IMEANDIKWA NA : CHANDE ABDALLAH
********************************************************************************
Chombezo : Joy, Joyce
Sehemu Ya Kwanza (1)
“Sijui kama umeshawahi hata siku moja kuwaza kuwa kuna kipindi katika maisha ya kila mtoto ambacho hupitia ambapo anagundua kuwa wazazi wake nao ni waongo japo kuwa wenyewe hujifanya wakweli siku zote. Mimi niligundua siku moja kuhusu baba yangu kutembea na rafiki yake mama yetu anayeitwa mama Diana.
Nilijua mama hafahamu, na mimi nilificha lakini hiyo haikuwa kwa pacha wangu Joyce ambaye pindi alipomuona tu mama Diana akiwa uchi chumbani kwa baba wakati mama ameenda kazini, akashindwa kufunga mdomo wake na kumwambia mama, mwisho wa siku ikapelekea ugomvi mkubwa sana.
Ugomvi huo ulipelekea mama yetu kufukuzwa nyumbani na sisi tukawa tunaishi kwa hofu, tukiwa kila siku tunashuhudia mama Diana akiingia na kutoka chumbani kwa baba, tena tulikuwa tukisikia kuwa siku yoyote baba atamuoa mama Diana.
Basi na yeye ndo akaongeza mikogo na kujifanya anatupenda kama wanawe.
Mimi na Joyce hatukukubali tukaanza kupanga mipango ya kumhamisha fisadi huyo wa mapenzi nyumbani kwetu, iwe isiwe, tulitaka mama yetu arudi.
Nakumbuka tukaanza kumchongea mama Diana kwa baba tena hadi kwa majeraha ya uongo tukisingizia kuwa Mama Diana ametupiga bila sababu. Lakini kwa baba ndiyo kwanza alikuwa akiongeza mahaba.
Jambo hilo lilimkera sana pacha wangu Joyce ambaye aliamua kufanya kitu cha ajabu na cha kikatili ambacho hadi leo nikikaa na kufikiria nasisimka
Tofauti na mambo mengine ambayo alikuwa akinishirikisha, hilo hakuniambia hata kidogo. Mara zote tukiwa tumetoka shuleni kwetu tulirudi na kufanya kazi za nyumbani, lakini mwenzangu alikuwa akijifungia ndani kimya.
Kadri siku zilivyozidi kwenda huku kwa baba na mama Diana ndiyo mapenzi yakazidi kushamiri mama Diana na mwanaye Diana wakaja kuishi na sisi pale nyumbani pika pakua.
Baadaye nilikuja kugundua kumbe mama Diana hakuwa mbaya kama tulivyokuwa tukimdhania. Saa nyingine yeye alikuwa akitupikia na kutufulia nguo zetu wote tena akizichanganya na za mwanaye Diana ambaye alikuwa ametuzidi kishule, mwenzetu akiwa sekondari; Sisi ndo kwanza tulikuwa darasa la tano.
Nilijitahidi kumwambia mwenzangu Joyce aachane na mipango yake, lakini Joyce alizidi kuwa mkali na kujiapiza kuwa lazima siku moja afanye jambo.
Siku hiyo nakumbuka ilikuwa ni jumapili mchana saa ya chakula, kikaandaliwa sebuleni na mama Diana mwenyewe ambaye tulianza kuambiwa na baba tumuite mama, na mimi nilimuita mama lakini si Joyce, bado alikuwa na kinyongo sana.
Baada ya kuweka chakula sebuleni,nilienda kumuita baba na Diana ili waje tule, wakati huo Joyce alikuwa ameshawahi sebuleni.
Tulipofika wote tulianza kupakua chakula na kuweka kwenye sahani kila mmoja na yake, Joyce naye alikuwa na chakula chake alichoanza kukila taratibu. Lakini kabla mimi sijapakua akaniambia maneno ambayo mpaka leo nayakumbuka sana.
Alisema : “Joy, kula hiki chakula changu, mimi nimeshiba.” Nikachukua chakula chake na kuanza kula kwa spidi maana kilikuwa kitamu na nilikuwa na njaa mno. Sote tulikula isipokuwa Joyce peke yake ambaye tukiwa tunaendelea yeye alienda zake chumbani, nikasikia akiongea na simu.
Nikajua kuwa lazima alikuwa akiongea na mama maana alikuwa akizungumza naye kila siku na mara nyingine hata sikuwa najua walikuwa wakizungumza nini.
Ghafla nilianza kuona hali ikibadilika pale mezani, maana wa kwanza kudondoka alikuwa ni Diana, akafuatia baba kisha mama Diana tena wote walianza kutoka povu midomoni huku wakishika matumbo yao kama ishara ya maumivu makali.
Sikuwa na akili za kujua kuwa pengine hiyo ilikuwa ni sumu aliyoweka pacha wangu Joyce kwenye chakula, nikajua pengine ni kitu kingine, nikamkimbilia baba yangu mpenzi na kuanza kulia, taratibu akanyosha miguu yake na kukata roho mbele yangu.
Wa pili alikuwa ni Diana na watatu akafuatia mama yake. Nilipiga kelele sana hadi majirani walipofika na baadaye mapolisi, wakati huo wote, Joyce alikuwa amejifungia chumbani kwake kimya bila kuzungumza na mtu.
Hapo ndipo nikaanza kupiga kelele kuwa huenda Joyce alikuwa ameweka sumu kwenye chakula. Baada tu ya kusema hivyo, wale maaskari wakamkamata na kumuweka chini ya ulinzi.
Sasa sijui kutokana na utoto, maana aliongea kwa hasira; “Joy! ndiyo nimewaua sasa, wewe unataka waendelee kukaa wao hapa, kwani kwao. namtaka mama yangu arudi!” alisema Joyce huku akiniangalia kwa chuki.
Baada ya vipimo kweli, iligundulika kuwa Joyce aliweka sumu kwenye chakula hivyo akapelekwa jela ya watoto kwa kuwa alikuwa na miaka 15 tu kama mimi.
Wakati huo ikabidi mama aje nyumbani kuishi na mimi pale nyumbani lakini alionekana kuwa na majuto makubwa. Baadaye ndio nikaja kujua kuwa kumbe ni yeye ndiye aliyemtuma Joyce atie sumu kwenye chakula.
Kwa kujiona mkosefu mama hakuishi sana, alijinyonga mwenyewe na kuacha ujumbe kitandani. Hilo lilinifanya nimchukie sana Joyce na kuacha hata kwenda gerezani kumtembelea.
Niliishi kwa amani miaka kibao, sasa nimefikia miaka 25 na nimepata mchumba ambaye ameahidi kunioa, nampenda na yeye ananipenda, lakini wakati nikijiandaa kujenga maisha yangu, Joyce anarudi kutoka sehemu alikokuwa na kuniharibia ndoto zangu kiasi kwamba natamani kumuua. EE Mungu nisaidie!”
Maneno hayo alinihadithia rafiki yangu, Joy baada ya kufika ofisini kwangu maeneo ya Mwenge kwa ajili ya ushauri. Kweli nilikuwa nikimkumbuka Joyce ambaye ni pacha wake, lakini ilikuwa ni muda mrefu tangu tulipokuwa tukisoma pamoja shule ya msingi Kongowe, hivyo maneno ya Joy kuwa Joyce amerudi na kumfanyia vimbwanga nilikuwa hata mimi ninapata habari kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo niliamini moja kwa moja maneno aliyokuwa akiyasema Joy kwa sababu siku zote alikuwa na moyo wa malaika, na Joyce alikuwa ni shetani mtu. Wakati natafakari nimsaidiaje Joy, ikabidi nimuulize kuhusu huyo mchumba wake na jinsi gani Joyce alivyoingilia mapenzi yake.
Akafuta machozi na kuanza kunihadithia maneno haya;
“kaka yangu Charles Chande (alipenda sana kuniita majina yote hayo mawili kwa pamoja) nakumbuka wakati Joy alipokuwa gerezani, mimi nilikuwa nikilelewa pale nyumbani na shangazi yangu. Nilijitahidi kusoma kwa bidii na hadi nakamaliza digrii yangu ya sheria.
Huyo mchumba wangu ni mwanaume tuliyekutana naye hukohuko chuoni Dodoma. Cha ajabu nilitambulishwa kwake na mwanaume wangu wa kipindi hicho aliyekuwa akiitwa Damian.
Damian alikuwa ni raia wa Kenya na tulikutana hapo chuo tukapendana na alikuwa ndiye mwanaume wangu wa kwanza. Nilimpenda hivyohivyo bila kujua kuwa kumbe mwenzangu moyoni alikuwa na yake.
Siku hiyo nakumbuka ilikuwa ni siku ya furaha kwa sababu tulikuwa tumeshamaliza mitihani ya mwisho na tulikuwa tukijiandaa kurudi nyumbani
Hivyo wanafunzi wengi walikuwa wamezagaa kila sehemu hasa kwenye kumbi za starehe wakifurahia. Kwa upande wangu mimi na mpenzi wangu Damian tulikuwa baa na rafiki yake Chriss .
Siku hiyo Damian alinitambulisha kwa Chriss kuwa ni rafiki yake sana na alikuwa akisoma naye kozi ya Diplomasia. Tuliagiza vinywaji na kuanza kunywa taratibu huku Chriss kila mara akinitazama kama vile alikuwa akinilinganisha mimi na Damian na kutupima kama tunaendana.
Mimi nikawa najifanya kama simuoni nikajishikiza kwa Damian wangu ambaye baada ya muda mchache alianza kulewa na kulala palepale.
Baada ya kuona hivyo ndiyo Chriss akaniomba nisogee kidogo kwa upande wake ili aniambie kitu, nikasogea na kumsikiliza nikijua hana lolote zaidi ya kutaka kunitongoza tu. Lakini nikasogea nikifuata ule usemi wa kubali wito kataa maneno.
Akaniambia; “shemeji yangu wewe ni msichana mzuri sana. Na Damian pia ni rafiki yangu lakini kuna kitu ningependa kukwambia, ambacho najua kitakukwaza sana.”
Nikajua alikuwa akipanga maneno ili kuanza kufitinisha na rafiki yake kwa kuwa amelewa na hajielewi.
Mimi sasa Wakati huo nikiwa namsikiliza Joy, niligundua alikuwa akihadithia maisha yake kwa urefu mno ambao kwa wengine angewaboa, lakini kwa kuwa ni mwandishi wa hadithi nikaona bora nisikilize kwa ufasaha ili nipate na kisa cha kuandika kwenye mkasa wangu mpya ambayo hata jina sikuwa nalo.
Joy akaendelea:
“ Damian amekuwa muda mrefu akiona aibu kukwambia kuhusu hili lakini, ameniomba mimi nikwambie kwa niaba yake tafadhali naomba unisikilize.” alisema Chriss hapo nikamtazama Damian na kurudisha macho yangu kwake, nikajiuliza ni jambo gani hilo ambalo alikuwa akishindwa kuniambia ana kwa ana mpaka kupitia rafiki yake? Sikupata jibu.
“Joy ilibidi haya maneno nikwambie wakati tupo wawili tu, lakini kwa kuwa Damian amelewa na hajielewi hiyo haijalishi hata sasa naweza kukwambia tu kama hautojali.
Baada ya kuniambia maneno hayo nikamruhusu aniambie; akasema;
“kwa kipindi kirefu sana Damian alikuwa akificha moyoni mwake kuwa ana mke na mtoto huko kwao, na kwa kuwa amemaliza chuo basi atarudi kwa familia yake.”
Wakati Chriss aliposema hivyo moyo ukapiga pah! nikashtuka na kugeuka nikumuangalia Damian nikihisi huenda ni utani, kwasababu alikuwa mtu wa masihara sana.. Lakini kimya kilipita dakika nzima, hapo ndiyo nikahisi hakukuwa na utani.
Nikamtazama Chriss kwa hasira, akaendelea; “Damian anajua unavyompenda ndiyo maana aliogopa kukukimbia na kukuumiza moyo, aliona akwambie mwenyewe lakini alishindwa. baadaye aliniomba mimi ndiyo nikwambie, tafadhali shemeji, najua itakuwa ngumu kwako lakini tafadhali muelewe Damian.”
Baada ya yeye kusema hivi nikanyanyua glasi ya wine nikaigida yote, nilipoishusha machozi yakaanza kunitiririka, lakini nikaongeza glasi nyingine na kuinywa yote kwa fujo, nikanywa ya tatu mpaka nikaanza kujisikia ganzi.
Nikafikia hatua nikawa kama sipo duniani, lakini nilijua nimeumizwa na mtu. Nilikunywa hadi nilihisi mkono wa mtu ukinizuia kuendelea kulewa. Nikainuka na kuanza kutembea lakini niliyumbayumba. Kilichoendelea hapo sikujua.
Nilikuja kuamka asubuhi nikiwa kwenye chumba nisichokitambua, lakini kilionekana ni chumba cha hoteli au lodge tena nilishtuka nikiwa na shuka tu lililonifunika.
Nilipoliinua na kujitazama nilijiona nikiwa kama nilivyozaliwa na bafuni nilisikia kama kuna mtu anaoga nikaanza kujiuliza jana nini kilichotokea. Nikakumbuka nilikuwa na Damian na Chriss, nikakumbuka pia machungu yote.
Roho ikaniuma nikaanza kulia kimyakimya, lakini nilikuwa na wasiwasi juu ya nani niliyekuwa naye mle chumbani? Nikajikagua isije ikawa nimengiliwa.
Dakika chache nilimuona Chriss akitoka na taulo kiunoni, cha kushangaza hakuonesha kushtuka aliponiona, akafurahi na kuketi pale kitandani na kunisalimia.
“shemeji, vipi hangover!” “bado kidogo najisikia kichwa kinauma!” nilimjibu kwa aibu maana kila nilipojiuliza jinsi nguo zangu zilivyonitoka mwilini mwangu sikupata jibu.
“Joy samahani nilishindwa kukuacha na nguo zako jana, kwa sababu ulizichafua sana, brauzi yako uliitapikia.”
“Na sketi yangu na chupi!?” niliuliza kwa hasira kidogo maana kama nilitapikia brauzi hizo nguo nyingine zilihusikaje.
“Ulizikojolea, ndiyo ikanilazimu nikuvue zote na kuzifua upya, pia nilikuogesha maana ulikuwa haujielewi hata kidogo.”
Aliposema hivi mwili mzima ukanisisimka, nikaona aibu mara mbili zaidi.
“samahani kwa kukusumbua shemeji Chriss, nisamehe sana.” Niliomba msamaha lakini aliniwahi na kunishika bega na kunitaka nisiwe na wasiwasi.
“shemeji kuhusu niliyokwambia jana, Damian amesharudi kwao Kenya leo, ameniambia amekutumia meseji,” Alisema Chriss lakini nikajikuta nikimtukana kila aina ya tusi Damian na sikuweza kuzuia machozi yasinidondoke.
Chriss aliona akanifuata na kunikumbatia lakini shuka nililolipitisha mabegani nikiwa pale kitandani, likanivuka nikawa kifua wazi, lakini sikujua hadi pale nilipoanza kusikia joto la kifua cha Chriss kwenye kifua changu.
Nilishindwa kujitoa kwa sababu alikuwa amenikumbatia kwa nguvu kweli tena akinifariji mno, nikaona nikijitoa harakaharaka itakuwa utoto, tena kwa mtu ambaye ameshaniona mwili mzima na hakunifanya chochote, mh wanaume wachache wanaweza wakawa na wema huo.
Tulikumbatiana muda kidogo hadi aliponiachia nikanyanyua shuka haraka na kujifunika tena. Nikainuka na kuomba kwenda kuoga nikaona nguo zangu zikiwa zimefuliwa vizuri. Wakati huo Chriss akawa anavaa nguo zake na kuniambia kuwa nimuagize kwenye hosteli zetu ambazo zilikuwa karibu na kwenye hiyo gesti ili akanichukulie nguo zangu
Nilimuagiza na baada ya dakika chache alirudi akiwa na nguo, akanipa na kutoka nje akinipa nafasi ya kuzivaa. Tukatoka nje kila mtu kwa njia yake na mimi nikapata nafasi ya kusoma ile meseji ya Damian. Nikagundua ilikuwa imeandikwa; “ Joy, samahani kwa yote yaliyotokea, nilikuwa nikifahamu hayo yalikuwa ni mapenzi ya chuo tu ambayo yataisha baada ya sisi kumaliza, lakini nasikitika kwako haikuwa hivyo siku zote uliniona kama mtu ambaye tungepanga future, kwa hilo naomba unisamehe. Mimi nimerudi kwetu Kenya huku nina mke na mtoto nakuombea umpate mtu akusahaulishe kuhusu mimi.” Nilipomaliza kusoma meseji hiyo niliifuta kwa hasira na kufuta hadi namba ya Damian, nikaingia zangu hosteli na kuanza kupanga mizigo yangu ili nirudi nyumbani kwetu kwa sababu wanafunzi wengi tayari walikuwa wameshaanza kuondoka.
Wengi tulikutana stendi ya mabasi lakini baada ya kupanda mabasi ya kurudi Dar ndiyo nilikutana na Chriss akiwa amekaa kwenye siti moja wapo, aliponiona alifurahi na kutaka nikakae naye. Japokuwa alikuwa akinikumbusha sana kuhusu Damian kiasi kwamba sikutaka hata kukaa naye lakini niliona siyo vyema nikaenda kukaa naye.
Baada ya wiki kadhaa kila mtu akiwa kwake, tukawa tunawasiliana na mwisho wa siku akawa anakuja kunitembelea nyumbani nikatokea kumuamini sana. Ilichukua muda sana hadi nikaelewa alikuwa akinipenda kwa vitendo lakini alikuwa akiogopa kuniambia.
Nikamrahisishia akanifungukia na kuniambia alikuwa tayari hata kunioa kabisa.
Nilifurahi kusikia hivyo lakini niliogopa kumkabidhi moyo wangu kirahisi hivyo, nikampima kwa staili ya kizamani, kuwa sitaki kufanya naye mapenzi hadi tutakapooana, kiunyonge akakubali. Tukawa tukiishi kwa staili hiyo tukiishia kukumbatiana tu kama ndugu katika Kristo.
Muda ulizidi kuyoyoma na mipango yetu ikawa vizuri na hatimaye ikafikia siku za sisi kuoana, maandalizi yote yalikamilika ikawa inasubiriwa tarehe tu na baadaye ikawa wiki moja tu.
Siku moja wakati nimetoka kutembea niliamua kupitia kwa mchumba wangu Chriss, ndiyo nikagundua kulikuwa na viatu vya mwanamke pale nje, nikafungua mlango na kugundua kuwa hakukuwa na mtu sebuleni.
Mbaya zaidi sauti zilikuwa zikitokea chumbani, kwa Chriss. Moyo ukaanza kunienda mbio nikijiuliza maswali mengi yasiyo kuwa na majibu.
Nikanyata na kusogelea mlangoni nikasikia huyo mwanamke anamwambia Chriss, “nimekutesa sana mpenzi wangu kila siku nimekuwa nikikwambia sikupi penzi mpaka unioe, lakini leo nipo tayari unifanye unavyotaka, mpenzi wangu.”
Sauti ya Chriss kwa upande mwingine ilisikika ikisema: “kweli Joy? Siamini,”
Nikashangaa huyo Joy mwingine zaidi yangu ni nani ambaye Chriss alikuwa tayari kunisaliti naye wiki moja tu kabla ya ndoa yetu, tumbo lilianza kuniuma. Nikajikaza na kusogelea mlango na kujaribu kuufungua taratibu nichungulie.
Huwezi kuamini Charles Chande.Nilimuona Joyce akimvulia nguo Chriss wangu, maskini Chriss naye alijua ni mimi. Huyu Joyce ametoka lini jela Mungu wangu!
Nikajiuliza nifanyeje? Nikashindwa kupata jibu maana kama ningeingia na kufanya fumanizi, nilikuwa namfumania nani sasa maana Chriss alikuwa akimuona Joyce ni mimi na mbaya zaidi sikuwa nimemwambia Chriss mambo yaliyotokea zamani kuhusu familia yangu na sasa ilikuwa inanicost naomba Charles Chande nisaidie.”
Alipofika hapo nikaanza kuumiza kichwa kufikiria jinsi gani ya kumshauri Joy maana alionekana amechanganyikiwa kweli.
Nikafikiria kwanza kabla ya kumshauri, hata hivyo na mimi nikaona njia pekee iliyosahihi ni kumwambia Chriss ukweli wote juu ya kila kitu kinachoendelea ili iwe nafuu kwake.
Alikubali kishingo upande nikawa nasubiri nikidhania pengine atachukua simu hapohapo na kumpigia huyo Chriss wake, lakini niliona hafanyi jitihada zozote za kufungua begi lake badala yake akawa anatazamatazama ofisi yangu na kuniangalia kuanzia chini hadi juu kama hanijui.
“Joy, si unampigia sasa hivi?” nilimuuliza akashtuka na kuniambia.
“Samahani yaani hata simu yangu sijui niliiacha kule kwa Chriss? hata sijui nitawasiliana naye vipi.” Alisema Joy ikawa mtihani juu ya mtihani.
Ikabidi tu nimuombe arudi nyumbani akapumzike na kesho nikimtaka aende kuongea na Chriss ana kwa ana, kabla mambo hayajaharibika rasmi. Lakini akakataa na kunitaka niongozane naye. Alinilazimisha sana na kweli nikakubali. Akaondoka na kuniacha nikiendelea zangu kuandika stori.
Dakika chache tu baada ya Joy kuondoka nikiwa sina hili wala lile, simu yangu ilipokea ujumbe nilipousoma nikagundua kuwa ni meseji kutoka kwa Joy akanitumia kuhusu habari za michango ya ndoa yake.
Nikashangaa inawezekanaje, Joy akarudi nyumbani haraka na kuipata simu yake aliyoipoteza na kunitumia ujumbe huo, wakati dakika chache tu alikuwa amechanganyikiwa kwa kupokonywa mume wake mtarajiwa na pacha wake Joyce.
Nikahisi moja kwa moja kuwa Joyce ndiye aliyekuwa akijifanya Joy tena kwa kuchukua simu ya pacha wake na kusambaza ujumbe huo ili mradi kutaka kuolewa haraka na Chriss badala ya pacha wake Joy.
Nikashangaa inawezekanaje mwanamke akawa katili kiasi hicho kwa ndugu yake. Hapa ndiyo ari yangu ya kufatilia kisanga hicho ikanipanda nikajiapiza kufuatilia kinaga ubaga ili niweze kuandika stori ambayo itafundisha na kusisimua.
Basi nikanyanyua ile simu na kujibu kwa kifupi; “hongera Joy, mchango mwisho lini?”
“mwisho wa mwezi huu tu besti angu Chaxy Charles Chande,” alinijibu lakini kwa kuyataja majina yangu matatu hapo kidogo nikajikuta nikitatizika, nikajiliuza huyo Joyce aliyerudi jela juzijuzi tu alijuaje majina yangu yote hayo.
“huyu mwanamke balaa ina maana alichunguza sana kila kitu kabla ya kufanya!” nilijisemea kimoyomoyo.
Nakumbuka siku hiyo nilipomaliza kuandika hadithi na kuziposti, nikafanya kazi nyingine za ofisi kama vile kusimamia studio ya muziki na kuhakikisha napitia malipo yote na nyimbo zilizotoka.
Giza liliingia nikiwa nimefanya kazi ya kuchosha mno, lakini niliyokuwa nikiipenda, sasa nikasahau kisanga cha Joy na pacha wake Joyce nikaanza kuwaza mambo yangu na mimi, maana mpenzi niliyekuwa naye ni pasua kichwa kwelikweli (jina lake hapa nitamuita Deborah japo siyo jina lake halisi).
Nikarudi zangu nyumbani nikiwa na wazo jingine la hadithi ambalo lilikuwa likinisumbua mno kichwani, nalo lilikuja baada ya kukutana na rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa kila siku akiniringishia kuwa na mademu wapya, yaani kwa wakati huo alikuwa nao sita kwa pamoja.
Nilipomchimba sana anieleze siri ya mafanikio yake kama alivyoyaita ndiyo akanifichulia kuwa amechanjia dawa inayoitwa ndele; basi kupitia aliyonisimulia ndiyo nikaona nianze kutunga kisa nilichokiita SWEET PANDEROSA ambacho kina ukweli kwa asilimia 60 ya aliyonihadithia. Kwa bahati nzuri hata yeye mwenyewe haijui stori hiyo kwa sababu hasomagi hadithi.
Lakini wakati nimechukua laptop nikianza kuandika huku Deborah akinipikia chakula, taratibu nilianza kukosa hamu ya kuandika baada ya kuhisi harufu inayotoka jikoni siyo ya chakula nilichokitaka.
“Nini! Samaki? Si niliagiza maharage na ukakubali!” niliongea kistaarabu lakini mwenzangu akanijia kwa sauti ya juu: “kama ungetaka si ungejipikia mwenyewe,wewe vipi!” Nadhani kwa sauti ile hadi wapangaji wenzangu walikuwa wamesikia. Kwasababu nilikuwa mtu wa kupenda kufanya mambo yangu kiustaarabu niliona yaishe, lakini hasira ilinifanya nisiwe na mudi ya kuendelea kuandika kuhusu lolote, nikakausha kimya na kuwaza jinsi maisha yanavyoenda huku nikipanga cha kuzungumza mapema kesho nitakapokutana na bwana ake Joy, Chriss.
Baada ya sekeseke na mpenzi wangu lililoishia kila mtu kulala mzungu wa nne, niliamka asubuhi na kujiandaa, kama kawaida nikimuacha mwenzangu amelala bila kuniandalia chai, wala maji ya kuoga na sikulalamika, nikaacha hela na kuondoka zangu.
Nilipofika tu kazini mtu wa kwanza kuonana naye hakuwa mwingine bali ni Joy kama kawaida, siku hiyo akiwa amevaa nguo nzuri mno na kujipamba, akanitaka niende naye moja kwa moja sasa kwa Chriss.
Kwa kuwa sikuwa na namba yake ya simu ikabidi niende naye kwa Chriss kwa staili ya kizamani. Tulipofika tukamkuta ndiyo anatoka, nadhani alikuwa akielekea mihangaikoni, alipotuona akashtuka nusura akimbie, hapo ndipo Joy akamuwahi kwa kumuonesha ishara ya kuziba mdomo, tukamvuta na kwenda naye kando.
“Wewe si nimekuacha sasa hivi ndani na nimekuaga, ukiwa kitandani, mbona upo nje huku tena umevaa nguo kabisa, au jinni!” alisema Chriss akiwa amechanganyikiwa. Ikabidi nimueleze tu kuwa mchumba wake ana pacha wake.
“Kwa hiyo wewe ni nani?” aliuliza Chriss akionekana kuelewa kidogo.
“mimi ndiyo mpenzi wako Joy, huyo uliyekuwa naye ndani ni Joyce, pacha wangu siyo mtu mwema hata kidogo, naomba tukae nikueleze jambo.” Alisema Joy huku akionekana kuwa mwepesi wa machozi na kila alichokiongea, Chriss alikuwa akitikisa kichwa akionekana kuwa haamini chochote kilichotoka mdomoni mwa Joy
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment