Chombezo : Housegirl Wa Kitanga (2)
Sehemu Ya Pili (2)
Maneno ya Endru yakampandisha hasira Fadhili na ghafla akashitukia akivutwa shingo na kutandikwa kichwa kimoja matata sana. Masikini kijana wa watu alipepesuka huku na kule na kudondoka chini kama kindege kilicholengwa na mwindaji.
Mungu wangu! Niliogopa sana baada ya kuona mtafaruku ule. Nikasema lile balaa lililotokea kule mgahani kwa dada Bupe lilikuwa linakwenda kutokea tena kwa taswira ileile pale Ubungo.
Nakwambia sikuweza kuendelea kushuhudia nikiingia katika tuhuma ambazo hazikuwa na msingi kwa mara nyingine. Yaliyonikuta kule mgahaani kwa dada Bupe yalikuwa yametosha. Nilichukua mizigo yangu na kutimua mbio kuelekea ndani ya stendi ya Ubungo. Sikutaka hata kufahamu kule nyuma kuliendelea kitu gani kati ya wale mafahari wawili waliokuwa wakipimana nguvu.
******
Kule nyumbani kwa mzee Sekiza Kaka Imran alikuwa pale sebleni ameketi lakini masikio yake yalikuwa yakisikiliza majibizano kati ya mama na baba yaliyokuwa yakiendelea kule chumbani. Alianza kuhisi mapigo ya moyo wake yakiongezeka spidi ya kudunda. Akasimama na kuvuta hatua za hapa na pale akizunguuka ndani mle pasipo kuwa na muelekeo.
Ghafla malano wa chumbani kwa mama ulifunguliwa na Baba akatoka huku akionekana kupoteza amani na matumaini ndani ya moyo wake.
“Baba vipi?” Kaka Imran akahoji kwa sauti ya chini mara tu alipomuona Baba akiwa katika hali ile.
Baba hakutoa kauli yoyote zaidi yakutikisa kichwa kutoa ishara ya kusikitika na kukata tamaa.
“Ni kitu gani kinaendelea?” kaka Imran akahoji kwa taharuki zaidi.
“Mambo si mambo mwanangu” Baba alizungumza na kwenda kuketi kwenye kochi kisha akaweka kidevu chake katikati ya viganja vya mikono yake kama vile kulikuwa na kitu anakitafakari kwa makini.
“Kumetokea nini?”
“Hakuna siri tena, kitumbua kimeingia mchanga” Baba akazungumza kwa sauti ya kukata tamaa.
“Kwahiyo mama anajua kilakitu?”
“Nafikiri kuna kamchezo kanaendelea hapa kati” alizungumza Baba kwa umakini.
“Au kumbukumbu zimeanza kumrejea?” alisema kaka Imran kwa hofu.
“Sio rahisi, nafikiri kuna mtu amemweleza yaliyotokea” Baba akazungumza na kumeza funda la mate.
“Atakuwa Fadhili tu sio mtu mwingine” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.
“Au Mainaya, mana nimewakuta wawili wanazungumza” Baba alaieleza kwa umakini.
“Na kama ni Mainaya basi atakuwa ameambiwa na Fadhili kwa maana mimi nilikwishampanga Mainaya na akaniamini” kaka Imran alisisitiza.
“Hivi tutaweka wapi sura zetu hizi Baba” alizungumza kaka Imran kwa masikitiko.
“Tufanye kila kitakachowezekana, Mainaya asifahamu jambo hili. Siku akilifahamu tu ujue tumekwenda na maji” Baba alizungumza kwa msisitizo.
“Mimi ninaamini Mainaya hafahamu kitu, hapa jino bovu ni Fadhili tu” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.
“Sasa na kama sio Fadhili atakuwa nani?” Baba aliendelea kuhoji huku akiamini Fadhili hakuhusika kutoboa siri ile kwa Bi.Fatma.
“Mmoja kati yenu atakuwa amemsaliti mwenzake” ilisikika sauti ya Mainaya akizungumza kutokea kwenye malango wa jikoni.
Duu! Kumbe Mainaya alikuwa amesimama pale kwenye mlango wa jikoni muda mrefu akisikiliza mazungumzo ya wawili wale walio onekana kuficha jambo fulani ndani ya nafsi zao. Mainaya akahusisha mazungumzo yale na maneno ya Bi.Fatma kuwa kulikuwa na jambo zito lililokuwa likimfanya arudi kijijini. Pia Mainaya akakumbuka kauli ya mama ya kumtetea Fadhili juu ya tuhuma zile.
Kaka Imran na Baba walipogeuza shingo zao na kumuona Mainaya akiwasemesha wakajikuta kama vile hawajavaa nguo.
“Kumbe upo hapa mama” alizungumza Baba kwa sauti ya kutokujiamini.
“Nipo kitambo tu” akajibu Mainaya huku amefunga mikono yake kifuani na kuwatazama wawili wale kwa jicho la kebehi.
“Hivi dada Mainaya, Fadhili amekueleza kitu gani?” Kaka Imran akajikuta akihoji pasipo kutarajia.
“Kuhusu nini?” akahoji Mainaya.
“Inamaana Fadhili hajakueleza jambo lolote?” Baba naye akadakia na kuhoji.
“Kwani ni kitu gani kinaendelea humu ndani? Mbona siwaelewi jamani!” Mainaya akahoji kwa mshangao huku akionekana wazi kuchanganyikiwa na mienendo ya watu wa familia ile.
“Basi kama Fadhili hajakueleza kitu, hakuna jambo lolote linaloendelea humu ndani” Baba akaeleza kwa sauti ya upole lakini iliyokuwa ikikatakata kutokana na wasiwasi.
“Jamani safari ndio imeiva hivi” ikasikika sauti ya Bi.Fatma ikiwaongelesha na kuwakatisha mazungumzo yao pale sebleni.
Walipogeuza macho yao kule kwenye mlango wa kutokea wakashuhudia mama amebeba mabegi yake tayari kwa safari.
“Inamaana we mwanamke unaondoka kweli?” Baba akahoji kwa mshangao baada ya kumuona mke wake amebebelea mabegi makubwa yaliyokuwa yamefungasha vitu vya kutosha.
“Alaa! Kumbe ulifikiri naigiza?” akahoji mama kwa kebehi.
“Mama unakwenda wapi, unajua bado haujapona vizuri” kaka Imran akazungumza kwa mshangao.
“Tena we nyamaza kunguru wewe!” alifoka mama huku akimnyooshea kidole kaka Imran kumpa onyo.
“Lakini mama…”
“Koma we ngedere! Mjaa laana mjukuu wa Shetwana!" Mama akazungumza kwa hasira zaidi.
“Sasa kwa taarifa yako humu ndani leo hatoki mtu!” Baba akazungumza kwa kukoroma.
“Unasemaje! Unasemaje?” Mama alihamaki na kuinua mabeki yake tayari kwa kutoka. Mwanamke yule wa kitanga alikuwa amepandwa na hasira kiasi cha kuwa kama koboko aliyejeruhiwa. Alikuwa anasubiria mtu ajiingize katika anga zake amuoneshe shughuli.
Baba akamfuata Mama kwa kasi akiwa na lengo la kuzuia safari ile ya Bi.Fatma ambayo kwa upende wake aliiona kama vile ingemletea kashfa hasa kule Tanga kwa wakwe zake.
Bi.Fatma aliusoma ule mchezo na kumsukuma Baba kwa nguvu kiasi cha kumfanya apepesuke na kwenda kujigonga kwenye fremu ya mlango wa kutokea nje. Maumivu aliyokuwa ameyapata Mzee yule yalimfanya ainame chini na kushika paji lake la uso.
Jamani nyie sisi wanawake tunaonekana wanyonge sijui wapole, bwana ukiingia katika anga zetu unaweza ukajikuta unapoteza maisha hivihivi. Hata sijui zile nguvu huwa zinatokeaga wapi.
“Siwezi kuishi kwenye nyumba iliyojaa mafirauni na mashetani kama ninyi” mama akazungumza kwa hasira huku akiinua mabegi yake.
“Twende mama nikusindikize” Mainaya akazungumza na kupokea begi moja kutoka kwa Bi.Fatma.
Pamoja na kwamba Mainaya hakuwa amefahamu sababu ya ugomvi ule lakini kutokana na mazungumzo aliyokuwa ameyasikia kutoka katika mazungumzo ya Baba na kaka Imran yalitosha kumuaminisha kuwa kulikuwa na jambo halijakaa sawa.
Baba na kaka Imran wakabaki wakitazamana pale sitting room, walikuwa kama vile wamenaswa na shoti ya umeme.
“Baba mbona unamuacha mama aondoke!” alizungumza kaka Imran kwa mshangao mkubwa. Hakutegemea kama Baba angeweza kuruhusu safari ile kirahisi namna ile.
“Unafikiri nifanye nini sasa” alizunumza Baba kwa sauti ya kukata tamaa.
“Hapana Baba, akifika kule kijijini atazungumza kila kitu halafu aibu itakuwa kwetu” alizungumza kaka Imran huku akivuta hatua kumfuata mama nje, Baba naye akamfuata kwa nyuma.
“Mama kama tumekosa naomba utusamehe lakini usindoke” alizungumza kka Imran kwa kubembeleza.
“Naomba urudi ndani we mwanamke!” Baba akazunumza kw amri.
“Humo ndani sirudi mbona hamnielewi jamani?” Mama akasisitiza huku akipakia beki ndani ya gari yake.
“Kumbe wewe mwanamke unataka kututania” alizungumza Baba na kumsogelea mama kwa kasi kisha akamkumbatia kwa kumbana mikono na kuanza kumvutia ndani.
Kaka Imran naye akasogea haraka na kumshika mama kwenye miguu, wakawa wamembeba utafikiri mgonjwa wa kichaa kwa jinsi walivyokuwa wanaminyana na mwanamke yule.
“Lete Kamba tumfunge mikono na miguu yake!” Baba alizungumza huku akibubujikwa na jasho kutokana na kuminyana na Bi.Fatma.
“Niachieni nyie mashetani wenye laana!” akazungumza mama kwa hasira huku akijaribu kujinasua kutoka mikononi mwa mafirauni wale wawili.
“We mainaya hebu kalete Kamba unatumbua macho tu hapo kama chura!” Baba alizungumza kwa ukali kumuambia Mainaya atoe msaada kwa kile ambacho walikuwa wanamfanyia Bi.Fatma.
Mainaya alivuta hatua kwa kukimbia kuelekea jikoni, nafikiri alikuwa ametii amri ya Baba ya kuhakikisha Bi.Fatma anafungwa Kamba ili asiondoke kama alivyokuwa anataka.
Bi. Fatma hakukubali kuvurugiwa mipango yake ya kuondoka ndani ya nyumba ile. Hivyo alijitahidi kukukuruka kwa namna moja ama nyingine na mara kadhaa alijaribu kumng’ata Baba kwenye mikono yake lakini haikusaidia kwani mzee Sekiza alionekana kuwa na ujanja wa kumzidi.
“M a m a N a k u f a a a !” ilikuwa ni sauti ya maumivu makali iliyotoka kwenye kinywa cha kaka Imran na kumuachia mama pasipo kupenda.
Kumbe Mainaya alipokwenda jikoni, alichukua kibao cha mbuzi na kuja kumtwanga nacho kaka Imran mgongoni upande wa bega la kushoto. Kaka Imran akapeleka mikono yake mgongoni kujishika kwenye ile sehemu aliyokuwa ametwangwa na kibao cha mbuzi.
Mainaya baada ya kumtandika kaka Imran na kuhakikisha hakuwa amemshikilia tena mama, akaona sasa ulikuwa ni wasaa wa kumtwanga Baba ambaye alikuwa bado amemshikilia mama kwenye mikono.
Thubutuuu! Usisikie kitu kupoteza maisha ndugu msomaji, nakwambia baba alimuachia mama na kuanza kutimua mbio. Mainaya akamuunganishia kwa nyuma huku ameshikilia vyema kibao cha mbuzi tayari kwa kushusha kipigo kwa kaka wa dada yake.
Baada ya Mainaya kuhisi Baba anamzidi mbio alirusha kile kibao cha mbuzi kwa nguvu sana kumlenga. Lakini kwa bahati mbaya au nzuri siku za kuishi za baba zilikuwepo bado, hivyo aliinama na kibao kile kikakita ukutani na kuganda. Yani kama kingetua kwenye shingo ya baba nafikiri yangekuwa mengine saa hizi.
Mainaya alikuwa kama vile mbogo aliyekuwa amejeruhiwa kutokana na hasira amabazo alikuwa nazo. Alichomoa kibao kile kutoka ukutani na kurejea mbio kwa lengo la kuendelea na mashambulizi kwa kaka Imran.
Kaka Imran alipoona kiama kikimfuata kwa spidi akajiinua na kuchomoka kama mshale kutoka pale alipokuwa ameinama akiugulia maumivu ya kibao cha mbuzi. Alikimbia huku mkono wake wa kuume ukiwa umekamata kwenye yale maeneo ambayo alisulubiwa kwa kibao cha mbuzi.
“She&^zi! Kama kweli ni vidume mbona mnakimbia?” alizungumza mama kwa hasira huku akijiinua na kusimama kutoka pale chini alipokuwa amegandamizwa na wale mafirauni.
“Wamekuumiza shangazi?” alihoji Mainaya kwa sauti ya hofu huku akitupa kibao ha mbuzi pembeni na kumsogelea mama.
“Si nimekwambia hawa sio viumbe wa ulimwengu huu!“ akazungumza mama kwa hasira.
“Basi shangazi achana nao” Akazungumza Mainaya kwa sauti ya upendo iliyokuwa imejaa huruma.
“Yani sijui familia yangu imepatwa na nini jamani!” mama alizungumza kwa masikitiko makubwa huku akibubujikwa machozi.
“Kwa moyo mmoja shangazi ninakuunga mkono na kuibariki safari yako ya Tanga” alizungumza Mainaya kwa msisitizo.
Mama alimtazama Mainaya na kuachia tabasamu la kujilazimisha kisha akavuta hatua kuelekea kwenye gari na kutoa begi lake.
“Vipi mbona unashusha mizigo shangazi, umeahirisha kuondoka?” Mainaya alihoji kwa mshangao baada ya kumuona mama akitoa mizigo yake kutoka kwenye gari.
“Tuchukue boda hadi Ubungo wachana na mikweche yao hiyo” alizungumza mama huku akinyanyua mizigo na kuvuta hatua kutoka nje ya geti.
Hakika mama alikuwa amedhamiria kuondoka na kuwaacha wanaume wale waliolaaniwa kwa vitendo vyao pale jijini Dar es salaam.
*****
Baada ya mikikimiki ya hapa na pale katika jiji lile hatimaye nilifanikiwa kupanda basi na safari ya kuelekea kijijini kwetu Tanganyika ikachukua nafasi yake. Kwa kiasi fulani nilihisi amani ndani ya nafsi yangu huku nikiapa kutorejea tena katika jiji lile lililokuwa limepambwa kwa miba za sumu. Hakika ukiona mtu anaendelea kuishi na kufanya shughuli zake vizuri ndani ya jiji lile basi kweli ni kidume ama ni mwanamke wa haja. Ndugu msomaji usione yale maghorofa marefu yaliyosimama kwa nyodo na ile migari inayopishana kwa mbwembwe ndani yake kuna moto wa jehanamu unafukuta.
Nikiwa ndani ya basi niliketi siti moja na kijana mmoja aliyekuwa akionekana mtanashati na mwenye kujipenda sana kutokana na mavazi aliyokuwa ameyavaa. Pamoja na kwamba tulikaa muda mrefu pasipo kusemezana lakini nilimuona wazi alikuwa akinitupia jicho la wizi. Alikuwa hatulii utafikiri pale kwenye kiti alikuwa amekalia miba ya mchongoma.
“Kumbe mwenzangu unashukia wapi?” kijana yule kavunja ukimya.
Niligeuza shingo yangu na kumtazama kwa sekunde moja na kugeukia dirishani huku nikijivuta kuketi vizuri kwenye kiti changu.
“Tanganyika” nikajibu kwa kujilazimisha.
“Woow! Mimi nateremkia Mkanyageni, wewe ni mwenyeji wa Tanganyika?” kijana yule akaendelea kuzungumza huku akiachia tabasamu la kujishebedua.
Niliitika kwa kichwa kukubali kuwa nilikuwa ni mwenyeji wa Tanganyika kama alivyokuwa anataka kufahamu.
“Basi nitakuwa nakutembelea kama hutojali” kale kakijana nikaona kanajitahidi kutengeneza mazoea na mimi, sikujibu chochote nikabaki kimya kama vile sikuwa nimemsikia.
“Mimi naitwa Sheby, sijui mwenzangu unaitwa nani?” alijitambulisha kwa sauti ndogo nafikiri hakutaka abiria wengine wasikie mazungumzo yetu.
“Hata sina jina” nikajibu kwa ufupi kwasababu sikuona ulazima wa kujitambulisha kwa kijana yule ambaye asingeweza kuwa na umuhimu wowote ule kwangu zaidi ya usumbufu tu.
“Mnh” kijana yule akaguna.
“Unaguna nini sasa?”
“Nashangaa unaposema huna jina, wakati hata misukule inamajina” Kaka yule alizungumza maneno ambayo yalinifanya niangue kicheko.
“Usinichekeshe bwana, sio vizuri. Unaona mwenzio nimecheka kwa sauti” nikazungumza huku nikijifuta mahozi.
“Haya nambie basi waitwaje weye?”
“Mimi naitwa Ndwadwa” nikajibu kwa ufupi huku nikitabasamu.
“Nani…?”
“Jinalangu ninaitwa Ndwadwa” nikazungumza kwa msisitizo huku nikijitahidi kujizuia kucheka mana niliropoka tu wala sikujua lilitokea wapi lile jina.
“Ndwandwa..”
“Sio Ndwandwa, sema Ndwadwa” nikamsahihisha baada ya kuona anakosea kutamka lile jina nililokuwa nimelitaja.
“Duh!”
“Vipi mbona unaguna, hujawahi kulisikia jina kama langu?”
“Ni jina zuri sana kama ulivyo wewe mwenyewe” alizungumza kijana yule kujifanya kunisifia.
Pumbavu kabisa, heti jina zuri kama nilivyo mimi mwenyewe! Mwanaume hana haya yule! Yani kweli kabisa amenifananisha na jina kama Ndwadwa? Jina limejaa mafundo na kona kona kibao, Duh!
“Asante..” nikaitika na kujifanya kuachia tabasamu la kinafki.
“Nimefurahi sana kufahamiana na wewe, tunaweza kusaidiana mambo mengi sana” kijana yule alizungumza.
“Kama yapi?”
“Ya maisha tu, unajua kukutana ndio mwanzo wa kufahamiana na kuanzisha udugu” alisema kijana yule.
“Umesema waitwaje vile?” nikahoji huku nikimtazama usoni kwa kuibia,
“Sheby..”
“Shabani au nimekosea?”
“Sio Shabani, bali ni Shebughe” Toba, kumbe ndiomaana ameona jina langu ni zuri kwasababu jina lake mwenyewe lilikuwa bovuuu! Bayaaaa! Chachuuu!
“Jina zuri kama wewe mwenyewe!” na mimi nikalipiza kumfananisha na jina lake Shenzi kabisa!
“Duh kumbe una masihara hivyo mrembo?” alizungumza huku anacheka. Mwenyewe bichwa lilimviiimba kuambiwa mzuri, angejua nilikuwa namaanisha kuwa jina lake lilikuwa ni baya wala asingechekelea vile.
“Umeolewa?” kijana yule aliendelea na maswali yake kama vile tulikuwa polisi.
“Na nani?” na mimi nikajichetua.
“Jamani si mume wako au bado haujaolewa?”
“Sina mpango wa kuolewa mimi” nikazungumza kwa msisitizo mana niliona dalili za kutaka kuniletea yaleyale ya kule jijini Dar.
“Lakini mpenzi unae au sio?” maswali yalizidi kutiririka utafikiri yanasukumwa na upepo wa kisurisuri.
“Mpenzi ndio ugonjwa gani?” nikahoji huku nikijitahidi kuficha hali ya kukerwa na ile mada yake.
“Kwahiyo unataka kuniambia haupo kwenye mahusiano na mwanaume yeyote?” kijana yule alihoji huku akijichekesha chekesha kama mwehu.
“Eeh Baba! Kwanini tusibadilishe mada?” nilijikuta nikishindwa kujizuia na kuzungumza kwa hasira huku nimekunja sura.
“Basi mtoto mzuri na yaishe, sikujua kama nitakuudhi” kijana wa watu nikmuona akiishiwa pozi na kujikohoza kama mgonjwa wa TB kisha akameza funda la mate.
Zilipita kama dakika tano hivi pasipo kuzunguma neno lolote lile kati yetu. Nafikiri alikuwa akijaribu kunitafakari nilikuwa ni mwanamke wa aina gani.
“Samahani Ndwadwa” akavunja ukimywa na kuniita kwa lile jina bovu ambalo nilizidi kulichukia.
Nikageuza shingo na kumtazama kwa lengo la kumpa ishara ya kumsikiliza kile alichokuwa anataka kukizungumza.
“Ninaweza kupata namba yako ya simu?” alizungumza kijana Sheby kwa sauti ya kubembeleza.
“Sijawahi kumiliki simu tangu nimezaliwa” nilizungumza kwa kujiamini huku nikitabasamu.
“Inawezekanaje mwanamke mrembo kama wewe ukose simu?”
“Sikuwa nimeamua kuwa na simu kwasbabu haikuwa na umuhimu wowoteule kwangu” nikaeleza.
“Basi nikupe namba yangu” sheby alizungumza kwa kusihi.
“Ya nini sasa kwangu?”
“Siku ukinikumbuka utanisalimia” Sheby alieleza na kunifanya niangue kicheko cha kebehi.
“Nitakukumbukaje sasa, wakati hata hatujuani?”
“Jamani Ndwadwa mbona tumejuana tayari”
“Sema tumefahamiana lakini hatujajuana”
“Mnh basi haya, hivyo hivyo” alizungumza kijana yule huku akitoa kipande cha karatasi kutoka kwenye mfuko wa shati na kuandika namba za simu.
Nilitupa macho pale kwenye karatasi aliyokuwa anaiandika kisha nikajikausha kama vile sikuwa nimeona kitu.
“Haya mama Ndwadwa chukua hii, shiku ukijisikia utanisalimia” alizungumza Shebughe huku akinikabidhi kile kikaratasi kilichokuwa na namba za simu.
“Mnh! Yani we kaka king’ang’anizi” nikazungumza huku nikipokea kikaratasi kile na kukitumbukiza kwenye kipochi changu kidogo nilichokuwa nacho.
Nilimuona kijana Shebughe akiachia tabasamu la matumaini kutokana na kupokea namba zake za simu. Akajikohoza na kuzungumza.
“Nina shida na msichana wa kazi, kama huko kwenu Tanganyika naweza kupata naomba unisaidie tafadhali” Kijana yule alizungumza kwa sauti ya upole lakini iliyokuwa imejaa msisitizo.
“Unashida na msichana wa kazi au msichana wa kuchezea?” nikahoji kwa msisitizo kwani alinikumbusha ile mikikimiki ya kule nyumbani kwa mzee Sekiza. Niliwachukia sana mabosi hasa wa kiume kutokana na tabia zao za kunyanyasa wasichana wa kazi.
“Unamaanisha nini?” alihoji kijana yule baada ya kutamkiwa maneno yale machachu kutoka kinywai mwangu.
“Hata mwenyewe sielewi ninachokimaanisha” nikajibu kwa ufupi huku nikitupa macho dirishani na kuangaza vizuri mazingira ya nje.
*****
Ilipita kama robo saa hivi ndipo Baba na kaka Imran wakaonekana wakivuta hatua kurejea nyumbani baada ya kufurumushwa na kibao cha mbuzi na Binamu Mainaya. Walikuwa wakitembea huku wakichungulia utafikiri wanavizia fumanizi la uswahilini.
“Baba..!” kaka Imran akamgutusha Baba ambaye alikuwa akichungulia getini.
Baba aLishituka kidogo na kuhisi ahuweni baada ya kumuona kaka Imran akiwa kwenye kona yake naye akichungulia.
“Vipi wameondoka kweli?” alihoji baba kwa sauti ya kunong’ona.
“Sina uhakika sana, lakini inawezekana wameondoka” akajibu kaka Imran kwa mashaka huku akiangaza kulia na kushoto kwa wasiwasi.
“Dah huyu mwanamke ni balaa!” alizungumza Baba na kumeza funda la mate huku akisogelea mlango wa kuingilia ndani.
“Lakini Baba umeshindwaje kumdhibiti Mama hadi ameondoka?” kaka Imran alizungumza kwa kulaumu.
“Kwanini usimzuie wewe?” Baba naye akahoji.
“We baba unasema tu, utafikiri ule mziki wa Mainaya ni wa kitoto?” alizungumza kaka Imran kwa sauti ya msisitizo huku akipeleka kiganja cha mkono wake wa kuume na kujishika mgongoni alipokuwa ametwangwa na kibao cha mbuzi.
“Sasa kama wewe mziki umekushinda kucheza ulitaka nani aucheze?” Baba naye akazungumza huku akisukuma mlango na kuingia ndani. Bado alikuwa amejawa na wasiwasi kwasababu hakuwa na uhakika kama mama na mainaya walikuwa wameondoka au laa. Alipohakikisha hapakuwepo na mtu akaingia na kuketi kwenye kochi sebleni huku kaka Imran akimfuata nyuma.
“Mimi nilikimbia lakini nilikuacha wewe umemshika mama!” alizungumza kaka Imran huku akijiweka kwenye kochi.
“Unafikiri kile kibao cha mbuzi kingeniacha salama, almanusura kinitoe roho!” alizungumza baba kwa msisitizo huku ametoa macho na kumeza funda kubwa la mate.
“Vimtu vingine vimezaliwa ili kuvuruga mipango ya watu tu” alizungumza kaka Imran na kuegemea kochi huku mikono yake ameikutanisha kichwani.
“Kale ka Mainaya nafikiri sikuhizi kanavuta bangi” mama alisema.
“Tena usikute kanachanganya bangi na pilipili kichaa” kaka Imran akaongezea maneno ya baba.
“Hebu tuwache porojo na tuumize vichwa juu ya nini cha kufanya” alisema Baba kwa sauti ya msisitizo.
“Yani kila kukicha ni matatizo hata sielewi baba” alizungumza kaka Imran kwa sauti iliyokuwa imejaa majuto.
“Matatizo umeyatengeneza mwenyewe, huu sio muda wa kujilaumu tena” baba alizungumza kwa sauti yake ya upole lakini iliyokuwa imejaa msisitizo.
“Lakini baba kama ingekuwa sio wewe haya yote yasingetokea” alizungumza kaka Imran kwa ile sauti yake ya lawama.
“Kosa langu mimi ni lipi sasa? Au unamaanisha kosa letu!”
“Sasa wewe ni mtu mzima umeanzaje kuingia kwenye mapenzi na vitoto vidogo?” kaka Imran alilaumu.
“Wewe mtoto hebu wacha ushenzi wako hapa! Unafikiri wewe ndio unalingana naye?” baba akajikuta akizungumza kwa hasira baada ya kusikia kauli za kaka Imran.
“Silingani naye miaka, lakini rika tunalingana”
“Kwahiyo unataka kusemaje Imran?”
“Umechemsa mzee!” kaka Imran alizungumza kwa hasira.
“Sio mchemsho tu, bali mtokoto!” sauti ya Fadhili iliwagutusha baba na kaka Imran pale sebleni.
Baba na kaka Imran waligeuza shingo zao na kumtazama Fadhili ambaye alikuwa anavuta hatua kuelekea kwenye jokofu.
“Kitimoto ameingia msikitini ibada ishavurugika” kaka Imran akazungumza na kujiweka vizuri kwenye kochi.
Baba alibaki kimya akimkodolea macho Fadhili pale kwenye jokofu ambako alionekana akichukua jagi la maji ya kunywa na mkono mwingine akiwa amekamatia birauli.
“Kwahiyo mmefikia wapi sasa?” alizungumza Fadhili huku akimimina maji kwenye birauli na kuliweka jagi mezani.
“Tumefikia wapi kwa safari ya kutokea wapi?” kaka Imran akahoji kwa jazba baada ya kubaini Fadhili alikuwa akiwakejeli.
“Nimepata taarifa kuwa Bi. Mkubwa ameenda Tanga” Fadhili alizungumza huku akisogea kwenye kochi na kujiweka taratiibu.
“Kwani kwenda Tanga kuna dhambi gani?” alihoji kaka Imran kwa jazba.
“Inategemea na namna alivyokwenda” Fadhili alizungumza huku akionekana kwenye kinywa chake amejawa na tabasamu na kupeleka glasi ya maji kinywani.
“Wacha majungu mtoto wa kiume, utaolewa wewe!” kaka Imran akazungumza kwa hasira.
Maneno yale ya kaka Imran ya kuolewa yalimuingia vyema Fadhili na kumfanya apaliwe na maji aliyokuwa akiyanywa, Masikini ya Mungu mtoto wa watu alijikuta akikohoa mfurulizo.
“Kufa tu papasi wewe hauna faida yoyote katika familia yetu” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.
“Kama mimi ni papasi, nitakuwa nimezaliwa na papasi. Mtoto wa papasi ni papasi, hivyo na wewe ni papasi kwasababu baba yako ni papasi” Fadhili alizungumza kwa taabu huku akikohoa.
Maneno yale ya Fadhili yalimchoma kaka Imran na kumuongezea hasira. Akasimama na kwenda kuchukua birauli ya maji na kummwagia Fadhili usoni.
“Nitakuua wewe! Leo mama yako hayupo, hakuna wa kukutetea” kaka Imran akazungumza kwa hasira.
Fadhili akasimama ghafla kwakuwa hakuwa ametegemea tukio lile alilokuwa amefanyiwa na kaka Imran.
“Sikuogopi Broo, nakuheshimu tu pamoja na kwamba mwenyewe haujiheshimu” Fadhili alizungumza kwa sauti ya upole lakini iliyokuwa imepambwa kwa tabasabu la dharau na kejeli.
“Hebu wacheni huo upuuzi, au hamjaniona hapa?” Baba akazungumza kwa kukoroma baada ya kuwaona watoto wake wakigombana mbele yake basipokuwa na hata chembe ya hofu.
Fadhili akavuta hatua kuondoka sebleni pale huku akikung’uta shati lake lililokuwa limelowana kutokana na Yale maji aliyokuwa amemwagiwa. Alipofika karibu na kona ya kutoka pale sebleni akageuta na kuwatazama baba na kaka Imran.
“Kwa ufupi ni kwamba, mama amekwenda Tanga na Mwantumu nimemsindikiza naye amekwenda Tanga. Sasa wakikutana huko sijui kutatokea nini?” Fadhili akazungumza na kuondoka akiwaacha Baba na Kaka Imran wakikodoleana macho kwa mshangao.
“Mwantumu yuko wapi?” alihoji baba kwa msisitizo.
“Mwantumu alikuwa ameshikiliwa na Polisi” kaka Imran alizungumza kwa wasiwasi.
“Sasa fanya haraka ukamtoe, vinginevyo mambo yatazidi kuharibika” baba akazungumza kwa msisitizo.
“Tumechelewa baba, mwenyewe si umesikia maneno ya huyu Ngadu!” alizungumza kaka Imran kwa sauti ya kukata tamaa.
“Hayo ni maneno tu Imran, Mwantumu ana kesi ya kujibu katika ile ishu ya Bupe” Baba akazungumza kwa kujiamini.
“Yote yanawezekana baba, huyu Ngadu wenu anazijua vyema fitina!” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.
Baba alianza kuelewa maneno ya kaka Imran, kwa mbali alianza kuamini kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa sana wa Fadhili kunitoa kule sero. Alivuta pumzi ndefu na kuziachia kisha akakuna kichwa kama vile kulikuwa na kitu anakitafakari. Baada ya sekunde kadhaa aliinua kichwa na kumtazama kaka Imran ambaye naye hakuwa katika hali ya Amani.
“Imran mwanangu..” Baba aliita
Kaka Imran aliinua macho kumtazama Baba pasipo kutoa sauti yoyote kuitikia wito ule.
“Hili jambo sio dogo kama tunavyolichukulia” Baba alizungumza.
“Afadhali mimi ni mtoto, kwa upande wako ndio baya zaidi. Zee zima na kitoto kadogo wapi na wapi!” kaka Imran alizungumza huku akigeuza shingo kutazama pembeni.
“Naona heshima imeshuka humu ndani, nisipokuwa makini tatizo hili litanigeuza kuwa midoli ya kuuzia nguo” alizungumza baba kwa msisitizo.
“Kwahiyo tufanye nini juu ya hili, mana likivuja hakika biashara zetu zote zinakufa” alizungumza kaka Imran kwa sauti ya heshima baada ya kubaini baba alikuwa amekasirika kutokana na kauli zake.
“Lazima tufanye kitu…” alisema baba
“Tena sasahivi” kaka Imran akakazia.
ENDELEA...
“Unafikiri tufanye nini?”
“Lazima mmoja wetu aende Tanga sasahivi” kaka Imran alizungumza kwa msisitizo.
“Tanga kufanya nini sasa?” alihoji Baba kwa umakini mkubwa.
“Kuwaziba mdomo wale wanawake” kaka Imran alizungumza kwa kujiani.
“Lakini tuna uhakika gani kama kweli Mwantumu ametoka mahabusu?” baba alihoji.
Maneno ya baba yalionekana kumuwazisha kidogo kaka Imran kwani alimeza funda la mate kisha akatoa pumzi kwa nguvu.
“Sasa Mzee inabidi wewe ufuatilie ukweli wa Mwantumu, halafu mimi nikimbie Tanga” kaka Imran alitoa wazo.
“Sawa wazo zuri…”
“Sasa usije ukamtoa mahabusu halafu ukafanya tena mambo yako!” kaka Imran alizungumza kwa msisitizo.
“Mambo gani sasa?”
“Shauri yako!....Mimi nitajitahidi kufika Tanga kabla ya Mama na Mwantumu” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.
“Utawezaje sasa wakati wameshatangulia” baba akahoji.
“Nitakwenda na gari yangu, nafikiri haitakuwa kikwazo” kaka Imran alizungumza kwa kujiamini.
“Kama ndivyo hivyo, basi tumia gari yangu” alizungumza baba kwa msisitizo.
“Yeah ni wazo zuri mzee Baba, ile ni ndege hata mimi naiaminia” kaka Imran alizungumza kwa matumaini.
“Lakini uwe makini na sheria za barabarani usije ukasababisha matatizo mengine” alizungumza baba kwa tahadhari.
“Hofu ondoa mzee wangu, mpira upo uwanjani ngoja nikuoneshe unavyochezwa. Kazi yako wewe ni kushangilia tu” alizungumza kaka Imran kwa kujiamini.
“Inuka basi uondoke, maneno mengi ya nini?” alizungumza baba kwa msisitizo.
“Usiwe na haraka mzee wangu kila kitu kitakaa sawa nimekwambia” alizungumza kaka Imran na kuinuka akaelekea chumbani kwake kwaajili ya maandalizi ya safari ya dharura iliyojitokeza. Yeye na baba hawakuwa tayari kuona kashfa ile ya uzinzi inaenea kwa namna yoyote ile na kuathiri biashara zao.
*****
Kule safarini ndani ya basi nilikuwa nimekwishafika katika kijiji cha Mkumbi kilichokuwepo jirani na kijiji chetu cha Tanganyika. Nilisimama tayari kwa maandalizi ya kushuka.
“Vipi unakwenda wapi sasa?” kijana Shebughe alihoji baada ya kuniona nimesimama.
“Nakutakia safari njema. Mimi nimeshafika” nilizungumza huku nikitoa begi langu kutoka kwenye keria ndogo mle ndani ya basi.
“Dah umeniacha mpweke mrembo. Mwenyewe nilishakuzoea” Shebughe alizungumza huku akitabasamu.
“Nakutakia mafanikio katika shughuli yako ya kusaka Housegirl” nikazungumza huku nikivuta hatua kuelekea kwenye mlango baada ya basi kusimama.
Kijana yule alinikodolea macho jinsi nilivyokuwa nikivuta hatua katikati ya viti vya basi hadi nilipoteremka.
Macho yangu hayakuweza kuamani kama nilikuwa nimeingia tena katika kijiji chetu cha Tanganyika kilichokuwa kimejaa amani na matumaini ya maisha. Hali ya matumaini ikaongezeka ndani ya moyo wangu. Hakika nyumbani ni kutamu jamani. Yale mauza uza ya kule Dar es salaam ndio basi tena sitakutana nayo tena.
Nilipokuwa nimesimama na begi langu likiwa chini kwa mbele huku vijana waliokuwa wanafanya biashara ya bodaboda wakinizunguuka na kutaka kujipatia kipato kwa kunibeba. Nikahisi kuguswa kwenye bega langu la mkono wa kushoto.
Ndugu msomaji huwezi kuamini lakini ukweli ni kwamba mtu aliyekuwa amenishika kwenye bega langu alikuwa ni mama Bi.Fatma. Nikahisi mapigo ya moyo wangu yakiongezeka spidi mara nane Zaidi. Nilitamani kutimua mbio kwani nilihisi mwanamke yule alikuwa amekuja Tanganyika kwa lengo la kulipiza kisasi cha kunifumania na mume wake.
“Vipi mbona umeshituka hivyo” mama alihoji kwa sauti ya upendo.
“Shikamoo mama” nikasalimia haraka huku nikihisi mwili wangu ukitetemeka kwa hofu na mashaka.
“Marahaba mwanangu, pole kwa matatizo” alijibu mama.
Mnh! Heti matatizo, hivi inawezekanaje mtu awe adui yako halafu aoneshe huruma kwa matatizo yanayokufika? Nikaona wazi kuwa mwanamke yule alikuwa ananikejeli. Sikujibu neno lolote lile nikabaki kimya huku nikitazama chini kwa aibu. Ogopa sana mtu umemkosea halafu anakufuata na kukuomba msamaha.
“Nisamehe sana mwanangu, niwie radhi kwa mambo yote yaliyokukuta” alizungumza mama kwa sauti ya huruma na kuzidi kunichanganya akili yangu. Kwa maana mimi ndio nimechukua mume wake, imekuwaje tena yeye ndio aniombe mimi msamaha! Nikaamini lile Balaa nililokuwa nimehisi nimelikimbia kule Bongo Daslam lilikuwa limenivizia kwa mbele Tanga kwetu.
“Lakini mama…” nilitaka kuzungumza jambo ambalo hata mwenyewe sikuelewa ningezungumza nini. Hata hivyo kabla ya kuzungumza hilo jambo Bi. Fatma alinikatisha.
“Hakuna cha lakini Mwantumu wangu, wewe bado ni mwanangu na utaendelea kuwa mwanangu milele daima” alizungumza mama yule kwa msisitizo.
Nakwambia mtoto wa kike nikabaki nimeduwaa na macho nimeyakodoa utafikiri roho ilikuwa inaacha mwili kwa kunyongwa shingo.
“Beba begi lako twende nyumbani, hata mimi nimeshuka sasahivi” mama alizungumza huku akiinua lile begi lake kubwa na lingine akilikokota.
“Inamaana tumepanda basi moja?” nikahoji kwa mshangao.
“Hata mimi nimeshangaa, sikutegemea kama Mungu angetenda muujiza kama huu” mama alizungumza.
Tulianza kuvuata hatua kuelekea nyumbani pasipo kuzungumza neno lolote lile. Nilijilaumu sana kwa kufika pamoja na mwanamke yule kijijini pale. Nikafikiri mara kwa mara jambo la kufanya ili aibu ile isije ikafika pale kijijini kwetu. Sikutaka kabisa wazazi wangu wafahamu kuwa niliondoka kule Dar es salaam kwa kufumaniwa, tena fumanizi la kidigitali.
“Mama..” nilivunja ukimya.
“Unasemaje mtoto wangu?” mama aliitika kwa sauti ya upendo.
“Naomba unisamehe sana kwa kilichotokea” ikabidi nijiongeze mtoto wa kike, haiwezekani mtu akukosee halafu yeye ndio akuombe msamaha.
“Hapana mwanangu, najua halikuwa kosa lako” mama alizungumza maneno ambayo yalinifanya nihisi ahuweni ndani ya moyo wangu.
“Naomba wazazi wangu wasilijue hili jambo” nikazungumza kwa sauti ya kusihi sana.
“Kwanini unataka wasifahamu?”
“Wataniua” nilizungumza kwa sauti ya masikitiko huku nikijikuta machozi yakinitoka jicho langu la kushoto.
Bi. Fatma aliponiona nalia alijikuta akiumia sana ndani ya nafsi yake. Alielewa wazi kuwa kosa lile halikuwa langu bali lilikuwa ni kosa la baba pamoja na kaka Imran ambao ndio walikuwa wameingia chumbani kwangu bila ya makubaliano yoyote yale na mimi.
“Usijali mwanagu, siwezi kukutia katika aibu hii. Nitahakikisha inabaki kuwa siri yetu mimi na wewe tu” mama alizungumza kwa msisitizo huku akionekana kuumia ndani ya moyo wake.
*****
Kaka Imran aliweza kukanyaga mafuta na kuendesha gari utafikiri alikuwa amevuta sigara kubwa. Sidhani kama kuna sheria hata moja ya barabarani ilikuwa imezingatiwa. Kwa maana Ndani ya masaa manne tu alikuwa amefanikiwa kufika Kijijini Tanganyika kama alivyokuwa amepanga na mzee Sekiza na kufunga breki nje ya nyumba ya Mama Kibo.
Mama Kibo ambaye alikuwa jikoni akiandaa chakula cha jioni alitoka nje haraka kuweza kumlaki mgeni wake ambaye alifika pasipo kutoa taarifa yoyote ile.
“Jamani Mjomba huyoo!” Mama Kibo alizungumza kwa hamasa baada ya kumuona kaka Imran akiteremka kutoka kwenye gari.
“Woow Mama huyoo!” kaka Imrana naye aliitika kwa sauti ya furaha na kuvuta hatua kueleke alipo mama Kibo na kumkumbatia.
“Hee! We mtoto mbona hujatoa taarifa kama unakuja?” mama Kibo alihoji huku akimtazama mgeni wake kwa furaha kubwa.
“Yani mama mkubwa nimekuja maramoja lakini nina haraka mno”
“Haraka ya kwenda wapi tena na wewe?”
“Yani leo hii natakiwa kurudi Dar”
“Mnh haya karibu ndani basi” Mama Kibo alimkaribisha kaka Imran na kuvuta hatua kuelekea ndani.
Kaka Imran aliketi kwenye kiti na mama Kibo akaelekea jikoni ambako baada ya dakika chache alirejea tena huku ameshikilia sahani iliyokuwa na mahindi ya kuchemsha.
“Haya baba karibu Mahede ugugute kidogo na wewe” alisema bibi huku akimkabidhi sahani ya mahindi kaka Imran.
“Duuh upo vizuri ma’mkubwa! Yani hata sijapumua ushanizawadia maguguta” alizungumza kaka Imrana huku akipokea sahani ile ya mahindi ya kuchemsha.
“Nakufahamu vizuri mtoto wangu, haukawii kusema una haraka na hutaki kula” alizungumza mama Kibo huku akiketi kwenye kiti kingine jirani na alipokuwa kaka Imran.
“Hata hivyo njaa ilikuwa inaniuma sana” alijibu kaka Imran huku akipeleka kipande cha hindi mdomoni.
“Haya hebu niambie kilichokuleta haraka kiasi hicho ni kipi?” Mama Kibo alihoji kwa hamasa kubwa.
“Ma’mkubwa nimekuja bwana mimi nataka kuoa!” kaka Imran alizungumza.
“Waaaooo! Rurururuuu ache baba….ache mama…ache mwana” mama Kibo alizungumza kwa furaha huku akipiga vigeregere kushangiria.
Kaka Imran aliendelea kutafuna mahindi ya kuchemsha huku akimuangalia mama yake mkubwa jinsi alivyofurahishwa na taarifa ile ya yeye kutaka kuoa.
“Haya huyo mchumba mwenyewe ni wa kabila gani mwanangu?” Mama Kibo alihoji kwa msisitizo.
“Sasa hilo mama Mkubwa ndilo lililotuleta”
“Kwani umekuja na nani?” alizungumza mama Kibo huku akichungulia nje.
“Tumekuja timu nzima, tena mimi nilifikiri imeshafika”kaka Imran alizungumza kwa kujiamini.
“Timu ya nani?” mama Kibo akahoji.
“Anakuja mama na wengine”
“Inamaana kuna ugeni mkubwa hivyo halafu hatuambiani jamani?” mama Kibo alizungumza kwa kulaumu huku akionekana kuwa na hamasa kubwa ya kupokea ugeni huo.
“Tungekuambia ungeteseka sana kufanya maandalizi ya ugeni”
“Haya hebu endelea kunieleza, huyo mchumba anatokea wapi?”
“Hapa hapa Tanganyika ma’mkubwa”
“Mnh,ni mtoto wa nani huyo?” mama Kibo alizungumza huku akijiweka vizuri kwenye kiti.
“M W A N T U M U ! “ kaka Imran alijikakamua na kutaja jina langu Mungu wangu! Mwanaume mbaya yule! Sijui kama nitakuja kumsahau katika maisha yangu.
“He inamaana kufanya kazi nyumbani mwenu ndio umempenda?” mama Kibo alihoji huku akionekana kuvutiwa na taarifa ile.
“Kwani vipi mama anafaa lakini?” alihoji kaka Imran kwa msisitizo.
“Mwanangu, Mwantumu umepata mwanamke. Kale katoto kamebarikiwa kila aina ya tabia njema” mama Kibo alizungumza huku akinimiminia masifa kibao mbele ya kaka Imran.
“Ndio hivyo mama mkubwa, nafikiri muda sio mrefu mama ataingia na natamani mipango iende haraka haraka ili nipate jiko langu” alizungumza kaka Imran kwa kujiamini.
“Basi sawa mwanangu hakuna tatizo lolote. Ngoja mimi niendelee na maandalizi ya chakula huku jikoni” alizungumza mama Kibo na kuinuka kuelekea jikoni kundelea na shughuli zake huku kaka Imran akiwa amebaki kwenye kiti akiendelea kutafuna mahindi.
*****
Mimi na Bi Fatma tulipokuwa tukiendelea na safari yetu huku tukipiga stori kila mmoja alijikuta akipatwa na mshangao baada ya kukaribia nyumbani kwa mama Kibo. Tuliweza kuiona gari ya baba ikiwa imesimama nje ya nyumba ya mama Kibo.
“Mwantumu mwanangu, hivi ninachokiona mbele ya macho yangu kipo sahihi au nina tatizo la macho?” alihoji Bi.Fatma huku akifinya macho yake kuweza kuona vizuri.
“Ile gari ni kama ya Baba” nikazungumza kwa kuhamaki.
“Mungu wangu! Inawezekanaje afike huku wakati nimemuwacha nyumbani” mama alizungumza kwa mshangao.
“Au sio lenyewe labda yanafanana tu” nikazungumza kwa kujipa matumaini mwenyewe.
“Huyu mwanaume ni shetani sana! Sasa ngoja nimkute atanitambua leo sitojali kitu chochote kile” mama alizungumza kwa jazba huku akiongeza mwendo.
“Lakini mama, mimi naomba niende nyumbani” nilizungumza tulipokuwa tunakaribia kwenye njiapanda ya nyumbani kwetu na nyumbani kwa mama Kibo.
“Hapana Tumu, twende kwanza tukashuhudie yale maajabu pamoja” mama alizungumza huku akiendelea kuvuta hatua ndefu.
Dah yale maneno ya Bi.Fatma yalinifanya niishiwe nguvu kabisa. Yani alikuwa anataka niende kule ambako nilikuwa nashuhudia kwa macho yangu kuwa shetani ibilisi alikuwa ameweka ngome yake tayari kwa mashambulizi!
“Au nipeleke kwanza hii mizigi yangu nyumbani halafu nitakuja” nikajaribu kujitetea.
“Hapana Tumu, mchuzi wa mbwa hunywewa ukiwa wamoto. Twende kwanza tukajue mbivu na mbichi” mama alikazia uamuzi wake.
“Lakini mama mbona kama vile mambo yatakuwa magumu zaidi kwangu?” nilizungumza kwa mashaka huku nikiamini kuwa kama kweli baba ndiye aliyekuwa amepaki gari pale nyumbani kwa mama Kibo basi ni lazima moto wa jehanamu ungewaka.
Mama aliweka mizigo yake chini na kunigeukia huku akinitazama kwa macho yaliyojaa msisitizo na umakini mkubwa.
“Tumu mwanangu naomba uniamini, siwezi kwenda kinyume na makubaliano yetu” mama alizungumza kwa msisitizo mkubwa kisi cha kunifanya nishawishike kufanya vile alivyokuwa anataka yeye.
Tulivuta hatua kukaribia nyumbani kwa mama Kibo huku kila mmoja wetu macho yake yakiwa yamekodolea lile gari la baba pale nje ya nyumba ya mama Kibo. Mama aliweza kuthibisha kwa asilimia zote kuwa lile lilikuwa ni gari la baba hasa baada ya kusoma namba za gari.
Tulipokaribia nyumbani pale tukaanza kutembea kwa tahadhari huku macho na masikio yakiwa na hamasa kubwa ya kufahamu kilichokuwa kimemleta mwanaume yule fedhuli ndani ya kijiji chetu tulivu.
Tulipofika Bi.Fatma alivuta hatua hadi malngoni na kuchungulia ndani pasipo kubisha hodi. Macho yake yakakutana na macho ya kaka Imran aliyekuwa ametulia akitafuna mahindi ya kuchemsha kama panya buku.
“Karibuni wageni, karibuni sana!” alizungumza kaka Imran kwa sauti ya kebehi.
“We mshenzi umefikaje huku?” alihoji mama kwa hasira lakini kwa sauti ya kunong’ona ambayo isingeweza kusikika na mtu mwingine.
“Nimepaa!” kaka Imran alizungumza huku akiachia tabasamu la kebehi na kuendelea kutafuna mahindi.
“Haya kilichokuleta ni kipi?” mama aliendelea kuhoji kwa sauti ya kunong’ona.
“Woow Kumbe upo na mrembo! Karibu Tumu” kaka Imran alizungumza baada ya kuniona nimesimama nyuma ya Bi.Fatma.
“Koma wewe! Umefuata nini hapa?” mama alizungumza kwa jazba.
“Nimewafuata ninyi” alijibu kaka Imran kwa kujiamini.
“Baradhuli wewe!” alizungumza mama kwa hasira huku akitamani kumvaa kaka Imran na kumtandika Makonde lakini alihofia kuanzisha vurugu na kuharibu mipango yetu.
Tukiwa tumesimama pale mlangoni tuligutushwa na sauti za vigeregere kutokea jikoni. Alikuwa ni mama Kibo akitoka jikoni kwa furaha huku akipiga vigeregere utafikiri kulikuwa na harusi pale nyumbani.
Mama alimsogelea mama Kibo na kumkumbatia huku akijitahidi kuficha hali yake ya hasira aliyokuwa nayo.
“Jamani sikuhizi mkisafiri hamtoi taarifa?” alizungumza mama Kibo huku akimuangalia mdogo wake kwa furaha.
“Tumeona tukufanyie surprise!” alizungumza Bi.Fatma huku akiachia tabasamu la kuigiza.
“Haya karibuni ndani. Wageni wengine wameshafika” mama Kibo alitukaribisha huku akipokea mabegi na kuyaingiza ndani.
Mama alikwenda kuketi karibu kabisa na alipokuwa ameketi kaka Imran. Nafikiri alikuwa ana lengo la kuendelea kumchachafya kijana wake.
“Karibu Mwantumu mwanangu, karibu sana mkwe wangu!” jamani nyie mwanamke yule alizungumza maneno ambayo sikuwa nimeyaelewa vizuri. Heti ananiita mkwe, kwa lipi hasa au kwa nani? Kwakweli sikuwa na jibu lolote lile kwa wakati huo.
“Jamani mambo mazuri kama haya hatuambiani mapema kwanini?” mama Kibo alizungumza kwa kulaumu.
Mimi na mama tukabaki kimya tusielewe kilichokuwa kinaendelea. Mama akavuta pumzi ndefu na kuziachia.
“Yeah mimi nimeshamueleza mama Mkubwa kila kitu” kaka Imran alizungumza kwa kujiamini na kuzidi kutuchanganya mimi na Bi. Fatma.
Niliogopa sana nikahisi jamaa yule ameamua kufunguka kwa mama yake mkubwa ukweli wote wa mama kunikuta na wanaume wawili chumbani kwangu. Hata hivyo sikuweza kuelewa alimueleza kwa namna gani kwasababu miongoni mwa wanaume ambao nilikuwa nimekutwa nao alikuwa ni pamoja na yeye mwenyewe Imran.
“Ndio kijana amenieleza kila kitu, ni habari njema sana” mama Kibo alizungumza kwa furaha.
Duh! Sasa kama habari yenyewe ingekuwa ni kufumaniwa, mama Kibo angezungumza kwa furaha kiasi kile kweli? Kusema kweli nilijikuta nikizidi kuchanganyikiwa. Halkadhalka Bi. Fatma naye alikuwa kwenye kiza kinene asielewe kilichokuwa kinaendelea kati ya mama Kibo na kaka Imran.
Ghafla tulisikia harufu ya kitu kikiungua. Mama Kibo aliinuka haraka sana na kukimbilia jikoni, kumbe alikuwa amebandika mboga halafu amejisahau na mboga ikaanza kuungua.
Mama alitumia mwanya ule kuzungumza na kaka Imrana ili aweze kuelewa kilichokuwa kinaendelea ndani ya nyumba ile.
“Ni kitu gani kinaendelea hapa ndani?” alihoji mama kwa umakini.
“Sikiliza mama unajua tunakupenda sana, lakini ninafahamu wazi kuwa chanzo cha kuvurugika kwa amani ndani ya nyumba yetu ni Huyu mwantumu” alizungumza kaka Imran na kunifanyi nihisi damu zikikimbizana kwenye mishipa. Nikahisi mwili ukizizima utafikiri nilikuwa nimemwagiwa maji ya baridi.
“Shika adabu yako Imran!” Bi Fatma alitukana kwa sauti ya chini.
“Hata kama utakataa mama ukweli utabaki kuwa huo tu!” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.
“Kwahiyo unataka kusemaje?”
“Mimi nimepata wazo ambalo litaweza kuwa suluhu ya tatizo letu na tutaishi kwa amani na upendo kama zamani” kaka Imran alizungumza kwa msisitizo.
“Hatuhitaji wazo lako hapa, tunaomba uondoke na utuache!” alizungumza mama kwa msisitizo.
“Mimi nimeona nifunge ndoa na Mwantumu” kaka Imran alizungumza na kumeza funda la mate.
“Unasemaje!” mama alihoji kwa mshituko kama ambavyo na mimi nilikuwa nimeshituka baada ya kusikia maneno yale kutoka kinywani mwa kaka Imran.
“Kufunga ndoa na Mwantumu ndio suluhisho la kilakitu” alisisitiza kaka Imran.
“Utakuwa unaugua ugonjwa wa kisulisuli wewe” mama akazungumza kwa mshangao. Maneno ya kaka Imran hayakumuingia akilini hata kidogo. Yani pamoja na ushenzi waliokuwa wamenifanyia bado wanaweza kusimama na kuzungumzia ndoa dhidi yangu!
“Lakini mama, mbona mwenyewe hajakataa” alizungumza kaka Imran kwa kujiamini.
“Heti Mwantumu unamuelewa huyu?” mama alihoji na kunifanya nishituke kama vile nilikuwa kwenye usingizi mzitio uliotawaliwa na ndoto za kutisha.
“Abee mama” nikaitika.
“Haya mambo umeyasikia vizuri?”
“Nimeyasikia lakini sijayaelewa” nikazungumza kwa mashaka.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment