Chombezo : Haunikomoi, Tunakomoana
Sehemu Ya Nne (4)
Nikajikuta na mimi huku napokea simu za mapaparazi na waandishi wa habari wengi mno. nikajaribu kumpigia rafiki yangu yule producer akaniambia angenisindikiza kwenye vyombo vya habari na kunielekeza nini cha kusema na nini cha kuacha.
siku hiyo wakati natoka sasa nyumbani na pikipiki yangu kwenda kwa Producer, nilijikuta nazomewa na watu wasionijua wakidai wangenipiga kama namkatili Merina, wengine wakanirushia hadi mawe, asante Mungu niliweza kukwepa, tazama jinsi maneno ya Merina yalivyonitia hatiani.
"sikia kaka leo usiku Merina anatoa wimbo anadai ndani ya huo wimbo ataelezea jinsi alivyokua akinyanyasika kwenye ndoa yake ili mashabiki zake wajue, kwa maana hiyo leo usiku anakumaliza kabisa," alisema Producer.
"dah, huyu mwanamke sijui amebadilika na nini?" nilinung'unika.
"lakini siyo hilo tu, chama cha wanasheria wanawake wameungana naye, wanadai wanamsapoti Merina na wanamtaka waziri wa jinsia,watoto na vijana aingilie kati na kukuchukulia hatua uwe mfano kwa kumnyanyasa mwanamke," aliongeza Producer huku akinionesha habari hizo zikitapakaa instagram.
"aisee, huyu mwanamke ni shetani.." nilijikuta naropoka.
"lakini kaka si ulisema Merina hana tatizo?" alinikumbushia Producer.
"dah, kuna mengi kifuani kwangu, kaka," nilisema kwa uchungu huku nikitetemeka.
"aisee, lakini yote hayo japo yamekumaliza ila kuna kitu tunaweza kukifanya ukarudisha hadhi yako, mwenzio anakuzidi kete kwasababu ni mwanamke, cha pili kwasababu ni msanii anasikilizwa sana kuliko wewe, wewe hauna kitu, ili kushindana naye, inapaswa tutembelee hihii skendo," alinipanga Producer.
"nielekeze nifanyeje?" nilisema.
"nimewapigia waandishi wa habari wachache, hapa cha kufanya utaelezea taratibu kuanzia ulivyokutana na Merinahadi hivi sasa na kuifanya kuwa stori ya kusisimua. Hii itakuwa ni interview ndefu sana, ambayo ukiielezea vizuri kwa simanzi ndipo utakapowagusa watu hisia zao na watambadilikia Merina, Na mimi hapo utakuwa umenisaidia kweli maana tangu nimemtoa msanii wako amenisahau na ameenda kurekodi kwa maproducer wengine. Pesa ambaz ningeweza kupata kwa ile kazi niliyomfanyia kishkaji kipindi kile ikamtoa, ningeweza kununua hata gari bro, inaniuma kweli,"
Alisema Producer nikakubaliana naye moja kwa moja.
Kweli waandishi aliowaita walikuwa wa gazeti la udaku mmoja, wa redio mmoja na wa televisheni mmoja, wote ni wa vyombo vikubwa tu, ambavyo naomba nisivitaje hapa.
Nikawaambia ningependa kuwasimulia Merina ni nani hasa kuanzia tulipoonana hadi tulipofikia hivi sasa na wao wakawasha virekodio vyao. Basi nikaanza kusimulia taratibu nikiweka simanzi zangu zote kama produceer alivyonielekeza, nikatoa na ushahidi wa vielelezo na interview ilikuwa ndefu na yenye kumaliza saa moja nzima na humo nilieleza kila kitu kabisa hadi nikalia na niligundua machozi hayakuwa ya kuigiza bali yalinitoka kweli kwa uchungu mkuu.
Wale waandishi wa habari wakasikitika sana na kusema wangeitoa haraka kesho yake ili ukweli ufahamike. Nikaachana na Producer nakurudi zangu nyumbani. Sebuleni nikamkuta Merina na wasanii wenzake na yule Promoter Omary wakiwa wanakunywa na kujiachia, nilipopita tu Omary akasema; " hivi Merina hii nyumba ni yako au? maana tusije tukapigwa bure!"
Merina akasema; "yangu bwanaa.." nyie kunyweni hata kulala niambieni mtalala hapahapa.
Kiunyonge nikaingia zangu chumbani kwangu, nikajitahidi kuuvuta usingizi nikikinzana na makelele ya huko sebuleni, lakini ghafla kelele zikaisha na nyumba ikatulia nikaweza kuupata usingizi walau. Mara hausigelo wangu akanigongea nakuniletea chakula, siku zote niliona ananionea huruma mno, lakini aliogopa kunisemesha, ila siku hiyo niliona ana kitu cha kuongea, nikamtaka aniambie, akasema alimsikia Meriina anapigiwa simu na watu wakitaka hela la sivyo kesho wanaachia interview yangu kwenye vyombo vya habari.
Doh haraka nikagundua kuwa ni wale wanahabari hawakuwa waaminifu, wanataka kutumia interview tuliyoifanya kujipatia hela kwa Merina. Nikamuuliza hausigelo kama Merina amesemaje.
Akaniambia kuwa Merina na Meneja wake wameondoka haraka kukutana na hao waandishi ili wakafanye malipo. Aisee nilisikitika sana, nikampigia simu Producer wangu nikimuelezea yote yaliyotokea, akasikitika sana lakini alinipa moyo kuwa nipo vitani na vita hii nitaishinda kwa sababu mimi naongea ukweli na Merina na kundi lake wanasimamia uongo.
Producer akaniambia kuna njia ya kumfanya Merina asiweze kutumia kiburi cha fedha, akanitaka nirudi tena haraka studio kwake.
Kweli nikamuaga dada wa kazi na nikarudi haraka kukutana naye, nikamkuta akiwapanga waandishi wengine nane. Akanitazama na kuniambia; "sikia, inavyoonekana kila mwandishi tutakayemtumia, Merina atampa pesa ili asiitoe hii habari. sasa tunawatumia waandishi hawa kumla pesa mkeo, hizo pesa zitakuja kwetu na kila akifurukuta tutazidi kumbana, matokeo yake atafilisika na hao wanamsaidia watamchoka na kumkimbia, kama upo tayari kwa hili tupe namba ya Merina..tumpigie hapahapa."
"Hii hapa," nilisema nakumpa Producer, producer akampatia mwandishi wa kwanza tukiwa wote palepale usiku huo.
"Hallow, Merina.. unaongea na Sanga hapa mwandishi wa habari kutoka gazeti la (jina kapuni), nina habari yako hapa nimetaka kuirusha kwenye gazeti langu lakini nataka kujua unalipi la kusema kwa upande wako," alisema huyo mwandishi akizunguka kama vile lengo lake sio kuomba rushwa.
"habari gani?" ilikuwa sauti ya Merina iliyokuwa na shaka mno.
"habari ya mumeo akisimulia tangu mlivyokutana hadi uhusiano wenu ulivyo sasa.."
"sikia kaka yangu, naomba hiyo habari usiitoe jamani, sema unataka shilingi ngapi?" alisema Merina, ikawa wazi kuwa alikuwa na jeuri ya pesa. Sasa kwa kusema hivyo yule producer wangu akamnong'oneza yule mwandishi kuwa aseme anahitaji shilingi milioni moja.
Naye bila hiyana akasema: "milioni moja."
"Sema nikutumie kwa namba ipi?" ilikuwa sauti ya Merina.
"Tuma kupitia namba hiihii," alisema huyo Sanga, dakika si nyingi ikaingia hela tukishuhudia palepale. Producer na yule mwandishi wakaenda haraka kuitoa, wakaileta mezani na sasa ikawa zamu ya mwandishi mwingine. naye akapiga simu, ikawa vilevile lakini safari hii Producer aliongeza dau na kufanya milioni mbili. Cha ajabu Merina akaitoa pia. zoezi likawa lilelile ikaenda kutolewa na kuletwa mezani.
Ikawa kwa mwandishi wa tatu, hapo kidogo Merina alikomaa na kusema hana kiasi cha milioni tatu alichotajiwa, akaomba atoe milioni moja ambayo hata hiyo producer alimwambia mwandishi asiikatae. Ikaenda kwa kushuka hadi mwandishi wa mwisho alikubali kwa laki tatu.
Kwa ujumla tukajikuta tuna milioni kumi na tano na laki nane. nilishangaa mno. producer akawapa wale waandishi milioni tano na laki nane wagawane, wakaondoka wakiwa wanafuraha kwa sababu hawakutegemea kuzipata pesa hizo kirahisi hivyo zilizobakia producer akaniambia tugawane sawasawa, mimi nikaondoka na milioni tano na yeye hivyohivyo. Na kama haitoshi akaniambia kesho yake, tutafanya zoezi lilelile kwa kutumia waandishi wengine.
Nilirudi nyumbani nakugundua mke wangu hakuwa amerudi ni wazi alikuwa amechanganyikiwa kiasi cha kutoa hela hovyo kiasi kile. Nikajiuliza atakuwa na pesa kiasi gani ndani kwake kiasi cha kukitapanya ovyo ili mradi kujiepusha tu na kudhalilika?
Kabla sijalaza ubavu wangu kitandani, nikapokea simu kwa namba mpya. Aliyezungumza alikuwa ni mwanaume mwenye sauti ya kilevi mno, nikagundua hakuwa mwingine bali ni Omary yule Promoter wa mke wangu; akasema: "hahaa, naona umeamua kumharibia mkeo eee! sawa lakini mapambano yako ni sawasawa na mende unataka kunyanyua kabati, mkeo ni mtu mkubwa anajuana na watu wakubwa, jiangalie sana la sivyo hautabakia uraiani."
Ilikuwa wazi ni kitisho kikubwa mno nami nilikuwa chap kumrekodi sauti yake tangu mwanzo nilipogundua kuwa ni Omary.
"Nafahamu mke wangu ni mtu mkubwa, lakini ningefanyaje wakati ananichafua kila siku kuwa mimi nampigaga, namjia na wanaume ndani na nimemuambukiza magonjwa, wakati yeye ndiye aliyenifanyia hayo yote?" nilisema.
"Kosa lako nilishakwambia unang'ang'ania sana kuwa na Merina, si umuache ale maisha mtoto wa watu? sasa nakupa onyo, tukiona mwandishi yoyote anatupigia simu na habari zako, ujue na wewe huko ulipo hautakuwa salama," alisema promoter bila kujua namrekodi akakata simu yake, ishara ya kuwa amemaliza alichopanga kuniambia.
Niliyamezea usiku ule na asubuhi nikaamkia kwa producer wangu niliyemkuta akifurahia mno kuniona, akanielezea mipango ilivyoenda na kusema kuwa siku hiyo waandishi wapya aliwaseti wataanzia pesa ya laki moja na jumla yao walikuwa watano.
"sikia ndugu yangu, jana nilipokea simu ya vitisho, isikie!" nilimfungulia simu yangu naye akaisikiliza kwa makini sauti ya Promoter Omary ikirindima.
"Duh! kaka umekuwa na akili sana kumrekodi, hii itatusaidia sana , nitumie," alisema nikamtumia. "Naomba tusiendelee na mchezo wa kumpigia Merina kwa kutumia waandishi wa habari." nilisema.
"kaka unambwela wenzio wanakutisha ili mradi usiwachome kwasababu ya huo wimbo walioutoa jana. Wenzio walikutumia wewe kama kiki yao ili wauze na sasa wanaogopa interview yako itawaumbua na watu watamchukia kabla hajafanya shoo yoyote..Na kuchukiwa kwake na mashabiki maana yake hatouza tena na kwenye gemu ya muziki itakuwa ndiyo kwaheri kwake..sasa nikuulize wewe kwanini unaogopa?" alisema Producer lakini nikakomalia kutofautiana naye kwenye hilo, japo alinishawishi sana kuwa maneno ya Omary yalikuwa ni mkwara mtupu.
hata hivyo bado sikukubaliana naye na ikamlazimu akubaliane na mawazo yangu; nikaondoka zangu, lakini kumbe yeye kisirisiri aliendelea kutumia waandishi kumkamua pesa Merina na hiyo ilinigharimu maana nilikuja kushtukia siku chache tu baadaye nafuatwa na askari kwa kosa lisilojulikana na kuishia kituo cha polisi Oysterbay.
Cha kushangaza nikiwa huko, sikusikilizwa na polisi; sikuambiwa nawekwa rumande kwa kosa gani na mbaya zaidi polisi hawakutaka hata niwataarifu ndugu zangu kuwa nipo wapi.
Yote haya nilikuja kufahamu kuwa ni kazi ya mke wangu Merina kwasababu alikuja usiku pale kituoni akanitazama kupitia nondo za rumande na kucheka sana kisha akasema atanikomesha na kama hiyo haitoshi nilimuona akiwa na yule Promoter wake Omary na mwanaume mwingine wakazungumza na mkuu wa kituo cha polisi pale wakimtaka aendelee kunishikilia hadi pale watakapoamua wao.
Ni kweli alionekana anafahamiana na watu wakubwa na kama kweli ningeendelea kushindana naye angeweza hata kuniua. Loh! ilikuwa ni ngumu kuwa huyo aliyenifanyia yote hayo alikuwa mwanamke wa maisha yangu ambaye niliwahi kulala naye hadi kitanda kimoja na kushea naye penzi.
Siku tatu mfululizo nilikuwa mle ndani, nikiwapokea wenzangu na kuwaaga wakaniacha mimi palepale, hatimaye nilishangaa tu usiku mmoja akija producer wangu mbiombio na kunitoa pale ndani.
"Aisee pole sana Cliff," alisema na kunihadithia kuwa yeye ni chanzo cha mimi kuwekwa rumande kwa kuwa aliendelea kumtishia Merina kutoa interview yangu, nilikasirika mno kulijua hilo, lakini aliniomba msamaha na kusema yeye pia ndiye aliyenitoa ndani na alidai sasa ameishammaliza Merina.
Nikamuuliza amemmalizaje; ndio akaniambia ameongea na wahariri wa magazeti mbalimbali na kufanikiwa kuchapisha habari nzima ambayo ilikuwa imeshaanza kutoka siku hiyo asubuhi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment