Search This Blog

Monday, January 24, 2022

JOY, JOYCE - 4

   

Chombezo : Joy, Joyce

Sehemu Ya Nne (4)



Usiku ule sasa Joy au sijui Joyce, akiwa ameondoka na mimi nikiwa peke yangu, nikaanza kuwaza na kuwazua yaliyonikuta, kwanza nilijipongeza kwa kuwa gemu niliicheza kibabe; la pili nililojipongeza ni kutoacha wanitumie tu bila kuambulia kitu. Lakini hapo sasa kwenye kuambulia kitu ndiyo kulikuwa na kihisia Fulani hivi ambacho nilibakiwa nacho.

Ona; Joy na Joyce ni wazuri ile mbaya, japo hawamzidi Deborah lakini wao wanamzidi kwa muonekano wa kishua kuanzia mavazi, kuongea na haiba kwa ujumla, lakini Deborah alikuwa wa uswazi, anaongea kwa kuropokaropoka, anavaa madela na anasikiliza mataarabu mno; tena wapi kuwe na ugomvi usimkute mwanamke Yule!

Sasa basi hicho kihisia kilichoniganda kilikuwa cha kunitaka niendelee kuwa na Joy au sijui Joyce. Maana ukiachia yote hayo ilikuwa ni vizuri maana hata hao majirani zangu niliwaacha wakivurugana huko nje. Ni wazi walijua kama niliachana na Deborah sitampata mzuri zaidi yake, ila kwa Joy au sijui Joyce aliyekuja siku ile nadhani heshima ilikuwepo.

Tena nami nilifanya sifa ya kuweka mahaba ya kumpa taulo langu na kumchotea maji ya kuoga ili wakina Fulani wapeleke taarifa.

So siku hiyo nilitembea nikiwa najua kwa mtindo Fulani hata mimi hiyo shere ya kina Joyce imenisaidia kunirudishia heshima ndani kwangu, maana we fikiri, unaachana na demu leo, kesho watu wanaona unaleta chuma kingine halafu kikali vilevile, mfyuuuu!

Sasa nikapata cha kuandika na kuanza kuendeleza kidogo stori yangu ya Joy, Joyce na kuandika vyote vilivyonitokea siku hiyo na kuombea mengi zaidi yanitokee ili nipate kuwapa mkasa huu.

Basi bwana nikiwa ndiyo kwanza naanza kuandika, simu yangu ikaita nikashtuka kuona namba ngeni lakini kama vile naijua hivi!

“Mmh Chande vipi mzima wewe?” ilisema sauti ya Deborah na hapo ndiyo nikagundua kumbe ile ilikuwa ni namba yake na sikujua tu maana nikiachana na mtu huwa najifanya jeuri wa kufuta kuanzia picha zake hadi namba za simu ili nisimkumbuke na Kwa Deborah ilikuwa hivyohivyo pia.

“Poa mzima niambie?” nilijibu kikawaida tu.

“mmmm upo wapi?”


JOY, JOYCE 36

“Nipo nyumbani. Kwanini unaniuliza?” niliongea nikijifanya naweka ghadhabu kidogo.

“usijali nauliza tu, vipi upo na nani?” alipouliza swali hilo nikashtukia kuwa inawezekana kabisa ameambiwa na wambea kuwa wameniona nimeingiza mtu maghetoni na hilo lilimchefua pengine.

“nipo peke yangu,” nilijibu, lakini ghafla simu ikakata na hatua nikazisikia koridoni, halafu ghafla mlango wangu ukafunguliwa. Shtuka shtuka na wewe; unajua nani aliyeingia?

Ni Deborah huyuhuyu, nikiwa kwenye hamaki ya kutaka kumtimua, loh! akafunga mlango kwa ndani na kunipigia magoti michozi ikimtoka tena akanikamata miguu kabisa.

“Chande naomba nisamehe, nilikosea tu, lakini akya mungu naapa mimi juu ya kaburi la marehemu mama yangu, sitarudia niliteleza tu mara moja, sitarudia tena naapa,” alilia.

Basi sauti ndani yangu ikaniambia; “Chande, ukimkubalia utakuwa bwege namba moja, maana alivyoondoka alitangaza mtaa mzima ukajua kuwa amekubwaga, so hiyo kurudi anarudije?”

Loh ilikuwa kweli, lakini na mimi nikajishtukia nikijiona sina akili kama nitamsamehe. Na Deborah alijua hilo na alijua nilidhamiria kuachana naye kweli ndiyo maana niliingiza mwanamke mwingine humo ndani, hivyo aliniomba msamaha nusu saa nzima. Tena siku zote hujisifia uzuri wake lakini, huwezi amini pamoja na uzuri wake wa kuunguza majani mabichi, lakini alinipigia magoti na kulia.

Nikamuonea huruma na kushindana na nafsi yangu nikisema; “kweli aliondoka na mikwara na pengine majirani wanajua! Lakini vipi basi kama nikimfanya arudi kwa aibu pia ili majirani wajue?”

nikamwambia: “sikia nitakusamehe ukifanya jambo moja, kama ulivyoondoka kwa kelele na kila mtu kujua, basi leo hii omba msamaha kwa kelele hivyohivyo, tena ulie hadi nihakikishe majirani wamesikia..” nilisema.

“sawa tu mme wangu Chande, mimi nipo tayari, “ alisema Deborah akaanza sasa kwa sauti: “Chandeee naomba nisamehe jamani, nimekosa sitarudia tena ni ujinga wangu tu kukujibu ujeuri, nitatulia na kila utakachosema nitafanya,iiiii iiiii, nisamehee!” alisema Deborah kwa sauti hadi nikajishtukia na kumziba mdomo maana kama wale wakina mama wa pale nje kusikia basi walisikia vilivyo na kama kidume cha nyumba nilishajulikana.

Sasa nikajiuliza nimsamehe kweli au nivunge?





Aliposema hivyo nikashangaa, nikamsubirisha kidogo kwanza ili niandike hicho kituko kwenye kompyuta nisije nikasahau, kisha nikarudi na kusema:

“sawa nimekusamehe lakini sitaweza kurudiana na wewe cha msingi nenda kwanza nyumbani kwenu nipe muda.”

Deborah akazidi kulia na kubembeleza na kunikumbusha kuwa amenifanyia kila kitu nilichosema ikiwemo kuomba msamaha kwa sauti, lakini kwanini sikumfikiria. Basi na mimi nikaangalia kwenye tenga la nguo, nikaona minguo kibao michafu, mivyombo michafu, loh nikimuacha ndiyo kufua na kuosha vyombo kutanihusu. na vile nilikuwa nafuliwaga, leo hii majirani wanione hapo nje nikifua si aibu hii!?

Pia nikafikiria, kuwa huenda Joy na Joyce wasinitafute tena kwa kuwa walichokifuata si wamekipata? kwa hiyo nikimuacha Deborah nitakuwa na nani wa kunipoza moyo; na mie kuwa mpweke sipendi hata kidogo napenda mapenzi shatashata kila saa deka nikudekeze ganda tugandane, mie mtu wa pwani shida sitaki.

Hesabu zangu zikasema nimsamehe ila kwa masharti, basi sharti langu la kwanza nikamwambie ahakikishe anaacha uswahili; yaani haongei kwa kuropoka hovyo, anasikiliza taarabu kwa sauti ya chini. Nikirudi nikute msosi, kutembea mwisho saa kumi na mbili na kote aendako aniage maana uhuru na mie nilimpa wa kuzidi. Na kingine nikataka anihadithie mambo ya unyago wa kimakonde maana yeye ni kabila lake na alichezwa, na tena yote hayo ilikuwa ni kwa ajili ya kuandaa ile stori yangu ya Nyoo nipe Mumeo ambayo mautundu yote alinifanyiaga yeye na kwa wale mlioisoma na Gululi ndiyo yeye enzi hizo akiwa kwenye chiputu.

Akakubali tukaandika makubaliano kwenye daftari na yeye akasaini.

Basi akafungua mkoba wake, na kutoa zawadi ya boksa nyeupe na singlendi, nilizipokea kwa kustaajabu. Usiku ule akaniuliza kama nimekula, nikamwambia sijala. Akaenda kununua urojo na chipsi zenye filigisi kwa hela yake au sijui aliyohongwa huko, akaniletea nikala vizuri tu.

Kama haitoshi usiku akanifanyia mambo ya pwani zaidi ya siku zote maana aliacha uvivu wake maana alinizoea na akawa anachanuaga tu lakini kwa kujua kuna mwenzake, akafanya kunikomoa.


JOY, JOYCE 38

Loh! Mie nilifurahia tu. Tena akaanza kufunguka tukiwa mchezoni eti kwanini natembea na wanawake wengine na shutuma kibao. Mie nikawa kimya tu.

Siku ya pili Joy akanipigia simu na kumbuka, nilishangaa lakini sikuonesha, baada ya salamu eti aliniomba nimtumie picha yangu nzuri. Basi nikapekenyua kwenye simu na kumtumia picha moja hivi ya photoshoot, akaichukua na cha kushangaza akaiweka kwenye akaunti yake ya instagram na nilijua tu kwa kujiuliza kiintelijensia kuwa picha yangu ataiweka wapi zaidi ya kuipost. Basi ndiyo nikaiona kaipost pale kwenye akaunti yake akaandika “my deshideshi”.

Kwa chini nikaona watu wakikomenti: vipi huyo ndiyo shemeji yetu nini?

Wengine wakimpongeza na mengi ya namna hiyo yaani. Nikafuatilia post zake za nyuma nikagundua kuwa hakupost kwa muda wa wiki kadhaa kabla ya kupost ile picha yangu.

Basi nikashuka kwenye post zake za nyuma na kuanza kukagua picha moja baada ya nyingine, picha zote zina comment za Chriss Yule bwana ake, wakiitana; my hubby na my wife. Nikaingia kwenye akaunti ya Chriss na kuona hivyohivyo hata Joy alikuwa akicomment kwake.

Wakati huo sasa nikarudi kwenye picha yangu ile aliyoipost muda sio mrefu. Loh pale chini kulikuwa na komenti mpya kabisa imeandikwa na Chriss. Ikisomeka: kwahiyo pamoja na kutumiwa ujinga wako, umeamua kumpost kabisa, sawa!

Hapo nikapiga hesabu kuwa sasa huenda picha zile alizopiga Joy au Joyce, alishatumiwa Chriss na ili kumtia wivu zaidi ndiyo Joy akaamua kufuata ushauri wa nduguye wa kunipost na instagram loh! Na hapo ningekuwa sijui ningejiona napendwa kama nini, lakini kumbe natumiwa! na kama nisingejiongeza ningekuwa mjinga duh wanawake hawa?!

Basi na safari hii na mimi nikajifanya chizi, nikachukua picha ya Joy moja na kuiremba na kuipost kwenye akaunti yangu ya Instagram ili nimvuruge na yeye nikamtag. Uzuri Deborah hakuwa mtu wa mtandao sana hivyo sikuhofia.

Loh kumbe nilimuweza, subiri ujue nini kilichotokea..




Sikukaa kidogo simu yangu ikaita, nikapokea, ujue ni nani! Ni Joy. Nikamchombeza kwa mahaba ya makengeza.

“hallow mtoto mzuri mambo!?”

“poa tu, lakini Chaxy naomba tukutane kuna jambo nataka kukwambia,” alisema akionekana kuchanganyikiwa hivi.

“sasa hivi!?”

“ndiyo, nipo hapa Hongera,”

“poa,” nilijibu na kujiandaa. Nikijiongeza kuwa huenda sasa ndiyo ile picha niliyompost ilimletea kizaazaa kwenye mpango wao huo wa kijinga.

Basi hapo nikanywa chai niliyopikiwa na Deborah kwa mahaba yote, maana alikuwa akijituma kama nini si anajua tena ndiyo ametoka kusamehewa! Na siku hiyo aliamkia kufua ile miguo.

Nilipomaliza nikasimama zangu mwana-kupuyanga mie ili nikafanye yangu huko duniani. Kidogo simu nyingine ikaingia saa hiyo kutoka kwa dada yangu, Alphonsina, ni mtoto wa mama yangu mdogo, lakini ni dada yangu ninayempenda mno. Yeye ndiye aliyenifundisha kuandika na kusoma nikaviweza nikiwa chekechea, tena nilisomaga gazeti mbele ya wazazi, shukrani kwake, sijafanikiwa tu. Lakini nikikaa vyema nitamzawadia jambo maana aliniokoa na ujinga mkubwa kuliko wote duniani, yaani wa kutojua kusoma.

Natamani nimwambie, sista ona ninavyozichezea herufi A hadi Z na kuumba mihadithi ya kufa mtu. loh lakini cha ajabu yeye hadithi hazipendi na yupo bize akipambana na hali yake.

Basi siku hiyo ndio nakumbuka niliambiwaga alikuja kukutembelea kutokea Songea, na alikuwa kwa mama Mbagala. Akataka kunisalimia lakini katika salamu hiyo akaniambia, maneno haya:

“mdogo wangu nasikia unakaa na mtu,”

“mmh na wewe nawe, umejuaje haya?” niliuliza maana habari ya kukaa na Deborah sikuwahi kumwambia mtu. mie tu ndiyo nilijitambulisha kwao, lakini kwa upande wangu hakukuwa na aliyekuwa akimjua hata nzi wala mende, maana mama yangu mlokole balaa na nikisema nakaa na mtu kihawara jua atanihubiria mithali, zaburi na agano jipya lote ili kuninyoosha, sasa masaa yote hayo ya kusimangwa na neno la Mungu, si bora nimfiche tu!

“hahaa, Chande bwana nimeona hapa Insta leo ndio naona kamrembo, kanaitwa nani?” duh aliposema hivyo ndiyo nikashtuka kuwa anayemzungumzia hapo si mwingine bali ni Joy niliyempost.


JOY, JOYCE 40

“mmh anaitwa Joy, lakini nimeachana naye,” nilidanganya, nikasikia anaguna halafu kuna sauti ya mama pembeni, ndiyo nikasikiliza vizuri mawimbi yake nikagundua kumbe nilikuwa laudispika na mama alikuwa akisikia! nikawa nimekosa kauli.

“we chande acha uongo, umempost leo hapa halafu unasema umeachana naye, halafu sio vizuri, usiwaache hovyo watoto wa watu, kuna magonjwa kibao. Aya basi tulijua ndiyo wifi !” alisema hivyo na kumalizia salamu za kwa heri nikakata simu.

Aisee nikaanza kuvuta picha naenda kumtambulisha Joy kwetu, mama angefurahi na hivi yupo peke yake nyumbani naye amezaa watoto wa kiume tu, nasi hata vitoto hatuna na hatujaoa. Hivyo amekuwa kijumbe wa upweke, hana wakucheka naye huko nyumbani.

Na mie nae nitaoa lini? Nilijilaumu lakini woga wangu hao wasichana nawaogopa mno, nawaandika kwenye stori wee lakini hawatabiriki na siyo wa kuwatumania pengine labda nikitaka kuoa nitafanya interview ya mapenzi niwapime wasichana katika mizani haswa ya maswali na mitego.

Mmh hapo ndiyo likaja wazo la kuandika stori ya Love Interview kwa wale walioisoma. Nikaichora njia zake kichwani huku natembea kuelekea kukutana na Joy.

Kidogo nikasikia kimeseji kimeingia kutoka kwa sista Alphonsina akisema nipigie, nilipopiga akaniambia:

“Chande, nilikuwa naongea na mama hapa, nilimletea hela yake ya mazao, akasema wanangu wangekuwa wanafamilia ningewapa vijihela vya mitaji wakwe zangu, lakini hawana acha nibakie nazo mwenyewe,”

“weee acha wee! Kama shilingi ngapi hivi?” niliuliza akiwa amenivuruga.

“nyingi anataka kutoa milioni mbili- mbili sasa nikasema mbona Chande ana mtu!“ alisema Sista. Jicho likanitoka.

“nilikuwa nakutania ninaye ndiyo yuleyule, sijaachana naye,”

“hahaa, kweli?”

“ndiyo, bwana,”

“sasa kama ni kweli njoo naye umtambulishe wiki ijayo si Christmass? Mie Nitakuwepo.” Alisema nikaona loh hapo sasa huyo Joy nitamtumia vizuri nyoko zake.

Basi nikafika zangu hapo Hongera Bar na kutafuta meza aliyopo Joy maana aliniambia ameshafika muda. Nikasikia psiiipsii. Nilipogeuka nusu nikimbie maana niliwaona Joy na Joyce wamekaa tulii wakinitazama. Yaani walikuwa kichekesho kwa walivyofanana kama yai na yai jingine.



Nilitembea kuwafuata nikijitahidi kuzuia ile jinsi nilivyoshangaa. Nikafika na kuketi nikaagiza maji na kusikilizia maana nilijishtukia balaa. Nikawa navungavunga maana baada ya salamu bado niliona wamekaa kimya, huyo mmoja akiwa ameinama kama vile ana wasiwasi na mawazo, huyo mwingine akiwa tu anachezea simu yake. So hapo nadhani hata wewe ungeng’amua kuwa Joy ni nani na Joyce ni nani.

“nimeshafika mbona kimya?” niliuliza.

“aah samahani Chaxy tunamsubiri Chriss,” alisema Joyce. Na mie nikajiongeza kuwa Chriss wamemuita ili kutaka kumaliza hili sakata.

Loh lakini mie ningependa liendelee ili nipate listori la kufa mtu, ikiishia hapo itakuwa fupi mno, bwana. nakumbuka nikakaa kabisa nikiombea mambo yaharibike aidha Chriss asije, na akija asikubali ukweli.

Lakini nikaumbuka maana Chriss alifika naye akashangaa kama mimi, akageuka na kunitazama kwa hasira. Nikainua mabega nikijifanyia amani.

“Jamani Chriss, nikwambie tu ukweli yaliyotokea, mchezo mzima niliucheza mimi kwa kutumia baadhi ya vitu vya Joy kuwagombanisha,” alianza kufunguka Joyce.

“Chriss mimi ndiye niliyepiga picha na Damian na kukutumia ili niwatenganisheni, na mimi ndiye niliyepiga picha na Chaxy nikijifanya Joy ili mradi tu kuwarudisheni penzi lenu,” alisema; Chriss akashtuka akimtazama huyo Joy wake aliyeinama pembeni.

Mie wala ndiyo kwanza nikanyanyua chupa langu la maji na kupiga tarumbeta. Joyce akaonekana ananitazama kwa mshangao maana alitegemea ningeshtuka pia.

“So, nini sababu ya kuyafanya yote haya Joyce?” aliuliza Chriss.

“nadhani Joy atakusimulia kila kitu, lakini nikwambie tu kuwa Joy anakupenda na alikuwa tayari kufanya lolote ili mipango yenu ya ndoa irudi, nilimuonea wivu tu,“ alisema Joyce.

Mie nikaweka sura ya kuboreka maana ilikuwa kama vile unaangalia muvi mwanzo mwisho halafu unarudia tena.

“kwa hiyo kwanini mimi mmeniita hapa?” niliuliza.

“Ah Chaxy kusema kweli nilitaka tu nikuombe msamaha mimi binafsi kwa kukutumia, najua hautanielewa lakini nilifanya vile ili nirudiane na Chriss, samahani sana,” alisema Joy sasa.

“haahaa hata msijali nilishajuaga hilo mapema, labda kikubwa ni mimi kuwaomba msamaha nyinyi kwa kuwatumia,” nilisema nikiwatega. Wakashangaa wote.

“Ulijuaje!” alisema Joyce.


JOY,JOYCE 42

Basi nikawaeleza nilivyofanya, nikiruka ile sehemu ya kuwa niliganda kwao nikiwachungulia wakipanga mikakati, nikajifanya tu nilitumia saikolojia, halafu sasa kuchanganya zaidi nikamwambia Joyce ajiangalie ile alama ya wino niliyombandika nayo. Loh akajipandisha brauzi na kuona akashtuka. Nikacheka tu.

“so nawe unaomba msamaha wa kututumia kivipi?” aliuliza Joyce.

“kuna stori nilianza kuandika tangu mara ya kwanza nilipokutana na visa vyenu, kwahiyo naomba msamaha kwa kuwa natumia mambo yenu kukamilisha kitabu changu,”

“mmmh! Chaxy acha utani! Kwani wewe unaandikaga stori?” aliuliza Joyce.

“ndiyo! Zipo mtandaoni instagram na Facebook..”

“napenda sana stori, hauna kitabu?”

“hapana nasubiri zikifika ishirini na tano hivi ndiyo nitaacha kuandika na kubakia kuchapisha tu,” nilisema, Joyce akaonekana amevutiwa kabisa na maongezi yangu. Wakati huo Joy na bwana ake waliomba kusogea meza jirani ili kuyamaliza vizuri.

Mie na huo mcharuko tukabaki pale.

“enhee Joyce hebu acha hayo Nina swali?”

“niulize.”

“ina maana hata lile penzi ulinipa siku ile ili mradi tu kuokoa penzi la Joy au?”

“hahaa kwanini unauliza hivyo?”

“unajua naandika hiyo stori, sasa wasomaji wangu wangependa kujua! Usiwanyime haki yao pliz!”

“hahaa! Okey, lile penzi nilikupa tu kwa sababu nilikuonea huruma,”

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG