IMEANDIKWA NA : CHANDE ABDALLAH
********************************************************************************
Chombezo : Haunikomoi, Tunakomoana
Sehemu Ya Kwanza (1)
Nyie wengine najua mkiulizwa mlikutana wapi na wenzi wenu, stori zenu zinaanziaga kwa kusema siku ya kwanza mlikutana kanisani, sokoni, shuleni au pengine kwenye daladala; lakini mimi na mke wangu kusema za ukweli tulikutana facebook.
Yeye akiwa ni msichana mzuri mwenye wingi wa likes, na comments chekwachekwa kwenye picha zake na inbox yake iliyojaa meseji za wanaume wakimuomba namba au penzi; vilevile friend requests zikiwa maelfu.
Katika hizo meseji zilizokuwa inbox ya Merina Paul, yangu ilikuwemo. Hizo friend requests zilizoshehheni kwake na yangu ilikuwemo; kwenye maelfu ya likes na comments zake na zangu zilikuwemo pia.
Niliamini kwa jinsi nilivyompenda nitampata tu kwani niliamini penzi langu limezidi wanaume wote wanaomtongozaga kila siku huko mtandaoni na mtaani pia.
wakati huo mimi nilikuwa hata kazi sina, hivyo posti na picha zangu za kinokia changu cha kubonyeza na sura yangu iliyopauka iliakisi hali yangu ya kimaisha na uwezo wangu wa kifedha kuwa ni hafifu.
Merina Paul! jina lake lilinisisimua na kila siku niliamka naye kwa salamu za asubuhi njema na kulala kwa usiku mwema. Nilijipa moyo kuwa kati ya wote mimi ndiyo nilizidi jitihada kwa Merina na nilijua kuwa pengine hiyo nitamfanya anikubalie friend request yangu na maombi ya kuwa rafiki yake ya maandishi ambayo niliyatuma messenger karibu kila wiki.
Lakini ikiwa kinyume chake, mwenzangu aliona usumbufu, nikaambulia kublockiwa ambayo hata sikuigundua hadi nilipoambiwa na rafiki yangu kuwa, nikiona sioni mtu facebook ujue nimeblockiwa.
Nilihuzunika na penzi hilo nikalikatia tamaa. Nikaendelea na maisha yangu na hatimaye nikapata kazi kwenye duka la jumla Kariakoo ambapo niliuza bidhaa mbalimbali za majumbani kuanzia sabuni,mafuta, sukari, chumvi na kadhalika, hapo maisha yangu kwa kiasi fulani yakapiga hatua.
Kwa miezi kadhaa na mimi nikaweza kufungua kimradi changu cha chipsi huku mtaani na kumuajiri mtu, nikawa nafanya kazi dukani na wakati huohuo kwenye biashara yangu, niliweza kuweka fedha zangu na malengo yangu yakawa yanatimia.
Ulipofika mwaka mzima niliweza kununua pikipiki pia na nikahama nyumbani kwa mama na baba na mimi nikaanza kujitegemea nikiwa na vimiradi vyangu mambo yakiniendea supa.
sasa nikaona ya nini nijinyime kupendeza kidogo ili niwe mwanaume wa kisasa? maana nilijisahau sana upande huo. basi nikawa naweka fedha zangu na sehemu ya faida naweka kwa ajili ya kununua nguo, kwenda bata kidogo na masela wangu na nyingine nikanunua simu nzuri ya smartphone.
Kwakua nilisahau hata password zangu za facebook nikafungua akaunti upya na kuanza kuwatafuta marafiki zangu tuliopotezana muda mrefu humo facebook. Nikawaomba urafiki akina Bitoz Juma, Mtu Chuma na wengine kibao, mwisho wa siku nikamkumbuka Merina Paul, nikaandika jina lake nikamsachi, loh! mwaka mzima ulikuwa na mabadiliko yake jamani. niliyemuona sikudhania kama ni yeye hadi nilivyomtazama vizuri.
Mbele yangu niliona picha ya msichana mrembo mno, rangi yake nyeupe zaidi na midomo iliyokolea lipshine ilionekana ikishereheshwa na tabasamu pana mno. ni macho tu yaliyonikumbusha kuwa huyo ni Merina, na kama siyo yeye basi anahusika naye mno.
Nikamuomba urafiki haraka, lakini tofauti na siku nyingine siku hiyo niliona nimekubaliwa fasta tu. nikafurahia mno, nikamtumia meseji inbox, mambo..
Akajibu poa, nikamsifia na kumuomba kama hatojali anipatie ruhusa ya kuchati naye bila kupitia vikwazo kama anavyowafanya wanaume wengine humo facebook.
Akacheka sana na kuniuliza: hivi nina vikwazo ee!
Nikajibu ndiyo, huku nikikumbushia enzi zile kwenye akaunti yangu aliyoniblock.
akashangaa sana na kusema nimebadilika, akaniomba msamaha.
Tangu hapo ndiyo tukajuana rasmi, akanitembelea nikamtembelea. Tukawa wapenzi, nikafurahia mno penzi hili. nami kwakuwa nilipenda mwenzangu awe na kazi ili tupige hatua kimaisha kwa kusaidiana, basi mwenzangu akaniambia anapenda sana mambo ya kuimbaimba, si biashara wala kuchoma maandazi.
Kwakuwa nilimpenda nikampeleka kwa mwanangu producer Magomeni akarekodi wimbo wake wa kwanza. haukuwa mzuri kivile, lakini alitushangaza maana tulipoupeleka redio ulipigwa mno, akaitwa sana kwenye interview hadi kwenye maredio makubwa.
Ikanipasa nimtolee bajeti ya video, ikashutiwa; na ndiyo kipindi hicho, rafiki yangu yule producer akaniita pembeni akaniambia: "sasa hivi shemeji utampoteza, kama vipi muachishe asiimbe tena au muoe!"
Nilielewa alichomaanisha, basi nikafanya mipango ya kumuoa haraka kwanza kabla ya kuendelea kuiachia video yake.
Na wiki chache tu tangu ile video tulipoiachia kwenye matelevisheni, mke wangu alijulikana sana. Yaani akipita hivi, watu walikuwa wakimsifu sana, jina la wimbo wake uitwao, Nakugawa. ulikuwa modomoni mwa wengi. Akajizolea mashabiki lukuki lakini wengi wao wakawa wanaume.
Hali hiyo ilinikera sana maana kwa mara ya kwanza nilipata kuona kuwa uzuri wa mke wangu haukunivutia mimi pekee bali ulikuwa ukiwavutia wengi na wengi walitamani awe wao. Hata simu yake ilisheheni meseji za kutongozwa na mbaya zaidi hata na watu maarufu wakiwemo wabunge, wasanii wakubwa wa maigizo na muziki pia.
Moyo wangu ulikuwa mdogo kuhimili haya mambo; sikujiandaa, nilipatwa na wasiwasi kila siku kiasi kwamba hata fedha tulizoziingiza kupitia muziki wa Merina kufikia tukanunua nyumba nzuri na gari la kutembelea, sikuziona utamu wake; nikasonona.
Kipindi hicho yule rafiki yangu producer ambaye jina lake aliitwa Piano Master kutokana na utaalamu wake wa kucharaza kinanda, akaniita tena pembeni akaniambia: "kaka shemeji utamkosa, aidha mpe mimba au muachishe mziki."
Loh! niliwaza na kuwazua kauli ile ya rafiki yangu, niliogopa kumwambia Merina wangu aache muziki kwa kuwa muziki upo rohoni mwake, na kwa maendeleo yote tuliyopiga kimaisha kwa muda mchache kupitia muziki wake, ni ujinga kumwambia aache muziki sasa wala baadae.
Nikaona nifuate ushauri wa pili wa rafiki yangu kuwa nimpe mimba. ndiyo ni wazo zuri ni bora awe na mimba ili wanaume wanaomzengea wajue kuwa ni mke wa mtu ili waondoke zao waniachie mke wangu.
Na mimba nilisikia ni njia moja wapo ya kumtuliza mwanamke mzuri ambaye ana mawenge. sijui kuhusu mke wangu kama ana mawenge au lah! lakini nilimuona ananiheshimu tu vizuri au labda pengine ni hofu yangu tu.
Hata hivyo sikutaka kuacha nafasi au kubeti penzi langu, wafitini ni wengi na vishawishi ni vingi pia mwanamke mzuri kama yeye kuvimudu peke yake akavishinda ni ngumu mno.
Nakumbuka jioni siku ile nilirudi nyumbani kwa kutumia pikipiki yangu binafsi ya kutembelea, nikamkuta mke wangu Merina na marafiki zake wasanii wakubwa wakike ambao hata mimi mwenyewe nilikuwa nawaonaga kupitia televisheni, majina yao naomba niyaweke sandukuni kwa sasa.
Nikawasalimia na Merina mke wangu akanitambulisha kwao. nikawaacha hapo sebuleni na mimi nikaingia chumbani kwangu, nikijilaza nikitafakari maneno ya producer. wakati kichwa changu kikiwa na mawazo mengi, masikio yangu hayakushindwa kusikiliza sauti za nasibu zilizokuwa zikipita kwenye kuta za chumba changu kutokea pale sebuleni ambapo mke wangu na rafikize walikuwa wamekaa.
Nikamsikia msanii mmoja wao akanisifia kwa Merina kuwa mimi ni Hendsamu, na Merina mke wangu akawaambia ndiyo sababu ametulia na mimi. nilifurahi kidogo kwa maneno hayo, na mi nikajipa moyo walau Merina wangu ananisemea vizuri.
Lakini wala mimi sio hendsamu kuliko baadhi ya wasanii mjini ambao kwa macho yangu nimeshuhudia wakimsumbua mke wangu! hii ilinipa homa ya moyo na kwenye tafakari ya ndani kabisa.
Nikiwa hapo ndani kidogo alinishtua Merina mwenyewe aliyeingia na kuniambia wageni wangependa kuniaga kwakuwa wanaenda makwao. basi nikatoka naye na pamoja tukawaaga wageni wetu, tena mke wangu alinikumbusha akaniambia.
"Cliff kaa nao nikupige picha, ya kumbukumbu." akachukua simu yake na mimi nikakaa katikati ya wasanii hao akanipiga picha na kutuonesha, aisee ilikuwa imetoka vizuri mno.
Basi tukaagana na mimi nikarudi ndani na mke wangu, nikianza kumpanga suala la mimi kutaka mtoto.
"Tuna kila kitu Merina, sidhani kama kuna tatizo sasa hivi ukinibebea mimba," nilisema.
"Na mimi nilikuwa nasubiri sana uniambie hivyo, maana kusema za ukweli mpaka sasa hapa sielewi najihisi kama nina ujauzito wako," alisema, nikastaajabu kwa furaha maana nilidhania angepinga suala la mimba kwa sababu ya kukuza jina lake, lakini la hasha.
"waoo mke wangu, basi kesho tukapime au?"
"sawa kesho mapema alfajiri," alisema..
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment