyekubali.

"Baba natambua kuwa mimi ni mwanenu wa pekee hivyo hamna budi kunipa furaha yangu,baba nakuomba ufanye kama ulivyo fanya kwa mwalimu Bernard,yaani huyu mtoto wa Herman ahamishwe pale shuleni vinginevyo tutapigana kila siku"aliongea Layla mbele ya wazazi wake.Baba yake alitafakari maneno ya mwanae yule na kubaki kumuangalia,kweli hakutaka mwanae yule akoswe furaha hivyo alimuondoa wasiwasi kuwa siku sio nyingi hitaji lake litatimizwa.Moja kwa moja baba yake alifanya mawasiliano na mwalimu mkuu huku akimhaidi pesa nyingi andapo atalikamirisha hilo,

"Usijali jambo dogo sana lile siku sio nyingi nalitimiza"yalikuwa maneno ya mwalimu mkuu akimwambia baba yake Layla kwa njia ya simu.Mchakato aliuanza mwalimu mkuu aliandika barua aliyompa Doris ili aiifikishe kwa wazazi wake.Doris aliipokea ile barua lakini moyoni akiwa na hofu kwani haikuwa kawaida hivyo kabla hajaifikisha nyumbani aliisoma kwanza,

"What!!(nini?),nihame shule?kwa sababu zipi?najua ni mpango alioufanya Layla labda kama nitahama na Gabi hapo sawa lakini vinginevyo nitafia pale shuleni"alijisemea Doris.Ule ujumbe aliupeleka mpaka kwa mama yake,kwa wakati huo baba yake alikuwa bado yuko jijini Dar es salaam,

"Sasa kwa sababu zipi uhame?hapana hapa kuna kitu ngoja tumsubiri baba yako tuone atasemaje"alisema mama yake Doris.

Huku kwa Layla mda mwingi alikuwa akiachia tabasamu alijua kuwa baba yake hajawahi kusema kitu halafu ashindwe kukikamilisha hivyo alijua mda wowote Doris anahamishwa pale shuleni hivyo Gabi atakuwa naye kwa urahisi.

Baada ya siku nne baba yake Doris alirudi kutoka jijini Dar es salaam,alimkuta mwanaye akiwa kwenye hali ya huzuni,

"Kwema kweli hapa?naona hali tofauti"aliuliza mzee Herman,

"Hapa kwema kabisa ila kuna hali ya huzuni kidogo imejitokeza lakini kwanza upumzike kwa sababu sio ya mhimu sana"aliongea mama yake Doris huku akimpokea mmewe baadhi ya mizigo.Mara baada ya kuoga na kupata chakula alikaa sebuleni na kuuliza swali lile la mwanzoni,

"Kiukweli hapa kuna hali ya sintofahamu,tumepokea barua kutoka kwa mwalimu mkuu akimtaka Doris kuhamishwa shule"aliongea mama yake Doris,mzee Herman alibaki mdomo wazi kusikia zile habari,

"Iko wapi hiyo barua hebu ilete niisome"barua ililetwa,

"Upumbafu gani huu,yaani mwanangu amechomwa kisu nimekaa kimya na leo eti ahamishwe shule?sikubali najua ni mchezo wa mzee Gozirbert anaoucheza lakini hatoweza.Doris mwanangu huwezi kahama shule kwa sababu za kijinga kama hizi,kama serikali mi pia ni serikali"alifoka kwa hasira mzee Herman dhahiri ile barua ilimchanganya.

"Mmmh yule mzee anajidai anapesa nyingi sana ndo maana hata kesi hii kaimalizia kituoni"aliongezea kusema mama yake Doris,

"Pesa?! hata mimi pesa ninayo na hawezi kunitisha kwa lolote,nimekaa kimya sasa anataka kunizoea sana kanipanda kichwani nilikuwa nampa heshima yake kama mzee mwenzangu lakini kumbe mtu mwenyewe hajiheshimu.Sasa nasema hivi wacha tuonyeshe jeuri ya pesa,na siku zote ukiamua kuchezea nyuki mchana kweupe basi usiogope manundu"alisema mzee Herman kwa sauti ya jaziba.



"Sikia nikwambie mama Doris, mimi hapa namheshimu sana mzee Gozirbert ila siwezi kumuogopa kama vita ianze kwani pesa kitu gani bhana"aliongea mzee Herman kwa hasira.Alitoka ndani na kuingia kwenye gari lake huku safari yake ikienda moja kwa moja mpaka kwa mwalimu mkuu,alikaribishwa ndani na mke wa mwalimu mkuu,

"Mkuu nimekuja hapa bwana na kitu kimoja cha kuongea,ujue siku zote kitu cha siku moja kinaweza kuharibu maisha yako ya siku zote,hivyo unatakiwa kuwa ufikirie kwenye maamuzi mengine kabla ya kuyafanya,mzee Gozirbert ana pesa sawa siwezi kulingana naye lakini hawezi kunitisha kwa lolote,je itakuwa sahihi na heshima yangu niliyonayo uone nagombana naye?"aliuliza Herman kisha akaendelea,

"Nakuheshimu kama mwalimu mkuu lakini kwa hili siko tayari,mwanangu hawezi kuhama hapa labda mpaka mwenyewe niamue na sio wewe na yule mtu aliyekupa hongo,nasema haiwezekani,pamoja na kuwa mwalimu mkuu lakini kiuwezo huwezi kunizidi ndo maana unashawishika kupokea rushwa jambo ambalo ni adui mkubwa wa nchi, okay nisiongee sana nimekuja hapa kukupa onyo kuwa mwanangu anatakiwa kusoma hapa shuleni akiwa na amani tele sitaki umpe vitisho hii tabia ikiendelea nitaenda mpaka kwa mkuu wa wilaya ili nitoe taarifa hizi,kwaheri",aliongea mzee Herman maneno mazito kisha akaondoka na kumuacha mwalimu akiwa mwingi wa mawazo,

"Kweli kibarua kinaweza kuota nyasi maana huyu mzee anaonekana hana masihara hata kidogo"alijisemea mwalimu mkuu.

Mzee Gozirbert akinyanyua simu yake na kuiweka sikioni,

"Hallow mwalimu,bila shaka umemaliza mchezo"aliongea mzee Gozirbert,

"Hapana unajua hii inshu inatakiwa kwenda pole pole ila usijali siku sio nyingi nitalikamilisha hilo"aliongea mwalimu mkuu hakutaka kusema vitisho alivyokuwa amepewa na mzee Herman.

Siku zilikatika huku Layla akiwa haoni dalili yeyote ya Doris kufukuzwa pale shuleni.Bado Gabi hakuishiwa sababu kwa wale mabinti wa kitajiri japo alifanya siri kubwa ili asigundulike,

"Tufanyeje ili huyu malaya aache kuuandama?"lilikuwa swali la Doris akimuuliza Gabi kwa wakati huo walikuwa kijijini,walichoamua kukifanya Gabi na Doris ni kuwa wanakutana wakiwa nyumbani na sio shuleni, mpango wao ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani hata Layla alipunguza hofu hasa baada ya kuona hakuna mazoea tena kama mwanzo,swala la Doris kuhamishwa shule liligonga mwamba mwalimu mkuu hakupata maamuzi sahihi hivyo aliliacha lile swala kama lilivyokuwa.

Mtihani wa mwezi wa kumi na mbili ulikaribia,walimu hawakuacha kusisitiza wanafunzi wasome kwa bidii,

"Kwa kipindi hiki hakuna masihara tena kama ulifanya vibaya mitihani iliyoisha basi jitahidi kufanya vyema ili kujiokoa na adhabu itakayowapata wale watakaoshika nafasi za ishirini kwenda juu"alisema mwalimu mkuu, kabla ya mitihani hizo kila mwanafunzi alihakikisha anasoma kwa bidii.Layla alikuwa na amani sana ndani ya moyo wake hasa alipoona mazoea kati ya Doris na Gabi yamepungua,alisoma kwa juhudi sana na alipania kushika nafasi ya kumi kushuka chini,

"Nakumbuka baba alinihaidi gari kuwa kama nitashika nafasi ya tano"alijisemea Layla alisoma usiku kucha lengo alitaka aweke heshima kulinganisha na mtihani wa mwezi wa sita alishika namba ya thelathini.

Siku ya mitihani iliwadia, kabla mtihani haujaanza Layla alimfuata Gabi na kumpa pesa itakayo msaidia ndani ya hizo siku za mitihani,

"Tukimaliza mtihani kuna ombi nitakalo hitaji kutoka kwako"alisema Layla,

"Ombi gani niambie"alisema Gabi lakini Layla alisema kuwa mitihani iishe kwanza.Kipindi Layla anampa pesa Gabi Doris aliweza kuliona tukio lile,moyo wa wivu ulimjaa aliwaza kitu cha kumfanya Layla aachane na Gabi hakipo zaidi ya kumuua,

"Ngoja mitihani iishe lazima nitamuua yeye si alinikosa?sasa ngoja"alijisemea Doris,kichwani mwake alianza kuunda mbinu za kumuua Layla.Wiki mbili ziliisha na mtihani iliisha hivyo matokeo yao yalitangazwa,Layla hakuyaamini masikioni yake kuwa amekuwa mtu wa sita,alilipuka kwa furaha sana huku akiyakumbuka maneno ya baba yake kuwa atafundishwa kuendesha gari.Gabi alishika nafasi ya ishirini na nane huku Doris akiwa mtu wa thelathini na mbili.

"Baba yuko wapi?"aliuliza Layla kwa furaha alipofika nyumbani kwao,

"Tulia basi kwanza mbona una furaha hivyo?"aliuliza mama yake,

"Nimeshika nafasi ya sita hivyo namsubiri baba aweze kutimiza ahadi yake".Mama yake alifurahi kuyasikia maneno ya mwanaye.Hata baba yake aliporudi naye alifurahi pia,yule dereva aliyekuwa anampeleka Layla shuleni ndo alipewa kazi ya kumfundisha Layla gari,mara baada ya wiki mbili Layla alikuwa tayari amefahamu kuendesha gari.

Sasa zilipita wiki tatu tangu shule ifungwe,ndani ya kipindi hicho Layla hakuonana na Gabi kutokana na kuwa bize na kujifunza gari,alimpania kumtafuta tarehe moja ya mwaka mpya,kwanza alienda mjini akiwa na gari kisha akanunua nguo nyingi alizokadiria kuwa zitamtosha Gabi,alizifunga vyema na zawadi nyingne nyingi na kuzipeleka mpaka nyumbani kwao na Gabi bila kuhofia chochote,alimkuta mama yake Gabi akiwa amekaa nje anamenya mihogo huku Gabi akiwa ndani,alisimamisha gari lake na kushusha ule mzigo wa zawadi kisha mama yake Gabi aliyesita kuupokea lakini Layla alimuondoa wasiwasi,Gabi alitoka ndani na kushtuka kumuona Layla alitaka kurudi ndani lakini Layla alimuita na mara baada salamu, maongezi mengine yaliendelea,

"Mama usiwe na wasiwasi na mwanao yale yaliyotokea hapo awali hayatajirudia tena"aliongea Layla,bado mama yake Gabi alikuwa na wasiwasi mkubwa,Layla alipolipoliona hilo alitoa noti nyekundu na kumkabidhi mama yake Gabi aliyebaki kushangaa,

"Eeh!na wewe nimekuletea nguo hivyo jiandae kuna sehemu tutakwenda sasa hivi"aliongea Layla.Gabi hakuwa na kipingamizi zaidi ya kuoga na kuvaa zile nguo zilizomtoa vyema,

"Haya mama sisi tunatoka kidogo"aliongea Layla huku akiufungua mlango wa gari ili Gabi aweze kuingia ndani.Mama yake Gabi hakuwa na la kusema alibaki kuwatazama,

"Watoto wetu wa siku hizi shida kweli,yaani zamani kama sisi tulipokulia haya mambo hayakuwepo kabisa,mwanamke wa sasa hivi hata mama mkwe wake hamuogopi tofauti na zamani"alijisemea mama yake Gabi,

"Sasa tunaenda wapi?"aliuliza Gabi baada ya kuona gari likiongeza kasi,

"Leo ni leo lazima unipe penzi lako"alisema Layla...




Safari ya Layla na Gabi iliishia hotelini,hapo waliweza kupata chakula na mara baada ya chakula waliingia tena ndani ya gari na kuendelea na safari,

"NDATU GEST HOUSE"Ilkuwa nyumba ya kulala wageni,Lalya kwa mwendo wa taratibu kabisa aliegesha gari baada ya kufunguliwa geiti,alitelemka na kumfungulia mlango Gabi aliyebaki kushangaa,mlinzi alishtuka alipoona watoto wenye umri kama ule wakiingia mle ndani,

"Wazazi wao wanawapa ruhusa kweli ya kuendesha gari?doh dunia imeisha"alijisemea yule mlinzi wa getini,

"Humu hawaruhusiwi kuingia watoto wenye chini ya miaka kumi na nane"ilikuwa ni sauti ya dada aliyekuwa mapokezi,

"We turuhusu tu,shika hii"alisema Layla huku mkono wake akiuzamisha kwenye pochi yake na kutoa hela kadhaa kisha akampa yule dada aliyepoa ghafla.Waliingia mpaka ndani na kupewa chumba kisha wakaingia mpaka ndani,wote walibaki kutazamana hakuna aliyemuongelesha mwenzake,lakini kimya hicho hakikudumu sana,

"Gabi hivi unataka nikupe nini ili uweze kumuacha huyu Doris?aliuliza Layla,Gabi alikaa kimya kwa mda akitafakari lakini hakupata jibu la kumjibu, maongezi yaliendelea huku kila mtu akiwaza namna ya kumshika mwenzake,walikuwa na aibu hata walipokaa hawakugusana.

Hadi yanafika masaa mawili hakuna aliyekuwa amemgusa mwenzie waliendelea na maongezi mengine.Saa moja jioni ndipo walipokumbuka kurudi nyumbani,walifungua mlango kisha wakaenda mpaka lilipoiuwa gari lao,Layla alitamani hata kumbusu Gabi lakini aliona aibu.Mwendo wa dakika kama kumi walikuwa tayari nyumbani kwao na Gabi,kabla hajafungua mlango Layla alivaa ujasiri na kumbusu shavuni Gabi,alifungua mlango wa gari kisha wakaagana na Layla akarudi nyumbani kwao,

"Mwanangu ujue bado kuna vita,yule mtoto wa Herman kaja hapa anakuulizia na nilipo mwambia kuwa haupo nimeona kasikitika kabisa na kuondoka kama ana jaziba hivi,hivyo mwanangu kuwa makini au wakatae kabisa,bora kuwa masikini mwenye amani na sio tajiri mwenye hofu mda wote"aliongea mama yake Gabi.Lakini Gabi alimuondoa hofu kabisa,

"Nadhani siku nikizotoa hizi hela mama hataamini na ndo utakuwa mwisho wa umasikini wetu"alijisemea Gabi.Siku zilisogea hatimaye shule zilifunguliwa.Doris baada ya kukaa na kuwaza sana aliamua atumie njia ya kumuua Layla ili aweze kufurahia penzi na Gabi,

"Lakini ngoja tumalize shule sahivi inaweza kuwa kesi kubwa"alijisemea Doris.

*******

Baada ya miezi sita Gabi alitamani kusihesabu zile pesa alizokuwa anafukia chini,lakini alijizuia huku akihesabu miezi michache ijayo kuwa atakuwa tajiri,bado alizidi kuonana na Doris kwa siri kubwa sana bila Layla kuweza kufahamu,hawakuacha kufanya mapenzi kila walipokuwa wanakutana kilichomfurahisha zaidi Gabi ni pesa alizokuwa anapewa na Doris.Siku zilisogea huku miezi ya kufanya mitihani ya kuhitimu shule ya msingi ikikaribia.Mwezi wa tisa mitihani ilianza,Gabi hakuwaza kufanya vizuri zaidi aliwaza biashara ya kufanya,

"Nitafungua duka kubwa"alijisemea Gabi akiwa kwenye chumba cha mtihani,hakuwaza masomo.Mara baada mitihani kuisha walisubili matokeo ambayo yalikuwa yanatoka mwezi wa kumi mbili.Layla alitamani sana kumpa Gabi penzi lake lakini alishindwa jinsi kumwambia licha ya kuonana naye mara kwa mara.

Habari mbaya kwa upande wa Gabi alifeli mtihani japo kwa upande wake alifurahi,Layla alifauru huku Doris akipita kwa nguvu ya pesa.Layla alihuzunika sana kuona Gabi hajafanya vizuri sana aliona hicho ndo kitakuwa chanzo cha kumkosa Gabi iwapo kama ataenda shuleni na Gabi kumuacha kijijini,

"Sasa mpenzi tutafanyaje maana mimi nitapaswa kwenda shuleni je wewe utanivumilia?"aliuliza Layla akiwa na Gabi,

"Ondoa shaka juu ya hilo lazima nikuvumilie we nenda kasome"alisema Gabi lakini Layla alisema kuwa hayuko tayari kwenda shuleni na kumuacha Gabi.

Taarifa zile alizipata mzee Gozirbert baada ya kutonywa na mke wake,

"Upumbafu gani huu?hataki shule sasa wacha nitamuonyesha"alifoka baba yake Layla.Huku nako Doris aligoma naye kwenda shule licha ya kuwa baba yake mzee Herman alitumia nguvu ya pesa ya kununua matokeo,

"Najua sababu ni yule kijana sasa wacha niongee na mzee Gozirbert tuone tunafanyaje"alisema baba yake Doris baada ya kupokea taarifa kuwa Layla naye kagoma kwenda shuleni.Kiliitishwa kikao cha wazazi wanne wa pande zote mbili bila Doris wala Layla kufahamu,

"Sasa mzee mwenzangu tunafanyaje maana hawa watoto wamegoma kabisa"alisema baba yake Doris.Mzee Gozirbert alimeza funda moja la mate kabla ya kujibu akainisha kichwa chake kisha akakiinua,

"Mimi nina wazo litalo weza kuwanusuru hawa watoto wetu,tunatakiwa kumtengenezea kesi huyu kijana itakayo sababisha kufungwa jela tofauti na hapo tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu"alitoa wazo baba yake Layla,

"Sawa wazo zuri sana hilo,je ni kesi gani hiyo?"aliuliza tena Herman,

"Kesi zipo nyingi sana mfano tunaweza kumtengenezea kesi kuwa kabebesha mimba mwafunzi hivyo itakuwa kesi rahisi sana huku na nguvu ya pesa itatumika kuliwezesha hilo,wazee wetu walisema kuwa ukicheza na nyani utavuna mabua"alisema baba yake Layla wazo lake liliungwa mkono.Kikao kilifungwa rasimi huku watu watakao wezesha kulifanikisha hilo wakianza kuandaliwa,mwanafunzi atakayeekiti kuwa ana mimba alianza kuandaliwa huku Daktari feki atakayeweze kutoa vipimo vya uongo naye aiwekwa tayari bila kuwasahau askari watakaoweza kuendesha kesi ile,yote hayo waliyapanga yatimie ndani ya mwezi mmoja huku wakihaidiana kuitunza siri ile watoto wao wasitambue kilichokuwa kinaendelea.




"Ndio mzee mwenzangu usipoziba ufa utajenga ukuta,tukiwaacha hawa watoto watakuja kuuana kabisa kwa mambo ya kipuuzi"alisema baba yake Layla wakati akiagana na mzee Herman baba yake na Doris.Mpango ulianza kufanyika mara moja hakuna lishindikanalo mbele ya pesa,askari wapenda rushwa walikuwa tayari kwa kusimamia kesi huku mwanafunzi atakayedanganya mbele ya mahakama akiwa tayari.Baada ya kujilidhisha kila kitu kuwa sawa walitumwa Askari kwenda kumkamata Gabi hakuna aliyejua mpango ule zaidi ya wazazi pekee na watu wengine walishirikishwa kulikamalisha hilo.

Gabi akiwa nyumbani kwao aliamua kuchukua panga lake na kwenda kuchimba pale alipokuwa anahifadhi pesa zake,

"Naenda kuwa tajiri mkubwa hapa jijini"alijisemea Gabi huku taratibu akianza kuchimba sehemu ile,

"Hodi.."Ilikuwa sauti ya kiume iliyomshtua Gabi alisitisha zoezi lile,

"Nasema humu ndani mpo au tutumie nguvu kuingia?"ile sauti iliuliza tena,moyo wa Gabi ulienda mbio sana,haikuwa kawaida kusikia sauti zile za vitisho.Akiri ya haraka ilimjia kuwa ajifiche uvunguni mwa kitanda,

"Afande Kamu hebu ingia ndani halafu mimi nabaki hapa"maongezi yale Gabi aliisikia vyema kabla hata hajajificha macho yake yaligongana na mwanaume aliyekuwa amevalia mavazi ya kiaskari,

"Unamkodolea macho nani mshenzi mkubwa wewe wa kubabesha mimba wanafunzi,hapo ulipo nyoosha mikono juu kisha geuka kama ulivyo unifuate"aliongea yule Askari,Gabi haja ndogo ilimtoka bila kutalajia,aligeuka na kutoka nje,

"Mtie pingu haraka"aliongea askari mmoja na bila kuchelewa askari wa pili akafanya kama alivyosema mwenzake.Majirani wa karibu walijitokeza na kujaribu kuulizia kilichosababisha Gabi kukamatwa lakini majibu yalitolewa na wale askari kuwa kitajulikana kituoni.

"Kosa langu nini mimi?"aliuliza Gabi huku akijaribu kugoma kutembea,

"Nyamaza utafikiri mliletwa hapa duniani kuharibu maisha ya wenzenu,pumbafu kabisa"alisema yule askari safari yao ilienda mpaka kituoni.Mama yake Gabi akiwa shambani siku hiyo hakuwa na nguvu kabisa,mwili wake ulikuwa mchovu sana jambo lililomfanya ashindwe kuendelea na kazi hivyo alifunga mzigo wa kuni na kuamua kurudi nyumbani,kabla hajafika aliwaona majirani wamekusanyika eneo nyumbani kwake,haikuwa kawaida hivyo alijua kutakuwa na tatizo lililotokea,akiwa na hofu alizipiga hatua za haraka haraka,

"Jamani hapa kwema?"aliuliza mama yake Gabi huku mzigo wa kuni ukiwa bado kichwani,mwanamke mmoja alishusha pumzi ndefu na kusema,

"Hapa sio kwema hata kidogo,mwanao kapelekwa kituoni na askari ambao hawajasema chanzo cha yeye kukamatwa"aliongea mama yule huku majirani wengine nao wakikazia pale pale.Mama yake Gabi aliurusha mzigo wa kuni chini mbio mbio mpaka kituoni ambapo hapakuwa mbali,

"Pole sana mama mwanao mbishi sana tulimwambia mapema kuwa aachane na haya mambo afate masomo lakini hajataka kusikia hatima yake amembebesha mwanafunzi mimba na Kama unavyojua adhabu inayowapata vijana au wanaume wanaobebesha mimba wanafunzi huwa ni miaka thelathini"alisema mkuu wa kituo.Mama yake Gabi alidondoka chini na kupoteza fahamu.Masaa mawili mbeleni fahamu zilimrejea tena machozi yalimtoka akiomba msamaha kuwa mwanaye asamehewe lakini mkuu wa kituo alizidi kusema kuwa uchunguzi unaendelea na kama atabainika basi hakuna namna,wakiwa kwenye ile hali mara kuna mwanafunzi wa kike aliletwa pale kituoni,mama Gabi alimuangalia kwa umakini lakini Ilikuwa sura ngeni kwake,

"Mwanafunzi aliyebebeshwa mimba ndo huyu hapa"alisema mkuu wa kituo.Gabi alipewa ruhusa ya kuongea na mama yake lakini alipoomyeshwa mwanafunzi yule kuwa ndo mwenye mimba alishtuka sana, akili yake yote aliwaza kuwa atakuwa ni Doris kwani ndo msichana pekee aliyekuwa ameshiriki naye tendo,

"Mmetengeneza kesi mimi huyo mwanafunzi simjui kabisa"aliongea Gabi kwa sauti ya juu sana,lakini mama yake alimzuia kuwa asipayuke,


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG