Chombezo : Joy, Joyce
Sehemu Ya Pili (2)
“Nini, Ujue unanichanganya! Ngoja nikamuite Joy ndani.” alihamaki Chriss jambo lililomfanya Joy amzuie Chriss akimuonya kuwa huyo anayeenda kumuita si mwingine bali ni Joyce, hivyo asubiri mpaka atakapomhadithia historia nzima.
Basi Joy akaanza kuelezea kama alivyonielezea mimi kuhusu familia yao. Chriss akamtazama Joy na kumwambia: “kama wewe ni Joy kweli nikumbushe tulikutana wapi mara ya kwanza,”
“UDOM,” alijibu Joy tena kwa ukakamavu.
“nitajie namba yangu ya siri ya Tigopesa,”
“mh! Sasa Chriss maswali gani hayo?”
“nitajie namba ya siri ya Tigopesa maana Joy wangu mimi anajua namba yangu.”
“aah..mh!” alianza kubabaika Joy.
“wewe ndiye Joyce siyo Joy wangu!” alisema Chriss kwa hasira na kurudi ndani kwake. Wakati huo msichana niliyeamini kuwa ni Joy ambaye alikuwa mbele yangu akanitazama kwa aibu na kukimbia, kumbe yeye ndiye alikuwa ni Joyce siyo Joy.
Nilicheka moyoni baada ya kugundua kuwa hata mimi alinidanganya kwa zile porojo zake za tangu jana, nikafurahi maana kama nitaandika basi stori hii itakuwa tamu balaa.
Sasa nikaamua kurudi kwa Chriss ambaye alidai kuwa Joy alikuwa amemwacha ndani ili nijionee kwa macho yangu, basi kwa kuwa hapa kuwa mbali na pale tuliposimama nikapiga hatua. Nikawakuta kumbe nao walikuwa wakitoka na kuja kule nilipokuwa mimi.
“Yupo wapi yule mwanamke uliyekuja naye!?” aliongea kwa hasira Chriss na kunitaka nimuoneshe alipo Joyce. “huyu ndiye kaja naye yupo wapi?” alizidi kufoka Chriss ikabidi Joy amtulize na kumwambia kuwa ananifahamu.
Ikabidi sasa tutulie naye chini ili kumuelezea kila kitu kilivyo. Kwangu mimi nikaanza kwa kujitambulisha na kuelezea jinsi Joyce alivyokuja kwangu kama Joy na kunitaka nimsaidie.
Kikao kiliisha kwa Joy kuomba msamaha kwa kutomwambia mpenzi wake kuhusu historia ambayo ilikuwepo kwenye familia yao ambayo ilikuwa ni ileile aliyotusimulia Joyce isipokuwa tofauti yake tu ni kwamba Joyce alituwahi kwa kujifanya ni Joy.
“kitu kinachonishangaza mimi ni kwamba kama ametoka jela hivi karibuni alijuaje mnapoishi? na kuhusu Chriss na wewe?” niliuliza huku nikivuta kumbukumbu jinsi Chriss alivyomuuliza Joyce sehemu waliyoonana na yeye akakimbilia tu kusema UDOM.
Kwa swali langu nikamuona Joy akajishika kichwa; “Haa! Atakuwa Kachukua dayari yangu; mama yangu nimeandika mambo mengi ya binafsi na mengine ya muhimu mno, Mungu wangu!” alihuzunika Joy nikawa najiuliza nini alichokiandika Joy kwenye hiyo dayari mpaka ashtuke hivyo. Nikaona hili jambo la kulifuatilia ili hadithi yangu ishibe.
“Kwani hiyo dayari wewe uliiweka wapi?” niliuliza.
“si ilikuwa kule nyumbani na vitu vyangu vya chuo, atakuwa alienda tu kule jamani!” alizidi kulalama Joy.
Nikawaacha wao wakibembelezana na mimi nikarudi zangu ofisini, nikaanza kuandika kisa hicho haraka, hata hadithi ya KISASI CHA KAPTENI TINONKO nikaweka pending kwanza.
Nashukuru Mungu ninakuwa na uwezo wa kuchapa haraka mno kwa vidole vyote, kiasi kwamba hata bosi wangu japo kuwa anajua ninatumia muda wa kazi kuandika hadithi, hanisumbui kwa sababu kazi zake zote namaliza haraka kuliko mfanyakazi yoyote na mbaya zaidi yeye mwenyewe ni mshabiki mno wa hadithi zangu hasa hadithi ya CHURA, wengi wenu mnaikumbuka hii.
Nilimaliza na kufurahia jinsi mapacha wanavyoweza kusababisha mgongano kwa marafiki na wapenzi zao. Nikacheka lakini bado akili yangu ikaganda kuhusu nini kilichomo kwenye dayari ya Joy?
Wiki ikapita nikashangaa kumuona Joy anakuja ofisini kwetu akilia na kuniambia kuwa ameachwa na Chriss.
“Kwanza samahani siwezi kukuamini kuwa wewe ni Joy au Joyce, tafadhali naomba niambie jana tukiwa na Chriss tulikaa wapi tulivyokuwa tunakula chakula?” nilimuuliza Joy pindi tu alipokuja ofisini ili nisije kujichanganya kwa kuongea na Joy wakati kumbe ni Joyce.
“Chaxy Chande, hatukula chochote,” alijibu Joy nikagundua alikuwa sahihi na Joy mtu wa kulialia si kama Joyce.
Baadaye akaanza kuniambia kuwa sababu kubwa ya Chriss na yeye kutengana ni baada ya Joyce kumtumia Chriss picha whatsapp ya kipande cha kurasa cha kwenye dayari yake alichokuwa ameandika mapenzi yake kwa Damian.
“Nilijua tu haya yatatokea na kweli Joyce ameenda kufanya kilekile kwa hakika sitakuja kumsamehe, angalia sasa ndoa yangu ndiyo basi tena,” alisema Joy kwa uchungu mno.
“kwani ujumbe gani hasa uliokuwa kwenye hiyo dayari?” niliuliza kwa shauku.
“Sijui nilikuwa na akili gani, lakini nilikuwa nikiwalinganisha kati ya Chriss na Damian kimapenzi yaani jinsi ninavyowapenda.” Aliongea Joy akiwa analia.
“hiyo ndiyo sababu ya Chriss kuachana kabisa na wewe!?” niliuliza nikiwa nimeshangaa kwanini Chriss akamuacha Joy sababu ikiwa ni kufananishwa tu eti na Damian.
“Tatizo ni kwamba, nilikuwa nimeandika kuwa kama Damian atakuja kuniomba msamaha hata nikiwa nimeolewa nitakuwa tayari kumsaliti mume wangu kwa ajili yake,” alisema Joy.
“Mh, hilo ni tatizo, lakini uliyoyaandika ni ya kweli?” niliuliza nikiwa nimeanza kuhisi Joy naye ana tatizo pia, atawezaje kuandika kitu kama hicho!
“Yaani Chaxy Chande kitu ambacho hauelewi ni kwamba, nilikuwa nimeandika tu hayo mambo zamani kipindi hicho hata sijamvulia chupi Chriss,” alisema Joy nikajikuta nikizidi kumuonea huruma.
“Lakini Chriss mwenyewe umemwambia?” “nimemwambia lakini ni mkali sana na kwa mara ya kwanza amenipiga sana leo, ukiachilia yote Damian mwenyewe yupo nchini na siku hizi amekuwa akitutembelea pale nyumbani, sasa na hayo maneno nadhani Chriss yamemchanganya,” alisema Joy.
“nini! Amekujaje?” nilishangaa.
“Amekuja kwa ajili ya harusi yetu na Chriss. Najua Chriss alipata hasira baada ya kuhisi huenda bado nampenda Damian na inawezekana nikafanya naye niliyoyaandika, tafadhali nisaidie Chaxy,” alilalamika Joy machozi yakimtiririka mno.
Mh! hata mimi nikaanza kuona ni kizungumkuti cha aina yake, yaani huyo Joyce alikuwa na akili ile mbaya maana alikuwa akitembea kwenye matukio vibaya mno. Sasa sijui alikuwa akimuumbua pacha wake kwa faida ipi.
“Joy, usilie kwanza unatakiwa kujua kitu gani kingine cha siri kilichopo kwenye dayari yako, ili ukiokoe kwanza. Lakini kwa wakati huu kwanini usingeenda nyumbani kwa shangazi yako ili umeuangalie kama Joyce yupo ili uchukue dayari yako?” nilitoa ushauri, nikashangaa Joy akiwa ameshika kichwa kwa mshtuko.
“mama yangu, Joyce atakuwa amenimaliza!”
“Kivipi?” “kuna email yangu na password, ooh kwenye mkoba kuna kadi yangu ya ATM, namba zangu za simu ikiwemo ya Damian na Chriss na watu wangu muhimu sana wakiwemo marafiki zangu wa chuo,” alisema Joy.
“Kwa email, nadhani cha msingi unaweza ukaibadilisha password hata sasa hivi, lakini kwa kadi ya ATM, mwenzako anaweza akaenda kutoa hata hela benki kama saini yako anaijua vizuri.
“Chaxy hebu ngoja mimi niende nyumbani kwanza, Joyce anaweza kuwa ameshafanya hayo mambo yote eee Mungu weee!” alisema Joy huku akitetemeka kwa kuchanganyikiwa.
Wakati huo ghafla nilipokea ujumbe kwenye simu yangu, ukiwa umeandikwa; “Mambo Chaxy Chande, soma meseji whatsapp nimekutumia sasa hivi. Mimi Joyce.”
Haraka nikawasha data na kusubiri meseji za whatsapp zilizotiririka kutoka sehemu mbalimbali nyingine zikiwa za wasomaji wangu wapendwa waliokuwa wakinipongeza kwa stori nzuri.
Baadaye nikapokea ujumbe kwa namba ileile ya mtu aliyejiita Joyce yaani pacha mbaya wa Joy, nikaifungua na kuona ni picha moja wapo. Nilipoidownload ilionekana ni picha ya kipande cha karatasi.
Nikaizoom na kuisoma vizuri, ilikuwa imeandikwa; “ningeweza kumpenda Chaxy Chande kwa sababu ni mpole, mkarimu, kijana kama mimi, lakini ameshawahiwa na Deborah, na wanaonekana na furaha wanayoitaka. Mungu nisaidie nimpate mwanaume kama huyu.” Kisha chini ya ile meseji ilikuwa imeambatana na viemojiemoji vya kimtu kikicheka.
Halafu baada tu ya kusoma ikaingia meseji kwa chini ikiwa imeandikwa; “Diary ya pacha wangu Joy. Imeandikwa Tarehe 22 Nov 2014. Imeonekana unapendwa kaka!”
Nikashangaa na kuona mh kumbe Joy alikuwa akinipenda na kuniheshimu kiasi hicho! Nikajiwazia maisha yangu na huyo Deborah ambaye Joy alimuona tunapendana sana, mh! angejua anavyonipasua kichwa hata asingesema.
“mh ina maana Joyce kweli anamfanyia hivi vitu ndugu yake?” nilijiuliza na kuona tatizo kubwa ambalo kama likiachwa linaweza kuleta maafa.
“Joyce, hivi nini faida ya kumharibia ndugu yako kiasi hicho?” niliutuma ujumbe huo nikaona umesomwa. Na sasa Joyce alikuwa anaandika.
“hahaa nitaendelea kupoteza furaha yake na kila kitu alichokivuna wakati mimi nikiteseka hadi tuwe sawa, na hakuna wa kunizuia,” aliandika Joyce.
“Joyce, fanya kila kitu lakini naomba mrudishie hata Chriss wake ili aolewe. Nakuomba.” Nilimuandikia meseji hiyo Joyce.
Lakini majibu yake yalikuwa ni picha tatu ambazo nilipozidownload alionekana mwanamke aidha Joy au Joyce akiwa amekaa kitandani utupu huku akiwa na mwanaume kitandani wote wakionekana sura zao.
Chini meseji ikaingia ikisema, “Kwa hizo picha sijui kama Chriss ataweza kumsamehe. Of coz huyo mwanaume ni Damian na huyo mwingine ni mimi, lakini unafikiri Chriss ataamini vipi kama huyo si mkewe mtarajiwa, kwa yale yote aliyoyaandika kwenye dayari yake!”
Mama yangu! nikajikuta nainua mikono na kushika kichwani.
“We Joyce usitume hizi picha sio vizuri, aisee!” niliandika haraka ujumbe huo.
“hahaaa nilishatuma muda mrefu sana, wewe unafikiri kwanini Chriss hamsamehi Joy?” Loh niliposoma ujumbe huo nilikuwa sasa nimeelewa sababu ya Chriss kupata ghadhabu hadi kufikia hatua ya kumpiga Joy.
Ikabidi nimpigie simu Joy haraka, nikapokelewa na kilio tena akidai kuwa anataka kujinyonga kwa kuwa hakuna cha muhimu ambacho anaweza kukifanya ili kuokoa ndoa yake.
Hata mimi nikachanganyikiwa na kuona hapo lazima nifanye chochote kumuwahi japo kuwa kwao ilikuwa ni Tabata na mimi ofisini ni Mwenge halafu ndiyo ilikuwa saa 10 jioni yaani bonge la foleniii.
Basi haraka nikaamua kupanda pikipiki na kibuku kumi changu cha ngama. nusu saa baadaye nikafanikiwa kufika hadi Tabata Chang’ombe kwa akina Joy.
Nikiwa na papara zangu, nikapitiliza ndani hadi sebuleni hola!
Nikasikia sauti zikitokea uani kama vile mtu alikuwa akilia na kubembelezwa na mwenzake.
Nikawahi haraka, kichwani nikijitahidi kufuta fikra kuwa Joy alikuwa amejiua kweli na sasa kulikuwa na msiba huko nje, nilitembea kwa tahadhari kubwa, lakini nilichokiona kilinifanya nibane kidogo kwenye kona ili kusikilizia nini ambacho kilikuwa kikiendelea, kabla ya kutokeza mzimamzima kabisa.
“Joy, basi nisamehe mimi sikutaka ufikie hatua ya kujiua bwana, mimi nilitaka nikuchemshe tu, usijiue bwana umesikiaeeh mimi pacha wako na nakupenda sana, sikuchukii mwaya,” alisema aidha Joy au Joyce maana hata mimi nilikuwa nikiwachanganya, lakini kwa jinsi nilivyoona huyo aliyekuwa akimbembeleza mwenzake ndiyo alikuwa ni Joyce na huyo aliyekuwa amekaa akilia chini, ni Joy.
“Niache, Joyce umenifanyia mambo ya kuniumiza sana, siweziii niache nife siwezi kuishi na aibu hii,” alisema Joy huku akilia mno.
“Joy, acha utoto unataka kujiua kisa nini? Mwanaume?” aliongea Joyce huku akionekana kumzuia mwenzake, mkono mmoja alioonekana kufinyanga midonge ya kila aina na kulazimisha kuiingiza mdomoni akiazimia kujitoa uhai mara moja ikiwa ataachiwa anywe kama anavyotaka.
“Joyce, hivi wewe ni binadamu au mnyama! Unawezaje ukawa mjinga wa kutojua umeniumiza kiasi gani?” alisema Joy kwa uchungu mno
“Sawa Joy, lakini vipi kama nikikwambia kuwa nitakurudishia Chriss wako na ndoa itakuwepo,” alisema Joyce sura yake ikionesha haina masihara hata kidogo.
“Joyce hebu niache, nimekwambia!” alikoroma Joy lakini sauti yake sasa ilikuwa kama imepoa kidogo akimsikilizia mwenzake kama alikuwa akimtania au lah.
“Sikia Joy, mimi nitakusaidia kumrudisha huyo mtu wako, lakini kuna gharama yake, upo tayari?” alisema Joyce akimsubiria Joy aliyelegeza mkono wake na kumsikiliza pacha wake alichotaka kumwambia.
Basi na mimi pale nilipokuwa nimebana nikabana nganganga ili nisikilizie Joyce anamlaghai nini tena Joy wa watu.
“sikia Joy, mimi ndo nimetoka jela, nimekuja na kukuta umepiga hatua, umesoma una mtu anataka kukuoa. Lakini mimi maisha yangu ndo kwanza naanza upya, nina elimu ya darasa la sita tu, nitafanya kazi gani? Nani atanipenda na ujinga wangu na mambo mabaya niliyoyafanya huko nyuma..
“nakuonea wivu sana Joy, natamani tungekuwa na mama yetu na baba yetu na wote tungekuwa tunaishi humu ndani maisha ya kawaida ili mimi niwe kama wewe,” Alisema Joyce huku akianza kutokwa machozi naye mfululizo. Kule nilipokaa nikashangaa he! Kumbe Joyce naye huwa analia?
Maana nakumbuka tangu tukiwa shule, alikuwa mtukutu na mgomvi kiasi cha kupigana hata na wavulana, na sikuwahi kumuona eti analia ila kwa Joy alikuwa chakulialia sana hilo halina ubishi, ; lakini kwa nilichokiona siku hiyo nikaamini kabisa kuwa Joyce alikuwa akiongea kitu cha moyoni ndiyo maana hadi akalia.
Basi, Joy naye akalainika wakaanza kubembelezana na pacha wake. “nimemmiss sana baba na mama,” alisema Joy, Joyce naye akadakia na kuongeza huzuni wakakumbatiana na kulia kwa pamoja.
“utanirudishia Chriss wangu kwa njia gani? Na gharama ipi unayoitaka mimi nilipie!” alisema Joy akijitoa kwa Joyce.
“gharama yake ni simpo na ni hiyohiyo itakayokurudishia Chriss wako, cha kwanza inabidi tumtafute Chaxy Chande popote alipo, unachotakiwa kufanya ni kumfungukia laivu kuwa unampenda,” alisema Joyce nikajikuta nashtuka kwa alichokitamka.
“He, nijitongozeshe kwa Chaxy Chande tena, sasa hiyo inahusiana nini na mimi kurudiana na Chriss,” aliuliza Joy akiwa na mshangao kama mimi.
“sikiliza, Joy mwanaume yoyote uliyeachana naye akiwa anakupenda kama Chriss, akijua upo na mwanaume mwingine tena una furaha, anajirudi na kutamani kuwa na wewe tena, na kwa Chriss akisikia upo na Chaxy Chande halafu akisikia kuwa mna mipango ya kuoana atakuja kukunyakua mwenyewe, wewe niamini nawajua wanaume. Najua haitakuwa ngumu kwa sababu najua unampenda Chaxy hata hivyo,” alichagiza Joyce. Nikashangaa kwa kauli yake aliyosema anawajua wanaume, aliwajuaje na wakati alikuwa jela miaka yote ya usichana wake.
“Mh! Sasa huyo Chaxy Chande si natakiwa nimpange kwanza kuhusu tunachotaka kukifanya?” aliuliza Joy swali ambalo hata mimi nilikuwa natamani kuliuliza.
“hapana yule usimwambie kitu, wewe mtumie tu ili muvi liwe la ukweli, mkiigiza itakuwa hainogi na Chriss atashtuka.”
“hapana Joyce! mimi siwezi kumuingiza mtu kwenye matatizo ambayo hayamuhusu halafu kwanini nimuingize kaka wa watu kwenye hili jambo na wakati hajanikosea chochote, mh hilo hapana.”
“unataka ndoa au hautaki!”
“nataka.”
“sasa hiyo ndiyo gharama yake, fanya ninavyokwambia, au nikuache unywe midawa yako tukutane ahera,” alisema Joyce kwa hasira.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment