Chombezo : Haunikomoi, Tunakomoana
Sehemu Ya Pili (2)
Tena kwa furaha ya habari njema usiku ule, Merina wangu akanipa cha kulalia kwa kupekuapekua ili kama huyo mtoto yupo azidi kuongezeka masikio na vinyamanyama huko tumboni na kama hayupo pengine ikawa tulighafilishwa na homa ya UTI ilomtia kichefuchefu basi mimba ikajitunge upya.
Kweli asubuhi tukaenda hospitali ya karibu, ile kushuka tu kwenye gari, wagonjwa walimshangaa mno Merina, wengine wakasahau na kuumwa kwao, wakaomba kupiga naye picha. Na madaktari wakatuhudumia kwa upendeleo.
"Merina; naupenda sana wimbo wako wa nakugawa; karibu sana," alisema dokta wa kiume.
Ikabidi nijitutumue na mimi niseme neno maana alikuwa akimtazama sana Merina wangu.
"Samahani dokta, nimemleta mke wangu umtazame kama ana ujauzito.." niliunguruma sauti yangu nikiweka msisitizo kwenye neno Mke wangu, ili ajue na aache kunidharau.
Akashtuka kidogo kwa kauli yangu, akawa kama vile anatuthaminisha. akainuka bila kusema neno akamuita nesi na kumuomba Merina aongozane naye kwa ajili ya vipimo kadhaa, wakati huo mimi nikarudi kwenye benchi la wagonjwa kusubiria.
Majibu yalitoka kuwa kweli Merina alikuwa ni mjamzito miezi miwili; hebu vuta picha furaha yangu.
Najua ilikuwa ni mapema mno kutoa taarifa za ujauzito kwa watu, lakini nilipagawa kiasi cha kumpigia rafiki yangu producer kumwambia kuwa tayari mke wangu ni mjamzito.
Akaniuliza; "vipi umepiga hesabu tarehe kuwa mimba ni yako?"
Doh! hapo nikajikuna kichwa, nikakata simu na kuanza kuhesabu kimoyomoyo kuanzia kipindi kile kabla ya Merina kutoka kimuziki na kipindi nilichokuwa naye. Nikaona tarehe zinakuja kwangu, mh lakini kama alichepuka? niliwaza, nikasonona zaidi lakini nikajipa moyo na kuona ni wasiwasi wangu tu, mbona Merina ananielewa!
hiyo sio kesi, mimba iliendelea kuchipua tumboni na ikaanza kudhihirika wazi, wakati huo nadhani ilifikia miezi mitatu na nusu kama sio minne kamili.
Merina alianza kuwa bongebonge, maziwa yakamjaa, uso ukamvimba na weusi wa ghafla ukamzonga; hali iliyomfanya kidogo asionekane vile watu walivyozoea.
Habari njema ni kwamba wazazi wangu na wake walitupongeza mno, lakini habari mbaya ni kwamba Merina alipondwa na mapromota, wasanii wenzake, wanahabari na mashabiki wake waliiojiita team Merina, kisa tu eti msanii mchanga kakimbilia kupata mimba hivyo atapotea kwenye muziki mapema mno.
Hapo wenyewe wakazungumzia kuwa eti kisa mimba atashindwa kufanya shoo kwa kipindi cha takribani mwaka na nusu na maana yake hata kwenye vyombo vya habari anaweza kupotea kwa kuwa hatakuwa na mvuto tena wa stori zao.
"Merina sio msanii mkubwa sana, na kusema ukweli mziki wake sio kitu kinachowavutia mashabiki wake, bali alivyolivyo. Watu wanampenda kuwa naye, wanamtaka hata walale naye, wana matumaini ya kumpata awe mpenzi wao; hivyo kuthibitisha kuwa ana uhusiano mwingine na kufikia kubeba mimba maana yake watu hawa wenye fikra hizo juu yake watamuacha na kuendelea kushabikia wasanii wengine chipukizi wakike wenye mvuto zaidi yake," alizungumza mtangazaji mmoja waziwazi kwenye redio nami nikasadiki ayasemayo maana kweli wanaume ndiyo mashabiki wa mke wangu.
Maneno yalikuwa mengi mno, na kiukweli nilijiandaa kwa yote na kumtia moyo mke wangu kuwa hakika tutayapita ikiwa tu tutayapa mgongo yasemwayo na kuyapuuzia. Lakini wingi wa miluzi humpoteza mbwa na mke wangu akapotezwa na lawama na vijembe, kisirisiri akaanza mipango ya kuitoa mimba, umaarufu ulimlevya.
Nilichokumbuka nilisafiri kwenda Muhoro mara moja, nilirudi kesho yake kwa haraka mno baada ya kupigiwa simu ya dharula nyumbani. Nilifikia hospitali nikimkuta mke wangu amelazwa, taarifa nilizopewa ni kwamba Merina alidondoka akiwa bafuni, akajiumiza tumboni na hatimaye mimba imechoropoka.
Ni uongo! ni uongo mtupu!
nilijuaje? usibanduke.
usiku mmoja nakumbuka niliweza kuvizia simu yake nikaipekua vizuri meseji zake na watu wake. Nyingi nikaona zipo whatsapp, nikafuatilia mazungumzo yao kwenye grupu la masupastaa kama wanavyojiita sikuona neno baya huko.
Macho yangu katika kupekuapekua kwangu yakaganda kwenye meseji ya mtu fulani aliyeseviwa Omary Promota.
Mengi kati ya mazungumzo yao yalikuwa ni ya sauti yaani voicenote, nikachukua earphone zangu na kuzichomeka nisikilize maana zilikuwa ni nyingi mno, zikitoka kwa mke wangu kwenda kwake huyo Omary na kwake kuja kwa mke wangu na mazungumzo yao yalikuwa yameanza tangu wiki iliyopita kama tarehe zilivyojionesha.
"Kuna show ya uarabuni, Oman unatakiwa kuja kufanya huku mwezi ujao," ilikuwa ni sauti kutoka kwa Omary.
"mh sidhani kama nitaweza kuja, si unajua mimi ni mjamzito, halafu shoo za ndani tu ndiyo nimezoea kufanya hizo za nje hadi mwakani nitaanza," alisema mke wangu.
"sikia, hilo suala la mimba kwanza ni kiherehere chako, na hapa utapishana na pesa nyingi sana za kiarabu, waulize wasanii wenzio pesa wanapopatia,"
"mh kwani hiyo show mimi watanipa shilingi ngapi?"
"ni kama milioni hamsini na nane, hapo nikishakata cha kwangu.."
"weee! muongo.."
"kweli tena kwasababu wewe una wimbo mmoja. halafu kitu ambacho hukijui huku kuna Sayeed Sayeed."
"ndio nani?"
"duh humjui?"
"simjui.."
"sikia huyo jamaa ni sponsor wa wasanii, ukienda Oman anakukaribisha kwake mnapiga stori, anakupa mihela ya kutosha na gari utakalo, ni tajiri wa kutupwa anamiliki visima vya mafuta na hapa nina mualiko wako kutoka kwake, sasa kama ukiwa mjanja ukimtumia vizuri huyu unarudi nyumbani na mamilioni."
"wee Omary hapana mimi mambo hayo unayoyazungumzia siyataki na siyawezi, mimi ni mke wa mtu na namheshimu sana mume wangu."
"kwani nani kazungumzia habari za kuvunjiana heshima, wewe njoo piga hela yako rudi kwenye miheshima yako na huyo bwege lako, kwanza ujue unanipa tabu sana mimi kama promota wako, watu hawakutaka uoleweolewe haraka hivyo, matajiri kibao wenye pesa za madini wanakutafuta,,"
"Omary naomba usimuite mume wangu Bwege..na hilo dili lako silitaki," alisema mke wangu nikapoa moyo na kumeza mate, nikamtazama Merina aliyekuwa bado amelala wala hajui kinachoendelea, nikaketi vizuri na nikaendelea kuzisikiliza hizi sauti nyingine, zilizoanzia tarehe iliyofuatia.
"oya vipi? kwahiyo bado unakaza?"
"kuhusu nini?"
"lile dili,"
"agh sitaki..tafuta msanii mwingine wewe si unao wasanii wengi kwanini mimi lakini.."
"dah kusema kweli, wenzako wote walishaendaga Oman na bwana Sayeed Sayeed anakutaka wewe ndiyo hajakuona kule,"
"mh weeeh ina maana hadi Dina naye alishawahi kwenda kwa Bwana Sayeed?"
"hee! we unadhani lile Prado kalipataje? au kisa anajifanya siku hizi anaimba nyimbo za dini!"
"duh na Frida naye?"
"hadi huyo nilishampeleka, tena anang'ang'ania nimrudishe balaa, si unakumbuka zile pesa alizokuwa akizirusha hadi kwa waandishi wa habari.."
"ndiyo!"
"basi jeuri ile ni kutoka kwa Sayeed, wewe kaa hivyohivyo na umasikini wako, utembelee daladala."
"mh, kwahiyo ninaenda huko Oman na nani?"
"utakuwa na wasanii wengine kama wanne hivi na bendi ya muziki wa dansi. hautakuwa peke yako hadi mimi nitakuwepo."
"mh, lakini mume wangu jamani sijui itakuwaje?"
"wewe, hao wanaume ni pasua kichwa tu, ukijifanya unamtunziatunzia heshima yake, yeye kesho au kesho kutwa anakusaliti bila kutarajia, sasa bora wewe unafanya haya kwa ajili ya pesa ndefu. Cha msingi wewe jiandae na hiyo mimba ichoropoe mwezi mzima unatosha kabisa kujiweka fiti na kwenda kupiga shoo ya nguvu Oman.."
"mh ngoja nifikirie.." hilo ndilo lilikuwa jibu la tamati kutoka kwa mke wangu. Sikutaka kujiuliza mara mbili ni wazi Merina ameamua kunisaliti na ameshaanza hatua ya kwanza ya kuteketeza kiumbe kilichomo tumboni mwake ambacho kilikuwa kimebeba damu yangu hakika.
Nilitetemeka kwa hasira na ghadhabu, nikajitumia hizo sauti kama ushahidi na nikaisevu namba ya huyo Omary kwenye simu yangu. nikatulia kimya nikisema ngoja nione kama hayo yaliyosemwa yatatimia au lah!
Kama nilivyotarajia ni kweli siku ya pili yake tu, usiku Merina alinionesha tangazo lake la show yake ya Oman.
"Mume wangu, nimepata shoo Oman, ona!" alisema Merina akiitazama picha yake iliyokuwa kwa ukubwa mno kwenye hilo tangazo.
"waooh! hongera mke wangu," na mimi nilisema kwa kujikaza homa ya joto baridi ikinipanda, tumbo likivurugika ghafla.
"Ni tarehe 25 mwezi wa nane, sijawahi kwenda nje ya Tanzania mume wangu, Mungu ameniona.." alisema na kumhusisha Mungu humohumo.
"Kikubwa ni kushukuru tu, sasa je wewe utakuwa umepona!?" nilisema nikikumbushia kidonda chake cha kutoa mimba.
"kupona hii huwaga ni wiki tu, hata usijali," alisema Merina hilo neno lake 'huwaga' likanifanya nishtuke kidogo nikajiuliza; ina maana amezoea kutoa mimba au?
Mpenzi msomaji fahamu tu kuwa suala hili nililiweka kifuani sikuweza kumwambia rafiki yangu producer maana ni ya kifamilia zaidi , lakini nilishangaa tu siku aliyonitumia meseji na kuniambia maneno haya nanukuu:
"kaka naona shemeji mimba yake bahati mbaya, halafu umemruhusu aende Oman..je umejiandaa kisaikolojia?"
Nilikaa kimya kama nimeloa maji ya baridi, nikasema sitamjibu chochote hadi nionane naye. siku kama mbili tatu hivi, niliweza kuonana naye, nikamuuliza alichomaanisha kwa kauli yake ile.
Akacheka sana na kuniambia kuwa ameweza kuwakuza wasanii wengi sana wa kike kimuziki, na anafahamu soko lao. Akanifafanulia kuwa ukiachilia na kuuza nyimbo zao kwenye miito ya simu na kufanya show; wanajiuza kwa waarabu Oman kwa pesa nyingi mno.
Kwa kusema hivyo maana yake alinitaka nijiongeze kuwa mke wangu anaenda kujiuza na nijiandae kisaikolojia kwa kuwa mwanamke akisaliti iwe kwa tamaa au kupenda basi hawezi kujidhibiti akamheshimu mumewe, daima kiburi atakitanguliza mbele.
Nilishusha pumzi machoni nikimuonesha nina imani na Merina, lakini moyoni maneno yake yalikuwa kama nyundo inayogongelea misumari ya maumivu ya ukweli niliokwisha kuufahamu tayari.
Niliondoka bila kusema neno, nikarudi nyumbani kwa mke wangu, niliyemkuta akifanya mazoezi ya viungo mepesimepesi huku akiimbaimba kama anavyofanyaga siku zote ili kutafuta pumzi.
Sasa kutokana na niliyonayo kifuani pangu, nilishindwa kuvumilia nikamuita pembeni nikamwambia kwa upole.
"mke wangu, naona usiende Oman, najisikia vibaya kuhusu hii safari yako."
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment