Search This Blog

Wednesday, January 25, 2023

CORONA AKEE - 4

   

Chombezo : Corona Akee

Sehemu Ya Nne (4)




Basi akaanza kuandika jina la Grace juu ya ukurasa, akapiga mstari katikati upande wa kushoto akaandika mabaya ya Grace upande wa kulia akaandika mazuri yake.

Huko kushoto, akaandika, hana tako, sio mzuri, kwanza polisi namuogopa, baba yake RPC jau, mama yake magereza nikimkosea jela njenje; akaenda upande wa kulia sasa; akaandika mazuri ya Grace; ana akili za maisha, ana magari na nyumba, ananiheshimu, ana mipango ya familia, nikiwa naye sitayumba kiuchumi, amenipa gari, nyumba,ananipenda, amenipa biashara, kazi na hela. Alimaliza kuandika Cliff na kuona upande wa mazuri ya Grace ukimhukumu; akawaza amfananishe na demu wake gani? akaona si Mwantumu wala Neema, lakini alipowaza kuhusu Neema nusura aombe Mungu amhamishie uzuri wa Neema uende kwa Grace; lakini Maulana si mjinga wa kumtia mtu ubovu asiwe na zuri, au wa kumtia mtu uzuri asiwe na ubovu maana itakuwa chachu na chachu kuchachua donge zima.

Sasa kwa akili ya mwanaume mwenye akili, Cliff akaona hana budi kumheshimu Grace ingawa lazima amle Neema maana imemcost sana. akawa kama vile mcheza kamari maana kadri anavyoliwa ndiyo anavyotia pesa. Akawaza sasa atamlaje akakosa njia; akaamua kumpigia kwanza Grace;

"Hallow mpenzi, mambo! pole sana kwema.. umekula?" alisema Cliff kwa mahaba yote.

"mie mzima tu, vipi kazini kwako lakini.. enhee umesoma meseji yangu?" alisema Grace, CLiff akamuahidi Grace kuwa lazima awepo na kufanya Grace wa watu amalize kuongea na Cliff roho yake ikiwa kwatu. Alipomaliza tu kuongea na Grace akampigia Neema.

"hallow Neema, umeona sasa! sijui tutafanyaje na wakati mimi nilikuwa nataka niwe na wewe huko!" alisema Cliff.

"sikia nimeshafikiria kuhusu hilo,saa tatu kamili nitamwambia meneja, mkuu wa askari na wewe tuungane kusali chumbani kwangu, tuombee hili janga la korona liishe hapa hotelini,"

"kusali tena!?"

"ndiyo, najua hawatakubali na atakayekubali nitasalisha sala ndefu mno, cha kufanya wewe uvumilie tu unaweza usinipate leo lakini ukanipata kesho kwasababu urefu wa sala ya leo utakuwa kiasi kwamba kesho nikiwaita tena, hakuna atakayekuja isipokuwa mimi na wewe na ndiyo hapo tutafanya yetu kwa kujinafasi badala ya kusali.."



"duh hiyo itakuwa nzuri sana, nimekubali.. mh kumbe na mimi unanifikiriaga eeeh!" alisema Cliff akijisikia na yeye kupendwa kiasi cha Neema kumtia kwenye mpango huo wa kishetani.

"hata mimi ninahamu na wewe Cliff, hujui tu we unafikiri nani alitaka kuwa mtawa kwa kupenda?" "aya Basi sawa, utaniambia kama atakubali," alisema Cliff katika hali ya kukata tamaa.

Loh kweli bwana huko alipo Neema akapiga simu mapokezi kutumia simu ya chumba cha hoteli na kuomba aunganishwe na meneja maana pia simu hizo za hoteli ziliruhusiwa kutumika kwa mawasiliano ya huduma mbalimbali hotelini humo bila kusahau wateja kutoa taarifa kama mwenzao anaumwa hususani kama ataonesh dalili za corona.

"hallow meneja, tumsifu ..Kristu... ni mimi sista Anne," alijitambulisha Neema akiongea kwa ustaarabu wa kinazareth kama si ki-galilaya.

"milele amina sista, kuna tatizo lolote kwani?" aliuliza meneja.

"hapana, nilikuwa nimepanga tufanye sala ya pamoja leo usiku, kumuomba Mungu wetu, watu wasiendelee kupata Corona hapa hotelini na Tanzania nzima," alisema Neema.

"Oh sawa sista, nitamwambia kamanda, lakini sidhani kama itakuwa rahisi kwasababu mkusanyiko wa watu hauhitajiki," alisema Meneja.

"hapana simaanishi watu wote, mimi nitakuwa na dereva wangu, wewe na kamanda wa polisi tunatosha," alisema Neema. Meneja akajiumauma akaona haya kumkatalia sista Anne. Akakubali kuwa saa tatu usiku watakutana ila chumba ndiyo akataja chumba fulani kitupu kilichopo kwenye ngazi za kushukia bawa la magharibi yaani katikati ya chumba cha Cliff na Neema.

Ikawa furaha kwa Cliff baada ya kupatiwa taarifa hizo akajisikia kama vile ameshinda jackpot bingo, lakini kimoyomoyo akamuogopa Neema mno, akahisi ushetani wake umemzidi yeye maana tangu aende huko Italia loh! sista gani anaweza kubuni uongo wa namna hiyo!

"Kwa hiyo kwenye sala nije na nini?" aliuliza Cliff maana japo ni mkatoliki lakini kanisani mara ya mwisho hakumbuki alienda lini.

"Njoo nitakupa rozali na chuo kidogo cha sala, si unajua kusali baba yetu na salaam Maria?" alihoji Neema.

"ndiyo.." "sawa hiyo itasaidia, njoo, saa tatu kamili," alisema Neema na kukata simu.



Basi ilipotimu saa mbili kamili wageni walihudumiwa vyakula kwenye vyumba vyao ili wasitoke kabisa. Msosi huu inasikika uligharamiwa na serikali.

Wakati Cliff akila chakula chake akatazama habari na kugundua habari kuu mitandaoni kote na kwenye televisheni ilikuwa ni kuhusu Corona kuibukia Arusha na hoteli waliyofikia ikawa ndiyo kielelezo cha picha kuu iliyopamba sura za magazeti na habari za matelevisheni.

Saa chache zikapita na Cliff akawa amepitiwa kabisa mara akatazama saa yake na kugundua ni saa tatu kamili usiku, akakurupuka na kupaniki; badala ya kwenda na kitakatifuzi chochote huko kwenye sala, yeye akabeba Condom kwa ajili ya dharula. Ombi lake kwa shetani wake likawa ni; "eeh shetani,mfanye meneja na kamanda wasije, au waage wakalale nimle Neema. Japo kidogo tu.. Ameen!"

"Tayari, Neema upo wapi?" alituma meseji hiyo Cliff, lakini saa hiyohiyo mlango wake ukagongwa hodi, akaenda kufungua, loh uso kwa uso alikuwa ni kamanda wa polisi.

"habari mkuu," alisalimia Cliff akinyoosha mkono wake, kamanda akagoma kuupokea.

"salama tu, mzee hatusalimiani kwa kushikana tena,kuna corona mzee," alisema kamanda akanyoosha mguu wake, Cliff akakumbuka mchezo huo wa kina joti naye akanyoosha mguu wake wakagongesha kisha wakafuatana.

Korido zilikuwa kimya,vyumba tu vya watu vikiwa vimewashwa taa kuonesha kuwa wote walikuwa wametii agizo la mkuu wa mkoa la kubakia vyumbani mwao.

Hatua zaidi ya mia moja wakatembea, katikati huko kuna chumba kikubwa kilikuwa wazi ambapo mlango ulifunguliwa milango ya nailoni ikishamiri humo ndani, kwa jicho la Cliff aliweza kuwaona madaktari mbalimbali waliojiziba sura zao kwa maski wakichunguzachunguza vitu kwenye hadubini zao, halafu kwenye kona kukiwa na vitanda na watu wakiwa wamelala.

"Hao ni wagonjwa wa corona walipatikana hapa hotelini, aisee, kaeni mbali na hiki chumba kama mnataka kuishi," alisema yule kamanda, Cliff akameza fundo la mate kooni maana alianza kujengeka hofu ndani yake.

Wakapita haraka hicho chumba na kusogea mbele kabisa wakakutana na hiyo sehemu tupu ya ngazi za kushukia floo ya chini hapo kwa pembeni kulikuwa na kichumba cha uchochoroni, cheupe kilichokuwa na mabenchi tu.



Cliff akatupia macho yake akagundua kulikuwa na Neema ndani yake kama kawaida akiwa na mavazi yake ya kitawa.Ameketi kama mtakatifu Maria Theresa vile na lirozali lake kubwa.

"tuanze kwa sala ya usiku jamani," alisema Neema na kuanza sala moja moja akipangua kitabu na vijitabu.Cliff kijicho pembe akiwatazama meneja na Kamanda kama watasalenda.

Likapigwa jaramba pale, nusu saa ikapita na wakawa wanaitafuta saa nzima, Loh Kamanda na ukakamavu wake akaanza kupiga miayo,akafuatia Meneja, Cliff aliyekuwa akiitikia sala za Neema kinafki lah moyoni akiwalaani meneja na Kamanda wasinzie, akaanza kuona matunda ya sala zake.

"EEe Mungu tujalie wanao wenye dhambi chafu kama madonge ya damu, tuwe weupe wa theluji kwa damu yako itutakase tusishikwe na magonjwa ya Corona na mengineyo, tunaomba hayo kwa njia ya Kristu bwana wetu, salaam Maria.." alisema Neema akilianzisha maana lilikuwa limeishapoa.

loh wakatimiza masaa mawili, kamanda na meneja pengine wangeondoka muda mrefu uliopita lakini walikaa kwa aibu tu, walipomaliza hawakuamini masikini.

"sista tunashukuru kwa sala nzuri, nina imani Mungu atatusikia na kutuepushia mbali ugonjwa huu," alisema Kamanda, meneja hakuwa na cha kupinga akabakia tu anatikisa kichwa.

"ameen, Mungu atatunusuru, nawakaribisha tena kesho kwa sala kama hii maana nimeweka nadhiri ya kusali novena hii kila siku kwa siku hizo kumi na tano nitakazokuwa karantini hapa,nawakaribisha muungane na mimi kama mlivyokuja hii leo," alisema Neema akatamani acheke kwa jinsi sura za meneja na kamanda zilivyokunjamana.

Basi wakaagana na kurudishwa vyumbani mwao, Cliff alikasirika kwa kulikosa tena punino la Neema, lakini hakulaumu maana aliona matumaini ya kupata mzigo kama si kesho basi keshokutwa, ili mradi tu afuate maelekezo ya Neema.



Basi usiku ule simu ya Grace ikaingia kwa Cliff, wakatakiana heri na baraka juu ya waliyotarajia kuyatimiliza hiyo kesho kutwa. Cliff asiseme kitu akatulia tu kimya hali akijua fika amefungwa huko karantini kwa siku kumi na nne zijazo; na mwenziye Grace alikuwa siriaz kwelikweli kwenye penzi lao.

"nitafikiria cha kufanya kesho, Grace atanielewa tu,"aliwaza Cliff maana hesabu zake za kufikiria chochote ziligoma mpaka pale atakapoonja penzi la Neema.

Wakati huo Neema chumbani kwake alikuwa ameshaongea na mzee wake, kuwa alizuiwa uwanja wa ndege Arusha kwa ajili ya vipimo vya corona kwa kuwekwa karantini.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

BLOG