Search This Blog

Wednesday, January 25, 2023

CORONA AKEE - 3

   

Chombezo : Corona Akee

Sehemu Ya Tatu (3)



BASI hivyo ndivyo alivyoandika Neema na kutuma meseji ile kwa Cliff aliyejibu kwa kifupi; "mh.."

Neema sasa akatoka taratibu mle chumbani gauni la bluu, kiremba cheupe, mawani ya kusomea yakiwa yameegeshwa vyema juu ya mianzi ya pua yake nyembamba; soksi ndefu zilizotokomea chini ya skuna za chini kabisa. Akafanana tikatika na picha ya kitambulisho chake cha utawa kutoka monasteri ya Italia jiji la Rome palepale mji wa mtakatifu Petro.

Hakika Neema sasa alikuwa ni sista Anne kama ambavyo jina lake la utawani lilipaswa kuwa. Akashuka kutoka mle hotelini na kutembea kama mfuasi thabiti wa Yesu Kristu, unadhifu na mabadiliko hayo hakika hakuna aliyeweza kusema kuwa huyo ndiye Neema aliyekuwa na Cliff.

Utofauti wake ukaufanya ukumbi mzima umtazame, naye macho ya watu akayakinga na ufito wa shaba ye pembeni ya miwani yake aibu ikavumilika. Naye Neema alikwishatarajia hilo kutoka kwa watu maana wakati wengine wakianza kukurupuliwa mahotelini na maaskari na kupimwa kwa shuruti, yeye akasalimiwa kwa heshima na viongozi.

"Tumsifu Yesu Kristu, sista, wewe ni mgeni wetu pia?" aliuliza Meneja wa Hoteli akiwa na wasiwasi na lugha yake maana rangi ya Neema ilikuwa na hatihati kuwa ni msauzi au mbrazili, wazo la kuwa ni mtanzania lilikuwa dogo mno kichwani mwa meneja huyo.

"milele amina, ndiyo ni mgeni nimefika jana kutokea Roma. nilisikia simu ikiita lakini nilikuwa kwenye sala ya asubuhi. tafadhali hapa tunaelekea wapi samahani sifahamu utaratibu," alisema Neema mikono yake ikiwa inazungusha tufe za rozali kubwa mkononi mwake.

"ooh nadhani utakuwa umemiss maelekezo ya mheshimiwa mkuu wa mkoa, ni hivi wageni waliotokea Italia wataenda upande ule pale. Utakuwa na passport size yako hapo ili nikushughulikie haraka?" alisema meneja, Neema akampatia passport yake, haraka Meneja akamuomba Neema aongozane naye, basi wakavunja utaratibu na sista akapishwa kupima yeye kwanza.

Vipimo vikaonesha hakuwa na chochote, wakati huo Cliff alikuwa akiduwaa huyoo, akaamini aliyoyasema Neema kuwa atatoka tofauti kabisa.

"Sista Anne, natumai hii dhalura ya leo haitakufanya uichukie hoteli yetu," alisema Meneja aliyejitenga kusimama na sista mahala,




Mikono yake ikionesha heshima na adabu, lakini kwa jicho la ndani kabisaalikuwa akidadisi kitu na Neema aligundua hilo.

"hapana, hii ipo kila mahali, fikiria hata Papa ameruhusu turudi na shughuli za kanisa zimesitishwa sasa hivi huko Roma, kwa hapa Tanzania hii hatua imechelewa lakini nashukuru kuna jitihada za kuzuia huu ugonjwa," alisema Neema kisomi akajibu.

"Aisee Mungu atunusuru," alisema Meneja.

"Ni mitihani tu na tutaushinda, Mungu daima ni mwema," "hivi samahani, ulifikia chumba gani? nataka nihakikishe unapata huduma zote stahiki," aliamua kusema Meneja akifungua kile kitabu cha register ya wageni.

Neema akakenua meno maana alikuwa ameshalijua hili kabla, akasema sasa ule uongo kuwa eti kutokana na ndege yake kughairishwa mara kadhaa akafanyiwa booking na dereva wa parokia ambaye ndiye Cliff, loh meneja akaomba hata Cliff pia apimwe haraka na kuheshimiwa.

Na ndiyo hapo sasa Neema akafanya kumpelemba meneja aweze kufanya iwezekanavyo apate kuondoka hotelini hapo siku hiyohiyo.

"Dah sista hapa kutoka ni ngumu, mwambie tu askofu atakuelewa maana hata mimi mwenyewe nipo kwenye lockdown sitakiwi kuondoka na wenye mamlaka ni mkuu wa mkoa na askari wake. Nakupa siri tu hapa mpaka sasa kuna wagonjwa watatu wamegundulika na sisi wengine tunaweza kuwa tumeambukizwa kifo njenje sista," alisema Meneja akihamisha macho yake kutoka kwa Neema hadi kwa Cliff kisha akauliza.

"sasa braza jana usiku ulivyomleta sista kutokea airport ulilala wapi? si ungetuambia tungekupa chumba kingine?"


Swali hilo lilikuwa kama vile mwiba kwa Cliff akashtuka akamtazama Neema huku kichwa chake kikiwaza kwa haraka mno.

"Nililala kwenye gari yangu maana ratiba zilionesha leo mchana tutaondoka kuelekea parokiani," alijibu Cliff akiunganisha uongo wake vizuri. Sista Anne ama Neema kama tumjuavyo akapumua taratibu chinichini maana alizuia hofu yake asiheme kwa muda;lakini wakati huo yule meneja alikuwa akipekuwa kiregister na kumuita pembeni Cliff.

"Niliambiwa na wahudumu wangu kuwa ulipanga hapa tangu majuzi na ulikuwa na binti fulani mkilala mle ndani kabla ya sista kuja; kwa sababu wewe ni mfanyakazi wa kanisa ninakukaushia sijamwambia sista uovu wako na jambo baya kabisa ilibidi hadi huyo msichana awepo hapa leo karantini," alisema meneja akikenua meno yake hadi mwisho.

Japokuwa Cliff alichukia lakini akazuga kujifanya anashukuru sana kwa meneja kumfichia siri yake na akacheka kimoyomoyo kuwa laiti kama meneja angefahamu kuwa huyo msichana anayemzungumzia ndiyo sista Anne sijui angefanyaje.

"Niliteleza tu meneja si unajua tena, sisi wote wanaume," alisema kwa aibu Cliff. Meneja akacheka na pamoja wakacheka kwa kuviziana.

"Sasa leo jioni nitafute nitakupa chumba kingine," alisema meneja na Cliff akashukuru. Meneja akaondoka zake kuelekea na majukumu yake na Cliff akarudi kwa Neema kijasho kikimtiririka.

"Alikuwa anasemaje?" aliuliza Neema kwa sauti ya wasiwasi ya chinichini huku akilinda haiba yake ya usista isiharibike.

Cliff akajitia naye kuwa na adabu akamhadithia sista Anne alivyoulizwa na meneja na namna alivyotumia akili kujibu maswali yake.

"Dah! hili limeisha,pia nitamdanganya baba nilifika hapa jana na kuzuiwa karantini; kwangu nitakuwa nimemaliza cha msingi tusubiri tu hizo siku kumi na tano za karantini," alisema Neema tabasamu likianza kumrejea.

"So..!?"" aliuliza Cliff akiulizia mpango wa kupata punino la Neema maana aliona kama kutenganishwa chumba na Neema ndiyo kunamkosesha masijala.

"we Cliff hebu kuwa na adabu kwanza bado tu unataka?"

"ndiyo.." alilalamika Cliff.

"tutaona itakuwaje, hebu kwanza tutulie tusikilize utaratibu," alisema Neema ikawa kwa vazi lake la kitawa Cliff mwenyewe akaona haya kuendelea kubembeleza zaidi.



Basi baada ya kupimwa pale, ikatangazwa wagonjwa wenye corona ni wanne, na waliokuwa wanatiliwa mashaka kwakuwa walikuwa karibu na wagonjwa hao ni watu kumi; wakati huo wengine wakatakiwa kuendelea kubakia kwa siku kumi na tano zilezile.

hofu sasa ikazuka kwa kila mtu kuwa hatihati ya kifo ilikuwa ikiwakabili lakini si kwa Cliff wala Neema. Wakaelekezwa jinsi ya kuziba nyuso zao na kusalimiana, wakaelekezwa jinsi ya kunawa kwa sanitizer na kutakiwa kubakia kwenye vyumba vyao wakiwasiliana na ndugu na jamaa zao kuwatoa wasiwasi.

Wakarudi mavyumbani mwao, wakati huo hoteli nzima ikawa inapuliziwa madawa ili kuondoa virusi watakaokuwa wamezagaa sehemu mbalimbali bila kujulikana.

Mbaya zaidi Cliff akapatiwa chumba magharibi kabisa mwa hoteli, Neema akawa mashariki kabisa. huku agizo la kila mtu kubakia chumbani kwake likitangazwa na askari wakilinda korido na varanda; asitoke mtu. ubaya wa tangazo hilo aliyekuwa singo alibakia singo chumbani mwake asitoke, aliyekuwa na mtu wake akatakiwa kujifungia na mtu wake hivyohivyo; Loh Cliff na Neema wakagundua japokuwa kujidhihirisha utawa kwa Neema kulisaidia kuondoa wasiwasi wa kushtukiwa kwa Neema lakini iliharibu mpango wao wa kuwa pamoja doh!

Cliff akapiga ukuta kwa hasira akiwaza ni siku kumi na tano mbele hadi waonane na Neema tena, kwa hiyo kwa mara nyingine anakosa penzi loh!

ghafla wakati akiwaza hivyo simu yake iliita, ni mpenzi wake polisi Grace kwa hasira akashindwa kupokea, lakini ikaingia meseji.

"sorry dia, nakukumbusha kesho kutwa ndiyo ile birthday yangu, nimeshaandaa kila kitu, miss you!" i



lOh! hiyo meseji ikamshtua Cliff ilionekana alikua bize mno na kuwaza penzi la Neema kiasi kwamba akasahau kabisa kuhusu ya demu wake, huyo Afisa wa jeshi la polisi Mwanza.

Kwa taarifa yako gari,utanashati na fedha alizokuwa nazo Cliff jeuri yote ilitoka kwa Grace, na ndiyo eti asionekane Marioo kwenye familia ya Grace akapachikwa kwa muda kwenye kiofisi cha bima hapo Arusha kwa koneksheni ya Grace pasina mshahara. Maana yake hata akitambulishwa kwenye familia ya Grace apate kuonekana ana kazi fulani kwasababu Grace kwao kuanzia bibi yake mpaka marehemu babu yake ni wanausalama tu, huyu kikosi cha magereza, yule afisa jeshi la kujenga Taifa na hata asiye na kazi kwao alikuwa ni afisa wa jeshi la zima moto.

Kwa tafsiri hiyo kwao ni watu wakubwa tu na baba yake sasa ndiye huyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, RPC Harlod Mabula; mtu mwenye manyota na wadhifa naye akamfanya hata mwanaye katika umri wake mdogo wa miaka 26 tayari alikuwa afisa.

Kusema za kweli sio kwamba Grace ni mzuri, hapana ila ukichanganya na fedha zake na cheo chake hata kama sio mweupe ataonekana mweupe; hata kama hana tako, tako litaonekana tu na atavumilika; huo ndiyo msimamo wa wanaume na ndio uliomfanya Grace akawa kipusa kwa Cliff.

Sasa nikupe tu siri msomaji wangu, ni kwamba huyo CLiff alikuwa ameshajipenyeza kwenye familia ya mzee Harlod na alikuwa ameshatambulishwa kwa mama yake Grace, lakini rasmi kabisa utambulisho wa Cliff kwa familia nzima ulipaswa kuwa ni hiyo siku ya tarehe 10 ambayo ndiyo birthday ya Grace, waliyopanga kupeleka posa na Mungu akibariki wavalishane pete hapohapo ukumbini.

kwahiyo basi meseji ya Grace kumkumbusha Cliff ilikuwa na maana kwamba kila kitu kwa upande wake kulikuwa shwari ni yeye tu kwenda ukumbini na pete yake.

Cliff akaisoma ile meseji na kutetemeka hadi utumbo, akapata homa yabisi mifupa ikamkakamaa. Akawaza cha kufanya. Akaona asikurupuke kujibu ile meseji; akashusha pumzi na kufumba kope zake alipofumbua macho akasogea kwenye droo akachukua notebook mpya aliyoiona juu ya meza ikiwa na peni; nadhani kila chumba cha hoteli hiyo kilikuwa na hizo notebook.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG