Search This Blog

Sunday, April 18, 2021

RAHA YA DAFU UCHOKONOLEWE - 2

  


Chombezo : Raha Ya Dafu Uchokonolewe 

Sehemu Ya Pili (2)


“Mwenzetu vipi? Huko darasani wamekubemenda nini?” Alizungumza Sarah akisindikiza maneno yake kwa kicheko.

“Au shemeji Babu amekuzingua nini Sarah?” Anitha alisema kwa uchokozi.

“Mwenzangu, Babu anayajua majambozi yule. Akinizingua kwanini nisichanganyikiwe” Alisema Sarah kwa lengo la kunitupia vijembe mimi ambaye nilikuwa nimeketi kitandani kwangu nimejiinamia kwa hasira.

“Au umeachika?” alihoji Anitha.

“Nimeachika shost, hapa lile gonjwa lenu la mapenzi na mimi limenikumba. Nipeni dawa mwenzenu miye nitakufa” Sarah alizungumza huku akining’ong’a kichwani pale nilikuwa nimejiinamia.

Anitha aliposikia maneno yale yaliyotolewa na Sarah kwa lengo la kunitupia mimi, akaanza kujichekesha kinafki. Alicheka na kujifanya kukaaukiwa kabisa hadi akapaliwa na mate.

“Koh….koh….koh koh koh!” Alikohoa kutokana na kicheko chake cha kishankupe.

“Nyoo utakufa kwa ushakunaku, hebu nipe dawa ya mapenzi huko namimi nipate ahuweni” Alizungumza Sarah huku akitabasamu na kunitazama mimi kwa kutumia pembe ya jicho lake la kushoto.

“Wacha nife hakuna hata anayenijua hapa” Anitha alizungumza na kumalizia kwa kupiga chafya mara mbili mfurulizo.

“Mnh na wewe usituletee Corona hapa” Alisema Sarah kwa utani huku akichezesha kiganja chake karibu na sura yake kama vile alikuwa akifukuza mbu usoni.

“Kwendeni zenu kule, humu ndani nyote mmeathirika. Tena hako kengine Kameambukizwa na Babu Mlinzi” Alisema Anitha huku alinitazama na kutabasamu.

“Huo sasa uchokozi Anitha, inamaana Farida ameambukizwa virusi vya Corona na babu Makwacha?”

“Kwani uwongo?” Anitha alizungumza kwa uchokozi huku akinitazama.

Dukuduku lilizidi kuongezeka na kukua ndani ya moyo wangu. Pumzi zilinijaa kifuani na kuhisi kukaribia kupasuka. Nilitamani kumvaa mmoja kati ya viumbe wale na kuwapatia kipigo lakini nikavumilia na kuinuka kutoka pale kitandani kwangu.

Nilivuta hatua kutaka kutoka nje ili kuepusha shari, lakini kabla sijafika mlangoni Sarah alinidaka mkono na kunivuta nyuma kwa nguvu.

“Njoo wewe unakwenda wapi?” Sarah alinambia alipokuwa ananivuta.

Nilijikuta nikirudi kwa nguvu pasipo kutaka. Niliyumbayumba mara mbili kabla sijatulia na kujitambua. Sifahamu niliingiwa na kitu gani, nilivuta mkono wa kulia na kumtandika Sara kofi takatifu la usoni.

“Mama nakufaaaa!” Sara alitoa ukulele na kuniachia pasipo shuruti wala hiyari.

Anitha alipoona mwenzie amepewa kitu kitakatifu hakutaka kusubiri zamu yake, alinisukuma kidogo na alipopata upenyo akatimua mbio mithili ya swala kutoka nje ya bweni na kutuacha mimi na Sarah chumbani mle.

Kibao kile kilimfanya Sarah kuhisi kuwashwa kama vile alikuwa amepakwa pilipili kwenye kidonda au amemwagiwa upupu. Hakutegemea kama msichana mrembo kama mimi ningeweza kutoa mkong’oto takatifu kama ule.

Akiwa ameshikilia shavu lake kwa mkono wa kushoto, nilimshika nywele na kumvuta juu kwanguvu. Namimi tayari hasira zilikuwa zimekwisha kunipanda kupita kawaida. Nilikuwa nikitetemeka mithili ya mgonjwa wa malaria.

Sarah alijivuta nyuma kwa nguvu na kujichomoa kutoka kwenye mikono yangu. Alijaribu kuvuta mkono kwa lengo la kunitandika kofi la usoni lakini nilimuwahi kwa kumkumbatia na kumsukuma nyuma kwa nguvu.

Alipepesuka na kudondokea kwenye kitanda alichokuwa analala Anitha. Nikamuona akishika kiuno chake na kuugulia maumivu. Alinitazama kwa hasira huku akionekana kutokuwa na hamu ya kunisogelea tena. Alivuta mdomo wake mbele kwa jazba huku sura yake akiwa ameikunja kutokana na maumivu aliyoyapata.

“Nafikiri heshima itakuwepo sasa hivi” Nikazungumza huku nikimtazama kwa kumkazia macho.

“Kwenda zako kule, unamtisha nani wewe!” Alisema Sarah huku akiwa bado ameshikilia kiuno chake kwa maumivu yaliyokuwa yametokana na kudondokea kitanda.

“Nitakung’oa meno yako hayo shetani mkubwa wewe” Nikazungumza kwa hasira huku nikitetemeka.

Sarah alinitazama kwa jazba kisha alijiinua kutoka pale chini kama mshale na kuja kunivaa nilipokuwa nimesimama. Kwakuwa sikuwa nimejiandaa na wala kutegemea kama msichana yule angeweza kufanya kitendo kama kile, nikayumba mara mbili na kujipiga kwa nguvu uso wangu kwenye chuma cha kitanda tulichokuwa tunalala mimi na yeye.

Kabla sijakaa sawa Sarah alivuta mkono wake wa kulia na kufanikiwa kunitandika kofi kali maeneo ya sikio langu la kushoto. Ndugu msomaji nilichokuwa nikikisikia pale hakikuwa kingine bali ni sauti za ving’ora ambavyo havikuwa na mpigaji.

Nilikuwa kama vile nimechanganyikiwa kutokana na kipigo kile kilichokuwa kimenibadilikia ghafla. Kumbe Sarah naye alikuwa ni mzima hadi katika masuala ya kutoa mfuweni, mimi nilidhani alikuwa ni mzungumzaji tu.

Nikajitahidi mtoto wa kike kujiinua na kupambana ili kuweza kutunza heshima yangu. Nilihofia sana kupigwa na Sarah kwasababu nilielewa baada ya pale kitu ambacho kingefuata ni dharau pamoja na manyanyaso zaidi.

Pale nilipokuwa nikijitahidi kuonesha ubavu wangu, Sarah alipitisha mkono wake wa kulia shingoni mwangu na kunikaba. Hewa ikawa haipiti kwenye koo langu. Nikawa siwezi kumeza mate wala kuzungumza zaidi ya kufurukuta na kusubiri msamaha kutoka kwa binti yule mwanaharamu. Jicho lilinitoka na ghafla nuru ya macho ikapungua na kutawala kiza. Nikawa sioni wala sisikii, tayari nguvu zilikuwa zimeniishia.



****

Wakati nilipokuwa nikipambana na Sarah kule bwenini, Anitha alikimbia moja kwa moja hadi getini kwa babu Makwacha. Alimkuta mzee yule ameketi kwenye kiti chake amesinzia huku kofia yake ya duara kama ya mgambo alikuwa amejifunika usoni.

“Babu!…Babuuu!….” Aliita Anitha alipofika karibu na alipokuwa ameketi Mzee Makwacha.

Mlinzi alishituka na kushika kirungu chake tayari kwa mapambano. Alipomuona Anitha amefika huku akihema juu juu aliangalia kushoto na kulia kuona kama kulikuwa na tatizo lolote.

“Vipi binti kuna nini?” Alihoji mzee Makwacha kwa wasiwasi huku akiangalia kule alipokuwa anatokea Anitha kuona kama kulikuwa na mtu anamfukuza.

“Wanauana Babu twende!” Alizungumza Anitha huku akimshika mzee Makwacha mkono na kutaka kumvuta.

“Ngoja kwanza binti….” Alisema Mzee Makwacha na kuchomoa mkono wake kutoka kwa Anitha.

“Twende haraka wataumizana” Anitha lizungumza huku akipigapiga chini miguu yake kuonesha kuwa alikuwa anasisitiza.

“Wapi?”

“Kule bwenini”

“Wakina nani?”

“Twende bwana babu, kwani we unawajua wanafunzi wote?”

“Wanauana kivipi sasa?”

“Wanapigana Babu twende ukanisaidie”

“Sasa kwanini unifuate mimi usiende kutoa taarifa kwa Matroni wako?”

“Babu hayo maswali utaniuliza baadae, kwanza twende ukawasaidie” Alizungumza Anitha na kugeuka kuanza kuondoka kurudi bwenini.

Babu mzee Makwacha alimtazama Anitha kwa sekunde kadhaa kama vile alikuwa anajishauri kwenda au kupotezea, lakini kutokana na roho ya ubinadamu aliamua kumfuata Anitha nyuma kwa haraka.

****

Nikiwa pale chini nilihisi upepo ukinitoka sehemu za kutolea haja kubwa. Sarah alikuwa amenikamata ipasavyo kiasi cha kuhisi roho ikiacha mwili.

Ghafla Anitha alifika chumbani pale akiwa ameongozana na mzee Makwacha. Ujio wa watu wale chumbani mle ulikuwa ndio ahuweni kwangu kwani nilihisi kama vile Mungu alikuwa amewashusha kutoka mbinguni kuja kutenda muujiza.

Mzee Makwacha alifika na kubabadua mikono ya Sarah kutoka kwenye shingo yangu. Sikuweza kuamini tukio lile, nikaanza kukohoa mfurulizo. Chezea kukanwa wewe!

“Niache…nicheni!” Sarah alilalamika huku akijaribu kuminyana na mzee Makwacha akitaka kunifuata na kunikanyaga tena.

Mimi nilikuwa nimejishika shingoni huku nikiendelea kukohoa mfurulizo bila nukta. Mate ambayo yalikuwa yamezuiwa kwa kitambo, yalipita kwa kasi kuelekea upande wa kupitishia hewa na kunifanya nizidi kukohoa zaidi.

“Niache nimfundishe adabu huyu mshenzi!” Sarah alizungumza huku akiminyana na mzee Makwacha.

Babu mlinzi alipoona binti yule alikuwa anataka kumletea mambo ya kipuuzi, alivuta mkono na kumtandika kofi takatifu kwenye shavu. Sarah alikuwa kama vile amemwagiwa siafu kwa namna alivyo charuka baada ya kupokea kofi lile.

“Weee! Unanipiga mimi umenizaa? Unajua uchungu alioupata mama yangu wewe? Hebu jiangalie una hadhi ya kuinua mkono wako na kunipiga wewe?” Sarah alizungumza kwa kiburi huku akiwa amemkazia macho Babu mlinzi.

Mzee Makwacha alimsukuma pembeni na kuja pale chini nilipokuwa nimeketi mimi. Alinishika kwenye mabega na kuniinua.

“Vipi binti upo sawa?” Alihoji mzee yule kwa sauti ya upendo.

Niliitika kwa kichwa kuashiria kuwa nilikuwa sawa lakini nilipeleka mkono wangu wa kulia usoni na kujifuta machozi. Mzee Makwacha alionesha kunihurumia sana kiasi cha kunifuta machozi kwa kiganja cha mkono wake.

“Pole sana binti” Alisema mzee Makwacha.

Wakati mimi nikiwa naendelea kuliwazwa na mzee yule aliyekuwa ameonesha roho ya imani na kuokoa maisha yangu kwa mara ya pili, Anitha na Sarah walitoka nje na kutuacha wawili ndani ya chumba kile kilichokuwa kikitumika kama bweni la wanafunzi.

Nilimtazama mzee makwacha na kuhisi faraja ndani ya nafsi yangu. Nilimuona mzee yule alikuwa ni mtu mwema sana kwangu kwani kama si uwepo wake shuleni pale ningekuwa nimekwisha kutendewa mambo ya kinyama mara kadhaa. Nilimtazama mzee yule usoni kwa sekunde chache kisha nikameza funda la mate yaliyokuwa machungu.

“Asante sana Babu Makwacha” Nikazungumza huku nimetazama pembeni.

“Usijali mwanangu, mimi nimekuja duniani kwaajili ya kutetea haki za wanyonge kama mimi mwenyewe” Alisema mzee yule.

“Hapana babu, wewe sio mnyonge” Nilizungumza huku nikihisi mzee yule alikuwa amejiita mnyonge kutokana na hali yake ya kimaisha kuwa duni.

Alinitazama kwa sekunde kadhaa kisha akatoa tabasamu la matumain ambalo kwangu lilizidi kunitia faraja.

“Hujui kitu Farida na ndio maana unazungumza hivyo” Alisema mzee yule kwa sauti ya chini huku akiwa ameweka mkono wake wa kulia kwenye bega langu la kushoto.

“Lakini babu tukiachana na hayo, ni kwanini umekuwa ukinisaidia kwenye matatizo yangu makubwa kama hili?” Nilihoji huku nikimtazama mzee yule kwa tabasamu.

“Sio ujanja Farida, bali Mungu mwenyewe ndiye anayepanga usaidiwe na mimi” Alisema mzee Makwacha.

“Mungu atakubariki sana kwa haya mema uliyonitendea” Nilizungumza kwa hisia.

“Usijali binti, ngoja mimi nirudi lindoni” Alizungumza mzee Makwacha huku akinipigapiga kwenye bega langu la kushoto kunifariji.

“Ngoja kwanza Babu” nilimzuia mzee yule kwa kumshika kwenye bega lake la kushoto ili asiondoke.

****

Kule nje Sarah alimfuata Anitha na kumkunja blauzi maeneo ya shingoni kwa hasira huku akiwa amemtolea macho na mashavu ameyavimbisha kwa jazba.

“Kwanini umekwenda kuliita lile libabu?” Alihoji Sarah hukua amemkamata vilivyo Anitha.

“Hebu niachie nikueleze basi Sarah” Alizungumza Anitha kwa sauti ya tafadhali.

“Sikuachii, leo nitafukuzwa shule kwaajili yako. Kwanini usingeniacha nimfundishe adabu yule mshenzi?” Alihoji Sarah kwa jazba.

“Nimefanya vile kwaajili yako Sarah, hebu niache basi nikueleze mpango wangu” Anitha akazungumza kwa msisitizo.

Sara alimuachia kwa kumsukuma kidogo nyuma kisha akasimama na kumtolea macho huku mikono yake akiwa ameipachika kiunoni kwa shari.

“Haya unataka kusema nini?”

“Hupaswi kunikasirikia wakati nafanya yote haya kwaajili yako”

“Heeh wewe! Nafikiri kidogo zimefyatuka. Umenizuia nisimtandike mshenzi yule halafu unasema ulikuwa unataka kunisaidi mimi?”

“Ngoja nikuulize swali dogo tu” Alizungumza Anitha kwa sauti ya upole.

“Unasemaje?”

Anitha alimvuta Sarah na kumnong’oneza maneno ambayo waliyafahamu wenyewe. Hata skuelewa ni mpango gani ambao waliupanga.

Sarah alihisi kaubaridi ka matumaini kakisafiri kwenye mishipa yake ya damu kuanzia utosini hadi kwenye kidole cha mwisho cha mguu.

“Duu, sikuweza kuwaza hilo hata kidogo aisee” Alizungumza Sarah huku akitoa tabasamu la matumaini.

“Okay, kama umekubaliana na hilo tusichelewe sasa” Alisema Anitha kwa shauku.

Unafikiri  hawa kumbikumbi wana mpango gani?




“Twende moja kwa moja kwa Matroni” Alizungumza Sarah na kumshika mkono Anitha kuelekea kwenye ofisi ya Matroni kukamilisha mpango wao.

****

Mzee Makwacha alirudi nyuma hatua moja na kunitazama kwa macho ya kuhoji

kwa sekunde kadhaa.

“Haya unasemaje?” Aliamua kuniuliza baada ya kuona nimenyamaza nikimtumbulia macho kama chura mjane.

“Mbona haujauliza sababu ya kupigana kwetu?” Nilihoji huku nikiwa nimetazama pembeni kwa aibu. Sikuwa na uwezo wa kumtazama mwanaume yeyote yule usoni kwa muda mrefu.

“Sina sababu ya kuhoji, mimi naelewa wazi kuwa umechokozwa” Alisema mzee Makwacha kwa sauti yake ya upendo.

“Hata kama nimechokozwa lakini lazima kuna sababu” Nikazungumza huku nikiwa bado nimetazama pembeni.

“Haya nauliza basi, ni kwanini umepigana?” Alihoji babu yule ili kuniridhisha pamoja na kwamba alionekana hakuwa na ulazima wa kujua sababu iliyokuwa imepelekea mimi na Sarah kukunjana bwenini mle.

Nilimeza mate na kumtazama kwa macho yaliyokuwa yamejaa masikitiko makubwa pamoja na huruma.

“Babu nashukuru sana kwa ukarimu wako ambao umekuwa ukinionesha katika matukio mbalimbali hapa shuleni, lakini nasikitika sana kukuambia kuwa sababu ya mimi kupigana siku ya leo ni wewe” Nilizungumza huku machozi yakinilengalenga.

“Farida…..” Aliita mzee makwacha kwa kuhamaki.

“Abee”

“Bado sijakuelewa unamaanisha nini?”

“Nimepigana kwasababu yako wewe” Nikazungumza kwa msisitizo huku nikijikuta nikishindwa kuzuia machozi kutiririka mashavuni mwangu.

“Umepigana kwasababu yangu mimi?” Alihoji mzee makwacha kwa msisitizo na mshangao wa hali ya juu.

Nilichezesha kichwa kuitikia swali lake kuwa alichokuwa amekisikia ndicho nilichokuwa nimekizungumza.

“Sijakuelewa binti, mimi na ninyi humu hosteli kuna uhusiano gani hadi mpigane kwasababu yangu mimi?” Alihoji mzee Makwacha kwa mshangao.

“Babu hata mimi sikupendezwa na maneno hayo na ndiyomaana nimeshindwa kuvumilia na kujikuta nikishikana na Sarah” Nikazungumza na kuangua kilio kwa sauti ya chini.

“Wewe binti hebu eleza kitu cha kueleweka, maana unanichanganya sasa” Alihoji mzee makwacha kwa sauti kali iliyokuwa imejaa msisitizo.

“Heti wanasema mimi nina uhusiano na wewe” Nikazungumza huku nikilia.

“Una uhusiano?” Mzee yule alizidi kushangazwa na maneno yangu.

“Ndio heti wanasema wewe ni mpenzi wangu”

“Mimi ni mpenzi wako?” Alihoji kwa mshituko mzee makwacha.

Niliitika kwa kichwa kama nilivyokuwa nimefanya awali kukubaliana na swali lake kuwa nilisema nina uhusiano na yeye.

“Nyie watoto mna laana sasa! Yaani mimi niwe na uhusiano na ninyi vifaranga, ninyi si bado vinuka mkojo kabisa? Au mna mpango wa kuharibu kibarua changu?” Alihoji mzee Makwacha kwa hasira.

“Hata mimi sikuwa nimependezwa na maneno hayo babu” nikasema.

“Pumbavu zenu! Ni nani ameropoka maneno hayo?” Alihoji mzee Makwacha kwa sauti ya ukali kidogo.

Niliinua macho yangu na kumtazama mzee yule kwa sekunde kadhaa na kubaini kuwa hakuwa amependezwa na taarifa zile nilizokuwa nimempatia.

“Ni Sara na mwenzake” nikajibu kwa sauti ya chini.

“Sarah ndio nani?”

“Ni yule niliyekuwa napigana naye hapa chini?” Nikaeleza na kuonesha kwa kidole pale chini nilipokuwa nimebanwa na roba ya Sarah.

“Shenzi kabisa! Na huyo mwenzake ni nani?” Alihoji mzee yule kwa jazba.

Ni yule uliyekuwa umeongozana naye wakati unaingia humu ndani” Nikaeleza huku nikihisi hali ya hatari kwa ambavyo mzee yule alivyokuwa akionekana.

“Pumbavu! Nyama ya Mbavu! Sura zao shupavu! Zenye ngozi ngumu kama ndovu! Hawa watoto wanataka kunizoea sasa, nafikiri niwaoneshe kuwa mimi sio wa kuchezewa chezewa na vifaranga” Alizungumza babu mlinzi kwa sauti iliyokuwa imejaa hasira na jazba lukuki.

“lakini babu, mi naona ungeachana nao, maana watakupotezea muda wako bure” Nilizungumza kwa tahadhari baada ya kubaini kuwa mzee yule alikuwa amekasirika sana kiasi cha kutetemeka mwili wake.

“Farida, ninyi ni watoto wadogo sana, bado mnanuka shombo. Hamuwezi kunivunjia heshima yangu na kuhatarisha kibarua changu halafu nikawachekea tu hivi hivi.” Alizungumza mzee yule.

“Lakini babu…..”

“Hakuna cha lakini hapa! Ni lazima mbuzi wale niwafundishe dunia” Alizungumza babu Makwacha kwa msisitizo.

Nilitulia kimya nikimsikiliza namna mzee yule alivyokuwa akiporomosha maneno makali yaliyokuwa yakitishia usalama wa watoto wawatu. Kusema ukweli mimi mwenyewe nilijikuta nikiogopa na kujutia uamuzi wangu wa kuzungumza ukweli kwa mzee yule. Laiti ningelijua kuwa mzee yule alikuwa vile, haki vile nisingefunua bakuli langu na kuropoka.

Mzee Makwacha alipoona namimi nilikuwa nimepoteza amani na kuingiwa na wasiwasi. Alinisogelea na kunishika kwenye mabega yangu kwa upendo huku macho yake akiwa ameyakazia usoni mwangu.

“Usiwe na wasiwasi binti, nitahakikisha suala hili halileti madhara yoyote kwako. Lakini ni lazima wale mbuzi niwape adhabu kali ili wawe fundisho. Na ikiwezekana nakwenda kuwaripoti kwa uongozi wa shule. Na nafanya yote haya kwasababu sitaki kukuona wewe ukisumbuliwa tena na viwatu vya ajabu katika masomo yako shuleni hapa” Mzee Makwacha alizungumza kwa sauti yake ya upendo ambayo iliufariji moyo wangu kwa kiasi kikubwa.

Namimi nikainua mikono yangu na kuishika ile mikono yake iliyokuwa juu ya mabega yangu.

“Asante sana babu, nimefurahia uwepo wako shuleni hapa” Nilizungumza kwa sauti laini ya upendo wa dhati kutokea ndani ya moyo wangu.

“Usijali mwanangu, mimi nipo kwa ajili ya wanyonge kama nilivyokwambia awali” alizungumza babu yule huku akiachia tabasamu la kujilazimisha.

Sote wawili tulitulia kimya kwa sekunde kadhaa kila mmoja akimtazama mwenzake usoni kwa umakini kama vile alikuwa na maneno ambayo alitaka kuyawasilisha lakini yalishindwa kutoka vinywani mwetu.

Tukiwa bado tumeshikana kwenye mabega yetu na kutazamana kama majogoo, ghafla mlango wa chumba kile kilichokuwa kikitumika kama hosteli ulifunguliwa na kundi la watu likatinga ndani. Kwakuwa kati yetu hakuana ambaye alikuwa ametegemea ujio ule ndani mle sote wawili tulishituka na kuachiana mikono ghafla.

Miongoni mwa watu wale waliokuwa wameingia chumbani mle walikuwa ni Matroni wetu, Mwalimu James, Mwalimu mwengine wa kike, pamoja na Anitha na Sarah.

Masikini ya Mungu tukajikuta tumepoteza muelekeo na kuhisi kama vile tulikuwa tumefumaniwa tukifanya majambozi. Ingawa haikuwa hivyo lakini watu wale waliamini kuwa huo ndio ulikuwa ukweli kwa namna ambavyo walikuwa wametukuta.

Babu Makwacha aliinamisha kichwa chake chini kwa sekunde kadhaa kama vile alikuwa akitafakari kitu cha kuzungumza ili kuweza kujinasua.

Mwalimu James alisogea hadi pale alipokuwa amesimama mzee Makwacha na kumshika kichwa chake kisha akamuinua kutoka kwenye lile pozi lake la kutazama chini.

Mzee Makwacha aliinua kichwa kile ambacho kilikuwa kimeshikwa na Mwalimu James. Sura yake ilikuwa ikionekana kujawa na wasiwasi mkubwa uliokuwa umechanganyikana na hofu ya kupoteza heshima pamoja na kibarua chake.

“Kumbe wewe ndio kidume hapa shuleni enh?” Alihoji Mwalimu James huku akiwa amemkazia macho babu Makwacha.

Ndugu msomaji mimi ninanyanyua mikono juu! Sarah popote alipo naomba umwambie  anisamehe! Nimekoma! Sitaki mimi! Sitaki matatizo na mtu! Nitaua mtu mjue Ohoo!




Mzee yule aliinamisha tena kichwa chake chini kujaribu kufikiria kitu cha kujitetea.

“Nakuuliza wewe!” Alihoji Mwalimu James kwa ukali hadi mzee Makwacha akashituka na kuinua macho kumtazama mwalimu yule ambaye alikuwa akionekana kujawa na hasira.

“Hapana kijana, mimi hapa nimekuja kumsaidia huyu mtoto…..” mzee makwacha alijaribu kujitetea lakini kabla haja maliza kuzungumza alikatishwa kauli yake.

“Kwahiyo wewe umekuwa shirika la misaada kwa watoto wetu si ndio?” Alihoji Matron kwa hasira huku akitetemeka midomo.

“Tena amezoea huyo, kila siku sisi tukiwa darasani wao wanaingia huku ndani wanakaa weee mpaka basi!” Alizungumza Sarah kwa msisitizo huku akiuyoneshea kidole kwa mzee Makwacha na kwangu mimi.

“We mtoto wewe, taratibu na mambo yako!” Mzee Makwacha alizungumza kwa kuhamaki huku akimtazama Sarah aliyekuwa ametoa ushuhuda wa uwongo.

“Ni kweli ndio kazi yenu” Anitha ambaye alikuwa amesimama pembeni huku mikono yake ameipishanisha kifuani alidakia.

“Sio kweli Matron, hawa wamepanga wani…..” Nikajaribu kujitetea na kutaka kuzungumza ukweli juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea ndani mle.

“Shut up! Malaya mkubwa wewe, umeletwa hapa kusoma ama kufanya ufirauni?” Matroni alizungumza kwa hasira huku akiwa ameweka mikono yake kiunoni na macho amenikodolea. Nakwambia kama macho yangekuwa yanatoboa, basi mimi siku hiyo ningekuwa na matobo matobo makubwa sana kwenye sura yangu.

“We mzee, umeletwa hapa kulinda getini ama vyumbani?” Alihoji Mwalimu James kwa msisitizo huku akionekana kuwa na kisasi dhidi yam zee yule. Inawezekana ni kwasababu ya lile tukio la kumfumania katika harakati za kunibaka kule ofisini.

“Jamani mimi sikufanya hicho mnachokifikiria ninyi” Alijaribu kujitetea mzee wawatu huku akionekana kukaribia kumwaga chozi.

Mwalimu James alivuta mkono wake wa kushoto na kuutua kwa nguvu kwenye shavu la mzee makwacha. Masikini ya Mungu mzee yule alijikunja na kuweka mkono wake kwenye shavu lake la kulia ambalo lilikuwa limepokea kipondo kile.

Pale nilipokuwa nimesisimama nilipatwa na maumivu makali sana utafikiri kibao kile alichokuwa amepigwa mzee Makwacha kilikuwa kimetua kwenye shavu langu mimi. Nilijikuta nimeziba macho yangu kwa mikono yote miwili.

“We kijana unathubutu kuinua mkono wako na kunipiga mimi?” Alihoji mzee Makwacha kwa hasira baada ya kuinua kichwa chake na kumtazama Mwalimu James usoni.

“Unasemaje! Unataka kupigana?” Alihoji Mwalimu James kwa shari.

“Unanipiga mimi, wewe?” Mzee makwacha alizungumza kwa hasira huku akitetemeka. Pamoja na kwamba alikuwa amekutwa katika mazingira ya kutatanisha lakini kitendo cha mwalimu yule kumtandika hakikumfurahisha kabisa.

“Haupigwi kwani wewe nani?” alizungumza Mwalimu James kwa kujiamini.

“Naomba usirudie tena kijana” alisema mzee Makwacha kwa tahadhari.

“Unanitisha, utanifanya nini wewe?” alihoji Mwalimu James kwa dharau huku akibinua midomo yake.

“Lakini Matron mimi sikufanya kitu chochote kibaya na mzee Makwacha” nilizungumza kwa kusihi huku machozi yakitiririka kwenye mashavu yangu.

“Yani wewe usizungumze kabisa, huna cha kujitetea. Lazima tukung’oe kabla hujaambukiza wengine ugonjwa wako” Matron alizungumza kwa hasira.

Niliposikia kauli ile ya kung’olewa shuleni pale nilihisi viungo vyangu vya mwili vikininyong’onyea utafikiri nilikuwa nimekunywa gongo. Nilifikiria haraka sana nyumbani kwetu ambako wazazi wangu siku zote walikuwa wakinisisitizia kukazana katika masomo.

“Hapana Matron, naombeni mnipe adhabu yoyote ile lakini msinifukuze shule” Nilizungumza huku nikiwa nimepiga magoti na shingo yangu ilikuwa imelalia upande mmoja kuonesha kuomba radhi.

“Mama mimi nipo tayari mnifukuze kazi, lakini huyu binti hana kosa ambalo amelifanya” Alizungumza mzee Makwacha kwa uchungu huku akionekana dhahiri kuwa alikuwa akinihurumia.

“Wewe huna mamlaka ya kutupangia cha kufanya, nyote hapa lazima tuwango’e” Alizungumza Mwalimu James kwa kiburi na jazba.

“Wanangu, mimi nimekuja hapa kumsaidia huyu mtoto alikuwa anapigana na huyu” Alizungumza babu Makwacha huku akionesha kidole kwangu na kwa Sarah ambaye alikuwa amesimama na Anitha pembeni kama vile na wenyewe hawakuwa wanajua kilichokuwa kimemleta mzee Makwacha ndani mle.

“Matroni, mimi sioni sababu ya kuendelea kuwabembeleza hapa wakati ushahidi tunao wa kutosha. Mimi nafikiri tuwafikishe kwa mkuu wa Shule” Alizungumza yule mwalimu mwingine aliokuwa ameogozana na msafara ule.

“Tena kweli hebu twendeni huku” Alizungumza Mwalimu James huku akimshika mzee Makwacha na kuanza kumsukuma kwa lengo la kumtoa nje ya chumba kile.

“We kijana, naomba uniheshimu” Alizungumza mzee Makwacha huku akiutoa kwa nguvu mkono wake uliokuwa umeshikwa na Mwalimu James.

“We mzee nini? Hebu twende huku.  Kama ungekua unajiheshimu ungekula vitoto ?” Alizungumza Mwalimu James na kumshika tena babu Makwacha na kumvuta nje kwa nguvu.

Masikini yamungu mzee yule alipepesuka na kutoka nje pasipo hiyari yake. Aligeuka na kumtazama Mwalimu James kwa hasira utafikiri alikuwa amemtukania mzazi wake.

Matron alinishika kwenye bega na kunisukuma nje kule ambako mzee Makwacha alikuwa amesukumwa na Mwalimu James

“Twende ukapate hukumu yako Malaya wewe! Unajifanya mtoto mwema kumbe shetani wa kuzimu” Matroni alizungumza alipokuwa akinisukumia nje.

Mwalimu James alimfuata tena mzee Makwacha ambaye alikuwa amesimama nje ya chumba kile akigoma kwenda ofisini kwa mkuu wa shule kwasababu alielewa kitendo cha kwenda huko kilikuwa ni sawa na njia ya kujifukuzisha kazi.

Mzee yule alifanya kitendo ambacho hakuna hata mtu mmoja ambaye alikuwa amekitegemea pale tulipokuwa, alimpisha ghafla mwalimu yule aliyekuwa akimsukumasukuma na kumfanya apepesuke. Mzee yule aliinua mkono wake wa kulia na kumtandika Mwalimu James kofi zito nyuma ya shingo.

Kwakuwa Mwalimu hakuwa ametegemea tukio lile alipepesuka na kwenda kusimama hatua kadhaa mbele yetu. Kisha mzee Makwacha akasimama sawasawa kumsubiri kijana yule aliyekuwa akinenge’neka mbele yake.

“Njoo nikufunze adabu. Peremende wewe!” Alizungumza mzee Makwacha kwa fhadhabu huku akiwa amesimama vizuri tayari kwa mapambano yale.

Mungu wangu! Hivi haka kababu kataweza kweli au kanataka kutufia tu hapa? Ndugu msomaji tafadhali toa neno kwa haka kazee hii ni madakesi ujue! 



Mwlimu James aligeuka na kumtazama mzee yule kwa hasira. Alikung’uta vumbi mikono yake kwa dharau na kuvuta hatua kurejea pale alipokuwa amesimama mzee yule tayari kwa kujibu Shambulizi.

Matron alinishika kisawasawa mkononi huku akiwatazama mzee Makwacha na Mwalimu Jmes walivyokuwa wamejipanga vizuri tayari kwa mapambano.

“We mzee unazidi kujitafutia matatizo tu” Akazungumza Matroni kujaribu kumtuliza mzee Makwacha ambaye alikuwa amebadilika na kuwa na hasira mithili ya mbogo aliyejeruhiwa.

Kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji. Mwalimu James aliendelea kumfuata mzee Makwacha kwa hasira zote.

Babu mlinzi alibonyea kidogo na kukunja ngumi. Mwalimu alipofika pale alirusha ngumi kali sana lakini mzee Makwacha aliuona mkono wa kijana na kuudaka ukiwa hewani kisha akaunyonga mkono ule kwa kujizunguusha nyuma mara mbili kama pia.

“Uuuwiiiii!” Mwalimu James alitoa ukulele mkali wa maumivu huku akijizunguusha kadri mzee makwacha alivyofanya.

Mlinzi alimuachia Mwalimu na kumtandika ngumi nzito kwenye mbavu za upande wa kushoto. Mwalimu akajikunja kuugulia maumivu ya ngumi ile huku akiwa ameshika sehemu aliyokuwa ametandikwa.

“Unafikiri nimeletwa hapa kusinzia eeh?” Alihoji mzee Makwacha kwa kebehi huku akiwa amekunja ngumi kwa mapambano yale. Hakuwa anafanana kabisa na mambo aliyokuwa akiyafanya pale. Kama ungemuona ungehisi pengine alikuwa ni mchovu tu na ameletwa kulinda shuleni pale kama picha ya mlinzi.

Matroni aliniachia na kumfuata Mwalimu James ambaye alikuwa amejiinamia akiugulia maumivu ya ngumi ya babu Makwacha.

Alimshika mgongoni na kuinama kumjulia hali mfanyakazi mwenzie aliyekuwa ameadhibiwa na babu kikongwe aliyekuwa na umri wa kutosha.

“Vipi Mwalimu amekuumiza huyu Mzee?” Alihoji Matroni huku akijaribu kumshika kwenye mbavu alipokuwa amepigwa.

“A a a a o o o shss!” Alipiga kelele Mwalimu James huku akiuondoa mkono wa Matroni kwenye mbavu zake kwasababu alihisi maumivu makali sana.

Matroni alimgeukia mzee Makwacha kwa hasira na wasiwasi wa kumsemesha.

“We mzee unajitafutia matatizo tu” Alisema matroni kwa hasira.

“Unasemaje wewe?” Mzee makwacha alihoji huku akitishia kumfuata Matroni pale alipokuwa ameinama.

“Ma ma a a a a a a!” Matron alipiga yowe baada ya kuomuona mzee yule alikuwa anamfuata. Alihisi zamu yake ilikuwa imefika.

“Nitakutandika na wewe! Unafikiri mimi nikifukuzwa kazi hapa watoto wangu watakufa na njaa?’ Alisema mzee Makwacha kwa jazba.

Mimi pale nilipokuwa nimesimama mapigo ya moyo yalikuwa yakienda mbio. Nilijua kabisa kuwa chanzo cha vurugu zote zile kilikuwa ni mimi. Na nilielewa kabisa baada ya pale nisingeweza kuachwa salama shuleni pale, ni lazima ningefukuzwa tu pamoja na kwamba sikuwa na kosa lolote.

Niligeuza macho yangu kwa hasira na kuwatazama Sarah na Anitha ambao walikuwa wakishangilia kile kilichiokuwa kikitokea pale. Walielewa kabisa baada ya pale mimi nisingeweza kuendelea na masomo.

Sarah alipoona namtazama kwa chuki alivuta hatua hadi pale nilipokuwa nimesimama na kunisukuma kichokozi. Nilirudi nyuma hatua mbili kuepusha shari. Akakunja uso wake kuning’ong’a.

“Tumekukomesha” Alisema Sarah kwa sauti ya Kunong’ona.

“Kwendeni zenu kule” Nikazungumza kwa jazba.

“Utakwenda wewe na babu yako sisi utatuacha hapahapa” Anitha alidakia huku akicheka kinafki.

“Mimi nikiondoka leo, ninyi mtanifuata kesho” Nikazungumza kwa jazba.

“Kwenda zako kule” Alizungumza Sarah kwa kebehi

“Achana na mimi wewe” Nikazungumza huku nikiangalia pembeni.

“Ndio umeshakuwa mwanakijiji hivyo shost, jiandae kuolewa tu. Wacha sisi wasomi tuendelee na fani yetu” Sarah alizungumza kwa kebehi huku akijitikisa na kurembua macho.

Maneno yale ya Sarah yaliingia vizuri sana kwenye mtima wangu na kutibua ubongo wangu wa medulla. Nilijikuta nikimvaa Sarah na kumtandika kofi moja takatifu sana maeneo ya shavuni karibu na jicho.

“Ma ma yangu! U u u wi i i i i!” Sarah alitoa ukulele mkali na kuinama chini huku ameshikilia jicho lake. Alikuwa akiona maruweruwe na kichwa kikizunguuka kutokana na kofi lile, chezea mimi wewe! Utakwenda mbinguni bila kupenda.

Anitha alipoona vile heti nayeye akanifuata kwa kasi ili kupigana na mimi. Nilijua kuinama chini tu nikainuka na funda la mchanga. Bila kujishauri wala kufikiri mara mbilimbili niliurusha mchanga ule usoni mwa Anitha.

“U u u u wiiiiiii!” Anitha naye akainama ghafla huku akifikicha macho yake kujaribu kuufuta mchanga uliokuwa umeingia kwenye mboni zake pasipo kubisha hodi.

Matroni Mwalimu James na kwenda alipokuwa ameinama Sarah.

“Kitu gani tena jamani?” Matroni alihoji huku akigeuka kumtazama Anitha ambaye alikuwa amejiinamia upande wake akilia kwa machungu ya kuwashwa na mchanga.

Timbwili lile lilikuwa ni zaidi ya lile la Asha ngedere. Nakwambia mastelingi tulikuwa tukifanya yetu eneo la tukio. Dakika chache watu hasa wanafunzi walikuwa wamejazana kushangaa mgogoro ule wa kukata na shoka.

Tulitazamana na mzee Makwacha kwa sekunde chache kisha tukajikuta tukiachia tabasamu la ushindi. Sielewi ni ushindi gani tuliokuwa tukiufurahia lakini kwa kiasi fulani tulijisikia faraja ndani ya nafsi zetu.

Ghafla gari ya Polisi ilifika pale kwa mwendo wa kasi sana kiasi cha kutimua vumbi utafikiri ilikuwa kwenye mashindano.

Kabla gari ile haikufunga breki walishuka makomandoo wa kikosi cha kuzuia ghasia kwa kuruka na kuja mbio kwenye kundi la wanafunzi waliokuwa wametuzunguuka.

Mimi na mzee Makwacha tukatazamana tena kwa sekunde chache huku tukiwa na wasiwasi wa kutiwa nguvuni na askari wale waliokuwa wamefika pale kwa mkwara wa hali ya juu. Chezea Polisi wewe, utaozea jela!



Kitendo cha Askari wale kushuka kwenye gari utafikiri wapo vitani kiliwatisha wanafunzi na kuwafanya wasambaratike kama siafu waliodondokewa na kaa la moto.

Mimi nilibaki nimesimama kwa mshangao huku nikitumbuliana macho na mzee Makwacha. Kwa kutumia ishara ya macho babu Makwacha aliniamuru niungane na wanafunzi wenzangu kutoweka katika eneo lile.

Sikutaka kupuuza amri ya mzee yule ambaye kwangu alikuwa ni mkombozi katika matukio kadhaa yaliyokuwa yakihatarisha usalama wangu shuleni pale. Hivyo nikatimua mbio na kumuacha yeye akiwa amesimama.

“Ni yupi?” Alihoji Askari mmoja mara tu alipofika pale walipokuwa wamesimama Matroni na Mwalimu James.

Matron alitumia kidole chake cha shahada kilichokuwa kirefu kama kalamu ya kuchorea katuni kuelekeza alipokuwa amesimama mzee Makwacha.

Babu mlinzi aliinua mikono yake juu kuonesha kuwa alikuwa amekubali kutiwa nguvuni na Askarii wale waliokuwa wamekuja utafikiri wanajeshi wa kimarekani wamemfuata Osama bin Laden kule kwenye mapango yake.

Askari wale walimvamia na mmoja kati yao alijivuta kwa hasira akiwa na lengo la kumzoa buti lakini babu Makwacha alitumia ukamanda wake na kuruka juu haraka kitendo kilichopelekea Askari yule kudondoka chini puuu!

Askari wengine wawili walimvaa na kuanza kumtandika virungu mzee wawatu kwenye miguu na kwenye magoti. Babu Makwacha alijitahidi kupambana nao lakini alijikuta akiishiwa nguvu kutokana na kile kipigo kitakatifu kilichokuwa kikitolewa na binadamu wenzake waliokuwa wamepoteza huruma dhidi yake.

Aliketi chini huku akiwaomba msamaha viumbe wale waliokuwa na roho za kinyama. Walimpiga kwa viatu vyao vya kijesho na kumkanyaga utafikiri walikuwa wakikanyaga udongo wa kufyatulia matofari.

Walimshika kwenye suruali kwa nyuma na kumnyanyua juu. Aliposimama walimnyanyua juu zaidi na kumsukuma kuelekea kwenye gari yao. Mzee Makwacha alikuwa akitembelea ncha za vidole kutokana na kile kitendo alichofanyiwa. Kwa upande wangu mimi nafikiri ni kinyume na haki za binadamu sijui wewe msomaji unaonaje?

Nikiwa nimejibanza kwenye kaukuta ka kuelekea msalani niliweza kushuhudia tukio zima lilivyokuwa limechukua sura yake katika mazingira yale. Roho iliniuma sana kwasababu nilielewa mimi ndiye nilikuwa chanzo cha matatizo yote yale yaliyokuwa yakimkabili mzee Makwacha. Nilitamani sana niende nikamsaidie lakini nilipokumbuka kuwa sikuwa na uwezo wa kufanya hivyo, ikabidi niendelee kujibanza kwenye kona ile kushuhudia unyama aliokuwa akifanyiwa binadamu mwenzangu.

Askari wale walitoa ishara kwa Matron pamoja na Mwalimu James waongozane. Hivyo Matron alimkokota Mwalimu na kupanda naye kwenye gari la Polisi.

Nilishuhudia gari ile ikiondoka kwa spidi kama ile iliyokuwa imefika nayo pale kiasi cha kuacha vumbi huku nyuma. Nilishindwa kuzuia machozi yangu yaliyokuwa na joto kali kutiririka kwenye masavu yangu makubwa.

Niliumia sana kuliko kawaida. Sikupenda hata kidogo vitendo alivyokuwa amefanyiwa mzee yule aliyekuwa na nia njema tu kwa wanafunzi. Alikuwa akitupenda na kutuheshimu wanafunzi wote. Huwezi amini wale wapuuzi wawili hawakuyaona yote hayo na kumsababishia matatizo mzee wa watu. Nikasali kwa mwenyezi Mungu kuviombea laana vibinti vile viwili, Sarah na Anitha.

*****

Kutokana na kitendo kile cha kukutwa chumbani na mzee Makwanda nilisimamishwa masomo heti wakidai ningewaharibu wanafunzi wengine kwa kuwaambukiza tabia yangu chafu ya umalaya.

Niliumia sana ndani ya nafsi yangu kwasababu ukweli ni kwamba tangu nilipokuwa nimezaliwa hadi kufikia wakati ule sikuwa nimelala na mwanaume hata mmoja.

Nilijaribu kwa kadri ya uwezo wangu kujitetea kwa kuzungumza ukweli lakini hapakuwepo na hata mmoja ambaye alinisikiliza na badala yake wakanifukuza kama mbwa wa mtaani wakidai kosa ni kukutwa na Babu Makwacha Hosteli iwe nimetembea nye au sijatembea naye.

Huku nikilia nilichukua mizigo yangu na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwetu. Nililia sana kwasababu nilielewa baba asingenielewa hata kidogo. Mwenyewe alikuwa amenipeleka kwenye shule ya bweni ili nisijihusishe na masuala ya ajabu kama yale.

Masikini ya Mungu niliamini wazi kuwa ndoto zangu za kusoma sana zilikuwa zimezimika ghafla. Nikapandwa na hasira dhidi ya Sarah na Anitha kwani wao ndio waliokuwa chanzo kikubwa sana cha mimi kufukuzwa shule.

Niliingia nyumbani majira ya saa tisa za Alasiri. Nikamkuta baba sebleni ameketi anaangalia runinga.

Mzee yule aliyekuwa akinipenda kuliko kitu chochote katika maisha yake alishituka sana aliponiona. Kitu ambacho kilimchanganya zaidi ni pale aliponitazama machoni na kukuta nimevimba kwa kulia.

“Farida!” Alihamaki na kubakia mdomo wazi huku akinitumbulia macho nilivyokuwa nikiingia na mabegi yangu ndani mle.

Nilijikuta nikianza kulia kwa kwikwi baada ya kumuona Baba. Sikujua mzee yule angechukua hatua gani baada ya kusikia kuwa nilikuwa nimefukuzwa shule.

Niliwega begi kwenye kochi dogo na mimi mwenyewe nikaenda kuketi kwenye sofa kubwa huku nikimwaga machozi.

Baba alikuja haraka sana poale nilipokuwa nimeketi na kuinama kwa wasiwasi. Alikuwa na hamasa kubwa ya kutaka kujua kitu kilichokuwa kimenisibu kipenzi cha roho yake.

“Ni kitu gani kimetokea mama, mbona hivyo?” Alihoji kwa wasiwasi huku akitazama begi langu nililokuwa nimeliweka kwenye kochi la pembeni.

Sikuweza kujieleza chochote, bali niliingiza mkono wangu kwenye mfuko wa sketi na kutoa barua, nikamkabidhi.

Baba aliipokea barua ile haraka haraka na kuanza kuisoma huku akiwa ametoa macho utafikiri anatafuta punje ya ulezi kwenye rundo la mtama. Baada ya sekunde kadhaa uso wake ulionesha kushituka. Akainua macho na kunitazama kwa makini.

“Umefukuzwa shule!” Alizungumza kwa sauti ya chini huku akinitazama kwenye macho yangu yaliyokuwa yamevimba kutokana na kulia sana.

Sikuweza kuzungumza chochote bali nilijikuta nikitoa kilio cha kwikwi. Niliumia sana ndani ya nafsi yangu.

Baba aliacha kunitzama na kushusha macho yake kwenye barua kuelendelea kusoma ili kujua sababu ya kufukuzwa kwangu. Zikapita sekunde kama ishirini na tisa hivi kabla ya kuinua macho yake na kunitazama tena usoni.

“Sasa umeanza kuijua dunia enh?” Baba alihoji kwa umakini huku akionekana wazi kukereka na kile kilichokuwa kimeandikwa kwenye barua ile. Sura yake ilikuwa imesawajika na kuvimba ghafla kwa hasira.

“Baba wamenisingizia, mimi sijawahi kufanya hivyo” Nikajaribu kujitetea huku nikilia.

“Sharap! Mwanahizaya wewe!” Baba alizungumza kwa ukali huku akinitolea macho utafikiri alikuwa amekabwa na mnofu wa nyama kwenye koromeo lake.




 Nilishituka sana kutokana na ile sauti ya ukali iliyokuwa imetolewa na baba. Kusema ukweli ndugu msomaji katika maisha yangu hadi kufikia siku ile sikuwa nimewahi kufokewa na baba. Mara nyingi sana mzee yule alikuwa akigombana na mama pale mkewake alipokuwa akijaribu kunirekebisha kwa kunifokea. Sasa siku hiyo mwenzenu nikajikuta nimeingia mwenyewe kwenye kumi na nane za mwanaume yule.

 “Umeanza lini kujua wanaume?” Baba alihoji kwa ukali.

 Nilinyamaza kimya huku machozi yakitiririka kwenye mashavu yangu. Nilitaka kujitetea lakini nikaogopa kwa namna ambavyo mzee yule alivyokuwa amekasirika.

 “Si nakuuliza wewe ngedere! Umekuwa bubu?” Baba alifoka tena na kunifanya nishituke kiasi cha kutaka kutimua mbio.

 “Baba kweli mimi siku….” Nilitaka kusema kuwa sikuwa nimefanya kosa lile la kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mlinzi kama ambavyo walikuwa wameandika kwenye ile barua yangu ya kusimamishwa masomo.

 “Nyamaza! Unajifanya unajua kutoa majibu si ndivyo?” Alizungumza mzee yule ambaye siku zote ndiye aliyekuwa rafiki yangu kuliko hata mama. Mtoto wa kike nikanywea na kuwa mpole kama kidonge cha asprini na mdogo kama piritoni. 

Nilishangaa sana yale mapenzi aliyokuwa akinioneshea baba siku zote yalikuwa yamekwenda wapi siku hiyo. Sikuwahi kufikiri kama siku moja ningeingia kwenye matatizo kiasi cha kunifanya nikosane na mtetezi wangu. Siku zote nilikuwa nafikiri mama alikuwa ni mkali kuliko baba, kumbe mzee yule alikuwa ni chui aliyeficha makucha yake kwa kuyafumbatia.

“Umefukuzwa shule kwasababu ya umalaya?” Akahoji tena kwa jazba.

 “Hapana baba wamenisingizia tu” Nilijaribu kujitetea.

 “Umesingiziwa! Wamekusingizia si ndivyo enh?”

 “Kweli baba, yule mzee alikuwa amekuja chumbani kwetu ku….” Nilitaka kueleza hali halisi ya tukio lilivyokuwa lakini kabla sijamaliza baba linitandika kofi takatifu la shavuni.

 “Sharap! Malaya mkubwa wewe unafikiri pesa tunaokota?” Alizungumza kwa ukali na kunifanya nizidi kumuogopa.

 “Sasa kwa taarifa yako, kama ulivyoingia hapa na mizigo yako ndivyo unavyotakiwa kutoka” Baba alizungumza kwa sauti ya taratibu lakini iliyokuwa na msisitizo kwa namna ambavyo maneno alivyokuwa akiyatamka.

 “Baba naomba unisamehe, napenda shule” Nilijikuta nikiangua kilio na kujaribu kujitetea.

 “Tena nikishazungumza huwa sipendi kupotezewa muda” Baba aliendelea kuzungumza taratibu kama masihara.

 Masikini ya Mungu mtoto wa kike nilipiga magoti na kuomba radhi utafikiri kosa lile nilikuwa nimelitenda kweli.

 “Umenitia aibu mtoto wewe, mwenyewe nilikuwa najisifu kila sehemu kuwa mtoto wangu ni mwema ana maadili, kumbe ninafuga pepo linaloishi kwenye mwili wa malaika wa dhambi” Baba alizungumza huku akirejea kwenye kochi na kuketi.

 Nilitembea kwa magoti kumsogelea huku mikono nikiwa nimeifumbata kifuani kutaka radhi za mwanaume yule aliyeonekana kubadilika na kuwa mkali kama moto wa kifuu.

 “Samahani baba, nakiri kutenda kosa naomba unisamehe sitarudia tena” Ilibidi nikubali kosa ili niweze kusamehewa pasipo kuelewa kuwa kama ni moto ndio nilikuwa nikichochoe kuni kavu na kujaribu kuuzima kwa petroli. 

 “Unakili kutenda kosa?” Alihoji baba kwa sauti yake ya upole tafauti na ile ya ukali aliyokuwa akiitoa awali. 

 “Sitarudia tena Baba” Nikazungumza kwa matumaini makubwa huku nikihisi ahuweni ndani ya moyo wangu baada ya kumuona Mzee amepoa na kuzungumza kwa sauti ya chini.

 “Pumbavu! Unakiri bila ya aibu kuwa umefanya utumbo! Unataka nikusifie au nikupe medali?” Mungu wangu binadamu yule akabadilika ghafla na kuwa mbogo mara mbili na alivyokuwa awali.

 Nilishituka sana na kujikuta nikitaka kutimua mbio lakini nilipoona bado ameketi kwenye kochi nikatulia lakini kwa tahadhari kubwa. Hata kama ningekimbia ningekimbilia wapi wakati pale ndio nyumbani kwetu. Nikasema kama ni kufa wacha tu waniulie mlemle ndani.

 “Wewe mtoto sio wangu! Nakwambia wewe mtoto sio damu yangu!” Alizungumza baba kwa jazba na kusimama kutoka pale alipokuwa ameketi.

 Nilijikunja na kuhisi pengine alikuwa amesimama kwaajili ya kunipa mfuweni lakini akaishia kuninyooshea kidole tu.

 Alikuwa akizungumza kwa kutetemeka huku mate yakimtoka kila alipokuwa akitokwa na maneno mdomoni mwake.

 Kusema ukweli ndugu msomaji siku hiyo sitakuja kuisahau katika maisha yangu. Nilitamani dunia ichanike katikati na mimi nitumbukie ndani yake ili kuepukana na mzee yule aliyekuwa amezidiwa na hasira.

 “Naomba uondoke nyumbani kwangu haraka sana!” Baba alizungumza kwa msisitizo huku akinipa ishara ya kutoka nje.

 Niliangua kilio ambacho sikujua kilitokea wapi. Niliumia sana ndani ya moyo wangu kwasababu sikuwa nimefanya kosa ambalo baba alikuwa akinituhumu kama ambavyo shuleni walikuwa wamenituhumu.

 Pengine ndugu msomaji ungekuwepo ungenitetea kwasababu ni wewe tu ndiye unayefahamu ukweli wa tukio hili. Nilibakia kimya kwani kila nilipokuwa nikijaribu kujitetea ndivyo nilivyokuwa nikizizidisha hasira kwa binadamu yule niliyekuwa nikijaribu kukabiliana naye.

 “Baba…” Nikaita kwa sauti ya huruma.

 “Koma wewe mimi sio baba yako! Nenda ukamuulize mama yako akwambie baba yako halali alipo. Nafikiri mimi amenichakachua tu. Siwezi kuwa na mtoto mshenzi kama wewe. Baradhuli mkubwa!” Baba alizungumza maneno hayo makali ambayo yaliuchoma sana moyo wangu.

 Ghafla mama alifika kutokea mlango wa nyuma na kusikia maneno yale machafu yaliyokuwa yakitiririka kutoka kinywani mwa mume wake.

 “Unasemaje wewe mwanaume? Hebu rudia tena!” Mama akahoji kwa kuhamaki.

 “Niondolee hiki kinyago chako sitaki kukiona hapa nyumbani kwangu” Baba alizungumza kwa tahayuri huku akijibaraguza. 

 “Sitaki kujua kumetokea nini, naomba urudie maneno yako uliyokuwa unayazungumza” Mama alizungumza kwa msisitizo huku akionekana kujawa na hasira.

 “Maneno gani?” Baba akajifanya haelewi.

 “Kwahiyo leo huyu mtoto sio wakwako si ndivyo?” Alihoji mama kwa sauti ya hasira.

 “Sina mtoto kama huyu mimi” Alisema baba na kurudi kuketi kwenye kochi.

 “Kwahiyo ndio umeamua kunitukana si ndivyo?” alihoji mama.

 “Sijui”

 “Sawa nitafanya kama unavyotaka, nakwenda kumtafuta baba wa huyu mtoto” alizungumza mama kwa kiburi na kwenda kuketi kwenye kochi lililokuwa upande wa pili na pale alipokuwa ameketi baba. Hivyo mimi nikawa nimepiga magoti katikati yao.

 “Enhe na wewe yamekufika mangapi?” mama alihoji kwa sauti yake ileile ambayo ilikuwa imepandishwa na maneno ya baba.

 Woga uliongezeka mara dufu kwasababu nilikuwa namuelewa vizuri sana mama hakuwa anapenda masuala ya kipuuzi puuzi na ndiyo maana mara zote alikuwa mkali. Hivyo nikahisi kesi yangu ilikuwa inapokelewa na jaji Iziraili mtoa roho za watu. Nikabakia kimya nikimtazama kama vile sikuwa nimesikia swali lake.



“Si nakuuliza wewe? Unanitumbulia mimacho mimi kama chura” Alizungumza mama kwa sauti kali.

Niliogopa kuzungumza na kujikuta machozi yakibubujika machoni mwangu utafikiri maji ya bomba.

“Amefanya nini huyu?” Mama alipoona sikuwa nazungumza ilibidi amgeukie mume wake na kuhoji.

“Liulize lenyewe toto lako si hilo hapo! Mimi sitaki hata kulizungumzia maana linanitia kichefuchefu” Baba alizungumza huku akiwa amenyoosha miguu yake na kuiweka juu ya meza na kugeuzia macho yake kwenye runinga.

“Wewe Farida umekuwa bubu siku hizi?” Alihoji mama kwa msisitizo.

“Wamenisingizia heti…” Nilitaka kuzungumza lakini nilijikuta nikishindwa na kuangua kilio.

“Limefumaniwa na wanaume huko shuleni kwao” Baba alizungumza kwa sauti ya taratibu utafikiri hapakuwepo na kitu chochote kilichokuwa kikiendeela ndani pale.

“Amekutwa na wanaume?” Mama alihoji kwa mshangao huku aihisi mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio.

“Unaniuliza mimi?” Alijibu baba kwa mkato.

“Hainiingii akilini kabisa.Ile shule ni ya wasichana watupu, sasa amekutwaje na wanaume? Au ametoroka shuleni?” Mama aliendelea kujawa na mshangao hasa baada ya kupata taarifa zile kutoka kwa baba.

“Kwani wanaume lazima wawe wanafunzi? Toto lako limekutwa likitoa burudani kwa walinzi wa shuleni kwao” Baba aliendelea kutoa taarifa zile kwa mtindo wa kujibu maswali ya mke wake.

“Mungu wangu wewe mtoto! Hicho ni kiranga cha aina gani?” Alizungumza mama kwa hasira.

“Ndio hivyo tena toto lako limekuwa kiburudisho kwa wafanyakazi wa shuleni kwao” Alisema Baba.

“Leo limekuwa toto langu! Kila siku nikisema unanijia juu kama moto wa kifuu na kunifokea kama mtoto mdogo. Leo limezuka la kuzuka unamuita mtoto wangu” Alizungumza mama kwa ukali na hasira.

Ghafla mwanamke yule alijiinua kutoka pale alipokuwa amekaa na kunivaa. Alinivuta juu na kunikunja nguo yangu maeneo ya kifuani.

“Wewe firauni kwanini unataka kutuaibisha?” Alizungumza mama huku akinitikisa kwa hasira. Alikuwa amekasirika kuliko siku zote ambazo nilikuwa nikikabiliana naye na kuja kutetewa na baba. Sasa siku hiyo baba alikuwa ametulia tuli kwenye kochi kama vile hakuwa ananiona nilivyokuwa nikitikiswa kama vile nazi sokoni.

Mama alivuta mkono wake wa kushoto juu na kuteremsha kofi takatifu lililofikia kwenye shavu langu la Kulia.

“Mama nakufaaaa!” Nilipaza sauti baada ya kupokea mkong’oto ule.

“Kufa Malaya wewe! Unafikiri tunalea watu wa ajabuajabu hapa” Baba ambaye alikuwa ameketi kwenye kochi alizungumza mara tu nilipotoa ukelele ule.

****

Kitendo kile cha kufukuzwa kwangu shule kilikuwa kimewafurahisha sana Sarah na Anitha. Waliingia chumbani mle ambako nilikuwa nikiishi nao pamoja. Walipofika walitazamana kwa sekunde chache kisha wakaachia kicheko cha kishambenga. Walicheka kwa sauti na kugongeana mikono.

“We Sarah Unachekaje hivyo?” Alihoji Anitha mara tu waliponyamaza.

“Mama yangu! kumbe haturuhusiwi kucheka hivi” Sarah alihamaki na kuzungumza huku ameziba mdomo wake kwa kiganja cha mkono.

“Shaurizako utamfuata shoga yako” Alisema Anitha.

“Mnh mwenzangu shoga tumemkomesha”

“Akafie mbele huko anajifanya mtuliivu angetuharibia tu kama tungemuacha” Anitha alizungumza huku akibenjua midomo yake ya juu utafikiri amepitiwa na harufu ya kinyesi.

“Mnh lakini na wewe Anitha una roho mbaya”

“Roho mbana nauza sumu?”

“Yani roho yako ina kutu! Afadhali hata ya muuza sumu”

“Kwa lipi baya nililolifanya?”

“Inamaana hujui?”

“Sijafanya dhambi yoyote ile” alisema Anitha huku akitabasamu.

“Una uhakika?”

“Asilimia laki tatu”

“Unajua Farida amefukuzwa kwaajili yako!” Alizungumza Sarah huku akimtazama Anitha kwa nyodo.

“Hovyoo! Mi nadhani unazungumzia kitu gani kumbe ni huyo mpuuzi” Anitha alizungumza huku akijilaza kitandani.

“Lakini Anitha una dhambi wewe!”

“Bwanaee kama ni dhambi wewe ndiye uliyesababisha” Alizungumza Anitha huku akijigeuza kitandani pale.



“Yeye ni mlinzi kilichomleta huku chumbani kwetu ni kipi? umbea wake umemponza”

“Kwakweli ni umbea wake, ngoja wakapumzike salama” Alizungumza Sarah

“Kwanza alikuwa anatubana humu chumbani, huoni sasa tumebaki wenyewe tunajimwagamwaga” Anitha alizungumza huku akitandaza miguu yake huku na kule kitandani pale.

“Tunajiachia!”

“Lakini mkuu naye mbona hakuwaita wazazi wa Farida wakazungumza?”

“Yapo makossa ya kuitwa mzazi lakini sio hilo ulilomtengenezea mtoto wa watu” Sarah akazungumza.

“Hilo nalo neno, sheria za hapa shule ni afadhali ukutwe na kosa lingine lakini sio kama lile”

“Kwakweli hapo hakuna cha kumuita mzazi na kuyazungumza. Ni nyumbani tu!”

“Nilikuwa nahofia kama angepimwa halafu ikabainika hajaguswa sijui ingekuwaje” Anitha akahoji kwa umakini.

“Hakupimwa kwasababu kosa lake ni kukutwa na mwanaume bwenini katika mazingira ya kutatanisha. Na sio kosa la kuguswa au kutokuguswa na mwanaume” Sarah akafafanua.

“Hapo safi angalau nina amani. Lakini Babu Makwacha naye yumo katika masumbwi!” Anitha alibadilisha mada huku akiinua kichwa chake na kumtazama Sarah ambaye alikuwa amejilaza kwenye kitanda nilichokuwa nakilalia mimi.

“Mnh nawewe usinikumbushe machungu, unajua amempiga mpenzi wangu” Alisema Sarah kwa masikitiko.

“He! Kumbe Mwalimu James ni mupenzi wako?” Anitha alihoji kwa mshangao.

“Chezea mimi wewe? Unafikiri ni kwanini alikuwa amekasirika?”

“Mnh basi makubwa! Mbona hata huniambii shoga yangu” Anitha alizungumza huku akitabasamu kwa kujilazimisha.

“Inamaana nilipokwambia kuwa nilishawahi kumpa mzigo haujanielewa?” Sarah akahoji.

“Najua kama alishakula mzigo lakini hukuwahi kuniambia kama mmekuwa wapenzi”

“Unafikiri amenitongoza lini?”

“Mie nitajuaje?”

“Ndio uulize sasa” Alisema Sarah huku akirembua macho yake kwa nyodo.

“Haya nauliza, hayo mapenzi yenu yameanza lini?”

“Jana”

“Mnh!” Anitha aliguna.

“Unaguna nini sasa?”

“Naona maajabu kwasababu nilichokuwa nakijua mimi Mwalimu James alilala na wewe kwa bahati mbaya tu lakini roho yake ilikuwa kwa Farida. Sasa leo hii nashangaa ameibukia kwako” Anitha alizungumza kwa mshangao.

“Ndio hivyo tena, unafikiri mbwa mwenye njaa ukimpa kazi ya kuwinda utaambulia nini?”


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG