Chombezo : Haunikomoi, Tunakomoana
Sehemu Ya Tatu (3)
"nini!? hapana haiwezekani.. mbona tulishaongea ukanikubalia?" alihamaki Merina na kwa mara ya kwanza nilimuona akichukia.
"Sikatai mke wangu, lakini nahisi kuna jambo sio zuri litaenda kufanyika huko.." nilisema nikamuona akitazama pembeni kwa aibu fupi halafu akakaza shingo kunielekea huku akirejelea ukavu wa macho yake.
"Jambo gani baya, nimekwambia naenda kufanya shoo kisha narudi, siwezi kuacha kwenda na kuacha pesa zote hizo!"
"Mwambie Omary nitamlipa ila usiende.." nilisema, sasa nilipomtaja Omary akashtuka. akaachia mdomo wazi kwa kuduwaa. nikagundua nilikosea kutaja jina lake kwa kuwa alifahamu sifahamiani naye na yeye hayo mambo ya mapromota wake na muziki wake huwa sihusiki nayo, niliyemfahamu ni producer wangu tu. hivyo jina la Omary najua lilimshtua kitu.
"ooh ulifungua simu yangu si ndiyo?!" alifura Merina akigundua kuwa lazima Omary nilikuwa nimemjulia kwenye simu yake na kwa maana hiyo ninajua mazungumzo yao yote; nikamuona akitetemeka midomo.
Sasa kiukweli sikuwa na haja ya kuficha, nikakubali kuwa kweli nilifungua simu yake na nilijua yote yanayoendelea.
Ghafla nikamuona anaenda nje na simu yake akiwa analia. Dakika si nyingi akarudi mbele yangu na kusema kwa kiburi cha chinichini: "Cliff sitaenda Oman, nimemwambia Omary amekubali lakini kanipa sharti kuwa nimlipe pesa zake alizogharamia kufanya matangazo, advance za wasanii na pesa aliyobukia ukumbi Oman, jumla ni shilingi milioni 34."
"tutamlipa," nilisema nikimaanisha pesa za Merina na zangu tukizikombeleza zitafikia hiyo pesa vizuri tu.
"weee, sema utamlipa wewe, tutamlipa kivipi! mimi pesa zangu sitaki. akha mwenzangu! kama kuolewa ndiyo huku najuta walahi! " aliwaka.
nikatafakari na kugundua kuwa hata iweje lazima Merina aende Oman kwa sababu kutokwenda kwake maana yake alitoa mimba bure na dhambi hiyo ingemhukumu akikaa hapa Bongo. Na ninauhakika ananikomoa kwa kunipa gharama hizi zote na kujitoa kwenye malipo makusudi ili nimruhusu aende, nilifahamu kuwa hata huyo Omary hajazungumza naye lolote ni muongo alizuga tu na simu nje na kurudi nayo ndani.
sasa mke wangu alijutia mimi kumuoa, aliona ninambana, maana yake ataniomba talaka au atanitenga?
Hapana niliogopa hayo yasijetokea. Nilimpenda sana mke wangu na sikutaka aniache au tutengane kwa chochote na zaidi kabisa naogopa ndugu, jamaa na marafiki wasijenicheka kwasababu wengi walinionya nisimfanye mke wangu awe msanii na mimi nilikataa.
Nikaona kabisa hali itakavyokuwa huko kwenye mitandao ya kijamii jinsi hao team Merina watakavyonipakazia wakijua tu nimeachana na Merina.
Nikajikuta najisemea kimoyomoyo; 'hapana ndoa lazima ibakie'.
Kwa kusema hivyo nikajikuta nazungumza kinyonge maneno ambayo wanaume wenzangu wamkiyasikia mtaniita MUME BWEGE; nilisema.
"sawa mke wangu, nakuruhusu nenda Oman, lakini naomba tafadhali jichunge.."
Loh! niliposema hivyo akaripuka kwa furaha na kuja kunibusu bila soni akiniahidi kuninunulia gari na nguo za kisasa kutoka huko Oman. Nikafarijika kumuona anafurahi, lakini moyoni niliumia nikivuta picha mke wangu anaenda kufanywa changudoa na waarabu, dah!
Siku zikafika hatimaye safari ikajiri; akaenda alipoenda huku nyuma nilichokiona kikubwa ni picha zake akiwa ameziweka whatsapp na kwenye insta akiwa kwenye ndege; simu yangu ya whatsapp moja niliyompigia kwa video call alinionesha kuwa ameishafika Oman na anaenda kwenye hoteli atakayolala.
Kuanzia siku hiyo sikumuona tena mtandaoni Merina na wala simu yake haikupatikana kwa whatsapp. Sikujua chochote kuhusu yeye isipokuwa kupitia Omary ambaye namba yake niliisevu siku ile.
NIlijaribu kumpigia huyo Omary Promota, akaniambia yupo bize nimtumie text. nikasema kuwa namuulizia mke wangu Merina kama yupo salama.
Akaniambia yupo salama salimini nisiwe na wasiwasi. Nikamwambia naomba nizungumze naye kupitia simu yake ili nijue anatatizo gani kiasi kwamba hapatikani hewani.
Akaniambia angefanya hivyo, lakini nahisi baadaye aliniblock maana hata nilipotuma meseji na kupiga simu kwa whatsapp pia simu ilikuwa haiendi.
Mpenzi msomaji hakika hakuna marefu yasiyo na ncha. kumbe yote kunichenga kote kule nilikuwa naigiziwa tu maana nilipojaribu kumpigia huyo Omary kwa kupitia namba nyingine alipokea na baada ya kugundua kuwa ni mimi mume wa Merina akaniambia maneno makali sana alisema hivi:
"Braza, Merina sio wa hadhi yako sasa hivi, achana naye nakushauri, oa mtu mwingine.. watu wanakula raha za dunia, acha kuwasumbua."
Roho ilinisigina nikajua ni wazi kuwa mke wangu ananisaliti na huyo Sayeed Sayeed, lakini ni mlaumu nani maana kama kumruhusu si nilimruhusu mwenyewe? Simjui huyo Sayeed Sayeed lakini kwakuwa niliambiwa ni mwarabu basi picha iliyokuwa ikinijia kichwani kila mara ilikuwa ni ya Osama Bin Laden akifanya mapenzi na mke wangu na hiyo fikra ndiyo ilikuwa ikiniamsha katikati ya usiku nikikosa usingizi kabisa.
Wiki ilikatika na hatimaye wiki ya pili iliingia, sikufichi nilijaribu mara kadhaa kumpigia mke wangu maana nilifahamu huenda ameishamaliza usaliti wake na sasa walauu atakuwa ametoa block aliyonipiga, lakini wapi hakupatikana bado si kwa simu yangu wala ya mtu mwingine.
Japo maumivu ya kusalitiwa yalikuwa makubwa, lakini kusema kweli nilimmiss sana Merina wangu nikimtazama tabasamu lake mitandaoni na kwenye magazeti nilikuwa nikiridhika mwenyewe.
Kweli bwana baada ya kusubiria sana kwa muda mrefu hatimaye mke wangu alirejea hakuwa na afya sana hata kwa kumtazama najua ni kutokana na aliyoyafanya huko, atakuwa amechoka mno.
Lakini pamoja na kurejea kwake nilikuwa nina hakika yule Merina niliyekuwa nimemuoa alikuwa amekufa hukohuko Oman, siye huyu.
Alikuwa ni yeye kiumbo sikatai, lakini tabia yake ilibadilika kabisa, alikuwa hatulii, safari za mara kwa mara, klabu na yeye, yeye klabu. Kulala nje ilikuwa kawaida. Alikuwa haniheshimu tena. alikuwa akivaa vinguo vya ajabuajabu mno na mbaya zaidi hata ile ahadi ya kuninunulia gari iliishia hapohapo japo alikuwa na hela na nilimuona kabisa akizitumia vibaya mno.
Sio uongo, ndugu msomaji, nilimheshimu sana mke wangu kiasi kwamba hata kuchepuka nilikuwa sichepuki. Wanawake wengi walinishobokea kisa tu walifahamu kuwa mimi ni mume wa msanii mkubwa, lakini niliwakataa na nikabakia na mke wangu tu pamoja na yote .
Nasema hayo kwa uchungu kwasababu siku niliyojikuta naupata ugonjwa wa gono nataka hata nyinyi mfahamu kuwa aliyeniambukiza hakuwa mtu mwingine isipokuwa mke wangu, na aliniambukiza kwa penzi lake alilonipa siku moja tu tangu arudi tena kwa kumuomba mno.
Kwa kuupata ugonjwa wa gono nilijua sasa siku moja nitaupata ukimwi kabisa nikiwa sipo makini, nilichoamua ni kumwambia mwenzangu afahamu alichonacho mwilini mwake ili ajirekebishe tabia yake na pengine aache kabisa anayoyafanya.
Lakini kitu kilichonishangaza ni kwamba, nilipojaribu kumwambia mke wangu kuwa nimegundulika nina gono na sikutembea na mtu mwingine yoyote, alinigeuzia kibao na kunituhumu mimi kuwa ndiyo niliyemuambukiza eti kwa sababu nilifahamu haraka kama nina gono kuliko yeye ambaye ninamtaja kuniambukiza.
Nilijaribu kumuelewesha kuwa dalili za gono na magonjwa mengine ya ngono yanaonekana haraka kwa mwanaume kuliko mwanamke, lakini hakutaka kukubaliana na maneno yangu; akawa kiburi zaidi japokuwa siku si nyingi nilimuona akitumia dozi hivyo nilikuwa nina uhakika alikutwa na gonorea pia na alikuwa akijitibia.
Nikajaribu sana kumfuatilia baada ya kupona kwake ili nijue amebadilika au lah! lakini nilijua kuwa hakubadilika hata kidogo.
Hilo ninalisema wazi kwasababu kuna siku nilivizia simu yake tena aliporudi akiwa amelewa, nikakuta kuna meseji zake za whatsapp akizungumza na mtu wakiambiana wakalale hoteli fulani, huyo mtu alimwambia wazi kuwa anataka kufanya naye ngono pasipokutumia mpira na cha kustaajabisha mke wangu akamwambia kuwa bei ya kufanya kavukavu inazidi ile ya kawaida.
Huyo mtu akajibu sawa.. na hizo meseji zilikuwa ni za juzi tu maana yake chochote kilichofanyika basi kilifanyika jana ambapo mke wangu hakurudi nyumbani. Siku nyingine nakumbuka nilimsikia akizungumza na simu nje akiwaambia wenzake, "najua shoga hii ndoa inaniharibia kweli biashara zangu.. kibaya huyu bwege hataki kuniacha kaning'ang'ania kweli, sasa mimi namkomesha makusudi.. na nakwambia hata uchafu wangu kwenye simu siufuti.. ndiyo anaijua password yangu vizuri, sasa akifungua akikuta mameseji ya madanga kama atalia basi akalilie hukohuko mbele."
Akyamungu baada ya kusikia hayo nilijuta, nikalia chozi la mwisho ambalo niliapia kuanzia siku hiyo sitalia tena. Nikasema hata kushiriki tendo la ndoa na mke wangu sitajaribu tena kwa sababu hana lengo zuri na mimi ila ananikomoa.
nilichofanya nikuwa nakopi ushahidi wa kila ninachokiona cha Merina kisha nikahamia kulala upande wa uani na waziwazi kabisa tukawa hatusalimiana, yeye akawa anaingia anavyotaka na mimi nikawa naingia nyumbani bila kumuuliza chochote. Taratibu nikaota sugu ya moyo japo iliniuma mno.
Ikanibidi nitafute mfanyakazi yaani housegirl ili anisaidie kunipikia na kusafisha nyumba kwasababu mke wangu hakuwa akifanya chochote, maana hata nguo zangu nilifua mwenyewe.
"Naona umeniletea demu wako..hahaa aya anisaidie na majukumu ya kitandani, mimi si sikupi siku hizi!" alisema mke wangu kwa kebehi akiniambia mbele ya dada wa kazi, nikamezea tu.
Kesho yake nikaona kama analipiza, maana alimleta kijana mmoja sharobaro nyumbani akanitambulisha kuwa alikuwa ni houseboy wake eti atamsaidia kufanya kazi. Nikaona wazi kama ananilipizia; nilipenda sana nimueleweshe kuwa mimi sikuwa nina maana aliyoimaanisha yeye lakini nilishindwa kuongea, na hata walivyoingia na kulala na huyo kijana chumba kimoja nilinyamaza kimya, nikaifanya iwe siri ya familia.
Hata rafiki yangu producer alipoaniambia mabaya ya mke wangu huko nje, nilimtetea mke wangu na kusema hayupo kama anavyoonekana huyo nje; nilimtetea. Kinyume kabisa na mwenzangu ambaye akiwa na marafiki zake aliniponda kadri awezavyo.
Kumbe bwana kuna majirani zetu walikuwa wakiuona mchezo mzima, hao ndiyo waliwaita mapaparazi wakawa wanavujisha habari huko kwenye magazeti kuwa Merina na mumewe paka na panya. mara Merina anaingiza wanaume ndani wakati mimi nipo.
Siku hiyo hizo habari zinatoka nikajikuta napokea meseji na simu nyingi sana kutoka kwa ndugu marafiki na jamaa wanaotujua, wakiniuliza kulikoni? nilijaribu kuwaelezea kuwa ni habari za uongo, lakini hawakuelewa kwani tayari walikuwa na habari ambazo mke wangu alizungumza kwenye interview na vyombo vya habari kuwa; chanzo cha yote ni mimi ambaye eti nilikuwa nalewa hovyo, nampiga, nilikuwa nikitembea na wanawake kiasi cha kuwaingiza ndani ya nyumba na mbaya zaidi eti nilimuambukiza ugonjwa wa gono.
ilikuwa kama vile kila alichonifanyia yeye alinigeuzia mimi na kuviongezea chumvi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment