Search This Blog

Sunday, April 18, 2021

HOUSEGIRL WA KITANGA (2) - 3

   


Chombezo : Housegirl Wa Kitanga (2)

Sehemu Ya Tatu (3)



“Anataka akuoe” mama alisisitiza.


“Nani?” nikahoji kama vile sikuwa nimeyasikia mazungumzo yale.


“Akuoe wewe, kumbe unafikiri nani!” Bi. Fatma akasisitiza.


“Hapana mama, mimi sitaki kuolewa! Tena sihitaji mwanaume wa aina yeyote yule katika maisha yangu!” nikazungumza mtoto wa kike kwa msisitizo huku nimetoa yale macho yangu makubwa utafikiri nilikuwa natolewa roho na Iziraili.


Vishindo vya miguu ya mama Kibo akielekea pale tulipokuwa tumekaa vikatufanya tunyamaze na kubaki kimya kama vile hapakuwa na jambo lolote lililokuwa likijadiliwa.


“Imran amenieleza kinagaubaga jinsi wanavyopendana na Mwantumu!” alizungumza mama Kibo huku akiketi kwenye kiti.


Nilishituka zaidi niliposikia maneno yale kutoka mdomoni mwa mama Kibo. Sikutegemea kama mwanaume yule angeweza kuzungumza mautumbo kama yale kwa mama Kibo.


“Nikweli dada, hilo ndilo kubwa lililotuleta hapa. Hakika watoto wangu hawa wanapendana sana” alizungumza Bi. Fatma kwa sauti kavu na kunigeuzia kibao kama vile sio yeye aliyekuwa akitukanana na kijana wake sekunde chache zilizopita.


“Kwani mama, huyo Mwantumu mwenyewe ni yupi?” ikabidi nihoji pengine kulikuwa na Mwantumu mwengine waliokuwa wanamuongelea pale.


“Sio mtu mwingine mkwe wangu, ni Mwantumu wewe” mama Kibo akazungumza kwa kujiamini.


Mungu wangu! Hata sikuweza kuamini kama Bi.Fatma angeweza kula njama na watoto wake na kunifanyia mambo kama yale. Niliumia sana ndani ya moyo wangu. Sikuwa tayari kuolewa na mwanaume yule ambaye alinisababishia matatizo makubwa katika maisha yangu.


Ukweli kutoka moyoni ni kwamba nilikuwa nimemchukia sana kaka Imran. Nikaomba Mungu anisimamie katika wakati mgumu kama ule. Hatimaye nikapata wazo ambalo nilihisi lingeweza kunisaidia kuepuka kikombe kile.


“Mama..” nikaita huku nimeinamisha kichwa changu chini.


“Zungumza tu mkwe wangu” Bi.Fatma naye aliniita mkwe kwa mara ya kwanza na kuzidi kuutibua ubongo wangu. Nikaomba dua Mungu aniongezee ujasiri na uvumilivu.


“Nilishindwa kueleza jambo hili mapema” nikazungumza na kumeza funda la mate.


“Jambo gani mama mkwe” mama Kibo alihoji kwa hamasa kubwa.


“Mimi ni mchumba wa mtu mwengine” nikazungumza kwa msisitizo na kumeza tena mate machungu.


“Wacha uwongo Mwantumu, mbona tulipozungumza hukueleza yote hayo? Hadi tumefunga safari na kuja kufuata utaratibu ndipo unazungumza maneno kama hayo?” kaka Imran akazungumza kwa kulalamika utafikiri kweli kulikuwa na makubaliano kati yetu.


“Nilikueleza kaka Imran na hata wewe unamfahamu vyema mwanaume ambaye ananipenda nami nampenda kwa dhati” nikaeleza kwa msisitizo. Ilibidi tuendelee kudanganyana kama ambavyo yeye ameamua kudanganya watu. Kilikuwa ni kikao cha uwongo na mauzauza. Kila mmoja alijitahidi kuficha ukweli halisi wa mambo kwa manufaa yake binafsi.


“Hapana mama Fadhili hampendi Mwantumu. Ukweli ni kwamba anamdanganya tu. Huwo ndio ukweli ambao Fadhili mwenyewe aliwahi kunieleza” kaka Imran alijikuta akizungumza maneno kibao ambayo hata hakuwa ameulizwa.


“Fadhili tena! Mbona sielewi jamani?” mama Kibo akahoji kwa mshangao.


“Mama mkubwa Fadhili ni mwanaharamu sana, siku zote yeye ni mtu wa kuvuruga mambo” kaka Imran akazungumza kwa hasira.


“Lakini kwanini haukuzungumza tangu tunapanga safari?” heti Bi Fatma naye akaungana nao utafikiri ni kweli kulikuwa na mipango.


“Nilijua nikiwaeleza mngenikatalia” namimi nikajifanya kujichetua, kama mbwai mbwai tu Ebo!


“Shangazi huyu binti anawazuga tu, ukweli ni kwamba mimi na yeye tunapendana sana” alizungumza kaka Imran kwa kujiamini.


Nilisugua kichwa na kutafakari jambo la kufanya ili niwaepuke viumbe wale waliokuwa wakiniletea mauzauza ya teja na muuza unga. Nikakumbuka kitu ambacho nikadhani kingekuwa ni msaada kwa wakati huo. Nikaingiza mkono wangu kwenye pochi na kuchomoa kipande cha karatasi.




“Chukua hii namba” nilimkabidhi Bi.Fatma kikaratasi kile.

“Ni namba ya nani?” mama alihoji huku akiitazama kwa makini.

“Naomba upige hiyo simu mama, nataka muamini maneno yangu” nikazungumza kwa msisitizo.

Mama alitoa simu yake na kuingiza zile namba kisha akagusa kitufe cha kupigia simu.

“Haya zungumza nae tusikie” mama alizungumza kwa kujifanya alikuwa na hamu kubwa ya kutaka kufahamu ukweli wa jambo lile.

Nilichukua simu ile kutoka kwa mama na kugusa kitufe cha sauti kubwa ambayo kila mtu aliweza kusikia. Punde simu ile ikapokelewa.

“Haloo” sauti ya kijana Shebughe ikasikika.

“Halo Sheby mimi nimeshaingia nyumbani Tanganyika vipi wewe umeshafika Mkanyageni?” nikajifanya kuhoji kwa sauti ya upendo.

“Ahaa mrembo huyo! Hii simu ni ya nani?” sauti ile ilihoji.

“Hii ni simu ya mama jamani pole kwa uchovu” nikazungumza maneno ya kujibebisha.

“Usijali, nimeshapumzika kidogo” Shebughe alijibu huku akiwa haamini masikio yake kama kweli nilimtafuta na kutaka kufahamu kama amefika salama.

“Nisaidie kitu kimoja rafiki yangu” nikazungumza kwa sauti ya kukaza kidogo.

“Haya niambie…”

“Kuna watu hawataki kuamini kama mimi na wewe ni wachumba, na wanataka kuniozesha kwa mwanaume mwingine….” Nilikuwa nikitoa maelekezo kwa kijana Shebughe lakini kabla hata ya kumaliza mama alinyakua simu na kuikata.

“Hakuna haja ya kuzungumza yote hayo” mama alizungumza huku akiweka simu yake kwenye pochi.

“Mwantumu mwanangu huwezi kufanya mambo kama hayo” mama Kibo alizungumza kwa kulalamika.

“Ma’mkubwa, naomba ufahamu kuwa nampenda sana huyu binti, nilikuwa tayari kufanya kila hila ilimradi nimuoe lakini kila kukicha amekuwa akiniletea vituko ilimradi nisiwe nae. Jamani nampenda sana Mwantumu mimi” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo na kulalamika.

“Kwahiyo unataka kusemaje?” mama akahoji kwa mkazo kidogo.

“Nataka niwaeleze kuwa, huyu binti ni mjanja kupita maelezo” alisema kaka Imran na kumeza funda la mate.

“Mimi nafikiri hakuna maelezo tena, binti ameshagoma hakuna haja ya kumlazimisha” alizungumza Bi.Fatma kwa sauti ya upole lakini iliyokuwa imejaa msisitizo wa hali ya juu.

“Hapana mama naomba uniache nizungumze kwasababu sikupewa nafasi ya kuzungumza kwa muda mrefu” Kaka Imran alizungumza kwa kulalamika.

“Mwache mtoto aeleze Bi.Fatma” alisema mama Kibo.

“Juzi usiku nilisikia sauti ya Mwantumu akipiga kelele za kuomba msaada chumbani kwake..”kaka Imran alitaka kuzungumza jambo lakini nikamuwahi na kumkatisha.

“Lakini mbona hayo yameisha kaka Imran” nikajikuta nikidakia kwasababu nilibaini alikuwa anataka kueleza kila kitu kuhusu mimi kufumaniwa chumbani nikiwa na baba pamoja na yeye katika mazingira ya kutatanisha.

“Wacha nizungumze ukweli watu waelewe kilichotokea” kaka Imran alisisitiza.

“Njia ya Muongo ni fupi Mwantumu, mwache azungumze” mama alisisitiza huku akiamini kaka Imran alikuwa anataka kujisafisha kwa kuzungumza uwongo.

“Ni kitu gani kimetokea tena?” mama Kibo akahoji na kuketi chini huku ameegemea ukuta na miguu kainyoosha mbele.

“Sasa baada ya kusikia kelele ikabidi nikurupuke na kuingia chumbani kwake ili kufahamu kilichokuwa kinaendelea” alizungumza na kumeza funda la mate kisha akaendelea na masimulizi yake.

“Sasa nilipofika nikakuta baba naye ameshafika lakini sasa baba alikuwa anaminyana na Mwantumu” kaka Imrana alieleza.

“Yaani mzee Sekiza?” Mama Kibo akahoji kwa mshangao.

“Ndio, sasa baada ya kushangaa kwa sekunde chache nikabaini Mwantumu alikuwa kama vile amepandwa na mapepo” alisema kaka Imran.

“Ikabidi muyapunge sasa?” mama Bi.Fatma alihoji swali la kebehi.

“Sasa katika purukushani zile kwa bahati mbaya nguo aliyokuwa amevaa baba ikafunguka na kudondoka chini” alieleza mwanamume yule kwa kuongopa bila hata ya aibu

“Enhe..” Shangazi aliendelea kusikiliza kisa kile.

“Sasa baba alipoona vile ikabidi akimbie nyuma ya kabati na kujificha ili asije akadhalilika mbele ya binti mdogo, nikabakia mimi najitahidi kumtuliza kwa kuminyana naye Mwantumu” kaka Imran alifafanua.

“Kwani Mwantumu ana mashetani?” Mama Kibo akahoji.

Bi. Fatma akabenjua mabega yake juu kuashiria kuwa hakuwa anafahamu jambo lolote kama nilikuwa na mashetani au laa. Hata hivyo alikumbuka siku moja aliyokuwa akitokea kazini na kunikuta nimeshika mwiko nikikimbizana na baba huku nikipiga kelele kama vile nimepandwa na mashetani. Lakini akajifanya hajui kama nilikuwa na mapepo au laa.

“Sasa Mama mkubwa jambo baya zaidi ni kwamba walifika mama na Fadhili na kunikuta mimi nikiminyana na Mwantumu wakati huo huo baba naye alishindwa kutoka kule nyuma ya kabati kwakuwa hakuwa na nguo” kaka Imran aliendelea kutoa masimulizi yake.

“Enhe… hadithi yenu ni tamu! Haya ikawaje?” alihoji mama Kibo huku akiketi vizuri.

“Mimi na baba tukabeba lawama ya ubakaji kwa kumlazimisha Mwantumu kufanya mapenzi, na mama naye alidondoka na kupoteza fahamu” kaka Imran alimalizia masimulizi yake yale kwa machozi. Alionekana kuumizwa sana na tukio lile alilokuwa analisimulia.

Bi. Fatma naye alikuwa ametulia kama vile kifaranga kilichokuwa kimemwagiwa maji ya baridi. Hakutegemea kama mambo yalikuwa yamekwenda kama vile ambavyo kaka Imran alikuwa anasimulia. Mawazo yake yeye ni kwamba Baba na kaka Imran walikuwa wamekula njama ya kuingia chumbani kwangu na kunifanyia ukatili wa kijinsia. Ukweli ndio huo pamoja na kwamba mwanaume yule alikuwa akijaribu kujitetea na kuficha ukweli halisi wa mambo.

Kwa upande wangu sikuwa nimeumizwa sana na uwongo ule wa kaka Imran pamoja na kwamba ukweli nilikuwa nao. Na nilifahamu kuwa zote zile zilikuwa ni jitihada za kujinasua tu. Sikuumia kwasababu sikutaka kashfa ile ifike kijijini kwetu na kunichafulia sifa nilizokuwa nazo. Nikajikuta nikishukuru Mungu kwa maelezo ya kaka Imran.

“We Mwantumu, ni kweli huwa unapandisha mashetani?” mama Kibo alihoji kwa msisitizo.

Nilipeleka mikono wangu kichwani na kukuna kichwa huku nikigeuza shingo na kutazama pembeni kama vile nilikuwa natafakari jibu la kutoa kwa lile swali la mama Kibo.



“We Mwantumu si nakuuliza wewe?” mama Kibo aihoji kwa msisitizo na kunifanya nishituke kidogo.

“Si nimewaambia mimi, huyu binti ana hila” kaka Imran alidakia.

“Mwache ajibu mwenyewe basi Imran!” alizungumza mama Kibo.

“Hawezi kukujibu kwasababu zote hizo zilikuwa ni hila za kunikataa mimi!” alizungumza kaka Imrana kwa msisitizo.

“Mamkubwa hata sielewi huwa inakuwaje, lakini wakati mwingine napoteza fahamu na zinaporejea watu wananieleza heti nimefanya mambo ya ajabu” nikaeleza na kujifanya kweli nilikuwa na mashetani ili kuzidi kuboresha yale maelezo ya kaka Imran.

“Kwahiyo na hiyo siku na yenyewe pia ulipoteza fahamu?” Shangazi akahoji.

“Nilijikuta nimeshikiliwa na mama, sikuelewa kitu ambaho kilitokea nyuma” nikaeleza.

“Dah pole sana mwanangu” mama Kibo alizungumza kwa sauti ya huruma.

“Asante mama…” nikazungumza na kujifuta machozi ya furaha huku wao wakiamini nilikuwa ninalia kwa uchungu. Sikuweza kuamini kama hatimaye nilikuwa nimefanikiwa kukiepuka kikombe kile cha kashfa ya ngono. Nakwambia kijiji chetu nilikuwa nakifahamu vizuri, hakikuwa na jambo dogo.

Mama alikuwa ametulia kama vile anajaribu kupima ukweli wa maelezo yale ya kaka Imran kama yalikuwa na ukweli wowote au ni mbinu tu za kujisafisha. Hakutoa neno lolote lile na kujikuta akifuta machozi.

Kaka Imran alipoona mama anafuta machozi akajipongeza kwa kujipigia makofi ndani ya moyo wake. Alihisi hali ya ushindi ikitawala katika kila kona ya maungo yake. Aliamini mimi nilikuwa nimejitolea kuwasaidia yeye na baba kutoka katika dimbwi lile la aibu.

“Mama mkubwa, ninaomba mumuulize Mwantumu ataacha lini kunifanyia vituko?” alizungumza kaka Imran.

“Hakuna haja ya kuuliza ilhali amebainisha kuwa anamatatizo” mama Kibo alizungumza.

“Kwahiyo inakuwaje kuhusu suala langu la kumuoa?” alihoji kaka Imran.

“Ameshasema haiwezekani, kwanini tumlazimishe!” alizungumza Bi.Fatma kwa msisitizo.

“Heti mwantumu unasemaje, mhurumie basi kijana wetu aishi na wewe kwa ndoa” mama Kibo alizungumza kwa kubembeleza.

“Mama Kibo siwezi kumsaliti mchumba wangu, nampenda sana tena sana” nikazungumza kwa msisitizo.

“Mama kweli nampenda sana Mwantumu lakini mapenzi hayalazimishwi. Ninaomba mniruhusu nianze safari niwahi biashara” alizungumza kaka Imran huku akionesha sura ya mkosaji.

“Huwezi kuondoka saa hizi, muda umekwenda sana” mama Kibo alizungumza huku akiangaia saa ya ukutani.

“Wacha niende mama, kilichonileta nimekikosa” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.

“Mwache aende tu dada” Bi.Fatma alizungumza kwa jazba kidogo.

“Mama ninyi mnakuja lini?” kaka Imran alizungumza huku amemgeukia mama.

“Siku Yesu atakaporudi na mimi ndipo nitakaporudi huko kwenu” alizungumza mama kwa msisitizo mkubwa kwasababu bado maelezo yale yalikuwa hayajamuingia akilini pamoja na kwamba kwa kiasi fulani alitaka kuamini.

“Lakini mama pamoja na kueleza ukweli wote lakini bado una hasira tu” kaka Imran alizungumza.

“Imran wewe nenda, kuhusu mama yako niachie mimi nitazungumza naye” mama Kibo alizungumza.

*****

Ilikuwa tayari umeshakatika mwezi mmoja tangu mimi na Bi. Fatma tuliporejea na kuamua kuendelea na maisha yetu katika kijiji cha Tanganyika. Lakini kwa upande wa mama Bi. Fatma, maisha yale ya kijijini kwake ilikuwa ni changamoto kubwa mno kwasababu mwenyewe alikuwa ni mwanamke mchakarikaji. Alikuwa amezoea kuchakarikia kwenye biashara kuliko kilimo.

Mama Kibo alimhurumia sana mdogo wake kwasababu alikuwa anamfahamu vizuri sana. Mara kadhaa alikuwa akijaribu kumshawishi arudi Dar kwa mume wake lakini mama alikataa. Hakuwa tayari kuishi nyumba moja na Baba pamoja na kaka Imran. Alitokea kuwachukia sana wanaume hao pamoja na kwamba kaka Imran alijitahidi kujitetea kwa kutengeneza ukweli wa uwongo.

“Bi. Fatma..” aliita mama Kibo jioni moja walipokuwa wameketi kibarazani na mama. Bi.Fatma hakujibu bali aligeuza shingo yake na kumtazama mama Kibo ili kusikia alichokuwa amekusudia kumueleza.

“Kwanini unajitesa hivyo?” alihoji mama Kibo.

“Kwanini dada..”

“Wewe umezoea biashara, kilimo kwako ni kitendawili. Tangu ulipokuwa mdogo ulikuwa hupendi kabisa kulima” mama Kibo alizungumza.

“Ni kweli dada, lakini simba akizidiwa hula hata nyasi” mama alijibu.

“Kwanini usirudi Dar mdogowangu?”

“Dada ni afadhali nife kwa kilimo hapa kwetu kuliko kurudi kwa mwanaume yule mshenzi” mama alizungumza kwa jazba.

“Simaanishi hivyo dada”

“Kumbe unamaanisha kitu gani?”

“Rudi Dar ukaendelee na biashara yako, na wala huna sababu ya kuishi huko kwa mume wako. Tafuta nyumba nyingine lakini shughuli zako za biashara ziwe zinaendelea” Mama Kibo alizungumza maneno ambayo yalionekana kumuingia mama na kwa kiasi fulani alijikuta akianza kushawishika.

“Lakini kweli dada, maana tangu niondoke duka limefungwa. Wateja wangu watakuwa wamehangaika sana” aizungumza Bi. Fatma kwa masikitiko.

“Wewe chukua Mwantumu wako, tafuta nyumba muishi” alizungumza mama Kibo kwa msisitizo.

“Nani Mwantumu tena?” Mama akahoji kwa mshituko aliposokia ushauri ule kutoka kwa dada yake.

“Ndio, Mwantumu atakusaidia hapa na pale usimuache abadani” mama Kibo alizungumza kwa msisitizo.

“Unafikiri Mwantumu atakubali kweli?”

“Kwanini asikubali, hakuna mtu anayependa ghahabu za shamba. Naamini atafurahi sana akisikia unaondoka naye tena” alizungumza mama Kibo kwa kujiamini pasipo kufahamu kama jiji la Dar Es salaam lilikuwa limenichefua na kunijaza ghahabu kiasi cha kulichukia kuliko kawaida.



“Sidhani kama atakubali yule binti, anaogopa kukutana tena na wale mafedhuli kule Mabibo” alizungumza mama Kwa msisitizo.

“Usiusemee moyo dada, woga ni jitihada za kushindwa” mama Kibo alizungumza.

“Basi utanipeleka nikaonane na wazazi wake” mama Bi. Fata alizungumza.

*****

Kutokana na amani ambayo nilikuwa nayo ndani ya nafsi yangu kwa maisha ya kijijini mwili wangu ulinawiri na kupendeza zaidi kiasi cha kuwa na mvuto hasa kwa wanaume wakwale.

Sikubabaishwa hata kidogo na wanaume ambao tayari walikuwa wamejitokeza kutaka kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mimi kwa sababu kule jijini Dar es salaam nilijifunza mbinu na mikwara mbai mbali ya wanaume waliokuwa wakijaribu kunitumbukiza katika vishawishi. Hivyo thamani na heshima yangu vikaongezeka mara dufu pale kijijini kwetu Tanganyika.

Kwa amani ile sikuwahi kujuta hata siku moja juu ya uamuzi wangu wa kurudi kijijini kuendelea na shughui za kilimo. Nilizaliwa na wakulima, nikalelelewa na kilimo na kwa wakati huo sasa nikaamua kufanya shughuli za kilimo, ndio mtoto wa nyoka ni nyoka hata kama nikivaa ngozi ya kondoo nitabaki kuwa nyoka tu.

Wazazi wangu walikuwa wakitoa sifa mara kwa mara kwa mama Bi. Fatma pamoja na mume wake mzee Sekiza kwa malezi mazuri waliyokuwa wamenipatia kwasababu mabinti wengi ambao walipata fursa ya kwenda jijini Dar Es salaam hawakuwa wakirudi salama. Wengi walibadilika na kuwa micharuko huku wengine wakirejea na mizigo ya mimba zilizokosa baba au magonjwa ya zinaa likiwemo gonjwa la UKIMWI.

Wazazi wangu hawakuwahi kufikiria wala kutambua kama binti yao niliondoka jijini Dar kwa kashfa ya kufumaniwa, tena fumanizi la mwaka. Walichokuwa wanakifahamu wao ni kwamba mimi na Bi.Fatma tulikuwa likizo kwa kipindi fulani tu, na baada ya likizo hiyo tungeondoka kurejea jijini Dar.

Jioni moja nikiwa chumbani nikipanga nguo zangu huku nikijiimbisha nyimbo moja na nyingine nilisikia sauti ya mama ikiniita kutokea nje. Nilipotoka niwakuta Bi.Fatma na mama Kibo wameketi kibarazani pamoja na mama.

“Shikamoo mama, shikamoo mamkubwa” nikaslimia kwa heshima.

“Marahaba Tumu hujambo?” wakaitika kwa pamoja.

“Sijambo, karubuni sana jamani. Leo mmetukumbuka jamani” nikazungumza huku nikiketi kwenye kipande cha gogo la mnazi kilichokuwa kikitumika kama kiti.

“Mama yako amekufuata mrudi kwenu” mama Bi.Zamda alizungumza kwa furaha.

Nilishituka sana baada ya kusikia maneno yale kutoka kwa mama. Sikutegemea kabisa kama kungetokea siku ambayo mtu angethubutu kunitamkia suala la kurudi tena jijini Dar Es Salaam. Nikavuta pumzi na kuzitoa kwa kuzisukuma kwa nguvu.

“Vipi mwanangu mbona unapumua kwa nguvu, haupo tayari kwenda mjini na mama yako?” mama yangu mzazi Bi .Zamda alihoji baada ya kuniona binti yake nikiwa na sura iliyosawajika.

Bi. Fatma alishaelewa mawazo yangu, alielewa wazi kuwa nisingekubali hata kidogo kurudi tena kwenye mikono ya wale wanaharamu wawili Baba na kaka Imran kule Dar.

“Mwantumu mwanangu nakuhitaji sana, maana safari hii nimehamia Kijitonyama ambako nitaishi mimi na wewe tu” alizungumza Bi. Fatma kwa upole na sauti ya ushawishi.

“Lakini mama..”

“Hapana mwanangu, nitateseka sana nikiwa pekeyangu” Bi. Fatma alizungumza kwa kubembeleza.

“Inamaana tutaishi wenyewe wawili tu?” niihoji kwa umakini.

“Hapana, nitazungumza na Mainaya tutakuwa naye. Wengine wote watabakia kule Mabibo kwenye nyumba kubwa” alizungumza mama kwa lengo la kunitoa wasiwasi.

Ama kweli dunia duara, yani kule nilipokukimbia leo hii ndipo watu wananishawishi heti nirudi tena! Kweli jamani? Hapana nikaamua kuweka msimamo mzito wa kugoma kurudi jijini Dar.

“Hapana mama, mimi sipo tayari kurudi tena huko Dar Es salaam” nikazungumza kwa kujiamini na msisitizo mkubwa.

“Kwani kuna shida yoyote ilitokea dada” mama yangu mzazi Bi. Zamda akahoji kwa umakini mkubwa hasa baada ya kuniona nimekataa safari ile.

“Hapana mama, hakuna shida yoyote iliyotokea…” nikazungumza harakaharaka ili kuepusha mama asije akabaini kitu.

“Kumbe ni kitu gani..?” alihoji mama yangu mzazi.

“Mama nimeamua kubaki na ninyi hapa kijijini ili niwasaidie shughuli za kilimo” nikajaribu kujitetea kwa kuongezea uzito umuhimu wangu wa kubaki pale kijijini.

“Mwantumu mwanangu, mbona ulipokuwa Dar ulikuwa unatutumia pesa za kulimia. Kusema ukweli tulipumzika kabisa habari za kushika mpini” mama Bi. Zamda alizungumza kwa msisitizo.

Maneno ya mama yaliniingia ndani ya mtima wangu na kujikuta nikiingiwa na huruma. Kumbe vile visenti nilivyokuwa nikiwatumia vilikuwa vikiwasaidia sana katika shughuli za kilimo.

“Mwanangu, umekuwa msaada mkubwa sana wakati wote ulipokuwepo mjini” mama alizungumza kwa msisitizo kiasi cha kunifanya nisisimkwe na mwili.

“Kwahiyo mama umesema tutaishi wapi?” nikahoji ili kuweza kupata uhakika wa usalama wangu.

“Nimepata nyumba Kijitonyama ili niweze kuwa karibu na biashara zangu” mama Bi.Fatma alieleza.

“Mama…” niliita na kumgeukia mama yangu kipenzi Bi. Zamda.

“Nakusikiliza mwanangu..” Bi. Zamda aliitika na kunigeuzia macho.

“Nimekubali kwenda Dar kufanya kazi ili niweze kuwatunza wazazi wangu” nilizungumza kwa hisia kali. Hakuna kitu kitamu kama kuwasaidia wazazi nao wakautambua msaada wako hata kama ni mdogo.


ENDELEA...20

“Na mimi nitakuongezea mshahara kuhakikisha malengo yako yanatimia” alizungumza Bi Fatma ili kuzidi kunishawishi.

Niliachia tabasamu la matumaini baada ya kumtazama mama yangu mzazi na kubaini kuwa alikuwa amefurahishwa kwa kile kitendo changu cha kukubali kuondoka na Bi. Fatma kurudi jijini Dares salaam.

*****

Maisha Mapya ya kijitonyama yaliweza kumfanya mama kuishi kwa amani na furaha ndani ya nafsi yake. Alikuwa tayari amezoea kuishi yeye kama yeye pasipo kuwepo baba mzee Sekiza wala watoto wake Imran na Fadhili.

Siku moja Bi.Fatma akiwepo Kariakoo dukani kwake alitembelewa na binamu Mainaya, yule mtoto wa dada yake mzee Sekiza.

“Shangazi unayaonaje maisha ya sasa na yale ya awali?” alihoji binamu Mainaya.

“Kwanini umeuliza mwanangu?”

“Naona kama vile kuna kitu hakipo sawa” alizungumza Mainaya kwa umakini mkubwa.

“Kawaida tu mwanangu!”

“Inamaana hautarudi tena kwa Mjomba?” mainaya alihoji.

“Amekutuma uje uniulize?” Bi. Fatma naye akahoji.

“Hapana mama, unajua sipendi kukuona ukiwa hauna furaha ya kutosha” Mainaya alizungumza kwa sauti ya kujipendekeza.

“Amani ninayo mwanangu, tena sana zaidi sana” Bi. Fatma alizungumza kwa msisitizo.

“Kweli mama?”

“Hakika…”

“Kama una amani kweli basi ni furaha kwangu…Ingawa..” Binamu Mainaya alitaka kuzungumza kitu.

“Ingawa nini..?”

“Kwanini umemrudisha tena yule binti?” Mainaya alihoji kwa umakini.

“Binti yupi..?”

“Tumu..”

“Kwani kuna ubaya mwanangu?” mama alihoji kwa umakini.

“Mama kale kabinti si ndiko chanzo cha familia yako kuvurugika?” alizungumza Mainaya kwa umakini mkubwa.

“Unajua sijazoea kuishi pekeyangu Mainaya, yule msichana ananichangamsha sana” alizungumza Bi Fatma kwa msisitizo.

“Kama ni hoja ya msichana wa kazi mimi nitakutafutia mwingine Shangazi” alizungumza Mainaya.

“Mwantumu ndio binti pekee ambaye anaweza kuishi na mimi” alizungumza mama kwa msisitizo.

“Shangazi unafuga nyoka mwenyewe unamuita binti kwanini usiachane naye?” alizungumza Mainaya kwa sauti ya ukali kidogo.

“Tuheshimiane Mainaya, tafadhali usidharau maamuzi yangu” Bi. Fatma naye akazungumza kwa ukali na kumfanya Mainaya kuwa mpole.

“Kusema kweli kale kabinti sikapendi” alizungumza Mainaya.

“Amekukosea nini mtoto wa watu Mainaya?”

“Mama tatizo Tumu ni mrembo mno” Mainaya alizungumza.

“Kwahiyo kuwa mrembo ni dhambi?”

“Tena sasa hivi ndio amezidi kupendeza kuliko hata alipokuwa tunaishi naye kule Mabibo” alisisitiza mainaya.

“Unajua usiniletee vituko! Kupendeza kwa mtu kuna ubaya gani au wivu?” mama alizungumza kwa mshangao.

“Najua simpati hata kidogo kwa uremo, lakini huo uzuri wake ndio uliosabaisha Baba na kaka Imran wakashawishika” Mainaya alifafanua maelezo yake.

“Naomba muniache na Mwantumu wangu, tena ukitaka tukosane zungumza habari za Mwantumu!” Bi.Fatma alizungumza kwa sauti ya ukali kiasi cha kumfanya Mainaya kujawa na hofu.

“Lakini Shangazi…”

“Lakini nini Mainaya wacha wivu wa kijinga! Kwataarifa yako Mwantumu hana muda wa kufanya hayo mautumbo, amefunzwa akafunzika mtoto wa watu” alizungumza mama kwa sisitizo.

“Haya tusije kulalamikiana tu huko baadae” Mainaya aliongeza.

“Hivi wewe mtoto una nini hasa! Umetumwa au?” mama alizidi kupandwa na hasira kutokana na vile vijineno vya Mainaya dhidi yangu.

“Tena nimekumbuka kitu Shangazi” Mainaya alisema.

“Nimekwambia achana na Mwantumu wangu!” Bi. Fatma akazungumza kwa msisitizo zaidi.

“Sio Mwantumu mama, ni mambo mengine”

“Enhe…”

“Ulinambia unataka nije tuishi wote Kijitonyama” Mainaya alizungumza.

“Wewe njoo tu lakini masuala ya Mwantumu niachie mwenyewe” mama alaieleza kwa tahadhari.

“Nitakufanyia kazi hadi usione tena umuhimu wa kuishi na Mwantumu” Mainaya alizungumza huku akijiinua kutoka kwenye kistuli alichokuwa amekalia na kunyoosha gauni lake kwa kiganja cha mkono wa kulia huku mkono wa kushoto akiwa amekamatia kipochi chake.

“Haya mimi natoka hivyo..” Alisema mainaya huku akivuta hatua kuondoka.

“Unatoka na ngoma gani?” alihoji mama kwa masihara.

“Natoka na mdumange” alizungumza Mainaya huku akiopndoka na kumuacha mama pale dukani akiendelea kupanga panga nguo kwenye henga.

*****

Maisha mapya ya jijini Dar Es Salaam yaliweza kunifanya nijifunze jamo moja la msingi sana. Kumbe sio kila mtu aliyekuwa anaishi ndani ya jiji lile alikuwa akiishi kwa taabu na mateso kama nilivyokuwa nikiisho mimi kwa mara ya kwanza.

Utulivu na amani ambavyo nilikuwa nikivipata kule kijijini kwetu Tanganyika ndivyo ambavyo kwa wakati huo nilikuwa nikivipata kule Kijitonyama. Ilikuwa ni tofauti kabisa na maisha ya kule mabibo nyumbani kwa mzee Sekiza.

Jioni moja nikiwa nimebeba ndoo ya uchafu nikienda kumwaga kwenye pipa la kutupia takataka nikasikia sauti ya mtu ikiniita kutokea upande wa pili wa barabara. Nikageuza shingo na kumuangalia mtu ambaye alikuwa ananiita.

“Huku nako vipi?” mtu yule alinisemesha.

Alikuwa ni mwanamke wa umri wa katikati lakini sura yake ilikuwa imejaa makovu kiasi cha kushindwa kumtambua. Kichwani alikuwa amevalia kofia ya chepeo. Nilijitahidi sana kukumbuka sehemu ambayo mwanamke yule tuliwahi kukutana lakini sikupata jibu.

“Mbona unashangaa tumu, inamaana haunikumbuki?” alihoji mwanamke yule.

Sauti yake haikuwa ngeni sana pamoja na kwamba sura yake sikuwa naikumbuka hata kidogo. Nikavuta hatua na kusogea hadi karibu kabisa na pale alipokuwa amesimama mwanamke yule.



“Samahani tumekutana wapi vile?” nikahoji kwa umakini mkubwa.

Yule mwanamke hakujibu swali langu bali nilimshuhudia akitokwa na machozi ambayo yalitiririka kwenye mashavu yake. Nikapatwa na wasiwasi na kujikuta nikivuta hatua taratiibu kurudi nyuma huku nikionekana wazi kwamba nilikuwa na wasiwasi dhidi ya mwanamke yule aliyekuwa ameamua kujitambulisha kwangu kwa machozi.

“Usiniogope Mwantumu, mimi ni BUPE” Mungu wangu! Mwanamke yule alijitambulisha kwa jina la Bupe.

Nilihisi mapigo ya moyo wangu yakienda mbio. Sikuweza kuamini macho yangu kwa kile ambayo nilikuwa nakishuhudia mbele yangu.

“Naomba unisamehe dada Bupe” nilizungumza kwa wasiwasi na woga.

“Nikusamehe kwa lipi mdogo wangu”

“Najua mimi ndio chanzo cha yote haya” nilizungumza kwa uchungu mkubwa.

“Hapana Mwantumu mdogo wangu, mimi mwenyewe ndiye chanzo cha adhabu niliyoipata” alizungumza dada Bupe na kujifuta machozi.

“Pole sana dada Bupe” Nilizungumza kwa huruma.

“Usijali mdogo wangu, huku nako vipi?” dada Bupe alihoji.

Kabla ya kujibu swali la dada Bupe nilitupa macho upande wa kushoto karibu na kwenye lile pipa la kutupia taka na kumuona mtu ambaye sikuwa nimetarajia kukutana naye katika mazingira kama yale. Alikuwa ni kaka Imran akivuta hatua kusogea pale nilipokuwa nimesimama mimi na dada Bupe.

“Mungu wangu..!” nilizungumza kwa kuhamaki na kutaka kukimbia lakini dada Bupe alinidaka mkono na kunizuia.

“Kuna nini Tumu!” alizungumza dada Bupe huku akinivuta mkono wangu.

“Sitaki kuonana na yule mwanaume” nilizungumza kwa sauti ya chini huku nikigeukia upande wa pili kuzuia kaka Imran asiweze kuiona sura yangu na kunitambua. Uwepo wangu katika jiji lile ulikuwa ni wa siri.

Dada Bupe aliinua macho yake na kumuangalia kaka Imran ambaye alikuwa akielekea pale tulipokuwa tumesimama? Alichofanya mwanamke yule ni kuvua kofia yake na kunibandika kichwani na kuivuta hadi usawa wa usoni.

“Pita hivi..” alinambia dada Bupe huku akinionesha kauchohoro.

Sikulaza damu bali nilikamata kale kauchochoro na kutoweka katika mazingira yale kama upepo. Nilipokata tu kona kaka Imran alikuwa ameshafika pale alipokuwa dada Bupe.

“Habari yako Bibie” alisalimia kaka Imran.

“Safi Imran habari za jioni?” dada Bupe naye akasalimia kwa sauti ya heshima.

“Mtoto wa wapi yule tena?” alihoji kaka Imran akimaanisha mimi.

“Mnh we mwanaume utakufa, hupitwi!” alizungumza dada Bupe huku akiachia tabasamu la kebehi.

“Nitapitwaje na vitu vizuri kama vile! Mimi nakataka kale” alizungumza kaka Imran.

“Yule ni mdogo wangu Imran” alijibu dada Bupe kwa ufupi.

“Kwani wewe hutaki shemeji bwana, fanya mpango basi. Mimi nimemuona kwa mbali tu nimempenda” kaka Imran alizungumza pasipo kuelewa kama binti waliyekuwa wakimzungumzia pale alikuwa ni mimi.

“Wacha tamaa zako za kimwili Imran, siwezi hata siku moja kukukaribisha kwa mdogo wangu” alizungumza dada Bupe kwa msisitizo.

“Huo ulokole umeanza lini Bupe, mimi ninajua vizuri sana kuwa wewe ni bingwa wa makrosi” kaka Imran alizungumza kwa masihara.

“Kwanini unadharau Imran, umelala na mimi halafu unataka kulala na mdogo wangu pia kweli huoni haya?” dada Bupe alizungumza kwa kulalamika.

“Yakwetu yamepita Bupe, sasa hivi hatuna uhusiano wowote, nipe mdogowako nidabue mate” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.

“Usinitanie Imran, wewe mwenyewe uliniahidi kuwa utanioa. Leo hii unajifanya mjanja” alizungumza dada Bupe kwa msisitizo.

“Bupe jamani ni mwanaume gani atakayekuwa tayari kuoa mwanamke kama wewe?” Imran alizungumza kwa kebehi.

“Unataka kusemaje we mwanaume?”

“Bupe tabia yako ya kukuwadia watoto wa kike inatia kichefuchefu”

“Wacha basi Imran, naomba usinihusishe na mambo ya kifirauni mimi!” dada Bupe alishindwa kuvumilia na kujikuta akizungumza kwa hasira.

“Usimdhihaki Mungu wewe! Hakuna ambaye hafahamu tabia zako”

“Imran naomba tuheshimiane baba”

“Kwenda zako kule, ndiomaana umeungua sura kwa tabia za kishetani” alizungumza kaka Imran kwa hasira baada ya kubaini kuwa dada Bupe hakuwa akiunga mkono mpango wake.

“Unasemaje we mende!” dada Bupe alizungumza kwa hasira.

“Tena kumbe hata nywele zimenyonyoka, yani umekuwa kama kinyago gani sijui” alizungumza kaka Imran kwa kejeli baaa ya kumuangalia kichwani na kubaini makovu yaliyosababisha kunyonyoka kwa nywele.

“Sasa kwa taarifa yako utanioa utake usitake!” Bupe akazungumza kwa msisitizo huku akipiga ngumi kwenye kiganja cha mkono wa kuume.

“Kwenda zako! Ulipokuwa mrembo ulikuwa unaniringia. Leo hii huna sura ndio unanihangaikia” kaka Imran alizungumza huku akimtazama dada Bupe kwa jicho la nyodo na kebehi.

“Lakini bado Nakupenda Imran, kumbuka ahadi zako za kuwa na mimi katika nyakati zote” alizungumza dada Bupe kwa kubembeleza.

“We Koma! Sihitaji kupendwa na kinyago mimi. Hivi siku ukivaa shera kwenye harusi utafananaje na hiyo sura yako kama nyani?” kaka Imran alidhihaki.




Maneno yale ya kaka Imran yalimuumiza sana dada Bupe kiasi cha kumfanya aondoke na kumuacha kaka Imran mwenyewe pasipo kuongeza neno lolote lile.

“Hiloo lione, ndio ukome siku nyingine kukuwadi watoto wa wanawake wenzako! Ngedere we!” kaka Imran alimsindikiza dada Bupe kwa maneno yaliyokuwa yamejaa kebehi na dhihaka.

*****

Nilitembea kwa wasiwasi hadi nilipofika nyumbani. Sikutegemea kama ningefanikiwa kumkwepa kaka Imran na kuondoka pasipo kukutana naye. Nilipumua kwa nguvu huku nikihisi kama vile nilikuwa nimenusurika kwa kupita kwenye tundu ya sindano. Nilikuwa nikihema kama vile nimefukuzwa na mnyama gani sijui.

Nilipotupa macho mlangoni niliona kuna mtu alikuwa amesimama akiniangalia nilivyokuwa nikivuta hatua kusogelea mlango ule. Hakuwa mtu mwingine bali ni Binamu Mainaya.

“Paka akiondoka panya hutawala, naona umeshaanza kuzurura kama mbwa!” alizungumza Mainaya kwa kebehi.

“Natoka kutupa takataka dada Mainaya” nikajibu kwa sauti ya upole na heshima.

“Unatoka kutupa takataka au kutafuta wanaume?” alizungumza dada Mainaya wakati nilipokuwa nikifungua mlango.

Maneno ya msichana yule yaliniingia hasa moyoni na kuhisi kichefuchefu. Sikuwa nimependezwa kabisa na kauli zake zile alizokuwa amekuja nazo siku hiyo. Nikatamani sijui nimvamie na kumrarua vipande vipande lakini nashukuru Mungu alinipa uvumilivu na kujikuta nikiropoka.

“Kawaida yangu huwa sitafuti wanaume, bali wanaume ndio wanaonitafuta” nilizungumza kwa majivuno na mimi ili kumkera.

“Unasemaje wewe mtoto!” alihoji kwa hasira.

“Nisamehe Binamu!” nikazungumza kwa kujishusha baada ya kubaini kuwa maneno yangu yalikuwa yamemgusa kama ambavyo nilikuwa nimetaka.

“Kwenda zako! Nani ni Binamu yako, Una hadhi ya kuwa binamu yangu wewe?” Jamani nyie mdada yule utafikri alikuwa akinisubiria anibandike yale maneno. Sasa kosa langu mimi ni lipi mbona hata sielewi.

“Kuna kosa gani nililofanya dada Mainaya jamani” nilizungumza kwa kulalamika.

“Inamaana hata makosa yako huyatambui, kweli we mtoto ni kashetani!” alizungumza Binamu Mainaya na kunisukuma mlangoni kisha akaingia ndani na moja kwa moja alielekea sebleni kuketi kwenye kochi kama vile mwenye nyumba.

Nilibaki pale mlangoni nimesimama huku nikiwa katika hali ya mshangao wa hali ya juu. Mainaya niliyekuwa nikimfahamu mimi alikuwa ni tofauti kabisa na Mainaya yule aliyekuwa amekuja kututembelea kule Kijitonyama tulipokuwa tukiishi na Bi. Fatma

“We Kunguru…!” nilisikia sauti ya Mainaya ikiita kutokea ndani.

Nakwambi pamoja na kwamba nilikuwa nimesikia vizuri sana akimuita huyo kunguru, lakini mtoto wa kike nikatulia kimya kama vile sikuwepo pale mlangoni.

“We Mwantumu..” akapaza sauti kwa nguvu kuniita mimi baada ya kuona Kunguru haitiki.

“Abee…” niliitika na kuvuta hatua kuingia ndani hadi sebleni ambako alikuwa ameketi kwenye kochi na miguu ameipachika juu ya meza utafikiri mwinyi Mpeku.

“Kwanini nakuita unakaa kimya?” akahoji kwa ukali huku amenitolea macho utafikiri fundi saa.

“Samahani dada, nilisikia unamuita kunguru!” nikajibu kwa upole.

“We unavuta bangi siku hizi ehn?” alihoji kwa mshangao.

“Kwanini dada?”

“Usiniulize, hebu nipe kahawa” alizungumza Binamu Mainaya huku akitikisa tikisa mguu wake wa kushoto aliokuwa ameupachika juu ya meza.

“Samahani dada leo sijaanda kahawa” nikajibu kwa heshima.

“Mungu wangu! Huvi unajielewa kweli we kadogoo?” alizungumza huku akiondoa miguu yake kutoka mezani na kunikazia macho zaidi.

“Mama alinambia leo nisimuandalie kahawa” nikatoa maelezo.

“Kwahiyo mama yako akisema na wewe unaacha! Sisi wengine unafikiri hatunywi?” alizungumza mwanamke yule kwa hasira na ukali.

“Sikujua kama utakuja dada Mainaya”

“Mama hakukueleza kama nitakuja kuishi hapa?”

“Alinieleza”

“Sasa kama unajua kwanini shea yangu umegoma kuiweka?”

“Hakuniambia kama leo utakuwepo hapa nyumbani”

“Wacha ushenzi we mtoto wa kike, hapa ni nyumbani na sipangiwi muda wa kuja ama kuondoka. Na kwa taarifa yako hivi ndio nimeshaingia” mwanamke yule alizungumza kwa msisitizo na jazba iliyokuwa imejaa kebehi.

“Sawa dada nimekuelewa, naomba basi nikaendelee na maandalizi ya chakula cha jioni” nikazungumza kwa sauti ya chini iliyolkuwa imejaa heshima na unyenyekevu wa hali ya juu.

“Kwahiyo ninayoyazungumza hapa hayana maana?”

“Sio hivyo Binamu”

“Naona umejua na Kiswahili sasa imekuwa shida, hebu njoo ukae hapa!” alizungumza huku akinielekeza kuketi kwenye kochi lililokuwa jirani na pale alipokuwa ameketi yeye.

Sikufanya hiyana yoyote zaidi ya kufanya vile ambavyo mwanamke yule alikuwa amenielekeza. Nikaketi kwenye kochi na kutega sikio langu kusikiliza kwa makini jambao ambalo alikuwa anataka kuzungumza na mimi.

“Naomba unipe ushirikiano kwa maswali ambayo nitakuuliza” alisema dada Mainaya kwa msisitizo.



Nilitulia kimya na kuendelea kusikiliza kwa makini hayo maswali ambayo mtu alitaka kunihoji.

“Hivi unayaonaje maisha ya huku?”

“Kawaida tu” nikajibu kwa ufupi.

“Kawaida enh?”

“Nafikiri huku ni kuzuri zaidi” nilizungumza makusudi kwasababu nilianza kuelewa alichokuwa anakitafuta kutoka kwangu.

“Nyooo! Shetani mkubwa wewe!” aliropoka kwa hasira mwanadada yule.

“Mnh!” nikaguna kwa mshangao.

“Nyoko nini! Hivi we umetumwa?” alizungumza Mainaya.

“Unamaanisha nini dada Mainaya?” nikahoji kwa mshangao.

“Kwenda zako! Kusoma hujui hata picha huoni. Hata hujali jinsi ulivyoisambaratisha familia yetu?” alizungumza Binamu Mainaya maneno ambayo yalinisababishia kichomi ndani ya tumbo langu. Sikutegemea kama siku moja ningekuja kubeba lawama ya kusambaratisha familia ile.

“Pamoja na kusambaratisha familia yetu, bado umeiganda tu kama ruba. Sikupendi! Sikupendi na ninakuchukia Mwantumu!” alizungumza Mainaya huku ametoa macho.

Kusema kweli nilishindwa kabisa kuzuia mafuriko ya machozi kukatiza katikati ya mashavu yangu. Nikayakumbuka maisha ya amani niliyokuwa nikiishi kule kijijini kwetu Tananyika.

“Najua umerudi kwaajili ya Fadhili, nitahakikisha hayo malengo yako yanapita kushoto” mainaya akazidi kunichachafya.

“Unanionea Binamu!” nililalamika huku nikilia.

“Haki ya Mgu vile naapa! Nitafanya kila hila penzi la Fadhili utalisikia kwa mbali. Wewe yanakufaa yaleyale makurubembe yako kina Imran”Alizungumza Mwanamke yule maneno mazito hadi yakanisababishia kizunguzungu.

“Usijifanye kulia kinafki binti, nitahakikisha nakusambaratisha kama ulivyoisambaratisha familia yetu” Mainaya alizungumza kwa hasira na sauti kubwa.

Nikiwa nimejiinamia na kulia kwa uchungu mkubwa, niligutushwa na sauti ya mtu akipiga makofi huku akiingia ndani ya nyumba ile. Nilipoinua macho yangu nikabaini kuwa mtu yule alikuwa ni mama Bi. Fatma.

“Hakika shughuli unaiweza binti!” mama alizungumza na kwenda kujitupa kwenye kochi la katikati.

“Shikamoo Shangazi” Mainaya alisalimia mara tu alipomuona mama ameingia kwa ile staili ya kupiga makofi ya pongezi.

“Shika yako, yangu niachie” alizungumza mama kwa kebehi.

“Lakini mama….” Mainaya alitaka kuzungumza lakini alikatishwa.

“Sikiliza binti, maisha yangu mimi na familia yangu wewe hayakuhusu” Bi. Fatma alizungumza kwa jazba akimwambia dada Mainaya huku akimuoneshea kidole kwa onyo.

“Mama we hujajua tu huyu mtoto ni nyoka!” alisema Binamu kwa msisitizo.

“Mainaya umetumwa na mjomba wako kuja kuharibu amani ya hapa nyumbani kwangu sio?” mama alizungumza kwa ukali huku akitetemeka.

“Sio hivyo mama, mimi nakusaidia yasije yakatokea mengine makubwa zaidi” Mainaya alijaribu kueleza kwa mke wa mjomba wake.

“Unanisaidia umekuwa nani wewe, wacha unafki na wivu wa kijinga binti” alizungumza mama Kwa hasira zaidi.

“Sawa mama lakini tusije kulalamikiana baadae” Mainaya alizungumza kwa sauti iliyopoteza ushirikiano huku akijiinua kutoka pale kwenye kochi.

“Sasa ni hivi, naomba uondoke kama ulivyokuja. Hatukuhitaji hapa ndani!” alizungumza mama kwa msisitizo.

“Lakini mama si ulisema unahitaji kuishi na mimi”

“Sihitaji tena, naona umeota mapembe sasa umesahau mipaka yako. Tunaomba uondoke sasa hivi” mama alizungumza kwa msisitizo.

Dada Mainaya alichukua pochi yake iliyokuwa mezani na kuipachika begani huku akionekana kujawa na aibu na hasira dhidi yangu.

“Sawa Shangazi mimi naondoka” alizungumza huku akivuta hatua kuusogelea mlango wa kutokea nje.

“Nenda bwana usituletee nzi hapa” alizungumza Bi. Fatma kwa hasira na kufunga mlango kwa nguvu baada ya Mainaya kutoka nje.

*****

Maisha ya kule mabibo kwa mzee Sekiza yalikuwa magumu kupita maelezo. Kwa kiasi kikubwa waliweza kuuona umuhimu wa mwanamke ndani ya nyumba ile. Kila mmoja alikuwa bize na shughuli zake kiasi cha kukosekana na utaratibu mzuri wa maisha ndani mle.

Majira ya jioni baba Mzee Sekiza alikuwa ameketi sebleni akitazama runinga na kaka Imran alikuwa jikoni akiandaa chakula cha jioni na Fadhili alikuwa ameketi sebleni pamoja na baba akitengeneza kachumbali.

Macho ya Baba pale sebleni yalikuwa juu ya paa kama vli kulikuwa na jambo kubwa sana akilitafakari. Utandu wa buibui uliokuwa umekatiza kwenye kona za ukuta zilimtoa kwenye lindi la mawazo.

“Hivi humu ndani tunaishi au tumekufa?” alizungumza Baba kwa sauti ndogo ya kukata tamaa.

Fadhili aliinua shingo yake kidogo kumuangalia baba kisha akarejesha macho na kuendelea kuandaa kachumbali.

“We Fadhili mi si ninauliza mbona hunijibu?” alizungumza baba kwa msisitizo.

“Naam Baba..” aliitika Fadhili kwa kushituka kidogo.

“Humu ndani tunaishi marehemu wangapi na maiti wangapi?” baba alihoji.

“Unamaanisha nini baba?”

“Mwite Imran atakuwa na majibu sahihi” Baba alisema huku macho yake yakiwa bado ameyakodoa juu ya dari.

“Broo..” Fadhili alipaza sauti na kumuita kaka Imran ambaye alikuwa jikoni akifanya maandalizi ya chakula.

Kaka Imran alitoka jikoni huku akiwa ameshikilia mwiko kwenye mkono wake wa kulia na shingoni akiwa amejifunga epron, kile kitambaa kinachotumiwa na wapishi ili kuzuia wasichafuke



ENDELEA..

“Mzee anakuita.” Fadhili alimtaarifu huku akimtazama mzee kwa jicho la tahadhari.

“Heti mimi unaniweka kundi gani?” mzee Sekiza alizungumza pasipo kumtazama kaka Imran wala Fadhili.

“Kwanini mzee wangu?” kaka Imrana alihoji kwa sauti ya upole.

“Naweza nikawa marehemu au maiti?” Baba alihoji na kuzidi kuwachanganya vijana wake.

“Unajua bado sijakuelewa Mzee?” Kaka Imran alizungumza huku akimtazama Fadhili ambaye alikuwa akitabasamu tu.

“Mimi nafikri humu ndani sisi sote ni marehemu, tulishakufa zamani” baba alizungumza kwa msisitizo.

“Kwani kumetokea nini Fadhili?” kaka Imrana akahoji.

“Tazama kule juu, unafikiri watu walio hai wanaweza kuishi katika mazingira kama haya” Baba alizungumza huku akionesha kidole kwenye wale buibui waliokuwa wamejenga kwenye dari.

“Mzee si unajua tena maisha ya kigetho getho haya” kaka Imran alizungumza na kugeuka kurejea jikoni.

“Huo ndio umuhimu wa mwanamke ndani ya nyumba” Fadhili alizungumza huku akiosha kisu.

“Sasa kama unajua mwanamke ni muhimu kwanini usioe ukatuletea?” Baba akahoji kwa msisitizo.

“Mzee mimi sina mpango wa kuoa leo wala kesho” Fadhili alizungumza huku akiangalia juu ya dari kwa wale buibui.

“Utapika hadi uote sugu za vidole” Baba alizungumza kwa msisitizo.

“Kupika kwangu sio shida, nitapika tu” Fadhili akajibu.

“Upikaji wenyewe ndio ule wa kujaziana michumvi kwenye chakula?” alizunumza Baba kwa msisitizo.

Maneno yale yalimfanya Fadhili kuinua macho kidogo na kumtazama baba yake kisha akaachia tabasamu la matumaini.

“Jamani msosi tayari” kaka Imran alizungumza huku akitokea jikoni na mkononi akiwa amekamatia sahani ya chakula.

“Sikuhizi tumesahau kabisa kutenga chakula mezani, tunakulia jikoni kama mapanya” Baba alizungumza kwa msisitizo kwasababu tangu mama alipoondoka, alikuwa anakwenda kujipakulia mwenyewe chakula jikoni.

“Mzee si unajua tena mambo ya getho, jiongeze tu” kaka Imran alizungumza huku akijiweka kwenye kochi ba sahani yake ya chakula.

“Hata aibu hamuoni. Mimi mzee mzima nainuka na kwenda kupakua chakula jikoni, kweli jamani?” Baba alilalamika.

“Hapa baba lazima kifanyike kitu, vinginevyo mambo yatazidi kuwa kizunguzungu” kaka Imran alizungumza huku akichota chakula kwa kijiko na kukipeleka mdomoni.

“Inabidi muoe ili tupate wa kutusaidia kazi humu ndani” baba alizungumza kwa msisitizo.

“Vipi kama tukitafuta mdada wa kazi akatusaidia wakati tunasubiri hizo ndoa” Fadhili alizungumza kwa umakini mkubwa.

“House girl utamtoa wapi sasa hivi. Huyo Mwantumu mwenyewe tulimpata kwa kubahatisha tu” Baba alizungumza.

“Tatizo House girl akiingia humu ndani anageuzwa kuwa mke wa familia” Fadhili alizungumza huku akiweka sahani iliyokuwa na kachumbali mezani.

“Hebu wacha mambo ya kipuuzi Fadhili, hapa tunajadili suala la msingi” alisema kaka Imran kwa hasira.

“Basi uoe tupate mtu wa kutusaidia kama anavyosema baba” Fadhili alisisitiza.

“Unadhani sitaoa, uliza uambiwe badao siku chache tu naoa toto la kitanga, nalileta humu ndani Kidii!” kaka Imran alizungumza kwa kujitapa.

“Duh afadhali utuletee toto la kitanga mana litakuwa bingwa la mapishi kama alivyokuwa Mwantumu” Fadhili alijibu huku akielekea jikoni.

“Unadhani nikimuoa namleta ndani humu, Karaga bahoo! Mke wangu ni wangu peke yangu” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.

“Huo utani wa ngumi sasa!” sauti ya Fadhili ilisikika ikitokea jikoni.

“Kwahiyo unahisi ukimleta humu ndani tutafaidika akitufanyia kazi?” baba ambaye alikuwa ametulia kwenye kochi alizungumza pasipo kumtazma kaka Imran.

“Tatizo sio kazi baba. Bro mkubwa anaogopa zee la kazi” Fadhili alizungumza huku akiwa anatembea kutokea jikoni na mkononi akiwa amekamatia sahani mbili zilizokuwa na chakula.

“Zee la kazi ndio nani?” alihoji baba huku akipokea sahani ya chakula kutoka kwa Fadhili.

“Suluhisho hapa baba ni moja tu” Fadhili alizungumza kwa kubadilisha mada huku akijiweka kwenye kochi.

“Usizuge dogo, fafanua hilo zee la kazi ndio lipi?” alihoji kaka Imran kishambenga akiwa anafahamu Fadhili amemaanisha zee la kazi ni baba mzee Sekiza.



“Jambo la kufanya we baba mtafute Bi mkubwa umshawishi arudi home” Fadhili alizungumza na kupuuza maneno ya kaka Imran ya kutaka aseme huyo zee la kazi alikuwa ni nani.

“Nimeshaongea sana na mama yenu lakini haelewi, sasa mimi nifanye nini!” Baba alieleza.

“Kama uliweza kumshawishi akakubali kufunga ndoa na wewe, utashindwaje kumshawishi arejee kwako?” Fadhili alizungumza kwa msisitizo huku akiendelea kutafuna chakula kilichokuwepo mdomoni.

“Swadakta, tangu uzaliwe leo peke yake ndio umezungumza maneno ya msingi dogo” kaka Imran aliunga mkono wazo la Fadhili.

“Kama ukishindwa mzee sisi tutaingilia kati, Bi mkubwa hawezi kukataa” alizungumza Fadhili kwa msisitizo.

“Unajua mzee usichukulie poa. Hakuna kitu ambacho sikipendi kama kujipikilisha” kaka Imran alizungumza kwa msisitizo.

“We unasema kupika, mziki upo kwenye kuosha vyombo na kusafisha choo” Fadhili aliongezea.

“Mkakati uliopo hapa kuanzia sasahivi ni kuhakikisha Bi Mkubwa anarejea ndani ya mjengo” kaka Imran alizungumza kwa msisitizo huku akichukua birauli iliyokuwa na maji ya kunywa na kuituma mdomoni.

Maneno ya kaka Imran na Fadhili yalimuingia sana baba kiasi cha kumfanya akili yake ifanye kazi mara tatutau zaidi. Alibaini ukweli na umuhimu wa maneno ya vijana wake pamoja na kwamba mziki wa kumrudisha Bi. Fatma pale ndani ulikuwa ni mzito.

“Sasa nani anajua anapoishi?” mama alihoji.

“Hiyo ni kazi rahisi sana, tukitaka kufahamu tutafahamu tu” alizungumza kaka Imran huku akipeleka kijiko cha chakula mdomoni.

“Sio lazima kufahamu anapoishi, hata dukani kwake tunaweza kumzukia tu” Fahili alizungumza huku akitafuna.

“Hapana mambo haya ni yakuzungumzia nyumbani na sio dukani” Kaka Imran akatoa wazo.

“Sasa nyubani kwake unapafahamu?” alihoji Fadhili.

“Tutamtuma Mainaya afuatilie” alizungumza kaka Imran kwa kujiamini.

“Mainaya hawezi kuwa msaada kwa hili, umesahau mziki wake wa vibao vya mbuzi?” baba alizungumza kwa tahadhari na kumfanya kaka Imran kuangua kicheko.

“Usijali mzee, Naya nimeshamtuliza kwa kumueleza ukweli kama nilivyomueleza mama na mamkubwa kule Tanga. Sasa hivi nimeshamuweka kiganjani hafurukuti” kaka Imran alizungumza kwa kujiamini.

“Kale kabinti kanavuta bangi sijui” baba alizungumza.

“Sasa kwa taarifa yenu mimi Mwantumu ameshanieleza kuwa Bi. Mkubwa anaishi Kijitonyama” kaka Imran alizungumza kwa kujiamini.

“Kijitonyama ni kubwa, anaifahamu nyumba yenyewe?” Fadhili alihoji kwa umakini wa hali ya juu.

“Amesema hafahamu nyumba wala mtaa lakini ni Kijitonyama” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.

“Huo ni mwanzo mzuri, nitafuatilia na nitawapa jibu ndani ya muda mfupi” Fadhili alizungumza kwa kujiamini.

Kikao kile cha dharura kilimalizika kwa makubaliano ya kuhakikima Bi. Fatma anarejea na kuishi kama zamani ndani ya nyumba ile. Kukosekana kwa uwepo wa mama ndani mle kulionesha pengo kubwa sana.

*****

Mkwara na maneno ya dada Mainaya yalinitikisa kwa kiasi fulani na kunifanya nitamani kurudi kijijini kwetu kuendelea na shughuli za kilimo, lakini maneno ya Bi. Fatma yalinitia moyo na nilipokumbuka maneno ya mama angu mzazi kuwa walikuwa wakinitegemea mimi kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kilimo nilijikuta nikipata nguvu na ujasiri wa kuendelea kubaki jijini Dar.

Kama ilivyokuwa kawaida yangu nilifanya shughuli zangu na kumaliza kazi zangu mapema kabisa. Nilikuwa nikitumia muda mwingi kupumzika na kusoma vitabu va simulizi kwasababu nilikuwa najituma ipasavo katika majukumu yangu. Ukizingatia zaidi familia yenyewe haikuwa kubwa kama ile ya kule mabibo. Kule Kijitonyama tulikuwa tukiishi watu wawili tu yani mimi na Bi. Fatma.

Nikiwa sebleni nimekamatia kitabu cha simulizi kilichokuwa kikijulikana kama BONGO DASLAM kile cha yule kijana Ayubu wa Tanga. Nilisikia mlango ukigongwa na kunifanya niweke kitabu kwenye kochi na kuelekea mlangoni.

Ndugu msomaji huwezi kuamini mtu aliyekuwa akigonga mlango alikuwa ni Fadhili. Nilishituka sana kwa sababu sikuwa nimetegemea kukutana na kijana yule katika mazingira yale. Nilichokuwa ninakifahamu mimi ni kwamba hapakuwa na mtu ambae alikuwa anapafahamu nyumbani pale zaidi ya Mainaya. Hivyo niliishi kwa uhuru na kujiachia pasipo kuwa na hofu wala shaka.

Fadhili hakuwa ameshangazwa baada ya kuniona kama ambavyo mimi nilikuwa nimeshangazwa na kitendo cha kumuona yeye pale nyumbani. Zilipita kama sekunde thelathini hivi tukitazamana pasipo kuzungumza neno lolote lile kati yetu.

“Kwanini unanipenda hivyo?” Fadhili alivunja ukimya na kuhoji swali ambalo sikuelewa maana yake.

“Nani amekuelekeza huku?” nikahoji kwa umakini.

“Hata kuzimu hapafahamiki lakini watu wanafika” Fadhili alijibu na kuingia ndani akiniacha nimesimama nikimkodolea macho kwa mshangao.

“Mama hayupo lakini!” nikaeleza huku nikiwa bado nimesimama pale mlangoni.

“Najua…” alijibu Fadhili na kuchukua rimoti ya runinga na kuwasha.

“Sasa kama unajua hayupo umekuja kufanya nini huku?” nilihoji huku nikivuta hatua kuelekea kule sebleni.

“Mama hayupo lakini wewe si upo, au hata wewe haupo?” alizungumza Fadhili huku akibadilisha vipindi kwenye runinga.

“We umejuaje kama mimi nipo hapa?” nilihoji huku nikiegemea juu ya mguu wa sofa nikawa kama vile nimesimama.

“Wacha maswali yako bwana, unafikiri mama anaweza kunificha kitu mimi?” alizungumza Fadhili kwa sauti ya kujiamini.

“Kwahiyo mama ndio amekwambia kama mimi nipo hapa?” nikahoji kwa mshangao kwasababu makubaliano yetu mimi na Bi. Fatma ni kwamba wale watoto wake pamoja na baba wasifahamu uwepo wangu pale nyumbani kwake.

“Mimi nimekufuata wewe, hebu kaa hapo tuzungumze” alisema Fadhili huku akinielekeza niketi kwenye kochi.

Nilipumua kwa nguvu na kwenda kuketi kwenye kochi na kumsikiliza Fadhili kama ambavyo ametaka.

“Nani amekwambia kama mimi nipo hapa?” nikaendelea kuhoji kwa msisitizo mara tu nilipoketi.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG