Search This Blog

Monday, January 24, 2022

LOVE INTERVIEW - 2

   

Chombezo : Love Interview

Sehemu Ya Pili (2)



Stanis akashangaa sana na kukubali kufanya ujinga wangu, tena najua alifurahi kimoyomoyo maana nitamuachia jumba langu lote akila kiyoyozi wakati mimi naenda kuvaana na mbu, mende, kunguni na viroboto kwenye gheto lake kwa kipindi kisichojulikana.

Akakubali, lakini sharti langu lilimtaka awe msiri mno kiasi kwamba hakuna mtu atakayejua chochote.

“Kwahiyo naanzaje kujakuja kwako,” aliniuliza. Hapo ndiyo nikamwambia asiwe na wasiwasi cha msingi, ahakikishe anachukua vitu vyake vya muhimu kule kwake, afue mashuka na kusafisha chumba chake, nikamuonya asiharibu vitu vyangu hasa tivii yangu ya Flat kubwa kama dirisha. Na wala asiguse magari yangu.

“okey sawa ila John wewe ni rafiki yangu wa muda mrefu sana, lakini pamoja na jinsi ninavyokujua kwa vyote hivyo ulivyokuwa navyo, lakini leo ndiyo nahitimisha kuwa kati ya watu machizi duniani wewe ni namba moja, kweli upo siriazi unataka kufanya hivi?” alisema Stanis akiwa haamini.

“Yah, nipo siriazi mbaba, inabidi tu nioe na sina njia nyingine zaidi ya kufanya hivi,” nilisema akanielewa basi tukapanga siku ya mkakati.

Basi siku ya siku nilianza kurudi kutoka kazini nikijifanya nimechanganyikiwa hata kula nilishindwa japo chakula kilikuwa kizuri mno, nilianza kusikia harufu ya kitu cha wali njegere aisee nikajikaza na kuigiza nimechanganyikiwa ili mradi tu Shose na mlinzi wanione.

“kaka vipi mbona upo hivyo,” aliniuliza Shose kwa hofu.


LOVE INTERVIEW 14

“acha tu!” wakati huo nikatoka nje na kujifanya nazungukazunguka bila mpango nikisonya na kupiga ngumi ukutani, mlinzi wangu mzee Masingili akanitazama kwa wasiwasi, nadhani alikuwa akipiga hesabu yake ya mwisho wa mwezi maana alishaona kimenuka tena jinsi januari ilivyo kuwa ndefu, nadhani alijua nina tatizo na pengine alikuwa akimuomba Mungu wake kuwa tatizo langu lisiwe linahusiana na mshahara wake.

Basi nikaingia ndani nikiwa na uhakika meseji imefika kwa wahusika.

“Kaka mbona upo hivi tatizo nini?” alizidi kuniuliza Shose.

“Usijali nitakwambia, muite Mlinzi uje naye kwanza,” niliposema vile harakaharaka Shose alitoka nje upesi, wakati huo nikaingia ndani nakutoa noti kadhaa nikakaa kwenye meza na kuanza kuzihesabu.

Mlinzi mzee Masingili aliingia akiwa ameongozana na Shoshe, kwa heshima akivua mabuti yake na kupitiliza sura yake ikizidi kuonesha wasiwasi, lakini alipoona nahesabu fedha kidogo roho yake nadhani ilipoa, Shose naye alikuwa akihofia mno niliweza kumuona tu kwa macho yake.

“jamani, nimewaita kwa sababu kuna tatizo limetokea kazini, sasa limenigusa hata mimi mwenyewe, sina jinsi.” Nilimeza mate na kukumbuka maneno mengine ya kusema maana nilikuwa nimeshayafanyia mazoezi kwa muda mrefu mno.

“mali zangu zote zinapigwa mnada kesho kutokana na madeni yangu benki, kwa hiyo nimeamua kuchukua fedha zangu zote za mwisho niwalipe mishahara yenu na fedha kidogo ya nauli ili mrudi makwenu, nashukuru tumefanya kazi vizuri pamoja kwa kipindi kirefu, naomba msihuzunike,” nilimaliza scene ya mwisho ya huzuni ya igizo langu.

Mlinzi akachukua kitita chake na kukihesabu vizuri akaona kimetimia na niongeza, akanipa pole, akashukuru na kurudi zake kizimbani akilinda vya mwishomwisho, lakini Shose hakunyanyua mikono wala mguu na hakuondoka pale nilipokuwa nimekaa mimi. Machozi yalikuwa yakimbubujika kama amefiwa.

“Jamani kaka kwa hiyo utaenda wapi?” aliniuliza Shose.

“hata sijui hapa nafikiria kwenda kupanga chumba uswahilini, nikajipange upya.”

“basi kaka chukua na hela hizi zikusaidie kulipia kodi,” alisema Shose na kunikabidhi zile hela nilizopanga kumpatia.

Itaendelea

LOVE INTERVIEW 15

Nilishangaa mno. Nikazirudisha zile hela kwake.

“Sikia Shose, hizi hela hakikisha unarudi kijiji kwenu, zikusaidie kujiendesha kimaisha, mimi nitapambana. siku moja naamini nitafanikiwa tena na nitakutafuta maana sijui nitaishije bila chakula chako,” nilisema maneno hayo kutoka moyoni kabisa, maana kweli nilitamani hata kwenye huo upumbavu wangu niondoke naye kwenda kwenye hilo gheto la Stanis kesho ili awe ananipikia chakula chake na huko.

Lakini hapana, watu wangepata la kusema maana tangu lini mwanaume rijali kama mimi akaishi na msichana chumba kimoja. Pia kuwa na Shose karibu kutaharibu mipango yangu ya interview hivyo bora nimuache tu aende kwao kwanza.

Wakati naongea na Shose ndiyo nikakumbuka simu yangu ambayo namba yake ndiyo niliisambaza kwa makatekista nilikuwa nimeiacha kwenye gari na sidhani kama ilikuwa hata na chaji. Nikaikimbilia na kwenda kuichaji maana ilikuwa imezima kabisa, tena usishangae ilikuwa hivyo kwa siku mbili nzima.

Cha kushangaza wakati huo wote, Shose alikuwa bado anaonekana na huzuni mno tena akiniangalia kila nikipita na kurudi kutoka chumbani kwangu. Mkono wake akiwa ameuweka mashavuni, weupe wake ukiwa mwekundu kwa mawazo.

“Shose si nimekwambia, usijali lakini..” niliongea huku nikijipakulia chakula na kula kwa fujo. Nikamsifia anavyopika vizuri na kadhalika, nikajirusha kwenye kochi na kuweka kipindi cha Shilawadu, nikacheka waliponichekesha na kusikiliza kwa makini walipoleta ubuyu mpya.

“Hivi kaka unawezaje kuwa na matatizo kiasi hicho halafu ukawa unachukulia tu kawaidakawaida,” aliuliza Shose nikajishtukia mama weee! nimeharibu maigizo. Harakaharaka nikamjaza kichwani @gabozigamba1 na @daudimichael_duma maana ni wataalamu wa scene za huzuni nikayavuta machozi lakini hayakutoka, aghh basi nikamvuta Chakoree.

Nikaongea kwa hisia halafu kila neno nikalipa nafasi.

“Sikia.. Shose..jua.. maisha ni kupanda na kushuka, sitakiwi kukata tamaa, siwezi kuendekeza majonzi yangu yanifanye nipoteze focus kwenye maisha.. halafu mimi ni mwanaume kulia kutanipeleka wapi sasa? Niliongea maneno ambayo hata sijui yametoka vizuri au lah.

“mh ila kweli, maana hata mimi baba yangu haliagi akiumizwa, anaishia kuumia tu ndani kwa ndani, lakini kwa nje anacheka tu,” alisema Shose.


LOVE INTERVIEW 16

Akaja pale nilipokaa akakaa upande mmoja wa kochi bado akionekana na mawazo mno juu yangu maana aliniangalia mpaka nikajishtukia.

Sijui aliwaza nini, basi akaanza kulia tena, katika kumbembeleza nikamvuta kifuani kwangu nikawa nampetipeti mgongoni taratibu. Basi akalia hadi akapitiwa na usingizi akiwa kifuani kwangu tena alilala akiwa amenyonya kidole chake nadhani mchezo huo wakitoto alikua nao hadi ukubwani.

Basi saa zilipoenda, nikambeba taratibu na kumpeleka chumbani kwake, mh alikuwa mzito kumbe, halafu hapo ndiyo niliweza kumuona vizuri miguu yake ya bia, ngozi yake laini, macho yake ya kusinzia kope zake zilivyokuwa zimejishepu kama za kuchora. Nikamsikia jinsi alivyokuwa akihema taratibu nikamtazama midomo yake minene ilivyokolea rangi nyekundu ya asili. Niliweza kuona kila kitu kwa ukaribu, Shose alikuwa ua livutialo macho. Abarikiwe mwanaume atakayemuoa huyu binti. Niliwaza.

Nikafungua mlango wa chumba chake kuupush na mguu nikamuingiza hadi kitandani na kumlaza taratibu ili asishtuke, nikamfunika na shuka na kuzima taa yake.

Nilipomaliza nilikumbuka hivyo nilionaga kwenye muvi za kizungu mtoto wa stelingi alisinzia kwenye kiti, basi yeye akambeba hadi chumbani na kumlaza kama mimi nilivyomfanyia Shose.

Lakini kibongobongo sasa, mtoto akilala tu kwenye kochi badala ya kitandani utasikia; “we **mamayo hebu amka kalale kitandani kabla sijakufumua!” na kama siyo hivyo basi mikofi ya kufa mtu itasikika.

Tena tuache watoto, vipi kwa wapenzi,inakuwaje unambeba mpenzi wako amesinzia na unaenda kumlaza chumbani. Niliwaza na kuona ni vema, nikaweka mawazo hayo moyoni mwangu nikitarajia baada ya interview yangu nitampata mpenzi wangu mzurimzuri wa kumbeba kama mwanasesele akisinzia kwenye kochi.

Mara ghafla narudi sebuleni nikasikia simu yangu ndogo ile niliyokuwa nikichaji ikiita chumbani, nikaiwahi na kuona namba ngeni nikaipokea.

“Hallow Tumsifu Yesu Kristu!” ilikuwa sauti ya kike iliyotiliwa vinogilishi haswaa. Kabla ya kusema neno nafsi yangu ikaniambia; Mpigaji huyu hana lolote! halafu sasa ndiyo nikakumbuka kumbe ni ile namba niliyoigawa kwa makatekista kanisani. He! ndiyo kimeanza sasa kufanya kazi.

Itaendelea..

LOVE INTERVIEW 17

“Hallow aah ameen!” niliitikia kihuni nikiwa nimesahau kabisa hata kuitikiana Kikatoliki kumbe mtu akisema: Tumsifu Yesu Kristu wanaitikia; Milele amina, maana ilinibidi kwenda kufanyia utafiti mara tu baada ya kuongea na huyu mdada.

“wewe ni Mr John?”

“ndiyo ni mimi.”

“ooh of coz, amm.. mimi naitwa Joana, nasali kanisa Katoliki la St Joseph. aammm mh ningependa kukufahamu if you don mind, sijui tunaweza kumeet wapi?” ilisema sauti hiyo, moja kwa moja nikampima kwenye uzani vyenye anajishongondoa nikaona ni jamii ya wale mademu fekiii kiasi kwamba wanajifanya wanaigiza u-rihanna au u-beyonce to the maximum wakati kwao wamechalalaa ile mbaya.

Halafu unakuta wanavaaga mawigi makubwaa halafu ndani wana kipilipili. Wana makucha marefuuu hawapiki wala hawafui, kazi yao kudanga tu mjini. Kama haitoshi utakuta mbayaa halafu mwenyewe anajiona mzuri kinomaa kiasi kwamba unaweza jiuliza, hivi hajioni kwenye kioo au anajichetua tu.

Ngoja sijamaliza; tena mademu wa hivi utakuta kwenye mitandao ndiyo wale wanaongezea majina yao maneno kama vile: Delicious,Baby, deshideshi mtamu Pretty, Sweet, Cute, Princess au Queen. Wanajifanya AKA nyingii, hawataki kukubali hali halisi; kama jina lako Zinduna, wewe Zinduna tu. Hiyo Cutie Zee imetoka wapi?

Halafu kwa taarifa yenu sisi wanaume ndiyo tuna kibali cha kuwaita wazuri, sasa wewe unajiitaje mzuri kihivyo wakati kwenye gredi zetu sisi tunakuona nyonzo tu.

Sasa huyu kaingia kwenye mingo zangu ngoja nimnyooshe. Nikamjibu: “Aah kesho tunaweza kuonana sehemu yoyote utakayohitaji.”

“Owkey basi I will come to your place, kwani unaishi wapi?” aliuliza huyo Joana, nikajiongeza kuwa siku hizi mademu wengi wanakimbilia kutaka kujua kwako ili mradi tu wakupime unauwezo wa kumuoa?

Maana enzi za Kikwete wenzangu na mimi tulikuwa tukiishia gesti tu, unakuta demu una mwaka naye lakini kwako hapajui na hajali. Lakini sasa hivi enzi za huyu Msukuma; mwe! Msichana kabla hujakupa jibu anataka kupajua kwako na ukijitela tu kwamba kwako kuzuri utakuja kushtukia amehamia.

LOVE INTERVIEW 18

Utashangaa tu: mimba, ndoa, mtoto na kwa wale wanawake wasiobahatika unakuta mchakato unaruka hatua moja, yaani mara mimba, mtoto, ndoa baadaye au hakuna tena maana kuna kuachana kwa kuchokana hapo mbeleni halafu kidume kinaoa demu mpyaa halafu kinamsusa mtoto kwa kigezo, cha ooh akikua atamtafuta mwenyewe baba yake.

Na huyu najua naye alikuwa akitaka kunipima hivyo nikamwambia laivu; “Mimi naishi Mbagala Charambe Majimatitu baada ya kwa Mbiku, Transfoma, mahakama ya simu, karibia na kwa mzee Maugado almaarufu barabara ya Maputo Gest House,”nilisema, akaguna maana nadhani aliona majina yote machachumachachu, nikaona sawasawa ili kama alidhani nitakuwa kibosile basi akajipange upya.

“mh, Mbagala! mbona mbali hivyo, au umejenga?” aliniuliza Joanna sasa nikagundua vile viswahili vyake vya kung’ata na viinglishi vimeisha ghafla.

“Maisha yenyewe yapo wapi Joanna? Nimepanga, chumba changu kimoja basi mie mwenyewe akaa!” nilijibu, nikashtukia simu imekatwa.

Nikampigia pengine aliishiwa salio au imezima chaji, ikaita kidogo halafu nikaona call ended.

Amekata, Nikacheka na kujisemea kimoyomoyo, nyoo ulidhani kusali St Joseph ndiyo mie kibopa si ndiyo?

Wakati nakata ile simu nikaona meseji kama mbili hivi mpya, zikionekana kuanza kwa mtindo uleule wa tumsifu Yesu Kristu.

Nikaingalia moja ilijitambulisha kwa jina la Theckla baada ya ile salamu kuona sijajibu akaandika, “Mambo?”. Mwingine anaitwa Marietha alikuwa ameandika: “Mzima?”

Nikajibu, Mzima kwa namba zote, nikaangalia saa ilikuwa saa tano usiku nikajua pengine watakuwa wamelala maana wakati huo hata mimi mwenyewe nilikuwa najiandaa kulala. Mara meseji ikaingia kutoka kwa Marietha: “kweli unahitaji mchumba?”

Nikajibu: “ndiyo?”

“vigezo vyake aweje?”

“awe mchamungu, ajue kupika, anipende kwa mazingira yoyote niliyokuwa nayo?”

“ooh! Mimi naweza kuwa mchumba unayemtaka, lakini naomba nikuulize kitu?”

“uliza tu”

“una miaka mingapi?”

“35.”

“hauna mtoto na haujawahi kuoa?”

“ndiyo, Wewe je?”

“nina miaka 23 nina mtoto ila sijaolewa,” alipoandika hivyo tu, nikafuta namba yake nikadelete. format. block. black list. call reject. haitoshi nikaingia playstore nikadownload message block.

Itaendelea..

LOVE INTERVIEW 19

Sasa nikashusha pumzi kwanza. Najua mtaniona mkatili, lakini kiukweli ni kwamba wanaume wengi hujivunia wanawake wao wakiwa wanajua wao ndiyo wa kwanza na tena ndiyo maana ile dhana ya kuoa bikra inapendwa sana duniani kote.

Lakini sasa wanaume tumekubali kuwa kumpata mwanamke mwenye bikra yake ni ngumu kwa dunia ya sasa hivi kwa sababu wanaume wenyewe ndiyo tunajifanya hatutaki kutunza miti ikue tuvune na kuipanda mingine, tunavuna tu. Matokeo yake ndiyo haya mabikra hakuna na inatukost sisi wenyewe wakati wa kuoa.

Okey sawa hauna bikra, ndiyo nitakuoa kwa vile ni jambo la siri ndugu na jamaa hata nikiwaongopea kuwa mimi ndiyo wa kwanza kukutoa bikra inaswihi na hakuna atakayetaka ushahidi, lakini kama una mtoto tena wa mwanaume mwenzangu. Inakuwa kama alama isemayo; we boya lea kidume mwenzako nimepitaga kabla yako.

Maana yake pia ndugu na jamaa zangu wataambizana: analea mtoto wa mwanaume mwenzake. Au basi na mimi ningekuwa na mtoto wa nje kidogo ingekuwa afadhali.

Hata sibishani na nyie mliooa wake wenye watoto wasio wenu, bwana awe nanyi maana upendo wenu ni mkubwa mno, wake zenu wawape yote.

Lakini hata hivyo nikafikiria kidogo na kuona mh naweza nikajishaua kuwa sitaki kuoa mwanamke mwenye mtoto wa nje, halafu nikaja kuoa kimwali na kuzaa naye nikiwa na uhakika mtoto wangu, kumbe nikabambikiwa mtoto, nikijua maumivu yake yakawa mara mbili.

Agh! nitapima DNA ya kila mtoto nitakayemzaa, lakini sitaki kuoa mwanamke mwenye mtoto. Basi kabla sijalala vizuri, nikasikia hodi mlangoni kwangu.

Nikawasha taa na kuvaa shuka nikasogea mlangoni. Nilipofungua nikamuona Shose akionekana kama ameona mzimu. Akaniambia anaogopa kulala peke yake chumbani kwake kwa sababu ameota ndoto mbaya mno.

“Pole mdogo wangu,” nilimuonea huruma maana hiyo ndoto ilionekana mbaya kweli kiasi kwamba machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni.


LOVE INTERVIEW 20

Nikamvutia chumbani kwangu na kumwambia alale kitandani na mimi nikawa nimepanga kulala kwenye kochi, lakini nikajiuliza kwani nahofia nini kulala na Shose kitandani? kwani nitafanya nini wakati ni mdogo wangu? Nikaona nikilala kwenye kiti, ndiyo nitakuwa naonekana na fikra chafu.

Basi nikaenda kulala pembeni yake yeye akiwa na night dress yake nyepesi.

Nikamuuliza: “uliota nini?”

Shose akanigeukia na kuniambia kwa sauti ya kitotototo: “nimeota umenikimbia.”

“Ndiyo hivyo tu?” nilimuuliza.

“ukiwa umenikimbia, nikawa nakulilia barabarani, lakini haukutaka hata kuja kunichukua..” alinijibu.

“mh! haya lala.. usiwe na wasiwasi.” Nilisema nikiwa najua ndiyo kitakachotokea kesho yake akiendelea kuning’ang’ania.

Shose kama kawaida yake akaingiza kidole chake mdomoni na kukinyonya akapitiwa na usingizi kabisa. Vile vipumzi vyake vikinitulia kifuani kwangu na hewa ya ujotoujoto ulionisisimua.

Nikalala zangu unono hadi asubuhi. Shose akawa wa kwanza kuamka akaniandalia chai, mikate na mayai na kuniwekea vitu vyangu vizuri kwenye mabegi.

Nilipoamka nikakuta chai nikanywa na kuanza kumtania, Shose kuhusu alivyosinzia kwenye kochi jana na nilivyombeba na kumpeleka chumbani kwake.

Lakini tofauti na siku zote, hakutabasamu wala kucheka. Akaniambia; “kaka usiniache, utakapoenda na mimi nitaenda hukohuko. Tutaenda wote.” alisema nikashtuka.

“Hapana, sitaki kwenda na wewe popote, wewe rudi tu nyumbani mimi ninapoenda hapakufai,” nilijitahidi kumkataza lakini alining’ang’ania ile mbaya. Nikajisemea kimoyomoyo ile ndoto yako itatimia tu.

Basi wakati huohuo kama tulivyopanga na Stanis, nikaona mlinzi anakuja na kunitaarifu kuwa kuna gari getini. Nikaenda na kuona ni Stanis, akaniminyia jicho na kuingia kwa mbwembwe akiwa na makufuli na briefcase.

“jamani, naombeni mtoke nje, nyumba na mali zote humu ndani ni za kwangu tangu hivi sasa, nimenunua kupitia mnada wa benki, natumai wewe ni Mr John,” aliongea Stanis akinionesha karatasi fulani.

Nikaichukua na kujifanya naisomasoma, mlinzi alipoona hivyo akaingia kwenye kibanda chake na kuchukua kibegi chake akaondoka. Soshe akaingia chumbani kwake na kuchukua begi lake na kuweka sebuleni akiunganisha na mabegi yangu akionekana kabisa amedhamilia ninapoenda na yeye anaenda.




“We fala weka sura ya huzuni!” alinong’ona Stanis, nilikuwa nimejisahau maana nilijikuta nikicheka kwa jinsi Stanis alivyojifanya siriazi halafu karatasi yenyewe aliyonionesha ilinifurahisha maana ilikuwa ni ya matokeo ya kidato cha nne ya shule ya Sekondari Tandahimba huko Mtwara na haikuwa na uhusiano wowote na mnada wala benki.

“Tokeni haraka kabla sijaita polisi,” alisema Stanis nikabeba baadhi ya mabegi yangu na Shose akabeba yakena kunisaidia begi langu moja hadi nje, nikasimamisha bajaji na kupakia mizigo ndani, lakini bado Shose alikuwa akiniganda.

“We shose mbona unaleta mzaha! Nenda kwenu!” ilibidi nikorome na kumtaka dereva bajaji aondoke.

Shose akabaki analia pale barabarani, huku akiwa ameweka mikono yake kichwani, kama vile ile ndoto yake aliyonisimulia jana usiku.

Nikajisemea kimoyomoyo huyu mtoto chizi nini? dereva akakanyaga mafuta nikatazama kupitia kidirisha cha nyuma nikamuona, akiwa amekaa kabisa juu ya begi lake kama mfiwa. Nikajisikia vibaya lakini sikujali maana ninaloenda kulikamilisha ni kubwa zaidi ya huo utoto wa Shose.

Tukakunja kona na vilima hadi kufika Mbagala ilikuwa mchana tena, tukaingia majimatitu na kuitafuta maskani ya Stanis. Nikamlipa dereva bajaji na kufungua mlango, ile naingia tu ndani kwanza nilijikuta napiga chafya maana Stanis hakufanya chochote, hakufua wala kufagia. Kwa kifupi alinifanyia uhuni.

Nikakaa kwanza kwenye kiti na kupiga hesabu, Mh kweli mie ni chizi, kweli naweza kuishi humu? Au nirudi nyumbani? Nilijiuliza yote lakini kwa kuwa maji niliyavulia nguo ngoja niyaoge.

Nilichofanya kwanza nikampigia simu Stanis na kumkoromea. Akajifanya eti alikuwa haamini kama ningefanya upuuzi wangu kweli hivyo hakufanya chochote.

“sikia, kwanza uwe unalala kile chumba cha hausigeli, sitaki kabisa uingie chumbani kwangu na mademu humo noo!” nilimchana Stanis.

Nikafungua kifriji chake na kuona kuna bia tu, mh! Nikaangalia pembeni nikaona kuna jiko la gesi, vyombo vichafu, yaani hadi kero. Nikaamua nitembee kwenye caféteria yoyote ili nikapate japo chakula cha mchana.


LOVE INTERVIEW 22

Nikafika kwenye mgahawa mmoja pale majimatitu Stendi, walikuwa na menu ya vyakula vingi nikaagiza wali kuku wa kienyeji, lakini cha ajabu hadi analetwa pale mezani hakuwa hata ukinukia.

Kwa mara ya kwanza nikamkumbuka Shose. Nikala sababu ya njaa tu, nikalipa na kurudi zangu gheto. Nikampigia simu daktari wa mama, Dokta Frank akapokea na kunielezea hali ya mama kuwa bado yupo chini ya uangalizi, nikaongea naye kupitia simu ya Dokta mama alionekana kufurahi kunisikia.

Nilipomaliza nikapiga hesabu nikaona kukaa humo ndani siwezi, maana ilifikia hatua hadi vyombo vilianza kutoa harufu. Nikawaza hapo angekuwepo Shose angeweza kubadilisha gheto na kuwa chumba ndani ya dakika chache tu.

Lakini uzuri hiyo ilikuwa Mbagala kila kitu mbele ya hela kinawezekana nikatoka nje na kwenda kuongea na baba mwenye nyumba wa Stanis uzuri nilikuwa namjua na alikuwa akiniona mara kwa mara nikija na kuondoka hapo kwake.

“kijana, upoo?”

“nipo mzee wangu,” nilimjibu na kwa adabu nikamuelezea kuwa nitakuwepo hapo nyumbani kwa muda fulani wakati Stanis hayupo. Lakini kikubwa nikamuomba anipatie kijana wa kusafisha chumbani kwa ujira wa shilingi elfu kumi.

Palepale mzee akamuita binti yake, Zainabu na kumtaka asafishe ndani kwangu.

“sasa baba hiyo hela nipe mimi.” Alisema yule mzee nikampa. Kisha nikaongozana na Zainabu hadi vyumba vya uani ambapo ndiyo kuna chumba cha Stanis.

Yule dada akaangalia na kuondoka akarudi na maji dekio na akatoa vyombo nje na kuanza kudeki mle ndani. Wakati huo nikatoka nje ili kumpisha.

“He! Kaka mbona unaondoka,” alisema Zainabu akiwa ameinama ileile, maana naye alikuwa siyo wa mchezomchezo alikuwa ni chura maji, ila sura sasa ndiyo n’katie kichwa (msemo wa wanaume wakimaanisha sura mbaya lakini shepu nzuri).

Nikakumbuka wanawake wa hivyo ndiyo kwenye instagram au fb ndiyo walianzisha kupost picha wametubinulia matako mtindo wa nangoja ageuke.wanawake wengine nao wakaiga, yaani nikiwatazamaga kama wanasema; “nyie wanaume si mnatakaga huku nyuma, na mimi ninapo njooni mnitongoze.” Itaendelea..


LOVE INTERVIEW 23

Sidanganyi, na kweli wanaume hatulazi damu twawatongoza, twa-comment mno na kuwasifia, tena twa-like sana picha zao, ingawa katika grupu la mchakato wa kuoa, wanawake wa hivi tunawatoa kabisa kundini.

Ndiyo maana Stanis anasemaga, kuna wasichana wa aina mbili kwa kuwatazama tu, kuna demu wa kuzugia na Wife material.

Demu wa kuzugia atapenda sana usasa, kuhudumiwa, kupenda kuangaliwa na umaridadi, bila kujali maisha yake ya baadaye hawana malengo na ufahamu wao kwenye maisha ni mdogo. Wengi wanakuwaga wazuri wa mtazamo wa nje na hata kama wabaya watajiongezea makorokoro wawe wazuri, hapo watajichubua, kujitoga heleni sikio zima, kujichora tatoo, kuvaa viguo-laana ili mradi tu atazamwe na asifiwe kuwa amefanana na @wemasepetu.

Wife material, utaona wengi wa kimya, wana uzuri wa kujificha, mtandaoni wanaangalia tu umbeya na kusoma hadithi na kuridhika, hawanaga likes wala followers wengi, hawajibinui wala kupiga picha wakiwa wamebetua miguu kama imechonjoka. Hawaonesha matiti nusu, wala mpasuo hadi kiunoni, wala hawapost video wanakata viuno nyimbo ya @DiamondPlatnumz mtandaoni, hapana. Nawapenda ma-wife material wote.

“Yaani nilikuwa nakupisha ili udeki uzuri,” nilijibaraguza nikimwambia Zainabu.

“Aku nataka uwe hapahapa, ili tupige stori,” alisema basi nikachukua kisturi na kufungua mlango na kukaa mlangoni kabisa ili tuongee vizuri.

“haya tuongee.” Nilisema Zainabu akacheka huku akiendelea kudeki.

“Hivi wewe ndiye rafiki yake Stanis uliyekuwa ukijaga hapa na gari?” alisema Zai.

“Ndiyo ni mimi.”

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG