Search This Blog

Sunday, April 18, 2021

HOUSEGIRL WA KITANGA (2) - 1

  


IMEANDIKWA NA : KIZARO MWAKOBA

*********************************************************************************

Chombezo : Housegirl Wa Kitanga (2)

Sehemu Ya Kwanza (1)


Jina langu ni MWANTUMU au TUMU kama wengi walivyokuwa wamezoea kuniita kule kijijini kwetu Tanganyika mkoani Tanga, kule jijini Dar es salaam na hata wasomaji waliowahi kufuatilia mkasa wangu katika msimu wa kwanza wa simulizi hii naopia walizoea kuniita hivyo.

Ndio! Mimi ni Mwantumu, yule Mwantumu ambaye nilikutana na changamoto za kutosha katika maisha yangu ya jijini Dar es salaam. Ni yule Mwantumu ambaye nilikumbana na changamoto ya kutakiwa kimapenzi na wanaume watatu wa familia moja kwa wakati mmoja. Ndio ni wanaume watatu tena wa damu moja na hata majina yao nayakumbuka vizuri sana. Mwanaume wa kwanza alikuwa ni kaka Imran, wapili Fadhili na wa tatu alikuwa ni Baba, yaani baba yao Fadhili mzee Sekiza ambaye alikuwa ni bosi wangu kwa kipindi hicho.

Hata hivyo kati ya wanaume wote hao watatu waliokuwa wakinihitaji kimapenzi chaguo langu mimi kutoka moyoni lilikuwa ni Fadhili. Nilimpenda sana kijana Fadhili pamoja na kwamba alichelewa sana kufunguka na kukubali kunikabidhi moyo wake jambo ambalo lilizidi kunipatia changamoto katika maisha ya mahusiano ya mapenzi.

Kwakuwa nilikuwa natamani sana kuwa na mpenzi ambaye angekuwa mfariji wa nafsi yangu muda wowote ambao ningemuhitaji hasa katika kukabiliana na changamoto za kimaisha, nikajikuta nikidondokea mikononi mwa kijana Endrus. Ndio nilijikuta nikianza kumpenda Endrus hasa baada ya kuona Fadhili hakuwa na msimamo juu ya penzi langu. Fadhili alinionesha waziwazi kuwa hakuwa ananihitaji kimapenzi tena ikafikia hatua akaonesha kunichukia. Hapo nikajikuta nikipokelewa na moyo wa Endrus ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es salaam.

Mtu pekee ambaye aliniunganisha na kijana Endru hakuwa mwengine bali ni dada BUPE. Hapa namzungumzia yule yule dada Bupe ambaye wasomaji wengi walitokea kumchukia kutokana na tabia zake chafu za kukuwadia watoto wa wenzake kwa wanaume. Ni huyo huyo Bupe aliyeniunganisha na Endru halafu baadae akataka kuniunganisha tena na Hance ilihali nilikuwa nimeshazama kwenye penzi la Endrus.

Miongoni mwa wanaume ambao hawakuwa hinivutia wala sikuwahi kuwaza kuwa nao ni pamoja na Hance. Hance hakufanikiwa kabisa kugusa mtima wangu hata chembe, hivyo sikuwa tayari kuwa na mahusiano naye. Hata kama angekuwa mzuri au mwenye mvuto kiasi gani asingeweza kunishawishi kusaliti penzi la Endrus wangu.

Dada Bupe aliendelea kukaza uzi kuhakikisha naingia mikononi mwa Hance. Mchezo huu mchafu uliweza kugundulika na Endrus ambaye ndiye aliyekuwa amepewa dhamana ya kutunza penzi langu. Ilikuwa pata shika nguo kuchanika. Siku hiyo sitokuja kuisahau katika maisha yangu.

Nakumbuka siku hiyo nilikuwa mgahawani kwa dada Bupe tukipiga soga kama ilivyokuwa kawaida yangu kila siku nikimaliza kazi za nyumbani nilikuwa nikienda mgahawani pale kujichangamsha. Mara alifika Hance ambaye alikuwa akinitaka kimapenzi, nikainuka haraka na kukimbilia jikoni kujificha. Masikini ya Mungu kumbe ndio nilikuwa najichimbia kaburi mwenyewe kwani Hance aliingia moja kwa moja hadi jikoni na kuanza kunilazimisha nimpatie majambozi.

Wakati nikiendelea kusumbuana na Hance kule jikoni, ghafla mpenzi wangu Endrus alifika mgahawani pale. Endru alikuwa amesimama nje akizungumza na dada Bupe pasipo kuelewa kama kipenzi chake nilikuwa nimebananishwa na mshenzi fulani hivi kule jikoni.

Katika purukushani na kukuru kakara kule jikoni nilifanikiwa kujichomoa kutoka kwenye mikono ya Hance na kutoka nje. Endru alifurahi sana baada yakuniona kipenzi cha roho yake. Sina uhakika sana lakini nafikiri alikuwa akinipenda sana kijana yule.

Ghafla Hance naye akajichomoa kama mzuka kutokea kule jikoni ambako mimi nilikuwa nimetokea. Kitendo kile kilimchanganya sana Endrus na vurugu kubwa sana ikaibuka hasa baada ya Hance kudai kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mimi.

Ndugu msomaji, ilikuwa pata shika nguo kuchanika. Katika maisha yangu sitokuja kuisahau siku hiyo. Mwisho wa vurumai ile ni pale Endru alipochukua sufuria lililokuwa likichemka uji jikoni na kutaka kumwagia Hance. Laahaula! Hance alikwepa ule uji na ukaishia kwenye uso wa dada Bupe.

Tukio hili lilipelekea dada Bupe kuugua kwa miezi kadhaa ndipo akapata ahuweni. Pamoja na kwamba alipata ahuweni na kupona kabisa lakini sura ya mwanamke wawatu ilisambaratika na kuharibika vibaya. Mungu atanisamehe lakini alikuwa anafanana na kinyago cha ngoma zile za kizaramo.

Watu wengi walikuwa wanatamani sana kufahamu ni kwanini nilikamatwa na Polisi na mwisho wangu ulikuwaje. Nakumbuka hapa ilikuwa pata shika nguo kuchanika kwa wasomaji kutokana na kutomalizia msimu wa pili.

Ukweli ni kwamba nilikuwa nimekamatwa kwa tuhuma za makosa makubwa mawili ambayo yalikuwa ni kushirikiana na Hance pamoja na Endru kufanya vurugu kule mgahawani kwa dada Bupe na kupelekea uharibifu mkubwa wa mali na majeraha kwa Dada Bupe.

Tuhuma ya pili ilikuwa ni kusababisha maafa kwenye familia ya bosi wangu mzee SEKIZA na mke wake Bi.Fatma kwa kufumaniwa nikiwa katika harakati za kukutana kimwili na watu wawili yani Imran pamoja na Baba yake jambo ambalo lilipelekea Bi.Fatma kupata mshituko na kupoteza fahamu.

Siku ambayo Hance na Endru walipigana na kupelekea dada Bupe kuungua vibaya usoni ndiyo siku ambayo Baba aliingia chumbani kwangu usiku na kunilazimisha kufanya mapenzi lakini kabla ya kufanikiwa, kaka Imran naye akaingia chumbani kwangu kiwizi wizi pasipo kufahamu kama Baba naye alikuwemo chumbani mle akifanya mawindo yake ya kimwili.

Kitendo cha Kaka Imran kubisha mlango wa chumbani, baba alikimbia na kujificha nyuma ya kabati na kumuwachia uwanja kijana wake Imran. Sikupenda kabisa kukutana na aibu kama ilekatika maisha yangu.

Ilikuwa ni siku ngumu sana hasa baada ya Fadhili na mama Bi.Fatma kuwakamata wanaume wale wawili wakiwa chumbani kwangu. Tena baba ndio alikuwa uchi wa mnyama. Hapo ndipo mama alipodondoka ghafla na kupoteza fahamu.

Ndugu msomaji, sikupanga wala kutegemea kama siku hiyo kwangu ingekuwa siku nzito na chungu kuliko shubiri. Niliumia sana ndani ya nafsi yangu na kujuta ni kwanini Muumba aliamua kunitengeneza mimi na kunifanya kuwa mrembo kiasi cha kufikia hatua ya kuleta mabalaa katika jamii! Nilijichukia sana kwa kweli na kutamani ningekuwa miongoni mwa wanawake ambao hawana mvuto wa kimahaba.

Siku zote majuto ni mjukuu na wala hayawezi kusaidia kwa chochote ambacho kimeharibika ama hakikwenda sawa. Nilichukua maamuzi ambayo niliyaona ni sahihi ya kutoroka jijini na kutaka kurejea kijijini kwetu Tanganyika wilayani Muheza kule mkoani Tanga.

Nilivaa juba na kujiziba usoni kwa nikabu na kuacha macho tu kama mwarabu wa Dubai. Nilichukua begi langu na kuanza safari ya kuelekea Ubungo kwaajili ya safari ya kurejea kijijini kwetu. Niliyakumbuka sana maisha ya kijijini na kujikuta nikiyachukia maisha ya jijini. Niliapa kuwa nisingerudi tena mjini hata kama kungetokea kitu gani.

Nikiwa kwenye siti yangu huku sina wasiwasi kutokana na mavazi niliyokuwa nimeyavaa kuwa vigumu kutambulika, Nilishitukia watu watatu wakiingia kwenye basi lile moja kwa moja wakasimama karibu na nilipokuwa nimekaa. Mmoja kati ya watu wale alikuwa mwanamke na wengine wanaume.

“Naomba tiketi yako” alizungumza mtu mmoja huku akinyoosha mkono kwangu.

“Tiketi yangu?” nikauliza kwa wasiwasi.

“Ndio, lete tiketi” alizungumza kaka yule kwa amri.

“Ya nini?” nikazidi kuhoji kwa wasiwasi.

“Acha maswali lete tiketi” kaka yule alizungumza kwa ukali kidogo.

Kutokana na mchecheto niliingiza mkono kwenye pochi yangu na kutoa tiketi yangu kisha nikawakabidhi pasipo kufahamu kuwa watu wale walikuwa ni wakina nani.

Kaka yule aliipokea tiketi ile na kuisoma, kisha akawapa wenzake nao wakaisoma. Nikaona wakinitazama kwa mkazo huku wakichezesha vichwa vyao kuashiria mafanikio. Yule kaka alirudi nyuma kisha yule mwanamke akanisogelea.

“Hebu vua hicho kitambaa?” alisema yule mwanamke.

“Kwanini?” nikahoji kwa mshangao.

“Sisi ni maafisa wa Polisi. Tuna mashaka na wewe tunataka kukukagua” alizungumza yule mwanamke huku akionesha kitambulisho chake.

“Lakini mimi sikufanya kitu” nikazungumza kwa wasiwasi huku nikihisi mwili ukitetemeka.

“Vua bwana usitucheleweshe” mwanaume aliyekuwa ananihoji awali alizungumza kwa msisitizo.

Nilijikuta nikiondoa kitambaa kile kilichokuwa kimeziba sura yangu huku nikitetemeka.

“Unatoroka sio?” yule mwanamke alihoji baada ya kuniona sura yangu.

“Hapana!” nilijibu kwa mshituko na wasiwasi.

“Kuanzia sasa hivi upo chini ya ulinzi” alizungumza mwanamke yule huku akinikamata mikono na kunifunga pingu.

“Nimefanya nini jamani?” nikahoji kwa wasiwasi hukunikitetemeka kwa hofu na mashaka.

“We twende utakwenda kujua huko mbele ya safari” askari wale walinichukua msobemsobe huku wakinisukuma na pingu zangu mikononi.

“Lakini ni haki yangu pia kufahamu kosa langu!” nikajikaza na kuzungumza.

“Usijifanye mjuaji binti, songa mbele!”alisema yule askari wa kike.

“Hapana, mbona kwenye video wanauliza na wanajibiwa?” nikaendelea kuhoji.

“Pumbavu! Unafikiri tunaigiza hapa?” yule askari wa kike alizunumza kwa kufoka huku akinisukuma kwa nguvu.

“Sikiliza binti, kwanza kabisa unatuhumiwa kusababisha vurugu na kupelekea uharibifu mkubwa wa mali na majeraha kwa mwenye mali” alizungumza askari mmoja wa kiume kwa sauti ya msisitizo baada ya kuona nimekazana kutaka kufahamu kosa langu.

“Mimi! Nimeleta vurugu? Mnanionea kwakweli” nikazungumza kwa kulalamika.

“Hapa sio mahakamani binti utaeleza mbele ya safari” yule askari wa kike alidakia na kunisukuma tena.

“Na kama hilo halitoshi, ukatembea na bosi wako na kupelekea mke wake kupoteza….”

“Achana naye” Askari yule wa kike alidakia na kumkatiza kauli mwenzake.

Niliogopa sana baada ya kusikia kuwa Bi. Fatma alikuwa amepoteza. Unafikiri kingekuwa ni kipi kimepotea kama sio maisha. Mungu wangu! Niliona Dunia inanielemea kila dakika zilivyokuwa zikibalidika. Sikuelewaningeanzia wapi kutoa maelezo katika kesi ile ya mauaji niliyokuwa nimeibeba.

“Mungu wangu jamani nyie mwanionea miye” nikazungumza kwa kulalamika huku nikitiririsha machozi kwenye mashavu yangu.

“Acha kufuru Malaya wewe! Mungu ndio amekutuma ufanye ufirauni wote huo? Utaozea jela” Jamani nyie nikasukumwa na kupakiwa kwenye kipira cha polisi.

“Sijui niseme nini mie, sijui nimlaumu nani mwenzenu mie. Tazama leo nimeishia wapi huku? Kwani kosa langu mimi ni lipi? Mbona kama ulimwengu unanionea na kunikanyaga bila huruma! Kama ni mapenzi nimekosea wapi? Ona mnaniita Malaya, mnaniita kicheche, limbukeni wa mapenzi, maji mara moja na majina kibao ambayo sio ya kiungwana. Lakini kumbukeni kuwa sikuwahi kutoka na hata mwanaume mmoja kati ya hao wote mnaowafahamu” Nilizungumza moyoni huku nikiwa nimekaa kwenye karandinga la polisi huku machozi yakibubujika kiasi cha kuzamisha mboni za macho yangu.


*****

Mtihani ule mzito haukuwa upande wangu tu, bali hata kwa wale mbuzi wawili waliokuwa wamenisababishia zahma ile nao pia walikuwa katika wakati mgumu.

Walimkimbiza Bi. Fatma katika hosptitali ya Muhimbili ili kuokoa maisha yake haraka sana. Ilikuwa kama vile sinema la mabubu kwasababu hapakuwa na mtu ambaye alimsemesha mwengine hadi mama yule alipopewa kitanda na kupumzishwa na kutundikiwa dripu la maji.

Mzee Sekiza alikuwa ameketi kwenye kitanda alichokuwa amelazwa Bi. Fatma na Fadhili amesimama kwa pembeni. Wakaingia kaka Imran huku wakiwa wameongozana na binamu yao MAINAYA.

“Vipi ameamka?” alihoji kaka Imran mara tu walipofika pale kitandani.

“Unamuuliza nani sasa?” Fadhili akajibu kwa jazba kwasababu alifahamu chanzo cha yote yale alikuwa ni Baba pamoja na kaka Imran.

“Sijakuuliza wewe kaa kimya!” kaka Imran akazungumza kwa kukoroma kidogo.

Kaka Imran alimtazama mama yake aliyekuwa amelazwa kitandani huku bado amepoteza fahamu na kurudisha macho yake kumtaza baba mzee Sekiza. Macho ya baba na macho ya kaka Imran yakakutana na kujikuta kila mmoja akikwepesha na kuangalia pembeni.

Mainaya alikwenda moja kwa moja na kuinama alipokuwa amelazwa Shangazi yake Bi.Fatma na kumtazama kwa wasiwasi.

“Ni kitu gani kimetokea?” alihoji Mainaya huku akimgeukia Fadhili.

Fadhili hakutoa jibu lolote zaidi ya kumeza funda kubwa la mate machungu yaliyokuwa yamejaa ghadhabu na hasira.

“Mjomba mbona sielewi?” Mainaya aligeuza macho yake na kumtazama Baba aliyekuwa amekaa kwa kujiinamia pale kitandani.




Baba aliposikia swali lile akashiuka kidogo lakini akajikaza kiume na kutoa jibu kwa mtoto wa dada yake.

“Alipata mshituko kadondoka na kupoteza fahamu” Baba akaeleza kwa ufupi.

“Kulitokea nini hadi akapata mshituko?” Mainaya aliendelea kudodosa.

Mzee Sekiza alivuta pumzi na kuziachia kwa nguvu kisha akameza funda la mate na kuzungumza.

“Huwa anatatizo la sukari mara kwa mara inapanda na kushuka” Baba aliongopa huku akitazama pembeni.

Fahili aliyekuwa amesimama pembeni akiwasikiliza kwa umakini, aliachia tabasamu kwa ghadhabu na kuvuta hatua kutoka nje ya wodi ile. Hakupenda kushuhudia dhambi ya uwongo ikitendeka mbele ya macho na masikio yake.

“Huyu mtoto wako ana maatizo gani?” kaka Imran alihoji baada ya kumuona Fahili ametoka kwa kiburi. Lengo la kaka Imran lilikuwa ni kumfanya Mainaya asifahamu kile ambacho kilitokea na kupelekea mama yao kupoteza fahamu.

“Achana naye sikuhizi anavuta bangi huyo” alijibu baba kwa ufupi.

Wakati mazungumzo yale yalipokuwa yakiendelea Bi.Fatma pale alipokuwa amelala alipiga chafya na kufumbua macho.

“Shangazi!” alizungumza Mainaya kwa kuhamaki.

Watu wote walikuwa makini wakimtazama mgonjwa wao aliyepata nafuu muda huo.

“Mwite daktari Imran” alisema Baba mara baada ya kumuona mke wake amefumbua macho

“Mume wangu!” Bi Fama aliita mara tu baada ya kufumbua macho.

“Rabeka mke wangu” aliitika mzee Sekiza kwa sauti ya kukatakata.

“Ni kitu gani kinaendelea hapa?” alihoji mama huku akionekana kuto kukumbuka kitu chochote.

Kabla mama hajajibiwa kitu chochote alifika Daktari akiwa ameongozana na kaka Imran.

“Naombeni mnipishe” alisema Daktari yule huku akiweka masikioni mwake kifaa na kuanza kumpima Bi.Fatma.

Baba, Mainaya pamoja na kaka Imran wakatoka na kusimama nje ya wodi ile wakai Daktari akiendelea kutoa matibabu kwa mama.

Mainaya alipotupa macho pembeni akamuona Fadhili amesimama huku ameinamisha kichwa na mikono ameiweka kiunoni.

“Fadhili!” Mainaya akaita huku akivua hatua kumsogelea Fadhili.

“Naam dada Naya, vipi huko ndani” Fadhili aliinua kichwa na kuitika kwa hamasa kubwa ya kutaka kufahamu kilichokuwa kikiendelea wodini.

“Shangazi ameamka” Mainaya alitoa jibu huku akizidi kumsogelea Fadhili.

“Alhamdulillahi, hakika Mungu ni mkuu” Fadhili alizungumza kwa sauti huku akivuta hatua kutaka kwenda wodini.

“No Fadhili, Daktari ameomba tumpishe ampatie huduma” Mainaya alieleza.

Baada ya maelezo yale ya Mainaya, Fadhili alirudisha hatua mbili nyuma na kusimama pale alipokuwa Mainaya.

“Hebu niambie Fadhili, ni kitu gani kimemkuta Shangazi?” Mainaya aliendelea kudodosa huku akionekana hakuwa ameridhishwa na majibu aliyokuwa amepewa na Baba kule wodini.

“Binamu we acha tu!” alisema Fadhili kwa ufupi.

“Usitake kunichanganya Fadhili hebu niweke wazi” alizungumza Mainaya kwa msisitizo.

“Ni ushenzi wa washenzi Fulani tu” Fadhili alizungumza kwa hasira kidogo.

“Ushenzi wa kivipi mbona unaficha ficha?” Mainaya akahoji kwa umakini mkubwa.

Wakati Fadhili na Mainaya walipokuwa wakizunumza waliweza kuonekana na Baba pamoja na kaka Imran.

“Aisee hebu nenda pale yule jamaa asije akaharibu” alizungumza baba kumuamuru kaka Imran.

“Unaogopa atakuchafua enh?” kaka Imran akahoji pasipo kumtazama machoni baba yake.

“Kunichafua au kutuchafua, wewe unafikiri ni aibu ndogo hii?” Baba akazungumza kwa umakini.

“Sasa baba na wewe umeanzaje kunyemelea vitoto vya kazi?” kaka Imran akahoji huku akionekana kukerwa na kitendo alichokuwa amekifanya Baba pasipo kukumbuka kuwa dhambi ile ilikuwa ni yakwao wote.

“Kama ni dhambi mbona na wewe umefumwa?” Baba akahoji huku akionekana kukerwa na mazungumzo yale ya kaka Imran.

“Hapa tatizo sio kufumwa, tatizo ni hizo ndevu zako!” alizungumza kaka Imran kwa jazba.

“Ndevu zangu ndio zimekutuma utake kumla mtoto wa watu?” Baba naye akahoji kwa jazba.

“Lakini baba mimi si nilishakueleza kuwa nampenda Tumu, nataka kumuoa” Imran akalalamika.

“Kwahiyo kule chumbani kwake ndio ulikuwa unatoa posa?” Baba akazunumza kwa hasira huku akijaribu kujivua kwenye aibu ile.

“Ndio, na wewe ulikuwa kwenye vikao vya harusi kule nyuma ya kabati. Sijui ulikuwa unakusanya michango kwa buibui, maana umetoka ndevu zimejaa vumbi na utandu wa buibui utafiiri kinyago” kaka Imran alizungumza na kujikuta akicheka kwa sauti na kupeleka kiganja chake cha mkono mdomoni kujaribu kujizuia.

“Pumbavu! Sasa wewe jifanye unajua kuongea, mwenzako kule anaharibu kila kitu” alizungumza baba kwa umakini mkubwa.

Kaka Imran aligeuza macho yake na kuwatazama Fadhili na Binamu Mainaya walio onekana kuzungumza kitu nyeti sana.

“Usijali mzee, nitafanya chochote kuhakikisha mzigo huu unatupitia mbali” alizungumza Kaka Imran kwa msisitizo.

“Usipoteze hata point moja” Baba alisisitiza.

“We niachie mwenyewe goma nimelivalia kibwaya, kazi yako wewe ni kupiga midundo tu” kaka Imran alizungumza huku akivuta hatua hatua kuwafuata wawili wale walioonekana kuzungumza kitu nyeti sana ambacho penine kingeweza kuzaa matatizo kwa kaka Imran na Baba.

*****

Safari ile ilielekea moja kwa moja hadi kituo kikuu cha polisi cha Ostabay. Hadi muda huo nilikuwa nimewiva sura kutokana na kulia mfurulizo. Mwenyewe niliamini machozi yangu yale yangeweza kunisaidia kwa kutokea msamalia mwema na kunihurumia lakini haikusaidia kitu.

“Teremka Malaya wewe!” sauti ya mwanamke ilinigutusha na kunifanya niinue macho kumuangalia. Alikuwa ni yule askari wa kike aliyekuwa akinisukuma sukuma tangu kule Ubungo waliponikamata.

“Acha kushangaa teremka uende kwenye makazi yako ya milele” mwanamke yule alizidi kunisakama kwa maneno machachu.

Mtoto wawatu wa kitana nikajizoazoa kutoka pale nilipokuwa nimeketi na kuteremka kutoka kwenye karandinga lile. Niliinua macho yangu juu na kuhisi dunia ikinizunuuka huku ndege wa angani pamoja na majengo ya jiji lile wakini nitazama kwa kebehi.

“Amefanya nini huyo Afande?” alihoji askari mmoja aliyekuwa amekamata mafaili akitokea jengo moja kwenda jengo lingine.

“Riuaji hiri, ngoja rikafaidi ugari na maharage wa Segerea. Na hakuna ugari wa bure kure. Kazi nzito ndipo ure” mwanamke yule alizungumza maneno ambayo yalizidi kunifanya nimwagike machozi.



ENDELEA...

Nilisukumwa mkuku mkuku na askari yule wa kike hadi pale mapokezi sijui wenyewe ndio wanapaitaje? Nakwambia nilikuwa sijielewi wala sijitambui kwa jinsi nilivyokuwa nimechanganyikiwa mwenzenu.

“Vua viatu” alisema Askari yule wa kike kwa amri.

Nikavua viatu na kusimama peku huku nikiwa natetemeka kwa hofu na mashaka ya kuozea jela akama amabavyo Askari yule wa kike alikuwa ameniambia.

“Toa vitu vyote kwenye pochi yako hiyo na uviandikishe hapa” alisema Askari yule.

Nilifanya kama ambavyo nilikuwa nimeamriwa na viumbe wale ambao kwa wakati ule nilikuwa nikiwaona kama vile malaika wabaya waliokuwa wametumwa na Bosi wao Shetani kuja kunipatia mateso hadi nisambaratike.

****

Kule Muhimbili Kaka Imran aliendelea kuvuta hatua kuwafuata Fadhili na binamu yao Mainaya pale walipokuwa wamesiamama wakionekana kuzungumza jambo Fulani la msingi zana.

“Ni jambo la kumshukuru Mungu, Mama ameamka” Kaka Imran alizungumza wakati akiwakaribia Fadhili na Mainaya.

“Vipi Daktari ametoka?” Mainaya alihoji.

“Bado anaendelea kumhudumia lakini nafikiri hali imekaa sawa” Kaka Imran alieleza.

“Imran hebu nieleze, Shangazi amepatwa na nini?” Mainaya alihoji baada ya kuona Fadhili anazunguuka kutoa ukweli wa jambo lile.

“Unajua Binamu, huyu mtoto ni mshenzi sana!” kaka Imran alizunumza kwa hasira.

“Nani sasa?” alihoji Mainaya.

“Si hako Kafadhili, yani katoto kana laana haka!” Imran akazungumza kwa jazba huku akitetemaka kwa hasira na macho ameyatoa.

Fadhili alisimama vizuri kuweza kusikiliza ndugu yake yule alikuwa amekusudia kuongea kitu gani mbele yaBinamu yao Mainaya.

“Kwahiyo Fadhili ndio amemuudhi mama?” akahoji Mainaya kwa mshangao.

“Nakwambia Sister haka katoto ni kashetani!” alizungumza kaka Imran huku akimuelekezea kidole Fadhili ambaye alikuwa ametuliapembeni akimsikiliza kwa makini.

Fadhili alihisi kifua chake kikijaa pumzi kutokana na hasira. Alipumua kwa nguvu na kuvuta hatua kuondoka eneo lile. Aliamini chochote kingeweza kutokea na kuharibu utaratibu wa pale Hospitali.

“Kwani amefanya nini?” Mainaya aliendelea kuhoji.

“Unamjua yule dada wa mgahawani amepata ajali jana?”

“Nani Yule aliyekuwa wifi yangu?”

“Bupe bwana!”

“Si ndio huyo wifi yangu, au sikuhizi humtaki tena?” Mainaya naye akazungumzakwa masihara. Kumbe Bupe alishawahi kuwa goma la kaka Imran.

“Acha masihara basi kwenye mambo ya msingi” alizungumza kaka Imran kwa msisitizo.

“Haya imekuwaje?”

“Ni ushenzi wa Fadhili na yule Kenge mwenzie” Imran akazungumza kwa jazba.

“Unajua Imran wacha kuzunguuka niambie kilichotokea”

“Imran alikuwa anamuuza Mwantumu kwa watoto wa chuo, sasa jana wale vijana wakakutana na kuanza kurumbana” Kaka Imran alizungumza na kumeza funda la mate makavu. Sura yake ilikuwa imekauka utafikiri chuma chakavu kutokana na uwongo aliokuwa anaumimina kwa Binamu Mainaya.

“Wale vijana walipigana wakavunja vitu vya watu na mbaya zaidi wakammwagia uji wa moto yule mama wa watu usoni” Imran alieleza kwa hisia kali.

“Mungu wangu! Huyu Fadhili amerogwa au anavuta bangi?” Mainaya akahamaki kusikia maelezo yale.

“Na hivi ninavyokwambia, Bupe amelazwa wodi namba 15 KIBASILA” Imran akaeleza.

“Mungu wangu! Jamani wifi yangu. Twende tukamuone basi” alizungumza Mainaya huku akivuta hatua kuelekea Kibasila ambako dada Bupe alikuwa amepokelewa na kitengo cha magonjwa ya dharula.

Kaka Imran alimtazama binamu yake alivyokuwa amechananyikiwa kutokana na taarifa ile. Aliachia tabaamu la matumaini na kuuma meno yake kwa nguvu kuhisi alikuwa amefanikiwa kupata goli la ushindi kwenye dakika za nyongeza.

“Potelea mbali kama noma na iwe noma, sitaki kuteseka na aibu hii” alizungumza Kaka Imran ana kuvuta hatua kumfuata Binamu kwa nyuma.

Wakati kaka Imran na Mainaya walipokuwa wakielekea Kibasila kumuona dada Bupe, Daktari aliyekuwa anamhudumia Bi.Fatma alitoka. Wakabadili muelekeo na kutaka kufahamu hali ya mama yao kipenzi.

“Vipi Daktari mama yetu anaendeleaje?” alihoji kaka Imran kwa hamasa kubwa.

“Anaendelea vizuri anaweza kuruhusiwa baada ya masaa mawili, lakini atahijaika kupata muda mrefu wa kupumzika” Daktari alieleza.

“Tunaweza kumuona?” Baba alihoji kwa sauti kavu na kukohoa kidogo.

“Hapana, mwacheni kama nusu saa hivi halafu mtaweza kuingia” Daktari alieleza na kuvuta hatua kuondoka.

Pale nje wakabaki wametazamana huku kila mmoja akionekana kukosa cha kuzungumza. Lakini baba alikuwa akijitahidi kukwepesha macho yake kukutana na macho ya Fadhili pamoja na macho ya mtoto wa dada yake Mainaya.

“Twendeni tukamuone Bupe” Mainaya alizungumza.

“Wapi tena dada Naya?” Fadhili akahoji huku akionekana hakuwa na taarifa yoyote ile iliyokuwa ikimuhusu Bupe.

Mainaya alimtazama Fadhili kwa jicho la kebehi na kuachia msonyo mrefu kisha akavuta hatua kuanza safari ya kuelekea kwenye wodi ya Kibasila kumsabahi wifi yake aliyewahikuwa mpenzi wa kaka Imran.

Kaka Imran alimgeukia Baba na kumtazama kwa jicho la wizi kisha akamkonyeza kwa ncha ya jicho la kushoto kumpa ishara ya ushindi. Baba naye aliachia tabasamu moja la kuficha sana ambalo asingeweza kuliona mtu mwingne zaidi ya kaka Imran.

Fadili alibaki ameduwaa asielewe kilichokuwa kikiendelea kati ya kaka Imran na Binamu yake Mainaya. Siku zote binti yule alikuwa akimheshimu sana Fadhili. Haikuwahi kutokea hata siku moja binti yule kuonesha dharau kama alivyofanya siku hiyo.

“Fadhili..” sauti ya baba ilimgutusha Fadhili kutoka kwenye dimbwi la mshangao na kugeuzia macho yake kumtazama Baba kwa makini.

“Hebu njoo..” Baba aliita kwa sauti ya chini.

“Baba ni kitu gani kinaendelea hapa?” Fadhili akahoji kwa umakini mkubwa.

“Kumetokea nini kwani?” Baba naye akarejesha swali kwa Fadhili.

“Hata mimi sielewi namuona Binamu ananisonya na kwa kebehi na dharau” Fadhili akazungumza kwa kulalamika.

“Achana nao” alizungumza Baba kwa ufupi huku akiamini yale yalikuwa ni matokeo ya fitna ya kaka Imran.

“Lakini baba…”

“Sikiliza Fadhili, naombe unisamehe kwa kilichotokea” Baba alizungumza kwa sauti iliyokuwa imejaa majuto.

“Baba..”

“Mwanangu..”

“Mama na Mwantumu ndio wakuombwa msamaha” Fadhili alizungumza kwa msisitizo.

“Naomba jambo hili liwe siri mwanangu!” alizungumza mama kwa unyenyekevu.

“Hapana baba, nahisi umechelewa. Jambo hili limeshafika kwenye vyombo vya dola” alizungumza Fadhili.



“Unasemaje Fadhili! Limefikaje na ni nani ametoa jambo hili nje ya familia?” Baba akahoji kwa hasira.

“Na hivi ninavyozungumza, Mwantumu amekamatwa na polisi leo asubuhi” Fadhili alizungumza.

“Haya mambo yameshakuwa makubwa tena” Baba alizungumza huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Mtu anayehusika kwa yote haya ni Fadhili” ilisikika sauti ikizungumza kutokea nyuma na pale walipokuwa wamesimama Fadhili na Baba.

Walipogeuza macho yao wakakutana na kaka Imran ameongozana na binamu yake Mainaya.

“Unasemaje Imran?” Fadhili akahoji kwa kuhamaki.

“Baba kumbe huyu kunguru alikuwa anafanya biashara ya kumuuza Mwantumu kwa wanaume kule mgahawani kwa Bupe” alizungumza kaka Imrani huku ametoa macho kwa hasira za kutengeneza na kumuoneshea kidole Fadhili.

“Unasemaje Imran! Fadhili amekuwa mshenzi kiasi hicho?” Baba alishituka sana baada ya kusikia msneno yale kutoka kwa Imran.

“Lakini kaka Fadhili mbona hufanani na mambo ya kishenzi hayo?” Mainaya alihoji kwa mshangao.

“Huyu ni joka! Tena Joka la jehanamu limevaa ngozi ya kondoo tu. Ukimuona ameinama kama kobe kumbe anaficha uchafu wake!” Imran alizungumza kwa msisitizo na kuzidi kumuweka Fadhili katika wakati mgumu ilhali kosa amefanya yeye na Baba.

“Bro angalia mdomo wako huo!” Fadhili akazungumza kwa tahadhari.

“Kwenda zako Malaya mkubwa wewe!” alizungumza Imran kwa jazba.

“Acha basi kuongopea nafsi yako, nani ni Malaya kati yangu mimi na wewe sasa?” Alihoji Fadhili kwa sauti ya upole lakini yenye maneno ya kukera.

“Tena nitahakikisha unakamatwa na kutiwa rumande. Hili sitolifumbia macho. Yule mwanamke wa watu amesambaratika sura kwaajili ya upuuzi wako” alizungumza Imran kwa hasira.

“Imran, naomba unyamaze” Baba alitoa sauti ya ukali kidogo kumnyamazisha kaka Imran.

“Baba hii ni aibu, huyu mtoto ametuletea aibu kubwa ndani ya familia yetu!” Jamani nyie kaka Imrani aliendelea kutoa maneno magumu bila hata huruma.

“Basi kaka Imran, tutazungumzia nyumbani achana nayo na tuangalie hali ya shangazi kwanza” Mainaya akatoa wazo huku akiwa hafahamu hali halisi juu ya mambo ambayo yamejiri.

“Huyu hawezi kufika nyumbani Binamu! Lazima achukuliwe hatua hukuhuku. Mwenyewe si umeona hali ya Bupe kule Kibasila!” alizungumza Imran.

Fadhili alihisi kuchefuliwa na mazungumzo yale ya kaka Imran amabayo hayakuwa na kichwa wala miguu. Alifahamu wazi kuwa yote ile ilikuwa ni kuchanganyikiwa kutokana na aibu iliyokuwa imemfika yeye pamoja na baba mzee Sekiza. Fadhili akatikisa kichwa kusikitika na kugeuka kuelekea wodini alipokuwa amelazwa mama yake huku ameweka mikono mfukoni na kichwa amekiinamisha chini.

Pale nje walibaki watu watatu wakimkodolea macho kijana yule ambaye alionekana kutembea kwa dharau. Kwa mara ya kwanza Binamu alianza kuhisi chuki na hasira dhidi ya Fadhili kutokana na matendo yake ambayo amesikia kwa kaka Imran.

Fadhili alifika kwenye kitanda alichokuwa amelazwa mama Bi. Fatma na kumtazama kwa sekunde kadhaa.

“Mama..” Fadhili aliita kwa sauuti ya chini.

“Fadhili baba” mama aliitika kwa sauti ndogo ya ugonjwa.

“Unaendeleaje mama yangu” alizungumza Fadhili huku ameinama pale kitandani.

“Nipo sawa kabisa mwanangu nafikiri naweza kuondoka sasa” mama alizungumza.

“Pole sana mama” Fadhili alizungumza huku akiketi na kushika kiganja cha mkono wa mama yake.

“Hawa mbuzi wapo wapi?” mama alihoji huku amekunja sura kwa hasira.

“Nani mama?” Fadhili akahoji huku akijifanya hakumuelewa mama yake.

“Imran na baba yake”

“Wapo hapo nje mama, nikawaite?” Fadhili alihoji kwa sauti ya upole.

“Hapana, sitaki hata kuona pua zao” Mama alizungumza huku akionekana kujawa na ghadhabu dhidi wa watu wale wawili.

“Inabidi uwe na moyo wa kusamehe mama” Fadhili alizungumza kwa sauti ya kusihi na iliyojaa upendo.

“Na huyu Mwantumu yuko wapi?”

“Mwantumu ameshikiliwa na Polisi” Fadhili alijibu.

“Kwanini ashikiliwe na Polisi?” mama alihoji kwa taharuki baada ya kupata taarifa ile.

“Kwasababu…” Yasini alitaka kutoa maelezo lakini kabla hajamalisa mama alimkata kauli.

“Sikiliza Fadhili mwanangu”

“Naam mama”

“Fanya unavyoweza, uhakikishe huyu mtoto wa watu anaachiwa huru” Bi.Fatma alizungumza kwa msisitizo.

“Sawa mama” alijibu Fadhiri kwa sauti ya unyenyekevu na heshima.

“Naomba ufuatilie kibali kwa Daktari nitoke humu, kwa sasa sijambo” alizungumza mama.

Pasipo kuzungumza kitu chochote kile, Fadhili alijiinua kwaajili ya kwenda kumtafuta Daktari na kuomba kibali cha ruhusa. Wakati anatoka alikutana na msafara wa Baba, kaka Imran na Binamu Mainaya wakiingia wodini mle. Wakapishana kama vile hawakuwa wakifahamiana na wala hakuna aliewahi kumuona mwenzake tokea mwanzo wa dunia.

“Unaendeleaje mke wangu” Baba alihoji baada ya kufika pale kitandani huku akiwa na wasiwasi na kuhisi mama angekuwa na hasira dhidi yake.

“Sijambo mume wangu, namshukuru Mungu naendelea vizuri” Mama alijibu kwa sauti ya upole na iliyokuwa imejaa upendo.

Kaka Imran pamoja na Baba walipobaini kuwa mama hakuwa na dalili yoyote ya hasira, wakajikuta nafsi zao zinaingiwa na matumaini ya amani.

“Nimepatwa na nini Mume wangu?” Bi. Fatma akahoji huku akijifanya hakuwa anakumbuka jambo lolote lililotokea.

“Inamaana hukumbuki kitu mke wangu?” Baba akahoji kwa umakini huku amemkazia macho mke wake.

“Hapana, Daktari amesema nitachukua muda kama wa miezi miwili ndipo nitaweza kurejewa na kumbukumbu zangu zote” mama alieleza kwa kuongopa.

Baba na kaka Imran wakatazamana kwa macho ya kupeana ishara ya ushindi halafu kila mmoja akatabasamu ndani ya nafsi yake.

“Usijali mke wangu ni vijimambo vidogo tu vya watoto” Baba alizungumza.

“Vimambo gani?” mama alihoji.

“Ah si unajua watoto wetu hawa, tutakwenda kuliweka sawa nyumbani” baba alizungumza.

“Siku moja Fadhili atakuua mama?” kaka Imran akadakia na kuzungumza. Lengo lake ni kuvuruga kabisa akili ya mama kwa kumchafua Fadhili na yeye pamoja na Baba kujiweka katika sehemu nzuri. Alikuwa akizungumza yote hayo pasipokuelewa kama mama alikuwa anaelewa kila kitu kilichokuwa kimetokea.



“Tayari mmeshaanza yani kila siku Fadhili Fadhili, huyo Fadhili amekuwa nani hasa asiyeenda dobi akatakata?” mama akajifanya amekasirika kutokana natabia mbaya za Fadhili.

Wakati mama alipokuwa akizungumza, Daktari alifika huku amekamatia fomu kwaajili ya kutolea Ruhusa. Wakatihuo Fadhili alikuwa anatembea nyuma ya Daktari yule.

“Vipi jamani mgonjwa wetu anaendeleaje?” alihoji Daktari mara tu alipofika pale alipokuwa amelakazwa Bi.Fatma.

“Naendelea vizuri Daktari nafikiri nimepona” Bi.Fatma alidakia na kutoa majibu kabla ya mtu yeyote yule kujibu.

“Una uhakika mama?” Daktari akahoji kwa umakini mkubwa.

“Amini nakwambia, nimepona kabisa mwanangu!” mama akasisitiza.

“Mama una uhakika upo sawa?” Fadhili akahoji kwa msisitizo.

“Kelele wewe wacha kimbelembele! Mgonjwa anasema amepona kipi amabacho unakitaka wewe?” kaka Imran aliingilia kati kauli ya Fadhili.

Fadhili alivuta pumzi na kuziachia kwa nguvu pasipo kuongeza neno lolote lile. Alichokifanya ni kumeza funda la mate machachu kisha akavuta hatua kutoka nje ya wodi ile. Alikuwa anaifahamu vyema hali ya mama yake kwasababu alishazungumza naye kabla ya wengine kuingia.

“Basi kama unaendelea vyema, nimekuja kukupa ruhusa mama” alizungumza Daktari huku akiandika kwenye faili alilokuwa amefika nalo pale wodini.

******

Kule kituoni mambo yaliendelea kuwa magumu kwa upande wangu, mtoto wa kike niliswekwa rumande utafikiri jambazi wa kutumia silaha.

“Hebu mlete huyo bibie” nilisikia sauti ya kiume ikitoa amri.

“Ndio Inspekta” nikasikia sauti ya kike ikijibu.

Komeo la sero ile lilifunguliwa nikatolewa nje huku nikiwa nimekamatwa mkono wa kushoto na yule askari wa kike aliyekuja kunikamata kule Ubungo nilipokuwa katika jaribio la kutoroka jiji.

“Kaa hapo chini” alizungumza yule Mwanaume aliyekuwa Ispeka kama ambavyo alitajwa na yule askari wa kike.

Nilitii ile amri na kuketi sakafuni huku nikisikiliza kwa makini maelekezo ambayo ningepatiwa.

“Mimi naitwa Inspekta Marwa, mkuu wa kituo hiki” alizungumza mzee yule huku amenitumbulia macho.

Niliitika kwa kichwa huku nikiwa sielewi umuhimu wa yeye kujitambulisha kwa mhalifu kama mimi amabaye tayari nilikwisha tabiriwa na yule Askari wa kike kuwa maisha yanu yangeishia Gerezani.

“Unaitwa nani?” alihoji Inspekta Marwa kwa sauti ya upole lakini iliyokuwa kavu.

“Jina langu Tumu” nikajibu kwa ufupi.

“Tumu ndiyo nini? Nitajie majina yako yote” Alizungumza Inspekta Marwa kwa sauti ya msisitizo.

“Naitwa Tumu Mudy” nikajibu haraka sana baada ya kubaini kumuudhi mtu yule niliyemuona kama mfuasi wa shetani.

“Binti wacha uhuni! Nitajie majina yako kwa ukamilifu, Mudy ndio kidudu gani?” Jamani nyie, Askari yule akazungumza kwa ukali sasa.

“Ninaitwa Mwantumu Mohamed” nikazungumza kwa unyenyekevu huku nikiwa nimetawaliwa na lindi la woga na hofu.

Inspekta Marwa aliandika kwenye lile likitabu lake kubwa na baada ya hapo akainua macho yake kunitazama usoni kwa sekunde kadhaa kama vile alikuwa akifikiria namna ya kuanza kuzungumza na mimi.

“Binti, kama utanipa ushirikiano wa kutosha nitakusaidia. Lakini usiponipa ushirikiano itakula pande yako” alizungumza Inspekta Mrwa kwa sauti ya kusisitiza.

Nikajibu kwa kichwa na kumeza funda la mate. Nikaona sasa muda wa kuhukumiwa ulikuwa umefika masikini ya Mungu mtoto wa watu wa kitanga miye.

“Unaishi wapi?”

“Nani mimi?” nikahoji huku nikiwa sielewi namna ya kujibu swali lile.

“Unafikiri nazungumza na nani?”

“Kwetu ni Tanga, lakini hapa nilikuwa naishi Mabibo” nikaeleza kwa kirefu.

“Huko Mabibo unaishi kwa nani?”

“Mzee Sekiza”

“Unafahamu kwa nini upo hapa?” alihoji yule Askari.

Nikatikisa kichwa kuashiria kuwa sikuwa nafahamu kosa langu amabalo lilikuwa limepelekea mimi kupelekwa pale polisi.

“Inamaana wakati unakamatwa haujaelezwa sababu ya kushikiliwa kwako?” alihoji Inspekwa Marwa.

“Walinieleza” nikajibu kwa ufupi.

“Sasa mbona unasema hufahamu” Inspekta Marwa akazungumza huku akiandika andika kwenye kitabu chake.

“Enhe, ulielezwa una kosa gani?” Inspekta alihoji.

“Walisema nimeua” nikajibu kwa ufupi huku nikihisi damu zikikimbizana kwenye mishipa yangu ya damu.

“Kwanini umeua?”

“Hapana Afande, mimi sikuua mtu yeyote yule” nikazungumza kwa kulalamika huku nikipiga magoni na mikono yangu nimeikutanisha kifuani kuomba nihurumiwe.

“Unamfahamu Bupe?” Alihoji inspekta Marwa na kufanya moyo wangu kushituka na kuhisi tayari dada Bupe alikuwa ameaga dunia kule Sewahaji.


“Nazungumza na wewe Mwantumu, unamfahamu Bupe?” Inspekta alihoji kwa msisitizo na sauti kubwa kidogo.

“Ndio namfahamu Afande” nikajibwa kwa sauti ya mshituko kidogo.

“Bupe ametoa maelezo kuwa hamuhusishi mtu yeyote juu ya ajali aliyokuwa ameipata” Inspekta Marwa alieleza.

“Kwahiyo dada Bupe kumbe yupo hai?” nikajikuta nikihoji huku nimetoa macho kwasababu nilikuwa naamini nahukumiwa kwa kosa la kusababisha kifo cha mwanamke huyo.

“Wewe ulitaka afe sio?” Ispekta Marwa akahoji kwa mshangao kidogo.

“Hapana Afande sina maana hiyo” nikajibu haraka sana kukanusha Imani ile ya Inspekta Marwa.

“Kutokana na maelezo ya Bupe ambayo ameyatoa kwa Afisa wetu wa upelelezi, hauna kesi ya kujibu juu ya jambo hili” Alieleza Inspekta Marwa kwa sauti ya upole.

Sikuweza kuamini kusikia maneno yale kutoka kwa Askari yule aliyekuwa akinihoji maswali ambayo kwangu niliyaona magumu na yaliyokuwa yamejaa mitego.

“Lakini kuna hii kesi nyingine nayo” Inspekta Marwa alizungumza huku akinitazama kwa macho ya udadisi.

Nilishituka sana baada ya kusikia maneno yale kutoka kwa yule mkuu wa kituo. Nikameza funda la mate na kutafuna memo yangu kwa nguvu huku nikiona matumaini ya kuwa huru yakitoweka tena.

“Unamfahamu yule….?” alihoji Inspekta huku akionesha kidole kule upande wa kaunta.

Ndugu msomaji nilihisi kufakufa maana mtu niliyekuwa naoneshwa na Askari yule alikuwa ni Fadhili amesimama pale mapokezi akinikodolea macho utafaikiri alikuwa anacheza gemu la mazombi.

“Ndio...Namfahamu” nikajibu kwa kujiumauma.

“Unamfahamu kivipi?”

“Ni mtoto wa Bosi wangu” nikajibu kwa ufupi.

“Sasa Fadhili amekuja kukutolea dhamana, lakini kutokana na maelezo yake imebainika kuwa wewe hauhusiki na chochote juu ya ugonjwa wa Bi.Fatma” Askari yule alizungumza kwa upole huku akiendelea kuandika kwenye lile faili lake.

Niliinua macho yangu na kumtazama Askari yule kwa makin huku nikihisi alikuwa amekosea kunipatia mimi taarifa ile.

“Ninachomaanisha ni kwamba, hauna hatia yoyote katika makosa uliyokuwa ukituhumiwa” Inspekta Marwa akazungumza kwa msisitizo huku akisogeza lile lifaili lake pale nilipokuwa nimeketi.

“Unajua kusoma Kiswahili?” alihoji Askari yule, name nikaitika kwa kichwa.

“Soma haya maelezo kwa umakini halafu usaini hapa chini” alizungumza Askari yule huku akinikabidhi kalamu.

Ndugu msomaji nakwambia kutokana na mchecheto na kihoro nilichokuwa nacho sikuona haja ya kusoma neno lolote lile kwenye maandishi yale. Nilichokuwa nakitaka mimi ni kutoka tu ndani ya shimo lile la jehanamu nililokuwa nimejitumbukiza pasipo kujielewa.

Amakweli Mungu yupo na anasikiliza maombi ya waja wake na kuayajibu kwa wakati. Pamoja na kwamba binadamu wa duniani walishindwa kunihurumia lakini mwenyewe Muumba aliye mtukufu hatimaye alitenda muujiza.

Nilipewa vitu vyangu vilivyokuwa vimehifadhiwa na polisi kisha nikafahamishwa kuwa kuanzia wakati ule nilikuwa huru na wala sikuwa na kesi yoyote ile niliyokuwa natuhumiwa nayo.

Pasipo kujielewa nikainua mikono yangu juu kutoa shukurani zangu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwingi wa Rehema aliyejaa kila sifa ya utukufu na anayestahiki kuabudiwa na viumbe vyote.

“Haya twende mama” ilikuwa ni sauti ya Fadhili aliyekuwa amesimama pale Kaunta akinisubiri.

Sikuzungumza neno lolote zaidi ya kuvuta hatua kumfuata Fadhili huku nikiwa siamini. Nilipofika nje nikakutana na yule Askari wa kike amesimama na Askari wengine wawili wa kiume kama vile kulikuwa na jambo wanalijadili.

“Naona umechomoa mama!” alizungumza Askari yule wa kike huku akinigeukia kwa aibu.

Sikujibu neno lolote zaidi ya kuendelea kuvuta hatua hadi kwenye gari alipokuwa amepaki Fadhili.

Fadhili alifungua mlango wa gari na kuingia. Mimi nikabaki nimesimama pale nje nikijaribu kujishauri niingie ama nisiingie.

“Ingia twende” alizungumza Fadhili huku akinichungulia pale nilipokuwa nimesimama.

“Unataka kunipeleka wapi?” nikahoji kwa msisitizo.

“Si nyumbani kwani we unataka kwenda wapi?” Fadhili akajibu.

“Asante Fadhili kwa msaada wako, lakini huko nyumbani mimi siendi” nikazungumza kwa msisitizo huku nikigeuka kutaka kuondoka.

“Wewe!” Fadhili akaniita.

Nilipogeuka na kumtazama ili kuweza kusikia alichokuwa anataka kuniambia nikamuona ameganda kunitazama kwa mshangao.

“Unasemaje?” nikahoji.

“Umeanza lini kuvuta bangi?” Fadhili akahoji kwa mshangao.

“Kwani kosa langu liko wapi?” nikahoji na mimi.

“Hebu ingia kwenye gari twende”

“Hivi ni kwanini hutaki kunielewa Fadhili, nimekwambia huko nyumbani kwenu mimi sikanyagi hata dunia isambaratishwe na kuanzishwa tena” nikazungumza kwa msisitizo na kujiamini.

“Kwahiyo wewe unataka kwenda wapi?” Fadhilia akahoji huku akionekana kuchoshwa na ule msimamo wangu.

“Kwetu!” nikajibu kwa ufupi.

“Sasa si tunakwenda nyumbani kwanza halafu utakwenda huko kwenu” Fadhilia aljaribu kunishawishi.

“Kwani nimesahau nini huko kwenu, au hunioni hapa nimekamilika na mabegi yangu? Baba hii ni Tanga line, nawatakia maisha mema na jiji lenu!” nikazungumza kwa msisitizo huku nimemkazia macho Fadhili.

Masikini ya Mungu kijana wa watu katika maisha yake hakuwahi kuniona nikiwa nimeshikilia msimamo kiasi kile. Alifikiri mimi ni yule Tumu niliekuwa ninababaikia mapenzi kila kukukicha. Wakati huo nilikuwa ni Tumu Mpya niliyekuwa najielewa na kujitambua vyema.



“Twende basi nikusindikize Ubungo ukapande mabasi ya kwenu” Fadhili aakazungumza kwa sauti ya chini.

Niligeuza macho yangu na kumtazama kama vile sikuwa nimesikia kile alichokuwa amekizungumza.

“Twende sasa, unashangaa nini au huoni kama muda unakwenda?” Fadhilia akahoji kwa msisitizo.

Nilifungua mlango wa gari na kuingia na mabegi yangu huku sura yangu ikiwa imepoteza kabisa nuru ya amani na matumaini ya kuendelea kuishi jijini Da res Salaam.

****

Mama aliruhusiwa na kurejeshwa nyumbani huku kila mmoja akionekana kujawa na furaha kutokana na afya ya mama mwenye nyumba kutengemaa. Hata hivyo kwenye mioyo ya Baba na Kaka Imran kulikuwa na hofu na wasiwasi wa hali ya juu kutokana na kile walichokuwa wamekifanya.

Wakati mainaya akipoza supu kwaajili ya mgonjwa kule chumbani, alishangaa kumuona Bi. Fatma akijiinua kutoka kitandani na kuanza kukusanya nguo kutoka kabatini na kuziweka kwenye begi.

“Shangazi imekuwaje tena?” alihoji Mainaya

“Hamna kitu mwanangu” alijibu Bi. Fatma huku akiendelea na zoezi zlilokuwa amelinzisha ghafla.

“Mbona kama unafungasha?” Binamu Mainaya alihoji.

“Ndio mwanangu, nimeona niende nyumbani nikaugulie huko” shangazi alijibu kwa ufupi huku akiendelea kukunja nguo zake na kuziweka ndani ya begi.

“Sasa unatoka mjini unakwenda kuugulia kijijini kweli shangazi?” Mainaya akahoji kwa mshangao.

“Unafikiri mimi ni mgonjwa kihivyo basi, niko sawa kabisa mwanangu” mama alieleza.

“Mimi hata sikuelewi, labda nimuite Baba mnaweza kuelewana” Mainaya alizungumza kwa msisitizo huku akiamini Bi. Fatma alikuwa ni mgonjwa sana.

“Mainaya” Bi. Fatma aliita huku akiwa amemkazia macho yake Binamu.

Mainaya aliinua macho yake na kumuangalia usoni hivyo wakawa wanatazamana kama vile majogoo.

“Wewe ni mwanamke kama mimi, wacha niende nyumbani” Bi.Fatma alizungumza kwa msisitizo.

Maneno yale yalionekana kumchoma sana binamu Mainaya na kuhisi kuzidi kumchukia Fadhili kwasababu alikuwa anaaamini ndiye chanzo cha matatizo yale aliyokuwa nayo shangazi yake.

“Inamaana unamsusia nyumba Fadhili” Mainaya akahoji kwa umakini mkubwa.

Mama akamtazama Mainaya kisha akaachia tabasamu la matumaini kiasi cha kupelekea nuru kuonekana kwenye uso wake.

“Mainaya Mwanangu, Fadhili ni mwanaume! Tena ni mwanaume anayestahili kila sifa ya kuitwa mwanaume” mama alieleza.

“Kwahiyo mama, mtu akifanya utumbo ndio anaitwa mwanaume?” alihoji Mainaya kwa mshangao kwasababu tayari alikuwa na picha mbaya dhidi ya Fadhili.

“Fadhili hayupo kama unavyofikiria, najivunia sana kuwa na mtoto kama Fadhili” alizungumza mama kwa msisitizo.

Wakati mama na binamu Mainaya walipokuwa wakijadiliana hili na lile, mlango ulifunguliwa na baba akaingia chumbani mle. Macho ya mwanaume yule yakatua kwenye begi la nguo zilizokuwa zimefungashwa na mama.

“Haya mbona mafurushi tena husubiri hata kupona?” alihoji Baba huku akiamini nguo zile alikuwa anafungasiwa Mainaya akazifue.

Mainaya alijiinua kutoka kitandani na kuvuta hatua kutoka chumbani mle kwa lengo la kupisha mazungumzo ya Maba na Mama.

“Samahani mume wangu, nilikuwa ninaomba niende nyumbani” Bi.Fatma alizungumza kwa sauti ya upole na iliyokuwa imejaa unyenyekevu.

“Unasema…?” Baba akahoji kwa kuhamaki.

“Naomba niende Tanga nikapumzike” mama alizungumza.

“Ukapumzike kwani hapa unabebeshwa mizigi ya vyuma kichwani?” alihoji baba kwa mshangao mkubwa.

“Yani mume wangu, ungeniacha tu niende” mama alizungumza kwa upole lakini kwa sauti iliyokuwa imejaa msisitizo.

“Kwani kuna kosa lolote nililolifanya mke wangu?” Baba akahoji ili kupima kama mama alikuwa amegundua jambo lolote juu ya lile fumanizi la kufunga mwaka lililokuwa limetokea siku iliyopita.

“Wala haujanikosea mume wangu, ila naomba tu niende nyumbani”

“Mke wangu, siwezi kukuacha uondoke katika hali kama hiyo” alizungumza Baba kwa msisitizo.

“Kama kweli unanipenda, ni afadhali tu uniache niondoke” mama alizungumza kwa msisitizo na ukakamavu utafikiri sio yeye aliyekuwa akiungua hoi mahututi na kupelekea kulazwa kule Muhimbili.

“Hata kama ningekuwa chizi kiasi gani, siwezi kukuruhusu utoke humu ndani” Baba akazungumza kwa ukali kidogo baada ya kumuona mama alikuwa anaelekea kumpanda kichwani na kusahau kama yeye ni mama na mzee Sekiza ni Baba katika familia ile.

“Namimi hata kama ningekuwa chizi kiasi gani, siwezi kubaki ndani ya nyumba hii” Mama naye akajikuta akizungumza kwa jazba.

Maneno yale yalimshitua sana baba na kuhisi pengine mama alikuwa ameanza kugundua kilichokuwa kimetokea usiku.

“Unataka kusemaje?” akahoji baba

“Tutaonana Paradiso” alizungumza mama kwa msisitizo akimaanisha kuwa kama angepata nafasi ya kutoka ndani asingeruni tena.

“Nini? Sasa hatoki mtu humu ndani” Baba kazungumza kwa msisitizo.

“Huna haya we mwanaume!” alizungumza Mama huku akibadili mavazi aliyokuwa amevaa na kuvaa mengine ambayo yalikuwa na hadhi ya kusafiria.

“Unanitusi! Unanitukana we mwanamke?” baba alizunumza kwa sauti ya ukali.

“Wala sijakutukana, hebu nitajie tusi hapo nililokutukana” Mama alizungumza kwa sauti a chini huku akifunga kiremba kichwani tayari kwa safari.

“Unajua mimi sijali kama unaumwa, nitakuvuruga hadi kijijini kwenu wakakushangae” Baba alizungumza kwa ile sauti yake ya ukali.




“Washangae mara ngapi wakati umeshaushangaza ulimwengu” Mama akazungumza maneno ambayo yalizidi kumchanganya baba na kumfanya atoke chumbani mle na kumuacha peke yake akiendelea na maandalizi ya safari.

*****

Sijui niseme nini ndugu msomaji, lakini naomba uelewe kuwa Fadhili alikuwa ni mtu poa sana. Yani kama ambavyo nilikuwa nataka mimi ndivyo alivyofanya pasipo kwenda kinyume na kuniudhi. Aliendesha gari moja kwa moja hadi nje ya stendi ya mabasi yaendayo mikoani pale Ubungo.

“Umefurahi sasa?” alihoji Fadhili baada ya kupaki gari karibu na restaurant moja iliyokuwepo karibu na stendi ya mabasi ya Ubungo.

Nilimtazama na kuachia tabasamu la kujilazimisha kisha nikakamata kitasa cha mlango kwaajili ya kuteremka, lakini kabla hata sijanyonga kitasa cha mlango Fadhili akanidaka mkono na kunizuia. Nikageuza shingo na kumtazama kwa macho ya kuhoji.

“Tafadhali Tumu, naomba japo dakika hizi…tatu nataka kuzungumza na wewe” Fadhili akazungumza kwa kusihi.

“Endelea nakusikiliza” nikajibu kwa ufupi.

“Hapana mama, naomba tukakae pale tupate angalau juice” Fadhilia alisihi.

Nilivuta pumzi na kuzitoa kisha nikakubali kwa ishara ya kichwa kuwa nilikuwa tayari kusikiliza mazungumzo yake.

“Naomba juisi za Ukwaju mbili” Fadhili aliagiza mara tu tulipofika na kuketi kwenye meza, sijui hata ni nani alikuwa amemwambia kuwa nilikuwa nataka kunywa juisi ya ukwaju. Lakini kwakuwa sikuwa nimepanga kunywa juisi sikupinga.

“Kwanini hutaki kurudi nyumbani?” Fadhili akahoji alipokuwa akipokea glasi za juisi kutoka kwa mhudumu.

Nikakaa kimywa kama vile sikuwa nimesikia swali lake ambalo kwangu halikuwa na umuhimu wowote zaidi ya kunichefua.

“Nazungumza na wewe Mwantumu au hujanisikia?” Fadhili akasisitiza swali lake.

“Sijui ni kwanini unapenda kurudia rudia mambo ambayo hayana umuhimu” nikazungumza kwa hasira baada ya kuona mwanaume yule alikuwa amekusudia kuharibu mpango wangu wa kurudi kijijini kwetu Tanganyika.

“Au unaogopa kugonganisha tena matera?” Jamani nyie sijui Fadhili alikuwaje maana hata maswali yake yalikuwa yamekaa uchokozi uchokozi tu, Daah!

“Nakuheshimu Fadhili, naomba uniache” nikazungumza kwa jazba.

“Sasa mwenzangu umewezaje kucheza na wanaume wawili kwa wakati mmoja?” alihoji Fadhili swali la uchokozi.

“Fadhili naomba uniache! Kama hauna kingine cha kuzungumza niondoke!” nikazungumza kwa hasira zaidi.

“Wala mimi sina shida na wewe, katika maisha yangu sijawahi kufikiria kutembea na wanawake vigwagula” Fadhili alizungumza na kupeleka birauli ya juisi mdomoni kisha akapiga funda kubwa kabla ya kuishusha mezani.

“Hivi unanionaje Fadhili, unafikiri mimi ni Malaya sana eeh?” nikahoji kwa jazba baada ya kuitwa kigwagula na Fadhili. Kule kwetu Tanga kigwagula ni mzee mchawi, sasa sijui yeye mwenzangu aliponiita mimi Kigwagula alikuwa na maana gani.

“Mimi sijasema hivyo, labda ndio unaniambia mwenyewe” alizungumza Fadhili huku akionekana kujaza mlima wa dukuduku kwenye mtima wake.

“Sasa sikiliza, kwa taarifa yako tangu nimekuja hapa Dar hakuna mwanaume hata mmoja aliyewahi kulala na mimi” nikaeleza kwa msisitizo kuhakikisha heshima yangu kwa Fadhili haishuki.

“Acha uwongo wewe! Hadi umefikia hatua ya kulala na wanaume wawili wawili halafu bado unajiona ni wa kawaida!” Fadhili akazungumza kwa kejeli.

“Kwahiyo unaamini mimi nimelala na wale washenzi?” nikazungumza kwa hasira.

“Usiwe mnafki wewe, leo hii ndio unawaita washenzi! Wakati unawakaribisha chumbani kwako walikuwa waungwana” jamani nyie sijui mwanaume yule alikuwaje! Inaelekea alikuwa amenipania sana kwa kile ambacho kilikuwa kimetokea. Hata hivyo kwa upande wangu mimi sikuwa na kosa lolote lile jamani.

“Habari zetu watu wa Mungu!” sauti ya mtu aliyetusalimia ilikatisha mazungumzo yetu mimi na Fadhili.

Sote wawili tuliinua macho yetu na kumtazama yule mtu aliyekuwa amesogea hadi pale kwenye meza yetu na kutusalimia kwa msisitizo kama vile alikuwa anatufahamu vizuri sana.

Mungu wangu! Alikuwa ni Endru yule kijana wa chuo ambaye aliwahi kuwa mpenzi wangu. Yule aliyepigana na Hance kule mgahawani na kuishia kumuunguza dada Bupe usoni kwa uji wa moto. Ndio alipigana na Hance kwasababu yangu. Sasa kwa wakati huo alikuwa amesimama pembeni ya meza tuliyokuwa tumeketi mimi na Fadhili.

“Karibu..” Fadhili akamkaribisha kwa sauti ya chini lakini iliyokuwa na mashaka.

“Samahani Bro, naweza kuzungumza na mrembo dakika mbili?” Endru alihoji kwa sauti kavu.

“Nani huyu... unamfahamua?” alihoji Fadhili kwa mashaka.

“Ndio tunafahamiana” Endru akajibu kwa kujiamini.

“We unikome! Tunafahamina tumeonana wapi?” nikazungumza kwa jazba huku nikijifanya simtambui hata kidogo kijana yule.

“We si Mwantumu au macho yangu yana makengeza?” alizungumza Endrus kwa msisitizo.

“We kaka vipi! Mbona mimi sikufahamu?” nikajifanya kuzungumza kwa mshangao zaidi.

“Mwantumu leo hunijui mmi! Wewe mwanamke kweli leo hunifahamu wewe?” Endru akazidi kuhoji kwa msisitizo baada ya kuona nimemkana hadharani.

“Kama mtu hakufahamu kwani lazima?” Fadhili alihoji kwa ile sauti yake kavu iliyokuwa imejaa mshangao lakini kwa wakati huo aliiyotoka kwa kukoroma kidogo.

“Huyu ni mpenzi wangu Brother, inakuwaje aseme hanifahamu” Endru alizungumza kwa kulalama.

“Nani Mpenzi wako! Unafahamu unachokizungumza dogo?” Fadhili akahoji huku akionekana kujaa upepo ndani ya kifua chake kutokana na hasira baada ya kusikia maneno ya mapenzi kutoka kwa kijana yule.

“We Malaya unanikana leo kwasababu upo na huyu kimba!” Jamani nyie Endru alizungumza maneno machachu, heti Fadhili ni kinyesi. Jamani nyie matusi mengine ya bei rahisi Dah!

“Unasemaje wewe!” Fadhili akahoji kwa jazba baada ya kusikia kauli ile kutoka kwa Endru.

“Ndio kimba tu kwani utanifanya nini?” jamani Jamni! Endru alizidi kumtibua Fadhili wa watu ambaye mwenyewe alikuwa na hasira zake zilizotokana na kile kitendo cha wanaume wawili kukutwa chumbani mwangu katika mazingira ya kutatanisha.

Nakwambia pale nilipokuwa nimeketi nikahisi kaubaridi kakalii kakipenya kwenye mishipa yangu ya damu. Nikatamani dunia igharikishwe na kuumbwa upya ili aibu ile isiendelee kunikuta mimi.



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG