Chombezo : Corona Akee
Sehemu Ya Tano (5)
"Mwanangu cha muhimu ni kumuomba Mungu tu, nakuombea sana; halafu father Filbert alikuwa anakuulizia, na yeye amewekwa karantini hapohapo airport nimempa namba zako anasema atakufuata ulipo kesho," alisema baba yake Neema, loh!
"sawa, lakini sidhani kama ataruhusiwa kuniona, mimi nipo huku geti jingine maana nimetokea Italia, yeye si ametokea ufaransa?" alisema Neema akipanga uongo mtakatifu maana alishajua kama huyo Father Filbert atagundua kuwa hayupo airport atamwambia baba yake.
"Ndiyo mwanangu, ametokea ufaransa, aya sawa, hakikisha unakaa mbali na watu wenye mafua mwanangu," alisema Mzee wake Neema; akimlinda mno mwananaye maana yeye ndiye baba na mama kwa Neema tangu mke wake afariki kwenye ajali ya moto, wakati huo Neema akiwa kichanga.
Neema mwenyewe aliishiaga kutazama picha tu za mama yake enzi zake, watu wakamuona na kumwambia amefanana mno na mama yake na hilo lilimpa simanzi mno.
"wewe ulipona tu kimiujiza, ndiyo maana nilitaka umtumikie Mungu maisha yako yote kama mtawa," ilikuwa ni kauli ya baba yake Neema miaka mingi iliyopita na alifurahia kuiona imetimia kwa Neema kurudi akiwa amepitia hatua ya mwisho kabisa ya kuwa mtawa na angelikuwa ameishaanza kazi yake huko Roma kama si Corona.
***
Father Filbert pamoja na kuwa padri wa muda mrefu mkoani Arusha, alikuwa na historia ndefu na familia ya kina Neema. Tangu ajali ya moto iikute familia hii amekuwa akitoa msaada wa hali na mali kwao.
Alikuwa kama baba wa pili wa Neema, alimlea kiimani na kumsaidia baba yake aliyekuwa amekwisha kata tamaa kurudi kwenye mstari wa matumiani mapya ya maisha katika Kristu.
kwa macho ya kidunia unaweza kusema bila huyu Father FIlbert, baba yake Neema asingekuwa mtu wa dini kupitiliza, wala Neema asingekuwa mtawa kilazima. Maana alichungwa, akafungwa na hata bakora alichapwa ili mradi asiwe kama wasichana wengine wa umri wake bali mtumishi wa bwana.
Ilikuwa ni mateso na safari ya miiba kwa Neema na ndiyo iliyomfanya hata kwenye ukubwa wa umri wake wa miaka 26 alionao, aendelee kumuogopa mno baba yake, lakini zaidi Father Filbert.
Sasa akatulia chumbani mwake akisikilizia simu yake na cha kudanganya kwa father FIlbert ikiwa tu atamtaka amuelekeze alipo, na kama tu atakua amekosea kuwa huenda huko karantini ya airport watu hutembeleana na siyo kutengwa vyumbani kama hapo hotelini.
Loh akakumbuka jambo, TAARIFA ZA HABARI! Kwanini hakuwaza hili muda mrefu kabla? Ni kweli ili kujua yote hayo lazima asome habari na kusikiliza hali ya ugonjwa huu wa corona unaendeleaje duniani; basi akawasha televisheni ya hoteli, akawasha redio kwenye simu yake ya kitochi akaweka laudispika kisha akafungua smartphone yake na kuanza kugoogle.
TANZANIA YARIPOTI KISA CHA SITA CHA CORONA, akasoma vizuri habari ile na kugundua visa vinne vya wagonjwa wa corona ikiwa ndani ya hoteli aliyofikia, huku viwili vikiwa ni Zanzibar na Dar.
Macho yake yakashuka kwenye kichwa cha habari kilichoandikwa; "WATANZANIA KUJIGHARAMIA WENYEWE KARANTINI" habari ya pili ikawa "HOTELI ARUSHA KUWA KARANTINI YA CORONA, KANDA YA KASKAZINI" loh akaingia kusoma habari hii kwa undani akagundua ni hoteli yao hii ndiyo aliyochaguliwa kurundikwa washukiwa wote wa ugonjwa wa Corona kuanzia kesho maana yake wasafiri wote wa kanda ya kaskazini wataletwa hapo hotelini.
Hii sasa ilikuwa na maana mbaya na nzuri, mbaya ni kwamba Father Filbert naye ataletwa hapo hotelini na kuharibu mipango yote ya yeye na Cliff; nzuri ni kwamba; ile ya yeye kukutwa hotelini haitakuwa skendo tena maana, hoteli sasa imefanywa karantini na hata father Gilbert atakuwepo, yeye ni nani basi hata aogope.
Lakini ndani kabisa ya moyo wake Neema akawa na hofu kuu zaidi iliyoletwa taswira ya ujio wa Father Gilbert hapo hotelini alipokuwa. je, ni hofu ipi hiyo nyingine?! mimi na wewe hatuijui; tusonge.
Mnamo saa sita za usiku, simu ya Neema iliita namba hii ndiyo aliyokuwa akiisubiria mno na kuitarajia; japo ilikuwa ni namba ngeni lakini muito wake ulimchezesha machale kuwa huyo si mwingine bali ni Father Gilbert.
"Tumsifu Yesu Kristu,"ilikuwa sauti ya nzito ya mwanaume umri sawa na ya baba yake, ilikuwa ni miaka kadhaa imepita lakini sauti ya Father Gilbert haikubadilika hata kidogo.
"Milele amina," aliitikia Neema akijifanya anasikilizia huyo mtu wa upande mwingine ajitambulishe kwanza ingawaje alimfahamu fika.
"Unaongea na Father Gilbert hapa,"
"Aagh Father,shikamoo; za masiku,"
"marhaba tu, mwanangu, niliongea na baba jana akaniambia na wewe upo karantini hapa airport,na mimi nipo hapa mbona sijakuona!"
"nipo Father, watu ni wengi kidogo ila natumai nitakuona kesho tu asubuhi!"
"Watu ni wengi? mbona tupo kumi na mbili tu!" alisema Father Gilbert.
"halloow! haloow .. Father sikusikii vizuri," alizuga Neema na kukata simu yake.
Haraka akamtumia meseji Cliff. ikasomeka hivi:
"Angalia habari,kesho hoteli inageuzwa karantini ya Corona kanda ya Kaskazini. Father Gilbert naye mmoja wao anakuja! tughairishe ule mpango kwanza."
Loh meseji hiyo ikamshtua pia Cliff, maana naye alimfahamu vyema Father Filbert, kuwa ni mmoja kati ya madingi waliombania kwa Neema tangu enzi zile sekondari wakati alipokuwa akimvizia Neema mafundisho kanisani; hivyo basi ujio wa Father Gilbert ukawa pigo jingine kwa Cliff.
Tena akakumbuka simu moja wakati Father Gilbert na baba yake Neema walipomkamataga huko kwenye vyoo vya kanisa na Neema; baada ya kumchapa bakora, Cliff aliondoka kwa hasira huku akisema:" Hata mnizuie vipi, Neema nitampata tu, atakuwa wangu!"
Cliff alikumbuka maneno hayo vizuri kama vile aliyasema jana yake tu. Akakumbuka hata sura ya Father Gilbert na baba yake Neema ikimkemea Cliff wa enzi zile kama pepo mchafu anayetaka kukwamisha uongofu wa mtoto wao Neema katika kuifuata njia ya bwana.
Na kama haitoshi alikuwa na uhakika hata sababu ya Neema kupelekwa kusomea utawa huko nchi za nje ilikuwa ni yeye.Hivyo basi,Cliff alijua lazima tu Father Gilbert akimuona atamkumbuka tu kwa sababu walikuwa na kisasi cha wazi kabisa, japo kuwa imepita miaka takribani kumi na moja tangu tukio lile na miaka saba na ushehe tangu waonane mara ya mwisho.
****
Basi kweli bwana asubuhi ilipofikia, magari ya ambulance kwa msululu yalikuwa yakitiririka kuingia ndani ya hoteli ile waliyokuwemo akina Neema na Cliff, pilika za watu zikasikika tu huko koridoni na sehemu nyinginezo kuonesha kuwa ugeni ulikuwa ikiingia humo ndani.
Ikawa mchana ikawa jioni na hatimaye usiku mwingine. Safari hii saa tatu kamili ilipotimu, hodi ikagongwa chumbani kwa Neema aliyekuwa mlangoni ni Father Gilbert akiwa na meneja wa hoteli.
"mwanangu, habari yako!" alisalimia Father Gilbert kwa tabasamu pana lakini akitunza mipaka ya mita moja kati yao ili asisababishe Corona.
"Salama tu father, nafurahi kukuona," aliitikia Neema kwa adabu na hofu kubwa ya kipi kifuatacho; wakati huo Meneja akadandia.
"Father tunashukuru sista Anne hapa amekuwa akifanya novena na maombi mazito kuombea wagonjwa wa corona. Na leo umefika wakati muafaka,"
"Kweli sista Anne!?" alisema kwa furaha Father Gilbert akionekana yupo tayari kujiunga na hiyo sala hata dakika hiyohiyo.
"Sista Anne,kamanda ameenda kumleta dereva wako, mimi kwa leo nitaomba udhuru, nyie kaendeleeni tu na sala,"alisema Meneja akimtazama Neema, loh Neema akatamani akae chini kwa maana mchango ulimkamata.
Ikawa basi kila hatua aliyopiga Neema kuelekea huko kwenye chumba cha sala ilikuwa ni maumivu makubwa kwake. Akajutia hata ujanja wake wa kujifanya anaanzisha sala kwa ajili ya kukutana kimapenzi na Cliff, akaona wazi Mungu anamuadhibu kwa mara nyingine kwasababu kama si Mungu ni nani mwenye nguvu ya kupangua kila wanachokuwa wakikipanga?
Dhima na tashwishwi zikawa hofu na wasiwasi kichwani mwa Neema, mavazi yake ya usista yakawa hayamtoshi, mbele akiwa meneja wa hoteli na pembeni yake akiwa Father Filbert aliyepiga hatua sambamba naye kuelekea kwenye safari ya kuumbuka.
"Ee Mungu naomba mfanye Cliff asije leo huku," alisema sista Anne ikawa ni sala yake ya mwisho kusali kwa imani kubwa mno, tena kama sala ile angeliuomba mlima uhame basi hakika andiko la Nabii Issa lingetimilika katika karne hii ya kizazi cha nyoka, majoka na manyoka.
Loh chumba kilikuwa kitupu na kamanda alifika na ujumbe kuwa hali ya dereva si nzuri jioni hiyo, hivyo pia alikuwa na udhuru ya kutofika ibadani. Kauli hiyo ikawa imemsuuza moyo Neema, akajifuta kijasho cha hofu kilichokuwa kikimtiririka usoni mwake.
Kwa mara ya kwanza akamshukuru Mungu kumnusuru maana yajayo yangefurahisha. Akamtazama kamanda na meneja waliokuwa wakijifanya kutaka kuondoka akasema: "Basi kwakuwa tupo wachache leo sidhani kama kuna kitu cha muhimu kuliko kumuomba Mungu, naomba kwa dakika kumi na tano tu tujitolee kwake kuwaombea ndugu zetu wanaopata tabu duniani na akhera."
"Oh sawa kama ni dakika kumi na tano, tafadhali tuanze," alisema Kamanda akikazia dakika kumi na tano huku suraye ikawa surambi maana alikumbuka sana jaramba la jana yake kwa kupigishwa sala kwa masaa mawili taslimu na hakutaka tena litokee.tena ukute hapo walikaa kitako kabisa na meneja kuwa wasingethubutu tena kusogelea sala za sista Neema, wangemuachia yeye na dereva wake.sasa vuta picha Cliff angevyojinoma.
Basi bwana, Sista Anne akapata nguvu akasalisha kwa ustadi mkubwa siku hiyo mbele ya Father Filbert,hata dakika kumi hazikufika,ikawa tayari sala imeisha. Kila mmoja alikuwa na nguvu na ikawa kama vile roho mtakatifu aliwaingia maana mzuka ulikuwa umewapanda hatari.
Sasa katika kuagana kila mmoja akipanga kurudishwa chumba chake ndipo, Father Filbert akakumbuka jambo.
"Samahani kamanda huyo mwenzetu ambaye anaumwa, vipi ni kwema kabisa?"
"aah huyo dereva wa parokia!?" aliuliza meneja.
"kwani ni dereva wa parokia!?" alihamaki Father akimtazama sista Anne.
"ndiyo," alisema sista Anne akijua kabisa anaongopea lakini akauongea uongo wake kwa kujiamini maana alihisi angetetema tu angedabwa kama si sasa basi ni punde maana hata hicho cheo cha udereva wa parokia alikitunga na hajui kama kipo au lah! na hapo akajiandaa kujibu swali la; dereva wa parokia ipi.
"Aisee, tatizo ni nini?" alisema Father Filbert akitoka kwenye mawazo ya sista Anne.
"Hatujui anaumwa nini, ila ameonesha ana homa hivyo tumempeleka haraka kile chumba cha wagonjwa anafanyiwa vipimo kwa uangalizi wa karibu sana, hatuwezi kuwa na uhakika zaidi ila ametengwa kwa muda," alisema kamanda.
"kwa hiyo kama atakutwa na Corona nini kitatokea!" aliuliza Neema.
"hapo lazima watakuchukua na wewe, mtatengwa. na najua mimi na Kamanda hatutasalia," aliongeza kamanda akitweta mno, lakini katika maneno hayo Neema akagundua kitu, na yeye saa ileile akapiga chafya ya kwanza, ya pili loh! kamanda, Father na meneja wakakimbia hali wakivaa vimaski zao mara kundi la madaktari wakambeba Neema kumpeleka chumba alichomo Cliff.
MWISHOOOOO
0 comments:
Post a Comment