Search This Blog

Wednesday, January 25, 2023

HANITHI MPEVU - 3

   

Chombezo : Hanithi Mpevu

Sehemu Ya Tatu (3)


"aar mimi naenda Tanga mjini, lakini baada ya hapo nitazungukazunguka tu nataka niimalize Tanga yote," alijibu Renee akiachia tabasamu.

"mh tanga utaimaliza weye!? haha ni kubwa, sie tunashukia Muheza," "nimesikia unaenda kuwacheza mabinti zako, hongera umekuza," alianza maongezi Renee.

"asante hahaa, si unajua tena wanawake sie tuna mambo mengi ya kuyajua,"

"eeh wanakwambia samaki mkunje angali mbichi, mie natamani ningeyajua hayo mambo sema sie wabara hata hatufundwi."

"mh weee, kwa hiyo wewe msungo!" alisema huyo mama, Renee akakumbuka neno hilo alilisikia mama huyo akimwambia mwanaye Fetty saa chache nyuma na Fetty alilia, sasa inaonekana kabisa lilikuwa ni tusi hivyo Renee akachukia lakini akaficha na kufanya akatishe maongezi na huyo mama.

Muda huohuo Fetty na Mwajabu waliingia wakiwa na vifurushi vyao na soda.

"Asante dada yetu, chenji yako hii," walisema kwa pamoja mabinti hao, Fetty akirudisha chenji kwa Renee kisha wakaketi wakianza kula kwa fujo.

Sasa hata abiria wengine wakaanza kurejea na baada ya muda basi likaanza kuondoka.

Renee akamuuliza Fetty kwa kumnong'oneza: "Eti Fetty msungo ndio nini?"

"Msungo ni mtu ambaye hajachezwa," alijibu Fetty. lakini Renee akahisi amemuongopea.

"wewe mbona ulilia ulipoitwa Msungo na mama yako? sio tusi hilo!"

"ndiyo ni tusi, si mtu haujachezwa!"

"mh sasa kama ukiambiwa hujachezwa ndiyo ulie?" aliuliza Renee.

"ndiyo inauma, naona kama kanitukana tusi kubwa vile, yaani kuitwa Msungo ni zaidi ya tusi, usimruhusu mtu akuite hivyo," alisema Fetty. Renee kichwani akaishia kuguna tu. na ndiyo ikamzidishia kutaka kujua mambo ya huko asije kuitwa Msungo bure!

Baada ya muda mrefu kupita gari ikipanda vilima na kukunja kona nyingi ndiyo hatimaye, huyo mama alimuaga Renee.

"mdada tunashukuru sana na safari njema, sie tunashukia hapo Muheza,"

"aya jamani, ila kuna jambo nitakuomba unisaidie, naomba namba yako, nitakupigiaga," alisema Renee, akitoa kidaftari chake na kuandika na peni. "ni, sufuri.saba.." alisema huyo mama.

"niandike nani?"



"we andika tu Dahuu,"

"aya nitakupigia nikifika maana simu imeisha chaji,” alidanganya Renee. Akaagana na hao wasafiri wenzake walioshuka kisha gari likiendelea na safari.

***

Tanga, bado lilikuwa jiji lililopoa mno kwa Renee, hakuona bado hayo wanayoyasema watu kuwa huko ni mapenzi tu. Hiyo ni baada ya kuishi mwezi mzima sasa.

Na katika kipindi hicho chote aliishi kwenye chumba cha kupanga cha bei rahisi kabisa barabara ya sita. Akawa anatoka asubuhi anazurura na kurudi jioni. alitumia hela yake ya madafu yote na ilipoisha akachenji dola chache kati ya kile kibunda chake. akajikuta bado ana fedha nyingi za kuendelea kupuyanga kwenye jiji hilo.

Pengine kweli Tanga ilipoa kama alivyoiona Renee, au siyo kweli kwa sababu kwanza, Renee mwenyewe alitembea mchana tu na giza lilipoingia tu alirudi kwake. Pia hakwenda klabu wala mahala popote pa starehe kwa kuogopa huenda kuna mtu wa Dar angemuona mahala na kumletea shida.

Tena isitoshe hakuwa na laini bado, aliogopa kuwa akitumia vitambulisho vyake kwenye usajili atakamatwa, akaishi bila mawasiliano na hiyo ilimzidishia upweke na kuihukumu Tanga kuwa siyo ile aliyoivutia taswira yeye.

Akachukia na kujichukia na kuyajutia makosa yote aliyoyafanya. Naye kwa vile hakuzoeana na mtu yoyote hapo mtaani akaishia kila siku kwenda kwa mdada fulani wa duka la Hardware ambaye ni mbena mwenzake, yeye ndiye aliyemuombaga simu na kutia namba za Dahuu kila mara akijaribu kuzipiga na kukuta hazipatikani kabisa.

Siku hii alienda tena na akajiapiza itakuwa ni siku ya mwisho kufanya hivyo na kama Dahuu hakupatikana basi angeondoka kuicha Tanga maana alichukua namba zake ili mradi ampigie amwambie kuwa naye angependa kuingia Unyagoni, lakini siku zote hizo hakupatikana na yeye hakujifunza chochote. Akaona ni bora aende mkoa wowote mwingine na kuachana na hayo mambo ya kujitia ufundi.

Saa hii akachukua ile simu na kuipiga. loh akashangaa inaita.

"hallow,," alisema mwanamke akiwa kama ametoka kulala.

"hallow Dahuu?" aliita Renee kwa furaha kidogo.

"ndiyo, wewe nani?"



‘Mimi Renee, tulikutana kwenye gari la kuja Tanga,” alijitambulisha Renee.

“Renee?”

“ndio wewe ulikuwa na wanao wawili ulikuwa unawapeleka kuwafunda, nilikuomba namba yako nikaiandika pembeni,” alifafanua Renee.

“weeee, anhaaaa aisee, nilisahau jamani, mzima mdada?” alisema Dahuu kwa furaha huko alipo.

“mimi mzima, vipi za kwako? Wakina Fetty hawajambo?”

“hawajambo na hatujambo. Wewe vipi bado upo Tanga?”

“ndiyo, bado nipo huku,”

“oooh, sisi tumerejea tuna wiki sasa,”

“doh, basi nimekutafuta sana kwenye simu, nikawa sikupati,”

“loh jamani nilitumbukiza simu kwenye maji, na sikununua tena hadi leo asubuhi na namba yako ndiyo ya kwanza kuingia, pole.. nini ulichotaka kunieleza kwanza hadi kunitafuta huko?” aliuliza Dahuu.

“mh sijui nitakuwa nimechelewa?”

“kuchelewa kwa jambo gani? Nieleze kama kukusaidia nitaweza nitakusaidia tu..”

“nilikuwa nataka na mimi nifundwe, sasa sijui nimechelewa sijui bado! maana mimi ni msungo.”

“ooh, kumbe hilo.. mh! kiukweli mafundo hayana kuchelewa kuna ya msimu, ya bibi harusi, lakini kuna ya mtu binafsi kama anataka kufundwa mwenyewe basi anamlipa tu nyakanga anamfunza.”

“mimi nataka hayohayo ya binafsi tu nimlipe nyakanga unayemkubali ili anifunze,” alisema Renee kwa furaha kidogo.

“sasa hayo nikupe namba sijui? Maana kuna huyo kungwi wa Kitanga na huyu wa Kizanzibari, sasa sijui ratiba zako maana wa Kitanga yupo Pangani, na wa Kizanzibari yupo Unguja. Ila kila mmoja ana ujuzi wake, mimi binafsi na wanawake wengi tunamkubali wa Zanzibari, huyo watanga anafundisha ukahaba ndiyo maana hatumpendi..mimi mwenyewe niliwakatisha wanangu maana niliona anawaharibu japo shangazi zao ndio walitaka sana aende huko,”

“mh sasa hapo sijui, nitafanyaje? Wewe unanishauri niende wapi?” aliuliza Renee.

“mimi nakushauri uende zanzibari, huyo wa Tanga hapana kwa kweli,”

“mh sawa, naomba namba zake nijaribu kuwasiliana naye,” alisema Renee.

“aya, ngoja nimpigie kwanza nimpange halafu nakutumia, isije akawa kaenda Dubai maana naye mwingi, anafundisha maharusi hadi wa kiarabu,”

“mh aya, basi mwambie anishushie bei nisijeshindwa kulipa,” alisema Renee akichanganywa aliposikia kungwi wake mtarajiwa anafundisha hadi huko Dubai.



“aya..” alisema Dahuu. Akakata simu na baada ya dakika tano akampigia simu Renee.

“aya Renee una bahati nzuri, Kungwi yupo hapahapa Dar anawafunda watu tena kaja jana, unaweza kuwahi darasa la huku, maana mkiwa wengi bei ndogo, ila ukiwa peke yako gharama zinazidi. Akitoka hapa huyoo anaondoka kwenda Oman nasikia,” alisema Dahuu kwa bashasha, lakini Renee kwake haikuwa bahati nzuri hata kidogo ilikuwa mara kumi aende Zanzibar, kuliko kurudi Dar, maana alichokifanya huko alikijua mwenyewe.

“mh, natamani kuja, lakini sijui kama nitaweza, yaani ingekuwa Zanzibar ingekuwa rahisi, lakini sio Dar,” alisema Renee.

“mh kwani kuna nini huku?”

“mh, dada angu ni stori ndefu, lakini kama utaweza naomba uende sehemu Fulani hivi ukaniulizie watu fulani hivi, sijui utaweza?’

“wapi?”

“Kimara Temboni..”

“we mimi mbona nakaa Kimara Temboni pia,”

‘wee kweli?”

“ndiyo, unataka nimuulizie nani?”

“mh, naomba iwe siri yako lakini”

“usijali, we niamini,”

“naomba niulizie msichana anaitwa Mage anakaa kule mtaa wa buchani, mdogo wake aliwahi kuolewa na Mmarekani anaitwa Mary, mtaa mzima anawajua.. mwezi uliopita walikuwa na harusi ya kifahari sana. Mtu wa pili anaitwa Hermez, naomba niulizie hapo madukani nahisi amekwishafariki, naomba niulizie kazikwa Dar au Kasafirishwa na kesi yake inaendeleaje polisi juu ya muuaji..” alisema Renee.

“mh, kazi hiyo ujue?.”

“sikia nakutumia shilingi elfu ishirini, naomba uifanye, bila hivyo nitashindwa kurudi Dar,”

“he, kama unatuma hela sasa hivi naenda, au ngoja niwatume wakina Fetty.. we Fettyyyyy, Mwajabuuuu!” Dahuu aliita wanaye baada ya kusikia kuna wadhifa.

“aya nakutumia, halafu naomba ukishakamilisha unipigie kwa namba hii maana nimeiazima tu hapa dukani,” alisema Renee na kukata simu kisha akatuma hela kwa Dahuu kama alivyoahidi.

Akakaa kimoyo kikimdunda mchana kutwa akisubiria jibu la hao akina Fetty.

Mara baada ya nusu saa simu iliingia; ni Dahuu..

“weee, Renee, hivi una nini.. lakini!?” alisema Dahuu kwa ukali. Renee tumbo likamshika.



“kwanini?” alijikaza kuuliza Renee.

“we unasema nimuulizie marehemu wakati mkaka wa watu mzima yupo hai, mbona kutuumbua mie na wanangu jamani?” alisema Dahuu.

“weee mzima!? Hermez mzimaa!” aliuliza Renee akiwa ameshtuka mno.

“ndiyo ni mzima, we unayemzungumzia labda mwingine lakini huyo uliyesema wa mtaa huo ni mzima kabisa na afya yake!”

“mh labda mwingine, kwani huyo yupoje?”

“ni mweusi mrefu ana pua kama msomali, halafu ni dereva wa mama mmoja hivi kwenye jumba la kishua hivi,”

“weee ndiyo huyohuyo, si anaendesha Noah jeusi?”

“ndiyo ni Jeusi,”

“loh Asante Mungu wangu,..nakuja Dar kesho Dahuu, nakuja mwambie kungwi nakuja, nimefurahi sana, dah hujui tu umenisaidia kiasi gani, jamani asanteni,” aliripuka Renee kwa furaha kiasi kwamba hata watu wakamshangaa.

“unarudi Dar kesho?” aliuliza yule mdada anayemuazimaga simu Renee kila siku.

“ndiyo narudi dar shoga yangu, Mungu akipenda.” Alisema Renee akiondoka zake kwa furaha mno. Siku hiyo akapitia na dukani kurinyuu laini yake kisha akaichomeka kwenye simu yake aliyoifunga kwa mwezi mzima.

Loh akajiona mjinga kumdhania Hermez amekufa wakati ni mzima wa afya, ona sasa hadi amekosa kwenda kijijini kwenye harusi yake. Akawaza sijui huko kijijini wanamfikiriaje?

Wazazi wake sijui wapo katika hali gani? Martin je?

Aliwaza Renee akiwa amerudi chumbani kwake. Siku hiyo japo alijisikia ni kiumbe huru kuliko siku zote, lakini upande mmoja alikuwa na majonzi mazito juu ya mambo ambayo aliacha kuyafanya akidhania, ameua.

Loh! Shauku na hamu yake ilikuwa ni simu yake iwake ili awasiliane na wazazi wake kwanza, hivyo akawa amekaa kama maamuma akisubiria masaa sita yatimie ili laini yake iwe hewani kama alivyoelekezwa na wakala wa mtandao.

Katika kusubiria huko akajikuta amepokelewa na usingizi mzito uliomuisha katikati ya usiku. Akashtuka na kusikia mlio wa simu yake. Akaivuta na kugundua ni meseji mpya. Akaifungua, ni namba mpya. “Renee, kwanini umenikimbia wakati unajua nakupenda na nilikuwa tayari kwa kila kitu kwako?



Najua hukunipenda ndiyo maana umefanya ulichokifanya, sawa namshukuru Mungu, na imani atanilipia. Nimeamua kufowadi meseji hii kila siku kwako nikiwa na matumaini siku moja itakufikia tu, hata kama umeamua kubadilisha na laini yako,”

Loh kwa meseji ile Renee akachanganyikiwa, kiupande akahisi huenda ni Martin lakini upande mwingine ukamfanya ahisi ni Hermez. Akaitia ile namba kwenye Tigopesa afanye kama anatuma salio. Loh kuja kuona, ilikuwa imeandikwa Hermez Nduta.

Doh sasa Renee akahakikisha kuwa kweli Hermez alikuwa hai, akatamani ampigie ili amsikie japo sauti yake; lakini akajiwekea tahadhari kuwa amuepuke Hermez kwa sababu kwanza ni kweli yeye hakumpenda hata kidogo; alikuwa ni uwanja wake wa mazoezi tu. Pili kumpigia kungemfanya ajielezee maneno mengi mno kuhusu kwanini alimkimbia Hermez siku ile, jambo ambalo aliona litampotezea muda wake bure. Tatu, Hermez alikuwa karibu mno na akina Mage, hivyo hawezi jua huenda anashirikiana nao kumtafuta na polisi kwa wizi wa hela je? alichofanya haraka ni kumblock Hermez, yu mzima basi yatosha.

Akatazama saa na kuona ni saa nane usiku, akaona siyo muda mzuri wa kumpigia mama yake, akawa anachezea tu simu yake akijitahidi kutazama kama kuna mtu wa kumpigia. Akagundua kuna namba ya Mage, lakini akaogopa hata kuwasiliana naye maana zilizomzuia zilikuwa ni sababu zilezile zilizomfanya asimpigie Hermez, basi na namba ya Mage akaiblock.

Akahisi hata Martin pia atamtafuta maana huenda alichukia mno kuona amechomeshwa mahindi bila ndoa na bibi harusi hapatikani. Naye pia akamblock.

Alfajiri mapema ilitimu, mdada akajitia miwalo na kufungasha virago vyake, safari ya Dar ikiwadia. Bado alikuwa na dollari ambazo kwa makadirio zilifika milioni mbili, akaona zitamwezesha kuishi na kufanya biashara yoyote mjini. Lakini kubwa ni hilo la kungwi mengine yatajileta yenyewe. Akajiongeza kuwa endapo atajua mapenzi, huenda atampata mwanaume mwenye pesa kama Mary alivyompata Mr X wake. Na hilo ndilo lilikuwa lengo lake la ndani haswa.

Basi gari la kwanza hilo likaondoka na Renee akaja Dar.



“Aya Dahuu nimeshafika Ubungo mbona sikuoni?” aliuliza Renee akimpigia simu Dahuu maana tangu asubuhi ile walikuwa wakiwasiliana kuwa atampokea hapo stendi ya mabasi ya mkoa.

“nipo hapa kwenye bango la Cocacola, karibu na daraja la mwendo kasi,” alisema Dahuu. Basi Renee akamtafuta na akaonana naye.

“mh Renee, Tanga kumekupenda mbona umeng’aa, tofauti na kipindi kile nakuona kwenye basi,” aliuliza Dahuu akimtazama Renee vizuri juu chini.

“mh mie mwenyewe najiona kawaida, sijui ni kwasababu nilikuwa sifanyi kazi nakaa tu ndani. we acha tu, enhee, nipeleke!” Alisema Renee akiwa haihai.

“mh yaani hata kutulia useme, uje kwangu upaone, uwaone na akina Fetty!”

“aarr kwenda Kimara siendi hata kwa bakora, niliyoyafanya huko we acha tu, shauku yangu nikamuone huyo Kungwi kwanza nisijepitwa mie, akina Fetty siku nyingine..”

“mh natamani ningekuwa na kahela niwatie na wanangu maana kule walipoenda hawafundwi ni ushenzi tu, mtu anijia nyumbani hata kuosha mwiko wa ugali hawezi kweli!? Wananiletea watoto wamelegea kama nini? Hapana kwa kweli Tanga kumenifika hapa..” alisema Dahuu akiweka mkono kooni pake.

“kwani ada yake shingi ngapi?”

“mtu mmoja ni elfu ishirini nasikia,”

“mh basi usijali wewe walete tu akina Mwajabu nitawalipia..” alisema Renee. Dahuu akafurahia kama nini.

“mh asante mdogo wangu, yaani unanisaidia mara ya pili hii, sasa twende kwanza wewe, hawa wengine nitamtaarifu Bi. Ummy,” alisema Dahuu akanyanyua simu yake kuipiga.

“Hallow, Dada Ummy, cheichei… ndiyo nakuja naye sasa hivi akuone, mjuane, halafu kesho na mie nakuletea wanangu.. sikukwambia kuwa mume wangu aling’ang’ania tuwapeleke kwa Kuruthumu, basi wamefundishwa ukahaba hao, halafu kichwani hamna kitu… eee.. sawa.. naja… eee, hajaolewa huyu ni binti tu kindakindaki. Sawa,” alisema Dahuu na kukata simu.

“Enhee tunaelekea wapi?” aliuliza Renee.

“ni Mabibo Hosteli, tutoke hapo nje tukapande gari, lete begi moja nikusaidie,” alisema Dahuu.

“hapana ngoja tu tuchukue bajaji,” alisema Renee akimpungia dereva mmoja hivi.



Wakati huo Renee akawa kichwani mwake, akimvutia picha huyo kungwi wa kizanzibari aliyepata kusikia jinale kuwa aitwa Ummy, akawaza jinsi alivyolivyo. Akajiuliza je huyo kungwi anajua zaidi ya Mary au? Akajisemea moyoni kuwa yampasa akasikilize na kuweka nidhamu na kujifanya hajui kitu kabisa hata kama atakuwa anajua jambo maana kwa muda aliokuwa huko Tanga, alikuwa ameshamaliza vitabu vyote vya Mr X, na hakuacha kufanya mazoezi binafsi ya mada zote alizozisoma, kilichobaki ni staili tu kadhaa na kujipimisha kwa mwanaume kama amefuzu.

Lakini pia akamfikiria huyo kungwi wa Tanga aliyesikia wakimuita Kuruthumu, eti anafundisha ukahaba, ndiyo upoje huo? Aliwaza, lakini akampuuza kwa kuwa mwenyeji wake alimpuuza na kumpa sifa mbaya.

Bajaji ilienda kwa kasi yake, hadi mabibo Hosteli, ikapanda kwa juu kama inaingia mtaa wa hosteli, ikaziacha na kuingia mitaa Fulani. “tumefika, sasa?”

“sasa sikia, hapa cha msingi ngoja nichukue chumba gesti niwe nakaa hapahapa karibu.”

“hapana, hata haina haja, wenzako wameweka kambi hapo kwenye nyumba,wamechangishana na wanakaa hapohapo, wanapika na kula hapohapo, cha msingi maelezo yote utapatiwa, we twende,” alisema Dahuu akimkokota Renee, begi moja kabeba yeye na begi jingine kabeba Renee.

Wakaingia kwenye nyumba kubwa yenye geti kwa nje. Kwa Uwani mle ndani, Renee akashangaa kuona wadada si chini ya kumi na sita wa makamo kama yeye, wakikunja kunja khanga, kama vile mchezo maana wote walikuwa na upande mmojammoja.

wakawasalimia nao wakaitikia huku wakiendelea na ubize wao.

Renee akasikia minong’ono: “mh Bi. Ummy atatuua na hili somo la Khanga.”

Basi Renee akadaka kichwani kuwa siku hiyo walikuwa wakifundishwa kuhusu Khanga,je khanga ina nini? Ni ya nini? Na kwanini wahangaishane kuzikunja!” Akajiuliza kichwani mwake wakati wakiwavuka hao wadada kumsogelea binti Fulani mrefu, mweupe sana, au chotara wa Kishirazi.mzuri balaa. Utasema mmbongo kwa jinsi alivyoumbika kwa nyuma.

“Bi.Ummy, jamani,nimekumissii,” alisema dahuu na kwenda kumkumbatia kwa furaha.

“ooh jamanii, waoh,” alisema huyo mdada aliyeitwa Bi.Ummy. Loh Renee akashangaa maana alidhania angekutana na mtu mzima.



Basi wakasalimiana marafiki hao, kisha Dahuu akabadilisha mirindimo wa sauti yake, kumfanya Bi.Ummy apokee maneno ya msingi yafuatayo.

“Bi.Ummy huyu ni mdogo wangu, anaitwa Renee, aliniomba muda mrefu nimuelekeze kwa kungwi mzuri ninayemkubali mimi, ndiyo nikamuelekeza kwako, sasa mengine kama tulivyoongea, anataka umfunde yote maana hapo alipo ni msungo haswa.. mpe utaratibu aanze leoleo maana hapo anaona kapitwa, katokea Tanga na moja kwa moja kafikia hapa.. ukimalizana naye kesho na mie nikuletee na wanangu hapahapa,” alisema Dahuu akiyashona maneno harakaharaka kama cherehani.

“mh Karibu sana Renee, mimi naitwa Bi Ummy,kama alivyokwambia Dahuu. Tunaheshimiana sana ndiyo maana kakuleta kwangu, mie sifundishi tu mtu asiye na staha kwanza, huwa hata wali wangu wakitoka kwangu wanapoenda wanakuwa na tabia njema mno, na tofauti na makungwi wenzangu, mimi ndiye pekee niliyeolewa na nimetulia kwenye ndoa mwaka wa kumi huu, tembea kote hakuna kungwi aliyeolewa akatulia bila kuachika. Naomba sasa kama umefika hapa kwa ajili ya kujifunza jinsi ya kuwa mwanamke nikukaribishe kwa mikono miwili,”

“nashukuru sana Bi, Ummy, naahidi nitajifunza kwa juhudi zote ili nikitoka hapa, niwe mwali mzuri,” alisema Renee akifurahi ustaarabu wa huyo mdada.

“basi haujachelewa, utaratibu wetu kuna mwenzako hapo nitamuita atakuelekeza baadaye, ila utalala na utakula hapa wote ni wa moja; kuna wenzio wanaojifunza kwa ajili ya kuolewa hapo, wengine maharusi wamerudishwa na waume zao kwa ajili ya kutojua nahari, na wegine ni kama wewe... Leta begi lako nikuwekee hapa nikakutambulishe kwanza.” alisema Bi. Ummy.

“aya na mimi ngoja niwahi nyumbani nikapike, Renee, hapo umefika huyo ni mwisho wa khabari,”

“aya asante Dahuu,” alijibu Renee akamkabidhi mabegi yake kungwi wake na kurudi kule kwenye uwa ambapo aliwaona wakina dada wakutosha wakiwa bize na vikhanga vyao.

“wadada, haya naombeni tusikilizane, huyu ni mwenzetu amekuja kutoka Tanga kuja kujifunza nasi hapa, tutakuwa naye kuanzia leo.. Mercey utamwambia utaratibu mzima wa malipo baadaye na atachagua alale na nani.



“Aya Renee kakae pale niwaelekeze pamoja somo hili..” alisema Bi. Ummy, Renee akaenda kukaa penye uwazi wa jamvi.

“Khanga nadhani wote tunaijua kuwa ni vazi la mwanamke wa pwani lakini limesambaa kote Tanzania.. lakini sifa hasa za Khanga kwa mwanamke aliyefundwa linatokana na maana zake na si tu yale maneno ya vijembe yanayoandikwa nyuma.

“Khanga mtu aliyefundwa havai tu ovyo, wala hamvalishi mumewe ovyo, lazima ajue khanga hii ni ya aina gani na muda haswa wa kuivaa ni upi?

Kuna khanga za kawaida, hizi unaweza kuzivaa asubuhi, ukapika nazo na kufanya shughuli zote za nyumbani, kuna khanga za msibani, kuna khanga za mume, kuna khanga za kufutia udelele na kumsingia mume na kuna khanga za kupambia kitanda kwa kuzifanya ziwe za maua kwa kila unavyotaka wewe. Ndiyo maana niliwajaribu kusema muumbe maumbo ya maua kwa khanga naona mmeshindwa hapo.. sasa tutaanza kufundana aina moja moja ya khanga na nitawaonesha vizuri.” Alisema Bi. Ummy.

Akina dada wakazizima maana Bi.Ummy aliwavuruga kweli hapo kwenye khanga, Renee naye alikuwa akiwashangaza wenzake maana alikuwa akiandika maelezo ya Bi.Ummy kama alikuwa darasani vile.

“Aya mpo tayari tuanze?” aliuliza Bi.Ummy.

“Mh Bi.Ummy naomba na mimi nikachukue daftari..” alisema Mercey baada ya kumtazama Renee. Doh naye Samrath akataka daftari, naye Samirah pia, Loh Ilham, wote wakaagizana, ikabidi darasa likatishwe dakika kadhaa kusubiri peni na vidaftari viletwe. Vilipoletwa kila mtu akaanza sasa kunakiri kutoka kwa Renee.

Renee akafurahia walau kwa siku ya kwanza ameanza vyema darasani hapo kwa kuwa mfano. Akaapa kujifunza hayo kwa umakini mkubwa maana hakuwa ameyasoma hata kwenye vitabu vya Mary.



Basi baada ya hayo Bi.Ummy akawafundisha wali wake kuhusu kila aina ya Khanga. Wakavaa wakizitambua uzuri kuwa ipi ni ipi, na wakajiona wajinga kwa sababu mwanzoni hawakuwa wanalijua hilo.

Walipomaliza somo hilo jua likawa limetua ikawa maandalizi ya chakula cha usiku na mapumziko yakiwemo kuoga na vitu vingine. “Renee, utapika na mimi leo, na tutalala na mie,” alisema Ilham akimuwahi Renee maana alimuona Mercey akimzengea.

“Sawa,” alisema Renee na kwenda kuweka begi lake kwenye chumba alichoelekezwa, akifurahia maana ilikuwa muda mrefu sana tangu awe na marafiki na angalau kuzungukwa na wanawake wenzake kama mahali hapo alijisikia vizuri mno. Akatoka na kuitwa na Bi.Ummy akaelekezwa taratibu za kulipia na kuingia kwenye mapishi na Ilham. Walipomaliza wakaenda nao kuoga na kurudi kupakua madikodiko na kuweka sebuleni kila mtu ajisevie.

Hapo sebuleni ndiyo wakapata kupiga stori na kuulizana mambo mengi pamoja Bi.Ummy naye akiwa pamoja nao.

“Enhee Renee, mwenzetu kwenu Tanga sehemu gani?” aliuliza Samrath.

“hapana kwetu sio Tanga, ni Iringa, Tanga nimekaa mwezi mmoja tu baada ya kutoka hapa Dar,” alifafanua Renee.

“ooh kumbe wa hapahapa Dar! Ulikuwa unakaa sehemu gani?” aliuliza Samira.

“nilikuwa naishi Kimara Baruti,”

“anhaa! Mie Sinza ,” alisema Samrath, wakamaliza kula na tayari ikawa muda wa kwenda kwenye darasa la pili la usiku. Kila mtu akakimbilia kidaftari chake kunukuu.

“kama nilivyowaambieni mimi nafundisha jinsi ya kuwa mwanamke haswa! Na sitaanza na mambo ya mbali, nitazunguka kwenye hayohayo maisha yenu. Nimeanza na khanga na maana yake, natumaini hamtaniangusha, si ndiyo? Sasa hivi, tunaenda kwenye vyumba vyenu. chumba.. nini maana ya chumba!? kina maana gani kwenye ndoa. Nini tofauti ya chumba cha msungo na chumba cha mtu aliyefundwa. Chumba kinatakiwa kiwe na nini ili kitimie? Nani anapaswa kulala chumbani, nani anapaswa kuingia chumbani kwako, heshima ya chumba ni ipi kwako kama mwanamke kamili?” aliuliza maswali mfululizo Bi.Ummy.

Akawatazama mamwali wake wakitazamana.



“Kuna mtu anaweza kujaribu kuniambia ili chumba kikamilike kinapaswa kuwa na mambo gani?” aliuliza Bi Ummy.

Wali wakanyoosha mikono juu..

“kiwe na A.C, kiwe na dirisha kubwa la hewa, mapazia mazuri, kiwe na choo na bafu ndani, kiwe na dressing table, kiwe na kitanda cha sita kwa sita..” alisema Mercey akijishaua maana alikuwa wakishuashua hivi, na ndiyo alifika hapo mafundoni na gari yake kabisa kapaki uwani.

“mh, Mercey, vipi kwa mwanamke aliyepo kijijini? Na ana nyumba ya udongo, hivyo vitu kweli ataviweza?” aliuliza Kungwi. Mercey akaufyata. Wengine wakazidi kuvurugwa maana kila mtu alivyotajiwa chumba aliwaza hayohayo aliyoyataja Mercey.

“Mwingine?” aliuliza Bi.Ummy, ikawa hakuna hata mmoja aliyejaribu kufungua kinywa chake tena hata Renee maana aliona ni mambo mapya haswa hakuwahi kuyasoma wala kuyajua.

Mara geti likagongwa, Samira akaenda kufungua, Loh alikuwa ni Dahuu na wanaye Mwajabu na Fetty. Visichana vikaingia vyenyewe shingo vimezisimamisha kama mbuni mgongoni na vibegi vyao, vikaongozana na mama yao havina habari na mtu.

“samahani Bi.Ummy, ndiyo hawa, naomba niwaache nirudi nyumbani kila kitu nimewakabidhi,” alisema Dahuu harakaharaka akimpungia mkono Renee kwa mbali.

“Aya hakuna shida, nyie kakaeni pale,” alisema Bi.Ummy, Mwajabu na Fetty wakaenda kukaa karibu na Renee wakimsalimia dada yao kwa kuchekacheka, wakawa ni wanafunzi wadogo zaidi kwa hilo darasa zima.

“Enhee tuendelee, ili chumba kitimie kinapaswa kiwe na vitu gani?”

Doh Mwajabu na Fetty wakanyosha mikono juu kama ugomvi.

“sharti kiwe safi, kiwe na vibakuli viwili kimoja kitiwe vitafunwa,ama tende, ama pipi, ama karanga, kingine kiwe na asali na kijiko kisafi, kuwe na bilauri na glasi ya maji, kuwe na khanga ya mume, kuwe na shanga za jumbe, kuwe na chetezo, kuwe na mafuta ya nazi. Kuwe na matandiko kama hamna kitanda, kama hamna sakafu, basi dongo unamwagia maji vumbi lisikae,” alisema Fetty kama cherehani. Loh darasa zima likashangaa, Bi.Ummy akatabasamu. Mercey akatumbua macho huyoo. Mwajabu akaropoka: “umesahau kisosi cha kuwekea wembe wa kunyolea vuz*”




“Waaoh tuwapigie makofi, hawajaacha kitu,” alisema Bi Ummy. Akijua yakini kuwa hao wasichana alishatahadharishwa na mama yao kuwa walitoka Tanga kwa Kuruthumu, hasimu wake, Hawaivi chungu kimoja. Hawapatani abadani. Ikawa japo aliwapongeza lakini Bi.Ummy alijua udhaifu wao na mambo waliyofundwa huko watokako, hivyo hakuwa na hofu nao kwa kuwa alijua mengine mengi hawataweza.

Basi makofi yakapigwa na kila mdada pale ndani, wote wakawatazama akina Fetty na Mwajabu kwa jicho la wivu. Wakasubiria Bi.ummy awaelekeze vizuri maana wa hayo mambo waliyoyasikia kwa sababu hawakuyajua hapo kabla.

Basi darasa likaishia usiku huo kila mtu akiwa amepata picha ya Chumba kichwani mwake kuwa haijalishi kiwe cha gharama au lah ili mradi tu vitu stahilivu vitiwe.

Muda ukatimia Bi.Ummy akaenda kulala zake hotelini alipofikia. Lakini cha ajabu wote wakabaki na Fetty na Mwajabu wakiwahoji mengi maana waligeuka kivutio, hata Renee pia alikuwepo humo.

“nyie kwani mmefundwa wapi?” aliuliza Samrath kwa shauku.

“sie kwa Kuruthumu, Tanga.”

“sasa mbona mmeletwa hapa tena?”

“mama huyo sijui naye na mambo yake, si tumeshajua kila kitu, yeye anadai ooh hatujui kuosha vyombo, mara sijui kusafisha ndani..ndiyo ametuleta huku, mimi sipapendi kama nini natamani kurudi tu nyumbani nikaolewe,” alisema Fetty na umachepele wake.

“eti da Renee, hapa mnafundishwa kupika na kufagia?” aliuliza Mwajabu.

“mh tunafundishwa jinsi ya kuwa mwanamke na kila kitu, kwani huko mtokako mlifundishwa kitu gani haswa..”

“tumefundishwa, kutembea, kuringa, kukatika bwindani, mikao ya kusex, kumtega mwanaume na mambo kibao, sio kama huku wala hakunogi,” alisema Fetty.

“tumefundwa pia na kumlea mwanaume kama mtoto mdogo, wenzenu hadi tunawabebaga mgongoni, tunawachanganya wasituache kabisa,” alisema Mwajabu, Doh kila mtu akatoa mimacho hapo.

“weeee, kweli kubeba midume mgongoni? Kumbe kweli!” aliuliza Mercey kwa mshangao.

“ndiyo, yaani nilipotoka tu mkoleni nimembeba mume wa mtu hapa hatoki, kapagawa haniachi kila saa anapigia ananiwaza mimi tu,” alisema Fetty hata hafananii.




“yaani Kuruthumu watu hawamuelewi tu, yeye anafundisha kumfanya mwanaume apagawe kama karogwa kumbe vitu tu vya kitanga na kila mwanamke unasikia anayetingisha mjini ujue amefundwa kwake,” aliongezea Mwajabu. Kwa stori hiyo fupi tu kila mtu akajikuta anatamani kama nini kwenda huko Tanga, wakaona kama vile kukaa hapo kwa Bi.Ummy walijichelewesha tu. Wakafanya kikao na kukubaliana wamuite Kuruthumu mjini na Bi.Ummy wamuachie tu hizo ada zao.

“hivi hamna namba yake huyo Kuruthumu, maana mie hapa kashanichanganya,” alisema Samrath.

“tunazo tatizo mama katupokonya simu zetu ndo kwanza tulizotunzwa wakati tumetoka kuchezwa, da Renee mpigie mama muombe wewe..!” alisema Fetty.

Basi wote wakamtazama Renee, Renee akanyanyua simu yake na kuipiga akaweka laudispika na kuwaomba wote wawe kimya.

“hallow Dahuu, samahani kwa kukupigia simu usiku,” alisema Renee.kwa mbali akasikia Dahuu akiongea na mwanaume mwenye bezi zito, huenda ni mumewe.

“enhee niambie Renee,” aliitikia Dahuu.

“Sasa Dahuu, unakumbuka nilikuomba unielekeze kungwi bora kabisa unayemkubali, mbona ulinielekeza kwa huyu Bi Ummy wakati kungwi mzuri ni Kuruthumu wa Tanga!”

“mh, we Renee, nani kakwambia Kuruthumu anamzidi Bi.Ummy?”

“wanao hapa wamekuja wanatuambia mafundo haswa, si kama ya huku kwa Bi.Ummy naona kumepoa, mimi ningejua ningeenda Tanga na mie, naomba namba ya Kuruthumu,” alisema Renee wenzake wakimsikiliza maana ilikuwa wapate tu namba wampigie na kuachana na Bi.Ummy.

“Renee, ukienda kule utapoteza muda wako bure, kule unafundishwa ukahaba mdogo wangu, haufundwi. Mimi nimefundwa kwa Bi.Ummy ninachokwambia kinatoka moyoni mwangu kabisa. Hautafundishwa staha, utafundishwa umapepe; hautafundishwa mapenzi, utafundishwa ngono, hautafundishwa kumvumilia mume, utafundishwa kudanga. Wanangu mie kaniharibia we waone mwenyewe unaona ni wanawake hao wenye akili zao? kaa nao utaona; kama unataka kuwa mke wa mtu kaa hapohapo, lakini kama unataka kudanga mjini nenda Tanga, namba ya Kuruthumu mbona nakupa tu haina shida kabisa,” alisema Dahuu na kukata simu, dakika si nyingi namba hiyo hapo.

Palepalekukazuka ubishani, wengine wakasema wanabaki, wengine wakasema wanaondoka. *wewe msomaji wapi??



Basi Renee akawapa mpango wenzake, akiwashauri kwanza wajifunze vya Bi.Ummy mwanzo mwisho na wakimaliza watashirikiana kumuita huyo kuruthumu waone ufundi wake!

Ikawa hivyo, siku zote wakakaa kimya kusikiliza mafunzo ya Bi Ummy, wakayaandika kabisa hadi wiki nzima mafunzo yalipoisha.

Wakasadiki kweli walipata kuwa tofauti na walivyokuwa zamani. Renee akakiri kuwa alichofunzwa ndiyo hekima ya mwanamke aliyefaa katika jamii.

Lakini Renee na wachache wenzake bado walikuwa na shauku, wakakubaliana kumuita Kuruthumu na ratiba ikawekwa kabisa.


Ikawa siku ambayo Bi. Ummy ndio alikuwa akiwaaga na kuondoka, aliwanasihi mno na kuwaombea wali wake wapite njia alizowafundisha na kuwaonya wasitake zaidi maana elimu ya mapenzi kama elimu nyingine, haina mwisho ni kama bahari.

“mh, ungejua wenzako bado wanataka kumuona na Kuruthumu,” aliropoka Mwajabu akikatisha maongezi ya Bi.Ummy aliyebadilika rangi kwa ghadhabu.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG